MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru sana Waziri Mkuu kwa ufafanuzi mzuri na ambao kweli ulitolewa na Waziri wa chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tunayo makundi mawili, kundi ambalo lina uwezo wa kifedha lakini bei iko juu na utaratibu wa Serikali ni kuwapelekea ili kwenda kupunguza mfumuko wa bei, lakini tunalo kundi pia ambalo lilitajwa na Waziri wa Kilimo, kaya kama 3,000 hivi ambazo zina hali mbaya na hazina uwezo hata wa kununua chakula. Je, Serikali sasa ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba jambo hili linaenda kuwasidia wananchi wake?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uwezo mkubwa, mdogo au wa kati wa kifedha ni jambo pana ambalo kila mmoja na katika kila familia inayo utaratibu wa kujiongezea uchumi kwenye maeneo yao badala ya Serikali kuwaahidi kwamba tutawapelekea fedha ili kuwaongezea fedha; na kwa kuwa tumesema chakula sasa kinapanda kwenye masoko, ni kweli, lakini ni kwa sababu ya hofu ya hali ya hewa ambayo tunayo ya msimu huu wa kilimo, watu wengi wameweka chakula ndani wakidhani, kutumia nafasi hiyo wanaweza kujipatia fedha nyingi. Jambo hili halikubaliki kimsingi kwa sababu tunawaumiza wale ambao wana kipato cha chini kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata kama hali ya chakula inakuwa nzuri, bado tuna kundi la watu ambao hawana uwezo wa kifedha. Muhimu zaidi watanzania wote tutambue umuhimu wa kila mmoja kuwa lazima apate chakula, aweze kupata mavazi, aweze kupata malazi kwa kile kidogo alichonacho.
Kwa hiyo, wafanyabiashara wetu nawasihi sana, tusijenge tabia ya kupandisha bei vyakula au bidhaa zetu bila sababu yoyote ile ili iweze kuwawezesha wale wote ambao wamezoea kuishi katika maisha ya kawaida, maisha ya kati na wale wapate chakula, waweze kupata huduma nyingine ili pia waweze kuendesha maisha yao. Huo ndiyo msingi imara wa jambo hilo.