MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa mujibu wa taratibu za kisera tulizonazo, Serikali ina wajibu wa kuangalia hali ya chakula nchini. Kwa taarifa ya Serikali, Halmashauri 55 zina upungufu wa chakula. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuleta chakula ili kupunguza mfumuko wa bei ulioko sokoni sasa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la chakula limeelezwa vizuri sana na Waziri wa Kilimo kupitia taarifa Bungeni juzi na taarifa yake imefafanua vizuri na hatua ambazo Serikali inazichukua za kuhakikisha kwamba Watanzania wanaendelea kuwa na akiba ya kutosha kwenye maeneo yao ili Watanzania waweze kuwa na uwezo wa kuendelea na uzalishaji mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, sikusudii kurudia maelezo ya Mheshimiwa Waziri, lakini Serikali inaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara wa ndani pia kutumia nafasi hii kufanya biashara kutoka Wilaya moja ambayo ni kwenye mazao mengi kwenda maeneo mengine ili kuweza kuongeza idadi ya chakula na kupunguza bei kwenye masoko na tunao ushahidi wa kutosha kwamba Mikoa ya Rukwa, Mbeya Songwe, Njombe, Iringa, Ruvuma bado ina chakula cha ziada, lakini pia hata kwenye soko letu la Kimataifa - Kibaigwa kuna mahindi ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wafanyabiashara wa ndani watumie nafasi hiyo kuweza kuchukua chakula na kupeleka kwenye maeneo ambayo yana upungufu. Hata jana tulikuwa tunazungumza pia na Mheshimiwa Mathayo, Mbunge wa Same Mashariki namna ambavyo Same imekuwa kame wakati wote, hata msimu ambao tunakuwa na mvua nyingi, kuona namna nzuri ambayo tunaweza kuwasaidia kupata chakula kwa kutumia pia hata wafanyabiashara wa ndani zaidi ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeanza kushuhudia kuona mvua zikinyesha ingawa siyo nyingi za kutosha, lakini basi pale ambako tunapata mvua angalau mara moja, mara mbili, tunawahamasisha wakulima kulima mazao ya muda mfupi ili yaweze kuiva kwa kipindi kifupi pia tuweze kujipatia chakula kwa msimu ujao wa chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kutakuwa na tatizo lolote lile, Serikali hii iko bado inajua na inafuatilia mwenendo wa hali ya chakula na ufumbuzi tutaupata kupitia Serikali yenyewe.