Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula (83 total)

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini kilichokuwa hasa kinatakiwa kipatiwe ufafanuzi, pamoja na majibu mazuri, tunafahamu namna ambavyo mapato ya Serikali yanapatikana kutoka Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Sasa tunachouliza hapa, miradi mingi ambayo imekuwa ikianzishwa kutoka kwenye Halmashauri inayotegemea fedha kutoka Serikali Kuu, fedha hizi haziji kwa wakati na badala yake miradi mingi sana inakuwa mwaka unaisha, miradi inakaa miaka mitano haikamiliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunataka tu kufahamu, miradi hii mingine ambayo kwa kweli ingekamilika ingekuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi; kwa mfano, kwenye Jimbo la Nyamagana, uko mradi wa maji wa Fumagila, una zaidi ya miaka mwili sasa na umebakiza fedha kidogo sana kutoka Serikali Kuu, kiasi cha shilingi milioni 256 hazijapatikana mpaka leo. Ni lini fedha hizi zitapatikana ili maji yanayokadiriwa kusaidia watu zaidi ya 16,000 yaweze kuwasaidia kwa wakati na kupunguza mzigo kwa akina mama? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba upungufu wowote unaotokana katika vyanzo viwili vya kuchangia katika bajeti yetu hupelekea tatizo hilo, lakini Serikali imejipanga na kwa pamoja tumeona kwamba fedha hizi sasa zimeanza kutolewa. Miradi yote ambayo haijakamilika, Serikali imedhamiria kuendelea kupeleka pesa ili miradi hii iweze kukamilika. Pamoja na mradi wake wa maji alioutaja wa Nyamagana uliobakiza shilingi milioni 200, ninamwahidi kwamba Serikali itapeleka fedha hizo ili kukamilisha mradi huo pamoja na miradi mingine yote ambayo imefikia katika hatua nzuri za utekelezaji.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri yaliyonyooka, ningependa sana kujua swali langu la kwanza kwamba, pamoja na fedha zilizotengwa, ni kiasi gani cha fedha hasa kilichotengwa kwa sababu hiyo ingetusaidia kuwa uhakika na hii bajeti kwamba fedha hizi zilizotengwa zitakwenda kukamilisha majengo haya, ili kuwafanya Askari hawa waliosubiri takribani miaka minne sasa walau hizi familia ishirini zipate makazi bora na salama ya kukaa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu tunafahamu Nyamagana ndiyo kitovu cha Mkoa wa Mwanza, nyumba hizi zinazotarajiwa kukamilika zinaweza kukidhi mahitaji ya familia zisizozidi ishirini na tano. Ukweli ni kwamba Askari ni wengi na umuhimu wa kambi hii ni mkubwa sana kwenye Mkoa wa Mwanza. Sasa ningependa tu kujua mpango wa Serikali, kuongeza nyumba zingine kwa muda na wakati ili Askari hawa wanaoishi kwenye kambi hiyo ya Mabatini na familia zao ambao sasa ina mwingiliano mkubwa na wananchi wa kawaida waweze kupata makazi mengine bora zaidi ili waweze kuwa kwenye mazingira salama nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mabula kwa jitihada zake za kushughulikia changamoto za Jimbo lake. Tulikuwa pamoja kwenye ziara wakati nilipokwenda kutembelea Nyamagana na alitupa ushirikiano mkubwa sana. Kuhusiana na kiwango ambacho kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo ni takribani shilingi milioni 565 kwa kuwa nyumba zenyewe zimefika katika hatua ya mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili alitaka kujua kwamba kwa kuwa hizo ni familia chache ambazo zitakidhi kukaa katika nyumba hizo, kuna mpango gani mwingine nilitaka nimjulishe tu kwamba, tuna mpango wa kujenga nyumba takribani 300 kupitia ile programu ambayo iko katika hatua nzuri za utekelezaji wa ujenzi wa nyumba 4,136 nchi nzima.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo ya Nachingwea yanafanana na matatizo yalioko kwenye Jimbo la Nyamagana, ningependa kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri, kauli ya Serikali juu ya barabara ya kutokea Kata ya Buhongwa kupita Kata ya Lwanima, Mitaa ya Sawa, Kanindo, Kishili, kutokea Igoma, lakini kutoka hiyo barabara inayokwenda Mkuyuni – Kanyerere – Tambuka Reli, kutokea Buzuruga kwa sabubu imekuwa ni ahadi ya muda mrefu na tunatambua namna ambavyo Jiji la Mwanza limekuwa likikua kwa kasi kila wakati. Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya ujenzi wa barabara hizi zitakazopunguza msongamano kwa kiwango kikubwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mabula, kwa kweli ni Mheshimiwa Stanslaus Mabula na Mheshimiwa Angelina Mabula (wote wawili) wamekuja tumejadili kuhusu hizi barabara, tulikubliana kwamba, tutawasiliana na Meneja wa TANROADS Mkoa ili tuhakikishe kwamba, tunaweka mikakati ya kutekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Naibu Spika, ninawahakikishia kwamba hiyo ahadi tuliyowapa tulipokutana ofisini ni ahadi ya dhati, inatoka katika sakafu ya mioyo yetu na tutahakikisha tunaitekeleza.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa matatizo yaliyopo kwenye Mkoa wa Kagera, Mkoa wa Mwanza pia ni moja kati ya mikoa iliyotajwa kuwa mikoa maskini, sasa ningependa kujua mikakati ya Serikali mbali ya majibu mazuri na mipango ya miaka mitano na mwaka mmoja, ina mkakati gani wa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati ili kuwa sehemu ya kuhakikisha na wao wanakuwemo kwenye mpango wa kuhakikisha umaskini huu unatoweka wakiwa wana nafasi nzuri ya kufanya biashara zao kwa uhuru?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema na kama tulivyoainisha kwenye mpango wetu wa mwaka mmoja na mpango wa miaka mitano kwamba sasa hivi tunaangalia jinsi ya kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo vidogo pamoja na viwanda vikubwa vikubwa, vya kati pia ili tuweze sasa kutengeneza ajira kwa watu wetu. Na hii ni pamoja na kuwawezesha wafanyabiashara hao wadogo na wa kati ili waweze kupata bidhaa zao kwa bei nafuu na pia tuangalie pia wafanyabiashara ambao wako katika sekta ya kilimo kwa sababu tumesema viwanda vidogo, viwanda vya kati na vikubwa vitatumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini kwa hiyo ni mpango wa Serikali yetu kuweza kuwawezesha watu hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa sababu tunakuja na Microfinance Act mwezi huu au mwezi wa 11 ni uhakika kwamba watu hawa, wafanyabiashara wadogo na wa kati watapewa elimu ya ujasiriamali na jinsi gani ya kuendeleza biashara zao pamoja na kuwezeshwa mitaji ni moja ya mikakati ya Serikali yetu.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Waziri kwa majibu yake mazuri na kwa mara ya kwanza Wizara hii imeonesha uhalisia wake kwa kutoa majibu kwa vitendo nawapongeza sana.
Pamoja na majibu haya mazuri ya vitendo, Halmashauri ya Jiji la Mwanza kama ambavyo imekuwa ikishiriki kwa asilimia kubwa katika kuboresha michezo, tayari imeshaandaa ramani ya uwanja mzima na imeshaanza kupita ngazi mbalimbali. Ninataka kupata tu maoni kutoka kwenye Serikali kwamba uwanja huu pamoja na kwamba utakuwa umetengenezwa eneo la kuchezea, lakini bado tutakuwa na changamoto kubwa katika eneo la mzunguko mzima kwa ajili ya kupata vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo, lakini jukwaa kuu na maeneo ya kukaa ili uwanja ukamilike na kuwa uwanja wa kisasa. (Makofi)
Je, ni lini Serikali itakuwa tayari kusaidia Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuhakikisha uwanja wa Nyamagana unakuwa ni wa kisasa na ambao unaweza kutumika na mechi za Kimataifa? (Makofi)
Swali dogo la pili tayari vifaa vimeshafika, ni lini ….
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Stanslaus naomba hilo swali la pili ufupishe kwa sababu la kwanza umelifanya refu.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini TFF waithibitishie Wizara watakuwa tayati kukamilisha uwanja huu maana tumesubiri sana na tunahitaji kuutumia haraka tunavyoweza? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba uwanja huu wa Nyamagana unakarabatiwa.
Katika kufuatilia tumebaini kwamba Mheshimiwa Stanslaus Mabula alipopata nafasi ya kuwa Meya tu mwaka 2012 Septemba alihakikisha kwamba anaondoa urasimu wa utoaji wa pesa mwezi Disemba, 2012 na mwaka 2013 mchakato wa kuanza kuagiza nyasi bandia ulikamilika, kwa hiyo nampongeza sana na ninaomba Waheshimiwa Wabunge tuige mfano wa Mheshimiwa Mabula. (Makofi)
Swali lake la kwanza ambalo ametaka kujua kwamba ni vipi sasa wanaweza wakakamilisha ule mzunguko mzima wa uwanja, nimhakikishie tu kwamba Wizara yangu ipo tayari kutoa ushirikiano (technical support) ili kusudi kuweza kuona kwamba ni jinsi gani sasa vile vyumba au eneo lote linaweze likazunguka, ikizingatia kwamba ni lazima kuwepo na facilities kama za vyumba za kubadilishia nguo na vyumba vya waandishi wa habari pamoja na vyumba vya matibabu ili kusudi uwanja huu uweze kukidhi viwango vya Kimataifa. Kwa hiyo, kupitia BMT Wizara yangu itatoa ushirikiano wa karibu sana na ninaomba Halmashauri pia iwe karibu na BMT.
Swali lake la pili sasa kwamba ni lini uwanja huu utakamilika, niseme tu kwamba Serikali inafanya kazi kama timu, kwa sababu nimeshatoa wito mkandarasi afanye kazi haraka, ninaomba Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Mwanza washirikane na Halmashauri, washirikiane na TFF ili kumsimamia mkandarasi huyu aweze kukamilisha haraka ujenzi wa uwanja huu.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu matatizo ya Jimbo la Igalula ni sawa na matatizo ya Jimbo la Nyamagana, nigeomba pia kutumia nafasi hii kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri.
Katika Jimbo la Nyamagana ziko nyumba za polisi ambazo zimejengwa toka mwaka 2010 tarehe 24 Mei zilitarajiwa kukamilika baada ya wiki 36. Lakini kwa masikitiko makubwa mpaka hivi ninavyozungumza leo nyumba zile hazijakamilika. Wangeweza kukaa askari zaidi ya 24 na familia zao na Jeshi la Polisi likaonesha motivation kubwa kwa askari hawa kuishi kwenye mazingira bora na salama ili waweze kufanya kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Mheshimiwa Waziri ananithibitishia nyumba hizi zitajengwa na kukamilika kama ambavyo mkataba wa mkandarasi unavyosema miaka minne baadaye?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mradi wa nyumba ambazo zingeweza kuwa na makazi ya takribani familia 24 pale Mwanza, ulikuwa umesuasua kidogo. Lakini katika bajeti yetu ya mwaka huu katika bajeti ya mendeleo tumetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi huo pamoja na miradi mingine ambayo imekuwa ikisua sua ikiwemo mradi ule wa nyumba ambayo familia 12 Kagera, kuna Musoma -Mara, Ludewa - Njombe, na Makao Makuu ya upelelezi ya Makosa ya Jinai pale Dar es Salaam.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na nishukuru pia kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo yaliyoko kwenye Jimbo la Makambako yanafanana sana na matatizo yaliyoko kwenye Jimbo la Nyamagana katika Kata za Kishiri na Igoma. Majibu ya Mheshimiwa Waziri ni mazuri sana ila nilitaka tu kupata uhakika kutoka kwake na sisi ambao tuna matatizo ya kupata huduma kati ya Kata ya Kishiri na Igoma tukirudia mchakato huu upya kuanzia kwenye ngazi zote ambazo amezitaja tukaleta kwake tutapata approval ya kufanya marekebisho kwa wakati? Nashukuru.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri Jafo, napenda niongezee kwenye swali la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Mabula kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumekuwa na migogoro mingi ya mipaka ambayo kimsingi si yote inaitwa migogoro. Wakati mwingine kulitokea makosa wakati wa kutafakari mipaka hiyo na kugawanya mamlaka za utawala lakini wakati mwingine inatokana tu na mabadiliko ya kijiografia na mahitaji yameelekea upande ambao pengine busara sasa inataka namna mpya itizamwe ili kuweza kurekebisha mipaka hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu niwashauri Waheshimiwa Wabunge kwamba michakato hii kwa mfumo wa kisheria na taratibu zake inaanzia huko huko chini. Kama ninyi huko chini mtatoa kwenye vikao vyote vya Wilaya na Mkoa mkawa mmekubaliana sisi huku kubadilisha hizi GN si tatizo kubwa. Kwa hiyo, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge mkazitaarifu mamlaka na vikao vinavyohusika viweze kufuata taratibu za kisheria kama zinavyotaka na kama walivyopendekeza mpaka tukafikia kuweka mipaka hiyo, wafanye hivyo hivyo katika kupendekeza kama wanataka kubadilisha mipaka hiyo na sisi Serikali hatutakuwa na pingamizi katika jambo hilo.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimwa Naibu Spika, hoja yangu bado iko pale pale kwamba pamoja na majibu mazuri ya Serikali na utaratibu mzima ambao Jiji la Mwanza unao sasa wa master plan ya miaka 20 ijayo lakini kama tunavyofahamu, pamoja na master plan bado kuna suala la fidia. Luchelele sasa ni takriban miaka kumi tangu wamethaminishwa na fidia wanaambiwa kila leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, imefika hatua sehemu wananchi wanachoka. Sasa ukopaji wa fedha hizi umeanza muda mrefu; ulianzia TIB ukashindikana; umehamia CRDB; lakini ili fedha ziweze kupatikana CRDB ni lazima kibali cha Serikali kutoka TAMISEMI kipatikane. Sasa lazima tuliweke vizuri, ni lini Serikali itakuwa tayari kutoa kibali cha fedha ili Halmashauri ipate fedha iende kulipa fidia na mipango inayotarajiwa hata ya master plan ifikie kwenye wakati wake na ikubalike vizuri na wananchi? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninayo barua ya tarehe 5 Mei, 2016. Barua hii inataka ufafanuzi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Nyamagana. Lengo kubwa ni kwamba akisha-meet haya maelezo ambayo yameandikwa humu, tofauti yake ni nini? CRDB kama nilivyosema awali, walikuwa na uwezo wa kutoa mkopo wa shilingi bilioni 5.5. Kulikuwa na tofauti pale kidogo ambapo kulikuwa na maelezo ambayo yalitaka ufafanuzi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya TAMISEMI tarehe 5 Mei ikaandika barua kwa ajili ya hayo maelezo, ambapo kwa mujibu wa barua hii, yenye kumbukumbu Na. CE.214/237/01/31 imani yangu kwamba Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza ataweza ku-meet hivi vigezo vya barua hiyo. Halafu mwisho wa siku ni kwamba Waziri mwenye dhamana ataipitia ile document. Lengo ni kwamba wananchi wa eneo hili ambao wanadai fidia, fidia yao iweze kufika.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua ni kweli jambo hili la muda mrefu, lakini naamini kwamba vigezo hivi vikipita na vikifika kwa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, basi atalitolea maamuzi sahihi.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nami naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kutokana na sababu ya msingi kwamba tatizo la Machinga, yaani wafanyabiashara ndogo ndogo pengine linaweza kuwa endelevu, hasa kwenye Halmashauri zenye miji mikubwa ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambayo ipo Jimbo la Nyamagana, napenda tu kuiuliza Serikali kwamba, pamoja na utaratibu huu mzuri ambao inaelekeza, Halmashauri zetu zimekuwa na changamoto kubwa ya kifedha. Je, Serikali sasa iko tayari kupitia Wizara ya TAMISEMI kuzisaidia Halmashauri kwa namna moja au nyingine kuweza kuboresha maeneo haya na yawe rafiki kwa hawa wafanyabiashara?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mabula kwamba siku zote Ofisi ya Rais, (TAMISEMI) iko tayari. Ndiyo maana katika nyakati tofauti tumekuwa tukitoa maelekezo mbalimbali, lakini siyo maelekezo ya maneno peke yake, mpaka ya kiutaalam. Ndiyo maana kuna Halmashauri mbalimbali hivi sasa, wengine wapo katika suala zima la uwekezaji kupitia asasi mbalimbali lakini wanaleta madokezo mbalimbali na miradi yao pale Ofisi ya Rais, (TAMISEMI), lengo ni kwamba tunayapima, yale ambayo yanaonekana kabisa kama jambo hili litasaidia Halmashauri lakini bila kukwaza Halmashauri hiyo kutokuingia katika mgogoro, tumekuwa tukizisaidia Halmashauri hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Stanslaus kwamba ofisi yetu sisi itashirikiana na Halmashauri zote. Tunajua kwamba zikipata uchumi wa kutosha zitaweza kujiendesha, zitapata own source ya kutosha, akinamama na vijana watapata mikopo, uchumi utabadilika. Kwa hiyo, sisi tupo tayari muda wote kuhakikisha Halmashauri zinafanya kazi zake vizuri.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, Mheshimiwa Jafo, nataka niongezee kwenye swali lililoulizwa na Mheshimiwa Mabula kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali inatambua ukuaji wa miji hii mikubwa na ongezeko la watu wengi wanaokimbilia mijini kwa ajili ya kutafuta riziki, ikiwemo na shughuli hizi zinazofanywa na wafanyabiashara wadogo wadogo. Hata hivyo, Serikali ina programu inayoendelea sasa ya miji mikubwa ya kimkakati ikiwemo na Mwanza ambapo tunatumia kiasi cha karibu shilingi bilioni 350 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kupanga vipaumbele hivyo, Halmashauri walihusishwa na walibainisha maeneo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo. Namwomba tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wajitahidi sana katika kuhakikisha kwamba watakapowapangia wafanyabiashara wadogo maeneo ya kufanyia biashara, basi wahakikishe kwamba mabasi madogo madogo yanayoweza kupeleka watu yanaweza kufika katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ni kweli kwamba wamachinga au wafanyabiashara wadogo wadogo ni muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu kwa sababu ni wengi na wanafanya shughuli ambazo zinasaidia uchumi wetu. Hata hivyo, niwasihi na niwaombe wajitahidi kufanya biashara katika maeneo yaliyopangwa. Kufanya biashara kwenye kila eneo ikiwemo barabarani na kuziba barabara ili watumiaji wengine wasitumie barabara, inaathiri shughuli nyingine za kiuchumi na kwa hiyo faida yao inakuwa haionekani kwa sababu inazuia shughuli nyingine za watu wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, busara hii wakiwa nayo, pia busara hiyo hiyo ya wajibu wa Serikali kwa maana ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Halmashauri zao kuwapangia maeneo mbadala yanayofikika na yanayofaa kwa biashara zao, jukumu hilo ni muhimu sana kufanywa na Serikali za maeneo hayo.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ningependa tu kufahamu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri kwamba pamoja na mikakati hii mizuri ambayo Serikali inayo katika kuwasaidia watumishi wakiwemo Walimu kupata mikopo ya muda mrefu, sasa ni lini Serikali itazishauri au itazielekeza hizi Halmashauri zetu zote nchini kuhakikisha kwamba kila zinapofanya zoezi la upimaji wa ardhi Walimu wanapewa kipaumbele katika kupata maeneo ambayo pamoja na mkopo watakaopata basi ardhi isiwe kikwazo kwao na waweze kumudu ujenzi huu wa sasa? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake anataka kujua ni lini Walimu watapewa kipaumbele kuweza kupewa viwanja pale ambapo Halmashauri zinapima. Ninachoweza kusema tu ni kwamba mipango ya upimaji katika Halmashauri zetu tunaiandaa wenyewe katika vikao vyetu. Kwa hiyo, katika kutoa vipaumbele kwenye kupima, nadhani kwa sababu tumeona kwamba Walimu wana tatizo kubwa ni jukumu letu pia kuhakikisha kwamba tunapopima maeneo basi tunatenga kwa ajili ya watumishi na si Walimu tu kama ambavyo tunavyofanya katika Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pale ambapo panakuwa pana hitaji kubwa, ni jukumu letu sisi wenyewe kuweza kusema sasa tunapima viwanja sehemu fulani tunawapa watumishi. Kwa upande wa Mwanza, tayari kuna viwanja zaidi ya 500 ambavyo vilipimwa kwa ajili ya watumishi wote kwa ujumla na sio Walimu tu. Kwa hiyo hii inawezekana inaweza kufanyika, ni mipango ya Halmashauri husika.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa hawa waajiriwa 779 walikuwa tayari wapo nchini wanafanya kazi kinyume na utaratibu jambo ambalo ni batili, ni hatua gani ambazo Serikali ilikwishachukua dhidi yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swal la pili, je, anafahamu kwamba utoaji wa vibali unaoendelea, unaendelea kunyima fursa vijana wengi wa Kitanzania kama alivyokiri kwamba wanazo sifa na wamemaliza vyuo vikuu, lakini wanakosa fursa za kuajiriwa kwa wakati kutokana na waajiriwa wengi kutoka nje kupata nafasi? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza anahoji juu ya watu hawa takribani 770 ambao waliomba vibali vya kazi na kwamba uwepo wao ulikuwa ni batili.
Kwa mujibu wa taratibu na sheria yetu inavyosema, watu hawa wakiomba vibali maana yake ni kwamba anaanzia katika Ofisi ya Kazi na baadaye anakwenda kupewa kibali cha ukaazi. Kama alikataliwa katika Ofisi ya Kazi kimsingi hapo yeye hastahili kuwepo nchini kwa sababu hiyo pia inamfanya asipate kibali cha ukaazi. Ndiyo maana tumekuwa tukifanya ziara mbalimbali na kaguzi za kuhakikisha kwamba tunawabaini watu wote wale ambao wanaishi nchini kinyume cha sheria na ambao wanafanya kazi kinyume cha utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusu utoaji wa vibali, kwa mujibu wa sheria yetu pia inamuelekeza Kamishna lazima ajiridhishe kibali anachokitoa ujuzi huo haupatikani nchini au mwajiri athibitishe kwa Kamishna kwamba alitafutwa mtu mwenye fani hiyo hakupatikana. Kwa hiyo, kwa suala la vibali, Kamishna anatoa vibali kulingana na sheria inavyomwelekeza na ni kweli kwamba Kamishna anafanya kazi hii kuhakikisha kwamba vijana wengi wa Kitanzania ambao wamesoma vizuri wao ndio wanufaike na nafasi za kazi za ndani. Ukiangalia katika mtiririko tumejitahidi sana kuzuia wageni katika kazi za kawaida ili vijana wetu wa Kitanzania wapate nafasi za kufanya kazi katika nchi yao.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili madgo ya nyongeza.
Swali la kwanza, pamoja na jitihada kubwa ambazo zimeshafanywa na Halmashauri yangu ya Jiji la Mwanza, namshukuru sana tu Mkurugenzi kwa jitihada zake anazozifanya kuhakikisha anasaidia wanawake na vijana wa Jiji la Mwanza kujikomboa.
Mheshimiwa Spika, niulize tu kwamba inawezekana haya yanafanyika vizuri kwenye Halmashauri ambazo Wakurugenzi wengi wana utashi wa kusaidia makundi haya. Ni nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba fedha hizi zinapaswa kutolewa siyo kwa hiyari, iwe ni kwa lazima kwa mujibu wa makusanyo ya mapato ya ndani ili kuwanufaisha vijana wengi zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, je, Serikali haioni sasa ni wakati muhimu wa kuongeza asilimia hizi kutoka 10 mpaka 15 kwa sababu ni ukweli usiofichika kwamba vijana na wanawake wanaendelea kuongezeka zaidi hasa katika masuala mazima ya kujitafutia riziki na familia zao pia ili waweze kujikwamua kiuchumi? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anauliza kwamba ni jinsi gani tutaweka uwe kama mkakati wa kisheria; ni kweli ukija kuangalia hata taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2013/2014, kuna outstanding ya fedha ambazo zilitakiwa zipelekwe karibu shilingi bilioni 37 hazikuweza kupelekwa. Ndiyo maana katika bajeti ya mwaka 2016/2017 tulitoa maelekezo mahususi kwa Wakurugenzi wote kama ndiyo miongoni mwa guideline kutengeneza bajeti ya Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, vilevile tuseme kwa kuwa tumeona
kuna changamoto kwa Halmashauri nyingine kutoa hizi fedha, ndiyo maana sasa hivi katika marekebisho yetu ya Sheria ya Serikali za Mitaa Sura ya 290, tumeweka kifungu ambacho kinatoa maelekezo ya kisheria sasa kwamba tunavyoipitisha hapa kwamba Halmashauri sasa haina hiyari isipokuwa ina lazima ya kutekeleza jambo hilo la kisheria.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, lengo kubwa ni kuwasaidia vijana
na akina mama na kuzikomesha Halmashauri zote zinazoona kwamba kupeleka ile fedha kama ni hisani, kumbe ni utaratibu. Lazima tunataka tuingize katika utaratibu wa kisheria ambapo nina imani sheria ile ikifika ha Bungeni, Wabunge wote tutashirikiana kwa pamoja kuipitisha kwa sababu ina maslahi mapana kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, katika jambo la pili la kuongeza asilimia 10 mpaka 15; nadhani ukiangalia mgao wa own source, asilimia kumi nadhani tuiweke hapo hapo, kwa sababu hata hizo asilimia kumi Waheshimiwa Wabunge wengine humu walikuwa wanalalamika. Jambo la kuzingatia ni kwamba tuhakikishe ile asilimia kumi inafika.
Mheshimiwa Spika, najua Mheshimiwa Mabula ni mpiganaji wa wananchi wake na mpiganaji wa Machinga pale Mwanza. Na mimi najua tukisimamia vizuri hapa kwa pamoja, jambo hili litawasaidia sana vijana na akina mama katika maeneo mbalimbali kujiingiza katika shughuli za ujasiriamali.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa inaonekana utaratibu wa usambazaji maji unakuwa mgumu sana na ziko mamlaka za maji kwa mfano mamlaka ya MWAUWASA pale jiji la Mwanza; Serikali ina mpango gani kuziwezesha mamlaka hizi ili ziweze kuwa zinatatua changamoto za maji zinakabiliana nazo kwenye maeneo zilizopo? Hii itakuwa msaada mkubwa sana kwa Halmashauri hizi lakini pia kwa wananchi wenyewe. Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawekeza, inaweka miundombinu ambayo ndio imekuwa chanzo cha maji. Kwa mfano tuna bomba la KASHWASA likishapita kwenye maeneo mamlaka Halmashauri na kwa sababu tunaendelea kutenga bajeti kila mwaka kile ndio chanzo chao cha maji. Kwa hiyo wanaweza wakatumia ile fedha; na tayari matoleo yanawekwa kila sehemu wanaweza wakaunganisha pale wakaendelea kusambaza maji ili wananchi wapate maji safi na salama.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibnu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa, Serikali inaendelea kufanya kazi nzuri kupitia miradi ya REA, lakini nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba yako maeneo mengine kwenye miji na majiji bado yanazo sura za vijiji; kwa mfano kwenye Jimbo la Nyamagana iko mitaa inafanana kabisa bado na maeneo ya vijijini kama Fumagila, Rwanima, Isebanda, Kakebe na maeneo mengine kama Nyakagwe. Ni lini Serikali itakuwa na utaratibu wa kuhakikisha na maeneo haya yanapatiwa umeme wa REA ili yaweze kupata sawasawa na mengine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mabula. Wakati ananiletea vijiji hivi tulipozungumza aliniletea vijiji vingine ambavyo vilikuwa kwenye hali ya kimtaa, lakini kisura vinaonekana kivijiji na tumeviingiza kwenye Mradi wa REA. Katika vijiji ambavyo ametaja hivi ambavyo inaonekana viko mjini, kwanza kabisa kuna mradi ambao unapeleka umeme kwenye miji yote nchi nzima na mradi huu unaitwa Urban Electrification na utapeleka katika miji na mitaa 314 kwa nchi nzima. Kwa hiyo, hata vijiji au mitaa ambayo iko mijini bado itapelekewa umeme kwa utaratibu huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tutakaa katika vijiji ambavyo amesema vya Fumagila pamoja na Kakene tuone hali itakavyokuwa. Nimwombe sana mara baada ya hapa tukutane na Mheshimiwa Mabula ili ikiwezekana vijiji hivi vipelekewe katika Mradi wa REA.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Natambua Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla wewe ni mtaalam na unafahamu kabisa kwamba katika prevention za malaria kuna primary prevention na kuna secondary prevention, nashukuru umeelezea vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri kiwanda cha viuadudu kama tutaweza kufanikiwa, dawa ikasambaa vya kutosha tuka-control wale vector kwenye hiyo level ya wale wadudu kutafuna larva, huoni kwamba tutakuwa tume-eradicate kabisa malaria na ni wajibu wa kila Hamashauri kununua zile dawa ili kusudi kile kiwanda kifufuke na tuweze kuzuia malaria? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Anachokisema ni sahihi kabisa, tukitumia hii teknolojia ya biolarvicides effectively tunaweza tuka-control malaria na hatimae kuidhibiti kabisa katika muda mfupi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza tukawa tupo constrained kibajeti na nadhani mkakati wetu kama nchi siyo kwa Wizara ya Afya kununua na kusambaza nchi nzima kwasababu majukumu yetu sisi kwakweli ni prevention, lakini pia tiba na mambo mengine na tuna support kwa kupitia pesa tunazozipata kutoka kwa wabia wa PMI pamoja na Global Fund.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana hili suala la biolarvicides tunawahamasisha Halmashauri zote nchini kwa kutumia mapato yao ya ndani washiriki kwa kutenga pesa kwa ajili ya kununua hizi biolarvicides na kuzisambaza na kuzitumia kwenye maeneo yao. Sisi kama Wizara ya Afya tumekwishakutengeneza mwongozo wa namna ya wao kutumia teknolojia hii ku-control hawa bio larvae kwa kutumia biolarvicides katika maeneo yao. Kwa hivyo, sisi kazi yetu ni hiyo tu, kutoa mwongozo na tumekwishatoa. Sasa Halamshauri zote including Halmashauri ya Maswa mnunue. Wenzenu wa Kondoa wameshaweka order, wenzenu wa Songwe, Namtumbo, Mbogwe na Geita pia wameweka order.
Waheshimiwa Wabunge, kwa hivyo Halmashauri nyingine na ninyi mhamasishe kwa kutumia mapato yenu ya ndani muweze kununua biolarvicides kwa ajili ya control ya malaria. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara ya lami inayotoka Nela kuelekea Kiwanja cha Ndege. Niulize swali dogo, kwa kiwango hicho hicho ni lini Serikali sasa itaanza mpango wa kuboresha barabara kwa kiwango cha njia nne kutoka mjini katikati kwa maana ya barabara ya Kenyatta kwenda Shinyanga kupitia Kata za Mkuyuni, Igogo, Mkolani, Nyegezi pamoja na Buhongwa ili na yenyewe iweze kufanana na yale mazingira yaliyopo? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Stanslaus Mabula na wananchi wa Mkoa wa Mwanza, ni kweli Jiji lile sasa lina hadhi kubwa na kwa kweli barabara zake nazo lazima tuhakikishe zinakuwa katika hadhi inayostahili Jiji lile. Nimepokea maombi yake, mimi nimechukulia hayo kama ni maombi, nitakwenda niyawasilishe kwa wataalam waanze kuangalia uwezekano wa kufikiria hilo ombi ambalo Mheshimiwa Stanslaus Mabula amelieleza.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kulichukulia kwa uzito suala hili na kutenga fedha hiyo. Imani yangu ni kwamba kifaa hiki kitakamilika na kitafika kwa wakati kwenye Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana. Sasa naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana inao ujenzi wa jengo kubwa lenye ghorofa mbili kwa ajili ya wodi ya wanaume. Nataka commitment ya Serikali, je, watakuwa tayari baada tu ya jengo hili kukamilika mapema mwakani mwezi wa tatu kutusaidia kwa ajili ya kupata vitanda na vifaa tiba vingine ili kutoa huduma iliyo bora kuendana na kasi ya Awamu ya Tano?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Wilaya ya Ilemela haina Hospitali ya Wilaya ya Ilemela lakini ni wilaya mpya na ujenzi wa hospitali yake umeanza kwa kusuasua sana. kwenye bajeti ya shilingi bilioni nne sasa hivi imeshapata milioni 500 peke yake. Nataka kujua je, Serikali itakuwa tayari kuhakikisha fedha zipatikane na kwenda kukamilisha ujenzi wa hospitali hii ya Wilaya kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Ilemela?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na upatikanaji wa vifaa ni dhahiri kwamba Serikali ina nia ya dhatikuhakikisha kwamba vifaa vinapatikana ili hospitali hiyo iweze kufanya kazi iliyotarajiwa na hivi sasa ninavyoongea tayari vitanda 25 vimeshapelekwa Nyamagana pamoja na magodoro yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba hospitali zote za Wilaya zinafanya kazi kwa kiwango cha hali ya juu kabisa. Tutakuwa tayari mara hospitali hii itakavyokuwa imekamilika tuhakikishe vifaa vyote vinapelekwa ili iweze kufanya kazi kwa ajili ya kusaidia Watanzania wa Nyamagana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza.
Pamoja na kazi nzuri na jitihada za Serikali katika kuhakikisha miji inapangwa na zoezi zima la urasimishaji wa makazi ikiwemo upimaji shirikishi, naomba tu kujua Serikali inayo mkakati gani kuhakikisha kwamba pamoja na upimaji huu unaofanyika sasa ile gharama ya premium inaonekana kuwa mzigo mkubwa kwa wananchi na matokeo yake wanashindwa kufikia hatua ya kupewa hati miliki, hivyo inawapelekea kubaki katika maeneo ambayo yamepimwa bila hati hizo.
Je, ni nini mkakati wa Serikali kuondoa kabisa hizi asilimia 2.5 zilizopunguzwa japo ilikuwa Saba ikapunguzwa, nini mkakati wa Serikali kuondoa hizi lakini kuongeza muda wa upimaji shirikishi ili wananchi wengi zaidi waweze kupimiwa kuhakikisha maeneo yao yote yamekamilika? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge hili Tukufu kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Mabula kwa sababu jana pia wakati anachangia Mpango wa Maendeleo amezungumzia suala la kuwajali sana wananchi na hasa katika suala zima la urasimishaji na mpango unaoendelea. Ametupa changamoto kama Wizara na sisi tunamshukuru na tumeona iko haja kweli ya kuangalia hawa wananchi ambao walitumia nguvu zao kujenga katika maeneo ambayo pengine hatukuwa makini katika kuwahi kupanga na wao wakavamia, basi tumesema kwa sababu hoja ni kupunguziwa mzigo, tumelichukua suala lake kuondoa premium na kabla ya mwisho wa mwezi huu tutakuwa tumempa jibu.
Je, ni lini zoezi hili litaendelea, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa maeneo yale ambayo yanarasimishwa na yamekwishaanza kwa mwaka huu tutavumilia mpaka mwisho wa mwaka huu wa fedha. Baada ya mwaka wa fedha tuna imani na mipango miji katika maeneo hayo, mipango kabambe katika maeneo hayo itakuwa tayari kwahiyo ukomo wao itakuwa ni mwisho wa mwaka wa fedha mwaka huu 2017/2018.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunafahamu kwamba biashara ya bodaboda imekuwa ni sehemu kubwa sana ya ajira kwa vijana, lakini naomba tu kufahamu ukichukulia Jimbo la Nyamagana peke yake zipo bodaboda takribani 6,700 lakini vijana hao wenye uwezo wa kujiajiri ni asilimia 30% peke yake, ni nini mkakati wa Serikali kutumia walau fedha za Mfuko wa Vijana na Fedha za Uwezeshaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu waweze kukopeshwa na fedha hizi watumie kama sehemu ya ajira yao ili kuepusha migogoro na waajiri wao na mikataba isiyokuwa rafiki kwao? Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mabula kwa kazi kubwa anayofanya kupambania vijana wa Nyamagana hasa vijana wamachinga na bodaboda amekuwa akifanya kazi hii vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ni nini katika hili? Ni kweli tunatambua kwamba asilimia kubwa ya vijana wangependa kumiliki pikipiki hizi ziwe mali yao lakini kikubwa ambacho kinawakwamisha ni upatikanaji wa mikopo ya masharti nafuu, lakini vilevile na fedha kuweza kununulia vifaa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali hatua ya kwanza ambayo tumekuwa tukiifanya ni kuhamisisha vikundi vya vijana kwanza wakae pamoja, wajisajili then baada ya pale sisi chini Ofisi ya Waziri Mkuu tunalo Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo linaratibu zaidi ya mifuko 19 ambayo inatoa mikopo na inatoa na ruzuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, rai yangu ni kuwaomba Waheshimiwa Wabunge ambao naamini kila Mbunge hapa kwake ana bodaboda ambao wana mahitaji haya kwanza kuwahamasisha kukaa katika vikundi, wajisajili na baadae tutawasaidia kuwaunganisha na mifuko mbalimbali na taasisi za kifedha ili waweze kupata mikopo ya aina mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko programu nyingi ambazo zinafanyika sasa hivi ambapo yule mwendesha bodaboda ana-deposit kiasi kidogo tu katika taasisi ya fedha na anakabidhiwa chombo chake na anakuwa anafanya kazi kurudisha taratibu taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote, najua ni kilio cha Wabunge wengi hakikisheni kwamba mnahamasisha uundaji wa vyama vya bodaboda na baadaye Ofisi ya Waziri Mkuu, sisi tutafanya kazi ya kuwasaidia kuratibu kwa maana mifuko gani inaweza kusaidia kuwezesha makundi haya.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na mikakati mizuri ya Serikali katika kusaidia wavuvi kuwawezesha kwa namna mbalimbali kwa mikopo na vifaa, kwa Kanda ya Ziwa na Ziwa Victoria kwa sasa hali imekuwa tofauti. Hivi tunavyozungumza wananchi wavuvi wa Kanda ya Ziwa, Mikoa ya Ziwa Victoria wanapata taabu kutokana na zana zao, nyavu, mitumbwi kuchomwa moto na faini zisizokuwa rafiki kwa maisha yao halisi na kazi wanayoifanya.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupambana na suala hili la uvuvi haramu kutokufika kwenye kiwango cha kumuumiza mvuvi ambaye tunataka tumsaidie afike mbali zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na mipango yake ya kuhakikisha kwamba inawawezesha wavuvi wadogo wadogo kote nchini ikiwemo wavuvi wa Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mabula amezungumzia juu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha tunapambana na uvuvi haramu. Ni kweli Serikali inaendelea na kazi ya kupambana na uvuvi haramu kwa kuzingatia Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2014 na Kanuni yake ya mwaka 2009 ambayo kwa pamoja na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 tumeendelea kuhakikisha kwamba tunafanya kazi kubwa ya kudhibiti uvuvi haramu kwa ajili ya ulinzi wa rasilimali za nchi yetu. Naomba niwahakikishie wavuvi wa Kanda ya Ziwa kwamba zoezi hili ni kwa manufaa ya Taifa letu na vizazi vyetu vya leo na vya miaka ijayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nyavu mbalimbali ambazo anazisema Mheshimiwa Mabula, tayari tumepata maombi ya kutoka kwa wadau mbalimbali ya kuhakikisha kwamba wanaagiza nyavu zilizo na viwango kwa mujibu wa sheria ili ziweze kusambazwa katika maduka ili wananchi wa kule Kanda ya Ziwa waweze kununua na kuweza kuendelea na shughuli zao za uvuvi bila ya kuvunja sheria.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Moja, kwa kuwa tunafahamu kwamba soko la kahawa bei yake imekuwa ikipanda na kushuka, Serikali haioni sasa umuhimu wa kuanzisha ruzuku maalum kwa ajili ya wakulima wa kahawa ili hata soko linapoporomka mkulima asipate maumivu sana kwenye upande wa mauzo? (Makofi)
Pili, tunaamini kwamba Vyama vyetu vya Ushirika vinayo nafasi kubwa sana ya kuhakikisha wakulima wan chi hii wananufaika. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha Vyama vya Ushirika vinaimarika na kuwa msaada kwa wakulima? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu ruzuku katika bei ya mazao. Naomba niseme kwamba bei ya ruzuku kwa upande wa Serikali, sisi tunatoa mazao yote katika standardization na vilevile tutaangalia siku zijazo kuhusu Vyama vya Ushirika kama vinafanya vizuri basi tutaoa hiyo standardization na ruzuku katika vyama na mazao yote yanayohusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake (b) ni kuhusu Vyama vya Ushirika. Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba tunafanya total transformation, vilevile operations katika Vyama vya Ushirika. Ni kweli vingi havifanyi vizuri na tumeangalia kabisa vingine hata havifanyiwi mahesabu lakini kama Serikali, kama nilivyosema tumefanya total transformation kuhakikisha kwamba Vyama vya Ushirika vitakuwa vinafanyiwa mahesabu, vitakuwa vinafanyiwa ukaguzi ili tuweze kupata bei nzuri na mazao bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wote naomba niwataarifu kwamba hivi majuzi mwezi uliopita Tume ya Vyama vya Ushirika imeundwa na tayari imeshaanza kazi. Nashukuru. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya namna ambavyo Serikali imejipanga katika kuhakikisha wafanyabiashara ndogo ndogo, machinga, mama lishe na wengine wanaofanana na biashara hizo wanatengenezewa mazingira mazuri ya kibiashara; lakini tungependa hasa kufahamu kwa mfano, habari za uwezeshaji wa mitaji inawezekana ikawa ni njia rahisi sana ya kuwa-contain machinga hawa pamoja na maeneo wanayopewa ili waweze kufanya biashara zao kwa uhakika kwa sababu tayari wanakuwa na kipato kizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu matatizo ya haya ya Dar es Salaam yanafanana sana na matatizo yaliopo Jiji la Mwanza, Wilayani Nyamagana, ambako pia kumekuwa na changamoto kubwa sana. Pamoja na maeneo mengi kupangwa, lakini Halmashauri zimefika sehemu zinakuwa zinabeba mzigo mzito kuona namna ya kuwawezesha hawa wafanyabiashara ndogo ndogo. Yako maeneo mengi yamepangwa, lakini uwezo wa wafanyabiashara hawa kwenda kule kutokana na miundombinu ambayo inakuwa siyo rafiki sana, maana Halmashauri inaweza ikatengeneza eneo vizuri, lakini miundombinu mingine ili iweze kufikika sawasawa inahitaji nguvu ya ziada.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali na Wizara inatuhakikishia kwamba iko tayari kushirikiana na Halmashauri hizi kuwatengenezea wafanyabiashara ndogo ndogo, machinga na mama lishe ili waweze kupata kipato na maeneo yao yawe sahihi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabla sijajibu swali hili, napenda kumpongeza kwanza Mheshimiwa Stanslaus Mabula na Mheshimiwa Angelina Mabula. Siku sita zilizopita, nilikuwa Mkoani Mwanza, lakini jukumu langu kubwa kule lilikuwa ni suala zima la kuwa cheque ya karibu shilingi milioni 900 wajariamali wa Mwanza ambao wamejiunga pamoja kwa ajili ya kuhakikisha kwamba katika makampuni yao walioyaanzisha yalikuwa takribani 24 waweze kufanya kazi vizuri. Mheshimiwa Mabula naomba niwapongeze sana, mmefanya kazi kubwa sana! (Makofi)
MheshimiwaNaibu Spika, sasa katika suala la mitaji, naomba niseme kwamba mitaji hii malengo yetu katika Serikali ya Awamu ya Tano itatoka katika maeneo tofauti. Eneo kubwa kwanza la mtaji katika hivi vikundi vidogo vidogo, tulisema hata katika bajeti yetu ya TAMISEMI kwamba mwaka huu tumeelekeza asilimia tano ya vijana na asilimia tano ya akina mama ambao takriban kuna karibuni shilingi bilioni 56.4. Imani yangu ni nini? Imani yangu ni kwamba, kama Halmashauri zetu zitahakikisha zile own source, ile ten percent ambayo tano kwa akina mama na tano kwa vijana, tukizielekeza vizuri shilingi bilioni 56.4, zitaleta mafanikio makubwa sana katika Halmashuri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili ni eneo moja la mtaji. Sambamba na hilo katika Ofisi ya Waziri Mkuu, kuna suala zima la uwezeshaji. Eneo hili nalo litaweza kufanya kazi kubwa kuwawezesha vijana waweze kuwa na skills za kutosha katika suala zima la uwekezaji katika maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, Serikali imejipanga na juzi tulikuwa na Benki moja inaitwa Covenant Bank, ambayo iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali. Lengo kubwa ni kukuza mitaji kwa watu wa eneo la chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikiri kwamba, sasa tunahakikisha kwamba hii mitaji sasa, wananchi wapate fursa, lakini sambamba na kupata elimu ilimradi waweze kupata mitaji kuweka uchumi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo la pili, kwa suala zima la kuboresha miundombinu. Ni kweli, maeneo mengine miundombinu inakuwa ni changamoto kubwa.
Kwa hili, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wote, lakini nawapongeza wale ambao tayari wameshajenga masoko kuhakikisha kwamba wanawa-accommodate wafanyabiashara mbalimbali. Sambamba na hilo, tubainishe; inawezekana kweli maeneo mengine masoko yapo, lakini hayapitiki vizuri, barabara siyo rafiki na hata maeneo ya mama ntilie hayajakuwa sawa sawa. Basi naomba tuibue mambo haya katika Halmashauri zetu, tushirikiane kwa pamoja, bajeti zetu zinazokuja tuweke kipaumbele jinsi gani tutafanya hawa akina mama ntilie, wauza mitumba na watu wa kada mbalimbali waweze kupata fursa kwa ajili ya uchumi wa nchi yao na maendeleo yao binafsi.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, lakini pamoja na maswali mawili ya nyongeza, nikiri kwamba sijaridhishwa kabisa na majibu ya Mheshimiwa Waziri na wala sikubaliani nayo kwa sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu, Nyamagana ndiyo kitovu cha Mkoa wa Mwanza na ni mji unaokua kwa kasi sana, barabara hii haijasemwa leo, imesemwa sana, sasa tukisema mwaka 2017/2018 ndiyo tuanze upembuzi yakinifu tunakuwa hatuwatendei haki wananchi wa Jimbo la Nyamagana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimwombe Naibu Waziri na akumbuke kwamba iko sasa hivi mikakati ya kuboresha miji ukiwemo Mji wa Mwanza, barabara hii itakuwa muhimu sana kwa mkakati wa Serikali wa ukusanyaji mapato, ni lini watakuwa tayari kutumia fedha za dharura kuhakikisha hii shughuli ya kufanya upembuzi yakinifu inafanyika kwa mwaka huu na mwaka ujao barabara hii ianze kujengwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa sababu zilezile kwamba Mji wa Mwanza ni mji unaokua kwa kasi na mara nyingi tumekuwa tukitumia fedha nyingi wakati wa dharura, tunaposubiri mvua nyingi zinanyesha na kuharibu barabara. Je, ni lini sasa fedha hizi za dharura zitatumika kuimarisha barabara ikiwemo barabara ya kutoka Mkuyuni kwenda Nyangurugulu kutokea Mahina, Buzuruga, lakini ya kutoka Mkolani kwenda Saint Augustine University kupitia Luchelele na Nyegezi Fisheries?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimjulishe Mheshimiwa afanye rejea katika maeneo ambayo tunafanya mikakati kama Serikali kuboresha barabara zetu likiwepo na Jiji la Mwanza. Kupitia mpango wetu wa strategic cities Mwanza ni eneo ambalo tunajenga miundombinu hiyo ikiwa sambamba na Shinyanga, Arusha, Iringa, Mbeya na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, najua kwamba barabara hii ni kweli haijakamilika, lakini nimesema kila jambo lina mpango na Mheshimiwa Mabula, anafahamu Mheshimiwa Rais alivyokwenda pale alisema siyo hizo barabara za eneo la Mwanza isipokuwa hata kujenga daraja katika Ziwa Victoria, nalo linafanyika katika Jiji la Mwanza, mpango mkakati huo unapoenda maana yake kutakuwa na uboreshaji wa hizo barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba najua, amesema ni muda mrefu, lakini anakumbuka huko nyuma alikotoka wapi na hivi sasa yeye yuko wapi. Naamini uwepo wake sasa utasukuma mambo haya yaende vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba Serikali imejipanga ile ring road itatengenezwa. Kwa mujibu wa Serikali ilivyojipanga ring road tutatengeneza na isitoshe na yeye anafahamu kule site kuna watu sasa hivi wanaboresha barabara za Jiji la Mwanza, naomba niwahakikishie watu wa Mwanza, Mheshimiwa Rais alivyotoa kwamba kujenga barabara mpaka kupeleka airport baada ya kuvunja sherehe maana yake hiyo ni commitment ya Serikali ili baadaye Watanzania wote wanufaike, amesema kwamba tuelekeze eneo hili kwa sababu ni eneo la mkakati, ni azma ya Serikali kuboresha miundombinu hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba nimwambie kwamba katika kipindi cha sasa Serikali ilivyojipanga tutaboresha barabara za aina mbalimbali na katika hilo la kwamba kwa kutumia fedha za dharura tutafanya nini. Juzijuzi nilikuwa katika Jimbo la Mheshimiwa Mabula kule Ilemela, kuna baadhi ya barabara tumefanyia ukarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia afuate rejea yangu ya kipindi kilichopita, kwamba tutafanya kila liwezekanalo barabara zilizoharibika kwa kadri rasilimali fedha itakavyopatikana tutaendelea kuiboresha. Kwa hiyo, nimwambie mtani wangu, asihofu, awaambie watu wa Mwanza kwamba wamempata jembe lakini Serikali itamsaidia kuboresha Jiji la Mwanza. (Makofi)
MHE: STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa matatizo ya vyumba vya upasuaji yako pia kwenye Wilaya ya Nyamagana hasa, kwenye Hospitali yetu ya Sekou Toure ambayo Miundombinu yake ya theatre iliyopo sasa iko mbali kutoka kwenye Jengo ambalo ni labour ward. Pale kwenye jengo la labour ward tayari kuna jengo ambalo lilishaandaliwa lakini halina vifaa kabisa. Ni lini Serikali itakuwa tayari kupeleka vifaa vya upasuaji kwenye jengo hilo ambalo liko karibu sana na chumba wanachojifungulia akinamama, tukiamini kupatikana kwa vifaa hivi kutasaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto yanajitokeza hasa wakati wa kujifungua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, huyu Mbunge anayeuliza hivi kwanza tuelewe kwamba yeye ni Msukuma, kwa hiyo lugha yake lazima tuielewe vizuri. Najua kwamba Mbunge huyu yuko makini katika Jimbo la Nyamagana kwa sababu kazi aliyoifanya akiwa kama Mwenyekiti, Meya wa Jiji lile tunaitambua wazi. Kwa hiyo, nimthibitishie, hata maamuzi waliyofanya kufuma mifumo ya electronic mpaka sasa hivi wanakusanya kutoka 150,000 mpaka milioni tatu kwa siku, ni mchakato mkubwa sana ambao Mbunge huyu ameufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama Serikali tunasema kwamba, kwanza mimi mwenyewe nilimwambia nilipoongea naye hapo awali kwamba nitakwenda Mwanza, tutatembelea Sekou Toure, tutapanga kwa pamoja jinsi gani tutafanya ili vifaa tiba vipatikane. Vitapatikana wapi, tutajua katika mpango wa pamoja tutakapokaa pamoja, lakini nitakwenda kule Mwanza kubainisha kwanza mapato yao ya ndani wanayoyapata, lakini pia kuangalia fursa zipi nyingine tutakazozitumia ili wananchi wa Mwanza waweze kupata huduma bora.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kwa kuwa Serikali inakiri kuwepo na tatizo kubwa la upungufu wa nyumba za makazi ya askari polisi na vyombo vingine ambavyo viko ndani ya Jeshi la Mambo ya Ndani. Serikali haioni sasa mipango na mikakati iliyonayo bado haiwezi kuwa ni kigezo cha kukamilisha tatizo hili kubwa tulilonalo nchini?
Swali langu la pili, pamoja na matatizo haya ziko nyumba ambazo zimeshaanza kujengwa takribani miaka mitano leo, zikiwemo nyumba za Mabatini Barracks katika Jimbo la Nyamagana na maeneo mengine kama Musoma na Mikoa mingine yenye matatizo kama haya.
Je, ni lini Serikali itahakikisha nyumba hizi ambazo zikikamilika kwa wakati kwanza tunaokoa upotevu wa fedha nyingi, lakini inasaidia watu wetu wanaohangaika kutafuta makazi kukaa kwenye makazi yaliyo bora na kuwafanya wafanye kazi yao kwa uaminifu na uhakika zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianzia na mradi wa nyumba ambazo zipo katika Jimbo lake nikiri kwamba nyumba zile zimefika katika hatua za mwisho kukamilika. Mimi na yeye tuliwahi kufanya ziara kutembelea, tuliona kwamba kuna umuhimu wa nyumba zile kukamilika kwa haraka ili kuweza kutatua tatizo la makazi katika eneo la Nyamagana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo Nyamagana tu, tuna nyumba maeneo mbalimbali nchini ambazo zipo katika hatua za kukamilika, ikiwemo Musoma Mjini, Kagera, Mtambaswala huku Mtwara, Ludewa na kadhalika. Kwa hiyo, kwa kutambua kwamba kuna haja ya kumaliza nyumba hizi ambazo zimefika katika hatua nzuri katika bajeti ya mwaka huu ya maendeleo ambayo tumetenga takribani zaidi ya shilingi bilioni 5.2 malengo ni kukamilisha miradi hii ambayo imefikia katika hatua nzuri na za mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatarajia katika kipindi cha mwaka huu wa fedha tutamaliza project ile ya Nyamagana (Mabatini) pamoja na nyingine ambazo nimezitaja. Kwa hiyo, ni miongoni mwa mikakati ya Serikali ya kutatua matatizo ya nyumba za askari nchini.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru tu Serikali kwa huu mradi wa World Bank wa Euro milioni 54 kwa niaba ya Jimbo la Nyamagana pamoja na Ilemela. Lakini niseme tu kwa hali ya kawaida kama wananchi wa Jimbo la Nyamagana wangekuwa wanapata maji kwa asilimia 90 sidhani kama Mbunge wao ningekuwa na sababu ya kusimama hapa na kuomba maji. Niseme tu ukweli ni kwamba inawezekana mtandao wa maji umesambazwa kwa kiasi kikubwa lakini upatikanaji wa maji sio sawa na takwimu zinavyosomwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; zipo Kata za Buhongwa, Lwanima, Kishiri, Igoma na Nyegezi ni lini Serikali itakuwa tayari pamoja na huu mradi wa Euro milioni 54 kuangalia uwezekano wa kuongeza fedha zingine nyingi zaidi ili wananchi kwenye maeneo haya ya Buhongwa na maeneo ya Lwanima na Kata zingine nilizotaja waweze kupata maji kwa uhakika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pale kwenye
Jimbo la Ilemela umekuwepo mradi wa Vijiji kumi toka mwaka 2010 mpaka hivi tunavyozungumza leo ni Kijiji kimoja peke yake cha Kayenze ndio kimepata maji.
Ni lini Serikali itahakikisha Vijiji vya Nyamadoke, Kahama, Kabangaja, Igogwe, Igombe, Kabusungu na Nyafula vinapata maji haya kwa wakati kama ambavyo ilikuwa imekusudiwa? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kumpokea Mheshimiwa Mbunge kwa sababu kila wakati anakuja ofisini kuhusu Mradi wa Maji wa Nyamagana, ndiyo maana Wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na juhudi za wafanyakazi wote na Serikali tumehakikisha kwamba tumepata hizi Euro milioni 54 tukiwa pamoja na Mheshimiwa Mbunge. Maana yake kila wakati alikuwa anakuja kuzungumza kuhusu wananchi wake na amekuwa anasema inakuwa ni aibu kwa sababu Ziwa Victoria liko pale na watu hawana maji, ndiyo maana amesaidia katika kulisukuma hili ili tuweze kupata mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amezungumzia baadhi ya Kata. Mradi huu utakapokuwa umekamilika zipo kata ambazo zitapata huduma ya maji, Kata hizi ni pamoja na Kishiri, Buhongwa, Bugarika, Nyegezi, Lwanima pamoja na Igoma. Aidha, vitongoji ambavyo vinazunguka katika hizo kata tutahakikisha kwamba zimepata maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema kwamba tunakarabati miundombinu iliyopo, ikiwa ni pamoja na mabomba yaliyochakaa, yakichakaa maana yake kupeleka huduma ya maji kwa wananchi inakuwa kidogo kuna shida tutahakikisha sasa na vijiji vingine vyote vilivyobaki vinapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia amehoji kuhusu tamko la asilimia 90. Hesabu ya asilimia 90 tunaihesabu kwa kuchukua population ya watu waliopo katika lile eneo na kuangalia ni watu wangapi wanaopata maji, hatu-cross over kwenda kwenye vijiji vyote, hapana! Tunaangalia una watu wangapi katika Kata ya Nyamagana, je, ni wangapi ambao wanapata maji ndiyo tunapiga mahesabu kuhakikisha kwamba sasa hiyo asilimia tunaipata. Kwa hiyo, kunaweza kukawa na Kata lakini kwa sababu zina watu wachache ukakuta kwamba asilimia hii ni kubwa kumbe kuna Kata ambazo bado hazijapata maji. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo tumeendelea kushirikiana kufuatilia suala la wananchi wa Nyamagana kupata maji, tuendelee kuwasiliana ili kuona ili mradi utakapokamilika kusiwe na eneo litakalobaki bila kupata maji. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba niulize maswli mawili madogo ya nyongeza na moja ni kwa sababu Serikali bado yako maeneo kwenye Jiji la Mwanza na hasa Wilaya ya Nyamagana kama Kata za Kishiri, Lwanima na Buhongwa bado hayajapata umeme wa uhakika.
Ni lini sasa Serikali kupitia Shirika la TANESCO itahakikisha maeneo hayo yanapata umeme wa kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Mji wa Mwanza bado unayo maeneo yenye taswira ya vijiji ikiwemo Jimbo la Ilemela. Ni nini mpango wa Serikali kupitisha umeme kwenye maeneo hayo hasa maeneo ambayo tayari yamebaki sambamba na Kata za Sangabuye, Bugogwa, Kahama na Shibula ili kuhakisha Mwanza yote inapata umeme wa uhakika? Ninakushukuru sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya swali la msingi, nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Mabula pia katika kufuatilia maeneo ya vijiji hivi 18.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa tulitenga fedha shilingi bilioni 8.7 kwa ajili ya kupeleka vijji tisa katika jimbo la Mheshimiwa Mbunge vipya, kupitia mradi wa TANESCO. Na nimwambie tu Mheshimiwa Mabula nimpongeze sana hivi sasa TANESCO wanapeleka umeme katika kijiji cha Lwanima na wakimaliza Lwanima wanakwenda Kanema, pamoja na Bukaga, Nyakwagwe watapeleka. Pia watapeleka mpaka Kigogo pamoja Isebanda na wakimaliza Isebanda Mheshimiwa wanakwenda pia kwenye kijiji cha Kigodo pamoja Nyangwi pamoja na mtaa wako wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimpe uhakika Mheshimiwa Mabula kwamba hadi kufika mwezi Juni ambapo mradi unakamilika wananchi wote wa vijiji vyote vinane, umbali wa kilometa 9.2 utakuwa umefikishiwa umeme na Mwanza itakuwa inapata umeme wa uhakikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swala lake la pili, ni kweli yako maeneo ambayo yako mjini na visiwani na vijiji. Tuna mradi wa (Peri-urban) ambao Jiji la Mwanza katika maeneo ya Kishiri, Buhongwa Pamoja na Kata za Lwanima pia ziko kwenye mpango huo. Kwa hiyo, watapelekewa kupitia mradi wa (Peri-urban) lakini pamoja na mradi wa Densification utakaoanza Julai mwaka huu.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nitumie nafasi hii kwa ruhusa yako niwape pole sana wananchi wa Jimbo la Nyamagana kwa mafuriko makubwa sana kwa siku ya jana ambayo yalisababisha shughuli za kijamii kusimama takribani masaa saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu dogo, Jiji la Mwanza ni moja kati ya majiji yanayokuwa kwa kasi sana Barani Afrika ikiwemo Nyamagana. Sasa nataka kujua barabara kubwa ya Kenyatta ambayo inatoka Mwanza Zero kupita Kata za Mkuyuni, Butimba, Nyegezi kwenda mpaka Buhongwa ikiwemo na Mkolani ni barabara finyu sana kwa sasa. Serikali inao mkakati gani kuhakikisha barabara hii inapanuliwa angalau kwa njia nne ili ionekane taswira halisi ya Jiji la Mwanza na ukuaji wake kwa kasi? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa ujumla kwamba Jiji la Mwanza linakua kwa kasi lakini shughuli za maendeleo ziko nyingi, nasi kama Serikali tunatazama ili kwamba miundombinu hii tunayoweza kurekebisha iende sambamba na kasi ya ukuaji wa shughuli za maendeleo na ongezeko la watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mabula na tumeshazungumza kwamba nitakwenda kutembelea Mwanza, tutaitazama kwa sababu hii anayoizungumza ya Kenyatta kwenda Buhongwa ikipitia maeneo ya Makuyuni - Mkolani kwenda Nyegezi kama alivyozungumza, ni muhimu. Ni nia yetu kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu ili iende sambamba na ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa ajira ambazo ni rasmi zimekuwa na ukakasi mkubwa kulingana na idadi kubwa ya vijana na Serikali ilishaanzisha mfumo wa kuwasaidia vijana kupitia ajira zisizo rasmi kwa vijana ambao tayari wana ujuzi, nini sasa mkakati wa Serikali kuwarasimisha vijana hawa ili wapate mafunzo na vyeti wanavyoendelea vitakavyowasaidia, hasa wale ambao ni mafundi gereji, mafundi uwashi na mafundi seremala walioko Nyamagana na nchi nzima kwa ujumla? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya kuwatetea vijana hasa vijana wa Jimbo lake la Nyamagana. Pia nimwondoe hofu kwamba chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu tuna mpango wa miaka mitano wa ukuzaji ujuzi kwa vijana ambao lengo lake ni kuwafikia vijana takribani milioni nne na laki nne ifikapo mwaka 2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huo moja ya component iliyopo tunaita ni RPL - Recognition of Prior Learning. Huu ni mfumo wa urasimishaji ujuzi kwa vijana ambao wana ujuzi lakini hawajapitia mfumo rasmi wa mafunzo. Hivi sasa tunao takribani ya vijana 22,000 ambao wameomba kupitia ofisi ya Waziri Mkuu kufanya mafunzo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza hivi sasa vijana 3,448 nchi nzima wamenufaika na nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka huu wa fedha tunaendelea pia kuwachukua vijana hawa kwa ajili ya kuwarasimisha katika ujuzi walionao na kuwapa cheti bila kupitia katika mafunzo maalum ya vyuo vya ufundi stadi. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda tu sasa kufahamu na niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kwa kuwa vifaa hivi vya uchunguzi ni muhimu sana kwenye Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa na Kanda, Serikali imeonekana kuwa inachukua muda mrefu sana bila kutekeleza ahadi za kupeleka vifaa hivi kwa wakati na izingatiwa kwamba suala la afya ni muhimu sana. Mheshimiwa Waziri atuambie kwa kuwa wanategemea mradi wa ORIO ambao muda siyo mrefu watapata vifaa hivyo, ni lini Hospitali ya Bugando itapata kipata kifaa cha MRI kwa sababu ya wananchi wengi wa Kanda ya Ziwa kupata huduma? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunayo hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure, vifaa hivi kama CT Scan kwenye hospitali ya Mkoa ni muhimu sana. Ni lini sasa Wizara kwa mpango ule watahakikisha walau kifaa kimoja, CT Scan kwenye Hosptali ya Rufaa ya Sekou Toure kinapatikana na kusaidia wananchi wengi zaidi? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa ufuatiliaji wa karibu katika masuala ya afya katika Mkoa nzima wa Mwanza vilevile katika Jimbo lake la Nyamagana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mabula ameuliza ni lini mashine ya MRI itapatikana. Kama nilivyojibu katika jibu la msingi nilisema kwamba Serikali inaendelea na maandalizi na tuko katika majadiliano na Serikali ya Netherlands kupitia mradi wa ORIO na awamu ya kwanza ya mashine ya kwanza ya X-Ray, vilevile na upatikanaji wa CT Scan na MRI kwa baadhi ya hospitali ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Bugando tunatarajia kabla ya mwisho wa mwaka huu itaweza kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza ni lini sasa tutapeleka mashine ya CT Scan ama MRI katika Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure. Kulingana na mwongozo wetu tulio nao sasa huduma ya CT Scan na MRI zinapatikana kuanzia ngazi ya Rufaa ya Kanda, lakini tumeona kwamba mahitaji yamezidi kuongezeka, idadi ya watu imezidi kuongezeka na mfumo wa uendeshaji hospitali za rufaa umebadilika, kwa hiyo, sasa hivi Wizara inafanya mapitio ya miongozo yake ikiwa ni pamoja na kuangalia mahitaji ya huduma kama ya CT Scan katika ngazi ya Rufaa za Mikoa. Tutakapokamilisha taratibu hizo basi huduma hizi CT Scan tutazishusha katika ngazi ya Rufaa ya Mkoa.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru na ninamshukuru Naibu Waziri kwa majibu.
Mheshimiwa Spika, Jiji la Mwanza ni moja kati ya majiji yanayokuwa kwa kasi sana hapa nchini na hasa kwa ongezeko la watu na kasi ya ongezeko la watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi inaendelea kuwa kubwa sana.
Sasa ningependa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, kasi ya idadi ya uundaji wa kamati hizi za ulinzi na usalama; kamati 11 kwenye mitaa11 peke yake kati ya mtaa 175, anadhani kasi hii inatosheleza kukabiliana na changamoto hii ambayo ipo katika Jiji la Mwanza na maeneo mengine?
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, tunafahamu kwamba pamoja na tafiti nyingi ambazo zimefanywa moja ya jambo kubwa ni hao wazazi kuwatumikisha watoto walioko kwenye mazingira yanayoonekana ni hatarishi. Nini sasa mkakati wa Serikali madhubuti kwa ajili ya wazazi wanaowatumikisha watoto na mifano ipo. Ukienda pale Dar es Salaam ukiwa unapita barabara ya Ali Hassan Mwinyi, barabara ya Nyerere pale Mwanza na Kenyatta wako wazazi wana kaa kando ya barabara wanatuma watoto kwenda kuomba magari yanaposimama na watoto wanapopewa wanapeleka kwa wazazi wao. Nini mkakati wa Serikali kukomesha masuala yote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kweli kasi hii ya uanzishaji wa kamati za ulinzi wa wanawake na watoto bado inasuasua.
Naomba nitumie fursa hii kuwahimiza na kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kwamba wanatekeleza agizo la Serikali la kuanzisha kamati za ulinzi kwa wanawake na watoto ambayo iko katika mpango wa mkakati wetu wa kitaifa wa kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. Tungependa kuona kabla ya mwaka huu kuisha kamati hizi zimeanzishwa katika ngazi zote kuanzia ngazi ya taifa mpaka katika ngazi ya vitongoji.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mabula lilikuwa linauliza kuhusiana na wazazi kuwatumikisha watoto, kwa maana ya omba omba. Watoto wana haki zao za msingi ambazo zimebainishwa kisheria katika sheria hii ya mtoto ya mwaka 2009. Baadhi ya haki hizi za mtoto ni pamoja na haki ya kutunzwa, haki ya kulindwa, na haki ya kutokutumikishwa kazi nzito.
Sasa Mheshimiwa Mbunge ametuuliza nini sisi kama Serikali tunafanya. Nimeeleza kwamba tumetengeneza mpango mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na moja ya mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba ukatili huu na kutumikishwa huku kwa watoto kunadhibitiwa kupitia mpango mkakati huu.
Vilevile kwa kupitia hizi kamati za ulinzi wa wanawake na watoto tunatarajia kwamba zikiweza kufanya kazi vizuri hii ni moja ya changamoto ambayo inaweza ikatatuliwa kwa kupitia kamati hizi.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa swali la nyongeza.
Naomba tu kuuliza; kwa kuwa uzazi wa mpango ni moja ya mkakati madhubuti kabisa wa kuzuia vifo vya mama na watoto na nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwamba kwa mpango ujao Mkoa wa Mwanza ni moja ya Mikoa iliyowekewa mikakati, lakini Wilaya ya Nyamagana ni moja ya Wilaya zinazoongoza kwa vifo hivi vya Mama na mototo kwenye Mkoa wa Mwanza. Ni nini sasa mkakati madhubuti kwa ajili ya Nyamagana ili kuhakikisha vifo vya Mama na mototo vinakwisha kabisa?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Mabula na hasa ukiona wanaume wanazungumzia suala la uzazi wa mpango maana yake tunatoka. Tutaongeza idadi ya wanawake wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango lakini nampongeza kwa kazi nzuri Nyamagana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza tusipochukua hatua madhubuti, mwaka 2030 Tanzania itakuwa na watu milioni 70 na haiendani na ukuaji wa uchumi na itakapofika 2050 tutakuwa na Watanzania milioni 100 ambapo hatuoni pia ikilingana na ongezeko la uchumi. Kwa hiyo, tumeamua kuja na mkakati wa kuhimiza wanawake hasa walio kwenye ndoa, naomba niliseme hili, wanawake walio kwenye ndoa hutumia huduma za uzazi wa mpango na asilimia 39 ya wanawake walio kwenye ndoa wameeleza kwamba wanapenda kuchelewa kupata watoto kwa kipindi cha miaka miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nirudie, kwa Mheshimiwa Mabula tunaanzisha vituo vya kutoa huduma za uzazi wa mpango katika miji kwa sababu suala la uzazi wa mpango siyo ugonjwa. Wanawake wa Dar es Salaam, wanawake wa Nyamagana hawataki kwenda hospitali kupanga foleni kwa ajili ya kupata huduma. Kwa hiyo, tutawafuata akina mama ambao wanauza mboga mboga…
…tutakuwa na mobile clinic. Kwa hiyo, mama akitaka huduma anapata palebadala ya kupanga foleni masaa mawili, masaa matatu na tunawashukuru sana wadau wetu wa maendeleo ambao wametusaidia kuhakikisha huduma hizi za uzazi wa mpango Mijini pamoja na Nyamagana zinapatikana kwa urahisi.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Nataka kuuliza jambo moja kwamba majengo haya ya Serikali yanachukua muda mrefu kukamilika na matokeo yake yanagharimu fedha nyingi zaidi ambapo yangejengwa na kukamilika kwa wakati yangesaidia sana matumizi ya fedha za Serikali kutumika kwa uchache.
Mheshimiwa Spika, sasa pamoja na Serikali na jitihada zake kubwa, ni miaka 10 leo. Mwaka ujao wa fedha Mheshimiwa Waziri anatuahidi kwamba jengo hili litakamilika. Naomba sana tufanye jitihada hiyo ili fedha hizi ziletwe na jengo hili likamilike. Hii itachangia hata ukuaji wa uchumi kwenye lile eneo ambalo Jengo la Mkuu wa Wilaya limejengwa. Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mabula na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, pamoja na mikoa yote na wilaya zote, tumepitisha hapa Bungeni shilingi bilioni 53 kwa ajili ya kujenga majengo ya Halmashauri na tumepitisha hapa shilingi bilioni 80 kwa ajili ya bajeti za maendeleo ya mikoa. Hizi fedha nataka niwahakikishie kwamba Serikali inaendelea kuwa stable kabisa katika masuala ya ukusanyaji wa fedha, fedha zitapelekwa, wala asiwe na wasiwasi wowote.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ukweli ni kwamba hospitali hii ya rufaa sio tu inahudumia wananchi wa Mkoa wa Mwanza, bali na wananchi wengi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu ya umuhimu huo, hospitali ya Sekou Toure ambayo kwa kweli inatoa huduma kubwa na nzuri kwa sasa, ni nini, mkakati wa Serikali kuwatumia hao hao Wakala wa Majengo (TBA) wakati wanaendelea na mikataba ikiwezekana kwa sababu wao ni Wakala wa Serikali, wawe wanatumia fedha zao za ndani kuhakikisha miradi waliyopewa inakamilika na wao wanabaki kudaiana na Serikali ili kutoa huduma kwa wananchi kwa haraka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, TBA pesa ambazo wanazipata zinatokana na project mbalimbali, sasa nadhani sio busara sana ukasema watumie pesa walizonazo ambazo zitakuwa zimetokana na project fulani ambayo labda haijajengwa, waanze kutumia wakisubiri kwamba Serikali ikipeleka pesa ndio ziende sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa kadri makusanyo yanavyokwenda na yeye mwenyewe ni shuhuda, kasi yetu katika ujenzi wa vituo vya afya na hospitali za Wilaya pamoja na hospitali za rufaa hautiliwi mashaka. Naomba avute subira haya mambo yatakwenda vizuri kabisa.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada kubwa za Serikali kupitia Wizara yake ya TAMISEMI kuhakikisha inaboresha vituo vingi vya afya kikiwemo na Kituo cha Afya hiki cha Ukerewe, kama Mheshimiwa Waziri anavyofahamu kwamba kumekuwa na changamoto kubwa ya watumishi, vifaa tiba ambavyo kwa kweli vingesaidia zaidi ufanisi na ubora wa utumishi kwenye hospitali hii. Je, ni lini hasa Serikali itahakikisha suala hili linafanyiwa kazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali dogo la pili, kwa sababu matatizo ya Ukerewe kwa namna fulani yanafafana sana matatizo yaliyoko kwenye hospitali ya Wilaya ya Nyamagana. Ni nini sasa mpango wa Serikali kwa sababu mara kadhaa hospitali ya Wilaya ya Nyamagana imeshaomba kupatiwa vifaa kama ultra sound na ni lini sasa Serikali inaweza kuhakikisha hospitali ya Nyamagana inapata ultra sound pamoja na X-Ray machine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, anauliza kuhusiana na Kituo cha Afya Nakutunguru kukamilika na hasa kuwepo na vifaa vya kutolea huduma, pamoja na suala zima la watumishi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba vituo vya afya vyote vinavyokamilika ni pamoja na kuwa na vifaa vya kufanyia kazi ikiwepo X-Ray, ultra sound hayo yote ni muhimu ili kituo cha afya kiweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili anaulizia hospitali yake ya Wilaya. Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mabula amekuwa akipigania hospitali hii kwa muda mrefu kuhakikisha kwamba inatoa huduma kwa kadri inavyokusudiwa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba hospitali zote za Wilaya zinakuwa na vifaa vya kutosha ili viweze kutoa huduma inayotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni azma yetu kuhakikisha kwamba hospitali ya Nyamagana ni miongoni mwa hospitali za Wilaya ambazo zitakua kwa viwango vinavyotakiwa ikiwa ni pamoja na kuwa vifaa vyote vinavyotosheleza.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimwia Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri. Kwa sababu makatazo yaliyokuwa yamefanyika Ziwa Tanzanyika yamemefanyika pia Ziwa Victoria hasa kwa kuzuia matumizi ya taa za solar kwenye shughuli ya uvuvi wa dagaa. Kwa sababu juzi Mheshimiwa Waziri niliona anatoa tamko kule Ferry, ni nini sasa kauli thabiti kwa wavuvi wa Ziwa Victoria ili waendee kutumia taa za solar mpaka pale utaratibu utakapo kamili?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimwa Mabula kwa swali lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba baada ya kutafakari sana malalamiko ya wavuvi wetu katika maziwa mbalimbali juu ya leseni nyingi, matumizi ya jenereta pamoja na matumizi ya taa za solar; na kwa mamlaka niliyonayo nikaamua kwamba sasa matumizi ya solar na jenereta yaruhusiwe na wananchi wasikamatwe kwa kutokuwa na leseni hivi sasa wakati tunatatua tatizo hili la kuwa na leseni nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachotaka kuwambia wavuvi wote na Mheshimiwa Mbunge ni kwamba nimeruhusu rasmi matumizi ya taa za solar na jenereta mpaka tarehe 1 Julai. Hata hivyo Serikali haikusudii kuzuia wananchi kutumia solar isipokuwa ni kuwa-guide kwamba ni solar zenye watts kiasi gani ambazo zitahitajika kutumika, hapo ndio tutatoa hizo guidelines tarehe 1 Julai.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Wizara wanakiri kwamba kumekuwa na changamoto kutokana na maboma mengi ambavyo yamekuwa katika Halmashauri zetu, lakini pamoja na mkakati wao, walipofanya utafiti waligundua kwamba Halmashauri hazina uwezo wa kukamilisha maboma yote yanayojengwa kule kwenye Majimbo yetu; na ni ukweli usiopingika kwamba Mfuko wa Pamoja bado hauwezi kutosheleza:-

Sasa ni nini mkakati thabiti hasa wa Serikali kuhakikisha aidha kuwe na mkakati wa kusema kiasi cha maboma kinachopaswa kujengwa kwenye kila Halmashauri ili wao waweze kumalizia au tuendelee na kusubiri ujenzi wa Vituo vya Afya na Zahanati kutoka Mfuko wa Pamoja?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimetoa majibu kwenye majibu yangu ya msingi; na Mheshimiwa Mbunge naye atakubaliana name kuhusu azma njema ya Serikali ambayo anaiona jinsi ambavyo tunapambana kuhakikisha kwamba tunapeleka huduma kwa maana ya kujenga Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya na Zahanati. Ndiyo maana katika majibu yangu ya msingi nimejibu kwamba ni vizuri tukafungua avenue pale ambapo Halmashauri zile ambazo ambazo zina uwezo, lakini pia kwa kushirikisha wananchi na wadau wengine tuendelee kujenga kwa kushirikiana na Serikali.

Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunasogeza huduma za matibabu karibu kabisa na wananchi, lakini pia vipaumbele ni vingi. Kwa hiyo, ni vizuri tukashirikiana pale bajeti inaporuhusu, Serikali inapeleka lakini pia na Halmashauri na wadau wengine ni vizuri wakashiriki katika suala hili muhimu sana kwa wananchi wetu.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nami nianze tu kwanza kwa kuishukuru Wizara kwa kuendelea na jitihada za kuboresha na kuimarisha Uwanja wa Nyamagana. Sasa kwa sababu tunaamini kwamba ili tuwe na vijana wengi ambao wanacheza mpira vizuri ni lazima tuwe na viwanja vingi kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wanasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Jiji la Mwanza tuna Milongo Sports Center ina viwanja takribani vitano kwa wakati mmoja. Ningependa sasa kumwomba Mheshimiwa Waziri apate nafasi aje atembelee viwanja hivi na tuone namna ya kuviboresha ili kupata vijana wengi zaidi; je, yuko tayari kufanya hivyo tukimaliza Bunge hili?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mabula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza Wabunge wote wa Jiji la Mwanza kwa jitihada kubwa sana na nzuri ambazo wanafanya katika kuboresha viwanja vyetu. Vilevile niseme kwamba ni juzi tu nilikuwa Wilaya ya Nyamagana na nikatembelea ule Uwanja wa Nyamagana ambao umekarabatiwa kwa jitihada za Halmashauri, Waheshimiwa Wabunge, pamoja na wadau. Niseme kwamba ombi lako nimelipokea na nitafika tena kwenye Jiji la Mwanza ili kuweza kuangalia namna gani ambavyo tutashirikiana pamoja. Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nami napenda kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mradi unaotegemewa kutekelezwa pale Magu unategemea sana chanzo kipya kitakachojengwa kwenye Jimbo la Nyamagana pale Butimba ambao utasaidia pia maji kule Buswelu kwenye Jimbo la Ilemela, ikiwemo Kata ya Buhongwa kama ilivyotajwa, Kishili, Rwanima pamoja na Igoma.

Mheshimiwa Spika, mradi huu tayari mkandarasi wa kusambaza bomba za maji ameshapatikana na mkandarasi wa kujenga chanzo hiki kipya ndio imekuwa inasuasua. Mheshimiwa Kiswaga ameomba commitment ya Serikali, sasa Mheshimiwa Waziri atuhakikishie kwamba hii financial agreement ni lini itakuwa tayari ili miradi hii iweze kutekelezeka kulingana na hali halisi ilivyo?

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa maji na uwepo wa Ziwa Victoria haufurahishi leo watu wa Mwanza, Nyamagana pamoja na miji inayozunguka kuendelea kuchota maji kwenye visima.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nampongeza kaka yangu Mheshimiwa Mabula kwa kazi nzuri anayoifanya katika Jimbo lake la Nyamagana, lakini atambue kabisa eneo ambalo litapata maji kwa asilimia 100 ni eneo la Nyamagana. Sasa sisi kama Wizara kuna kazi kubwa sana inayofanyika, hiki kilichobaki ni kiasi kidogo sana.

Mheshimiwa Spika, kubwa, nataka nitengeneze commitment kwake kwamba sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji na siyo Wizara ya Ukame tutafanya mawasiliano ya haraka na Wizara ya Fedha kuona ule mkataba unasainiwa kwa haraka ili mwisho wa siku mkandarasi yule aweze kuhakikisha chanzo kile cha maji kinatekelezwa kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mji wa Mwanza unaendelea kukua kila siku na miundombinu ya barabara hasa barabara ya Kinyata inayotoka Mwanza Mjini kwenda Usagara hali yake kimsongamano siyo nzuri; na leo nauliza karibia mara ya nne:-

Ni lini sasa Wizara itakuwa tayari kuhakikisha barabara inayotoka Mwanza Mjini kupitia Igogo - Mkuyuni na Butimba - Nyegezi mpaka Buhongwa, inapanuliwa kwa njia nne sasa na kuweza kuwa barabara inayofanana na maziringira halisi ya mji wenyewe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Jiji la Mwanza linapanuka kwa kasi sana na ni mipango ya Serikali kuhakikisha kwamba Jiji hilo linaundiwa program maalum ya kupanua barabara zake kupunguza msongamano. Namshauri Mheshimiwa Mbunge, baada ya kikao hiki, baada ya kipindi cha Maswali na Majibu, tuambatane naye mpaka Wizarani akaone mipango ya Serikali kuhusu Jiji la Mwenza kurekebisha barabara zake.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa matatizo yaliyoko Lulindi ni sawa kabisa na matatizo yaliyoko Jimbo la Ilemela, hasa kwenye Kata za Sangabuye ambapo kuna Kituo kikubwa cha Afya na upatikanaji wa mawasiliano umekuwa ni adimu sana, sambasamba na Kisiwa cha Bezi ambako hakuna kabisa mawasiliano na kuna wakazi wengi sana na Mheshimiwa Naibu Waziri ameshapata nafasi ya kutembelea kule; anawaambia nini wakazi wa Bezi na wakazi wa Sangabuye ni lini watapata mawasiliano ili na wao wawasiliane ukizingatia pale kuna Kituo cha Afya ambacho watu wengi wanaweza kupoteza maisha kwa kukosa mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli nilitembelea Kata ya Ilemela kwa Mheshimiwa Angelina Mabula, Naibu Waziri wa Ardhi na nilionyeshwa mpaka eneo la Bezi ambako kunahitaji mawasiliano. Nakiri kwamba kuna changamoto ya mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie tu kwamba maeneo mengi ya nchi yetu Waheshimiwa Wabunge wengi sana minara yao ya mawasiliano haifanyi kazi vizuri. Tunakwenda kutuma timu ya wataalamu kwa ajili ya kurekebisha minara hiyo ya mawasiliano ili iweze kutoa mawasiliano vizuri kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Bezi tumeshafanya tathmini, tumeshatuma mafundi na wataalam kwa ajili ya ukaguzi. Hivi karibuni tutatangaza tenda na Kisiwa cha Bezi kitakuwemo kwa ajili ya kupelekewa mawasiliano. Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

(i) Kwa kuwa Msitu wa Makele kusini ambao tayari umesha poteza sifa ya uhifadhi, na kwa kuwa tayari yapo maelekezo ya kutoa sehemu ya misitu hii kwa sababu ya wafungaji ili kuondoa usumbufu uliopo kwa nini sasa Serikali isitoe msitu huu wa Makele kusini kwa ajili ya wafugaji?

(ii) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala hili la mifugo imekuwa na changamoto kubwa, sambamba na Jimbo la Nyamagada unapozungumzia masuala ya mifugo kwenye minada ya upili watu wana Nyamagana hawana kabisa eneo la kufanyika shughuli zao za uchinjaji na kwa maana mnada. Na kwa sababu na mifugo hii imekuwa inatangatanga mtu anayetoa mfugo Magu lileta Mwanza au anayetoa mfugo Kwimba kuleta Mwanza analazimika kupeleka Misungwi kwenye mnada wa upili ndio arudishe Nyamagana kwa ajili ya uchinjaji au Ilemela na matokeo yake kuongeza gharama za mchinjaji. Ni nini Serikali inatoa kauli gani juu ya minada hii kwa nini usirudishwe pale pale ulipo Nyamgana na watu wakachinja kwa uzuri?
NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni juu ya kuomba msitu wa Makele kusini kupewa wafugaji. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwaka 2016 alipotembelea katika Mkoa wa Kigoma, alipita katika Wilaya Kasulu na wananchi wa Kasulu walimpa maombi yao ya kuomba msitu huu wa Makele kusini upewe wananchi kwa maana ya shughuli za ufugaji na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alielekeza hekta zipatazo 10,000 zitolewe kwa vijiji viwili 5,000 na 5,000 zigawiwe kwa Halmashuri ya Kasulu. Watendaji wa TFS kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii wametekeleza agizo hili na wananchi wa Kasulu wamepatiwa. Hivi sasa tulichokipendekeza baada ya maelekezo mengine juu ya Rais wetu juu ya kuwapa wafugaji na wakulima maeneo ya ziada kwa ajili shughuli zao tumependekeza eneo la Mkuti katika Wilaya Kasulu na Uvinza ndio sasa yaelekezwe kuangaliwa kama yamepoteza sifa yapewe wafugaji na wakulima. Naomba Mheshimiwa Vuma na wafugaji na wakulima wote katika Wilaya ya Kasulu waendelee kuwa na subra pindi jambo hili litakapokuwa tayari watapata manufaa hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili linahusu minada ya Upili na kwa nini wachinjaji wa pale Mwanza Jiji wanalazimishwa kupeleka mifugo yao katika mnada wa Upili wa Msungwi ndipo waende kuchakata mifugo hiyo pale Mwanza Jiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni urasimu kwa sababu mifugo tumekubaliana ya kwamba minada ya Upili dhumuni lake ni kwa ajili ya wafanyabishara kwa kiwango cha kati na kuwango cha juu. Kwa wale wafanyabishara wadogo wadogo wenye ng’ombe mmoja wawili ama mbuzi mmoja wawili wanaruhusiwa kununua katika minada yao ya misingi na kwenda kuchakata moja kwa moja kwa ajili yakuweza kufanya shughuli hizi za kujipatia kipato na kuhudumia wananchi. Natoa maelekezo kwa watendaji wetu wasimamie sheria kanuni zetu bila kuathiri wananchi wetu na kuinua vipato vyao na kuendeleza maisha yao.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza, naipongeza sana Serikali kwa miradi mikubwa ya maji ambayo inatekelezwa kwenye Mkoa wa Mwanza likiwemo Jimbo la Nyamagana na hakika ikikamilika miradi hii itakuwa suluhisho kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu dogo la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri, tunao mradi kwenye Kata ya Lwanima wa ujenzi wa tenki la karibia lita 450,000. Ni takribani miaka mitatu sasa na changamoto ni malipo ya certificate ya mwisho hayajalipwa mpaka leo. Ni nini kauli ya Serikali kwa watu wa Lwanima ambao mradi huu na tenki hili lenye matoleo zaidi ya 17 katika kila Mtaa? Ni lini fedha hizi zitatoka ili wakazi wa Lwanima waweze kupata maji ya uhakika na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji kwanza nipende kumpongeza na nithaminishe kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lake la Nyamagana, lakini kikubwa maji ni uhai. Ninachotaka kumhakikishia, sisi kama Viongozi wa Wizara hatutakuwa kikwazo kwa Wakandarasi ambao wamefanya kazi yao thabiti kabisa na yenye weledi kuhakikisha kwamba tunawalipa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie, katika mfuko huu tutalipa ili mradi ule ukamilike na wananchi wake waweze kupata huduma hii muhimu ya maji. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza; lakini uniruhusu niseme jambo moja dogo ambalo siku zote nimekuwa nikitafakari wahenga wakisema kua uyaone, lakini hatimaye nimeyaona jana goli kuwa kona kwa watani zangu wa Yanga; kwa kweli, nimestaajabu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba swali langu dogo la nyongeza lipate majibu yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Serikali imedhamiria kuhakikisha barabara zote ambazo ziko kwenye ahadi zinajengwa na kukamilika kwa kiwango cha lami ikiwemo Barabara ya kutoka Buhongwa – Lwanima – Kishiri mpaka Igoma. Sasa, ni lini Serikali itakuwa tayari kuhakikisha barabara hii inakamilika kwa kiwango cha lami kama ambavyo iliahidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mabula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo Mheshimiwa Mbunge anaitaja ni barabara ambayo iko chini ya TARURA. Na kipekee Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiipigania barabara hii kwa muda mrefu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge; usanifu wa barabara hii umeshakamilika; na kitakachofuata katika bajeti ya mwaka 2020/2021 tutaanza kuijenga hatua kwa hatua, ili barabara yote iweze kukamilika.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ahsante kwa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na kazi nzuri ya urasimishaji wa ajira lipo kundi la madereza na makondakta wa daladala wamekuwa kwenye ajira kwa muda mrefu sana lakini ajira zao zimekuwa hazithaminiwi kwa maana ya kupewa thamani ya mikataba na wao kuwafanya waweze kuwa na akiba kwenye mifuko yetu ya hifadhi pale wanapokuwa wameacha kazi hii. Ni lini Serikali itahakikisha ajira hii na yenyewe inakuwa rasmi na kutambuliwa kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Stanslau Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo anawapigania sana waendesha bodaboda na daladala katika eneo lake la Nyamagana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake anasema Serikali tuna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba madereva wa daladala na bodaboda wanakuwa na mikataba na kufanya kazi zenye staha. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Jenista Mhagama amekwishatekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu la kuwaita na tumekaa nao kwa pamoja wamiliki wa vyombo mbalimbali vya moto pamoja na Chama cha Madereva katika kutengeneza mpango wa pamoja wa kurasimisha ajira za madereva. Mpaka hivi sasa tunaendelea na ushirikiano mzuri pamoja na wamiliki wa vyombo hivyo na tumepeana muda ambapo baadaye tutafanya ukaguzi kujiridhisha kwamba makubaliano yetu yamefikiwa ili tuhakikishe kwamba Tanzania nzima madereva wote wa magari makubwa, mabasi, magari madogo wanapata mikataba ya ajira kama sheria inavyoelekeza katika kifungu cha 14 cha Sheria Na.6 ya mwaka 2004.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na kwa kuonesha wazi kwamba kama Wizara wanatambua namna ambavyo Mji wa Mwanza una vivutio vingi na unaweza kuwa sehemu ya utalii kwenye nchi hii. Sasa nilikuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa spika, moja ni kwamba pamoja na mazingira na vivutio vingi vilivyopo ni nini sasa mkakati wa Wizara kuhakikisha kwamba ili watalii waje ni lazima wapatikane watu wanaosababisha watalii kuja. Tunatambua ili watalii hawa waje wanatakiwa wawe na watu wenye weledi ambao vijana wamefundishwa kwa kuona maeneo ambayo tunaweza kuwa na ma-tour guide wazuri ni nini mkakati wa Wizara kuhakikisha vijana wengi waliopo Mwanza wanapatiwa mafunzo haya na kufanya kazi hii vizuri.

Mheshimiwa spika, la pili; tunatambua kwamba TTB tayari kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Mwanza pamoja na St. Augustine University wameanzisha Mwanza Tourism na kupitia mkakati huo tayari Wizara kwa maana ya halmashauri pamoja na Ubalozi wa Ujerumani wameanza ukarabati wa ile Gunzeki House ambayo iko pale Makoroboi itakayokuwa ni moja ya majumba ya maonesho ya historia pamoja na ile Gallostream Nini mkakati wa Wizara kuhakikisha maeneo haya yanapewa kipaumbele na kuwa moja ya vivutio katika Mji wa Mwanza, nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mabula kwa namna ambavyo tumekuwa tukishiriki kwa pamoja katika juhudi hizi za kuifanya Mwanza kuwa hub ya utalii wa Mikoa ya Kaskazini Magharibi. Tulikuwa nae kwenye kongamano hilo ambalo nimelisema na alishiriki kwenye kuchangia mambo mazuri sana ambayo Wizara inayafanyia kazi, kwa hiyo nampongeza sana.

Mheshimiwa Spika, ameuliza ni mkakati upi wa Wizara katika kuhakikisha kwamba tunapata washiriki wengi katika shughuli za utalii katika mikoa hiyo. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Wizara katika nyakati mbalimbali imefanya mikutano na wadau katika Mkoa wa Mwanza na tumeendelea kufanya semina mbalimbali kupitia ofisi yetu ya idara ya utalii lakini pia kupitia TTB na hivi karibuni tutafanya mkutano mwingine kutathmini kikao tulichokifanya pale awali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wito wangu tu ni kwamba naomba kuwakaribisha wadau wote wa utalii wa Mkoa wa Mwanza na watu walio na interest ya kufanya biashara ya utalii kama alivyosema mwenyewe, watalii wanaletwa na watu na watalii wanatafutwa lazima wawepo wapo Mkoani Mwanza wanaotafuta watalii. Sisi tutakuwa tayari kufadhili mafunzo hayo ili kuhakikisha kwamba tunapata watu wengi wanaoshirikiana na jambo hili.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili amezungumzia kuhusu ukarabati wa jengo lililopo Makoroboi na kwamba ni upi mkakati wa Wizara. Wizara yetu imeendelea kutoa utaalam katika maeneo haya na katika maeneo mengine kwa mfano pale Mkoani Iringa lilikuwepo pia jengo la mkoloni ambalo zamani ilikuwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya lilikarabatiwa na kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha RUCO sasa hivi jengo hilo ndilo ambalo linaonesha makumbusho na historia mbalimbali ya Mkoa ywa Iringa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawapongeza sana Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino kwa kuandaa kila mwaka Mwanza Tourism ambapo wamekuwa wakipeleka watu mbalimbali katika Kisiwa cha Saa Nane na kuwazungusha katika Jiji la Mwanza. Juhudi hizi tunaziunga mkono tutaendelea kushirikiana na Mkoa wa Mwanza.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa, lakini kwa kuwa circuit ya Kaskazini Magharibi ni circuit ya Kimkakati kwenye Serikali ya Awamu ya Tano hususan kwenye Sekta ya Kiutalii, napenda niongeze mambo yafuatayo ambayo tunayafanya na tunakusudia kuyafanya katika circuit hii ya Kaskazini Magharibi.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, Serikali inawekeza kwa kiasi kikubwa sana kwenye miundombinu (hard infrastructure) kama vile Reli ya SGR ambayo itafika mpaka Mwanza, viwanja vya ndege; Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kitakuwa cha Kimataifa na sasa hivi ujenzi unaendelea pale. Vile vile ukiunganisha na mtandao wa Viwanja vya Ndege vilivyopo katika circuit hii, Kiwanja cha Ndege cha Chato, Kiwanja cha Ndege cha Bukoba, Kigoma, Tabora pamoja na cha Musoma vyote vinafanyiwa first lifting ili kuhakikisha kuna ndege zinatua regularly katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, hiyo ni sambamba na mtandao wa lami. Pia tunawekeza katika softly infrastructures ambapo sasa hivi tumewaelekeza Chuo cha Taifa cha Utalii wafungue Tawi kwa ajili ya kuongeza idadi ya vijana ambao wanasomea mambo ya utalii, tour guiding, upishi na vitu vingine katika Jiji la Mwanza.

Mheshimiwa Spika, mbali na hayo yote, circuit hii ya Magharibi ina bahati ya kuwa na maziwa na mito na tumeona kwamba hii ni unique feature ambayo kama tukiitumia vizuri itaifungua kwa kasi sana circuit ya Kaskazini Magharibi ambapo kwa kuanzia, tumewaelekeza TANAPA na tayari wameshafanya manunuzi ya boti ambayo itakuwa ni luxury kwa ajili ya utalii, itakuwa inachukua watu 50 na itakuwa inazunguka kutoka spix gulf kwenye eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, inakwenda, ina-dock Mwanza, itakuwa ina-dock pale Kisiwa cha Saa Nane, Kisiwa cha Rubondo lakini pia kwenye eneo la Katete ambapo Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato inaanzia. Hii boti itakuwa ni luxury na itakuwa inatumia masaa takribani matatu na nusu mpaka manne kutoka Serengeti kufanya huo mzunguko wote.

Mheshimiwa Spika, tunakusudia boti hiyo itakuwa ni ya business class lakini tumewaelekeza pia TANAPA wawekeze kwenye manunuzi ya boti nyingine ambayo itakuwa economy class ambayo itachukua watu 300 kwa ajili ya kuwazungusha kwenye Ziwa Victoria ili kuvinjari katika Ziwa, lakini pia Visiwa vilivyoko pale na maeneo ya Hifadhi ambayo yanaungana moja kwa moja na Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilipenda kuongezea hayo. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA:Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nitumie nafasi hii pia kumshukuru sana Naibu Waziri pamoja na Waziri kupitia Wizara ya Ardhi kwa kazi kubwa ambayo kwa kweli katika suala zima la urasimishaji makazi wamejitahidi.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu kubwa ilikuwa ni namna gani wakazi hawa walioko kwenye maeneo ya milima watapatiwa nafuu kubwa hasa angalau kwa kutambulika. Sasa niishukuru Serikali kwasababu imeliona hili na kulifanyiakazi; ni jambo jema sana na mimi nawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inaendelea na utaratibu wa urasimishaji wa makazi, na tunafahamu kwamba ili urasimishe makazi yako maeneo ambayo yalikuwa na michoro ambayo ilikuwa na maeneo mbalimbali. Kwa mfano, maeneo kwa ajili ya maziko, kwa maana ya Makaburi; Serikali ina mpango gani sasa? Maana kumekuwa na mgogoro mkubwa, kwamba eneo lilitengwa kwa ajili ya makaburi lakini linakuta wananchi wameshajenga sana kwasababu halikulindwa na badala yake wanalazimika aidha sasa tuamue wananchi waondoke tubakishe eneo kwa ajili ya makuburi au wananchi wabaki ili tutafute eneo lingine la makaburi. Maeneo ya kule Sawa, Mwalukila pamoja na Igwambiti liko tatizo la namna hii; na namshukuru Waziri amefanya jitihada kubwa amefika kule.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili; ili uweze kupima na kupanga unahitaji fedha na Serikali imekuwa na utaratibu wa kutoa fedha kwenye halmashauri zetu kama mkopo. Sisi kama Wilaya ya Nyamagana, Jiji la Mwanza tulishaomba fedha na mikataba yote ikafungwa kwa ajili ya kupata fedha bahati mbaya sana hatujapata fedha hizi mpaka leo ni nini kauli ya Mheshimiwa Waziri? Ni lini tutapata fedha hizi hizi ili tupime na kupanga maeneo ambayo tunadhani yanaweza kuiingizia Serikali na Halmashauri mapato?(Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ili uweze kupima na kupanga unahitaji fedha na Serikali imekuwa na utaratibu wa kutoa fedha kwenye Halmashauri zetu kama mkopo.

Sisi kama Wilaya ya Nyamagana, Jiji la Mwanza tulishaomba fedha na mikataba yote ikafungwa kwa ajili ya kupata fedha bahati mbaya sana hatujapata fedha hizi mpaka leo. Ni nini kauli ya Mheshimiwa Waziri kwamba lini tutapata fedha hizi ili tupime na kupanga maeneo ambayo tunadhani yanaweza kuiingizia Serikali na Halmashauri mapato? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Stanslaus Mabula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mabula kwa namna ambavyo amekuwa akipigania watu wake kwa ajili ya kurasimishiwa maeneo. Wote kama mnavyojua, Mji wa Mwanza umezungukwa na milima usipokuwa makini unaweza ukapata ajali kwa ajili ya watu pengine kuporomekewa mawe na kadhalika lakini amekuwa mvumilivu, amefuatilia na kuhakikisha kwamba taratibu zilizopangwa na Serikali zinafuatwa, namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali yake mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anazungumzia habari ya maeneo ya maziko ambayo tayari yameshavamiwa na ni kweli nilitembelea katika eneo lile nikakuta sehemu kubwa ya eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili ya maziko limevamiwa na watu. Nitoe rai kwa Halmashauri zote kusimamia maeneo haya kwa sababu tunapanga maeneo hatuyasimamii matokeo yake watu wanavamia halafu kuwatoa inakuwa ni kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, lakini katika eneo alilolisema kwenye Kata ya Sawa, kuna maeneo ambayo yako wazi kidogo ambayo hayajavamiwa na kama wako watu hawazidi watano, bado tunaweza tukafanya mabadiliko katika ramani ya eneo lile ili watu wakapangwa kwenye maeneo yale wakaendelea na maisha yao halafu sehemu ya maziko nayo ikapatikana kwa sababu huduma zote tunazihitaji. Kwa hiyo, hilo ni suala la kumuelekeza Mkurugenzi wa Mipango Miji aweze kusimamia shughuli hiyo ili upangaji ufanyike upya katika eneo lile tupate eneo la maziko na watu warasimishiwe maeneo yale waweze kuishi kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anazungumzia suala la Halmashauri kuwezeshwa ili waweze kupata pesa za upimaji. Napenda tu nitoe taarifa kwenye Bunge lako, Wizara ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 6.2 katika Halmashauri zipatazo 24 kwa ajili ya kuwapa mkopo usio na riba ili waweze kupima na kurejesha na wengine waweze kupewa. Nasikitika kusema kati ya Halmashauri 24, ni Halmashauri tatu tu ambazo zimeanza kurejesha mikopo yake. Kati ya hizo shilingi bilioni 6.2 ni shilingi milioni 906 ndiyo zimerejeshwa ambapo Halmashauri ya Ilemela imerejesha shilingi milioni 800 kati ya shilingi bilioni 1.5 iliyopewa; Halmashauri ya Ukerewe imerejesha shilingi milioni 20 kati ya shilingi milioni 73 na Halmashauri nyingine ambazo zimepelekewa bado hazijarejesha mpaka leo.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai ili na wengine waweze kufaidika na pesa hiyo tunaomba sana Halmashauri hizi waweze kurejesha pesa hizo ili wale wengine waweze kupata. Sifa ni moja tu, ni kuandika andiko ambapo utaonesha mchanganuo mzuri namna utakavyofanya upimaji wako, utakavyolipa fidia na utakavyorejesha mkopo. Kwa hiyo, ni kitu kidogo tu watu wanafahamu wafanye kazi hiyo na Wizara itapokea lakini kwa kusubiri pesa zirejeshwe.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa ucheleweshaji wa ukamilishwaji wa miradi ya maji wakati mwingine imepelekea kuwa na matatizo makubwa hasa kwa watumiaji. Hii inaenda sambamba na mamlaka zinazosimamia maji kulazimika kuangalia utaratibu mpya wa kuongeza gharama za maji kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na matokeo yake bill za maji zimekuwa zikipanda sana kila wakati. Hivi tunavyozungumza kuna upandishwaji wa bill ambao unatokana tu na upungufu wa miradi mingi inayoweza ikazalisha maji kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, nini mkakati madhubuti wa Serikali wa kuendelea kuwapunguzia wananchi mzigo wa kulipa bill kubwa kila wakati kutokana na miradi mingi kukwama pengine kutokana na mikataba ya kifedha iliyocheleweshwa ili fedha hiyo iweze kutoka na miradi hii iweze kukamilika kwa wakati?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Stanslaus Mabula, kiukweli ni Mbunge ambaye anayefanya kazi na anawatendea haki wananchi wake wa Nyamagana.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwa wakati, sisi Wizara ya Maji tumejipanga baadhi ya miradi mingi tutaitekeleza kutumia Force Account kwa maana ya wataalam wetu kuweza kutekeleza miradi ile ili iweze kukamilika na wananchi wapate huduma ya maji.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la bei za maji, tulipata malalamiko kwa wananchi wa Mwanza na Mheshimiwa Waziri ametoa maagizo maalum kwa EWURA kuhakikisha zile bei zinapitiwa ili wananchi wa Mwanza na maeneo mengine waweze kupata bei ambazo zitakuwa rafiki na waweze kupata huduma hii kwa urahisi. Katika kuhakikisha tunaondoa changamoto hii ya bill, sisi kama Wizara ya Maji tumejipanga na agizo maalumu la Mheshimiwa Waziri ni kuhakikisha kwamba tufunga pre-paid meter katika kuhakikisha wananchi wanalipa kutokana na kile ambacho wamekitumia.

Mheshimiwa Spika, kingine naomba niwasisitize wananchi matumizi ya maji yasiyokuwa na ulazima yanasababisha kuongezeka kwa bili za maji. Leo mvua inanyesha lakini mwananchi anatumia bomba kumwagilia maji maua, haipendezi na wala haifurahishi. Hii ni changamoto lakini naomba Waheshimiwa Wabunge tutoe elimu hii ili kuhakikisha kwamba wananchi wanatumia vizuri maji na wanapata nafuu kabisa katika matumizi haya ya maji.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninakiri kutambua kazi kubwa inayofanywa na Wizara hii kuhakikisha kwamba maeneo mengi yanapata umeme na kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni dogo tu, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa nguzo kwa wateja wapya hasa kwenye Jimbo la Nyamagana, lakini pia ni lini sasa Serikali itahakikisha Nyamagana ambayo inajengeka kwa kasi kubwa sana kwenye maeneo yote kuanzia Kishiri, Fumagira, Rwanima, Bwigoma na Maina watapata umeme wa uhakika kabla hatujafika kwenye mwisho wa mwaka tuliokusudia? Nakushukuru sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-

Ni kweli, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana mwaka jana tulifanyakazi kubwa sana kuhakikisha wananchi wa mitaa yote ya Nyamagana wanapata umeme na hivi sasa tunavyoendelea kuzungumza vijiji na maeneo ya Kishiri, Fumagira, Buhongwa pamoja na Nyamagana yote kuna wakandarasi wanne wanaofanyakazi na nguzo zaidi ya 2000 zitaondoka tarehe 18 mwezi huu kwenda kufanyakazi Nyamagana. Niwaondoe wasiwasi wananchi na wakandarasi nguzo zipo za kutosha hapa Nchini kuliko hata mahitaji yetu. Kwa hiyo kazi zitafanyika na Nyamagana nzima itapata umeme. Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba niulize swali la nyongeza, kwa kuwa barabara ya Kenyatta itokaya Mwanza Mjini kwenda Usagala kuelekea Shinyanga ni barabara ambayo inahudumia watu wengi na kwa sasa inaendelea kuwa finyu sana. Ni lini Serikali kupitia mipango yake ya uboreshaji miundombinu itaitolea fedha barabara hii walau iwe ya njia tatu mpaka nne ili kuweza kukidhi mahitaji makubwa ya watu wa Mwanza?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanua barabara, kuongeza reli, hatuendi hivi hivi lakini mpaka traffic iweze kufikia kwamba sasa yanapita magari 20,000 au 40,000 kwa siku ndiyo tunaipanua ili kuiongezea uwezo. Kwa hiyo, itakapofikia itafanyika.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Name naomba nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa miradi hii ya kimkakati ambayo tunaizungumzia imekuwa na msaada mkubwa sana kwenye Halmashauri zetu na hasa kuisaidia TARURA kwenye kuhakikisha miradi inafanikiwa zaidi, tunao mradi mwingine mkubwa wa Tacticambao Serikali imeshauanzisha ikiwemo Jiji la Mbeya pamoja na Jiji la Mwanza na Manispaa nyingine.

Je, ni nini sasa mpango wa Serikali kuhakikisha mradi huu unaanza haraka ili tuone matokeo yake makubwa kama TSCP?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya maswali ya awali. Pia naomba nimpongeze ndugu yangu, mtani wangu Mheshimiwa Stanslaus Mabula Bin Jongo wa kutoka Pwani kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Jiji ambalo tumefanya kazi kubwa sana ni Jiji la Mwanza. Kwa hili, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa waliyofanya kwa kushirikiana na TAMISEMI kubadilisha Jiji la Mwanza kuonekana katika sura iliyokuwepo. Hata hivyo, mpango wetu kama nilivyosema wakati natoa budget speech yangu katika mwaka uliopita kwa mwaka wa Fedha 2021, kwamba tumekuwa na ile miradi ya Tactic, ambapo matarajio yetu makubwa ni kwamba tutakwenda kugusa maeneo 45 zikiwepo Halmashauri za Miji, Mafinga ikiwa ni mojawapo, Nzega, Kasulu, Handeni Mjini na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge wawe na subira tu, kazi inakwenda vizuri. Ni imani yetu kwamba mradi huu unakwenda kubadilisha kabisa nchi yetu. Katika miaka mitano ijayo, Tanzania miji yake yote itakuwa ni ya ajabu kutokana na kazi kubwa tunayokwenda kuifanya. Kwa hiyo, msihofu, kazi inafanyika vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa Serikali inasisitiza Halmashauri zetu ziweze kujitegemea na kukusanya mapato kwa wingi; Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambayo kwa sasa haina machinjio ya uhakika, imetumia fedha za ndani kukarabati pamoja na wadau machinjio ambayo kwa sasa ina uwezo wa kuchinja ng’ombe 200 peke yake na mahitaji ni takribani ng’ombe 800 kwa siku.

Je, Serikali iko tayari sasa kuipa Halmashauri ya Jiji la Mwanza fedha kwa ajili ya kununua mashine zitakazowekwa kwenye mashine mpya ili iweze kufanya kazi, kutoa ajira na kuzalisha mapato kwa wingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imewezesha ujenzi wa machinjio ya kisasa katika Jimbo la Nyamagana kwa lengo la kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma katika jamii na kuiwezesha Halmashauri kupata mapato ya kutosha ili iweze kugharamia shughuli za maendeleo katika Jimbo lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba pamoja na kukamilika kwa machinjio ile, bado haijaweza kutumika ipasavyo kuchinja ng’ombe kwa uwezo wake; na kwa sasa inachinja ng’ombe 200 kati ya mahitaji ya ng’ombe 800 kwa siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tumelichukua. Naomba tukalifanyie kazi ili tuweze kuweka mpango wa kuiwezesha machinjio ile kupata vifaa vya kutosha ili iweze sasa kutoa huduma kwa uwezo unaostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili tutalifanyia kazi.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, matatizo ya Mto Msimbazi ni sawa kabisa na matatizo ya yaliyoko kwenye Mto Milongo katikati ya Jiji la Mwanza, ninataka tu kufahamu mto huu umekuwa unasababisha maafa mara kwa mara mvua zinaponyesha.

Je, ni lini Serikali inao mkakati wa kuhakikisha mto huu unajengwa upya na kuwekewa tahadhari zote kuepusha maafa yanayowakuta wakazi wa Kata za Mabatini, Milongo, Mbugani pamoja na Kata yenyewe ya Nyamagana. Ni lini Serikali itachukua hatua kuhakikisha mto huu na wenyewe unakuwa kwenye hesabu ya kushughulikiwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Mabula Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameleta ombi jipya la Mto Milongo ambao na wenyewe umekuwa na athari zinazofanana na Mto Msimbazi. Kwa hiyo, tunalipokea kwa sababu Serikali muda wote iko kazini, kama ambavyo tunakwenda kufanyia kazi Mto wa Msimbazi maana yake na la kwake vilevile tunalipokea na tukishalipokea maana yake tutafanya tathimini na katika mipango ya baadaye tutaliweka katika mipango yetu. Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na changamoto za kifedha kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameeleza lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo jibu la Waziri linasema ujenzi wa barabara hii baada ya Mkandarasi Mshauri kuwa amekamilisha kazi yake itategemea na upatikanaji wa fedha. Upatikanaji wa fedha ni kweli kwamba unaweza ukachukua hata zaidi ya miaka mitatu au minne. Swali langu la kwanza, kwa sababu barabara sasa hivi imekuwa na magari mengi takriban 2,000 kwa siku kutoka Nyegezi kwenda Usagara mpaka Mjini, Serikali itakuwa tayari angalau kuanza kwa hatua mbili; walau baada ya Mkandarasi Mshauri kumaliza itakuwa tayari kuanza kujenga hata kwa km 10 kwa phases na baadaye km 10?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, wako watu kutoka Kata ya Nyegezi na Mkolani ambao wameongezeka zaidi ya mita 7.5 kwenye barabara hii na watu hao wanastahili kulipwa fidia. Je, Serikali itakuwa tayari kuwalipa fidia stahiki kwa sababu za msingi ili barabara hii iweze kujengwa bila vikwazo na wananchi wapate huduma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, usanifu wa kina utakamilika Septemba na baada ya hapo barabara hiyo itaanzwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Kuhusu upatikanaji wa fedha na ni kwa kiasi gani tunaweza kujenga, matarajio ya Serikali ni kukamilisha barabara lakini tutaanza kadri fedha itakavyopatikana ndiyo tutaanza kujenga kama ni km 5, km10 ama ikiwezekana zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu fidia, hatutajenga bila kufanya tathmini na ndiyo maana ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao unachukua masuala yote; kuangalia ni kiasi gani cha fedha kinatakiwa ili wananchi wa Kata za Buhongwa na Nyegezi ambao wameongezeka sana watafidiwa. Ni utaratibu kwamba ni pale ambapo wananchi wa Kata za Buhongwa na Mkolani watakapokuwa wamefidiwa ndipo ujenzi utaanza. Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kifupi sana uniruhusu. Ninafahamu kwamba mradi wa TACTIC ni mradi mbadala baada ya mradi wa TSP. Mradi wa TSP umekuwa mkombozi mkubwa sana kwenye nchi yetu kwenye miji, majiji na Serikali kwa pamoja. Utakumbuka hata ukiitazama Mbeya leo ukaitazama Mwanza, Tanga, na Manispaa nyingine za Kigoma, Ujiji na maeneo mengine, zaidi ya kilometa 457 zilijengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu toka Juni, 2019 barabara nyingi sana zilitangazwa na wakandarasi wakahitajika, wakajaza fomu ili wapate kazi. Sioni jitihada za Serikali ambazo zitatusaidia kuhakikisha barabara hizi zinatengenezwa kwa wakati. Barabara ziko nyingi, mfano ukienda hata Mbeya leo barabara ya kutoka machinjio ya Ilemi kwenda Mapelele inategemea fedha hizi ili ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda barabara ya Buswelu ambayo itakwenda kuunganisha soko la mbogamboga mpaka stendi mpya inategemea barabara hii. Barabara ya Mkuyuni kwenda Nyakato inategemea fedha hizi. Soko jipya la Kirumba linategemea fedha hizi. Hata ukienda kule kwa Mheshimiwa Ummy, barabara ambayo inakwenda Masiwani kwenda Hospitali ya Wilaya inategema fedha hizi. (Makofi)

Sasa jitihada za Serikali za Serikali kuhakikisha fedha hizi zinapatikana: ni lini Serikali itahakikisha mradi huu unaanza mara moja ili fedha hizi zipatikane tuone matokeo?

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali inafahamu kwamba TARURA haina uwezo wa kujenga barabara hizi bila fedha hizi tunazozitegemea leo zipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali lake la kwanza la msingi Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula Mbunge alijaribu kuainisha umuhimu wa mradi huu wa uendelezaji wa miundombinu katika miji kwa maana ya TACTIC kwa kutaja maeneo mbalimbali ikiwemo katika Jimbo ambalo anatokea Naibu Spika wetu Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson. Ametaja Jimbo ambalo anatokea Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Jimbo lake Mheshimiwa Mbunge, Jimbo la Nyamagana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunatambua umuhimu wa barabara hizi na tunatambua umuhimu wa mradi huu. Ndiyo maana tumesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na hata katika ile miji yote ambayo imeainishwa kwenye huu mradi mtaona tumetuma wataalam katika kila Halmashauri, wameshafika huko kujadiliana mambo gani ya msingi yaingizwe katika huo mradi. Hiyo yote ni nia njema ya kuhakikisha kwamba huu mradi unakamilika kwa wakati. Ninaamini chini ya uongozi wa Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Hassan Suluhu; chini ya uongozi wa Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Ummy Mwalimu jambo hili litakamilika kwa wakati na huu mradi utatekelezeka kwa vitendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili amesema kwamba TARURA haina uwezo wa kuzijenga barabara hizo. Ni kweli, ndiyo maana tumekuja na huu mradi wa TACTIC kuhakikisha zile changamoto za barabara katika hayo maeneo yote yaliyotajwa tunazitatua. Kwa hiyo, lengo letu ni kuhakikisha tukidhi vigezo, tumalize majadiliano na mwisho wa siku barabara zianze kujengwa kwa sababu hilo ndiyo lengo la Serikali. Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nitumie nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuliangalia suala hili kwa kipekee na kulipa uzito na kuwapa matumaini wafanyakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nafahamu ya kwamba taasisi nyingi za Serikali zimekuwa na utaratibu wa kuchukua wafanyakazi kwa muda, kwa maana ya vibarua na wengine wanakuwepo kwa mikataba ya muda mfupi. Inapotokea suala la ajira, mara nyingi sana watu hawa wamekuwa wanasahaulika na kuchukuliwa watu kutoka nje. Kwa mtindo ule ule wa Serikali kuamua kuboresha maslahi ya wafanyakazi, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha vibarua na wale ambao wana ajira za muda, zinapopatikana fursa wanaajiriwa kwanza wao kama kipaumbele na wengine ndio wanafuata?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sera ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambayo ilipitishwa mwaka 2008 inaeleza wazi namna ya kupata Watumishi wa Umma kwa njia ya ushindani. Sasa nafahamu kuna maeneo mengi hata majimboni kwa Wabunge wengi kuna watu wengi wanajitolea katika taasisi za Umma.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Ummy Mwalimu alieleza mbele ya Bunge lako hili kwamba kuna database ambayo inaanzishwa kukusanya majina ya wale wote ambao wanajitolea maeneo mbalimbali nchini ambapo watapewa kipaumbele pale ambapo ajira zitajitokeza. Sasa nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wote wale ambao wanajitolea kuwasilisha majina yao Ofisi ya Rais, TAMISEMI kama ambavyo alikuwa ametoa maelekezo Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, kwa wale ambao hawapo katika ajira za Serikali za Mitaa, wao pia waorodheshe majina yao na kuyafikisha Ofisi ya Rais, Utumishi ili tuweze kuwa na database ya pamoja na pale ajira zinapotoka, basi tutaangalia. Kwa sababu kumekuwa kuna scenario ambazo watu wanajitolea pale tu wanaposikia ajira zinatoka ili waweze kupata favour ya kuweza kuingia kazini. Ili kudhibiti hilo na kuhakikisha ushindani upo katika kuajiri watu katika Utumishi wa Umma, ndiyo maana ajira zile zinatangazwa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo hao wanaojitolea, naamini watakuwa na added advantage kwa sababu wameshaifanya ile kazi kwa vitendo na hivyo wanapoenda kwenye usaili watakuwa wako vizuri zaidi katika kuweza kupata ajira hiyo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa Serikali inatambua ufugaji wa samaki kwenye mabwawa kule ukanda wa Ziwa Victoria na maeneo yote yanayozunguka na hasa maeneo ya kandokando kwenye miji mikubwa, zoezi la ufugaji wa samaki kwenye vizimba linaendelea kukua kwa kasi na tunaamini linaweza likatoa ajira nyingi sana kwa vijana.

Je, ni upi sasa mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba vijana wengi zaidi wanaingizwa katika shughuli hizi na kupewa fedha ili waweze kuwekeza kwenye ufugaji wa vizimba?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mkakati wetu ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ni kwamba tumeweka hela kiasi cha shilingi milioni 154. Pesa hizi ni kwa ajili ya kwenda kufanya mpango wa matumizi bora, kwa lugha nyepesi, katika eneo la Ziwa Victoria, Mkoa wa Mwanza na Mkoa wa Kagera. Tunakwenda kufanya demarcation na pesa hii tumeipeleka katika Taasisi yetu ya Utafiti ya TAFIRI kwa lengo la kutuandalia maeneo mahsusi ambayo vijana watakwenda kuyatumia kwa ajili ya ufugaji wa vizimba.

Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, vijana hawa tutawaweka katika ushirika ambao utawasaidia kuweza kupata mikopo na kuweza kujifanyia shughuli zao.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, na ni matarajio ya wananchi wa Jimbo la Ukonga ya kwamba barabara hizi zitatekelezwa kwa wakati kama Serikali ilivyoagiza.

Mheshimiwa Spika, swali dogo la nyongeza; kwa kuwa Serikali inao mpango na barabara nyingi zimeahidiwa ikiwemo barabara ya Msongola – Mbande yenye jumla ya kilometa 4.95. Ni lini Serikali inatoa ahadi ya kuanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kwa niaba ya Mheshimiwa Jerry Silaa wa Ukonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara ya Msongola – Mbande hadi Mbagala (kilometa tano) sisi tunasema bado hazijajengwa kwa kiwango cha lami. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeanza mpango na tayari zabuni zimeshatangazwa. Tutaanza kuijenga kilometa mbili kwa mwaka huu wa fedha, ahsante. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Naishukuru Serikali kwa sababu wakati natoa swali hili nilikuwa na mahitaji ya kata mbili zenye mitaa zaidi ya 14, yenye sura za vijiji. Sasa hivi ninavyozungumza Kata za Lwanima na Kishiri, mkandarasi wa REA, kwa gharama ile ile ya Shilingi 27,000/= anaendelea kufanya kazi na wananchi wangu wanafurahia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Serikali. Nitoe tu msisitizo uchambuzi huo utakapokamilika utatusaidia kujaziliza maeneo ambayo yatakuwa yamebaki kwa gharama nafuu kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kupokea pongezi na maombi ya Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa yamagana na kwamba tunashukuru ameona Serikali inavyojitahidi kuendelea kutekeleza huduma hii ya kupeleka umeme kwa wananchi kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Spika, hili la kukamilisha zoezi la utambuzi wa maeneo kama tulivyojibu kwenye swali la msingi, tutahakikisha linakamilika kwa wakati na liweze kutusaidia katika maeneo yetu sote.

Mheshimiwa Spika, nami Jimbo langu la Bukoba Mjini likiwemo linafanana na la kwake pia.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri, kwani barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wa Jimbo la Nyamagana na Jiji la Mwanza kwa ujumla, ukizingatia kwa sasa tuna mradi mkubwa wa daraja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na upembuzi yakinifu unaokamilika mwezi huu, naomba Mheshimiwa Waziri anihakikishie kwamba baada ya upembezi yakinifu kukamilika na bajeti itakuwa imeshaanza, kwenye mapitio ya bajeti, Serikali itakuwa tayari kuhakikisha barabara hii inaingia kwenye mpango na kuanza kujengwa upya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mwezi huu wa Nne tarehe 27 tutakamilisha usanifu wa kina. Kama alivyoomba kwamba baada ya kukamilika Serikali itafanya nini kwenye mid review ya bajeti ya Wizara?

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imesikia ombi lake, nasi tunajua msongamano wa barabara hiyo. Tumelichukua na tutaangalia jinsi ya kufanya pale itakapokamilika na kujua gharama ya barabara hii. Ahsante. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa swali la nyongeza, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri barabara ya kutoka Tambuka Reli, Nyagulugulu mpaka Mahina ni lini Serikali itaanza kuijenga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFRY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeza Mheshimiwa Mabula, amekuwa akija ofisini kuhusu barabara hii. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Nyamagana kwamba Serikali inakamilisha usanifu wa kina wa barabara hii na ina mpango wa kuanza kuijenga barabara hii kwa haraka sana kwa kiwango cha lami kwa sababu kwa watu ambao wamefika Mwanza, ndio barabara pekee ambayo inapotokea changamoto yoyote kati ya Mkuyuni, Igogo kwenda mjini ndiyo inaweza kuwa ni bypass kwa ajili ya watu kufika mjini.

Mheshimiwa Spika kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango wa Serikali ni kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami haraka inavyowezekana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa sababu Serikali inao mpango wa kutafuta fedha na kuhakikisha vyuo hivi vinajengwa. Wilaya ya Magu imeshatenga zaidi ya hekari 30, ikitegemea Serikali ipeleke fedha kwenye eneo hili na wananchi waweze kufaidika na vyuo hivi vya VETA. Sasa Serikali tunaomba commitment yake kwamba itakapopata fedha, Wilaya ya Magu iwe ya kwanza kwa sababu hata kule Kwimba, wanajenga kituo ambacho kina miaka miwili leo na hakijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pamoja na Serikali kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kupeleka kwenye ujenzi wa vyuo vingi vya VETA, vyuo vingi vimekuwa havina vifaa vya kufundishia na matokeo yake wanafunzi wengi wanajifunza kwa theory peke yake.

Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kila Chuo cha VETA kinapoanzishwa kilichopo kinakuwa na vifaa vyote stahiki kwa ajili ya kufundishia. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mabula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwennyekiti, ni kweli katika sera yetu ya Serikali kwamba tutakwenda kujenga Chuo cha VETA katika kila Wilaya na Mkoa katika Taifa letu. Nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na kumpongeza vilevile kwa ufuatiliaji wa karibu, iwapo Serikali itapata fedha, basi kipaumbele cha kwanza kitakuwa katika Wilaya hiyo ya Magu na Wilaya nyingine ambazo tayari zimeshatenga maeneo kwa ajili ujenzi wa vyuo hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimtoe wasiwasi vilevile katika eneo hili la pili la vifaa. Kama anavyofahamu Mheshimiwa Mbunge katika awamu ya kwanza tunakwenda kujenga Vyuo 25 katika Wilaya 25 mbalimbali nchini, tayari Vyuo hivyo viko mwishoni kabisa katika kumalizika kwake na tunaamini ifikapo Julai, vyuo hivi vinaweza kuanza kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili Serikali tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya vyuo hivi ili basi vitakapofunguliwa pamoja na ufundishaji wa nadharia lakini ufundishaji wa vitendo uwe umepewa kipaumbele zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuondoe wasiwasi tayari Serikali inafanyia kazi jambo hili na fedha tayari imeshatengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kufundishia. (Makofi)
STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kujua. Pamoja na maandalizi ya vifaa kwenye vituo vinavyojengwa, tunavyo takribani vituo vinne ambavyo vimeshakamilika; kule Igoma, Fumagila, Bulale pamoja na Nyegezi;

Ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kupeleka vifaa kwenye vitu hivi ambavyo vipo tayari na kuanza kutoa huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele sasa cha Wizara ya Afya na Waziri wa Afya ameshaelekeza wataalam wote, kwamba vituo vingi sasa vimeshakamilika na ujenzi wa kwa kiasi kikubwa sasa umeshafanyika.

Sasa kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha kuwa vituo ambavyo vipo tayari vinaanza kazi na kuhakikisha vina vifaa na watumishi. Kwa hiyo ndani ya mwaka huu kabla ya mwezi wa 10 vituo vyote vitakuwa vimepata vifaa tiba na vitakuwa vimeanza na wataalam watakuwa site. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa usanifu wa ujenzi wa barabara ya Kenyatta kutoka Mwanza Mjini kwenda Buhongwa – Usagara na Airport – Nyanguge zimeishakamilika ni lini ujenzi huu utaanza mara moja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mabula Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali hazma yake ni kuijenga hii barabara na kuipanua lakini tayari tumeisha kamilisha usanifu na sasa hivi tunaendelea kutafuta fedha. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira kwa sababu ndiyo tunaelekea kwenye bajeti tuone Serikali imepanga nini kwenye hiyo barabara, ahsante. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa, zoezi la upelekaji umeme kwenye Miji na maeneo yanayofanana na Vijiji bado haijakamilika kama inavyotakiwa.

Je, ni lini, Serikali itahakikisha maeneo yote yaliyoko Mijini hasa kwenye Kata za Buhongwa, Runhima na Kishili yanapata umeme uliokusudiwa kwa wakati na wananchi waweze kufaidi matunda hayo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Mabula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli zimekuwepo awamu mbili za kupeleka umeme kwenye maeneo ya Mijini yenye picha ya Vijiji ambayo tunaita miradi ya peri-urban, katika Jiji letu la Mwanza awamu ya kwanza ilifika ambayo iligusa pia, maeneo ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza. Ipo awamu ya pili ambayo ilikuja Dodoma na Mbeya na sasa iko awamu ya tatu ambayo kuna baadhi ya maeneo tayari imeshaanza kufanyika, Mkoa wa Kagera Jimbo la Bukoba Mjini likiwa ni mojawapo Geita, Mbeya tena Tanga na maeneo mengine ambayo yana uso wa Vijiji lakini yako Mjini yanaendelea kupelekewa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuahidi Mheshimiwa Mabula pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine ambao Majimbo yao yako Mjini kwamba miradi hii inaendelea kufanyika kadri ya upatikanaji wa fedha awamu kwa awamu. Pale ambapo tunapambana kuhakikisha kwamba REA III round II inakamiliishwa kwenye vijiji, vivyo hivyo ndivyo tunavyopambana kutafuta pesa kwa ajili ya kupeleka umeme katika maeneo ya Mijini lakini yenye uso wa Vijiji.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, kwamba maeneo mengi yaliyojengwa vituo vya polisi ikiwemo kituo kikuu cha polisi pale Nyegezi ambacho kitasaidia maeneo mengi sana, kwa maana ya ukanda wa kata za Buhongwa, Mkolani, Ruanima, Nyegezi, Luchelele pamoja na Mkolani yenyewe.

Je, ni lini sasa Serikali itafanya ukamilishaji wa kituo hiki?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mabula kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekeze Mkuu wa Polisi Nchini (IGP) Wambura kupitia Kamanda wake wa Mkoa wa Mwanza wapiti kituo hiki cha Nyegezi alichokieleza Mheshimiwa Mbunge kuona kiasi gani cha umaliziaji unaotakiwa kufanyika ili gharama zake ziweze kutengewa fedha na kikamilishwe ili kiweze kuwanufaisha wananchi wa maeneo yaliyotajwa.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali; naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza;

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zoezi hili la upandishaji wa madaraja kwa maeneo mengine ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Mwanza inaonekana kwa mara ya mwisho ni tangu mwaka 2020/2021, na idadi ya watumishi walio kasimiwa kupandisha madaraja hailingani na waliopandishwa mpaka sasa;

Mheshimiwa Mwenyekiti, na suala la pili, kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wa likizo kwa watumishi hasa kada ya Walimu;

Je, Wizara ina mpango ngani kuhakikisha kwamba Wizara ya Fedha sasa haitapunguza ile ceiling ya fedha za likizo zilizopo na badala yake waongeze zaidi?

Nashukuru Mheshimiwa Mwenyekiti.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na jambo la watumishi kupandishwa madaraja nimeeleza katika jibu langu la swali la msingi; kwamba Serikali imeendelea kupandisha madaraja ikiwemo utaratibu wa mserereko, ambao ndio maarufu sasa hivi ambao unaingiza kundi kubwa la wafanyakazi katika kipindi kimoja ili kuweza kuwapandisha katika madaraja stahiki. Pamoja na hilo pia nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali haina mpango wa kupunguza fedha za wafanyakazi katika masuala yanayohusu likizo kama alivyoeleza katika swali lake la pili. Nashukuru sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumuuliza swali Mheshimiwa Naibu Waziri. Barabara ya Kenyatta itokayo Mwanza Mjini kwenda Shinyanga ambayo tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na umeshakamilika, pia usanifu umekamilika. Barabara imezidi kuwa na msongamano mkubwa;

Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha barabara hii inapanuliwa kwa njia nne? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE), Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli moja ya barabara katika majiji ambayo sasa hivi ina magari mengi ni hiyo Barabara ya Kenyatta kwenda Usagara kuelekea Shinyanga. Serikali imeshafanya usanifu na sasa hivi inatafuta fedha kwa ajili ya kuijenga barabara hiyo kwa njia nne ili kupunguza changamoto kubwa ya foleni katika Jiji la Mwanza, ahsante. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa Serikali imekuwa na utaratibu wa kutenga fedha kutokana na tozo mbalimbali; ni lini sasa itaweka vipaumbele kwenye majimbo ambayo yana changamoto kubwa sana za barabara ikiwemo Jimbo la Nyamagana Jijini Mwanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inazingatia vipaumbele kulingana na mahitaji ya kila jimbo ikiwemo Jimbo la Nyamagana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, ahsante; ni lini Serikali itakuwa tayari kupeleka gari la wagonjwa Kituo cha Afya Bulale kulingana na Geografia yake ilivyo mbali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Bulale nakifahamu tulishafanya ziara pale, kiko mbali na kinahudumiwa wananchi wengi naomba Mheshimiwa Mbunge shirikiana na halmashauri kuweka kipaumbele cha kituo au hospitali ambayo tunahitaji kupata gari ili ikipatikana tupeleke hapo, lakini baadaye tutaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kupeleka magari katika kituo hicho pia.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa tayari upembuzi yakinifu unaelekea mwisho na barabara hii kwakweli ni muhimu sana kwa wanachi wa Jimbo la Nyamagana hususani takribani kata tano za Mkuyuni, Mahina, Mhandu pamoja na Butimba; sasa Serikali ipo tayari kuhakikisha kwamba baada tu ya upembuzi yakinifu barabara hii inaanza kujengwa?

Mheshimiwa Spika, pili; barabra hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais; ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kuhakikisha ahadi za Mheshimiwa Rais zinatimizwa kwa wakati? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ni kweli ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati huo akiwa ni Makamu wa Rais na sasa ni Rais na ndiyo maana barabara hii tayari tumeshaanza kutekeleza ahadi na tayari tunaifanyia usanifu ili iweze kukamilika na tuanze kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, na barabara hii kwa swali lake la pili; tunaipa uzito mkubwa sana kwa sababu ni barabara ambayo tunaamini inakuwa ndiyo barabara kama bypass kwa mtu akitokea Nyegezi kwenda Mwanza Mjini ikitokea changamoto yoyote basi hii barabara ndiyo inayoweza kutumika kwa ajili ya kuwapeleka watu katikati ya Mji wa Mwanza. Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa kuwa Serikali sasa imeamua kujenga vituo hivi vya polisi kuanzia ngazi ya kata. Ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Nyegezi kwa ajili ya Kanda ya Ukanda wa Nyegezi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Mabula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba ni nia ya Serikali kujenga vituo vya polisi, kuimarisha usalama wa raia ngazi ya kata na ni kwa msingi huo tumeweza kutoa askari kata katika kata zote nchini.

Sasa hili suala la ujenzi wa vituo ni suala la gharama na kwamba katika kipindi kifupi hatuwezi kufanya hivyo kulingana na mpango wetu wa ujenzi. Tutaanza na mikoa ambayo haina Ofisi za RPC, lakini Wilaya ambazo hazina vituo vya OCD. Kwa hiyo, vilivyo kwenye ngazi za kata tumuombe Mheshimiwa Mbunge kushirikiana na wadau waanze ujenzi ili Serikali ije isaidie kukamilisha vituo hivyo. Nashukuru.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri kwamba mradi wa umeme jazilizi kwa kiasi kikubwa sana umefanikiwa, lakini kuna changamoto za upatikanaji wa fedha ili kukamilisha maeneo mengi zikiwemo Kata za Rwanima, Mahina Fumagila pamoja na Kishiri.

Ni lini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha fedha nyingi zinapatikana ili mradi jazilizi uoneshe maana halisi ya kujaziliza kwenye maeneo ambayo hayajapata umeme mpaka leo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mabula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Mabula ananufaika na mradi unaoitwa Peri-urban ambao unapeleka umeme katika maeneo ya miji lakini yenye asili ya vijiji. Katika mwaka wa fedha unaokuja imetengwa pesa na eneo lake ni mojawapo ambalo litapelekewa umeme wa kuongezea kwenye yale maeneo ambayo bado hayajapatiwa umeme. Nimwahidi tu kwamba Serikali ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan imejikimu na kuamua kupeleka umeme katika kila eneo na pesa imetengwa ya kuanzia itapatikana katika mwaka huu wa fedha unaokuja, na muda sio mrefu ataona wakandarasi wakiwa site. Pia ziko jitihada za ziada za kuendelea kutafuta pesa kwa ajili ya kufikisha kwenye maeneo yote ambayo tunayo.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa zipo halmashauri ambazo zimefanya vizuri kwa kurejesha fedha hizo ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Mwanza. Je, Serikali ina mpango gani wa kuziongezea mkopo halmashauri hizi ili ziweze kufanya kazi hii ya kupanga, kupima na kumilikisha kwa uzuri zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama inavyofahamika Mfuko huu ni Mfuko ambao fedha zake ni fedha za kuzungushwa. Kwa maana hiyo, kwa zile halmashauri ambazo zitakuwa zimefanya vizuri kwa kufanya marejesho vizuri na ndani ya muda, maelekezo ya mwongozo tulioutoa ni kuhakikisha kwamba halmashauri hizi zinabuni tena miradi na fedha hizi zinapelekwa katika halmashauri hizo ili kuendelea kuzalisha viwanja na kutengeneza makazi kwa ajili ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba, kwa zile halmashauri ambazo zimekwishakamilisha kurejesha fedha hizo tunawakaribisha ndani ya ofisi yetu ili tuweze kuendelea kuwakopesha ili waweze kupima ardhi, kupanga na kutengeneza utaratibu mzuri kwa ajili ya makazi yaliyo bora kwa wananchi wa Tanzania kama ambavyo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kupitia Mradi huu wa Kupanga, Kupima na Kurasimisha Ardhi ya Tanzania. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa kumekuwa na utaratibu wa Serikali kufanya upembuzi yakinifu na unapokamilika barabara zinachukua muda mrefu, barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wa Wilaya ya Busega, Wilaya za Nyashimo, Ndutwa na Ngasamo na maeneo mengine kuunganisha na Mkoa wa Simiyu kwa maana ya Mkoani. Ni nini sasa kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba pindi tu upembuzi yakinifu utakapokuwa umekamilika barabara hii itajengwa? (Makofi)

Swali la pili, barabara kuu itokayo Mwanza Mjini kwenda Shinyanga kupitia maeneo ya Igogo – Mkuyuni – Buhongwa – Usagara ambayo imeshafanyiwa upembuzi yakinifu takribani miaka miwili sasa imepita, kwa kweli Mji umebanana sana. Ningependa kujua sasa kauli ya Serikali, ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha njia nne na kuondoa usumbufu uliopo sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni utaratibu wa kawaida kwamba kabla barabara haijaanza kujengwa kwa kiwango cha lami, tunatakiwa tufanye upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, hii inaisaidia Serikali kuweza kujua gharama ya hiyo barabara. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, ukishafanya usanifu inakusaidia hata kama ni wahisani ama Serikali inakuwa kwenye nafasi ya kuweza kuipangia bajeti. Kwa hiyo, kuifanyia usanifu maana yake ni mpango wa Serikali kuijenga kwa kiwango cha lami kwa sababu ni kweli hiyo barabara ni muhimu sana kwa wananchi wa Busega.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili la barabara kubwa, barabara kuu ya kutoka Mwanza – Mkuyuni – Buhongwa – Usagara ambayo inakwenda mpaka kati ya mpaka wa Mwanza na Shinyanga, barabara hii iko kwenye mpango wa kuijenga njia nne. Tumeshakamilisha usanifu. Ni mradi mkubwa na tunajua Mwanza sasa ni Jiji kubwa ambalo foleni ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali imeweka kwenye mpango barabara hii, kutafuta fedha kuijenga barabara yote kwa njia nne kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa barabara ya kutoka Mkuyuni - Kanyerere mpaka Nyangurungu – Mahina ilishafanyiwa upembuzi yakinifu na TANROADS na ulishakamilika takribani miaka miwili. Je, Serikali sasa haioni ni muhimu kuanza kuijenga barabara hii kwa kiwano cha lami yenye jumla ya kilometa 9.8?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba TANROADS ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii kutokana na maelekezo ya viongozi wa kitaifa, lakini barabara hii kwa sasa bado inaendelea kusimamiwa na wenzetu wa TAMISEMI, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tutawasiliana na wenzetu wa TAMISEMI, kwamba baada ya kufanyia usanifu kinachofuata sasa ni kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mji wa Mwanza umeendelea kukua kwa kasi na watu wameongezeka na kujenga maeneo ya pembezoni, Serikali ipo tayari sasa kufanya upya tathmini ya mawasiliano na kupeleka minara?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante, tupo tayari kufanya tathmini mpya.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ilishakuwa na makubaliano ya awali kuchukua eneo ambalo siyo zaidi ya ndani ya meta 700 kulipa fidia na sasa inaonekana itakwenda zaidi ya kata tano zikiwemo Kata za Shibula pamoja na Bulyanhulu na wakazi zaidi ya 1,400, je, Serikali haioni kuchukua eneo lote hili kwa wakati mmoja kutaathiri maisha ya baadhi ya wananchi ambao wako nje kabisa ya eneo la uwanja wa ndege?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali kwa kuanza ujenzi wa jengo la abiria, ni lini mkakati wa Serikali kuhakikisha Uwanja wa Ndege wa Mwanza na wenyewe unakuwa moja ya viwanja vya Kimataifa hapa nchini? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la pili kisha nirudi swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inatambua umuhimu wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kuufanya wa Kimataifa na tayari mambo kadhaa yameanza kufanyika. La kwanza, tuko kwenye hatua za ndani za documentation. Ili uwanja uweze kuwa wa Kimataifa, kuna taratibu za kisheria ambazo lazima zizingatiwe.

Mheshimiwa Spika, la pili, ni pamoja na kuondoa wavamizi wapatao 1,000 katika uwanja huu ili waweze kupisha kiwanja hicho kiweze kuwa salama. Pale kuna milima na maeneo mbalimbali ambayo wananchi wamevamia. Kwa hiyo, huwezi kukifanya cha kimataifa wakati huo huo usalama wa kiwanja uko mashakani.

Mheshimiwa Spika, la tatu, tunafanya kazi ya uboreshaji wa miundombinu. Kama unavyofahamu, tarehe 28 mwezi huu Waziri wetu Mheshimiwa Mbarawa alikwenda kushuhudia ujenzi wa jengo la abiria. Iko mikakati mingi, lakini nimetaja mitatu ya kuufanya uwanja huu kuwa wa kimataifa.

Mheshimiwa Spika, sasa nikirudi kwenye swali lake la kwanza, nafikiri litakuwa limeshajibiwa na hoja hii ya pili, kwa sababu hatuwezi kuacha eneo ambalo nimeshalisema pale juu, kwa sababu tu tunataka tuufanye uwanja wa kiamataifa. Kwa hiyo, lazima watu wapishe ili tuweze kuupa hadhi inayostahili, ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, umuhimu wa barabara hii ambayo inapita Mwasonge – Bulale – Nyakagwe mpaka Mkolani, inaungana moja kwa moja na Daraja la Busisi na tunafahamu liko zaidi ya 90% sasa, linaelekea kukamilika. Serikali haioni umuhimu wa kutengeneza barabara hii ili kupunguza msongamano wa njia kubwa ili hii ndiyo itumike kama njia mbadala?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi na bahati nzuri binafsi naifahamu hii barabara. Tumeomba wenzetu wa Mkoa wa Mwanza kupitia vikao vyao vya kisheria ambavyo tumevitaja, waweze kuleta maombi katika Wizara ya Ujenzi na wataalamu watakwenda kufanya tathmini. Kama itathibitika kwamba, ina vigezo Wizara haitasita kuipandisha hadhi hiyo barabara na sasa ianze kumilikiwa au kusimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, umuhimu wa barabara hii ambayo inapita Mwasonge – Bulale – Nyakagwe mpaka Mkolani, inaungana moja kwa moja na Daraja la Busisi na tunafahamu liko zaidi ya 90% sasa, linaelekea kukamilika. Serikali haioni umuhimu wa kutengeneza barabara hii ili kupunguza msongamano wa njia kubwa ili hii ndiyo itumike kama njia mbadala?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi na bahati nzuri binafsi naifahamu hii barabara. Tumeomba wenzetu wa Mkoa wa Mwanza kupitia vikao vyao vya kisheria ambavyo tumevitaja, waweze kuleta maombi katika Wizara ya Ujenzi na wataalamu watakwenda kufanya tathmini. Kama itathibitika kwamba, ina vigezo Wizara haitasita kuipandisha hadhi hiyo barabara na sasa ianze kumilikiwa au kusimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuwa Barabara ya kutoka Mkuyuni kwenda Tambuka Reli – Butimba - Nyangulugulu mpaka Mahina upembuzi wake na usanifu umeshakamilika kwa 100%, kinachosubiriwa ni kuanza kwa ujenzi wa kiwango cha lami na fedha ilishatengwa. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii kwa ajili ya kusaidia wananchi wanaotumia barabara hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, baada ya mvua kukatika, wakandarasi wataingia uwandani na barabara hiyo itaanza kujengwa. Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wako, watapata barabara hii kwa kiwango cha lami hivi karibuni baada tu ya mvua kukatika kwa kuwa wakandarasi wataingia site.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kwamba, pamoja na majibu ya Serikali kwa swali langu, lakini miundombinu yetu ya barabara imeimarika sana, hususan barabara kuu. Hizi sheria zilizotunga speed limit ya 50 na 80 kiukweli ni kama zimepitwa na wakati. Sasa hivi tuna magari yanakimbia mpaka speed 280 na yeye kama Naibu Waziri atakuwa shahidi; je, hawaoni sasa uko umuhimu wa lazima wa kubadilisha sheria ya speed 50 kwenda angalau 80 na ile ya 80 kwenda angalau mpaka 100 hadi 120. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwango vilivyopo sasa hivi vya kilometa 50 kwa saa na 80 kwa saa viliwekwa baada ya kufanya tathmini ya hali ya barabara na kupokea maoni ya wadau mbalimbali na hatimaye zikawekwa kisheria. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itafanya tathmini ya hali ya barabara ilivyo nchini na kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kabla ya kubadilisha sheria hii ya viwango vya 50 kwenda 80 na 80 kwenda 100. Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya kutoka Mkuyuni – Igelegele – Mahina – Mandu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais toka mwaka 2021. Nimekuwa nikiuliza barabara hii kila leo na leo ni mara ya sita. Mara ya mwisho Mheshimiwa Naibu Waziri alituahidi mvua zitakapokamilika barabara hii itatangazwa na kuanza kujengwa kwa sababu kila hatua imeshakamilika. Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya kuhakikisha barabara hii inaanza kujengwa mara moja na kuwapunguzia adha wananchi wa maeneo karibia kata sita za barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiiulizia sana hii barabara hapa Bungeni lakini hata huko mtaani tukikutana bado huwa anaulizia mustakabali wa ujenzi wa barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, ahadi za Viongozi Wakuu (ahadi ya Mheshimiwa Rais) aliyoitoa mwaka 2021 ni kipaumbele katika utekelezaji wa mipango ya Serikali na tayari fedha zimeshatengwa kwa ajili ya kuanza kujenga barabara hii. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kawaambie wananchi wako tunakuja kujenga barabara hii. (Makofi)