Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joseph Michael Mkundi (77 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa hii. Kwanza naitumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii, lakini nawashukuru sana wananchi wa Wilaya ya Ukerewe kwa kuniamini na kunituma niwawakilishe kwenye chombo hiki muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mchango wangu utajikita kwenye maeneo kadhaa. Nikianza na eneo la Afya; Mpango ulioletwa katika Bunge ni Mpango wa Maendeleo kwa ajili ya wananchi kwenye nchi yetu na kaulimbiu ni kutengeneza Tanzania ya Viwanda, lakini hatuwezi kutengeneza Tanzania ya Viwanda kama tutakuwa na jamii yenye afya dhaifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la Afya kwa mfano nikiongelea kwenye eneo langu la Ukerewe; Ukerewe ni kisiwa. Kwa ujumla tuna visiwa zaidi ya 30; visiwa kama 38 hivi, lakini huduma za afya kwenye eneo la Ukerewe ni mbovu sana, kiasi kwamba ikitokea dharura kwa mfano, tuna hospitali ya Wilaya pale, ina matatizo makubwa, wahudumu wachache na tukizingatia mazingira ya jiografia ile, watumishi wengi wanapangiwa kwenye kisiwa kile hawaendi.
Kwa hiyo, naomba katika mipango yenu mliangalie jambo hili na hasa watu wa Utumishi kwamba watumishi wanaopangwa kwenye maeneo ya visiwa kama Ukerewe mhakikishe kwamba wanafika kwa ajili ya kuwahudumia kwa sababu Ukerewe ni eneo muhimu kama yalivyo maeneo mengine katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu zaidi, ukizingatia kwamba ni kisiwa, tuna usafiri wa meli pale. Kutoka Ukerewe kuja Mwanza, tunatumia zaidi ya masaa matatu, ni masaa matatu kama na nusu hivi. Kwa hiyo, ikitokea dharura, mtu akipata tatizo la dharura la kiafya, kuletwa Mwanza ni tatizo kubwa sana. Wakati fulani tulileta mapendekezo ikaletwa ambulance boat, cha ajabu ambacho tulitegemea kwamba itakuwa ni speed boat, badala ya kutumia chini ya masaa matatu, boti natumia masaa manane kwa ajili ya kumsaidia mgonjwa.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Wapi na wapi? Kwa hiyo, pendekezo langu kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Ukerewe, hebu tusaidieni ambulance boat ili kusaidia huduma za kiafya kwa wananchi wa Ukerewe waweze kushiriki kwenye shughuli za maendeleo na kuimarisha uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile bado katika mgao wa watumishi kama nilivyosema ni jambo muhimu sana, watu wa utumishi hakikisheni kwamba kwenye maeneo yaliyoko pembezoni kama Ukerewe, basi watumishi wakipelekwa wanafika kwenye maeneo yale wanawasaidia wananchi wa maeneo yale waweze kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuliongelea ni suala la miundombinu. Tuna barabara inayotuunganisha na maeneo mengine kama Bunda. Tuna barabara ya Bunda, Kisorya, Nansio mpaka Ilangala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu uliowasilishwa nimeona tu eneo la Kisorya, Bunda. Sijaona mwendelezo wa kwenda Nansio, Ilangala, kitu ambacho ni muhimu sana kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Ukerewe. Kwa sababu tunapoongelea habari ya Tanzania ya Viwanda tunahitaji tujenge uchumi wa wananchi na hatuwezi kujenga uchumi wa wananchi hawa kama miundombinu ina matatizo na mojawapo katika miundombinu hiyo ni eneo la barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara hii wakati itakapokuja na Mpango, ioneshe ni mpango gani uliopo juu ya ujenzi wa barabara hii ya Bunda - Kisorya - Nansio –Ilangala. Barabara hii ijengwe kwa lami ili kuimarisha uchumi wa wananchi wa Ukerewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuliongelea ni eneo la uvuvi. Uvuvi ndicho chanzo kikubwa cha uchumi wa wananchi wa Kanda ya Ziwa na specifically eneo la Ukerewe kama Wilaya. Tunazungukwa na Visiwa na ajira kubwa kwa wananchi wa Ukerewe, ni Sekta ya Uvuvi, lakini uvuvi huu kama chanzo kikubwa cha mzunguko wa pesa na kuimarisha uchumi wa wananchi wa Ukerewe, inakabiliwa na changamoto nyingi sana kubwa; ambapo Mheshimiwa Waziri katika Mpango wako, kwa kushirikiana na Wizara inayohusika na masuala haya ya uvuvi, mwangalie namna gani mnaweza mkawasaidia wavuvi wa Ukerewe ili angalau waweze kuimarisha mazingira yao ya kiuchumi na kujenga uchumi wa Kitaifa kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wa Ukerewe wanapata shida kubwa sana, kimsingi katika eneo lote la Ziwa Victoria; wanafanya shughuli zao hawana uhakika na usalama wa maisha yao; wanafanya shughuli zao huku wanavamiwa, wananyang‟anywa rasilimali zao kwenye Ziwa Victoria; wengine wanajeruhiwa, wanapoteza maisha yao. Ni lazima Tanzania kama nchi, tufike mahali tuone umuhimu wa jambo hili, tuhakikishe usalama wa watu hawa ili waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi wakiwa wana uhakika na usalama wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, shughuli zao za uvuvi vile vile watu hawa wanapofanya shughuli zao, uvuvi unakuwa na tozo nyingi mno ambazo zinafanya hata kile wanachokipata, kisiwasaidie sana kuimarisha uchumi wao. Mvuvi mmoja anakuwa na tozo takriban 12, 13, leseni za uvuvi; mtu analipa leseni katika Wilaya moja, akienda Wilaya nyingine anatozwa tena leseni, kitu ambacho kinawaathiri sana kiuchumi. Ni lazima katika Mipango yenu mtakapokuja na Mpango wa jumla, mwangalie namna gani mnaweza mkasaidia watu hawa ili waweze kuwa imara kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Ukerewe kama visiwa, ni eneo ambalo ni very strategic tunaweza tukalitumia kwa ajili ya kuimarisha utalii. Maeneo mengine kwenye nchi nyingine wametumia visiwa kwa ajili ya kuimarisha pato la kiutalii kwenye nchi zao. Tunaweza tukaitumia Ukerewe. Kwa mfano, kuna eneo moja la Ukara kuna jiwe linacheza, ambalo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya, mnaweza kuona ni namna gani tunaweza tukatumia vyanzo kama hivi kuvutia Watalii, ikasaidia kuongeza pato la nchi yetu. Kwa hiyo, naombeni mlichukue na muweze kulifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado kuna changamoto kwenye eneo la usafiri. Kama nilivyosema, sisi tunaishi katika Visiwa, lakini tuna meli moja ya Serikali ambayo ni chakavu. Tulikuwa na meli ya MV Butiama, miaka mitano sasa haifanyi kazi. Wananchi wanasafiri kwa shida kweli kweli na wala hatuoni kama kuna utaratibu wowote au mpango wowote wa kutengeneza meli ile na kuwasaidia Wananchi wa Ukerewe.
Kwa hiyo, napenda kusikia wakati mtakapokuja na Mpango wenu, tujue kwamba ni mpango gani mlionao juu ya kuimarisha hali ya usafiri kwa wananchi wa Ukerewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuliongelea kwa sababu naona muda siyo rafiki, ni juu ya suala la umuhimu wa Halmashauri katika ujenzi wa uchumi ya nchi yetu. Halmashauri hizi kama tutazitumia na hasa kwa kuimarisha watu walioko katika Halmashauri, ni bahati mbaya sana kwamba katika nchi hii, kwa sababu tunaziita Local Government, tunahisi kwamba hata watu waliopo kule, basi ni local tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzitumie Halmashauri hizi kwa ajili ya kuimarisha uchumi wetu. Halmashauri hizi haziwezi kuwa imara kama hatutaimarisha Viongozi wa Serikali za Mitaa. Kwa sababu tunaongea habari ya kujenga uchumi, lakini tunapojenga viwanda, tunaimarisha mazingira, kuna watu watahitaji kusimamia shughuli kule chini. Kuna Wenyeviti wa Viijiji, Wenyeviti wa Vitongoji, tuwaimarishe ili waweze kusaidia kujenga uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naomba kuwasilisha.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na shukrani kwa kuingiza katika mpango
(a) Ukarabati wa meli ya MV. Butiama; na
(b) Ujenzi wa barabara ya Bunda-Kisovya-Nansio.
Mheshimiwa Naibu Spika, Naomba yafuatayo yawekwe katika Mpango:-
Kwanza, Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi katika Kisiwa cha Ukerewe; jambo litakalowasaidia vijana kupata msingi wa kujiajiri na kupunguza utegemezi wao katika Ziwa Victoria kwenye shughuli za uvuvi na kwa sababu hawana uwezeshwaji, wanajiingiza katika uvuvi haramu.
Pili, ujenzi wa Daraja la kuunganisha Kisorya (Jimbo la Mwibara) na Lugezi (Wilaya ya Ukerewe) ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano ya kijamii na kiuchumi na hivyo kuimarisha hali ya maisha ya wananchi wa Kisiwa cha Ukerewe. Hivyo Daraja hilo nashauri liwekwe katika Mpango.
Tatu, utafiti wa udongo katika Kisiwa cha Ukerewe na maeneo mengine ambayo udongo umechoka, itasaidia kupunguza upungufu wa chakula kwani utafiti utasaidia kujua aina ya mazao tutakayopaswa kulima kulingana na aina ya udongo kulingana na utafiti.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, mabadiliko ya vyeo yasiyoendana na mabadiliko ya mishahara. Kwa mfano, waliokuwa Nursing Officers waliambiwa kuwa ili waendelee kuwa na vyeo hivyo basi wanatakiwa kuwa na degree, lakini hata baada ya kwenda shule na kuwa na kiwango hicho cha elimu bado mishahara yao imebaki vile vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni mafao ya kustaafu kwa Watumishi waliohamishwa kutoka Serikali Kuu (RDD) na kupelekwa Halmshauri (W). Mfano, Marcela Ndagabwene aliajiriwa 1986 hadi 1992 (RDD), 1993 hadi 2011 (DED). lakini baada ya kustaafu mwaka 2011 amelipwa sh. 1,915,311.20. Pia Ndugu Florida Mhate ameajiriwa mwaka 1979 na kustaafu mwaka 2010 na amelipwa sh. 1,445,569,28
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba msaada wako kwani aina ya Watumishi hawa ni wengi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya A-level kisiwani Ukerewe; Wilaya ya Ukerewe ambayo inaundwa na Visiwa na kwa maana hiyo ki-jiografia iko vibaya lakini tayari Wilaya ina shule za sekondari za Serikali 22 na za binafsi 2. Lakini pamoja na historia ya Wilaya hii kielimu kuwa nzuri hasa kwa kuzalisha vipaji vingi bado hakuna shule ya kidato cha tano na kidato cha sita. Tayari Halmashauri imeandaa shule ya Bukongo sekondari na Pius Msekwa Sekondari kuzipandisha kuwa za high school na tayari kibali kimepatikana. Ninashauri Wizara itoe ushirikiano wa kutosha na kufanikisha uanzishaji wa shule hizi ili kunusuru maisha ya vijana wengi ambao wanamaliza kidato cha Nne na kukosa nafasi ya kuendelea na kidato cha Tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, posho ya mazingira magumu Ukerewe; kutokana na mazingira ya kijiografia kuwa magumu katika Visiwa vya Ukerewe, walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana na wakati mwingine wanapopangiwa kuja Ukerewe kwa mara ya kwanza, Serikali haitoi kwa wakati pesa za kujikimu hivyo kuwapa shida sana walimu wetu. Ninashauri Serikali kupitia Wizara hii itoe kwa wakati pesa za nauli na kujikimu kwa walimu wanaopangiwa vituo kwa mara ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, itolewe posho ya mazingira magumu kwa watumishi hasa walimu wanaofanya kazi katika Visiwa vya Ukerewe ili iwape motisha katika kukubaliana na changamoto zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upandishaji wa madaraja; Kumekuwa na malalamiko mengi sana toka kwa walimu yanayotokana na ucheleweshaji wa upandishaji madaraja sambamba na mishahara. Ushauri wangu ni kwamba Wizara ilisimamie jambo hili ili madaraja na mishahara vipandishwe kwa wakati kwa walimu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wa walimu kiutumishi; Serikali kupitia Wizara ya Elimu iangalie upya namna ya muundo wa utumishi kwa walimu. Hali iliyopo sasa kwa walimu kusimamiwa na zaidi ya Wizara moja ni tatizo kwa watu hawa. Hivyo nashauri walimu wawe chini ya usimamizi wa Wizara moja tu badala ya hali ilivyo sasa ili kuongeza ufanisi wa kada hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukerewe kama sehemu ya maeneo yanayozalisha samaki kwa wingi panahitajika kiwanda cha kusindika samaki. Hivyo tunaomba ushawishi wako kwa wawekezaji ili wajenge viwanda vya kusindika/kuchakata samaki Kisiwani Ukerewe kitu kitakachosaidia upatikanaji wa ajira na hivyo uwezo wa kununua kwa walaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa fursa hii, kwanza kabisa nitumie fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kunipa nafasi hii ya kutoa mchango wangu, lakini nitumie fursa hii vile vile kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Manaibu wake na watendaji kwa uwasilishwaji wao bila kusahau Kamati ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa na mchango kwenye maeneo kama mawili, kama muda utaruhusu basi nitaongeza eneo lingine moja. Eneo la kwanza ni juu ya flow ya pesa kwenye halmashauri zetu, dhamira ya uundwaji wa Serikali za Mitaa ni kurahisisha au kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia wananchi katika mazingira yaliyo mazuri na wapate huduma hizi katika mazingira yaliyo safi.

Mheshimiwa Spika, na pale ambapo halmashauri hizi zinaanzisha miradi, inatakiwa fedha ziende miradi ikamilike na iweze kuwa na tija ile thamani ya fedha iweze kuonekana. Bahati mbaya kumekuwa na shida kwa namna fulani kwenye flow ya pesa kwenda kwenye halmashauri zetu, matokeo yake ni kwamba miradi ama haikamili au wakati mwingine inakamilika lakini haiwezi kufikia thamani ile ambayo inakuwa imetarajiwa ili kuweza kuwasaidia wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, niki-cite kwa mfano taarifa ya CAG ya Mwaka 2019/2020 kwa mfano, utaona kwamba CAG katoa mfano kwenye mwaka huo kuna karibu bilioni 184 zilipelekwa kwa ajili ya miradi, miradi hii haijakamilika, matokeo yake nini, ni kwamba kile kilicho tarajiwa kwa ajili ya wananchi wale, ili huduma iweze kuwafikia haikuweza kuwafikia kwasababu miradi ile haijakamilika.

Mheshimiwa Spika, na hili linatokea kwasababu gani, inawezekana watumishi tulionao hawasimamii vizuri miradi ile ikaweza kukamilika, au fedha hazijaweza kwenda kama ambavyo ilitarajiwa ili thamani ile iweze kuonekana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe tu kama ushauri, Serikali ihakikishe kwamba miradi inapokuwa inabuniwa kwenye halmashauri zetu basi Serikali ihakikishe fedha zinakwenda kama zilivyotarajiwa ili yale tuliyotarajia kama manufaa kwa wananchi wetu, yaweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna wakati mwingine miradi inakamilika lakini haitumiki, niki-cite kwenye taarifa ya CAG, vile vile, utaona kwamba CAG anasema kwenye Mwaka 2019/2020, kuna bilioni 18 zimepelekwa kwenye miradi ya maendeleo, miradi imekamilika lakini haitumiki.

Mheshimiwa Spika, tafsiri yake ni kwamba ama kuna shida kwenye ushirikishwaji wa wananchi, matokeo yake sasa miradi imebuniwa lakini siyo kwa manufaa ya wananchi na hili linatokea wakati mwingine ushirikishwaji unakuwa siyo mzuri kwasababu kuna tatizo kwenye uwakilishwi wetu.

Mheshimiwa Spika, asubuhi kuna mchangiaji mmoja ameonyesha umuhimu wa kuboreshwa kwa maslahi ya Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Vitongoji.

Mheshimiwa Spika, ni jambo la msingi sana, kwasababu miradi yetu inayotekelezwa kwenye halmashauri zetu wasimamizi wakuu ni Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji na Waheshimiwa Madiwani, lakini maslahi yao ni duni sana! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe sana Serikali iliangalie jambo hili iweze kuboresha maslahi ya wawakilishi wetu hawa ili angalau waweze kusimamia shughuli hizi za maendeleo katika kiwango kilicho kizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili ambalo nilitaka nichangie ni kwenye eneo la TARURA, wengi wamesema juu ya TARURA na kupitia michango mbalimbali tumesema juu ya umuhimu wa kuboresha TARURA. TARURA mpaka inaanzishwa ilikuwa na umuhimu wake na ina majukumu mazito sana kwa ajili ya kuboresha miundombinu kwa ajili ya watu wetu kwasababu barabara zinazohudumiwa na TARURA nyingi ni zile barabara ambazo wananchi wetu kwa wingi wao wanatumia kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni muhimu sana TARURA ikaangaliwa kama ambavyo tulivyokuwa tunapendekeza, na kwangu mimi ningependekeza maeneo mawili ambayo ni muhimu sana yaangaliwe kwenye eneo la TARURA.

Mheshimiwa Spika, la kwanza ni muundo wake, ilivyo hivi sasa TARURA menejiment ya TARURA na hasa kwenye eneo la bajeti linasimamiwa zaidi na uongozi wa mkoa, lakini huku wilayani ambako kuna watu ambao wanajuwa kwa uhalisia matatizo na changamoto za barabara zilizoko kwenye maeneo yao, hawana nguvu yoyote ya kibajeti, kiasi kwamba wanashindwa kushughulikia matatizo madogo madogo yaliyoko kwenye maeneo yao ambayo yangewasababisha sasa waweze kuondoa hizi changamoto za barabara na hatimaye ziweze kuwasaidia watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe Serikali iangalie marekebisho ya muundo, ili angalau Mameneja wa TARURA kwenye wilaya nao wawe na nguvu ya kibajeti, jambo ambalo litawasaidia angalau kuweza kushughulikia matatizo madogo madogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile, suala lingine ni ambalo tumelizungumza mara kwa mara kusaidia uwezeshaji kwa TARURA, fedha wanazozipata kimsingi ni ndogo sana, haziwezi kuwapa uwezo wa kushughulikia matatizo ya barabara zilizoko kwenye maeneo yetu. Kwa hiyo, ile fomula kama itaweza kubadilishwa, itasaidia sana barabara zetu ziweze kuwa bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la Ukerewe kuna changamoto kadhaa na niombe Mheshimiwa Waziri, tumeleta mara kadhaa karibu miaka mitatu mfululizo tunaleta ombi kwenu, mtusaidie hasa hapa pale Ukerewe, angalau mtupe kilometa moja mbili za lami ili tuweze kuchochea mzunguko wa kiuchumi kwa wananchi wa Ukerewe, jambo ambalo litatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vile vile kwenye eneo la Ukerewe, kuna eneo moja linaitwa Namakwekwe, kuna eneo ambalo kuna mto ambao nyakati za mvua watu hawapiti na inasimamisha hata shughuli za kiuchumi na hata watoto hawawezi kwenda shule, kwenda upande wa pili eneo la Mibungu. Mtusaidie Mheshimiwa Waziri, angalau tuweze kujengewa daraja pale kuweza kuunganisha eneo hili ili wananchi waweze kufanya shughuli zao vizuri.

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Waziri nikumbushe tu ahadi wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyokuja Ukerewe, aliahidi kupitia maelezo tuliotoa lakini na changamoto alizoziona kutujengea kituo Kituo cha Afya kwenye Kisiwa Ilungwa, lakini vile vile kutujengea zahanati kwenye Kisiwa cha Ghana, mtusaidie sana ili anghalau visiwa hivi viweze kupata huduma nzuri za kiafya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo, kuna mradi wa barabara mradi wa Tanzania Strategic Cities Projects, ambao ulikuwa unahudumia barabara kwenye miji, mradi huu sasa umekwisha kamilika na tumeanza mradi mwingine wa Tanzania Cities Transforming Infrastructure Competitiveness yaani TAIC ambao utasaidia miji 40 kujengewa barabara za mawe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali, kupitia mradi huu na barabara hizi za mawe zikianza kujengwa, maeneo mengi kama Ukerewe tuna fursa ya kutumia mawe kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizi, lakini bahati mbaya na barabara hizi kwasababu zinafadhiliwa na Benki ya Dunia, kuna kikwazo kimoja ambacho kinafanya kama zinafanyika, basi watu wetu hawapati fursa ya kunufaika na barabara hizi. Sasa niombe Serikali, kwasababu kuna ile Sera ya Ujenzi ya Mwaka 2003, hebu Serikali muone kama mnaweza kuifanyia mabadiliko ili angalau kiwekwe kipengele kinachoweza kuruhusu matumizi ya nguvu kazi (labour based), hili litasaidia sana watu wetu angalau kuweza kunufaika na barabara hizi kwa kupata ajira, kwa sababu shughuli hizi za kuponda mawe kufanya nini, kupanga yale mawe barabarani itasaidia sana kuchochea uchumi wa watu wetu. Kwasababu likifanyika hili ni jambo jema sana na watu wetu ndiyo watakao nufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hizi barabara ni nzuri ukilinganisha na lami kwa mfano kwa tathimini, ujenzi wa barabara za mawe gharama yake ni karibu robo ya barabara kilomita moja ya barabara ya mawe, ni karibu robo ya barabara ya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo, angalau ikifanyika kama nilivyopendekeza, itasaidia sana kuchochea uchumi wa watu wetu kwasababu watu wetu angalau hasa vijana wataweza kunufaifa kwa kupata ajira ndogo ndogo katika kufanya shughuli kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine la mwisho ambalo nilitaka nichangie ni juu ya upungufu wa watumishi kwenye halmashauri zetu. Wamesema wachangiaji waliotangulia, kwenye maeneo tunayotoka hasa maeneo ya pembezoni kama ilivyo visiwa vya Ukerewe kwasababu ya jiografia yetu mara nyingi watumishi wanapopangwa kwenda kwenye maeneo yale, wanafika wanaripoti na kuondoka! Niombe wizara, kwa changamoto kama hizi, tuone namna ambayo tunaweza tukatoa hata posho ya mazingira magumu. Ili angalau watumishi wetu wanapopangiwa kwenye maeneo haya, waweze basi kukaa na kuwahudumia wananchi wetu, angalau wananchi waweze kufaidika na Serikali yao kupata huduma zile zinazostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye maeneo kwa mfano Ukerewe mwaka juzi tumepambana sana kuhamasisha wananchi tukajenga madarasa zaidi ya 400; tumejenga maboma kwa ajili ya zahanati yote haya yamekamilika tunahitaji msaada angalau muweze kutushika mkono tumalizie kazi hizi. Pamoja na fedha mlizozitoa kwenye bajeti hii kwa ajili ya kusaidia ukamilishaji wa maboma Ukerewe kama specific area tunaomba mtusaidie angalau haya maboma tuliyoyajenga kwa kushirikikana na wananchi zaidi ya 400 tuweze kuyaezeka. Jambo hili litasaidia wananchi wetu kupata moyo na kuona Serikali inawajali na wakati mwingine hata ukiwahitaji waweze kushiriki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa fursa hii, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuna umuhimu mkubwa wa Kiwanda cha Samaki kujengwa Wilayani Ukerewe ili kutumia malighafi (samaki) wanaozalishwa kwa wingi Wilayani Ukerewe. Kwa kufanya hivyo itasaidia matumizi sahihi na yenye ufanisi ya rasilimali zinazozalishwa(samaki) na itazalisha ajira kwa watu wetu na hivyo kukuza uchumi wao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, kuna waliokuwa watumishi Serikalini mfano Magereza baada ya kustaafu wanapata malipo kidogo sana ya kila mwezi jambo ambalo linapelekea wastaafu hawa kuishi maisha magumu sana.

Mheshimiwa Spika, ombi lwangi; Serikali ipitie upya mafao ya wastaafu wetu ili wasidhalilike sana baada ya kustaafu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, mradi wa barabara wa Nyamuswa – Bunda - Kisorya itambulike kama Nyamuswa - Bunda - Kisorya - Nansio kama ilivyokuwa inatambulika toka awali (sehemu ya Kisorya - Nansio ikiwa (Lot No.3). Kutoitambua kwa jina hilo kunahamisha na kupotosha jina la mradi.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Lugezi - Bukongo - Masonga (sehemu ya Bulamba - Murutunguru - Masonga kilometa 32) ijengwe kwa kiwango cha lami kuepusha gharama kubwa zinazotumika kwa matengenezo ya mara kwa mara kutokana na aina ya udongo uliopo maeneo yale.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa hii. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia bajeti, natumia fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Ukerewe kwa kunituma katika chombo hiki muhimu. Mchango wangu utajikita kwenye maeneo matatu yote lakini kwa mazingira tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na eneo la kilimo, wamesema wachangiaji wengi hapa kwamba kwa mazingira tuliyonayo na kwa kuamini kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi hii, ni muhimu sana tukahusisha utafiti halafu ndiyo tukapanga mipango yetu ili kuboresha mazingira ya kilimo na kwa maana hiyo hali ya uchumi wa wananchi wetu.
Hata kama tutafanya research, tukaandaa mipango, bila kuitekeleza bado haitakuwa na msaada mkubwa sana kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali, wakati tunapokuwa tunapanga mipango hususan kupitia Bunge hili, basi tuitekeleze kwa namna tunavyoipanga hasa kama Serikali itatoa pesa kwa kiwango kile ambacho Bunge linakuwa limepitisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina changamoto nyingi sana; kwa mfano, kwenye eneo la Ukerewe bahati mbaya sasa ardhi ya Ukerewe imechoka na Serikali mwaka juzi iliahidi kwamba ingeleta watu kwa ajili ya kufanya research ili sasa ione namna gani itafanya; kwa sababu Ukerewe tulitegemea zaidi zao la muhogo, lakini zao lile sasa linakumbwa na matatizo mengi likiambatana na kuchoka kwa ardhi. Mpaka leo hakuna utafiti wowote uliofanyika kwenye eneo lile ili kuwezesha wananchi wa Ukerewe ambao sasa imekuwa kila wakati wanakabiliana na upungufu wa chakula, waweze kukabiliana na jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati wa ku-wind up labda Waziri angeweza kusema ni wapi ambapo amefikia juu ya jambo hili. Bahati mbaya zaidi, mwaka 2015 ilikuwa Ukerewe wapate mgao wa voucher za pembejeo; na kimsingi kwa mazingira ya mvua, ilitakiwa at least mwezi Septemba voucher hizi ziwe zimekuja ili wakulima wapate pembejeo na vifaa vilivyokuwa vinatakiwa, lakini mpaka mwezi Novemba vitu hivyo havikuwa vimetolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana ni kwamba wananchi wali-reserve baadhi ya maeneo ili kwamba baada ya kupata zile pembejeo waweze kutumia maeneo hayo. Hawakuweza kuyatumia na mpaka sasa maeneo yale yamebaki bila kutumika pamoja na uhaba wa ardhi uliopo kwenye eneo la Ukerewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la voucher za pembejeo, wamesema Wabunge wengi hapa, ni jambo muhimu sana na kwa eneo kama Ukerewe ardhi ni chache, ardhi imechoka, kuna tatizo kubwa sana la upungufu wa chakula, ni lazima Serikali itilie mkazo na ione umuhimu wa jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna wataalamu wa kilimo kwenye maeneo yetu, lakini bahati mbaya sana kwenye bajeti tunazo zipanga Serikalini pesa haitoki kushuka kwenye maeneo yale kuweza kusaidia wataalam kufanya na kutekeleza majukumu yao. Tumetoa miongozo, kwa mfano, Serikali imetoa miongozo kwamba wataalam waende kwenye maeneo ya vijiji kutembelea wakulima, lakini pesa zile zinazoweza kuwawezesha wataalam hao kwenda kwenye maeneo ya wakulima hazitoki. Tuchukulie kwa mfano Ukerewe, Idara ya Kilimo OC kwa mara ya mwisho wamepata mwezi Februari mwaka 2015. Wakati huo huo wanawaelekeza wataalam hao waende vijijini kusisitiza mambo ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Serikali iwe serious na jambo hili ili kwamba wakati tunapoandaa mipango, tunapokuwa tunatoa maelekezo ya kutekeleza sera, basi tupeleke rasilimali fedha ili wataalam wetu wafanye majukumu yao kwa mujibu wa maelekezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Ukerewe pale ili kukabiliana na hili tatizo la njaa tuna mabonde pale ambayo tungeweza kuyatumia kwa ajili ya kilimo cha mpunga. Tuna bonde kwa mfano la Mihogwezi, tuna bonde la Muhande, tuna bonde Ilangala labda Mheshimiwa Waziri atakapokuja wakati ana-wind up atoe maelezo kwamba ni wapi kwa mfano kuna bonde la Mihogwezi. Tume-invest pale!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imewekeza pesa zaidi ya shilingi milioni 700, lakini sasa bonde lile liko pale pamoja na pesa zile tume-dump pale, liko vilevile. Sasa Serikali ina mpango gani na bonde hili, pamoja na kutumia mabonde mengine haya ili kwamba tuweze kukabiliana na tatizo la upungufu wa chakula linaloikabili Ukerewe lakini pamoja na maeneo mengine yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la mifugo, wamesema wachangiaji wengi hapa lakini mimi nitaongelea kwenye eneo moja tu. Kuna mchangiaji mmoja amesema tuna chuo ambacho kinafundisha wataalam wetu lakini wataalam hawa hatuwatumii, wako mitaani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukerewe tuna Kata 25, lakini tuna Maafisa Ugani saba pekee. Kwa hiyo, unaweza kuona ni upungufu kiasi gani uliyopo kwa wataalam hawa ambao ni muhimu sana wa ajili ya kuwasaidia wakulima wetu kufanya shughuli hizi katika kiwango kizuri kikawa na tija na kikasaidia jamii kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuongelea ni eneo la uvuvi. Namshukuru Mheshimiwa Waziri, mara kadhaa tumeonana katika kujadiliana juu ya suala hili la uvuvi na ninashukuru kwa ushikiano wako, lakini bado kuna changamoto ambazo Serikali ni muhimu sana ikazifanyia kazi. Baadhi umezisema kwenye hotuba yako, kwa mfano, suala la tozo nyingi ambazo wavuvi hawa wanakabiliana nazo, ni muhimu sana sheria hii ikaangaliwa upya tozo hizi zikapunguzwa ili wavuvi wafanye shughuli zao kwa tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile sheria inayoelekeza aina ya nyavu ambazo zinatumika kwenye Ziwa Victoria, ni jambo muhimu sana. Kwa mfano, kwa sheria ile ya mwaka 1983 kama sikosei, inaelekeza uvuvi wa dagaa kwa mfano kwenye Ziwa Victoria kutumia nyavu zenye matundu ya milimita 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kupata dagaa wa milimita 10 kwenye Ziwa Victoria. Ile research inawezekana ilifanyika kwa Ziwa Tanganyika, lakini dagaa walioko katika Ziwa Victoria hawakui zaidi ya kiwango kile walichopo ambacho ni kama milimita sita tu. Bahati nzuri ni kwamba dagaa wanavuliwa kwenye kina kirefu, siyo kwa kuvutwa, ni kwa kuchotwa.
Kwa hiyo, huwezi kutegemea kwamba kwa sheria ile mvuvi katika Ziwa Victoria atapata chochote. Ni lazima sheria ile iangaliwe ifanyiwe marekebisho iendane na mazingira halisi ya Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni muhimu sana ni suala la usalama kwenye Ziwa Victoria. Watu wameimba sana, wamepiga kelele sana, naomba tafadhali Mheshimiwa Waziri alitilie mkazo, ashirikiane na Wizara nyingine zinazohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wanataabika sana kwenye Ziwa Victoria. Imagine watu wanafanya shughuli zao kwenye Ziwa Victoria, wamechukua rasilimali zao wakawekeza pale, watu wachache wanaenda wanawanyang‟anya rasilimali, wanawakata mapanga, wanawaua, wananyang‟anya mali zao, siyo jambo jema kuendelea kwenye nchi kama hii ya kwetu. Lazima tuwe serious na jambo hili, tulikomeshe kwa gharama yoyote ile, watu wetu wafanye shughuli zao za kiuchumi wakiwa na amani wapate rasilimali zile wanazozitarajia, waboreshe maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye maeneo yanayotoa madini, kumekuwa na habari ya mrahaba. Hivi katika maeneo yanayozungukwa na ziwa ambapo samaki wanatoka kwenda kwenye viwanda vya kuchakata samaki, hakuna namna yoyote ambayo katika mapato yanayotokana na ziwa, asilimia fulani ya mapato yale yakarudi kwenye maeneo yale kusaidia uharibifu wa mazingira kwenye maeneo yale? Kwa sababu kutokana na shughuli za uvuvi, mazingira yanaharibika sana, jamii inaharibika kitabia, kwa mfano, watoto wanashindwa kwenda shule na matatizo mengine kama hayo. (Makofi)
Kwa hiyo, iangaliwe namna ambayo wakati shughuli za uvuvi zinapofanyika, samaki wanapopelekwa viwandani, basi viwanda vile angalau vitozwe asilimia fulani ambayo itarudi kwenye maeneo yale kuweza kusaidia jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa hii ya kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii. Mchango wangu utakuwa kwenye maeneo kama matatu hivi. Nilitamani niongelee suala la reli lakini watu wengi wameliongelea, kwa hiyo sitaelekea huko, nitaelekea kwenye maeneo yanayohusu Jimbo langu la Ukerewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wengi mnavyojua Ukerewe inaundwa na visiwa zaidi ya 30. Mategemeo makubwa ya wananchi zaidi ya 300,000 wa Ukerewe kuunganishwa na mji wa Mwanza na maeneo mengine ni kupitia meli. Bahati mbaya usafiri wa meli kutoka Mwanza kwenda Ukerewe umekuwa na matatizo makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri nimeona hapa kuna pesa zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya meli ya MV Butiama. Suala la MV Butiama limekuwa ni wimbo wa muda mrefu sana, miaka takribani mitano usafiri ni wa shida kweli kweli kwenye eneo lile. Sijui kama Serikali inafurahi muda wote iwe inatoa rambirambi kwenye mazingira kama haya, si jambo jema sana. Yametokea maafa pale Zanzibar, yametokea maafa ya MV Bukoba, sitamani sana jambo kama lile litokee kwenye eneo la Ukerewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna meli moja MV Clarias, napenda kuwapongeza kampuni binafsi ya Nyehunge, wanatoa huduma ya usafiri pale, lakini meli zile zinazotoa usafiri bado hazitoshi, wananchi wanataabika sana kwa usafiri wa meli. Kama kwenye bajeti mmetenga hii pesa kwa ajili ya kutengeneza hii meli ya MV Butiama, itengenezwe iweze kuhudumia wananchi wale. Si hiyo tu, hata meli iliyopo sasa hivi ya MV Clarias haiwezi kumudu muda mrefu, imekuwa ni meli ya muda mrefu sana kila wakati inasumbua, inaharibika. Kwa hiyo, pendekezo langu, pamoja na kutengwa kwenye bajeti shilingi bilioni tatu na point kwa ajili ya marekebisho ya MV Butiama, Wizara iangalie uwezekano wa kutengeneza meli nyingine mbadala wa MV Clarias ambayo ni ya muda mrefu na imechoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niombe Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuangalia suala la uwekezaji katika visiwa hivi. Ukerewe ni eneo ambalo linaweza kutumika kwa shughuli za utalii, naomba kama kunaweza kufanyika ushawishi ufanyike au Wizara yenyewe itengeneze speed boat kwa ajili ya huduma za usafiri kuunganisha Mwanza na visiwa vya Ukerewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuongelea ni eneo la vivuko. Kama nilivyosema Ukerewe inaundwa na visiwa na kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeonesha kwa mwaka 2015/2016 kuna vivuko kadhaa ambavyo vimefanyiwa marekebisho kikiwemo kivuko cha MV Nyerere. Sawa, lakini kuna maeneo ambayo wananchi wanataabika sana kama kwenye visiwa vya Ilugwa, Izinga na maeneo mengine, niombe Wizara itengeneze vivuko vingine kwa ajili ya kusaidia wananchi wa maeneo yale ambao wanataabika sana na usafiri kutoka kwenye visiwa vile wanavyoishi kuja kwenye kisiwa kikubwa cha Ukerewe na hatimaye kutafuta mazingira ya kusafiri kwenda Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hiki kivuko cha MV Nyerere ambacho kinafanya kazi kwenye eneo la Bugolola na Bwisa kisiwani Ukala, hivi kunakuwa na tatizo gani, kwa mfano Wizara ndiyo inayohusika na vivuko hivi na meli kutoka Mwanza kuja Nansio, ni kwa nini kusiwe na matching ya ratiba kwamba wasafiri wanaotoka Mwanza waweze kuingia Nansio lakini wakawahi vilevile usafiri wa Bugolola kwenda Kisiwa cha Ukala? Sasa hivi wananchi wanataabika sana, wanatoka Mwanza wanakaa Nansio pale zaidi ya saa sita wakisubiri ratiba ya ferry ya kutoka Bugolola kwenda Ukala.
Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri, inawezekana akatoa maelezo ni kitu gani kinaweza kufanyika lakini litakuwa jambo jema sana kwa maslahi ya wananchi wa Ukerewe, hususan kwenye visiwa vya Ukala ratiba hii itawekwa sawa angalau iweze kuwiana na ratiba ya kutoka Mwanza kwenda Ukerewe.
Vilevile uangaliwe uwezekano kutengeneza vivuko vingine kwa ajili ya kusaidia wananchi kwenye visiwa vidogo vidogo vinavyounganisha Ukerewe na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la tatu ambalo nilitaka nigusie ni suala la barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo sera ya Serikali hii ya kuunganisha mikoa yote ya Tanzania Bara kwa barabara za lami, kuna barabara ya kutoka Bunda – Kisolya - Nansio ambayo kimsingi inaunganisha mkoa wa Mara na Mwanza kupitia Ukerewe. Kwenye hotuba inaonekana kuna mpango wa kuendelea kujenga kati ya Bunda - Kisolya, lakini kuna kipande hapa cha kilometa 11 kutoka Lugezi kufika Nansio, ni kwa nini kipande hiki kisiunganishwe mradi huu ukakamilika wote kwa pamoja? Ni kilometa chache sana hizi, kwamba sehemu moja itengenezwa halafu hizi kilometa 11 zibaki zitafutiwe fedha nyingine au mradi mwingine ndipo ije ikamilike na barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Ukerewe. Tunasema tunatengeza Tanzania ya viwanda, ni muhimu basi tujenge mazingira ya kiuchumi ya wananchi wetu. Kwa wananchi wa Ukerewe, kama barabara hii itatengenezwa kwa kiwango cha lami itasaidia sana mawasiliano na hasa kiuchumi kati ya wananchi wa Ukerewe, Bunda na Mwanza Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niombe vilevile Wizara hii, ninaamini si eneo la Ukerewe tu, maeneo mengi barabara nyingi zimeharibika. Sasa niombe fedha za Mfuko wa Barabara ziwe zinatolewa mapema na kwa kiwango kile ambacho kinaweza kikasaidia ili Halmashauri zetu ziweze kurekebisha barabara zile zinazokuwa zimeharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kutokana na barabara zetu kutokuwa katika hali nzuri, Halmashauri ya Ukerewe tuliomba kununuliwa greda kwa ajili ya kutengeneza barabara na Wizara ikale greda kwenye Halmashauri ya Ukerewe. Niombe Mheshimiwa Waziri kama anaweza kunisaidia hili, lile greda Halmashauri ya Ukerewe imekuwa haina mamlaka nalo sana kiasi kwamba ikitaka kulitumia liweze kurekebisha barabara za Wilayani Ukerewe inakuwa ni shida kweli kweli kulipata wakati kimsingi Halmashauri hii ndiyo iliyo-process mpaka greda hilo likapatikana. Ni kwa nini sasa kama Wizara msitoe mamlaka, kwa sababu Halmashauri hii ndiyo iliyoanzisha mchakato mpaka greda hili kununuliwa, kwa nini lisikabidhiwe kwenye Halmashauri ile? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jiografia ya Ukerewe ni ngumu sana, msiifananishe na maeneo mengine. Mkifanya hivi mtakuwa mmelisaidia sana eneo la Ukerewe kuboresha barabara zake na inawezekana ikapunguza gharama nyingini ambazo zingekuja kwenu Wizarani. Kwa hiyo, niwashauri kama Wizara, likabidhini greda hili kwenye Halmashauri hii ilisimamie. Kama kuna masharti na taratibu nyingine muhimu basi waelekezwe lakini greda lile liwekwe pale Halmashauri lifanye shughuli za kuboresha barabara za Ukerewe hatimaye basi mazingira ya Ukerewe yawe bora angalau ukilinganisha na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikiendelea kusisitiza, niombe tafadhali, kwenye hii barabara ya Bunda – Kisolya – Nansio, haina sababu kilometa 11 hizi kuziacha, ziunganisheni. Pia kulikuwa na mpango wa kujenga daraja kati ya Lugezi - Kisolya, sijui imefikia wapi Mheshimiwa Waziri nitaomba maelezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa maono yake, kwa uongozi wake thabiti na imara sana na kwa namna anavyowatumikia wananchio wa Taifa hili. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake wote kwa namna walivyobeba maono ya Mheshimiwa Rais na kuwasilisha bajeti katika Bunge lako Tukufu, bajeti ambayo ni moja kati ya bajeti bora ambazo nimeshuhudia nikiwa Bungeni hapa. Jukumu letu ni kutoa ushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitachangia kwenye maeneo kama manne iwapo muda utaniruhusu na kwa kuanzia nitaanza na eneo la elimu. Kwenye hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 51, ameongelea maamuzi ya Serikali kuanzisha dirisha kupitia TASAF, kusaidia watoto ambao hawana uwezo wa kulipa ada. Ni jambo jema, lakini kwenye eneo hili ningeshauri watu wanaonufaika na Mfuko wa TASAF haujajumuisha wale wote ambao wangestahili kufaidika na Mfuko ule. Kwa mfano, kuna viongozi wa Serikali za Vijiji, kuna Viongozi wa Vyama vya Siasa, haijalishi kama kiuchumi hayuko vizuri, lakini kwa sifa hiyo tu ya kuwa kiongozi hanufaiki na Mfuko wa TASAF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo tafsiri yake ni kwamba, watoto ambao kutokana na baba yao kutokuwa na uwezo kiuchumi hawawezi kunufaika na Mfuko huu. Kwa hiyo, ningeshauri kwenye eneo hili iangaliwe namna nyingine bora ambayo itabainisha watoto ambao watanufaika na mfuko huu na dirisha hili la TASAF ambapo kwa kuanzia Mheshimiwa Waziri amesema unaweka bilioni nane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la elimu vilevile niipongeze Serikali kwa kufuta ada ya kidato cha tano na cha sita. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi huu, lakini niombe pamoja na kuondoa ada bado sehemu kubwa ya wanafunzi wetu na vijana wetu wanaathirika sana na michango mbalimbali. Kwa hiyo, ningeshauri Serikali iangalie namna bora ya kudhibiti michango hii na kuwe na chombo kama ni Wizara ya Elimu na chombo kingine chochote ili kuainisha ni michango ipi ambayo itapaswa kutozwa kwenye shule zetu, isiwe kikwazo kwa watoto wanaoenda kupata elimu kupata yale manufaa ya kufuta ada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mipango yetu, sera zetu zinapaswa kujibu matatizo ya vijana wa Taifa hili, vilevile kwa dhamira hii njema ya kufuta ada ya kidato cha tano na cha sita, lakini na kuweka dirisha hili kupitia TASAF, bado kuna umuhimu wa Serikali kuona haja ya kugharamia ada za vijana wanaoingia kwenye vyuo vya kati, Vyuo vya VETA, tunajenga vyuo vingi sasa hivi, kuna Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, ni daraja ambalo linatengeneza vijana wengi sana ambao wanaingia kwenye soko la ajira, lakini wengi wanashindwa kuendelea kwa kukosa pesa za kugharamia mafunzo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaishauri Serikali ione umuhimu vilevile wa kugharamia level hii ya kati ambayo ndiyo ya watenda kazi ambao tunawaingiza kwenye soko la ajira lakini vilevile kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na baadae kuwa walipa kodi wazuri na kuweza kusaidia Taifa letu kujijenga kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni eneo la utalii. Ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa kutengeneza filamu ya Royal Tour. Dhamira ya Mheshimiwa Rais ni njema na ina matokeo chanya, kwa mujibu wa Ilani yetu ya uchaguzi ni kweli na kwa kupitia Royal Tour itatusaidia sana, lakini nishauri pamoja na dhamira hii njema ya Mheshimiwa Rais ambapo ameonesha njia ametengeneza skelton wajibu wetu sisi Wizara nyingine nyingi, taasisi na watu binafsi ni kujaza nyama sasa kwenye skelton hii ili hii Royal Tour iwe na taswira iwe na impact chanya kwenye eneo la utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyo vivutio vingi sana vya utalii lakini bado hatujaweza kuvitangaza ni jukumu sasa la Wizara mbalimbali Wizara ya Uwekezaji, Wizara ya TAMISEMI kwenye miundombinu, Wizara ya Utalii yenyewe na maeneo mengine yote ili kuweza sasa ku-compliment hiki alichokifanya Mheshimiwa Rais ili kiweze kuwa na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kuna vivutio vingi kwa mfano mimi kwenye eneo langu la Ukerewe kuna vivutio vingi. Kuna jiwe linacheza kule, kuna beach ya Rubya kuna mapango ya Andebezi ambayo tokea shule za msingi tunasoma na maeneo mengine ninaamini hata maeneo mengine kuna vivutio vingi vya utalii lakini bado havijaweza kutambulika na kutengenezewa miundombinu ili hawa sasa tunaowashawishi waje kutembelea Taifa letu waweze kuvijua na kuweza kuvitembelea. Kwa hiyo, tu-compliment hii Royal Tour sisi kama Wabunge lakini na taasisi nyingine zote ili angalau iweze kuwa na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo ningetamani kuchangia ni eneo la kilimo. Ninaipongeza Serikali kwa mara ya kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais bajeti ya Wizara ya Kilimo imepanda kutoka Bilioni 294 mpaka Bilioni 954, haya ni mapinduzi makubwa sana na kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri lengo ni kuongeza uzalishaji kwenye kilimo cha umwagiliaji kutoka asilimia 10 mpaka asilimia 50, ninaamini tunaweza tukafikia lengo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia trend ya kukua kwa uzalishaji kwenye eneo la kilimo imekuwa siyo nzuri sana. Ukiangalia kwa mfano, mwaka jana kwenye Pato la Taifa kilimo kimechangia asilimia 26.4 mwaka jana tukashuka mpaka 26.1 lakini kwa haya mapinduzi na mtizamo wa Serikali sasa kuongeza bajeti, ninaamini tutaenda mbele zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuweka nguvu kwenye kilimo hiki cha umwagiliaji ninaamini tuna maeneo ambayo tunaweza tukayatumia tuna-quick wins nyingi sana, ni vizuri tukaangalia sasa maeneo ambayo tunaweza tukawekeza kidogo kwa kuanzia lakini tukapata tija hasa kwenye maeneo ambayo yanazungukwa na maji, kuna vyanzo vya maji tayari badala ya kwenda kwenye maeneo ambayo tunahitaji kuweka uwekezaji mkubwa, kuna maeneo yanayozungukwa kwa mfano na maziwa, yanazungukwa na mito tunaweza tukawekeza kwa kuanzia na kukawa na matokeo chanya kwa sababu tayari kuna vitu vya kuanzia kuna chanzo cha maji. Sisi Ukerewe pale kwa mfano, tuna hekta zaidi ya 2000 ambazo tungeweza kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji tukapata mavuno mengi sana mavuno makubwa, sambamba na Ukerewe lakini kuna maeneo mengine vilevile yana taswira kama hiyo, ni vizuri tukaangalia maeneo haya kwa kuanzia tukawekeza tukaweza kupata tija kwenye eneo hili la umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunawekeza nguvu kubwa kwenye kilimo cha umwagiliaji ni lazima tuangalie tumejiandaaje kwa sababu tumewekeza lazima tutapata matokeo chanya, tutapata mavuno mengi, tumejiandaaje sasa kupata soko la mavuno haya ambayo tutayapata kutokana na kilimo hiki cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri siyo vibaya Serikali vilevile ikatengeneza matajiri wazalendo kwenye Taifa hili, ikatengeneza watu ambao inaweza kuwatengenezea njia, kuwatafutia masoko ikawapa mitaji ili wakiwa wazalishaji wazuri na wakawa wametengenezewa masoko wakaweza ku-supply mavuno hayo ambayo tutakuwa tunayapata. Kwa sababu moja kati ya changamoto ambazo tumekuwa nazo kwenye Taifa hili ni kwamba tunazalisha chakula, tunapata masoko nje ya nchi, lakini sasa kunakuwa hakuna consistence ya uzalishaji wa mazao yale, kitu ambacho kinapelekea wale tunaowasambazia bidhaa zile wanakata tamaa na kuingia mikataba na watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kulea watu wetu, tukawapa mitaji, tukawajengea mazingira wakawa wazalishaji wazuri, ina maana itatusaidia hata kuweza kupata masoko ya uhakika lakini tukaweza kuwasambazia na kusaidia Taifa letu kwenye kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la mifugo na uvuvi ninaipongeza Serikali kuongeza bajeti kutoka Bilioni 100 mpaka Bilioni 268, kwenye eneo la uvuvi pekee imeongezeka karibu Bilioni 176. Ninaendelea kuisisitiza Serikali iwekeze nguvu kwenye ufugaji wa Samaki kupitia vizimba, yatakuwa mapinduzi makubwa sana na kwenye eneo hili, itasaidia hata ajira kwa vijana wetu ambao tumekuwa tunawasemea ili waweze kupata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la nne na la mwisho ni kwenye eneo la ufanisi wa miradi ya maendeleo. Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 21 umeongelea juu ya eneo hili, ukasema Mheshimiwa Rais amekuelekeza kuangalia upya taratibu za ununuzi na thamani ya fedha kwenye miradi ya maendeleo, ni kweli tunapoteza pesa nyingi sana kwenye eneo hili, wamesema wachangiaji wengine kama tutaangalia vizuri kwenye eneo hili itatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee mfano kwenye eneo langu la Ukerewe, mwaka jana nashukuru tumepata pesa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya lakini kuna sintofahamu namna gani mradi huu unatekelezwa, ni vizuri kwenye eneo hili Serikali ikasimamia kwa makini, tunapoteza pesa nyingi sana hasa kwenye Halmashauri zetu kwa sababu ya mifumo hii kwa kutumia sheria zetu za manunuzi, kwa hiyo, kama tutaliangalia vizuri jambo hili itatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea kuhusu umeme katika visiwa vidogo na vikubwa vilivyopo Ukerewe. Pamoja na sera ya Serikali kusambaza umeme vijijini bado kuna tatizo la nishati ya umeme katika visiwa mbalimbali vilivyopo katika Jimbo la Ukerewe. Nashauri Wizara itoe kauli ya matumaini juu ya upatikanaji wa umeme katika visiwa hivi kwa sababu nishati hii ni kichocheo cha maendeleo kwenye visiwa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo line kubwa za umeme zimepita basi vijiji hivyo vipatiwe nishati mbadala ya kushuhudia tu nyaya zimepita kwenye maeneo yao. Pia pale ambapo tayari kupitia REA umeme umefika kwenye eneo basi wananchi wanaohitaji nishati hii wapewe haraka badala ya kuzungushwa hadi wanakata tamaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kisiwa cha Ukara umeme wa jua kupitia kampuni binafsi ya JUMEME umewekwa lakini gharama za nishati hii ni kubwa mno kiasi kwamba wananchi wanashindwa kuimiliki. Naomba Wizara iingilie na kuhakikisha kuwa gharama zinakuwa nafuu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri kukosa mamlaka ya moja kwa moja kuyawajibisha Mabaraza ya Ardhi imekuwa kero na kufanya wananchi kudhulumiwa haki zao na Mabaraza haya kwa sababu ya rushwa na uonevu mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kupitia Wizara hii iangalie upya sheria iliyounda Mabaraza haya ikiwemo na namna ya kuyawajibisha ili wanaojiona miungu watu wanaoweza kufanya chochote badala ya kupunguza migogoro badala yake wameongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya ardhi katika kitabu sijaona Ukerewe kama sehemu inayokabiliwa na migogoro ya ardhi, hivyo naomba Wizara itambue kuwa Ukerewe kuna migogoro kadhaa ya ardhi ikijumuisha ifuatayo:-
Mpaka wa kijiji cha Nampisi na majirani zake, kijiji cha Muriti vs kijiji cha Kitangaza, mipaka katika vijiji vya Buzegwe vs Murutanga, kijiji cha Bulamba Vs Musozi, kijiji cha Bukindo vs Kagunguli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia ya maeneo yaliyotwaliwa ya vijiji vya Bugegwe, Kakerege, Nyamagana, Selema, Kasulu - Nakoza itolewe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ukerewe kama kisiwa inaweza kuwa chanzo kikubwa cha utalii endapo vyanzo kadhaa katika Wilaya hii vitawekwa sawa na kujengewa mazingira mazuri ya kutembelewa na watalii.
(a) Mapango ya Handebezyo ni mapango ambayo watu wa kale waliyatumia kwa ajili ya kujilinda na kufanya shughuli nyingine mbalimbali wakati wa mashaka kiusalama. Halmashauri ya Wilaya imekuwa ikijitahidi kuyahifadhi mapango haya yaliyoko Kata ya Nduruma.
(b) Nyumba ya Ghorofa ya Chifu Lukumbuzya ni jengo lililokuwa linatumika kama makazi ya Chifu wa Wakerewe, Chifu Lukumbuzya. Hiki kimekuwa kivutio kutokana na muundo wake ikilinganishwa na nyakati za ujenzi wake. Jengo hili liko katika kijiji cha Bukindo na limekuwa likivutia watu wengi, lakini faida yake kwa Taifa haina tija.
(c) Ufukwe wa Rubya ni ufukwe wa aina yake ulioko katika Kata za Ilangala na Muriti ambao umekuwa ni kivutio kikubwa sana kwa watu mbalimbali, kitu ambacho kama Wizara itaweka nguvu yake, basi kinaweza kuwa chanzo kingine kizuri cha mapato kupita utalii.
(d) Katika Kisiwa cha Ukara, Wilayani Ukara kuna jiwe ambalo ni la kimila na ambalo linasimamiwa na moja ya familia zilizoko katika kijiji cha Nyamangana. Jiwe hili limekuwa ni moja ya maajabu ambayo yamekuwa yanavutia watu wengi wanoenda kushuhudia kile kinachotokea. Bahati mbaya limekuwa halitangazwi sana kiasi kwamba ukiachilia mbali watu walioko kule Ukara ni watu wachache kutoka nje ya Wilaya wanaojua jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe itumie wataalam wa utalii utembelee vivutio hivi na kufanya maboresho na kuvitangaza ili Taifa liweze kufaidika kupitia mapato yatakayotokana na vyanzo hivi (vivutio) vya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, uharibifu wa wanyama kama viboko, limekuwa ni tatizo na kikwazo kikubwa cha maendeleo ya wananchi katika Kata za Nduruma, Bukindo na Kagunguli. Tatizo hili kwa kuwa ni la muda mrefu na Halmashauri imeshindwa kulidhibiti, basi naomba Wizara ichukue hatua za haraka kudhibiti na kunusuru hali hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia yafuatayo:-
Kwanza, Usafiri wa Majini. Vivuko; Kivuko, cha MV Nyerere kinachofanya kazi kati ya Bugorola – Ukara, kina matatizo makubwa ya kuchoka/ubovu wa engine zake zote mbili, hali iliyopelekea mara kwa mara kuzua taharuki kwa wasafiri kutokana na kuzima ikiwa katikati ya maji. Jambo hili ni hatari sana kwa maisha ya abiria na hata kinapofanya safari zake kivuko hiki kinatumia karibu masaa mawili kwa umbali huo badala ya nusu saa hadi dakika 45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri; zinunuliwe engine nyingine kwa ajili ya kivuko cha MV Nyerere ili kuepusha matatizo yanayoweza kuhatarisha maisha, pia Serikali ione umuhimu wa kutengeneza kivuko kwa ajili ya wakazi zaidi ya 20,000 wa Kisiwa cha Irungwa na Nansio ambao wanatumia mitumbwi na hivyo kusafiri kwa zadi ya masaa matano (5) wakiwa majini. Awali MV Ukara ilikuwa inafanya kazi eneo hili kabla ya kuharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu meli; kuharibika kwa meli ya MV Butiama na uchakavu wa meli ya MV Clarius kumepunguza ufanisi na kuleta shida ya usafiri kati ya Mwanza – Nansio. Ushauri wangu ni kwamba, mchakato wa matengenezo ya meli ya MV Butiama ukamilike haraka ili meli hii iweze kutoa huduma na kupunguza tatizo lililopo la usafiri. MSCL ipewe fedha za kutosha ili iweze kuboresha meli ya MV Clarius ili meli hiyo iweze kumudu ushindani na kushindanishwa kibiashara.

Pili, Mawasiliano; kuna tatizo kubwa la mawasiliano kwenye baadhi ya maeneo yakiwemo eneo la Bwasa na Bukiko, wananchi katika maeneo haya hupanda vilimani ili kupata mawasiliano. Ombi langu, ijengwe minara kwa ajili ya mawasiliano; Bukiko katika Kata ya Bukiko na Bwasa katika kata ya Igalla.

Tatu, Barabara; barabara ya Bunda – Kisorya – Nansio ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa maeneo haya inajengwa kwa kasi ndogo sana. Barabara hii ikamilike mapema ili iweze kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke katika bajeti ya kila mwaka mpango wa kujenga kilomita moja kila mwaka kwenye barabara ya Bulamba – Mavutunguru – Kakukuru badala ya kutumia fedha nyingi kila mwaka kwa ajili ya kufanya ukarabati usio na tija katika barabara hiyo. Fedha hiyo iongeze kilomita moja (1) ya lami kila mwaka kwenye hiyo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, formula ya ugawaji wa fedha za Mfuko wa Barabara ibadilishwe na kutoa mgao ulio sawa kati ya TANROADS na Halmashauri za Wilaya. Hii itawezesha Halmashauri kuwa na uwezo wa kutengeneza barabara nyingi zinazosimamiwa na Halmashauri zetu ambazo zinakabiliwa na uharibifu mkubwa lakini hazina uwezo wa kuzihudumia kikamilifu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano ambayo ni muhimu sana. Kwanza naunga mkono hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pili, nikitambua kwamba kuna maeneo nimekwishatoa mchango kwa maandishi niombe sasa nichangie hasa kwa kusisitiza kwenye maeneo kama matatu ambayo kwangu naona ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Jimbo langu la Ukerewe. Sisi ni watu tunaotoka Visiwani, nimekuwa namsikia ndugu yangu Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau analalamika juu ya mazingira ya Mafia, mazingira ya Ukerewe kama nilivyosema ni visiwa na usafiri wetu mkuu ni lazima tu-cross maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea kutumia vyombo vya usafiri kama meli, cha kusikitisha tuna shirika muhimu sana la Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) ni kampuni muhimu sana. Ukerewe tumekuwa na Meli za MV. Butiama, MV Clarias, bahati mbaya sana zimekuwa na matatizo kwa muda mrefu mfano MV Clarias, kila mara inaharibika. MV Butiama ina zaidi ya miaka minne haifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri nimeona wanaongelea utengenezaji wa Meli ya MV Butiama, haiko specific kwamba utengenezaji huu unatarajia kukamilika lini ili kuwasaidia wananchi wa Ukerewe wanaotaabika na usafiri usio wa uhakika wa meli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwamba kuna kampuni binafsi ya MV. Nyehunge ambayo ina-operate pale sasa hivi, lakini hii Kampuni ya Huduma za Meli ni kampuni muhimu sana, nimekuwa naongea na watumishi wa kampuni hii wanachoomba wao wanataka tu uwezeshwaji ili Kampuni hii ianze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita kuna mchangiaji mmoja ametoa mfano akasema kwamba ni vigumu sana kwa kampuni za meli kupata harasa. Ni kweli nakubaliana naye, Kampuni kwa mfano hii ya Huduma ya Meli kama itawezeshwa ni moja kati ya makampuni ambayo yanaweza kutoa pesa kwa Serikali kutokana na utendaji wao, imani yangu ni kwamba watafanya kazi vizuri na kwa faida na sehemu ya faida ile wataipa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni mwaka mzima hata pesa za ruzuku OC Serikali imeshindwa kuwapa kampuni hii, wameshindwa kulipwa mishahara, hata Bima ya Afya wamekatiwa kwa sababu wameshindwa kulipa pesa, matokeo yake naambiwa kuna wakati mpaka watumishi wanaenda kupanga foleni ili viongozi wa kampuni hii waweze kuwasaidia watumishi angalau familia zao zipate matibabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali wasaidieni Kampuni hii iweze kuwa imara, iweze kusimama na kufanya kazi zake, kwa sababu wanachoomba wao kampuni hii ya meli wanataka tu uwezeshwaji ili waanze kazi. Kama wataanza kufanya kazi wana uhakika wa kuendelea kulipana mishahara na kufanya shughuli zao bila matatizo. Kwa nini Serikali mnaicha Kampuni hii inataabika kiasi hiki. Hebu niombe Serikali tafadhali MSCL waweze kusimama wa- take off kuliko kuwaacha katika mazingira wanaishi kama yatima, hawalipani mishahara, watumishi wanaugua hawawezi kwenda hospitali kwa sababu hawana bima tena, wasaidieni tafadhali. Iwezesheni MSCL iweze kufanya kazi, hii ni Kampuni muhimu sana kuweza kuisaidia hata Serikali kama chanzo chake cha mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kama nilivyosema, kule tunaishi visiwani, kuna vivuko kwa mfano cha MV Nyerere nimekuwa nawasiliana na Mheshimiwa Naibu Waziri mara kwa mara, ambacho kina operate kati ya Ukala na Bugolola. Kivuko hiki kina muda mrefu na sasa injini zake zimechakaa zimeanza kuleta matatizo. Kwa mfano, wiki mbili zilizopita kivuko hiki kimezima katikati ya maji zaidi ya mara mbili na kuzua taharuki kwa abiria waliokuwa katika meli ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri wakati anafunga mjadala aweze kutuambia na hasa wananchi wa Jimbo la Ukerewe wanaotumia kivuko hiki nini suluhisho la kudumu la Kivuko cha MV Nyerere? Kinahitaji kitengenezwe ili watu wanaosafiri katika kivuko kile wawe na uhakika wa maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kivuko kinasafiri, kwanza mahali kinapofanya kazi ni umbali ambao hauwezi kuzidi hata dakika arobaini na tano, lakini kivuko kile kwa sababu ya kuchoka kwa injini zake kinasafari zaidi ya masaa mawili, sasa fikiria kina safiri masaa mawili bado kinazima katikati ya maji! Hii inazua taharuki na kukatisha watu tamaa. Wakati Mheshimiwa Waziri anapokuja ku-wind up ningeshukuru sana kama atanipa suluhisho la kivuko hiki na kuweka mazingira ya kudumu na ya uhakika ya usafiri kwa wakazi wa Kisiwa cha Ukala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisiwa cha Irugwa vilevile pale Ukerewe, kina wakazi zaidi ya elfu 20, lakini wanasafiri kutoka kule kwa mfano watumishi wanasafiri kwa siku tatu. Ili atoke Irugwa aje atape huduma kwenye Makao Makuu ya Wilaya inabidi apite Musoma Vijijini kwenye Jimbo la Profesa Muhongo, aende Musoma Mjini kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mathayo, aende Bunda kwenye Jimbo la Mheshimiwa Ester Bulaya apite Kisolya ndiyo aje Nansio. Naomba Mheshimiwa Waziri mtuangalie kwenye eneo hili Kisiwa cha Irugwa lini Serikali itafikiria kuweka usafiri wa kudumu katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo la barabara, nimesoma kwenye hotuba hapa sijaona chochote juu ya ujenzi wa daraja linalounganisha Kisolya na Rugezi. Serikali ina mpango gani juu ya ujenzi wa daraja hili ambalo litakuwa suluhisho la matatizo ya usafiri kwa wakazi wa Ukerewe. Ningeshukuru sana kama Mheshimiwa Waziri wakati wa kufunga atanipa maelezo ni nini mkakati wa Serikali juu ya ujenzi wa daraja hili, kwa sababu tayari hatua za awali zilishaanza, nini kinaendelea, nitashukuru sana kama Mheshimiwa Waziri ataniambia nini kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mradi wa ujenzi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Bunda – Nansio, nimeona kwenye hotuba kuna awamu ya pili ambayo inaongelea ujenzi wa kilometa 51 kati ya Kibala na Kisolya. Niombe sana Mheshimiwa Waziri. Kutoka Kisolya ambapo awamu hii ya pili inakomea mpaka Nansio Mjini ni kama kilomita kumi na zinabaki, naomba badala ya kujenga kilometa 51 kilometa 10 zikabaki ni bora Serikali ikaunganisha kilometa hizi katika kilometa 51 ili ufanyike mradi wa pamoja, badala ya kutengeneza kwa awamu miradi miwili tofauti ambayo naamini itakuwa ni gharama zaidi kuliko kama itaunganishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la mawasiliano; nimeona jitihada za Mfuko wa Mawasiliano kusambaza huduma hii ya mawasiliano, lakini bado kuna matatizo makubwa sana ya mawasiliano kwenye kisiwa cha Ukerewe hasa katika Kisiwa cha Ukara. Katika karne hii si jambo jema sana kwamba unaenda mahali unakuta wanakijiji wanakusanya eneo moja ili wapate mawasiliano ya kupiga simu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri tuweze kupata mawasiliano kwenye kisiwa cha Ukerewe, maeneo yote yaweze kupata mawasiliano, ambayo yatasaidia hasa kuharakisha shughuli za kiuchumi za wananchi kwa eneo la Ukerewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema, niweze kutoa mchango wangu kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Natumia nafasi hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kutuletea maendeleo kama Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imesheheni mambo mengi na kuonesha dira ya Taifa letu na namna gani mambo mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo namna ilivyotekelezwa. Nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote kwenye Wizara hii na watendaji wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua Mheshimiwa Jenista na wasaidizi wake namna gani wanafanya kazi kubwa, na Ukerewe ni moja kati ya maeneo yaliyonufaika na miradi mikubwa ya maendeleo ambayo Mheshimiwa Rais ameweza kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utakuwa kwenye maeneo kama mawili na muda ukiruhusu basi nitaongeza eneo la tatu. La kwanza, ni eneo la kilimo. Tanzania tumebahatika kuwa na eneo kubwa lenye sifa ya kuweza kutumika kwa ajili ya uzalishaji wa mazao mbalimbali. Kwa kuangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuanzia aya ya 46, inaonesha namna gani kupitia mradi wa ASDP II ulivyotunufaisha ingawa pamoja na mafanikio tuliyoyapata kwa sababu kwa mujibu wa hotuba mpaka sasa tumefanikiwa kwa asilimia 66 na mradi wenyewe unaenda mpaka mwaka 2027/2028.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kupitia Sekta ya Kilimo tunaweza tukafanya mambo makubwa sana kupitia hii ASDP II, tunaweza tukafanya vizuri sana na tukitumia maeneo tuliyonayo yenye rutuba na uwezo wa kuzalisha mazao, tukawa na uchumi mkubwa na endelevu kwenye Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna maeneo mengi hatujaweza kuyafanyia kazi pamoja na dhamira ya Serikali kuweza kuongeza uzalishaji kwenye maeneo yetu mpaka kufikia hekta zaidi ya 1,200,000, lakini bado kuna maeneo mengi na hasa rasilimali maji hatujaweza kuitumia vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua jitihada za Serikali kutengeneza mabwawa na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, lakini bado hatujaweza kufanya vizuri. Nikitoa mfano, mimi natoka Jimbo la Ukerewe ambapo tumezungukwa na maji. Katika eneo tulilonalo, zaidi ya kilometa 6,400, asilimia 90 ni maji. Inasikitisha kwamba pamoja na eneo tulilonalo ambalo tuna hekta karibu 31,000, lakini kwa sababu hatufanyi kilimo cha kisasa ambacho kinaweza kuleta tija kila mwaka katika maeneo tuliyonayo, tunaona mahitaji ya chakula ni tani 151,000, lakini uwezo wa kuzalisha chakula ni tani 104,000 pekee.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake, pamoja na kwamba kitaifa tuna ziada ya chakula karibu tani 400,000 lakini bado Ukerewe kila mwaka tunakuwa na upungufu wa chakula karibu tani 40,000. Naomba kwamba, pamoja na jitihada kubwa ambazo zinafanyika kwenye kuimarisha kilimo, maeneo yenye rasilimali kama Ukerewe ambayo ina rasilimali maji, basi itumike kwa ufanisi ili angalau tuweze kuzalisha chakula kwa wingi na eneo husika vile vile liweze kujikidhi kwa mahitaji yake ya chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni aibu kwenye eneo lililo na maji kwa kiasi kile kila mwaka kuendelea kuwa na upungufu wa chakula, kuwa na shida ya usambazaji wa maji safi na salama. Wakati Wakerewe wanaona wamezungukwa na maji, ukiwaambia tuna shida ya maji, watu hawawezi kuelewa. Kwa hiyo, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla wake ione namna, na haja ya kutumia rasilimali tulizonazo kwa ajili ya uzalishaji na kuondokana na changamoto zinazotukabili kama nilivyotoa mfano kwenye eneo la Ukerewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa uwekezaji kwenye Sekta ya Uvuvi. Ni kweli siku chache zilizopita katika uwekezaji uliofanyika wa zaidi ya shilingi bilioni 13 kwenye kununua boti, lakini na ufugaji kwa kutumia njia ya vizimba, sisi Ukerewe ni wanufaika wa mradi ule. Nashauri kwamba, pamoja na jitihada zote hizi, kama ilivyofanyika kwenye eneo la kilimo kuanzisha BBT, lifanyike BBT vilevile kwenye eneo la uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri hivi kwa sababu Ukerewe tuna visiwa karibu 38 na vyote vinafanya shughuli za uvuvi, kwa hiyo, kinaweza kutengwa hata kisiwa kimoja kikatumika kama eneo la kutengeneza mradi wa BBT ili tuone matokeo yake yanakuwaje, kwa sababu zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa Ukerewe wanategemea Sekta ya Uvuvi. Kupitia BBT sasa inaweza kuwa njia ya kuonesha wananchi wa Ukerewe namna gani uvuvi kwa kutumia vifaa vya kisasa unaweza kuwatoa kwenye shida waliyonayo na kuweza kupata mafanikio ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nilitamani kuchangia ni eneo la nishati. Kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aya ya 73 mpaka 75, amelezea namna gani tulivyo na changamoto kwenye eneo la nishati, lakini nafarijika kwa sababu Serikali imeonesha jitihada zinazofanyika kuimarisha Sekta ya Nishati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mpaka sasa kama Taifa tuna umeme kidogo, tunazalisha Megawatt chache pamoja na kwamba kupitia Bwawa la Mwalimu Nyerere tunategemea zaidi ya Megawatt 2,000 kuongezeka kwenye Grid ya Taifa, lakini bado tunahitaji kuzalisha zaidi nishati ya umeme, kwa sababu umeme kama nishati, ni kichocheo cha maendeleo ya eneo lolote lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Ukerewe ni kweli kwamba karibu vijiji vyote vimefikiwa na nishati ya umeme, lakini bado maeneo ya visiwa yana changamoto kubwa. Natambua jitihada za Wizara kuweka mradi wa kutoa umeme kwenye kisiwa kikubwa cha Ukerewe kwenda kwenye visiwa, kwa mfano kama Ukara, lakini bado kuna changamoto kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, pamoja na jitihada inazozifanya, bado kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba vitongoji vyote vinapatiwa nishati hii ya umeme ili wananchi sasa waweze kutumia nishati hii kujiletea maendeleo kupitia uanzishaji wa shughuli mbalimbli za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, natambua harakati zinazoendelea kufanya Bwawa la Mwalimu Nyerere lianze kutoa uzalishaji katika uwezo wake wa juu, lakini pamoja na jitihada zinazofanyika, kuna changamoto ninayoiona katika miaka michache ijayo inaweza kukwamisha jitihada zote hizi. Tumewekeza pesa nyingi sana kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, lakini tunatambua vyanzo vya maji yanayoenda Bwawa la Mwalimu Nyerere ni kuanzia Morogoro, Iringa na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kosa moja linalofanyika, tumeruhusu mifugo mingi sana kuwepo kwenye eneo la Morogoro, jambo ambalo miaka michache ijayo itaathiri mazingira kwenye eneo lile na vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji kuelekea kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere kuathirika. Sasa matokeo yake ni kwamba jitihada na rasilimali kubwa zinazowekezwa na Taifa hazitakuwa na tija kwenye miaka michache ijayo, jambo ambalo itakuwa ni hasara na tutakuwa hatujawatendea haki wananchi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali ichukue hatua madhubuti kudhibiti uwepo wa mifugo mingi sana kwenye eneo la Morogoro ili sasa maji na vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji kuelekea kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere visiathirike na kufanya rasilimali nyingi na pesa nyingi tunazozitumia kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere zisiwe na faida tena hapo baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua tuna changamoto kubwa ya miundombinu kutokana na mvua kubwa zilizonyesha. Eneo la Ukerewe ni moja kati ya maeneo yaliyoathirika sana kwenye miundombinu yake. Barabara nyingi zimeathirika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha. Natambua kwamba Serikali iliahidi kutenga pesa kwenye kila jimbo ili kuweza kurekebisha miundombinu hii. Naomba sasa vile vile Ukerewe iangaliwe kwenye eneo hili, kwani barabara zetu zimeathirika sana. Kwa hiyo, Serikali iangalie namna ya kutusaidia pesa ili barabara zinazotengenezwa kwenye maeneo haya ziweze kuwa imara.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba Serikali tayari imepata mkandarasi kwa ajili ya barabara ya kutoka Kisorya kuja Nansio, ninashukuru, lakini bado kuna umuhimu wa kuimarisha barabara ya kutoka Nansio kuelekea Ilangala ambako ndiko lango la uchumi wa Ukerewe liko, ambako kuna uzalishaji mkubwa wa samaki. Naomba Serikali ione umuhimu wa kutengeneza barabara hii ili wananchi wa Ukerewe waweze kunufaika na rasilimali zinazozalishwa kwenye eneo hili, hasa mazao ya uvuvi. Natambua kazi kubwa wanaifanya, lakini naomba sana hili jambo liweze kutiliwa nguvu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni juu ya ugawaji wa majimbo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili, Mheshimiwa Mkundi, ahsante. Mheshimiwa Raymond, atafuatiwa na Mheshimiwa Nashon William Bidya.

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu maradhi yasiyo ya kuambukiza. Kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaosumbuliwa na maradhi kama shinikizo la damu, kisukari na kadhalika ambayo hayakuwa ya kawaida siku za nyuma, lakini kuna matatizo makubwa ya upatikanaji wa huduma ama matibabu kwa maradhi haya hasa kwenye maeneo ya vijijini. Tofauti na waathirika wa UKIMWI ambapo huduma zimesogezwa hadi katika zahanati na vituo vya afya, wagonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na mengineyo yanayofanana na haya wanapata wakati mgumu kupata huduma. Naishauri Serikali isogeze huduma za maradhi haya kama ilivyofanya kwa huduma za waathirika wa UKIMWI.

Pili, ugumu wa huduma Visiwani Ukerewe. Kwa sababu za kijiografia wagonjwa wengi kisiwani Ukerewe wamekuwa wanapoteza maisha kwa kukosa huduma hasa panapohitajika kuwapeleka Hospitali ya Rufaa ya Bugando. Kwa mujibu wa ratiba ya meli, usafiri wa mwisho toka Ukerewe kwenda Mwanza unapatikana saa nane mchana, na njia ya kivuko (ferry) usafiri wa mwisho ni saa 11 jioni, baada ya hapo usafiri mwingine hadi siku inayofuata. Kwa hiyo, inapotokea dharura inapopelekea kutoa rufaa ili mgonjwa apelekwe Hospitali ya Mkoa au ya rufaa baada ya muda huo litakuwa ni kudra ya Mwenyezi Mungu ili awe hai hadi kesho yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la ushauri wangu kwaSerikali ni kwamba itoe ambulance boatkwa Halmashauri ya Wilaya Ukerewe ili kusaidia kwenye matukio ya dharura kuwahisha wagonjwa kwa ajili ya matibabu zaidi.

Tatu, ni kuhusu Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Kuna tatizo la upatikanaji wa huduma kwa wanachama wa CHF hasa upungufu wa dawa na huduma kutotolewa kwenye maeneo mengine tofauti na pale ambapo mfaidika amejiunga. Jambo hili linakatisha tamaa. Nashauri Serikali iangalie upya na kuweka mfumo mzuri wa upatikanaji huduma kwa wanachama wa CHF ili kumwezesha mwanachama kupata huduma eneo lolote ama kituo chochote nchini ili mradi yeye ni mwanachama na ana kitambulisho.

Nne, ni kuhusu huduma kwa wazee. Halmashauri nyingi bado hazijatoa vitambulisho kwa wazee wala kutenga dirisha maalum la wazee, jambo hili linasababisha usumbufu mkubwa kwa wazee pale wanapohitaji kupata huduma za afya. Nashauri Serikali itilie mkazo na ikiwezekana kuweka muda maalum ili kuzibana Halmashauri zote nchini kutekeleza jambo hili.

Tano, kuongeza vituo vya afya na zahanati. Kwa kuwa ni sera ya Serikali kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya na kila kijiji kinakuwa na zahanati, Serikali ihakikishe mahali ambapo vituo na zahanati vimejengwa basi maeneo hayo yasaidiwe na kupewa vifaa na watumishi ili kuwezesha zahanati hizo na vituo vya afya vifanyekazi ya kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, Halmashauri ya Wilaya Ukerewe imeweza kujenga kituo cha afya Nakatunguru, lakini sasa ni zaidi ya miaka mitatu toka kimekamilika kimeshindwa kuanza kwa kukosa vifaa na majengo yanaanza kuchakaa. Lengo la kituo hiki ilikuwa ni kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali ya Wilaya. Nashauri Wizara iwezeshe kituo hiki ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Sita ni uhaba wa watumishi. Kuna uhaba mkubwa wa watumishi wa afya kwenye maeneo ya pembezoni kama Ukerewe. Jambo hili linapelekea uhafifu wa utoaji wa huduma kwenye maeneo haya. Nashauri Serikali itoe motisha kama vile posho ya mazingira magumu kwa watumishi waliopo na kufanyakazi kwenye maeneo haya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na utalii. Tanzania kama nchi ina vivutio vingi sana vya utalii kwenye maeneo mengi mbalimbali lakini tatizo lililopo ni vivutio vingi kutojulikana, hivyo nashauri:-

(a) Kuwa na chombo mahsusi kwa ajili ya kutangaza vivutio hivi, chombo hiki kiwe na jukumu la kubaini vivutio hivi maeneo viliko na kuvitangaza kwenye maeneo mbalimbali duniani kupitia Balozi zetu na namna nyingine zinazowezekana. TTB ibaki na usimamizi na uratibu na kuacha chombo hicho maalum kibaki na kazi ya kutangaza utalii.

(b) Wizara iwekeze pesa za kutosha katika utangazaji wa utalii badala ya kufikiria kupata mapato ya kutosha kupitia utalii bila kuwekeza katika utangazaji. Mfano, vivutio vilivyoko Wilayani Ukerewe kama vile:-

(i) Jiwe linalocheza la Nyabureke;
(ii) Makazi ya Chifu Lukumbuzya;
(iii) Mapango ya Handebezyo;
(iv) Kaburi la mtunzi wa kwanza wa vitabu Hamis Kitelezya; na
(v) Pwani ya Rubya yenye mchanga mweupe na adimu sana na kadhalika.

(c) Mapato yanayotokana na maliasili yawafaidishe wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hizi. Jambo hili litafanya watu hawa wajione ni sehemu ya hifadhi hizi na hivyo kushiriki kuzitunza bila kinyongo.

(d) Miundombinu kama barabara zinazoekea kwenye vivutio hivi vya utalii iboreshwe ili watu wenye nia ya kuvitembelea waweze kuvifikia bila matatizo jambo litakalowahamasisha kuendelea kutembelea vivuto hivi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, Ukerewe ni moja kati ya maeneo ambayo yana rasilimali za kutosha kwa ajili ya malighafi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uzalishaji mkubwa wa samaki na matunda (mananasi, machungwa na maembe), Wizara ielekeza wawekezaji kwa ajili ya viwanda vya kuchakata samaki na matunda katika eneo hili ili kuokoa matunda mengi kuharibika kwa kukosa soko. Jambo hili litasaidia pia kukuza uchumi wa wananchi hasa vijana na akinamama kwenye visiwa hivi vya Ukerewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kutokana na uzalishaji mkubwa wa samaki katika Visiwa vya Ukerewe, litakuwa jambo lenye maslahi kwa Taifa iwapo vitajengwa viwanda vya kuchakata samaki kwenye maeneo haya badala ya kuwasafirisha kuwapeleka katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia. Kwanza niunge mkono wale wote walioonesha concern ya bajeti ndogo ya Wizara hii ya Kilimo. Tukizingatia umuhimu wa kilimo na namna tunavyoelekea kwenye uchumi wa viwanda kwenye nchi yetu, sekta ya kilimo ni muhimu sana kwa ajili ya uzalishaji wa mali ghafi lakini ajira na kutengeneza kipato kwa wananchi wetu ili waweze kununua bidhaa zitakazozalishwa na viwanda hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunapofikiria kuingia kwenye uchumi wa viwanda ni muhimu sana tukaimarisha kilimo chetu kuwa kilimo cha kisasa zaidi na hasa kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji. Tunaweza kuwekeza vizuri kwenye kilimo cha umwagiliaji kama tutazingatia rasilimali tulizonazo kwenye maeneo yenye resources kama maji, kwa mfano kwenye maeneo ya Ziwa Viktoria hususani eneo la Ukerewe kidogo inaleta shida kwenye eneo kama Ukerewe ambalo limezungukwa na maji wananchi wa Ukerewe kulalamika kutokuwa na chakula cha kutosha. Tuna maeneo ya kutosha ambayo Serikali inaweza kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji tukazalisha chakula cha kutosha tukaweza kukabiliana na hali tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nitake tu kujua kuna Mradi wa Kilimo wa Umwagiliaji kwenye Bonde la Miyogwezi na Bugolola. Kwenye bonde la Miyogwezi iliwekezwa zaidi ya shilingi milioni 600 na Serikali lakini pesa ile imewekwa pale ule mradi haukuendelea, lakini kama Serikali ingeweka mkazo ikaweka pesa nyingine ya kutosha mradi ule ukaanza kufanya kazi, kusingekuwa na tatizo la chakula kwenye eneo la Ukerewe, inawezekana wangeweza kutoa chakula zaidi nje ya eneo la Ukerewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kufanya vizuri kama hatuwekezi kwenye utafiti kwenye eneo la kilimo. Ni vizuri sana tukawekeza kiasi cha kutosha cha pesa kwenye utafiti, kutambua kwamba changamoto zinazokabili maeneo yetu hususani kwenye udongo tulionao ni zipi, ni mbegu zipi tunaweza kutumia ili tuweze kutoa mazao ya kutosha yanayoweza kutusaidia kuhimili changamoto tulizonazo za chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni uvuvi. Uvuvi kwenye eneo la Ziwa Viktoria ni muhimu sana na kimsingi kama Taifa uvuvi unachangia sehemu kubwa sana ya pato la wananchi wetu. Kwenye maeneo ya ziwa kwa mfano Ziwa Viktoria, sehemu kubwa ya vijana kwenye Mikoa ya Kanda ya Ziwa wanapata riziki yao na kuchangia kwenye uchumi wa nchi hii kupitia ziwa hili lakini kumekuwa na changamoto nyingi sana kwenye sekta ya uvuvi hususani kwenye Ziwa Viktoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua kutoka kwenye Wizara ni kwa nini wavuvi wetu hawafikiriwi sana kupata mikopo. Kuna Benki ya Wakulima, ni namna gani inawasaidia wavuvi? Kwa sababu wavuvi hawa kama watapata mikopo, itawawezesha kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri na kuweza kutengeneza ajira nyingi zaidi lakini sioni kama benki hii ina msaada kwa wavuvi wetu. Hata taasisi nyingine za kifedha ni namna gani wavuvi hawa wanaweza kupata mikopo kupitia rasilimali walizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana katika mazingira yalivyo sasa wavuvi hawawezi hata kutumia rasilimali walizonazo kama dhamana kuweza kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha. Niiombe Serikali ione umuhimu wa kuwajengea mazingira mazuri wavuvi wetu kupata mikopo ili watengeneze mitaji yao kuwa imara zaidi na kuzalisha ajira nyingi lakini na kutengeneza uzalishaji mkubwa wa mazao ya ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sekta ya uvuvi inakabiliwa na changamoto nyingi sana ambazo ningependa Serikali iweze kuzifanyia kazi. Nashukuru kwamba Serikali imeanza kuona matatizo ya tozo zilizopo kwa wavuvi lakini bado kuna tatizo kubwa la tozo nyingi kwa wavuvi wetu. Niombe Serikali iendelee kulifanyia kazi, kwa mfano, kuna tozo za SUMATRA, leseni za uvuvi na tozo za kupaki.

Ningeomba Wizara inieleze hivi inakuwaje mimi ninayemiliki gari naweza kuchukua leseni na bado nikafanya shughuli zangu na gari langu kwenye maeneo yote Tanzania nzima lakini mvuvi anapokuwa na leseni ya uvuvi akitoka Halmashauri moja kwenda nyingine analipa tena leseni nyingine ya uvuvi, akitoka Halmashauri hiyo akienda Halmashauri analipa tena leseni ya uvuvi ni kwa nini kuwa na matatizo haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mazingira ya uvuvi yanabadilika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kama uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa letu bado hakipewi uzito unaostahiki. Pesa zilizotengwa katika bajeti hazitoshi kukabili mahitaji yaliyopo, hata hivyo nashauri yafuatayo:-

(a) Utafiti ufanyike ili kujua matatizo katika ardhi na kwa maana hiyo ushauri ufanyike ni mbegu gani itumike kwenye eneo husika kulingana na utafiti uliofanyika. Mfano, ardhi ya Visiwa vya Ukerewe inahitaji kufanyiwa utafiti na hatimaye lipatikane suluhisho la aina ya mbegu, mazao na kilimo kinachopaswa kufanyika.

(b) Ufanyike uwekezaji wa kutosha katika kilimo cha umwagiliaji hasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi hali inayoathiri kilimo chetu kinachotegemea zaidi mvua. Mfano, eneo linalozungukwa na maji kama Ukerewe ingepaswa kuwa wazalishaji wakubwa wa chakula iwapo tu Serikali itawekeza katika kilimo cha umwagiliaji katika visiwa hivyo. Kuna mabonde makubwa ya Bugorola na Miyogwezi ambapo Serikali imewekeza zaidi ya shilingi millioni 700, lakini mradi huo umetelekezwa. Naomba kujua Serikali ina mpango gani na miradi ya umwagiliaji wa Miyogwezi?

(c) Zitolewe ajira kwa Maafisa Ugani wengi na wasambazwe kwenye maeneo mbalimbali ili kutoa ushauri kwa wakulima wetu na hivyo kuongeza tija katika kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za uvuvi zinatoa ajira kubwa kwa wananchi wengi katika nchi hii lakini kuna changamoto nyingi sana na hivyo naomba kushauri yafuatayo:-

(a) Sheria Na. 22 ya mwaka 2003 ipitiwe upya na ufanyike utafiti wa kina kwa kushirikisha wadau hasa wavuvi wenyewe ili tuwe na sheria nzuri na rafiki kulingana na mazingira. Mfano, kuzuia nyavu ‘piece 3’ kunahamasisha wavuvi wa sangara kuvua kina kifupi cha maji na hivyo kuharibu mazalia ya samaki. Pia nyavu za mm10 kwa nyavu za dagaa ni kuwanyima fursa wavuvi hasa katika Ziwa Victoria ambapo ni vigumu kupata dagaa size hiyo.

(b) Wavuvi wamekuwa wanavamiwa na kujeruhiwa au kuuawa wanapokuwa wanafanya shughuli zao za uvuvi katika ziwa. Nashauri Serikali iweke mfumo thabiti wa kiulinzi ili wavuvi hawa wafanye shughuli zao kwa usalama.

(c) Bado tozo ni nyingi sana katika sekta hii zinazowakabili wavuvi na hivyo Serikali ipunguze tozo hizi ili wavuvi wetu wafanye shughuli zao kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza hatua ya kuondoa ada ya usafiri kwa mitumbwi midogo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwa na uchumi imara na kuwa na mchango mkubwa wa pato katika uchumi ni muhimu Wizara kama msimamizi wa uchumi nchini iwe na kipaumbele katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. Nashauri kwamba Wizara iwekeze katika viwanda vinavyohusiana na kilimo ili kuchochea uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo jema kuwa suala la pension kwa wastaafu limezingatiwa katika bajeti hii. Nashauri kwamba uhakiki ukamilike mapema na malipo yafanyike kwa wakati wakiwemo waliokuwa watumishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ni muhimu sana katika kudhibiti nidhamu ya matumizi Serikalini, lakini imekuwa haiwezeshwi kwa kiwango cha kutosha. Hivyo, nashauri CAG apewe fedha za kutosha kulingana na bajeti yake na fedha hizo zipatikane kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa umuhimu wake ipewe mtaji wa kutosha na kutanua mtandao wake ili iweze kuwafikia watu wengi zaidi wanaohitaji huduma yake hasa walioko vijijini, mfano, Ukerewe. Pia ukopeshaji katika benki hii utoe fursa vile vile kwa Sekta ya Uvuvi kunufaika na benki hii jambo ambalo litaongeza sana nguvu ya kiuchumi ya watu wetu hasa vijijini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mabaraza ya Ardhi; migogoro mingi ya ardhi inachangiwa sana na muundo wa Mabaraza haya ya Kata hasa kutokana na kutawaliwa sana na rushwa. Hii inasababishwa na kukosekana kwa mafunzo ya mara kwa mara na hivyo wajumbe kukosa weledi katika kutafsiri sheria hata kufikia maamuzi jambo ambalo linaishia kugombanisha jamii. Pia wajumbe wa mabaraza haya hata Makatibu wa Mabaraza kutokuwa na pato lolote kunapelekea vitendo vya rushwa. Hivyo nashauri yafuatayo:-

(a) Kutolewe mafunzo ya mara kwa mara kwa mabaraza haya (semina) ili kuwaongozea uelewa na uzoefu Wajumbe wa Mabaraza ya Kata. Jambo hili litawawezesha kukabili kesi zinazojitokeza kwenye maeneo yao.

(b) Kutolewe ruzuku kwa ajili ya kuendesha mabaraza ya ardhi ya Kata, kukosekana kwa ruzuku kunasababisha mazingira magumu sana ya uendeshaji na hivyo kujenga mazingira ya rushwa.

(c) Halmashauri zipewe nguvu/mamlaka ya kuyavunja mabaraza haya pale inapothibitika kuwa yamekiuka maadili. Kwa hali ilivyo hivi sasa, kuna urasimu mkubwa katika kuchukua hatua kwa Mabaraza ya Ardhi. Jambo hili limepelekea matatizo yetu na bado wajumbe hawa wanakuwa na jeuri kwa kuamini kuwa si rahisi kuchukuliwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la ardhi Wilaya, katika ngazi ya Wilaya Mabaraza yetu yanakosa wataalam. Mfano, katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, kuna mrundikano mkubwa wa kesi kutokana na kukosa Mwenyekiti wa Baraza. Mara kwa mara Wilaya imekuwa inapata huduma ya Mwenyekiti ambaye haishi pale na matokeo yake anahudumia mara moja kwa mwezi na kwa muda usiozidi masaa sita. Hili limepelekea kuwepo kwa kesi za mipaka miaka miwili zisizofanyiwa maamuzi. Ombi, Baraza la Ardhi la Wilaya ya Ukerewe lipangiwe Mwenyekiti wa Baraza ambaye atakuwepo muda wote ili kupunguza migogoro ya ardhi hasa ikizingatiwa kuwa eneo katika Wilaya hii ni dogo na hivyo kuwa na migogoro mingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vifaa vya upimaji; kuwe na utaratibu mzuri wa kupatikana kwa vifaa vya kupima ardhi ili mipango mizuri ya matumizi ya ardhi iwezekane.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa dakika zangu tano nitachangia mambo machache katika Mpango huu wa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza, sote tunajua tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda kama kauli mbiu ya Serikali ilivyo, lakini hakuna namna yoyote kama walivyosema wachangiaji waliotangulia kwamba tuelekee kwenye uchumi wa viwanda bila kufanya mapinduzi ya kilimo. Kwa hiyo, ni muhimu sana kwanza tukaboresha kilimo chetu na hasa aina ya kilimo tunachokifanya. Tuna vyanzo vingi, tuna rasilimali nyingi lakini sasa ni namna gani tunatumia rasimali zile. Wamesema wachangiaji wengi, malalamiko ni mengi, wakulima wamelima mazao mengi lakini hayawezi kuendelezwa na kuweza kusafirishwa ili waweze kuimarisha uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hoja yangu kwenye eneo hili ni kwamba tuangalie ni namna gani tunavyoweza kutumia rasilimali tulizonazo kuimarisha kilimo chetu nahasa kujenga mfumo wa kilimo cha umwagiliaji. Kanda ya Ziwa kuna Ziwa kwa mfano na maeneo mengine, lakini namna gani tunatumia rasilimali hii ya maji kuweza kutengeneza kilimo cha umwagiliaji tuweze kuzalisha mazao ambayo yanaweza kutumika kama rasilimali kwenye viwanda vyetu lakini hasa kuimarisha uchumi wa wanachi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la afya. Tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda, tunapojenga mfumo wa kuimarisha uchumi wetu ni vizuri na ni muhumi sana tukaimarisha afya za watu wetu vilevile ili waweze kushiriki kwenye uchumi huu. Lakini namna gani sasa maeneo yetu na watui wetu tumewajengea mazingira ya kuimarisha afya zetu? Nimepitia mpango huu lakini sioni eneno lolote linaloongelea kuendelea kutoa elimu kwa watu wetu katika kujikinga na maradhi lakini na kuimarisha mazingira ya afya kwenye ngazi za msingi. Tumeongelea kuimarisha Hospitali za Rufaa na Hospitali nyingine za Mkoa lakini tunaweza tukapunguza msongamano kwenye hospitali hizi kama tutaimarisha vituo vya afya na zahanati kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutawekeza nguvu kubwa sana kweye hospitali za level ya juu tukasahau maeneo ya chini, bado watu wetu wanapoteza sana maisha kule chini kwa sababau katika ngazi za msingi huku zahanati na vituo vya afya hazina uwezo, wataalam wa kutosha, vifaa vya kutosha kuweza kuimarisha afya zao. Vilevile hawana elimu ya kutosha kujikinga na maradhi. Kwa hiyo, kwenye mpango huu tuweke kipengele kinachojumuisha kutoa elimu na kuongeza package kwa ajili ya kujenga zahanati, kumalizia maboma yaliyojengwa huko nyuma ambayo hayajakamilika ili tuweze kuimarisha afya kwenye maeneo ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini eneno lingine ni eneno la mawasiliano, kwa sababu hatuwezi kuimarisha uchumi wetu kama mawasiliano kwenye maeneo yetu hayako vizuri. Wamesema wachangiaji waliotangulia, haiwezekani kwamba tujenge uchumi ulio imara kama mazao yanayolimwa hayawezi kusafirishwa kutoka point moja kwenda point nyingine. Maeneo yetu mengine bado hayako vizuri sana kimawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mpango huu inaonesha kwamba kuna kuimarisha usafiri kwenye maziwa yetu, lakini bado hatujaimarisha sana Shirika la Meli (MSL). Tungeweza kuimarisha Shirika hili tukaweza kuwapa uwezo wa kutosha, watajenga mfumo mzuri sana wa mawasiliano kwenye maziwa yetu na kwa maana hiyo sasa watu walioko visiwani na maeneo mengine yaliyoko pembezoni wanaweza sasa kusafirisha mazao yao kwenda kwenye masoko na hivyo kuimarisha uchumi wa watu wao kimsingi kwenye maeneo yake yaliyo pembezoni. Vile vile kuweka mfuatano wa usafiri wa mazao na watu kwenye mazingira yetu. Bila kufanya hivyo bado huu wimbo wa ujenzi wa uchumi ulioimara utakuw ana kasoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningeshauri, pamoja na mambo mengine yote yaliyoongelewa kwenye mpango tuimarishe vilevile Shirika hili la Wakala wa Meli ili kuiweza kuwa na nguvu ya kutosha kuimarisha usafiri kwenye maeneo ya maziwa. Kwa mfano sehemu kama kutoa Ukerewe kuunganisha na sehemu ya nchi kavu, kuna matatizo makubwa sana ya usafiri wa meli, hali ambayo inafanya mazao mengi ya watu kutoka kwenye visiwa hivyo kupotea na kwa maana hiyo kuathiri uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilifikiri niliongelee, wamesema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kuhusu uhaba mkubwa wa watumishi wa afya; kutokana na jiografia ya Visima vya Ukerewe upatikanaji wa watumishi ni tatizo kubwa na hivyo kusababisha vifo vya mara kwa mara hasa mama wajawazito na watoto. Muda mfupi Kituo cha Afya cha Buisya kitakamilika lakini hakina wataalam wa kutosha ili kituo hiki kiwe na ufanisi. Watumishi sita pekee kwa kituo kama hiki ni jambo lisilo na afya. Hivyo, tunaomba watumishi wa afya wenye utaalam kwa ajili ya Kituo cha Afya Buisya na Ukerewe nzima kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma ya afya kwa wazee; pamoja na Sera ya Afya kwa Wazee kutaka vitambulisho kutolewa bure kwa wazee bado wazee (hasa Wilayani Ukerewe) wamekuwa wanatozwa shilingi 1,000 ili kupata vitambulisho hivyo. Naomba Serikali itoe maelekezo/ kauli katika hili jambo ili kuepusha manyanyaso kwa wazee hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uimarishaji wa Hospitali ya Wilaya; kwa kuwa Hospitali ya Wilaya ya Nansio (Ukerewe) ndiyo Hospitali ya Rufaa kwa Visiwa vya Ukerewe lakini hospitali hii ina upungufu mkubwa wa madaktari pamoja na vifaatiba jambo ambalo limekuwa linaathiri sana utoaji wa huduma kwa wananchi wa visiwa hivi vya Ukerewe. Naomba hospitali hii iangaliwe kwa namna ya pekee kuhakikisha kuwa afya ya wananchi wa Visiwa vya Ukerewe inawekewa mazingira salama.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana. Kwa kuanza nitambue jitihada za Mawaziri na timu zao kwenye Wizara hii kwa kazi wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu kwa leo kwanza niongelee juu ya magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ambayo yamekuwa common sana kwenye jamii yetu na kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri sikuona kama kuna eneo yamepewa msisitizo sana. Kuna magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu na kadhalika kama hayo, yamekuwa ni ya kawaida sana kwenye jamii yetu na yamekuwa yanapoteza maisha ya watu wengi sana kwenye maeneo hasa ya vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ushauri wangu kwenye eneo hili, niombe Serikali kupitia Wizara kama ambavyo imekuwa inafanya kwenye matatizo ya UKIMWI, zahanati zetu vituo vya afya na hospitali viwe na dawa hizi na ikiwezekana kusiwe na gharama wakati wa kupata dawa hizi ili watu wetu waweze kupata madawa haya na huduma kwa urahisi kwenye maeneo yetu ya vijijini na kwa hivyo kuweza kuokoa maisha ya watu wetu wengi sana wanaopoteza maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nafikiri nilichangie, nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kaongelea namna ambavyo kumekuwa na mkakati wa kuimarisha hospitali za rufaa na hospitali za mikoa. Nikizungumzia kwenye Jimbo langu ya Ukerewe, sisi hospitali yetu ya rufaa ni hospitali ya wilaya hasa kutokana na jiografia yetu na kwa maana hiyo msaada mkubwa ambao tungeweza kuupata kwenye Visiwa vya Ukerewe na akatusaidia sana ni kuimarisha hospitali yetu ya Wilaya Hospitali ya Nansio.

Mheshimiwa Naibu Spika, sawa tumekuwa na maboresho ya wakati fulani lakini bado tuna tatizo kubwa sana la wataalam kwenye hospitali yetu ya Wilaya. Kama mnavyojua jiografia ya ukerewe ni ya visiwa, sasa yanapotokea matatizo ya dharura kwa mfano wagonjwa wanaohitaji kupata rufaa na wakati huo usaifiri wetu una limited time, ikifika jioni hakuna usafiri wa kuvusha wagonjwa kwenda maeneo mengine. Tunashukuru kwamba tumepata shilingi milioni 200 kwa ajili ya kununua boti, lakini bado haiondoi umuhimu wa kuongeza wataalam na Madaktari kwenye hospitali yetu ya Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, tunashukuru kwamba tumepata shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Afya cha Bwisya ambayo itasaidia sana. Kituo kile kinahudumia zaidi ya watu 30,000 kwenye Kisiwa cha Ukala, lakini wakati tunakamilisha ujenzi wa kituo kile cha afya Mheshimiwa Waziri niombe sana sambamba na kukamilisha kituo kile Wizara basi ione uwezekano, kama jambo la muhimu sana kufanya maandalizi ya wataalam kwa ajili ya kuhudumu kwenye vituo hivi ambavyo tumekuwa tunaviboresha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kile ni kituo kikubwa, kinakamilika lakini mpaka sasa kina watumishi sita pekee, jambo ambalo kama litaendelea kuwa namna ile hata kama kitakamilika hakitakuwa na tija. Kwa hiyo, niombe sana kwa Mheshimiwa Waziri, hiki Kituo cha Afya cha Bwisya kinaelekea kukamilika, basi tupatiwe wataalam wa upasuaji lakini na Madaktari kwa ajili ya kutoa huduma, sambamba na upatikanaji wa gari la wagonjwa kwa ajili ya kuhudumia kwenye kituo kile.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema mwanzo kutokana na jiografia yetu tuna matatizo makubwa ya afya na ningefurahi sana kama wakati wa kuhitimisha Mheshimiwa Waziri angeongelea maeneo tata hasa kimazingira kama Ukerewe, Serikali ina mkakati gani kuweza kuboresha huduma za afya ili kuweza kuokoa maisha ya akinamama na watoto ambao mara kwa mara wamekuwa wanapoteza maisha kutokana na jiografia au mazingira kama hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Visiwa vyetu vya Ukerewe bahati nzuri Mheshimiwa Waziri, tumekuwa mara kwa mara tunabadilishana mawazo juu ya kutusaidia kwenye visiwa vyetu vya Ukerewe. Kisiwa cha Ilugwa, kutoka Kisiwa cha Ilugwa kuja Wilayani kuna karibu saa tano ambazo mgonjwa anatakiwa asafiri na kule tuna zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ili kuweza kuwasaidia wananchi wale ambapo Ilugwa ile zahanati inahudumia zaidi ya visiwa vitano, inahudumia watu zaidi ya 20,000, tuombe basi zahanati hii iweze kusaidiwa kupandishwa kuwa kituo cha afya ili iweze kutoa huduma zinazostahili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kivuko cha MV Nyerere kimekuwa na matatizo ya mara kwa mara ya kuzimika katikati ya maji hali inayohatarisha maisha ya abiria, kwa mara ya mwisho nilipewa taarifa kuwa engine za kivuko hiki zingekamilika na kufungwa kabla ya mwezi Februari lakini sioni kinachoendelea. Ni lini engine za kivuko cha MV Nyerere zitafungwa na kuondoa kero ya usafiri kati ya Bugorola na Ukara?

Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ya usafiri kati ya Kisiwa cha Irugwa na Ukerewe ni ya hatari kutokana na ukweli kwamba inahitajika zaidi ya masaa manne kwa abiria kusafiri kati ya visiwa hivi viwili wakitumia mitumbwi jambo ambalo ni hatari. Ombi langu kwa Serikali itafakari na kusaidia upatikanaji wa usafiri wa boti/kivuko kati ya Irugwa kwenye wakazi zaidi ya 20,000 na Ukerewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu malipo kwa watumishi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), baada ya kampuni hii kudorora na meli nyingi kushindwa kufanya kazi, wafanyakazi wa kampuni hii hawajalipwa mishahara kwa miezi 23 jambo lisilo na afya. Serikali itumie vyombo vyake kubaini watumishi walio na matatizo waondolewe na wale waadilifu walipwe haki yao na hivyo kuongeza morali ya utendaji kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya nauli katika vivuko; utaratibu wa jumla kutoza kiwango fulani cha pesa kwa mizigo chini ya kilo 20 umekuwa na migogoro ya mara kwa mara kwa sababu wananchi wamekuwa wananyanyasika kwa kutozwa nauli kwa mizigo isiyostahili kama vile mabegi na vitu vingine vidogo vidogo ambavyo havistahili, hivyo, napendekeza malipo yoyote yaondolewe kwa mizigo ya chini ya kilo 20.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa dakika tano hizi nitajikita kwenye maeneo mawili. Kwanza kabisa nipende kupata kauli ya Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri, ni suala ambalo tumekuwa tukilishughulikia mara kwa mara. Tuna kivuko kinachounganisha Kisiwa cha Ukerewe na Kisiwa cha Ukala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kivuko hiki kinahudumia zaidi ya wananchi 50,000, kimekuwa kinaleta shida mara kwa mara na nimekuwa nawasiliana na Wizara. Sipendi siku moja tuje hapa kuomba rambirambi kwa sababu ya wananchi waliozama katika kivuko kile. Naomba nipate kauli ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka jana tumeahidiwa kwamba mpaka mwezi Desemba mashine mbili zilizokuwa zimeagizwa zingefungwa kwenye kivuko kile lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea. Niombe kauli ya Serikali mashine kwa ajili ya kivuko cha MV Nyerere kinachofanya kazi kati ya Bugolola na Ukala zinafungwa lini na kivuko hiki kiweze kuwa katika utendaji kazi mzuri na ulio salama kwa wakazi wa eneo lile?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine katika maeneo hayo hayo ya vivuko tuna Kisiwa cha Ilugwa. Wananchi wanasafiri zaidi ya masaa manne kuja Ukerewe. Wana-risk sana, wanasafiri kwa kutumia mitumbwi. Serikali ina mkakati gani kutupatia kivuko kwa ajili ya eneo lile?

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nichangie ni juu ya Kampuni ya Huduma za Meli. Kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 75, anaongelea juu ya kampuni hii. Mwaka 1999 kampuni hii ilibinafsishwa, lakini baada ya kubinafsishwa na kukosa watu wa kuichukua iliendelea kufanya kazi. Bahati mbaya sana kwamba vile vifaa na mashine kwa ajili ya matengenezo vilibinafsishwa lakini wale watumishi waliobaki kwenye kampuni hii walijikongoja wakaendelea kufanya kazi pamoja na kwamba kulikuwa na matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni nini, watumishi hawa waliobaki wakiwa wanafanya kazi kwenye kampuni hii wana miezi 23 sasa hawajalipwa mishahara. Hebu tuweze kutafakari kama ni sisi hawa watumishi wanaweza kuishi vipi? Inawezekana kweli kuna watu wamefanya vibaya kwenye kampuni ile, lakini basi Serikali iweze kufanya uchambuzi; ina vyombo vyake; ijue ni watu gani hawajafanya vizuri, watu gani wamehujumu kampuni ile na wasio na makosa waendelee na kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kukaa na watumishi miezi 23 hawajalipwa mishahara halafu tutegemee waendeshe kampuni hii wakiwa na tija na ufanisi, si kweli. Wakati wanasikia kwamba kuna trilioni moja sijui point tano imepotea halafu wao miezi 23 hawajalipwa mishahara hawawezi kuelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni muhimu sana Serikali iangalie namna gani ya kufanya watumishi hawa wapate haki yao ili waweze kufanya kazi katika mazingira yaliyo salama. Ni jambo jema kwamba sasa tuna Mtendaji Mkuu, Mkurugenzi ambaye wamemteua mwaka jana, ni mtu makini, mchapakazi, mbunifu, basi Serikali impe support.

Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya kumteua kumpa kampuni ile ambayo ilikuwa inaelekea kufa halafu wakam- dump wakamtelekeza pale hawatakuwa wamemsaidia, wampe nguvu, wamtie moyo, wampe msaada wa karibu ili aweze kusaidia kwenye kampuni hii ili iweze kufanya kazi kwa sababu ni kampuni muhimu sana kwa usafiri unaounganisha Ukerewe, Mwanza lakini na maeneo mengine; Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa, basi Serikali ifanye kile ambacho inapaswa kufanya wafanyakazi hawa waweze kulipwa mshahara wao waweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Mradi wa Maji Mjini Nansio. Bado mradi huu haujaweza kuwa na tija kufikia malengo yaliyotarajiwa kuondoa tatizo la maji kwa wananchi zaidi ya 70,000 katika Mji wa Nansio. Hili linatokokana na matatizo ya mara kwa mara kwenye mfumo wa mradi huu. Mfano, kupasuka kwa mabomba na wakati mwingine kukatwa kwa umeme kwenye mtambo wa kusukuma maji, kutopanuliwa kwa mtandao wa mabomba na kadhalika. Hali hii imekuwa inachangia kuendelea kwa maradhi mengi yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyokuwa safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri/ombi, Mamlaka ya Maji Mwanza (MWANAUSA) iweze kusimamia na kufuatilia kwa karibu ili kuondoa tatizo la maji katika Mji wa Nansio.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji vijijini (vijiji kumi) kutokamilika kwa haraka kwa mradi huu ni kikwazo kwa upatikanaji wa maji salama katika vijiji mbalimbali katika Wilaya ya Ukerewe. Hii inasababishwa pamoja na sababu nyingine kutokuwa na watumishi wa kutosha wenye utaalam katika fani ya maji mfano, wahandisi, mafundi mchundo na kadhalika. Ombi/ushauri wangu ni moja, Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ipatiwe wataalam wa kutosha katika Idara ya Maji. Mbili, wakandarasi wanaohusika katika usambazaji maji wafuatiliwe kwa karibu kupitia Mhandisi wa Maji Wilayani kulipwa kwa wakati ili mradi huu ukamilike kwa wakati/haraka na kutoa huduma kwa wananchi wengi kadri iwezekanavyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa dakika tano hizi kwangu ni chache sana lakini nitajitahidi niweze kuwasilisha ujumbe wangu. Uchumi wa Taifa kwa ujumla wake unategemea sana uchumi wa mtu mmoja mmoja na Wizara hii ya Uvuvi na Mifugo ni Wizara muhimu sana specifically kwenye eneo la uvuvi linachangia asilimia 2.2 ya pato la Taifa, lakini sioni kama Taifa tunaweka umuhimu kwenye uvuvi na mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa napitia, kwa mfano nilipitia mwongozo wa maandilizi ya mpango wa bajeti 2018/2019, sioni eneo lolote ambalo mpango huu unagusa eneo la uvuvi, kidogo imenisikitisha sana. Hata hivyo, uvuvi kwa ujumla wake kwa mfano kwenye eneo la Kanda la Ziwa ni siasa, ni maisha na ni kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikiongelea kwa mfano operesheni sangara, Mheshimiwa Kanyasu ameongea vizuri sana kinachofanyika kwenye Kanda ya Ziwa hususani operesheni sangara ni unyanyasaji, ni uonevu, ni dhuluma, inafanyika dhidi ya wavuvi. Matendo wanayofanyiwa si mambo ambayo yanapaswa kuendekezwa wala kuyakubali katika Taifa hili. Watu wanafilisiwa, wanapoteza maisha wanafanyiwa vitendo vya ajabu sana ambavyo vinatia simanzi na huzuni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukizingatia kwamba hii Sekta ya Uvuvi, kwa mfano, watu takribani milioni nne wanategemea uvuvi na implication yake ni nini hata wale wanaotegemea watu hawa zaidi ya watu milioni tano, milioni kumi wanategemea sekta hii ya Uvuvi. Kwa hiyo, unapovuruga Sekta hii ya Uvuvi wananchi zaidi ya milioni kumi ambao ni zaidi ya asilimia 20 ya wananchi wa Taifa hili wanaathirika na mambo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende moja kwa moja kwenye ushauri kwa sababu hatuwezi kuendelea kufanya haya wananchi wanaathirika, leo asubuhi tumeahirisha Bunge hapa na toka nje napigiwa na wavuvi kutoka Ukerewe. Kwa sababu Operesheni Sangara sasa kuna watu ama ni wahuni tu au namna gani wanatumia njia hii kuwabughudhi watu kule. Wameenda kule kwa sababu walichomewa nyavu zao wametafuta rasilimali pesa wakanunua nyavu nyingine zinazotakiwa, wameenda watu tena leo wanataka kuwachomea zile nyavu kwamba siyo halali, sasa maisha gani watu wataishi katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niende tu kwenye ushauri; la kwanza nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, lakini sijaona sehemu yoyote ambayo kuna eneo la mafunzo kwa wavuvi wetu, kwa sababu haiwezekani kwenda kuwaadhibu tu wavuvi hata kama ni mtoto huwezi kwenda kumuadhibu kabla ya kumwonesha ni kitu gani anapaswa afanye. Sasa tunatakiwa tutoe elimu kwa wavuvi wetu, tujue kwamba hawa ni wavuvi na shughuli zao ni uvuvi. Sasa ni uvuvi gani sasa wanatakiwa waufanye, ni wajibu wetu kama Serikali kutoa elimu hii lakini kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijaona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kuna marekebisho ya sheria namba 22 ya mwaka 2003, kwenye hotuba wameonyesha iko kwenye mchakato, kwenye hatua nzuri, lakini je, sheria hii wakati wa kufanya marekebisho wadau wameshirikishwa kwa kiasi gani. Kwa sababu moja kati ya malalamiko ni kwamba tumekuwa tunatunga sheria na kufanya marekebisho, lakini hatuwahusishi wadau kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo ni kwamba, tunatunga sheria za upande mmoja bila wadau kushiriki na kutoa changamoto na mtazamo wao juu ya yale ambayo tunayatunga. Kwa hiyo, niombe kwamba sheria hii au marekebisho haya yatakapokuwa yanaletwa tujiridhishe kwamba wadau hasa wavuvi wameshirikishwa katika mabadiliko ya sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mwingine ni juu ya nyavu. Tumezuia nyavu hizi walizokuwa wanatumia kwamba ni nyavu haramu, sasa hizi nyavu zinazopaswa kutumika ziko wapi? Kwa sababu wavuvi hawana nyavu hizi, wale ambao walikuwa wanaagiza nyavu hizi wamezuiliwa kuingiza nyavu hizi, sasa nini kitakachotumika na wale waliopewa jukumu ya kutengeneza nyavu hizi walikuwa wanatengeneza vyandarua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nyavu zinazotumika sasa hivi kwa mfano za dagaa watu wanatumia ndani ya mwezi mmoja nyavu zile zimeharibika, inabidi wanunue nyavu nyingine, ni gharama kubwa kwa wavuvi wetu hawa ambao kwanza tumewatia umaskini kwa kuwachomea nyavu zao, halafu inabidi watafute rasilimali pesa nyingine kununua nyavu nyingine. Kwa hiyo, kama hatuna uwezo wa kuzalisha nyavu hapa nchini turuhusu nyavu kutoka nje ziweze kuingizwa nchini ili wavuvi waweze kufanya shughuli zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwa Mheshimiwa Waziri niombe, wadau wangu Ukerewe sisi tunavua samaki aina nyingi. Kuna samaki aina ya gogogo kwetu maarufu kama ngere ni samaki maalum na muhimu sana wanavuliwa kwa msimu, watuambie wanavuliwa kwa nyavu size gani na wale wanapatikana kwa msimu. Msimu wake ni kuanzia mwezi huu kuendelea mpaka mwezi wa Nane.

Mheshimiwa Naibu Spika, watafiti wa Mheshimiwa Waziri inawezekana hawajui kwamba samaki hawa wanapatikana kwa msimu, lakini wale wanatakiwa sasa ndio waanze kuvuliwa. Kwa hiyo, tunaomba sasa watuambie tunavua kwa nyavu size gani ili wananchi waweze kupata, lakini…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, vivutio vya utalii visivyotambuliwa na hivyo kutangazwa; kuna vivutio vingi sana katika visiwa vya Ukerewe ambavyo vikitambuliwa na kutangazwa vinaweza kuingizia Taifa pesa nyingi sana, miongoni mwa vivutio hivi ni:-

(a) Jiwe linalocheza Kisiwani Ukara katika Wilaya ya Ukerewe;
(b) Mapango ya Handebezyo;
(c) Makazi/Majengo ya Chifu Lukumbuzya; na
(d) Fukwe za kipekee maeneo ya Rubya na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, hivyo Wizara ione umuhimu wa kutambua vivutio hivi, kuvijengea mazingira mazuri na kuvitangaza ili viweze kuliingizia Taifa mapato.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi katika maeneo ya pembezoni, mazingira yao ni magumu. Kutokana na jiografia ya Ukerewe ambapo ina visiwa (38) Watumishi wengi wanakuja kuripoti na kuondoka, hali ambayo inasababisha upungufu mkubwa wa watumishi hasa katika maeneo ya afya na elimu. Zahanati zetu, vituo vya afya pamoja na shule zina upungufu mkubwa wa watumishi katika Visiwa vya Ukerewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi au ushauri wangu ni kwamba, moja; pamoja na Halmashauri zetu kuwa na mipango mbalimbali ya motisha kwa watumishi wanaopangwa kwenye Halmashauri zetu, Serikali iwe na mpango maalum wa kuhakikisha kuwa watumishi wanaofanya kazi katika maeneo kama ya Ukerewe wapate package fulani ya mazingira magumu ili wasijione kama watu waliopewa adhabu na hivyo kutafuta kila njia kuondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; kutokana na changamoto ya watumishi kuripoti na kuondoka katika maeneo kama Ukerewe, katika mgao wa watumishi Visiwa vya Ukerewe viangaliwe kwa mtazamo wa pekee na hivyo kupewa idadi ya kutosha ya wataalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malipo ya Wenyeviti wa Vijiji/Mitaa na Vitongoji; wananchi ndiyo injini kubwa ya maendeleo kwenye Halmashauri zetu lakini wanaweza kuwa na tija pale wanaporatibiwa na kusimamiwa na viongozi wetu wa ngazi za chini, mfano, Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji lakini viongozi hawa wamekuwa na mfumo mbovu na malipo duni wakati wanafanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza au nashauri kuwa, mfumo wa malipo kwa viongozi hawa ubadilishwe ikiwezekana basi Serikali Kuu iweze kuwalipa moja kwa moja badala ya kupitia Halmashauri kwa sababu nyingi zimekuwa haziwalipi viongozi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango kinacholipwa kwa viongozi hawa kiongezwe ili kiendane na hali halisi ya maisha ikizingatiwa kwamba wanatumia muda wao mwingi kuhamasisha na kusimamia shughuli za maendeleo, muda ambao wangetumia katika shughuli zao binafsi za uzalishaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kumekuwa na mafanikio yasiyo endelevu kwenye Sekta ya Michezo, hii ni kwa sababu wanamichezo wetu wanakosa misingi imara ya kitaaluma kimichezo. Msingi wa kitaaluma unaweza kupatikana vizuri zaidi kupitia shule zetu kwa ngazi mbalimbali kuanzia Shule za Chekechea na kuendelea. Kikwazo kikubwa kimekuwa ni kutokuwa na Walimu ambao ni Wataalam wa Michezo na Miundombinu ya kutumia kushiriki michezo, hali ambayo imekuwa inaathiri sana vipaji vya wanamichezo.

Mheshimiwa Spika, hivyo nashauri, michezo iwe ni moja ya masomo katika mitaala ya shule zetu hali ambayo itafanya watoto wote wenye vipaji mbalimbali waweze kuviendeleza. Kuwe na mkakati maalum wa kuandaa walimu watakaotumika kuwafunza vijana wetu na kukuza vipaji mbalimbali kwenye shule, vilabu vya michezo na kadhalika. Kwa mfano, timu zetu za mpira wa miguu hivi sasa zinafundishwa na walimu kutoka nje na hakuna idadi kubwa ya walimu wa Kitanzania wanaofundisha soka nje ya nchi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya Chuo cha Ufundi Stadi Mkoani Ukerewe, ongezeko kubwa la vijana wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari usioendana na uwepo wa miundombinu wezeshi kwenye taasisi za elimu umeathiri sana ufaulu wa vijana wetu. Hivyo ukichangiwa na jiografia ya Visiwa vya Ukerewe vijana wengi wamekuwa wanaona kuwa uvuvi ndiyo suluhisho lao kimaisha, hali hii imepekelekea uharibifu wa mazingira na uvuvi usio endelevu kwa sababu tu ya kukosa njia mbadala ya kuwawezesha kukabiliana na changamoto za maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hii uwepo wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika Visiwa vya Ukerewe kutasaidia kwanza kuandaa vijana wetu kuelekea kwenye nchi ya viwanda, kuwaandaa vijana kuwa na fikra za kujiajiri kiufundi zaidi badala ya fikira za kuajiriwa hali ambayo imekuwa inapelekea kutumia muda mwingi kutafuta kazi badala ya kujiajiri na kupunguza uvuvi haramu unaotokana na wimbi kubwa la vijana kuamini katika uvuvi tu, kumbe kupitia ufundi wangeweza kufanya shughuli nyingine za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa kuruhusu vijana kurudia shule hasa elimu ya msingi. Maeneo ya vijijini ambapo kutokana na mazingira, vijana wengi wamekuwa wanamaliza elimu ya msingi katika umri mdogo lakini pia wakiwa na uwezo mdogo kitaaluma hali ambayo huwapa mazingira magumu sana wazazi au walezi wa watoto hawa. Hivyo, iwapo Wizara itaruhusu watoto hawa kurudia shule, itawasaidia kuimarika kitaaluma na kukomaa kiakili kabla ya kuingia katika hatua inayofuata ya elimu ya sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa washauri kwa watoto pale wanapohitaji kuchagua masomo (mchepuo). Vijana wengi wamekuwa wanachagua masomo kwa mkumbo tu ama fasheni na baadaye hugundua kuwa hawakuwa wamefanya chagua sahihi. Hii ni kutokana na kukosa ushauri wakati wa uchaguzi wa masomo. Hivyo, ni muhimu Serikali kupitia Wizara kuhakikisha kunakuwa na Walimu washauri kwenye mashule yote ili kusaidia kuwashauri vijana pale ambapo wanahitaji kufanya uchaguzi wa masomo ya kitaaluma.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia. Kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii ya uhai na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu lakini nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa sababu ni bajeti yangu ya kwanza nikiwa upande huu lakini hasa kwa sababu ni bajeti ya kwanza tokea limetokea tukio baya sana la kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere, nitumie nafasi hii kumwomba Mwenyezi Mungu ampumzishe roho za marehemu wote 228 waliopoteza maisha kwenye ajali ile. Tatu, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa sana anayoifanya kuliongoza Taifa hili na kuwaletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Jafo na wasaidizi wake na Mheshimiwa Mkuchika na wasaidizi wake wote. Hakika wanafanya kazi kubwa sana, wanatendea haki Wizara zao na wanawatendea haki wananchi wa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utakuwa kwenye maeneo mawili. La kwanza niombe tutambue kwamba tunaweza kwenda kasi sana kwa maendeleo katika nchi hii kama tutakuwa na Serikali za Mitaa zilizo imara. Kimsingi tunaposema uimara wa Serikali za Mitaa ni kwa sababu huduma zote za kijamii ziko chini ya Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, kama tutaimarisha Serikali za Mitaa, kasi ya maendeleo kama inavyokwenda sasa itakuwa nzuri na itawagusa zaidi wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa mpaka sasa mambo yanaenda vizuri, naipongeza Serikali kwa kazi kubwa sana wanayoifanya kwa mfano Ukerewe kwenye eneo la afya kazi kubwa sana imefanyika, vituo viwili vimepata pesa, vinakamilika. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI lakini nimpongeze zaidi Mheshimiwa Rais kwa sababu baada ya matatizo yale alielekeza pesa zijenge Kituo cha Afya cha Bwisya, kituo kinaelekea kukamilika na naipongeza sana Serikali kwa uamuzi huu. Tatizo kubwa ambalo napenda Serikali itambue, ujenzi wa vituo hivi vya afya iende sambamba na upatikanaji wa watumishi ili viwe na tija, visikamilike halafu vikashindwa kutoa huduma ile iliyokuwa inatarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la elimu kazi kubwa sana imefanyika kupitia elimu bila malipo, watoto wengi sana wameweza kusajiliwa kwenye shule zetu za msingi. Kusajiliwa kwa watoto wengi kumeenda sambamba na upungufu wa miundombinu kama madarasa. Niipongeze sana Serikali hivi karibuni imejitahidi kuleta pesa kwa ajili ya kuboresha miundombinu na kwenye eneo letu la Ukerewe kupitia Mfuko wa Jimbo lakini pamoja na wananchi, niwapongeze sana wananchi wa Visiwa vya Ukerewe, tumehamasishana tumejenga maboma zaidi ya 300 kwa ajili ya madarasa, niombe Serikali sasa itusaidie kuezeka madarasa haya. Kwa sababu wananchi wamejitoa sana na Mbunge wao nimejitoa, nimepeleka mifuko zaidi ya 3,000 kwenye shule zetu mbalimbali, basi Serikali itusaidie tuweze kuezeka maboma haya ili angalau watoto wetu wapate madarasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwenye utekelezaji nimeona kuna wazee zaidi ya 700,000 wametambuliwa lakini katika wazee hao ni asilimia 33 tu ya wazee hawa ndiyo waliopata vitambulisho ili waweze kupata huduma ya afya. Kuna tatizo kubwa sana huko chini, wazee wetu wananyanyasika sana wanapokwenda kupata huduma za afya. Niombe Wizara ya TAMISEMI iweke ukomo wa muda ili Halmashauri zetu ziweze kuwatambua wazee hawa na kupata vitambulisho ili wapate huduma za afya kuliko kuendelea kunyanyasika kama ambavyo imekuwa inatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende eneo la TARURA, wamesema Wabunge wengi sana, niwapongeze TARURA lakini nampongeza sana Mtendaji Mkuu wa TARURA amekuwa msikivu pamoja na changamoto mbalimbali anazokabiliana nazo. Kwa kazi kubwa wanazozifanya TARURA tukizingatia kwamba wana mtandao mkubwa sana wa barabara kilomita zaidi ya 100,000 ni nyingi sana lakini kwa fedha wanazozipata tutaendelea kulalamika. Kwa hiyo, niombe katika bajeti tunayoendelea nayo Serikali ilete pendekezo tuweze kubadili fomula ya ugawaji wa pesa hizi ili TARURA angalau waweze kupata asilima 40 au asilimia 50 tuweze kuwapa uwezo washughulikie barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipoanza kuzungumza nilisema juu ya umuhimu wa kuimarisha Serikali za Mitaa na hasa Halmashauri zetu kwa sababu ndipo sehemu ambapo miradi mingi inayowagusa wananchi inasimamiwa. Tunapoongelea Serikali za Mitaa hasa Halmashauri tunaongelea Madiwani na watumishi. Kuna changamoto kubwa katika suala zima la posho kwa ajili ya Madiwani wetu. Hili ni tatizo kubwa sana ambalo linaathiri utendaji wa Madiwani wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni umetolewa mwongozo juu ya posho za Madiwani katika vikao vyetu vya Halmashauri. Madiwani hawa wanafanya kazi kubwa sana lakini wanapokwenda kuhudhuria vikao wanalipwa Sh.40,000 ni fedha ndogo sana. Kwa hiyo, niombe TAMISEMI muangalie upya suala hili ili angalau kuweza kuwajengea kujiamini Madiwani hawa ambao wanafanya kazi kubwa sana ya kusimamia miradi yetu kule chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji, hawa ni watu muhimu sana lakini malipo wanayopata; posho zao za kila mwezi lakini hata baada ya kutoka kwenye nafasi zao wanazotumikia ni kitu gani wanakipata? Nashauri TAMISEMI aingalie eneo hili pamoja na kwamba inawezekana wakawa wengi sana Serikali isiweze kuwalipa wote lakini tuangalie kama inawezekana baada ya kipindi chao cha utumishi kuwe na package fulani ambayo wanaweza kuipata ili wawe na moyo wa kuendelea kufanya kazi na kusimamia maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano Ukerewe, Mwenyekiti wa Kitongoji analipwa Sh.3,000 kwa mwezi. Tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba kwa siku analipwa Sh.100 kwa ajili ya kusimamia shughuli za maendeleo, inawavunja moyo. Kwa hiyo, niombe Serikali iliangalie sana suala hili.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Kwanza niunge mkono hoja iliyo Mezani kwetu tunayoijadili lakini nitumie fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote katika Wizara hii. Kimsingi mnafanya kazi kubwa sana ingawa hamjafikia asilimia 100 kulingana na matarajio yetu, lakini niwapongeze mnafanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii vilevile kumpongeza sana Eng. Sanga, amekuwa msaada mkubwa sana kwa watu wa Kanda yetu na hasa kwenye eneo letu la Visiwa vya Ukerewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utakuwa katika maeneo kama matatu kama muda utaniruhusu. La kwanza, nianze na eneo la Ukerewe. Ukerewe tuna miradi takribani mitano, inakwenda vizuri tunashukuru sana lakini nimepitia hotuba, ukurasa wa 64 unaongelea mradi wa vijiji 301 vitakavyofaidika na mradi ule wa maji kutoka Ziwa Victoria. Ni mradi mzuri, kwenye Jimbo la Ukerewe kama utakamilika utatusaidia vijiji takribani 33 na kwa ujumla wake utakuwa umesaidia tatizo la maji mpaka kufikia zaidi ya asilimia 80. Rai yangu tu ni kuomba utekelezwe mapema ili uweze kutusaidia hasa kwenye eneo la Visiwa vya Ukerewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, Ukerewe pale tuna mradi mkubwa sana wa maji, ulizinduliwa na Mheshimwa Rais mwaka jana; Mradi wa Maji wa Nansio. Ni mradi mkubwa sana lakini kwa mazingira yalivyo mpaka sasa kimsingi uko under-utilized. Una wateja kama 2,900 pekee na una uwezo mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ni kwamba Mamlaka ya Maji Nansio haina uwezo wa ku-extend ile distribution network matokeo yake Serikali sasa kupitia Wizara mmekuwa mna-support Mamlaka ile ili iweze kujiendesha. Ushauri wangu ili kuondokana na kila wakati kuisaidia Mamlaka kujiendesha mnge-inject fedha kwenye mradi huu ili Mamlaka ya Maji Nansio pale iweze ku-extend hii network ya usambazaji wa maji kwa vile ikiwa na wateja wengi inaweza ikajiendesha kwa kukusanya makusanyo makubwa badala ya kuwa mnai-support kila wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana Wizara ifanye jambo hili, kwa sababu sioni kama ni tija sana kila wakati kuendelea kuiwezesha Mamlaka hii iweze kujiendesha kuliko kama mnge-inject tu kiasi fulani cha fedha ili mamlaka hii ikaweza ku-extend usambazaji wa maji; mtakuwa mmetusaidia sana. Pamoja na changamoto nyingine ndogo lakini mambo yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, kuna watu wana eneo wanahitaji maji pale Ukerewe. Mheshimiwa Waziri ulipokuja Ukerewe nilishauri jambo hili. Inawezekana uwezo wa ku-apply kupata maji ni mdogo; mngeandaa programu fulani ili ikiwezekana wananchi hawa wakafungiwa maji na baada ya kufungiwa maji, hata kama ni kwa madeni ili kwamba maji watakapoanza kulipa zile bills za maji watakatwa pamoja na kile kiwango cha pesa ambacho Wizara ime-subsidize wakati wa kuwaunganishia maji. Inawezekana miradi hii ikawa na wateja wengi na hatimaye mamlaka hizi ziweze kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, hili nilitaka kushauri. Kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge, miradi mingi ya maji inasuasua sana, kuna matatizo mengi makubwa. Hata hivyo kwa mtazamo wangu tuna tatizo kubwa sana la wataalam wa maji kwenye halmashauri zetu na maeneo yetu. Ukichunguza matokeo makubwa yanaanzia hata kwenye usanifu wa miradi, matokeo yake tunakuwa na miradi ambayo inakuwa haina tija. Kwa hiyo tuhakikishe kwamba tunaajiri watu wa kutosha, hususan wenye kada hii ya maji ili angalau miradi yetu iweze kukamilika na iwe na tija kuweza kutoa manufaa tunayoyatarajia kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani nilikuwa kwenye kamati ya LAAC tulitembelea miradi mingi sana. kwenye maeneo ya vijijini miradi hii ikishakamilika uankuta wananchi hawana uwezo wa kuiendesha miradi hii kwa sababu gharama za uzalishaji zinakuwa kubwa kwa sababu chanzo cha maji ama kinatumia mafuta au kinatumia umeme. Tunaweza tukaepuka hili kama tutaondoa kodi kwenye mashine zile zinazoingia kwa ajili ya kuzalisha maji. Vile vile kama tutatumia solar systems kwenye uzalishaji wa maji inawezekana production cost itakuwa ndogo na kwa maana hiyo wananchi wa kawaida hawa wanaweza wakamudu gharama hizi za kuendesha miradi hii ya maji na ikaweza kufanya kazi vizuri wananchi wakafaidika na miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kama mapendekezo yalivyoletwa na Kamati husika, sina shaka, ninaomba tuungane na mapendekezo ya Kamati hii kama ambavyo tumekuwa tukijadili kwa miaka mitatu. Kwa sababu matatizo mengi makubwa tuliyo nayo kwenye maji ni kwa sababu hatuna pesa za kutosha. Kama tukiongeza pesa kwenye mfuko wa maji inawezekana tukaondokana na tatizo hili kwa sehemu kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kunakuwa na kigugumizi, kwamba ama kutoa kwenye mafuta au namna gani, lakini kama Serikali ridhieni pendekezo hili, kwa namna yoyote itakayoonekana kwamba inawezekana, ama kutoa kwenye mawasiliano. For instance tukichukua labda kwa gigabyte moja tukitoa shilingi mia moja ninaamini tunaweza kuwa na makusanyo makubwa sana ambayo yanaweza kutunisha mfuko huu wa maji kuliko hiki cha maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tukiangali kwa bajeti ya mwaka huu inatolewa asilimia 51 ambayo ni ndogo sana kuweza kukabiliana na tatizo la maji tulilo nalo kwenye nchi hii. kwa hiyo ninaungana kabisa na mapendekezo ya Kamati, kwamba ni muhimu tukaboresha mfuko wa maji ili hatimaye usambazaji wa maji hususan kwa wananchi wa vijijini ukawa kwenye kiwango kikubwa ili tuweze kutimiza azma ya kumtua mama ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache nashukuru sana kwa nafasi hii uliyonipa. (Makofi)

MWENYEKITI: Unga mkono hoja.

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitangulia mkono hoja; kwa mara nyingine ninaunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, vifaa kwa ajili ya ICU. Pamoja na mazingira magumu kijiografia kwenye visiwa vya Ukerewe bado Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe haikuwa na ICU. Hivi sasa tumepata mfadhili anayetujengea jengo la upasuaji (theatre). Hivyo basi, lililokuwa jengo la upasuaji linabadilishwa kuwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) lakini patakuwa hakuna vifaa kwa ajili ya chumba hicho. Naomba Wizara isaidie kutoa vifaa kwa ajili ya chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwenye Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe (Nansio).

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la umeme. Shughuli za utoaji huduma za afya zinaathiriwa sana na tatizo la umeme. Mpango wa wilaya ilikuwa kutumia shilingi milioni 70 kutoka mfumo wa RBF lakini pesa hizo zimezuiliwa mpaka sasa kutokana na mgongano kati ya Wizara mbili, pesa hizi ilikuwa zitumike kununua generator/solar system kama standby power system. Naomba Wizara itusaidie kupata ruhusa ya kutumia pesa hizi kutatua tatizo la umeme kwenye Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, gari la wagonjwa. Baada ya ajali ya MV Nyerere tarehe 20/09/2018 katika Kisiwa cha Ukara, Mheshimiwa Rais alielekeza ujenzi/ukarabati wa Kituo cha Afya Bwisya ambacho kiko hatua za mwisho kukamilika. Tarehe 15/11/2018 Mheshimiwa Waziri wa Afya wakati akijibu swali langu Bungeni aliahidi kutupatia gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Bwisya. Gari hili ni muhimu sana kuokoa maisha ya watu wetu katika visiwa hivi. Naomba gari hili litolewe na kupelekwa kwenye Kituo cha Afya Bwisya.

Mheshimiwa Naibu Spika, vituo vya afya. Ili kufika katika Kisiwa cha Irugwa inakubidi utumie zaidi ya saa nne kwa usafiri wa majini. Hali hii ya kijiografia inaweka hatarini maisha ya wananchi walio katika Visiwa hivi vya Irugwa vyenye wakazi zaidi ya 20,000. Hivyo, Kituo cha Afya kinahitajika kwenye kisiwa hiki ili kuokoa maisha ya watu wetu. Kwa kuwa wananchi wameanza ujenzi wa Kituo cha Afya Irugwa basi Wizara ituunge mkono ili tukamilishe kituo hiki kwa kukiingiza kwenye mpango wa uboreshaji wa vituo vya afya nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi na vifaa. Kwa kuwa Kituo cha Afya Bwisya kinakamilika kama ilivyo Kituo cha Afya cha Muriti, Wizara ifanye maandalizi ya kupeleka vifaa na watumishi kwenye vituo hivi bila kusahau Hospitali ya wilaya ili wananchi wetu wapate huduma ili kukidhi malengo tarajiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, kivuko kipya kati ya Bugorola – Ukara. Pamoja na jitihada za Serikali kuanza mchakato wa utengenezaji wa kivuko kipya baada ya ajali ya MV Nyerere, mchakato huu unaenda taratibu. Kivuko kilichopo sasa cha MV Saba Saba kina matatizo mengi hali inayoendeleza hofu kwa watumiaji wa kivuko hiki. Ombi, kivuko hiki kikikamilika mapema ili kinusuru maisha ya watu wetu. Pia uangaliwe uwezekano wa kuweka usafiri wa uhakika kwenye maeneo ya Kitale – Irugwa na Kakukuru – Gana.

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa kifusi kwa ajili ya utengenezaji wa barabara. TANROADS wamekuwa na kawaida ya kuchimba kifusi/changarawe pembezoni mwa barabara jambo ambalo limekuwa linaacha mashimo makubwa sana na kusababisha vifo. Mfano, wiki iliyopita tarehe 9 Mei, 2019 shimo lililochimbwa kwa ajili ya kifusi eneo la Kijiji cha Nakamwa, Kata ya Namilembe, Wilaya ya Ukerewe limesababisha vifo vya watu wawili baada ya gari kutumbukia katika shimo hilo. Hii ni moja ya matukio ya kifo na majeruhi ambayo yamekuwa yanatokea mara kwa mara Wilayani Ukerewe. Ushauri, baada ya shughuli za ujenzi wa barabara mashimo haya yamekuwa yanafukiwa.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara ya lami; kwa kuwa barabara ya Bukindo – Murutunguru – Bukonyo ni muhimu sana kwa uchumi wa ukerewe na sehemu ya barabara hii ilishafanyiwa upembuzi yakinifu, michoro na makadirio tayari yalishaandaliwa tayari yakisubiri upatikanaji wa fedha ili ijengwe. Naomba Wizara isaidie upatikanaji wa fedha ili barabara hii iweze kujengwa kwani ni kilometa saba tu.

Mheshimiwa Spika, wakati wa ujio wa Mheshimiwa Rais Visiwani Ukerewe tarehe 5 Septemba, 2018 aliahidi ujenzi wa barabara kilometa 14 kutoka Lugezi – Nansio kwa kiwango cha lami. Naomba Serikali itekeleze ahadi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nachangia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, umuhimu wa uwekezaji katika utafiti; ni muhimu sana kuwekeza katika utafiti hasa kubaini aina ya udongo na kutambua/kushauri ni aina gani ya mazao yalimwe na kupandwa kwenye eneo husika. Jambo hili litasaidia kufanya kilimo chenye tija na mazao mengi yatakayotokana na ushauri wa kitaalam. Mfano, Visiwa vya Ukerewe vyenye eneo la kilomita za mraba 6400, ni asilimia 10 tu ambayo ni nchi kavu. Kwa sababu ya kilimo cha kujirudiarudia hatimaye sasa ardhi yake imechoka na haina rutuba tena. Zao kuu ambalo ni muhogo halistawi tena pamoja na mazao mengine.

Mheshimiwa Spika, hivyo, Wizara pamoja na maeneo mengine inatakiwa ipeleke wataalam wake visiwani Ukerewe ili wafanye utafiti wa kisayansi kubaini aina ya udongo na kushauri yapandwe na kwa utaratibu upi. Jambo hili itasaidia eneo letu dogo litumike kwa ufanisi na kwa tija na kuondoa tatizo la upungufu wa chakula kwenye Visiwa vya Ukerewe.

Mheshimiwa Spika, uwekezaji na umuhimu wa umwagiliaji, ni jambo lililo wazi kwa kuwa zama za kufanya kilimo cha kutegemea mvua kimepitwa na wakati. Kwa kuwa nchi yetu imebahatika kuwa na vyanzo vingi vya maji ni vizuri sana kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji tukitumia vyanzo hivi vya maji. Mfano, Visiwa vya Ukerewe ambavyo vimezungukwa na maji havitakiwi kuwa na shida ya chakula na vingeweza kuhudumia maeneo mengine kwa chakula kama tu Wizara ingewekeza kwenye umwagiliaji. Mradi wa umwagiliaji wa Miyogwezi na Bonde la Bugorola umesimama kwa sababu ya kukosa fedha.

Mheshimiwa Spika, ushauri, Wizara ifufue mradi wa umwangiliaji Miyogwezi na Bungorola ili kutumia rasilimali maji yaliyopo Ukerewe na kuifanya Ukerewe kuwa wazalishaji wakubwa itakayofanya wajitoshereze kwa chakula na ikiwezekana kuhudumia maeneo mengine kwa chakula.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata fursa hii ya kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Mchango wangu utakuwa zaidi kwenye eneo la uvuvi, na hii ni kwa sababu ninatoka Ukerewe; na Ukerewe inaundwa na Visiwa. Katika eneo letu square kilometer 6,400 zaidi ya asilimia 90 ni maji. Katika idadi ya watu tuliyonayo 400,000 na sehemu zaidi ya asilimia 95 wanategemea zaidi uvuvi; kwa hiyo mchango wangu utajikita zaidi kwenye eneo la uvuvi.

Mheshimiwa Spika, uvuvi na mifugo unachangia sehemu kubwa ya Pato la Taifa. Ninaipongeza Serikali kwa jitihada zake za kulinda rasilimali za nchi hii ili ziweze kuwasaidia Watanzania kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na operesheni ambazo zimekuwa zinaendelea kwenye maeneo mbalimbali kwenye uvuvi na mifugo; lakini kwenye eneo la uvuvi operesheni hizi zimekuwa na madhara. Binafsi nimekuwa muumini mkubwa sana wa uvuvi endelevu na nimekuwa ninaunga mkono operesheni hizi kwa dhamira ya kulinda rasilimali zetu; lakini madhara kadhaa ambayo yamekuwa yanasababishwa na operesheni hizi nimekuwa siku zote sikubaliane nazo.

Mheshimiwa Spika, tunafanya mambo haya, tunatengeneza sera, tunatunga sheria, tunafanya operesheni hizi ili kulinda rasilimali lakini wakati huohuo tukihakikisha kwamba maisha ya wananchi wetu kule chini hayaathiriki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa zimefanyika operesheni hizi, bahati mbaya sana hapo nyuma tulikuwa na dada mmoja ametajwa jana anaitwa dada Judith, alitusababishia madhara makubwa sana kwenye eneo la Ukerewe, amepelekwa Kigoma kule. Sasa operesheni hizi niombe sana Wizara, kwa mfano kule Ukerewe kwenye Jimbo langu wananchi wengi wameathirika na operesheni hizi. Wamedhulumiwa, wamenyanyaswa, wamechomewa nyavu zao.

Mheshimiwa Spika, lakini tatizo kubwa linalonisumbua mimi, tunafanya operesheni hizi lakini mbadala wake ni upi? Kwa sababu tukumbuke sehemu Kama Kanda ya Ziwa specifically kwa Ukerewe zaidi ya asilimia 95 ya vijana wameajiriwa na kujiajiri kupitia uvuvi. Kwa hiyo unapovuruga mfumo wote wa uvuvi automatically unaathiri maisha yao lakini unaathiri vilevile maisha ya ujumla ya kiuchumi ya Visiwa vya Ukerewe kwa sababu kila kitu kiuchumi kinategemea shughuli za uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna marekebisho ya sheria kwa mfano kwenye nyavu zitakazotumika kuvua dagaa. Nimewahi kusema hapa dagaa hawavuliwi kwa kunyoosha wavu kwamba wale dagaa wanase kwenye wavu ndio uwakusanye hapana, dagaa wanavuliwa maji marefu tena kwa kuchotwa, sasa kule tulikuwa tunatumia nyavu za milimita sita, wameleta milimita nane mpaka milimita kumi inakuwa ni hasara kubwa sana kwa wavuvi wetu wanaoafanya shughuli za uvuvi hususani uvuvi wa dagaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nashauri; la kwanza, badala ya kuweka vikwazo kwenye uvuvi huu kwa ku-limit saizi za nyavu jambo ambalo linaathiri sana wavuvi wetu, kwa sababu mvuvi tuchukulie gharama anazoingia kwenda kuvua ni kubwa sana, halafu tuchukulie anatumia mafuta ya taa, anatumia petroli bado kuajiri wale watumishi anatumia zaidi ya shilingi 300,000 au shilingi 400,000 kwa siku halafu kwa kutumia nyavu za milimita kumi anapata dagaa sijui thamani yake shilingi 30,000 au shilingi 40,000 bado kuna kodi nyingi anapaswa alipe tunakuwa hatuwatendei haki wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo badala ya ku-limit saizi za nyavu, nishauri Wizara iangalie uwezekano wa kufanya uvuvi wa msimu, kwamba kuanzia mwezi fulani mpaka mwezi fulani kusifanyike uvuvi, baadaye mwezi fulani na kuendelea uvuvi ufanyike. Mbaya zaidi tunaweka limitation hizi kwenye maeneo yetu, wenzetu majirani zetu Kenya, Uganda wanaendelea na shughuli za uvuvi, samaki hawako eneo moja, tunapowazuia hapa leo wanahama wanaenda Kenya, wanaenda Uganda na Congo wenzetu kule wanawavua wale samaki. Kwa hiyo tunawasababishia umasikini wananchi wetu kwa faida ya majirani zetu, kwa hiyo ni muhimu sana Wizara iliangalie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiachilia mbali eneo hili la uvuvi wa dagaa sijui na vitu gani, tumeweka saizi za nyavu, tukumbuke kuna species nyingi sana za samaki ziwani, kuna samaki wengine ambao ukiweka wavu wa milimita tatu, kuna samaki wengine wadogo ambao hawakui kufikia kiwango hicho, sijui mmefanya research kwa kiwango gani. Tukumbuke ecological disaster kwenye Ziwa Victoria imesababishwa na upandikizaji wa sangara kwenye ziwa lile. Kwa hiyo katika species zilizokuwepo zaidi ya 500 nyingi zimepungua kwa sababu samaki wengi wanatumika kama chakula na wanaliwa na sangara. Sasa tunawalinda sangara, hawa samaki wengine tunatumia mfumo gani kuwalinda, matokeo yake tunawaadhibu wananchi kwamba wasivue samaki wale kwa sababu tu kwamba wanapungua kitu ambacho wanaliwa na sangara, sasa hatuwatendei haki wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule Ukerewe kila wakati wananisumbua wananipigia simu bwana tunazuiliwa kuvua ngere kwa sheria ipi, kwa utaratibu upi? Tunazuiliwa kuvua furu kwa utaratibu huu, kwa sheria ipi? Kwa hiyo niombe Wizara itoe tamko la kuruhusu uvuvi wa ngere na furu, kwa sababu kupungua kwao ni kwa sababu wanaliwa na sangara. Ningu kwa mfano tunavua kwa nyavu zipi? Kwa hiyo niombe Wizara iliangalie jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati wa operesheni hizi kama nilivyosema awali, wananchi wengi sana walinyang’anywa mali zao, wamenyang’anywa mashine, nyavu zimechomwa, mitumbwi imeharibiwa mpaka leo mashine zile za wavuvi ambao wamehangaika kweli kwa jasho na damu kupata mashine zile zimeshikiliwa kwenye vituo mbalimbali. Niombe Mheshimiwa Waziri atoe tamko wananchi wetu vifaa vyao vile waweze kupewa ili waendelee na shughuli zao za uzalishaji mali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafanya yote haya lengo ni kulinda rasilimali, lakini tuimarishe uchumi wa wananchi wetu. Tunaweza kuimarisha uchumi wa wananchi wetu tunapochoma nyavu, tunawapa njia mbadala, tumekuwa tuna- encourage uvuvi wa vizimba, je, tunapata faini, tunakusanya mapato, tunarudishaje pesa hizi kuweza kuelimisha vijana wetu kujifunza namna ya uvuvi wa vizimba? Bahati mbaya uvuvi huu wa vizimba ukianza kufuatilia kwa mfano ukitaka kuweka vizimba vyako kuna taratibu nyingi mno, kuna tozo nyingi mno zaidi ya sita, saba, sasa kwa mtu wa kawaida kuvuka vikwazo vyote hivi ni ngumu sana na gharama ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, leo hii kwa mfano nikiuliza kwa Mheshimiwa Waziri hapa leo wanipe kama wana database wanipe orodha ya maeneo ambayo yana sifa za kuweka vizimba kwenye maeneo mbalimbali. Kwa mfano, waniambie kwamba Ukerewe ni eneo lipi ambalo wameainisha, wamefanya research, wakaona kwamba eneo moja, mbili, tatu yanafaa kwa ajili ya uvuvi. Kwa hiyo, mtu anapotaka kufanya uvuvi huu anaanza kuhangaika hatua moja baada ya nyingine, vikwazo vingi hatimaye sasa hata ile dhamira yake inakuwa imepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe sana kama nilivyoshauri mambo matatu ambayo ni muhimu sana. La kwanza, Mheshimiwa Waziri kama nilivyosema aruhusu, atoe tamko, vifaa vilivyokamatwa vya wavuvi warudishiwe ili waendelee na shughuli zao, lakini watoe tamko la…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Joseph.

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, Mabadiliko ya Sheria milimita 10 mpaka milimita nane (8) nyavu za dagaa. Ni jambo jema kwa mabadiliko haya, lakini tatizo ni kubwa zaidi kwenye Ziwa Victoria kuliko bahari. Dagaa wanaopatikana katika Ziwa Victoria wana size ndogo kiasi kwamba, kuvuliwa kwa nyavu za milimita10 si sahihi na ni uonevu kwa wananchi wanaofanya kazi katika Ziwa Victoria. Ikumbukwe dagaa wanavuliwa kwa kuchotwa, kwa hiyo, mabadiliko haya yaguse pia, dagaa wanaovuliwa katika Ziwa Victoria ili pia, iruhusiwe kuvua dagaa kwa kutumia nyavu za milimita nane.

Mheshimiwa Spika, Samaki Wadogo Wasiokua zaidi ya Size iliyowekwa; naomba Kauli ya Serikali kuhusu uvuvi wa samaki kama furu, ngere na kadhalika. Samaki aina hii ni maalum sana kwa maeneo kama Ukerewe. Ikumbukwe kwamba, samaki hawa walianza kupungua baada ya kupandikizwa kwa sangara kwenye Ziwa Victoria, lakini badala yake wananchi ndio wanaadhibiwa kwa kuzuiliwa kuvua samaki hawa. Wananchi wa Ukerewe na maeneo mengine yanayozunguka Ziwa Victoria waruhusiwe kuvua samaki aina ya ngere, furu na wengineo ambao hawawezi kukua kufikia size inayowekwa na sheria.

Mheshimiwa Spika, Uvuvi wa Vizimba; urasimu ni mkubwa sana kwa watu wanaotaka kuwekeza kwenye vizimba na mchakato unagubikwa na rushwa. Kuna tozo nyingi sana mpaka kupata kibali, jambo linalokatisha tamaa. Hakuna uwekezaji wowote kwa watu hasa, vijana wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa ziwa kama njia mbadala ya kuimarisha uchumi wa watu wetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, kuchelewa kukamilika miradi ya umeme jua katika Visiwa vya Ukerewe; mradi wa usambazaji umeme kwenye visiwa mbalimbali vya Ukerewe unaendelea kwa kusuasua sana. Mfano, Kisiwa cha Ukara (JUMEME), mradi umesimama kwa muda mrefu kwa sababu mbalimbali hali inayokatisha tamaa wananchi waliokuwa wanasubiri kwa hamu. Ushauri wangu, Wizara itie msukumo ili miradi hii ikamilike kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, bei ya umeme unaozalishwa na JUMEME kuwa na bei kubwa mno; bei ya umeme unaozalishwa na JUMEME ni kubwa sana kiasi ambacho kinakatisha tamaa wananchi kuutumia umeme huo. Mfano, unit moja katika Kisiwa cha Ukara (Eneo la Bwisya) ambapo tayari wameanza kutumia huduma hiyo ni Sh.3,000. Bei hii ni kubwa sana kiasi ambacho wananchi wanashindwa kumudu na kusitisha huduma.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa jambo hili tayari limeongelewa na kuachiwa EWURA kutoa maelekezo, basi naomba Wizara iweze kufuatilia kwa karibu na kuisukuma EWURA iweze kutoa maelekezo ili wananchi wanaotumia umeme huu wafarijike na kuongeza watumiaji jambo litakalotia moyo wawekezaji hawa vilevile.

Mheshimiwa Spika, kukatikakatika kwa umeme kwenye eneo la Ukerewe; kumekuwa na tatizo la kukatikakatika kwa umeme kwenye Visiwa vya Ukerewe. Maelezo yanayotolewa ni kuanguka kwa nguzo kila mvua ikinyesha, hali hii inaathiri sana uchumi wa visiwa vya Ukerewe. Ushauri wangu, itafutwe suluhu ya kudumu ya tatizo hili ili tatizo hili la kukatika mara kwa mara kwa umeme liishe na kuwaondolea hasara wananchi wa Ukerewe wanaoshughulika na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, kusuasua kwa Mradi wa REA. Pamoja na jitihada kubwa za Wizara, bado vijiji vingi na vitongoji havijaweza kupata umeme na hata maeneo yaliyofikiwa na umeme, wigo wa watu wanaopewa umeme huo umekuwa mdogo sana na hivyo tija kutoonekana. Mfano, katika kijiji chenye kaya zaidi ya 300 unapopeleka umeme kwenye kaya 10 tu ni tatizo kubwa.

Mheshimiwa Spika, lakini pia mradi wa ujazilizi uende kwa haraka hasa Wilayani Ukerewe ili kuondoa tatizo la nishati ya umeme kwenye maeneo yaliyorukwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri yafuatayo: kwanza, kutambua na kutangaza vivutio vya utalii tulivyonavyo kwenye maeneo mbalimbali. Mfano, Wilayani Ukerewe kuna mapango ya Handebezyo, jiwe linalocheza la Nyaburebeka (Ukara), beach ya Rubya na kadhalika, lakini bado havitangazwi kama inavyostahili na hatimaye viliingizie Taifa letu pesa na kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kuwekeza kwenye miundombinu inayozunguka vivutio vya utalii. Mfano, vivutio nilivyovitaja hapo juu kwa sababu ya kukosa uwekezaji na maeneo haya hayafikiki. Kwa, hiyo nashauri Wizara ishirikiane na Halmashauri kujenga barabara na njia za kufikia vivutio hivi hasa Wilayani Ukerewe ambako vivutio hivi havifikiki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata fursa hii ili niweze kutoa mchango wangu kwenye hotuba ya bajeti iliyosomwa na Waziri Dkt. Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote katika Wizara hii kwa kutuletea hotuba nzuri inayoonesha muelekeo mzuri wa nchi yetu kiuchumi na kazi kubwa inayofanywa na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hotuba hii imezingatia mambo mengi ambayo tumekuwa tunashauri, mambo mengi ambayo yamekuwa yanaleta kero kwenye jamii hotuba hii imezingatia kwa hiyo kwa moyo wa dhati kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi kubwa sana ya kuandaa hotuba hii nzuri. Jukumu letu sasa nikushauri maeneo machache ambayo tunafikiri yanatakiwa yafanyiwe marekebisho au yaongezwe kwa ajili ya kuboresha kile kilichowasilishwa kwetu. Kwangu mimi nitajikita kwenye maeneo makuu mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, uchumi wetu unaonesha kupanda na kwa mujibu wa takwimu hizi, uchumi wetu sasa umekuwa kwa asilimia saba na asilimia saba hizi zimetokana na sekta mbalimbali za kiuchumi ambazo zimekuwa zinafanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, katika sekta zilizofanya vizuri ni sekta ya kilimo ambayo kwa ukuaji wake ni sekta ya nne kwa kukua, lakini kwenye eneo hili, sekta hii ya kilimo kama inavyoonekana imekua kwa asilimia 5.3 na tunatambua sekta ya kilimo ni sekta inayojumuisha watu wengi, inaajiri watu wengi na kama tutaiwekea mkazo inaweza kuongeza kwa kiwango kikubwa sana ukuaji wa uchumi wetu kama Taifa na kwenye eneo hili la kilimo likijumuisha uvuvi, mifugo na kilimo chenyewe bado hatujawekeza sana kwenye sekta hii ya kilimo. Kwa mfano, tukiangalia kwenye sekta hi, tukijumuisha uvuvi, mifugo na kilimo chenyewe kwa ujumla wake aukiangalia sehemu ya uvuvi ndiyo imechangia sehemu kubwa sana karibu asilimia tisa, lakini eneo hili la uvuvi ambalo linaajiri watu wengi sana bado kuna vikwazo vingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona kwa mujibu wa hotuba kuna maeneo mengi hasa kwenye eneo la uvuvi ambako tozo nyingi zimeondolewa, lakini bado kwenye sekta ya uvuvi yenyewe bado kuna tozo nyingi sana ambazo zinawafanya wanaoshiriki kwenye shughuli za uvuvi wasiweze kufanya vizuri sana na kuchangia pato la Taifa. Kwa hiyo, bado ni muhimu sana Serikali iliangalie hili. Niombe Mheshimiwa Mpango uangalie namna gani tunaweza tukaifanya sekta ya uvuvi ikachangia sehemu kubwa sana ya pato letu na tukiangalia kwa mfano kwenye mazao ya kilimo, kwenye bidhaa tulizouza nje kutoka bilioni 790 mwaka huu tumeuza zaidi ya trilioni moja ya mazao, lakini tunaweza tukafanya vizuri zaidi kama tutaboresha sekta ya uvuvi na wakafanya kazi vizuri, bila vikwazo vingi na tukaweza kuuza mazao mengi nje.

Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri niombe sekta ya uvuvi vilevile iangaliwe, tozo wanazokutana nazo wavuvi ni nyingi sana ziweze kuangaliwa kama zilivyopunguzwa kwenye eneo la mifugo, sekta ya uvuvi vilevile zipunguzwe kwa sababu kama tunavyojua vijana wengi wanaajiriwa kupitia sekta hii ya uvuvi kwahiyo kakam tozo hizi zitapungua wataweza kujiajiri, watafanya shughuli zao lakini uzalishaji utakuwa mkubwa zaidi na kuwezesha Taifa letu kuweza kuuza kwa ukubwa snaa mazoa ya uvuvi nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niongelee eneo la kilimo; kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, kilimo kinaajiri zaidi ya nusu ya wananchi wa Tanzania na sehemu kubwa tunayouza nje yanatokana na kilimo. Tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda, bila kuboresha eneo la kilimo hatutaweza kufikia kwa ufanisi kwenye uchumi wa viwanda, kwa hiyo, ni lazima tuwekeze wka kiwango kikubwa sana na kwa dhati kwenye kilimo hasa kilimo cha kisasa, kilimo cha umwagiliaji. Bahati mbaya sana tuna eneo zuri sana, eneo kubwa tukilinganisha na mataifa mengine yanayotuzunguka. Juzi tumemuona Mheshimiwa Rais amefanya ziara nje, watu wengi sana wanaotuzunguka wanahitaji chakula kutoka nchini kwetu. Sawa, tunaweza tukawapelekea chakula, lakini tuna uwezo wa kuzalisha zaidi na zaidi tukaweza kuza chakula kingi sana na tukaipatia nchi yetu pesa za kutosha sana za kigeni, lakini kilimo tunachokifanya bado ni kilimo cha kawaida sana cha mazoea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachoweza kushauri ni muhimu tuangalie, tuangalie comparatively maeneo tuliyonayo. Kwa mfano, Kanda ya Ziwa inalimwa pamba, Nyanda za Juu Kusini wanalima mahindi, kuna eneo wanalima mpunga, tunaweza tukatenga kwa mfano, eneo la Kilombero ihawa hub ya kuzalisha mazao kwa mfano ya mpunga, eneo la Nyanda za Juu Kusini ikawa eneo maalum kwa ajili ya kuzalisha mahindi, eneo la Kanda ya Ziwa ikawa eneo maalum kwa ajili ya kuzalisha pamba, Serikali ikaangalia ni watu gani ambao wanaweza wakatusaidia kuzalisha mazao haya, tukawekeza kwenye maeneo haya tukiamini kwamba namba kadhaa ya watu Serikali ichukue jukumu la kuwawezesha kimkakati na kuweka malengo kwamba watu hawa Serikali inawawezesha wazalishe kiasi fulani cha mazao ili sasa mazao haya na wati huo Serikali ikiwaandalia masoko waweze kuzalisha mazao haya na vilevile wakiwa na uhakika wa masoko yao. Tukifanya hivyo kwa miaka miwili, mwaka mmoja, miaka mitatu tunaweza tukawa na uzalishaji mkubwa sana wa mazao mbalimbali ya kimkakati na Taifa letu likaweza kuuza mazao mengi nje na kuweza kuisaidia Nchi yetu kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, tuynatambua kwamba kupanda kwa uchumi wetu kumechangiw ana stabilization ya bei ya mazao ya chakula lakini vilevile inflation rate kuwa stable, lakini yote haya yanawezekana tu kama tunaweza kuwa na chakula cha kujitoseheleza ndiyo tunaweza tukafikia hapa.

Kwa hiyo ningeomba sana Serikali iangalie na hasa Mheshimiwa Waziri tuone namna gani tunaweza tukafanya kilimo cha kimkakati badala ya kulima kilimo cha kawaida tu kila mmoja analima jinsi anavyojisikia hatutaweza kufikia malengo yale tunayoyatarajia.

Mheshimiwa Spika, lakini eneo lingine ambalo nilitaka nichangie…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Joseph bahati mbaya ni kengele ya pili.

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai mpaka leo, lakini nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hotuba zake zote. Ni hotuba ambazo zimeonesha mwelekeo, zimeonesha dira, lakini zinatuonesha dhamira ya msingi aliyonayo Mheshimiwa Rais katika uongozi wakena kulipeleka Taifa hili mahali sahihi, tunakila sababu ya kumpongezea nakumtia moyo.

Mheshimiwa Spika, ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Rais, kwanza hotuba ya 2015,halafu ukija kusoma hotuba ya mwaka 2020 inaonesha namna gani mambo mengi makubwa yamefanyika kwenye Taifa hili chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais katika Awamu hii ya Tano. Ukiangalia kwa mfano katika jitihada ambazo Mheshimiwa Rais amezifanya na kusimamia, mapambano dhidi ya rushwa na ndiyo maana utaona kwa mujibu wa Transparency International, katika nchi 35 za Afrika Tanzania imekuwa ya kwanza, lakini hata katika dunia vile vile utaona imekuwa nchi ya 28 katika nchi 136 katika matumizi bora ya rasilimali. Ni jambo jema nakwahiyo tunakila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu mambo mengi yamefanyika kwenye miaka hii mitano.

Mheshimiwa Spika, ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Rais inaonesha dira na kimsingi uelekeo ni mzuri, ndiyo maana ukiona kwa mfano uchumi wetu umekuwa mpaka kufikia kukua kwa asilimia saba ni jambo jema, pato ghafilimeongezeka kutoka trilioni 94 point kuelekea 139 ni jambo jema lakini mfumuko wa bei umeshuka, ni jambo jema vile vile katika maendeleo ya kiuchumi. Pia utaona hata mauzo ya nje vile vile yameongezeka kutoka dola bilioni 8.9 mpaka bilioni takribani 9.0,ni jambo jema. Kwa hiyo haishangazi hata mwezi Julai mwaka jana Tanzania ilivyotangwa kuingia sasa kwenye uchumi wa kati.

Mheshimiwa Spika, jukumu tulilonalo sasa ni kuona namna gani kukua kwa uchumi huu tunakuoanisha na maendeleo ya wananchi wa kawaida ili kukua huku kwa uchumi kuwaguse kwenye maisha ya kawaida ya wananchi wetu. Mwananchi aliyepo pale Ukerewe anayeshughulika na uvuvi aone namna gani katika shughuli zake za kujipatia kipato zinaendana na uhalisia wa kukua kwa uchumi. Kwa mawazo yangu, tunasekta za kijumla na ambazo ni muhimu sana ambazo zinagusa sehemu kubwa ya wananchi wetu ambazo Serikali kama itawekeza kwa kiasi kikubwa zitasaidia sana ku-link kukua huku kwa uchumi.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati njema sana kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Rais matarajio yake na ambayo ni matarajio yetu sote kwamba, sasa uchumi wetu uweze kukua kwa asilimia nane, ni jambo jema sana, lakini kama tutakuza sekta na kuzisimamia sekta kwa mfano sekta ya kilimo, uvuvi, mifugo, lakini hata nishati ni maeneo ambayo yanaweza kusaidia sana ku-link kukua huku kwa uchumi na maisha ya kawaida ya mwananchi kuwa bora ili mwananchi huyu wa kawaida aweze ku-feel kukua kule kwa uchumi.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kwenye eneo la kilimo wamezungumza watu wengi hapa, kilimo kinaajiri sehemu kubwa sana wananchi wa Taifa zaidi ya asilimia 70 kwa mujibu wa takwimu, lakini uzalishaji huu wa kilimo bado unachangamoto nyingi, wamesema wachangajiaji waliotangulia kuna matatizo kwenye mbegu, kuna matatizo kwenye utaalam, lakini bado maeneo mengine ambapo uzalishaji umekuwa mkubwa kumekuwa na tatizo kupata masoko hasa masoko ya nje, bado tunachangamoto kubwa.

Mheshimiwa Spika, sasa niishauri Serikali, lakini kwanza niishukuru Serikali angalau kwa taarifa nilizonazo kwa yale makubaliano ambao Serikali ya Tanzania imeingia na Serikali ya Israel ili angalau kila mwaka vijana takribani 100 wawe wanaenda Israel kupata mafunzo ya kilimo, ni jambo jema sana.

Mheshimiwa Spika, sasa niishauri Serikali, iweze kuwalea vijana hawa,iweze kuwawezesha iliwanapokuwa wamemaliza mafunzo yale wakirudi nchini watusaidie kufikia kwenye malengo yetu ya kufanya mapinduzi ya kilimo kwenye Taifa hili; kwa sababu kama kila mwaka vijana 100 wakienda wakarudi wakawezeshwa, wakaweza kutusaidia kitaalam ni kweli tutafikia mapinduzi haya tunayotarajia kwenye eneo la kilimo.

Mheshimiwa Spika, niipongenze Wizara ya Mambo ya Nje inafanya kazi kubwa sana kutafuta wawekezaji, lakini vile vile katika kutafuta masoko kwa ajili ya bidhaa zetu tunazozalisha hapa nchini. Hata hivyo, bado naona kuna ombwe ambapo niishauri Serikali, iweze kuimarisha mahusiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Uwekezaji ili angalau wakulima wetu wanapolima mazao yao, basi yaweze kupata masoko ya uhakika nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika,eneo lingine kama nilivyosema ni eneo la uvuvi; kama ilivyokwenye kilimo, uvuvi unaajiri sehemu kubwa sana ya wananchi wa Taifa hili. Kwa mfano kwenye eneo letu la Kanda ya Ziwa, mimi natoka Ukerewe, katika kilometa za mraba 6,400 za Ukerewe, asilimia 90 ni maji, kwa hiyo utaona wananchi wengi wa Ukerewe wanashughulika na uvuvi na hivyo uvuvi unaajiri vijana wengi Ukerewe, Kanda ya Ziwa lakini hata maeneo mengine. Hata hivyo, kama Serikali itawekeza katika uvuvi huu inaweza ikasaidia sana kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja. Bahati mbaya sana bado hatujaweza kufanya vizuri kwenye eneo hili la uvuvi.

Mheshimiwa Spika, alisema mchangiaji mmoja asubuhi hapa miaka miwili iliyopita kulikuwa na operesheni zile za kuzuia uvuvi haramu haisaidii sana, wavuvi wetu wadogowadogo hawa ambao tunahangaika kuwatafutia mikopo ili wajiimarishe kiuchumi hata kama kafanya kosa unakwenda unavunja mtumbwi wake, unachoma nyavu zake, haimsaidii sana. Nishauri Serikali iwekeze zaidi kwenye kutoa elimu. Bahati nzuri wananchi wetu ni wasikivu sana; kama wanashirikishwa, wanapata elimu, ni walinzi wazuri sana wa rasilimali zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niiombe Serikali, kwenye eneo hili la uvuvi kwa mfano, ili tuweze kuufanya kwa tija na uweze kuwasaidia wananchi wetu kuweza kuimarisha uchumi wao kwa mwananchi mmoja mmoja na katika uchumi jumuishi, basi Serikali iwekeze kwenye kutoa elimu. Vilevile kama ambavyo tumekwishaanza tayari kwa ajili ya kuwasaidia kuwawezesha ili kuimarisha mitaji yao, jambo ambalo naamini litasaidia sana sehemu kubwa ya jamii yetu kuweza kuimarika kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ingawa kumekuwa na changamoto vilevile kwenye sekta hii ya uvuvi; wavuvi wetu wanakabiliana na changamoto nyingi sana lakini ninahisi kunakosa kiunganishi kati ya wavuvi na Serikali; chombo ambacho kinaweza kikawatetea, kikawasemea na wakati mwingine kikashauri Serikali namna gani ya ku-deal na masuala ya uvuvi ili sekta hii ya uvuvi iweze kuwa na manufaa kwenye taifa letu. Kwa hiyo, nishauri Serikali iweze kuliangalia jambo hili.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo linaweza kusaidia sana kufanya uchumi wa mwananchi mmoja mmoja uweze kuimarika ni kwenye eneo la nishati. Nishukuru sana, kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Rais, mwaka 2015 wakati anahutubia Bunge, katika vijiji 12,000 ni vijiji karibu 2,000 tu ndiyo vilivyokuwa na umeme…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ni kengele ya pili Mheshimiwa Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe.

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii. Kwanza kabla sijaendelea nitamke naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia kwenye maeneo kama manne kama muda utaniruhusu. Mwaka 2018 mwezi Septemba, ilitokea ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere pale Ukara ambacho kilipoteza maisha ya watu kama 228 hivi na Serikali ikaahidi kuleta kivuko kipya ambacho kitasaidia wananchi wa eneo lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo faraja kutamka kwamba, Serikali imetimiza ahadi yake. Toka mwezi Oktoba mwaka jana kivuko hicho kilianza kufanya kazi. Kwa hiyo, kwa niaba ya wananchi wa Ukerewe naishukuru sana Serikali na kuipongeza sana kwa kutekeleza ahadi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili ninayo mambo kama matatu ambayo ningetaka kushauri. La kwanza ni kuzingatia ratiba ya kivuko kile kwa sababu, toka kimeanza juzi hapa ratiba ya kivuko kile imebadilika, lakini msingi wa malalamiko kwenye kivuko cha kwanza ilikuwa ni ratiba ambazo hazikuwa sahihi na kwa maana hiyo kwenye safari moja kukawa na mlundikano mkubwa sana wa abiria. Niombe kama kilivyokuwa kimeanza kwa ratiba ya safari tatu kwa kila upande ningeshauri ratiba ile iendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na malalamiko kwa mfano ya uchache wa abiria, namna pekee ambayo tunaweza tukadhibiti jambo hili ni kuboresha barabara ambazo zinasafirisha watu kuelekea kwenye kivuko kile. Kwa mfano Barabara ya kutoka Nansio – Bulamba mpaka Murutunguru kwenda Bugorola ikiboreshwa abiria watakuwepo wengi, lakini kutoka Bwisya mpaka Kome ikiboreshwa abiria wako wengi. Badala ya kupita kwenye mitumbwi watapita kwenye route ile na kufanya kivuko kile kuwa na abiria wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile baada ya ajali ile iliundwa tume kwa ajili ya kufanya uchunguzi chanzo cha ajali na watumishi waliokuwa wanafanya kazi kwenye kivuko kile walisimamishwa. Uchunguzi ulishafanyika, ripoti imekwishatolewa tayari, lakini watumishi waliosimamishwa wakati ule mpaka leo bado wako nje ya mfumo, jambo ambalo linasababisha kuwa katika mateso makubwa. Niishauri Serikali, maadam watumishi wale walionekana hawana hatia, baadhi yao, warudishwe kazini waendelee kufanya kazi, wajikimu na maisha yao badala ya kuendelea kuteseka kisaikolojia, lakini vilevile kimaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo ningependa kuchangia ni juu ya ujenzi wa vivuko vipya. Kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi, ukurasa wa 84, Chama Cha Mapinduzi kimeelekeza Serikali kutengeneza vivuko vipya vitatu kwenye eneo la Ukerewe. Cha kwanza ni kutoka Bukondo kwenda Bwiro, kingine kutoka Murtanga kwenda Ilugwa na kingine ni kutoka Kakukulu kwenda Ghana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwenye bajeti hii Serikali imetenga pesa, milioni 180 kwa ajili ya kujenga magati kati ya Bukondo kwenda Bwiro, lakini vilevile imetengwa bilioni moja kwa ajili ya kutengeneza kivuko kwenye eneo hilo. Nashukuru sana, lakini niombe yale maeneo mengine mawili ni muhimu sana yakazingatiwa kwenye bajeti zinazokuja pesa zitengwe ili vivuko viweze kutengenezwa. Mazingira yetu Ukerewe ni mazingira ya usafiri wa majini, kwa hiyo, tunapokuwa na changamoto ya usafiri, hasa kwenye vivuko, inakuwa ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kwenye eneo la Ilugwa. Kutoka Ilugwa kuja Kisiwa kikubwa cha Ukerewe inahitaji mtu apite majini a-cross maji saa nne. Kwa hiyo, kutokuwepo kwa kivuko ni jambo ambalo kidogo linasababisha watu ku-risk maisha yao. Kwa hiyo, kama nilivyosema niombe Serikali izingatie sana kutenga pesa kwa ajili ya kutengeneza vivuko hivi vingine vipya.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu, ambalo natamani niliongelee ni juu ya Barabara ya Nyamswa – Bunda – Kisolya na Kisolya – Nansio. Najua lot one na lot two tayari zimeanza kufanyiwa kazi, bado lot three ambayo inahusisha Daraja la Kisolya – Rugezi na kutoka Rugezi kwenda Nansio kilometa 14.3.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kwenye bajeti hii Serikali imetutengea bilioni mbili kwa ajili ya kutengeneza kivuko kipya kitakachofanya kazi kati ya Rugezi na Kisolya, lakini imetenga milioni 700 kwa ajili ya ukarabati wa Kivuko cha MV Ujenzi. Ni jambo jema, lakini wakati tukisubiri pesa za ujenzi wa Daraja kati ya Kisolya na Rugezi, kama ambavyo nimekuwa ninasema hapa ndani, Serikali ione umuhimu wa kujenga barabara ile kilometa 14.3 kutoka Rugezi kwenda Nansio Mjini. Ikiunganishwa barabara hii itaboresha sana mazingira ya usafiri, lakini hata kuimarisha uchumi wa wananchi wa Ukerewe. Kwa hiyo, niombe sana Serikali iweze kuzingatia jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la nne ambalo nataka kuchangia ni juu ya Bandari yetu ya Nansio kwenda Mwanza. Natambua Serikali imefanya juhudi kubwa na kutumia pesa nyingi kuboresha meli ya MV Clarius na MV Butiama, tayari MV Butiama inafanya kazi, MV Clarius bado inaendelea na matengenezo, lakini kumekuwa na shida kubwa sana ya usafiri hasa wa mizigo kwenye eneo hili. MV Butiama ikifanya kazi at full capacity ina uwezo wa kubeba mizigo tani mpaka 80, lakini hivi tunavyoongea meli ile ya MV Butiama haijawahi kubeba mizigo tani 10 tokea imeanza kufanya kazi, jambo ambalo ni hasara kwa Serikali, lakini kwa nini imekuwa haibebi mizigo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mkanganyiko wa gharama zinazotozwa kwenye mizigo kwa tani kati ya TPA na MSCL. TPA charge yao ni kubwa sana, inafanya sasa watu wanaosafirisha mizigo kwenye kivuko hiki cha Serikali, wanatakiwa kulipa pesa nyingi sana na matokeo yake wana-opt kwenda kwenye vivuko binafsi, jambo ambalo linaleta hasara kwenye kivuko cha Serikali. Kwa hiyo, niombe Serikali ione namna ambavyo inaweza kufanya gharama hizi kushuka na zikishuka ishawishi sasa wasafirishaji waweze kutumia kivuko hiki cha Serikali kusafirisha mizigo na ile dhamira ya Serikali kutumia kivuko hiki kusafirisha abiria, lakini na kusafirisha mizigo iweze kufikiwa kwa gharama ya chini na hatimaye basi kiweze kuwa na ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, Uwanja wa Ndege wa Mwanza ni uwanja ambao ni muhimu sana kwa uchumi wa Taifa hili hasa kwa Ukanda wetu ule wa Ziwa, unafanya kazi kubwa sana. Nashukuru sasa hivi uko kwenye matengenezo, lakini nishauri Serikali ione umuhimu wa kukamilisha ujenzi wa uwanja huu hasa jengo la abiria mapema kadiri inavyowezekana. Najua kwenye bajeti hii imetengwa karibu bilioni 6.3 kwa ajili ya kujenga jengo hili, lakini bado niendelee kushauri ni jambo la msingi sana uwanja huu ukakamilika mapema, ili kuweza kuchangia kwenye uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nikushukuru sana. Ahsanteni sana na naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa hii. Nawapongeza kwanza Mheshimiwa Waziri, Naibu na Watendaji wote kwenye Wizara hii. Kwa muda huu mchache nitachangia kwenye maeneo matatu kama muda utaniruhusu. Kwanza, ni kuhusu upatikanaji wa madawa kwenye vituo vyetu vya kutoa huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatambua juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali kujenga miundombinu kwenye maeneo ya kutolea huduma za afya; hospitali zimejengwa, vituo vya afya na zahanati. Kama miundominu hii itakuwepo katika mazingira yaliyo mazuri, lakini kukawa na shida ya upatikanaji wa madawa, bado haitakuwa na tija sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na shida kubwa sana ya upatikanaji wa madawa bado. Pamoja na kwamba tumeongeza bajeti ya huduma za afya hasa kwenye eneo la madawa, lakini bado kuna shida kubwa sana ya upatikanaji wa madawa kwa watu wetu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya. Hili linachangiwa sana na deni lililoko MSD. Nikitolea mfano case study ya Ukerewe; Ukerewe ili tuwe na madawa ya kutosha kwa mwaka mzima, tunahitaji karibu shilingi milioni karibu 80, lakini mpaka mwezi Desemba mwaka 2020 ndiyo wamepata shilingi milioni 20. Kwa hiyo, utakuta kuna shida kubwa sana ya madawa kwenye Hospitali yetu ya Wilaya, kwenye zahanati na vituo vya afya.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Hospitali yetu ya Wilaya inahudumia watu mpaka wanaotoka eneo la Bunda kutoka Kisolya wanakuja kutibiwa pale. Sasa yanahitajika madawa mengi sana. Kwa hiyo, kunapokuwa na tatizo la kibajeti kunakuwa na shida sana kwa wananchi wetu. Kwa mfano, kwenye hospitali yetu ile, wanakwenda kununua madawa, wanakuta MSD kule madawa mengi hawana, wanawaelekeza kwenda kununua kwa Mshitiri. Wanapokwenda kwa mshitiri, anataka pesa cash, hospitali hawana. Matokeo yake sasa kunakuwa na shida kubwa sana ya madawa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali, pamoja na jitihada zinazofanyika kudhibiti matumizi matumizi mabaya kwenye mnyororo huu wa madawa, lakini tuhakikishe tunapata solution ya haraka ili madawa yawe available kwenye hospitali zetu ili wananchi wetu wapate huduma hizi kwa kiwango kinachotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukizingatia tuko kwenye jitihada za kushawishi watu wetu wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii, kama wanakwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na hawapati madawa, inawakatisha tamaa hata kujiunga na Mifuko ya Afya. Hata hili tunaloendelea nalo la kutaka tutengeneze Sera ya Afya ya Jamii kwa watu wote, tunaweza tukapata kikwazo sana kwa sababu wananchi wanakosa imani kwamba hata wakiwa wanachama, basi zile huduma wanazozitarajia watazipata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, naipongeza Serikali kwa kukubali ombi letu la kupandisha Kituo cha Afya cha Bwisya kuwa Hospitali ya Wilaya na Hospitali yetu ya Wilaya ya Nansio angalau sasa kuwa Referral Hospital, ni jambo jema.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naiomba tu Serikali, zile taratibu ambazo zimebaki, ziweze kukamilishwa ili basi vituo hivi viweze kutoa huduma kwa wananchi wetu, kwa sababu dhamira ni kufanya Visiwa vya Ukerewe hasa kwa changamoto za kijiografia, iwe kama eneo linalotoa huduma kama self-contained. Huduma zote ziweze kupatikana kwa sababu ikitokea changamoto ya kiafya Ukerewe, kumpeleka mgonjwa kwenye Referral Hospital kwa mfano Sekou Toure ni changamto kubwa sana. Kwa hiyo, tukiwa na huduma zote kwenye kisiwa kile, angalau itasalimisha na itaokoa maisha ya wananchi wetu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu sasa, pamoja na jitihada ambazo zinaendelea, najua kuna timu imepelekwa pale kufanya tathmini kuona upungufu uliopo. Naomba hasa wodi ya uzazi ya akina mama ina matatizo makubwa sana. Katika maboresho yatakayofanyika, liangaliwe kwa kipekee.

Mheshimiwa Naibu Spika, jengo la mama na mtoto ambalo limejengwa kwenye miaka 1960 huko nyuma lina hali mbaya sana, nalo vile vile liangaliwe liweze kuboreshwa, lakini hata idadi ya watumishi kwenye maeneo yetu yale, bado yaangaliwe sana hasa kwenye Hospitali yetu ya Wilaya ili kuwe na staffing ya kutosha kuweza kuhudumia watu wetu na hasa kama itakuwa Referral Hospital. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hili litafanikiwa kufanya Hospitali ya Nansio ambayo ni Hospitali yetu ya Wilaya kuwa Referral Hospital, itahitaji vituo vingine vya afya kwa ajili ya ku-support eneo hili. Ndiyo maana nimekuwa ninaomba Mheshimiwa Waziri mtusaidie Kituo cha chetu cha Afya cha Nakatunguru ambacho kimejengwa mwaka 2012 chenye upungufu kidogo wa majengo na vifaa tiba, kiweze kukamilika ili kiweze ku-support hospitali yetu hii ya Wilaya. Kama itakamilika, mzigo mkubwa uwe unaelemea huku ili Hospitali yetu ya Wilaya iwe kweli ni referral hospital. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, kitakwimu ukienda hospitali ya Ocean Road kuna wagonjwa wa cancer wengi, lakini asilimia kubwa ya wagonjwa waliopo pale wanatoka Kanda ya Ziwa. Ndiyo maana mwaka 2009 Hospitali ya Bugando ikaanza kuhudumia wagonjwa wa cancer. Wakati ule ilianza na wagonjwa takribani 300, lakini hivi leo ina hudumia wagonjwa karibu 14,000 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2017 imeanza kutoa huduma ya mionzi, lakini bado ina upungufu wa miundombinu. Ina vitanda 20 pekee na kwa siku wanapokea wagonjwa karibu 200; ni wagonjwa wengi sana. Bado kuna upungufu mkubwa sana. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mkundi, kuna taarifa kutoka Mheshimiwa Ester Bulaya.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nampa taarifa mchangiaji na mchango wake mzuri, naamini mkakati wa Serikali ilikuwa ni kuhakikisha hizi mashine za mionzi zinakwenda katika hospitali zote za Kanda, kwa sababu tatizo la cancer ya shingo ya uzazi limekuwa ni kubwa sana hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hivi, wewe unajua Mbeya pale, kwenye Hospitali ya Mbeya, kuna tatizo na mashine haipo na iliahidiwa kupelekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nampa taarifa mchangiaji.

NAIBU SPIKA: Sasa hiyo taarifa sijaelewa kama niipokee mimi au mchangiaji. Mheshimiwa Mkundi unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, maadam ina dhamira njema, haina shida. Ninachotaka kusema, Serikali ione namna ya kuisaidia Hospitali ya Bugando. Sasa hivi wana ujenzi wa wodi ambapo itasaidia kupokea wagonjwa wengi zaidi, basi Serikali ifikirie maombi yao katika bajeti waliyonayo ya karibu shilingi bilioni tano, wodi ile iweze kukamilika. Iwasiaidie mashine za ku-backup za mionzi ili zile zilizopo zikiharibika, kuwe na mashine nyingine kwa ajili ya ku-support. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo vituo vimekamilika na hospitali zimekamilika, Serikali ipeleke vifaa tiba na wataalam viweze kufanya kazi. Kama nilivyosema, Kituo chetu cha Nakatunguru kinahitaji kuwezeshwa, majengo yaliyobaki yakamilike, vifaa viwekwe ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo kwa mfano Ilemela, hospitali yao ya Wilaya imekamilika muda mrefu, kimebaki kuwekwa tu vifaa na watumishi kiweze kufanya kazi, iweze kuwasaidia wananchi. Naomba Serikali vilevile kama ilivyo Hospitali ya Wilaya ya Ilemela, kama ilivyo Vituo vya Afya cha Nakatunguru Ukerewe na vingine vyote nchi nzima, basi vipelekewe vifaa na wataalam viweze kuanza kutoa huduma kwa wananchi wetu ili wananchi wapate kile ambacho tunakitarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa nafasi, Mwenyezi Mungu akubariki sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, lakini nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri Naibu Waziri na watendaji wote kwenye wizara hii na mimi nina mada moja tu ambayo itachangia mada ya mifugo nitajikita kwenye mifugo, baada ya mifugo kufanya vibaya kwenye bonde la Ihefu, Serikali ilifanya maamuzi ya makusudi kupeleka mifugo ile kwenye Mkoa wa Lindi na sisi Mkoa wa Lindi kuna wilaya mbili ndio tumepokea wafugaji Wilaya ya Kilwa na Wilaya ya Liwale. (Makofi)

Mheshimies Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale tulitenga vijiji vitatu; Kijiji cha Lilombe Ngapata na Kimambi ndio vijiji viliidhinishwa kupokea wafugaji, lakini kutokana na sababu sitofahamu ninyi wenyewe mnajua wafugaji sasa hivi Liwale nzima kuna wafugaji. Jambo ambalo nataka kuliongelea hapa Serikali hapakufanywa maandalizi ya kawaida au maandalizi mahususi ya kupokea mifugo. Hapakuwa na miundombinu yoyote ya kupokea mifugo ile naninavyoongea mpaka leo hakuna majosho hakuna malambo hapakuandaliwa lolote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, palihitaji maandalizi kwanza ya kimuundo mbinu, halafu maandalizi ya kielimu kwa maana kwamba watu wa kuandaa saikolojia kwa sababu sisi kwa asili sio wafugaji. Leo ninavyozungumza hapa ni zaidi ya miaka 10 mifugo iko Liwale lakini Halmashauri ya Wilaya ya Liwale haijawahi kunufaika na chochote kutokana na mifugo ile, hii ni kwa sababu hapakuandaliwa na miundombinu yoyote na vilevile sisi wenyewe wafugaji wana Liwale hatukuandaliwa kupokea mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie jambo moja mwaka 76 mzee Rashindi Mfaume Kawawa waziri wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alituletea ng’ombe sisi Liwale kila Kijiji ng’ombe 20 na kila shule tulipata ng’ombe ishirini lakini ng’ombe wale walidumu miezi sita tu sababu ni nini hakuna mzazi aliyekubali mwanae kumpeleka kuchunga ng’ombe ilikuwa ni adhabu. Kwa hiyo, Mwalimu akimpangia kwenda kuchunga ng’ombe huyo Mwalimu haamki, lakini ng’ombe wa kijiji nao walikufa kwa mtindo uleule hakuna mtu aliyekubali kwenda kuchunga ng’ombe akiwa na akili timamu. Ukimwona kwetu mtu anachinja ng’ombe basi ujue dishi limeyumba. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo ng’ombe wale walikufa sisi kwetu mfugaji anafuga bata tena dume kwa hiyo kwa msingi huo kwetu tulikuwa tuandaliwe kisaikolojia namna ya kuwapokea wale ng’ombe vilevile tuandaliwe kwa miundombinu. Sasa nini kinatokea hatuna wataalam wakutuelimisha namna ya kukuaa na wafugaji wale na vijiji vyetu havikuingia kwenye matumizi bora ya ardhi. Jambo hili linatuletea migogoro sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua jukumu la matumizi bora ya ardhi ni jukumu la halmashauri lakini halmashauri inaingia kwenye jukumu hili kwa faida ipi ambayo tumeipata kutokana na mifugo ile? Naiomba sana Serikali, ije Liwale ije itusaidie kuanza kuhakikisha vijiji vile ambavyo tayari vina wafugaji vinaingia kwenye matumizi bora ya ardhi ili kutupunguzia migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi pia tunatakiwa tuwe na malambo kwa ajili ya wafugaji wale, jambo linalofanya sasa Liwale nzima isambae mifugo, kwa sababu wafugaji wanatafuta maji, hawana mahali pa kupata maji, kwa hiyo, tumeruhusiwa vijiji vitatu sasa vijiji vyote 70 vina wafugaji na miaka mitano, sita ijayo idadi kubwa ya wafugaji itakuwa kubwa kuliko wenyeji wa pale kwa hiyo tunaomba tuletewa wataalam kwa ajili ya miundombinu tuletewe wataalam kwa ajili ya kutuelemisha namna ya kufuga mifugo ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuhusu minada tunaomba sana tupate mtu specific ambaye anajua mambo ya minada, aje atufunguliwe mnada Liwale, Kilwa ng’ombe wanakwenda Mtwara wanakula ng’ombe Mtwara wanakula ng’ombe Songea wanakula ng’ombe wapi lakini ng’ombe wanachukuliwa kutoka Liwale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwambia, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale haijawahi kupata hata shilingi, tunahitaji juhudi za makusudi ili na sisi tuone faida ya kuwepo ile mifugo pale Liwale. Hilo ndio jambo mahususi niliyokuwa nimeomba nafasi hii kulizungumzia kwa siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa dakika tano hizi; naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha Itifaki hii ambayo ni muhimu sana kama walivyotangulia kusema watangulizi. Nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati yetu mimi kama Mjumbe wa Kamati, kwa uwasilishaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Itifaki hii ni muhimu na hasa kwa kupata mustakabali mwema wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Taifa letu. Sisi Tanzania kama moja ya nchi ambazo siyo kisiwa tunachangamana, tunashirikiana katika nyanja mbalimbali na mataifa mengine yanayotuzunguka, hatuna namna yoyote tunayoweza kutafuta maendeleo ya Taifa letu kama kuna shida ya usalama kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka ya karibuni kumekuwa na shida ya usalama hasa kutokana na matukio ya kigaidi. Jambo ambalo limepelekea jumuiya mbalimbali kujipanga ili kukabiliana na matukio haya. Inapoletwa Itifaki hii leo katika Bunge lako Tukufu, niombe Waheshimiwa Wabunge kwa umoja wetu tuweze kuliridhia Itifaki hii. Kwa sababu kupitia Itifaki hii, itafanya Taifa letu liweze kushirikiana na mataifa mengine kudhibiti lakini na kukabiliana na matukio ya kigaidi, lakini na kuzuia matukio ya namna hiyo vilevile. Leo tupo kwenye harakati za kujenga misingi imara ya kiuchumi ya Taifa letu. Hatuwezi kunufaika na misingi hii kama kutakuwa na shida ya usalama kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namna pekee ni kushirikiana na wenzetu katika kukabiliana na matukio hayo. Tuweze kutambua ni angle zipi ambazo wahalifu kupitia ugaidi wanaweza kuzitumia na ni namna gani tunaweza tuka-train watu wetu kushirikiana na watu wengine katika kukabiliana na matukio haya. Yote haya hatuwezi kuyafanya sisi kaka Taifa tukiwa tumejitenga, ni lazima tushikamane, tushirikiane na mataifa mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama ambavyo Mwenyekiti wa Kamati yetu amesoma taarifa yetu, tumechambua Itifaki hii, ni Itifaki muhimu na ya msingi sana Bunge letu kuweza kuridhia ili sasa kama mataifa mengine tuweze kushirikiana kudhibiti, lakini na kuhakikisha usalama wa watu wetu na mali zao unakuwepo ili sasa tuweze ku-concentrate kwenye kushughulikia mafanikio katika uchumi kwenye Taifa lakini na kwa mwananchi mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa uchache, niombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu, kama ambavyo sisi taarifa yetu tumeiwasilisha kama Kamati, tuungane kwa pamoja kuridhia Itifaki hii ili sasa nchi yetu iwe nchi ya 22 kuridhia Itifaki hii, kuungana na mataifa mengine kushughulikia na kudhibiti matukio ya kigaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuchangia nitakuwa na mambo machache sana kwenye wizara hii na kimsingi kwa leo mchango wangu utajikita kwenye eneo la uvuvi, na nina sababu ya msingi. Natoka visiwa vya ukerewe na katika square kilomita 6400 ni asilimia 10 tu ya nchi ya kavu zaidi nimezungukwa na maji kwa hiyo watu wangu wengi ni wavuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze viongozi wa wizara Mheshimiwa Waziri, naibu na watendaji wote wa wizara hii, wamejitahidi sana kuitendea haki wizara hii na niombe mwenyezi mungu aendelee kuwasimamia kama mjadala ulivyoendelea kwa siku chache zilizopita uchumi wa Taifa hili unategemea sana sekta ya kilimo ikihusisha uvuvi na mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, zaidi ya asilimia 90 ya wavuvi wetu ni wavuvi wadogo. Kwa hiyo, katika mambo ya msingi ambayo tunapaswa kuyafanya ni kujenga msingi, hasa kuwezesha sekta hii ya uvuvi kupitia wavuvi hawa wadogo ili kuweza kuifanya sekta hii ya uvuvi iweze kuwa na impact kwenye uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka michache iliyopita wavuvi wetu walikuwa na shida sana na watumishi wa Wizara ya Uvuvi. Walikuwa kama wanawindana hivi, kama watu mahasimu. Sasa ili tuweze kujenga msingi imara kwenye sekta hii ya uvuvi, lazima kwanza tuanze kujenga mazingira mapya kwenye sekta ya uvuvi. Tu-harmonize hali tofauti na mazingira yaliyokuwepo kipindi cha mwaka mmoja au miwili iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma ilitokea operesheni, kama ambavyo nimekuwa ninasema, watu wengi sana walipoteza mali zao. Sasa ni wakati ambao tunahitaji tujenge mazingira ambayo watumishi, wataalam, wavuvi, wataaminiana ili kama nilivyosema, sekta ya uvuvi iweze kuwa na impact. Kwa sababu tukiweza kuimarisha sekta hii; na kama nilivyosema, zaidi ya asilimia 90 ya wavuvi wetu ni wavuvi wadogo; na kwa maana hiyo sekta hii itatusaidia kutengeneza ajira, itaongeza kitoweo na vitu vingine kama hivyo ili kuweza kusaidia watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo la kwanza ambalo nafikiri nichangie kwenye eneo hili, kwanza naomba Wizara yetu itambue kwamba wavuvi wetu wanahitaji sana elimu. Kuna matatizo kadhaa yamekuwa yanajitokeza, lakini hasa ni kwa sababu wavuvi wetu wanakosa elimu kutoka kwa wataalam. Watu wanapotoka Wizarani kwenda kutoa tu adhabu kwa watu wale kwa sababu wamefanya makosa, haijengi dhana iliyo nzuri kuwawezesha watu wetu kuwa imara na kuimarisha mitaji yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutolee mfano wakati ule Wizara inatuma watu kwenda kuchoma makokoro na mitumbwi, hebu imagine mwananchi wa kawaida amejikokota kapata mtaji wake, kaanzisha biashara yake ya shilingi milioni 10 au shilingi milioni 15, siku moja tu ule mtaji unaporomoka. Lazima atakuwa frustrated. Kwa hiyo, kwanza tujikite kwenye kutoa elimu. Tuwe na kitengo maalum kwa ajili ya kuzunguka kwenye maeneo yetu kutoa elimu kwa wavuvi wetu ili yale wanayoyafanya, basi yaendane na miongozo, taratibu na mambo mengine kama hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Wizara, kupitia hotuba yao, nimeona wako kwenye hatua nzuri ya kutafsiri sheria, miongozo na kanuni zetu kwa Lugha ya Kiswahili. Ni jambo jema kwa sababu wavuvi wetu wengi hawaelewi lugha hii tunayotumia kwenye sheria zetu. Kwa hiyo, kama itatafsiriwa kuwa Lugha ya Kiswahili itatoa fursa kwa wavuvi wetu kuweza kusoma na kuelewa miongozo, kanuni na sheria zinazohusu kazi wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu, kazi hii itakapokamilika, basi sheria hizi kwa Lugha ya Kiswahili iweze kusambazwa kwenye wilaya zetu ili wavuvi wetu waweze kuzipata na kuzisoma, waweze kuzielewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni juu ya tozo. Mwaka juzi, 2019 tulifanya marekebisho ya sheria hapa Bungeni; na katika sheria hizo tulipunguza baadhi ya tozo zilizokuwa zinakabili wavuvi wetu. Kwenye eneo hili, ni kweli baadhi ya tozo zile zimeondolewa, lakini bado kuna tozo ambazo ni kero kwa wananchi wetu. Naomba Serikali iendelee kuziangalia kupitia Wizara, iangalie tozo nyingine ambazo siyo za msingi sana tuweze kuzitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naiomba Wizara, wavuvi wetu hawa wa kawaida wanasumbuliwa sana pale ambapo mamlaka zinapoenda kukusanya tozo. Kwa mfano, kuna tozo za TASAC, ushuru wa mitumbwi, leseni na kadhalika. Mbaya zaidi ni kwamba tozo hizi zinatozwa kwa nyakati tofauti tofauti, jambo linaloleta usumbufu kwa wavuvi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ione uwezekano wa kuunganisha tozo hizi ili zote ikiwezekana ziwe zinatolewa kwenye center moja halafu sasa Serikali inaweza kuchambua tozo zile kama ni ya TASAC au sehemu nyingine, kuliko kila wakati taasisi inakwenda kuwatoza wavuvi wetu, inakuwa ni usumbufu kwa watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nafikiri nilichangie ni kwenye uvuvi wa vizimba. Tumekuwa tunahamasisha sana wavuvi wetu kufanya uvuvi wa vizimba; ni jambo jema. Kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, inaonekana kwenye Ziwa Victoria kwa mwaka mmoja; mwaka 2019/2020 vizimba vilikuwa 431. Mwaka huu kwa mujibu wa utafiti wao, vizimba ni 473; ni jambo jema. Bado kwa mtazamo wangu tunahitaji kufanya zaidi. Tunahitaji tuwekeze zaidi kwenye uvuvi wa vizimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namna pekee ambayo tunaweza tukawasaidia watu wetu, kwa sababu moja kati ya changamoto zilizopo kwenye uvuvi wa vizimba ni gharama za kuanzisha shughuli hizi za ufugaji wa samaki. Kwa mwananchi wa kawaida kwa gharama zilizopo hivi sasa, ili mtu aanzishe kizimba anahitaji zaidi ya shilingi milioni 10. Ni wananchi wachache sana wa kawaida wenye uwezo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana kumekuwa na shida sana kupata vifaranga vya samaki. Hata chakula cha samaki hawa kimekuwa na shida kubwa. Kwa hiyo, naomba Serikali kupitia Wizara, ione uwezekano ili chakula cha vifaranga hawa kiweze kupatikana kwa bei nafuu. Vilevile vifaranga wazalishwe kwa wingi wapatikane. Pia zile gharama nyingine kwa mfano za kufanya Environmental Impact Assessment, angalau zake zipungue ili mwananchi wa kawaida awe na uwezo wa kuanzisha kizimba akafuga samaki, jambo litakalotusaidia kuondokana hata na ile migogoro ya uvuvi usio halali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, nashukuru sana kwa nafasi, Mwenyezi Mungu akubariki sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii ya kusema maneno machache kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwa kuanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara. Wamefanya kazi kubwa sana kwa kipindi hiki.

Mheshimiwa Spika, na kwa mfano mdogo ukiangalia usambazaji wa umeme kimsingi kumekuwa na ufanisi kwa sababu kwa kipindi cha miaka takribani mitano, vijiji zaidi ya 8,000 vimepewa umeme kama nyongeza kwenye vijiji vya awali vilivyokuwa na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili nitoe ushauri tu; pamoja na kwamba tumepeleka umeme kwenye vijiji zaidi ya 10,000 lakini ukiangalia wigo wa maeneo yaliyopelekewa umeme kwenye kijiji chenye vitongoji saba, umeme umepelekwa makao makuu ya kijiji na katika makao makuu ya kijiji umeme unapelekwa kwenye kaya zisizozidi 20. Bado wigo ni mdogo sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utakuta vitongoji zaidi ya vitano, vitongoji sita kwa mfano kwa Ukerewe, vijiji vyenye vitongoji saba, kitongoji kimoja kwa kaya 20 pekee ndizo zimepata umeme, sehemu kubwa ya wanakijiji wanakuwa hawajapata umeme.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, bado tunahitaji kuwekeza pesa nyingi kwa TANESCO ili mradi unapofikisha umeme kwenye makao makuu ya kijiji basi TANESCO wabaki na jukumu la kusambaza umeme kwenye eneo la vitongoji ili mwisho wa siku basi wananchi wapate umeme na lile lengo tunalolitarajia la wananchi kunufaika na nishati hii, kujiletea maendeleo, tuweze kulifikia.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo ninataka kuliongelea – nitaendelea kuongelea suala la umeme – ni juu ya kukatikakatika kwa umeme; Ukerewe tumekuwa na shida kubwa ya kukatikakatika kwa umeme kwa takribani miaka miwili sasa. Na chanzo cha kukatikakatika kwa umeme ni tatizo la submarine cable inayotuunganisha kati ya Kisiwa cha Ukerewe na Bunda.

Mheshimiwa Spika, ile cable imechoka na kwa maana hiyo imekuwa mara kwa mara maji yakigusa inakatika. Sasa imesababisha adha kubwa sana kwa wananchi wa Ukerewe, wawekezaji wanakimbia, wenye dhamira ya kuwekeza wanashindwa kuwekeza.

Mheshimiwa Spika, inaathiri kwa ujumla uchumi wa wananchi wa Ukerewe. Na wakati mwingine wananchi wenye uwekezaji wao kwenye Visiwa vya Ukerewe wanapata hasara kwa sababu vifaa vyao vingi vinaharibika.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri na timu yako niwapongeze; mmekuwa na jitihada kadhaa ambazo mmekuwa mnazifanya. Na hivi tunavyoongea ninashukuru angalau sehemu fulani ya kipande cha cable ile mmeweza kuipata. Lakini niombe; ile sehemu ya kipande kingine cha cable iweze kupatikana haraka, tuweze kupata suluhisho la kudumu la umeme kwenye Visiwa vya Ukerewe na hasa Kisiwa kikubwa cha Ukerewe.

Mheshimiwa Spika, wakati wa kusoma hotuba hapa Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako ukurasa wa 51 umeongelea umeme wa maeneo ambayo yapo nje ya Gridi ya Taifa, pia maeneo ya visiwa. Ukerewe tuna visiwa 38, katika hivyo, kisiwa kikubwa kile, sawa tuna umeme wa Gridi ya Taifa; visiwa 37 vinavyobaki vyote tunategemea umeme wa jua na umeme mwingine kama ambavyo mtautoa kwenye maeneo yaliyo nje ya Gridi ta Taifa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, unajua katika visiwa 37 vya Ukerewe, ni visiwa vitatu pekee vidogo vyenye umeme; Kisiwa cha Ukara ambacho kinakuwa-supplied na watu wa Jumeme; Kisiwa cha Ilugwa ambacho kiko supplied na watu wa Jumeme na Kisiwa cha Liegoba ambacho kinakuwa supplied na watu wa Power Gen.

Mheshimiwa Spika, hawa watu wa Liegoba kwa umeme wanaopewa wanatozwa shilingi 1,000 kwa siku, wananunua umeme kwa bundle, bundle lile inanunuliwa shilingi 1,000, haijalishi yule mteja ametumia umeme ule au hajatumia mwisho wa siku lile bundle inakuwa haifanyi kazi tena na matokeo yake kesho yake yule mteja anatakiwa kununua tena bundle lingine la shilingi 1,000, kitu ambacho ni gharama sana kwa mwananchi wa kawaida. Mheshimiwa Dkt. Kalemani, nimekuwa ninakueleza jambo hili. Hii si sawa kwa mwananchi wetu wa kawaida, mwananchi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la Ilugwa na Kisiwa cha Ukara ambapo wako supplied na watu wa Jumeme, ni kweli walikuwa wanatiozwa shilingi 3,500 kwa unit. Ulisema hapa Bungeni ukatoa maelekezo wakapunguziwa mpaka shilingi 100, lakini baada ya kupunguziwa na kuanza kulipa shilingi 100 wananchi hawa wakawa wanapata umeme kuanzia saa nne asubuhi mpaka saa 12.00, baada ya saa 12.00 usiku mzima wananchi hawana umeme.

Mheshimiwa Spika, nimeendelea kupiga kelele na hatimaye mwezi Machi wananchi wakaingia makubaliano mapya na watu wa Jumeme kwamba wako tayari kulipa shilingi 2,000 kwa unit ili tu waweze kupata umeme kwa saa zote 24. Hivi ninavyoongea pamoja na wananchi hawa kuendelea kulipa shilingi 2,000 lakini hawapati umeme kama inavyotarajiwa.

Mheshimiwa Spika, niombe sana Serikali iliangalie jambo hili, nimekuwa ninalisema mara kwa mara hapa lakini ifike mwisho sasa tuone kwamba huu mradi wa kusambaza umeme kwenye maeneo yaliyo off-grid angalau basi Visiwa vya Ukerewe viweze kunufaika na mradi huu. Vile ambavyo havijapata umeme moja kwa moja viweze kupelekewa umeme.

Mheshimiwa Spika, kwenye Visiwa kwa mfano vya Ghana, Bulubi n.k. mkandarasi alipeleka nguzo tokea mwaka 2016 akaziacha pale. Mpaka leo hakuna chochote kilichofanyika. Niombe watu wa Ukerewe wanahitaji huduma hii ya umeme, wanahitaji kuchochea maendeleo na maisha yao kwa ujumla wake, basi wapate nishati hii ya umeme. Hasa watu wa visiwa vidogo vile; watu wa Jumeme ule mgogoro wa bei uliopo uweze kutatuliwa na mwisho wa siku waweze kupata huduma hii ya umeme na waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi kama tunavyowatarajia.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Ndiyo, endelea na taarifa hiyo.

T A A R I F A

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, nataka tu kumueleza mzungumzaji kwamba tatizo la watu wa kwenye visiwa kutozwa gharama kubwa ya umeme halipo kwenye visiwa vyake peke yake. Natoka kwenye Visiwa vya Maisome pamoja Zilagula ambako kwa hivi sasa tunavyoongea wananunua unit moja ya umeme kwa shilingi 2,400; nilitaka kuzungumzia jambo hilo. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mkundi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa hiyo kwa mikono yote miwili. Na unaweza kuona namna gani wananchi wetu wanavyotaabika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mwananchi wa kawaida wa kijijini kununua unit moja kwa shilingi 2,000 au kama wanavyotoza kwenye Kisiwa cha Liegoba, ananunua unit kwa shilingi 1,000, bundle ile, halafu mwisho wa siku ile bundle iki-expire kesho yake anatakiwa kununua tena haijalishi ametumia au hajatumia, ni lazima Serikali i-intervene katika jambo hili. Ifike mahali wananchi hawa tuwape fursa ya kujiletea maendeleo kupitia nishati ya umeme.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nilitaka kusema kwenye hayo maeneo matatu tu juu ya umeme. Lakini niombe sana Mheshimiwa Waziri; suala la cable inayotuunganisha kati ya Lugezi na Kisorya pale kupeleka umeme kwenye Kisiwa kikubwa cha Ukerewe, tupate ufumbuzi wa kudumu. Lakini suala la visiwa vidogo hasa kwenye eneo la bei vilevile tupate solution ili mwisho wa siku wananchi wa Ukerewe waweze ku-enjoy maisha na maendeleo ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana kwa fursa. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa kunipa fursa hii. Kwa kuanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kunifanya nisimame mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia nitume nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya na anayoendelea kuifanya.

Vile vile nimpongeze Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Serikali nzima kwa ujumla, wanafanya kazi kubwa sana. Mwisho, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu na Watendaji wote chini ya Katibu Mkuu ndugu yangu Tutuba. Nafahamu umahiri wake, naamini tutaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti tunayoijadili ni bajeti nzuri sana na nitumie nafasi hii kuwaomba sana Watanzania na hasa wa eneo la Ukerewe waipokee bajeti hii kwa sababu ni bajeti nzuri, inagusa mambo mengi ya msingi yanayogusa maisha ya waanchi wa ujumla wake. Pia bajeti hii inaonesha uelekeo mzuri na zaidi na inatia matumaini, kwa hiyo niwaombe Watanzania waipokee kwa moyo ya dhati kabisa kwa mikono miwili kwa sababu ni bajeti inayotuonesha tunapoelekea ni pazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kushauri kwenye maeneo machache sana. La kwanza, bajeti hii kama nilivyosema ni bajeti nzuri, imegusa mambo mengi sana ya msingi na imezingatia ushauri ambao Wabunge tumeutoa katika mijadala mbalimbali. Bajeti hii ili tuweze kuitekeleza vizuri na yale manufaa tunayotarajia tuweze kuyaona, ni lazima tu-maintain walipakodi tulionao, lakini tutengeneze walipakodi wengine ili tuweze kupata nguvu ya kutekeleza haya tuliyoyapanga kwenye bajeti, kwenye mpango, mwisho wa siku yale tunayotarajia yaweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo katika mambo yaliyosaidia sana kuchochea kukua kwa uchumi mpaka tukafikia uchumi wa kati ni pamoja na kusambaa kwa umeme, jitihadi zilizofanywa na Serikali kusambaza nishati ya umeme, kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma za afya, maji na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia eneo hilo hilo, ningependa kuongelea kwenye eneo la nishati ya umeme. Umeme ni injini kubwa sana ya kuchochea maendeleo ya wananchi kwa ujumla wake na nimefarijika kwenye bajeti hii, bajeti kuu lakini hata bajeti ya Wizara ya Nishati, Serikali imeonesha dhamira yake ya kuendelea na program ya usambazaji wa umeme kwenye vijiji ambavyo havikufikiwa na umeme lakini mpaka kwenye vitongoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo jema sana na likifanyika hili itasaidia sana kuchochea uchumi wa watu wetu na litasaidia kuongeza wigo wa walipa kodi kwasababu tuna vijana wengi ambao wana mawazo, wangependa kujiajiri, lakini wanaweza kujiajiri kama watakuwa na nishati ya umeme ili kuweza kuanzisha shughuli zao ndogo ndogo. Kama hili litafanyika litakuwa ni jambo jema sana. Kwa hiyo niiombe Serikali iweke mkazo na iweze ku-finance fully kwenye eneo hili la usambazaji wa umeme. Tusisahau kwenye bajeti ya Wizara ya Nishati ilionekana katika mipango waliyonayo ni pamoja na kusambaza umeme kwenye maeneo ya visiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo la Ukerewe kwa mfano, ambalo linaundwa na visiwa 38, katika wakazi zaidi ya 400,000 tulionao karibu asilimia 40 ya wakazi wanaishi katika visiwa vidogo vidogo ambavyo bado havina umeme. Kwa hiyo kutofikiwa na umeme kunadumaza maendeleo ya watu hawa na kwa maana hiyo kunadumaza vile vile jitihada za kuongeza walipakodi wengine kupitia shughuli mbalimbali ambazo wangezifanya kupitia ujasirimali. Kwa hiyo niiombe Serikali tuhakikishe kwamba kupitia bajeti hii tunaweza ku- finace kwa kiwango kikubwa ili kuhakikisha kwamba program tuliyonayo ya upelekaji umeme vijijini na hasa visiwani tunaikamilisha kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Mpango wa Pili wa Maendeleo vile vile unaonesha kwamba Sekta ya Kilimo hasa kwenye eneo la uvuvi iliongezeka na ndio maana utaangalia hata kwenye uchakataji wa minofu ya samaki kwa kipindi kilichopita tani zaidi ya 26,000 zilisafirishwa ukilinganisha na tani 23,000 zilizosafirishwa miaka minne, mitano kabla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni jema sana na shabaha ya Mpango wa Tatu ni kuchochea maendeleo ya watu. Katika kuchochea maendeleo ya watu ni pamoja na kukuza uchumi wa watu wetu hasa kwenye maeneo ambako shughuli mbalimbali za uzalishaji zinafanyika. Sasa niombe, Kanda za Ziwa ambao wanazunguza ziwa Victori kuna uzalishaji mkubwa wa Samaki. Kama nilivyoonesha hapa kumekuwa na ongezeko kubwa sana na ufanisi kwenye sekta ya uvuvi. Katika samaki wanaozalishwa katika ukanda ule karibu asilimia 30 ya samaki wale wanapatikana kwenye Visiwa vya Ukerewe, lakini bahati mbaya sana Ukerewe hakuna Kiwanda cha Kuchakata Samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali ilione hili, ili kuweza kuchochea maendeleo ya watu wa eneo lile na kwa sababu ndio shabaha ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo, basi Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Mwigulu aangalie uwezekano wa kuwa na Kiwanda cha Kuchakata Samaki kwenye eneo la Ukerewe pale. Kwa sababu samaki wanazalishwa pale na wakichakatwa pale, shughuli za ujasiriamali zitakuwepo na kwa maana hiyo kuongeza wigo wa walipakodi na wananchi wengi watashiriki kwenye kuchangia pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe Wizara iweze kuliangalia jambo hili. Eneo lingine ambalo napenda kushauri ni kwenye eneo la Madiwani. Niipongeze sana Serikali kwa kufanya uamuzi wa kuchukua jukumu la kuwalipa Madiwani kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali. Sasa pamoja na kuchukua jukumu hili kumekuwa na kilio kikubwa sana cha Madiwani wetu kuomba posho hizi wanazozipata ziweze kuongezwa. wamesema Wabunge wenzangu ni jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile pamoja na kuchukua jukumu la kulipa posho za Madiwani kuna kundi kubwa sana la viongozi wetu wa vijiji na vitongoji na mitaa; Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji na Wenyeviti wa Mitaa. Niiombe Seirkali itoe mwongozo kupitia TAMISEMI, basi lile eneo ambalo Halmashauri zilitumia kulipa Madiwani zihakikishe mafao ya Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa yaweze kulipwa effectively ili kuweza kuhamasisha shughuli za maendeleo kwenye maeneo yetu. Nakushukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuweka mchango wangu kwenye Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajadili Mpango wa Mwaka Mmoja katika Mpango wa Miaka Mitano wa 2021/2022 hadi 2025/2026 ambao vipaumbele vyake ni pamoja na kuchochea uchumi shirikishi na shindani, vilevile kuimarisha uwezo wa uzalishaji. Ili mpango huu uweze kutekelezeka ni lazima Serikali iwekeze kwenye sekta ambazo kwanza zitaongeza uzalishaji na kwa maana hiyo katika kuongeza uzalishaji tutaongeza mauzo yetu nje jambo ambalo litasaidia kuongeza Pato la Taifa. Vilevile Serikali iwekeze kwenye sekta ambazo zitatengeneza ajira kwa wingi, jambo ambalo litasaidia kutengeneza nguvu ya manunuzi kwa mtu mmoja mmoja na kwa maana hiyo kuongeza mzunguko wa kifedha na kwa level ya chini kuongeza hali ya kipato kwa Halmashauri zetu na kuimarisha mfumo wa utendaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuhimarisha sekta hizi nilitaka nichangie kwenye maeneo kama matatu hivi: Kwanza ni eneo la uvuvi. Ninatambua mpaka mwaka jana sekta ya uvuvi imekua kwa karibu asilimia Sita na kuchangia kwenye Pato la Taifa kwa asilimia kama 1.71. Tunaweza kuzalisha zaidi kama tutawekeza kwenye sekta hii ya uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana kwa mfano mavuno ya samaki, tumevuna tani karibu laki nne na elfu kumi na tano. Niipongeze Wizara, pamoja na kuwekeza karibu Bilioni 20 kwenye mfumo wa ufugaji wa samaki kupitia njia ya vizimba, jambo ambalo litasaidia angalau vizimba 800 kuanzishwa lakini tunaweza tukazalisha zaidi kama tutawekeza zaidi kwenye ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu pamoja na Serikali kupitia Wizara ya Uvuvi, kuwekeza Billion 20 kwenye ufugaji wa vizimba. Ninashauri kuwe na mnyororo wa ufuatiliaji kutoka Wizara na wale watakao pewa mikopo ili kuweza kuwasaidia kutoa ushauri wa kitaalam, vilevile kusaidia kutafuta masoko ya bidhaa ambazo watu hawa watakuwa wanazalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni la utalii. Pamoja na kwamba kwenye mwaka uliyopita sekta hii ya utalii imechangia karibu asilimia 17 ya Pato la Taifa na zaidi ya asilimia 25 ya fedha za kigeni lakini tunaweza tukafanya vizuri zaidi. Nimpongeze Mheshimiwa Rais, kupitia Royal Tour sekta ya utalii imefanya vizuri sana baada ya uzinduzi wa Royar Tour, lakini nishauri maeneo kama mawili:

Kwanza, bado tuna vivutio vingi sana vya utalii atujaweza kuvitambua na kuvitangaza. Eneo kama Ukerewe tunavyo vivutio vingi, tumekuwa tunasema hapa tuna jiwe linalocheza, tunazo fukwe nzuri sana lakini bado azijaweza kutambuliwa na kuweza kutangazwa pamoja na maeneo mengine, nishauri Wizara ya Utalii, iweze kutafuta bado, kubaini vivutio vingine vingi vya utalii vilivyopo iweze kuvitangaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pili, lingine ni eneo la kilimo. Ni muhumu sana, wachangiaji wengi wamesema juu ya sekta ya kilimo, nami bado nashauri tunahitaji kuwekeza nguvu kubwa kwenye sekta ya kilimo. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, anafanya kazi kubwa sana kwenye sekta hii ya kilimo lakini bado tunahitaji tuwekeze kwa kiasi kikubwa sana, tuweze ku-utilize rasilimali tulizonazo ili ziweze kuwa na tija na kuongeza Pato la Taifa kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo kama Ukerewe wiki iliyopita tumeomba chakula Wizara ya Kilimo lakini kwetu Ukerewe tumezungukwa na maji, tunaweza tukafanya kilimo cha umwagiliaji tuna hekta zaidi ya elfu mbili ambazo ziko tayari kwa kilimo cha umwagiliaji. Tunachohitaji ni msaada tu wa Serikali kuwekeza ili tuweze kutumia maeneo yale kwa tija. Jambo hili pamoja na Ukerewe lakini hata maeneo mengine. Kwa hiyo, nishauri bado tunahitaji kuwekeza kwa kiasi kikubwa sana kwenye kilimo cha umwagiliaji kwenye Taifa hili kwasababu tunayo ardhi ya kutosha tunazo rasilimali maji za kutosha jambo ambalo linaweza likatufanya tukafanya kilimo cha umwagiliaji na kikawa ni kilimo cha tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uwekezaji huu kwenye sekta za uzalishaji. Kwenye sekta zinazotengeneza ajira bado haitokuwa na tija sana kama wananchi wetu hawawezi ku-move kutoka upande mmoja kwenda eneo lingine kufanya shughuli zao za kiuchumi. Nimeona kwenye mpango juu ya uimarishaji wa barabara zetu mbalimbali. Niombe kwa utulivu kabisa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, wanisikilize kwa makini kwenye ukurasa wa 24 wa mpango imetajwa barabara Na. 4141 imetajwa kwa jina la Nyamswa, Bunda, Kisolya ningeomba barabara hii ifanyiwe marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii kwa asili tokea upembuzi, usanifu wa kina imetajwa kwa barabara kwa jina la Nansio, Kisolya, Bunda, Nyamswa. Kwa hiyo, ifanyiwe marekebisho na kwenye hoja yangu kwenye eneo hili, ili kuimarisha mawasiliano kwa sababu barabara hii ilitengenezwa kwa Lots tatu, lot ya kwanza na lot ya pili tayari inaendelea basi ikamilishwe lot ya tatu ya kutoka Kisolya kwenda Nansio ili kurahisisha mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii nitumie nafasi hii. Kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kutupa nafasi hii kuweza kujadili mambo mbalimbali yanayotugusa na yanayogusa jamii yetu. Nimshukuru sana pia Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kazi kubwa sana anayoifanya kwa ajili ya kuleta maendeleo kwenye taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu yake yote kwa hotuba nzuri iliyowasilishwa ambayo kwa ujumla wake inaota muelekeo wa nini kimefanyika nini kinapaswa kifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi hii nitachangia kwenye maeneo machache. La kwanza, mwaka 2020 Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara pale Ukerewe; haya ni yanayohusu jimbo langu. Tukiwa kwenye Kisiwa cha Ilugwa tuliwasilisha ombi letu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kutambua changamoto za afya zilizo kwenye eneo lile, tukaomba tusaidie Serikali iweze kutujengea kituo cha afya kwenye Kisiwa cha Ilugwa. Nitumie nafasi hii kuishukuru sana Serikali, kwa hatua ya awali tumepata Milioni 250 na kituo kile kimeanza kujengwa kwa hiyo, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile tuliwasilisha ombi la kusaidia kupandisha hadhi ya Hospitali yetu ya Wilaya ya Nansi pamoja na ile ya Kisiwa cha Ukara. Ombi lile Mheshimiwa Waziri Mkuu alilichukua ,na nashukuru vilevile Serikali imeweza kulifanyia kazi; na hatua iliyopo sasa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Nansio tayari mkandarasi amepatikana na Serikali imetupa pesa takriban bilioni tatu, jambo ambalo litasaidia sana kusaidia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe tu Serikali itusaidie, kwamba maadamu wakandarasi wamepatikana basi mkataba usainiwe haraka na kazi ifanyike kwa mapema ili ianze kutoa huduma kwa wananchi ambao wanaathirika sana na jiografia ya eneo lile kuweza kupata huduma kwenye maeneo ya Mwanza Mjini na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tulimueleza Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyokuja pale. Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. Magufuli mwaka 2018 tulimueleza tatizo la barabara kilometa 14 kutoka Lugezi kwenda Nansio Mjini, na akatoa maelekezo barabara ile ijengwe kwa haraka. Alipokuja Mheshimiwa Waziri Mkuu tulimueleza jambo hili akasema atalichukua ili iweze kufanyiwa kazi kwa haraka. Niombe sana Serikali itusaidie kilometa 14 hizi ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami zinazotuunganisha kati ya Bunda na Nansio ili kuweza kuboresha uchumi wa watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kupitia Ilani ya Uchaguzi, Ilani ilielekeza, na wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu anakuja Ukerewe tuliwaahidi wananchi wetu kwamba tutafanikisha upatikanaji wa vivuko, kivuko cha kutoka Bwiro kwenda Bukondo na vilevile kutoka Rugezi kwenda Kisolya. Niashukuru kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 47 Serikali imedhamiria mwaka huu kulifanyia kazi jambo hili. Lakini niombe tu, pamoja na haya bado kuna maeneo mengine ambayo yanahitaji msaada wa haraka sana. Usafiri wa kutoka Bukindo kwenda Ilugwa pamoja na kutoka Kakukuru kwenda Kisiwa cha Gana ni muhimu sana ukafanyiwa kazi haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu kwenye hotuba ya Waziri Mkuu ni kwenye maeneo mawili sana sana. Kwanza eneo la Afya. Tukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 51 inaonesha namna gani Serikali yetu imefanya kazi kubwa sanaya kujenga vituo vya afya. awamu ya tano vimejengwa vituo zaidi ya 300, awamu ya sita mpaka sasa vimejengwa zaidi ya vituo 200, kwa hiyo utakuta kwamba tuna vituo karibu 600. Lakini bado kuna zahanati nyingi zimejengwa; na kwa sera yetu tuliyonayo tunatakiwa tujenge kituo cha afya kila kata, zahanati kila kijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nina wazo mbadala. Kwamba, badala ya kuendelea kujenga vituo vya afya na zahanati ilhali hizi ambazo tayari zimejengwa hazitoi huduma zile tulizozitarajia kwa wananchi wetu ninaona kama litakuwa si jambo jema sana. Ushauri wangu, ningeshauri kwamba maadam tayari tumejenga vituo hivi zaidi ya 500 tuna zahanati nyingi lakini bado hakuna watumishi, hakuna vifaa tiba na kadhalika, angalau tungeweka pending kwa mwaka mmoja ili ile pesa ambayo tungeendelea kujenga vituo hivi vya afya tuweze kuboresha vituo hivi ambavo tayari tumejenga ili vipate vifaa tiba kwa mfano x-ray machines, ultra-sound, darubini na kadhalika. Pia vipate watumishi wa kutosha ili wananchi wetu waliopo kwenye maeneo haya waweze kupata huduma, na baada ya hapo sasa tufanye tathimini nini kinatakiwa tena kiweze kujengwa kama ni kuendelea basi yale maeneo ambayo ni strategic area yaweze kuendelea kujengewa vituo vya afya wakati huo haya ambayo tayari yamekwisha pata vituo, vituo hivi viwekwe katika mazingira ambayo yanaweza kusaidia watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini eneo lingine ambalo nilitamani kuchangia nii kwenye eneo la elimu. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa pesa zile za UVIKO 1.3 trillion angalau kwenye maeneo ya sekondari imesaidia. Sasa niombe, kwamba kilichofanyika kwenye eneo la sekondari kifanyike vilevile kwenye eneo la primary kwa kuwa kuna shida kubwa sana kwa sababu hakuna madarasa hakuna nyumba za walimu ikifanyika kwa namna hiyo one time investment inaweza kusaidia sana kuondoa changamoto zilizopo vilevile kwenye eneo la shule za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Serikali, naomba kushauri yafuatayo; kwanza Hospital ya Wilaya ya Nansio haina x-ray machine. Naomba mtusaidie digital x-ray machine ili kuokoa maisha ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Kituo cha Afya cha Nakatunguru kiongezewe miundombinu ili kipunguze msongamano katika Hospital ya Wilaya natatu, kuhusu upungufu wa watumishi kwa kada za afya na elimu unaathiri sana utoaji wa huduma kwa wananchi Wilayani Ukerewe, naomba katika mgao ufuatao wa watumishi Jimbo la Ukerewe liangaliwe kwa upekee.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya pembezoni kama Ukerewe yana upungufu mkubwa wa watumishi, hivyo nashauri katika ajira zinazotolewa basi maeneo haya yapewe kipaumbele. Kwa mfano, Ukerewe ina upungufu wa zaidi ya 50% ya watumishi, hivyo yaangaliwe kwa ukaribu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa watendaji wa vijiji na kata unaathiri sana shughuri za maendeleo; kwa mfano, Wilaya ya Ukerewe ina upungufu wa watendaji wa kata na vijiji 26 hali inayoathiri shughuli za maendeleo kwa wananchi. Hivyo nashauri Halmashauri zipewe haraka vibali vya kuajiri watendaji wa kata na vijiji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshiiwa Spika, kwa kuwa vyuo vipya vya VETA kikiwemo cha Ukerewe vinaelekea kukamilika, nashauri yafuatayo; kufanyike maandalizi ya vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia ikiambatana na mafunzo kwa walimu na wakufunzi wa vyuo hivi ili waweze kutoa elimu inayoendana na mabadiliko ya kiteknolojia na hivyo kutoa mazao yenye uelewa wa teknolojia ya sasa na hivyo kuwa rahisi kushiriki kwenye mapinduzi ya uchumi kwenye Taifa letu.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu cha Murutunguru bado haujakamilika kutokana na fedha kutokupelekwa. Kutokana na umuhimu wa chuo hiki katika kuzalisha walimu kwa ajili ya kufundisha vijana wetu, nashauri fedha zipelekwe ili mradi huu uweze kukamilika na kutoa huduma iliyotarajiwa.

Katika Wilaya ya Ukerewe, kuna ongezeko kubwa sana la watoto na hivyo kuwa na mrundikano mkubwa wa watoto mashuleni, nashauri kuwe na programu maalum ya kufanya tathmini na zijengwe shule nyingine mpya au shikizi na zipewe raslimali pesa pea za kutosha kuwezesha program hii. Kwanza, kidato cha nne baada ya kuhtimu, waliofaulu waanze kidato cha tano mapema.

Kutokana na maendeleo ya TEHAMA na masuala mazima ya IT, matokeo ya kidato cha nne yamekuwa yakitoka mapema, Kuna wakati by January/ February matokeo yanakuwa yameshatoka. Hata hivyo kwa mujibu wa kalenda ya kitaaluma, wanafunzi hawa hulazimika kukaa almost miezi mitano idle. Kwa kuwa siku hizi wanafunzi wanamaliza mapema sana, wapo watoto wanamaliza wakiwa na miaka 15 umri ambao ni risk sana mtoto kukaa idle miezi mitano. Nashauri tuone uwezekano wa wanafunzi hao wanaomaliza na kufanya kidato cha nne mwezi Novemba, waanze masomo ya kidato cha tano mapema mwezi Machi walau kupunguza muda wa kukaa idle nyumbani. Aidha, pawepo na link kati ya Wizara ya Elimu/ TCU na Wizara ya Utumishi/Sekretarieti ya Ajira.

Katika miaka ya karibuni vyuo vimekuwa vikibuni course ambazo ni mpya ili kuendana na mahitaji. Hata hivyo inaonekana kuwa ni kama hakuna mawasiliano kuwezesha course hizo mpya kutambulika katika mifumo ya ajira. Kwa mfano hivi karibuni TRA ilitangaza kazi kupitia Sekretarieti ya Ajira lakini baadhi ya applicants wameshindwa ku-apply kwa sababu tu course hiyo haitambuliki.

Kwa mfano course hii; Development Finance& Investment Planning inayotolewa na Chuo cha Mipango, ndani ya course hii wanafunzi wanasoma course ambazo zinafundishwa pia IFM kama vile Public Finance And Taxation, Accounting, International Finance, Cost Accounting na kadhalika, hata hivyo mwaka 2020 wanafunzi wa course hii mfumo haukuwatambua katika nafasi zilizotangazwa za Tax Management na nafasi Customs Management. Huu ni mfano mmoja halisi ambao mnaweza kujiridhisha katika Chuo cha Mipango Dodoma.

Ushauri; nashauri Serikali ishirikiane kuzitambua course na kuziingiza katika sifa/mifumo ya ajira, ndio maana nasema pawepo na link kati ya Wizara/TCU na Utumishi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, napenda kutoa hongera kwa utekelezaji wa majukumu yao na nashauri yafuatayo: -

Kwanza pump kwa ajili ya Mradi wa Kazilankanda, Wilayani Ukerewe ni suluhisho la changamoto ya maji vijijini. Kupitia pesa za UVIKO tulikubaliana na MD RUWASA sehemu ya pesa hizo kununua pump mpya lakini jambo hili limechukua muda mrefu. Naomba pump hii ipatikane mapema kuondoa adha ya maji Ukerewe.

Mheshimiwa Spika, pili ni kuhusu Mradi wa Maji Mjini Nansio, pamoja na jitihada kubwa zinazoendelea, lakini bado wananchi wengi Mjini Nansio hawana maji kutokana na gharama kubwa za kuunganisha maji.

Nashauri Wizara kuikopesha mamlaka iweze kusogeza maji maeneo ya jirani halafu wananchi wakiunganishiwa basi mamlaka iweze kurejesha pesa hizo. Hii itasaidia jamii kupata maji safi na salama.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii, lakini nikushukuru.

Mheshimiwa Spika, kwa namna pekee nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii Pamoja na wasaidizi wake wote, kwanza kwa kufanya utaratibu wa kukutana na Wabunge wa Majimbo yote angalau kwa kujua changamoto za majimbo yetu; lakini pili kwa taarifa ya mtiririko wa fedha zilizoenda majimboni kwetu, jambo linalotusaidia kufatilia na kusimamia fedha hizi. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri pia kwa kukubali pendekezo letu la kutoa bei elekezi za vifaa vya ujenzi kulingana na jiografia za maeneo yetu. Ingawa ninatambua uamuzi wake ni mzuri lakini bado kwenye eneo kama la Ukerewe bado changamoto ni kubwa sana. Kwa hiyo pamoja na kutoa bei elekezi kwa Mkoa wote wa Mwanza Ukerewe ichukulie kama special area katika kutoa bei elekezi ya ununuzi wa vifaa.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwa mtitiriko wa fedha kwenye Jimbo la Ukerewe pekee kwa mwaka huu wa fedha mpaka hivi ninavyoongea tumepata takriban bilioni nane kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, kwa kweli ni jambo kubwa linahitaji kupongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye eneo hili nimshauri Mheshimiwa Waziri, Mhehsimiwa Rais anapoleta fedha hizi kwenye maeneo yetu, pamoja na lengo la msingi la kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo lakini vilevile ni pamoja na kuchochea uchumi wa maeneo husika. Kwa sababu kwa mfano kwenye eneo la Ukerewe imekuja takriban bilioni nane, inapokuja bilioni nane kwenye eneo la Ukerewe basi ioneshe reflection kwenye maisha ya wananchi wa Ukerewe; kwamba kweli kwenye eneo letu imekuja bilioni nane. Na kwa sababu hiyo inapokuja bilioni nane vifaa vya ujenzi vitanunuliwa nje ya Ukerewe, wananchi wa Ukerewe hawawezi ku - feel ile bilioni nane kama imekuja kwenye eneo lile.

Mheshimiwa Spika, sasa, inawezekana huko nyuma tulikuwa tunanunua vifaa nje ya eneo husika kwa sababu ya bei, lakini sasa kwa hii bei elekezi mlioyitoa, nimuombe Mheshimiwa Waziri atoe mwongozo. Kwamba, kama hakuna sababu zozote za msingi basi vifaa kwa ajili ya ujenzi viweze kununuliwa kwenye maeneo husika ili angalau hata ile hali ya maisha ya wananchi wenye eneo husika iweze kuonekana kutokana na ile fedha iliyoenda kwenye eneo husika.

Mheshimiwa Spika, lakini tunaleta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yetu; na kwa mwongozo alioutoa Mheshimiwa Waziri, ametoa maelekezo viongozi wa Serikali za Mitaa washiriki katika kusimamia miradi hii pamoja na kuhamasisha wananchi katika kupanga namna ya kutekeleza miradi hii. Hiyo ni taswira ya umuhimu wa viongozi wa vijiji na vitongoji kwenye utekelezaji wa mirdi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maslahi ya viongozi wa Serikali za mitaa bado yako chini sana. Niombe Mheshimiwa Waziri, hebu tuiangalie, Serikali iangalie ni namna gani kuboresha maslahi ya viongozi hasa wa vijiji na vitongoji. Bado ni changamoto kubwa sana pamoja na kazi kubwa wanayoifanya katika kusimamia miradi yetu ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo nilitamani kuchangia ni eneo la TARURA. Nitumie nafasi hii kupongeza sana Serikali, lakini nimpongeze sana Eng. Seif, Mtendaji Mkuu wa TARURA, anafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi kubwa inayofanyika kwenye eneo hili la TARURA barabara zilizo chini ya TARURA ndio barabara kiunganishi kati ya wananchi kwa maeneo mbalimbali, ili kusafirisha bidhaa zao, lakini na kurahisisha shughuli zao za maendeleo za kila siku.

Mheshimiwa Spika, hali ya barabara zetu kwenye eneo la Ukerewe kwa mfano, bado haziko vizuri sana. Pamoja na jitihada kubwa, Ukerewe tulikuwa tunapata bajeti ya milioni 700 leo tunapata zaidi ya bilioni 2 ni maendeleo, lakini bado pesa hizi hazitoshi. Niombe, kama walivyosema wachangiaji waliotangulia kuna umuhimu wa kuangalia namna ya kuongeza fedha zitakazoweza kusaidia TARURA kuweza kufanya kazi kubwa zaidi kwenye ujenzi wa barabara zetu.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na kazi hii kubwa inayofanywa na TARURA, kuna mambo mawili ambayo ningependa kushauri. La kwanza ni hili la mgawo wa pesa
ambalo tayari nimekwishalisemea, lakini la pili ni namna wakandarasi wanaotekeleza miradi hii wanavyopatikana.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, tunatoa hamasa na tunahamasisha kwamba, wakandarasi wazawa wapewe fursa za kujenga barabara zetu, lakini kuna wakandarasi wazawa ambao wamekuwa kikwazo kwenye kutekeleza miradi hii ya barabara.

Mheshimiwa Spika, niombe Wizara wakati inapotoa kazi za utengenezaji wa barabara ichunguze na kujiridhisha wakandarasi hawa kama kweli wanaweza kumudu kazi hizi ndipo wapewe kazi hizo, lakini bila kufanya hivyo fedha hii haitakuwa na thamani sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nikushukuru sana na Mwenyezi Mungu awabariki sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, natambua kazi kubwa inayofanywa na Wizara katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji, lakini naomba kushauri yafuatayo: -

Kwanza baadhi ya maeneo yanazungukwa na rasilimali nyingi lakini kwa sababu ya kukosa mkakati wa kuzitumia bado jamii inayozunguka ni masikini. Kwa mfano Visiwa vya Ukerewe; uzalishaji wa samaki ni mkubwa lakini hakuna kiwanda cha kusindika hali inayopelekea mazao hayo kutokuwa na tija. Pia Ukerewe ndio wazalishaji wakubwa wa machungwa katika eneo lote la Uganda wa Ziwa, lakini sehemu kubwa huharibika na kutoisaidia jamii.

Mheshimiwa Spika, ombi na ushauri wangu kwa Wizara isaidie kushawishi uwekezaji wa viwanda vya kusindika samaki na matunda Wilayani Ukerewe ili kusaidia uchumi wa eneo hilo na Taifa kwa ujumla.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi kubwa inayofanyika, nashauri yafuatayo; kwanza, miundombinu kuelekea kwenye vivutio vya utalii ni mibovu sana kiasi cha kukatisha tamaa watalii kuvitembelea; pili, Ukerewe kuna vivutio vingi kama jiwe linalocheza la Nyabulebeka, fukwe za Rubya, mapango ya Handebezyo na vingine vingi, lakini hakuna mfumo maalum uliopo kwa ajili ya kuvitangaza.

Mheshimiwa Spika, nashauri wataalam wa Wizara watembelee Ukerewe na kukaa na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ili wapate masada wa kitaalamu katika sekta ya utalii ili vivutio hivi vilinufaishe Taifa na jamii ya wananchi wa Ukerewe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Uvuvi na Mifugo. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza, niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu na Watendaji wote katika Wizara kwa kazi wanayoifanya na hasa kwa hotuba yao waliyowasilisha leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021 wakati kama huu na wakati nachangia hotuba ya Wizara hii, nilishauri juu ya umuhimu wa Wizara kuwekeza kwenye ufugaji wa samaki kupitia vizimba. Nimefarijika angalau kwenye hotuba iliyosomwa leo kuna mabadiliko yanaonekana angalau jitihada zimeweza kufanyika na kuongeza idadi ya vizimba, dhamira ikiwa ni kuimarisha ufugaji wa samaki na kuongeza mazao ya ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado hatujafanya vizuri sana kwenye uzalishaji wa mazao ya samaki na ndiyo maana kama mchangiaji mmoja alivyosema hapa wakati anachangia ukiangalia mazao tunayozalisha na kusafirisha kwenda nje Tanzania pamoja na advantage tuliyonayo ya kuwa na maziwa, kuwa na bahari, bado hatujafanya vizuri sana. Ndiyo maana ukiangalia kwenye sources mbalimbali katika idadi ya nchi ambazo zinazalisha na kusafirisha samaki kwa wingi, kwa mfano Morocco ndiyo inaongoza kwa Afrika, Namibia, South Afrika, Mauritius na Senegal, lakini Tanzania kwenye tano bora bado hatumo, bado hatujafanya vizuri sana. Pamoja na kwamba kwa mwaka huu kwa takwimu zilizosomwa na Mheshimiwa Waziri, tumezalisha metric ton karibu 415,000. Mwaka juzi 2020 tulikuwa na metric ton karibu 393,000, ninaamini bado tunastahili kufanya zaidi ya hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tu kwamba pamoja na jitihada hizi tunazozifanya kuimarisha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, ni vizuri tukaangalia vile vile athari hasi za vizimba ili tuweze kuzifanyia kazi zisije kuathiri ufugaji wa asili wa samaki. Kwa sababu tunaweza kuwa tunalalamika samaki wanapungua, kumbe ni matokeo ya athari hasi za vizimba hizi; kunaweza kuwa na athari za kijenetiki na kadhalika. Kwa hiyo, ni vizuri tukaangalia vile vile kiutafiti kama zipo athari hizo, basi tuweze kuzifanyia kazi ili wakati tukiendelea na mpango huo ili wavuvi wetu wa asili wasije kuathirika na ufugaji wa vizimba ambao tunawekeza hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nilitaka kulichangia ni juu ya uvuvi wa samaki aina ya dagaa. Dagaa ni samaki wanaopatikana kwenye maziwa tuliyonayo kwenye nchi yetu hii; Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Ziwa Victoria; na kwa sehemu kubwa inatoa ajira nyingi sana kwa wananchi wetu hasa akina mama na vijana. Hata hivyo kumekuwa na shida kubwa sana, na kwa mtizamo wangu Serikali haijawekeza ipasavyo katika kuongeza thamani ya mazao ya samaki hawa aina ya dagaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, kwa mfano, mwaka 2021, Shirika la Chakula Duniani (FAO) kwa mujibu wa ripoti yao iliyotolewa mwezi Desemba inaonesha samaki hawa aina ya dagaa, pamoja na kuzalishwa lakini post-harvest loss ipo kwa karibu asilimia 16 na wakati wa masika/wakati wa mvua inaenda mpaka asilimia 60 jambo linaloifanya Serikali yetu kukosa mapato ya karibu Shilingi bilioni 50 kila mwaka kwa sababu ya kushindwa kuwekeza kwenye uvuvi huu na kuweza kuongeza thamani ya mazao haya yaweze kuuzwa na kusafirishwa nje ya nchi na kuweza kusaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naombe sana kama nilivyotangulia kusema, hii ni ajira kubwa sana ya wananchi hasa vijana na akina mama. Kwa takwimu mlizotoa kwenye hotuba yenu, wananchi karibu milioni nne wanapata kula yao na maisha yao kutokana na uvuvi. Pia uvuvi huu wa dagaa unaajiri karibu asilimia 70 ya wananchi na kutengeneza mzunguko mkubwa sana wa kipato kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali kupitia kwenye Wizara, wekezeni kwenye uvuvi huu wa dagaa mwasaidie wananchi wetu, tusiwe tunatoka tu kwenda kufanya operation na kuathiri maisha ya uvuvi wa watu wetu. Tuwekeze vile vile, tuweze kuwaelimisha na kuongeza mitaji yao wafanye uvuvi wa kisasa na kuongeza thamani ya mazao ya samaki hawa hasa dagaa. Kwa sababu ikiongezeka thamani ya dagaa kama nilivyotangulia kusema, itaboresha sana maisha ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mchango wangu ulikuwa kwenye maeneo hayo mawili. Naomba sana wekezeni kwa kiwango kikubwa sana kwenye uvuvi wa dagaa. Tunapokuwa tunapoteza kwa mwaka Shilingi bilioni 50, ni pesa nyingi sana ambazo tungeweza tukafanyia mambo mengine mengi. Kwenye eneo kama la kwangu la Ukerewe pale, sehemu kubwa, zaidi ya asilimia 90 ya vijana na akina mama wanapata maisha yao kutokana na uvuvi wa dagaa, tuwawezeshe, tuwasaidie, tuongeze thamani ya mazao yao. Leo dagaa wanaovuliwa wanaanikwa kwenye mchanga, wakati mwingine wakati wa mvua hawakauki, inaathiri kipato kwa ujumla na maisha ya wananchi wa eneo langu la Ukerewe, naamini na kwenye maeneo mengine katika Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Serikali kupitia Wizara wekezeni kwenye eneo hili muweze kuwasaidia wavuvi wetu wa dagaa tuongeze thamani ya mazao yao, itasaidia sana uchumi wao na uchumi wa Taifa kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naungana mkono hoja. Ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kunifanya nisimame leo mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya na hasa kwenye sekta hii ya maji. Mambo makubwa sana yamefanyika, uwekezaji mkubwa sana umefanyika na changamoto nyingi tulizokuwanazo kwenye sekta ya maji sasa zimepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawapongeza Wizara ya Maji. Mheshimiwa Waziri, Naibu na timu yote ya watendaji, kwa kweli mnafanya kazi kubwa sana. Mimi ni shuhuda kupitia Jimbo langu la Ukerewe, mmefanya kazi kubwa. Pamoja na kwamba kuna changamoto bado, lakini tulipokuwa, na hapa tulipo, kuna kila sababu ya kuwapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tanzania kama Taifa, tuna vyanzo vingi vya maji. Sisi Ukerewe tunazungukwa na Ziwa Victoria. Katika ukubwa wa eneo la Wilaya ya Ukerewe, squire kilometer kama 6,400 ni asilimia 10 tu iliyo nchi kavu. Asilimia 90 yote ni maji. Sasa kwa kusema hivyo, wakati mwingine inaleta shida unapomwambia mtu kwamba Ukerewe tuna shida ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza Wizara, mmefanya kazi kubwa. Mwaka 2022 mmetupa pesa nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, tumepiga hatua. Miradi hii ikikamilika, kimsingi tutabakiza eneo dogo sana. Hivi sasa tuna chini ya asilimia 70 ya maeneo ambayo yanapata majisafi na salama, lakini miradi yetu ikikamilika, tutakuwa tumeenda mpaka zaidi ya asilimia 90, ni jambo la kupongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla, kwa mwaka huu wa fedha mmetutengea zaidi ya Shilingi bilioni tano kwa ajili ya vijiji vyetu vitano vya maji; Kijiji cha Chabilungo, Kamea, Mkuno, Halwego na Bugorora, jambo ambalo litafanya coverage ya watu watakaokuwa wanapata majisafi na salama, kama miradi hii itakamilika, kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, tuna shida kubwa moja ambayo niliona ni muhimu niiseme hapa ili Mheshimiwa Waziri uone namna gani utaweza kutusaidia. Mwaka 2021 tulikuwa na tatizo kubwa sana kupitia mradi wetu wa maji vijijini, maarufu kama Mradi wa Kazilankanda, ambao unahudumia zaidi ya vijiji 10. Mradi ule unapata umeme kutoka TANESCO lakini bahati mbaya wana-treat mradi huu ambao unatoa huduma kwa wananchi kama mradi wa kibiashara, jambo ambalo limekuwa linafanya kila mwezi kunakuwa na service charge kwenye bili zaidi ya Shilingi milioni tatu.

Mheshimiwa Spika, haingii akilini kwamba inakuja bili ya Shilingi milioni tano, lakini service charge pekee ni zaidi ya Shilingi milioni tatu. Jambo hili lilitufanya tuweze kukaanao na kushauriana. Wakatushauri tutafute pump nyingine ambazo zitaendana na kiwango kile cha matumizi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nawashukuru, mlinisaidia sana tukaweza kuagiza pump, tukazifunga. Wakatuomba tulipe deni, tumelipa, lakini bado wanakuwa wagumu sana kubadili mita yao, jambo linalopelekea bili iwe kubwa, na inakuwa ni mzigo kwa wananchi. Wanaingia gharama kubwa sana kulipa deni lile. Mwisho wa siku katika mwezi, wananchi wanapata maji wiki moja, wiki tatu hawapati maji.

Mheshimiwa Spika, sasa naiomba Wizara, sioni sababu ni kwa nini TANESCO, Taasisi iliyo chini ya Serikali, RUWASA Taasisi iliyo chini ya Serikali, mnashindwa kukaa na ku-solve tatizo kama hili, mwisho wa siku wanaoteseka ni wananchi.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Ukerewe wanaopata maji kupitia mradi huu wa maji vijijini, Mradi wa Kazilankanda wanapata mateso makubwa sana. Leo kwa mfano ninavyozungumza hapa, wananchi wanaopata maji kupitia mradi huu, wana zaidi ya wiki tatu hawajapata maji, kwa sababu tu ya kukosa muafaka kati ya Wizara ya Maji na Wizara ya Nishati, juu ya nini kifanyike kwenye suala la umeme ili wananchi wapate huduma wanayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru wakati Mheshimiwa Naibu Waziri, amekuja Ukerewe alisaidia angalau ku-solve tatizo hili. Baada ya hapo, atakumbuka tulikubaliana kwamba sasa baada ya ku-clear deni, TANESCO wabadili mita, lakini bado jambo hilo halikufanyika. Kwa hiyo, naiomba Serikali ilichukulie jambo hili kwa uzito. Haiwezekani tunazungukwa na maji halafu bado wananchi wa Ukerewe waendelee kuathirika na maradhi yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama. Ni jambo lisilokubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri alichukulie jambo hili kwa uzito wa pekee. Nawashukuru, tulileta maombi tusaidiwe angalau kuongeza mtandao wa usambazaji wa maji kwenye eneo la mjini. Kwenye bajeti hii tumekubaliwa, wametupa angalau shilingi milioni 300. Ni jambo jema, lakini bado nitaendelea kuomba, kwa lile ombi la karibu shilingi 1,200,000,000 waendelee kutusaidia.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza Mameneja wa Maji wa eneo la wilaya na mkoa, wanafanya kazi kubwa sana. Mtusaidie kutupa pesa hizi tuongeze mtandao. Wana uwezo wa kujisimamia na kukusanya mapato yatakayowafanya waweze kuongeza mtandao kwa gharama zao, lakini kinachokosekana ni ule mtaji tu wa kuongeza mtandao. Watusaidie kwenye eneo hili, ili mamlaka ya maji pale iweze kujiendesha. Sina mashaka nao. Zaidi ya hilo, nawapongeza, wanatusaidia kwa sehemu kubwa sana ukiachilia mbali eneo hilo la mradi wa maji vijijini, sehemu nyingine tunaenda vizuri na wametusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, niwashukuru kwa zaidi ya shilingi bilioni tano walizotutengea kwa mwaka huu kwa ajili ya kuongeza mtandao. Ni jambo jema, lakini bado naomba with a serious note, kwenye hili eneo la Mradi wa Kazilankanda, watusaidie huu mgogoro wa umeme tuondokane nao ili wananchi wa Ukerewe wa-enjoy matunda ya kazi inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyedhamiria kuondoa shida ya maji kwenye jamii yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa na hayo machache, nashukuru sana kwa nafasi. Mwenyezi Mungu akubariki sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kunipa fursa hii ya kuendelea kuvuta pumzi hii ya bure. Nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa sana anayoifanya kwenye maeneo yote yanayohusu huduma za jamii kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Ukerewe ni wanufaika wakubwa sana wa mapenzi mema ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nikupongeze Mheshimiwa Waziri,Dada yangu Ummy, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara. Mheshimiwa Ummy na Naibu Waziri, ninyi ni watu wema sana, ni watu wasikivu, ni watu wafuatiliaji lakini zaidi ni watendaji wazuri na watendaji bora sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sijui nini nitawalipa lakini Mwenyezi Mungu atawalipeni. Hamna baya kwangu na ninaamini hamna baya kwa wananchi wa Ukerewe, hasa kwa mapenzi mema mliyonayo na mipango mliyonayo kwa wananchi wa ukerewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ukerewe nimekuwa ninasema kila wakati tuna changamoto nyingi lakini huduma za afya ni moja kati ya changamoto zinazotusibu sana wananchi wa Ukerewe. Nishukuru kwa miaka michache hii kuna jitihada kubwa za kuboresha upatikanaji wa huduma za afya. Tumeongeza zahanati, tumeongeza vituo vya afya, Serikali imetuletea pesa tumejenga kituo cha afya cha Ilugwa. Mwaka 2022 tumepata pesa tunaendelea na ujenzi wa kituo cha afya cha Murutilima lakini pamoja na zahanati nyingi zinazoendelea, tumejenga Kituo cha Afya cha Igala, yote ni mema.

Mheshimiwa Naibu Spika, maombi yangu kwako Mheshimiwa Waziri, pamoja na changamoto tulizonazo lakini niombe sana vituo hivi tulivyovijenga bado havina vifaa. Niwaombe sana mtusaidie vituo hivi vitatu vya afya vipate vifaa. Lakini zahanati ambazo tumejenga kwa kushirikiana na wananchi, zahanati zaidi ya sita, vilevile, tupate vifaa ili zianze kutoa huduma kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, pale Bwise mmetuletea pesa tumekamilisha ujenzi wa kituo cha afya kikubwa sana ambacho tumekipandisha kuwa Hospitali ya Wilaya na Kituo cha Afya cha Muliti, bado vituo hivi havina majokofu kwa ajili ya kutunzia miili ya wenzetu walioaga dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotokea kwa mfano pale Muliti hata pale Ukara, ikitokea mwenzetu kaaga dunia inabidi tusafirishe kupeleka hospitali ya wilaya kumhifadhi halafu ndio taratibu nyingine ziendelee. Ni mateso kwa wananchi wetu, mtusaidie ili tuweze kuboresha kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna changamoto ya watumishi. Mheshimiwa Waziri, nishauri sijui kama itawezekana lakini ni jambo jema. Sisi pale Ukerewe kwa sababu za kijiografia wanakuja watumishi lakini muda mfupi wanaondoka kwa sababu mbalimbali. Mnaonaje mkianzisha chuo cha uuguzi na uganga pale Ukerewe? Ili kupitia Chuo kile wanafunzi wakiwa wanapata mafunzo yao pale wakiwa wanatumia muda wao wa mafunzo kufanya mazoezi kwenye zahanati, hospitali na vituo vyetu vya afya, inawezekana ikasaidia sana kupunguza changamoto ya watumishi tuliyonayo kwenye hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri na wizara kwa ujumla, tulileta kilio kwenu kuonesha changamoto tulizonazo kwenye visiwa vya ukerewe hasa tunapopata wagonjwa wa dharura wanaohitaji rufaa kwenda kupata huduma kwenye hospitali ya mkoa. Mlitusikiliza mkaridhia kujenga hospitali ya rufaa kwa ngazi ya mkoa kwenye Visiwa vya Ukerewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo jema sana ninashukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Ukerewe. Lakini niwapongeze sana kwa changamoto zilizojitokeza namna mlivyotusaidia kuzishughulikia mpaka hapa tulipo leo. Mheshimiwa Waziri, ulinipa jukumu la kutafuta eneo ili tuendelee na ujenzi wa hospitali yetu ile ya rufaa ngazi ya Mkoa. Nikuhakikishie tayari kwa kushirikiana na viongozi wenzangu tumekwisha kamilisha mchakato huo eneo limepatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe baada ya bajeti yako kupitishwa, ninaimani wala sina shaka tutaipitisha, twende ukerewe, ukajiridhishe na eneo lile ili kazi iendelee. Hautakuwa na baya kwa wananchi wa Ukerewe, hautakuwa na baya kwangu na kama nilivyosema wema wenu Mwenyezi Mungu atawalipeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na haya yote bado tuna changamoto ya madawa, kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya bado shida kubwa sana ni upatikanaji wa madawa. Wamesema wenzangu waliotangulia kuchangia, kwenye eneo la MSD ambao tunatarajia kwamba wawe waokozi wetu kwenye eneo la madawa, bado kuna shida kubwa sana kwamba hawana mtaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, ili kuweza kuondokana na hili na Kamati yetu inayohusika na masuala ya Afya wametoa pendekezo, Mheshimiwa Waziri, niombe sana tuwawezeshe MSD. MSD wakipata uwezo kwa mfano kwa mapendekezo yaliyotolewa na Kamati, wakipata fedha hizi bilioni 500 ninaamini matatizo makubwa tunayokutana nayo sasa kwenye upatikanaji wa huduma za afya hasa kwenye eneo la madawa inawezekana tukaondokana nalo.

Mheshimiwa Naibu Spika kwa hiyo, niungane na waliopendekeza hasa Kamati, tuwape mtaji MSD, tukiwapa mtaji MSD haya matatizo tunayokutana nayo inawezekana yakaondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa Waziri, pamoja na kazi kubwa sna mnayofanya na pamoja na kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Rais, bado kuna shida hasa kwenye sera yetu ya afya kwenye utoaji wa huduma za afya kwenye kundi la wazee, lakini na watoto wachanga chini ya miaka mitano. Bado kuna tatizokubwa! Kuna kila sababu ya Mheshimiwa Waziri kupitia shida iko wapi? Kwenye eneo la watoto wachanga, kinamama wajawazito lakini vilevile kwenye kundi la wazee. Ili changamoto zilizopo basi tuzifanyie marekebisho ili sera yetu tuitekeleze kikamilifu na watu wetu waweze kupata huduma ile inayotarajiwa. Kama tutaweza kuboresha eneo hili hata changamoto tunazozipata katika ku-initiate hili suala la Bima ya Afya kwa watu wote inawezekana tukaondokana nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niliona nichangie kwenye maeneo hayo; lakini nimalizie kwa kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri na timu yako yete kwa kweli mnafanya kazi kubwa sana. Mmetembelea Ukerewe mmetutia moyo na changamoto tulizokuwa nazo mmezifanyia kazi, na niwaombe muendelee kuzifanya kazi. Zaidi ya yote niendelee kuwashukuru sana na kuendelea kuwakaribisha Jimboni Ukerewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kutoa mchango wangu wa mawazo kwenye hotuba ya Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa nafasi aliyonipa, kuendelea kupumua lakini nitumie nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utendaji kazi wake mzuri lakini na ujasiri wake mkubwa katika kufanya maamuzi na kutenda kwa maslahi ya wananchi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nitumie nafasi hii kukupongeza sana kwa umahiri wako mkubwa katika kutuongoza Bunge hili. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama nisipowapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara ya Nishati, kwa kweli wanaonesha umahiri mkubwa na wanatenda mambo mengi yenye maslahi kwa Taifa letu, tuna kila sababu ya kuwatia moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utakuwa kwenye maeneo mawili, nikitambua umuhimu wa nishati kwa sababu tafiti mbalimbali zimeonesha mahusiano ya moja kwa moja kati ya nishati ya umeme na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwenye Jumuiya mbalimbali, umeme hasa kwa ujumla ni jambo muhimu sana na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali yetu kusambaza nishati hii ya umeme tuna kila sababu ya kupongeza.

Mheshimiwa Spika, ninaushauri kwenye maeneo mawili, eneo la kwanza ni eneo la REA. Kazi kubwa imefanyika na kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake, tuna vitongoji zaidi ya 36,000 ambavyo havijapata umeme, bado kuna kazi kubwa inatakiwa kufanyika. Ni kweli kwamba katika usambazi vijiji vingi vimepata nishati hii ya umeme lakini tuna kila sababu ya kufanya tathmini sasa tukiangalia vitongoji lakini tuende zaidi kwa kuangalia idadi ngapi ya kaya ambazo zimepata nishati ya umeme, itatupa changamoto na kuona namna gani tuna kazi nyingine kubwa ya kufanya ili tuweze kufikisha nishati hii ya umeme, kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba REA imefanya kazi kubwa lakini bado tunahitaji tubuni vyanzo vingine kuweza kusaidia Mfuko wa REA ili angalau mfuko huu ukiweza kutuna basi nishati hii ya umeme iweze kusambaa zaidi kwenye vitongoji vyetu. Kwa hiyo, mimi kwa nafasi yangu ningeweza kupendekeza ikiwezekana hata kwenye nishati kwa mfano, kwenye mafuta ikiongezwa hata shilingi moja tuweze kuongeza vilevile kutunisha Mfuko wa Nishati hii ya umeme ili maeneo yetu yaweze kupata umeme. Kwa sababu pamoja na nishati hii kusambaa kwenye vitongoji, kwenye Jimbo kwa mfano la Ukerewe bado tuna vitongoji vingi havijapata umeme, mbaya zaidi kuna vitongoji ambavyo vimefikishiwa umeme umefika kwenye kitongoji lakini kaya nyingi bado hazipata nishati hii ya umeme. Kwenye vijiji kwa mfano kama Muruseni, Hamuyebe umeme umefika lakini bado kaya hazipata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nilitamani nichangie ni kwenye maeneo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa. Jimbo la Ukerewe tuna visiwa vingi ambavyo viko mbali na Gridi ya Taifa. Nikupongeze Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu, mmepata ujasiri mkaweza kututembelea Ukerewe mkaangalia changamoto zilizoko kwenye Visiwa vyetu vya Ukerewe. Bado visiwa vyetu vingi havijaweza kupata nishati hii ya umeme. Kisiwa kama cha Ukara, Mheshimiwa Waziri unakifahamu kuna watu pale Jumeme wanatoa umeme kama wanavyotoa kwenye Kisiwa cha Ilugwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nitoe ushauri kwenye Kisiwa cha Ukara, hebu kaa na wataalamu wako ikiwezekana na inawezekana angalieni, uwezekano wa kutumia sub-marine cable ili kuweza kuiunganisha Ukara na Gridi ya Taifa na kwa sababu sasa hivi mnapeleka umeme mkubwa, nikupongeze Mheshimiwa Waziri na Wizara yako, kwa mradi ambao mmeuandaa mnapeleka umeme kwenye Visiwa vya Ukerewe ambao kutoka KV 66 mpaka KV 132, umeme huo utahitaji kupata mzigo na ili mzigo huu uweze kupatikana ni muhimu sana visiwa kama cha Ukara ambacho kina Kata zaidi ya tatu ili kiweze kuunganishwa na Gridi ya Taifa kuongeza mzigo kwenye umeme huu mnaopeleka kwenye Visiwa vya Ukerewe. Kwa hiyo, nikushauri kaa na wataalam wako ikiwezekana muweke cable, sub-marine cable muweze kuunganisha kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile katika ukurasa wa 39 wa hotuba yako umeonyesha namna ambavyo mnajiandaa kupeleka umeme kwenye maeneo yaliyoko mbali na Gridi ya Taifa. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri visiwa kama Gana, visiwa kama Burudi, Bwilo, Bweru, Sizu na kadhalika ambavyo kulikuwa na Wakandarasi walienda kwa ajili ya kupeleka umeme lakini wakaishia njiani, niombe sana kwa kushirikiana na halmashauri tunajitahidi kuondoa vikwazo vilivyopo ili sasa hawa wakandarasi walio tayari waende kupeleka umeme kwenye maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu ambalo nilitaka nichangie, yote haya tunawapongeza tuna wasifu kwa sababu kuna kazi inafanyika hasa kupitia Shirika letu la Umeme la TANESCO, lakini yote haya yanafanyika kwa sababu kuna watendaji, kuna watumishi, kuna wafanyakazi wanafanyakazi nzuri ndiyo maana shirika linafanya kazi nzuri. Mheshimiwa Waziri kuna minong’ono inaendelea chini kwa chini, wafanyakazi wako kwenye Shirika hili la TANESCO wanalalamika kuna mambo hayako vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mkataba wa kiutumishi waliokua nao kwa ajili ya kuboresha maslahi yao ya kiutendaji kazi, lakini katika haya moja katika malalamiko yao Mheshimiwa Waziri kuna mabadiliko yamefanyika, huko nyuma ilikuwa watumishi wakienda likizo wanalipwa mshahara wa mwezi mmoja ili waende likizo wakirudi wanaendelea na majukumu yao, lakini katika mabadiliko yaliyofanyika sasa inasemekana kwamba sasa watumishi wakiondoka kwenda likizo hawapewi pesa yoyote, anatakiwa aende kwa nauli yake, akishalipa nauli yake atunze risiti, akirudi ndiyo aanze kudai alipwe fidia kwa zile risiti kutokana na namna ambavyo amesafiri.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri jambo hili litawakatisha tamaa watumishi, liangalieni upya ikiwezekana mliondoe urudishwe utaratibu wa zamani ili watumishi hawa wafanye kazi wakiwa na morale, wakiwa na moyo kwa ajili ya kuleta sifa kwa shirika na tija kwa Taifa letu ili wananchi wetu waweze kupata huduma wanayoitarajia. Vilevile, Mheshimiwa Waziri wamekuwa hawana uhakika na mambo yao, wamekuwa na hofu kwamba inasemekana kwamba mnatarajia kupunguza watumishi kwenye shirika hili, mbaya zaidi taratibu hizi zinaendelea bila kuhusisha Chama cha Wafanyakazi, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri, kama kweli haya yapo Mheshimiwa Waziri ninaomba uyafanyie kazi ili changamoto hizi ziondoke, watumishi wetu katika Shirika la Umeme la TANESCO wafanyekazi wakiwa na moyo, wakiwa na morale ili tija ile tunayoitarajia kutoka kwenye shirika letu hili iweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia nikushukuru sana kwa nafasi hii, lakini ninakuomba tena Mheshimiwa Waziri Ukerewe tunakupenda tunakuhitaji na niwapongeze tena kwa ujasiri wenu kuja kututembela na kuona changamoto tulizonazo. Mtusaidie sana Visiwa vyetu vya Ukerewe ili waweza kufikia maendeleo tunayoyatarajia nishati ya umeme ni jambo muhimu sana, tusaidie sana, zaidi ya yote kwenye eneo la kisiwa cha Ukara kama nilivyoshauri, tafadhali kaa na wataalamu wako, wekeni sub - marine cable pale, muweze kuunganisha Kisiwa cha Ukara na Gridi ya Taifa. Vile Visiwa vingine vidogo ambavyo vina changamoto, changamoto zake mnazifahamu, tafuteni ufumbuzi wa haraka ili wananchi wetu waweze kwenda na kasi ya maendeleo na hasa kwa tija na kasi anayoionesha Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi, Mwenyezi Mungu akubariki sana. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa ili na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii. Kwanza kabisa nimshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenipa fursa ya kuwepo hai na kutoa mchango wangu leo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uimara, uhakika na usalama wa miundombinu ni muhimu sana kwenye jamii yetu, na tafiti mbalimbali zimeonesha mahusiano ya moja kwa moja kati ya uimara, ubora na uhakika wa miundombinu na maendeleo ya jamii inayohusika.

Ninatambua suala la miundombinu ni mchakato ili iweze kuwa imara nakwenye nchi yetu kwa ujumla tumejitahidi kwa kiasi kikubwa na ndiyo maana nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha kwamba miundombinu yetu inakuwa imara, lakini nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara hii kwa kweli kazi kubwa wanaendelea kuifanya pamoja na changamoto kadhaa ambazo bado zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utakuwa kwenye maeneo mawili; eneo la kwanza ni suala la vivuko; Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 57 inatoa maelekezo kwa Serikali kuimarisha miundombinu hasa barabara na vivuko na ukisoma ukurasa wa 84 Ilani inaelekeza si kwa bahati mbaya, kwa makusudi kwamba Serikali ihakikishe pamoja na maeneo mengine yote lakini eneo la Ukerewe, Kivuko cha Bukondo kwenda Bwiro kitengenezwe, kivuko cha kutoka Murutanga kwenda Irugwa kitengenezwe, kivuko cha kutoka Ghana kwenda Kakukuru kitengenezwe pamoja na vingine kikiwemo cha Kisorya kwenda Lugezi.

Niipongeze Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Waziri angalau kwenye bajeti hii nilisikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameonesha dhamira ya Serikali kukamilisha matengenezo ya kivuko cha kutoka Bukondo kwenda Bwiro, lakini vilevile kivuko cha kutoka Kisorya kwenda Lugezi, ni jambo jema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizi bado kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha kwamba hivi vivuko vingine hasa cha kutoka Kakukuru kwenda Ghana na kutoka Murutanga kwenda Irungwa vina kamilika ili viweze kutoa huduma kwa wananchi wetu. Ukiongolea mazingira na maisha ya visiwa inawezekana watu wengine wasiweze kuelewa, lakini yanachangamoto nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kusema hapa mwaka 2017 nikataadharisha bahati mbaya mwaka 2018 tukio likatokea, lakini bado niendelee kutaadharisha ni muhimu sana mazingira ya visiwani yachukuliwe kwa uzito mkubwa na suala la vivuko lipewe umuhimu mkubwa. Juzi hapa kulikuwa na matatizo ya usafiri baada ya mafuta kupanda, boti hii ya kutumia engine yenye uwezo wa kuchukua abiria 50 mpaka 40 wanachukua abiria mpaka 80 kitu ambacho kinaatarisha maisha yao.

Kwa hiyo ni muhimu sana Serikali ika-intervene ikahakikisha kwamba vivuko hivi vinakuwepo ili kuweza kusafirisha wananchi wakaweza kusafirisha katika mazingira yaliyosalama, lakini nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameongelea dhamira ya Serikali kukamilisha majengo ya abiria ya kusubiria. Ni jambo jema sana lakini niombe sana abiria wanataabika sana kwenye maeneo yale, kasi iongezeke ili majengo haya ya abiria kusubiria yaweze kukamilika haraka. Jengo kwa mfano la Bugolola, Jengo la Ukara, Bukimwi pale lakini hata Kisorya ni muhimu sana wakati wa mvua wakati wa jua wananchi wanataabika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka nizungumzie ni juu ya ujenzi wa barabara. Barabara inayojengwa sasa ya kutoka Bunda kuja Bulamba mpaka Kisorya na kimsingi inatakiwa kwenda mpaka Nansio inajengwa kwa lots tatu, lots mbili zile sasa moja imekwishakamilika kilometa 51 lakini inayojengwa sasa ni kutoka Bulamba kwenda Bunda sawa imekamilika kwa asilimia takribani 30 ni jambo jema, lakini barabara hii ili kukamilika inatakiwa ijumuishe vilevile lot ya tatu inayotoka Kisorya kwenda Nansio.

Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako sijaona unaongelea chochote juu ya eneo hili ambalo linajumuisha barabara na kilometa 14 za kutoka Lugezi kwenda Nansio. Kilometa hizi utakumbuka Hayati Dkt. Magufuli wakati ule akiwa Rais alivyokuja Nansio alitoa maelekezo eneo hili lijengwe kwa haraka kutokana na umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyokuja pale Nansio vilevile akatoa maelekezo kwamba kama ilivyoahidiwa mwanzo itekelezwe kwa haraka, lakini sijaona unaongelea chochote juu ya eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara nyingine vilevile ambayo Mheshimiwa Waziri nimeteta na wewe mara kadhaa, Mheshimiwa Naibu nimeteta na wewe, lakini mama yangu Katibu Mkuu tumezungumza wote vilevile, nikawaambieni kuna barabara hii ya kutoka Bukongu kwenda Bukonyo mpaka Masonga, lakini vilevile kuna barabara ya Bukongo kwenda Rubya ambayo kuna msitu mkubwa sana mpaka Bukonyo ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Ukerewe. Nikawaomba kwamba sawa tunatenga nimeona hata katika bajeti hii imetengwa shilingi milioni 100 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida hayatusaidii sana haya kwa sababu barabara ile kwa nature yake inamatatizo makubwa na kwa nature ya udongo wa Ukerewe hatuwezi kupata kifusi cha uhakika cha kuweza kutengeneza barabara ile kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaomba basi tutengeneze barabara hii hata kama ni kwa awamu, lakini angalau tuwe na uhakika wa ubora wa barabara ile na kwa sababu inapitisha magari mengi sana kwenda kwenye lango la uchumi wa wananchi wa Ukerewe mtusaidie angalau tuweze kuijenga kwa awamu iweze kukamilika kusaidia kuimarisha uchumi wa waanchi wa Ukerewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado niwaombe sana Mheshimiwa Waziri zingatieni ushauri wangu, lichukueni hili mtusaidie na bahati njema sana kuna kilometa takribani 10 zishafanyiwa upembuzi na usanifu wa kina mtusaidie muweze kuijenga barabara hii iweze kusaidia kuimarisha uchumi wa wananchi wa Ukerewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wetu pale Ukerewe lango lake ni kutoka kwenye eneo la Kakukuru ambako barabara hii inaenda, niwaombe sana Mheshimiwa Waziri mtusaidie barabara hii iweze kujengwa na mtakuwa mmeimarisha uchumi wa wananchi wa Ukerewe ambao sehemu kubwa inategemea mazao ya ziwa, kwa hiyo niombe sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho, nimeona kwenye hotuba yako kupitia TEMESA mna mpango wa kujenga karakana pale Nansio, ni jambo jema sana natumia nafasi hii kuwapongeza kwa sababu tumekuwa tunapata mazingira magumu sana wakati mgumu sana kusafirisha vyombo vyetu kwenda mpaka Mwanza Mjini kwa ajili ya matengenezo. Kwa hiyo, iwapo itatengenezwa karakana hii itakuwa ni msaada mkubwa sana kwetu kama wananchi wa Ukerewe kuondoa usumbufu ambao tumekuwa tunaupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ya yote niwashukuru sana kwa hotuba yenu, lakini yale ambayo mmeyaweka kwenye mipango hasa kujenga vivuko mtusaidie kazi hii iweze kufanyika kwa haraka, lakini ombi langu juu ya barabara yetu ile kujengwa kwa awamu ni jambo muhimu sana lipeni uzito mkubwa sana ili muweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na kutuwezesha kuwepo hapa. Kwa nafasi ya pekee niwapongeze wawasilishaji wa taarifa zote mbili, ni taarifa nzuri na mpango ni mzuri. Nami mapema kabisa nitamke kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu kama ulivyosomwa inaonesha namna gani kiuchumi tunaenda vizuri. Kwa mujibu wa taarifa hii, kwa taarifa iliyotolewa na Benki ya Dunia mwezi Septemba, kwa miaka mitatu mfululizo uchumi wetu kama Taifa umeendele kukua. Achilia mbali kwamba kidunia uchumi umekuwa unapungua lakini kwetu imekuwa kwa asilimia kadhaa uchumi unaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matarajio kwamba mwakani uchumi utaendelea kuongezeka. Nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa sababu pamoja na changamoto kadhaa, kwa miaka takribani minne mitano mfululizo ame-stabilize hali na uchumi wetu umeendelea kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukua kwa uchumi, kimaandishi uchumi wetu unakua, ni lazima sasa tutakafari zaidi je, hali ya watu wetu inaendana na kukua kwa uchumi huu katika maandishi (katika tarakimu)? Ni lazima tuone je, kuna uwiano? Kwenye mpango kama ulivyosomwa na Mheshimiwa Waziri, kuna mabadiliko makubwa yamefanyika kwenye hali ya kiuchumi ya watu wetu na hili limetokea kwa sababu ya uwekezaji uliofanyika kwenye sekta za kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tufanye vizuri zaidi na ili tufikie athari chanja kwenye eneo hili, ni lazima uwekezaji zaidi uwe kwenye maendeleo ya watu, hasa kwenye eneo la kijamii na kwenye maeneo ya kiuchumi hasa tukiweka mkazo kwenye maeneo ya vijijini. Ni lazima tuimarishe uwezo wa uzalishaiji kwenye sekta muhimu kama kilimo, uvuvi na nyinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili nimekuwa najiuliza, tuna rasilimali nyingi sana kama Taifa, lakini kwa mtazamo wangu, bado hatujaweza kuzitumia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna rasilimali maji ambayo tungeweza kuitumia kwa ubora zaidi na kwa ufanisi kufanya kilimo cha umwagiliaji kuwa msingi wa Uchumi wa Taifa letu. Bado pamoja na jitahada kubwa sana zinazofanywa na Serikali ninatambua mwaka jana tumeongeza bajeti kwenye Wizara ya Kilimo, Wizara ya Kilimo inafanya kazi kubwa sana kujaribu kufufua kilimo kwenye nchi hii. Tunahitaji tufanye zaidi ya hapo tuweze kutumia rasilimali tulizonazo kama maji, tuweze kuitumia vizuri ili kukuza kilimo chetu vilevile kufanya wakulima wetu waweze kunufaika na rasilimali hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa ninatafakari eneo kama Ukerewe ambako tunazungukwa na maji. Katika eneo la square kilometa karibu 6,400 zaidi ya asilimia 90 ni maji. Tuna eneo pale, ni kwa nini Ukerewe watu walalamike kukosa chakula, kuwa na upungufu wa chakula kila mwaka? Ni kwanini, tusiwekeze kwenye umwagiliaji kwa kutumia rasilimali maji yaliyopo kwenye eneo hili kufanya kilimo cha umwagiliaji, kutumia eneo dogo lililopo kwa ufanisi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni sehemu moja lakini kuna maeneo mengi ambayo kwa rasilimali tulizonazo tunaweza tukatumia vizuri tukaweza kuwekeza tukafanya watu wetu kwenye maeneo yaliyopo kule chini kuweza kutumia rasilimali hizo kujiimarisha kiuchumi. Niombe kama nilivyotoa mfano kwenye eneo la Ukerewe pamoja na maeneo mengine, tutumie rasilimali hizi kwa ufanisi ili kuweza kufanya watu wetu kule chini wawe imara kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwenye kilimo hata kwenye uvuvi bado kama alivyokuwa anachangia Mheshimiwa Sanga bado kuna vikwazo vingi sana kwa watu wetu kule chini wanapokuwa wanafanya biashara lakini wanapokuwa wanafanya shughuli za uzalishaji vilevile. Sekta ya uvuvi ni sekta muhimu sana kwenye Taifa hili katika kuimarisha uchumi wetu, wavuvi wetu wanakutana na vikwazo vingi sana vya tozo mbalimbali. Kwa mfano, leo kwenye maeneo ya kanda ya ziwa kuna kitu kinaitwa tozo ya control namba na kadhalika ni kikwazo kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ningeshauri kupitia Wizara ya Uvuvi, ondoeni tozo hii. Inaleta kero kubwa, inaathiri uzalishaji kwa wavuvi wetu kwenye maeneo yale jambo ambalo kiujumla linaathiri uchumi wa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyotajwa kwenye mpango, tukiwekeza kwenye huduma za kijamii, uchumi wetu utaendelea kukuwa kwa kiwango kikubwa sana. Na hili ndiyo maana nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uwekezaji mkubwa sana alioufanya kwenye Sekta ya Huduma za Kijamii, kwenye elimu, afya, kwenye maji, kazi kubwa imefanyika hata miundombinu na maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna maeneo ambayo miundombinu yetu hasa ya usafirishaji kuna changamoto kubwa sana. Niki-sight kwa mfano eneo la Ukerewe, kwenye ilani yetu ya uchaguzi ili kurahisisha mazingira ya watu wetu, kufanya waimarishe uchumi wao kupitia sekta ya usafirishaji, Ilani ilielekeza kujenga vivuko kwa ajili ya kusaidia wananchi wetu kusafiri kutoka eneo moja kwenda eneo jingine kusafirisha mazao yao. Leo eneo kama la Ihugwa kisiwa cha Ilugwa pale Ukerewe, mwananchi anasafiri masaa matano eneo ambalo angeweza kusafiri kwa nusu saa kwa sababu tu mazingira ya usafiri kwenye eneo lile sio bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilani imeelekeza vivuko vitengenezwe kwenye eneo lile. Niombe Wizara zinazohusika katika mpango wa bajeti unaokuja, pesa kwa ajili ya kuelekeza kwenye eneo hili kukamilisha miradi hii iweze kutengwa na iweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kitila katika hotuba yake ameelezea kwamba katika nguzo zinazoshikilia mafanikio ya utekelezaji wa mipango yetu, moja ni kuwa na nidhamu ya utekelezaji wa mambo tunayoyapanga. Wakati Mheshimiwa Sanga anachangia hapa, ameelezea namna ambavyo ni muhimu sana kuwekeza kwenye mifumo ya kiteknolojia (Mifumo ya TEHAMA), lakini mifumo hii hata kama tutaifunga, kama hakutakuwa na ufuatiliaji na tathmini ya namna gani mifumo hii inafanya kazi bado hatutakuwa na mafanikio katika mifumo hii hata kama tutaiweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita tulikuwa tunajidili Ripoti ya CAG. Mambo mengi sana, miradi mingi inakwama kwenye utekelezaji kwa sababu hakuna mfumo wa tathimini na ufuatiliaji. Ndiyo maana niombe Mheshimiwa Kitila, bado kama nilivyosema wiki iliyopita ni muhimu sana tuwe na sera ya kitaifa ya ufuatiliaji na tathmini ili mipango yote hii tunayoipanga tuhakikishe kwamba kweli inatekelezwa kwa namna ambavyo tumedhamiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, tukiwa na national policy ya monitoring and evolution itasaidia kwanza kuongeza uwajibikaji, itasaidia miradi yetu kufanyika katika kiwango bora na thamani ya pesa tuliyowekeza kwenye miradi ile kuonekana. Itaongeza uwazi kwa sababu kutakuwa na ufuatiliaji lakini kutakuwa na tathmini itakayokuwa inafanyika, kutakuwa na ujumuishaji wakati wa utekelezaji wa miradi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, achilia mbali hiyo bado maadili ya watumishi wetu katika kusimamia na kutenda kwenye usimamizi wa miradi hii utaongezeka jambo ambalo litasaidia rasilimali pesa tunazozitomia kuwekeza kwenye miradi mingi ya maendeleo, tathmini yake ikifanyika inakuwa na tija na inakuwa na maslahi kwa Taifa letu. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Kitila katika plan zako zote ulizonazo, bado kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na national policy ya monitoring and evolution ili kuhakikisha rasilimali pesa tunazowekeza kwenye miradi yetu ya maendeleo inafanyika kwa tija na yale tunayotarajia kwa maslahi ya maendeleo ya Taifa letu yanapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nilitaka niuweke kwenye eneo hilo. Ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kutujalia uhai. Nipongeze Kamati zote zilizowasilisha taarifa kwa niaba yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na mchango kwenye maeneo matatu. Kwenye Taarifa ya Kamati ya LAAC ukurasa wa 10 wanatoa mapendekezo baada ya kufanya tathmini na kuona kwamba kuna shida kwanye makusanyo kwenye halmashauri zetu. Kwa maana hiyo, Kamati ya LAAC inapendekeza ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo jema, na kwa uzoefu wa miaka kadhaa tukipokea taarifa za CAG kumeonekana udhaifu kwenye makusanyo ya Halmashauri zetu, lakini vilevile kuna umuhimu wa kuanzisha vyanzo vipya vya mapato. Lakini mimi nilikuwa na mtazamo tofauti. Tuna vyanzo vingi vya mapato na katika vyanzo tulivyonavyo, baadhi vinakuwa ni kero kwa wananchi. Hii ni kwa sababu, moja, kunakuwa hakuna ufanisi kwenye vyanzo tulivyonavyo katika makusanyo yake. Matokeo yake ni kwamba kila mwaka taarifa inayoletwa inaonekana kwamba hatufikii malengo; lakini si kwamba vyanzo havipo. Vyanzo vipo lakini tuna udhaifu kwenye makusanyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo kinachopaswa si kuendelea kubuni vyanzo vipya kila kukicha bali mimi ninachokifikiri, katika vyanzo tulivyonavyo tuweke mifumo thabiti ya kuhakikisha kwamba ukusanyaji wa mapato kwenye vyanzo tulivyonavyo unakuwa ni wenye ufanisi; lilevile tunaziba mianya ya upotevu wa fedha kwenye vyanzo tulivyonavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mianya mingi sana inayopelekea upotevu wa mapato kwenye halmashauri zetu kupitia vyanzo vya mapato tulivyonavyo. Kwa hiyo, badala ya kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ambavyo vingi vinaweza vikawa ni kero kwenye jamii, zaidi tuwekeze kwenye kuongeza ufanisi kwenye makusanyo kwenye vyanzo tulivyonavyo na kuziba mianya ya upotevu wa fedha kwenye vyanzo hivi na hatimaye tutafikia malengo kuliko kuendelea kubuni kila kukicha vyanzo vipya ambavyo vingine vinakuwa ni shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye ripoti ya CAG kama ambavyo imewasilishwa na Kamati, kupitia mashine za ukusanyaji (POS). Kulikuwa na upotevu wa takriban shilingi bilioni 11.07. Fedha hizi ni kwa sababu tu, ya kutokudhibiti mianya hii ya upotevu wa mapato. Kwa hiyo, niendelee kusisitiza, kwa kutumia Kamati zetu; lakini kwa kuwa Serikali mpo, tujenge mfumo ambao utaondoa udhaifu huu ili vyanzo hivi tulivyonavyo viwe ni vyenye tija lakini vilevile ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kwenye vyanzo hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nilitaka kuchangia ni kuhusu ubadhilifu kupitia manunuzi kwenye halmashauri zetu. Nimpongeze Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa sana. Hakuna kipindi ambacho tumepokea fedha nyingi kwenye majimbo yetu kama kipindi hiki. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba fedha zinapatikana, miradi ya maendeleo inapatikana kwenye majimbo yetu. Jukumu tunalokuwa nalo na ambalo tumeonesha udhaifu mkubwa ni kwenye kuthibiti fedha kwenye maeneo yetu kama ambavyo wachangiaji wengi wamesema, juu ya ubadhilifu unaofanywa na watendaji kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natafakari baada ya kupitia taarifa hii, kwamba kwa mfano tumepoteza kwa sample ya halmashauri kadhaa zilizohojiwa na Kamati; kwamba bilioni 3.29 zimelipwa kwenye halmashauri zetu kwa ajili ya manunuzi ya vifaa ambavyo havijaweza kupokelewa; unaweza kuona. Kwa mujibu wa sheria, ukiangalia Sheria ya Manunuzi, Kanuni namba 242 na 248 inaonesha wazi taratibu gani zinapaswa zifuatwe wakati wa manunuzi. Kama inatokea fedha zinalipwa, bidhaa hazijaletwa matokeo yake halmashauri itapokea bidhaa ambazo zina mapungufu au zisizokidhi viwango.

Mheshimiwa Mwneyekiti, na kama imechukuliwa kwa sampeling pekee, je, kwa halmashauri zote tumepoteza fedha kiasi gani? Kwa hiyo, tuna jukumu kama Bunge kuishinikiza Serikali iweze kusimamia eneo hili. Kwa sababu kanuni zipo, kusingekuwa na kanuni tungekuwa hakuna mahala ambapo tunaweza tukasema kwamba inawezekana kuna udhaifu, lakini udhaifu uliokuwepo sasa ni kwenye usimamiziwa kanuni hizi. Kwa hiyo niombe Serikali iliangalie jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo nilifikiri nilichangie ni juu ya miradi inayotekelezwa kwa force accont. Kwenye Taarifa ya Kamati imeonesha udhaifu kwenye miradi inayotekelezwa kwa mfumo wa force account. Kifungu namba 64 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni zake, inaoneshani miradi gani na kwa mfumo upi miradi miradi inaweza kutekelezwa kwa force accout.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mmoja kati ya watu wanaoamini katika mfumo wa Force account katika utekelezaji wa miradi yetu. Tatizo tunalokuwa nalo ni kwenye usimamizi. Hii ningependekeza, ukiangalia uzoefu wa miradi yetu tunayoitekeleza kwa mfumo wa force account, shida kubwa sana inatokea kwenye usimamizi na kufuata taratibu zinazoweza kusimamia utekelezaji bora wa miradi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri, kama ambavyo baadhi ya nchi nyingine zimefanya. Nilikuwa ninapitia kijarida hapa cha nchi ya Zambia ambacho ninafikiri na sisi kama taifa tungeona umuhimu kwamba, tuwe na sera ya monitoring and evaluation ya kitaifa ambayo inaweza kufanya kazi kwa kusimamia miradi yetu ya maendeleo kwenye ngazi zote. Kwenye eneo la kitaifa, mikoa, wilaya, Wizara na kadhalika. Tukiwa na national policy ya monitoring and evaluation ninaamini miradi yetu mingi kwa kutumia mfumo huo wa force account inaweza kuwa na tija na fedha tunazozitumia kwa ajili ya kutekeleza miradi hii ikawa na tija kwa taifa letu na wananchi waka-benefit kutokana na fedha hizi ambazo zinapelekwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi kwenye maendeleo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa nafasi. Ahsanteni sana. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE.JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati, nampongeza sana Mwenyekiti wa Kamati yetu ya NUU kwa uwasilishaji mzuri sana. Vilevile, nawapongeza Wajumbe wa Kamati yetu kwa kazi kubwa tuliyoifanya mpaka kuleta taarifa hii leo Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utakuwa kwenye maeneo kama mawili kama muda utaruhusu. Eneo la kwanza ni lile linalohusu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu ni moja kati ya mataifa yenye heshima kubwa sana duniani. Taswira yake ni nzuri kimataifa na inajulikana tokea harakati za uhuru mpaka kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya kimataifa. Mfano mzuri ni namna Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyoshiriki kwenye mambo muhimu na ya msingi sana ya kimataifa, jambo linaloongeza taswira nzuri ya Taifa letu nje na kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na changamoto moja, majengo yetu na balozi zetu huko nje hazina taswira nzuri yenye kuakisi heshima tuliyonayo kimataifa. Naipongeza Serikali kwa mpango wake wa miaka 15 wa kutekeleza miradi 16, kuboresha mazingira na balozi zetu huko nje, lakini mpango huu umekuwa unakumbwa na tatizo kubwa la kibajeti. Mpaka leo tunavyozungumza, katika mpango huu wa miaka 15, miaka mitano sasa umekuwa unasuasua na utekelezaji wake umekuwa ni wa shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya changamoto zinazosababisha mpango huu kutokutekelezeka kwa muda uliopangwa kama nilivyosema, ni bajeti. Pamoja na tatizo la kibajeti na Wizara kuanza sasa kufikiri kuingia kwenye makubaliano na sekta za umma na sekta binafsi ili kuweza kushirikiana na kufanya maboresho kwenye majengo yetu na balozi zetu kule nje. Vilevile, shida kubwa imekuwa ni muda unaochukuliwa kwa ajili ya kufanya majadiliano na taasisi hizi ili ziweze kufanya kazi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majadiliano haya yasichukue muda mrefu, kwa sababu tokea mwaka 2017, leo ni mwaka 2024 bado miradi hii haijaanza kutekelezwa. Tutaweza kujikuta tunafikia miaka 15 hatujafanya jambo lolote na bado taswira yetu kule kimataifa inakuwa ni hasi. Heshima yetu inapungua kwa sababu majengo yetu yanatia aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana 2023 Kamati yetu ilipata fursa ya kutembelea ubalozi wa Ethiopia, Addis Ababa pale. Tuna viwanja viwili ambavyo vimezungukwa na majengo ya balozi nyingine ambazo zimejengwa vizuri, lakini eneo letu limebaki pori, limezungushiwa tu, wahuni wanakaa pale, jambo linalotia aibu na kuharibu taswira yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri sana, Kamati yetu ilipata fursa ya kufa…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Joseph kuna taarifa kutoka kwa Mheshiwa Sophia Hebron Mwakagenda.

TAARIFA

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa mchangiaji kwamba pia katika Ubalozi wa Msumbiji tulikuwa na viwanja viwili Samora Machel alitupatia. Kiwanja kimoja angalau kimejengwa, lakini hicho kingine mpaka leo kipo, imefikia hatua kimeweka uharibifu utafikiri ni kiwanja ambacho hakijatoka katika Taifa la Tanzania. Kwa hiyo, ni viwanja vingi sana ambavyo kama Taifa hatujaviendeleza. Namuunga mkono kwa hilo analosema.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mkundi, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea. Bahati nzuri sana Kamati ilipata fursa ya kukaa na Mheshimiwa Rais wa Ethiopia na katika mambo ambayo Kamati ilijadiliana naye, ni namna ambavyo anaweza kutusaidia katika uendelezaji wa viwanja vile. Rais wa Ethiopia alisihi sana kwamba viwanja vile viendelezwe na vilitakiwa kuchukuliwa, lakini kwa heshima ya Taifa lile na mahusiano yake na Tanzania, akaomba visichukuliwe lakini akatupa nafasi tuviendeleze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ethiopia walitupatia Watanzania miezi tisa kuanzia mwezi Februari ili tuweze kuendeleza viwanja vile. Nasikitika kusema kwamba mpaka leo viwanja vile havijaweza kuendelezwa jambo ambalo linahatarisha kuchukuliwa kwa viwanja vile na kuendelea kututia aibu. Kwa hiyo, naomba Wizara na hasa Serikali ione umuhimu wa kufanya marekebisho kwenye viwanja vyetu na maeneo yetu ya balozi ili taswira yetu kama Taifa iendelee kuwa chanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni eneo la Wizara ya Mambo ya Ndani. Miaka kadhaa huko nyuma jamii ilikuwa na taswira hasi juu ya Magereza yetu. Watu wengi waliamini ukienda gerezani unaenda kuteswa, taswira ambayo ni hasi. Hali halisi ya Magereza yetu leo siyo kwenda kuteseka, bali kufanya urekebu wa tabia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi yetu tumepata fursa ya kutembelea Magereza yetu. Magereza leo yana hali nzuri, usafi ni wa kiwango cha juu tofauti na huko nyuma ambako ulikuwa ukienda Magereza, maeneo mengi yanatoa harufu na taswira nyingine ambayo siyo nzuri kwa hali ya kiafya ya binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Magereza yetu yako vizuri. Kama walivyosema wachangiaji wa awali, uwezo wa Magereza yetu ni kuchukua mahabusu na wafungwa 29,000 lakini ninafarijika kukutaarifu kuwa leo Magereza yetu yana wafungwa takribani 27,000. Tafsiri yake ni kwamba Magereza yetu yana upungufu wa wateja karibu 2,000 jambo ambalo ni maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hatua mbalimbali alizozichukua ili kuhakikisha kwamba hali hii inaweza kufikiwa. Changamoto tuliyonayo ni kwamba haya mafunzo ya urekebu kuna changamoto ya ukosefu wa fedha ili kusaidia Magereza haya kupata vifaa vinavyowawezesha…

MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa kuna taarifa kutoka kwa Ali Juma Mohamed.

TAARIFA

MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba nimpe taarifa ndugu yangu, licha ya kuwa idadi ya wafungwa pamoja na maabusu imepungua, lakini sasa hivi katika Magereza yetu wafungwa pamoja na mahabusu wamekuwa wanalalia magodoro mazuri kabisa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Joseph, taarifa hiyo unaipokea? Malizia mchango wako.

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ni ukosefu wa fedha ili vifaa vya kisasa viweze kupatikana kuwasaidia wafungwa hawa wanapotoka wawe na mwanzo mzuri wa kutumia ufundi na ujuzi wanaopata kutoka Magerezani kuanza maisha mapya uraiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mafunzo ya urekebu kwa mtaala ulipo na namna yanavyotolewa, yanatakiwa kufanyiwa tathmini sasa ili yaweze kuakisi hali halisi ya kisasa tofauti na mfumo uliopo sasa ambao unatolewa katika mazingira ya kizamani. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali ifanye tathmni ya mfumo wa mafunzo ya urekebu yanayofanyika sasa iweze kuendana na mazingira ya kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Kwa mara nyingine namshukru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na kunipa fursa ya kutoa mchango wangu kwenye Taarifa ya Kamati ya Miundombinu. Kwanza namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa anaoufanya kwenye sekta hizi za mawasiliano kwa sababu Taifa bila mawasiliano uchumi hautakuwa imara na mambo mengi na maendeleo ya wananchi yatakuwa duni, kwa hiyo, nampongeza sana kwa uwekezaji mkubwa anaoufanya kwenye sekta hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Kamati pia kwa taarifa nzuri na nami mapema kabisa nisema nakubaliana na taarifa yao na naunga mkono taarifa yao. Nitakuwa na mchango kwenye maeneo kama mawili muda ukiruhusu maeneo matatu. Kwanza, ni eneo la sekta ya mawasiliano. Miezi kadhaa iliyopita tulishuhudia uzinduzi wa mradi mradi wa mawasiliano kupitia sekta hii ya mawasiliano na hasa taasisi hii ya UCSAF.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa imefanyika naipongeza Serikali na naipongeza Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya. Utakuwa ni shahidi mara kwa mara tunapokuwa Bungeni hapa kunakuwa bado na maswali mengi juu ya mawasiliano hasa kwenye eneo la minara, kwa mujibu wa Kamati yetu ya Miundombinu kasi ya utekelezaji wa miradi ya mawasiliano hasa kwenye ujenzi wa minara bado hairidhishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kupitia Wizara tuangalie kama kuna changamoto yoyote, kama kuna shida ya uhaba wa fedha kwenye utekelezaji wa miradi yetu kupitia UCSAF, tuone nini tunaweza kufanya ili kuharakisha utekelezaji wa miradi hii ya mawasiliano ili wananchi wetu waweze kupata mawasiliano kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitolea mfano kwenye eneo langu la Ukerewe bado changamoto ni kubwa sana kwenye maeneo kama ya Bukiko na maeneo mengine kiasi kwamba bado wananchi wanahitaji kwenda kwenye maeneo yenye miinuko ili waweze kupata mawasiliano. Kwa hiyo, naiomba Wizara inayohusika na sekta hii ifanye kazi kubwa ili miradi hii ambayo inatakiwa kutekelezwa itekelezwe kwa haraka na wananchi waweze kupata mawasiliano katika mazingira yaliyo mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo natamani kuchangia ni eneo la usafirishaji. Kupitia taarifa ya Kamati imeonesha kwamba bado kunahitajika pesa ili kuweza kusaidia kampuni ya usafirishaji wa meli MSCL iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi. Ni kweli kwamba Tanzania tuko kwenye eneo ambalo ni la kimkakati, tuna ukaribu na mahusiano na nchi za Jirani, nchi kama DRC, Uganda kuna Visiwa vya Ushelisheli, Visiwa vya Comoro na mataifa mengine ya jirani na yote ni maeneo ya kimkakati kibiashara. Maeneo haya ili yaweze kufikika ni muhimu sana tukaimarisha kampuni yetu ya MSCL ili iweze kuwa na meli za kusafirisha mizigo na abiria kwenda kwenye maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna fursa kwenye nchi hizi za jirani ni fursa za kiuchumi kwa wananchi wetu, ni lazima tuwekeze kwenye kampuni hii ya MSCL iweze kufanya ukarabati na iweze kutengeneza meli ili meli hizi ziweze kufikia maeneo haya ya masoko na kufanya wananchi wetu waweze kuwa imara kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kwa safari za nje tu hata kwa ndani bado tuna changamoto. Kwa mfano, kwenye Ziwa Viktoria tuna meli ambazo bado ziko kwenye matengenezo na wananchi wetu wanapata wakati mgumu sana kwenye huduma za kila siku kuweza kusafiri kutoka eneo moja kwenda eneo jingine. Nitumie nafasi hii kwa sababu sisi kwa mfano kwenye eneo langu ninalotoka, Eneo la Ukerewe tunategemea usafiri wa meli. Sasa kunapokuwa na upungufu wa uwekezaji kwenye utengenezaji wa meli inakuwa ni changamoto kubwa ya usafiri kwa watu wanaotoka visiwani kama Ukerewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ikiwezekana inisaidie kutoa ufafanuzi. Siku za karibuni kumekuwa na utaratibu wa usafiri kwa mfano kutoka Ukerewe kwenda Mwanza. Meli zipo, napongeza kuna uwekezaji wa watu binafsi lakini wanapeana zamu kiasi kwamba badala ya meli kusafiri zote kwa wakati mmoja inasafiri meli moja au meli mbili wanapeana zamu jambo linalopelekea kunakuwa na mrundikano mkubwa sana wa wasafiri kwenye vyombo hivi vya usafirishaji, jambo ambalo ni risk kwa wananchi hawa, inaweza kutokea ajali halafu likawa jambo jingine kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini Serikali inaruhusu jambo hili badala ya kuruhusu vyombo vyote vikafanya kazi, vikasafirisha wasafiri katika mazingira mazuri lakini inapokwa wanaruhusu wanapeana zamu inakuwa ni risk kwa wasafiri wanaosafiri kupitia vyombo hivi. Naiomba Serikali iwekeze itoe pesa iwasaidie MSCL. Bahati nzuri sana MSCL ina uongozi mzuri na imara ambao kama watapewa mtaji wanaweza kufanya mambo makubwa na kufanya shirika hili kuwa na nguvu kuweza kuvutia uwekezaji kwenye nchi zilizo jirani na kuimarisha uchumi wa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu na la mwisho ni eneo la TANROADS, wamesema wachangiaji wengi na Kamati imeeleza. Bajeti ya kuwezesha TANROADS kuweza kuimarisha barabara zetu ni karibu shilingi trilioni tano. Mwaka jana tumepitisha bajeti ya shilingi trilioni moja nukta kadhaa lakini siyo jambo la siri barabara zetu hivi sasa, hasa kutokana na mvua nyingi zilizonyesha barabara zetu zina matatizo mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna haja ya TANROADS kujengewa uwezo ili waweze kuimarisha barabara zetu hasa zinazotuunganisha kutoka kwenye maeneo ya Mikoa na maeneo mengine yaliyo imara kiuchumi ili kusaidia kuimarisha uchumi wa watu wetu. Pamoja na kuongeza pesa hizi vilevile wale Wakandarasi wanaopewa miradi hii nashukuru Mheshimiwa Kalogeris amesema hapa kwamba ni dhamira ya Mheshimiwa Rais kuimarisha wakandarasi wetu wa ndani lakini bado nimekuwa nina mashaka sana na baadhi ya wakandarasi wetu. Mara kwa mara nimekuwa nasafiri kwa barabara kwenda Mwanza, kuna barabara ya kutoka Shinyanga Eneo la Hungumalwa kama sikosei kuja mpaka Mwanza, eneo lile linatengenezwa karibu kila mwaka lakini kila linapotengenezwa muda mfupi kunakuwa na matatizo kwenye barabara ile, sasa sijui tatizo ni wakandarasi au mazingira ya eneo lile lakini hoja yangu hapa naiomba Wizara iweze kuwasimamia wakandarasi wetu ili wanapopewa miradi hii thamani ya pesa vilevile iweze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Rais lakini na Wizara, Mheshimiwa Bashungwa najua unafanya kazi kubwa sana, barabara yetu ya kutoka Nansio kuja Kisorya ilitengewa pesa mkandarasi amekwishapatikana lakini haijaanzwa kujengwa kwa sababu ya changamoto za Wizara ya Fedha kupitia TRA, naomba sana utusaidie kuamua eneo hili ili barabara hii muhimu sana ianze kutengenewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana kwa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu kwenye hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Kitila mate wangu. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia afya na kuweza kusimama mbele ya Bunge hili kutoa mchango wangu huu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, kwa kazi kubwa anayoifanya, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake wote (watendaji wote). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli pamoja na kwamba Wizara hii ni Wizara mpya, lakini inafanya kazi kubwa, maono yao ni makubwa. Mimi ni mmoja kati ya watu tulio na matumaini makubwa sana na Mheshimiwa Kitila na Wizara hii kufanya Taifa hili liweze kuwa Taifa imara kiuchumi, lakini liweze kutenda yale ambayo wananchi wanatarajia, kuwaimarisha kiuchumi lakini na kuboresha maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri nikitambua kwa ujumla wake kazi kubwa inayofanyika kwenye Taifa letu. Kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba mipango inayopangwa inatekelezeka, lakini wananchi wa Taifa hili wananufaika na rasilimali za Taifa hili tulizojaliwa na Mwenyezi Mungu. Pamoja na changamoto kadhaa tulizozipitia hapo nyuma ikiwemo habari ya UVIKO, vita huko duniani lakini bado tumepata wawekezaji wengi kwenye Taifa hili. Jambo ambalo limeongeza hata pato la Taifa na Taifa letu kimsingi linafanya vizuri hata kwenye mtiririko wa kupanda kiuchumi lakini na namna linavyoendelea. Ndiyo maana kwa mfululizo karibu kila mwaka GDP imekuwa inaongezeka kwa zaidi ya asilimia tano na kufanya Tanzania kuwa moja kati ya nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais pia na Wizara ya Mipango. Pamoja na haya kuna maeneo ambayo nilitamani nitoe mchango wangu. Mheshimiwa Waziri anaonesha jinsi Wizara yake inavyojiandaa kuandaa mpango wa mwaka mmoja, lakini vilevile kuelekea kuandaa Mpango wa 2050.

Mheshimiwa Spika, kupitia FDI uwekezaji mkubwa umefanyika na ajira nyingi zimezalishwa. Kama nilivyosema ni kweli kwamba kama Taifa uchumi unapanda na natambua kwamba kwenye kukua kwa uchumi wetu kuna sekta mbalimbali zilizochangia kukua kwa uchumi wetu ikiwa ni pamoja na kilimo. Ni kweli kupitia uwekezaji ajira nyingi zimezalishwa lakini nafikiri katika mipango inayokuja bado ni muhimu sana kufikiri na kuwekeza kwenye uendelezaji wa kilimo kwa sababu tumejaliwa ardhi nzuri na kubwa ya kutosha. Kilimo hiki ambacho kinaajiri zaidi ya 70% ya wananchi tulionao kiweze kuchangia vilevile kujenga kwanza uchumi wetu kama Taifa pia na kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja, ili kuwapa nguvu ya kufanya manunuzi ili uwekezaji unaofanyika kupitia FDI uweze kuwa na reflection kwenye maisha halisi ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo ndiyo maana naona pamoja na jitihada kubwa zinazofanyika bado hatujaweza kutumia vizuri rasilimali maji tuliyonayo ili tuweze kufanya kilimo chenye tija, kilimo cha umwagiliaji. Amesema mchangiaji mmoja hapa tuna maziwa mengi mojawapo ni Ziwa Victoria, tumetumia Ziwa Victoria kwa ajili ya maji ya kunywa, maji safi kwa ajili ya Taifa letu, lakini naona bado hatujalitumia vizuri Ziwa lile kufanya kilimo cha kisasa, kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, Mheshimiwa Rais kupitia Wizara ya Kilimo, amewekeza kiasi kikubwa kwa miaka michache iliyopita kuhakikisha kwamba tunafanya mapinduzi ya kilimo. Ni kweli kwamba, kuna maeneo tumewekeza kwa ajili ya kujenga mabwawa ili tufanye kilimo cha umwagiliaji, lakini naamini kama tutatumia vizuri maziwa tuliyonayo, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Maziwa mengine tunaweza kufanya mapinduzi makubwa sana ya kilimo na hatimaye kuzalisha ajira nyingi sana zitakazoleta mapinduzi ya kiuchumi kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo kama Ukerewe, limezungukwa na maji, tuna maeneo mengi ambayo tunaweza tukafanya kilimo cha umwagiliaji, nashauri tufanye uwekezaji mkubwa sana kwa kutumia maji ya Ziwa Victoria ili tuweze kufanya mapinduzi ya kilimo. Hata zile hekta karibu 2,000 zilizoko Ukerewe na kwa sababu imezungukwa na maji tuweze kuzitumia vizuri tufanye mapinduzi ya kilimo, tuondokane na shida ambazo tumekuwa nazo ambazo zinadhoofisha hasa uchumi wa wananchi wetu kupitia maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo nilitamani kuchangia ni kweli tunakaribisha wawekezaji, uwekezaji mkubwa unafanyika. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati hali ya umeme sasa inaridhisha, lakini bado pamoja na uwekezaji mkubwa tulionao, natambua katika energy mix karibu 30% na zaidi ya umeme kwenye energy mix inategemea hydro. Sasa kama inategemea hydro tuna kila sababu ya kulinda vyanzo vya umeme huu ili huko mbele pamoja na kukaribisha wawekezaji, baada ya wawekezaji kumewekeza, isitokee energy failure ikaathiri mfumo mzima wa uwekezaji na kuathiri uchumi wa Taifa letu kwa hapa tulipofikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati nachangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nilishauri katika vyanzo tulivyonavyo, kwa mfano sasa tunajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, tuna Kihansi, tuna Kidatu na kadhalika lakini vyanzo vya maji yanayotiririka kuelekea kwenye vyanzo hivi bado hatujaweza kujenga mfumo au sera ya kulinda vyanzo hivi ili kesho na kesho kutwa tusipate janga la kupungukiwa na maji na hatimaye kuathiri mfumo mzima wa umeme, kwa sababu katika megawati karibu 2,000 tunazozitegemea sasa ikitokea 31% hiyo inayotegemea hydro ikaathirika, mfumo mzima wa kiuchumi kama Taifa utaathirika, jambo ambalo litaathiri hasa uchumi wetu kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Mipango, katika mipango wanayoipanga moja katika hiyo aangalie ni namna gani wanakuwa na mipango endelevu ya kuhakikisha kwamba, hatuwezi kupata athari za kinishati, jambo ambalo litaathiri uwekezaji na mambo mengine yote na nguvu kubwa tunazoziwekeza, sasa kutafuta wawekezaji na kadhalika zikawa hazina maana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana hilo liwe jambo muhimu sana, kwenye issue ya kilimo katika mipango tunayoipanga tuhakikishe kwamba ni ajenda muhimu na ulinzi wa nishati tuliyonayo, tunayoitegemea na tunayoitengeneza kwa ajili ya kuwezesha viwanda vyetu, tuweke mifumo, tuweke mipango na tuweke sera kuhakikisha kwamba tunailinda ili kuhakikisha kwamba haiathiriki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo, nikushukuru kwa nafasi hii, niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, amefanya uchumi wetu umeendelea kuwa stable, ndiyo maana leo pamoja na kwamba kuna malalamiko ya wananchi juu ya mfumuko wa bei, lakini napata faraja kwamba mfumuko wa bei kwa Taifa letu upo kwenye asilimia zaidi ya nne ukilinganisha na maeneo yanayotuzunguka. Kwa mfano, Zimbabwe wana zaidi ya 90%, Sudan wana zaidi ya 80% na Ghana wana 50%, kwa hiyo hili ni jambo ambalo linatia faraja. Pia nikiona namna ambavyo pato letu la Taifa linavyoongezeka inatia faraja. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ili kuhakikisha kwamba, Taifa letu linaendelea ku-prosper kiuchumi ili hatimaye wananchi wa Taifa hili waweze kunufaika.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na mambo mengi makubwa aliyofanya kwa jimbo la Ukerewe katika sekta mbalimbali. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wote katika Wizara. Hata hivyo nina ushauri na maombi kadhaa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze na maombi ya kutekelezwa kwa ahadi ya ujenzi wa kilometa mbili za barabara ya lami eneo la Bwisya iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka 2020; pili, kukamilishwa kwa maboma yaliyoanzishwa na wananchi kwenye Sekta ya Elimu na Afya jimboni Ukerewe; tatu, fedha za dharura kwa ajili ya kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa na mvua ikiwemo barabara ya Bwisya - Nyamanga – Kome; na nne, kusaidia upatikanaji wa watumishi ili kukabiliana na upungufu uliopo kwenye Sekta za Afya na Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri; Wizara isimamie vyema rasilimali zote zinazoletwa wilayani kuhakikisha zinasimamiwa vizuri; Wizara ikemee vitendo vya watendaji wenye madaraka kuwanyanyasa watumishi wasiokubaliana nao kimaslahi katika miradi jambo linalowakatisha tamaa watumishi, na kwa mfano, kuna mambo kadhaa yanayoendelea katika Ofisi ya Mkurugenzi dhidi ya watumishi wilayani Ukerewe inawakatisha tamaa na kuathiri ufanisi katika utendaji wao na baadhi kufanya jitihada za kuhama na kuathiri maisha ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.8) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii, nimpongeze Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu na wawasilishaji wote waliowasilisha marekebisho ya sheria, nina mchango kwenye eneo moja, eneo la marekebisho Sheria ya Uvuvi, Sura 279, kwenye marekebisho haya kwenye Sura 279 sehemu ya 21 kwenye marekebisho yanaongelea juu ya iwapo Local Authority itashindwa ku-manage shughuli za uvuvi, Wizara ya Uvuvi itainyang‟anya mamlaka na kupewa mamlaka nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia marekebisho haya mbali na kwamba inapora mamlaka ya Halmashauri hizi za Wilaya kwa mujibu wa ugatuaji wa madaraka, lakini si kutendea haki wananchi wa Halmashauri zinazousika na maeneo haya. Kwa sababu haiwezekani, kosa na tatizo individual kushindwa kutimiza wajibu wake akashindwa kufanya shughuli za uvuvi kuzisimamia vizuri halafu Halmashauri nzima ikaazibiwa kwa kunyanganywa mamlaka ya kusimamia shughuli zote zinazousu uvuvi halafu baada ya kunyanganywa alafu baada ya kunyang‟anywa ndiyo waziri sasa aende kwa Waziri anayeshughulika na Local Government kumtaarifu uamuzi aliyeuchukua, this is not fair. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri badala kufanyika jambo hili kama itaonekana na Wizara ya Uvuvi ikajiridhisha kwamba authority imeshindwa ku-manage shughuli za uvuvi iwasiliane kwanza na Waziri anayeusika na Serikali za Mitaa halafu baada ya hapo sasa itoe mapendekezo nini kifanyike ili usimamizi uweze kwenda vizuri kama ambavyo Wizara ya Uvuvi ingekuwa inatarajia. Lakini inapofanya uamuzi wa kuchukua mamlaka ikawanyang‟anya mamlaka ya kusimamia uvuvi halafu ndiyo ikaenda kutoa taarifa kwenye Wizara inayoshughulika na Serikali za Mitaa hii si kuitendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiendelea kwenye sehemu ya 22 inaongelea juu ya adhabu, hivi ni wavuvi wapi tunaowaongelea hawa? Ni wavuvi hawa hawa Watanzania ninaowafahamu mimi ninayetoka kwenye eneo la uvuvi? Wavuvi ambao siku zote kwa sababu wamezaliwa, wamekua, wanafanya local fishing, leo kwa sababu moja mbili tatu tunaona kwamba kuna modern fishing hii waliokuwa wanafanya traditional fishing tunaona kwamba haipaswi, halafu tunawaukumu mvuvi huyu wa kawaida, mvuvi mdogo apigwe fine ya milioni moja, milioni kumi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwatendea haki wavuvi hawa, adhabu hii ni kubwa sana kwa wavuvi ninaowafahamu mimi na zaidi ya hapa kinachofanyika hapa kuna mambo mawili ama sehemu kubwa ya wavuvi zaidi ya asilimia 90 ninaweza nikafikiri labda wataishia magerezani au tunatengeneza mwanya mkubwa sana wa rushwa kama zile ambazo zilikuwa zinafanyika wakati wa operation wa uvuvi haramu. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mvuvi gani wa kawaida atakaye mudu kutoa milioni 10 mpaka milioni 50 kwa sababu tu amekutwa anafanya shughuli za uvuvi haramu tunajua wavuvi wetu, wanaenda kule ziwani wanavua furu, wana kamtego ka shilingi sijui 2,000 halafu umpige fine ya shilingi milioni 10 itawezekana wapi? Mazingira haya siyo ya Tanzania haya tuangalie upya sheria hii lakini adhabu hizi ni kubwa sana kwa mvuvi mkubwa ninayemfahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nichangie kwenye maeneo hayo tu tunahitaji kuangalia sheria hii na haya marekebisho ili tunachokibadili na tunachokitaka kiendane na mazingira halisi ya wavuvi wetu tulionao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana kwa fursa ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai, lakini nikushukuru kwa kunipa nafasi hii nitoe mchango wangu kwenye Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Waheshimiwa Naibu Mawaziri wao na watendaji wao wote kwa kuleta mpango huu mzuri. Mpango huu una mambo mengi mazuri na kwa sababu hiyo tuna kila sababu ya kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kama msimamizi na kiongozi katika utekelezaji wa mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ambao una dhamira ya kujenga uchumi jumuishi, kupunguza umaskini, kuzalisha ajira na kuongeza mauzo ya bidhaa za nje. Kwenye hili la mauzo ya bidhaa za nje ukiona taarifa ya mpango ilivyowasilishwa inaonesha mauzo ya nje tumeuza chini ya kile ambacho tumenunua na kwa maana hiyo tuna urari hasi. Kwa namna yoyote ile katika mpango unaokuja ni lazima tuendelee kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji ili kuendelea kujenga msingi wa uchumi jumuishi, kupunguza umaskini na kuzalisha ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili hakuna namna yoyote tutakwepa kuimarisha na kuendelea kuwekeza kwenye Sekta ya Kilimo. Kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati ya Bajeti inaonesha kwamba Taifa letu lina watu takribani milioni 28 wanaohusika moja kwa moja na kilimo ambao ni karibu zaidi ya 40% wananchi tulionao. Kwa hiyo, hakuna namna yoyote ile tutakwepa kuwekeza kwenye kilimo, kuendelea kuwekeza kwa nguvu kubwa. Kwa maana hiyo nitaongelea kwenye eneo hili la kilimo, lakini nitaongelea vilevile kwenye uhifadhi wa mazingira nikihusianisha na uwekezaji kwenye nishati ya umeme, lakini pamoja na miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tuna kilometa za mraba takribani 945,000. Katika eneo lote hili karibu kilometa za mraba 61,500 ni eneo la maji na katika eneo hili tuna hekta karibu milioni 29.4 ambazo tunaweza tukazitumia kwa kilimo. Tafsiri yake ni nini? Tukiendelea kuwekeza kwenye kilimo yote haya kama kipaumbele tunaweza tukayafikia, kupunguza umaskini, kutengeneza ajira na kutengeneza uchumi jumuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia malengo waliyonayo Wizara ya Kilimo, kwa mfano, mpango wa mwaka jana, walipanga mpaka kufikia mwaka 2025 angalau kilimo cha umwagiliaji tuwe tumefikia hekta milioni moja, lakini hivi tunavyoongea bado tuko kwenye hekta laki saba pekee jambo ambalo linaonesha kwamba tunahitaji kuendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya kilimo hasa kilimo cha umwagiliaji, lakini siyo kuwekeza tu kwenye kilimo cha umwagiliaji, tuwekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji chenye tija, ndiyo maana jana, Mheshimiwa Mwijage alichangia hapa, tunapaswa kuangalia maeneo yenye rasilimali tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa tunawekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji, lakini kuna maeneo ambayo yana rasilimali maji, ni namna gani tumetumia rasilimali hizi. Nimelisema hili takribani kila mwaka, lakini tuna kila sababu ya kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji tukitumia rasilimali tulizonazo. Tufanye kilimo cha umwagiliaji, lakini kilimo cha umwagiliaji chenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wananchi wetu wanafanya kilimo cha jembe la mkono, uwekezaji unaotakiwa ni kuwatoa kwenye kilimo cha jembe la mkono ili wafanye kilimo chenye tija. Wenzetu pale Misri wanategemea maji kutoka Ziwa Victoria kupitia Mto Nile, kule ni jangwa, lakini wanazalisha mazao wanalisha nchi karibu 17 kwa kilimo chenye tija, kilimo cha umwagiliaji na sisi twende kwa mfumo huo ili tuweze kukabiliana na changamoto tulizonazo za ajira na kujenga uchumi jumuishi kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo kama Ukerewe, tuna kilometa za mraba 6,400 ni 10% pekee ndiyo ardhi, lakini tuna hekta karibu 4,000 zinazoweza kufanyika kilimo cha umwagiliaji. Ninashukuru kwamba Wizara ya Kilimo kuna jitihada inafanya, lakini ni vizuri rasilimali kama hizi tukazitumia kwa tija ili kupunguza changamoto tulizonazo kama ilivyo Ukerewe na maeneo mengine ambayo yana rasilimali maji kama ilivyo kwenye hilo eneo. (Makofi)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa wapi?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa, Kunambi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunambi, umehama sehemu yako.

TAARIFA

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafurahishwa sana na mchango wa Mheshimiwa Mbunge anayechangia sasa. Kimsingi ukisoma historia ya maendeleo yaliyofanyika huko Ulaya, karne ya 16 wenzetu walianza na mapinduzi ya kilimo baadaye wakaenda kwenye teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mchango wake ni mchango mzuri sana na ametaja maeneo ambayo kimsingi ukiwekeza kwenye umwagiliaji huna sababu ya kuweka fedha nyingi. Maeneo hayo ni pamoja na Morogoro, Mkoa wa Morogoro…

MWENYEKITI: Malizia Taarifa yako, maana unachangia sasa, mpe Taarifa.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamueleza tu, ninasema maeneo kama Morogoro kuna mito ya kutosha, kimsingi ukiwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji, huna sababu ya kuweka fedha nyingi, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mkundi, unaipokea taarifa hiyo kutoka kwa Mheshimiwa Kunambi?

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ni muhimu sana kuwekeza, jana nilimsikiliza Mheshimiwa Profesa Manya akichangia juu ya umuhimu wa kuwekeza kwenye gesi na alitoa mawazo na ufafanuzi mpana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwekeza kwenye sekta ya kilimo, lakini tuhakikishe sekta ya nishati, uwekezaji wake unakuwa mkubwa na nishati inawafikia wananchi kwenye Taifa hili. Nipongeze Serikali, tumejenga vyuo vingi vya ufundi kupitia VETA, tuna shule za sekondari, masomo ya sayansi watoto wanasoma, lakini bila nishati ya umeme haya yote tunayoyafanya bado tutaendelea kwenda kwa kusuasua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali, katika vijiji zaidi ya 64,000 tuna vijiji karibu 36,000 ambavyo tayari vina nishati ya umeme, lakini tuna vitongoji vingi bado havina nishati hii ya umeme. Ninashauri ili twende vizuri zaidi, ni vizuri sana tukafanya tathmini kwa kuangalia kaya zenye nishati hii ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kwa pendekezo langu ninashauri, sioni tija sana kwamba maeneo yaliyoko mjini yalipe umeme shilingi 300,000 kupata nishati hii ya umeme, maeneo ya vijijini walipe shilingi 27,000, tungeweka kiwango sawa. Pendekezo langu ninashauri, ikiwezekana wananchi wapewe umeme bure halafu wanapokuwa wanalipa bill ndiyo wawe wanakatwa kiasi fulani ili kufidia gharama iliyotumika kupeleka umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili litaongeza tija kwenye uzalishaji, litaongeza tija kwenye ubunifu na watu wetu watatumia nishati ile kujiletea maendeleo na kujenga uchumi kwenye Taifa hili ikiwa ni pamoja na kuongeza walipa kodi kwenye Taifa hili na kupandisha uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kutoa mchango wangu kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara hii ya ujenzi.

Mheshimiwa Spika, kwanza, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii na nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana anayoifanya, pamoja na changamoto mbalimbali lakini kwa muda huu mfupi aliokaa madarakani kazi kubwa sana imefanyika kuimarisha miundombinu yetu. Nisiwe mchoyo wa fadhila kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu na timu nzima, kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana pamoja na changamoto kubwa wanazozipitia lakini wanafanya kazi kubwa sana, mnastahili pongezi.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitampongeza meneja wangu wa TANROADS Mkoa Mhandisi Ambrose, ni moja kati ya watendaji wahandisi wanaoifanya kazi kubwa sana. Amekuwa anatupa ushirikiano, mimi binafsi amekuwa ananipa ushirikiano mkubwa sana, kwa kweli anastahili pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa muda huu mfupi nita-concentrate kwenye Jimbo langu la Ukerewe. Moja ni kutoa shukrani. Tunayo barabara yetu ambayo ni sehemu ya barabara ya Bunda - Kisorya – Nansio, kwa muda mrefu sana ilikuwa ni tatizo kubwa lakini kwa namna ya pekee ndiyo maana nina kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais, fupa ambalo limewashinda viongopzi wengi yeye safari hii ameliweza na hatimaye sasa barabara ile kilomita 12 inaanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Nampongeza sana lakini nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake yote.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili naomba tu kushauri Mheshimiwa Waziri, wakati mkandarasi kafika site, basi alipwe pesa yake ya awali ili asikwame katika eneo lolote lile. Nashauri vilevile ubora wa kazi ile uwe ni wa kiwango cha juu, ina maana kuwe na usimamizi mkubwa, ingawa sina mashaka sana na Meneja wangu wa TANROADS Mkoa kama nilivyosema, kwa hiyo nasisitiza.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa hatua iliyofikiwa sasa ya kuanza kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Kisorya – Rugezi, ni hatua nzuri sana. Daraja lile ni muhimu sana kwa wananchi wa Ukerewe na hata Bunda kwa sababu ni kiunganishi kikubwa na ndiyo misingi wa uchumi wa maisha ya watu wa Ukerewe. Kuwepo kwa daraja lile kutaimarisha sana mawasiliano na uchumi wa wananchi wa Ukerewe. Kwa hiyo, nashukuru na napongeza na ingependeza sana kama vifaa vilivyoko Kigongo Busisi baada ya mradi ule kukamilika vikahamia pale ili kupiga ile kazi, ikafanyika mara moja na maisha yakaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo ningependa kuchangia ni juu ya vivuko. Ukerewe ndiyo wateja wakubwa wa Wizara hii kwenye eno la TEMESA kwa upande wa vivuko. Nashukuru Kivuko cha Bukondo – Bwiru kinaendelea vizuri lakini pia Kivuko cha Kisorya - Rugezi. Naomba tu yale madai anayodai mkandarasi wetu Songoro Marine alipwe ili akamilishe kazi ile vivuko vile viende kutoa huduma kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukisoma Ilani yetu ya uchaguzi Ibara ya 57 (j) ambayo inaongelea vivuko; kwenye Ilani ya 2020/2025 tuliahidi wananchi kuanza kutengeneza vivuko nane. Katika vile vivuko nane tulivyoahidi, mojawapo ni kivuko cha Irugwa kwenda Murutanga na Kakukuru kwenda Ghana. Bado vivuko hivi havijaanza kutengenezwa.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kisiwa cha Irugwa wanaishi maisha magumu sana. Wanapotaka kusafiri kuja Ukerewe inabidi wapite Jimbo la Musoma Vijijini, wapite Jimbo la Musoma, wapite Bunda, wapite Mwibara ndiyo warudi kuja kupata huduma Ukerewe. Kwa hiyo, ni muhimu sana kivuko hiki kikatengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, wananchi wa visiwa vya Ghana, Kamasi na vinginevyo, visiwa vyote karibu saba, kutoka Kakukuru wanapata wakati mgumu sana kusafiri kwenye eneo lile. Ndiyo maana vivuko hivi ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huu na kama ilivyoelekeza Ilani, Mheshimiwa Waziri, mimi ningeomba kushauri. Kwa sababu kivuko cha Mv Ukara namba moja tayari kimeenda matengenezo na kwa mujibu wa hotuba yako, kimefikia asilimia 10. Vilevile, Kivuko cha Mv Nyerere nacho kiko matengenezo kinakaribia kukamilika. Mheshimiwa Waziri, ushauri wangu, vivuko hivi vikikamilika virudishwe Ukerewe ili kimoja kiweze kufanya kazi kati ya Irugwa kuja Murutanga na kingine kifanye kazi kati ya Kakukuru kwenda Ghana. Tutaokoa sana maisha ya watu wetu na vilevile kuimarisha uchumi wa wananchi wa Ukerewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bila kufanya hivyo mazingira yetu yatakuwa magumu sana. Ninaamini, Mheshimiwa Waziri sina mashaka na wewe kwa sababu kama nilivyosema, vivuko hivi vilikuwa vinafanya kazi Ukerewe, vimeenda matengenezo. Nishauri sana na niombe vikikamilika kutengenezwa virudi Ukerewe. Kimoja kifanye kazi kati ya Murutanga kwenda Irugwa na kingine kutoka Kakukuru kwenda Ghana kama nilivyoshauri. Litakuwa limefanyika jambo kubwa na la maana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu, Mheshimiwa Waziri, tulizungumza juu ya barabara ya kutoka Bulamba kwenda Murutunguru – Bukonyo – Masonga kilometa 28. Ni barabara muhimu sana, ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa wananchi wa Ukerewe. Pamoja na kwamba wanapitia changamoto kubwa sana za kifedha lakini niombe tafadhali, hata kama ni kwa awamu, kwa sababu tunatumia pesa nyingi sana kutengeneza barabara ile kila wakati na ikitengenezwa muda mfupi baadaye inaharibika tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu, kama itawezekana tutafute rasilimali fedha ili tuwe tunaitengeneza hata kwa awamu ili mwisho wa siku barabara ile iweze kutengenezwa kwa kiwango cha lami na kuepusha gharama kubwa ambazo tunazitumia kwa ajili ya matengenezo ya mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja na Mwenyezi Mungu awabariki sana, ahsanteni sana. (Makofi)