Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jesca David Kishoa (19 total)

MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-
Moja ya njia ya kuimarisha uchumi ni kupunguza uagizaji wa bidhaa nje ya nchi, Taifa linatumia fedha nyingi za kigeni kuingiza mafuta ya kula wakati kuna vyanzo vingi vya mafuta kama vile alizeti - Singida na Michikichi – Kigoma.
Je, ni lini Serikali itaweka msukumo kwa mazao haya katika mikoa hii kwa faida ya nchi na wakazi wa mikoa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvivi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa linatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza mafuta ya kula wakati kuna vyanzo vingi vya mafuta kama alizeti na michikichi kwa sababu mbalimbali. Ili kukabiliana na changamoto hii Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeandaa mikakati inayolenga kuongeza tija na uzalishaji wa mbegu za mazao ya mafuta hususani alizeti ambazo uzalishaji wake umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.
Aidha, katika Mkoa wa Singida vikundi mbalimbali vimeundwa na taasisi mbalimbali za Serikali na zile zisizo za kiserikali. Mojawapo ya malengo ya vikundi hivyo ni kuongezea thamani kwa maana ya value addition ya zao la alizeti na upatikanaji wa pembejeo ili kukuza tija na uhakika wa masoko kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kigoma ni mkoa pekee nchini unaolima zao la mchikichi kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na maeneo mengine nchini. Hadi sasa mkoa una zaidi ya hekta 18,924 za michikichi zenye tija ya tani 1.6 kwa hekta. Uzalishaji huu bado ni mdogo sana ikilinganishwa na tani 4.0 kwa hekta zinazoweza kuzalishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza tija, mkoa kupitia Halmashauri zake unaendelea kuhamasisha wananchi kufufua mashamba ya zamani ya mchikichi kwa kuyapalilia, kuondoa majina yaliyozeeka na kuanzisha mashamba mapya yatakayokuwa yanapandwa mbegu bora. Vilevile Mkoa kwa kushirikiana na wadau wengine umeshaanza kuzalisha miche bora ya michikichi ambayo itasambazwa kwa wakulima kwa gharama nafuu ili kila mkulima apande miche 137 inayotosha hekari moja.
Pia wajasiriamali wanawezeshwa kupata mashine bora za kusindika michikichi; Serikali Kuu na Serikali ya Mkoa tunakaribisha wawekezaji zaidi kuwekeza katika uzalishaji mkubwa na viwanda vya kati na vikubwa vya kukamua mafuta na bidhaa nyingine zitokanazo na michikichi.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwa na habari za uamuzi wa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kujenga kituo cha kuzalisha umeme wa upepo Mkoa wa Singida:-
Je, ni lini mradi huo utatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na TANESCO imekuwa ikifanya tafiti kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa kutumia upepo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo na maeneo ya Mkoa wa Singida. Kufuatia tafiti hizo, maeneo ya Kititimo pamoja na Kisaki Mkoani Singida yameonekana kuwa na chanzo kizuri cha kuzalisha umeme kwa njia ya upepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni binafsi ikiwemo Kampuni ya Wind East Africa pamoja na Makampuni mengine kama Six Telecoms na mengine yameonesha uwezo huo kutoka UK. Uwezo wa nguvu inaopata ni pamoja na kuzalisha umeme wa Megawatt 100 katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majadiliano kati ya Serikali kupitia TANESCO na Kampuni ya Wind East Africa sasa yanaendelea vizuri na yatakamilika mwezi Desemba mwaka huu, lakini ujenzi wa mradi sasa utaanza mwezi Aprili mwaka ujao, 2016 na utakamilika mwaka 2019. Ujenzi wa mradi huu utagharimu Dola za Marekani milioni 264.77
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni nyingine inayoonesha kuwekeza katika mradi huo ni pamoja na Kampuni ya Geowind ambayo pia itazalisha Megawatt 50 na mradi utagharimu Dola za Kimarekani milioni 136 na utakamilika...
… katika mwaka ujao wa fedha.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-
Lengo la Serikali ni kusaidia sekta binafsi hasa wajasiriamali wadogo ili waweze kujiajiri, lakini tatizo kubwa la wajasiriamali hao katika sekta ya binafsi Tanzania ni tozo kubwa ya riba inayotolewa na benki hapa nchini kuwa kubwa kuliko nchi yoyote Afrika Mashariki.
(a) Licha ya Tanzania kuwa na benki nyingi zaidi kuliko nchi zote Kusini na Mashariki mwa Afrika, je, kwa nini wingi huo bado haujaleta unafuu katika tozo ya riba?
(b) Je, kwa nini Serikali isiweke ukomo wa riba kisheria kwa benki hizi ili kumsaidia mjasiriamali wa sekta binafsi Tanzania kama ilivyofanya nchi ya Kenya?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya sekta ya fedha ya mwaka 1991 yalisababisha Serikali kujitoa katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kibenki nchini ili kuruhusu mfumo wa soko huria, hususan nguvu ya soko kuamua viwango vya riba za mikopo, riba za amana na gharama zingine za huduma za kibenki. Viwango vvya riba za mikopo hupangwa kwa kuzingatia gharama za upatikanaji wa fedha, gharama za uendeshaji, gharama ya bima, sifa za mkopaji na hatari ya mkopaji kutolipa mkopo pamoja na kasi ya mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya uhitaji na utoaji wa mikopo (demand and supply theory) si kigezo pekee kinachoweza kupunguza viwango vya riba hapa nchini. Hatari ya kutolipa mkopo ni kigezo kikubwa kinachotumiwa na benki kupanga viwango vya riba za mikopo hususan kwa wajasiriamali wadogo. Uzoefu uliopo sasa unaonesha kuwa benki zinapendelea kukopesha wajasiriamali waliojiunga katika vikundi kuliko mjasiriamali mmoja mmoja ili kupunguza kiwango cha mikopo isiyolipika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kanzidata ya mikopo (credit reference bureau) ina umuhimu mkubwa katika kuwatambua wakopaji kwa kuwa huhifadhi historia na sifa za wakopaji. Kwa sehemu kubwa, historia na sifa za wafanyabiashara wakubwa zinapatikana kutoka kwenye kanzidata ya mikopo. Hivyo basi wafanyabishara wakubwa wanaaminika na kupata mikopo kwa riba nafuu ikilinganishwa na wajasiliamali wadogo kwa sababu taarifa na sifa zao zinapatikana kirahisi.
Kwa kuwa wajasiriamali walio wengi taarifa zao hazipo kwenye kanzidata ya mikopo, ni vigumu benki kuwatambua, kuwaamini na kuwapa mikopo kwa riba nafuu. Pia kiwango cha mikopo mibovu kwa wajasiliamali wadogo ni kikubwa ikilinganishwa na makundi mengine.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Fedha ya mwaka 1991 iliyotungwa kwa kuzingatia misingi ya mfumo wa soko huria, Benki Kuu imepewa jukumu na mamlaka ya kusimamia na kuzichukulia hatua taasisi za fedha zinazoendesha shughuli zao kwa hasara. Kutoa maelekezo kwa benki kutumia viwango fulani vya riba, kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya kuzichukulia benki hatua endapo zitapata hasara kwa kutumia riba ambayo Benki Kuu imeelekeza. Hivyo basi, Serikali haina mamlaka ya kuweka ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na benki katika kutoa mikopo kwa wajasiliamali.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-
Mkoa wa Singida kwa sasa ni mkoa wa kimkakati, hasa kufuatia kazi ya kuleta Makao Makuu Dodoma.
Je, ni lini Serikali itahakikisha mkoa huo unapata uwanja wa ndege hasa kutokana na umuhimu wake?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha uwanja wa ndege wa Singida. Kutokana na umuhimu huo, Serikali ya Awamu ya Tano tayari imechukua hatua za kuwezesha kuimarisha uwanja wa ndege wa Singida ambapo hadi kufikia mwezi Mei, 2017 imekamilisha upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kufanya ukarabati na upanuzi wa uwanja huo kwa kiwango cha lami. Uwanja wa ndege wa Singida ni miongoni mwa viwanja 11 vya ndege vilivyopata ufadhili wa Benki ya Dunia katika hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi wa uboreshaji wa viwanja hivyo. Viwanja vingine ni Lake Manyara, Musoma, Iringa, Tanga, Songea, Kilwa Masoko, Lindi, Moshi, Njombe na Simiyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina niliourejea hapo juu, Serikali imeanza kutafuta fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa viwanja hivyo ukiwemo uwanja wa ndege wa Singida. Mradi huo ukikamilika utawezesha kuruka na kutua ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba takribani abiria 70. Aidha, kazi ya ukarabati na upanuzi zitahusisha ujenzi wa jengo la abiria, jengo la mawasiliano na kuongozea ndege, kituo cha hali ya hewa pamoja na miundombinu mingine. Utekelezaji wa mradi huu utaanza mara tu fedha za mradi huu zitakapopatikana.
MHE. MARTHA M. MLATA – (K.n.y. MHE. JESCA D. KISHOA) aliuliza:-
Je, Serikali imejipangaje kuwatengea eneo la kuchimba madini katika Mgodi wa Shanta ulioko Mang’onyi (Singida), wachimbaji wadogo wadogo wa Wilaya ya Ikungi na Mkoa wa Singida wanaotegemea kupata kipato kwa shughuli hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nitoe pole kwa Mheshimiwa Jesca David Kishoa kwa ajali mbaya aliyoipata juzi na kupata maumivu, basi tumwombee kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kupata unafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, naomba sasa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, nijibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya tarehe 10, Novemba, 2004 na tarehe 1, Aprili, 2005, wachimbaji wadogo wa madini wa Wilaya ya Ikungi waliwasilisha maombi 34 ya leseni ya uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu katika eneo la Mang’onyi. Hata hivyo, maombi hayo yalikataliwa kutokana na kuombwa juu ya leseni ya utafutaji mkubwa wa madini yenye namba PL 2792/2004 ya Kampuni ya Shanta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 14(1) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017, kinaeleza kuwa mwombaji ambaye maombi yake yalipokelewa kwanza ndiye anayestahili kupewa leseni na hairuhusiwi leseni kutolewa juu ya leseni nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa mujibu wa kifungu cha 7(2) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake ya mamlaka ya utoaji wa leseni, kwa ridhaa ya mmiliki wa leseni, inaweza kutoa leseni zaidi ya moja katika eneo moja la uchimbaji madini iwapo leseni inayoombwa ni ya madini tofauti na leseni iliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo mwezi Mei, 2014, Kampuni ya Shanta ilifanya mazungumzo na Kampuni ya Mang’onyi Company Limited ili iachie baadhi ya maeneo ya leseni inayomiliki na kukubali kutoa leseni tatu za uchimbaji wa madini ya dhahabu kwa wachimbaji wadogo wa Vijiji vya Sambaru, Mang’onyi na Mlumbi vilivyopo katika Kata ya Mang’onyi, Wilayani Ikungi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji hivyo vitatu vinazunguka leseni ya Mgodi wa Shanta. Pia kampuni ya Shanta imetoa kwa kikundi cha Aminika Gold Mining Co-operative Society Limited chenye wanachama 193 ambao ni moja ya wanufaika wa leseni hizo, kiasi cha dola za Marekani 25,000 kama fedha za mtaji wa kuendesha shughuli za uchimbani zilitolewa. Aidha, kampuni hiyo imepanga kutoa elimu ya usalama migodini ikifuatiwa na elimu ya uchimbaji ukiwemo uchorongaji wa miamba ili kuwezesha kikundi hicho kufanya shughuli za uchimbaji wenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya mazungumzo na kampuni ya uchimbaji wa madini Shanta na kampuni hiyo imekubali kuachia eneo lote la leseni yake ya utafutaji mkubwa wa madini ya dhahabu iliyoko Muhintili Wilaya Ikungi yenye ukubwa takribani kilometa za mraba 71.3 ili itengwe kwa ajili ya uchimbaji mdogo wa madini. Kiasi cha leseni 714 zinatarajiwa kutolea kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa leseni 92 zimekwishatolewa kwa vikundi vya watu binafsi hivyo Wizara inawahimiza wachimbaji wadogo wa madini kuwasilisha maombi yao ili waweze kupatiwa maeneo ya uchimbaji. Hata hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutenga maeneo zaidi kwa ajili ya wachimbaji wadogo kwa madini kadri yanavyoweza kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipekee niishukuru Taifa kubwa Simba Sports Club kwa ushindi walioupata, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga barabara inayounganisha Mkoa wa Singida na Bandari ya Tanga inayoanzia Kijiji cha Unyankhanya kupitia Makyungu Misughaa – Chemba hadi Tanga ili kuchochea maendeleo ya Mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Makyungu – Chemba hadi Tanga inayoanzia Kijiji cha Unyankhanya ni sehemu ya mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Handeni – Kiberashi – Kijungu – Chemba – Kwamtoro hadi Singida yenye urefu wa kilometa 460 ambapo kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina pamoja na uandaaji wa nyaraka za zabuni iliyofanywa na Mhandisi Mshauri aitwaye Inter-Consult Limited ya Dar es Salaam ikishirikiana na Mhandisi Mshauri aitwaye Consult Aurecon kutoka Afrika Kusini ilikamilika mwaka 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuhudumia mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga eneo la Chongoleani, Serikali itahakikisha barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. JESCA D. KISHOA) aliuliza:-

Kwa muda mrefu sasa Mkuu wa Wilaya ya Ikingu amekuwa akijichukulia sheria mkononi na kuwanyanyasa wananchi wa Kata za Ighombwe, Iglansoni na maeneo ya Wilaya ya Ikungi.

Je, Serikali inaweza kutoa majibu ni mamlaka yapi aliyonayo Mkuu huyo wa Wilaya ya kuwanyanyasa na kuamrisha mali za wananchi kuchomwa moto au kuporwa na Serikali bila utaratibu wowote wa kisheria kwa kisingizio kuwa wanaishi maeneo yasiyoidhinishwa kwa makazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Igombwe, Iglasoni na maeneo ya Wilaya ya Ikungi zinapakana na hifadhi ya Msitu wa Minyughe yenye ukubwa wa hekta 264,600. Kwa nyakati tofauti shughuli za kibinadamu kwenye vijiji vinavyozunguka msitu huu zilianza kuhatarisha mazingira ya hifadhi hasa baada ya wananchi kadhaa kuhamia eneo la hifadhi na kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kupitia vikao vya kisheria vya Baraza la Madiwani liliazimia kuulinda msitu huu na kuwaondoa wavamizi, hivyo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambayo ndiyo yenye mamlaka aliyopewa na Sheria ya Tawala za Mikoa ya Regional Administrative Act ya mwaka 2002, chini ya Kifungu cha 15 kutoa amri halali, iliwataka wananchi hao kuondoka katika maeneo ya Hifadhi ya Msitu wa Minyughe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la kuwaondoa wavamizi lilifanyika kwa awamu mbili, yaani Mei na Oktoba, 2017 ambapo watu 119 waliondolewa kwenye hifadhi hiyo pamoja na ng’ombe 2,243, mbuzi 455 na kondoo 169. Zoezi hili lilishirikisha Askari wa Jeshi la Polisi waliofanya kazi yao kwa weledi wa hali ya juu kwa sababu hakuna raia aliyejeruhiwa wala kupoteza mali zake. Ni dhahiri uwepo wa Askari Polisi ambao ni wasimamizi wa sheria uliwezesha operesheni hiyo kufanyika salama na hakuna kielelezo wala ushahidi kwamba haki zao za msingi zilivunjwa.
MHE. JESCA D. KISHOA Aliuliza: -

Je Serikali inatumia mikakati gani kudhibiti mapato yatokanayo na gawio kutoka kwenye makampuni ambayo Serikali inamiliki hisa chini ya 50%?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina ambaye ndiye msimamizi wa uwekezaji wa Serikali katika Taasisi na Mashirika ya Umma pamoja na Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache, inadhibiti mapato yatokanayo na gawio kwa kuhakikisha kuwa kila kampuni ina sera ya gawio, kurejea kwa mikataba ya mauzo ya hisa katika kuhakikisha maslahi ya Serikali yanalindwa pamoja na kufanya chambuzi za mara kwa mara kuhusu utendaji wa taasisi hizo. Aidha, Serikali inauwakilishi kwenye bodi za wakurugenzi wa kampuni ambapo pamoja na mambo mengine husimamia maslahi ya Serikali kwenye kampuni ikiwa ni pamoja na malipo ya gawio.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati hii imeiwezesha Serikali kuongeza makusanyo yake ya gawio kutoka kampuni ambazo ina hisa chache kutoka shilingi bilioni 34.92 mwaka 2015/2016 hadi kufikia shilingi bilioni 155.10 mwaka 2020/2021.
MHE. GRACE V. TENDEGA K.n.y. MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Mkalama?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mkalama ni Kituo cha Daraja A. Ujenzi wake ulianza mwezi Juni, 2015 na ulisimama kutokana na kukosekana kwa fedha. Katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi 467,148,000 ili kukamilisha ujenzi wa kituo hiko. Nashukuru.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa mradi wa umeme wa upepo Singida utaanza?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO imekuwa ikifanya jitihada za kuendeleza miradi mbalimbali ya kufua umeme nchini, ikiwemo miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati jadidifu ya upepo katika maeneo ya Mkoa wa Singida inayotekelezwa na wawekezaji binafsi wenye nia ya kuzalisha umeme na kuiuzia TANESCO.

Mheshimiwa Spika, miradi hiyo ni pamoja na mradi wa upepo MW 50 unaotekelezwa na Kampuni ya Upepo Energy eneo la Msikii Halmashauri ya Singida Vijijini, ambapo majadiliano ya mkataba wa kuuziana umeme (Power Purchase Agreement) kati yake na TANESCO yanaendelea. MW 300 unaotekelezwa na Kampuni ya GEO Wind eneo la Kititimo Halmashauri ya Singida Mjini ambapo majadiliano baina ya Mwekezaji na Mfadhili Green Climate Fund (GCF) yanaendelea. Pia MW 100 unaotekelezwa kwa ubia wa TANESCO na kampuni ya Abu-Dhabi (Masdar) eneo la Ikungi, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambapo Upembuzi Yakinifu unaendelea.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa miradi hii inatarajiwa kukamilika kati ya mwaka 2023 na 2027.
MHE. NUSRAT S. HANJE K.n.y. MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuiwezesha GST kufanya utafiti wa madini yanayohitajika kwenye soko la dunia kutengeneza nishati safi?
WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa ni asilimia 16 tu ya nchi yetu ndiyo imefanyiwa utafiti wa kina kubaini aina na kiasi cha madini mbalimbali yanayopatikana kwa kutumia teknolojia ya urushwaji wa ndege (High Resolution Airborne Geophysical Survey). Teknolojia hiyo hutoa picha ya chini ya ardhi inayoonesha mikondo na miamba inayobeba madini ya aina mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wizara ya Madini imekwisha andaa mpango mkakati wa utafiti utakaowezesha kutafiti asilimia 50 ya nchi yetu ili kupata na taarifa za kina ikiwemo za madini ya nishati safi. Mpango huo umekwisha kuainishwa na maeneo ya kipaumbele kulingana na aina ya madini yanayohitajika zaidi nchini kwa sasa. Ili kufanikisha azma hiyo, Wizara inajadiliana na sekta binafsi zinazoonesha nia ya kushirikiana na GST ili kuwezesha utafiti wa kina wa madini mkakati wa teknolojia ya utafutaji, uvunaji na uongezaji thamani madini ya mkakati kwa kuwa ni gharama kubwa sana.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA kwenye Vijiji 23 Wilayani Mkalama?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili, katika Wilaya ya Mkalama unatekelezwa na Mkandarasi CRJE – CTCE Consortium. Mradi unalenga kupeleka umeme katika vijiji vyote 25 vya Wilaya ya Mkalama ambavyo havina umeme na Mkandarasi yupo katika eneo la site akiendelea kuwasha umeme.

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, mradi huu wa kusambaza umeme katika Wilaya ya Mkalama unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Disemba, 2023, nakushukuru.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaweka wazi mikataba ya sekta ya uziduaji kama The Extractive Industries Transparency Initiative inavyotutaka?

NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni mwanachama wa Asasi ya Kimataifa ya EITI (Extractive Industries Transparency Initiative). Ambalo jukumu lake kuu ni kuhamasisha Serikali kuweka mifumo ya uwazi katika rasilimali madini, mafuta na gesi asilia ili kuboresha mapato na manufaa yanayotokana na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza takwa la uwekaji wazi wa mikataba Taasisi ya TEITI imeandaa Mpango kazi (Roadmap) kwa ajili ya utekelezaji wa kazi ya uwekaji wazi mikataba. Mpango huo umewekwa wazi kwa ajili ya utekelezaji kulingana na matwaka ya Kimataifa ya Taasisi ya EITI. Kwa hivyo, katika mwaka wa fedha 2023/2024 TEITI imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa mikataba inawekwa wazi, ikiwa ni pamoja na kushauriana na mamlaka nyingine za Serikali namna bora ya kutekeleza mikataba na takwa hili. Ahsante.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kuingia mikataba mipya isiyo na dosari kwani Mwaka 2024 ndio mwisho wa mkataba wa Songas?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Songas utaisha muda wake mwezi Julai, 2024. Ili kuhakikisha kwamba Serikali inakuwa na mkataba usiokuwa na dosari, Serikali haitaongeza muda wa mkataba utakaoishia mwezi Julai, 2024. Badada yake, Serikali itajadili mkataba mpya na iwapo pande zote zitakubaliana, mkataba mpya wenye tija kwa Taifa na usiokuwa na dosari utasainiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali kupitia TANESCO imeunda timu ya kupitia masuala ya msingi ya kuzingatiwa kwenye mkataba mpya kwa ajili ya maslahi kwa Taifa.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-

Je, makubaliano ya mkataba ujao kati ya SONGAS na Serikali yamefikia hatua gani ikiwa mkataba wa awali upo katika mwaka wa mwisho?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mwaka 2001, TPDC iliingia mkataba wa kuuziana gesi asilia iliyotengwa na Songas. Kiasi cha futi za ujazo bilioni 320 za gesi asilia iliyotengwa zilitengwa kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa miaka ishirini (20) kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2024. Mwaka 2004, TANESCO iliingia mkataba wa kuuziana umeme ambapo kwa sasa kiwango kinachozalishwa ni Megawatt 189.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa TPDC na TANESCO wameanza majadiliano na Songas kuhusu mikataba hiyo. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kunakuwa makubaliano ambayo yanazingatia maslahi ya pande zote mbili. Ahsante.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme wa REA kwenye vijiji 20 vilivyobaki – Mkalama?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mkalama lina vijiji 70 na vyote vimepatiwa umeme, vikiwemo vijiji 25 vilivyokuwa katika Mradi wa Kusambaza Umeme, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili, uliotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Aidha, Jimbo hilo lina vitongoji 388 ambapo vitongoji 192 vimepatiwa umeme na vitongoji 196 bado havijapatiwa umeme. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia REA imetenga fedha za kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 15 vya kila jimbo ikiwemo Jimbo la Mkalama. Kwa sasa, REA inakamilisha taratibu za kuwapata Wakandarasi watakaotekeleza mradi huu. Vitongoji vitakavyobakia vitapatiwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza madaktari bingwa na wauguzi katika vituo vya afya Mkalama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuajiri wataalamu wa kada mbalimbali za afya wakiwemo madaktari na wauguzi na kuwapanga kwenye vituo vya kutolea huduma kote nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka mitatu 2021 hadi 2023, Serikali imeajiri wataalamu 18,418 wa kada mbalimbali za afya na kuwapangia vituo kote nchini. Aidha, katika kipindi cha miaka mitatu, mwaka 2021 hadi mwaka 2023 Serikali imeajiri jumla ya wataalamu 102 wa kada mbalimbali na kati yao madaktari ni sita, wauguzi 43 na kada nyinginezo 53 na kuwapangia Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mwongozo wa Wizara ya Afya hauruhusu madaktari bingwa kufanya kazi katika ngazi ya kituo cha afya. Serikali inaendelea kuajiri madaktari bingwa na kuwapanga katika hospitali za halmashauri kote nchini ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Mkalama. Ahsante.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-

Je, makubaliano ya mkataba ujao kati ya SONGAS na Serikali yamefikia hatua gani ikiwa mkataba wa awali upo katika mwaka wa mwisho?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Mkataba wa ununuzi wa umeme kati ya TANESCO na SONGAS unafikia ukomo wake tarehe 31 Julai, 2024. Kwa sasa, Serikali imeunda Timu ya Wataalam (Government Negociation Team - GNT) iliyoanza majadiliano mwezi Aprili, 2023 na inatarajia kukamilisha majadiliano haya kabla ya mkataba kuisha. Serikali itahakikisha maslahi ya Taifa yanazingatiwa kabla ya makubaliano yatakayofuata. Ahsante.
MHE. GRACE V. TENDEGA K.n.y. MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-

Je, lini barabara ya Iguguno hadi Nduguti – Mkalama itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Barabara ya Iguguno – Nduguti – Gumanga – Mkalama yenye urefu wa kilometa 89 unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imepanga kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami katika Mji wa Nduguti kwa sehemu ya kutoka Nduguti Roundabout kuelekea Iguguno (kilometa 7.5), Nduguti Roundabout kuelekea Gumanga (kilometa 2.0), Nduguti Roundabout kuelekea Nkungi (kilometa 0.5). Taratibu za zabuni ziko hatua za mwisho na mkataba unatarajiwa kusainiwa Mwezi Julai, 2024. Ahsante. (Makofi)