Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kunti Yusuph Majala (49 total)

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri, ni masuala yale yale kwamba tupo kwenye mchakato. Naomba kupata majibu katika maswali yangu mawili.
(a) Ni lini sasa TAMISEMI itakamilisha mchakato wa marekebisho ya sheria hiyo ili Halmashauri zetu ziweze kujipatia mapato yake stahiki?
(b) Ni lini kikao hicho cha wadau kitakwenda kufanyika ili tuweze kuokoa mapato mengi yanayopotea katika sekta hii? Asante.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli kumekuwa na kero kwa Waheshimiwa Wabunge wote katika Majimbo yote kwa sababu minara imeenea maeneo yote.
Mheshimiwa Spika, kila mtu katika Jimbo lake ana mnara na kila mtu anatarajia kukusanya kodi. Lengo ni kuhakikisha Halmashauri zinapata mapato, ndiyo maana ofisi yetu imeona, kwa sababu suala hili linagusa Halmashauri zote, lazima tuwe na mfumo ambao utakuwa muafaka kuhakikisha kwamba fedha zinakusanywa hali kadhalika Halmashauri zinapata fursa ya kukusanya hayo mapato vizuri na ndiyo maana mchakato huo umeshaenda.
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri sana kikao cha wadau kimeshakamilika, na jukumu linalofanyika ni kwamba paper itaondoka katika Baraza za Mawaziri, itajadiliwa na itakuja huko. Hata hivyo, tumeenda mbali katika marekebisho ya sheria hii, tunaenda kuangalia suala zima la crop cess, watu wanajua ushuru wa mazao umekuwa ni changamoto kubwa sana.
Kwa hiyo, sheria hii inakutanisha mambo mengi ili mradi Sheria ya Fedha Sura Namba 290 itakapokuja hapa Bungeni, basi iweze kukidhi mahitaji ya Waheshimiwa Wabunge wote katika Halmashauri zao, fedha ziweze kukusanywa na wananchi wapate huduma bora. Asante.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza kwenye Wizara ya Nishati na Madini. Wilaya ya Chemba ni miongoni mwa Wilaya mpya na upatikanaji wa huduma ya nishati kwa maana ya umeme ni kwa vijiji 60 tu kati ya vijiji 112. Nataka kufahamu ni lini sasa kwa REA Awamu ya Tatu itakwenda kukamilisha vijiji hivi 52 vilivyobaki ili Wilaya yetu na wananchi wale waweze kupata huduma hii ya umeme wa REA Awamu ya Tatu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Jimbo la Chemba tulipeleka umeme katika vijiji 62 na vikabaki vijiji 52; kwa hiyo viko 124. Niseme tu vijiji 52 vilivyobaki tumeshazindua katika maeneo ya Chemba na Wilaya zote, Mkoa wa Dodoma na tunaelekea katika Mikoa ya Singida na mingine. Upelekaji wa umeme katika REA Awamu ya Tatu umeanza tangu mwezi Machi na utakamilika kwa nchi nzima ikiwemo pamoja na Jimbo la Chemba mwaka 2020. Mradi huu unakwenda kwa awamu, baadhi ya vijiji na vitongoji vitakamilika mwezi Machi, 2019 na baadhi yake kwenye densification ni miezi 15 kuanzia sasa. Kwa hiyo, vijiji vyote 52 kati yake vijiji 12 vitapatiwa umeme 2019 na vilivyobaki vya Chemba mwaka 2020.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Kwa kuwa Serikali inatoza VAT kwenye vifaa vya ujenzi lakini pili tena tuna suala zima la tozo kwenye majengo, je, Serikali haioni sasa kuna sababu ya kumtoza mwananchi huyu kodi moja tukaondoa ya majengo tukabaki na hiyo tozo ya vifaa vya ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kodi hizi mbili ni kodi tofauti kabisa huku tuna- charge kodi ya VAT kwa mlaji wa mwisho na hasa ambaye yuko registerd kwa VAT, ambaye anavuka mapato yake kwa shilingi milioni 100 na kodi ya majengo hii ni kodi tofauti kabisa wala hazina sababu ya kuunganishwa pamoja. Mheshimiwa this isproperty tax na hii ni kodi ya mlaji, ka hiyo, kodi hizi haziwezi kuunganishwa na ikawa kodi moja.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Kata ya Makole, Manispaa ya Dodoma walisitishiwa uendelezaji wa nyumba zao kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege ulioko hapa wakati huo kuna wananchi wa Kata ya Msalato 89 wanaidai Serikali tangu mwaka 2005.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kujua wananchi wa Msalato watalipwa lini lakini pili wananchi wa Makole waliositishiwa uendelezaji wa nyumba zao…
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumekuwepo na upanuzi wa uwanja wa ndege au tutautumia sasa hivi hapa Dodoma na wananchi wa Makole madai yao ya fidia yanashughulikiwa kupitia Wizara ya Fedha na sasa hivi Wizara ya Fedha wako kwenye uhakiki wa kuhakikisha kwamba wanalipa hayo madai yao wakati watakapomaliza uhakiki.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kituo cha Afya cha Hamai kilichopo Wilayani Chemba kina upungufu mkubwa wa vifaatiba. Kituo hicho ndicho kinachotumika kama hospitali ya wilaya, kinahudumia wananchi wote wa Jimbo la Chemba, lakini pili, majirani zetu kwa maana ya Chilonwa na Jimbo la Kiteto mpakani kule. Sasa nataka kujua Wizara imejipangaje kutupatia vifaatiba zikiwemo x-ray machines pamoja na ultrasound? La pili suala zima la ambulance yetu, imechoka haitamaniki, haithamaniki. Nataka kupata majibu ya Waziri kuhusiana na hicho kituo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu lililotangulia, kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba vituo vyote vya afya vinapelekewa vifaa. Niruhusu nichukue fursa hii kuiagiza MSD kuhakikisha kwamba zile oda zote ambazo zimepelekwa kuwe na msukumo wa kuhakikisha kwamba hivyo vifaa vinapatikana mapema ili viweze kutumika katika vituo vya afya kama Serikali tulivyokusudia. Pia ni ukweli usiopingika kwamba MSD safari hii wanakwenda kuagiza kutoka kwa manufacturer, sio habari ya kuagiza kutoka kwa mtu wa kati na kuna specifications ambazo lazima tuzingatie, lakini ni vizuri tukahakikisha jambo hili linafanyika mapema.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi tena ya kuweza kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Wilaya ya Chemba tuna upungufu wa walimu wa kike chini ya asilimia 50. Huyu mwalimu ambaye amepelekwa Shule ya Msingi Donsee ametolewa kwenye shule nyingine, wamemhamisha kutoka shule hiyo wamempeleka shule nyingine, lakini nataka kwenye mpango wa Serikali nimeambiwa hapa Serikali iko kwenye mpango.

Ni lini Serikali itatuletea walimu wa kike kwa ajili ya kunusuru maisha ya watoto wetu wa kike?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, changamoto zinazosababisha walimu wetu wa kike wasikae kwenye shule zetu hizo ni ukosefu wa nyumba za walimu, miundombinu ya barabara, ukosefu wa umeme, kuna changamoto nyingi kadha wa kadha. Walimu wakifika kule kwa mfano Shule ya Msingi Birise iko umbali wa zaidi ya kilometa 160, bodaboda ni shilingi 45,000 mwalimu wa kike unampeleka pale, hawezi kukaa mazingira ni magumu. Hata zahanati tu hawana.

Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza Serikali, ni lini itakwenda kujenga nyumba za walimu, kuboresha miundombinu ya barabara, lakini pia suala zima la umeme ili tunapopeleka walimu wetu wa kike waende wakakutane na mazingira rafiki wapate kuishi kule na hatimaye watoto wetu wa kike waweze kupata na wao fursa ya kuhudumiwa na walimu hawa wa kike? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba nitumie fursa hii kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunti Yusuph Majala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameuliza lini Serikali itapeleka walimu wa kike katika Halmashauri ya Chemba? Kama ambavyo nilijibu katika swali langu la msingi, Serikali bado imeendelea na utaratibu wake wa kawaida wa kuajiri walimu mara kwa mara na bahati nzuri sasa hivi tuko katika mpango wa mwisho wa kutoa ajira mpya kwa walimu kwa hiyo, hilo suala lake tutalizingatia na tutaangalia zaidi jinsia, ili kuhakikisha kwamba, tunawasaidia watoto wa kike katika shule zote nchini.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili, alikuwa anauliza moja ya changamoto kubwa ni ukosefu wa miundombinu, hususan nyumba za walimu, na ndio sababu ambayo imesababisha walimu wengi kutokufika katika baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali inatambua kwamba changamoto hiyo ipo na katika moja ya mkakati wa Serikali ambao umekuwepo sasa hivi, Serikali ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, imekuwa ikijenga miradi mingi kwa maana ya miundombinu katika sekta ya elimu. Tumekuwa tukijenga mabweni, madarasa, mabwalo, miundombinu ya vyoo pamoja na nyumba za walimu za two in one.

Mheshimiwa Spika, sasa lini tutajenga, mimi niseme tu kwamba, kwa sababu tuna mpango mwingine wa tatu ambao tutaueleza katika bajeti na kwa sababu umeelezeka huko ndani kulingana na bajeti, tutapeleka hizo nyumba za walimu katika yale maeneo ambayo yana shida zaidi ili kuhakikisha kwamba walimu wa kike wanafika maeneo hayo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Changamoto ya soko la tumbaku inafanana kabisa na changamoto kubwa inayowapata wananchi wa Wilaya ya Chemba kwa soko la mbaazi pamoja na ufuta.

Je, ni lini Serikali itahakikisha wakulima wa Wilaya ya Chemba na maeneo yote Tanzania wanapata soko la uhakika kwa mazao ya mbaazi pamoja na ufuta? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti kama ifuatavyo kwa niaba ya Waziri wa Kilimo:-

Kwanza nikiri katika kipindi cha mwaka mmoja, miwili iliyopita soko la mbaazi limekumbwa na changamoto. Sio sisi tu Tanzania peke yake bali nchi nyingi zinazozalisha mbaazi duniani na hii ilitokana na restriction iliyowekwa na nchi ya India. Lakini hatua iliyochukuliwa na Serikali, ni kufanya mazungumzo na hivi karibuni katika msimu ujao wa mbaazi restriction iliyokuwa imewekwa na India itakuwa imeondoka na tutakuwa na uhakika wa kuuza mbaazi katika nchi ya India. Mazungumzo yanaendelea na majadiliano yanaendelea. Nitamkaribisha Mheshimiwa Mbunge na baadhi ya Wabunge mwezi ujao tutakapokuwa na kikao cha wadau wa mbaazi, ufuta, choroko na dengu hapa Dodoma, Mwenyezi Mungu akijaalia kujadili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ufuta, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali. Biashara ya mazao ni biashara ambayo kidogo ni complex, mkulima anapozalisha anapokuwa hana taarifa ya soko ndiyo maana Serikali sasa hivi tumeanza kutumia mfumo wa TMX kwa ajili ya price discovery na hii itatusaidia sana kuweza kupata the real value ya mazao ya kilimo na sasa hivi commodity market exchange yetu imeanza majadiliano na commodity market exchange za dunia. Kuna maongezi yanaendelea kati ya commodity market exchange ya Tanzania na commodity market exchange ya India na vile vile tumeanza maongezi na nchi ya China ili tuweze kufungua masoko haya na hatua zinaendelea kuchukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka ujao wa fedha Tanzania tutafungua the first display ya mazao yetu ya kilimo. Wizara ya Kilimo. tutaleta bajeti hapa ili Bunge lituidhinishie kufungua display ya mazao ya kilimo katika nchi ya China ili wafanyabiashara wetu wawe na eneo ambalo wana display mazao yao na kutafuta masoko moja kwa moja. Hii ni hatua ambayo tunachukua. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya mimi kuuliza swali la nyongeza kwenye Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Chemba ni kati ya wilaya ambazo zinachangamoto kubwa sana ya maji. Nilitaka kujua tu Serikali, ni lini itawapatia maji wananchi wa vijiji; Chandama, Changamka, Babayo, Maziwa pamoja na Ovada?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kunti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa Wilaya ya Chemba pia taasisi yetu ambayo iko pale inaendelea kufanya jitihada kuona vijiji hivi ulivyovitaja vinapata maji mapema iwezekanavyo. Naomba mtupe muda tuweze kufanya kazi, siku si nyingi kabla ya mwaka huu wa fedha tayari tutapunguza idadi ya vijiji ambavyo havina maji kwa Chemba.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kunipatia niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kata hizi ilikuwa zipatiwe umeme REA awamu ya pili, lakini mpaka tunamaliza REA awamu ya pili kata hizo hazijapatiwa umeme. Je, Serikali inawahakikishiaje watanzania wa Wilaya ya Chemba kwenye kata hizi nilizozitaja, kwamba kwenye awamu hii ya REA awamu ya tatu iliyoanza Machi, 2021 kwamba vijiji hivi na kata zake hazitakwenda kukosa umeme?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya ukatikaji wa umeme kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Wilaya ya Chemba na kwenda kusababisha uharibifu wa mali za watumiaji wa umeme. Je, Serikali sasa haioni ni wakati wa kuanza kulipa fidia kutokana na tatizo la ukatikaji wa umeme bila taarifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe tamko la Serikali kwa niaba ya Serikali, kwamba tunawahakikishia wananchi wote wa Tanzania kwamba vijiji vyote ambavyo vilikuwa havijapata umeme vilivyoko katika kata pamoja na hivyo alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge kwamba vitapelekewa umeme katika awamu ya pili ya mzunguko wa tatu wa REA, bila kuacha kijiji hata kimoja. Hiyo ni commitment ya Serikali na tayari mradi umeanza na vijiji vyote vilivyokuwa vimebakia takriban 1,900 vimechukuliwa katika mradi huu na vitapatiwa umeme.

Mheshimiwa naibu Spika, timekuwepo changamoto kadhaa katika awamu zilizotangulia na zile baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa yamebaki katika awamu hii ya tatu mzunguko wa pili hakuna hata kimoja kitakachobaki; na hiyo ni commitment ya Serikali. Kwa hiyo Mheshimiwa namuhakikishia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimshukuru Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Chemba Mheshimiwa Monni amekuwa naye mstari wa mbele katika kufuatilia umeme wa wananchi wake; na sisi kama Wizara na Serikali tutahakikisha kwamba tunapeleka umeme katika mazingira hayo kwa kushirikiana na Wabunge wa maeneo yote. Ndio maana sasa swali lililoulizwa limejibiwa lakini pia na wengine wanaendelea kufuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika swali la pili alizungumiza kuhusu kukatika kwa umeme na nizungumzie katika eneo la Chemba. Yapo matatizo ambayo yanapelekea umeme kukatika; na kwa eneo la Dodoma tunalo tatizo moja kubwa sana. Udongo wa Mkoa wetu wa Dodoma ni udongo tepetepe inaponyesha mvua, kwa hiyo nguzo zimekuwa zikianguka na kulala panapokuwa panatokea hali ya hewa yenye mvua nyingi na udongo kuwa tepetepe. Na katika kulitatua hilo tumehakikisha basi tumeanza kuweka vitu vinavyoitwa concrete poles ambazo ni nguzo za zege zinaweza kwenda chini zaidi na zitahimili mzingo kwa sehemu kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa Jimbo la Chemba umeme unaokwenda Chemba unaenda katika sub-station yetu ya Babati unapita Kondoa, unakwenda Chemba, unakwenda Kiteto, unakwenda mpaka Kilindi, kwa hiyo ni parefu sana. Kwa Mkoa wa Dodoma imeamuriwa kwamba zijengwe sub-station nne zinazoitwa ring circuit ambazo zitakuwa zikiuzunguka mji wa Dodoma na zitapunguza mahitaji ya umeme kwenye msururu mrefu. Kwa mfano kutoka Kondoa kwenda Chemba kuna kilometa kama 30. Sasa ile Kiteto na Kilindi zitaondolewa kwenye mstari huu ili umeme unaokwenda Chemba uwe wa uhakika na uuhudimie wale wananchi walioko pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumekuwa tukiwaelekeza wenzetu waendelee kutoa taarifa kwa wananchi wao ili waweze kupata taarifa kwamba umeme utakatika na wajiandae kwa mazingira kama hayo.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuweza kuuliza swali la nyongeza kwenye sekta hii muhimu. Suala zima la maji ya Mradi wa India imekuwa ni changamoto kubwa sana katika hii miji 28 na ambayo inasababisha Watanzania wengi kukosa maji. Nataka tu kujua, Mji wa Chemba ambao umekuwa kwenye ahadi ya Miradi ya India miaka nenda miaka rudi, ni lini Serikali itapeleka mradi mbadala wakati Watanzania wanaendelea kusubiri huo Mradi wa India ambao umeshindwa kutekelezeka kwa kipindi cha muda mrefu?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nimtoe hofu dada yangu Kunti, Mheshimiwa Mbunge. Serikali haijashindwa, Serikali ipo kwa ajili ya kutatua matatizo ya maji katika Taifa letu na ndiyo maana tuna miradi mikubwa mbalimbali ambayo tunaitekeleza. Katika eneo hili la miji 28, wewe ni mmojawapo ambao sisi umetumia hatua ya kutuita kuona hatua ya utekelezaji wake. Nataka nimhakikishie ukiona giza linatanda ujue kunakucha, timu yetu ya evaluation imekamilisha kazi. Naomba watupe nafasi waone namna gani Serikali hii ya mama yetu Samia Suluhu ambaye ametupa maelekezo mahsusi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunawatua akinamama ndoo za maji kichwani itafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Chemba pamoja na hiyo miradi mikubwa ambayo ipo kimkakati, Mheshimiwa Mbunge tumekwishakutana nae ametuomba visima vya dharura katika eneo lake la Chemba ili wananchi wake waweze kuapat huduma ya maji. Ahsante sana.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; suala la mradi huu wa Dola za Kimarekani milioni 500 ni mradi ambao umekuwa wa kila siku tunaendelea kusimuliwa, kuandikiwa kwenye vitabu, lakini utekelezaji wake hauleti tija kwa Watanzania. Kama Waziri alivyosema kwamba mradi huu ndio ulitarajiwa kwenda kukidhi maji kwa wananchi wa Wilaya ya Chemba ukiwemo Mji wa Chemba. Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya visima viwili ambavyo vimechimbwa mwaka 2017 lakini mpaka leo visima vile havijafungwa pump wala miundombinu yoyote haijaweza kutekelezwa? Lini Serikali itatoa fedha ili kwenda kukamilisha huo mradi wa visima hivyo viwili ambavyo vimechimbwa mwaka 2017 na mpaka sasa ni miaka minne? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Wilaya ya Chemba tunatarajia kupata maji ya kutosha kutokana na mradi mkubwa wa Bwawa la Farkwa, lakini bwawa hilo si tu kwa Wilaya ya Chemba bali litasaidia pia kupunguza adha ya maji kwenye Jiji la Dodoma, Wilaya ya Bahi na Wilaya ya Chamwino. Natamani kusikia kauli ya Serikali, ni lini mradi huu utakwenda kuanza rasmi kwa sababu hata kwenye bajeti ya maji hakujatengwa fedha za kwenda kuanzisha huu mradi badala yake tunasubiri fedha za wafadhili. Kwa hiyo nataka nijue Serikali ni lini inaenda kuanza Mradi wa Farkwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunti Majala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kumpongeza Mheshimiwa Kunti, amekuwa ni mfuatiliaji mzuri pamoja na kwamba ni mjumbe katika Kamati yetu ya Maji, amekuwa na mchango mkubwa, lakini vilevile nipende pia kumpongeza kwa sababu ana mahusiano mazuri na Mbunge wa Jimbo, wamekuwa wakifuatilia kwa pamoja masuala haya. Sisi kama Wizara tumesema kwamba Chemba maji lazima yaje. Pamoja na kwamba kuna visima hivi viwili vilichimbwa mwaka 2017, lakini mwezi Machi, 2021 tumeongeza kuchimba visima vinne, ili visima vile vinne vya mwaka huu tunakuja sasa kutengeneza mtandao wa usambazaji maji kuelekea kwenye vituo vya uchotaji maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anaongelea Bwawa la Farkwa. Hili bwawa ni juzi tu Mheshimiwa Waziri ametoka kuliongelea kama moja ya mikakati ya kuhakikisha maji Chemba yanafika. Pamoja na hilo tuna Mradi mkubwa wa Ziwa Victoria ambao pia Chemba utafika. Kwa hiyo bwawa hili litakwenda sambamba na mradi huu mkakati wa Ziwa Victoria. Tuendelea kuvuta subira, tumetoka mbali tunakokwenda ni karibu, maji Chemba yanakuja bombani.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Jiji la Dodoma takribani sasa ni miezi mitatu mfululizo kumekuwa na mgao wa maji usiokuwa na taarifa. Leo mitaa mbalimbali kwenye Kata ya Ipagala, Kata ya Dodoma Makulu, lakini Kata ya Nzuguni wana siku ya tano hakuna maji.

Nataka kupata kauli ya Serikali ina mkakati gani madhubuti wa dharura wa kuondoa changamoto hii kubwa inayowakumba wakazi wa Dodoma, lakini na wageni mbalimbali wanaoingia kwenye Jiji letu hili kufanya shughuli zao mbalimbali? Kwa sababu, imekuwa ni kero kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Jiji la Dodoma tumepitia kidogo changamoto katika mitambo yetu ya Mzakwe na pale Mailimbili. Tatizo kubwa ilikuwa ni umeme na tumewasiliana kwa karibu sana Mheshimiwa Waziri Aweso, pamoja na Mheshimiwa Makamba. Wamefanyia kazi hili suala kwa pamoja kuona kwamba lane ile ya umeme inayofanya uwezeshaji pale kwenye vile vyanzo usiwe disturbed. Kwa sababu, imekuwa disturbed huko mbele kulingana na ugawaji huu wa umeme wa REA, lakini sasa hivi wanaendelea kufanya maboresho ili kuona kwamba umeme usikatike kwenye vyanzo vyetu.

Mheshimiwa Spika, kwa dharura sana pale inapobidi sana Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira hapa Dodoma anajitahidi kuona kwamba maboza yanazunguka huko kutoa huduma pale inapobidi sana, lakini tayari maji yanarejea katika mfumo wake baada ya umeme kidogo kuwa unapatikana.

SPIKA: Labda Mheshimiwa Waziri kwa kuunganisha tu. Kwa kuwa ufumbuzi wa uhakika ni maji haya kutoka Ziwa Victoria, nini kinaendelea hivi sasa kutoka Ziwa Victoria kuja Mji wa Dodoma? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuja hapa Dodoma ni katika miradi yetu mikubwa ambayo tunategemea fedha kutoka nje. Wiki iliyoisha siku ya Ijumaa Wizara (wataalam) waliweza kuketi na World Bank kuendelea kufanya mazungumzo kuona huu mradi sasa unaingia kwenye utekelezaji.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali wa kupunguza uhaba wa mafuta nchini pamoja na zao la mchikichi lakini Serikali ilitangaza zao la alizeti kuwa ni zao pia litakaloingia kwa ajili ya kwenda kupunguza uhaba wa mafuta ya kula nchini. Katika mkakati huo wa Serikali Waziri Mkuu alitangaza Mikoa mitatu Mkoa wa Dodoma, Singida pamoja na Simiyu kuwa ndiyo Mikoa itakuwa kinara cha uzalishaji wa zao la alizeti.

Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo kwenye zao hili ni upatikanaji wa mbegu bora pamoja na gharama nafuu, sasa nilitaka kujua Serikali ama Wizara wamejipangaje kwenye suala zima la upatikani wa mbegu bora ambayo pia itakuwa ni bei nafuu itakayoweza kukidhi wakulima wetu kuweza kupata mbegu hiyo?

Mheshimiwa Spika, naomba kupata majibu ya Serikali kuhusiana na zao hili la alizeti. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kunti Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali tulitangaza zao la halizeti kuwa zao la kimkakati na sisi kama Wizara, ni vizuri Bunge lako Tukufu likafahamu kwamba tumetangaza Mikoa mitatu kuwa ni Mikoa kinara ikiwepo Dodoma, Singida na Simiyu. Hatua tulizochukua kwenye suala la mbegu, Wizara tumeshaandaa jumla ya tani 1,600 za standard seed ya record ambayo tunaiuza kwa shilingi 3,500. Tulichokitaka kutoka kwenye Halmashauri husika ni Halmashauri ilete mahitaji ije tuipatie mbegu, watasaini petition ya makubaliano na Wizara ya Kilimo kuonyesha kwamba hiyo subsidies rate ya shilingi 3,500 fedha yake italipwa namna gani.

Mheshimiwa Spika, tumetoa aina tatu ya namna ya kulipa, cash 50 percent ama kulipa mwisho baada ya mkulima kuvuna, tunawaomba Wakurugenzi wa Halmashauri za Dodoma, Singida na Simiyu tumeshasema tumeongea na Wakuu wa Mikoa na leo tumewaambia Wakuu wa Mikoa tulipokuwa nao kwenye kikao walete. Mheshimiwa Mbunge na wewe karibu umlete Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chemba aje tuweze kukubaliana namna ya kulipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu long term sisi kama nchi tunahitaji high breed seed zaidi ya tani Elfu Tano ili tuweze kuipeleka kwa wakulima. Kwa hiyo, hatua tunayoichukua kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha ni kwamba tutaingia mikataba na wazalishaji binafsi, watu binafsi siyo lazima tuzalishe mbegu Serikali, tutasaini nao makubaliano na wapo watu ambao wameshajitokeza mfano ni mtu anaitwa Ndugu Sumri ambae ana jumla ya hekta 8,000 kule Rukwa tunaingia nae makubaliano tunampa parent seed yeye anatuzalishia sisi serikali, halafu zile mbegu ndiyo tutazi-subsidies ili wakulima waweze kuzipata, ili tuondoke kwenye vicious cycle ya mbegu ni lazima turuhusu sekta binafsi ishirikiane na Serikali na huo ndio mwelekeo wa Wizara, tunaamini baada ya mwaka mmoja ama miwili tatizo la mbegu za alizeti katika nchi litakuwa historia.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo la uwepo wa vituo vya polisi kwenye wilaya mbalimbali limekuwa ni changamoto. Tarafa ya kwa Mtoro na Farqwa, Wilayani Chemba tuna kituo kimoja ambacho kipo kwa Mtoro. Kituo kile kimejengwa kwa nguvu za wananchi, ni kwa miaka zaidi ya 10 sasa baadhi ya majengo yamebomoka kutokana na Serikali kutokuunga juhudi za wananchi nguvu zao wanazojitolea. Pia kituo hicho hakina gari kwa ajili ya kuwasaidia polisi kwenda kuhakikisha wanawahudumia wananchi. Je, ni lini Serikali itawapatia fedha kituo cha polisi kwa Mtoro, kwa ajili ya kukarabati na kukamilisha majengo yaliyopo kwa sasa na kuwapatia gari kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu. Lilitakiwa liwe swali moja kwa hiyo nitachagua moja katika haya mawili kwa mwongozo wako.

MWENYEKITI: Ndiyo.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na aidha ni suala la gari ama jengo. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kunti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya swali hili yanafanana na majibu ya maswali mawili ambayo nimeshayajibu. Kwa hiyo, naomba nirudie majibu yale yale ya maswali mawili ambayo nimeyajibu. Kuhusiana na kwanza pongezi kwa wananchi ambao wameshiriki katika kuunga mkono jitihada za Serikali, kuhakikisha vituo vyetu vya polisi vinajengwa ama vilivyokuwa katika hali mbaya vinakuwa katika hali nzuri, pamoja na kuhakikisha kwamba tunaweza kuwasaidia, askari wetu kuweza kuwa na usafiri kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba kwa kuwa kituo hiki kinahitaji ukarabati, kwanza nitafanya jitihada, aidha, mimi au Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwenda kukitembelea, tuone kituo hiki kiko katika hali gani. Tutakapokuwa tumefika hapo na kuona mazingira tutafikiria, sasa ni njia gani ambayo ni muafaka zaidi ya kuweza kukifanyia aidha ukarabati kituo hiki. Pamoja na suala la usafiri kama ambavyo nimejibu katika maswali mengine ya msingi kwa sasa hivi, gari hatuna lakini tutakapokuwa tumepata gari, basi vilevile tutazingatia na kituo hiki. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Barabara ya kutoka Kilindi – Kiteto
– Chemba mpaka Singida ni barabara ya kimkakati ya kuchochea uchumi kwenye mikoa hii minne na wilaya zake. Bajeti hii tunayokwenda kumaliza ilikuwa inaze lakini mpaka sasa michakato yake bado ni mirefu na hatuoni dalili ya kwenda kuanza ujenzi wa barabara hii. Je, ni lini sasa ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami unaanza? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti Yusuph Majala, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoisema ni sehemu ya barabara inayoanzia Kilindi – Kiberashi – Kiteto hadi Kwamtoro, Singida. Naomba nimhakikishie kwamba kama nilivyosema, barabara hii ndiyo inayopita kwenye Bomba la Mafuta la kutoka Tanzania kwenda Uganda. Kwa hiyo Serikali ya Awamu hii ya Sita imejipanga kuhakikisha kwamba kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha barabara hii inaanza kujengwa. Hivi ninavyoongea barabara hii inaanza kujengwa kwa kiwango cha lami, tuko kwenye hatua za manunuzi kwa barabara hii. Ahsante. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Waziri mlikuja kwenye Kijiji cha Handa Kata ya Lahoda pamoja na timu ya Mawaziri watano na wewe ukiwemo mlikutana na changamoto kubwa sana, kuhusiana na Hifadhi ya Swagaswaga na wananchi walieleza changamoto wanayoipata kutokana na hifadhi hiyo na mkaunda timu ya wataalam kwa ajili ya Kwenda kutafsiri mipaka.

Je, ni lini Serikali itakwenda kuwaeleza wananchi tafsiri ya mipaka hiyo kwa sababu bado wananchi wale wanapigwa, bado wananchi wale wananyang’anywa mazao yao, wanadhalilishwa; nataka kujua ni lini mtakwenda kutoa hayo majibu kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya wataalam kufika katika maeneo hayo na kufanya tathmini niwaombe wananchi waendelee kusubiri maamuzi ya Serikali, wasiendelee kuvamia maeneo hayo na kujichukulia mamlaka ya kwamba tayari tumeyaachia. Ni mpaka pale Serikali itakapotoa tamko kwamba sasa tunaachia eneo hili, basi wananchi waendelee kufanya shughuli hizo.

Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge wasubiri kuwa tunachakata tutayaleta majibu.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Ni ukweli usiopingika kwamba migogoro ya ardhi imekuwa ikileta changamoto kubwa ikiwemo maafa na pia udumavu wa uchumi wa Taifa letu: Je, Serikali haioni sasa ni wakati umefika wa kuipanga ardhi kuitambua kwamba hii ni ardhi ya kilimo, hii ni ardhi ya mifugo na matumizi mengine kwa Taifa letu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Kunti Majala, swali lake la nyongeza juu ya utaratibu wa kutambua ardhi za Tanzania. Naomba kwanza nimrudishe Mheshimiwa Mbunge katika Sheria zetu zinazoongoza usimamizi yaani Sheria Na. 4 na Sheria Na. 5 ambazo zinatambua uwepo wa mgawanyo huu ambao yeye ameusema.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, pia Wizara imeendelea kufanya semina mbalimbali na elimu mbalimbali kwa wananchi ili kuweza kuwatambulisha. Pia ziko hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na ufahamu juu ya mgawanyiko wa maeneo ya ardhi ikiwemo kufanya hatua kubwa za kuelewesha Umma wetu kwa jumla yake. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Serikali ina mkakati gani wa kujenga kiwanda cha kukamua mchuzi wa zabibu ili kuweza kuondoa adha ya wakulima wa zabibu wa Mkoa wa Dodoma wanaotembea na mabeseni barabarani wakitembeza zabibu na kuiuza bila faida yoyote? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti Majala, kuhusiana na sekta ya kilimo hasa kwenye zao la zabibu.

Mheshimiwa Spika, tayari tumeshaanza juhudi mbalimbali za kusaidia kuchakata zabibu ili ziweze kuwa katika hali ya mchuzi wa zabibu anaosema, ambapo tayari kuna wadau mbalimbali wameshaanza kuchukua, wakiwemo kiwanda cha Jambo ambao wapo Shinyanga. Vilevile wengine wameshaanza kuchukua zabibu hizo ambazo naamini wadau hawa ambao tumewahamasisha watapunguza adha ya kutembea kuuza zabibu ambazo hazijachakatwa ambazo wakulima wenzetu wa Mkoa wa Dodoma wanahangaika nazo. Nakushukuru.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, Skimu ya Umwagiliaji ya Kidoka ni kati ya skimu zilizopo kwenye Mkoa wa Dodoma, lakini skimu ile miundombinu yake imekuwa chakavu na wakulima wetu wamekuwa wakijiendesha kwa hasara sana kutokana na gharama kubwa za umeme wanazozitumia ku-pump maji.

Je, ni lini sasa Serikali mtakwenda kuweka miundombinu rafiki ya skimu ile ili wananchi wetu waweze kujiendesha vizuri kwa faida? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti Yusuph Majala, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja kati ya kazi kubwa ambazo tuliwapa watu wa tume ni kuhakikisha wana-take stock ya miradi yote ambayo imekwama na yenye changamoto, na tumekamilisha zoezi hilo. Hivi sasa ni kuanza kupitia na kuona namna gani tunaweza tukaboresha skimu hizo.

Mheshimiwa Spika, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba nitatoa maelekezo kwa watu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuhakikisha Jumatatu wawepo katika eneo la Kidoka kuangalia changamoto ni ipi na tuone namna ya kuweza kurekebisha skimu hiyo.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Changamoto iliyopo Mkoa wa Songwe inafanana kabisa na changamoto iliyopo Mkoa wa Dodoma katika Wilaya ya Chamwino na Wilaya ya Chemba.

Ni lini Serikali itajenga barabara ya kutokea Itiso, Zajirwa mpaka Kimaha kwa maana ya Kata ya Kimaha kuunganisha na Wilaya ya Chemba?

Pili, ni lini Serikali itajenga barabara ya kutokea Kimaha – Soya – Msada mpaka Wilaya ya Kondoa? Ninakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunti Majala, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa hizi barabara ikiwemo Itiso – Kimaha na nyingine Kimaha – Soya na maeneo yote ambayo ameyaainisha kwamba, anataka kujua tu commitment ya Serikali ni lini itajenga barabara hizo.

Mheshimiwa Spika, ninaamini katika bajeti ya fedha ya mwaka unaokuja ziko sehemu za hizi barabara alizoziainisha tumezitengea fedha na nyingine tutaendelea kutafuta fedha ili kuhakikisha barabara hizi zote zinapitika kwa wakati wote. Kwa hiyo, hilo ndio jibu la Serikali. Ahsante.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri Kata ya Kinyamsindo, Lahoda pamoja na Sanzawa zilishafanyiwa tathmini kwa ajili ya kujengewa minara. Je, ni lini sasa wataziingiza kata hizi kwenye zabuni ili zitangazwe na hatimaye wananchi wetu waweze kupata mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Kunti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tuna miradi ambayo inaendelea na pili kuna miradi 763 ambayo tayari Serikali imeshatangza zabuni, lakini vile vile tuna vijiji 216 ambavyo Serikali tayari imeshavifanyia tathmini. Kwa hiyo, tunaamini kwamba kwa kadri fedha itakapokuwa inapatikana, tunaamini kwamba vijiji hivyo, ikiwa pamoja na kata hiyo itaingizwa katika utekelezaji ili kuhakikisha kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi ianendelea kutekelezwa kwa niaba ya Rais wa Tanzania. Ahsante sana.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Pamoja na uwepo wa hiyo sheria Mheshimiwa Waziri aliyotuambia, lakini ni dhahiri kwamba watumishi tulionao hawatoshi, lakini pili miundombinu siyo rafiki. Huko vijijini ambako ndiko wakulima waliko, wakulima wetu wa mazao mbalimbali nchini wamekuwa wakiuza kwa lumbesa kwa sababu tu kwanza mtu anayeratibu ni wafanyabiashara kwa maana ya madalali, ndio wanaopanga wakulima wetu wauzaje na kwa uzito upi. Je, Serikali haioni sasa muda umefika kwa wafanyabiashara wa mazao kutoa maelekezo wanapokwenda vijijini kununua mazao, waende na mizani na wananchi wetu wapewe maelekezo pia na elimu kwamba wasiuze kwa mfumo wa lumbesa?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti Majala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna changamoto ya watumishi katika maeneo yote ikiwemo hili la Wakala wa Vipimo kwa maana ya wanaosimamia mambo ya vipimo. Kwa kweli kazi kubwa inafanyika kwa kushirikiana na halmashauri kuhakikisha tuna washirikisha Maafisa Biashara ambao ndio wanaowasadia na pia Maafisa Ugani ambao wako katika maeneo hayo ili kuhakikisha tunawalinda wakulima katika maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, sio katika lumbesa tu, kwa sababu lumbesa kama alivyouliza muuliza swali la msingi kwenye viazi, lakini pia hata katika maeneo mengine ambako wanatumia vitu kama ndonya, kangomba, bakuli na vitu kama hivyo. Kwa hiyo tunajitahidi kuhakikisha Maafisa Biashara na Maafisa Ugani hawa wanawasaidia wakulima ili kuhakikisha kwamba wanakuwa na maeneo ya kuuzia ambako watawasaidia.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwaelekeza Maafisa Biashara ambao tumekwishawapa nafasi ya kuwa wafanyakazi pia katika Idara za Uwekezaji, Viwanda na Biashara, wasaidie na wasimamie hili suala ili tuondokane na unyonyaji huu unaotumika wa kunyonya wakulima kwa kununua katika vifungashio au bila kutumia vipimo katika maeneo ya mashambani ili tuondokane na masuala haya ya lumbesa.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. KUNTI Y MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna changamoto kubwa ya umeme nchini lakini wamekuwa wakikata umeme bila kuwapa taarifa wateja wao na kusababisha uharibifu mkubwa wa vifaa vya majumbani, lakini pia na miundombinu ya viwandani. Je, Serikali sasa iko tayari kuanza kuwalipa fidia wateja wao wanaoathirika na kukatika kwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti Majala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukatikaji wa umeme ni wa aina mbili, kuna kukata kwa vile tumepanga kukata ili tufanye matengenezo, lakini kukatika kwa sababu ya hitilafu ambazo ziko hata nje ya uwezo wa binadamu. Katika vitu ambavyo Shirika letu la TANESCO limejitahidi sana kufanya ni kutoa taarifa ya makatizo ya umeme yale ambayo tumeyapanga. Kiukweli katika hilo Myonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Tumewaelekeza na wamejitahidi katika siku za hivi karibuni matengenezo ambayo yanafanyika tunahakikisha tunayaratibu na taarifa zinatolewa kwa wateja wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye yale makatizo ambayo hatukuyatarajia, ni mashine imezidiwa kama ndugu zetu wa Kariakoo. Juzi tarehe 23 transformer moja ilipata hitilafu kwa sababu ilipokea mzigo mkubwa kuzidi ilivyotarajia, mvua zimenyesha, waya zimekatika na vitu kama hivyo. Tunaendelea kuhakikisha kwamba matukio hayo hayatokei. Hata hivyo tunaweza kufika kwenye utaratibu wa kawaida kuona namna gani ambayo sheria inaweza ikachukuliwa ili sasa ambaye anastahili kupata haki fulani anaweza kuipata kwa mujibu wa sheria tulizonanzo.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Chuo cha Ufundi VETA Wilaya ya Chemba kimekamilika zaidi ya asilimia 80; ni lini sasa Serikali itaanza kudahili kwa kozi hizo ndogo ndogo za muda mfupi kwa maana miwili/miezi mitatu ili vijana wetu walipo mitaani waondokane na adha ya ajira na hatimaye waweze kujiajiri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kunti Majala, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye swali la Mheshimiwa Ndulane, Chuo cha Chemba ni miongoni mwa vile vyuo 25 ambavyo vilikuwa bado havijakamilika. Kwa hiyo, kuna snag ndogo ndogo ambazo zilikuwa za kumalizia. Zaidi ya shilingi milioni 400 ilikuwa inahitajika na Mheshimiwa Rais tayari ameshatoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 10.3 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyuo hivi 25. Tayari fedha hizi tumeshazipeleka pale Chemba na maeneo mengine na tunatarajia kuanzia mwezi wa nne kozi hizi za muda mfupi tuweze kuanza kudahili na ziweze kutolewa katika maeneo ya Chemba na maeneo mengine vyuo hivi 25 vinapojengwa.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kata ya Soya, Wilaya ya Chemba ni kati ya Kata ambayo inahudumia wafanyabiashara wa mazao pamoja na wafanyabiashara wa mifugo, lakini Kata hii haina kituo cha polisi pamoja na kwamba kutokuwepo kwa kituo cha polisi michakato aliyoisema Naibu Waziri hapo tulishaikamilisha. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka kituo cha afya, samahani, Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Soya ili kukidhi mahitaji na matakwa ya usalama wa Jeshi la Polisi ya kulinda raia na mali zao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru maana mwanzoni afya ilinichanganya kidogo. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti Majala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ikiwa kuna mahitaji makubwa ya kujenga Kituo cha Polisi Kata ya Soya, nishauri mamlaka za utawala, kwa maana ya Serikali ya Mtaa Chemba lakini na uongozi wa Wilaya kupitia Kamati yao ya Usalama wajenge hoja hii kama nilivyoeleza, wanyambue mahitaji yao ili wawasilishe kwa IGP, then taratibu ya kuingiza kituo hiki katika mpango wa ujenzi iweze kufikiriwa. Hata hivyo, kama tulivyokwishasema kwenye majibu ya maswali yaliyotangulia, tunahamasisha ushiriki wa Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na wananchi waanze ujenzi ili Serikali isaidie kukamilisha vituo hivi wakiwa na haja ya kuwa na kituo cha polisi. Ahsante.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa swali. Mheshimiwa Waziri ametuambia kwamba Balozi zote nchini zimepewa viwanja Dodoma.

Je, ni changamoto gani kubwa inayosababisha Balozi hizi zishindwe kuja kuendeleza viwanja hivyo na kuhamia Dodoma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza utaratibu wa kuhamisha makazi ya Kibalozi kutoka iliyokuwa makao makuu ya nchi yetu kuja Dodoma ni utaratibu sawa na nchi nyingine zilivyofanya wakati huo. Kwa mfano, sisi tulihama kutoka Borne kwenda Berlin lakini tulichukua muda mrefu sana kwa sababu, hili ni suala la mipango ya kila nchi kujiwekea mpango wa uhamisho ambao unahitaji fedha. Kwa hiyo, upo uwezekano kabisa mkubwa wa nchi hizi ku-delay kuhamia hapa Dodoma kwa sababu, lazima ziingie kwenye mipango yao ya fedha na ziruhusu katika utaratibu wa kawaida Balozi zao kuhamishia makazi yake hapa makao makuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo tukumbuke wakati tunafanya mchakato wa uhamisho baadhi ya Balozi zetu hapa ambazo zinawakilisha nchi zao hapa ndio zilikuwa zinamaliza majengo yao mapya Dar es Salaam. Kwa hiyo, unaweza ukaona namna ambavyo kunakuwa na misukosuko ile ya kimaandalizi kuanza kufikiria upya kuhamia Dodoma, ahsante. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba pamoja na hayo majibu ambayo hayaridhishi, nina maswali mawili madogo ya nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja wa ndege, awali upanuzi ulikuwa ni mita 300 na upanuzi huo umeanza mwaka 2016. Mpaka tunavyozungumza sasa, ni miaka saba, wamepanua mita 150. Mita nyingine 150 waliwazuia wananchi wa Kata ya Makole kutokuendeleza maeneo yao, na mpaka sasa tunavyoongea nyumba zile zimekuwa ni magofu, watu walihama mle: Je, Serikali haioni wana sababu ya kuwalipa wananchi wa Kata ya Makole, kaya 50 zilizobaki kifuta jasho, ili waweze kufanya ukarabati wa nyumba zao na warudi kwenye makazi yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Ni sera ya Serikali kwamba, inapotwaa maeneo ya wananchi, inatakiwa ilipe fidia kwanza ndipo iendelee na utekelezaji wa miradi. Imekuwa ni kawaida ama ni tabia ya Serikali kuendelea kutwaa maeneo ya wananchi bila kuwalipa fidia na kuendeleza utekelezaji wa miradi, na matokeo yake wananchi wengi wamekuwa wakidhulumiwa. Hivi tunavyoongea…

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa Kunti?

MHE. KUNTI Y. MAJALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, watu 46 walioko Mkonze hawajafanyiwa uthamini na Waziri hapa anasema waendelee kuvuta subira. Ni lini wananchi 46 waliobaki Mkonze watalipwa fidia yao kwa sababu tayari maeneo yao yameshachukuliwa na mradi umeshatekelezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunti Yusuph Majalla, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mwaka 2016 Serikali ilikuwa na nia kwa ajili ya ujenzi ama upanuzi wa uwanja wetu wa ndege wa hapa Dodoma, lakini Serikali ilipoanza ujenzi mwingine mpya, hususan katika kiwanja cha Msalato, ikaona haina sababu ya kuendelea kupanua uwanja mkubwa zaidi wakati uwanja mkubwa wa Kiwanja cha Msalato unaendelea kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, ilipofika mwaka 2018 na kupitia Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo pamoja na timu yake na wataalamu wetu kutoka TAA walipewa taarifa wananchi hawa kwamba eneo hilo, na kusudio la Serikali kuendelea kuupanua uwanja huu halitakuwepo tena, bali tutalipa zile fidia za mita 150 ambazo tayari tumeshalipa kwa kiasi cha Shilingi 1,900,000,000/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili, kuhusu Mkonze, ni kweli kwamba, katika ujenzi wa TRC, kawaida unapojenga SGR, tunasema ni Design and Build, maana yake huwezi kufanya tathmini yote na ukalipa wananchi wote. Maana yake, inafanyika tathmini na wakati huo huo ulipaji unaendelea. Kwa maana hiyo basi, ifikapo tarehe 17 ya mwezi huu wa Aprili, wananchi wote wa eneo la Mkonze ambao hawajalipwa fidia zao tukutane eneo la SGR Station hapa Mkonze na waje na nyaraka zao, ahsante.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kituo cha Polisi Kwamtoro ni kituo cha majengo ya mkoloni, kimechakaa, hakitamaniki, hakithaminiki. Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, kulingana na upatikanaji wa bajeti tunaendelea kuvikarabati Vituo vyote vya Polisi vilivyochakaa. Hiki cha Kwamtoro pia tutakiingiza kwenye mpango wa matengenezo kadri tutakavyopata fedha kutoka Serikalini, nashukuru.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri, maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, lakini ni ukweli usiofichika kwamba mazingira ya walimu wetu kwa maeneo ya vijijini ni tofauti kabisa na maeneo ya mjini. Sasa kumekuwa na upungufu mkubwa wa walimu wa kike kutokana na mazingira hususan kwenye halmashauri ama majimbo ama wilaya za vijijini.

Swali langu la kwanza; je, ni lini Serikali itaanza kulipa posho kwa ajili ya mazingira magumu kwa walimu wetu Tanzania, hususan wa kike? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kutokana na upungufu mkubwa wa walimu, Wilaya ya Chemba tuna shule zaidi ya sita ambazo wanafunzi wameshindwa kuendelea na masomo, hatuna walimu. Shule hizo ni Shule ya Magarasta Sanzawa, Mialo Kwa Mtoro, Hanaa Gwandi, Magandi Soya, Mkandinde Soya pamoja na Lugoba Kata ya Kimaha.

Je, ni lini Serikali itapeleka walimu hawa ili watoto wetu kwenye shule hizi sita waanze masomo ili na wao waweze kutumiza haki yao ya kikatiba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA YA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge; swali lake kwanza la mazingira, Serikali hakuna incentive maalum ya mazingira na hivi sasa Serikali inaandaa mwongozo kwa ajili ya posho ya masaa ya ziada. Incentive kubwa ambayo inatolewa na Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kwamba inaweka mazingira bora kwa kujenga nyumba, kutengeneza miundombinu ya barabara, kuvuta umeme kwenye vijiji vyote vya nchi yetu hii ambayo nayo inatengeneza mazingira bora kwa watumishi wetu kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, nikijibu swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge la maeneo haya ambayo ni Sanzawa, Gwandi, Soya ni lini yapata watumishi. Kama nilivyosema hapo awali Serikali imetangaza ajira zaidi ya 21,000 ambapo katika ajira hizi za Walimu na maeneo haya yaliyotajwa nayo yatapata. Nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ajira za mwaka uliopita, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ndio ilipata Walimu wengi zaidi wa kike katika Mkoa huu wa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Kata ya Soya, Wilaya ya Chemba tulijengewa na wafadhili, kuna baadhi ya vifaa tiba vipo na baadhi havipo ikiwemo x–ray machine, lakini na watumishi mpaka leo kituo kimekamilika tangu mwaka jana. Hivyo vifaa tiba havijakamilika na watumishi hatuna kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itatupelekea vifaa tiba pamoja na watumishi ili hospitali kwa maana ya kituo cha afya hicho kiweze kufanyaa kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kituo cha Afya cha Kata ya Soya, Wilayani Chemba Serikali itapeleka watumishi, katika hawa watumishi wanaoajiriwa kama nilivyokwisha sema katika majibu yangu ya msingi na kwenye vifaa tiba tutaangalia kwenye bajeti iliyotengwa ni kiasi gani inatakiwa kwa ajili ya kwenda kununua hivi vifaa kama x–ray na vinginevyo basi Serikali iweze kupeleka fedha hizo na vifaa hivi viweze kununuliwa na wananchi wa Soya waweze kupata huduma hii.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Jiji la Dodoma limeendelea kukumbwa na kadhia kubwa ya uhaba wa maji: Je, Serikali ni lini mtakamilisha mradi wa visima vya Nzuguni ili kuondoa kadhia hii inayowakumba wananchi na wakazi wa Jiji la Dodoma? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti Majala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ukamilishaji wa visima vya Nzuguni, kadiri tunavyopata fedha tutaendelea kumwezesha mkandarasi ili viweze kukamilika ndani ya miezi ya mkataba tuliyokubaliana naye. Tunafahamu changamoto kubwa inayokumba Jiji la Dodoma na tunaendelea na jitihada nyingi sana kuona kwamba pamoja na visima hivi na vyanzo vingine, tuweze kuondoa adha ambayo ipo kwenye Jiji la Dodoma.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Suala la andiko tayari Wilaya ya Chemba mwaka 2020/2021 tulishaandika hilo andiko na likaenda TAMISEMI na TAMISEMI wakatushauri tuanze kwa mapato yetu ya ndani. Mpaka sasa tumeshatumia zaidi ya milioni 36 kwa ajili ya ulipaji wa fidia pamoja na kufanya usafi katika eneo hilo. Sasa tunataka kujua, je, ni lini Serikali inakwenda kutekeleza maagizo yake kwenye suala zima la ujenzi wa stendi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, stendi hii pia mwaka 2020 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli alipopita Wilaya ya Chemba wananchi wa Wilaya ya Chemba walimwomba ujenzi wa stendi hii na akaahidi itajengwa haraka iwezekanavyo. Sasa na Mheshimiwa Waziri umesema hapa kwamba mko kwenye mchakato wa kukamilisha ahadi zote za viongozi. Je, ni lini Serikali inakwenda kutekeleza ahadi hii ya Hayati John Pombe Magufuli ili tuweze kumuenzi wananchi wa Wilaya ya Chemba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunti Majala, hili la kwanza la andiko. Mpaka sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI haijapokea andiko lolote kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chemba juu ya ujenzi wa stendi hii, si kusema kwamba Serikali haijapokea, andiko hili huenda liliandikwa likapelekwa moja kwa moja Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafuatilia juu ya andiko hili la Chemba na nitakaa na Mheshimiwa Mbunge kuweza kuona andiko hili limefikia wapi na kama kuna marekebisho yoyote, basi yaweze kufanyika na kurejeshwa tena kufanyiwa tathmini ili fedha iweze kutafutwa kadri ya upatikanaji wake kwenda kujenga stendi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili la ahadi ya Mheshimiwa Rais, nirejee tena kusema ni kipaumbele cha Serikali kuhakikisha inatekeleza ahadi zote za Viongozi wetu Wakuu wa Nchi kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kadri ya upatikanaji wa fedha na tutaangalia ili tuone tunatenga fedha kwenye mwaka upi wa fedha kadri bajeti itakavyoruhusu.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Mnada wa Kata ya Soya ni kati ya minada mikubwa ambayo inafanya shughuli za uuzaji wa mifugo kwa maana ya mbuzi, ng’ombe, kondoo pamoja na punda lakini mnada ule miundombinu yake ni chakavu.

Je, Serikali mko tayari kuutembelea mnada ule nakujionea halia halisi ili muweze kutenga fedha itakayoweza kukarabati mradi huo ili wakulima wa mifugo waweze kuutumia mnada ule kwa tija na kwa maana ya afya kwa watumiaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tuko tayari kufika katika eneo la Soya, bahati nzuri ni karibu hapa tunaweza tukapanga tu baada ya muda wa Bunge tukafika na kujionea hali halisi ili tuweze kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati huo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tumeona changamoto kubwa kwenye suala zima la mikopo; je, Serikali iko tayari sasa kubadili mfumo wa mikopo badala ya kutoa fedha kwenda kuwapa huduma kama ni ufugaji wa kuku, Serikali ikaamua kuwanunulia kuku ikawapatia wana kikundi badala ya kuwapa fedha ambazo haziendi kutimiza malengo ya ule mkopo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, baada ya maelekezo yale ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kufanya mapitio ya utoaji wa mikopo hii ya asilimia kumi na maelekezo ya Kamati yako ya Bunge ya TAMISEMI, hivi ni vitu ambavyo vinaenda kuangaliwa na timu ile ambayo ameiteua Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa kwenye jibu la msingi Waziri ametuambia chanzo ni upungufu wa chembechembe nyekundu kwenye mwili wa mtoto. Sasa je, tunamshauri nini mama mjamzito ili kuondokana na tatizo hili? (Makofi)

Swali langu la pili; mtoto akishazaliwa na akagundulika ana tatizo hili la manjano, wataalam wetu huwashauri wazazi kuwaanika watoto juani. Ni, lini tiba ya ugonjwa huu itapatikana ili kuondokana na changamoto kubwa ya wazazi wanaokumbana na ugonjwa huu wa manjano, baadhi wanapoteza maisha na hatimaye kupunguza nguvu kazi ya Taifa letu? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Swali lake la kwanza anasema kwamba tumesema chanzo ni upungufu, siyo upungufu, wakati mwingine watoto wanapokuwa wamezaliwa halafu wanakuwa na chembechembe nyingi za damu ambazo alitoka nazo tumboni zinapokuwa zinasafishwa kunakuwepo sasa na bilirubin ambayo inasababisha hiyo hali ya umanjano kwamba sasa hicho ndiyo kinachotokea. Wakati mwingine kwa sababu ini la mtoto anapozaliwa ndani ya siku 14 anakuwa bado ini lake halijakua vya kutosha, kwa hiyo, uwezo wa kubadilisha ile kitu kinachosabisha umanjano haina uwezo wa kutosha ndiyo maana unaona huo umanjano, kwa hiyo, ni kitu cha kawaida. Ikitokea kama tulivyosema ndani ya masaa 24 basi ni tatizo tunalifuatilia na kujua. Hata hivyo ikitokea baada ya masaa 24 ni muhimu vilevile wataalam kumuangalia.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni suala la kwamba watoto wanaanikwa juani. Nimuambie tu Mheshimiwa Mbunge, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshafanya revolution kubwa sana, ndiyo maana umeona trilioni 1.3 imefanya mabadiliko makubwa sana ya tiba ya afya. Leo unaona vifaa vingi sana vimesambazwa kwenye maeneo yetu na vituo vyetu vya afya, utaona kuna vifaa maalum vya kuwaweka watoto ambavyo vinatoa mionzi maalum kwa ajili ya kuondoa hilo tatizo. Kwa hiyo, watoto wetu kwa revolution aliyoifanya Dkt. Samia Suluhu Hassan mpaka kwenye vituo vyetu na zahanati sasa vifaatiba vinaenda kununuliwa na hili tatizo litaondoka. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Waziri Kata ya Lahoda, Sanzawa- Mpendo na Kinyamshindo zilikuwa zipate umeme REA phase II lakini hazikufanyiwa hivyo. Na sasa tuko kipindi cha REA phase III. Nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kata hizi na vijiji vyake vinapata umeme katika Mradi huu wa REA phase III? ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kunti Majala kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya REA III round II kuisha ninatoa maelezo ya Serikali hakuna Kijiji kitakuwa hakijafikiwa na Nishati ya Umeme. Commitment ya Serikali ni kuhakikisha kwamba katika awamu hii ya tatu mzunguko wa pili vijiji vyote Tanzania Bara vinapata umeme. Kwa hiyo, nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo hilo pia litapata umeme.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati ya Mwaiksabe majengo yake yamekuwa ni ya muda mrefu lakini pili walikuwa hawana jengo la mama na mtoto; wananchi wale wamejenga jengo la mama na mtoto na mpaka wamepaua.

Je, Serikali ni lini itawapelekea fedha kwa ajili ya kukamilisha hatua zilizobaki kwa maana ya plasta pamoja na vifaatiba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze wananchi hawa katika zahanati hii kwa kutoa nguvu zao na kujenga jengo la mama na mtoto na hicho ni kipaumbele cha Serikali. Naomba nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kufanya tathmini ya gharama zinazohitajika kukamilisha jengo hilo ili tuone kama wanaweza kutumia fedha za mapato ya ndani kukamilisha au Serikali Kuu. Lakini nikuhakikishie kwamba vifaatiba Serikali imetenga bilioni 69.9 mwaka ujao wa fedha tutapeleka pia katika jengo hilo. Ahsante.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi na mimi niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu ya Umwagiliaji ya Chinangali ni kati ya skimu kubwa na kongwe katika Mkoa wa Dodoma na skimu hii Serikali tayari mlikuwa mmeshaanza suala zima la ukarabati ili wakulima wale waweze kupata maji kwa ajili ya kukidhi kilimo chao.

Je, ni lini sasa Serikali mtaanza rasmi na kukamilisha ukarabati wa skimu ile, ili wakulima wetu wa zabibu waweze kupata tija katika kilimo chao cha zabibu mkoani hapa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kunti Majala, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Skimu ya Chinangali ni kati ya skimu kubwa ambazo zinazalisha sana zao la zabibu na Serikali kupitia TARI na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji tuliamua kwa dhati kabisa kuifufua skimu hiyo na hivi sasa ninavyozungumza kazi inaendelea na tunategemea mwaka wa fedha ujao kwa maana ya tarehe 1 Julai kazi zitaendelea kukamilisha skimu hii kubwa ili mwisho wa siku wakulima wa zabibu wa Dodoma waweze kuzalisha kwa tija na kwa malengo ambayo tumejiwekea kukuza zao hili la zabibu Mkoani Dodoma. (Makofi)

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na mimi kunipatia nafasi nimuulize Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza. Kwenye majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kuna Kampuni tatu ambazo Serikali ilishatoa maelekezo kwa ajili ya kufungasha mbolea kwenye kilo tano, kumi na kadhalika; lakini mpaka sasa ni Kampuni moja tu ambayo ndiyo imeanza kufunga mbolea kwa hivyo vifungashio vidogo vidogo. Nayo imeenda kufungasha na imefanya hujuma, imeweka na mbolea ambayo haistahili, wamefunga. Nini kauli ya Serikali kwa Makampuni haya ambayo tayari Serikali imetoa maelekezo kufungasha mbolea kwenye vifungasho vidogo vidogo wasipotekeleza hili kwa wakati ili wakulima wetu waweze kupata mbolea na iweze kutumika kwa kuleta tija kwa wakulima wetu?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani labda wakati najibu Mheshimiwa Mbunge hakunielewa vizuri. Nimesema Kampuni tatu zimeishaanza kufungasha, tatu, ambazo ni ETG, YARA na Minjingu kati ya hizi tatu ni moja ndiyo tumeikuta na tatizo katika mikoa miwili; Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Iringa, na tunaendelea kuzihamasisha kampuni zote ziendelee kufungasha katika ujazo mdogo mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukafahamu kwamba segment inayotumia mbolea kilo moja na segment inayotumia mbolea kilo tano ni wakulima wadogo, wadogo wa bustani ambao si sehemu kubwa na tujue kwamba hii ni biashara. Kwa hiyo tutaendelea kuwahamasisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile Wizara sasa hivi tumeiwezesha TFC ili TFC Kampuni ya Serikali ifanye kazi kubwa ambayo kampuni binafsi hazioni maslahi makubwa katika eneo hilo na TFC hivi karibuni na yenyewe itaanza kufungasha katika vifungashio vidogo vidogo ili wakulima waendelee kupata huduma wanayotaka. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na mimi kunipatia nafasi nimuulize Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza. Kwenye majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kuna Kampuni tatu ambazo Serikali ilishatoa maelekezo kwa ajili ya kufungasha mbolea kwenye kilo tano, kumi na kadhalika; lakini mpaka sasa ni Kampuni moja tu ambayo ndiyo imeanza kufunga mbolea kwa hivyo vifungashio vidogo vidogo. Nayo imeenda kufungasha na imefanya hujuma, imeweka na mbolea ambayo haistahili, wamefunga. Nini kauli ya Serikali kwa Makampuni haya ambayo tayari Serikali imetoa maelekezo kufungasha mbolea kwenye vifungasho vidogo vidogo wasipotekeleza hili kwa wakati ili wakulima wetu waweze kupata mbolea na iweze kutumika kwa kuleta tija kwa wakulima wetu?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani labda wakati najibu Mheshimiwa Mbunge hakunielewa vizuri. Nimesema Kampuni tatu zimeishaanza kufungasha, tatu, ambazo ni ETG, YARA na Minjingu kati ya hizi tatu ni moja ndiyo tumeikuta na tatizo katika mikoa miwili; Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Iringa, na tunaendelea kuzihamasisha kampuni zote ziendelee kufungasha katika ujazo mdogo mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukafahamu kwamba segment inayotumia mbolea kilo moja na segment inayotumia mbolea kilo tano ni wakulima wadogo, wadogo wa bustani ambao si sehemu kubwa na tujue kwamba hii ni biashara. Kwa hiyo tutaendelea kuwahamasisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile Wizara sasa hivi tumeiwezesha TFC ili TFC Kampuni ya Serikali ifanye kazi kubwa ambayo kampuni binafsi hazioni maslahi makubwa katika eneo hilo na TFC hivi karibuni na yenyewe itaanza kufungasha katika vifungashio vidogo vidogo ili wakulima waendelee kupata huduma wanayotaka. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, Barabara ya Kiberashi – Chemba – Kwa Mtoro mpaka Singida tumeshasaini mkataba, lakini mpaka leo ni kimya; nini kauli ya Serikali kuhusiana na barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kauli ya Serikali kwa barabara hizi zote pamoja na hiyo ya Handeni – Kiberashi – Chemba – Kwa Mtoro ni barabara ambazo zipo kwenye mpango na Serikali kweli tusaini mkataba, tuko kwenye hatua za mwisho za manunuzi. Baada ya wakandarasi hao kuzipitia hizo barabara ili tuweze kuzijenge kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Mheshimiwa Naibu Waziri ulifika Kata ya Soya, Kijiji cha Mbarada na ukakutana na wananchi na wakakueleza kilio chao cha uhaba wa maji, ukawaahidi upatikanaji wa maji haraka iwezekanavyo. Ni lini unapeleka mitambo hiyo Kijiji cha Mbarada ili waweze kupata maji safi na salama kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kunti, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sikosei Kijiji cha Mbarada kiko Wilaya ya Chemba na katika maeneo ambayo tulisikitishwa sana kama Serikali, baada ya kukuta hali ya upatikanaji wa maji ambayo wanayatumia wananchi wa pale yalikuwa mabaya sana, lakini napenda nimpe taarifa kwamba baada ya ile ziara na mpaka sasa, tukimaliza kipindi cha Bunge hapa, naweza nikakuonesha mitambo imeshafika pale na maji tayari wameshaanza kuona namna ambavyo yanatoka. Tunaamini kwamba uchimbaji na usambazaji wa miradi ya maji una hatua, kwanza kupata chanzo, kutengeneza tenki, kujenga mtandao na baadae kutengeneza maeneo ya kuchotea maji. Kwa hiyo, mradi huu utakamilika na wananchi watapata huduma ya maji, ahsante sana.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Hospitali ya Wilaya ya Chemba tuna jengo la mortuary, lakini hatuna majokofu, ni lini Serikali itapeleka majokofu ili kutoa huduma kwa wananchi wanaotumia hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mbunge, nikimaliza kujibu maswali hapa, aje tuwapigie MSD mara moja mimi na yeye ili tuweze kumpa exactly tarehe ngapi hizo fridge za mortuary zinaweza zikafika kwenye Wilaya yake ya Chemba.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Dodoma bado linakumbwa na adha kubwa ya upatikanaji wa maji. Pamoja na jitihada kubwa za DUWASA kuchimba visima Nzuguni lakini maji bado ni shida kwa wakazi wa Dodoma. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuiongezea fedha DUWASA ili iweze kukidhi mahitaji ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Jiji la Dodoma? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua na Serikali inatambua changamoto ya maji. Tunatambua umuhimu wa kuwa na maji ya kutosha kwa wakazi wa Jiji la Dodoma kwa sababu ndiyo Makao Makuu ya Nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mkakati wa muda mfupi wa kuchimba visima vya Nzuguni pamoja na Nala vile vile tuna mpango wa kati na muda mrefu. Juzi hapa tumetangaza tender ya Bwawa la Farkwa ambapo tunaamini kwamba Bwawa hilo likishapata mkandarasi na kuanza kujengwa litatatua. Huo ni mpango wa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imejipanga kuhakikisha kwamba DUWASA inaongezewa nguvu ili iweze kutatua changamoto ambazo zinajitokeza kila mara. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Hivi karibuni kumekuwa na sintofahamu kwenye suala zima la zao la mbaazi. Mheshimiwa Waziri, zao la mbaazi sasa hivi linauzwa shilingi 1,300 mpaka shilingi 1,400; lakini pili, hao wanunuzi wanaonunua hiyo mbaazi nao wamegoma kununua mbaazi kwa sababu wanasema hawana mahali pa kupeleka. Kwa hiyo, wakulima wetu wamebakia stranded, hawajui mbaazi wapeleke wapi, lakini na bei pia hawaelewi ni bei ya namna gani inanunuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini kauli ya Serikali kuhusiana na suala zima la wanunuzi hao? Pili, bei elekezi ni ipi sasa? Serikali inamsaidiaje mkulima kujua bei elekezi ya zao la mbaazi hususan Wilaya ya Chemba na Kondoa?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kunti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kauli ya kwamba hakuna pa kupeleka mbaazi siyo sahihi, ni kauli ambayo inasemwa na madalali ili kuweza kuiangusha bei ya mbaazi. Pili, ni kauli ambayo inasemwa kwa sababu watu hawataki kwenda kwenye Mfumo wa Stakabadhi ya Ghala na kupitia Vyama vya Msingi vya Ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali tumeweka mguu chini, mbaazi, ufuta na mazao tuliyoyatangaza kupitia COPRA ni lazima yauzwe kupitia stakabadhi ya ghala na lazima yauzwe kupitia Vyama vya Msingi vya Ushirika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu nikwambie leo hii sisi kama nchi tayari tumeji-register kupitia TMX kwenye Commodity Exchange Market za dunia. Bei ya mbaazi leo India ni dola 810, hatutarajii kwenye mnada bei ya mbaazi idondoke kati ya shilingi 1,700/=, au shilingi 1,800/= kupitia mnadani. Kwa hiyo, huo ndiyo mwelekeo wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaombe wakulima wa Kondoa, Chemba na maeneo hayo kuwa changamoto hii katika nchi yetu ipo maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni Chemba kwa maana ya Wilaya ya Kondoa yote. Suala la stakabadhi imekuwa ni changamoto...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, kwa kifupi please.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kusukuma ajenda ya Stakabadhi Ghalani kwa sababu kupitia TMX ndiyo inayotusaidia kupata price discovery. Kuna matatizo kwamba wanunuzi wa kati hawataki, lakini ni lazima twende huko. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema watoto wanaoathirika ni kuanzia miaka tisa mpaka 17, watoto hawa wote bado wako shuleni. Ili kuweza kuokoa kizazi hiki, Serikali mko tayari kusitisha michezo hii hususani michezo ya kubahatisha ya bonanza ambayo ndiyo ipo huko kwenye halmashauri zetu na ndiyo hao watoto wadogo wanayoicheza ili kutoa elimu na kwa ajili ya kuokoa kizazi chetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo tayari kulinda maadili ya vijana wetu na siyo tu vijana hata wananchi wake. Tunachomhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, Serikali itaenda kufuatilia na ikijiridhisha kama yanayofanyika yako kinyume na sheria na taratibu, basi Serikali inaweza kuchukua hatua yoyote ambayo inastahiki. Ahsante. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amesema kitu pekee ambacho kitaweza kutusaidia Watanzania kukabiliana na gharama kubwa za matibabu ni Bima ya Afya kwa Wote, lakini mpaka sasa mchakato bado unasuasua, Serikali haioni sasa ni wakati umefika wa kuwasaidia wagonjwa wetu hapa nchini kupunguza gharama ya usafishaji wa figo kutoka shilingi 300,000 mpaka shilingi 50,000? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakupongeza Mheshimiwa Kunti kwa swali hili zuri, lakini ninakuhakikishia dada yangu, wiki hii ulimuona Mheshimiwa Waziri Mkuu akiwa Arusha na aki-launch programu kubwa sana ambayo sasa inaenda kuanza ya kuhakikisha Watanzania wote wanaenda kuingia kwenye Bima ya Afya kwa Wote ambayo ndiyo suluhu kubwa kwa kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba Mheshimiwa Kunti, jinsi ambavyo anajipanga sasa hivi kurudi Bungeni, hivyo hivyo ninakuomba ujipange kuhakikisha wale wanaotakiwa kukurudisha Bungeni, wakati unawaambia nirudisheni Bungeni, basi nguvu hiyo hiyo utumie kuwashauri wakate kadi ya Bima ya Afya. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia siyo tu suala la Bima ya Afya, ninazungumzia ku-access vifaa kutoka viwandani moja kwa moja, itashusha gharama za matibabu. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, kivuko hiki kimetumia muda mrefu sana na wananchi wa Kigamboni na watumiaji wengine wa kivuko hiki wameendelea kupata adha kubwa lakini Serikali imekuwa na ahadi zisizotekelezeka. Mheshimiwa Waziri umesema mwaka 2024 kivuko hiki kinakwenda kukamilika. Ni tarehe ngapi? Kwa sababu suala la miaka imekuwa kila leo mnatupa. Tunataka tarehe ili wananchi hawa waondokane na adha hii, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza ninamkumbusha tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Kigamboni na Dar es Salaam kwa ujumla wake kwamba, ukarabati unaofanyika kwenye MV Magogoni ni kama kukijenga upya, kutokana na ukweli kwamba kivuko kilikuwa kimechoka na tunakileta katika hali ambayo ni mpya kabisa. Ndiyo maana kimeendelea kuchukua muda mrefu ili kuboresha kiwe kivuko cha kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu tarehe ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge; sisi kivuko unaweza ukasema tarehe mbili lakini katika safari ikachukua muda. Tunachotaka kukuhakikishia ni kwamba, kabla ya mwisho wa mwezi Desemba 2024, kivuko kitakuwa kimefika na kuanza kutoa huduma Kigamboni na Dar es Salaam, ahsante. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, Barabara ya Kiberashi – Chemba – Kwa Mtoro mpaka Singida tumeshasaini mkataba, lakini mpaka leo ni kimya; nini kauli ya Serikali kuhusiana na barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kauli ya Serikali kwa barabara hizi zote pamoja na hiyo ya Handeni – Kiberashi – Chemba – Kwa Mtoro ni barabara ambazo zipo kwenye mpango na Serikali kweli tusaini mkataba, tuko kwenye hatua za mwisho za manunuzi. Baada ya wakandarasi hao kuzipitia hizo barabara ili tuweze kuzijenge kwa kiwango cha lami, ahsante.