Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Ridhiwani Jakaya Kikwete (53 total)

MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itayachukua Mashamba Pori yasiyoendelezwa kwa Shughuli iliyokusudiwa yakiwepo Mashamba ya Aghakan, Lucy Estate na Gomba Estate na kuyagawa kwa Wananchi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kama ilivyo ada waliyofanya wenzangu naomba kabla sijajibu swali nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kunichagua mimi na mwenzangu Mheshimiwa Dkt. Angelina Mabula kuwa katika Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; ahadi yangu kwake na kwa viongozi wote wa juu yetu ni kwamba hatutowaangusha tutafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kwa ruhusa yako nijibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu Mbunge wa Arumeru Magharibi kama ifuatavyo. Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi, Sura ya 113, hatua za ubatilishaji wa milki nchini hutekelezwa ikiwa mmiliki wa shamba au kiwanja amekiuka masharti ya umiliki yaliyoainishwa kisheria.

Mheshimiwa Spika, Shamba la Agakhan kwa sasa lipo ndani ya eneo la mpangomji ambalo limeingizwa kwenye Mpango Kabambe wa uendelezaji wa Jiji la Arusha. Kwa kuzingatia mpango huo, eneo la shamba hilo limepangwa kuendelezwa kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo Kikuu, eneo la biashara na makazi. Mmiliki wa eneo hilo alipaswa kuendeleza kwa kuzingatia mpango huo. Kutokana na kubadilika kwa mpango wa matumizi ya eneo hilo, Serikali ipo katika mazungumzo na mmiliki ili kuona namna bora ya kutekeleza mpango huo.

Mheshimiwa Spika, shamba la Gomba Estate ni miongoni mwa mashamba ambayo wamiliki walichukua mikopo na kushindwa kurejesha kwa hiyo shamba hilo kwa sasa lipo chini ya uangalizi wa taasisi ya benki ya Standard Chartered na Shirika la NSSSF. Ili kutatua changamoto ya urejeshaji wa mkopo, Serikali kwa kushirikiana na wamiliki na taasisi tajwa imeanza zoezi la kupanga, kupima ardhi husika ili kupata viwanja vitakavyouzwa ili mkakati wa kurejesha mkopo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu shamba la Lucy Estate, miliki ya shamba husika ilibatilishwa mwaka 1999 kutokana na kukiukwa kwa masharti ya umiliki. Hata hivyo, mmiliki wa shamba hakukubaliana na hatua hiyo na hivyo alifungua shauri Na. 50/2015 katika Mahakama Kuu ya Arusha dhidi ya Serikali kupinga ufutaji huo. Baada ya majadiliano ya kisheria, ilikubaliwa kwamba aliyekuwa mmiliki alipwe fidia ya maendelezo yaliyokuwepo. Hivyo, Serikali inaandaa mpango wa matumizi wa shamba hilo kwa ajili ya matumizi mbalimbali na sehemu ya shamba husika itatumika kupata fedha kwa ajili ya fidia.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, ni lini wananchi wa Kata ya Makurunge watapatiwa eneo la makazi la Razaba baada ya maeneo yao kuchukuliwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 147 la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wakati eneo hili linachukuliwa na Serikali kwa ajili ya uwekezaji wananchi waliokuwa wakazi wa eneo hilo walilipwa fidia stahiki kwa mujibu wa sheria. Aidha, tunatambua uwepo wa wananchi 16 ambao wamekuwa wakidai kulipwa fidia zao, Serikali inaendelea kushughulikia madai hayo na yatakapokuwa tayari tutawapa taarifa.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani kwa wananchi wa Kata ya Majengo Tunduma waliovunjiwa nyumba zao?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 133 lililoulizwa na Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba kabla sijajibu swali nitoe maelezo machache ya utangulizi. Kikao cha Makatibu Wakuu wa Nchi za Tanzania na Zambia kilichofanyika mwezi Oktoba, 2013, pamoja na mambo mengine kiliazimia kwamba alama za katikati ya mpaka (Intermediate Boundary Pillars) kwa sehemu ya mpaka yenye urefu wa kilomita 50 ziongezwe ili kuzuia ongezeko la shughuli za kibinadamu na pia eneo la hifadhi ya mpaka lipunguzwe kutoka mita 100 kila upande zilizokuwa zinatambulika hapo awali hadi mita 50 kila upande. Hata hivyo, pamoja na maazimio hayo kutekelezwa, baadhi ya wananchi waliendelea kuvamia eneo la hifadhi ya mipaka kwa kujenga makazi.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017, Serikali ilitoa tamko la kuvunja nyumba zote zilizojengwa katika eneo la hifadhi ya mpaka suala ambalo lilipingwa na wananchi 134 kwa kufungua Shauri Na. 195/2017 katika Mahakama Kuu, Mbeya. Shauri hilo lilifutwa mwaka 2019 na hatimaye jumla ya nyumba 193 zilizokuwa ndani ya eneo la mita 50 za hifadhi ya mpaka zilibomolewa.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua hiyo, wananchi 35 walifungua tena shauri Na. 12/2019 katika Mahakama Kuu Mbeya kudai fidia kutokana na kubomolewa kwa nyumba zao. Baada ya mazungumzo nje ya Mahakama (mediation) yenye lengo la kuwapatia viwanja mbadala, wananchi hao kushindikana, shauri hilo limepangwa kuendelea kusikilizwa tarehe 5 Oktoba, 2022.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua shauri hilo na kauli yetu ni kwamba tusubiri mwongozo au maamuzi ya mahakama ili tujue hatua zinazofuatia.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kurekebisha ramani ya nchi yetu baada ya baadhi ya maeneo kujazwa mchanga kuongeza ukubwa wa ardhi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali namba 80 la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali la msingi la Mheshimiwa Mbunge, napenda kutoa maelezo mafupi kuwa, ukubwa wa eneo na mipaka ya nchi unajulikana na ipo bayana. Hivyo kujazwa mchanga kwenye baadhi ya maeneo hakuongezi wala kupunguza ukubwa wa eneo la nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ramani ya nchi inaonesha sura ya nchi huandaliwa ili kuonyesha hali halisi iliyopo ardhini ikijumuisha taarifa za kijiografia za asili ambazo ni pamoja na mito, maziwa, milima na bahari; na zile zisizo za asili ambazo zinazojumuisha barabara, reli, mabwawa na miji. Moja ya sababu ya kuhuisha ramani ni kuonesha uhalisia wa sura ya nchi na kuhakikisha kuwa mabadiliko yanayotokea katika ardhi yanaoneshwa kwenye ramani mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ina mpango wa kuandaa ramani mpya nchi nzima zinazoonesha sura ya nchi Tanzania Bara. Ramani hizo zitaandaliwa kupita mipaka kupitia Mradi wa Kuimarisha Miundombinu ya Upimaji na Ramani (Project for Improvement of National Land Data Infrastructure) utakaotekelezwa kwa mkopo utakaotolewa na Serikali ya Korea kwa muda wa miaka minne (2022/23 -2025/2026).
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, Serikali ipo tayari kufanya mapitio ya upimaji wa vijiji nchini kwa kuwa migogoro mingi imesababishwa na upimaji usio shirikishi wa mwaka 1970?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kabla ya kujibu swali lake la msingi kuwa kilichofanyika katika miaka ya 1970 haikuwa upimaji wa vijiji bali ilikuwa ni Operesheni Maalum ya Serikali ya kuanzisha Vijiji vya Ujamaa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya 2000 Serikali ilitekeleza Programu ya upimaji wa vijiji kwa lengo la kuvifanya vijiji kuwa mamlaka kamili za usimamzi wa ardhi za vijiji. Mathalani, katika Mkoa wa Lindi jumla ya vijijii 401 kati ya vijiji 523 vikiwemo Vijiji vya Wilaya ya Liwale vilipimwa kwa njia shirikishi na kuwekewa alama za mipaka.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua migogoro ya wakulima na wafugaji katika Jimbo la Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa changamoto mbalimbali zinazosabisha migogoro ya matumizi ya ardhi ikiwemo hiyo ya wakulima na wafugaji. Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha migogoro ya matumizi ya ardhi katika Mkoa wa Morogoro hususan Wilaya ya Kilombero inatatuliwa.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kumilikisha ardhi kupitia Mradi wa Kuwezesha Umilikishaji wa Ardhi (LTSP) ambapo jumla ya vijiji 58 viliandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi na Hakimiliki za Kimila 150,006 zilisajiliwa. Kati ya vijiji hivyo 58, vijiji 32 vipo katika Halmashauri ya Mlimba ambapo jumla ya Hakimiliki za Kimila 41,797 zimesajiliwa na 30,699 zimechukuliwa na wananchi.

Mheshimiwa Spika, nasisitiza Serikali za Halmashauri kuhakikisha zinasimamia mipango ya matumizi ya ardhi iliyoandaliwa ili kupunguza uwezekano wa kuibuka au kuendelea kwa migogoro baina ya watumiaji wa ardhi.

Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni kudhibiti na kuimarisha mbinu za utatuzi wa migogoro kwa kutoa elimu kupitia mikutano ya wananchi kuhusu mipango ya matumizi ya ardhi iliyowekwa kwa pamoja, kutungwa kwa Kanuni za Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi na kuhimiza matumizi ya ardhi yenye tija.

Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara kwa kushirikiana na Wizara nyingine za kisekta zitaendelea kudhibiti na kushughulikia migogoro na kuitafutia ufumbuzi iliyopo ili kuimarisha ustawi wa jamii baina ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kutatua migogoro ya ardhi kati ya Wananchi na Wawekezaji wenye mashamba makubwa Kibaha Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendelo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 17 la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua jitihada za kutatua migogoro ya ardhi kati ya wananchi na wawekezaji katika maeneo mbalimbali hususan katika Jimbo la Kibaha Vijijini. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kufanya ukaguzi wa ardhi iliyomikishwa kwa wawekezaji ili kubaini iwapo masharti ya umiliki yanazingatiwa.

Pili, kuchukua hatua za ubatilisho kwa wawekezaji waliobainika kukiuka masharti ya uwezekezaji; na Tatu, kupanga upya ardhi iliyobatilishwa kwa kushirikiana na Mamlaka za Upangaji kulingana na mahitaji halisi ya sasa hususan hazina ya ardhi, huduma za kijamii na makazi. Aidha, Wizara inaendelea kutoa elimu kwa jamii na wawekezaji kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na miongozo ya sekta ya ardhi ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani juu ya mashamba makubwa yanayomilikiwa na wawekezaji na hayatumiki kuzalisha mali na ajira nchini?
NAIBU WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa yapo mashamba makubwa nchini ambayo yamegawiwa kwa wawekezaji ambapo baadhi ya mashamba hayo yanatumika kwa uzalishaji mali na ajira na mengine hayatumiki kama ilivyokusudiwa. Wizara kwa kushirikiana na taasisi nyingine imeanza kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji kwa kufanya ukaguzi na kuainisha changamoto zilizopo.

Mheshimiwa Spika, hatua inayofuata ni kufanya majadiliano na wawekezaji waliobainika kuwa na changamoto ili kuzipatia ufumbuzi kwa pamoja kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji. Kwa mashamba ambayo yametelekezwa, Wizara imeendelea kuchukua hatua za kisheria kwa wamiliki walioshindwa kutekeleza masharti ya uwekezaji ikiwemo kuyarudisha na kuyapangia matumizi upya kwa manufaa ya umma.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza migogoro ya Wafugaji na Wakulima katika Wilaya za Liwale, Nachingwea na Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa Niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kumjibu swali lake Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Mkoa wa Lindi Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa migogoro ya ardhi katika Wilaya zote zilizotajwa ikiwemo Liwale, Nachingwea na Kilwa, lakini pia ni pamoja na maeneo ya Lindi Vijijini. Migogoro hii inatokana na kuongezeka kwa mifugo katika maeneo hayo, changamoto ya tafsiri ya mipaka ya ardhi katika vijiji hivyo, usimamizi mbovu wa mipango ya matumizi ya ardhi. Kwa kutambua hilo, Serikali imeendelea kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ambayo kimsingi ndiyo suluhisho la migogoro ya mwingiliano baina ya watumiaji wa ardhi. Hadi sasa jumla ya vijiji 114 katika Wilaya ya Kilwa, Nachingwea na Liwale vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2204, Serikali imepanga kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 40 ikiwemo Liwale (17), Nachingwea (12) na Kilwa (11) katika Mkoani wa Lindi, ahsante.
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -

Je, nini kauli ya Serikali kuhusu majengo yaliyopo maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam ambayo ujenzi wake umesimama kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 45 lililoulizwa na Mheshimiwa Tarimba Abbas Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Serikali ni kwamba majengo yote yaliyosimama yaendelezwe kwa kikamilifu kama ilivyoainishwa kwenye milki zao na vibali vya ujenzi ili majengo hayo yasitumike kwa matumizi yasiyofaa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: -

Je, Serikali ina kauli gani juu ya maeneo ya ardhi yanayotumika na Serikali au Taasisi zaidi ya miaka 12 yakiwa hayana hatimiliki?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Na. 62 lililoulizwa na Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa maeneo mengi yanayomilikiwa na Taasisi za Umma yana hatimiliki. Hata hivyo, Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa maelekezo kwa Taasisi na Idara za Umma kuhakikisha maeneo yao yanapangwa, kupimwa na kupatiwa hatimiliki.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua migogoro ya Wakulima na Wafugaji Kata za Hembeti, Mkindo, Sungaji, Mtibwa, Kanga, Mziha na Doma?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali Na. 63 la Mbunge wa Mvomero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa migogoro ya wakulima na wafugaji katika Kata za Hembeti, Mkindo, Sungaji, Mtibwa, Kanga, Mziha na Doma Wilayani Mvomero. Kwa kutambua hilo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo hatua ya mwaka 2013 ya kutenga kwa kutumia fedha za ndani kwenda kutatua migogoro katika jumla ya vijiji 72 kati ya vijiji 130 vilivyomo katika Wilaya hiyo ambavyo vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kurasimisha, kupanga na kupima ardhi katika Miji Midogo ya Mawengi, Lugarawa, Luilo na Manda – Ludewa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Na. 89 lililoulizwa na Mheshimiwa Joseph Kamonga, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Wizara kupitia Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi iliikopesha Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kiasi cha shilingi milioni 405 kwa lengo la kupanga na kupima na kurasimisha miji midogo ya Mlangali, Mavanga, Ludewa na Mudindi ambapo jumla ya viwanja 7,911 vimepangwa na viwanja vingine 2,120 vimekamilika katika utaratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa maelekezo wataalamu wa ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kuanza kukusanya takwimu muhimu kwa ajili ya kupanga na kupima katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja.
MHE. NANCY H. NYALUSI K.n.y. MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itarudisha Shamba la Kijiji cha Ng’ang’ange kwa wananchi kufuatia mauziano kati ya EFATHA na Kijiji kutofuata sheria?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2003 Taasisi ya Efatha Ministry iliomba eneo lenye ukubwa wa ekari 200 katika Kijiji cha Ng'anga'nge kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi, Kilimo na Mifugo. Taratibu zote za utoaji eneo husika zilifuatwa ikiwemo Kikao cha Halmashauri ya Kijiji, Mkutano Mkuu wa Kijiji na Kamati ya kugawa ardhi ya Wilaya pamoja na fidia za mali zililipwa.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, ni lini maeneo mengi ya Mji wa Lushoto yatapimwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, halmashauri ni mamlaka ya upangaji kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007, hivyo majukumu ya kisheria ya kutenga bajeti, kwa ajili ya kupanga na kupima yapo ndani yao. Hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetoa mkopo wenye thamani ya shilingi bilioni 55.6 kwa halmashauri 55, Vyuo vya Ardhi vya Tabora na Morogoro na Chuo Kikuu Ardhi Dar es Salaam, kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ni miongoni mwa halmashauri zilizokopeshwa fedha hizo ambapo jumla ya shilingi milioni 208 zimetolewa kwa ajili ya kupima viwanja takriban 2,600 katika maeneo ya Lushoto Mjini, Mnazi, Mlola, Mlalo na Lukozi. Pamoja na jitihada hizi za Serikali, natoa rai kwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na Halmashuri zote nchini kuhakikisha kuwa zinatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -

Je, Serikali inachukua hatua gani kwa viongozi wanaowanyima wananchi kwa makusudi haki yao ya kuwa wanufaika wa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali namba 18 lililoulizwa na Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji naomba kutumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini. Nataka nimwakikishie yeye na watanzania wote kwamba tutaendelea kufanya kazi na kazi itaendelea.

Mheshimiwa Spika, Sasa, kwa niaba ya Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji Mbunge wa Mwera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, zoezi la utambuzi wa wanufaika wa TASAF ni zoezi shirikishi na hujumuisha Wataalam kutoka Halmashauri, Maafisa wa TASAF, Wananchi wa maeneo husika yanayosimamiwa na viongozi wa vijiji/mitaa/shehia.

Mheshimiwa Spika, inapotokea kiongozi au viongozi wamewanyima haki wananchi kwa makusudi bila sababu yoyote ile hatua zifuatazo huchukuliwa dhidi yao: -

(a) Endapo uongozi wa vijiji/mitaa/shehia utashinikiza kuondoa majina ya kaya kwenye orodha ya utambuzi bila kuafikiwa na jamii, zoezi la utambuzi husitishwa na taarifa hupelekwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri/Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Zanzibar) na nakala hupelekwa kwa Mkurugenzi wa TASAF.

(b) Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri/Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Zanzibar) huchunguza tuhuma hizo na ikithibitisha tuhuma hizo mhusika husitishwa kujihusisha na shughuli zozote za Mpango wa TASAF. Aidha, baada ya kusimamishwa, mhusika huchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kupewa karipio au kuondolewa kwenye nafasi yake.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzisaidia Kibajeti Taasisi za Wenza wa Viongozi Wakuu wa nchi ili ziweze kujiendesha na kupata ufadhili?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ta Utumishi wa Umma na Utawala Bora naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakar Damian Asenga Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria za nchi, taasisi za wenza wa viongozi wakuu wa nchi zinasajiliwa na kuendeshwa kwa taratibu zinazotumika kusajili na kuendesha taasisi nyingine binafsi na zisizo za Kiserikali. Hadi sasa Serikali haina mwongozo wa kisheria au kikanuni unaoielekeza kutoa usaidizi wa kibajeti kwa taasisi za wenza wa viongozi wakuu wa nchi.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya upungufu wa Watumishi katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Menejementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Mariki, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Katavi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi wa Mkoa wa Katavi kila mwaka kwa kuendelea kutenga Ikama na Bajeti kama inavyopitishwa na Bunge lako. Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali ilitenga nafasi 522 za kada mbalimbali kwa Mkoa wa Katavi na katika mwaka wa fedha ujao (2023/2024) tunakusudia kutenga Ikama ya ajira mpya 914 kwa Mkoa wa Katavi iwapo Bunge lako likiridhia na kuipitisha Bajeti ya Serikali iliyopendekezwa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaajiri watumishi wa kada ya ulinzi, upishi na makatibu muhtasi katika shule za sekondari za kata nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, naomba kujibu swali namba 82 lilliloulizwa na Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa ajira kila mwaka. Kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga nafasi 201 za Makatibu Muhtasi na tano za Wapishi. Watumishi husika wataajiriwa kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha. Aidha, kwa katika Kifungu cha 6(1) cha Sura ya 298 cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Toleo la 2019, Waajiri mbalimbali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa hutenga bajeti kwa kuzingatia kada na maeneo yote ya vipaumbele ikiwemo Walinzi, Wapishi na Makatibu Muhtasi na kuwapanga katika maeneo yenye uhitaji ikiwemo shule za sekondari za kata nchini.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutimiza masharti ya ajira kwa Watumishi ikiwemo kuwapandisha madaraja na stahiki zingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutekeleza matakwa ya kisera, kisheria na miongozo mbalimbali ya kiutawala na kiutumishi inayolenga au inayoelekeza Serikali katika kumtimizia masharti na haki za mtumishi wake. Aidha katika kufanya hivyo Serikali imeendelea na Utaratibu wa kupandisha madaraja watumishi ikiwemo utaratibu wa mpandisho wa mserereko. Pamoja na hilo Serikali imeendelea pia kuongeza kima cha chini cha mshahara na pia kuongeza allowance katika kazi za ziada na posho za muda wa ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hilo pia mwaka 2021/2022, Serikali ililipa shilingi bilioni 124.3 kwa watumishi 75,007 ikiwa ni malimbikizo (arrears) ya mishahara. Vilevile, Serikali iliongeza umri wa watoto wa watumishi wa umma kunufaika na huduma ya bima kutoka miaka 18 hadi miaka 21 ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja jumla ya watoto 65,353 wamesajiliwa.
MHE. AMINA DAUD HASSAN aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kufuatilia miradi ya TASAF iliyokamilika ili kuhakiki uendelevu wake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Daud Hassan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ili kuhakikisha kuwa miradi ya TASAF inakuwa endelevu, jamii huunda kamati ya matunzo na ukarabati ambayo jukumu lake ni kuweka sheria na taratibu za kusimamia matunzo na kuendeleza miradi hiyo. Mradi unapokamilika hubaki chini ya uangalizi wa wataalamu na TASAF wakishirikana na Halmashauri husika kwa kipindi cha miezi sita na baadaye mradi huo hukabidhiwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri husika ambayo huendelea na jukumu la usimamizi, uendeshaji na matengenezo kwa kushirikiana na idara au taasisi inayohusika na miradi hiyo.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, kwa nini wanufaika wa TASAF wasilipwe mkononi badala ya kupewa kwa njia ya simu na benki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu Swali lililoulizwa na Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwaka 2019 Serikali ilifanya majaribio ya mfumo wa kieletroniki wa malipo kwa walengwa katika mamlaka za utekelezaji 19. Baada ya majaribio, mwaka 2020 mfumo wa malipo kwa njia ya kielektroniki ulipitishwa rasmi na walengwa kuanza kutumia mfumo huo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inakiri kutokea changamoto katika baadhi ya maeneo ya utekelezaji. Hivyo utaratibu wa malipo kwa sasa upo katika njia tatu; kwa njia ya simu, akaunti ya benki na njia ya malipo ya fedha taslimu.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huu ni uchaguzi wa mnufaika mwenyewe atumie njia gani kadri ya mazingira yake. Aidha, naomba kutoa rai kwa Mheshimiwa Mbunge tusaidiane kuelimisha walengwa juu ya njia hizi kuu tatu za malipo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafufua upya Tume ya Taifa ya Mipango?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali namba 138 lililoulizwa na Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya Muswada wa Sheria kuanzisha Tume ya Mipango. Muswada huu unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni katika Mkutano huu wa Kumi na Moja wa Bunge lako unaoendelea sasa. Muswada wa Sheria ukipitishwa Bungeni, Tume ya Mipango inatarajiwa kuanza shughuli zake katika mwaka wa fedha 2023/2024 yaani tarehe 1 Julai, 2023.
MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana wanaojitolea kutumikia katika kada mbalimbali za utumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, naomba kujibu Swali Na. 239, lililoulizwa na Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali iliweka mazingira ya kuwawezesha vijana wanaohitimu katika vyuo mbalimbali kujitolea katika Taasisi za Umma kwa lengo la kuwawezesha kujipatia sifa za ziada zitakazowawezesha katika ushindani pindi nafasi mbalimbali za ajira zinapotangazwa. Hata hivyo, kwa mujibu wa Kifungu Na. 2.1.2 cha Sera ya Menejimenti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la Pili la Mwaka 2008 na Kanuni D. 6 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 ikisomwa pamoja na Kanuni Namba 12(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022, ajira kwa nafasi zilizo wazi katika Utumishi wa Umma hujazwa kwa ushindani na uwazi kwa kufanya usaili na kupata washindi katika nafasi husika.

Mheshimiwa Spika, hivyo, nitumie nafasi hii kuwashauri na kuwahamasisha vijana wanaojitolea katika kada mbalimbali za utumishi wenye sifa stahiki, kuomba nafasi za kazi pindi zitakapotangazwa ili waweze kushindana na waombaji wengine wenye sifa stahiki.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, ni watumishi wangapi wa umma wamefikishwa Mahakamani kwa rushwa, wangapi wameshinda kesi na kurejeshwa kazini kwa kipindi cha 2010 – 2020?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2010 mpaka 2020, jumla ya Watumishi 2,060 walifikishwa Mahakamani na kushtakiwa kwa makosa mbalimbali ya rushwa. Kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 ya Sheria za Tanzania. Kati ya watumishi hao 2,060 walioshtakiwa, watumishi 1,157 walitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu mbalimbali kwa mujibu wa sheria, huku watumishi 863 wakishinda kesi na kuachiwa huru waendelee na kazi.
MHE. JANEJELLY J. NTATE aliuliza: -

Je, lini Serikali itarekebisha Sheria za Utumishi zilizopitwa na wakati hasa kipindi hiki cha teknolojia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, naomba uniruhusu nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini kuendelea kudumu katika Wizara hii ya Utumishi na Utawala Bora. Sasa naomba kujibi swali la Janejelly James Ntate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa maendeleo makubwa ya kiteknolojia ambayo yamekuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha utendaji kazi katika utumishi wa Umma. Ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia, Serikali imeendelea kufanya mapitio ya Mfumo wa Kisheria unaosimamia Utumishi wa Umma ambapo mwaka 2019 Serikali ilitunga Sheria ya Mamlaka ya Serikali Mtandao Namba10 ya Mwaka 2019 ili kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya teknolojia katika utendaji kazi wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitishwa kwa Sheria hiyo kumeisaidia Serikali kuboresha utendaji kazi wake kupitia matumizi ya teknolojia. Pamoja na mambo mengine Sheria hiyo imewezesha kusanifiwa na kujengwa kwa jumla ya mifumo zaidi ya 860 ya TEHAMA Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na hatua za kupitia na kufanya marekebisho ya Sheria mbalimbali zinazosimamia Utumishi wa Umma na Kanuni zake ili kuhakikisha kwamba zinaendana na mabadiliko ya teknolojia.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -

Je, lini Serikali italeta marekebisho ya Sheria ya Ajira ya Utumishi wa Umma kuongeza kigezo cha kujitolea ili kutoa fursa kwa wanaojitolea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Olelekaita Kisau, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa inafanya mapitio ya Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura Na. 298, Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la Pili la mwaka 2008, Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 na Miongozo inayohusu masuala mbalimbali likiwemo suala la ajira.

Mheshimiwa Spika, endapo itabainika bayana kigezo cha kujitolea kitatakiwa kuingizwa katika marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma, Serikali italeta Marekebisho ya Muswada wa Sheria Bungeni kwako. Kwa sasa Serikali imeandaa mwongozo unaoweka mazingira wezeshi kwa vijana wanaohitimu katika vyuo mbalimbali kujitolea katika Taasisi za Umma kwa lengo la kuwawezesha kujipatia uzoefu utakaomuwezesha katika ushindani pindi nafasi mbalimbali zitakapotangazwa.

Mheshimiwa Spika, mwongozo huu unalenga kuziba ombwe lililopo kutokana na kutokuwa na utaratibu mmoja ndani ya Taasisi za Umma kuhusu kujitolea.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa semina elekezi kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya mara kwa mara kuhusu utawala bora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa mafunzo elekezi kwa viongozi wa ngazi mbalimbali katika kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeendelea kutoa semina elekezi kwa viongozi wanaoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Katika kipindi cha mwezi Februari hadi Agosti, 2023, Serikali ilitoa mafunzo elekezi kwa viongozi wa ngazi ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya ambapo agenda moja wapo ilikuwa ni ya utawala bora.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Je, kwa nini Serikali inaajiri kwa kigezo cha mwaka wa kumaliza chuo na kupitia mafunzo ya jeshi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kutoa ajira kwa kada mbalimbali zinazohitajika katika Utumishi wa Umma, Serikali imekuwa ikizingatia Sera ya Menejimenti ya Ajira na Utumishi wa Umma Toleo la 2 la mwaka 2008 aya ya 4.2 ambayo inataka zoezi la ajira katika Utumishi wa Umma liendeshwe kwa wazi na ushindani ili kuwezesha Serikali kupata watumishi wenye utaalam na sifa stahiki kwa kuzingatia uwezo, weledi na umahiri wa waombaji fursa za ajira.

Mheshimiwa Spika, ili kuleta ushindani katika soko la ajira, vigezo mbalimbali hutumika kuzingatia mazingira maalum au mazingira mahsusi ya waajiri. Katika vyombo vya Ulinzi na Usalama na Taasisi zilizoingia katika mfumo wa Jeshi USU kutokana masharti ya kazi hizo na mahitaji maalum au mahsusi ya vyombo husika, ajira zinazotolewa kwa kigezo cha ukomo wa umri na kigezo cha kupitia Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, kada nyingine katika Taasisi za Umma nje ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Taasisi zenye mfumo wa Jeshi USU kigezo cha Kupitia Mafunzo ya Jeshi hakitumiki. Hata hivyo, waombaji wa fursa za Ajira Serikalini kwa masharti ya kudumu Serikali wanatakiwa kuzingatia Kanuni ya D. 39 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 ambayo inawataka wasiwe na umri usiopungua miaka 18 na wasiozidi umri wa miaka 45 kwa lengo la kuwawezesha kuchangia katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii walau kwa miaka 15 ili kustahili kulipwa pensheni.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaweka wazi vigezo vya kubaini kaya maskini zinazostahili kupokea msaada wa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kumjibu Mheshimiwa Injinia Mwanaisha Ng’azi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalam, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, vigezo vya utambuzi wa kaya za walengwa viko wazi na vinatambulika. Vigezo hivyo ni kama ifuatavyo ili kuweka record sawa katika Bunge lako:-

(i) Kaya ambazo hazina uwezo wa kupata kwa uhakika angalau milo miwili kwa siku;

(ii) Kaya isiyo na kipato cha uhakika na inayo wategemezi wengi wakiwemo watoto wanaokosa huduma za elimu na afya;

(iii) Kaya zinazoishi kwenye makazi duni yanayohatarisha usalama wa kaya;

(iv) Wazee wasio na msaada wowote;

(v) Watoto wanaoishi wenyewe bila wazazi au walezi.

Mheshimiwa Spika, vigezo hivi ndivyo vimewezesha Serikali kuweza kuhudumia kaya za walengwa 1,378,000 ambao wanaendelea kunufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF).
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:-

Je, kwa nini viongozi wastaafu wa vitongoji na vijiji wenye sifa siyo wanufaika wa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa uratibu wa awamu ya kwanza ya mpango wa kunusuru walengwa wa kaya maskini ulipoanza, taratibu zilibainisha kuondoa baadhi ya makundi wakiwemo watumishi wastaafu wanaopokea pensheni, watu walioajiriwa na kuwa na kipato cha uhakika, Viongozi wa Vijiji na Wajumbe wa Kamati za Usimamizi za Jamii miongoni mwao ni Viongozi wa CCM katika ngazi za Kata na vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia maboresho ya taratibu za utambuzi na uandikishaji wa walengwa ya mwaka 2021, Kaya za Viongozi wa kisiasa wakiwemo Mabalozi wa Nyumba Kumi na Viongozi waliopo na wastaafu wa vijiji na vitongoji zinazokidhi vigezo zilipewa fursa ya kutambuliwa na kuandikishwa kwenye mpango huo wakati wa zoezi la utambuzi na uandikishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa viongozi wastaafu wa vijiji na vitongoji ambao kipindi cha zoezi la utambuzi wa walengwa linafanyika walikubalika na jamii kuorodheshwa awali kuwa katika kaya maskini wajiandishe ili nao waweze kuingia katika mpango huo.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-

Je, Serikali ipo tayari kuwapandisha vyeo kwa mserereko kufikia daraja wanalostahili watumishi waliosubiri zaidi ya miaka 8 Kyerwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, upandishwaji vyeo kwa mserereko ni utaratibu unaotumika kuwapandisha vyeo watumishi ambao imethibitika kuwa walicheleweshwa kupandishwa vyeo kwa wakati kwa kuzingatia miongozo ya upandishaji vyeo iliyopo, uwepo wa nafasi iliyoidhinishwa katika Ikama na uwepo wa fedha za kugharamia upandishwaji vyeo kwenye bajeti, sifa za kielimu na kitaaluma na utendaji kazi mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi wa maelezo hayo, Serikali itakuwa tayari kuwapandisha vyeo kwa mserereko watumishi waliotajwa na Mheshimiwa Mbunge endapo itathibitika kuwa wana sifa zilizoainishwa.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA K.n.y. MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza siku za likizo kwa wazazi wanaojifungua watoto njiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa likizo ya uzazi kwa watumishi kwa mujibu wa Kanuni H12 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2009 ambapo pamoja na Kanuni Pili ya Kanuni ya 12 inabainisha kuwa muda wa likizo ya uzazi kwa mtumishi mwanamke ni siku 84 ambazo hutolewa mara moja katika kipindi cha miaka mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuongeza siku za likizo pale mtumishi anapojifungua mtoto njiti, suala hili halijawekewa utaratibu wa kikanuni kutokana na taratibu wa uendeshaji wa shughuli za Serikali. Hivyo, Mtumishi (Mzazi) anaweza kuomba ruhusa ya kawaida kutoka kwa Mwajiri wake inapotokea changamoto kama hiyo.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -

Je, utaratibu gani unatumika kutangaza ajira nchini ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata haki ya kupata taarifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, swali namba 722, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti ya Ajira Toleo Na. 2 la mwaka 2008, Sura ya Nne, Aya ya 4(2) ikisomwa pamoja na ya Kanuni 12(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, nafasi za ajira katika Utumishi wa Umma ni za ushindani na zinazingatia sifa, taaluma, uwazi na usawa.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, matangazo ya ajira kwa ajili ya kujaza nafasi wazi ndani ya Utumishi wa Umma hutolewa kupitia tovuti za taasisi husika, mitandao ya jamii, magazeti na mbao za matangazo katika ofisi husika. Maombi ya nafasi hizi hudumu kwa muda wa siku kumi na nne 14 kwa kada za masharti ya kawaida na siku 21 kwa waombaji wa nafasi za Watendaji Wakuu na nafasi za Uongozi za Taasisi za Kimkakati.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: -

Je, nyumba bora ya kuishi inatakiwa kuwa na sifa zipi na ni kwa nini Serikali haiweki ruzuku kwenye vifaa vya ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kumjibu Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge na Chifu wa Wakonongo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba ni mojawapo ya mahitaji muhimu ya mwanadamu. Nyumba bora ni ile yenye huduma bora kwa usalama na afya kwa wakazi wake. Jitihada za Serikali kuhakikisha nyumba bora zinajengwa kwa gharama nafuu ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya uanzishwaji wa viwanda vya kuzalisha vifaa vya ujenzi, kufanya utafiti na kuwezesha matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kazi za ujenzi na kuhamasisha taasisi za fedha kutoa mikopo kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na ununuzi wa nyumba.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: -

Je, Serikali inatoa tamko gani kwa waajiri wanaowanyima safari watumishi wanaonyonyesha kwa kigezo cha kutumia fedha nyingi kujikimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2008 aya ya 5(1) ikisomwa pamoja na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 zinaelekeza watumishi wanaosafiri safari za kikazi wakiwemo wanaonyonyesha kupewe posho ya kujikimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo, Serikali inaelekeza tena na kusisitiza kwa waajiri wote wa watumishi wa umma kuwa watumishi wa umma wahudumiwe kwa usawa na haki kwa kuzingatia sera na kanuni zilizopo. (Makofi)
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuwapa Likizo ya uzazi zaidi ya siku 120 wanaojifungua watoto njiti ili kuwa na muda wa kutosha kuwatunza watoto hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa tuwatendee haki Wananchi wa Shinyanga waliyomchagua Mbunge Santiel Eric Kirumba, kwa kujibu swali Na. 176 kama lilivyoelekezwa kwenye Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali Na. 176 lililoulizwa na Mheshimiwa Santiel Eric Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Utumishi wa Umma, likizo ni miongoni mwa haki za watumishi wa umma ambazo wanastahili kupewa na waajiri wao kwa mujibu wa Kanuni H.12 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma mwaka 2009, kanuni hiyo ikisomwa pamoja na Kanuni ya 97 ya Kanuni ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la likizo ya mtumishi aliyejifungua mtoto njiti halijaelezwa bayana katika Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma. Hata hivyo, kwa mujibu wa Kanuni ya 135 ya Kanuni ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2022, linapotokea suala ambalo halikuelezwa bayana katika Kanuni ya Utumishi wa Umma, mtumishi atamtaarifu mwajiri kuhusu suala hilo. Mwajiri anaweza kutumia busara kulitatua pale inapobidi na anaweza kutumia sheria nyingine au kushauriana na Katibu Mkuu Utumishi kwa ufafanuzi wa suala hilo ikiwemo nyongeza ya siku katika likizo.
MHE. CHARLES M. KAJEGE aliuliza:-

Je, kwa nini Serikali imewaacha wananchi wengi wenye sifa na vigezo vya kunufaika na TASAF katika Jimbo la Mwibara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles Muguta Kajege, Mbunge wa Jimbo la Mwibara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mwibara lipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na lina jumla ya walengwa 5,320 ambao walipatikana kwa mujibu wa taratibu zinazotumika kuwapata Walengwa. Taratibu hizi zinatoa nafasi kupitia Mkutano Mkuu wa Kijiji au Mtaa au Shehia ambapo wananchi wenyewe wanapata nafasi kupendekeza, kuchuja na kuamua juu ya nani wawepo kwenye mpango kwa mujibu wa Mwongozo wa Utambuzi wa Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Toleo la mwaka 2019 na marejeo yake ya mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, iwapo bado kuna wananchi walipendekezwa kuwa wanufaika ila hawakuingia kwenye mpango, wawasilishe rufaa kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na rufaa hizo zitaletwa kwenye Ofisi za TASAF Makao Makuu kwa ajili ya mapitio.
MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza: -

Je, Serikali haioni kigezo cha uzoefu katika kuomba kazi ni ubaguzi dhidi ya vijana waliohitimu vyuo wanaolenga kuingia katika soko la ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, naomba kujibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Ajira za Serikali zinatekelezwa kwa kuzingatia Sera ya Menejimenti na Ajira ya mwaka 2008. Kwa mujibu wa Aya ya 4.2(i) ya Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma inaelekeza kuwa Ajira kwa mara ya kwanza (entry point) hususan kwa wale wanaoajiriwa kwa cheo cha kuanzia kwenye miundo itafanyika kwa kuzingatia vigezo vya utaalam bila kujali uzoefu, isipokuwa kama kazi husika itahitaji kuwa na uzoefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uzoefu huwekwa kwenye nafasi ambazo si madaraja ya kuingilia kazini mfano nafasi za waandamizi, viongozi au kada ambayo uzoefu ndio sifa ya msingi ya kuingilia kama vile kada ya udereva ambapo lazima mtumishi huyu ajue kuendesha gari kwa viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa Muundo wa Utumishi wa Kada hiyo.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kupandisha madaraja kwa mserereko Walimu wenye changamoto ya kupandishwa madaraja wakiwemo wa Ngara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 6(a) na (3) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298 kikisomwa pamoja na Kanuni ya 17(5) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022; upandishaji vyeo watumishi wa umma pamoja na vigezo vingine huzingatia sifa za kielimu na kitaaluma zilizoainishwa katika miundo ya maendeleo ya utumishi, utendaji mzuri wa kazi, uwepo wa bajeti na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na ofisi yangu kuhusu utekelezaji wa ikama na bajeti kwa mwaka husika.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia miongozo hiyo, ofisi yangu imeendelea kuhakiki taarifa na kuwapandisha vyeo watumishi wa kada ya ualimu waliobainishwa na waajiri kuwa na changamoto katika upandishwaji vyeo wakiwemo Walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara.

Mheshimiwa Spika, naliahidi Bunge lako kuwa, zoezi hili litakapokamilika, watumishi wa kada ya ualimu waliobainishwa na waajiri wao, wakiwemo Walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara waliothibitishwa kuwa wametimiza sifa za kupanda madaraja watapandishwa.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kwa Watumishi wanaohusika kutumia vibaya fedha za miradi ya Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia masuala ya nidhamu katika Utumishi wa Umma kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 6(1)(b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 ambacho kimewapa Mamlaka Wakuu wa Taasisi kusimamia masuala ya nidhamu kwa watumishi walio chini yao pale wanapokiuka kiapo cha ahadi ya uadilifu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia uvunjifu wa maadili katika utekelezaji wa majukumu ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Serikali imeendelea kuwachukulia hatua mbalimbali za kinidhamu Watumishi wa Umma wanaotumia vibaya fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo kuwasimamisha kazi na kuwaanzishia mashauri ya kinidhamu.

Mheshimiwa Spika, mathalan, katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Desemba, 2023, TAKUKURU ilifuatilia matumizi ya rasilimali za umma kwenye utekelezaji wa miradi 2,541 yenye thamani ya shilingi trillioni 8.26, ambapo miradi 467 ilibainika kuwa na upungufu mbalimbali ikiwemo uvujaji na kutokuwa na thamani ya fedha. Kutokana na matokeo hayo, hatua kadhaa zilichukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329, ikiwa ni pamoja na kuanzisha uchunguzi kwa miradi 274 ambapo watumishi 51 walichukuliwa hatua za kinidhamu.
MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani wa kutoa motisha kwa watumishi wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Same Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutoa motisha za kifedha na zisizo za kifedha kwa watumishi wa Umma wakiwemo watumishi wanaofanya kazi katika mazingira magumu kwa kuboresha viwango vya posho za kazi baada ya masaa ya kazi, posho ya kujikimu wakati wa kusafiri, posho za mawasiliano, kufikisha huduma za umeme katika maeneo yao, kutoa magodoro na nyumba za walimu zenye staha na mengineyo mengi

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika Halmashauri yalipo maeneo yenye mazingira magumu kwa kutambua umuhimu wa kutoa motisha, zinatekeleza mipango yao ya motisha kwa kufuata miongozo inayotoka kwenye Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kusimamia utoaji wa motisha mbalimbali kwa watumishi hao kutegemeana na hali na mazingira magumu ya sehemu wanapofanyia kazi.
MHE. AMINA DAUD HASSAN aliuliza:-

Je, Serikali inatambua uwepo wa rushwa kwa wanafunzi katika vyuo vyetu hapa Nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Daud Hassan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa rushwa katika sekta ya elimu kwa kuzingatia matokeo ya utafiti wa Hali ya Utawala na Rushwa wa Mwaka 2020. Rushwa ya Ngono ni kosa la jinai kwa mujibu wa Kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329. Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuzuia rushwa katika vyuo vyote nchini kupitia tafiti na mikakati ya kuzuia rushwa ikiwemo programu mbalimbali za kuelimishaji umma na vilabu vya wapinga rushwa shuleni na vyuoni.

Mheshimiwa Spika, mathalani mwaka 2019, Serikali ilishirikiana na wadau kuendesha kampeni ya Vunja Ukimya kwa ajili ya kupiga vita rushwa hususani rushwa ya ngono kwa kuhamasisha jamii isikae kimya dhidi ya vitendo hivyo. Katika kipindi cha mwaka 2020 - 2023, taarifa 11 za malalamiko ya vitendo vya rushwa ya ngono katika vyuo vyetu zilipokelewa na majalada tisa ya uchunguzi yalianzishwa; ambapo majalada mawili yamefungwa baada ya kukosekana ushahidi. Jalada moja limepata kibali cha kumfikisha mtuhumiwa mahakamani na majalada mawili yamependekeza watuhumiwa wake wachukuliwe hatua za kinidhamu na jalada moja, kesi imeshindwa mahakamani. Majalada manne yanaendelea na uchunguzi.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza: -

Je, Serikali inafanya nini kuhakikisha Miradi ya TASAF inakuwa yenye tija kwa wanufaika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa TASAF unatekelezwa ukiwa na dhumuni kubwa la kuzikwamua kaya zisizojiweza kiuchumi ili ziweze kumudu kukabiliana na changamoto za kiuchumi kupitia afua mbalimbali kama vile uhawilishaji fedha, uundaji wa vikundi vya kuweka akiba na kuinua uchumi wa kaya na utekelezaji wa miradi ya ajira za muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa miradi ya TASAF inakuwa yenye tija kwa wanufaika wake, Serikali imeweka mifumo na mikakati mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Mchakato wa uteuzi kuwa shirikishi na jumuishi, kuweka mfumo wa uwajibikaji na Ufuatiliaji, Utoaji wa taarifa za utekelezaji, kuwapa wanufaika mafunzo ya kuwajengea uwezo, kushirikisha wadau mbalimbali katika ngazi zote za kuhakiki taratibu na miongozo kwenye utekelezaji ikizingatiwa ili kufika ubora, pamoja na hilo pia, viwango na tija inayokusudiwa viangaliwe.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kupandisha madaraja kwa mserereko Walimu wenye changamoto ya kupandishwa madaraja wakiwemo wa Ngara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 6(a) na (3) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298 kikisomwa pamoja na Kanuni ya 17(5) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022; upandishaji vyeo watumishi wa umma pamoja na vigezo vingine huzingatia sifa za kielimu na kitaaluma zilizoainishwa katika miundo ya maendeleo ya utumishi, utendaji mzuri wa kazi, uwepo wa bajeti na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na ofisi yangu kuhusu utekelezaji wa ikama na bajeti kwa mwaka husika.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia miongozo hiyo, ofisi yangu imeendelea kuhakiki taarifa na kuwapandisha vyeo watumishi wa kada ya ualimu waliobainishwa na waajiri kuwa na changamoto katika upandishwaji vyeo wakiwemo Walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara.

Mheshimiwa Spika, naliahidi Bunge lako kuwa, zoezi hili litakapokamilika, watumishi wa kada ya ualimu waliobainishwa na waajiri wao, wakiwemo Walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara waliothibitishwa kuwa wametimiza sifa za kupanda madaraja watapandishwa.
MHE. TECLA M. UNGELE K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, kwa nini baadhi ya miradi inayoibuliwa na jamii kupitia TASAF hukataliwa na kutekelezwa miradi ambayo haikuibuliwa na jamii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi yote inayotekelezwa kupitia TASAF huibuliwa na jamii kwa kutumia utaratibu shirikishi unaokutanisha jamii yote katika Kijiji/Mtaa au Shehia katika mkutano wa kuchagua miradi inayoondoa kero za wananchi, inayokubaliwa na jamii na inayokidhi vigezo vya kisekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo jamii itaibua mradi ambao haukidhi vigezo vya sekta na kuangalia manufaa ya miradi ya kipaumbele cha kwanza kwa jamii, mradi wa pili katika orodha ya vipaumbele vya jamii hutekelezwa.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO K.n.y. MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-

Je, lini watumishi wa umma watarekebishiwa madaraja hasa walimu waliopandishwa na kunyang’anywa mwaka 2016 - 2018 kupisha uhakiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 Serikali ilisitisha mambo mbalimbali ya kiutumishi ikiwemo upandishaji vyeo ili kupisha zoezi la uhakiki wa taarifa za kiutumishi na vyeti vya elimu kwa watumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua changamoto zilizojitokeza kutokana na sitisho hilo mwaka 2021/2022 Serikali ilianza kutekeleza zoezi la kuwarejesha watumishi wa umma wa kada mbalimbali kwenye nafasi na vyeo vyao stahiki kwa njia mbalimbali ikiwemo msawazo wa vyeo na mserereko wa madaraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi sasa jumla ya watumishi 375,904 wamepandishwa vyeo wakiwemo watumishi 85,471 walioathirika na zoezi la uhakiki. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali inatarajia kuwapandisha vyeo watumishi 81,503 wakiwemo walimu walioathirika na zoezi la uhakiki.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -

Je, hadi sasa Serikali ina madeni kiasi gani ya watumishi wa umma yanayohusu likizo, uhamisho na kusafirisha mizigo baada ya kustaafu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2024 madeni ya watumishi wa umma yaliyohakikiwa na kukidhi vigezo vya kulipwa yanayohusu likizo, uhamisho na kusafirisha mizigo baada ya kustaafu yalikuwa na jumla ya shilingi bilioni 285.1. Katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 jumla ya madeni yenye ujazo wa shilingi bilioni 55.9 yamelipwa. Aidha, Serikali itaendelea kulipa madeni ya watumishi yasiyo ya kimshahara kila mwaka kwa kuzingatia taarifa ya uhakiki wa madeni.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, ni kwa nini wanufaika wa TASAF wanalazimika kufuata fedha benki hata fedha hiyo ikiwa ni kidogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa malipo kwa wanufaika wa TASAF unafanyika kwa njia kuu tatu: kwanza, kupitia akaunti ya Benki; pili, kupitia akaunti ya simu ya mkononi; na tatu, kwa malipo taslimu kupitia kwa wakala au katika kituo cha malipo. Uamuzi wa njia gani ambayo mlengwa atapenda kulipwa, unabaki kuwa wa kwake mwenyewe mlengwa ambaye anatambulika wakati wa uandikishaji wa daftari la walengwa.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapandishia mishahara wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jukumu la Serikali kupandisha mishahara ya watumishi wake. Hivyo, Serikali inaendelea na itaendelea kupandisha mishahara ya watumishi. Mathalani, Julai, 2022 Serikali iliongeza mshahara kiwango cha kima cha chini kwa Watumishi wa Umma kwa asilimia 23.3, kutoka shilingi 300,000 hadi shilingi 370,000/= kwa mwezi. Nyongeza hiyo ya mishahara ilitolewa pia kwa watumishi wote wa umma kwa viwango tofauti tofauti kulingana na viwango vya mishahara vya watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 153.9 kwa ajili ya nyongeza ya mwaka ya mishahara (annual salary increment) kwa watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, katika sherehe za Mei Mosi mwaka huu, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dr. Philip Isdor Mpango wakati wa kujibu risala ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA), kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, alieleza kuwa suala la nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma ni jambo linaangaliwa.

MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza wimbi la vijana wanaomaliza masomo na kukosa kazi kutokana na sharti la vigezo vya uzoefu wa miaka miwili na zaidi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwezesha vijana wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kuwa na uzoefu wa kazi pamoja na sifa nyingine za kujiajiri ndani na nje ya nchi, Serikali inaendelea na programu mbalimbali za mafunzo ya uzoefu wa kazi ikiwemo internship na maboresho ya Sera ya Taifa ya Vijana ya mwaka 2007 ambayo inahimiza uwepo wa mfumo endelevu wa kuwajengea vijana ujuzi na stadi mbalimbali ili waweze kuajirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu ninaomba kutoa wito kwa wahitimu kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia programu za elimu, mafunzo na uwezeshaji wa kiuchumi kwa kutoa mikopo na mitaji, fursa za ajira rasmi na zisizo rasmi katika miradi ya Serikali inayopatikana katika Wizara za Kisekta na Sekta Binafsi.
MHE. EDWIN E. SWALE aliuliza:-

Je Serikali ina Mkakati gani wa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutekeleza hatua na afua mbalimbali za kuboresha maslahi ya watumishi wa umma kwa uchache, naomba nizitaje.

Mosi, Julai, 2022 Serikali iliongeza kima cha chini cha Mishahara kwa Watumishi wa Umma kwa 23.3%;

Pili, Serikali imeweka nyongeza ya mwaka ya mishahara (annual salary increment) ambapo jumla ya shilingi bilioni 153.9 zimetengwa katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 na shilingi bilioni 150 katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 ili kugharamia nyongeza ya mwaka ya mishahara;

Tatu, Serikali imehuisha viwango vya malipo ya posho ya safari za kikazi ndani ya nchi na posho ya masaa ya ziada kwa lengo la kuwawezesha watumishi wa umma kumudu gharama za maisha kwa kuzingatia hali halisi ya kiuchumi;

Nne, Serikali imerejesha utaratibu wa kuwapandisha vyeo watumishi wenye sifa stahiki kila baada ya miaka mitatu badala ya miaka minne kuanzia mwaka huu wa fedha. Kwa msingi wa uamuzi huo, Serikali inaendelea na zoezi la kuwapandisha vyeo watumishi 81,515 waliokasimiwa katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 kwa gharama ya shilingi bilioni 130.4 kwa mwaka na watumishi wengine 219,924 wamekasimiwa kupandishwa vyeo katika Ikama na bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 kwa gharama ya shilingi bilioni 252.7. Aidha, Serikali imeridhia kulipa mishahara ya wafanyakazi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa 113 zilizopo hapa nchini zenye jumla ya watumishi 691 kwa awamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma ikiwemo, kutenga fedha katika bajeti yake kwa ajili ya kugharamia nyongeza za mishahara ya kila mwaka, posho na marupurupu kwa watumishi kwa kadri ya hali ya uchumi itakavyoruhusu ili kuongeza motisha na chachu ya uwajibikaji.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO K.n.y. MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-

Je, lini watumishi wa umma watarekebishiwa madaraja hasa walimu waliopandishwa na kunyang’anywa mwaka 2016 - 2018 kupisha uhakiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 Serikali ilisitisha mambo mbalimbali ya kiutumishi ikiwemo upandishaji vyeo ili kupisha zoezi la uhakiki wa taarifa za kiutumishi na vyeti vya elimu kwa watumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua changamoto zilizojitokeza kutokana na sitisho hilo mwaka 2021/2022 Serikali ilianza kutekeleza zoezi la kuwarejesha watumishi wa umma wa kada mbalimbali kwenye nafasi na vyeo vyao stahiki kwa njia mbalimbali ikiwemo msawazo wa vyeo na mserereko wa madaraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi sasa jumla ya watumishi 375,904 wamepandishwa vyeo wakiwemo watumishi 85,471 walioathirika na zoezi la uhakiki. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali inatarajia kuwapandisha vyeo watumishi 81,503 wakiwemo walimu walioathirika na zoezi la uhakiki.