Supplementary Questions from Hon. Ridhiwani Jakaya Kikwete (15 total)
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza ambayo akinijibu vizuri basi nitaridhika zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sheria hii ya Cyber Crime hasa ibara ya 39, inampa mamlaka Waziri ya kuamua kutoa au kuruhusu content gani iingie katika mitandao, lakini matusi, kejeli, picha za ngono zimeendelea kuwepo katika mitandao na Waziri hafanyi jambo lolote lile. Sasa naomba kuuliza, je, Waziri huyu anaangalia computer kama kazi yake inavyomtaka au naye amejikita katika makazi mengine ili tuweze kujua hapa kama sheria hii ina uzuri au ina upungufu wake?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Sheria ya Mtandao inampa nafasi pia Mkuu wa Kituo cha Polisi chochote kile kuweza kukamata computer, kukamata mali za mtu ambazo zinahusiana na hilo ambalo yeye analisema ni kosa. Je, Mheshimiwa Waziri, haoni kwamba hapa sasa ndipo tunapoanza kuharibikiwa baada ya kutumia njia halali ya kimahakama kupata ile order ya kukamata mali za watu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, mamlaka aliyopewa Waziri anayehusika na masuala ya mawasiliano si kama yalivyotafsiriwa na Mheshimiwa Kikwete. Isipokuwa pale
inapotokea malalamiko ndipo vifungu hivi vinapotokea. Pamoja na kwamba yeye anadhani masuala haya yanaendelea lakini nimempa taarifa kwamba masuala haya yamekuwa yakipungua sana. Kwa mfano, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, matukio yalikuwa 459 yaliyoripotiwa Polisi, maana yake kuna watu waliolalamika kuhusu matukio hayo wakaripoti Polisi; matukio 459, lakini baada ya sheria kuanza hakukuwa na tukio lolote lililoripotiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mambo yanaweza yakawa yanaendelea lakini kinachoangaliwa hapa ni yule anayetendewa; anapoona kwamba amekosewa anatakiwa atoe taarifa Polisi ili Polisi wachukue hatua. Hivyo vifungu vilivyotajwa vya Mheshimiwa Waziri na hicho cha Polisi ndivyo vinavyotumika. Si kazi ya Polisi kupita kwenye makompyuta na kutafuta makosa hayo, hapana! Kazi ya Polisi ni kupokea malalamiko na ndipo kuyafanyia kazi na kutafuta ushahidi kwa mujibu wa sheria ilivyotungwa.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza pamoja na kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri ya mwanzo lakini pili nimpongeze pia na kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuja kuyaona
mambo yanayoendelea Chalinze.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Chalinze
wamechoka kusubiri maji na kwamba sasa imefikia sehemu sijui nisemeje maana yake Waziri yeyé mwenyewe ameyaona. Sasa je, Serikali pamoja na kutoa notice ya siku 100 imejipangaje kusimamia utekelezaji wa kusitisha mkataba
huu, kwa sababu tunavyofahamu sisi kwa mahitaji ya matanki 19 ujenzi wa vituo tisa na vioski vya kuchotea maji 351 sina hakika sana kama huyu mjenzi anaweza akamaliza. Pamoja na hilo pia naomba nimkumbe Mheshimiwa Waziri
kwamba mjenzi huyu ndiye yule ambaye amenyangwa passport na Mheshimiwa Rais kule Lindi, sasa je, Serikali imejipangaje juu ya wayforward baada ya kusitisha mkataba na mjenzi huyu? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tunapokea pongezi ambazo anazitoa kwa Waziri Mkuu kwa kuweza kutembelea mradi huu. Kuhusu suala la notice tuliyoitoa kitu kinachofanyika sasa kwanza tulitoa barua kwa mfadhili ili kuomba no objection kwa sababu ni miradi ambayo ina ufadhili lazima
wao waidhinishe kama unataka kusitisha mkataba na kwamba wao watakuwa tayari kuendelea kufadhili kazi zilizobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tulichokifanya
kwamba tumetoa notice ya siku 100 na tunafanya monitoring kufatilia kila siku kazi ambazo nazalisha, na sasa hivi na yeye mwenyewe anaweza kushuhudia ameongeza kasi ambayo
wala hatukutarajia, kazi inakwenda kwa nguvu sana. Ikifika tarehe 31 Mei tutafanya tathmini kuangalia kwa speed hii anayofanya je, anaweza akamaliza katika muda mfupi, lakini kwa wakati huo huo Serikali imechukua hatua kwamba
malipo yote ambayo yatakuwa yanatolewa anakatwa tozo ya ucheleweshwaji wa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeweza kumwagiza Mhandisi Mshauri kwamba aandae makabrasha ya zabuni ikifika tarehe 31 Mei kama itakuwa kasi ile hairidhishi tunaajiri mkandarasi mwingine kwa sababu fedha zile za kufanya ile kazi zipo na hakuna fedha ambayo imelipwa kwa kazi ambayo haijafanyika. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie wananchi wa Chalinze kwamba Serikali ina dhamira ya dhati ya kukamilisha mradi huu wa maji Chalinze.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na mimi kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kuwa matatizo waliyonayo wananchi wa Bukoba Vijijini yanafanana moja kwa moja na matatizo waliyonayo Wananchi wa Chalinze na kwa kipindi kirefu sana wamesubiri maji na sasa hivi hawaoni kinachoendelea. Sasa swali langu, Mheshimiwa Waziri ni lini mkandarasi yule utamfukuza ili wananchi wa Chalinze wajue wanaanza upya? Swali langu la kwanza na swali la pili, nini mpango mkakati sasa wa kuwakwamua wananchi wa Chalinze? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, ni kweli pale Chalinze kuna mradi Awamu ya Tatu ambao unatekelezwa na Kampuni moja kutoka India (OIA) na utendaji wake wa kazi hauridhishi na tulikuwa tumetoa muda kwamba mpaka mwezi wa kumi awe amefikisha mahali ambapo Serikali inaweza kumruhusu au kufuta mkandarasi yule. Tunafuatilia kazi hiyo kwa karibu sana, naomba nikuhakikishie Bunge hili kwamba ikifikia mwezi wa kumi na hakuna kazi ya maana inayoendelea pale, tutachukua hatua zaidi za kimkataba.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nami nimpongeze Mheshimiwa Dotto kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo naomba niombe kuuliza au kupata kauli ya Serikali juu ya lini Serikali itaruhusu mwekezaji wetu Gulf Concrete awalipe fidia wananchi wapatao 80 wanaoishi katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Lugoba ili waweze kuendeleza eneo lile na wao waweze kuondoka na kulinda afya zao?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO): Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji wa Gulf Concrete and Cement Product ambaye yuko Chalinze kwenye Kijjiji cha Nguza amekuwa akichimba kwa muda mrefu kwenye eneo hilo; na kwa kweli anachimba kwenye eneo hilo ametengeneza ajira zaidi ya 170 kwa watu wa Chalinze ambako Mheshimiwa Mbunge anafuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumetoa mgogoro mdogo ambao sisi kama Wizara ya Madini tunaushughulikia. Mwekezaji huyu amechimba na akaingia kwenye eneo la mwekezaji mwingine ambaye ana leseni anaitwa Global Mining; ameingia kwenye eneo ambalo lina ukubwa kama hekta 1.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichofanya kwa sasa, tunataka tuumalize kwanza mgogoro huu ambao yeye Gulf Concrete ameingia kwenye eneo la mtu mwingine. Tukishamaliza twende kwenye hatua ya pili sasa ya kumsaidia Mwekezaji huyo ambaye kwa kweli ana tija kwa watu wa Chalinze na watu wa Mkoa wa Pwani aweze kulipa fidia ili aendeleze mradi wake.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona, Mheshimiwa Waziri, katika gazeti la Mwananchi la leo imeandikwa kwamba dawa zote zinazotakiwa wagonjwa wapate kuanzia leo au kuanzia mwaka huu zitakuwa zinalipiwa. Sasa tunatambua kwamba kuna mpango wa Serikali hasa katika dawa za watu wenye UKIMWI, Kifua Kikuu na baadhi ya magonjwa, kwamba dawa hizi zinatolewa bure. Sasa nataka Mheshimiwa Waziri atuambie; je, hizi taarifa zilizotolewa leo kwenye gazeti ni za kweli? Kwanza, lakini pili kama zina ukweli ni dawa gani ambazo kuanzia sasa zitakuwa zinachajiwa, kwa maana ya kutoa pesa na dawa gani ambazo zitakuwa bure? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimtoe shaka yeye, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla kwamba pengine gazeti hilo litakuwa limekosea tu, limefanya misconception ya kilichosemwa pale Muhimbili. Sijalisoma binafsi, lakini kama Naibu Waziri kwenye Wizara ambayo inasimamia utekelezaji wa Sera ya Afya natoa maelezo yafuatayo:-
Kwamba hatujabadilisha sera ya kuwahudumia Watanzania kwenye eneo la kugharamia dawa. Kwa maana hiyo utaratibu ni ule ule, hakuna dawa za UKIMWI zitakazouzwa, hakuna dawa za Kifua Kikuu zitakazouzwa, hakuna mama mjamzito wala mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano ama mzee mwenye umri zaidi ya 60 atakayeuziwa dawa, hiyo ndiyo Sera ya Afya kwenye mambo ya gharama. Kwa hiyo, kama gazeti limeandika hivyo pengine limem-miss quote aliyekuwa ametoa kauli inayofanana na kitu cha namna hiyo, hii ndiyo kauli ya Serikali.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nataka kuongeza nguvu kwamba tutaitaka, maana maneno hayo yameandikwa kwenye gazeti la leo la Mwananchi, kwa hiyo tutaitaka Muhimbili ituletee maelezo rasmi. Kwa sababu sera yetu kama alivyosema Naibu Waziri dawa ni bure kwa magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na magonjwa yale ambayo yamesamehewa kwa mujibu wa sera. Kwa hiyo, nikitoka hapa tunatoa maelekezo kwa Muhimbili watuletee maelekezo rasmi na tutarudisha mrejesho hapa Bungeni.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE:Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Waziri nafikiri leo unatambua kwamba leo ndio tarehe ya mwisho ya ule mradi maji Chalinze, ninachotaka hapa ni kusikia kauli ya Serikali juu ya nini sasa kinafuata baada ya leo kuwa deadline ya ule mkataba wetu wa ujenzi wa Mradi wa Maji Chalinze?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kauli hiyo unayoizungumza iko katika taratibu za kimikataba, nikishauri tu Mheshimiwa Mbunge sisi wanasiasa watunga sera si vyema tuingilie mikataba, tusubiri kwanza utekelezaji wa mikataba ufanyike hatua zitakazochukuliwa basi tutazitolea taarifa.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini mahitaji ya umeme katika maeneo mengi hasa katika Vitongoji vya Halmashauri ya Jimbo la Chalinze imekuwa ni muhimu sana. Kwa mfano, kule Msinune, Kiwangwa bado umeme haujafika na ahadi ya Serikali ni kwamba umeme hautaruka Kitongoji chochote.
Je, Serikali imejipangaje katika kuhakikisha kwamba inawapelekea umeme wananchi wanaoishi katika vitongoji hivyo vikiwemo vile ambavyo vipo katika Kata ya Vigwaza na Mbwewe na maeneo mengine ya Halmashauri yetu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nami niwe mmoja wa kumtakia heri katika siku yake ya kuzaliwa Mbunge wetu wa Chalinze, Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete.
Mheshimiwa Ridhiwani atakumbuka kwamba mwezi wa Kumi na Mbili tulifanya ziara pamoja naye na Waheshimiwa Wabunge wengine wa Mkoa wa Pwani kwenye majimbo yao; tulipita katika maeneo ya Kata ya Kiwangwa, Msinune na Bago na Mheshimiwa Mbunge atakumbuka pia tuna mradi wa densification unaoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Chalinze.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maeneo ambayo ameyataja ya Msinune na Bago ni maeneo ambayo yapo katika mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza. Kwa hiyo, nimthibitishie Mhesimiwa Mbunge Serikali ya Awamu ya Tano kwa kweli kupitia miradi yake hii inayoendelea itapeleka umeme katika vitongoji mbalimbali ambavyo vina changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana kwa kazi yake ya kufuatilia hasa upatikanaji wa nishati ya umeme Jimboni Chalinze. Ahsante. (Makofi)
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka nimkumbushe tu kwamba jambo hili lipo ndani ya Ilani na kwa kuwa ni msikivu na Mheshimiwa Eng. Kamwelwe ni msikivu zaidi, naomba jambo hili walisimamie ili liweze kukamilisha ndoto ya Watanzania ambao wamekuwa wanalala pale, hasa panapotokea matatizo ya ajali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali dogo, pamoja na matatizo yaliyopo katika Daraja la Wami, lakini pia iko ahadi ya Serikali ya kutengeneza barabara inayotoka Mbwewe - Mziha - Kibindu, je, hili jambo nalo Mheshimiwa Waziri mmefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nizipokee pongezi nyingi ambazo amezitoa kwa Serikali, lakini pia nimpongeze yeye binafsi kwa namna anavyofuatilia masuala mbalimbali katika jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ya Mbwewe – Mziha – Kibindu inafanyiwa matengenezo makubwa. Kuhusu kuiboresha barabara hii, nimuombe tu Mheshimiwa Ridhiwani, kwa sababu ni mfuatiliaji mzuri, baadaye tuonane ili tuangalie kwenye bajeti na mipango yetu ili niweze kumpa taarifa sahihi ili aweze pia kuzitumia kuwajulisha wananchi wa Jimbo la Chalinze. (Makofi)
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza na kumshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya, lakini pia kwa kutuliza joto la wananchi katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa na mambo mawili makubwa ambayo nilikuwa nataka niishauri Serikali. Kwanza, nimwambie Mheshimiwa Waziri, sikusudii kumzungumza au kuwatetea wavamizi wa hifadhi hizo. Ila swali langu linalenga katika hifadhi zilizovamia vijiji vyetu, maana kesi ya watu wa Chalinze ni hifadhi imevamia vijiji.
Mheshimiwa Spika, la pili, nikushukuru na kukupongeza, naona leo umemwalika Bwana Pierre Liquid, ni jambo jema, lakini ushauri wangu naomba kwa Wizara, inapofanya kazi katika kuweka hivyo vigingi na beacons itushirikishe sana sisi wawakilishi wa wananchi ili tuweze kuwapa ushirikiano na kuwakumbusha vizuri ili wasije kuvuruga kabisa zoezi zima.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nipokee pongezi hizo ambazo amempa Mheshimiwa Rais. Ni kweli kwamba hata kabla ya tamko la Mheshimiwa Rais maeneo haya yamekuwa ndani ya migogoro mingine kwa zaidi ya miaka 20; na yapo maeneo ambayo yalikuwa yana GN mbili; eneo lina GN ya uhifadhi lakini pia kuna GN ya kijiji au kata katika eneo la hifadhi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais alichokifanya ni kulifanya tatizo hili liweze kushughulikiwa.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza, amesema kwamba hifadhi ndiyo zimevamia maeneo ya vijiji. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, baada ya kazi ya Kamati tutakwenda katika maeneo husika yote yenye migogoro na tutashirikisha wawakilishi wa wananchi, wakiwemo Wabunge na Madiwani, kuhakikisha kwamba eneo tutakaloliwekea mipaka halitakuwa na migogoro tena.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mwezi Januari, 2019, Wizara ya Elimu ilitoa Mwongozo juu ya Muundo wa Bodi za Shule kuanzia shule za msingi mpaka Serikali. Katika muundo ule, Wizara imeelekeza katika shule ya sekondari na shule za msingi muundo utoe nafasi kubwa sana kwa walimu ambapo watakuwa watano lakini pia wazazi au nje ya walimu wanakuwa watatu. Je, katika maana nzima ya makusudio ya Bodi kwenda kuangalia ufanisi wa taaluma na majengo na mambo yanayoendelea shuleni, Wizara haioni kwamba jambo hili limekosewa na kwamba linahitaji lirekebishwe haraka sana kabla hapajaharibika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba hivi karibu tumetoa Mwongozo mpya wa Bodi za Shule na lazima niseme kwamba baada ya kuutoa tumegundua kuna maeneo ambayo yangeweza kuwa bora zaidi na mojawapo ni hilo alilosema Mheshimiwa Kikwete. Naomba nimhakikishe kwamba tayari Wizara inaupita upya tena Mwongozo ule kwa kushirikiana na wadau ili tuwe na Mwongozo ambao utakotupeleka mbali zaidi.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, naomba nirejee katika swali la msingi, siko katika mambo ya laini ya Mheshimiwa Selasini.
SPIKA: Uliza, uliza.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyopo Babati Vijijini yanafanana moja kwa moja na yaliyopo katika Halmashauri ya Chalize. Nimemwandikia sana Mheshimiwa Waziri na Wizara yake lakini utekelezaji umekuwa ni wa taratibu sana. Sasa kwa kuwa jambo hili nimeshamwandikia Mheshimiwa Waziri, naomba anijibu wamefikia wapi juu ya matatizo ya mawasiliano katika Kata ya Kiwangwa, Msata na Lugoba kama ambavyo tumeelekezana? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, Mbunge wa Chalinze, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Vijiji vya Kiwangwa katika baadhi ya maeneo yana tatizo la huduma ya mawasiliano lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo lake analolitaja la Kiwangwa linahitaji kuongezewa nguvu kwenye mnara wa mawasiliano ulioko pale. Kwa hiyo, namshauri aje tuonane baadaye tuangalie vijiji vingine ambavyo tumeviingiza kwenye mpango wa kupelekewa huduma na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kuniona. Matatizo yaliyopo Handeni-Mziha- Kibindu mpaka Mbwewe yanalingana kabisa na hii barabara ya kutoka Handeni kwenda Mziha. Je, ni lini Serikali inakuja kutujengea barabara ile kwa kiwango cha lami kama ambavyo sasa hivi nyumba zote zimepigwa X kupisha ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Mbunge anauliza juu ya barabara ya kutoka Mbweni inakwenda Kibindu ikipita kwa Luhombo itaungana na barabara hii niliyoijibia swali la msingi kwa maana ya kwamba kuwaunganisha wananchi wa maeneo haya na barabara hiyo itakuwa inakwenda Tanga na sehemu hii kweli ina uzalishaji mkubwa. Niombe tu Mheshimiwa Ridhiwani kwamba avute subira kwa sababu najua barabara karibu zote zipo kwenye mpango mkakati wetu wa Wizara na ikimpendeza tuonanane baadaye tuitazame hii barabara
kwamba kwenye mpango wetu wa kipindi cha miaka mitano tumekipangia nini kipande hiki cha barabara kwa maana ya kwamba inajengwa kwenye kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa sasa tunaiboresha barabara hii na mimi nimeipita mara kadhaa kwamba iko katika kiwango kizuri kwamba inaendelea kuwapa huduma nzuri zinazohitajika wananchi wa maeneo haya.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Serikali, lakini ninataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri; sasa ni lini Serikali itakuja na mkakati ulio mzuri zaidi ukiangalia kwamba maji yanayopotea katika bonde lile ni mengi sana na ile tija ya kilimo haipatikani katika lile ambalo tunaita usalama wa chakula katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Ridhiwani.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba utilization level ya Ruvu na mito mingine mikubwa katika nchi yetu haijafikiwa kiwango ambacho tunakitarajia na tunacho-expect, lakini hatua tulizochukua sasa hivi katika mpango wa umwagiliaji wa mwaka 2018 ambao tumeuandaa kama Wizara na hivi karibini chini ya uongozi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo ambayo tumekaa na Wizara ya Fedha kwa ajili ya kubadilisha model za financing za umwagiliaji na sasa tunaelekea kwenye mfumo wa EPC ambayo tutafanya miradi mikubwa ya kielelezo kwa ajili ya kuchagua maeneo machache na kuweza kuyapa kipaumbele na moja ya eneo ni Mto Ruvu na Mto Ruvuma.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niunge katika swali alilouliza ndugu yangu Mheshimiwa Dunstan Kitandula, kwamba kumekuwa na utaratibu au zoezi ambalo linaendelea kule Msata katika maeneo ya Kihangaiko na Pongwe Msungura wakipima maeneo ya wananchi katika maana ya kulipa fidia, lakini kwa taarifa nilizozipata za juzi ni kwamba zoezi lile limesimama kwa sababu ya Mkataba ambao walikuwa wamepeana baina ya Wizara na yule mpima kuhusiana na eneo lile. (Makofi)
Mheshimimiwa Mwenyekiti, sasa katika spirit ya kuondoa migogoro iliyoko baina ya Jeshi na wananchi…
MWENYEKITI: Sasa uliza swali.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasemaje? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, maarufu kama Baba Aziza, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira yetu kupima maeneo yote yanayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Kwa hiyo huo ni utaratibu unaoendelea na nimhakikishie tu Mheshimiwa Ridhiwani, sio kwamba zoezi limesitishwa, zoezi la upimaji maeneo yote linaendelea lina hatua zake. Kwa hiyo niwatoe wasiwasi tu wananchi wa eneo la Msata Kihangaiko, wanavyoona wale wapimaji hawapo wanafikiri labda shughuli imesita, hapana.
Nimtoe wasiwasi pia Mheshimiwa Ridhiwani zoezi linaendelea, tutahakikisha maeneo yote tunamaliza kufanya upimaji na wananchi wanapata haki zao. (Makofi)
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, nami naomba niulize swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri wa Mifugo.
Mheshimiwa Spika, zaidi ya jumla ya hekta 2,208 zimegawiwa kutoka kwenye Ranchi ya Ruvu kwenda kkwetwa wanavijiji vinavyozunguka au katika Halmashauri ya Chalinze vikiwemo vijiji vya Kindogonzelo, Kitonga, Magulumatali, Vigwaza na Milo. Je, ni lini Serikali inakuja kutukabidhi vipande hivyo vya ardhi kwa ajili ya wananchi wetu sasa kuweza kugawana ili kuweza kutengeneza utaratibu mzuri wa kufuga. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa
Spika ahsante sana umetupa elimu nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali zuri la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Mrisho Kikwete kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba tumetenga hekta 2,208 hii ni kwa sababu ya lile jibu la msingi nililolitoa lililoulizwa na Mheshimiwa Mwakamo la kuondosha migogoro kati ya wakulima na wafugaji ni moja ya jitihada za Serikali na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika, tayari hatua za mwanzo za kiutawala ndani ya Wizara zimeshafanywa, vimeshapimwa na kutengwa maeneo haya, hatua inayofuata sasa ni kwenda kuwakabidhi Halmashauri ya Chalinze na Kibaha na hasa Jimbo la Chalinze, Jimbo la Kibaha Vijijini na Jimbo la Bagamoyo. Mara tu baada ya Bunge Wizara itakuwa iko tayari kabisa kuhakikisha kwamba sherehe hizi za kwenda kuwakabidhi na waweze kujipangia matumizi zinakwenda kufanyika. Ahsante sana. (Makofi)