Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Abdallah Hamis Ulega (22 total)

MHE. ABDALLAH HAMISI ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu haya mazuri ya Serikali naomba sasa niulize majibu ya maswali mawili ya nyongeza.
(a) Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuongozana na mimi kwenda Jimboni Mkuranga katika vijiji hivi vya Magawa, Msonga Makumbeya na vinginevyo pata athari hii ili aweze kujionea yeye mwenyewe na kuona namna iliyobora zaidi ya kutusaidia?
(b) Ningeomba niulize Serikali sasa ipo tayari kuhakikisha kwamba viuatilifu kwa maana ya sulfur, iweze kupatikana kwa wingi na kwa wakati katika Jimbo letu la Mkuranga ili kuepusha madhara haya ya ugonjwa wa mikorosho na kuhakikisha uzalishaji mkubwa zaidi ili kuwaondolea wananchi wangu umaskini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lake la kutaka tuongozane naye kwenda Jimboni tumelipokea na ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia hili suala tayari tulishapanga kufika Mkuranga na kipindi cha bajeti kitakapoisha mimi binafsi nitaongozana naye kwenda Mkuranga ili kujionea hali halisi na kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni kweli kwamba kumekuwepo na changamoto ya upatikanaji wa viwatilifu kwa wakati hasa sulfur na huko nyuma tayari kumeshatokea matatizo kwa sababu hiyo, kama nakumbuka mwaka 2011 kulikuwa na changamoto wakatia wa matumizi ya kiatilifu cha aina eugenol 880, lakini kwa sasa Wizara kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba viwatilivu hivyo na hasa sulfur zinapatikana kwa wingi na kwa wakati. Hivyo, ninamuahidi kwamba changamoto hii imeshafanyiwa kazi.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Kwa kuwa, tatizo hili la Ushetu la mawasilinao lipo pia katika Jimbo langu la Mkuranga katika vijiji kama vile vijiji vya Mkuruwiri, Nyanduturu, Kibesa, Msolwa, Kibewa na kwingineko. Je, Serikali ina mipango gani ya kuhakikisha kwamba wananchi hawa wa vijiji nilivyovitaja na vinginevyo viweze kupata mawasiliano ya simu na wao waweze kuwasiliana na ndugu zao na shughuli zao zingine za kijamii na kiuchumi.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza, nimepokea maombi yake. Tutayafanyia kazi na tutawasiliana naye mara nitakapopata taarifa kamili kuhusu maeneo haya aliyoyaelezea.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa tatizo hili la kifaa cha x- ray katika Hospitali ya Nyamagana ambalo Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI amelijibu na sisi katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Mkuranga linatusumbua; je, Serikali inaweza kutuhakikishia kwamba katika mgao huo wa vifaa tiba hivi hospitali ya Wilaya ya Mkuranga itakuwa ni miongoni mwa hospitali zitakazopata kifaa hiki cha x-ray ili kuwaondoa wana Mkuranga na adha ya kusafiri umbali mrefu mpaka Dar es Salaam katika Hospitali ya Temeke? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Hospitali ya Mkuranga haina x-ray, hali kadhalika na Hospitali ya Mafia na maeneo mengine yote. Lakini katika harakati zilizofanyika sasa hivi wenzetu wa Mafia angalau kupitia Mbunge Mheshimiwa Dau sasa wamepata x-ray, nadhani wiki iliyopita walinijulisha kwamba Mafia inapata x-ray.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Mkuranga vilevile tunajua kweli hakuna. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge tukae pamoja, kwa sababu katika bajeti ya mwaka huu nadhani haikutengwa, lakini tutakaa kwa mikakati ya pamoja tuangalie jinsi gani tutafanya kuwashirikisha wadau mbalimbali ambao katika njia moja au nyingine wanaweza kutusaidia kupata x-ray kwa sababu kifaa hiki ni muhimu sana ukiangalia au ukizingatia suala zima la ajali za pikipiki zinazotokea maeneo mbalimbali ambapo lazima mtu apimwe aangaliwe jinsi gani amepata majeruhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile nilipenda kuongezea yale majibu, kwamba vile vifaa havijafunguliwa katika hospitali nyingine. Kweli mimi nimepita maeneo mbalimbali, nilipita mpaka Bukene kwa rafiki yangu Mheshimiwa Zedi kuona center ambazo hazijafunguliwa; na tumetoa maagizo, ndiyo maana hata juzi hapa nimezungumza kwa ukali sana juu ya suala zima la Hospitali ya Singida. Lakini nimesikia, na leo nimekutana na Mbunge wa Singida amesema lile jambo limeshashughulikiwa sasa, hata vile vitanda havihami kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika ziara zangu ambazo natarajia kuzifanya, lengo langu ni kufika katika Nyanda za Juu Kusini kuhakikisha kwamba kwa sababu tunapeleka madaktari wapya maeneo mbalimbali hizi zahanati ambazo hazijafunguliwa; ambapo tunawashukuru sana wenzetu wa Mkapa Foundation, wamefanya kazi kubwa sana; center hizi zinafunguliwa ili wananchi wapate huduma katika maeneo yao ya karibu zaidi.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa majibu ya nyongeza kwenye maswali yote yanayohusu vifaa tiba kama x-ray hapa nchini kwamba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendesha mradi mkubwa wa vifaa tiba unaoitwa ORIO. Mradi huu utahusisha ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa kama MRI, CT Scan, x-ray, ultrasound na vifaa vingine na kuvitawanya nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Hospitali ya Mkuranga kwa mujibu wa kumbukumbu zangu ni mojawapo ya vituo ambavyo vitapatiwa mashine ya x-ray.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali fupi la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la wafanyakazi hasa vijana kufukuzwa kazi kiholela, kutokulipwa stahiki pindi wapatapo ajali kazini, kulipwa ujira mdogo sana wa shilingi 4,500 kwa kutwa ya siku, kufanyishwa kazi kwa muda mrefu kinyume cha sheria na taratibu za nchi lipo pia katika Wilaya yangu ya Mkuranga.
Je Serikali ina mpango gani wa kuwalinda vijana hawa wafanyakazi ili waweze kazi zao kuwa ni kazi zenye staha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ya kwamba Serikali kupitia Wizara ya Kazi tumekuwa tukisimamia sana Sheria Namba Sita ya mwaka 2004 ambayo imetoa haki na wajibu kwa wafanyakazi lakini na kwa waajiri pia. Sheria hii imetusaidia sana kutatua migogoro mingi mahali pa kazi, hasa pale inapoonekana sheria hii imekiukwa Serikali imekuwa ikichukua hatua stahiki kama ambavyo imekuwa ikionekana katika mazingira hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikija katika swali lake la msingi sasa ya kwamba Serikali tunawalindaje hawa ambao wanafukuzwa kazi kiholela hasa pale wanapoonekana wamepata ulemavu wakiwa kazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimkumbushe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kupata ulemavu ukiwa kazini sio kigezo cha dismissal na kwamba waajiri wote ambao wamekuwa wakikiuka taratibu hiyo ya sheria, sisi kama mamlaka ambayo tunasimamia sheria hizi kazi tumekuwa tukitoa elimu, lakini na kuchukua hatua stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie tu ya kwamba tumekuwa tukiendelea kufanya kaguzi nyingi sana za kazi kwa lengo la kubaini haya mapungufu na tumekuwa tukichukua hatua pindi inapobainika kwamba mwajiri amekiuka sheria hizi. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tutaendelea kusimamia Sheria Namba Sita ya mwaka 2004 kuhakikisha kwamba tunalinda haki za wafanyakazi na wafanyakazi hawa basi wasipoteze haki zao zile za kuwa wafanyakazi kwa kufukuzwa tu kiholela na mwajiri; na sisi tutahakikisha kwamba waajiri wote wanafuata sheria za nchi zinavyoelekeza.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa fursa hii uliyonipatia.
Kwa kuwa tatizo la ujambazi linaloipata Mikoa ya Kagera na Kigoma lipo pia tatizo la namna hiyo katika Jimbo letu na Wilaya yetu ya Mkuranga ambapo hapa karibuni tulipata tatizo la uvamizi wa majambazi katika Benki yetu ya NMB, Bupu na pale Mbagala Rangitatu na mengineyo.
Je, Serikali sasa iko tayari kuhakikisha kwamba Wilaya yetu ya Mkuranga inapata nyongeza ya vifaa kazi lakini pia na Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kwa kuwa hili ni ombi, basi tunalichukua, halafu mimi na yeye tutakaa, tunajuana ma-comrade, tuweze kuona uwezekano wa kulitimza hilo.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nasi wananchi wa Mkuranga tumeomba miradi ya umeme katika baadhi ya vijiji vyetu zaidi ya 30, vikiwemo Vijiji vya Mlamleni, Lugwadu, Mkola, Kazole, Lukanga, Mwajasi, Vianzi, Malela na vinginevyo, je, miradi hii itakamilika katika muda gani ili wananchi wale waweze kujiandaa kupokea miradi hii ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimesema, kwa sasa hivi tunafanya uhakiki katika utekelezaji wa REA Awamu ya II na mradi kabambe wa REA Awamu ya III unaanza Julai, 2016 na kukamilika kwa mradi huu ni miaka mitatu hadi minne. Kwa hiyo, ifikapo mwaka 2018/2019, Watanzania wote ambao watakuwa kwenye miradi ya REA Awamu ya II vikiwemo Vijiji vya Rugumu, Rukola, Malela pamoja na maeneo mengine ya Mkuranga vitapatiwa umeme ndani ya kipindi hicho.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu haya, ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi. Kama Serikali ilivyosema kwamba tunayo barabara ya lami ya kutuunganisha na Dar es Salaam. Sisi watu wa Mkuranga tunataka barabara itakayotuunganisha, Kisarawe mpaka Kibaha moja kwa moja, uwezekano wa kufanya hivyo upo, tunayo barabara ya kutoka Kimanzichana mpaka Mkamba, Mkamba mpaka Mkuluwili, Mkuluwili inapita katika Bonde la Saga, na kwenda kutokea Msanga, takapofika pale Msanga, itakwenda kuungana na barabara ya Manelomango inayotoka Mzenga, Mlandizi, inakwenda mpaka Mloka.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo imeahidiwa katika ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Namuomba Waziri aichukue barabara hii, aziagize mamlaka zinazohusika ziweze kutuunganisha sisi watu wa Mkuranga, Kibiti, Rufiji kwa pamoja na Wilaya ya Kisarawe mpaka Kibaha.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI, NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimelisikia ombi lake amelisema kwa sauti kuu, ninafahamu barabara anayoielezea, ya kutokea Kimanzichana hadi Msanga. Ni barabara ambayo ipo, sana sana katika barabara hiyo, kuna tatizo dogo tu la bonde, hilo bonde linaloitwa Bonde la Saga, ambalo nadhani Halmashauri haina uwezo wa kulihudumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda tu nimwambie kwamba kutokana na sauti hiyo kuu, Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, wajenge hoja ya kipande hiki kama cha kilometa mbili hadi cha kilometa tatu cha Bonde la Saga. Katika Mfuko wa Barabara kupitia Mkoa na hatimaye uje Taifa, tuangalie namna ya kufanya kama ombi maalum la kushughulikia hili bonde; nina uhakika bonde hili likishughulikiwa, uwezo wa Halmashauri kuishughulikia hiyo barabara upo.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza, matatizo haya ya watu wa Tarime Vijijini ni sambamba na matatizo ya watu wa Jimbo la Mkuranga kuhusu barabara ya kutoka Mkuranga Mjini mpaka Kisiju kwani ni barabara inayounga wilaya mbili za Mafia, ni barabara inayobeba uchumi wa korosho, ni barabara inayobeba watu zaidi ya laki moja na ni barabara ambayo itakuwa ni tegemezi katika uchumi wa viwanda vitakapojengwa katika Kata ya Mbezi. Je, kwa kuwa hii pia ni barabara iliyoahidiwa na Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Tano, ni lini na yenyewe itajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoiongelea naomba nikiri kwamba nimeisikia sasa, huyu Mheshimiwa tumekuwa tukiongea akifuatilia barabara zake za Mkuranga, lakini huko nyuma hii barabara hakuwahi kuitaja, ameitaja leo, nimeichukua na wataalam wangu tutamletea majibu sahihi kuhusu barabara hii.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Matatizo haya ya mawasiliano yaliyopo katika Jimbo la Korogwe Vijijini, yako pia katika Jimbo langu la Wilaya ya Mkuranga katika Kata ya Panzuo, katika Vijiji vya Mkuruwili, Kibesa na Kibuyuni, Kisegese, Chamgoi; Kata ya Kitomondo katika Kijiji cha Mpera na Mitandara na katika Kata ya Bupu katika Kijiji cha Mamdi Mkongo, Mamdi Mpera na hata kule Tundu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa Mheshimiwa Waziri aniambie, ni lini wananchi hawa wa vijiji nilivyovitaja katika Wilaya ya Mkuranga watapata mawasiliano ili na wao waweze kuendeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ulega ameshaleta orodha ya hayo maeneo yote; kuanzia Kata ya Panzuo na hizo nyingine ambazo amezitaja katika Wizara yetu ili tuweze kuzifanyia kazi. Nami namhakikishia, orodha hiyo tumeipokea na tulishaiwasilisha kwenye Kampuni ya Viettel pamoja na UCSAF kwa maana ya Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ili hatimaye watupe ratiba ya maeneo hayo yapangwe ratiba na bajeti kwa ajili ya kutekeleza kile ambacho Mheshimiwa Ulega anakipenda ili na wale wananchi wake waweze kunufaika na mawasiliano.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa MWenyekiti, pamoja na majibu hayo mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jimbo langu la Mkuranga utafiti ulishafanyika na ikagundulika gesi asilia katika kijiji cha Kiparang‟anda na kisima kiko pale. Naomba sasa Serikali inieleze ina mpango gani wa kuhakikisha kisima kile cha gesi kilichopo pale Mkuranga kinatumika kwa manufaa ya Taifa letu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha gesi hii inatumika ipasavyo katika kuzalisha umeme wa uhakika ili kikidhi haja ya viwanda na makazi yanayokuwa kwa kasi katika Jimbo hili la Mkuranga? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa makampuni ya utafiti yamefanya utafiti wa mafuta na gesi katika maeneo mbalimbali hasa katika maeneo ya Pwani ikiwepo eneo la Kiparang‟anda. Nimhakikishie Mheshimiwa Ulega kwamba eneo la Kiparang‟anda bado linafanyiwa utafiti na kazi inayofanyika sasa ni kuthibitisha kama kweli gesi na mafuta vipo. Mara baada ya kuthibitika hatua itakayofuata ni appraisal kuangalia kibiashara kama mafuta hayo bado yanaweza kuchimbika. Hatua itakayofuata baada ya hatua hiyo ni eneo la kufanya uendelezaji yaani development na baada ya hapo sasa hatua inayofuata ni uchimbijaji wa mafuta. Kwa hiyo, nimshukuru sana Mheshimiwa Ulega, kazi inaendelea kufanyika na hatua zikifikia mwisho Mheshimiwa Ulega na wananchi wake watafahamishwa rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na manufaa ya gesi kutumika kwa ajili ya umeme. Ni kweli kabisa kwani kwa sasa asilimia kubwa ya umeme tunaotumia hapa nchini ni kutokana na gesi asilia. Ni vyema niwahakikishie wananchi pamoja Waheshimiwa Wabunge kwamba sasa hivi megawati 743 za umeme zinatokana gesi na ni kiasi kikubwa sana cha gesi. Kwa hiyo, wananchi wa Mkuranga na maeneo mengine ya Pwani na siyo Pwani tu Mtwara pamoja na Lindi hata maeneo mengine ya Ukanda wa Kaskazini tutaendelea kutumia umeme wa gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Ulega vijiji vyake pamoja na vijiji vingine vya Rufiji, vijiji ambavyo ni 42 pamoja na 43 vya Mheshimiwa wa Rufiji pamoja na Kibiti vyote vitapata umeme kwa kutumia umeme wa gesi.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la dogo nyongeza. Barabara ya kutoka Mkuranga Mjini mpaka Kisiju Pwani ni miongoni mwa barabara ambayo zimekuwa zikiahidiwa pia kuwekwa lami na Awamu ya Nne na hata Awamu hii ya Tano. Barabara hii inapita katika Makao Makuu ya Wilaya yetu ya Mkuranga lakini pia inapita katika Hospitali yetu Kuu ya Wilaya ya Mkuranga. Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa Serikali itatusaidia kuhakikisha barabara hii inawekwa lami kutoka Mkuranga Mjini kupita Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Hospitali ya Wilaya mpaka Kisiju Pwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niweke kumbukumbu sawa, kwanza Mheshimiwa Ulega juzi kwa uchapakazi wake mzuri juzi alikuja ofisini kwetu kwa ajili ya kuhakikisha suala zima la miundombinu ya barabara katika jimbo lake na hii ni miongoni mwa barabara ambayo tulikuwa tukiijadili na Katibu Mkuu wangu pale jinsi gani tutafanya, kwa sababu yale ni Makao Makuu ya Halmashauri na kila Makao Makuu ya Halmashauri lazima angalau barabara ya lami iweze kufikika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali tutaangalia jinsi gani tutafanya lakini nikijua wazi barabara ile ambayo inaenda mpaka Kisiju Pwani ni jambo la mkakati mkubwa sana na kuna barabara nyingine kutoka Kimanzichana inapita katikati kule mpaka inakuja maeneo ya Msanga katika Jimbo la Kisarawe, hizi zote ni barabara za kimkakati kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Mkoa wa Pwani unafunguka, lengo kubwa ni kwamba katika uchumi unaofunguka wa viwanda sasa wananchi waweze kushiriki vizuri katika mchakato wa viwanda. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ulega naomba nikuahidi tutakupa ushirikiano wa kutosha kujenga miundombinu yetu ya barabara za lami katika maeneo yetu.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali fupi la nyongeza. Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji ningeomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie sawa na jibu lake la msingi ya kwamba kazi mojawapo ya Polisi ni ulinzi wa raia na mali zao. Je, Serikali inawahakikishiaje wananchi wa Wilaya hii ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji juu ya usalama wao na wa mali zao kipindi hiki cha operesheni ya kutafuta wahalifu ili waweze kufanya kazi zao kwa uhuru bila ya kubigudhiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Mkuranga, Kibiti na Rufiji kama ambavyo kila mmoja anafahamu kwamba limekuwa na changamoto ya matukio mbalimbali ya uvunjifu wa amani ambapo mpaka sasa hivi kuna raia wengi wamepoteza maisha, pia mnakumbuka hivi karibuni Askari wetu takribani nane walipoteza maisha kwa mpigo. Mimi binafsi nilifanya ziara katika maeneo hayo ambayo nimeyazungumza na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi. Katika mambo ambayo tumeyazungumza alifanya ziara Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi; kuna mambo makubwa matatu ambayo tumeyasisitiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, tumeendelea kuwasisitiza wananchi kulisaidia Jeshi la Polisi kutoa taarifa juu ya matukio ya uhalifu na wahalifu ambao wanawashuku katika maeneo yao ili kazi ya Jeshi la Polisi iweze kuwa rahisi. Pili, tumeendelea kuwahakikishia wananchi wa Mkoa huo kwamba Serikali itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba kwamba amani na usalama wa wananchi wa maeneo hayo linakuwa ni jambo la kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanya hivyo ni lazima Jeshi la Polisi liwe karibu na wananchi vilevile, wananchi wawe karibu na Jeshi la Polisi na Jeshi la Polisi liwe karibu na wananchi, kwa maana ya kujenga mahusiano mazuri kati ya pande hizi mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kukiomba kwa Mheshimiwa Mbunge akiwa Mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Mkuranga pamoja na Wabunge wengine wa maeneo yale, kuhakikisha kwamba wanaendelea kuwaelimisha wananchi waendelee kuwa karibu na Jeshi la Polisi, kuwasaidia kupata taarifa mbalimbali za uhalifu wakati huu ambapo Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla inafanya jitihada kuhakikisha kwamba maisha ya wananchi wa maeneo hayo yanalindwa pamoja na mali zao, pamoja na maisha, usalama wa Askari wenyewe ambao wanalinda usalama huo wa raia.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa rufsa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo haya yaliyopo kwenye Mkoa wa Katavi yako pia katika imo jimbo langu la Mkururanga kilometa 60 tu kutoka katika Mkoa wa Dar-es salaam ambapo kata za Kwanzuo Kisegese, Mkamba na kwingineko ikiwa ni pamoja na kijiji ambacho wewe unalima kijiji cha Koragwa Tundani na pale Mkuranga maeneo ya Kiguza. Yote yana shida ya mawasiliano.
Je, Mheshimiwa Naibu yuko tayari yeye na hao viongozi wa huo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kushirikiana name kuhakikisha maeneo haya yanapata mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwa dhati kabisa niko tayari.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba inaondoa migogoro hii ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo na kwetu sisi wakulima wa korosho, hapa juzi Serikali imetutangazia kutupatia sulphur kwa maana ya pembejeo ya kilimo bure. Je, Serikali imejipangaje katika usambazaji wa sulphur hii ya bure ili iweze kutufikia kwa wakati na ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuja kueleza wakati wa hotuba ya bajeti yetu Ijumaa kuhusiana na hatua mbalimbali ambazo tumechukua kuboresha mifumo ya usambazaji wa pembejeo katika mazao mbalimbali ikiwepo zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niseme tu kwamba sulphur itagawiwa kwa utaratibu ambao umewekwa na Bodi ya Korosho. Kimsingi, hatuamini kwamba itawezekana tena sulphur ichelewe, kwa sababu kwa sasa maana yake inakuwa inatolewa bure na yule ambaye anagawa inakuwa ni Bodi. Kwa hiyo, tusubirie tutasikia kuhusu huo utaratibu.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu kuhusiana na ujenzi wa kituo cha mabasi ya Kusini katika eneo la Jimbo la Mkuranga; na kwa kuwa uratibu wa zoezi zima la ujenzi wa kituo cha mabasi ya Kusini linasimamiwa pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuhakikisha wanashirikiana vema, Wizara ya TAMISEMI, Maliasili na nyingine zinazohusika kuhakikisha kituo hiki cha mabasi ya Kusini kinapatikana kwa haraka katika eneo la Wilaya ya Mkuranga hasa maeneo ya msitu ule wa Vikindu? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba ujenzi wa vituo hivi vya mabasi ni uwekezaji mkubwa sana na ni vyanzo vikubwa vya mapato kwenye Halmashauri zetu. Ukizingatia Sheria ya Fedha ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, huwezi kwa namna yoyote ile ukafanya mradi kwenye mamlaka ya Serikali ya Mtaa husika na mradi ule ukawa na wadau wengi nje ya utaratibu wa kuibua na kutekeleza mradi ule kutoka kwenye Halmashauri husika.
Kwa hiyo, kwa kuzingatia dhana ya ugatuaji wa madaraka (D by D), katika kusimamia sisi kama TAMISEMI tutajaribu sana kuhakikisha kwamba miradi hii ya vituo vya mabasi itafanywa na mamlaka za Serikali za Mitaa husika kwa kushirikiana na wadau wowote whether ni PPP au kwa kushirikiana na taasisi zetu za Mifuko ya Jamii, kwa vyovyote vile lakini mwenye mradi na mmiliki wa mradi atakuwa ni Halmashauri husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kumueleza kwamba sisi kama Serikali kwa kushirikiana na TAMISEMI na Wizara ya Maliasili tutakuwa tu ni facilitator lakini pia kuwaondolea vikwazo ili waweze kutekeleza mradi huo. Hii naisema ni kwa maeneo yote, kwa Mbezi Luis lakini pia kwa Boko, utaratibu utakuwa ni huo huo.(Makofi)
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu hayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa ni wa muda mrefu sasa, wao wenyewe wameridhi kutoka kwa wazazi wao ambao wameshafariki, na wao wenyewe miongoni mwao wanaelekea kuwa watu wazima sasa, ni lini Serikali itawalipa haki zao wananchi hawa, ilimradi wale warithi wao wasisumbuke kama ambavyo wao sasa hivi wanavyoishi, wakiwa hawaelewi ni lini watalipwa pesa zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu la swali la msingi, ni kwamba wananchi hao waliowekewa alama ‘X’ hawatakiwa kufanya maendelezo, lakini hawatakiwi kubomoa nyumba zao, wataendelea kuzitumia mpaka pale Serikali itakapokuja kuyatwaa maeneo hayo kwa ajili ya upanuzi au ujenzi wa barabara.
Kwa sasa kwa wale ambao wako ndani ya mita 22.5 wanatakiwa wabomoe na waondoke wakajenge sehemu nyingine. Wale ambao wako kati ya mita 22.5 na mita 30 wanaendelea kuyatumia maeneo yao mpaka pale Serikali itakapolitaka hilo eneo, na ndipo uthamini utafanyika na fidia watalipwa. Tumetoa hizo alama ‘X’ barabara zote Tanzania nzima, sidhani kama ni sahihi kwamba wewe uliyewekewa alama ya kijani ya ‘X’ ulipwe fidia nchi nzima hata bajeti yote tukiitumia kulipa fidia haitatosha. Kwa hiyo, tutakuwa tunalipa pale tu ambapo sasa tunataka kuanza kulitumia hilo eneo. (Makofi)
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Spika, asante sana, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu lake lenye kuleta matumaini ya kwamba siku moja na sisi watu wa Mkoa wa Pwani tunaweza tukapata madini ya dhahabu, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza ninependa kujua ni lini sasa Wizara itaanza kukitumia kisima cha gesi kilichopo katika eneo la kijiji cha Kiparang’anda ndani ya Wilaya ya Mkuranga ili kiweze kupata na kutuletea faida watu wa Mkuranga na Taifa letu kwa ujumla?
Swali la pili, ningeomba Naibu Waziri wa Nishati na Madini anieleze Wilaya ya Mkuranga tunachimba madini ya aina ya mchanga, madini ambayo kwa sasa Mkoa wa Dar es Salaam hayachimbwi yanachimbwa tu Mkuranga. Je, Wizara iko tayari kushirikiana na sisi watu wa Mkuranga kuboresha ushuru na tozo mbalimbali ili madini haya yaweze kuleta tija kwa watu wa Mkuranga?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Ulega, tumeshirikiana na wewe sana katika suala la mchanga na wananchi wa Jimbo lako najua wananufaika sana, kwa hiyo, hongera kwa hilo Mheshimiwa Ulega.
Mheshimiwa Spika, labda nianze na lini kwamba gesi asilia itaanza kutumika maeneo ya Kiparang’anda. Shughuli zinazofanyika sasa katika eneo la Kiparang’anda ni ukamilishaji wa utafiti wa madini ya gesi asilia na Kampuni ya Moran and Promi inakamilisha sasa, Mheshimiwa Ulega madini haya ya gesi asilia yataanza kutumika kwenye eneo lako baada ya utafiti kukamilika mwezi Agosti, 2018 na wananchi wa Mkuranga wana matumaini makubwa, kwa hiyo jitihada zinafanyika ili kuhakikisha kwamba gesi asilia inakamilika na mwakani yataanza kutumika maeneo ya Kiparang’anda na maeneo mengine ya Dar es Salaam pamoja na Pwani kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na madini ya mchanga, Mheshimiwa Ulega nikupongeze sana, eneo la Pwani kwa ujumla wake jumla ya hekta kama 182 zinatumika sana kwenye uchimbaji wa madini ya mchanga pamoja na kokoto. Kinachotakiwa wakandarasi wote na nitumie nafasi hii kuwataka wakandarasi wote kwa niaba yako Mheshimiwa mwenye Jimbo la Mkuranga waanze sasa kulipa tozo za Serikali za Mitaa kwa mujibu wa sheria ambayo ni 0.3%. Lakini pia waanze sasa kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa sababu ni takwa la kisheria, lakini nitumie nafasi hii kuwaagiza Wakurugenzi wote nchi nzima sasa waanze kuyataka makampuni yanayochimba mchanga, kokoto kuanza sasa kutoa ushuru katika Serikali za Mitaa ili wananchi wa Mkuranga na Tanzania nzima wanufaike kwa ujumla wake.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Jimbo langu la Mkuranga liko tatizo la wafanyakazi wanaofanya kazi katika viwanda hivyo vya Wachina, kulipwa malipo madogo kwa muda mrefu wa kazi. (Makofi)
Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuja Mkuranga kuonana na vijana wale wanaofanya kazi katika viwanda vile na kuzungumza nao na hatimaye kuweza kuwapa matokeo ya kuweza kuwasaidia kama Serikali?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA, NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ulega (Baba Tulia) kama ifuatavyo:- (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Ulega, ni kweli amewaleta hao wafanyakazi mpaka ofisini kwangu na anafuatalia sana suala hilo. Nami kama Waziri, naomba nimhakikishie kwamba tutampa ushirikiano. Tutaangalia Sheria inataka nini na hao wawekezaji ni kwa kiasi gani wanavunja sheria ambazo ziko katika nchi yetu, basi ninathubutu kusema kwamba nitaongozana na Mheshimiwa Ulega (Baba Tulia) kwenda katika maeneo hayo anayoyasema na tutapanga utaratibu. Ila tu tutamwomba mtoto Tulia asiingilie utaratibu wa ziara yangu na Mheshimiwa Ulega kwenda kuangalia matatizo hayo.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba kwa namna ya kipekee kabisa wakati nikijielekeza kuuliza swali hilo niipongeze sana Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanya ya kuwalinda wakulima wetu na wananchi wetu wa hali ya chini. Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hiyo pia nimpongeze Mkuu wetu wa Mkoa Engineer Evarist Ndikiro kwa kazi nzuri aliyoifanya mwaka wa jana wa kuyalazimisha Makapuni mawili ya Alpha Choice na Kaisari ambayo yaligoma kuwalipa kwa wakati wakulima wa korosho wa vijiji vya Msonga, Kalole, Mkuranga mjini na Kimanzichana Kusini. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu la msingi la Mheshimiwa Waziri anaeleza kwamba wanapochelewesha…
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Ahsante sana. Wanapochelewesha kulipa malipo ya wakulima wa korosho huchelewa. Je, Serikali ipo tayari sasa kuhakikisha inawasimamia ipasavyo na madhubuti kabisa wanunuzi hao ili wawe wanaondoa mazao yao katika maghala yetu mapema iwezekanavyo ili mzigo mwingine wa wakulima uingie kwa wakati na waweze kupata pesa za kuinua maisha yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona zao la korosho kama mfano wa namna ambavyo tunaweza tukafanya kilimo chetu kifanikiwe. Mafanikio makubwa na ya kihistoria ambayo yamepatikana katika korosho katika msimu uliopita ni kielelezo tosha cha namna Serikali ya Awamu ya Tano inavyotaka kushughulikia changamoto za kilimo. Kwa hiyo, hatutakubali mtu yoyote aje avuruge mafanikio yetu na ndiyo maana hizo kanuni zimeweka wazi kama unaenda ku-bid kununua korosho ni lazima kuweka dhamana. Hiyo inatusaidia kuwashughulikia wanunuzi wababaishaji ambao wanaenda ku-bid lakini baadaye korosho zinahifadhiwa halafu baadae wanakuja kulalamika kwamba zimepoteza sifa. Kwa hiyo, kwa sasa haiwezekani tena na niwahakikishie tu wakulima na Waheshimiwa Wabunge kwamba mtu yeyote ambaye ameshinda tender ya kununua korosho atalazimika kulipia na haiwezekani baadaye akaja kuleta malalamiko mengine, kwa hiyo, hilo halitatokea.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu haya ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu katika majibu ya msingi ameeleza kwamba Wilaya za Kibiti, Rufiji na Wilaya yangu ya Mkuranga ni miongoni mwa Wilaya ambazo wavuvi wake hajaomba mikopo. Inawezekana kabisa kutokuombwa kwa mikopo hii ni kutokana na ukosefu wa elimu ya kuweza kuwafahamisha na kuwawezesha waweze kuwa na uelewa wa kuomba hii mikopo.
Sasa swali langu, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie moja kwa moja ni lini tunaweza tukashirikiana sisi na wao ili kwa haraka zaidi Watanzania hawa wa Kisiju, Kibiti Delta na Rufiji mpaka Bagamoyo waweze kutumia fursa hii ya mikopo inayotolewa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ulega siyo mgeni sana kwenye Ofisi ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kwa hiyo, naendelea kumkaribisha amekuja mara nyingi sana kufuatilia changamoto za wananchi wake, aje ofisini hata akitaka leo mchana tuongee na tuangalie namna ya kufikisha elimu hii kwa ukubwa zaidi kwa sababu tayari Halmashauri zinatakiwa zitoe elimu kwa wavuvi na kuwafahamisha kwamba kuna fursa hiyo. Kama nilivyosema niko tayari kukaa naye tuweke mkakati wa kupeleka elimu zaidi.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana kwa kupata fursa hii. Kama ilivyoshida ya walimu katika jimbo la ndugu zangu wa Mbagala na sisi watu wa Mkuranga tunashida kubwa ya upungufu wa walimu. Serikali inanipa ahadi gani ya kuhakikisha kwamba upungufu ule wa walimu unapungua? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Ulega, kama alivyokuwa makini kusimamia shughuli za maendeleo katika jimbo lake, naomba nimuhakikishie kwamba katika mchakato huu wa sasa wa kuelekea kuajiri walimu Mkuranga tutaipa kipaumbele, na nikijua kwamba jimbo lako lile limetawanyika sana, tutakupa kipaumbele ili elimu kwa wananchi wa Mkuranga iweze kupanda na hatimaye waweze kupata mafanikio mazuri ya Serikali yao.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri napenda niongezee sehemu kidogo tu. Waheshimiwa Wabunge ni karibu maeneo mengi yana upungufu wa walimu na hasa kwenye shule zetu za msingi. Pamoja na jitihada za Serikali kuwapeleka walimu ambao wanaonekana wamezidi katika baadhi ya maeneo lakini baadhi ya shule bado walimu hao ni wachache, kwa sababu ya changamoto za miundombinu zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapopokea mipango ya Halmashauri na vipaumbele vyao inasikitisha kuona wakati mwingine mipango hiyo, na kwa sababu utawala wa nchi hii unatoka chini kwenda juu na si juu kwenda chini na ndio maana bajeti inaanza kupangwa kutoka chini baadaye juu tunakuja kumalizia, tungelitegemea vipaumbele viwe nyumba za walimu na miundombinu kama hiyo inayotegemea kujenga mazingira bora ya watumishi hawa kwenda kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokizungumza Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza swali la msingi inaonekana ni mazingira magumu ya kule milimani ya kule Same ndiyo maana walimu hawakai, hivyo ukijiuliza hakuna nyumba na hata walimu hawa wakifika uongozi tu wenyewe kuwapokeana kujenga mazingira mazuri ni vigumu sana, hawashughuliki nao, na ndiyo maana kuna upungufu.
Kwa hiyo niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, sisi ndio tunaoshiriki kwenye vikao vya maamuzi makubwa, sisi tunashiriki kwenye vikao ambavyo vinapanga mipango na bajeti. Tupange mipango hiyo inayotatua kero za nyumba za walimu ndipo tutakapoweza kuwa-retain walimu hawa katika shule zetu.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mji wa Mkuranga ni miongoni mwa miji inayokua kwa kasi sana; na kwa kuwa visima vya maji vilivyoko katika Mlima Kurungu vilishachimbwa na maji yanamwagika kuelekea mashambani; na kwa kuwa tumeshaomba shilingi milioni 800 Serikalini ya kuhakikisha tunayatoa maji yale ya Mto Kurungu kuyaleta Mkuranga Mjini na Vijiji vya jirani vya Kiguza, Dundani, Kiparang’anda, Magoza, Tengelea na kwingineko. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kunihakikisha kwamba milioni 800 zile tutazipata kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mkuranga na vijiji hivyo vingine nilivyovitaja?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Ulega, ni kweli ameniletea andiko kuhusiana na maji ya Mlima Kurungu. Maji ni mengi, yanamwagika, yanapotea na sasa hivi Wizara yangu tayari nimeshawakabidhi wataalam lile andiko wanalifanyia kazi. Nimhakikishie kwamba milioni 800 itatolewa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na wataalam washirikiane na Halmashauri ili yale maji yasipotee wananchi wayatumie. (Makofi)