Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Tunza Issa Malapo (39 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu na Chama changu makini CHADEMA kwa kunipa nafasi hii. Pia napenda kuwapa pole wananchi wa Mtwara Mjini kwa kadhia ya mvua waliyoipata siku ya jana, lakini hii yote imesababishwa na miundombinu mibovu iliyowekwa na Serikali ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia mpango huu nitajikita katika mambo mbalimbali. Mtwara imewekwa katika eneo la uwekezaji kwa maana ya viwanda, lakini tatizo kubwa la Mtwara ni maji ya kutosha kuhudumia viwanda. Mtwara Mjini kuna mradi unaotakiwa utoke Mto Ruvuma kuja Mtwara Mjini kuleta maji. Huu mradi umepitia process zote, kilichobaki ni kuwekeana saini kati ya Serikali ya China kupitia Exim Bank ya China na Wizara ya Fedha ya Tanzania, lakini huu mradi ulitakiwa uanze tangu mwezi wa Saba mwaka 2015 lakini mpaka leo haujaanza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri unayehusika, tunaomba mlifuatilie jambo hili ili tuweze kupata maji ya uhakika yatakayotosheleza kwa ajili ya kuhudumia hivyo viwanda vyetu.
Hatuwezi kuhudumia viwanda mfano, Dangote maji anayoyahitaji na maji yanayopatikana sasa hivi, akipewa yeye, maana yake sisi wananchi wa Mtwara Mjini hatuwezi kupata maji ya kutosha. Lakini suala la maji Mtwara Mjini, Serikali hailipi Idara ya Maji. Kinachotokea ni nini? Watu wa Idara ya Maji wameambiwa wajitegemee, wanajitegemea vipi wakati Serikali pale Manispaa ya Mtwara Mjini inadaiwa Shilingi milioni 581? Pesa zinakwenda, mpaka Mkuu wa Mkoa nyumbani wake anadaiwa Shilingi milioni moja na ushee. Kwa hiyo, tunachokisema, Serikali wapeni pesa Idara ya Maji waweze kujiendesha ili hata hivyo viwanda vinavyokuja viweze kufanya kazi. Maji ni muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitaongelea elimu. Nasikitika sana, kila yanapotokea matokeo yawe ya Darasa la Saba, yawe ya Form Two, yawe ya Form Four na kwingine kote Mtwara lazima iingie kwenye kumi za mwisho. Hii ni aibu na ni fedheha kwetu, hatupendi. Nataka niwaambie, shule tatu katika mtihani wa Form Two zilizofanya vibaya, matokeo yaliyotoka juzi juzi zimetokea Mtwara. Mbili kati ya hizo, zimetoka Tandahimba ambako kuna shida kubwa ya maji; na watoto wanaohangaika wanafeli ni watoto wa kike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia Mtwara ya Viwanda wakati elimu yetu iko chini. Ndugu zangu tusifanye mambo yale yale kila siku, tusifanye kazi kwa mazoea. Mimi ni Mwalimu wa Walimu, naelewa vizuri. Nimekuwa nikifanya kazi na wanafunzi katika Shule. Mwanafunzi hawezi kusoma kwa kumtolea ada ya Sh. 20,000/= mwanafunzi ili aweze kusoma vizuri, anahitaji apate vitabu, anahitaji akae pazuri, anahitaji ashibe, anahitaji apate maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wetu wa kike wa Mtwara, mnawalalamikia wanaolewa mapema, amefika Form Two maji yalikuwa yamhangaisha, amefeli, kinachofuata ni nini?
MHE. TUNZA I. MALAPO: Kwa hiyo, Serikali tunaomba muweke kipaumbele kwenye upatikanaji wa maji. Huu mradi wa Mto Ruvuma utahudumia vijiji 26; miongoni mwao vipo Mtwara Vijiijini na huko Mtwara Vijijini kuna shule ya mwisho imetokea huko kama sijakosea. (Makofi)
inatumiwa Bandari ya Dar es Salaam, wakati sisi tuna eneo kubwa. Kwa kuja kuwekeza kule na kui-upgrade hii bandari tunaamini vijana wenzangu kama mimi watapata ajira za kutosha na kuondokana na umaskini ambao unawatala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho maana naona muda umeisha, nataka kusema, Chama cha Mapinduzi kilitengeneza majipu kwa miaka 55, sasa wameanza kuyatumbua hatujui watatumia miaka mingapi! Kwa hiyo, ninachosema, wala msiwaaminishe wananchi kwamba mnafanya kazi kubwa, hayo majipu mliyatengeneza wenyewe. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naomba suala la maji lipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nauliza jambo moja, naomba ufafanuzi mtakapokuja kujumuisha. Suala la umeme; mimi najua mafuta yanakotoka bei inakuwa ndogo kuliko kwingine. Sisi Mtwara tunanunua mafuta bei kubwa. Kwanini umeme wote tunalipa sawa wakati unazalishwa kule kwetu? Tunalipa sawa na sehemu nyingine! Pia hilo naomba ufafanuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la elimu, mimi natambua kila Wizara ina Kitengo cha Sheria; na Wizara ya Elimu bila shaka itakuwa na Kitengo cha Sheria. Sasa kama Sheria za Elimu zimepitwa na wakati, zinaruhusu matamko ya Mawaziri yanayorudisha elimu yetu nyuma, Kitengo cha Sheria Wizarani wakae wachambue wasiwape Mawaziri mamlaka yanayodidimiza elimu yetu.
Mama yangu Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako, hapa katika kuzungumza, wanazungumzia Shule za Sekondari na Shule za Msingi. Nataka nikukumbushe kwamba kuna Vyuo vya Ualimu, ndiyo huko nilikotokea mimi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sehemu yenye matatizo katika tasnia ya Ualimu ni pamoja na Vyuo vya Ualimu. Watu wa Vyuo vya Ualimu naomba ukawasikilize. Sasa hivi wameingiziwa, kuna NACTE, kuna Wizara, kuna TSD, hawaelewi, wanayumbayumba. Nenda ukawasikilize, ujue matatizo yao, wanashindwa kufanya kazi. Nimetoka huko, mpaka nachaguliwa kuwa Mbunge, nilikuwa nafundisha Chuo cha Ualimu Mtwara kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea barabara. Sijui watu Mtwara tufanye nini ili mtusikie kuhusu barabara ya kutoka Mtwara Mjini, inapita Nanyamba, inapita Tandahimba, Newala Mjini mpaka Masasi. Tufanye nini ili mtusikie? Tunaomba mtujengee barabara. Korosho zinatokea huko kwa asilimia kubwa.
Mhesimiwa Mwenyekiti, vile vile Bandari yetu ya Mtwara kwanini hamtaki kui-upgrade? Kwa saabu ukisoma huu Mpango, asilimia kumi tu ndiyo inaonekana Bandari ya Mtwara na hizo nyingine, lakini asilimia kubwa
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu. Naunga mkono hoja za kamati zote tatu ambazo zimewasilishwa na wenyeviti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naanza kuchangia; mengi wenzangu wameyasema. Serikali kama ni ya kusikia itasikia lakini kama itafanya kama ilivyozoea miaka yote kwamba tunasema mwisho hatimaye yanayotendewa kazi ni machache basi wataendelea na utaratibu wao kwa sababu labda wanaona unafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ripoti za CAG pesa zinapigwa kwelikweli, yaani watu wanatumia pesa kinyume cha utaratibu tena bila woga. Mimi nimejipa muda kidogo nikasoma. Ukiangalia ile ripoti ya Hesabu za Serikali za Mitaa, nakupa tu mfano wa maeneo manne halafu uone ni pesa kiasi gani ambazo zimeliwa na wajanja wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza CAG ile ripoti ya Serikali za Mitaa anasema matumizi yasiyo na manufaa, yaani kwamba yametumika tu, ukiuliza yamefanya nini hakuna manufaa yoyote ambayo yanaonekana kwa wananchi, milioni 664 na point, ukurasa wa 275, kasome utakuta kaeleza vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine malipo ya bidhaa na huduma zisizopokelewa. Watu wameandika tutatoa huduma hii, tutaleta vifaa hivi lakini havikupokelewa, shilingi ngapi bilioni 8.44 watu wamekula na mambo yako kimya. Malipo yaliyofanywa bila kudai risiti za electronic; tunaambiwa ukiuza toa risiti, ukinunua toa risiti; mimi mwananchi wa kawaida tu nikienda kwenye kituo cha mafuta, nikinunua chochote nadai. Lakini Serikali hiyo inayosisitiza wanafanya manunuzi risiti hakuna, shilingi ngapi; bilioni 6.07. Hapa sizungumzii namba tu nazungumzia pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo Mheshimiwa Deo Utumishi simuoni Mheshimiwa Jenista mimi nahudumia Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI); kila siku za Mungu tunakuja kufundishwa mifumo, kwamba kuna e-government lakini mpaka leo ripoti ya CAG siyo maneno yangu mimi leo sisemi ya kwangu. CAG anasema hivi mpaka mwaka unaoishia Juni kuna wafanyakazi wamelipwa ambao hawako kazini. Mifumo ipo lakini waliostaafu wamelipwa milioni 343. Mifumo ipo inajua Tunza unastaafu lini lakini unalipwa. Watoro kazini wamelipwa milioni 81 mifumo ipo Mheshimiwa Deo. Waliofariki wamelipwa milioni 63 mifumo ipo, wengineo, yaani ambao hawaeleweki tu. Hawa ambao walistaafu, watoro, ambao hawako kazini ni wengineo, sasa sijui CAG alikuwa na maana gani; maana hawa walikuwa wanarandaranda, tu wamelipwa milioni 68, na mifumo ipo na kitengo cha mifumo kipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nahudumia Utawala na Serikali za Mitaa ambayo ndiyo kamati yangu. Tumekwenda kuangalia mifumo, wataalamu wa mifumo wapo kwa nini haya mambo yanatokea? Maana watu wanapiga tu, huku tunasifia mama anaupiga mwingi anapita kutafuta hela huku watu wanakula na siku zinakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko kwenye ulimwengu wa sayansi na teknolojia. Leo tunaambiwa Kariakoo ilipoungua moto na nyaraka zote za mapato na matumizi zimeungua, yaani hazijulikani. Shilingi ngapi sasa hizo tunazungumzia? tunazungumzia bilioni 3.562; ni hela nyingi. Tupo tuna mifumo na kuna watu wanalipwa lakini tunaambiwa Kariakoo ilipoungua moto na mambo yote yameungua. Kwakweli kama taifa hatupo serious. Kwa sababu, sasa hivi wewe ukiwa na simu yako ikaibiwa unaweza ku-recover data zako; sikwambii kitu ambacho kinaingiza mapato mengi hivi kwa nchi. Unaambiwa soko la Kariakoo lilipoungua moto basi kila kitu kimeungua. Haya si maneno yangu ni maneno ya CAG, someni ripoti mtaona. Wameshindwa kuleta udhibitisho hizi hela ziko wapi, hakuna, vimeungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na MSD. Watu wamechangia MSD mimi nikasema ngoja kwanza nikasome.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Naibu Waziri Utumishi na Utawala Bora Mheshimiwa Deo Ndejembi.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpatia taarifa Mheshimiwa Tunza Malapo ambaye kweli Mheshimiwa ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, ambayo inatusimamia sisi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimtoe mashaka yeye na wewe Mwenyekiti na Bunge lako. Hiyo taarifa baada ya kuwa imetoka Serikali hii ya Awamu ya Sita, kwa kuwa ni Serikali makini sana, imehakikisha mfumo wa HCMIS, umetengenezwa kupitia Wakala wa Serikali Mtandao (e- GA), na tayari mfumo huo umeanza kutumika Mei, mwaka jana. Hivi sasa kuna kitu kinaitwa auto- termination. Mtu akishafika umri wa miaka 60 automatically anatolewa nje ya mfumo. Wakati CAG anafanya ukaguzi wake mfumo huu ulikuwa bado haujaanza kufanya kazi; lakini kwa sasa mtu yoyote anayetoka nje ya utumishi wa umma tayari kuna auto- termination.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii Mheshimiwa Tunza, iko makini sana chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, na yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais ametuelekeza kuhakikisha tunakwenda kwenye mifumo zaidi na Ofisi yake hii ya Utumishi, nawe ni shuhuda tumekuonesha hata huu mfumo wa HMIS namna unavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha taarifa.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Tunza Malapo, unapokea taarifa?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa yaani ipo half half. Upande naweza kuipokea na upande siipokei. Siipokei kwa maana ipi? Hawa wanakuwa wana-exit meeting, yaani haya yote wangeelezana huko CAG asingeendelea kuyaleta. Yaliwashinda wapi kumweleza? Kwa hiyo, hapa ndiyo maana nikasema, leo siongea maneno yangu, naongea kutoka kwenye ripoti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hizi ni fedha za wananchi walipa kodi, kwa hiyo, ndiyo maana nasema, kwa upande mwingine kama mmeutengeneza mfumo, niwapongeze. Sina roho mbaya, nawapongeza mfanye vizuri, haya mambo yasijitokeze, kwa sababu hizi fedha zingeweza kusaidia mambo mengine. Hiyo ndiyo hoja yangu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na MSD. Nimesoma ripoti ya CAG kuhusu MSD. Wenzangu wameongea vizuri tu. Sasa (MSD - Medical Stores Department), yaani Bohari Kuu ya Dawa Tanzania, maana yake Bohari, yaani ukisema tu neno bohari, ni kama godown, sehemu ambayo watu wanahifadhi au vitu vinahifadhiwa. Tunategemea nini? Tunategemea tukute wataalamu wa kumbukumbu, wataalamu wa kuhifadhi vitu. Kinachoingia mwanzo ndiyo inabidi kitoke mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye ripoti ya CAG jambo la ajabu kabisa anasema hivi, halmashauri zinapelekewa dawa ambazo zimekaribia kwisha muda wake. Kwa nini zinapelekewa hivyo? Kwa sababu watu wa MSD hawana utaratibu mzuri wa kutoa dawa. Labda yeye ananunua huko anaponunua kwa wazalishaji, leo hii tunaongelea Novemba, dawa nyingine ananunua Januari, anaacha kuitoa hii ya Novemba iende kwenye halmashauri, anaenda kutoa ya Januari. Kitu kama hicho ninyi mnaamini? Binafsi siamini. Ninachoona, kuna madili yanapigwa. Labda wanaenda kununua dawa huko za bei nafuu ambazo zimekaribia ku-expire halafu wanafanya dampo halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakupa mifano michache, leo mimi nina ripoti tu ya CAG hapa na namba na kila kitu. Dawa zinazohitaji kuteketezwa mwaka huu ulioshia Juni, Shilingi bilioni 3.5. Bilioni! Nikaenda kusoma sasa, ni halmashauri gani hizo zinazoenda kuteketeza dawa? Katika hizo halmashauri 46, halmashauri nne zinatoka Mkoa wa Mtwara. Halmashauri ya Wilaya ya Masasi dawa za Shilingi bilion
188. Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Shilingi milioni 97, Hamashauri ya Mji wa Newala Shilingi milioni 119, Hamashauri ya Wilaya ya Tandahimba, Shilingi milioni 76. Hizi ni fedha. Dawa zenye thamani ya fedha hizi zinaenda kuteketezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikajiuliza, hivi kweli Wamakonde wenzangu wanavyoumwa, wanakwenda hospitali wanaambiwa dawa hakuna, leo unasikia dawa za fedha zenye thamani hiyo zinakwenda kuteketezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa nia ya dhati kabisa, tuongeze azimio lingine kwenye maazio ya LAAC, tuseme hivi, hawa MSD wasipeleke dawa halmashauri ambayo labda bado miezi sita ku-expire, wapeleke dawa ambazo zina mwaka, zina miezi 24 kulingana na shelf life ya dawa. Wanachofanya MSD wakishaona hawajafanya utaratibu mzuri, dawa zinakaribia ku-expire ili lile bomu lisiwalipukie wao, wanachukua mzigo wanapeleka halmashauri. Kwa hiyo, kule wanafanya dampo. Sasa halmashauri tuongeze azimio. Halmashauri zisipokee dawa ambazo zimekaribia ku-expire, waziache hapo hapo bohari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua mpaka moyo unauma. Unateketeza dawa za Shilingi bilioni saba! Mwaka 2018/2019 wameteketeza dawa za shilingi bilioni 7.3, mwaka 2019/2020 dawa za shilingi bilioni 1.5, hapo ilipungua, tunashukuru. Sasa maajabu na kweli mwaka 2020/2021 wanaenda kutekeza dawa za shilingi bilioni 3.5. This is not fair. Siyo sawa! Kwa hiyo, watu wa Bohari Kuu tunaamini ni wataalamu, kama ni wataalamu, wafanye mambo kitaalamu, hizi ni fedha za walipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanaumwa, wewe mwenyewe ni shahidi, ukiwa kama Mbunge, hivi umewahi kuwachangia watu matibabu mara ngapi? Halafu leo uambiwe dawa za fedha zote hizi zinateketezwa. Huu ni uzembe wa hali gani? Tuweke azimio kuhusu MSD. Unajua watu wanatufanya sisi kama hatujielewi, lakini sisi tunajielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwenye Bodi ya Mikopo. Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inafanya mambo, kuna mengine nimejipa muda nimesoma. Kulingana na sheria yao, wao wanatakiwa wa-support wanafunzi wanaosoma shahada, lakini kuna maagizo yanatoka Wizarani. Wizara ya Elimu walipieni wanaosoma Diploma, hiyo ndiyo ripoti ya CAG inavyosema. Sasa hayo ni matatizo, lakini CAG pia anakwenda mbele anasema, kuna wanafunzi karibia 500 wana-drop kwa sababu ya kukosa ada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani mwanachuo kasoma mwaka wa kwanza, mwaka wa pili anakosa ada, ana- drop. Kwa hiyo, tunaposema kwamba shule za msingi na sekondari wana-drop na Vyuo wana-drop. Wizara ya Elimu inashindwa kusimamia Bodi ya Mikopo. Wamewaacha pale wakati wajibu wa kuwasimamai Bodi ya Mikopo ni wa kwao, wasikwepe jukumu, wawasimamie. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, Serikali ina mkakati gani wa kukuza utalii wa fukwe hasa katika Mkoa wa Mtwara, fukwe za Bahari ya Hindi ambazo ni nzuri na bado hazijachafuliwa lakini uwekezaji wake upo duni sana. Hali hii inanyima fursa mbalimbli katika mkoa wetu. Pale Msimbati kuna fursa kubwa ya uwekezaji katika utalii, Serikali inasema nini?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. TUNZA I. MALAPO:Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika Wizara hii ya Elimu, mimi nitajikita zaidi kwenye vyuo vya ualimu kwa sababu nina experience huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vya ualimu wamebadilisha mtaala kwa mfano chuo ambacho kilikuwa kinafundisha diploma ya ualimu wa ngazi ya sekondari unakuta sasa hivi kimepangiwa diploma katika ngazi ya elimu ya awali. Mtaala huo umebadilishwa sijui kwa vigezo vipi, sijui kwa tafiti zipi sasa mbaya zaidi mtaala umebadilishwa, wakufunzi hawajui nini wanachotakiwa kufundisha, mtu anapewa kozi pale mwezi mmoja ama miwili unatafuta material hujui uanzie wapi, hakuna kitabu, hakuna rejea na kama rejea zipo zimeandikwa kwa lugha ya kiingereza lakini wale watoto tunatakiwa tufundishe kwa lugha ya kiswahili; shida sio kutafsiri lakini ipi ni tafsiri sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukichezea elimu utafikiri ni kitu ambacho hakina msingi. Sera ya Elimu inasema elimu bure, Sera ya mwaka 2014 tumekubali elimu bure maana yake ni nini? Serikali inajinasibu wanafunzi wengi wanasajiliwa shuleni, shule za msingi lakini nataka niwaambie jambo la kusikitisha Mheshimiwa Ndalichako pita kwenye vyuo vya ualimu, nenda kaangalie capacity ya chuo ni wanafunzi 450 unakuta waliosajiliwa ni wanachuo 50; maana yake ni nini? Baada ya muda wanafunzi wale wa shule za msingi wataongezeka kuwa wengi lakini walimu hakuna, tunatengeneza kitu gani? Tusifanye vitu kwa siasa wakati tunaongezea wanafunzi pia tuhakikishe walimu idadi yao inaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naongea kwa ushahidi nenda Chuo cha Ualimu Mtwara Kawaida kaangalie capacity ya chuo na kaangalie wanafunzi misuse of resources.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaitwa Wizara ya Elimu, Teknolojia na huko inaendelea. Jambo la kusikitisha sana tunapoenda kwenye vyuo vya ualimu mtandao wa internet hakuna wa uhakika, maana yake mwalimu huyo hana vitabu vya uhakika, mtandao wa internet hakuna na kulikuwepo na programu inaitwa ICT implementation in teacher education.
Mheshimiwa Waziri unapokuja kuhitimisha naomba nipate ufafanuzi programu ile imefikia wapi, ukienda kwenye vyuo vya ualimu utakuta kuna kompyuta nyingi ni mbovu, mtandao wa internet hakuna kabisa, naongea kwa ushahidi, walimu wale mnataka wafanye kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia elimu hatuwezi kumuacha mwalimu. Wakufunzi wa vyuo vya ualimu na vyuo vya ualimu kwa ujumla wake vimeingia kwenye mfumo wa NACTE ingawa mimi sijui na sioni utekelezaji wake,
lakini mfumo ule wa NACTE una stahiki zake lakini mpaka leo tunapoongea baadhi ya wakufunzi wa vyuo vya ualimu wanalipwa kwa stahiki za Wizara ya Elimu, wanafanya kazi mpaka muda wa ziada kwa sababu ule mfumo una mambo yake, mwisho wa siku mtu analipwa kama bado anahudumiwa na Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunataka ufafanuzi wale watu wapo katika mlengo gani, kama mmeamua kuwapeleka NACTE wapelekeni NACTE na stahiki zao zote na kama mnaamua wabakie Wizara ya Elimu basi wabakie na stahiki zao zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza vyuo vya ualimu ni vichache siji tatizo ni nini, mnashindwa kukaa mkajua mahitaji ya wakufunzi mnashindwa kuboresha miundombinu, ukienda kwenye Chuo cha Ualimu Mtwara Kawaida nakiongelea kwa experience, mabwenini kule hali ni mbaya, unamfundisha nini mwalimu? Hali ni mbaya, miundombinu mibovu, madarasa yapo hayaeleweki yaani ule utanashati wa mwalimu unapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze kwenye vyuo vyote vya ualimu kulikuwa na shule za mazoezi, shule ya msingi ya mazoezi na shule ya sekondari ya mazoezi, lakini zile shule zote sasa hivi zimerudi TAMISEMI. Sasa naomba kupata ufafanuzi kila kitu ambacho kilifanya muanzishe shule shule za mazoezi ambazo sisi tuliokuwa tunafundisha kule tuliona umuhimu wake kwa nini sasa hivi shule hizo zimerudishwa kupelekwa TAMISEMI?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ule umuhimu umepotea ama kuna kuna kitu gani hapo kilichopo katikati? Tunaomba ufafanuzi kwa sababu mwenyewe nimesoma shule ya mazoezi ya msingi na katika miongoni mwa shule ambazo zilikuwa zinafanya vizuri ni shule za mazoezi na pia wale wanachuo wa ualimu walikuwa wanaenda kufanya practice kwenye shule za mazoezi. Lakini sasa hivi, ukitaka kuitumia ile shule ni lazima uende ukaombe kibali TAMISEMI na vitu kama hivyo, kwa hiyo kuna mzunguko mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mikopo. Mheshimiwa Waziri juzi nimekuona ukiitumbua TCU, mimi nasema umechelewa sana kwasababu malalamiko yalikuwa mengi ya muda mrefu. Watoto wa maskini ambao wana stahiki ya kupata mikopo hawapati, watu wanapeana mikopo kwa kujuana, tunaomba hilo suala ulifuatilie na wale wote waliohusika wawajibike na wale ambao walishindwa kusoma kwa sababu ya mikopo na sifa wanazo tunaomba wasome kwa sababu ni haki yao ya msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenzangu asubuhi hapa ametoka kuongea, kuna vyuo vinafundisha masomo ya sayansi lakini havina maabara, Vyuo vya Ualimu. Tunategemea tunazalisha watu wa namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo mwalimu leo unamfundisha kwa alternative to practical, unataka akifika shuleni umejenga maabara kwa kuwakimbiza wazazi, kwa michango mbalimbali, unataka akafundishe real practical, is it possible? If it is not possible we should be more serious ili elimu yetu tuione inapaa.
Mimi kila siku nasema masomo ya sayansi sio magumu ila mfumo wa elimu ya Tanzania ndio unapelekea masomo ya sayansi yawe magumu, masomo ya sayansi is very simple, ukipata mazingira wezeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaeongea hapa nimesoma PCB na nimefaulu kwani hao wanaofeli wamekosa kitu gani? Ni mfumo mbovu, mazingira mabovu, tunatakiwa tuone namna ya kuweka miundombinu yetu vizuri ili watoto wetu wasome kila mtu ana uwezo wa kusoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti …
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua Serikali imejipangaje katika mambo yafuatayo kwa Wizara hii:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyuo vya Ualimu baada ya kupelekwa NACTE vimekuwa vikikosa wananfunzi wa kutosha kulingana na capacity ya Chuo na ukilinganisha na idadi kubwa ya wananfunzi wanaosajiliwa katika shule za msingi kutokana na Sera ya Elimu Bure. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha nchi yetu inakuwa na walimu wa kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyuo vya Ualimu vimeingia NACTE, lakini stahiki za Wakufunzi bado hazijabadilishwa kuendana na mfumo wa NACTE. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Wakufunzi nao wanapata stahiki zao vizuri bila ubabaishaji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Je, Serikali imejipangaje kuzuia ombwe kubwa la Walimu kuacha kazi na kutafuta kazi nyingine hivyo kupelekea ukosefu wa Walimu hasa katika shule za Vijijini mfano, katika Mkoa wa Mtwara, ambao mimi ninauwakilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vyuo vingi vya Ualimu vinafundisha masomo ya sayansi, lakini havina maabara. Hivyo, kufanya ufundishaji na ujifunzaji uwe mgumu na kadhalika. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha maabara hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliahidi kuwakopesha wanachuo, ambao wanasoma katika vyuo vya ualimu masomo ya sayansi, lakini haijafanya hivyo, ni kwa nini na kuna mpango gani uliowekwa kuhakikisha ahadi hiyo inatekelezeka kwani inawanyima haki wanachuo hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vingi vya Ualimu havina mtandao wa internet wa uhakika. Je, Serikali inalijua hilo na imejipangaje kuhakikisha mtandao unapatikana ili kuwezesha ufundishaji na ujifunzaji unaenda vizuri ukizingatia hakuna vitabu vya kutosha katika vyuo hivyo.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya napenda kuzungumzia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula. Hospitali ile imepandishwa kuwa ya Rufaa ya Mkoa lakini jambo la kusikitisha sana tena naomba mnisikilize na Mheshimiwa Kigwangalla nilikufuata nikakuuliza lakini haukunipa majibu. Hatuna mtaalam wa x-ray wa uhakika, vijana wetu wanapopata matatizo ya kuvunjika miguu na kadhalika, ni kama sawa mtu anaendelezwa kwenda kutiwa kilema, kwa sababu karibu watu wengi wanaofungwa mikopa (P.O.P) pale wanaopata tiba za mifupa hakika tiba zile siyo za uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha zaidi inabidi watoke kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa waende Ndanda ama Nyangao bila Rufaa kwa sababu zile ki-rank ni ndogo kuliko hii ya Rufaa ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mtuangalie, mmeipandisha hadhi sawa tunashukuru, lakini tukienda kwenye wodi ya wazazi vitanda ni vichache mno, mtu ametoka kwenye uchungu wa kujifungua anaambiwa alale kitandani watu watatu. Nina uhakika ninachokizungumza, nilikaa pale wiki mbili namuuguza wifi yangu hali iko hivyo, haijalishi huyu mtu kajifungua kwa operation, ama kajifungua kawaida. Kwa hiyo, tunaposema hali ni mbaya ninamaanisha hali ni mbaya kwa sababu ni kitu ambacho nakijua nanime- experience. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu duka la MSD la Kanda ya Kusini linaenda kujengwa Ruangwa kwenye Jimbo la Waziri Mkuu, sina shida na hilo. Shida yangu kubwa iko wapi, kama kweli mnakujua Ruangwa, Ruangwa ni ndani barabara ile ya kilometa 45 kutoka Nanganga kwenda Ruangwa ni ya vumbi na kipindi cha masika hakufikiki. Barabara ile na Jimbo la Ruangwa lipo ndani haliunganiki zaidi na Wilaya zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini duka hili lisikae Masasi ambako ni centre mtu wa Tunduru analikuta, mtu wa Mtwara analikuta, mtu wa Lindi na anayetoka Newala analikuta, kwa nini lisikae pale mkaamua kwenda kulipeleka kule? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kama mnaona kabisa ni lazima liende likakae Jimboni kwa Waziri Mkuu, mtengeneze zile kilometa 45 za barabara ili kusudi watu wanapoenda kuchukua madawa wasihangaike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu dawa za watu wenye ulemavu wa ngozi. Siku ya maadhimisho ya wanawake nilienda shule ya msingi Masasi ambayo inatoa elimu jumuishi. Nimewakuta watoto pale takribani 39 wenye ulemavu wa ngozi, wana ari ya kujifunza lakini yale mafuta hawapati.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninakuomba muwafikirie watoto wale ili nao wapate haki yao ya elimu. Pia kuna watoto wenye uoni hafifu na ambao hawaoni kabisa lakini vifaa vya kujifunzia vya kutosha hakuna, hivyo wanashindwa kupata haki yao ya elimu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya nafikiri mna jukumu la kuhakikisha watoto wale wanapata haki yao ya elimu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Mangaka ambayo inahudumia Nanyumbu. Hospitali ile imepandishwa hadhi kuwa ya Wilaya lakini haina x-ray. Kwa hiyo, naomba katika mpango wako Mheshimiwa Waziri, basi ufanye kila linalowezekana ili x-ray ile ipatikane iweze kuwahudumia watu wa Nanyumbu na majirani zao. Tunasema afya kwanza ili twende kwenye mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri ukurasa wa 76 amezungumzia suala la kuhakikisha wodi za watoto wachanga zinaanzishwa katika hospitali zote za rufaa. Namuomba Mheshimiwa Waziri suala hili lisiwe kwenye makaratasi na maneno… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami pia naungana na Wabunge wenzangu wa UKAWA kuona kitu kinachofanywa kulizuia Bunge hili lisioneshwe live si sahihi. Kwa sababu sisi ni wawakilishi wa wananchi, tumetumwa na wananchi kuja hapa kuwatetea, kuwasimamia na wanatamani watuone. Sijui hata huyo aliyeanzisha huu mjadala Bunge lisioneshwe live alichukua maoni kutoka wapi. Ama aliamka asubuhi kwa matakwa yake binafsi akaamua Bunge lisionehswe live. Mjue kabisa hamuwatendei haki wananchi, kodi zao mnachukua lakini hamtaki kuwatendea haki. Wananchi wanajua si kwamba ni wajinga kama mnavyowafikiria, kwa hiyo, hilo mkae kabisa mnalijua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kuchangia…
TAARIFA...
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili.
TAARIFA...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Malapo, naomba uendelee.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niende moja kwa moja kuchangia kwenye TAMISEMI na naanza na elimu. Kwa masikitiko makubwa sana, kama kila siku ninavyozidi kusema mimi ni Mwalimu lakini tunapozungumzia suala la elimu, tunakuja humu ndani tunajitutumua kusema kwamba tumedahili wanafunzi wengi, tumedahili lakini output yake itakuwaje? Hilo ni swali la msingi la kujiuliza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kitu cha kusikitisha, Mkoa wa Mtwara, wakati mnazungumzia Walimu hawana nyumba, lakini nataka kuwaambia katika ripoti ya Mkuu wa Mkoa ametuambia shuleni kuna upungufu wa viti elfu moja mia mbili kwenda juu. Kwa hiyo, Mwalimu huyo amelala sehemu mbaya, akienda shuleni pia hana sehemu ya kukaa. Tunavyolalamikia watoto wanakaa chini pia kuna Walimu wanakaa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, afya. Tukienda kwenye suala la afya kwa Mkoa wa Mtwara ni majanga. Natoa mfano mkubwa wa kusikitisha, ukienda Mtwara Vijijini kwenye Kituo cha Afya cha Nanguruwe mganga wa pale anatamani afunge kile kituo kwa ukosefu wa maji. Maji hayo pesa yake ilishatolewa shilingi milioni tano kurekebisha hitilafu iliyotokea ila kuna wajanja wachache wamekula. Kwa bahati mbaya hata ukienda kwa Mkurugenzi, sijui anamwogopa nani, hataki kutoa ushirikiano wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri alifuatilie suala la Kituo cha Afya Nanguruwe kwa sababu kituo kile kinahudumia watu wengi lakini mazingira yake ni mabovu, hakuna matundu ya vyoo ya kutosha, hakuna dawa, hakuna maji, wananchi wa pale kila siku wanalia. Naomba akifuatilie kituo kile ili tujue mwisho wake ni nini, watu wa pale wapate haki yao ya msingi kwa sababu na wao ni Watanzania wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye asilimia kumi kwa ajili ya akina mama na vijana, hili suala tunaomba lipewe kipaumbele. Ukienda Mtwara kwa tafiti zilizofanywa inaonesha asilimia 54 ya nyumba zinalelewa na akinamama kwa sababu labda waume zao wamefariki au matatizo ya ndoa yalitokea, kwa hiyo, wanahitaji wawezeshwe. Nami nasimama hapa kwa uhakika kabisa kusema kwamba wanawake na vijana wa Mtwara ni watu ambao wako tayari kutafuta maendeleo wanachokosa ni kuwezeshwa tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Wenyeviti pamoja na Madiwani. Unamlipa posho Mwenyekiti wa Mtaa Sh. 20,000 kwa mwezi tena si guarantee, kuna mwezi anapata, kuna mwezi hapati. Hata hivyo, tukumbuke kukitokea matatizo yoyote katika mtaa, Mwenyekiti ndiye wa kwanza kufuatwa na wananchi wake kwenda kulalamikiwa, tujiulize Sh. 20,000 anafanyia kitu gani? Diwani kwenye kata ana majukumu mengi mazito, posho mnayompa inamsaidia?
Mheshimiwa Naibu Spika, tujiweke tungekuwa ni sisi, wewe Mheshimiwa Waziri sasa ndiyo ungekuwa Diwani unalipwa ile posho wanayolipwa ungeweza kuendesha maisha yako? Hii inaweza kuwapelekea wale watu kufanya mambo ya kupokea ama kutamani kupokea rushwa kwa sababu ni binadamu, wanahitaji kuishi vizuri. Naomba tuwaangalie kwa sababu Udiwani ndiyo kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye suala la masoko ambapo katika Halmashauri ya Mtwara Mikindani ni chanzo pia kikubwa cha mapato. Kwa masikitiko makubwa nimetembea kwenye masoko manne ya pale hakuna soko hata moja lenye choo cha uhakika. Wananchi pale wanatozwa ushuru, wafanyabiashara wale wanatozwa ushuru, wanalipa kila siku lakini hatuna choo cha uhakika kwenye soko lolote, naongea kwa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, tuna vizimba vya takataka vimejengwa kwa masikitiko makubwa, sijui hata huyo injinia alikuwa anafikiria nini, kuna kizimba kipo mtaa wa Magomeni, chini yake limepita bomba la maji kubwa na maji yanamwagika pale, takataka zinaoza, funza wanatoka, wananchi wapo karibu lakini tunaambiwa Injinia wa Manispaa amekuja kujenga pale wakati anajua chini limepita bomba. Tunaomba vitu hivi mfuatilie kwa sababu sisi kila tukisema inaonekana tunaongea kisiasa, hatuongei kisiasa, tunawaongelea wananchi wale wanaoendelea kupata shida kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia suala la maji katika Mkoa wangu wa Mtwara. Ukienda Jimbo la Nanyamba kuna shida kubwa ya maji. Sisi kule tunasema watu wanatumia maji ya kuokota. Ukisikia maji ya kuokota maana yake mtu anakuwa amechimba kisima cha chini halafu anaelekeza mifereji, yale maji ya mvua yanayotiririka barabarani yanaingia kwenye kisima. Mwisho wa siku huyu mwananchi anakuja kunywa yale maji, tutaepukaje kipindupindu, tutaepukaje magonjwa ya matumbo yanayosababisha dada zetu wasishike ujauzito kwa sababu vizazi vinaharibiwa? Hali hii hatuitaki na tunaomba irekebishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa sababu ya muda, nataka niulize, Serikali ya Magufuli inafanya vizuri, kwa nini inaogopa kuwa transparency? Kwa nini haitaki kuonekana kama kweli inafanya vizuri, maana yake ina shida. Kama ingekuwa inajiamini Bunge lingeonekana live. Ninachosema, Serikali ya Magufuli haijiamini na ndiyo maana haitaki wananchi waone kinachoendelea. Hilo Bunge analosema linaoneshwa saa nne mimi jana nimeangalia, hakuna kitu, sasa mtu hapa anakuja kutuambia linaoneshwa, tuwe serious.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nataka niwakumbushe kidogo hili suala la vitabu kuonekana vina makosa humu Bungeni siyo jambo geni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka jana Mheshimiwa Susan Lyimo alisema hapa kwamba hivi vitabu vina makosa na Mheshimiwa Simbachawene alitoka kule kuja kuangalia na akajibu kwa mbwembwe na kejeli kwamba anachokisema Mheshimiwa Susan Lyimo siyo kweli. Sasa Mwenyezi Mungu kila siku yupo na wanadamu, nashukuru tu kwamba tumeona, kila mtu ameona ama amesikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Elimu, naomba uchukue hatua stahiki, tumepoteza pesa, lakini pia tumewapoteza watoto kwa maana wamepewa knowledge ambayo siyo sahihi. Wakati sijaingia Bungeni nilikuwa namsikia sana Mheshimiwa Mbatia anazungumzia mambo ya mtaala na vitabu vina mapungufu, lakini tumechukua hatua gani naona kila siku hali inazidi kuwa mbaya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Elimu nafikiri una jukumu kubwa la kuangalia na inawezekana kwenye somo la Sayansi labda alipelekwa mwalimu wa historia maana hivyo vitu vipo, watu wanaangalia zaidi mshiko (kipato) kuliko kuangalia maslahi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Vyuo vya Ualimu mwaka jana nililizungumzia na leo ninalizungumzia. Mradi wa ICT implementation katika Teachers Education; server zote sasa hivi kwenye Vyuo vya Ualimu ambako mradi ule umepita hazifanyi kazi, lakini ukifungua kitabu cha hotuba ya Waziri anazungumza zaidi mfano, hata pale ukurasa wa 27 anazungumza suala la kuhakikisha TEHAMA inafundishwa, kuhakikisha walimu wanaandaliwa na TEHAMA na vitu kama hivyo. Nikuhakikishie tuma watu wako ama nenda mwenyewe kwenye Vyuo vya Ualimu vingi kama siyo vyote hakuna computer na kama zipo ni mbovu na pia server hazifanyi kazi na wala hawapewi GB wala kitu gani, tunategemea hiyo TEHAMA itaendaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taarifa ya Kamati tuna upungufu wa vyumba vya madarasa 158,674; lakini kwenye bajeti mwaka ujao wa fedha tumetenga kujenga vyumba vya madarasa 2000 tu kama pesa itapatikana. Kwa maana hiyo, kwa mahitaji haya 158,674 kila mwaka tukijenga vyumba vya madarasa 2000 maana yake tutatumia miaka 79 ili tuweze kukamilisha. Nafikiri inatakiwa kuwe na mkakati wa makusudi, madawati tunajua yalipatikana yaliyo mengi mengine yapo nje yanalowa mvua yanaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshauri Waziri ili kusudi tuboreshe elimu yetu na watoto wetu wakae katika vyumba vya madarasa kunahitaji pia mkakati wa makusudi. Wakati wa kuhitimisha Mheshimiwa Waziri naomba anijibu maswali yangu haya rahisi, tunaposema quality education Tanzania tunamaanisha nini? Pia napenda kujua falsafa yetu ya elimu sasa hivi ni nini? Bado ni ile elimu ya ujamaa na kujitegemea ama kuna kitu kingine? Kama ndivyo basi tujue mitaala ambayo tunaitumia kweli inawafanya watoto wetu kwenda kwenye kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Wakaguzi ama sasa hivi wanaitwa Wadhibiti Ubora. Mheshimiwa Waziri nikuombe kile kitengo kipo chini yako, Wizarani kwako, naomba ukipe kipaumbele kwa umuhimu wake, kwa sababu bila ukaguzi kwenye elimu ni sawa na hakuna. Maana yake hawa Wadhibiti Ubora wa elimu ndiyo CAG kwenye elimu, ndiyo wanaangalia kila kitu na kujua kuna matatizo gani. Inawezekana hata hili suala la vitabu leo tusingekuwa tunaliongelea hapa kama wangekuwa wanafanya kazi zao vizuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wakulima wa korosho kuuza korosho zao katika minada tangu mwezi Novemba, 2017 mpaka leo hawajalipwa fedha zao linasababisha wakulima hawa kukosa fedha kwa ajili ya kujikimu, kusomesha watoto wao na pia kuandaa mashamba kwa wakati kwa ajili ya msimu wa mwaka huu. Je, Serikali imeshindwa kulisimamia suala hili ili wakulima hawa wapate fedha zao kwa wakati kwa ajili ya kutatua shida zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa mbegu bora za mazao mbalimbali unasababisha wakulima kupata mavuno kidogo ikilinganishwa na nguvu inayotumika kulima kwa sababu tu ya kukosa mbegu bora. Pia hata zikipatikana basi bei inakuwa kubwa sana ambayo mkulima wa kawaida anashindwa kumudu kununua. Ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wakulima wa mazao mbalimbali hapa nchini wanapata mbegu bora kwa ajili ya kufanya kilimo chenye tija?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji kinaleta tija? Mfano katika Mkoa wa Mtwara kuna bonde kubwa katika Kata ya Kitere, Mtwara Vijijini ambalo kama lingetumiwa vizuri lingesaidia uzalishaji wa kutosha wa zao la mpunga na kuwawezesha wananchi kujipatia chakula na kipato. Pia bonde hilo lingewezesha kulima mboga mboga kwa ajili ya biashara na matumizi mengine ya kifamilia. Ni nini mkakati wa Wizara utakaoleta tija kwa wakazi wa Mkoa wa Mtwara wenye mabonde yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, kama vile Kitere, Mahurunga na Ruvuma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupata ufafanuzi juu ya madeni yanayodaiwa na mawakala waliosambaza pembejeo za kilimo, kwa sababu kuna kauli zinazochanganya kutoka upande wa Serikali na mawakala, nani ni mkweli? Mawakala wanasema wanadai madai halali wakati Serikali inasema mawakala waongo. Je, Serikali imebaini nini baada ya kufanya uhakiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali imeshindwa kutoa bure pembejeo ya zao la korosho, ikizingatiwa kwamba zao hili linachangia pato la Taifa hili la Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la wakulima wa korosho kucheleweshewa malipo yao yaliyopitia benki, kwa hiyo nashauri Serikali kuzitaka benki kuwalipa wakulima mara moja pindi tu wanunuzi wanapolipa hela za wakulima.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia naomba tu niwaulize hawa Mawaziri wa Maji, hivi ni kwa nini ninyi hampewi hela? Kuna tatizo gani? Labda wakitueleza tutatoka hapo tukajua tuwasaidie vipi, kwa sababu tunajua sekta ya maji ni sekta muhimu, lakini ukienda kwenye pesa walizopewa za maendeleo ni asilimia 19.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunakaa hapa tunajadili, tunafanya nini, lakini mwisho wa siku utekelezaji finyu, kwa hiyo, wakati wanakuja kujibu watueleze kwa nini Wizara ya Maji haipewi pesa za kutosha?

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo ni lazima nichangie tu. Kuhusu Mfuko wa Maji, naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba, pesa ziongezwe kwa ile tozo kutoka shilingi 50/= kwa lita mpaka shilingi 100/=, lakini katika kuongeza huko naomba ile pesa ikiongezwa ikafanye jambo lililokusudiwa. Sisi lengo letu watu wa vijijini wapate maji, angalau ile pesa asilimia 70 ikatumike vijijini ili kuwawezesha akinamama wa vijijini wapate maji; isiwe kwamba ile pesa ichukuliwe ikafanye mambo mengine kama administration na vitu kama hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma. Mimi Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha hii hoja naomba aje na majibu. Kila siku wanatwambia mkandarasi yuko site anafanya hivi, anafanya hivi. Tunataka tupate jibu la uhakika, pesa ya kufanya huu mradi ipo ama haipo? Swali la kwanza. Hata hivyo, pale unapopita mradi wamewaambia watu wasiendeleze, lakini mpaka leo hakuna fidia yoyote waliyolipwa? Watu wale mnawaachaachaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Serikali ya China na Serikali ya Tanzania kwenye mradi huu tunaomba sisi watu wa Mtwara tupate maelezo ya kina kwa sababu mradi huu ukikamilika, kama kweli tunasema tunaitaka Mtwara ya Viwanda maji haya yatatusaidia kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye Manispaa ya Mtwara Mikindani; pale maji yapo ya kutosha, tatizo miundombinu. Miundombinu ya tangu mwaka 47 wakati watu wanavaa kaptula badala ya suruali ndiyo hiyo hiyo iko mpaka sasa hivi, haitoshelezi. Huwezi kuamini watu wa Mtwara Mjini kuna watu wengine ukienda mitaa ya Komoro wanachota maji, kule kwetu tunaita ya kuokota; unasubiri mvua inyeshe unachimba kisima unachota, hiyo ndiyo Manispaa ya Mtwara Mjini. Sasa nafikiri kuna haja ya makusudi kabisa Mheshimiwa Waziri wa Maji atueleze mikakati thabiti ya kuitekeleza ili kusudi tuepukane na matatizo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Mkoa wa Mtwara kwa matokeo ya elimu kila siku ni karibu unashika nafasi za chini; kwa mfano mwaka jana shule tisa katika 10 za mwisho zimetoka Mkoa wa Mtwara kwenye mtihani wa form two; na waathirika wakubwa ni watoto wa kike. Wanaathirika kwa sababu, pamoja na mambo mengine maji hakuna, wanatumia muda mwingi kwenda kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa cha kusikitisha Mheshimiwa Rais ametoa amri ya Kata Umeme. Kweli umeme umekatwa, umekatwa mpaka kwenye vyanzo vya maji, ukienda kwenye Mradi wa Makonde umeme umekatwa, wananchi wamehangaika maji hakuna.

Sasa najiuliza mwananchi wa kawaida akipelekewa maji nyumbani kwake bili analipa, wale wanaenda kukata umeme kwenye chanzo ambacho maji yale wanaowadai si wananchi wa kawaida; wanadai Jeshi, wanadai Polisi, wanadai Hospitali, lakini wanaenda kukata maji ambayo wananchi wote hawapati; wanaenda kukata umeme kwenye ule mtambo ambapo unasababisha wananchi wengine huku wote wasipate maji, hata wale ambao wanalipa bili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hilo hilo la kukata maji; kwa mfano ukienda katika Manispaa ya Mtwara Mikindani watu wa maji wanadai sana madeni. Ukiangalia wanadai Jeshi, wanadai Polisi, wanadai Hospitali, lakini na wao kwa sababu hawalipwi, wanadaiwa umeme! Ikafikia stage wakakata maji Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula siku nne. Niambie yule mama yule tunayemtaka akajifungue, yule mtoto anayeumwa anatibiwa katika mazingira gani? Mpaka maabara ilifungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo mimi nayaongea kwa uchungu sana kwa sababu wale watu wanateseka tatizo sio la kwao, tatizo la Serikali hii hampeleki hela za kulipia hizi huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Umwagiliaji. Naomba nipate maelezo ya kina, inavyoonekana issue ya umwagiliaji kwetu si kipaumbele. Sasa kama si kipaumbele watu wakilalamika njaa msiwazuie waacheni waseme, kwa sababu nina mfano. Kuna Skimu ya Umwagiliaji Mtwara Vijijini katika Bonde la Mto Kitere, ile skimu ilifunguliwa na mbio za mwenge mwaka 2014, lakini cha ajabu sijui walifungua kitu gani. Ndiyo maana sometimes tunasema mwenge tuuweke makumbusho! Walienda pale wametumia hela chungu nzima, wamefungua, lakini hakuna kinachofanyika. Sasa walifungua ili iweje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bonde lile likitumiwa vizuri sisi watu wa Mikoa ya Kusini naamini hatutahangaika kwenda kufuata mchele Ifakara, hatutahangaika kwenda kufuata mchele Mbeya. Mheshimiwa Waziri anakiri kabisa kwamba miradi mingi ya umwagiliaji ilifanyika kifisadi.

Sasa tunamwomba afanye jitihada za makusudi kuhakikisha miradi ile inafanya kazi na wale watu ambao walihusika katika kuhujumu miradi ile wachukuliwe hatua za kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, magonjwa mengi, karibu asilimia tisa ya wagonjwa wanaolazwa hospitali matatizo yao yanatokana na kutumia maji ambayo si safi na salama. Serikali inatumia pesa nyingi kutibu watu wetu. Kwa hiyo, ushauri wangu tuwekeze kwenye maji kwa sababu tutapunguza kutibu watu na kuwafanya watu wakose vizazi, kwa sababu haya magonjwa ya UTI na nini yanaenda kusababisha watu wengine wakose vizazi kwa sababu, vinakuwa vinapata matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala la uvunaji wa maji ya mvua, nafikiri wenzangu wengi wameliongea, tuweke msisitizo kabisa, tuweke mkakati maalum kama tunavyofanya mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa pesa nyingi za dawa zinapotea kwa ajili ya kununulia dawa za malaria. Wakati tuko kwenye Kamati tumefika Kibaha kwenye kiwanda kinachozalisha dawa za viuadudu, viluilui wa mbu, lakini kusema ukweli tumekuta hakuna jitihada za makusudi za kutangaza dawa ile ili watu waweze kuitumia na kuua yale mazalia ya mbu, ili watu wasing’atwe na mbu na kupata ugonjwa wa malaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namshauri Mheshimiwa Waziri watilie maanani utumiaji wa dawa hii kwa ajili ya kuua hivi vimelea, ili pesa ya kununua dawa za malaria ipungue na tufanye mambo mengine katika sekta ya afya kwa sababu, ina mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Hospitali ya Kanda ya Kusini, wenzangu wengi wameongea na mimi naomba niongee. Sisi tumechoka, tumechoka kwa sababu kila siku tunaongea. Safari hii imetengwa bilioni moja, bilioni moja ni pesa ndogo lakini tunaomba hiyo hiyo ndogo iende. Maana hapa tunaongea ndogo, lakini hatimaye hata hii ndogo haiendi. Mmetutengea bilioni moja kwa mwaka huu wa fedha unaokuja, tunaomba hii pesa iende, ili ikaweze kujenga hospitali ile na sisi tupate huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula. Ukifika pale ni masikitiko makubwa, mvua hizi za masika zinaponyesha jengo la OPD linavuja. Vile vile theatre yetu ya Hospitali ya Mkoa wa Ligula inahitaji matengenezo makubwa. Kama mwenzangu alivyosema X- Ray mbovu, jengo lenyewe linahitaji ukarabati mkubwa. Kwa mwezi OC inakwenda shilingi milioni ishirini na tano, ni ndogo, hospitali ile inatoa huduma ya watu wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hivi tunavyosema hatuna hospitali ya kanda, tunategemea hiyo hospitali ihudumie watu wengi, lakini mazingira yake ni magumu, mazingira yake ni duni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwenda pale Machi, 2016 palikuwa na matatizo. Madaktari 13 wakahamishwa, tangu Machi, 2016 mpaka leo ninapoongea hata daktari mmoja hajaletwa. Tunatarajia hawa waliopo wafanye kazi kwa kiwango kipi? Hawa wahudumu wenyewe wa pale wana madeni, mpaka sasa hivi wanadai si chini ya milioni mia tano na kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi watu wa Kusini, sisi watu wa Mkoa wa Mtwara pia tunahitaji huduma bora za afya. Tunaomba waone kwamba kule kuna watu ambao wanahitaji huduma bora. Tuna korosho tunachangia pato kubwa la Taifa hili; kwa hiyo nasi pia tunahitaji tupate huduma, si kwamba kila siku tukiingia humu tunaongea yanawekwa kwenye vitabu wanafunika, tukirudi kwenye bajeti nyingine mambo ni yaleyale, kitu kama hicho hatukipendi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ile hospitali, tunaisemea hii hospitali kwa sababu kama unakuja Mkoa wa Mtwara huwezi kuacha kuongelea Hospitali ya Ligula. Ni hospitali tunayotaraji iwe na mazingira mazuri kwa ajili ya kuwahudumia watu. Tukienda kwenye wodi ya wazazi majanga, wodi ni ndogo, watu wanarundikana, hospitali mmesema ya rufaa ya mkoa, lakini inatoa huduma utasema labda ni hospitali ya wilaya. Watumishi wana madai mengi, watumishi wako asilimia 39 tu, maana unapohitaji watumishi 10 wewe unao wanne tu, tunategemea watafanya kazi katika mazingira gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema Wizara inahusika na watoto pia tunajua ina wajibu wa kulinda haki zao. Leo watoto wanadhalilishwa kwenye vyombo vya habari, wanadhalilishwa kwenye mitandao ya kijamii; mtoto ametelekezwa na mzazi wake, pata picha kama ni mwanao wewe kesho anaambiwa na wenzie shuleni; wewe baba yako alikutelekeza; hivi kweli huyo mtoto ataweza kujifunza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusifanye vitu just for kwa ajili ya show up, tuonekane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto yule tunampa athari ya kisaikolojia. Mimi ni Mwalimu najua mtoto hawezi kujifunza vizuri.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, kuna mkakati gani uliowekwa na Serikali kuhakikisha kuwa miji mikongwe inatangazwa na kukarabatiwa ili iwe kivutio cha utalii kwa mfano Mji wa Mikindani katika Manispaa ya Mtwara, Mikindani umetekelezwa, mchafu, miundombinu mibovu na kadhalika. Naamini mji ule ukiendelezwa na kutangazwa vizuri utawavutia watalii hivyo kuongeza pato la Manispaa na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina makakati gani wa kuhakikisha inautangaza na kuuendeleza utalii wa bahari na fukwe zake. Wananchi wanaoishi maeneo yenye bahari mfano Mtwara, tulitarajia kuwa Serikali ingefanya uwekezaji mkubwa katika fukwe za bahari kwa kushirikiana na wawekezaji wengine ili kuwezesha uchumi kukua maeneo husika. Kinyume chake fukwe hizi zimeachwa chafu bila uwekezaji wowote. Je, Serikali inaridhika na hali hii?

Mheshimiwa Spika, naomba kujua msimamo wa Wizara hii juu ya kutoa elimu mbalimbali zinazohusu uhifadhi wa watu na wanyama pori ambavyo vimekuwa vikitekelezwa na watu mbalimbali ikiwemo Serikali mfano kibali cha kukata miti mingi sana katika mbuga ya Selous.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote nataka kusema kwamba elimu ni uwezo si idadi tu ya watu ambao wanaingia shuleni. Tunatarajia watoto wanaoingia wafundishike, wawe na uwezo wa kutatua changamoto zilizopo katika mazingira yao; hapo tutapata maendeleo katika elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri akija atujibu kwa ufasaha kuhusu hivyo vitabu vya darasa la nne ambavyo mpaka sasa hivi bado havijafika shuleni, watoto wetu wanajifunza kwa kutumia kitu gani? Ukifungua katika hotuba yako ukurasa wa 69 yaani tunaanza mbele kabla ya nyuma. Ukurasa wa 69.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 69 pale namba 62 roman (ii) inasema; “Mradi wa kuendeleza elimu ya ualimu imeandaa mapitio ya mitaala wa elimu ya ualimu ili kuwa na mtaala unaokidhi mahitaji ya sasa na unaoendana na mtaala wa elimu msingi ulioboreshwa.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, muone mambo ya ajabu ya Serikali ya CCM, kumbe mpaka wanapeleke mtaala shule za msingi, huku kwenye ualimu hawajawafundisha. Tunategemea walimu wale wakawafundishe wale watoto ambao mtaala ule hawaujui sasa wanaenda kufundisha kitu gani. Mheshimiwa Waziri naomba unapokuja hapa uje na majibu, haya ni maneno yako siyo ya kwangu nimekwambia ukurasa wa 69 roman (ii). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia vyuo vya ualimu; hawa watu wamesahaulika sana. Wakufunzi wa vyuo vya ualimu wamesahaulika, mimi nimetoka kule, takriban wazungumzaji wote waliozungumza hapa hawajataja vyuo vya ualimu. Wakufunzi wanadai, morale imeshuka, wana matatizo mengi katika kazi yao ya ualimu. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri una vyuo 35 tu vya ualimu nchi hii, mwenzako Mheshimiwa Jafo ana shule za msingi ngapi, ana shule za sekondari ngapi lakini wewe una vyuo vya ualimu 35, naomba uende ukawasikilize, utatue matatizo yao. Shida ya ualimu inatokea huko kwa sababu watu wamechoka, mpaka leo unamwambia amfundishe mwalimu, mtaala wenyewe maskini haujui anamfundisha kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye fedha za ruzuku. Hizi fedha zimekadiriwa tangu mwaka 2001; mwaka 2001, shilingi 10,000 kwa mtoto wa shule ya msingi, shilingi 25,000 kwa mtoto wa sekondari. Katika hiyo shilingi 10,000 shilingi 4,000 inabakia Serikali haiendi shuleni kwa ajili ya ununuzi wa vitabu. Sasa nakuuliza Mheshimiwa Waziri shilingi 6,000 inayoenda shule kumgharamia mwanafunzi kwa karne hii inatosha? Na kama haitoshi utuambie mkakati wa makusudi ambao umeuweka wa kuhakikisha kwamba hiyo fedha inaongezwa. Pendekezo langu ifike shilingi 20,000 kwa mtoto wa shule ya msingi na ifike shilingi 50,000 kwa mtoto wa shule ya sekondari. Pia uniambie katika hiyo 4,000 inayobakia Serikali Kuu imenunua vitabu kiasi gani na kwa takwimu zipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za maendeleo; katika Wizara ya Elimu fedha zinazotengwa ni chache karibu zote asilimia 100 ya fedha za maendeleo mnategemea wahisani, ninyi mapato yenu ya ndani hayatengi fedha za maendeleo. Sasa nataka kukuuliza Mheshimiwa Waziri tunajua kuna miradi mingi, kwa mfano mradi wa KKK, ni mradi mzuri ambao implementation yake ingekuwa nzuri tunaamini ingesaidia, lakini mnategemea wahisani. Mtuambie nyinyi kwenye mradi huu mmeweka kiasi gani na mmefuatilia kwa kiasi gani mradi huu unaweza kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la walimu wa sayansi tumekuwa tukiliongea na tutaendelea kulio... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la masomo ya sayansi katika sekondari. Mahitaji Walimu 35,136, waliopo 19,459 upungufu 15,677; je, Tanzania ya viwanda itafanikiwa kwa hali hii? Serikali imefanya sensa ya Walimu wa sayansi wanaoacha kazi katika shule za sekondari na kujua sababu zilizopelekea kuacha kwao na kujua namna ya kuzitatua kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mfuko wa Wanawake na Vijana. Kwa nini katika Halmashauri hakuna akaunti maalum kwa ajili ya fedha hizi, mwisho wake lini Halmashauri kuchangia Mfuko huu kwa sababu huu Mfuko fedha zake zinazunguka. Ni matarajio yangu kwamba baada ya muda Mfuko huu uweze kujiendesha na fedha zinazotolewa na Halmashauri ziweze kufanya au kutoa huduma nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila halmashauri ina chanzo kimoja cha uhakika ambacho ni ardhi, lakini Serikali Kuu imekuwa ikichukua fedha hizo na kushindwa kurudisha 30% inayotakiwa kwenye halmashauri. Je, hapa Serikali Kuu inatenda haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni ya Kamati yanasema halmashauri nyingi zimeshindwa kukusanya mapato hata chini ya 25% na kushauri Halmashauri hizo zitafute vyanzo vingine vya mapato. Je, vyanzo hivyo vinatoka wapi ikiwa kila chanzo halmashauri zinazobuni Serikali Kuu inachukua? Je, vyanzo hivyo vipya vya mapato ya Halmashauri vinavyotakiwa kubuniwa ni kama vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mradi wa utekelezaji wa Manispaa ya Mtwara Mikindani. Taa zilizofungwa katika barabara ya Zambia haziwaki, naomba ufafanuzi wa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha ujenzi wa stendi ya kisasa katika eneo la Mkanaledi, Manispaa ya Mtwara Mikindani. Stendi iliyopo sasa ni ndogo haikidhi mahitaji, naomba ufafanuzi kuhusu hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kuna kitu kimoja bado sijakielewa vizuri. Serikali hii wanatuambia kwamba wanakusanya makusanyo yanapita mpaka lengo kwa mwezi, lakini cha kushangaza kwenye bajeti ya maji inaenda asilimia 22, sasa hizo hela zinazokusanywa zinakwenda wapi? Mtakapokuja kuhitimisha Waziri wa Fedha atueleze, wanatudanganya hawakusanyi ama wanakusanya lakini pesa zinatumika nje ya bajeti tunazopitisha hapa Bungeni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka tupate ufafanuzi huo, asilimia 22 kwenye utekelezaji wa mambo ya msingi, mambo ya maji ni jambo la aibu, la kusikitisha na linalokatisha tamaa wananchi wa Tanzania. Ukiangalia kwenye Ripoti ya CAG ya mwaka 2016/2017 ukurasa wa 99 hadi 100 inaonekana kuna pesa shilingi bilioni 410 zilikusanywa na TRA ikiwepo pesa kwa ajili ya usambazaji wa maji, lakini kuna pesa haikutolewa kwenda kule inakotakiwa kwa ajili ya kusambaza maji katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Mkoa wa Mtwara, tuna tatizo kubwa la maji katika sehemu mbalimbali. Ukienda maeneo ya Newala Mjini, Newala Vijijini, Nanyamba ukiingia huko ndani Mtwara Vijijini, Mtwara Mjini kwenye kata za pembezoni kuna tatizo kubwa la maji; wale watu wanafikia wananunua mpaka dumu moja la lita 20 shilingi 1,000, shilingi 800, shilingi 500; lakini wale watu wa Mtwara kila siku nasema wanachangia pato kubwa la nchi hii kupitia kilimo cha korosho ingawa nako pia kuwalipa hawalipwi kwa wakati lakini wanachangia. Kwa nini hatukai tukaangalia suala la maji likawa ni suala la kipaumbele? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka nipate ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha kuhusu ule mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma kuja Mtwara Mjini ambao tunaamini ungefanyiwa utekelezaji wake ungesaidia kwa kiasi kikubwa pale bomba lilipotaka kupita. Mwaka jana tumeona pesa zimetengwa tunaambiwa kuna processes zinaendelea, hizo processes zitaisha lini? Sisi tunachotamani tuone maji safi ya baridi yanapatikana ambayo hayo maji pia yangeenda kusaidia katika uwekezaji wa viwanda ambao mnausisitiza lakini tuna tatizo kubwa la maji katika mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la maji ni suala mtambuka. Tukikosa maji ya uhakika maana yake magonjwa yatakuwa mengi, hata kama Serikali itakuwa inatoa fedha nyingi kwa ajili ya dawa lakini tukumbuke bajeti ya dawa itakuwa kubwa kwa sababu ya matumizi ya maji ambayo siyo safi na salama. Nasema pia ni suala mtambuka kwa sababu mama anapoamka asubuhi kwenda kutafuta maji kule anakumbana na vikwazo vingi, anaweza akabakwa, akibakwa kesho mnamuita tupime DNA, mnapimaje DNA wakati ninyi ndio mliosababisha hayo yote yanayotokea? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tusifanye vitu kwa ajili ya kutaka kujionesha, twendeni tutoe hela. Kama hela zinakusanywa kupita kiwango hizo hela zinakwenda wapi? Watu wakihoji hapa kwamba kuna hela shilingi 1.5 trillion zimepotea watu mnakasirika, lakini mnasema mnakusanya, kwenye maji haziendi, kuziona hatuzioni. Tunataka tupate majibu ya uhakika ili tujue mustakabali wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ungeniuliza mimi kipaumbele ningekwambia maji ni kipaumbele kwa sababu ni mtambuka. Kama huna maji kiwanda hakifanyi kazi, kama huna maji hata hiyo ndege hauwezi kupanda kwa sababu hautakuwa na afya nzuri, unaumwa na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sina mengi ya kuyasema lakini tunaomba tupate kueleweshwa, nakushukuru.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Naomba nipate majibu ya haya mambo ambayo nitayaongea na sidhani kama nitatumia dakika zote kwa sababu mengi yameongelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasikia hapa wanasema kwamba kuzalisha umeme kwa njia ya gesi ni gharama kuliko kwa njia ya maji ndiyo maana wanakwenda kwenye Stiegler’s. Swali langu; wakati wanakwenda kukopa pesa nyingi, mabilioni kwenda kuwekeza kwenye bomba la gesi, wananchi wetu wa Mkoa wa Mtwara wamepigwa, wanawake wajawazito walijifungua kabla ya siku zao, walikwenda kukopa na kuwekeza wakati hawajafanya utafiti wa kutosha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate majibu ya swali hilo kwa sababu hiyo Stiegler’s ipo kabla hata hiyo ya gesi, ama vyote vilikuwa pamoja wakaenda kuwekeza kwenye gesi kwa pesa nyingi ambayo kama nchi tutatakiwa kulipa. Sasa hivi tunatumia kati ya asilimia sita mpaka saba, leo wanahamia kwenye Stiegler’s kwa mbwembwe nyingi wakisema huu huku ni gharama kuliko huu, waliingia bila utafiti? Tukiwaambia kwamba tunakwenda kwa mizuka wanakasirika, huu haukuwa mzuka? Naomba nipatemajibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho, lazima tu niiseme yaani hakuna namna. Unapozungumzia uchumi wa Mikoa ya Kusini, Mkoa ninaotoka mimi Mtwara huwezi kuzungumza bila ya kutaja korosho, yaani no way out. Sasa kama kuna mtu anafikiria hizo pesa tunazozizungumzia zaidi ya bilioni mia mbili si za wakulima, hivi kama wakulima wale wasingenyeshewa na mvua, wasingeng’atwa na nyoka, jua lisingewawakia, hizo trilioni moja nukta ngapi ambayo ilipatikana kwenye export levy ingepatikana kutoka wapi? Kwa hiyo hatuwezi kuona kwamba hizo pesa siyo za wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimezaliwa Mtwara mpaka leo ninavyokwambia naishi Mtwara, mimi si Mbunge wa Mjini, kwetu ni huko huko Mtwara. Wakati huo sisi tunakua, Bandari ya Mtwara ilikuwa inafanya kazi kutokana na korosho zikaanza hujuma. Mara meli haiwezi kufika hapo, mizigo hakuna na vitu hivi, Bandari ile ikaanza kudorora. Mama lishe, vijana ambao walikuwa wanafanya kazi pale wakawa hawafanyi kazi kwa sababu ya kutokuijali bandari ile na kuiendeleza kutokana na zao la korosho. Sasa tumeanza kurudi kidogo tunaonekana Wamakonde wale wanapeleka watoto wao shule ili waondokane na ile dhana ya watu wa Kusini hawakusoma kwa ajili ya kilimo cha korosho, leo hawataki kupeleka hela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kusikitisha kabisa, kama mnakumbuka, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mtu ambaye namheshimu sana; mnakumbuka mwaka jana alipita kuzindua miche kupanda, kuwahamasisha watu, ile miche mpaka leo haijalipwa, wale watu ambao wameotesha hawajalipwa, is it fair? Wanawatakia nini Waziri Mkuu na watu wake wa Kusini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate majibu na pia naomba nipate majibu ni nini mkakati wa Serikali, tuna kiwanda kinachozalisha cement pale cha Dangote, lakini kwa kiasi kikubwa cement ile inasafirishwa kwa barabara, hatujaona meli ya mizigo na barabara ile kila siku ukipita kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam kila siku ina viraka kwa sababu inabeba mzigo mkubwa. Maendeleo yoyote ni gharama. Sasa nataka nijue kama Serikali ina mkakati wowote wa kuleta meli ya mizigo ili kusudi bandari yetu itumike kusafirisha mizigo ikiwemo na ile cement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia madhumuni ya hiyo pesa ya wakulima, mimi sina namna nyingine ya kuiita hiyo pesa ya korosho, kuna madhumuni mengi kwa nini ikaanzishwa, wadau wa korosho wakafikiria ili tuliendeleze hili zao, tutenge pesa ambayo itasaidia. Dhumuni mojawapo tumesema ni kuwa na mikakati endelevu kuhusu zao la korosho ambapo mikakati hiyo inafanyika kwenye utafiti katika Chuo cha Naliendele ambapo 90 percent ya matumizi ya pale yanategemea hiyo export levy. Kwa hiyo kama hatupeleki tujue tumeua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kitu kingine, zao la korosho ukiliangalia, yaani wale Watafiti ukienda pale Naliendele wana mashamba ya mikorosho ambapo ile mikorosho inatunzwa vizuri ili iweze kutoa mbegu bora, hivi wanataka wale watafiti wetu waende wenyewe shambani wakalime ili watunze mikorosho wapate mbegu bora za kuendeleza hili zao ambao wanasema kwamba liende kwenye mikoa mingine ambapo sasa limesambaa katika mikoa 17?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbegu za korosho ni tofauti na mbegu zingine, kwamba unachukua shambani unaleta, hizi ni lazima kwanza uanze kutunza ile mikorosho iwe katika standard, unavuna then unakuja kuotesha, watu wanapata miche, wanakwenda kuiotesha kwa ajili ya kuendeleza zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhumuni lingine ni kufanya usimamizi na uratibu mzuri wa stakabadhi ghalani. Hawataki watu wauze Kangomba wanataka watu wauze korosho zao ghalani, hivi wale watu wote ambao watakuwa wanafanya hizo shughuli wanazifanya kwa kupata pesa kutoka wapi kama hawataki kutoa pesa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mpango ameitwa kwenye kikao si mara moja wala mara mbili, alikataa kuja. Angekuja, akatoa majibu watu wangemwelewa kwa nini alikataa kuja, pesa wamezipeleka wapi? Hilo ndilo swali la msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunapoongea ni mwezi wa Sita, msimu kule umeshaanza hakuna sulphur, hakuna madawa, hakuna nini, hivi anategemea mwakani hata kama hiyo sheria yake ikapita na naamini itapita kwa sababu ni tumezoea, hakuna kitu kinachoingia humu ndani kikashindwa kupita. Hiyo Sheria yake imepita, anataka pesa zote zikusanywe ziwekwe kwenye huo Mfuko wa pamoja, atakusanya kitu gani kama korosho hakuna?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ni suala tu la kujiongeza, kwamba, tunahitaji tuhudumie vizuri ili mazao yawe mengi, aidha atakusanya yeye, atakusanya nani kwa sababu yote ni Serikali, hapa issue siyo kukusanya, issue pesa ikusanywe lakini pia itumike kwa matumizi yaliyokusudiwa. Atakusanya nini kama hakuna korosho? Atakusanya nini kama sulphur haijakwenda? Atakusanya nini kama madawa hakuna? Atakusanya nini kama kwenye taasisi ya utafiti hakufanyiki utafiti? Nafikiri hilo jambo wala halihitaji akili kubwa sana, ni jambo tu la kawaida, kwamba unahitaji uwekeze ili upate mavuno, sisi hatutaki kuwekeza, tunataka tupate mavuno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhumuni la tatu, tunasema kuendeleza ubanguaji wa korosho nchini, sasa hapo ndiyo majanga. Viwanda havieleweki, mashine hakuna, matatizo chungu mzima, Waziri wa Viwanda ukimuuliza kwamba kuna kiwanda gani kimetengewa eneo Mtwara Mjini? Anakwambia eti Chikongola kuna eneo, Chikongola hapo mnapopasikia ni katikati sokoni. Sasa sijui ametenga sehemu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya nimeuliza hili swali mwenyewe sikuwepo, nikajibiwa kwamba eti Chikongola sokoni wametenga eneo sijui sehemu gani. Kwa hiyo, yaani kuna vitu ambavyo ukikaa, ukivitafakari yaani ni lazima ushangae kwamba uelekeo wetu uko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimalize; tunachotaka watu wa Kusini ni pesa siyo maneno kama maneno tumeyasikia mengi tu. Hayo maneno aliyoyasema Mwenyekiti, Mheshimiwa Bwege wa Lindi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kangomba yaani kule kwetu kuna bakuli kubwa hivi ambalo lile wanapima kwa ujazo siyo uzito.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote niombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie kwanini kwenye Mpangu huu hatuoni Hospitali ya Kanda ya Kusini, haipo kwenye mpango huo, haionekani kabisa kwa hiyo hatuelewi kama haitakuja kutekeleza ujenzi wake kuendelezwa au vipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo niseme kwamba wafanyabiashara siku zote wanabembelezwa au kunatakiwa kuwe na majadiliano yenye kuleta tija na sio vitisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiona watu tukisema biashara zinakufa mnasema zinazaliwa zingine. Wewe hata ukiwa na watoto 10 hautamani hata mmoja afe, isipokuwa unachokuwa unatamani uzae wengine waongezeke. Sasa mtu leo akiona biashara zinafungwa anashangilia kwamba wale walikuwa wezi, walikuwa nini! Baba yangu Dkt. Mpango huko tunakoelekea sio kuzuri.

Mimi nakusahuri kwa nia njema kabisa kaa na wafanyabiashara, muelewane, muone vikwazo vyao, mnatakiwa mtatue vipi na mfikie negotiation, ukija kwa mfano kwenye suala la korosho, watu wameitwa wamekaa mezani, wameitikia labda kwa hofu baada ya kuitikia tumefuata nini wewe mwenyewe unajua mimi sina la kulieleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie hili la kusema kwamba kuna wafanyakazi wachache TRA, vifaa havitoshelezi; ni kweli hata ukisoma ripoti ya CAG imeeleza Halmashauri ya mama yangu pale Dkt. Kijaji inatakiwa kuwe na mashine 100, ziko 22 kwa mujibu wa ripoti ya CAG. (Makofi)

Sasa mimi nishauri mzee wangu Mkuchika hapa wa Utumishi, hebu muangalie wapatikane wafanyakazi wa kutosha kwa ajili ya TRA, kutokuwa na wafanyakazi wa kutosha ndiyo huko kunakosababisha wale wachache wanawafikia watu wale wale kila siku, wanawalazimisha kulipa kodi zisizowezekana wakati kuna sehemu zingine mnaziacha. Kidogo kidogo hujaza kibaba kuliko mnapotamani mkamue ng’ombe kwa kiasi kikubwa, matokeo yake mnamfilisi, anakufa! At the end of the day hamfaidiki ninyi wala hafaidiki yule mfanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ninalotaka nilizungumze, ukiangalia kwenye mpango nimesoma kwenye hotuba ya Kamati wanasema kwamba bajeti ijayo mnapendekeza iwe trilioni 33.5 kutoka trilioni 32.47 na wakati huo huo utekelezaji ulikuwa 57%. Sijaelewa ni kwanini mnataka iongezeke wakati huo huo ukienda kwenye misaada na mikopo mnasema imepungua lakini kuna ongezeko la asilimia 26.3 kwenye pendekezo lijalo. Hii pesa inatoka wapi wakati mnasema imepungua, kwa nini tena mnazidi kuongeza na kwa nini wamepunguza?

Je, mmefanya analysis mkajua kwanini inapungua? Mahusiano yetu na hizo nchi wahisani yakoje? Labda ndiyo yanasabbisha haya mambo kwa hiyo utakapokuja kuhitimimisha naomba tupate majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine ninalotaka kulizungumzia nataka kuzungumzia mradi wa gesi katika Mkoa wa Mtwara. Kuna issue ya LNG plant pale Lindi nataka kujua Serikali hivi vitu vimewashinda au mna mkakati gani wa dhati wa kuhakikisha vinatekelezeka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo uwekezaji katika sekta ya gesi ungefanyika kikamilifu nchi hii ingekuwa na umeme wa kutosha na ninyi Wabunge ndiyo mlikuwa mnashangilia tunafanya uwekezaji katika gesi, gesi itatusaidia, gesi ina manufaa mengi, lakini leo wote tumegeuka tunashangilia, wote mmegeuka mimi simo, wote mmegeuka mnashangilia Stiegler’s Gorge habari ya gesi tena basi! Sasa tunakwenda wapi? Our vision ni nini? Kwa sababu kwenye gesi tungepata viwanda vya mbolea, kwenye gesi tungeongeza ajira na vitu kama hivyo.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimwia Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Awali ya yote, nataka kusema kitu kimoja kieleweke, Halmashauri zote Afisa Masuuli ni Mkurugenzi ambaye anateuliwa na Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, tukiona Halmashauri ya Kigoma Ujiji inapata hati chafu, tatizo sio Zitto tatizo ni Mkurugenzi na watendaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia suala la barabara ya Tubuyu – Nanenane na Maelewano ya kilometa 4.6...

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waitara.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tunza Malapo unaipokea taarifa hiyo?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, asitafute umaarufu kupitia mimi, kwa hiyo, niache niendelee na hoja zangu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasema barabara hii ya kutoka Tubuyu kwenda Nanenane mpaka Maelewano katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kilometa 4.6 imejengwa kwa shilingi bilioni 12.6 maana yake ni kwamba kila kilometa moja imejengwa kwa shilingi bilioni 2.74. Sio highway tuelewane, ni barabara ya mtaa. (Makofi)

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mlinga.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tunza Malapo, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee, taarifa yake sipokei.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara ni ya mtaa na tumeitembelea sehemu nyingi haina hata vituo vya daladala, unajengaje kilometa moja kwa shilingi bilioni 2.74 na ni mkopo kutoka Benki ya Dunia, sisi Watanzania maskini tutakuja kulipa. Kitu chochote unapofanya lazima uangalie value for money. Hii barabara ni ya mtaani sio highway kwamba labda itapitisha malori, unaenda kujenga barabara ya mtaani ya kwenda nyumbani kwako kwa shilingi bilioni 2.7 halafu ni pesa ya mkopo ambayo tunakuja kulipa mtu anasema kama tuko Ulaya! That is the shame. Mimi sikubaliani nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niingie kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kuhusu Ukaguzi Maalum. Wakati naongelea hii naomba yaeleweke mambo yafuatayo; Mkuu wa Mkoa wa kipindi hicho Bi. Fatma Mwassa alikuwa na uhusiano wa karibu, mtu na mume wake na mkandarasi ambaye alipewa tender hizo. Wakati huo huo, kwa sababu ukaguzi unaozungumziwa hapa ulifanyika kuangalia mambo ya fedha ya mwaka 2012/2013 mpaka 2016/2017; wakati huo huo miongoni mwa Wakurugenzi ambao walihudumu katika Halmashauri hiyo, ni Dkt. Athumani Kihamia ambaye sasa hivi ni Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati naongea hapa, naomba nieleweke hivi…

MHE. AMINA S. MOLLEL: Kuhusu Utaratibu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tunza Malapo, kuna kanuni inavunjwa, Mheshimiwa Amina Mollel, kanuni.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mimi naomba twende taratibu, Hansard naomba ichukuliwe, mimi nilichosema, kwanza mimi ni Mjumbe wa LAAC mnielewe, nimesema hivi Ukaguzi Maalum wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua umefanyika kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 mpaka 2016/2017. Nikasema miongoni mwa Wakurugenzi waliohudumu kipindi hicho ni pamoja na Mheshimiwa Dkt. Athumani Kihamia, nimesema lipi la uongo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niendelee.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tunza cha kuelewa ni kwamba ulivyotaja kuanzia 2012 mpaka 2017 Wakurugenzi wengine wote hukuwataja ikiwa ni pamoja na aliyekuwepo 2014 aliyeingia mkataba, ni jambo rahisi tu. Kwa hiyo, maana yake ni hivi…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tuelewane, maana yake ni hivi, kama lengo ilikuwa ni kuonesha Wakurugenzi waliopita basi ungemtaja aliyekuwepo wakati wa mkataba ndiyo hoja iliyopo hapa.

Kwa hiyo, naomba twende vizuri, hiyo ndiyo hoja, usiseme miongoni mwao halafu unamtaja mmoja kwa kuwa yeye anahusika sana. Kwa hiyo, inakuwa kana kwamba yeye ndiyo aliingia huo mkataba wakati wewe unajua wazi hakuingia yeye aliingia mwingine lakini wewe umemchagua yeye. Kwa hiyo Mheshimiwa Tunza Malapo endelea na mchango wako. (Kicheko/Makofi)

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi bwana naomba mniache nichangie, mbona hiyo mmeonesha sana interest, nimemtaja hapa Mkuu wa Mkoa, nimemtaja hapa mkandarasi, lakini ngoja niache sasa niendelee na hoja yangu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilichokuwa nataka kusema ni kwamba kumekuwa na ubadhirifu mkubwa katika Halmashauri hiyo ya Kaliua wa shilingi bilioni 3.5. Sasa ukiangalia mambo yenyewe, nasoma ukurasa wa 41 kwenye Ripoti ya Kamati ili twende sawa, ukiangalia ile namba (xii) inasema, malipo mbalimbali yenye viashirio vya ubadhirifu na kugushi nyaraka yenye kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 1.2. Mpaka sasa hivi hatujui hatua zilizochukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, namba (xi), usimamizi dhaifu katika ukusanyaji wa ushuru wa tumbaku uliopelekea kutokukusanya mapato zaidi ya shilingi bilioni 1.35. Sasa hapa kwenye ushuru kuna mambo mawili, mimi ni Mjumbe wa Kamati. La kwanza, hawakutoza ushuru kwa maana hawakuchukua tu lakini la pili ilikuwa wametoza ushuru siku wanaenda kulipa ushuru wao, kwenye exchange rate wakaenda kwenye Bureau De Change ambazo zinabadilisha kwa kiwango kidogo kuliko ya Benki Kuu. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Duh.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, ukiangalia namba (viii), malipo kwa mkandarasi kwa fedha za Mfuko wa Barabara kwa kazi ambazo hazikufanyika, hakufanya kazi lakini alilipwa. Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua hiyo. (Makofi)

Mheshimwa Naibu Spika, ukienda namba (i), malipo ya awali ya shilingi milioni 121.7 yalifanyika kwa kutumia nyaraka za dhamana toka Benki ya Equity, nyaraka hizo ziligushiwa. Kugushi maana yake ni jinai lakini mpaka sasa hivi bado wanatanua mtaani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, malipo ukienda ile namba (iv) malipo yalifanyika kwa mkandarasi bila kuonyesha vipimo vya kazi na mchanganuo wa kazi zilizofanyika kiasi cha shilingi milioni 197, bado wanatanua mtaani. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuongea jioni ya leo, nina mambo machache tu, la kwanza nilichojifunza kwenye hii Wizara ya Maji, kuna matatizo makubwa mawili, tatizo la kwanza ni kutopewa fedha za kutosha kulingana na bajeti yao. Tatizo la pili, hata hizo pesa kidogo wanazopewa bado hawazitumii vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa maana ipi, ukiangalia tunapotembea na Kamati kwenye halmashauri nyingi unakuta miradi mingi ya maji inasuasua, usanifu mbovu sijui pressure ya maji ndogo, DP hazitoi maji, mtu, mfano tumeenda Mkoa wa Kagera zimejengwa DP kumi na saba, lakini tisa hazitoi maji, unajiuliza?. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu si wasomi? Wamesoma wanajua kufanya usanifu kwa nini haya mambo yanatokea? Lakini nilichojifunza ni kwamba watu hawako serious katika kufanya hizi shughuli hata hicho kidogo wanachokipata basi hawakitumii vizuri achilia kwamba nayo Serikali pia haiko serious kutoa pesa za kutosha, ili kuleta maji ya kutosha katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate ufafanuzi kuhusu ile miradi ya vijiji kumi kila wilaya ambayo ilikuwa inafanyika kupitia mikopo ya Benki ya Dunia, miradi mingi haifanyi vizuri, kwa hiyo, nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie kama Tume aliunda imeona nini na inatatua vipi changamoto hii. Kwa sababu kama ni pesa za mkopo tutakuja kuzilipa kwa hiyo tulitarajii watu wafaidike na kuna tabia imezoeleka. Wakijua Kamati inapita, basi maji watayafungua, ama Kiongozi anapita, maji wanayafungua. Kiongozi akiondoka anaondoka na maji yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni tabia mbaya watu wa maji, Wizara ya Maji, hiyo ni tabia mbaya, tunatamani tuone wananchi wetu wanapata maji siku zote, hatutaki mambo ya geresha, kwamba tu kwa sababu leo Rais anakuja basi maji yanatoka. Kwa sababu leo Kamati ya Bunge inakuja basi maji yanatoka. Hilo ni tatizo tumeliona na ninao mfano dhahiri tumeenda kule Karagwe na wakatuambia kwamba haya maji, mmekuja nayo ninyi na mtaondoka nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate ufafanuzi kuhusu mradi wa maji kutoa maji Mto Ruvuma kuleta Mtwara mjini ambao ulikuwa ufaidishe vijiji 26 katika Jimbo la Mtwara Vijijini, naomba tu nipata ufafanuzi kwanza ule mradi bado upo ama haupo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nikisoma katika hiki kitabu cha kwako Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 150 umesema kwamba Serikali itagharamikia imetenga bilioni moja, lakini mwanzoni tuliambiwa ule mradi utatekelezwa kutokana na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China, which is which? Huu mradi bado upo, ama haupo? Na kama haupo ni kwa nini? Na kama upo utatekelezwa lini? Tangu nimeingia Bunge hili Kila nikisimama lazima niuongelee huu mradi lakini umekuwa unasuasua hatujui hatima yetu. Naomba tupatiwe ufafanuzi wa kutosha ili kusudi sisi watu wa Mtwara tujue huu mradi kama upo ama kama haupo mtuambie. Si oleo mnatuzungusha, Benki ya China, kesho Serikali tunataka tujue hatima yake ni nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ukurasa wa 112 kwenye Hotuba ya Waziri, Mamlaka nyingi za maji zinadai Taasisi za Serikali, deni limefika bilioni 21.84 na Mamlaka zile tunajua zinajiendesha zenyewe. Sasa nataka kujua kauli Waziri zile Taasisi za Serikali zinapewa pesa kwa ajili ya kulipia huduma zinazotumia ikiwemo na maji, kwa nini hazilipi kwenye hizi Mamlaka za Maji, na hizi Mamlaka za Maji zinajiendesha zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zina mambo mengi ya kufanya, hizi pesa zinazodaiwa ni nyingi nataka kujua Mkakati wa makusudi kabisa wa kuwaweka hadharani watu hawa ambao hawataki kulipa maji kwa sababu sisi wananchi wa kawaida kwa mfano kule Mtwara, ukishatumia maji, yakafika deni 30,000 wanakuja kukata maji. Kwa nini kwenye hizi Taasisi tunaacha mpaka madeni yanakua, kama Serikali haitoi pesa basi mtuambie, na sio kuzunguka zunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia nipate ufafanuzi ukiangalia ukurasa wa 90 katika hotuba ya Waziri, kuna ule mradi wa maji katika Miji ya Mtwara na Babati, ukisoma pale umeongea tu kwa ujumla kwamba usanifu unaendelea mradi utafanya kazi, usanifu utakapo kamilika. Nataka nijue hili suala liko siku nyingi, linaongelewa ni lini, usanifu unakamilika na lini mradi unaanza kufanya kazi huu mradi katika hii Miji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio mambo ya jumla ya kutuambia kwamba ukikamilika hamna deadline, hamna kipindi maalum umesema umemaliza hilo halikubaliki kabisa, tunaomba tupatiwe kwa sababu tunahitaji huduma hiyo ya maji. Miundombinu yetu pale Mtwara ni chakavu haitoshelezi, kulingana na watu ambao wapo kwa kipindi hiki. Miundombinu ile ni tangu enzi za Mkoloni, kwa hiyo sasa hivi tunapata shida za maji ingawa maji tunayo lakini kwa sababu miundombinu ni mibovu ni michache haiwezi kukidhi haja ya wananchi ambao wapo katika Mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo machache, ukifungua, naomba tu niulize swali moja, ukifungua kwenye hotuba yako ukurasa wa 134, kuna kampeni za maji na usafi wa mazingira chini ya mafungu mengine, lakini ukisoma pale, unakuta fedha zote ni fedha za nje. Sasa tunaenda kufanya kampeni za maji, na usafi wa mazingira, lakini fedha zote tunategemea kutoka nje, maana yake ni nini? Serikali haijatenga fedha za ndani kugharamia hii kampeni. Na tunajua mambo ya maji na usafi wa mazingira ni jambo nyeti, kwa nini Serikali inategemea zaidi pesa kutoka nje. Naomba nipatiwe majibu ya suala hilo. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kengele ya pili imelia.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naskushukuru. Awali ya yote napenda kuipongeza Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ina mambo mengi mazuri, Serikali itulie isome na ifanyie kazi ushauri ambao wameutoa. Pia ukiangalia kwenye kitabu cha Kamati nacho pia kina mambo mazuri, kina ushauri nzuri, pia Serikali itulie isome ifanyie kazi kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Mtwara, Mtwara kuna Bahali ya Hindi. Ukifika Mtwara Mjini sasa hivi samaki wengi ambao tunakula wanatoka Msumbiji. Wanatoka Msumbiji si kwa sababu sisi watu wa Mtwara hatuna bahari ama hatuwezi kuvua ni kwa sababu vyombo vya uvuvi vilivyopo ni duni. Wavuvi wengi wanatumia mitumbwi kwa makasia hivyo wanashindwa kuvua samaki kwenye kina kirefu. Pia ukienda upande wa Msumbiji nyavu zilezile ambazo Tanzania kwa kiasi kikubwa zinachomwa kule zinatumika na samaki hao wanarudishwa wanakuja kwetu kuuzwa na sisi tunanunua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna bahari kubwa ambayo tulitarajia kitoweo cha samaki kiwe ni chakula kikuu, lakini sasa hivi Mtwara kula samaki ni anasa, kwa sababu samaki utaambiwa wanauza shilingi 2000 au shilingi 3000 ni samaki mdogo lakini bahari tunaiangalia. Sasa ushauri wangu kwa Serikali nawaomba waone haja ya makusudi kabisa ya kuwekeza, tukipigwa kwenye korosho basi tukimbilie kwenye uvuvi. Korosho hali tete kwenye uvuvi hali tete mambo yanakuwa tafrani haipendezi, tunashindwa hata pamoja pa kujishikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifungua katika ukurasa wa 41 wa hiki kitabu cha Kamati unaona wameeleza kuna uvuvi wa samaki aina ya Jodari, wanasema asilimia 67 ya samaki waliouzwa huko nje duniani mwaka 2018 wamevuliwa kutoka ukanda wa bahari kuu ya Tanzania na watu wengine sio sisi Watanzania. Pia ukisoma pale kwenye ukurasa wa 41 Kamati imetoa ushauri ndio maana nikasema, Serikali ijitahidi kusoma hiki kitabu ili wapate ushauri, wamesema kuwa na ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki aina ya jodari kwenye ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia masuala ya viwanda naona kwa asilimia kubwa amelekezwa kwenye maeneo ambayo kuna Ziwa, maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria, lakini ukija huku kwenye ukanda wa bahari sijajua kama kuna kiwanda chochote, kule kwetu Mtwara najua hakuna kiwanda cha uchakataji wa samaki, lakini tuna bahari ule ukanda wote ule kutoka Mtwara, Kilwa huko mpaka unakuja Dar es Salaam, sijakiona kiwanda cha kuchakata mazao yanayotokana na samaki wa maji chumvi. Ndio mpaka sasa hivi ukipita humu madukani kwenye mabucha ya samaki, samaki wa maji baridi ni wengi kuliko samaki wa maji chumvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakatoa ushauri mwingine, (b) ununuzi wa meli za kufanya uvuvi katika bahari kuu ya eneo la Tanzania, hakuna meli kubwa za uvuvi, hawa samaki kama jodari ndugu yangu huwezi kuwavua kwa kutumia mitumbwi ile ya kwetu ya asili huwezi. Kwa hiyo, ni lazima wawekeze haya mambo mengine ya kukimbilia vitambulisho, mtu mama anauza mboga unamng’ang’aniza atoe kodi uchumi tunauacha kwenye bahari kuu. Pesa tunaziacha huku, ndio maana kila siku tunataka tuwafinye watu wenye biashara ndogo ndogo lakini huku zinapokuja kupatikana pesa nyingi hatuwekezi ili kusudi tuongeze pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatakiwa tuwe serious, kuna mambo mengine yangekuwa yanafanyika for free, watu wanafanya biashara za mboga mtu ana mchicha wake, lakini wewe mtu wa uvuvi unachotegemea mtu afanye kosa ukamtoze faini, ndio uje hapa maduhuli yameongezeka, maduhuli yameongezeka, lakini ukiangalia mengi ni faini, hatuwekezi vya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa huo wa 41, Kamati ikashauri ujenzi wa maeneo ya kuhifadhia samaki na mazao yake, hakuna ya kutosha. Kwa hiyo niwashauri wasome vizuri, hatuna bandari za uhakika za uvuvi, watu wanauza tu holela holela, mtu akienda na hicho kimtumbwi chake, akivua visamaki viwili, vitatu, anakuja anauza, matozo kibao matokeo yake maendeleo ya wavuvi wetu yanakuwa kila siku ni duni yaani mtu ili apate tu kitu cha kula kwa siku ambapo hii ingekuwa ni sekta iliyoendelezwa nafikiri ingesaidia Watanzania na pia ingeongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kidogo kuhusu ufugaji wa kuku wa nyama na mayai. Ukiangalia kwa kiasi kikubwa hii mifugo inawasaidia wajasiriamali wadogo ambao wengi wao ni wanawake ambao mimi nawawakilisha hao wanawake, tumekuwa na tatizo kubwa sana la upatikanaji wa vifaranga, lakini pia hata hao vifaranga wakipatikana kuna changamoto kubwa sana ya masoko, hakuna masoko ya uhakika. Mtu anafuga kuku mpaka wanafikia stage ya kuuza hapati soko kuku wanakaa wiki mbili wiki tatu zaidi matokeo yake anaamua kuuza kwa bei ya hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kama Wizara waangalie kwa undani nimekuwa na interest kidogo na sehemu hii, waangalie kwa undani na kufuatilia tatizo hasa ni nini, watoe ushauri kwa wafugaji hawa wadogo ili waweze kujiongezea kipato, kwa sababu kama mtu anafuga kuku thamani yake shilingi 5,000 halafu anakuja kuuza kwa shilingi 4,000 anapata hasara, wategemezi wanazidi kuongezeka, Taifa halipati kipato, lakini hizi sekta zikiangaliwa kwa undani kama kuna changamoto wawaaambie watu, kama kuna kuku wanaongia kutoka nje wafanye utaratibu mzuri, kama kuna mayai yanayoingia kutoka nje ili kusudi ili soko litengamae, watu waweze kuuza na kufuga kwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenisababisha mimi na wenzangu leo tukawa hai, tuko ndani ya Bunge hili Tukufu. Suala la nishati ya umeme, ukiangalia kwenye Mpango wa Pili, target ilikuwa kufikia megawatt 4,915 lakini zilizofikiwa mpaka sasa hivi 1,602.3. Maana yake lengo halijafakiwa, kwa hiyo kama Serikali inayokusanya kodi za wananchi ina wajibu wa kuhakikisha inafikisha malengo ambayo wameahidi kwenye Mpango.

Mheshmiwa Mwenyekiti, licha ya kutofikiwa hivyo, kuna suala lingine ambalo ni la muhimu sana nataka niliseme. Kumekuwa na kusema vijiji elfu kumi na ngapi vimefikiwa na umeme, lakini tuangalie katika katika vile vijiji ni nyumba ngapi zimeunganishwa na huduma ya umeme. Mpaka sasa hivi kwa mijini ni asilimia 39.9 ya nyumba ndiyo zimeunganishwa na umeme na kwa vijijini ni asilimia 24.3 ya nyumba ndiyo zimeunganishwa na umeme, maana yake una nyumba 100 kwa vijijini, ni nyumba 24 tu zilizounganishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu kwa Serikali kwa umuhimu wa nishati ya umeme wanapopeleka umeme vijijini, basi wahakikishe wanapeleka nguzo karibu na maeneo ya wanaoishi watu ili iwe rahisi kwa wao kujiunganishia umeme kwenye nyumba zao.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tunza Malapo, kuna taarifa Mheshimiwa Hussein Amar.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa mchangiaji, vile vijiji ambavyo vimeshafikiwa na umeme ni vijiji zaidi ya elfu tisa na kitu, haya masuala ya kuunganisha ni kaya ngapi zimeunganisha ni yule mhusika, mwenye nyumba yake alipie na awashiwe umeme, siyo jukumu la Serikali. Nilikuwa nampa taarifa hiyo. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tunza Malapo, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei. Kazi ya Serikali ni kupeleka huduma karibu na wananchi. Kuna nguzo kumi ndiyo mtu umfikie kwenye nyumba yake, unamwambia ajiunganishie kwa nguzo kumi? Tuache bla bla bwana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mdau wa elimu sana, elimu ni uwezo, tunategemea mtu ambaye anapata elimu aelimike aweze kupambana na changamoto zilizoko katika maisha yake au maeneo yanayomzunguka. Tatizo kubwa ninaloliona kwenye elimu yetu ya Tanzania, tunaanza kufeli tangu mtoto anapoingia darasa la awali. Kimataifa ration inayokubalika ni Mwalimu mmoja wa awali kwa wanafunzi 25, lakini katika nchi yetu Mwalimu mmoja wa awali anafundisha watoto 104. Pata picha watoto wadogo, Mwalimu anahitajika kila mtoto amfuatilie, amejua kuandika, hiki ameelewa, una watoto 104 darasani, unawafuatilia vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tatizo linaanzia hapo. Ukienda shule za msingi mimi sisemi, kila mmoja wenu anajua hali ilivyo. Mwalimu unapita uandike ubaoni hata pakupita hakuna, tunataka watoto wakifika vyuo vya kati, wakifika vyuo vikuu wawe na ujuzi wawe na uwezo, wameutoa wapi wakati msingi huku chini ni mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, ione umuhimu wa kutafuta data zilizo sahihi ili kusudi madarasa ya kutosha yajengwe, madawati ya kutosha yapatikane, Walimu wa kutosha wapatikane; kwa sababu ndiyo maana tunaambiwa kuna projection una project kwamba leo wameingia watoto 2,000 maana yake mwakani wanaweza kuingia 2,500 au 3,000; unatakiwa ujiandae leo, usiwaache watoto nyumbani unasema mpaka madarasa, mpaka madawati yatengenezwe ndio watoto waende shule. Serikali isipende kuzima moto. Kuna sensa ya watu, kuna wataalam wa kuangalia population ya watu, watumie hizo data katika kuweka miundombinu ya elimu ili kusudi watoto wasome katika mazingira yaliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongelea bandari ya Mtwara; natokea Mtwara, Mbunge wa Mtwara. Wakati sisi hatujaingia Bungeni, mimi Tunza sijaingia Bunge mwaka 2015 kwenda huko nyuma, Bandari ya Mtwara ilikuwa inafanya kazi. Kipindi cha msimu wa korosho meli nyingi kubwa zilikuwa zinakuja katika Bandari ya Mtwara. Nini maana meli za korosho kuja katika msimu, maana yake watu wa Mtwara walikuwa wanapata shughuli za kufanya.

Sasa kwa masikitiko makubwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani meli Bandari ya Mtwara hakuna. Ukiuliza unaambiwa meli zina kuja Dar es Salaam, korosho zisafirishwe kwa barabara mpaka Dar es Salaam, kwa sababu kuzileta Mtwara meli ni gharama hakuna mizigo ya kupakia kutoka Dar es Salaam kuja Mtwara. Naomba niulize, kipindi kile meli zilipokuwa zinakuja Mtwara mizigo ilikuwa inapatikana wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, kama wanaona hakuna mizigo ya kuja Mtwara, wajitahidini kukaa na wafanyabiashara wapunguze kodi ili na Bandari ya Mtwara itumike, mtu aone nikienda kupakia korosho Mtwara kuna ahueni fulani kwa sababu uchumi wa kwetu sisi watu wa Mtwara tunategemea asilimia kubwa korosho. Korosho ukienda kupakia Dar es Salaam tunawaacha vijana na wanawake wa Mtwara hawana kazi. Sasa hivi Mtwara ukienda kuko kama msibani, korosho haieleweki, zinapakiliwa Bandari ya Dar es Salaam, watu wa Mtwara wanafanya shughuli gani? Hapa wanasema wamewekeza bilioni mia moja hamsini na ngapi sijui, zinakwenda kufanya nini wakati hakuna mkakati thabiti wa kuhakikisha bandari ile inatumika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huo uwekezaji unaofanywa uendane sambamba na kuchochea meli zije Mtwara ili kusudi zifanye kazi katika Bandari ya Mtwara. Kama ni issue ya tozo ya kodi, Waziri wa Viwanda akae na wafanyabiasha aone ni kwa namna gani anakwenda kuiboresha bandari ile iweze kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la muhimu kwenye zao la korosho bado kuna malalamiko mengi, wakulima wa korosho wanalalamika, wanadai, ili kuepusha malalamiko hayo na watu wapate haki zao, naishauri Serikali imwombe CAG, akafanye ukaguzi maalum, wale watu wote wanaodai walipwe madai yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo kidogo; kuna siku nilikuwa kwenye semina iliyoandaliwa na Wizara ya Kilimo, naambiwa nyanya za kwetu zinaoza, zinatupwa kwa sababu hazina fibber zinazotesheleza kutengeneza tomato source, mananasi ya kule Mkuranga na kwingine, yanaoza yanatupwa kwa sababu hayana ubora, maana yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiniambia mimi Serikali imeshindwa kupeleka pesa, wataalam wetu wakatafiti, wajue hitaji la soko ni nini. Mkulima akiletewa mbegu bora atalima. Leo mkulima analima, anavuna nyanya zinaishia kuliwa na mbuzi, lakini leo tunamwambia akalime. Hivi nyie mnaijua kazi ya kulima, ilivyo ngumu. Kwa hiyo tunataka wakulima walime, wazalishe kwa tija na mazao wanayopata yaweze kutumika katika viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba hayo niliyoyaongea yafanyiwe kazi kwa maendeleo ya watu wa Kusini na kwa Taifa kwa ujumla. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu na nataka kuwaambia umma wa Watanzania kwamba Mheshimiwa Gwajima Josephat ameshindwa kuthibitisha mbele ya Kamati, kuleta kielelezo chochote cha zile tuhuma nzito ambazo amezitoa kwa Viongozi Wakuu wa Nchi hii. Alisema ana vielelezo, atakuja kusema, nawaambia hakuja hukusema jambo lolote la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Watanzania kwanza watambue hilo, amekuja pale na vituko tu, mara hataki kiti, mara hataki microphone, mara leo nasimama, lakini hakuleta kielelezo chochote, tulimhoji maswali na sisi tulikuwa sober, inawezekana angetusaidia jambo kuna jambo analijua, lakini kwa masikitiko makubwa hajui lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, amesema chanjo ya J&J imeletwa kwa sababu watu wamekula pesa. Tukamwambia tunaomba Ushahidi, hana. Akasema watu watakao chanjwa watakuwa vichaa, watakuwa hawazai, sijui tutatembea barabarani tunaongea wendawazimu, tuletee Ushahidi, hana.

Mheshimiwa Spika, akatoka hapo tulipomwambia hivi haya mambo unayoyasema wewe huoni kama unaleta taharuki kwenye nchi. Halafu mbaya zaidi huyo kiongozi aliyeyazungumza haya yupo kwenye chama chako, kwa nini usitafute venue ya kwenda kuongea naye ukamshauri, unakuja kuyatoa mbele ya umma? Kwa masikitiko makubwa alisema hivi; yale ameyasema, atasema akiwa ndani ya Bunge, atasema akiwa nje ya Bunge, atasema akiwa juu ya dari na atakayemsemesha atasema zaidi ya mara mbili.

Mheshimiwa Spika, nakupa taarifa, Mheshimiwa Gwajima alitwambia kwenye Kamati kwamba, ataendelea kusema, sasa kazi kwenu ninyi wenye mamlaka. Yeye amesema ataendelea kusema, amesema mbele ya Kamati na Hansard zipo zimerekodi vizuri sana, kwa hiyo tujiandae. Leo jumatatu, tusubiri jumapili inayokuja hatujui kitakwenda kusemeka kitu gani. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niongee suala la Mheshimiwa Jerry Silaa. Hapa mkononi mwangu nimechukua salary slip, hii ni ya kwangu mimi Tunza Issa Malapo. Siwezi kutaja mshahara wangu, mshahara ni siri, siwezi kutaja figure, naogopa na mimi ndiyo nitarudi kule kule kwa mwenzangu, lakini nataka kuwaambia Watanzania, nitakupa hii ya kwangu kwa ridhaa yangu uione labda inawezekana hujapata muda wa kuangalia, mimi hii ya kwangu nakatwa kodi. Ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tena nakatwa kodi ya kutosha tu, ukilinganisha na watumishi wengine wa umma, sisi Wabunge tunakatwa kodi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipokuwa kwenye Kamati tunashangaa, huyu mwenzetu haya mambo ameyapata wapi? Tukajua basi angalau atajirudi, aseme labda niliteleza, kama aliteleza basi tumwinue, twende naye, lakini mwenzetu ndiyo kwanza ametuletea vitabu mpaka vimemziba hatumwoni. Sasa yale ya vitabu sisi tukayavumilia kwa sababu, jamani Waheshimiwa Wabunge tunaongea leo tunaongea kwa fact, hivi hili suala la Jerry lilipaswa lifike hapa lilipofika? (Kicheko)

WABUNGE FULANI: Wala, hapana.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, katika hali tu ya kawaida, kwa sababu binadamu yeyote kukosea ni jambo la kawaida na ndiyo maana tunaenda Misikitini na Makanisani tunaenda kuomba msamaha. Hili suala lake mimi kwa akili yangu ya kawaida tu ndogo, ni kwamba mwenzetu mimi nilichukulia ameteleza, sasa kama ameteleza mwenye mamlaka Mkuu wa Mhimili alimwambia, you just go there, kawaambie watu kwamba niliteleza kwa sababu ushahidi si upo. Hapa hatupigi ramli ndio maana mimi mkononi kwangu nimeshika salary slip, hatufanyi ramli tunaongea vitu ambavyo vipo na vinaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lilikuwa ni suala la kwenda tu kusema kwamba nimeteleza, lakini kwa nini hawezi kwenda kusema? Ninachoona mwenzetu ana kiburi, yaani amejaa tu, ile wanayosema kunyanyua mabega, kwamba nionekane mimi nakwenda kusema nimekosea, nimefanya hivi, which is not good, katika maisha ya kawaida ya mwanadamu yoyote.

Mheshimwia Spika, sasa Mheshimiwa Jerry anatakiwa, kwanza naunga mkono adhabu aliyopewa, lakini nafikiri, sijajua sijui niseme anatakiwa apate psychological counselling sijui kitu kama hicho. Siongei hivyo kwa maana kwamba namtukana au nini, mimi ni mwalimu na Saikolojia ni somo ambalo tunafundishwa, sometimes mtu unaweza ukakuta anafanya mambo wewe unashangaa, kwa nini huyu mtu anafanya hivi! Hili suala kwa upande wangu naliona ni kubwa, lakini ni dogo, endapo tu yeye angeamua kuli-handle kwa namna ile ambayo mimi naiona.

Mheshimiwa Spika, sisi tunakatwa kodi na ile posho ambayo hatukatwi kodi ina matumizi, kama mimi nimepewa hela ya mafuta ya lita 10, nitalipia kodi hivi nitapata yale mafuta lita 10? Sipati, kwa hiyo ni mambo ya kawaida ambayo yanataka tu uelewa wa kawaida. Nawaambia Watanzania sisi Waheshimiwa Wabunge tunakatwa kodi kwenye mishahara yetu, tena kodi ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha sisi sote kukutana kwenye ukumbi huu tukiwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda kuzungumzia issue ya elimu kwa sababu ni mwalimu na nina interest kubwa sana kwenye elimu. Tumekuwa tukizungumza suala la miundombinu ya elimu kwa maana kuanzia Shule ya Msingi mpaka Kitado cha Sita kwa TAMISEMI. Pia tumekuwa tukizungumzia uhaba wa nyumba za walimu, hilo linajukana hivyo Serikali tunawaomba mwendelee kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Mtwara. Changamoto kubwa ninayoiona kwenye Mkoa wetu ni kwamba kuna baadhi ya maeneo upungufu wa walimu hali yake inatisha. Inatisha kwa maana ipi? Unakuta shule moja ina walimu wawili au watatu. Ukimwuliza Afisa Elimu, anasema, sisi tunagawa walimu kulingana na idadi ya wanafunzi; mwalimu mmoja wanafunzi 45, sawa. Kwa mfano, shule ina wanafunzi 90, maana yake unapeleka walimu wawili. Sasa wakati unapeleka walimu wawili ujue wale watoto kuanzia Chekechekea au kuanzia Awali mpaka Darasa la Saba wanasoma masomo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hao walimu wawili, maana yake pale una Mkuu wa Shule, una Makamu wa Mkuu wa Shule, hapo anatakiwa atokee Mtaaluma, atokee mtu wa nidhamu, atokee mtu wa mazingira, apatikane Mwalimu wa Zamu; hawa walimu wawili, pata picha wanajigawaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, hao hao walimu wawili, Mkuu wa Shule kila siku anaitwa kwenye vikao. Maana yake na huyu mmoja akiumwa au akipata tatizo, shule inafungwa, watoto wanakaa nyumbani. Kwa hiyo, wakati tunapiga kelele sana kwamba mtaala ubadilishwe, sijui kitu gani kibadilishwe, tuangalie pia, hao tunaowapa kazi ya kufundisha watoto wetu wako katika mazingira gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta Darasa la Saba lina masomo saba lakini una walimu wawili. Mimi ni mwalimu, ndiyo maana nimeanza kusema hivyo. Kuna kitu tunaita content mastery, yaani mimi leo kwa sababu nimesoma Physics, Chemistry na Biology, huwezi kuniambia nitakuwa mzuri kwenye Chemistry, nitakuwa mzuri kwenye Biology na nitakuwa mzuri kwenye Physics, never! Kwa hiyo, ni saw ana wale walimu wawili waliopo kwenye shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninazo shule ambazo nitakuletea Mheshimiwa Waziri, siongei kutoka hewani. Wale walimu wawili waliokuwa kwenye zile shule, unamtaka huyo mwalimu afundishe history, afundishe geography, afundishe hesabu na kadhalika, mtu mmoja haiwezekani. Ndiyo hapo tunapoanza kuwaharibu Watoto. Wakija huku juu tunataka wawe competence based. Competence hiyo wameipata wapi ikiwa kule chini alikotoka hali ilikuwa hiyo bora liende!

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu suala la kufundisha niwaambie ndugu zangu, haliishi darasani, ama halianzii darasani. Kuna kitu kinaitwe Scheme of Work unatakiwa uandae kila somo, kuna kitu kinaitwa Lesson Plan, unatakiwa uandae kila somo na kila kipindi. Mwalimu kwa siku anaingia madarasa matano au sita, tofauti tofauti aandae hivyo vitu vyote, unategemea atamfundisha mtoto vizuri! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule ziko Halmalshauri ya Wilaya ya Newala. Ninayo orodha hapa, zipo kama tisa, zina walimu wawili au watatu. Nikutajie kwa mfano, halafu ufuatilie na mpeleke walimu. Matokeo yanapotoka, hatutaki kusikia Mtwara imekuwa ya mwisho, tunataka iwe ya kwanza kwa maana watoto wapate walimu, wafundishwe vizuri. Wanazo akili, lakini hawapati mazingira bora ya kuweza kujifunza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna shule inaitwa Mpalu, ina walimu watatu; kuna shule inaitwa Mpotola, ina walimu watatu; kuna shule inaitwa Chikalule, ina walimu wawili; ziko nyingi, orodha ninayo na nitakuletea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kulisema, walimu wetu hawapati mafunzo kazini. Mwalimu akishamaliza mafunzo yake yawe ya cheti au ya nini, akiingia ndiyo tumemsahau hiyo mazima. Tunaomba walimu wapatiwe mafunzo kazini. Kuna TRCs kwenye Vyuo vya Ualimu viliwekwa kwa sababu ya kuwasaidia walimu kutoka kwenye hizi shule kwenda kupatiwa ujuzi, kama mnabadilisha vitabu, mtaala, na kadhalika, tunategemea walimu wale waendee kule. Hata hivyo, sasa hivi ukienda zimekufa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimetokea Chuo cha Ualimu ndio nikawa Mbunge, naelewa hakuna kinachoendelea kule. Kwa hiyo, hizo Teachers Resource Centre zilikuwa zinawasaidia sana walimu kwenda kunolewa ili kuongeza ujuzi kwa sababu elimu kila siku inabadilika, kuna mambo mapya, kuna zile crosscutting issues ambazo tunategemea mwalimu aweze kuzipata na kuongezewa ujuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu huyu mwenye stress ya kutokupandishwa madaraja, kutokuongezewa mshahara, hana nyumba ya kuishi, anakotoka ni mbali mpaka afike kazini, bado leo unamlundikia vipindi kufundisha kutoka awali mpaka Darasa la Saba, halafu tunakuja humu ndani tunalalamika kwamba watoto wetu sasa hivi hawaelewi, hawafanyi nini, hata wale kule wanachoka. Tuwaangalie kwa jicho la huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuongea hayo, sasa naomba nizungumzie issue ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Suala hili naliunga mkono sana kwa sababu najua umuhimu wake, lakini naomba Serikali iangalie, hata ukisoma hotuba ya Kamati imewapa ushauri. Tusiwaze sana kwenye mambo madogo madogo. Leo siyo wakati wa kumpa tu mtaji wa shilingi 50,000, anafanyia nini? Ndiyo swali tujiulize. Mnawaambia watu wakae kwenye vikundi 10, wanakaa hapo, wanazunguka usajili mpaka waje wasajiliwe unawapa shilingi 500,000. Tunataka tuwatoe kweli kwenye umasikini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huu mfuko kwanza uangalie vizuri, uwekewe utaratibu vizuri na watu tuwe na mind kubwa ya kuona kwamba tunataka tuwawezeshe watu. Unaweza ukampa mtu shilingi milioni 100 akafanya shughuli, akaajiri watu hata 20, 30, wakawa wanapata kipato kupitia yeye. Tusiangalie sana kwenye mind ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naongelea kidogo kwenye Jimbo la Mtwara Mjini, Manispaa ya Mtwara Mjini. Niliuliza swali juzi, tuna tatizo kubwa Mheshimiwa Waziri mkatuangalie, maji yanajaa sana. Yaani watu wa Mtwara Mjini sasa hivi wakiona wingu limekaa huko juu, wanajiuliza, hii mvua ikishuka hapa itakuwaje?

Mkatuchimbie mifereji, barabara nyingine zinajengwa, maana yake zinasababisha yale maeneo yawe chini. Sasa kama yako chini na mifereji haiko ya uhakika, matokeo yake kila siku maji yanaingia ndani ya nyumba za watu. Kata ya Magomeni, Kata ya Chuno, Kata ya Likombe, Shangani, maji yanaingia kweli kweli ambapo zamani maji yalikuwa hayaingii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kabisa, mfanye jitihada za makusudi mwende Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkaangalie tatizo lile na mjue mnalitatuaje kwa sababu wananchi wale walipimiwa viwanja, wananchi wale wana maeneo yao ya biashara, lakini kila siku maduka yanaingia maji. Hiyo haileti afya kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nakushukuru sana. Mimi ni mtu wa kwenda muda. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi asubuhi ya leo niweze kuchangia.

Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Nianze kuchangia kwenye issue ya kubadilisha mtaala. Kwangu nafikiri Serikali inatakiwa ifanye hili jambo kwa utulivu kwa kusikiliza wadau, ninachoona elimu yetu ya Tanzania wakati mwingine inaathiriwa sana na matamko ya kisiasa. Mwanasiasa mwenye madaraka akiamka asubuhi analolifikiria yeye bila kufuata ushauri wa kitaalam kwasababu, kwenye elimu kuna mambo mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia kubadili mtaala sio jambo la siku moja. Tunatakiwa tufanye need analysis kwa nini huu uliopo haufai na kama haufai tunaongeza nini au tunapunguza kitu gani? Sio suala la kuamka siku moja ukasema watoto wasijifunze hiki wajifunze hiki na kunatakiwa kuwe na taratibu lakini kuwe na maandalizi. Kwa sababu, unapobadilisha mtaala ukumbuke unatakiwa walimu nao uwafundishe waweze kwenda kuutekeleza ule mtaala ambao wewe unautaka. Lakini unakwenda kubadilisha mtaala elimu za msingi, walimu ngazi ya cheti wanafundishwa yale yale ya zamani, hiko ndio kilichopo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fuatilia mtaala wa ngazi ya cheti unaofundishwa, halafu fuatilia mambo tunayoyataka watoto wetu wa shule za msingi wayasome. Kwa hiyo, ninachoomba tufanye mambo kwa utulivu tuangalie, tumetoka wapi? Tuko wapi? Na tunataka kwenda wapi? Tuache mihemko tuna wataalam wazuri kweli kweli tuepuke mambo ya kisiasa.. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kuzungumzia Idara ya Udhibiti Ubora, kwangu natambua sana umuhimu wa Idara ya Udhibiti Ubora, lakini kila tukisimama humu ndani hata ukisoma hotuba ya kamati imeeleza wana changamoto kubwa ya fedha. Tunaweza leo tukaona udhibiti ubora hawafanyi kazi zao sawasawa pamoja na mambo mengine, lakini wanakosa bajeti ya kutosha. Ili mtu aweze kukagua ni lazima afike, anafikaje kama hana gari, hana mafuta, hana vitendea kazi ama watumishi wachache? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anajua namna Idara hii ilivyo na changamoto ingawa kuna baadhi ameanza kuzitatua. Nikiri kwasababu, nafuatilia najua kuna baadhi zimeanza kutatuliwa lakini nguvu zaidi inahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kitu kingine ninachotaka kusema, kila mtu anahitaji watoto wasome, yaani mimi Tunza ukiniuliza ninahitaji wamakonde wenzangu kule kwetu wasome. Lakini, issue inakuja mdhibiti ubora yeye ana checklist ili asajili shule kuna vigezo ambavyo vimewekwa. Shule iwe na choo, iwe na madarasa mangapi, iwe na ofisi, iwe na madawati, kuwe na vitabu, kuwe na walimu kuwe na nini, anaweza kuisajili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sio kwamba akikuta tu wanafunzi wamekaa wanasoma anaweza kusajili. Sasa pendekezo langu kwa Wizara, tunataka wasome lakini pia tunataka wasome katika mazingira bora. Kwasababu, tendo la kujifunza linahitaji mazingira bora tusichukulie tu kwamba, watu tunataka wasome no! Tunataka wasome katika mazingira bora. Labda, kwasababu, population inaongezeka mahitaji ya watoto kusoma ni makubwa. Labda tuangalie mrudi kwenye zile checklist ikiwezekana basi hizi shule zipangwe kwa madaraja. Kwamba, hii imesajiliwa imekidhi vigezo vyote, hii tumeisajili tunaipa uangalizi miaka mitatu, hii tunaisajili tunaipa uangalizi mwaka mmoja urekebishe hiki na hiki na hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda twende kwa mtindo huo tunaweza tukafanikiwa, lakini tukiacha tu kwamba kila shule mtu akitaka isajiliwe basi isajiliwe, hata kama haijatimiza vigezo maana yake ni nini? Tunaweza kwenda kusajili shule lakini zikatoa elimu ambayo sisi hatukuitarajia. Matokeo yake tukija humu ndani tena tutakuja kulalamika kwamba, watoto wetu wanajifunza lakini hawaelewi hawawezi kuajirika kumbe tumeharibu msingi tangu kule wakati tunasajili zile shule zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hilo suala kwasababu, tunataka watoto wetu wasome ni suala la kukaa wakaguzi waangalie namna gani wanakwenda kuweka vigezo mbalimbali na shule zingine ziwe kwenye uangalizi ili kusudi watoto wasikose kusoma lakini pia wasome katika mazingira ambayo yataweza kuwafanya wao wajifunze vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kumalizia kwenye hoja ya vyuo vya ualimu. Natambua kwamba, Serikali kuna baadhi ya jitihada imefanya ikiwemo kuboresha majengo ya vyuo vya ualimu. Kwa mfano, Chuo cha Ualimu Mtwara kawaida kweli majengo yameboreshwa, lakini uboreshaji ule wa majengo yale uende sambamba na uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi. Unaweza ukawa na majengo mazuri lakini wafanyakazi waliopo pale kama huwatekelezei matakwa yao kwa mujibu wa sheria, wafanyakazi wa vyuo vya ualimu hata annual increment ya mishahara yao ni shida. Hata kupata pesa za likizo, kupata nauli, kupandishwa madaraja, kulipwa kwa wakati kwao ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wale wafanyakazi wa vyuo vya ualimu wakufunzi ni watu wa kuwaangalia kwa jicho la pekee. Kwasababu, elimu yote tunayozungumza shule za msingi ndio wao wanakwenda kutengeneza walimu. Lakini pia, Mheshimiwa Waziri namuomba akaangalie namna mtaala wa grade A ule wa cheti, unavyoendana na mabadiliko yanayofundishwa shule za msingi. Kama kuna gap tunaomba hilo gap walitoe kwasababu, nimekuwa nikifuatilia sana wakufunzi wanalalamika kwamba, kile kitu ambacho kiko huku kwenye ngazi ya cheti, ni cha zamani ukilinganisha na kitu ambacho kinafundishwa shule za msingi sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zile TRCs, Teachers Resource Centers naomba zitumike kwasababu, niliongea hapa hata kisu kinatakiwa ukikinunua unakitumia baadaye unakinoa kuongeza makali yake. Kwa hiyo, zile TRCs zilikuwa zinasaidia walimu kufanya mafunzo kazini, wanakwenda pale wanaongezewa maarifa kwa hiyo, mambo yanakwenda vizuri. Naomba uangalie sana Idara ya Ukaguzi kwa jicho la pekee kwasababu, Idara ya Ukaguzi ndio CAG wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo machache nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha sisi sote kuwa hai na kukutana kwenye Bunge hili leo. Maji ni uhai. Sisi watu wa Mtwara nafikiri katika mikoa ambayo inaongoza kutokuwa na maji ya uhakika ni pamoja na Mkoa wa Mtwara. Leo ninataka niongelee mambo muhimu matatu.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, naishauri Serikali, sehemu ambapo maji yanaanzia au yanakotoka kama ni kisima, kama ni mto, kama ni bwawa muanze kuwapa huduma wale halafu yaendelee sehemu nyingine. Kumekuwa na changamoto kubwa sana, unakuta chanzo cha maji kipo pale, wameweka mabomba lakini maji yanakwenda kupatikana sehemu nyingine na wale watu ambao wanaishi pale kwenye kile chanzo cha maji hawapati maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, kuna Kata moja inaitwa Naliendele. Kuna mradi mmoja wa maji unaanzia Mtaa wa Mbawala chini, huko mbawala chini wenyewe wanaona mantenki, wanaona mabomba lakini hawapati maji. Ile inakatisha tamaa. Mradi ule pia nimeona umeuzungumzwa kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri, kwa sababu unasuasua, tunaomba ukarekebishwe ufanya kazi vizuri kama alivyoandika kwenye hotuba yake ili kusudi wananchi wale wapate maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine huduma ya maji ni huduma lakini kwa wakati mwingine ni biashara. Kumekuwa na masuala ya kusuasua sana, wananchi wanalalamika sana, mtu anakwenda Idara ya Maji, wanamfanyia tathmini analipia, lakini kuja kuunganisha maji inachukua muda mrefu. Vifaa hakuna, mita hakuna, mabomba hakuna.

Mheshimiwa Spika, unapotaka kufanya biashara wakati unatoa huduma ni lazima ujidhatiti. Kwa hiyo, suala hili nalo pia katika Manispaa ya Mtwara Mikindani lipo, watu wanalipa lakini wanachelewa kuunganishiwa maji kwa sababu ya ukosefu wa vifaa. Tunaomba wenye mamlaka walifanyie kazi kwasababu tumeongea sana. Ukiona nakuja kuongea huku Bungeni, nimeanza kuongea kwenye Baraza la Madiwani. Tunaomba lifanyiwe kazi ili mtu akilipa fedha yake anataka huduma ya maji, basi apatiwe kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine la mwisho kubwa ninaloliongelea ni mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma kuleta katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, mradi huo ukipita katika baadhi ya Vijiji vya Jimbo la Mtwara Vijijini.

Mheshimiwa Spika, kama unakumbuka nilikuwepo kwenye Bunge lililopita. Huu mradi kuandikwa kwenye hotuba za Waziri umeandikwa sana, lakini haujawahi kutekelezwa kwa hatua yoyote. Hata leo Mheshimiwa ameuandika, nimeuona na nimeusoma. Ameandika kwamba huu mradi umetengewa shilingi bilioni sita; shilingi bilioni moja kutoka Serikali yetu ya Tanzania na shilingi bilioni tano kutoka Benki ya Afrika. Ombi langu kubwa tunaomba sasa isiwe historia.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kubwa, tunaomba sasa isiwe maneno matupu, huu mradi uende ukafanyiwe kazi na sisi watu wa Mtwara tunatamani tupate maji safi ya baridi na salama. Kwa mfano sasa hivi ukija Manispaa ya Mtwara Mikindani maji tunapata hatuwezi kumkufuru Mungu tukasema maji hatupati, maji tunapata, lakini Mheshimiwa Waziri anayajua ladha ya yale maji, akasema ili tutatue tatizo la maji ni lazima huu Mradi wa Mto Ruvuma ufanyiwe kazi.

Mheshimiwa Spika, huu Mradi wa Mto Ruvuma ni mradi mkubwa na naamini ukifanyiwa kazi utakwenda kutatua changamoto ya maji kwenye majimbo mbalimbali ya Mkoa wa Mtwara ikiwemo Mtwara Manispaa, Mtwara Vijijini, Nanyamba, Tandahimba na Newala kule Nanyumbu huu mradi utakwenda kufanya kazi kwa sababu wananchi wa Mkoa wa Mtwara walio wengi ukiacha Mtwara Mjini na hizi sehemu kidogo za mjini hawajui kufungua maji bombani.

Mheshimiwa Spika, RUWASA wanasema maji bombani sisi kule kwetu tunasema maji ya kuokota. Mtu unasubiria mvua inyeshe yale yanayotiririka chini ndiyo yaingie kwenye kisima. Watu kila siku wanaumwa matumbo, watu wanaumwa typhoid kwa sababu ya maji ya kuokota. Sasa leo sitaki kuongea sana Mheshimiwa Waziri ameandika mradi huu na hii siyo mara ya kwanza kuandika, naomba kwa heshima na taadhima, mradi huu uende ukafanyiwe kazi. Ni bora afanye mradi mkubwa hata ikiwa kwa awamu, lakini ukiisha unakwenda kutatua changamoto kubwa ya maji ambayo inaukumba Mkoa wa Mtwara.

Mheshimiwa Spika, naishi Mtwara na najua ukipita Mtwara unakuta mashimo yanayoitwa visima, kama mtu hujazoea unaweza ukashangaa. Tunataka nasi tuvute maji majumbani kwetu yaliyo safi na salama ili kusudi tuweze kuishi kama Watanzania wengine, tunalipa kodi kubwa sana kwa nchi hii, tunaongeza pato la Taifa kubwa sana kwa nchi hii kwa sababu sisi tunazalisha korosho ambayo ni among of the big five cloves zinazoleta pesa katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naamini nimesikika na nimeeleza yale yaliyoko moyoni kwangu. Ahsante sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa zawadi ya uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati napitia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi nimepata mshituko wa moyo, kwa nini nimepata mshituko, ukiangalia kwa miaka mitano mfululizo wanatenga pesa za maendeleo, lakini haziendi. Kwa mfano nakupa ya miaka mitatu huko nyuma sitaki kurudi, mwaka 2017/2018 walitengewa bilioni nne haikwenda hata sumni, mwaka 2018/2019 Sekta ya Uvuvi peke yake ilitengewa bilioni saba ikapewa bilioni nne, 2019/ 2020 ilitengewa bilioni 14 ikapewa bilioni tatu, mwaka huu ambao tunaumaliza kesho kutwa 2020/2021 walitengewa bilioni 13 mpaka leo wamepewa bilioni nne.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilichonishtua nini? leo wametengewa bilioni 99, ikiwa bilioni nne, bilioni 13 zinawashinda kupeleka, hizi bilioni 99 wanazitoa wapi? Ndio maana nakwambia nimeshituka, sasa Mheshimwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atueleze mkakati wao, kutengwa kwa pesa nyingi maana yake tunaraji tukapate maendeleo makubwa kwenye hizo sekta kwa sisi ni furaha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, furaha hii inakwenda kuingia huzuni kwa sababu walikuwa wanatengewa kidogo, lakini haziendi mpaka huu mwaka tuliopo sasa hivi tupo mwezi wa tano tunaumaliza wamepewa asilimia 31 tu katika bilioni 13, leo wanapata wapi courage ya kutenga bilioni 99, nataka akija hapa atueleze ni kitu gani hicho kilichowapelekea wao kufikiria watapata bilioni 99, hatutaki maneno, maneno tunakata vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mshtuko wangu wa pili, sisi Watanzania tuna maziwa makubwa, tuna Ziwa Victoria, tuna Ziwa Nyasa, tuna Ziwa Tanganyika, sisi watanzania tunaukanda mrefu sana wa bahari, sisi Watanzania tuna deep sea, bahari kuu maana yake. Unaamini kwamba kwa mwezi tunaagiza samaki tani 24,000 zinaingia nchini kwetu, pamoja na kuwa na hivyo vitu vyote, nimepata mshituko kwa sababu safari hii wakati naelekea kuchangia Wizara hii niliamua nijipe muda kidogo nisome, kwa hiyo huo mshituko wangu wa pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshtuka kwa sababu sisi kama Taifa tunatumia takribani bilioni 58 kwa mwezi kuagiza samaki nje, tuna Bahari ya Hindi, tuna Ziwa Victoria, tuna Ziwa Tanganyika, tuna Ziwa Nyasa. Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha atupe majibu tunakwama wapi? na kwa nini tunakwama? Mwenyezi Mungu atupe nini? kwa kiasi cha maji tuliyokuwa nayo sisi na hivyo nimekutajia makubwa, tunayo madogo karibia kila mtu kwao hapa utakuta kuna bwawa, ukienda Morogoro bwawa Mindu sijui huko wanavua, sijui nini, kuna mito midogo midogo watu wanavua, nimekutajia haya makubwa. Tuna sababu gani ya kuagiza Samaki wengi hivyo kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati naendelea kutafuta baadhi ya sababu ndiyo hizi zingine kwa sababu hela haiji, hela kama haiji wizara inashindwa kuwekeza, ama wizara haina mikakati thabiti kwa sababu gani, binafsi yangu sifikirii mpaka leo wavuvi wetu waingie baharini wakatafute Samaki wakati, yaani wakienda na ile kwamba Mungu akipenda nitapata. Kuna vifaa vya kisasa vinavyotambua tu kwamba ukiingia baharini sehemu fulani ndiyo Samaki wapo wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unamwomba Mungu, lakini Mungu huyo ndiyo katupa sisi maarifa, Mheshimiwa Ulega wewe hii ni taaluma yako na unaijua, unatakiwa uwe serious my brother sasa hivi tunatakiwa twende kwenye uvuvi wa kisasa, jamani Samaki tunawaacha huko baharini kama mnakumbuka ile meli iliyokuwa inaitwa meli ya Magufuli hivi wale walivua Samaki kiasi gani? wenye ukubwa gani? nyinyi wote hapa ni mashahidi, lakini leo sisi tunavua Samaki ndio hao wanakujaga kupimwa na ruler hapo kwenye kantini. Maana yake hata kile kimo hajafika kwa sababu gani, kwa sababu ya kukosa zana bora za uvuvi, Serikali iwekeze hapo ndipo tunapofeli haya matatizo yote yanatokea hivyo, leo mwenzangu hapa jirani yangu wakati anachangia alikuwa anasema matumbawe yanaharibiwa, lazima yataharibiwa si wanatafuta mabomu, akipiga pale anapata samaki wake anarudi nao nyumbani, hana zana bora unategemea atavuaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, twendeni tukawekeze hapo. Uchafuzi huu wote watu kuhangaika kukimbizana na samaki wadogo wadogo hakuna mtu anayetaka apate samaki kidogo ama apate samaki wadogo ni kwa sababu anakosa dhana bora za uvuvi. Badala ya kukimbizana kuchoma nyavu fanyeni jitihada za makusudi mwambie mtu nyavu hii usivulie, vulia kifaa hiki, hakuna mtu anayependa maisha magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa jambo moja dogo, lakini lina umuhimu wake. Sisi wanawake tuliowengi ndio wafugaji wa kuku, tuliowengi, iwe wale wa kisasa iwe wa kienyeji hata mwenyewe nafuga kwa kiasi kidogo, lakini nafuga. Kuna changamoto kubwa sana kwenye sekta hiyo na wanawake wengi ndio wanaponea huko, hiyo mikopo ya halmashauri ya asilimia kumi sijui nini wengine wanachukua kwenda kufuga. Hata hivyo, tunapata changamoto, kwanza upatikanaji wa vifaranga siyo wa uhakika, unaweza kutafuta kifaranga leo mwezi wa tano ukaambiwa order utaipata mwezi wa tisa, jiulize tangu leo mpaka mwezi wa tisa hapo hiyo hela unaifanyia nini. Ukipata kifaranga chakula bei juu, ukipata chakula chanjo hazieleweki, unaweza kuweka kuku bandani umewapiga chanjo zote wakaja kufa usitoke hata na kuku mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali iweke mkakati wa makusudi wa kunusuru wanawake na hata wanaume ambao wanafuga kwa kuhakikisha wanapata huduma bora za usaidizi, wanapata chakula kwa bei nzuri ili kusudi iendane na soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo mengi yenye umuhimu, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi mchana wa leo nami nichangie kidogo kwenye Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la kilimo cha umwagiliaji hapa pana changamoto nyingi. Tunafahamu kilimo kinahitaji maji na siyo lazima yawe maji ya mvua ndiyo maana tunasisitiza kwamba kuwe na kilimo cha umwagiliaji. Ukiangalia eneo linalofaa kwa umwagiliaji ni asilimia ndogo sana inatumika. Hata ile inayotumika ufanisi wake bado ni mdogo.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa kwenye Kamati ya Kilimo, tumepita kwenye miradi ya umwagiliaji, utasema nao kule kwenye miradi wanalima kwa kutegemea mvua. Binafsi nilikuwa nategemea kwamba tunapokwenda sehemu ambayo ina skimu ya umwagiliaji tukute shughuli za kilimo zinaendelea mwaka mzima lakini mambo yanayoendelea pale hayaridhishi. Unaambiwa pesa nyingi za Serikali ziko pale lakini kinachoendelea hakieleweki. Huko kwenye umwagiliaji miradi mingi pesa imepigwa, vyanzo vya mapato havieleweki ile miradi ambayo ipo…

T A A R I F A

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Kunti.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nimuongezee tu Mheshimiwa Tunza kwamba vyanzo vya mapato vinavyotarajiwa kukusanywa mwaka huu wa fedha kupitia sekta ya umwagiliaji ni uuzaji wa nyumba pamoja na magari chakavu ambapo wanatarajia kukusanya shilingi milioni 15.

Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo sekta ya umwagiliaji. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Tunza, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa mikono miwili, inaonesha ni namna gani Serikali haiko serious kuwekeza kwenye umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano ukija Mkoani kwetu Mtwara, Mkoa mzima wa Mtwara wameainisha kwenye hotuba yao kwamba eneo linalofaa kwa umwagiliaji ni hekta 24,317 lakini zinazotumika ni 3,729, ni asilimia 15 tu. Matatizo haya ya kutokuwekeza kwenye kilimo kingine tofauti na korosho ndiyo maana watu wa Mtwara korosho ikifanya vibaya utasema tuko msibani. Kama sasa hivi nenda Mtwara uikute hali yake, mimi nimetoka huko juzi. Kilimo cha mazao ya korosho, mpunga, mahindi hayaeleweki, kilimo cha umwagiliaji kiko asilimia 15 tu; nenda huko kwenye skimu kwenyewe hakuna kinachoeleweka.

Mheshimiwa Spika, hii Wizara inatakiwa iwe serious. Ukipita kwenye skimu zote za umwagiliaji zina migogoro. Kwa nini wanawekeza pesa sehemu ambazo hawajatatua migogoro? Watu wanashindwa kulima kwa sababu ya migogoro iliyopo pale; Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri ni mashahidi. Tatueni migogoro, wawezesheni watu walime ili tutoke hapa tulipo tusonge mbele. La sivyo, kila siku tutakuwa tunaimba lakini kile tulichokikusudia hakiwezi kuleta tija kwa sababu hatuweki misimamo iliyo sahihi na thabiti kukiendea kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee korosho kidogo, wenzangu wameongea sana, mwenye masikio asikie. Sisi watu wa Mtwara hatutaki kuchanga ile pesa ya pembejeo; yaani huo ndiyo msimamo wetu, hatutaki. Hatutaki kuchanga kwa sababu gani? Mtu hauwezi kukataa bila kuwa na sababu. Sisi hatutaki kuchanga kwa sababu kuna export levy imekusanywa, ninyi mnajua, siyo chini ya bilioni 400.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, hawa Wamakonde wakikwambia kitu fulani hatutaki yaani wanamaanisha. Ukisikia hatutaki chichi hicho kitu yaani ujue hawataki. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Tunza, endelea. (Kicheko)

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru unatuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa watu wana hela zetu na wanajua wanazo, kwa nini leo wanatulazimisha tuchange? Zile hela zetu ambazo mnazo kule tangu msimu wa 2017/2018 mpaka leo mmezitumia kufanyia nini?

Mheshimiwa Spika, mimi nikiwa Mbunge ninayetokea Mkoa wa Mtwara, tunawaambia kabisa tafuteni namna sisi tupate pembejeo, watu walime tuvune korosho tuuze. Hizo habari za kutuzungukazunguka kutuambia sijui tukatwe shilingi 110 kutoka kwenye kila kilo ya korosho hatutaki kwa sababu hela zetu mnazo. Yaani ninyi msituzugezuge kutuona kama sisi hatuelewi, sisi tunaelewa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho nalotaka kumalizia; mimi najiuliza sisi kama nchi hivi ni zao gani kabisa tunajivunia kwamba hili zao ndiyo tunalilima kwa kiasi kikubwa?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Tunza, dakika ndiyo hizo.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya siku ya leo, nianze mchango wangu kwa kutoa shukrani za dhati kabisa kutokana na ile kauli ya Waziri Mkuu aliyosema msimu huu wa korosho korosho zote zitasafiri kupitia bandari ya Mtwara. Watu wa Mtwara, watu wa Kusini tunajua na tunathamini mchango huo kwa sababu tunatambua ni nini kinakwenda kutokea, hicho kilikuwa ni kilio chetu cha siku nyingi ndani miaka mitano korosho zilikuwa zinasafirishwa nje ya bandari ya Mtwara hivyo kusababisha mambo mengi ya kiuchumi kusimama Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kama korosho zitasafiri kupitia bandari ya Mtwara tunategemea watu wenye maghala watakodisha pale, tunategemea wafanyabiashara wadogo wadogo, mama lishe, wanawake wenzangu mimi Tunza, watafanya biashara pale na mambo mengine yatakwenda kuwa sawasawa. Nishauri bandari ile isiishie kutumika kwenye zao la korosho tu itumike pia kwenye mazao mengine na kwenye shughuli nyingine, kwa sababu Serikali imewekeza pesa nyingi pale ambazo ni kodi za Watanzania hivyo ikiendelea kutumika tunasema ile value for money itaonekana pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe shukrani za dhati kwa hilo na naiomba Serikali iondowe zile changamoto za makontena za tozo kubwa kubwa ili kusudi ivutie wafanyabiashara waje kuitumia bandari ya Mtwara nasi watu wa Kusini Watanzania halisi tupate kunufaika na hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwenye zao la korosho naiomba Serikali iangalie kwa undani suala la pembejeo kumekuwa na malalamiko mengi kama tunaenda kutumia bandari basi pembejeo nazo zipelekwe kwa wakati na kwa ubora na kwa uwingi unaotakiwa ili kusudi watu walime wapate korosho nyingi ili ile bandari inayokwenda kutumika sasa ipate manufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungumzie kidogo TRA, unapotaka kupata pesa ni lazima uwekeze, usitegemee kupata pesa bila kuwekeza. Naishauri Serikali kama kuna mtu anakwenda TRA ukabahatika kufika na ukahudumiwa na mfumo bila kuambiwa mfumo, sijui mtandao uko chini, mtandao unasumbua, mtandao unafanya nini, ni bahati sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha hili ufanya maendeleo ni lazima upate pesa. Waliopewa dhamana kukusanya pesa ni TRA sasa tunaomba mboreshe mfumo wa TRA ili kusudi mtu ukitoka nyumbani siku hiyo, maana yake nisiwaambie kulipa kodi nako ni moyo, mtu ametoka nyumbani amebeba pesa yake anatamani aende TRA akalipe kodi anafika pale anaambiwa mfumo haufanya kazi, akirudi nayo ile pesa nyumbani hatuna uhakika kama kesho atarudi tena kwenda kuufuata mfumo unafanya kazi ama haufanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naiomba Serikali kwa moyo wa dhati kabisa wekezeni kwenye mifumo hii inayotumika kukusanya mapato ili kusudi mtu anapoamua kwenda kulipa akifika pale alipe aondoke. Uwe ndiyo mfanyabishara hawezi kutamani kufika TRA akae masaa matatu, manne matano mwisho wa siku unamwambia mfumo haufanyi kazi akirudi nyumbani ile pesa anaingiza kwenye mzunguzuko wewe Serikali unakuwa hujapata chochote. Mkaimarishe kwenye vitengo vyote hata kule LATRA nako pia kuna usumbufu wa mtandao ukienda inawezekana usipate huduma, mitandao yetu haijakaa sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wananchi watalipa kodi kwa hiyari wakiona maendeleo. Mfano watu wa Mtwara tumekuwa tukilia kila siku kuhusu ile barabara ya kutoka Mtwara Mjini inayopita Nanyamba, Tandahimba, Newala, inakwenda Masasi, kilometa 210 tu zimezungumzwa na Wabunge waliopita sisi wengine tumeingia hiki ni kipindi cha pili tunazungumza mpaka leo mmejenga kilometa hamsini, hivi kilomita 210 kwenye eneo ambalo zinatoka korosho! Korosho hizo zinazochangia Pato la Taifa la nchi hii kwa kiasi kikubwa kilomita 210 just kilomita 210 zinawashinda kitu gani, twendeni mkatutengenezee hizi hili na sisi tutakapokuwa tunalipa kodi tulipe kodi kwa kujivuna kabisa kwamba tunalipa kodi na maendeleo tunayaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukienda kule Mtwara katika Mikoa inayoongoza ukosefu wa maji ni pamoja na Mtwara, mkatutekelezee mradi wa maji ya kutoka Mto Ruvuma ili tunapolipa kodi tujue kodi zetu zinatumika kutuletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika hii miradi ya REA kama kuna mkoa umefanya vibaya kwenye miradi ya REA ni Mkoa wa Mtwara, kuna vijiji vingi havina umeme tunashukuru Mheshimiwa Waziri wa Nishati alituita sisi Wabunge wa Mtwara kutuhakikishia kwamba Wakandarasi ambao wamekwenda safari hii watakwenda kufanya vizuri. Tunaomba msituache nyuma kila kitu, ukienda maji tatizo Mtwara, umeme Mtwara, barabara Mtwara tunaomba muende mkatutekelezee na hospitali ya Kanda ya Kusini tunaomba iende ikafunguliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani tupate huduma tukiwa kwenye Kanda zetu wala siyo lazima tufike Muhimbili, kule kukiwa kuko poa tutaishia huko huko ingawa huku kwingine tutakuja kufanya mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nishauri kwenye issue za fursa za mapato, mimi nimekuwa kwenye Kamati mbalimbali, Wakurugenzi wanapokuja kwenye Kamati tunawashauri mkatafute vyanzo vipya vya mapato, mimi naishauri Serikali kuwe na kitengo maalum chenye wataalam wa kuweza kufanya utafiti, analysis ya kutosha kujua kwa mfano ukienda Mkoa wa Mtwara Halmashauri fulani inaweza ikawa na fursa ya mapato moja, mbili, tatu, wawashauri wale halafu yale malengo yanayowekwa yale, wale Maafisa Mipango wetu yule mtu atakayefanya vizuri basi aonekane amefanya vizuri amefikia malengo na yule ambaye ajafanya vizuri aambiwe ajafanya vizuri na pia kuwe na training. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua mimi tatizo lingine ninaloliona sijui kwa sababu ni mwalimu huwa naona kama wafanyakazi wengi wa Serikali wakishaajiriwa hakuna mafunzo kazini, wakati mambo yanabadilika, mambo hayako vilevile watu wanatakiwa wapewe mafunzo waambiwe sasa hivi kama nchi tunaelekea huku tunaomba mfuatilie moja mbili tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi Tunza ukiniuliza fursa ambazo zinaweza zikapatikana Mkoa wa Mtwara naweza nikakuambia tuna fursa ya gesi ule mradi wetu wa LNG ufanyiwe kazi, tuna fursa ya korosho lakini kwa masikitiko makubwa nakuambia hakuna kiwanda chochote cha maana kinachofanya kazi ya ubanguaji. Hizo ndiyo fursa tuna bahari hatuna bandari ya uvuvi, hatuna meli, hatuna viwanda vya samaki pesa tunazitoa wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliambiwa kiwanda cha mbolea mpaka leo hatukioni hizi ndio fursa za mapato ambazo mimi ukiniuliza layman tu ambaye sijui uchumi naweza nikakuambia, Wachumi wetu watushauri vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie jambo moja hili ni ombi kwa Serikali, katika Manispaa ya Mtwara Mikindani kuna mgogoro unaendelea kati ya wafanyabishara wadogowadogo ambao walikuwa wanafanya biashara soko la sabasaba Serikali imejenga soko zuri na soko la kisasa, wafanyabiashara walizoea kufanya biashara kwenye hilo soko la sabasaba sasa hapa pana mgogoro, wale wafanya biashara ni wafanyabiashara wadogowadogo, wengine ni wanawake wana mitaji midogo naomba Serikali iangalie suala hili kwa busara zaidi kuliko kutumia nguvu. Waone ni namna gani ya kukaa na hawa wafanyabiashara ili kusudi wafanye biashara zao kwa amani watumie lile soko letu la kisasa ambalo limejengwa lakini waangalie na huku wanawaachaachaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha nakuuliza swali langu la mwisho ile issue yetu ya export levy kutoka kwenye zao la korosho unatuachaachaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kukutana leo na mimi nikapata kuwa mchangiaji wa kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiunga mkono hotuba ya Kamati ya Bajeti wamechambua vizuri na kutoa ushauri mzuri sana kwa Serikali. Kwa hiyo pamoja na yote ambayo sisi Wabunge tutaendelea kushauri lakini Serikali itulie isome hotuba ya Kamati ya Bajeti kuna mambo mengi ambayo yatasaidia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hotuba ya Bajeti ukurasa wa 27 wameeleza Serikali imekuwa ikileta vipaumbele vingi. Serikali imekuwa ikileta miradi mingi ya mikakati, lakini ni kama tu inatajwa kwenye mpango, inatajwa kwenye bajeti, lakini haifanyiwi kazi. Kwa mfano, kule kwetu Mikoa ya Kusini kuna ule mradi wa LNG kuna mradi wa Reli ya kutoka Mbamba Bay mpaka Mtwara kila siku inatajwa. Kuna mradi wa Makaa ya Mawe wa Liganga na Mchuchuma kila siku ile miradi imekuwa ikitajwa, lakini haifanyiwi kazi ama haitekelezwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo mradi wa Makaa ya Mawe, huo mradi wa reli ungekuwa umetekelezwa leo hii tusingekaa humu ndani Wabunge wa Mikoa ya Kusini kulilia Bandari ya Mtwara haifanyi kazi vizuri, kwa sababu mizigo ingekuwa ina uwezo wa kusafirishwa vizuri kwa njia ya reli, Makaa ya Mawe kila siku yangekuwa yanaingia pale bandarini kwa uwingi wake maana yake meli zingekuwa zinafika na leo tusingekuwa tunahangaika kwamba makasha hakuna, meli hakuna, korosho badala ya kusafirishwa Bandari ya Mtwara ziende zikasafirishwe Bandari ya Dar es Salaam. Haya yote ni kwa sababu kuna miradi ambayo ingetekelezwa ingesaidia ku- boost Bandari ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakapokuja kuhitimisha atuambie huu mradi wa Reli kutoka Mbamba Bay mpaka Mtwara unakwenda kutekelezwa ama hautekelezwi? Kama hautekelezwi basi auondoe kwenye mpango, siyo kila siku tunauona lakini haufanyiwi kazi. Pia aje atueleze mradi wa Makaa ya Mawe wa Liganga na Mchuchuma unakwenda kutekelezwa ama hautekelezwi kama hautekelezwi asifanye kazi ya kuandika kwenye mpango kila mwaka, mimi huyu leo nipo Bungeni mwaka sita tunauona, lakini haujawahi kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wenzetu wa Kamati ya Bajeti wameshauri kama anafikiri hawezi kutekeleza aandike vipaumbele vichache ambavyo vitatekelezeka akishamaliza basi ahamie kwingine si kila siku anaandika halafu hatekelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na bandari naomba mtuangalie watu wa Mikoa ya Kusini hususani Mtwara kwa jicho la huruma, kuhusu pembejeo za kilimo ya zao la korosho, unakumbuka kulikuwa na mjadala mkubwa hapa wa export levy na nini na nini, mwaka huu watu wamelima hivyo hivyo ingawa pembejeo zimechelewa korosho zimepatikana korosho tulitegemea zitasafiri kwa Bandari ya Mtwara, lakini pana changamoto haya zinaenda huko Dar es Salaam lakini tunaomba kwenye msimu ujao mpango huu uende ukatueleze unakwenda kuhakikisha vipi pembejeo za wakulima iwe wa korosho, iwe wa mahindi kwa sababu wenzetu huko Mikoa mingine nao pia wanalia mbolea imepanda bei na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango ukaeleze unakwenda kujipanga kwa namna gani kuhakikisha wakulima wa Tanzania ambao ni wengi wanachangia Pato kubwa la Taifa ingawa wanafanyakazi katika mazingira magumu na hatarishi wanakwenda kuwawezesha namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu nyingine kuhusu madeni ya Wakandarasi. Ukisoma kwenye mpango, ukisoma hotuba mbalimbali unakuta kwamba nchi yetu hii inapoteza pesa nyingi sana kwa sababu ya kuchelewa kuwalipa Wakandarasi. Wakandarasi wanakuwa wamefanya kazi wamemaliza wamepeleka certificate kule, lakini Wizara ya Fedha inachelewa kutoa pesa. Inapochelewa kutoa pesa kinachotokea ni nini, kunakuwa na riba, kunakuwa na tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ripoti ya CAG amekagua miradi saba tu, karibia Shilingi Bilioni 14 zinapotea kwa sababu ya Wizara ya Fedha kuchelewa kuwalipa Wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano tu, ujenzi huu wa reli ya kisasa umetoa riba na tozo kama hasara karibia Bilioni Mbili na point fedha hizi Wizara ya Fedha ingekuwa inalipa kwa wakati maana yake hizi fedha zingekwenda kufanya mambo mengine ya maendeleo. Kwa hiyo, katika huo mpango tunamuomba Mheshimiwa Waziri atueleze anakwenda kuhakikisha vipi certificate za Wakandarasi zikifika anawalipa kwa wakati na pia asizalishe madeni mengine. Wakandarasi waliowengi ni wafanyabiashara wadogo wadogo, wanakopa benki wakitegemea wafanyekazi warudishe zile pesa, usipowalipa kwa wakati unawakwamisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee mambo mawili ya mwisho, la kwanza sisi watu wa Kusini tuna Mto unaitwa Mto Ruvuma una maji safi na mengi kweli kweli, lakini nikikuambia jambo la kusikitisha katika Mikoa yetu ya Kusini hususani Mkoa wa Mtwara ndiyo Mikoa ambayo inaongoza kwa ukosefu wa maji kwa kiasi kikubwa. Huu mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma kuja Mkoa wa Mtwara umekuwa ukizungumzwa siku nyingi unaandikwa lakini hautekelezeki. Naomba kwenye Mpango aende akatueleze ana mkakati gani wa makusudi wa kuhakikisha mradi huu wa maji kuyatoa Mto Ruvuma kuleta katika Miji ya Mtwara, Mtwara Mjini, Nanyamba, Tandahimba na kwingine unakwenda kutekelezeka kwa namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ile barabara yetu kila siku tunaiongelea ya kutoka Mtwara Mjini inapita Tandahimba, Newala mpaka Masasi ya kilometa 210, wamejenga kilometa 50 tu hizo zingine wanakwenda kuzimaliza lini. Tunaomba mpango uje ueleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la mwisho kabisa, sasa hivi Serikali imekuwa ikikusanya mapato yake mengi kupitia mifumo, unapokwenda ardhi utapewa control number, unapokwenda TRA utapewa control number na kokote kule, lakini suala hili nimekuwa nikiliongea Serikali inapoteza mapato mengi kwa siku kwa sababu ya mifumo mibovu ukienda utaambiwa network ipo chini hatuwezi kupokea pesa, mwananchi anarudi na pesa yake. Mpango uje utueleze umejipanga vipi kwenda kuhakikisha wanaboresha hii mifumo ikiwezekana kuwe na utaratibu wa kukusanya off line mfumo ukirudi vizuri basi pesa iingie kwenye mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Huo ni mchango wangu kwa leo. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uhai siku ya leo tukakutana kwenye Bunge hili. Napenda kuunga mkono hoja ya Kamati kwa sababu nami ni Mjumbe wa Kamati hii ya Utawala na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu ni machache. La kwanza, hoja ya asilimia 10; ukiangalia karibia kila Mjumbe aliyesimama kuchangia ameiongelea. Ukiona watu wengi wanaongelea jambo moja, ujue aidha jambo hilo limefanyika vizuri ama jambo hilo limefanyika vibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya asilimia 10, pamoja na lengo lake jema, hatuwezi kuisema vibaya moja kwa moja. Ina lengo jema na kuna baadhi ya watu wamefaidika na wanaendelea kufaidika; hilo tunalifahamu. Tatizo linakuja kwenye uendeshaji wake, kuna konakona nyingi sana. Kuna matatizo mengi sana hizi fedha, unapozungumzia mapato ya ndani maana yake ni kodi za wananchi. Serikali inakusanya kodi, inapata mapato, inatenga asilimia 10. Tunachotarajia ni kwamba zile fedha ziende zikatumike kweli kuwakwamua wananchi kiuchumi kama lengo au makusudi tuliyoyakusudia sisi Wabunge au Wawakilishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo inakuja tofauti; tunapokuwa kwenye Kamati tukihoji, tupate vikundi vingapi vimekopeshwa? Wamekopeshwa fedha kiasi gani? Wamerudisha fedha kiasi gani? Je, huu mfuko kila siku tutakuwa tunatoa tu fedha asilimia 10 hazirudi zikaenda kuzunguka? Zile za mwanzo ziko wapi? Hatupati majibu ya kueleweka. Unaambiwa mara kumbukumbu hazipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha zinatolewa benki, yaani ili mwanakikundi apate fedha, lazima wasajili. Sasa fedha imepitia benki, inakuwaje leo mtu anakwambia hakuna kumbukumbu? Kwa sababu, kumbukumbu ingekuwa ni fedha tu ambayo mtu anatoa mfukoni, haina maandishi, haina nini, tungeelewa. Maana yake kuna tatizo. Kwa hiyo, naiomba Serikali, tunajua hili jambo ni zuri, lakini uzuri huu unakwenda kutiwa dosari na watendaji ambao sio waaminifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoongelea kwa mwaka, kwa mfano huu mwaka wa fedha 2021/2022 karibia shilingi bilioni 70, ambapo zingeingia kwa wananchi ipasavyo, tulitegemea tuone mabadiliko kwa wale wananchi wetu katika Halmashauri. Kuna Halmashauri, mfano zile za Jiji la Dar es Salaam, kawaangalie kwa mwaka mapato yao ya ndani asilimia 10 ni fedha kiasi gani? Hata hivyo, ukienda kuangalia ufanisi, haupo. Kwa sababu gani? Ni kama kijiwe, watu wamekaa kupiga fedha. Serikali inabidi iangalie suala hili kwa jicho la tatu. Fedha hizi ni nyingi, zingekwenda kubadilisha uchumi wa haya makundi ambayo tumeyakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, masoko yanaungua. Limeanza kuungua Soko la Kariakoo; tukakaa kidogo tukasikia Moshi soko limeungua; hatujatulia, Karume likaungua; hatujatulia Mbagala soko limeungua. Wakati soko la Kariakoo linaungua mpaka Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwenda, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kipindi kile alikuwa Waziri wa TAMISEMI, alikwenda. Tukaambiwa imeundwa Tume, watatupa majibu. Naomba niwaulize Wabunge wenzangu, hivi ninyi wenzangu mlisikia majibu ya uchunguzi uliofanyika Soko la Kariakoo? Mimi binafsi sijasikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kulisema hili ni nini? Unapofanyika uchunguzi, mimi nafikiri lengo; tujue kwa nini soko limeungua, ni sababu gani zimepelekea soko kuungua na kuna utaratibu gani wa kuzuia masoko mengine yasiungue? Kwa sababu, hizo fedha za asilimia 10 zinazochukuliwa mikopo nyingine zinaingia kwenye masoko humo; bidhaa/mali za watu zinaungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wanakwenda kuchukua fedha benki wanakwenda kufanya biashara, mtu hawezi kurudisha kwani mali zake zimeungua. Maana yake kule nyumbani sisi tunasema ni sawa na unasuka ukambaa jikoni; huku unasuka, huku unaungua. Mwisho wa siku ukiinuka pale ukindu wako umeisha, hauna chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kukisema hapa, haya masoko ndiyo wananchi wetu wanafanya biashara zao huko. Tuangalie namna ya kuyaweka katika hali ya usalama. Yanapoungua, wanaoathirika ni wengi. Hizo fedha za Halmashauri kwani leo mtu kama ulimpa asilimia 10, kama mtu leo alikopa benki halafu bidhaa zake zimeungua, analipa kutoka wapi wakati yeye alitegemea auze pale halafu akalipe? Wewe utamfanya nini? Kweli soko limeungua; kwani hata huyo wakimwongezea muda wa kulipa miaka mitano kama hana biashara, atalipa kutoka wapi? Kwa hiyo, suala hili la kuungua masoko liangaliwe kwa jicho la tatu; hii trend siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sitaki kuongea sana. Jambo langu lingine ni kuhusu Sekretarieti ya Ajira. Tungekuwa serious hii nchi sasa hivi ilibidi itangaze janga la wafanyakazi kwenye sekta ya afya na kwenye sekta ya elimu. Leo tunakaa hapa tunasema ufaulu kwenye hisabati asilimia 19, wakati kwenye sayansi huko nako hakueleweki, lakini Serikali inataka viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mtu anakwenda kuchanganya chemical kama hajasoma physics, hajasoma chemistry na kadhalika? Sasa Sekretarieti ya Ajira Mheshimiwa Jenista iko chini yako; tunafanya kazi na wewe vizuri tu, janga la walimu mashuleni, janga la watumishi wa afya; umejenga vituo, hakuna watoa huduma, yatageuka magofu. Kila kitu inabidi kiende kwa plan. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tunza Malapo ni janga ama ni upungufu wa hao watumishi?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa asilimia 19 ufaulu, utasemaje upungufu? To me, hilo ni janga tu, yaani hakuna namna ya kuisema. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, hiyo siyo tafsiri ya janga. Haya malizia.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwambia dada yangu Mheshimiwa Jenista, wakae wajipange. Tunataka tuone walimu na watumishi wa afya ili iendane na ile nguvu na jitihada za fedha za walipa kodi ambazo zimekwenda kujenga yale majengo ya vituo vya afya na madarasa, yatufae katika kuendeleza vizazi vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii ya uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ya TAMISEMI ndio ina jukumu kubwa sana katika ustawi wa maisha ya wananchi kwa kwa sababu ndio inagusa moja kwa moja kila kitu ambacho kinafanyika kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la fedha kutengwa na fedha kwenda na zikishakwenda kule kwenye halmashauri zetu, zile fedha zinatumika sawasawa? Hiyo ndiyo hoja ya msingi. Kodi ya wananchi ambayo inakwenda kule tunataraji iendee ikatekeleze miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi swali la kujiuliza je, zile fedha zikifika kule, zinafanya lile ambalo limekusudiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukisoma ripoti ya CAG hii aliyoiwasilisha juzi kwenye miradi ya maendeleo ukurasa wa 137 CAG anasema kumefanyika uwekezaji wa bilioni 533.68 ambao hauna tija. Uwekezaji huu umefanyika kwenye mambo gani? Uwekezaji huu umefanyika kwenye ujenzi wa masoko, kwenye ujenzi wa vituo vya mabasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakutolea mfano mdogo kule kwetu Mtwara, kuna soko limejengwa linaitwa Soko la Chuno, limejengwa kwa kodi ya Watanzania bilioni 5.5. Kwanza katika hali ya kawaida, unaweza kujiuliza huyo mtu ambaye alikuwa amependekeza lile soko lijengwe kule alikuwa anawaza kitu gani? Ni tofauti na uelekeo wa watu wanakoelekea, watu wanaokaa kule ni wachache, kwa sababu sisi Watanzania tumezoea, unatamani sokoni unatoka kwenye shughuli zako you just go there una-pick unaondoka. Sasa kama amekujengea tofauti na uelekeo wa watu wengi wanaokaa unategemea hilo soko wateja wake wanatokea wapi? Maana yake nini bilioni 5.5, zimelala pale, hazina tija. (Makofi)

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Tunza Malapo kuna taarifa kwa Mheshimiwa Kunti Majala.

T A A R I F A

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru napenda kumpa taarifa mzungumzaji, kwamba changamoto iliyoko Mtwara haina tofauti na changamoto ya Jiji la Dodoma. Soko limejengwa Nzuguni, lakini ukiangalia kata nyingi zilizoko zipo upande huu wa magharibi, kwa hiyo, uwekezaji unaofanywa na Serikali na wataalam wetu wanao- design miradi hii wamekuwa wakipoteza kodi kubwa za Watanzania pasipokuwa na tija. Nakushukuru ilikuwa atambue tu hilo Mheshimiwa mchangiaji anayeendelea.

SPIKA: Mheshimiwa Tunza Malapo, unapokea taarifa hiyo?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa mikono miwili. Serikali inachotakiwa kufanya ni kujitathmini kwa sababu hizi ni kodi za wananchi, tunataraji ziende zikawekeze kwenye miradi ambayo ina tija. Kabla Serikali haijapeleka fedha nyingi kiasi hicho, ifanye tathmini hapa tunapokwenda kuwekeza uwekezaji huu utaleta tija. Hilo ni suala la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili, tukienda kusoma ripoti ya CAG hii mpya siyo kwamba kila mwaka hakuna ubadhirifu, lakini hii nayo imesheheni kwa ubadhirifu. Kila ukienda kwenye halmashauri shida ni watu wanapiga fedha, maana yake ni nini? Wizara inatakiwa ijitathimini ina Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, waende wakafuatilie fedha zinazopelekwa. Nikupe mfano mwingine mdogo, nili-take time nikasoma, kule kwetu Mtwara kulikuwa na mradi wa kufunga taa za barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye mkataba, nakupa mfano mdogo, kwenye ripoti ya maendeleo ukurasa wa 54, ripoti ya CAG, malipo ya ziada ya taa za barabarani Mtwara hiyo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani; taa moja ilitakiwa ilipwe milioni 7.5, taa moja imeendwa kulipwa milioni 18,142,000, hata kama ni tofauti kwamba bei imeongezeka, bei imepanda kutoka milioni saba mpaka milioni 18.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo fedha zimepotea shilingi milioni 588, si zinajenga kituo cha afya kabisa hizi, kwa sababu kituo cha afya kilikuwa kinajengwa kwa shilingi milioni 450 mpaka 500, hizi mtu kalipwa tu kwa matakwa ya watu wachache. Ndio maana nimesema pamoja na hizo fedha kidogo ambazo zinakwenda, wao kama Wizara wana kazi kubwa sana ya kufuatilia kuhakikisha fedha zinazokwenda kule zinaleta tija kwa wananchi. Naambiwa Mawaziri vijana, maana yake vijana tunatambua mchakachaka, wanapaswa wakimbie. Kama walikuwa wanakimbia kwa speed mia moja, inatakiwa waende mia moja ishirini, mia moja hamsini. Hali huko, chini sio shwari sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee issue ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu; kwa mwaka huu wa fedha hii bajeti tunayokwenda kuipitisha, sina uhakika kama itapita, hii bajeti ambayo tunaijadili sasa hivi kwa makusanyo ya ndani asilimia 10 ikitengwa kwenye halmashauri ni bilioni 75.98 zinatakiwa ziende kule kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, hoja ni kwamba, Wizara inatakiwa ifanye tathmini, je, hizi fedha nyingi zinazokwenda kule, kweli zinabadilisha maisha ya wananchi hawa? Tusiseme tu zinatengwa, zinaenda na zingine, hazirudi, zinakwamia wapi? Wakati tuko kwenye Kamati kwa sababu ni mjumbe wa Kamati hiyo wakati tupo kwenye Kamati tumemweleza mengi, waende wakafanye utaratibu wa kuhakikisha fedha hizi zinakwenda kuleta tija, zile ambazo hazieleweki, ziliko zirudi kwa sababu zote walipewa watu hazikupotea angani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nina suala moja, vitu huko mtaani vimepanda bei. Naomba Serikali ifanye tathmini, sasa hivi ndio wa wale wachumi wetu, wale maprofesa wa uchumi waliopo Tanzania watuambie hivi mafuta, kwa mfano, mafuta ya petrol yameongezeka labda kwa shilingi 500 mpaka 800 ndio inahalalisha mafuta ya kula leo ndoo ya lita kumi iliyokuwa inauzwa 28,000 iuzwe 70,000? Hivi vitu haviendani mafuta ya gari yamepanda sawa, lakini kwa hicho kiwango ambacho yamepanda yanahalalisha leo, kitu kilichokuwa kinauzwa 10,000 kiuzwe 30,000? Ndio hoja yangu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nafikiri watuambie tu kuna remedy gani ambazo zinaweza zikafanyika. Mimi Mtanzania wa kawaida ungeniuliza nikiona maisha yangu magumu, naacha kujenga, naangalia watoto wangu wale na watibiwe. Kwa hiyo watu wa uchumi washauri nchi, sasa hivi mtu akipata 10,000 anajiuliza 10,000 hii nitafanya nini ili aweze kula na watoto kwa namna vitu vilivyopanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, muda ni mchache na mambo ni mengi. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, mimi ni mwalimu na nimefundisha darasani kwa muda wa miaka isiyopungua tisa, kwa hiyo haya ninayotaka kuyaongea leo kwa uchache nayaongea kwa uzoefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namba moja, hakuna mtoto ambaye hafundishiki akifundishwa. Kinachotokea kwa hawa watoto wetu hawa tunaona wanafeli masomo, wanafeli kwa sababu hawafundishwi. Kwa nini hawafundishwi? Kwa sababu hakuna waalimu wa kuwafundisha. Nina maana ipi, ametoa data nzuri sana Mheshimiwa Husna mimi siwezi kuzirudia kwa sababu ya muda. Mtoto anaanza form one, mwalimu wa hesabu hayupo, mwalimu wa physics hayupo, mwalimu wa chemistry hayupo, mwalimu wa biology hayupo. Akifika form two tunamtaka mtoto huyo afanye, mtihani wa form two ambao unahusisha hayo masomo yote unajumlisha hayo masomo yote ambayo hajafundishwa tunamtaka afanye mtihani na afaulu. Hakuna kitu kama hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa watoto tunaowaona wa shule zingine wanafaulu vizuri hakuna muujiza wowote, ni kwa sababu wanafundishwa. Hiyo ndiyo hoja yangu ya msingi leo. Sasa sisi kama Taifa tujiulize, kwamba kipaumbele chetu ni nini? Kama elimu hatuitilii mkazo kwa namna hiyo, kila siku matamko mbalimbali ambayo hayatekelezeki tunafikiri yatatufikisha mahali? Kwangu mimi kama mwalimu nasema hayo matamko yanayotolewa na viongozi wa kisiasa kila siku bila utekelezaji hayatufikishi mahali kokote. Kwa taarifa, naongea kwa uzoefu, issue ya kufundisha haianzii darasani pale pale kwenda kusimama kushika chaki kufundisha. Issue ya kufundisha inaanzia mbali.

Mheshimiwa Spika, kuna kitu kinaitwa scheme of work, kuna lesson plan. Mimi natakiwa nisome ile content, nisome ile mada ninayokwenda kufundisha nielewe, niingie darasani ndipo nifundishe. Sasa unapewa darasa ukafundishe lina wanafunzi 1,000. Hivi ninyi mnawajua watu 1,000? Wakikaa hapa yaani ukaambiwa watu 1,000 sisi humu ndani tuko 400 kasoro humu watu wote sisi. Sasa ndiyo umepewa darasa la watu 1,000 ukafundishe wewe mmoja na nimewaambia kufundisha hakuishii pale darasani kusimama kama kweli unataka wanafunzi wafaulu. Una watu hawa 1,000 ufundishe, ukimaliza kufundisha haki bin haki inapaswa uwasimamie je, wameelewa? Wameelewa, umewapa zoezi wamefanya. Ili ujue wameelewa ni lazima nisahihishe. Lazima nisahihishe na hakuna somo linalotaka kusahihisha kama somo la hesabu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kama hausahihishi unajuaje kama watoto wako wameelewa? Nitasahihishajke mimi wanafunzi 1,000 mimi siwezi wala wewe Mheshimiwa Spika huwezi wala mwingine hawezi? Huo ndiyo uhalisia. Watoto 1,000 leo niingie nisahihishe madaftari 1,000 kesho niingie nisahihishe madaftari 1,000. Mimi Tunza Issa Malapo siwezi wala mtu mwingine hawezi. Kwa hiyo tusikae tukatafuta mchawi, kaangalieni matokeo ya form four, kuna shule ipo inaitwa Taifa, wanafunzi 1,032. Form four, yaani darasa moja, management inakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nachotaka kushauri, tunakaa hapa tunasema madarasa mengi yamejengwa, ndiyo yamejengwa lakini hayatoshi kwa sababu kila siku population inaongezeka. Population ya mwaka jana si ya mwaka huu. Kwa hiyo jitihada za makusudi bado zinahitajika kuwekeza katika elimu kuanzia kwenye miundombinu, waalimu na hawa waalimu hawa; unajua katika maisha hamna kitu kibaya kama kufanya kazi wakati una stress, asikudanganye mtu. Yaani wewe unatamani wanafunzi wako waelewe, ukiingia darasani unakutana na wanafunzi 1,000 unafundisha unajiona kabisa mimi hapa sijaeleweka, inaumiza sana kama mwalimu mwenye wito kama nilivyo mimi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, suala lingine nalotaka kusema kuhusu mgogoro wa ardhi wa hapa Dodoma. Mgogoro huu ni mkubwa sana, wananchi wanalalamika, wamedhulumiwa. Sisi kama Bunge, kama Kamati tumetoa ushauri. Ukisoma kwenye maoni yetu tumeeleza. Tunaomba Serikali ifanyie kazi kwa usimamizi wetu sisi Bunge kwa sababu Bunge kazi yetu ni kuisimamia na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii ya uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Sina shida na hotuba, imeandikwa vizuri tu, kama kuandika, Mheshimiwa Waziri umeandika. Tatizo linakuja kwenye utekelezaji wa yale ambayo anayaandika. Yaani kama kwenye kuandika, kupangilia hoja, aah uko vizuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia dhima ya Sekta ya Uvuvi inasema, “kuhamasisha, kuwezesha na kusimamia uvuvi endelevu, ukuzwaji viumbe kwenye maji, uzalishaji bora wa viumbe wakuzwao kwenye maji pamoja na mazao yake.” Tatizo linaanza hapo. Kule Mtwara na sehemu nyingine za nchi yetu wananchi wamehamasika kufuga viumbe wa majini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kule kwetu Mtwara, watu wako tayari kulima mwani, na kufuga majongoo bahari. Kasheshe inayowakumba, ndiyo hayo ninayokwambia kwamba kuandika siyo hoja, hoja ni kutekeleza. Watu wamehamasishwa, Mheshimiwa Silinde tuliongea, ulienda kuzindua. Hivi tangu umeenda kuzindua, umewauliza hata wanaendeleaje? Tangu umeenda kuzindua mpaka leo, hivi vifaranga vya majongoo havijapatikana na hawajui hatima yao. Ukumbuke wale watu wamewekeza fedha zao. Huko huko tunapohamasisha kwamba watu wakuze viumbe vya majini, walime mwani na kadhalika, lakini wameweka vile vizimba vizuri, wanawalipa walinzi, wanafanya uangalizi mbalimbali; majongoo, vifaranga vitoke Bagamoyo, vikifika Mtwara vimekufa, lakini mnawaambia wafanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasubiri watakuja; watakuja lini? Kwa hiyo, unapokuja kuhitimisha Mheshimiwa Waziri wafugaji wale wa majongoo Mtwara wanataka wapate jibu la uhakika, suala lile linafikia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kuhusu mwani, pia wamehamasika sana, tatizo linakuja kwenye masoko ya uhakika. Suala siyo kuuza kwa sababu hata ukiuza shilingi 200 si umeuza? Tunataka wauze kwa bei yenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko kwenye mazao ya bahari kuna fedha nyingi ambazo Serikali inazipoteza. Kuna fursa nyingi ambazo Serikali ingewekeza ingeweza kupunguza baadhi ya matatizo ya ukosefu wa ajira kwa sababu watu wamehamasika na watu wanatamani wafanye, wanachoshindwa ni uwezeshaji na uwezeshaji huu ndiyo huo ninaosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Hotuba ya Mheshimiwa Ulega, utaona sisi tunaenda kuwa matajiri lakini mwaka jana hapa niliongea vizuri sana nikasema issue siyo kutenga, issue kutekeleza. Sasa nataka nikupe mifano michache kama kawaida, nasoma yule ambaye hakupitia aone hali halisi ya Sekta ya Uvuvi. Sisi tunatoka kwenye bahari tunajua umuhimu wa Sekta ya Uvuvi! Kwa nini Serikali hii haioni umuhimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti ya Maendeleo, hiyo bajeti hiyo tulitegemea iende ikajenge Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko. Hiyo bajeti tulitegemea hiyo ya maendeleo tulitegemea itoe mafunzo itafute masoko, ijenge majengo ya utawala kwa ajili ya Sekta ya Uvuvi kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kushangaza humu ndani kila siku tunaimba, uchumi wa buluu na uchumi wa buluu ni mtambuka kwa sababu unahusu vitu vingi. Kuna utalii ndani yake, kuna ufugaji wa samaki na uvuvi wake na mazao yote yanayoendana humo. Kuna mambo mengi. Bajeti ya maendeleo, Mradi wa Uchumi wa Buluu. Kwanza fedha zenyewe zinazotegemewa za nje. Walitenga shilingi ngapi? Shilingi bilioni 13, mpaka hapa ninapoongea hakuna hata shilingi kumi iliyotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukikaa humu tunaimba uchumi wa buluu na kwenye hotuba yake Mheshimiwa Ulega ameandika uchumi wa buluu sehemu nyingi lakini hakuna fedha hata shilingi kumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi, ilitengewa shilingi ngapi? Shilingi bilioni 50, hapa leo tunapoongea kuna shilingi ngapi ambayo imetoka? Hizo fedha za ndani. Shilingi bilioni 50 imetoka shilingi milioni 426 sawa na 0.9% hata asilimia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi nikawa naongea na wenzangu, kwa hiyo, ukijumlisha hizi fedha zote za maendeleo hizi shilingi bilioni 135 kwenye Fungu 64 Uvuvi mpaka sasa hivi fedha iliyotoka nimekwambia shilingi bilioni 135 fedha za maendeleo, mpaka sasa hivi fedha iliyotoka ni shilingi bilioni 6.47 sawa na 4.8%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa asubuhi nilikuwa nawauliza watu kama mambo ndiyo haya, kuna haja ya kukaa hapa kujadili bajeti ambayo haitekelezeki? Tungesema tu kwamba ikifika kwenye mifugo na uvuvi akamalizie kwanza hiyo ya mwaka jana. Akishamaliza ndiyo arudi hapa. Tunakuja kujadili nini kitu ambacho hakitekelezeki? Ndiyo swali langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo kwenye huo ujenzi wa bandari ya uvuvi umetenga shilingi bilioni 50 umetoa shilingi milioni 426. Leo tena kaweka shilingi bilioni 50 zingine, hizi huku hata 1% haijafika. Tunaenda kuipitisha tunaenda kukubaliana ndiyo? Ndiyo hiyo inahusu nini wakati utekelezaji wake hafifu namna hii? Ndiyo swali langu mimi hilo la msingi. Ikibidi naelewa kwamba bajeti yetu sisi ni cash basis kwamba tukusanye ndiyo tutumie, naelewa wala sina shida juu ya hilo lakini najiuliza; Serikali haijaona umuhimu wa Sekta ya Uvuvi? Ndiyo swali langu ambalo najiuliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa nyingine nayokupa, Serikali ilisema itanunua maboti 158 igawe kwa wavuvi. Kule kwetu Mtwara Mheshimiwa Ulega Manispaa ya Mtwara watu mpaka sasa hivi wako kwenye michakato tu. Kuna boti limeenda kule? Halipo, wako kwenye michakato tunapitisha bajeti nyingine ile ya mwanzo haijatekelezwa. Kwa nini Mheshimiwa tunafanyiwa hivi hasa kwenye Sekta hii? Sisi wengine hatuna madini, hatuna nini tunategemea uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu hapa, ombi langu, yale maboti ile michakato ifike mwisho. Vile vikundi wale watu binafsi wapatiwe ili waweze kufanya kazi zao za uvuvi, hiyo ndiyo hoja yangu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kila nikitamani kuongea, kila nikitamani kuongea najikuta ninahuzunika kwa sababu kuna wataalam wengi sana kwenye Sekta ya Uvuvi ambao wangekuwa wanawezeshwa imani yangu tungekuwa tunasonga mbele sana. Wakati anatoa hotuba yake Mheshimiwa hapo kawataja wengine walimu wake, wengine nini lakini wamekaa tu hawatekelezi kwa sababu hawana fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda TAFIRI hakuna fedha, FETA hakuna fedha, ukienda TAFICO hakuna fedha lakini wale watu wanalipwa mishahara, wale watu wana other charges fedha ambazo wanazitumia kwa matumizi mengine lakini hawafanyi kazi zao kwa sababu hakuna fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Serikali pamoja na kwamba keki ya Taifa inaenda kwenye mambo mengi, wangejitahidi angalau hata isipungue 20%, 30%, 40% lakini unapotoa bajeti 4.8% unategemea wafanye nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, nakushukuru sana. Mheshimiwa Ulega wakati unaandika naomba pia uende kwenye mamlaka wakupe fedha utekeleze, kuandika bila vitendo sawa na hakuna kitu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii jioni ya leo kuchangia katika Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, MSD wanaomba wapatiwe mtaji wa bilioni 593, bilioni 592.9, hiyo ndiyo tunasema bilioni 593. Mimi sina shida, hata mimi naunga mkono wapatiwe ili waweze kutekeleza majukumu yao, maana yake watakuwa wamejipima, wame-discuss wakaona wakipatiwa hii fedha wataweza kutekeleza majukumu yao vizuri. Shida yangu kubwa, wakati ule wa taarifa za Kamati tuliona ripoti ya CAG inaeleza dawa nyingi zinafika vituoni zikikaribia kuisha muda wake (ku-expire).

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati MSD wanaomba kuongezewa fedha na Bunge hili na Kamati imeongea maana yake tunaunga mkono, hata mimi naunga mkono, lakini na wao MSD wanapaswa wajitathmini, wanapaswa wafanye kazi yao kwa weledi. Wanapaswa wawe waaminifu, wapeleke dawa huko zinakohitajika katika Mikoa yetu na Halmashauri zetu wakati zina muda mrefu kabla ya kufikia muda wa ukomo wa matumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanaumwa katika hospitali, wanaumwa majumbani wanashindwa kwenda hospitali lakini unaambiwa dawa zinateketezwa. Kwa hali ya kawaida hilo jambo halifurahishi. Kwa hiyo, wakati Bunge linataka kusema MSD ipewe fedha na watumishi wa MSD nao wajione wana jukumu na wana dhamana waliyoibeba kwa nchi yetu hii ya Tanzania, hilo jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kule kwetu Mtwara tunasumbuliwa sana na ugonjwa wa Malaria, hilo linajulikana. Miongoni mwa Mikoa ambayo ni hatarishi kwa ugonjwa wa Malaria, kuna mmbu wengi sana ni pamoja na Mikoa ya Mtwara na Lindi. Sasa naomba niiulize Serikali, kama Zanzibar imeweza kudhibiti mmbu na kudhibiti Malaria, huku Tanzania Bara ni kitu gani kinashindikana? Katika hali ya kawaida tunasema kinga ni bora kuliko tiba, sasa hivi tungekuwa tujadili zaidi kukinga kuliko tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunacho kiwanda pale kila siku nikichangia Wizara hii ya Afya naongelea kile kiwanda chetu cha Kibaha. Kila siku ukikisikia kina-underperform, kwa nini kina-underperform wakati matatizo bado ni makubwa? Sisi watu wa Mtwara giza likianza kuingia mmbu wanang’ata utasema wana meno. Sasa Serikali ione namna. Hapo Zanzibar ukienda kuna unafuu wa hali ya juu na Mheshimiwa Waziri unajua, kwa nini huku Tanzania Bara na hii yote ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Zanzibar wamefanya miujiza gani iwezekane na huku Tanzania bara kinashindikana kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naiomba na kuiomba Serikali iangalie jambo hili, maisha ya watu yanateketea sana kwa ugonjwa huu wa Malaria. fedha za Serikali, za walipakodi, zinatumika sana kwa sababu ya ugonjwa huu wa Malaria. Tujitahidi sana kuweka kinga kuliko kusubiri tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine la mfumo. Bado hii mifumo katika hospitali zetu inasumbua. Unajua ukimwona mtu ametoka nyumbani amefika hospitali anaumwa na Mtanzania ukimwona amekwenda hospitali walio wengi maana yake ameshindwa, yaani anaumwa. Anachotamani yeye akifika hospitali atibiwe arudi nyumbaji. Unafika hospitali unaambiwa cheti hawawezi kukata kwa sababu mfumo haufanyi kazi, sijui network iko chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafikiri hili katika Hospitali yetu ya Mkoa Ligula pale Mtwara linatokea, ingawa ndiyo hivyo mkiwasiliana na wahusika wanasema tunaandika pembeni tutakuja kuingiza na vitu kama hivyo. Kwa hiyo mimi nafikiri kuandaliwe utaratibu, mgojwa akifika atibiwe hayo mengine ya mfumo mnayajua ninyi. Mimi nikiumwa nahitaji nitibiwe, sihitaji kuambiwa habari za mfumo kutokufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali yetu ya Kanda ya Kusini, wananchi wa Kanda ya Kusini, ukiwemo Mkoa wa Mtwara, tunashukuru hospitali ipo, imefunguliwa. Lakini hospitali ile bado inahitaji iendelee kutengewa fedha na fedha zitolewe. Kuna ujenzi ule wa awamu ya pili, bilioni mbili bado hazijapelekwa, tunaomba zipelekwe. Pia hakuna ambulance, Hospitali ya Kanda ya Kusini haina ambulance, hakuna gari la Mkurugenzi, naye yupo tu, yaani ndiyo ile tunasema anaazima azima.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia karibia asilimia 80 ya watumishi wanaohitajika katika Hospitali ile ya Kanda ya Kusini hawapo. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ione umuhimu, sisi tunafurahi na tunapenda wananchi wa Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara tukitaka kwenda Dar basi tuende kwa mambo mengine siyo kwenda kutibiwa, tukitaka kwenda kutibiwa tuende tukatibiwe katika Hospitali yetu ya Kanda ya Kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ambayo sasa hivi ipo bado kuna changamoto ambapo tunaomba Mheshimiwa Waziri, tunaiomba Serikali iangalie kwa jicho la upekee hospitali ile ya Kanda ya Kusini ili sisi tusilazimike. Unapokwenda Dar es Salaam wakati unaumwa bado unafikiria huduma zingine za malazi na chakula ambazo ni ghali ukiwa nje ya mji wako. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ichukulie jambo hilo kwa uzito wake na kwa umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la mwisho jioni ya leo nataka niiombe Serikali ukikaa ukisoma kwenye mitandao mingi, unakuta watu wanapostiwa wanaumwa magonjwa makubwa makubwa yakiwa katika stages za mwisho sana. Mtu utaona anaumwa cancer, anaumwa ugonjwa gani, unajiuliza huyu mtu imekuaje alikaa nyumbani mpaka amefikia stage hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali – sielewi labda ni elimu kwamba Watanzania hatuna ule uelewa zaidi wa kwenda hospitali, sielewi. Naiomba Serikali itilie mkazo, kwa sababu kila sehemu kuna watumishi wa Serikali, waone wanawashauri vipi wananchi. Mwananchi yeyote anapopata tatizo la kiafya sehemu ya kwanza iwe hospitali, tusikae tukasubiri hali imekuwa mbaya ndiyo unakwenda hospitali, hata kutibiwa inakuwa ni vigumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nashukuru sana, MSD wawe makini wananchi wanaumwa na wanahitaji dawa, hatutaki kuona dawa zinachomwa kwamba zime-expire. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naanza kuchangia, binafsi naona Serikali imefanya kazi kubwa kwenye kuhuisha sera hii, ile ya mwaka 2014 kuileta hili toleo jipya la mwaka 2023, labda kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati, lakini naona wamezingatia kwa kiasi kikubwa maoni na matamanio ya Watanzania kwenye elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa hilo niipongeze Serikali, lakini bado ushauri wangu unabakia pale pale tusiishie kwenye kuandika. Kwa kweli ukisoma, ukatulia na ukafuatilia kama kweli yatakwenda kwenye utekelezaji, kama kweli uwekezaji utakuwa namna ile ambayo tunaambiwa, mimi naamini tutakwenda kwenye step nyingine.

Kwa hiyo, nitofautiane kidogo na mwenzangu aliyetangulia kwa sababu pale kuna financial management, kuna mambo ya music, watu wanaopenda music, kuna mambo chungu mzima ambayo tulikuwa tunasema kwamba watu wasifanye kwa mazoea. Sasa hivi yamewekwa kwenye sera na kwenye mitaala, na mimi kwa sababu ni Mjumbe wa Kamati ya Elimu tumepata nafasi mbalimbali za kupitia kushauri na kuelezwa na kuelekezwa ni kitu gani kinakwenda kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo suala la msingi Serikali kweli ikafanyie kazi yale ambayo wameyaweka kwenye maandishi ili kile tulichokikusudia kama nchi tukifikie. Sasa sambamba na hilo, ukisoma ile sera inakwenda zaidi kwenye mambo ya ujuzi, hapo tutapata vyuo vya kati. Lakini sasa wasiwasi wetu ama wasiwasi wangu unakuja hapo kwenye vyuo vya kati ndio inaonekana kuna ugumu wa wanafunzi kusoma kwa sababu ya kukosa mikopo. Serikali sasa itueleze imejipanga vipi ili kuhakikisha wale ambao hawatakwenda kwenye mkondo wa jumla wanakwenda huku kwenye hivi vyuo vya kati kwa ajili ya mafunzo ya amali, wamejipanga vipi kuwawezesha kufikia ndoto zao? Ndio hiyo ninayosema ya utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vyuo vya VETA vinajengwa nchi nzima. Nayo Serikali itueleze imejipanga vipi kuhakikisha wakufunzi wanakuwepo? Sio wakufunzi kwa maana tu wamekaa pale, mkufunzi mwenye sifa stahiki ya kufundisha kile ambacho tumekikusudia mtoto wetu akipate. Serikali ije ieleze kwa undani. Hayo ndiyo mambo ambayo tunataka tuyaone yasiishie kwenye maandishi yaende kwenye utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nifahamu, lile suala la kufanya Chuo cha Ualimu Mtwara kawaida kuwa tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam limefikia wapi? Kwa sababu miaka inapita tunaambiwa, natamani Mheshimiwa Waziri atapokuja kuhitimisha atuambie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotamani kufahamu; kwenye uandaaji wa mfumo wa usajili wa shule kwa njia ya kielektroniki nao umefikia wapi utekelezaji wake? Pia na hilo natamani nipate kuelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka nisisitize, mimi kama mwalimu ukiniambia elimu ya awali Mheshimiwa Waziri unasitasita kusema ya lazima au watu wasome tu kwa kujisikia. Mimi natamani nisikie ya lazima, kwa sababu pale kwenye elimu ya awali watoto wale wadogo ndiyo tunategemea pale wafundishwe namna ya ushirikiano. Unajua tatizo linalokuja tunaona elimu zetu za awali labda kwa sababu zinafundishwa na walimu ambao wengi wao hawajapitia mafunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tunaona wanafundisha mambo makubwa tofauti na umri wa watoto. Kwenye elimu ya awali watoto wacheze wakati wanajifunza, watoto wafundishwe namna ya kushirikiana kwa sababu nyumbani mwingine anatoka peke yake hajui kushirikiana na mwenzie, lakini pia wafundishwe zile language skills mbalimbali, ndivyo tunavyotegemea viwepo kwenye elimu ya awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri ukisitasita ilhali tunajua kabisa hapo nyuma kulikuwa na movement kwamba kila shule ya msingi kuwe na darasa la awali? Sasa leo kimeingia kizungumkuti gani cha kusema kwamba hii elimu iwe ya lazima? Hapo ndipo ambapo mimi hapo bado nina question mark ambayo natamani ukija kuhitimisha utueleze. Ulieleza pale Pius Msekwa, binafsi mimi sikukuelewa, yaani mpaka leo sijakuelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niseme, mchangiaji aliyepita yeye ameongea kwamba shule za private zinaajiri walimu, zina wanafunzi na mimi ninakubaliana naye. Mimi nakupeni data; leo hivi tunavyoongea kuna walimu 25,926 wako katika shule za msingi za private; tuna walimu 21,343 wako katika shule za private za sekondari ambapo hizi shule zisingekuwepo hawa walimu wote wangekuwa wako mtaani wanasotea ajira za Serikali. Lakini leo tunapoongea kuna wanafunzi wa shule za msingi 591,005; pia kuna wanafunzi wa shule za sekondari 291,882 wako private school. Sasa tujiulize, maana hizi shule leo zisingekuwepo hawa wote wangekuwa wamerundikana wapi kwenye shule zetu za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa ninachotaka kukisema, mimi sina shule wala sina interest ya kuanzisha shule, ninachotaka kusema jukumu la kuendeleza au la kutoa elimu kwa wananchi wake ni la Serikali, hii inajulikana kwa asilimia 100. Sasa hawa wawekezaji wanapojitokeza Mheshimiwa Waziri mkae chini, mtatue changamoto kwa amani kwa sababu hawa watoto wanaosoma kule ni watoto wa Kitanzania. Wakielimika wameelimika kwa ajili ya Taifa la Tanzania. Kwa hiyo, yale makandokando mnayoyaona yanaweza upande mmoja yanaleta shida na upande mwingine yanaleta shida, mjitahidi kuyatatua ili tusonge kwa sabaabu hawa ni Watanzania, yaani mtoto akisoma private habadiliki kuwa si Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kuhusu uhaba wa walimu. Mheshimiwa Waziri kwenye Kamati yetu alituletea; unajua hapa zinasomwa data nyingi, inategemea mtu ameitoa wapi data yake. Mimi data ninayoongea ni data tuliyoletewa na Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwenye Kamati yetu ya Elimu alisema hivi, uhaba wa walimu. Elimu ya awali, mahitaji ni 61,487; waliopo ni 8,619; uhaba ni 52,868. Elimu ya msingi, mahitaji ni 300,702; waliopo ni 167,245 na upungufu 133,457. Elimu ya sekondari, mahitaji ni 174,632 waliopo ni 84,700, upungufu ni 89,932. Kwa hiyo, mimi ninaachana na hiyo habari ya awali nikachukua tu msingi na sekondari, si kwa maana awali haina mantiki, ina mantiki sana, nimetoka kusema hapa. Upungufu uko 223,389 ukitoa hiyo ajira mpya ambayo imekuja walimu 13,130 upungufu bado unabakia 210,259. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua wahisani wanaweza kutusaidia kujenga miundombinu lakini hawawezi kutusaidia kuajiri walimu. Kama nchi na kama Serikali, hivi vitu inabidi viende sambamba. Kwa maana ipi? Wakati tunasema elimu bila ada tukumbuke wanafunzi wengi watoto wengi watandikishwa. Tena sasa hivi sera ile inatupeleka mpaka form four. Tuone ni kwa namna gani Serikali inajipanga kuajiri walimu wa kutosha, kujenga miundombinu ya kutosha, vitabu huko shuleni ni majanga. Fedha ya ruzuku mpaka leo mtoto wa shule ya msingi anatolewa shilingi 10,000 kwa mwaka, tena 10,000 hiyo 4,000 inabaki Wizarani huko wanasema ya kununua vitabu, na hapo hapo hiyo 6,000 anapoenda shule ukisoma ripoti ya CAG anasema mwaka 2021/2022 ilikuwa iende bilioni 33.7 lakini katika hiyo hela haikwenda yote, bilioni tano haikwenda, mnategemea walimu wetu wafanye kazi kwa namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Serikali iende kwenye utekelezaji wa sera na mitaala mipya ambayo inaanzishwa. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kuwa hai na kuwa na afya njema ya akili jioni ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Mtwara. Mtwara tuna Bahari ya Hindi yenye kina kirefu na samaki wengi sana tu, lakini tunashindwa kuwapata kwa sababu ya uwekezaji finyu katika sekta hii, hivyo kupelekea uvuvi kuonekana kama ni shughuli ndogo ndogo ya watu wanyonge ambao hawajiwezi. Ukisoma, utaona kuna nchi nyingi duniani zimenufaika, zinaingiza pato kubwa la Taifa kwenye nchi zao kutokana na sekta hii ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unajua hii Wizara ya Mifugo na Uvuvi ina watu wawili. Mheshimiwa Ulega yeye ni mtaalam wa uvuvi, tulitarajia kwamba tunavyokwenda kwenye mambo ya uvuvi, kwa sababu yupo mtaalam, aweze kulipeleka hili gurudumu mbele. Mheshimiwa Ndaki yeye ni mtaalam wa mambo au ana uzoefu na mambo ya mifugo, tulitarajia kule kwenye mifugo nako kufanye vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa sana la kusikitisha, miongoni mwa Wizara ambazo mimi naweza kusema kama Serikali haizitilii maanani ni Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Wakati mwingine tunatamani kuwalaumu hawa Mawaziri, lakini watafanya kazi wakati fedha hawana? Mimi ndiyo swali langu la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2021 wakati nachangia kwenye Wizara hii, nilisema nimepata mshtuko, watu wakacheka. Nilisema nimepata mshtuko kwa sababu fedha za maendeleo ambazo zimetengwa ni nyingi wakati hii Wizara hawawapi fedha, kwa nini wanawaacha wanatenga fedha nyingi na hawawapi? Kilichotokea ni nini? Wamewatenga fedha za maendeleo kwenye Sekta ya Uvuvi, (mimi leo nitajikita tu kwenye uvuvi) wametenga Shilingi bilioni 99.14; fedha za ndani shilingi bilioni 62.5 na fedha za nje shilingi bilioni 36.5.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka tunakuja leo kwenye Hotuba ya Waziri, fedha ya maendeleo ambayo imepelekwa Wizara hii ni Shilingi ngapi? Shilingi bilioni 3.95. Tunakaa hapa tunafanya nini? Huyo ndio unamtegemea sasa aende akafanye shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye sekta ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakupa mifano michache, si tuliwapitishia hizi! Kazi ya Bunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali, tukapitisha, tukasema tunawashauri, tunawasimamia; sijui tumefeli kuwasimamia, sielewi, lakini habari ndiyo hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nakupa mifano, katika bajeti ile walikuwa na malengo, pamoja na mambo mengine wanasema: “ukarabati na utanuzi wa kituo cha ukuzaji viumbe maji, Ruira Songea. Shilingi ngapi imetengwa? Shilingi milioni 791. Mpaka hapa tunapoongea, hata shilingi 10/= haijaenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati na utanuzi wa kituo cha ukuzaji viumbe maji Nyengedi, Lindi; kuna Tandahimba huko kwetu Mtwara na wapi; shilingi ngapi zimetengwa? Shilingi milioni 715; mpaka leo tunapoongea hata shilingi 10 haijaenda. Ujenzi wa kituo cha ukuzaji viumbe maji bahari cha Ruvula, kipo Mtwara kwetu huko; shilingi ngapi? Shilingi milioni 983; mpaka hapa tunapoongea, hata shilingi 10 haijaenda. Sasa nimekupa mifano michache. Kuna watu wa TAFIRI ndiyo tunategemea huko utafiti na vitu vingine vikafanyike. Walitengewa shilingi milioni 700; hata shilingi 10 haijaenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakaona wajifariji kidogo, wakapunguza tena bajeti ya maendeleo kwa mwaka huu ambao tunaoujadili; kujifariji tu kwa sababu umetoka shilingi bilioni 99, umepewa shilingi bilioni tatu. leo unapunguza, shilingi bilioni 92, unataka kuniambia huo muda uliobaki ninyi mtapata hizo fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, concern yangu kubwa, sisi tunaotoka maeneo ya wavuvi, tunajua ni namna gani Sekta ya Uvuvi ina umuhimu kwa watu wetu na kwa wananchi wetu. Yaani kama mnavyoona kwenye maeneo mengine, wao wana migodi huko ya madini wanachimba wanapata fedha, nasi tunaotoka kwenye maeneo ya uvuvi, tunajua umuhimu wake. Kutufanyia mambo kama haya, siyo sawa. Wapeni hela hawa Mawaziri wafanye kazi, tuje hapa tuwaulize hawafanyi kazi wakati fedha mmewapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha yupo hapa, mwaka 2021 alitusikia, na leo anatusikia, na nawaambia tukirudi mwakani Mwenyezi Mungu akitupa uhai, tunakuja kuyajadili mambo haya haya. Tunafanya mambo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa, kule Kilwa Masoko wametenga shilingi bilioni 50 mwaka 2021 kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya uvuvi, haikutoka hata shilingi 10; mwendelezo ule ule! Mwaka huu tena wametenga shilingi bilioni 59, Mheshimiwa Waziri akija hapa kumalizia hoja yake, naomba atueleze zile shilingi bilioni 50 za mara ya kwanza zinakwenda lini? Vile vile hizi zitakwenda? Tunachotaka sisi, bandari ile ikijengwa vizuri ndiyo ile dhana ya Uchumi wa Bluu inaanzia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jamani, hivi tangu nchi hii ipate uhuru, leo ni miaka sitini ngapi, bado tunazungumzia watu wanaenda kuvua na boti za kusukuma na makasia? Wapeni fedha TAFIRI wafanye utafiti, wawaambie watu samaki wako wapi? Waambie watu mazalia ya samaki yako wapi? Mnafanyaje, hamtoi fedha? Kuna Waziri, kuna Katibu Mkuu, wanafanya nini kama Serikali, kama Wizara ya Mheshimiwa Mwigulu haitoli fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na kusema hii Wizara haifanyi kazi, lakini anayekwamisha kwa kiasi kikubwa Wizara hii isifanye kazi ni Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba. Kwa hiyo, tukimtafuta mchawi, wa kwanza ni Wizara ya Fedha na Mipango. Yaani hawa watu wa Mifugo na Uvuvi, nitakuja kuwasema hapa baada ya kuona wamepewa fedha na wameshindwa kufanya kazi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, ni kengele yako ya pili.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, lakini ujumbe huo ufike na ufanyiwe kazi. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama kuchangia jioni hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Serikali kama kweli imedhamiria kukuza michezo nchini, ni lazima iwekeze kwenye michezo bila kuleta masihara. Yaani hatuna namna nyingine ya kuongea. Serikali itoe fedha, ipeleke kwenye Wizara yetu ya Michezo ili kusudi waweze kutekeleza majukumu ambayo wamejipangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wajumbe wa Kamati ambao tunaisimamia Wizara hii tunajua ni kwa namna gani Wizara ina-struggle kuhakikisha michezo inaimarika nchini. Kama alivyotoka kuongea mwenzangu, sasa hivi michezo hatuchukulii mazoea, watu wanatakiwa wacheze michezo kitaalamu. Ili ucheze michezo kitaalamu ni lazima kama nchi iwekeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumeenda kuangalia ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa, bado mambo hayafurahishi. Kuna uwanja ujenzi wa uwanja wa michezo Dodoma, Arusha na maeneo mengine lakini upelekaji wa feda katika wizara hii bado hauridhishi. Kwa hiyo, hatuna namna nyingine ya kuongea Serikali ichukulie kwa nama ya pekee kwa sababu pamoja na mambo mengine huko inawasaidia vijna wetu wengi ambao wana interest hizo kuweza konesha vipaji vyao na kusonga mbele katika michezo mbalimbali walio wengi wanafikia hapo walipofika kwa jitihada zao binafsi. Sasa tunataka tuone Serikali ina jitihada gani za makusudi za kuwezesha michezo katika nchi yetu inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tulitembelea Chuo Kikuu cha Dodoma, nimwambie Waziri anayehusika na mambo ya maji, watu wa Chuo Kikuu cha Dodoma hawana maji. Hapo UDOM karibu tu na hapa, wafanye jitihada ya kuhakikisha maji yanapatikanawafanye jitihada ya kuhakikisha maji yanapatikana. Tumeenda siku zile ripoti yao inasema wanapata maji 30% tu. Sasa chuo kikubwa kina wanafunzi wengi tunategemea kitoe wataalam wa mambo mbalimbali maji nayo yanakosekana, kweli? Kwa hiyo, wale ambao wanahusika na mabo ya maji wakiangalie kwa jicho la tatu Chuo Kikuu cha Ddoma wahakikishe wanapata maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya watu wazima, wenzangu wameizungumza kwa kasi kikubwa na pia nizungumzie kidogo kwenye eimu ya watu wazima. Hapa tunategemea wale watu ambao walikosa fursa kwa namna moja ama nyingine ya kusoma kwenye hizi shule katika mifumo hii ya kawaida waende wakasome kule lakini hali ya vile vituo vyetu vya elimu ya watu wazima ni dhoofu kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wana malengo mazuri na mipango mizuri lakini wanaitekelezaje katika hali ambayo wako nayo. Nikupe mfano, katika Mkoa wa Mtwara mwaka jana 2023 kuanzia mwezi Januari mapaka mwezi Oktoba wanafunzi wa kike 6,906 walipata mimba, kwa miezi 10 wanafunzi 6,906 katika Mkoa mmoja wa Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hao ndiyo tunawatarajia waende huko na kwenye sehemu nyingine hizi zinazotoa elimu nje ya mfumo rasmi lakini wakifika kule wanaambiwa walipie ada. Ada wanaitoa wapi? Huyu mtu ambae kakatisha masomo kwa sababu mbalimbali kwa kukosa ada na huduma nyingine leo unamwambia akiingia kule alipe anatoa wapi hiyo fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa zilizopo sisi Wabunge wawakilishi wa wananchi tujue sasa hivi dropout ziko kwa kiasi kikubwa kwa watoto wa kiume kuliko wakike. Kwa hiyo, wakati tunawapambania watoto wa kike tukumbuke pia kuwapambania watoto wa kiume. Huo ndiyo wito wangu. Nao wanakumbwa na madhila mengi makubwa lakini kila tukisimama tukiongea nikiwepo na mimi mwenyewe tunana kama watoto wa kike wanachangamoto nyingi, sikatai wanazo lakini tusiwaache nyuma Watoto wa kiume nao wanachangamoto nyingi na Mheshimiwa Waziri wa Eimu ametuambia atatuletea takwimu anafanyia utafiti waone ni kwa kiasi gani watoto wa kiume wanaacha shule na sababu ambazo zinazosababisha kuacha shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda naomba nimalizie jambo moja. Kila siku tumekuwa tukiongea upungufu wa walimu tunaongea general. Sasa tumeletewa takwimu naomba niwape taarifa kidogo kwa takwimu tulizoletewa yaani hapa nchini kwetu walimu wa Civics wanaotakiwa ni 16,695 lakini tunao walimu wa Civics 68. Walimu wa English wanaotakiwa 23,663 tunao 12,000 na walimu wa Physics tunatakiwa 13,000, tunao 6,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeyasema haya muone huku tunahamasisha uzalendo na utamaduni sijui vitu gani wakuwafundisha darasani watoto wetu wako 68. Huku tunazungumza ujasiramai na vitu gani walimu wa Bookkeeping wa commerce hawapo. Huku tunazungumza viwanda kuwekeza kufanyaje walimu wa physics, wa hesabu hawapo, tunaendaje namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kama nchi tunatakiwa tujitafakari na tujue hasa lengo letu ni nini. Tunaenda kwenye Mfumo wa Amali kwangu nasema kila siku naunga mkono hoja hiyo ya Mfumo wa Amali lakini ni lazima Serikali iwekeze vya kutosha ili kusudi tuwapate walimu wenye ujuzi wa kuweza kufikia malengo ambayo nchi itakuwa imejipangia. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi watu wa Mtwara katika ule mgao wa zile boti za kisasa zimetufikia boti tano; tunaishukuru sana Serikali kwa hilo. Namwomba Mheshimiwa Waziri atume wataalam wake wakaangalie mchakato wa zile boti, kwani inaonekana kama zinasumbua vitu fulani havijakaa sawa sawa. Naomba tu hilo lifanyiwe kazi ili lile lengo ambalo limekusudiwa na Serikali basi liweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namuomba Mheshimiwa Waziri pale katika Manispaa yetu ya Mtwara Mikindani, waangalie kwa jicho la karibu pale ferry ambapo samaki wanauzwa, kununulia, kukaangwa, kutayarishwa na kila kitu. Tunaomba miundombinu ya pale ferry katika Manispaa ya Mtwara Mikindani paboreshwe. Kwa sababu wanawake wengi wanafanya biashara zao lakini mazingira yaliyopo pale siyo rafiki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye issue ya nishati bado mpaka leo kuni zinatumika pale kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, kwenye storage facilities (sehemu ya baridi ya kuhifadhia samaki) bado uwezo wake siyo mkubwa. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri wafanye kila linalowezekana ili kusudi sehemu ile iweze kuboreka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna changamoto kubwa ya mbegu ya majongoo bahari. Mheshimiwa Waziri, mwaka jana nililisema na mwaka huu nalisema. Vijana, wanawake na watu wazima wamehamasika sana kufuga majongoo bahari kwa sababu soko lake ni la uhakika lakini upatikanaji wa mbegu bado unasuasua. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba walitilie mkazo suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, Mheshimiwa Waziri tunasema mchango mdogo wa Sekta ya Uvuvi katika pato la Taifa. Sababu zinajulikana, ukisoma kwenye hiyo hiyo hotuba amesema uvuvi unachangia pato la Taifa kwa kiasi kidogo. Akasemaje? Kwa sababu kuna uwekezaji mdogo katika uvuvi wa Bahari Kuu na usindikaji wa mazao ya uvuvi kuna athiri mchango wa Sekta ya Uvuvi katika pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwenye mipango yake mingi imeeleza kuboresha uvuvi wa Bahari Kuu kwa kununua meli za uvuvi. Mara ya kwanza walisema watanunua meli nane. Zikaja wakasema watanunua tano, leo nazungumzia nne. Sasa nataka kujua, meli zinanunuliwa au hazinunuliwi? Yaani wanatuachaachaje sisi watu ambao tuko kwenye ukanda wa Bahari Kuu? Watueleze tu, from nane kwenda tano na sasa hivi tunaongelea nne. Wananunua au hawanunui? Waziri akija kuhitimisha hapo atueleze. Pia, naomba kama anaenda kununua, basi ya kwanza kabisa ipelekwe Mtwara kwa sababu kuna ukanda mrefu sana wa Bahari ya Hindi ili kusudi uvuvi utekelezeke kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, boti za kisasa za doria. Sitaki kuamini na siamini, bahari yetu ina samaki wengi wakubwa. Tunachokosa sisi ni nyenzo za kuvulia hao samaki. Meli inunuliwe, maboya yanunuliwe lakini wanunue boti za doria za kisasa ili ziweze kufanya kazi ya kuchunga rasilimali ambayo ipo ili tuwezeshe Taifa letu kupata pato kubwa linalotokana na Sekta ya Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, samaki hawajawahi kwisha baharini hata siku moja isipokuwa sisi tunashindwa kuwafikia kutokana na zana duni ambazo tunazitumia kwenda kuvulia. Kwa hiyo, bado nasisitiza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepata mshtuko kidogo. Bajeti ya maendeleo kutoka shilingi bilioni 194 mpaka shilingi bilioni 363 wakati iliyopita imetolewa mpaka sasa hivi hata 50% haijafika. Ongezeko hili kubwa kama litakwenda kutolewa, naona mabadiliko makubwa kwenye sekta hii. Kwa hiyo, ombi langu na hoja yangu ni kwamba, fedha hizi zilizotengwa zisiishie kwenye makaratasi. Ziishie kweli kutolewa zikatekeleze miradi ya maendeleo ambayo imekusudiwa kwa manufaa ya nchi yetu na manufaa ya wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache nakushukuru sana na namtakia heri kaka yangu Mheshimiwa Ulega. Waende wakayatekeleze haya yaliyopangwa na Serikali itoe pesa ili waweze kutekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo nami niongee machache kuhusu hii Bodi ya Kitaalam ya Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ambayo napenda Waziri mhusika aje anipe ufafanuzi kuhusiana na hii Bodi. Concern yangu ni kwamba, sisi kama walimu tulikuwa tunatamani tupate chombo kimoja ambacho hakitakuwa na matatizo katika kushughulikia mambo yetu ili tufanye kazi kwa weledi na kwa utulivu na kwa amani katika kuleta elimu ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema naomba kupata maelezo machache, kwanza naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri, sisi kama nchi, je, tunatengeneza walimu ambao ni wataalam kulingana na mifumo yetu ya kuandaa walimu? Kama nchi ukasema kabisa mimi leo natoa wahitimu 200 waliopata labda stashahada ya elimu ni wataalamu? Hilo ni la kwanza, naomba nije nipate majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nimekuwa katika chuo cha ualimu, nimeona mambo mengi yaliyokuwa yanaendelea pale yalikuwa yanaturusisha nyuma kwa maana kila siku mitaala inabadilika, mazingira ya kufundishia hayako sawasawa na mambo kama hayo. Kwa hiyo, naomba nipate ufafanuzi, sisi kama nchi tunaleta chombo hiki ambacho tunataka walimu wajisajili kama wataalam, je, are we preparing professional teachers? Hilo swali langu la kwanza la msingi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nalotaka kuzungumza, kama walivyosema wenzangu wengi, ukiangalia huu Muswada umejikita zaidi kuzungumzia maadili ya mwalimu ambaye anaandaliwa katika mazingira ambayo siyo rafiki, anafanya kazi katika mazingira ambayo siyo rafiki, lakini mwisho wa siku tunataka tumpe mzigo mkubwa wa kumwangalia maadili yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano mmoja, jambo hili hata tulipokuwa kwenye Kamati ya LAAC lilijitokeza na tukalizungumza. Kwa mfano, mwalimu alishakopa benki, akabakiza 1/3 ya mshahara wake, walipokuja watu wa Bodi ya Mikopo wakaongeza ile asilimia wakawa wanakata asilimia 15 badala ya asilimia 8. Kilichotokea mtu anapokea mshahara Sh.100,000, unamtaka awe na maadili ya kuamka asubuhi, mfano, anakaa Banana, anafanya kazi mjini, aende mjini, kwa sababu ukizungumzia suala la maadili ni pana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutaki kuweka mazingira ambayo tukimhukumu, tumhukumu kweli kakosa. Kuna mazingira ambayo yanamfanya akose, siyo kwa makusudi lakini ni mazingira ambayo yametengenezwa. Kwa mfano, mtu huyo anapokea mshahara kwa mwezi Sh.100,000, wapo walimu hao baada ya Bodi kuongeza yale makato, nina uhakika na ninachokizungumza. Anakaa sehemu anakotakiwa atumie nauli, unamtegemea kila siku saa 1.00 atakuwepo ofisini? Maana umeshampa leseni kwamba huyu ni mwalimu, ana leseni hii ya kitaalam lakini mwisho wa siku hatimizi yale anayotakiwa ayatimize na kuna mtu anamkwamisha ili asiweze kuyatimiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo, huu Muswada umemzungumzia zaidi mwalimu lakini simwoni mwajiri. Nataka nipate ufafanuzi kwamba endapo mwajiri atakuwa hamtendei haki mwalimu huyu, kwa sababu Tume ni kama imeshindwa kazi kuwatetea walimu. Sasa in case mwajiri hamtendei haki mwalimu huyu, nafasi ya Bodi ni nini kwa mwalimu huyu? Naomba nipate ufafanuzi wa jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nachotaka kukizungumza kwa kifupi ni hizo ada za leseni ya kuingilia na ya mwaka, tuziangalie kwa kiwango chake. Hata kama mtu anasema tusiwaone walimu kwamba ni watu maskini, hawana uwezo, sisi hatuzungumzii vyanzo vingine, tunazungumzia chanzo chake alichokisomea mshahara wake, je, unakidhi haja ya haya mambo? Kama mtu ana chanzo kingine, hiyo ni out of our business, huko ni kujishughulisha kwake. Tunamchukulia mwalimu ambaye anaamka asubuhi, kama mnavyojua mwalimu ana kazi nyingi, aandae scheme of work, lesson plan, log book, kuna vitu chungu nzima. Wakati anaviandaa hivyo vitu, ana utulivu wa mind kwenda deliver? Unampimaje weledi wake? Ndiyo swali la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye hii taarifa ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa tano pale kwenye matokeo ya kuwa na Bodi ya kitaalam ya Walimu, kipengele cha 1 anasema, kuinua hadhi ya taaluma ya ualimu na walimu kwa kusajili walimu wote kulingana na viwango vyao. Kwangu nafikiri hadhi ya mwalimu haiwezi kuinuliwa na kusajiliwa. Hadhi ya mwalimu itainuliwa na kufundishwa atakayofundishwa, mambo atakayopewa na thamani yake yeye kama mwalimu. Kumsajili hakumaanishi kwamba utainua hadhi yake na wala weledi wake hauwezi kuinuliwa kwa kumsajili. Weledi wake utainuliwa kule chuoni anakopata mafunzo. Wakati huo huo weledi huu utainuliwa endapo wale wakufunzi wanaomfundisha wapo katika mind ambazo hazina stress. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.