MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali, majibu ambayo yanatia moyo na kuonyesha kwamba ni kweli kuna uratibu. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa sababu ahadi hizi huwa zinatekelezwa kwenye Wizara za Kisekta. Je, Serikali haioni umuhimu, huko kwenye Wizara za Kisekta kukawekwa mafungu maalumu, yaani kwenye bajeti ikaonekana kwamba fedha hizi zinakwenda kutekeleza ahadi fulani ili Wabunge waweze kufuatilia pale ambapo bajeti hiyo inaweza kutekelezwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kule kwangu barabara ya Nangurukuru – Liwale na Nachingwea – Liwale, ni miongoni mwa ahadi za Uchanguzi wa 2015/2020. Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya utekelezaji wa ahadi hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kumpongeza Mheshimiwa Kuchauka kwa kazi, lakini nimwambie kwenye hili la Wizara za Kisekta, ahadi za viongozi ni kipaumbele cha kila sekta wanapowasilisha bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wamekuwa wakiendelea kuziweka kila wanavyowasilisha bajeti zao. Sisi Ofisi ya Waziri Mkuu, tunafanya kazi ya kuratibu kuhakikisha kwamba ahadi hizi zimewekwa na kama nilivyosema kwenye dashboard tunaona kila ahadi imefikia hatua gani na asilimia ngapi kwenye utekelezaji, kwenye kila sekta.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Halmashauri ya Liwale kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI mwaka jana tu tumetoa fedha kwenye yale maafa yaliyotokea ya El Nino na Kimbunga Hidaya, shilingi bilioni 1.3 ili kuweza kuendelea kutengeneza barabara zile. Lakini pia, bajeti yako Mheshimiwa Mbunge Kuchauka imeongezeka kutoka shilingi milioni 839 hadi tunavyoongea leo ni shilingi bilioni 2.4. Nataka nikuhakikishie, ahadi zote za Viongozi wetu Wakuu tunaendelea kuzifanyia kazi. Sisi tunawaomba Watanzania waendelee kutuamini, waendelee kuiamini Serikali ya Awamu ya Sita, kwa sababu ahadi zote ni vipaumbele vya Serikali, ahsante. (Makofi)