Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Josephat Sinkamba Kandege (31 total)

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo yaliyopo Matai kwenda Kasesya ni ahadi ya muda mrefu ya Serikali na Ilani ya CCM tangu mwaka 2010:-
(a) Je, Serikali itaanza lini kukamilisha ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami?
(b) Je, ni lini ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Sumbawanga hadi Kasanga Port utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshmiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Matai hadi Kasesya yenye urefu wa Kilometa 50 ni sehemu ya Barabara Kuu inayounganisha nchi za Tanzania na Zambia katika mpaka wa Kasesya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali ya Tanzania imekwishaanza kutekeleza mpango wa kuijenga kwa lami. Kazi ya usanifu wa kina na maandalizi ya zabuni ilianza mwezi Julai, 2014 na kukamilika Januari, 2015. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 11.614 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya Matai – Kasesya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Sumbawanga – Matai hadi Kasanga Port yenye urefu wa Kilometa 112 imekamilika kwa takriban asilimia 53 ambapo kilometa 56 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 32.01 ili kukamilisha ujenzi wa barabara ya Sumbawanga – Matai hadi Kasanga Port ambapo ujenzi unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2017.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itafufua barabara ya Mkoa wa Mbeya kwenda Kasanga Port pamoja na kivuko cha Mto Kalambo ambayo pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoizungumzia Mheshimiwa Mbunge ni barabara iliyokuwa inatumika zamani enzi za Wajerumani inayoanzia Wilayani Momba katika Mkoa wa Songwe hadi Kasanga Port. Barabara hiyo ilikuwa inapita katika Vijiji vya Kapele – Kakosi - Ilonga, ambapo jumla ni kilometa 55, ambayo kwa sasa ni sehemu ya barabara ya wilaya inayohudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Momba. Aidha, katika Mkoa wa Rukwa barabara hiyo ilikuwa inapita katika Vijiji vya Mambwenkoswe – Kalepula - Mwimbi - Kasanga Port.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya maeneo katika barabara hiyo ya zamani, kati ya Mwimbi - Kasanga Port hayapitiki kabisa hasa wakati wa masika na katika maeneo mengine barabara inapitika kwa shida hususan katika eneo la Mto Kalambo kwa kuwa hakuna barabara rasmi. Serikali inawaasa wananchi wanaosafiri kutoka Momba na Mbeya kwenda Kasanga Port kutumia barabara ya lami ya Mbeya – Tunduma - Sumbawanga na kuunganisha katika barabara ya Sumbawanga - Matai - Kasanga Port inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumiaji barabara wanaweza pia kutumia barabara ya Wilaya ya Kapele – Kakosi - Ilonga Mkoani Mbeya, barabara ya Mkoa ya Mwambwenkoswe – Kalepula - Mwimbi - Matai na kuunganisha katika barabara kuu ya Sumbawanga – Matai - Kasanga Port Mkoani Rukwa.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Je, ni aina gani ya madini yanapatikana ndani ya Wilaya ya Kalambo kulingana na tafiti ambazo zimekwishafanywa na Serikali?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na tafiti za awali zilizofanywa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) pamoja na taarifa kutoka kwa wawekezaji wanaomiliki leseni katika maeneo ya Kalambo, madini yanayopatikana ni pamoja na madini ya chuma, dhahabu, galena kwa maana ya lead, shaba pamoja na madini ya ujenzi. Hata hivyo, GST wanaendelea kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wilaya ya Kalambo ili kubaini kama kuna madini mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nitumie nafasi hii kuwaomba wananchi wenye nia ya kupata taarifa kuhusu rasilimali za madini yaliyopo katika maeneo hayo, wafike katika ofisi zetu za madini pamoja na Wakala wake. Aidha, taarifa hizo zinapatikana kwenye tovuti ya Wizara, tovuti ya GST pamoja na machapisho mbalimbali ambayo yapo katika Ofisi zetu za madini.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Serikali ilielekeza nguvu zake katika kutangaza vivutio vya utalii na wawekezaji kuja Kanda ya Kusini ili kupunguza msongamano wa utalii Kaskazini mwa Tanzania:-
(a) Je, ni kwa kiasi gani Serikali imeyatangaza maporomoko ya Kalambo ambayo ni ya pili Afrika baada ya yale ya Victoria kuwa kivutio cha utalii?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Hifadhi ya Msitu wa Kalambo pamoja na maporomoko haya yanakuwa chini yake kupitia Shirika lake la TANAPA?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Msitu wa Kalambo pamoja na maporomoko yake ipo chini ya Wizara yangu na inasimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Na.14 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Bodi ya Utalii nchini imekuwa ikitangaza utalii katika maeneo ya Kusini na Magharibi mwa Tanzania ikiwemo maporomoko ya Kalambo kupitia Jarida Maalum la kutangaza maeneo ya utalii yenye changamoto ya kimiundombinu lijulikanalo kama Hard Venture Tourism, majarida mengine ya utalii, vipeperushi, tovuti mbalimbali ikiwemo the destination portal chini ya Bodi ya Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANAPA ni shirika la umma chini ya Wizara yangu lililoanzishwa chini ya Sheria ya Hifadhi za Taifa kwa madhumuni mahsusi ya kuendesha na kusimamia matumizi endelevu ya maeneo yote yaliyopitishwa kisheria na Bunge kuwa Hifadhi za Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Hifadhi ya Msitu wa Kalambo, maporomoko ya Kalambo yakiwa ni sehemu yake siyo Hifadhi ya Taifa, hivyo kusimamiwa chini ya Sheria ya Misitu. Kwa sasa Serikali itaendelea kusimamia msitu huu kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na siyo TANAPA.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Serikali ilipata mkopo kutoka Benki ya Dunia na kujenga miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo kasi Jijini Dar es Salaam. Baada ya ujenzi wa mradi huo kukamilika Serikali ilitoa msamaha wa baadhi ya kodi wakati wa uingizaji nchini mabasi yanayotumika kusafirisha abiria katika mradi huo. Serikali inamiliki asilimia 49 ya hisa za mradi huo na mwekezaji asilimia 51.
(a) Wakati wa kukokotoa hisa kati ya Serikali na mwekezaji, je, sehemu ya msamaha imejumlishwa katika ukokotoaji wa hisa?
(b) Je, ni nini faida na hasara za msamaha huo wa kodi upande wa Serikali?
(c) Wakati wa kulipa mkopo huo, je, ni nini wajibu wa mwekezaji katika mkopo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kimsingi mwekezaji hakupata msamaha wa kodi wakati wa kuingiza mabasi nchini bali alipewa punguzo la kodi hiyo (import duty) kutoka asilimia 25 inayotozwa hadi asilimia 10. Punguzo hilo lilitolewa kwa makubaliano na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(b) Mheshimiwa Spika, punguzo la kodi hiyo limesaidia kutoa unafuu wa nauli zinazotozwa kwa abiria wanaotumia mabasi ya UDART. Endapo punguzo hilo lisingekuwepo ni dhahiri kwamba gharama hizo zingejumuishwa katika viwango vya nauli kwa watumiaji.
(c) Mheshimiwa Spika, mwekezaji anawajibika kurejesha mkopo aliochukua kwa ajili ya kununulia mabasi pamoja na kulipa kodi Serikalini kwa mujibu wa sheria za nchi. Kwa upande wake, Serikali inawajibika kulipa mkopo Benki ya Dunia ambao ulitumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi
wa DART awamu ya kwanza kwa kuzingatia makubaliano (financing agreement).
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Ulumi kilichopo Kata ya Ulumi ambao ulianza kujengwa mwaka 2010 haujakamilika mpaka sasa.
(a) Je, ni sababu zipi zimefanya mradi huo kutokamilika mpaka sasa na ni lini utakamilika?
(b) Je, Serikali ilitenga kiasi gani cha fedha katika bajeti ya mwaka 2017/2018 ili kukamilisha mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Jimbo la Kalambo lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa ujenzi wa Mradi wa Umwagiliaji Ulumi ulianza kujengwa mwaka 2012 kwa kujenga banio lenye gharama ya shilingi milioni 213,279,000 kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Msaada wa Chakula baina ya Serikali ya Tanzania na Japan bila kuhusisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji mashambani ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.3 zinahitajika kukamilisha kazi zote. Aidha, Wizara yangu hivi sasa inafanya mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 kwa lengo la kuihuisha ili uendane na hali ya sasa. Kazi hii inatarajia kukamilika mwezi Septemba mwaka 2018 na kupitia mpango huu Mradi wa Ulumi ni miongoni mwa miradi iliyopewa kipaumbele kwa ajili ya uendelezaji wa kilimo cha umwagiliaji kwa manufaa ya wananchi wa Ulumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa mradi huu kwa wananchi wa Kalambo, Wizara yangu katika mwaka wa fedha 2018/2019 itaingiza mradi huu katika bajeti kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili mradi huu uweze kuanza utekelezaji.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Jimbo la Kalambo lina kata 23 na vijiji 111; katika awamu ya kwanza na ya pili ya mradi wa REA ni vijiji vichache tu vilipata umeme.
Je, katika utekelezaji wa REA III ni vijiji vingapi vinategemea kupata umeme ili wananchi wa maeneo hayo waweze kujiandaa kujiendeleza kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi kabambe wa usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu umeanza rasmi tangu mwezi Machi, 2017. Mradi huu utajumuisha vipengele mradi vitatu vya densification, grid extension pamoja na off- grid renewable vinavyolenga kuongeza wigo wa usambazaji katika vijiji vyote vilivyobaki nchi nzima, vitongoji vyote, taasisi za umma, na maeneo ya pembezoni ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya umeme. Mradi wa REA Awamu ya Tatu katika jimbo la Kalambo utajumuisha vijiji 89 kupitia vipengele
- mradi vya densification grid extension, utaokamilika mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka umeme kwenye maeneo ya vijiji hivyo itajumuisha ujenzi wa njia ya msongo umeme wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 413.49; ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 745; pamoja na ufungaji wa transfoma 149. Kazi nyingine itakuwa ni kuwaunganishia umeme wateja wa awali 9,816 kazi ya gharama hii ni shilingi bilioni 36.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE Aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga reli ya TAZARA kutokea Tunduma kwenda Kasanga ili kuwa na manufaa mapana ya kiuchumi na matumizi mazuri ya Bandari ya Kasanga na kuufungua Mkoa wa Rukwa kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na mkakati wa ujenzi wa miradi mbalimbali ya reli nchini ambayo utekelezaji wake unazingatia kipaumbele kutokana na utekelezaji wa miradi ya reli kuhitaji fedha nyingi. Hivi sasa, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu wa Reli ya Mpanda – Karema na ni matumaini yetu kwamba, mradi wa reli hii utakapokamilika, utaifungua Mikoa ya Rukwa na Katavi kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kujenga reli ya kutoka Tunduma hadi Kasanga, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, ushauri wake umepokelewa na Wizara itaufanyia kazi. Aidha, kama nilivyosema awali, kwa kuwa miradi ya reli inahitaji fedha nyingi, utekelezaji wa ushauri huu utazingatia matokeo ya upembuzi yakinifu utakaofanywa kuhusu kipande hicho cha reli ikiwa ni pamoja na vipaumbele vya nchi. Ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, mpango wa Serikali wa ujenzi wa uwanja wa ndege eneo la Kisumba, Wilayani Kalambo umefikia hatua gani kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa imejikita katika kukamilisha ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga kilichopo Mkoani Rukwa ambacho ni miongoni mwa Viwanja vya Ndege vinne (4) vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kupata ufadhili kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank - EIB). Aidha, Serikali imekamilisha taratibu za kupata Mkandarasi na kupewa Idhini (No Objection) kutoka EIB, kinachosubiriwa ni kupata fedha baada ya taratibu za kimkataba kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege kwamba, baada ya Serikali kukamilisha Ujenzi wa Viwanja vya Ndege vya mikoa vilivyosalia ikiwemo Sumbawanga, Serikali itaendelea na ujenzi wa viwanja vidogo vya ndege kwa hadhi ya airstrip ikiwa ni pamoja na Kiwanja cha Ndege cha Kalambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwashauri wananchi wa Kalambo kutumia Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga mara ujenzi wake utakapokamilika.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Mahakama ya Mwanzo katika Tarafa ya Mambwenkoswe ili kuwapunguzia wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta haki?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kalambo ina Tarafa tano ambazo ni Mambwenkoswe, Matai, Mwimbi, Kasanga na Mwazye. Kati ya hizo, ni Tarafa nne ambazo zina huduma ya Mahakama ya Mwanzo isipokuwa Tarafa ya Mambwenkoswe.

Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Tanzania inao Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) ambao unajumuisha mahitaji yote ya ujenzi na ukarabati wa Mahakama katika ngazi zote za Mikoa, Wilaya na Makao Makuu yote ya Tarafa nchini.

Mheshimiwa Spika, napenda kumwahidi Mheshimiwa Mbunge kuwa katika kipindi hicho Tarafa yake hiyo moja iliyosalia pia itazingatiwa katika mpango huo. Ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais ya Mwaka 2015 ya ujenzi wa Kivuko cha Mto Kalambo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege Mbunge wa Jimbo la Kalambo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais ya mwaka 2015 na vilevile ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais ya mwaka 2020 ambaye kwa sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan umeanza, ambapo upembuzi yakinifu (Detailed Design) wa kivuko hicho umekamilika mwaka 2018, ambao ulifanywa na Mhandisi Mshauri Advanced Engineering Solutions Limited ya Tanzania kwa kushirikiana na Teknicon Limited ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Kivuko hicho chenye urefu wa mita 80 unategemea kugharimu Shilingi Bilioni Nne milioni mia sita themanini na tisa mia saba themanini na tatu elfu mia saba kumi na mbili na senti hamsini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua iliyofikia sasa ni kwa Serikali kuendelelea kutafuta fedha za ujenzi wa kivuko hicho, pindi fedha zitakapopatikana ujenzi utaanza mara moja.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya kuanzia Matai kwenda Kasesya border inayounganisha nchi yetu na nchi ya Zambia?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kazi ya Upembuzi yakinifu, Usanifu wa Kina na Uandaaji wa Nyaraka za Zabuni wa Barabara ya Matai - Kasesya yenye urefu wa kilomita 50 imekamilika. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ipo katika hatua za mwisho za manunuzi kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa kilometa 25 sehemu ya Matai – Tatanda ambapo rasimu ya mkataba imepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali tarehe 27 mwaka huu kwa ajili ya kupata ridhaa (vetting) ili mkataba uweze kusainiwa. Aidha, Serikali kupitia TANROADS iko kwenye maandalizi ya kutangaza zabuni ya kazi ya ujenzi kwa sehemu iliyobaki ya kutoka Tatanda – Kasesya yenye urefu wa kilometa 25. Zabuni itakuwa imetangazwa kabla ya mwezi Juni mwaka huu.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kujenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilayani Kalambo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Jimbo la Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo, kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Spika, Kalambo ni miongoni mwa Wilaya 63 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi katika mwaka huu wa fedha. Nakushukuru sana.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, kwa mujibu wa tafiti ni madini aina gani yanapatikana katika Mkoa wa Rukwa na katika maeneo gani?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege Mbunge wa Jimbo la Kalambo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa iliyobarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali. Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) mkoa huu una madini yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dhahabu katika kata za Kabwe, Namanyere, Msenga na Ninde. Shaba katika Kata za Kirando, Namanyere, Msenga, Kala na Ninde. Risasi katika Kata za Namanyere na Ninde, Makaa ya Mawe katika Kata za Chala, Kipande, Muze na Ntendo. Madini ya viwandani kuna chokaa Kata ya Ntendo, na Kyanite Kata ya Msenga. Chumvi Kata za Kirando, na Kipeta. Ulanga Kata za Mkwamba, Mwazye, Kaoze na Senga. Vito katika Kata za Chala, Kipande, Senga na Malangali. Rare Earth Elements Kata za Mkwamba na Msenga. Chemichemi za majimoto zenye kuambatana na gesi ya helium katika Kata za Kirando na Msenga, na Chuma katika Kata ya Katazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madini mengine ni madini ujenzi ambayo ni kokoto na mchanga ambayo yanapatikana katika Wilaya zote za Mkoa wa Rukwa ahsante sana.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Mkoa wa Rukwa unalima zao la maharage ya soya lenye uhitaji mkubwa zaidi duniani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa ni moja ya mikoa inayozalisha maharage ya soya kwa wingi nchini kwa ajili ya chakula na biashara. Katika mwaka 2020/2021 mkoa ulizalisha jumla ya tani 121,356 katika eneo la hekta 120,432. Mwaka 2021/2022 mkoa umelenga kuzalisha jumla ya tani 128,672 za maharage katika eneo la hekta 121,961.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuendeleza kilimo cha maharage ya soya Mkoani Rukwa, Serikali kwa kushirikiana na wadau imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora za maharage ya soya nchini kupitia sekta binafsi, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI-Uyole) na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na kupitia vikundi vya wakulima wazalishaji wa mbegu za daraja la kuazimiwa ubora (QDS) na kutoa mafunzo ya uzalishaji wa maharage ya soya kwa Maafisa Ugani 64 katika ngazi ya Halmashauri, kata na vijiji ili kuwezesha wakulima kuzalisha kwa tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, Maafisa Ugani hao wanatumika katika kutoa ushauri na kuandaa mashamba ya mfano ya kilimo cha maharage ya soya katika maeneo yao, kupima afya ya udongo ili kuwezesha matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo, kuhamasisha kilimo cha mkataba kati ya wakulima na wanunuzi ili kuwa na uhakika wa soko la mazao ya wakulima wanaolima maharage ya soya nchini.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, lini mpaka wa Kasesya/Zombe utafanya kazi kwa ufanisi ili kupunguza msongamano wa malori katika mpaka wa Tunduma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa mpaka wa Tunduma/Nakonde na mpaka wa Kasesya/Zombe ambayo inatumika kupitisha mizigo inayokwenda au kutoka Zambia. Aidha, wasafirishaji wana hiari ya kuchagua mpaka upi wautumie katika kusafirisha mizigo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa Tunduma/Nakonde umekuwa ukitumiwa zaidi na wasafirishaji wanaosafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Zambia na DRC kwa kuwa ndiyo mpaka wenye umbali mfupi ukilinganishwa na mpaka wa Kasesya/Zombe. Kwa mfano, kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma ni kilomita 922, kutoka Dar es Salaam kwenda Kasesya kupitia Tunduma na Laela ni kilometa 1,172; kutoka Dar es Salaam kwenda Kasesya kupitia Tunduma na Sumbawanga ni Kilometa 1,249; na kutoka Dar es Salaam kwenda Kasesya kupitia Dodoma,Tabora na Mpanda ni Kilometa 1,530. Ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Mahakama yenye hadhi ya Wilaya katika Wilaya ya Kalambo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuanza ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Kalambo katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 ambapo taratibu zote za awali za kupitia michoro na makadirio ya gharama vimekamilika. Aidha, hatua ya kupata Mkandarasi wa ujenzi ipo katika hatua za mwisho. Hivyo, tunategemea muda wowote jengo hili litaanza kujengwa na kukamilika katika mwaka ujao wa fedha, ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, ni lini ahadi ya kujenga Kituo cha Afya Kata ya Kasanga itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Jimbo la Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kasanga kama iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyotembelea Kata ya Kasanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati kote nchini kikiwemo Kituo cha Afya Kasanga kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
MHE. JONAS W. MBUNDA K.n.y. MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, kuna mpango gani kuboresha utendaji wa Shirika la Mbolea (TFC) ili kusambaza pembejeo kwa wakulima kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu wa mwaka 2022/2023 Serikali imeunda Bodi ya Wakurugenzi na kuajiri Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania. Vilevile, Serikali imeipatia TFC mtaji wa Shilingi bilioni sita ambao umeiwezesha kununua jumla ya tani 4,500 na kusambaza jumla ya tani 3,851.35 za mbolea kwa wakulima 20,271.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imepanga kuiongezea TFC mtaji wa Shilingi bilioni 40 kwa ajili ya kununua na kusambaza pembejeo za kilimo kwa wakulima. Aidha, mpango wa muda mrefu ni kampuni kujenga kiwanda cha kuchanganyia mbolea na eneo la ekari 14.5 limepatikana kwenye Kijiji cha Visegese, Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, ambapo ujenzi utaanza katika mwaka wa fedha wa 2023/2024.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Watumishi wa Kada ya Afya Wilayani Kalambo kwa kuzingatia upungufu uliopo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Jimbo la Kalambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka huu wa fedha imepanga kuajiri watumishi wa kada ya afya 7,612 watakaopangiwa katika Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha Maporomoko ya Kalambo yanatangazwa ili yawe na mchango wa kiuchumi kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege Mbunge wa Jimbo la Kalambo kama ifuatavyo:-

Katika kuhakikisha maporomoko ya Kalambo yanatangazwa kikamilifu, hatua zifuatazo zimeanza kuchukuliwa. Hatua ya kwanza ni kutumia vyombo vya habari kuandaa machapisho na majarida kushiriki katika maonyesho matamasha matukio na makongamano ya utalii na biashara yanayofanyika ndani na nje ya nchi. Aidha, jumla ya watalii 2,365 walitembelea maporomoko hayo mwaka 2021 ikilinganishwa na watalii 300 kwa mwaka 2016 na kuweka mabango katika viwanja vya ndege ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Songwe na maeneo mengine katika Mkoa wa Rukwa.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA K.n.y. MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, lini Mkoa wa Rukwa utaunganishwa na Gridi ya Taifa ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuunganisha Mkoa wa Rukwa na Gridi ya Taifa, Serikali inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa Kilovolt 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma kwa Mradi wa TAZA, umbali wa kilomita 620. Mradi huu pia unahusisha ujenzi wa vituo vya kupooza umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa, Wakandarasi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wameshapatikana na Wakandarasi wa ujenzi wa vituo vya kupooza umeme wapo katika hatua za majadiliano. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi huu wa Novemba, 2023 na kukamilika mwezi Desemba, 2025, ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kurasimisha na kurahisisha ubadilishaji wa fedha za kigeni kati ya Tanzania, Zambia, Malawi na Msumbiji?
WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Benki Kuu imeendelea kurahisha taratibu za usajili wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini ili wananchi wenye uwezo waweze kufungua na kuendesha maduka hayo katika sehemu mbalimbali, ikiwemo sehemu za mipakani. Hadi Desemba 2023, huduma za kubadilisha fedha katika mipaka ya Tunduma, Mtwara, Mtukula na Namanga zinapatikana katika matawi 25 ya benki na maduka mawili (2) ya kubadilisha fedha.

Mheshimiwa Spika, wananchi na wafanyabiashara katika mipaka ya Tanzania na nchi jirani ikiwemo Zambia, Malawi na Msumbiji wanashauriwa kutumia taasisi rasmi za fedha, yaani benki za biashara pamoja na maduka ya kubadilisha fedha ili kurahisisha miamala ya kibiashara za kigeni. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na jumuiya za kikanda, ikiwemo EAC pamoja na SADC zimetengeneza mifumo ya malipo ili kurahisha malipo baina ya nchi wanachama kwa lengo la kupunguza matumizi ya fedha taslimu katika biashara.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanza ujenzi wa kipande cha Reli ya TAZARA kutoka Tunduma hadi Bandari ya Kasanga?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuunganisha reli ya TAZARA na Bandari ya Kasanga ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo katika ukanda huo hususani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa TAZARA inamilikiwa na Serikali mbili; Tanzania na Zambia, tumeanza mazungumzo na wenzetu Zambia ili kutenga fedha katika bajeti ya TAZARA kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa reli hiyo kwa lengo la kubaini gharama za ujenzi wake na manufaa yake kiuchumi.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Sekta ya Kilimo inakuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kujenga msingi imara wa muda mrefu wa ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kiwango cha asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. Mpango huo, utaweka msingi wa kukabiliana na athari za majanga ya asili na yasiyo ya asili ikiwemo mdororo wa uchumi ili kulinda sekta hiyo na pia kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi. Ili kufikia dhamira hiyo, Serikali imelenga kujitosheleza katika chakula, kuongeza thamani ya mauzo ya mazao, kuongeza idadi ya mashamba makubwa, kuongeza eneo la umwagiliaji, kujihakikishia upatikanaji wa malighafi, kuimarisha utafiti, kuongeza uzalishaji wa mbegu bora, kuongeza mitaji, kuongeza mauzo ya mazao ya bustani na kuimarisha upatikanaji wa pembejeo.

Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Shilingi Bilioni 298 ya mwaka 2021/2022 hadi kufikia Shilingi Bilioni 954 kwa mwaka 2022/2023 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele kwa ajili ya kufikia lengo kuu la ukuaji wa sekta wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. (Makofi)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, kuna utafiti wa kisayansi unaoonyesha kufunga shughuli za uvuvi Ziwa Tanganyika kuruhusu kuzaliana kwa Samaki kutakuwa na tija?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha uvunaji wa rasilimali za uvuvi katika Ziwa Tanganyika unafanyika kwa njia endelevu, Wizara kwa kushirikiana na nchi zinazounda Mamlaka ya Ziwa Tanganyika inatekeleza Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika unaoweka hatua za usimamizi wa uvuvi endelevu katika Ziwa Tanganyika na Bonde lake. Aidha, miongoni mwa hatua za usimamizi ni kuanzishwa kwa utaratibu wa kupumzisha shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kila ifikapo tarehe 15 Mei hadi 15 Agosti ya kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upumzishaji wa Ziwa Tanganyika katika kipindi cha miezi mitatu, unatarajiwa kuwa na tija ya muda mrefu kwa kuwa tafiti katika nchi zinazozunguka ziwa zinaonesha kuwa kipindi hicho kunakuwepo na samaki wengi wachanga aina ya migebuka na dagaa. Samaki hawa wanahitaji kipindi cha miezi mitatu mpaka minne kufikia kiwango cha kuvuliwa. Aidha, kupumzisha ziwa katika kipindi hicho kutaruhusu samaki kukua na mavuno kuongeza.
MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, lini chanzo cha uhakika cha maji ya Ziwa Tanganyika kitatumika katika Vijiji vya Mwambao wa Ziwa na maeneo mengine Mkoa wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, dhamira ya Serikali ni kutumia vyanzo vya maji vya uhakika katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini ikiwemo mito na maziwa. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali tayari imeanza na inaendelea kutumia vyanzo hivyo kwa ajili ya kusambaza maji, huduma ya maji safi na salama kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mkoa wa Rukwa, chanzo cha Ziwa Tanganyika kimenufaisha wananchi wapatao 47,349 waishio kwenye mwambao wa ziwa hilo kupitia utekelezaji wa Miradi ya Maji ya Kipwa, Kapele Wilayani Kalambo, Kabwe, Kabwe camp, Udachi, Mkinga, Majengo, Ntanganyika, Kalungu, Mtakuja, Kamwanda, Kichangani na Itete Wilaya ya Nkasi. Vilevile Serikali ipo kwenye hatua za mwisho za kuajiri mtaalam mshauri kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina (feasibility study and detailed design) kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji utakaotumia chanzo cha Ziwa Tanganyika kwa lengo la kuhudumia mikoa ya Rukwa na Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali itatekeleza miradi ya maji kwa kutumia chanzo cha Ziwa Tanganyika itakayonufaisha vijiji 16 vya Kazovu, Kisambala, Mandakerenge, Msamba, Uhuru, Utinta, Kalila, Isaba, Izinga, Kala, Kasanga, Muzi, Kisala, Samazi, Pamoja na Kipanga na Katili.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya katika Mji Mdogo wa Matai, Wilayani Kalambo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kalambo ni miongoni mwa wilaya zenye changamoto ya miundombinu chakavu ya Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa huduma za Mahakama ya Wilaya zinapatikana katika Jengo la Mahakama ya Mwanzo Matai. Aidha, zabuni ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Kalambo ambayo pia itajumuisha Mahakama ya Mwanzo ya Matai imeshatangazwa na ujenzi unatarajiwa kuanza mara baada ya kukamilika kwa taratibu za manunuzi, nashukuru. (Makofi)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuhakikisha maporomoko ya Kalambo yanatangazwa kitalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kwamba maporomoko ya maji ya Kalambo yanatangazwa kitalii, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuyaendeleza na kuyatangaza maporomoko hayo, ikiwemo kuboresha miundombinu mbalimbali kwenye hifadhi ya mazingira asilia ya Kalambo, ikiwa ni pamoja na kufanya kampeni za kuyatangaza. Mathalani katika uboreshaji wa miundombinu, Serikali imeboresha barabara, njia za waenda kwa miguu, ngazi za kushuka na kupandisha kwenye maporomoko, miundombinu ya vyoo, mabanda ya kupumzika wageni na eneo la maegesho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa matangazo, makala maalumu ziliandaliwa na kurushwa kwenye televisheni, kumekuwa na uandaaji wa matukio na vifurushi vya misimu maalumu, zimefanyika jitihada za kuandaa mabango na vipeperushi na kutumia njia za kidijitali katika kutangaza maporomoko hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea na jitihada za kuyatangaza maporomoko hayo ili kuvutia watalii wengi kutembelea eneo hilo asilia. Aidha, nitoe rai kwa uongozi wa Mkoa wa Rukwa kuendelea kushirikiana na Wizara katika kuhamasisha wadau na wawekezaji waliopo katika Mkoa wa Rukwa na nje ya mkoa huo kuwekeza huduma mbalimbali za kijamii, kama vile huduma za malazi kuzunguka maeneo ya maporomoko ya Kalambo kwa lengo la kuwapatia huduma stahiki watalii na wageni wetu wanaotarajiwa kutembelea maporomoko hayo. (Makofi)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani juu ya eneo lililochukuliwa bila fidia na halijaendelezwa katika Kijiji cha Kasesya mpakani mwa Tanzania na Zambia?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili lilikuwa linafanyiwa marekebisho jana na niombe radhi tu kwamba sasa tunawasilisha jibu linalotakiwa kukaa kwenye records zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1995 Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ilitwaa sehemu ya Ardhi ya Kijiji cha Kasesya kilichopo mpakani mwa Tanzania na Zambia ili kulifanya eneo kuwa la uwekezaji kwa kuwa lipo mpakani. Eneo hili lilitwaliwa kwa Sheria ya Ardhi ya wakati huo ambayo ilibainisha fidia kwa kuzingatia maendelezo tu, ambapo wakati huo eneo halikuwa na maendelezo yeyote hivyo hakukuwa na suala la fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lililotwaliwa lilipangwa na kupimwa na kutoa viwanja 52 ambapo halmashauri ilivitangaza viwanja kuanzia namba 5-36 vilichukuliwa na Taasisi ya Tanzania Chambers of Commerce Industries and Agriculture kwa Barua ya Toleo yenye Kumb. Na. LD/SDC/178/3 ya tarehe 10 Desemba, 2002, kwa matumizi mchanganyiko. Taasisi ya Tanzania Chambers of Commerce imeendeleza eneo dogo sana kwa kujenga machinjio na bucha chache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imeanza mazungumzo na Taasisi hiyo ambayo inamiliki eneo hilo kihalali ili kuona jinsi ya kufikia makubaliano ya kuona uwezekano wa kulirejesha eneo hilo kwa wananchi kwa kuwa halijafanyiwa maendelezo makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia jambo hili linalohusu wananchi wake wa Kijiji cha Kasesya, nimwombe Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Kijiji cha Kasesya kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa suala hili. Ahsante sana.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha mbegu ya Ng’ombe ya asili ya Ufipa haipotei?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha mifugo ya asili ikiwemo ng’ombe aina ya Ufipa haipotei, Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) ilianzisha vituo viwili vya Kongwa na West Kilimanjaro kwa ajili ya kuhifadhi mifugo ya asili ambapo Kituo cha Kongwa kinahifadhi mbari za ng’ombe wa asili na kituo cha West Kilimanjaro kinahifadhi mbari za mbuzi na kondoo wa asili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati mwingine unaotekelezwa na Wizara wa kuhifadhi mifugo ya asili ni kuvuna na kuhifadhi mbegu za mifugo ya asili ikiwemo mbari aina ya ufipa katika kituo cha Taifa cha Uhimilishaji cha NAIC – Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara imepanga kununua madume nane ya ng’ombe wa asili aina ya Ufipa, Gogo, Iringa red, Singida White, Ankole, Tarime, Sukuma na Maasai kwa ajili ya kuvuna mbegu na kuanza uhifadhi wa vinasaba vya mbari za mifugo ya asili iliyo hatarini kutoweka hapa nchini.