Supplementary Questions from Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama (25 total)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa vile suala hili la maji ni suala la kisera; na kwa vile miraji mingi ya maji inayotekelezwa kwa kupitia Halmashauri za Wilaya inakwama; na kwa vile ni Wizara inayohusika na maji ndiyo inayopeleka miradi hii isimamiwe na Halmashauri za Wilaya; na Halmashauri za Wilaya hizi hazitekelezi majukumu yake vizuri na kukwamisha Wizara kufikia yale malengo waliyojiwekea. Na kwa vile Wilaya ya Songea katika kijiji cha Maweso na Lilondo, miradi hiyo imekwama kwa sababu tu certificate za wakandarasi hazijafikia Wizara mpaka leo;
Ni hatua gani Wizara ya TAMISEMI inachukua pale ambapo miradi inakwamishwa na Halmashauri, ni miradi ambayo kimsingi inatoka kwenye Wizara zingine? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa kujibu vizuri sana maswali aliyoulizwa ya nyongeza kwenye sekta ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu spika, tumetoa maelekezo kwenye Halmshauri wakiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Sekta ya Maji kwamba kwa sasa hivi tunapeleka fedha baada ya kuletwa certificate. Sasa Mheshimiwa Mbunge kama unayo certificate ya kazi ambayo imeshafanyika naomba uniletee hata leo, tutakwenda kulipa. Kwa sababu wanasema certificate zipo lakini tumeangalia uhalisia kule Wizarani certificate hazipo, sasa kama ipo certificate na kazi imefanyika tunakwenda kulipa ili kusudi wakandarasi warudi wafanye kazi miradi ya maji iweze kukamilika.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, niliomba niulize swali lingine la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile huduma hizi za kibenki ni suala la kisera; na kwa vile ni haki ya kila Mtanzania kupata huduma hizi; na kwa vile imebainika kwamba mabenki yetu ya kibiashara hayawezi kufika yale maeneo ambayo hayana tija sana kibiashara; ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba Benki ya Kilimo inayafikia maeneo hayo ambayo hayana tija kwa wafanyabiashara wa kibenki likiwemo Jimbo la Madaba na Jimbo la Mlalo kama ilivyoulizwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mhagama kama ulivyosikia wakati tunaweka Mezani bajeti yetu ya Wizara ya Fedha, moja katika benki ambazo tunategemea kwamba zitafungua matawi yake zaidi, ni hiyo Benki yetu ya Kilimo. Kwa hiyo, tunaendelea kuijengea uwezo na muda siyo mrefu Benki hii itafungua matawi yake katika maeneo yenye wakulima wetu ili waweze kufaidika na huduma za Benki yetu ya Kilimo.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kwa vile Halmashauri ya Wilaya ya Madaba sasa ipo kisheria na tayari kumekuwa na mgawanyo wa mali na miradi mbalimbali kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Songea; na kwa vile Halmashauri ya Wilaya ya Songea ipo mbali sana kijiografia na Halmashauri ya Wilaya ya Madaba; kwa nini sasa miradi isikabidhiwe kwa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba ili iweze kusimamiwa kwa ukaribu na kwa ufanisi zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa vile yapo mabomba ambayo yalinunuliwa kwa kupitia mradi huu na mkandarasi na kwa miaka zaidi ya miwili yapo nje, yapo juani, yanazidi kuwakiwa jua na yanapoteza ubora; kwa nini sasa Wizara isimshauri mkandarasi kwa kushirikiana na Halmashauri ili yale mabomba sasa yaweze kufukiwa katika njia ambazo zimekusudiwa na mradi huu ili miradi midogo midogo ya maji ambayo wananchi wameianzisha na wanaiendeleza iweze pia kuingia kwenye mtandao huu na kuanza kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, miradi hii iliibuliwa ikiwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea na sasa hivi Madaba sasa ni Halmashauri. Anasema, kama vitu vingi vimeshagawiwa tayari, kwa nini ile miradi ibakie kuwa Songea? Hatuna tatizo na hilo na halitakuwa la kwanza. Kuna Halmashauri nyingi mpya. Kwa hiyo, kama wameshakamilika, basi utuletee barua kuomba hilo na Wizara itakubaliana na hiyo hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwamba kuna mabomba ambayo yameshanunuliwa na mkandarasi na yanaungua na jua; kwa nini yasifukiwe ili wananchi wapate maji?
Mheshimiwa Mhagama, kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha 2016/2017 ulitengewa zaidi ya shilingi milioni 800 ambayo matumizi yake inapanga Halmashauri yenyewe. Naomba tu kushauri kwamba Halmashauri yako basi watumie hizo fedha kwa sababu mnazo ili waweze; ama kwa kutumia nguvu ya wananchi ama huyo mkandarasi basi, kwa nini asiyafukie kwa sasa na hela inatolewa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba tu Mheshimiwa tuwasiliane ili tuweze kulijadili hili kwa pamoja, mabomba haya yafukiwe haraka wananchi wapate huduma ya maji.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa vile barabara hii ya Makambako - Songea uharibifu wake umechangiwa kwa kiwango kikubwa na usafirishaji wa magari na mizigo mizito kutoka na kuelekea Songea. Ni lini sasa Serikali itajenga reli kutoka Makambako kuelekea Songea kupitia Madaba? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile mizigo mingi pia inatoka Mbeya kuelekea Songea mpaka Mbinga, ni lini sasa Serikali itakamilisha meli ya kutoka Kyela kwenda Mbamba Bay ili mizigo mingi inayopita barabara ya Mbeya kuelekea Songea ipite kwa kutumia meli na kuokoa barabara zetu?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali haijafikiria kujenga reli kutoka Makambako kwenda Songea, badala yake inafikiria na kwa sasa inatekeleza upembezi yakinifu na usanifu wa kina wa reli kutoka Mtwara - Songea hadi Mbamba Bay. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu meli, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mhagama, hivi karibuni tu TPA wamekamilisha ujenzi wa meli mbili aina ya tishali zinazojiendesha ambazo zitafanya safari za kubeba mizigo kati ya Itungi pamoja na Mbinga. Kwa hiyo, meli hizo zitasaidia sana kupunguza mizigo inayopita katika barabara ya Makambako hadi Songea. Meli hizo zitazinduliwa hivi karibuni zinaitwa Self Propelled Barges, ni meli aina ya tishali.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafsi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile vikao halali vya Halmashauri ya Wilaya ya Songea vilishamaliza jukumu la kihalmashauri kuhusu matumizi ya eneo hili la ardhi; na kwa vile katika mazungumzo na ufuatiliaji Wizara ya Kilimo walishaelekeza kwamba sasa Mkoa ukabidhi sehemu ya eneo la shamba hilo kwa wananchi ili waweze kuendelea na shughuli za kilimo; na kwa vile msimu wa kilimo umekaribia sana na wananchi hawana sehemu ya kulima mazao ya chakula, na kwa vile wafugaji tayari wameanza kufuga katika eneo hilo.
Je, Serikali ipo tayari sasa kutoa maelekezo kwa Serikali ya Mkoa kuhusu kutekeleza jukumu hili haraka iwezekanavyo?
Pili, iwapo zoezi hili litaendelea kuchelewa kutekelezwa, je, Serikali ipo radhi sasa kuruhusu wananchi wa Ngadinda na kwa vile mipaka inafahamika, kuiagiza Serikali ya kijiji iweze kuanza kushirikiana na wananchi kuwatengea maeneo hayo waweze kuanza kuzalisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa hizo initiative zote walizozifanya mpaka wamefikia hapo. Mimi nafahamu kwamba kama hatua nyingi za msingi zimeshafanyika kikubwa zaidi ni sehemu yetu ya Mkoa. Nichukue fursa hii kuiagiza Ofisi ya Mkoa wa Ruvuma iangalie jinsi gani ya kufanya kama mijadala yote imeshakamilika iende haraka kurekebisha jambo hili ili wakulima na wafugaji tusiwe na mgogoro tena katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua wazi kwamba jambo hili likiwa na ukakasi wake mwisho wa siku tunakuja kuzalisha matatizo makubwa sana ya uvunjivu wa amani. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kuiagiza timu ya Mkoa wetu wa Ruvuma iende ikalifanyie kazi jambo hilo haraka iwezekanavyo na ikiwezekana mpaka mwezi wa Kumi jambo hilo liwe limekamilika na ofisi yetu ya TAMISEMI tupate taarifa ya jinsi gani jambo hilo limekamilishwa kwa sababu vikao vyote halali kwa taarifa niliyoipata kutoka kwa Mbunge zimeshakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili kwamba kukiruhusu kijiji kwenda kuhakikisha kwamba wanaenda kugawa hilo eneo, naomba tuvute subira kwanza, timu ya Mkoa ifanye kazi yake vizuri baadaye tukishapata taarifa tutajua nini kifanyike. Lengo kubwa kama unavyowapigania wananchi wako Serikali itaingilia kati kwa nguvu zote sisi tukishirikiana na Wizara ya Kilimo tutafanya kila liwezekanalo eneo lile liwe katika utaratibu mzuri, wananchi wa eneo lile waweze kupata ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ondoa hofu Mheshimiwa Mbunge tunalifanyia kazi jambo hili.(Makofi)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsantekwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Naomba nimuulize Waziri, kwa vile imethibitika kwamba baadhi ya ajali zinazotokea barabarani au zinasababishwa na ubovu wa barabara, au zinasababishwa na ukosefu wa alama mahususi za barabarani jukumu ambalo amekebidhiwa wakala wa barabara yaani TANROADS. Je, Serikali ina mpango gani wa kuiwajibisha TANROADS pale ambapo sababu ya ajali inaonekana ni kutotekeleza wajibu wa wakala huyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna ubovu wa barabara na Serikali imekuwa ikiendelea kufanya jitihada za kurekebisha ubovu huo kuhakikisha kwamba barabara zetu kuu na barabara za mikoa zimapitika kila wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito tu kwa Watanzania wenzetu, kumetokea tabia ya hivi karibuni wananchi kuchukua hatua wenyewe ya kuweka matuta barabarani na hicho kimekuwa ni chanzo kimojawapo cha ajali mbalimbali kwa sababu wanapoweka matuta bila kuwashauri au bila kuwaambia TANROADS ina maana yale matuta yanakuwa hayana alama na magari yanapokuja yanafika, yanavamia yale matuta na kusababisha ajali. Niwashauri Watanzania, tunawaomba wasiweke matuta barabarani bila kuviambia vyombo husika vinavyohusika na barabara ili kuweka alama kuwaonyesha madereva kwamba kuna tuta mbele wanakokwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge Ndugu yangu Joseph Mhagama kwamba TANROADS wanajitahidi sana kufanya kazi zao kwa uadilifu na kwa umakini wa hali ya juu kuzingatia usalama wa Watanzania. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wa shule zote za Wilaya ya Songea walisimamishwa wakati Wilaya zingine wamepandiswa madaraja na maslahi yao yameongezeka, walimu wa Songea Vijijini hawakufanyiwa hivyo kwa sababu taarifa kutoka kwa Mkurugenzi zilichelewa kuifikia Wizara. Suala hili limefuatiliwa kwa miaka miwili sasa na walimu hawa hawajapata stahiki zao mpaka sasa.
Je, Serikali inatoa tamko gani kwa walimu waliopo Songea, kwa maana ya Songea Vijijini na Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kuhusu madai na malalamiko yao? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna kesi za aina mbalimbali, na hata jana nilipata kesi inayofanana na hiyo kutoka kwa Mheshimiwa Kanyasu. Nimewaelekeza wataalam wetu wafanye tathmini maeneo mbalimbali yenye changamoto, nikifahamu kwamba lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba watumishi wetu wanafaya kazi kwa amani. Maeneo mengine wamefanya vizuri, maeneo mengine bado hawajafanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimewaelekeza wataalam wangu waweze kufanya kufanya tathmini maeneo mbalimbali yenye changamoto ili tuwasaidie watumishi wote ambao wana changamoto mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuweze kubaini utendaji wa kazi wa baadhi ya watu tuliowapa mamlaka. Wale wataonekana kwamba wamekuwa ni kikwazo basi ni vyema tukaweza tukawachukulia hatua za kinidhamu kwa sababu katika njia moja au nyingine wanaweza wakasababisha Serikali ikalaumiwa kumbe kutokana na uzembe wa watu wachache.
Kwa hiyo jambo hili tumelichukua na toka jana timu yangu inafanyia kazi jambo hilo kwa sababu lilitoka vile vile katika Mkoa wa Geita. Maeneo mbalimbali kuna kesi kama hizo, kwa hiyo Serikali tunaichukulia yote kwa ujumla wake na kuyafanyia kazi. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niipongeze sana Serikali kwa mkakati huu mzuri ambao umeiuweka na kwa sehemu imetekeleza lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile moja kati ya migogoro ambayo inatokana na tatizo hili ambalo limeelezwa ni migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Na kwa vile migogoro hii kwa sehemu kubwa inachangiwa na ukosefu wa mipango bora ya matumizi ya ardhi kwa baadhi ya maeneo, na kwa vile pamoja na jitihada nzuri za Serikali migogoro hii imechangiwa na Halmashauri za wilaya hasa watumishi ambao hawapo tayari kwenda kufanya kazi hii bila kulipwa posho, sasa je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba vijiji vyote ambavyo havina mpango bora wa ardhi vipatiwe mpango huo? Na pili ina mpango gani kuhakikisha kwamba watumishi ambao hawapo tayari kwenda kufanya kazi hizi bila kupata posho wanachukuliwa hatua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama kwa kuijali sana hii sekta ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu, hata viwanda vinategemea sana sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vijiji ambavyo hadi sasa havina mipango ya matumizi bora ya ardhi tunayo changamoto kubwa sana, moja, ili kijiji kipime, kiwe na mpango wa matumizi bora ya ardhi yake bajeti ambayo inahitajika angalau kuweza kuwezesha upimaji huo inaanzia kati ya shilingi milioni tano hadi milioni nane na baadhi ya vijiji ambavyo ni vikubwa hadi milioni kumi. Sasa kwa sababu Halmashauri nyingi bado hazijawa na uwezo wa kuwa na fedha hizo utekelezaji umekuwa ni wa pole pole sana, ikiwemo Halmashauri yake ya Madaba hadi sasa ni vijiji nane tu ndio vina mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa wito kwa vijiji ambavyo vina fedha, vipo vijiji ambavyo vina fedha, vigharamie mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa manufaa ya kiuchumi ya wananchi wa vijiji hivyo. Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini wafanye mapitio ya vijiji vyote na kuvishauri vile ambavyo vina uwezo wa kugharamia zoezi hilo viweze kugharamia, na vile ambavyo havina kabisa uwezo halmashauri ijipange kugharamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunawachukulia hatua gani watumishi ambao hawataki kwenda kufanya kazi vijijini hadi walipwe posho. Nataka nitoe angalizo kwao, kwamba walipoajiriwa walipewa maeneo ya kufanya kazi. Kama mtu amepewa eneo la kijiji halafu ndani ya kijiji hataki kufanya kazi mpaka alipwe posho huyu mtu tunatakiwa tupate taarifa zake mapema iwezekanavyo ili tuweze kumchukulia hatua na Wakurugenzi wa Halmashauri waanze kuchukua hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatoa maagizo wale watumishi ambao wana mazoea ya kukaa Makao Makuu ya Halmashauri bila kwenda kutembelea vijiji waanze kupangiwa kazi na Wakurugenzi wa Halmashauri bila kujali kama kuna posho au hakuna, ili mradi tu aweze kuwezeshwa vyombo vya usafiri vya kuweza kuwafikisha kwenye vijiji wanavyotakiwa kwenda kufanya kazi, basi. Kwa hiyo, hiyo ndio ushauri wangu na maelekezo yangu kupitia Bunge lako Tukufu.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru sana Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa majibu yake mazuri kulingana na swali lililoulizwa juu ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi. Wizara imejipanga vizuri katika mwaka wa fedha unaokuja kwa ajili ya kupima maeneo ambayo yana migogoro mingi, hasa yale maeneo yanayozunguka kwenye mbuga za wanyama. Tayari ile Tume ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi imeshaingia makubaliano pia na wenzetu wa TANAPA, kwa hiyo kuna vijiji vingi ambavyo vitapimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo tukumbuke tu kwamba mpango wa kupanga matumizi bora ya ardhi au masuala ya mpango miji ni jukumu la Halmashauri zenyewe husika. Kama alivyosema Naibu Waziri bado pia vijiji na maeneo ambayo yanakuwa na pesa wanayo fursa hiyo. Kama Wizara tuna-facilitate uwezekano wa kuweza kuwapa elimu na namna bora ya kupima, lakini Wizara tumejipanga vizuri na tutakwenda kupunguza sana kero hii. Kwa hiyo, tunachowaomba sana wananchi tuwe tayari katika suala hilo.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba niongezee na niliarifu Bunge lako tukufu kwamba Wizara ya Kilimo tumeandaa mpango mkakati wa kilimo ASDP II ambao utahusisha zaidi ya Wizara sita. Hata hivyo kutokana na swali la msingi ni kwamba katika hizi green house tumepanga kila halmashauri iweze kuwa na green house ili wananchi waweze kujifunza, kwa sababu hizo green house ambazo tunazizungumzia zinachukua eneo dogo lakini uzalishaji wake unakuwa ni mkubwa zaidi na vile vile ni katika kuendeleza hii tasnia yetu ya horticulture.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni kwamba Wizara tunatoa mafunzo na maelekezo ambayo yanafanyika kwa kutumia udongo na teknolojia mbalimbali za kuhifadhi udongo huo ili kuzuia mmomonyoko na vile vile kuweza kuongeza tija kwa ajili ya kupunguza tatizo hili nililolisema, ahsante.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:
Mheshimiwa Spika, awali ya yote niipongeze sana benki ya TPB kwa kufanya kazi vizuri na kuendele kujiboresha, nina maswali mawili ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja ya sababu ya kuanzisha benki zinazosimamiwa na Serikali popote duniani, sababu za kuanzisha Benki za Umma ni kwenda kua-address mapungufu ambayo sekta binafsi, Mabenki Binafsi yameshindwa kuyashughulikia. Miongoni mwa mapungufu hayo ambayo tunayo hapa Tanzania ni kwamba Wajasiriamali wengi wadogo wanashindwa kufanya biashara zao kwa sababu hawana mitaji, ni kwa namna gani Benki hii ya Posta inajitofautisha na benki zingine za kibiashara katika kusaidia Wajasiriamali wadogo nchini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sehemu ya pili swali langu tumeona kwamba Benki ya Kilimo Tanzania haina matawi katika Mikoa mingi na Wilaya nyingi na Wakulima wanakosa mitaji ya biashara ni kwa namna gani sasa Serikali imejipanga kuitumia Benki ya Posta kama Tawi kama tawi la Benki ya Kilimo Tanzania.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni jinsi gani TPB inajitofautisha katika kutoa huduma na benki nyingine za biashara, naomba kumpa taarifa kwamba Benki ya TPB kwanza ina Matawi katika Mikoa yote Tanzania na imekwenda katika Wilaya ambazo tunasema ni kama Wilaya za Vijijini ambako Mabenki mengi ya biashara hayajafika, kwa hiyo hilo ni jambo la kwanza walilolifanya kuwafikia wananchi wetu kule walipo. Pia, Benki ya TPB ina mfumo wa kukaa na Wajasiriamali kuwapa mafunzo na kuwapa mikopo ambayo ina riba nafuu ikishirikiana na Benki yetu ya Kilimo Tanzania.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni jinsi gani inaweza kushirikiana naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu tayari Benki yetu ya Kilimo ilishafungua matawi yake kwenye Kanda, Kanda ya Mwanza na Kanda ya Kati, tayari wameanza kufanya kazi na sasa wanajiandaa kwenda kufungua Tawi lao Mkoani Mbeya ili kuhudumia Nyanda za Juu Kusini. Wakati tukiendelea kufungua matawi ya Benki yetu ya Kilimo, Benki ya Kilimo pamoja na Benki ya TPB wanashirikiana na kwa mwaka huu wa fedha peke yake wametoa mikopo zaidi ya bilioni 431 kwa wakulima wetu kwenye maeneo yale ambapo TADB haina matawi lakini TPB imeweza kufika.
Mheshimiwa Spika, ni imani yetu sisi kama Wizara tunayosimamia sekta hii kuhakikisha kuwa wananchi wetu wakiwemo wajasiriamali wadogo pamoja na Wakulima wetu wanafikiwa na huduma hizi kupitia Benki hizi za Umma zinazoendeshwa kwa kodi zao.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Awali ya yote naomba kwa niaba ya wananchi wa Madaba niishukuru sana Serikali pamoja na kutoa milioni 900 imetenga tayari milioni 500 kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Wilaya ya Madaba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile Halmashauri ya Madaba inachangamoto ya wauguzi kwa maana ya wataalam katika eneo la afya na kwa vile Mganga Mkuu sasa tangu amehama ni zaidi ya miezi 3 hatujapata Mganga Mkuu mwingine kwa ajili ya kutoa huduma. Na katika Kituo cha Afya cha Madaba ambacho kinatoa huduma tuna mganga mmoja tu ambaye yuko active. Ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba Madaba inapata Mganga Mkuu na inapata waganga kwa ajili ya kutoa huduma hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa vile katika zahanati hizi mbili ya Mbangamawe na Magingo wananchi wapo tayari kuendelea kutoa ushirikiano wa nguvu kazi na baadhi ya vitendea kazi. Ni lini sasa Serikali itatuhakikishia kwamba hizi fedha ambazo Serikali imekusudia kutupa zitapatikana ili wananchi waendelee kutoa nguvu kazi zao na kuhakikisha zahanati hizi zinakamilika na zinageuka kuwa vituo vya afya, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kipekee naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mhagama pamoja na wananchi wa Jimbo lake na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla. Kama kuna sehemu ambayo wananchi wamekuwa wakijitoa katika kuhakikisha kwamba wanatoa nguvu yao ni pamoja na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza anaulizia suala la mganga ambaye alikuwa amepangiwa na nilikuwa nateta naye kabla sijaja kujibu swali hapa. Kuna mganga alikuwa amepangiwa sasa hivi yapata miezi miwili hajaenda kuripoti naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada tu ya kumaliza shughuli za Bunge leo nitafatilia nijue nini ambacho kimetokea ili nafasi ile kama mganga hajaenda kuripoti basi tumpeleke mganga mwingine kwa ajili ya kwenda kuziba pengo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ameongelea suala zima la upungufu wa watumishi naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo kuna upungufu tunategemea kuajiri hivi karibuni na tutazingatia ikama ili maeneo ambayo yana upungufu mkubwa yaweze kupelekewa waganga.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anaongelea suala zima la wananchi kujitolea, jambo ambalo limekuwa likifanywa ndani ya Mkoa mzima wa Ruvuma na nini jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba pesa zinapelekwa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge maeneo yote ambayo wananchi wanajitoa kama ilivyo katika Mkoa wa Ruvuma, Serikali itakuwa tayari fedha ikipatikana kuwaunga mkono wananchi.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa vile uhaba huu wa walimu kwa sehemu nyingine unachangiwa na kutokuwa na msawazisho sawa wa shule zetu mbalimbali hasa baina ya shule za mijini na vijiji na hivi kusababisha shule za vijiji ziwe na walimu wachache zaidi ukilinganisha na sehemu za miji. Ni lini sasa Serikali itakamilisha mchakato wake wa kuhakikisha kwamba kuna kuwa na msawazisho wa walimu ili uhaba au toshelevu wa walimu ulingane mijini na vijijini?
Mheshimiwa Spika, pili, kwa vile tumeona vijana wengi waliohitimu taaluma ya ualimu bado wapo mtaani kwa muda mrefu sasa na wengine zaidi ya miaka minne/mitano na bado Serikali inawekeza fedha nyingi kwenye kusomesha vijana hawa katika vyuo vyetu vikuu kwa nini sasa Serikali isiangalie utaratibu mpya wa kusomesha vijana wetu kwa kulingana kwa mahitaji ya soko la ajira na mahitaji ya Taifa katika ujumla wake na kuwawezesha vijana wetu waweze kuwekeza zaidi katika ujasiliamali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA W. WAITARA): Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maoni na mtazamo wake, lakini wiki iliyopita nilitoa taarifa kwenye Bunge lako tukufu kwamba tumepeleka fedha katika Halmashauri zote ambazo kazi, moja, nikumalizia maboma ya shule za Msingi lakini pia lingine ni kusawazisha au ku- balance ikama katika shule zetu. Tumeelekeza Wakurugenzi, Walimu na Makatibu Tawala wa Mikoa kwamba wahahakishe kwamba fedha hii inatumika kuwahamisha walimu ili moja, kuangalia kusambaza walimu katika upungufu uliopo katika maeneo ya mjini ili waende maeneo ya pembezoni; lakini la pili kuangalia zile hoja kwamba kuna shule ina mwalimu kike haina mwalimu wa kiume au wakiume haina wakike pia izingatiwe hilo. Kwa hiyo kazi inafanyika tunatarajia kwamba Wakurugenzi na viongozi wa mikoa watasimamia hili na Waheshimiwa Wabunge ni kwa sababu ni sehemu ya mikoa yenu hili ni taarifa rasmi naomba mtusaidie kusimamia.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anasema tufundishe wanafunzi wetu kulingana na mahitaji, juzi Mheshimiwa Waziri wa Nchi alitangaza matokeo ya form four na mojawapo ya kazi iliyofanyika ni kugawanya wanafunzi katika maeneo mbalimbali, sasa hili la kusema tuweke kulingana na idadi, ni kweli kwamba walimu wapo mitaani lakini ukweli kwamba tunahitaji walimu wengi katika sekta zote shule ya msingi na sekondari.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu kila mwanafunzi amelekwa mahali ambapo anahitaji, na tunatarajia kuna shule za Serikali na watu binafsi lakini pia na shughuli binafsi na tunaendelea kuangalia mchakato wa kuhakikisha wanafunzi hawa badala ya kutegemea kuajiriwa na Serikali ambalo ni jambo la kitaifa kwa kweli ni lazima tuanzishe utaratibu wa watu kufanya kazi hata kwa shughuli binafsi yaani isiwe ile knowledge based, iwe ni competent. Kwa hiyo tunalichukua tunafanyia kwa siku za usoni tutaweza kulizingatia, ahsante.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile swali la msingi linalohusu Mbinga Vijijini linafanana kwa kiasi kikubwa na tatizo la Madaba na kwa vile Madaba ilishatengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na kwa vile kwa miaka miwili mfululizo fedha hiyo haijatoka. Ni lini sasa Serikali itapeleka fedha Madaba ili ujenzi wa hospitali ya wilaya uanze?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mhagama, Mbunge wa Madaba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za halmashauri.
Katika kipindi cha miaka mitano sote tumeona kazi kubwa iliyofanyika kwa kujenga hospitali za halmashauri zaidi ya 101 na katika mwaka huu wa fedha, kiasi cha shilingi bilioni 27 zimetengwa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika vituo na hospitali za halmashauri ambazo zitajengwa Jimbo lake la Madaba pia litapewa kipaumbele.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa vile moja katika migogoro mikubwa ya wafugaji na wakulima yapo kwenye Kijiji cha Ngadinda, Halmashauri ya Madaba; na moja ya sababu ni kwamba wafugaji ambao wameambiwa wahame kwenye eneo la hekta 1,800 ambazo zilitolewa na Serikali kwa wakulima hawajahama. Nini kauli ya Serikali kuhusu kuwaondoa hawa wafugaji ambao wamekaa kwenye eneo ambalo lilitolewa kwa ajili ya kilimo? Ni lini wafugaji hawa wataondoka?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni lini Serikali sasa itachukua hatua za makusudi za kuwawezesha wafugaji nchini ili waweze kufanya ufugaji wa kisasa na hivyo kuondoa migogoro ya wafugaji na wakulima?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Mhagama kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ukweli kwamba shamba la Serikali na Ngadida lililoko pale Songea lilikuwa na ekari 6,000 na miaka michache nyuma tuliligawa; 1,800 tukawapa wanakijiji na takribani 4,200 tukabaki nazo Serikali na kugawa vitalu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kusikia kauli ya Serikali. Naomba niseme kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tayari 1,800 tulishazigawa kwa wanakijiji kwa ajili ya shughuli zingine ikiwemo kilimo, sasa iwe ni marufuku kwa wale ambao hawakupewa eneo hilo kufanya shughuli nyingine za kuwaingilia wale wanaokwenda kufanya shughuli za kilimo kule. Na hili ninaielekeza halmashauri ya wilaya kulisimamia. Kinyume na hapo ndiyo linakwenda kusababisha migogoro isiyo ya lazima ya wafugaji kuweza kuingia katika maeneo ya wakulima.
Mheshimiwa Spika, mkakati wetu kwa jambo hili la pili la Serikali kuwawezesha wafugaji; hivi sasa tunaendelea na mkakati wetu wa kugawa vitalu katika maeneo yetu yote tunayoyamiliki; na vitalu hivi sasa tunakwenda kuviboresha. Tumetoa maelekezo kwa watendaji wetu kuongeza muda wa uwekezaji katika vitalu ili anayepewa kitalu aweze kuwa na muda wa kutosha na asiwe na wasiwasi juu ya uwekezaji wake.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo tumeielekeza Bodi ya Nyama kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha juu ya unenepeshaji, na hivi sasa tunaunganisha na Benki yetu ya Kilimo iliyo tayari kuwapa mikopo watu wote waliojiweka katika utaratibu mzuri wa unenepeshaji. Na tayari tumeshatoa maelekezo kwa viwanda vinavyochakata nyama kutoa mikataba ya biashara kwa wanenepeshaji wote nchini ili waweze kutumia fursa hiyo ya kuweza kuongeza uchumi wa taifa letu vizuri.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, nilikuwa na swali la nyongeza.
Kwa vile migogoro hii kwa sehemu kubwa inachangiwa sana na kutokamilika kwa utengenezaji wa mipango bora ya matumizi ya ardhi katika Mikoa, Wilaya na Vijiji vyetu. Ni lini basi Serikali itakamilisha upimaji na utekelezaji wa sera ya kuwa na mipango ya kuwa na matumizi bora kwa kila Kijiji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Mhagama, Mbunge wa Madaba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge alikuwa anauliza kwamba moja ya sababu kubwa ya hii migogoro ni sisi ama Serikali kushindwa kwa wakati kukamilisha hii mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimwambie tu jambo moja kwamba ili Serikali iweze kupima hizo ardhi katika maeneo mengine yote. Ni lazima ngazi za Halmashauri zote nchini zipange bajeti ili watu/sisi kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi tuje tupime hayo maeneo ili kuhakikisha kabisa tunaondoa hiyo kero iliyopo.
Kwa hiyo, nizitake Halmashauri zote nchini kuhakikisha katika bajeti zao wawe wanatenga fedha kwa ajili ya upimaji wa ardhi ili kuhakikisha kwamba hii migogoro tunaiondoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu matumizi ya ardhi katika ngazi za vijiji nafikiri ni kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba tutaendelea kuhamasisha ngazi za Halmashauri kuhakikisha wote wanafuata sheria lakini tutaendelea kutenga fedha na kuainisha maeneo yote ili kuondoa hii migogoro ambayo inaendelea kujitokeza kila wakati. Kwa sababu hilo ndiyo lengo la Serikali kuhakikisha kwamba migogoro hii ya mipaka pamoja na maeneo inatatuliwa kabisa. Ahsante.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Mkoa wa Ruvuma umejaaliwa kuwa na mito mingi mikubwa, mito hiyo ipo pia katika eneo la Jimbo la Madaba moja katika mito mikubwa ni mto huo Ruhuhu, lakini kuna Mto Hanga.
Nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha maeneo hayo yote yanayofaa kwa umwagiliaji tunakuwa na miundombinu mikubwa na rafiki itakayoboresha kilimo cha mpunga na kilimo cha umwagiliaji katika ujumla wake maeneo ya Mkoa wetu wa Ruvuma?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mhagama kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali sasa hivi tunachokifanya ni kufanya review ya master plan yote ya umwagiliaji na kubadili mfumo wa Tume yetu ya Umwagiliaji ili kuweza kupata tija katika miradi yetu ya umwagiliaji na kuwa na gharama ambazo ni affordable na kuna value for money, hili ni jambo la kwanza.
La pili tunachokifanya sasa hivi tutatambua maeneo ya kimkakati ambayo Serikali itaenda kuwekeza yenyewe 100% na maeneo mengine ya umwagiliaji tuta-encourage sekta binafsi kuweza kufanya hayo maeneo na kuwekeza sekta binafsi kwa makubaliano ya long term ili kupunguza mzigo. Kwasababu siyo lazima kila sehemu ndiyo Serikali iweze kujenga yenyewe. Kwa hiyo, tunafanya jitihada za namna hiyo kuweza kuzi-cruster hii miradi ya umwagiliaji katika maeneo ambayo itawekeza sekta binafsi na maeneo ambayo Serikali itakwenda kuwekeza kwenye miradi mikubwa ambayo sekta binafsi haiwezi kuwekeza.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa vile uzalishaji wa chakula nchini kwa sehemu kubwa unawategemea wakulima wadogo ambao kipato chao kifedha ni kidogo kuweza kumudu kununua pembejeo za kilimo kwa maana ya mbolea na mbegu; na kwa vile kwa sehemu kubwa bei ya mbolea imeongezeka sana mwaka huu kutokana na ugonjwa wa UVIKO – 19 katika nchi ambazo zinazalisha mbolea: Ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba nchi yetu inajitosheleza kwenye uzalishaji wa pembejeo muhimu kama mbolea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba mbolea na mbegu zinapata ruzuku ili wakulima wadogo waweze kuzalisha kwa tija? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mhagama, Mbunge wa Madaba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la ruzuku, nataka tu nilihakikishie tena Bunge lako Tukufu kwamba maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kutengeneza legal framework ambayo itatusaidia kama Serikali kutoa ruzuku kwenye pembejeo ambazo ruzuku hizo zitakwenda ku-benefit wakulima. Nataka nilihakikishie Bunge lako Tukufu, tuko kwenye hatua za mwisho ku-design Stabilization Fund ambayo itahusika na masuala ya ruzuku na pale ambapo bei za mazao zinaanguka, Serikali inaweza kufanya intervention ili kuweza kuwalinda wakulima wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ni ahadi ya Serikali na sisi tutaifanya kuanzia mwaka ujao wa fedha. Kuhusu suala la kujitosheleza pembejeo za kilimo kwa maana ya mbolea na viuatilifu, sasa hivi kama nchi sisi mahitaji yetu hayazidi tani 600,000 za mbolea. Tunacho Kiwanda cha INTRACOM ambacho kimewekeza hapa Dodoma kina capacity ya tani 600,000. Wenzetu wa Wizara ya Madini wametusaidia kutoa leseni kwa ajili ya upatikanaji wa phosphate na jana walikuwa Mkoa wa Manyara kulipa fidia wananchi waliozunguka eneo hilo. Wamelipa zaidi ya shilingi bilioni moja. Kiwanda hiki kitaanza trial mwezi wa Saba kufika mwaka kesho 2023 tutakuwa tumefika 100 percent capacity ya uzalishaji wa tani 600,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha Minjingu tumewasaidia wamepata financing zaidi ya Dola milioni 20 ili waweze ku-expand capacity yao wafike tani 120,000. Nataka niwahakikishie ni drive ya Serikali kuvisaidia viwanda vya ndani viweze kufanya mambo mawili; moja kuzalisha organo-chemical fertilizer na pili, kufanya blending ili tuweze ku-blend chemical fertilizer wenyewe ndani ya nchi kwa mahitaji yetu ya nchi na tuweze ku-export. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mbegu, sasa hivi tumeanza ku-review makampuni binafsi kuyaruhusu kuanza kuzalisha mbegu ili siku moja Tanzania tuache kuwa importer wa mbegu, tuanze kuweza ku-export mbegu kwenda nje kwa mahitaji yetu. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninalo swali moja la nyongeza.
Kama Serikali inaamini kuwa Ushirika ndiyo njia bora ya kufikisha huduma za kilimo kwa wakulima wadogo wadogo, ikiwemo huduma za Stakabadhi za Ghala na pembejeo hasa mbolea. Je, kwa nini Serikali katika msimu huu haikuona haja ya kutumia Vyama vya Ushirika ili kufikisha mbolea za ruzuku kwa wakulima kwa njia ambayo yenye tija zaidi?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mhagama, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza, siyo kwamba tumeviacha vyama vya ushirika, sasa hivi Bodi ya Mazao Mchanganyiko ndiyo inachukuwa mbolea kwa wingi na kukabidhi Vyama vya Ushirika. Sasa hivi tumeanza utaratibu wa kutambua maghala ya Vyama vya Ushirika na Chama cha Ushirika cha Tumbaku cha Mkoa wa Ruvuma kimepewa jukumu la kuanza kupeleka maeneo ambayo sekta binafsi imeshindwa kuyapeleka.
Mheshimiwa Spika, tunaendelea kufanya hivyo, Mkoa wa Rukwa tutashirikiana na Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Rukwa kwa ajili ya wakulima wa mahindi, Kanda ya Ziwa tunashirikiana na Vyama vya Ushirika vya zao la pamba kwa ajili ya kuongeza usambazaji wa mbolea ya ruzuku.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaishukuru Serikali kwa majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imepita miaka minne tangu Serikali Kuu ilipobaini kwamba andiko la mradi wa Stendi ya Madaba halikukidhi vigezo. Ni hatua gani za haraka ambazo Serikali Kuu ilizichukua wakati huo ili kuhakikisha kwamba stendi hii inajengwa na inawanufaisha wananchi wa Madaba ili kuongeza mapato kwa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kama upembuzi yakinifu unakusudiwa kufanywa kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023, ni lini sasa kwa uhakika stendi ya Madaba itajengwa? (Makofi)
NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge aliuliza tu kwamba andiko la awali ambalo limechukua takribani miaka minne na alichotaka kufahamu ni hatua gani ambazo Serikali ilizichukua baada ya hili andiko kukataliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ambacho tulikifanya kwa kutumia wataalam wetu tulilirudisha lile andiko katika Halmashauri ya Madaba na baada ya kufanya hivyo waliainishiwa maeneo ya kufanya marekebisho. Kwa hiyo, jukumu la kuandika andiko ni la Halmashauri ya Madaba na ndio maana hata sasa hivi tumewarejea tena ili waandike upya haraka iwezekanavyo ili sisi tutafute fedha hii stendi iweze kukamilika. Kwa hiyo, mara watakapokuwa wamekamilisha kwa wakati basi na sisi tutatafuta fedha ili tuweze kujenga stendi hiyo kwa manufaa ya wananchi wa Madaba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu upembuzi yakinifu mara utakapokamilika ameuliza lini, ni kwamba watakavyomaliza andiko na mimi naamini tutajiridhisha kwamba kama andiko linakidhi vigezo likishakamilishwa mara baada tutakapopata fedha tutaanza mara moja kuhakikisha mradi ule unaanza. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante, wananchi wa Jimbo la Madaba, na wananchi wa Ludewa wamesubiri kwa hamu sana ujenzi wa Barabara ya Mababa – Mkiu – Ludewa kwa kiwango cha lami na hii imekuwa ahadi ya kudumu ya Serikali. Ni lini sasa Serikali itatekeleza azma hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFRY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Mhagama, Mbunge wa Madaba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mkiu kwenda Madaba ni barabara ambayo inaanzia Itoni, Lusitu, Mkiu kwenda Madaba ambayo ndiyo inaenda kwenye madini ya chum ana makaa ya mawe. Usanifu ulishakamilika kwa kipande cha Mkiu kwenda Luhuu hadi Madaba, Serikali inaendelea kutafuta fedha sasa kuianza kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo itajengwa kwa sababu pia ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu ya Tanzania, Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Ifinga kipo kilometa 48 kutoka Kijiji cha Wino ndani ya Halmashauri ya Madaba. Kijiji hiki kiliahidiwa umeme tangu miaka Mitatu iliyopita na mpaka sasa hakuna utekelezaji.
Je, ni lini wananchi wa Ifinga watanufaika na kodi za Watanzania kwa kupata umeme wa uhakika?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Mhagama Mbunge wa Madaba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hiki basi tuonane pamoja na wataalam wetu wa REA tuone iwapo kuna changamoto mahsusi ambazo zimepelekea hata Wakandarasi kutokuwepo site katika vijiji ambavyo imani yetu ni kwamba vijiji vyote nchini vimejumuishwa katika REA awamu ya tatu mzunguko wa pili.
MHE. DKT. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara ya Makambako - Songea hasa eneo la Madaba kuanzia Igewisinga mpaka Mtiangimbole limebomoka vibaya sana kiasi cha kuhatarisha usalama wa watumiaji. Je, ni lini sasa Serikali itaijenga hii barabara kwa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nimemuelewa vizuri hii ni barabara kubwa ya kutoka Makambako kwenda Songea, hii barabara ipo kwenye mpango wa kukarabatiwa na World Bank, sasa hivi tutaanzia Lutukila kwenda Songea ikiwa ni pamoja na bypass ya Songea Mjini, wakati huo sasa inatafutwa fedha kuanzia Makambako hadi Lutukila.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ipo mifuko ya halmashauri ambayo pia inatoa huduma kwenye vikundi vya wajasiriamali na mfuko huu wa maendeleo wa jimbo umeonesha ugumu wa utekelezaji kutokana na masharti yaliyowekwa, kwa nini sasa Serikali isione haja ya kuleta hii sheria ili iboreshwe ili kukidhi mahitaji ya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu kama ambavyo wananchi wamekusudia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimesema kwenye majibu yangu ya msingi, kwamba mfuko huu upo kisheria na ulianzishwa kisheria. Nachukua maoni ya Mheshimiwa Mhagama na tutaona ni namna gani tunakusanya maoni pia kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wengine humu ndani kabla Serikali haijaanza mchakato wa kubadili sheria hii.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara hii kwa kipindi cha miaka mitatu imetumia zaidi ya Bilioni Moja kuijenga na Serikali imeashaweza kutoa fedha hizo, hii ni dhahiri kwamba Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la barabara hii. Haa hivyo, barabara hii bado kuna kipande cha kilomita 18 kutoka Ifinga Mjini kuelekea Kitongoji cha Muungano na Ruhuji kilometa 18.
Je, ni lini sasa Serikali itaifungua barabara hii kuelekea eneo hilo la Ruhuji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba, kama ifutavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inafanyakazi kubwa na kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge ameomba ongezeko la eneo la barabara la kilomita 18 kutoka Ifinga kwenda kwenye Kitongoji cha Muungano, basi naawagiza TARURA Mkoa wa Ruvuma pamoja na Halmashauri ya Madaba waende wakapitie barabara hiyo na wafanye tathmini na baada ya hapo watuletee fedha ili tuweze kui-extend. Ahsante sana.
MHE. DKT. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile Serikali imeona kwa uhakika kabisa uwezo wa TARURA wa kuhudumia barabara ya Wino - Ifinga yenye urefu wa kilometa 48 ni mdogo. Ni lini sasa Serikali itakubali maombi ya Halmashauri ya Madaba kupitia mkoa kuijenga Barabara ya Wino - Ifinga kwa kupitia Mfuko wa TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara ambazo zinakuwa na sifa na zinakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi tunafanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tayari barabara yake imeshakuja ofisini kwetu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba timu ya wataalamu itakwenda kuhakiki hiyo barabara na kama itakidhi vigezo, Wizara ya Ujenzi kupitia Waziri wa Ujenzi hatasita kuipandisha barabara hiyo ili iweze kuhudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
MHE. DKT. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile Serikali imeona kwa uhakika kabisa uwezo wa TARURA wa kuhudumia barabara ya Wino - Ifinga yenye urefu wa kilometa 48 ni mdogo. Ni lini sasa Serikali itakubali maombi ya Halmashauri ya Madaba kupitia mkoa kuijenga Barabara ya Wino - Ifinga kwa kupitia Mfuko wa TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara ambazo zinakuwa na sifa na zinakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi tunafanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tayari barabara yake imeshakuja ofisini kwetu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba timu ya wataalamu itakwenda kuhakiki hiyo barabara na kama itakidhi vigezo, Wizara ya Ujenzi kupitia Waziri wa Ujenzi hatasita kuipandisha barabara hiyo ili iweze kuhudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).