Supplementary Questions from Hon. Anthony Peter Mavunde (5 total)
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, changamoto katika Jimbo la Singida Magharibi inafanana na changamoto inayowakumba wananchi wangu wa Tihanga, Makutupora, Mchemwa, Nzansa na Gawale; na kwa kuwa kumekuwa na changamoto upatikanaji wa ndege ya kunyunyiza kwa wakati.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza ndege ya kunyunyiza kwa ajili ya udhibiti wa ndege na nzige, ili kuweza kuyafikia maeneo mengi kwa wingi na kwa muda mfupi zaidi kuliko ilivyo hivi sasa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anthony Mavunde, Mbunge wa Dodoma Jiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sasa hivi kumekuwa na athari kubwa ambayo inatokana na ndege waharibifu, lakini vilevile wadudu na kama tulivyokuwa safari hii tumekuwa tukipambana mpaka sasa hivi na nzige na Wizara na Serikali kwa ujumla katika bajeti ya mwaka kesho mtaona tunafufua uwepo wa kilimo anga.
Mheshimiwa Naibu Spika, na katika bajeti yetu tukipitishiwa katika Bunge hili tutakuwa tumetenga fedha kwa ajili ya kutumia teknolojia za drones pale ambapo tutahitaji kutumia drones, lakini sasa hivi hatua ya kwanza tuliyochukua, pamoja na kutumia ndege na helikopta tulizonazo ambazo tunazipata kutoka kwenye mashirika mbalimbali ya kimataifa ambayo sisi ni wanachama, lakini kama Serikali tunafanya mazungumzo na taasisi za kimataifa kama World Bank na taasisi nyingine ili tuwe na uwezo wa kutosha na tuwe na ndege zetu za kutosha tuweze kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao.
Kwa hiyo, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge mtaona kwenye bajeti inayokuja katika Bunge hili, tutakuwa tumetenga fedha yaku-strengthern Kituo cha Kilimo Anga kwa kuwa na vitendea kazi wenyewe badala ya kutegemea vitendeakazi ambavyo tunavipata katika taasisi mbalimbali za kimataifa.
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii ya maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo ametusaidia sana kuchochea zao hili la zabibu, na kupitia yeye wakulima wamehamasika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi sasa ninavyozungumza zabibu zimejaa katika mashamba ya wakulima pale Hombolo, Matumbulu na Mpunguzi na hawana sehemu ya kupeleka. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha kwamba zao hilo la zabibu linapata soko la uhakika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ipo tayari sasa kuwapeleka wataalamu wetu Maafisa Ugani waende kujifunza nje ya nchi namna ambavyo zabibu inalimwa ili kuongeza tija kwa mkulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anthony Mavunde Mbunge wa Dodoma Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, cha kwanza hatua tunayochukua sasa hivi, kama Wizara tunaanza utaratibu wa kuweka restriction ya ku-import mchuzi kutoka nje kwa kampuni zinayotumia zabibu ndani ya nchi kabla hawajanunua zabibu yote inayozalishwa ndani ya nchi. Kwa hiyo tutatengeneza utaratibu wa quarter system kwamba aneye-import mchuzi lazima tuone contract zake na wakulima wa ndani; kwamba amenunua zabibu yote na imekuwa exhausted zabibu ya ndani.
Mheshimiwa Spika, kwahiyo tutatumia model kama tunayotumia, ya sukari, ili tuhakikishe kwamba zabibu yetu kwanza inapata soko kama inatumika kwenye wine ama inatumika kwenye vinywaji vikali ili kuhakikisha wakulima zabibu yao yote ina nunuliwa kabla ya kuruhusu kibali cha kuingiza mchuzi kutoka nje. Kwa hiyo huu ni utaratibu na tutaanza nao hivi sasa. Ndani ya siku mbili au tatu zijazo tutakutana na kampuni zote tatu kubwa ambazo ni off taker wa mazao ya zabibu katika nchi ili kutengeneza hii program na kuhakikisha kwamba jambo hili tunalisimamia.
Mheshimiwa Spika, la pili, tunahakikisha sasa kwenda kwenye hatua ya pili. Kwamba badala ya wakulima wa zabibu kuuza tunda waanze kuuza mchuzi. Kwenye hili tumeanza kuongea na wenzetu wa TEMDO Pamoja na wa SIDO ili tuanze kutengeneza centres ambazo wakulima watapeleka zabibu zao. Kama tulivyokwenda pamoja tukiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu tukaona ile pilot ya kile chama cha ushirika cha WAMAKU kilichopo barabara ya Iringa ambacho kinachakata mchuzi na kuuza mchuzi badala ya kuuza zabibu, kwa hiyo hili ni jambo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, kuhusu wataalamu sasa hivi wizara tunatambua Maafisa Ugani sita ambao tutawapeleka katika nchi ya South Afrika ili waweze kujifunza; na tunashirikiana na sekta binafsi kwa ajili ya ku-train watu wetu hawa. Na mtaalamu mmoja tuliyenaye nchini, ambaye ni mbobezi ambaye anastaafu hivi karibuni tunafanya mchakato na wenzetu ndani ya Serikali angalau apate extension baada ya kustaafu wakati tuna-train hao wataalamu sita nje ya nchi ili wakirudi tuwe tuna wataalamu wa kutosha wa zabibu.
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa taasisi za SIDO na TEMDO zilizopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara zimeonesha ufanisi mkubwa kwenye kutengeneza mtambo wa destemming na crushing ya zabibu ambayo inapelekea kutengeneza mchuzi wa zabibu ambao umeonekana una tija kubwa sana kwa wakulima. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuziwezesha taasisi hizi mbili ili zitengeneze mashine nyingi zaidi za kuchakata mchuzi wa zabibu ili wakulima waondokane na kuuza zabibu na badala yake wauze mchuzi wa zabibu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anthony Mavunde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali kupitia taasisi za SIDO na TEMDO tumekuwa tukiwawezesha ili waweze kubuni na kutengeneza teknolojia mbalimbali ambazo zinachakata mazao ya kilimo ikiwemo zao la zabibu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali sasa imeamua kwa dhati, kwanza kuziwezesha taasisi hizi kifedha, lakini pia na kuongeza uwezo kwa maana ya Rasilimali watu ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha 2020/2021, tayari tumeshawezesha SIDO kama nilivyosema zaidi ya bilioni nne lakini pia TEMDO zaidi ya milioni mia tano ili waweze kusanifu na kutengeneza teknolojia mbalimbali ikiwemo za kuchakata zabibu.
Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyosema kwa wengine kwamba kwa wale ambao wana hitaji teknolojia maalum kulingana na mahitaji ya mazao yao kama hili la zabibu, basi naomba nimkaribishe Mheshimiwa ndugu yangu Anthony Mavunde, katika ofisi zetu za SIDO ili tuweze kuona namna ya kukamilisha mahitaji yake ambayo yatafaa kwa ajili ya kukamua zabibu.
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ubovu wa Barabara ya Ihumwa – Hombolo unaleta adha kubwa kwa wananchi wa Chahwa, Ipala na Hombolo yenyewe na hivyo kuongeza gharama za usafiri: Je, ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kutekeleza mpango wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kuanzia Ihumwa mpaka Hombolo ili kuwaondolea adha wananchi hawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kujenga barabara zote kwa kiwango cha lami, lakini suala hili linafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Barabara ya Ihumwa – Hombolo hadi Mayamaya yenye urefu wa takribani kama kilometa 7.3 ni ya kiwango cha changarawe na kama fedha itapatikana, itajengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba muda wote inapitika ili wananchi wa eneo hilo ikiwa ni pamoja na wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo cha Hombolo wasiweze kupata taabu. Kwa hiyo, tumetenga fedha kwa matengenezo ya muda na kuhakikisha kwamba maeneo yote yale korofi yanatengenezwa ili kusiwe na changamoto ya usafiri na usafirishaji kwa barabara hiyo. Ahsante.
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa mradi huu unaligusa pia na Jiji la Dodoma na kwa kuwa wataalam walishakaa na kuibua miradi hii kuanzia ngazi ya mtaa, kata mpaka Ofisi ya Rais, TAMISEMI: -
Je, ni lini sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Wizara ya Fedha mtakaa pamoja mkwamue vikwazo vilivyopo ili wananchi waweze kunufaika na huu mradi? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde kwa majibu mazuri, pia namshukuru Mheshimiwa Anthony Mavunde na mleta swali, mtani wangu Mheshimiwa Mabula kwa swali zuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, tunatambua kwamba mradi wa TACTIC ni mradi wa kimkakati katika Halmashauri za Majiji na Miji 45. Serikali ya Awamu ya Sita kama alivyosema Naibu Waziri, tumeweka mradi huu kuwa ndiyo mradi wetu wa kielelezo katika kujenga miundombinu ya barabara, masoko pamoja na madampo ya taka katika miji 45.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la Mheshimiwa Anthony Mavunde ni lini TAMISEMI tutakaa na Wizara ya Fedha? Ndiyo maana nilitaka kusimama. Jumatatu ya tarehe 10 Mei, 2021 nilikaa mimi pamoja na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mwigulu kwenye Ofisi ya Wizara ya Fedha pamoja na wataalam wetu na tukakubaliana kwamba majadiliano yamekamilika, sasa tunapeleka World Bank kwa ajili ya taratibu za kusaini mkataba wa kuanza ujenzi wa mradi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu mradi huu ni muhimu sana kwa Jiji la Mbeya, nafahamu mradi huu ni muhimu sana kwa Jiji la Arusha, nafahamu mradi hii ni muhimu sana kwa Jiji la Dodoma, pia ni muhimu sana kwa Jiji la Mwanza. Na mimi Tanga Jiji mradi huu kwangu ndiyo utanipa kura za kurudi Bungeni mwaka 2025.
Kwa hiyo, kutopatikana kwa TACTIC maana yake sitarudi Bungeni 2025. Kwa hiyo, naubeba kama mradi wangu, lakini na kwa Majiji mengine yote 45 tutahakikisha tunaanza utekelezaji mara moja. Ahsante sana. (Makofi)