Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Tulia Ackson (11 total)

MHE. DKT. TULIA ACKSON: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo hili la Rungwe ni kubwa sana. Hiyo ahadi iliyotolewa hapo na Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu Kituo cha Mpuguso na Isongole, ndiyo, wadau wameendelea kuchangia lakini sijasikia namna ambavyo Serikali imejipanga. Kwa sababu amesema shilingi milioni 100 zitatoka katika mapato ya ndani, hayo yamekuwepo kila wakati, je, Serikali imejipangaje? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Mbunge wa Kuteuliwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika jibu la msingi nimeeleza kwamba halmashauri ya wilaya imetenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa OPD katika Kituo cha Afya cha Mpuguso ambacho wameanza wenyewe kujenga kwa kushirikiana na wananchi. Nimetoa ahadi kwamba Serikali katika mwaka 2018/2019 itahakikisha kwamba vituo hivi viwili; cha Mpuguso na Isongole vinakamilishwa kwa utaratibu uleule ambao tumeutekeleza mwaka huu wa fedha. Kwa hiyo, kwa Rungwe, tutakuwa na vituo hivyo viwili kwa kuanzia. Naomba sana Mheshimiwa Mbunge tuwe na mawasiliano ya karibu, inapofika mwezi wa Agosti au Septemba kusudi tuhakikishe kwamba vituo hivi viwili vinapatiwa fedha za ujenzi ili viweze kukamilika 2018/ 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapo hapo tuendelee kuwa na mawasiliano ya karibu kwa sababu Jimbo la Rungwe ni kubwa sana ili kusudi tuangalie na maeneo mengine.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, nimeletewa ujumbe hapa. Siyo utaratibu, utusaidie kuzungumza lile katazo lako, wale waliokuwa wamenyang’anywa majenereta na taa zao za solar watarejeshewa ama utaratibu utakuwaje?

Majibu Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwamba nimeruhusu matumizi hayo ya generator, taa za solar na wananchi wote ambao wameshikiwa zana hizo, warudishiwe bila masharti yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nilikuwa nataka kusisitiza katika hili jambo la kwamba suala la ulinzi wa rasilimali zetu hizi ni suala ambalo linahitaji kuungwa mkono na wananchi wote. Rasilimali hizi tulizonazo hapa nchini asilimia 37 ni maji, lakini mazao yetu ya uvuvi mengi yameharibiwa sana na suala la uvuvi haramu. Kwa hiyo, wananchi wote wanawajibika kuziangalia hizi sheria na kuziheshimu. Kwa sababu hata huyo Mama Ntilie anajua samaki wasioruhusiwa. Tukitengeneza mtandao huu wa huyu mama mdogo anaweza kuingia kwenye soko na samaki wasioruhusiwa, tutatengeneza mtandao ambao utawezesha kuwepo kwa soko hili.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, nawaomba sana, katika kipindi hiki kigumu cha
kubadilisha watu kuwaondoa kwenye uvuvi haramu, mtuvumilie. Kwa sababu hata huyo mama mjane tunayemhurumia leo, kesho hatapata samaki wa kuuza. Hata mama mjane, mtoto yatima, watoto hawaendi shule; hawataenda shule kabisa kwa sababu samaki hawatakuwepo majini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika kipindi hiki ambacho tunafanya transformation hizi kubwa, nakuomba sana na bunge lako Tukufu mtuvumilie kwa nia nje kwa sababu hatua hizi zote tunazochukua ni kwa ajili ya
Taifa letu na hatima ya uchumi wa nchi hii.
MHE. DKT. TULIA ACKSON: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, changamoto zilizopo Wilaya Mbarali zipo pia Wilaya ya Rungwe hususani kwenye eneo la Bonde la Mwakaleli lakini pia Kata ya Ikuti. Maeneo haya yanazungukwa na mito lakini hayana miundombinu ya kupelekea wananchi maji. Nataka kujua ni lini Serikali itapekeza miradi ili wananchi waweze kupata maji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, changamoto hizi pia zipo kwenye kata mbalimbali ya Mbeya Jiji. Baadhi ya kata hizo zenye changamoto ni pamoja na Kata ya Mwasekwa, Mtaa wa Ilembo na Mengo; Kata ya Iganjo, Mtaa Mayombo na Rumbila; Kata ya Iduda, Mtaa wa Muhala; Kata ya Uyolem, Mtaa wa Hasanga; Kata ya Msalaga, Mtaa wa Ntundu na Itezi Mashariki; Kata Iwambi, Mtaa Mayombo na Lumbila, Itagano kwenye mtaa mingi, Itenda baadhi ya mitaa. Nataka kujua ni lini Serikali itapeleka maji kwa wananchi Kata hizi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda tutambue kwamba maji ni uhai. Nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Spika kwa kutetea uhai wa wananchi wa Mbeya. Kama Wizara ya Maji jukumu letu ni kuhakikisha Watanzania wakiwemo wananchi wa Mbeya wanapata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu la Bonde la Mwakaleli tuna mradi pale wa zaidi ya shilingi bilioni 6 ambao utaweza kunufaisha wananchi wa Kata ya Masebe pamoja na Suma. Kwa Kata ya Ikuti katika Jimbo lile la Rungwe, tunamuagiza Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Rungwe afanye usanifu haraka ili wananchi wale waweze kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la Jiji la Mbeya, uzalishaji wa Mamlaka ya Maji ya Mbeya ni lita milioni 48, 45 kwa siku. Mkakati wa muda mfupi ni kuhakisha tunatumia miundombinu ya sasa iliyopo ili wananchi wa Iwambi, Iganzo, Iduda, Itende, Uyole na Isesya nao wanapata maji. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Naibu Spika hata maeneo yenye miinuko kwa maana Mwansekwa pamoja na Itagano nao tutawapelekea maji kwa sababu sisi siyo Wizara ya ukame. Kwa hiyo, nataka nimhakikshie Mheshimiwa Naibu Spika sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kwa wananchi wa Jiji la Mbeya kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza.
MHE. DKT. TULIA ACKSON: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, yanayoonesha kwamba sasa Vijiji vya Ibungila na Lubiga vitapata maji kupitia mradi huu, upo mradi wa Masoko Group ambao umesuasua kwa muda mrefu, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri atuambie ni lini mradi huu utakamilika ili wananchi wa vijiji vya Kata ya Masoko waweze kupata maji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, uchakavu wa miundombinu katika Kata mbalimbali za Mbeya Jiji hususan Kata ya Ilomba, Mtaa wa Hayanga – Ituha, Tonya na Ihanda, Kata ya Iganzo Mtaa wa Igodima na Mwambenja, Kata ya Iyunga Mtaa wa Sistila, Kata ya Ghana Mtaa wa Magharibi na Mashariki, Iganjo Mtaa wa Iganga na Igawilo Mtaa wa Sokoni na Chemi: Ni lini Kata hizi zitapelekewa miradi ili ziweze kupata maji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, Dkt. Tulia kwa kazi nzuri sana anayoifanya na katika kuhakikisha anawatetea wananchi waweze kupata maji. Kubwa sana ni kuhusu suala zima la kusuasua kwa mradi wa maji wa Masoko Group.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge, nilifanya ziara katika eneo lile la Masoko Group na tukaona usuaji wa mradi ule, tukaagiza timu ya Wizara ili iweze kufika na kuongeza nguvu katika kuhakikisha mradi ule unakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Naibu Katibu Mkuu Engineer Kalebelo, alifika na timu ya Wizara pale na wakazungumza na Mkandarasi na wakampa mikakati mpaka sasa asilimia 60 ya mradi umeshakamilika na wananchi wa Mpera gwasi na Nsanga sasa hivi wanapata maji safi na salama na ya kutosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Wizara ya Maji tutahakikisha tunausimamia mradi ule kwa dhati kabisa ili uweze kukamilika na vijiji takribani 15 vilivyopangwa kunufaika, viweze kunufaika na mradi wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, Mheshimiwa Mbunge hii ni wiki ya pili ananiulizia swali la maji katika Jiji la Mbeya. Nataka nikuhakikishie, ukimwona mtu mzima analia, ujue kuna jambo. Hivyo, katika wiki ya kwanza tuna maswali mawili katika Jiji la Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, nipo tayari sasa kukutana na wataalam wetu wa Jiji la Mbeya kwa maana ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Jiji la Mbeya ili tujipange ni namna gani tunaweza tukapeleka maji kwa haraka katika maeneo ambayo ameyasema ya Ilomba, Iganzo, Iyumba, Ghana na Iganjwa.
MHE. DKT. TULIA ACKSON: Mheshimiwa Spika, nakushuru kwa fursa pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza Kata ya Lupepo haina umeme kabisa na hivyo shule ya Sekondari Lupepo haina huduma hiyo na pia zahanati ya Lupepo watu wanajifungulia gizani, ni lini kwenye Kata hii tutaletewa umeme wa REA? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri alipokuja Jiji la Mbeya alitoa ahadi kwa Kata ya Usalaga na Kata ya Iduda kwamba wananchi wa maeneo haya watawekewa umeme kwa shilingi 27,000. Lakini kuna Kata zingine za Jiji la Mbeya ambazo pia hazina umeme na ningependa kusikia msimamo wa Serikali kuhusu bei ya umeme kwenye kata hizi, na kata hizi ni Kata ya Itende, Kata ya Iziwa, Kata ya Nsoho, Kata ya Iwambi, Kata ya Mwasanga, Kata ya Itezi, Kata ya Mwansekwa, Kata ya Nsalaga na Kata ya Idunda na Kata ya Itagala? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika swali la msingi la msingi la Mheshimiwa Naibu Spika kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge wa Rungwe.

Mheshimiwa Spika, napenda nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Naibu Spika kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge wa Rungwe kama ifuatavyo;-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli kabisa katika shule ya sekondari katika Kata la Lupepo pamoja na kituo cha afya havijapatiwa umeme, lakini nilipotembelea Rungwe niliwaomba sana Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Halmashauri waweze kulipia ili shule pamoja na zahanati zipelekewe umeme. Niombe tu Mkurugenzi wakandarasi wetu wako site na wamemfuatilia mpaka wiki iliyopita alipe ili shule ya sekondari na zahanati zote zipatiwe umeme ikiwezekano wiki ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kweli nilitembelea Mbeya Mjini na maeneo mengine na katika maeneo ambayo nilitembelea nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Spika kwa niaba ya Mbunge na Wabunge wengine wa Mbeya kwa kufuatilia ipasavyo sana katika kupeleka umeme katika vijiji vya Mbeya Mjini.

Mheshimiwa Spika, nilipotembea Mbeya Mjini kwanza aliomba maeneo saba yapelekewe umeme ikiwemo eneo la Kitunda, Msalaga na maeneo mengine yote yameshapelekewa umeme nakupongeza Mheshimiwa Naibu Spika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ameendelea kuomba maeneo mengine14 katika Jiji la Mbeya ili nayo yapelekewe umeme kwa shilingi 27,000, tumeanza kuyapelekea kuanzia mwezi huu Kata zote za Nsalaga mpaka Relini zitapelekewa umeme wa 27,000, nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Spika. (Makofi/ vigelegele)
SPIKA: Ahsante sana. Waheshimiwa Wabunge, tukiwa hapo kwenye Ujenzi na Uchukuzi, nilikuwa nimesema habari ya TARURA, naona Naibu Mawaziri wameshaingia humu ndani, Naibu Waziri anayehusika na TARURA aseme jambo kwa sababu huko tunapigiwa sana simu barabara zimekatika kwenye majimbo.

Sasa kila Mbunge hapa hawezi kupata nafasi ya kueleza, sasa toeni maelekezo ya jumla kwa TARURA nchi nzima ili barabara zinazosimamiwa na TARURA ambazo zimekatika na hazipitiki wao waende wakazitazame ili wananchi waweze kupata huduma ya barabara. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu mwongozo ama maelekezo ambayo Ofisi yako imeyatoa kwetu Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nimelipata suala hili vizuri, nawaagiza Mameneja wote wa Mikoa wa TARURA pamoja na halmashauri zote nchini kuanzia siku ya kesho waende katika maeneo yote nchi nzima kwenda kufanya tathmini haraka iwezekanavyo na kutupatia Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia kitengo chetu cha TARURA ili angalau tuweze kutoa fedha katika zile fedha zetu za dharura. Katika yale maeneo ambayo bajeti yake ipo maana yake tutapeleka zile fedha kuhakikisha zinakwenda kufanya hiyo kazi ambayo imekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie tu kabisa hili agizo ambalo tumelitoa litatekelezeka na hiyo taarifa ikishafika tutaileta katika Bunge lako Tukufu kabla ya Bunge hili kwisha. Ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, mradi wa maji Kiwira unaanza lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu kabisa naomba kujibu swali hili kwa heshima kubwa.

Mheshimiwa Spika, mradi umeshaanza kutekelezwa kwa maana ya kwamba tayari maeneo kama ya New Forest na Mchangani Mkandarasi ameshaanza kujenga camp ili kuona kwamba anafanya mobilization lakini maeneo ya Intake na maeneo ya Sistila kule juu karibu ya MUST wanaendelea na clearance kwa ajili hiyo ya kujenga camp kuona kwamba kazi zitaanza mara moja lakini suala lililoko mezani kwa sasa hivi, tayari Wizara ya Fedha imetoa exchequer ambayo imeingia kwenye Wizara ya Maji ukiisoma unaiona sasa hivi tunachosubiri tu ni fedha kuingia kwenye account na mamlaka kuweza kuingiziwa hiyo fedha mara moja Mkandarasi alipwe aendelee na mradi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa hiyo hela zinachelewa wapi kwenu au Wizara ya Fedha?

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, hii bajeti tuliyopitisha ya juzi ni kama mlishauriwa kuangalia ukubwa wa majimbo, siyo? Maana jimbo lenye kata nne kwa mfano, linafanana na lenye kata 36, lenye kata 39, hapo itakuwaje hapo wote wanapewa 15 vijiji na mitaa ama? Maana mlituahidi, sasa hili ni jibu unatoa leo, mnaenda kuangalia na ukubwa wa majimbo au ukubwa wa majimbo utakuja 2024/2025?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa bajeti tuliyokuwanayo sasa na kwa uhalisia uliokuwepo tumeona kipindi hiki cha kuanzia iwe ni vitongoji 15 kwa kila jimbo kwa sababu ni mwaka wa fedha mmoja, lakini katika mwaka wa fedha 2024/2025 hivi vitongoji 36,101 vyote tunatarajia kuvipatia fedha. Kwa hiyo, kipindi hicho sasa tutaanza na wale wenye mahitaji makubwa zaidi tukielekea kwenye mahitaji madogo zaidi. (Makofi)

SPIKA: Hivi Mheshimiwa Waziri wa Utumishi, ule Mwongozo wa Ajira ambao mlisema, kwa wale watu wanaojitolea umeshakamilika ama bado? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, tunaendelea, lakini tumeshamaliza na ninadhani tutakuja kutoa tamko hapa Bungeni. (Makofi)
SPIKA: Sasa huyo anayebadilishia hapo katikati ni nani kama mkulima huwa anapata pembejeo kwa dola na yule mnunuzi ananunua kwa dola, nani anayembadilishia mkulima hapo ghafla kwamba yeye ndiyo apewe shilingi?
SPIKA: Sasa huyo anayebadilishia hapo katikati ni nani kama mkulima huwa anapata pembejeo kwa dola na yule mnunuzi ananunua kwa dola, nani anayembadilishia mkulima hapo ghafla kwamba yeye ndiyo apewe shilingi?
SPIKA: Mheshimiwa Kassinge nimekuona, lakini ulipaswa kusimama anaposimama yule mwenye swali lake sasa umesimama baadaye. Kwa hiyo, utatafuta fursa nyingine itakapojitokeza.

Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali imeshapiga hatua kubwa kwa kweli, siku hizi wastaafu wengi wanalipwa mafao kwa wakati lakini hii ya miezi miwili kwa nini? Kwa sababu huyu alikuwa mfanyakazi kwa hivyo alikuwa anategemea mshahara mwisho wa mwezi, hii miezi miwili anayochelewa kulipwa anakuwa anaishije? Kwa sababu yeye anasubiri. Lengo la mafao ni kwamba inachukua ile nafasi ya mshahara. Kwa hiyo, mshahara unapokata ile tarehe aliyokuwa anapokea mshahara anapaswa kupokea mafao na kwa sababu kustaafu sio dharura, anakuwa ameshajua na ninyi mmepewa taarifa miezi kadhaa nyuma. Kwa hiyo, badala ya mwajiri, sasa anapelekwa huku ilipoenda michango na hili ulilolisema la changamoto ya michango ya mwajiri tulilisemea hapa ndani na tumaini ni mojawapo ya marekebisho mnayoleta.

Kwa kweli sio kazi ya mfanyakazi kufuatilia michango kama mwajiri anapeleka au hapeleki, kwa sababu yeye hana uwezo wa kujua, hana uwezo wa kumfuatilia huyu mwajiri la sivyo atafukuzwa kazi. Kwa hiyo, hili nalo muangalie namna ya kulifanyia kazi kwa kweli. Ahsante sana Mheshimiwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante, hilo la siku 60 ambazo tumeziweka kisheria ukweli ni kwamba hata siku moja kama nyaraka zake na taarifa zote zipo sahihi na wanalipwa wapo wengine siku tatu, siku nne. Hizo 60 tumeweka tu threshold ambayo ndani ya kipindi hicho mstaafu huyo asiweze kupata shida. kwa hiyo, analipwa wakati wowote anapostaafu.

Mheshimiwa Spika, la pili la kuhusiana na zile asilimia, ni Bunge lako Tukufu liliamua kwamba tuweke interest kwa yule ambaye anachelewesha michango na tumekwishafanya hivyo kwenye sheria zinazohusiana na watumishi wa umma, lakini pia kwa upande wa private sector; na moja ya sehemu ya marekebisho ni pamoja na huu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ambao tunauleta mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, kuna hatua kali pia ambazo tunaendelea kuzichukua za kuwafikisha mahakamani, pia kutakuwa na pendekezo la kuhakikisha kwamba yule ambaye hata akipelekwa mahakamani maamuzi yafanyike kwa summary procedure na zaidi ya hapo alipe kwanza fedha ndipo aweze kusikilizwa ili kulinda hali ya wanachama wetu huko. Zamani ilikuwa wanatafuta sana procedure ya kupata ruhusa ya mahakama ili aweze kusikilizwa wakati mwanachama wetu anazidi kuumia. Ahsante.