Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Eng. Stella Martin Manyanya (22 total)

MHE. NAPE M. NNAUYE K.n.y. MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha gharama za kuhamisha umiliki wa ardhi ambazo siyo rafiki hasa kwa wanyonge na kusababisha wengi kuwa na miliki bubu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali hili naomba uniruhusu nimshukuru kwanza Mwenyezi Mungu kwa fursa ambayo amenipatia kuweza kuendelea kulitumikia Taifa hili, lakini zaidi sana nimshukuru Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini tena na kutuamini Wizara yetu na kuendelea kutuweka pale ili tuendelee kuitumikia Serikali hii. Namshukuru sana kwa imani hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, uhamishaji wa milki za ardhi huzingatia Sheria ya Ardhi (Sura Na. 113), Sheria ya Usajili wa Ardhi (Sura Na. 334), Sheria ya Ushuru wa Stempu (Sura Na. 189) na Sheria ya Kodi ya Mapato (Sura Na. 332) ambayo inahusika na Kodi ya Ongezeko la Mtaji. Kwa mantiki hiyo, Wizara yangu inasimamia gharama za Ada ya Uthamini, Ada ya Upekuzi katika Daftari la Msajili, Ada ya Maombi ya Uhamisho wa Milki na Ada ya Usajili ambazo ni gharama nafuu na wananchi wa kawaida wanaweza kuzimudu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu katika nyakati tofauti imekuwa ikiboresha gharama za uhamishaji na umilikishaji wa ardhi. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2018/2019 gharama za tozo za mbele yaani (premium) ilipunguzwa kutoka 7.5% kwenda 1% ya thamani ya ardhi ambayo hutozwa mara moja tu wakati wa umilikishaji kwa maeneo ya urasimishaji mijini na hadi 2.5% kwa maeneo mengine. Aidha, Wizara pia imeboresha gharama za urasimishaji kwa kupunguza kutoka shilingi 250,000/= hadi shilingi 150,000/= na katika Halmashauri nyingine wanatoza shilingi 50,000/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zinazotekelezwa na Serikali zinalenga kuboresha gharama za umilikishaji na uhamishaji wa milki kuwa rafiki hususan kwa wanyonge. Aidha, kwa kuhakikisha kuwa ada na tozo zinakuwa rafiki na zinazingatia maoni ya wananchi, Serikali sikivu ya Awamu ya Tano kupitia Kamati Maalum (Task Force on Tax Reform) kila mwaka inapitia sheria za kodi ili kufanya maboresho.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, Serikali iko tayari kupokea maoni na ushauri wa wadau kuhusu viwango vya tozo zinazohusu uhamisho wa milki za ardhi na tozo nyingine zinazohusu Sekta ya Ardhi kwa ujumla ili kuboresha huduma kwa wananchi.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, kwa nini mikopo ya injini za boti isitolewe kwa mtu mmoja mmoja aliye tayari kuliko kutoa kupitia vikundi jambo ambalo linachelewesha ukuaji wa Sekta ya Uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ibara ya 43(h) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025 inaelekeza Serikali kuhamasisha uanzishaji na uimarishaji wa Vikundi na Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Wavuvi Wadogo kwa lengo la kuwapatia mtaji, ujuzi na vifaa pamoja na zana za uvuvi katika maeneo ya mwambao wa bahari ya Hindi, Maziwa, Mabwawa na mito ili kuongeza uzalishaji, ajira na kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza ilani hiyo, kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali iliazimia kuhamasisha wavuvi na wakuzaji viumbe maji kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili kuwa na sauti ya pamoja, kufikiwa kirahisi, kutatua changamoto zinazowakabili pamoja na kuwa na usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi. Aidha, Serikali imekuwa ikiviwezesha vyama vya ushirika kwa kuvipatia elimu, zana na vifaa bora vya uvuvi kama vile injini za boti pamoja na kuviunganisha na taasisi za kifedha ili kupata mikopo yenye riba na masharti nafuu kwa lengo la kufanya shughuli zao kwa tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Serikali itaendelea kuhamasisha na kuwezesha vyama vya ushirika. Aidha, mtu mmoja mmoja anayo fursa ya kuomba kukopeshwa injini za boti kupitia taasisi za kifedha nchini. Hivyo, natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote kuhimiza wavuvi na wakuzaji viumbe maji wa maeneo yenu kujiunga kwenye vyama vya ushirika vya wavuvi kama chachu ya kuwaletea maendeleo.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA K.n.y. MHE. ENG.STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Bonde la Mto Ruhuhu lililopo Kata ya Lituhi linawanufaisha wananchi kwa kuweka miundombinu ya Kilimo na umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Jimbo la Nyasa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Bonde la Mto Ruhuhu linalojumuisha sehemu ya Wilaya Ludewa Mkoni Njombe na Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma linalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji. Upembuzi yakinifu wa awali kuhusu kilimo cha umwagiliaji katika bonde hili ulifanyika mwaka 2013/2014 na kubaini uwezekano wa kujenga bwawa kubwa; matumizi mbalimbali ikiwemo kilimo cha umwagiliaji kwa takribani hekta 4,000 na kufua umeme wa megawati 300. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania linaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Bwawa la Kikonge lililopo ndani ya Bonde la Mto Ruhuhu kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na uendelezaji wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji chini ya Bwawa la Kikonge.

Mheshimiwa Spika, mara baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu itakapokamilika na kutathimini gharama halisi, Serikali itatafuta fedha za ujenzi wa bwawa hili pamoja na fedha za ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji chini ya Bwawa la Kikonge ili kuongeza uzalishaji na tija ya mazao ya kilimo katika eneo hilo. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha biashara kupitia Diplomasia ya Uchumi kati ya Tanzania na Malawi kwa kutumia meli ya MV Mbeya II?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, meli ya MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo ilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 5 Januari, 2021. Meli hii kwa sasa inafanya safari kati ya Bandari za Tanzania tu za Kyela na Mbambabay.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi ni miongoni mwa majukumu makubwa ya Wizara yangu. Kutokana na umuhimu mkubwa wa kukuza biashara kati ya Tanzania na Malawi na katika kuhakikisha kuwa meli ya MV Mbeya II inatumika ipasavyo, Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, ukishirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imeanza mawasiliano na Serikali ya Malawi na taasisi zake kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya Malawi ili kuweka mazingira mazuri ya kuwezesha MV Mbeya II kufanya safari zake nchini Malawi.

Mheshimiwa Spika, ubalozi wetu uliopo Lilongwe, Malawi pia unafuatilia kwa karibu kufikia makubaliano (MoU) baina ya Serikali ya Tanzania na Malawi kuhusiana na uanzishaji wa Ofisi za TPA mjini Lilongwe ambazi zitasimamia utekelezaji na uendeshaji wa shughuli zote za kibiashara zinazotumia huduma za bandari za Tanzania. Hii inatokana na maazimio ya Marais wa Tanzania na Malawi wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais wa Malawi nchini Tanzania iliyofanyika tarehe 7 - 8 Oktoba, 2020.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa taratibu hizo na kukamilika kwa kipindi cha majaribio ya meli hiyo na hivyo kuanza safari zake nchini Malawi, ni dhahiri kuwa biashara kati ya Tanzania na Malawi kwa kutumia Ziwa Nyasa itaimarika. Ahsante sana.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa kipaumbele wa kuongeza mtandao wa barabara za lami za Mji Mkongwe na wakitalii wa Mbamba Bay?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya Mbunge wa Jimbo la Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (TARURA) inaendelea na ujenzi wa lami kilometa moja unaogharimu jumla ya shilingi milioni 473.50 unaotekelezwa na Mkandarasi VAG Contractors Ltd. katika eneo la Makao Makuu ya Wilaya kwa maana ya Bomani kwa mwaka wa fedha 2021/2022 pamoja na ujenzi wa kilometa 0.5 Kata ya Kilosa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa eneo la Mbamba Bay kama eneo la utalii na shughuli za Uvuvi. Hivyo, Serikali itaendelea kutenga fedha kujenga barabara kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha katika eneo la Mbamba Bay.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, kwa mwaka 2018 hadi 2021 ni walemavu wangapi wenye sifa husika wameajiriwa katika nafasi zilizotolewa na Serikali, na ni sawa na asilimia ngapi ya watu wenye ulemavu wenye sifa hizo nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2018 hadi 2021 Serikali imeajiri watumishi wenye ulemavu wapatao 312 wenye sifa stahiki katika fani mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu zilizopo za wahitimu wenye ulemavu ambao wamejiorodhesha katika kanzidata ya Serikali inaonesha kwamba, kuanzia mmwaka 2018 hadi 2021 wahitimu wenye ulemavu walioajiriwa katika utumishi wa Umma ni asilimia 56 ya wahitimu wenye ulemavu waliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kutoa rai na kusisitiza wahitimu wenye ulemavu wenye sifa za elimu na taaluma mbalimbali ambazo zipo ndani ya utumishi wa Umma kuomba kazi pindi zinapotangazwa ili waweze kuajiriwa katika utumishi wa Umma kwani ajira hutolewa kwa usawa na kwa watu wote wenye sifa zinazohitajika katika nafasi husika pamoja na kuzingatia ujumuishaji wa watu wenye ulemavu. Vile vile, nitumie fursa hii kuwakumbusha waajiri wote kuzingatia ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika ajira zote zinazotangazwa na Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya Mwaka 2010.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, ni lini RUWASA Nyasa itapatiwa gari ili kurahisisha utendaji kazi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI k.n.y. WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Stella Martin Manyanya Mbunge wa Nyasa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuijengea uwezo RUWASA Mkoa wa Ruvuma ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya magari 86 yatanunuliwa na kupelekwa kwenye Wilaya mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Nyasa. Ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, ni lini Hospitali ya Kanda ya Kusini iliyopo Mtwara itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4.4 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma za mama na mtoto katika Hospitali ya Kanda ya Mtwara.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa hospitali hii inatoa huduma ya wagonjwa wa nje (OPD) na wagonjwa wa kulazwa (IPD). Aidha, Serikali itaendelea kuipa hospitali hii kipaumbele katika mpango wa bajeti ili kuhakikisha kuwa inakamilika ifikapo mwaka 2025.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha SIDO Wilayani Nyasa?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Bajeti ya mwaka 2022/2023 Wizara kupitia shirika la kuendeleza viwanda vidogo (SIDO) imetenga jumla ya shilingi milioni 950 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mitaa ya viwanda. Kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi milioni 100 ni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Mafunzo na Uzalishaji cha SIDO Wilayani Nyasa. Hivyo, pindi fedha hizo zitakapopokelewa, ujenzi wa kituo hicho utakamilika. Nakushukuru.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Luhindo hadi Ndondo katika barabara Kuu ya Nyoni hadi Mitomoni Wilayani Nyasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.046 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali kwenye barabara ya Nyoni - Liparamba hadi Mitomoni. Tayari Mkandarasi yupo eneo la kazi akiendelea na kazi za matengenezo ambapo katika sehemu korofi zenye miinuko na miteremko mikali anazijenga kwa zege na kuweka makalvati maeneo kadhaa. Kazi hizi zinategemewa kukamilika tarehe 30 Juni, 2023, ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipatia maji Vijiji vilivyopo mwambao wa Ziwa Nyasa?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika; naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Ziwa Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwambao wa Ziwa Nyasa una vijiji 39 na kati ya hivyo vijiji 18 vinapata huduma ya maji na vijiji 21 havina. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali inatekeleza Miradi ya Maji ya Lituhi, Liuli, Ngumbo, Puulu, Songambele na Nangombo-Kilosa, inayotarajia kukamilika katika mwaka wa fedha 2023/2024 na kunufaisha vijiji 17.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali ipo katika hatua za mwisho kukamilisha usanifu wa Mradi wa Maji Ndengele-Mbuyula utakaohudumia vijiji vitatu na itaendelea na usanifu katika Kijiji cha Ndonga. Ujenzi wa miradi hii utafanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, lini Mahakama ya Wilaya ya Nyasa itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nikushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kujenga Mahakama ya Wilaya ya Nyasa katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023, ambapo taratibu zote za awali za kupitia michoro na makadirio ya gharama zimekamilika, na hatua za kupata mkandarasi wa ujenzi ipo katika hatua za mwisho.

Mheshimiwa Spika, Tunategemea muda wowote jengo hili litaanza kujengwa, na kukamilika katika mwaka ujao wa fedha wa 2023/2024.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga wodi katika Kituo cha Afya Kihangara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya Mbunge wa Jimbo la Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha huduma za afya nchini, Serikali imeanza na uboreshaji wa miundombinu ya Vituo vya Afya, kipaumbele kikiwa ni utoaji wa huduma za dharura na upasuaji ambapo fedha iliyotolewa ilielekezwa kujenga jengo la wazazi, jengo la upasuaji, jengo la maabara, jengo la kufulia na nyumba ya mtumishi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Ofisi ya Rais, (TAMISEMI) inakusudia kuanza ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa kwenye Vituo vya Afya ambavyo vilikwisha pokea fedha za ukarabati na ujenzi jumla ya vituo vya afya 807 vinahitaji kujengewa wodi za kulaza wagonjwa kikiwemo Kituo cha Afya Kihangara.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, lini soko la samaki Mbamba Bay litaanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Jimbo la Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa soko la samaki la Mbamba Bay unafanyika kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ulianza mwezi Mei 2021 na kukamilka mwezi Machi, 2022. Katika awamu ya kwanza Serikali ilijenga jengo kuu ambalo lina vizimba au meza za kuuzia samaki. Kwa sasa, Serikali inaanza awamu ya pili ya ujenzi wa soko hilo ambao unahusisha ujenzi wa miundombinu ya maji safi, maji taka pamoja na choo. Aidha, zabuni ya ujenzi huo imeshatangazwa na kufunguliwa Tarehe 23 Mei, 2023. Kazi ya uchambuzi na tathmini ya nyaraka za zabuni inaendelea ili kumpata mzabuni wa kuanza kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali inatambua umuhimu wa soko hilo na litaanza kutumika tu mara tu baada ya ujenzi wa miundombinu hiyo kukamilika.
MHE. ENG STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, ni kwa nini Serikali isitoe rasilimali za Kiwanda cha Mang’ula Mechanical and Machine Tools kilichopo Kilombero kwa Taasisi za Ufundi kama DIT na nyinginezo ili ziweze kutumia?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA, alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Jimbo la Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeamua kukihuisha upya kiwanda cha Mang’ula Mechanical & Machine Tools Co. Ltd. kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) ili kiendelee kutekeleza majukumu yaliyokusudiwa hapo awali. Ikiwa kutakuwa na haja ya kuzihusisha Taasisi za Ufundi Serikali itafanya hivyo.

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka alama za kuongoza meli katika eneo la kuegesha meli kwenye Ziwa Nyasa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) ina mpango wa kujenga miundombinu ya bandari katika Ziwa Nyasa hususani Bandari ya Mbamba Bay. Ujenzi wa bandari hizi utahusisha pia usimikaji wa vifaa vya kuongozea meli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, TPA ina mpango wa kuweka alama za kuongozea meli katika bandari za maeneo mengine kuanzia mwezi Machi, 2024 kwani kupitia Mradi wa Upanuzi na Maboresho ya Miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam (Dar es Salaam Maritime Gateway Program – DMGP) maboya yaliyopo Bandari ya Dar es Salaam yataondoshwa kwa sababu mradi huo unahusisha pia uwekaji wa maboya mapya katika Bandari ya Dar es Salaam lakini kwa kuwa maboya hayo bado yapo katika matumizi yatasimikwa katika bandari nyingine.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, kwa nini ukumbi wa VETA Nyasa haujawekwa vipooza joto?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshafanya makadirio ya gharama za kufunga vipooza joto katika Chuo cha VETA cha Wilaya ya Nyasa ambapo katika Mwaka huu wa Fedha 2023/2024, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 20 kwa majengo yote. Kati ya fedha hizo shilingi milioni 7.5 zimetengwa kwa ajili ya kuwezesha kununua vifaa vitakavyofungwa katika ukumbi huo ili kuondoa changamoto ya joto kali, nakushukuru.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka alama za kuongoza meli katika eneo la kuegesha meli kwenye Ziwa Nyasa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) ina mpango wa kujenga miundombinu ya bandari katika Ziwa Nyasa hususani Bandari ya Mbamba Bay. Ujenzi wa bandari hizi utahusisha pia usimikaji wa vifaa vya kuongozea meli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, TPA ina mpango wa kuweka alama za kuongozea meli katika bandari za maeneo mengine kuanzia mwezi Machi, 2024 kwani kupitia Mradi wa Upanuzi na Maboresho ya Miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam (Dar es Salaam Maritime Gateway Program – DMGP) maboya yaliyopo Bandari ya Dar es Salaam yataondoshwa kwa sababu mradi huo unahusisha pia uwekaji wa maboya mapya katika Bandari ya Dar es Salaam lakini kwa kuwa maboya hayo bado yapo katika matumizi yatasimikwa katika bandari nyingine.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kufanya mafunzo ya mgambo kuwa sehemu ya mafunzo kwa vijana wanaokosa nafasi ya kujiunga na JKT?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Akiba (Jeshi la Mgambo) lilianzishwa kwa Sheria ya Jeshi la Akiba Na.2 ya mwaka 1965 ili kuandaa nguvu ya akiba kwa ajili ya kusaidia Jeshi la Kudumu wakati wa vita, operesheni, majanga na kuuandaa umma wa Watanzania ili waweze kuelewa kuwa dhana ya ulinzi wa Taifa ni jukumu la kila Mtanzania. Vijana 600 kutoka kila Mkoa hupata mafunzo kila mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa kupitia Sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa Na.2, Sura ya 193 ya mwaka 1964 ambayo ilirejewa mwaka 2002 kwa malengo ya ulinzi wa Taifa, kujenga uzalendo na mshikamano, uzalishaji mali na kutoa elimu ya kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzishwa kwa vyombo hivyo kulilenga mahitaji tofauti. Kwa muktadha huo, hakuna mpango wa kuyafanya mafunzo ya Jeshi la Akiba kuwa sehemu ya mafunzo ya vijana wanaokosa nafasi za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa. Aidha, vijana wenye sifa wanaruhusiwa kuomba kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Akiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha
MHE. DKT. THEA M. NTARA K.n.y. MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kupeleka gari RUWASA Wilaya ya Nyasa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Jimbo la Nyasa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) inaendelea kutatua changamoto za uhaba wa vitendea kazi ikiwemo magari katika mikoa 25 na Wilaya 128 Tanzania Bara zinazohudumiwa na Taasisi hiyo. Katika kutekeleza azma hiyo, RUWASA katika mwaka wa fedha 2023/2024 imeshalipia ununuzi wa magari mapya 35 na yanatarajiwa kupokelewa hivi karibuni kwa ajili ya kusambazwa kwenye mikoa na wilaya zenye uhitaji nchini ikiwemo Wilaya ya Nyasa.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakabidhi majengo yaliyotumiwa na Mshauri wa Ujenzi wa Barabara ya Mbinga hadi Mbamba Bay kwa Halmashauri ya Nyasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, majengo ya kambi yaliyokuwa yanatumiwa na mhandisi mshauri wa ujenzi wa Barabara ya Mbinga – Mbamba Bay yenye urefu wa kilomita 67 yalirudishwa Wizara ya Ujenzi mnamo Tarehe 13 Aprili, 2023. Kwa sasa majengo hayo yanatumika kama nyumba za watumishi, wauguzi na madaktari, wa Hospitali ya Wilaya ya Nyasa. Ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, lini Bandari mpya ya Mbambabay itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI K.n.y WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TPA (Mamlaka ya Bandari ya Tanzania) imeanza utekelezaji wa ujenzi wa bandari mpya ya Mbamba Bay ambapo mkataba wa utekelezaji wa mradi huu ulisainiwa tarehe 4/12/2023 na mkandarasi alianza kazi mnamo tarehe 27 Januari, 2024 ambapo hadi kufikia sasa hivi mradi umefika asilimia nane ya utekelezaji na mradi uliwekwa jiwe la msingi tarehe 25 Septemba, 2024 na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, muda wa utekelezaji wa mradi huu ni miezi 24 na gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni 75.853 ambapo kazi mbalimbali zinazotarajiwa kufanyika zikiwemo; ujenzi wa gati na jengo la abiria, ujenzi wa majengo ya kuhifadhia mizigo pamoja na ujenzi wa barabara ya kuingia eneo hilo la bandari zitafanyika. Ahsante.