MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Jimbo la Madaba ni miongoni mwa wananchi walioathirika sana na mbegu feki ambazo zilisambazwa msimu uliopita. Wapo wengi wamepata hasara kabisa katika mashamba yao, na kwa vile yule ambaye alisambaza hizo mbegu feki alishakamatwa.
Mheshimiwa Spika, je, Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha kwamba hasa wakulima waliopata hasara kwa kutumia zile mbegu wanafidiwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilikuwa najibu katika swali ambalo lilitangulia, ni kwamba, baada ya yule msambazaji wa mbegu feki au pembejeo feki kukamatwa, sisi kama Wizara hatua ambazo tumechukua ni kumfutia leseni ya kushiriki katika shughuli zote za mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, hatua ya pili, tumeshapeleka Mahakamani, na jambo hili lipo katika hatua za kisheria. Kwa hiyo, baada ya hatua za kisheria, ninaamini sasa tunaweza tukawa na neno la kusema kuliko kuingilia Mahakama, ahsante.