Primary Questions from Hon. Daimu Iddi Mpakate (31 total)
MHE. MPAKATE D. IDDI aliuliza:-
Katika Wilaya ya Tunduru kuna miradi mingi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia ambayo imesimama kwa muda mrefu bila kukamilishwa na wakandarasi kwa sababu ya ukosefu wa fedha:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kumalizia miradi hiyo ambayo wananchi wanajua kuwa fedha zilitolewa na Benki ya Dunia lakini hazijulikani zilikwenda wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mpakate Daimu Iddi, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambapo ugharamiaji wa maji chini ya programu hii hutokana na fedha za Serikali na wadau wengine ikiwemo Benki ya Dunia. Hivyo, upelekaji wa fedha kwenye halmashauri hutegemea upatikanaji wa fedha kutokana na bajeti ya Serikali na fedha za wadau wa maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza ya utekelezaji wa programu hii, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ilipanga kutekeleza jumla ya miradi 11. Hadi sasa jumla ya miradi miwili katika Vijiji vya Nandembo na Nalasi imekamilika na inahudumia wananchi 21,224. Miradi minne ya Vijiji vya Lukumbule, Amani, Mtina na Matemanga ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Mradi wa maji katika Kijiji cha Mbesa umesimama kutokana na mkandarasi kukiuka masharti ya mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika, mpaka kufikia Februari 2016, Wizara imeshatuma kiasi cha shilingi milioni 537.2 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa ajili ya kuendelea kukamilisha miradi hiyo. Aidha, miradi minne katika Vijiji vya Majimaji, Muhuwesi, Nakapanya na Mchoteka haijaanza kutekelezwa kutokana na kukosa vyanzo vyenye maji ya kutosheleza. Miradi hii itatafutiwa vyanzo mbadala katika utekelezaji wa awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Maji.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Wilaya ya Tunduru iko miradi mingi ya REA ambayo kampuni mbili zimepewa kazi hiyo lakini wakandarasi wanasuasua kukamilisha miradi hiyo na muda wake umeisha kwa kigezo cha kutolipwa:-
Je, ni lini Serikali itatoa pesa kukamilisha miradi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mradi kabambe wa REA Awamu ya II katika Wilaya ya Tunduru na kazi hii imeshaanza na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu, mwaka 2016. Kazi ya kupeleka umeme katika Wilaya ya Tunduru inaunganisha pia kazi ya ujenzi wa njia ya umeme Msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 293.2, ujenzi wa njia ya umeme Msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 77.1 lakini pia ufungaji wa transfoma 38 zenye ukubwa mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi hizo, kazi nyingine inayofanyika ni kuwaunganishia umeme wateja wa awali 3,330 lakini pia mradi umekamilika kwa asilimia 79 ambapo ujenzi wa laini kubwa umekamilika kwa asilimia 83, laini ndogo asilimia 74, transfoma saba zimeshafungwa na wateja 182 wameshaunganishiwa umeme. Gharama ya mradi wa Mkoa wa Ruvuma ikiwemo Wilaya ya Tunduru ni shilingi bilioni 32.56. Kiasi ambacho mkandarasi hadi sasa ameshalipwa ni shilingi bilioni 27.22 ambayo ni sawa na asilimia 83.6. REA wanasubiri kupata uthibitisho kutoka kwa mkandarasi kuhusu madai ya shilingi bilioni 3.19 ili aweze kulipwa mara tu baada ya uthibitisho huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Tunduru vijiji vinne vya Jimbo la Tunduru Kusini ambavyo ni Azimio, Chiwana, Mbesa na Mkandu, vimeunganishiwa miundombinu ya umeme ambayo inafanyiwa marekebisho na matayarisho kwa ajili ya kuwashwa. Hivi sasa mkandarasi anaendelea kufunga transfoma na mita za Luku katika vijiji vingine 34 ambavyo vimesalia katika Wilaya ya Tunduru ili viweze kupatiwa umeme ifikapo tarehe 30 Juni, 2016.
MHE. MPAKATE D. IDDI aliuliza:-
Sehemu kubwa ya Jimbo la Tunduru Kusini imepakana na Mto Ruvuma na vijiji vingi vipo pembezoni mwa mto huo, hivyo wananchi wake hupata baadhi ya bidhaa kutoka Msumbiji kwa kutumia mitumbwi ambayo siyo salama kwa maisha yao wanapovuka mto:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia kivuko wananchi wa Wenje na Makande ili waweze kuvuka Mto kwenda Msumbiji kwa usalama?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupata mahitaji halisi ya kivuko kwa wananchi wa Wenje na Makande Wilayani Tunduru, Wizara yangu itatuma mtaalam kutafiti uwezekano wa kuweka kivuko eneo hilo. Utafiti huo utajumuisha upatikanaji wa eneo lenye kina cha maji cha kutosha kuwezesha kivuko kuelea wakati wowote wa mwaka, wakati wa masika na wakati wa kiangazi pamoja na kupata kibali cha kuweka maegesho ya kivuko upande wa Msumbiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo ya utafiti huo yatawezesha Wizara kuweka mpango wa kuweka kivuko hicho kwenye bajeti yake.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru kulikuwa na Chuo cha MCH kilichokuwa kikitoa mafunzo ya taaluma mbalimbali za afya kwa vijana wengi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru lakini mwaka 1980 chuo hicho kiliungua moto:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukikarabati chuo hicho ili kiweze kuendelea kutoa wataalam wa afya kama hapo awali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Tunduru ni mojawapo wa vyuo vilivyokuwa vimefungwa baada ya kusitisha mafunzo ya Martenal and Child Health Aider mwaka 1998. Chuo hiki ambacho kipo katika eneo la Hospitali ya Tunduru kiliungua moto sehemu ya bweni na bwalo la chakula. Katika utekelezaji wa mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) vyuo vinne vya aina hii ambavyo vilikuwa vimefungwa vilifanyiwa tathmini mwezi Agosti 2008 kwa nia ya kuvifufua kuanza kutoa mafunzo kwa wauguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika tathmini hiyo ilipendekezwa Vyuo vya Nzega, Nachingwea na Kibondo vifufuliwe na kuanza kutoa mafunzo ili kuchangia kuongeza idadi ya wataalam kutokana na mahitaji ya Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya Chuo cha Tunduru hakikukidhi vigezo vya kufufuliwa kutokana na gharama kubwa iliyohitajika kufanya ukarabati. Aidha, nafasi ya upanuzi wa chuo ilikuwa ndogo hivyo kupendekeza sehemu hiyo ya chuo kujumuishwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Tunduru.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika upande wa kusini mwa Jimbo la Tunduru Kusini wananchi takribani 200 wa Tanzania na Msumbiji huvuka Mto Ruvuma kila siku kutafuta mahitaji yao ya kila siku, upande wa Msumbiji wameweka Askari wa Uhamiaji ambao huwanyanyasa sana Watanzania kwa kuwapiga na kuwanyang’anya mali zao kwa kukosa hati ya kusafiria.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka Kituo cha Uhamiaji katika kijiji cha Makande Kazamoyo na Wenje ili kuwapatia Watanzania huduma ya uhamiaji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya juhudi za kuhakikisha kuwa inasogeza huduma karibu na wananchi ikiwa ni pamoja na huduma za Uhamiaji. Katika kutekeleza hilo Wilaya zilizo nyingi ikiwemo Tunduru zina Ofisi za Uhamiaji. Aidha, Serikali inatambua umbali mrefu wa takribani kilometa 90 uliopo kutoka vijiji vya Makando, Kazamoyo na Wenje kutoka Mjini Tunduru zilipo ofisi za Uhamiaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo na uhitaji
wa huduma za uhamiaji katika vijiji hivyo ili kuwawezesha wanakijiji kuingia na kwenda nchini Msumbiji kihalali, tunafanya ufuatiliaji ili kujua gharama za kufungua ofisi za Uhamiaji katika kijiji cha Makando. Kwa kuanzia Ofisi hiyo itahudumia vijiji vya Kazamoyo na Wenje ili kuwawezesha kuvuka mpaka Kihalali. Tunawaomba wananchi na Mheshimiwa Mbunge kuwa na subira kwa kuzingatia kuwa suala hili linahitaji kutengewa fedha katika bajeti.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Jimbo la Tunduru Kusini kuna vituo vitatu vya afya. Kituo cha Afya Mtina kina zaidi ya miaka 30 hakijafanyiwa ukarabati na pia hakuna wodi ya wazazi.
Je, ni lini Serikali itajenga wodi ya wazazi katika kituo hicho na kufanya ukarabati ili kiweze kutoa huduma bora kwa wakazi wa vijiji vya Nasya, Semeni, Nyerere, Angalia na wakazi wa kata ya Mchesi na Lukumbule?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na nguvu za wananchi imekamilisha ujenzi wa zahanati sita za Njengi, Mwenge, Tuwemacho, Nasumba, Semeni na Kazamoyo ambazo zimeanza kutoa huduma.
Aidha, nampongeza Mbunge wa Jimbo kwa kuweka kipaumbele na kutumia shilingi milioni 6.2 kwa ajili ya ukarabati wa chumba cha kujifungulia na chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha afya Mtina.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaweka kipaumbele na kuhakikisha fedha zinatengwa kupitia Halmashauri katika mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi katika kituo cha afya Mtina kinakamilika. Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Jimbo la Tunduru Kusini kuna vituo vitatu vya afya ambapo Kituo cha Afya Mtina kina zaidi ya miaka 30 hakijafanyiwa ukarabati na pia hakuna wodi ya wazazi.
Je, ni lini Serikali itajenga wodi ya wazazi katika kituo hicho na kufanya ukarabati ili kiweze kutoa huduma bora kwa wakazi wa Kata za Nasya, Semeni, Nyerere, Angalia na wakazi wa Kata ya Mchesi, Vijiji vya Likumbula, Tuwemacho na Namasakata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina vituo vitano ambapo vituo vya afya viwili vipo katika Jimbo la Tunduru Kusini na vitatu katika Jimbo la Tunduru Kaskazini. Kituo cha Afya Mtina kilianzishwa mnamo mwaka 1970 na kimekuwa kikiendelea kutoa huduma za kujifungua na huduma za matibabu ya kawaida kwa kipindi chote. Kwa sasa chumba cha kupumzikia akina mama baada ya kujifungua kimetengwa ndani ya wodi ya kawaida ya wanawake. Serikali kupitia wadau wa maendeleo (Walter Reed Program) waliweza kufanya ukarabati wa jengo la tiba na matunzo (CTC) kwa wagonjwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa msingi wa wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya Mtina unaendelea kupitia fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo la Tunduru Kusini ambapo kiasi cha shilingi milioni nne zilitolewa. Aidha, Halmashauri katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/ 2019 imetenga kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya ukarabati na kuboresha Kituo cha Afya Mtina.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Tunduru, Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018 imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukarabati wa Kituo cha Afya Mkasale kilichopo katika Jimbo la Tunduru Kusini. Aidha, Halmashauri inajenga wodi mbili za upasuaji katika Hospitali ya Wilaya, nyumba ya mganga katika zahanati ya Naikula, ukarabati wa nyumba mbili za watumishi katika Kituo cha Afya Mchoteka na kuendeleza ujenzi wa zahanati ya Legezamwendo kupitia mapato yake ya ndani. Serikali itaendelea kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya kwa kadri fedha zitakavyopatikana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Mji wa Tunduru yako mabango mengi yanayoelezea ununuzi wa madini jambo linaloashiria upatikanaji mkubwa wa madini kutoka kwa Wachimbaji wadogo wadogo ambao hawatambuliwi kwa mujibu wa sheria:-
Je, ni lini Serikali itawatengea maeneo ya kuchimba madini na kuwatambua Kisheria Wachimbaji hao wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini na kabla sijajibu swali hili naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Profesa Idris Kikula kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume mpya ya Madini.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2017 inawatambua wachimbaji wadogo. Kwa kutumia sheria hiyo Serikali inatoa leseni za uchimbaji za madini (Primary Mining Licenses) kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kuna mabango na maduka mengi yanayotangaza uwepo wa madini ya vito katikati ya Mji wa Tunduru huko Mkoani Ruvuma. Baadhi ya madini ya vito hayo yaliyopo Wilaya ya Tunduru ni pamoja na Sapphire, Ruby, Garnet na kadhalika. Maduka ya madini yenye mabango ni ya wafanyabiashara wakubwa wenye leseni kubwa (Dealers License) ambazo huhuishwa kila mwaka kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2013 Serikali ilitenga eneo la Mbesa, Wilaya ya Tunduru, lenye ukubwa wa hekta 15,605.3 kwa tangazo la Serikali Namba tano la tarehe 22 Februari, 2013, kwa ajili ya uchimbaji mdogo wa madini ya shaba. Hadi Aprili, 2018 jumla ya leseni hai 649 za wachimbaji wadogo wa madini yaani (PML) zimetolewa Wilaya ya Tunduru.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo kadri taarifa za utafiti katika maeneo hayo zitakavyoandaliwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushirikiana na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ili wachimbaji wadogo hao waweze kuchimba madini siyo kwa kubahatisha.
Mheshimiwa Spika, aidha, wachimbaji wadogo wanahimizwa kuomba leseni ili wafanye shughuli za utafutaji wa madini kwa mujibu wa sheria za nchi ili kuinua vipato vyao kutoa ajira kwa Watanzania, kuchangia pato la Taifa kupitia tozo mbalimbali zinazotokana na shughuli za madini.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina jumla ya kata 39 na vijiji 157. Halmashauri iliomba kuigawa Wilaya hiyo ambayo ina ukubwa zaidi ya Mkoa wa Mtwara wenye Wilaya sita:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuigawa Wilaya ya Tunduru ili iwe rahisi kutoa huduma karibu zaidi na wananchi?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzigawa Kata za Mchoteka, Mtina, Namasakala, Lukumbule, Mchasi, Tuwemacho na Misechela ambazo zina wakazi zaidi ya 30,000 kila Kata?
(c) Je, Serikali itaidhinisha lini mgao wa vijiji uliopendekezwa na Halmashauri mwaka 2015 ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, taratibu za kuanzisha au kugawanya maeneo ya kiutawala zimeainishwa kwenye Sheria ya Serikali za Mitaa Sura ya 287, pamoja na Mwongozo wa Serikali wa mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, maombi ya kugawa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru na kuanzisha Halmashauri ya Wilaya ya Nalasi na kuzigawa Kata za Mchoteka, Mtina, Namasakala, Lukumbule, Mchasi, Tuwemacho na Msecheke yaliwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI yakiwa pamoja na ombi la kuanzisha mkoa mpya wa Selous. Serikali imetafakari maombi haya na kuyaona kuwa ni ya msingi, hata hivyo, kutokana na changamoto ya kuimarisha kwanza miundombinu kama majengo ya ofisi na nyumba za watumishi na mahitaji mengine kama vifaa vya ofisi, watumishi wa kutosha na vyombo vya usafiri kwenye maeneo mapya ya utawala yaliyoanzishwa tangu mwaka 2010 na 2012, Serikali imesitisha uanzishwaji ya maeneo mapya ya utawala hadi yaliyopo yaimarishwe kikamilifu.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika kampeni za uchaguzi mwaka 2010 Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kujenga Kituo cha Afya katika Mji wa Nalasi na kutoa gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya
Mchoteka:-
(a) Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Nalasi?
(b) Je, ni lini Serikali itatoa gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya Mchoteka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Afya - Nalasi ulianza Oktoba, 2013 kwa gharama ya shilingi milioni 80 ambapo awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa msingi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD). Katika mwaka wa fedha 2017/2018, kiasi cha shilingi milioni 75 zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hicho kituo cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka kipaumbele na kutoa shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya nane katika Mkoa wa Ruvuma ambapo kati ya hivyo, vituo vya afya viwili vinajengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ambavyo ni Msakale kilichogharimu shilingi milioni 400 na Kituo cha Afya Matemanga kilichogharimu shilingi milioni 500.
(b) Mheshimwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina gari moja ambalo linahudumia vituo vyote vya afya kikiwemo Kituo cha Afya Mchoteka. Hata hivyo, gari hiyo kwa sasa ni chakavu kwa kuwa ilinunuliwa tangu mwaka 2007. Halmashauri inashauriwa kuweka kipaumbele na kutenga fedha katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya ununuzi wa gari lingine la wagonjwa.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Serikali imeweka zuio la kusafirisha shaba ghafi kabla ya kuchakatwa, jambo ambalo limesababisha uchimbaji mdogo wa Mbesa wa Shaba usimame na wachimbaji wadogo kukosa kazi za kufanya:-
Je, ni lini Serikali itajenga mtambo wa kuchenjua shaba katika Kijiji cha Mbesa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa tarehe 3 Machi, 2017, Serikali iliweka zuio la kusafirisha nje ya nchi madini ghafi na kuelekeza madini yote yanayoongezewa thamani yaongezewe thamani hapa nchini. Zuio hilo lilikuwa na nia njema ya kutaka shughuli zote za uongezaji thamani madini zifanyike hapa nchini ili kuongeza manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kutokana na rasilimali ya madini.
Mheshimiwa Spika, kutokana na zuio hilo, kuna GN Na. 60 ya mwaka huu, yaani tarehe 25, Januari, 2019, Serikali imetoa mwongozo wa kuhakiki uongezaji thamani madini au miamba nchini kabla ya madini hayo kupata kibali cha kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, madini ya shaba yanapatikana katika maeneo mbalimbali nchini. Hivyo, kwa kuzingatia hilo, Serikali imepokea maombi ya kampuni 11 zenye nia ya kujenga vinu vya kuyeyusha madini hayo (smelters) baada ya kutangaza uwepo wa fursa hiyo. Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuteua kampuni zitakazojenga smelters hizo ili kuwaondolea adha ya soko la madini hayo wachimbaji wadogo na wakubwa.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Jimbo la Tunduru Kusini lina jumla ya vijiji 65, kati ya hivyo ni vijiji vinne tu ndiyo vimefikiwa na umeme wa REA Awamu ya I na ya II:-
Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA katika vijiji 61 vilivyobaki?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Idd Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza miradi ya kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini. Jimbo la Tunduru Kusini lina vijiji 65, kati ya vijiji hivyo Vijiji vinne vya Azimio, Chiwana, Mkandu na Mbesa ndivyo vimekwishapata umeme kupitia mradi wa REA II na Vijiji vingine vinne vya Mchuluka, Umoja, Masalau na Msinji vinatarajiwa kupatiwa umeme kupitia mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaoendelea na unaotegemea kukamilika mwezi Juni, 2020.
Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka umeme katika Jimbo la Tunduru Kusini inahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovolt 33 yenye urefu wa kilometa 9.4, ujenzi wa njia ya msongo wa umeme wa kilovolts 0.4 yenye urefu wa kilometa nane, ufungaji wa transfoma nne za KVA 50 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 275. Gharama za kupeleka umeme katika vijiji hivyo ni shilingi milioni 644.
Mheshimiwa Spoika, vijiji 57 vya Kata za Chiwana, Mchuluka, Mtina, Nalasi, Mchoteka, Ligoma, Tuwemacho na Lukumbulu vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya III, mzunguko wa pili unaotarajiwa kuanza mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2021. ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Jimbo la Tunduru Kusini lina changamoto ya maji kutokana na mabadiliko ya tabianchi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuchimba visima virefu na vifupi katika kata ya Tuwemacho, Mchuluka, Mchoteka, Mbati, Marumba, Wenje, Nasomba, Namasakata na Lukumbule.
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa maji naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate Mbunge wa Tunduru Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Jimbo la Tunduru Kusini lina jumla ya miradi mitano ya maji ya bomba kwenye vijiji 11. Miradi hiyo ipo kwenye Kata za Mbati, Nalasi, Namasakata, Misechela, Mtina, Ligoma, Mchesi na Lukumbule. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika Sekta ya Maji Help for Underserved Communities imechimba visima 72 katika Kata za Tuwemacho, Marumba, Lukumbule Mbesa na Mtina. Visima hivyo vimefungwa pampu za mkono. Vilevile Wilaya ya Tunduru kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Maji All Mother and Child Count imechimba visima virefu katika kata za Mchuluka, Namasakata, Chiwana na Lukumbule. Visima hivyo vitatumika kujenga miradi ya maji ya bomba katika maeneo hayo. Tayari utekelezaji umeanza kwa kata ya Chiwana na Namasakata
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha huduma ya maji inakuwa ya uhakika katika Wilaya ya Tunduru, Serikali kupitia Wakala ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini imetenga na kutoa fedha katika bajeti ya mwaka 2019/2020 kiasi cha shilingi milioni 974 kwa ajili ya kujenga, kukarabati na kufanya upanuzi wa miradi ya maji katika vijiji mbalimbali vilivyopo wilaya hiyo vikiwemo vijiji vya Jimbo la Tundurru Kusini. Vijiji hivyo ni Mbesa, Airport, Nasomba, Namasakata, Chiwana, Semeni, Nalasi, Misechela, Angalia, Ligoma na Mchekeni. Aidha, Serikali imepanga kuchimba visima Virefu viwili katika vijiji vya Wenje na Likweso vilivyopo Jimbo la Tunduru Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga na kutoa fedha kadri zinavyopatikana ili kuweza kujenga na kukarabati miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Jimbo la Tunduru Kusini ili wananchi waweze kunufaika na huduma ya majisafi na usafi wa mazingira.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Jimbo la Tunduru Kusini limepakana na Msumbiji kupitia Mto Ruvuma kuanzia mpaka wa Wilaya ya Nanyumbu na Wilaya ya Namtumbo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua barabara ya ulinzi inayounganisha mikoa yote ya Kusini yaani Mtwara na Ruvuma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate Mbunge wa Tunduru Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara anazozungumzia Mheshimiwa Mbunge ni barabara ya Mahangamba, Madimba, Tangazo, Kitaya, Mnongodi, Mapili, Mitemaupinde yenye urefu wa km 351 na barabara ya Mtwara pachani Lusewa, Tunduru yenye urefu wa km 300 zinazohudumiwa na Wakala wa barabara Tanzania TANROADS Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa kutambua umuhimu wa barabara hizi, hasa kwenye ulinzi wa mipaka ya nchi yetu Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mtwara tayari imefungua sehemu ya barabara kuanzia Mahangamba, Madimba, Tangazo, Kitaya na Mnongodi – Mapili yenye urefu km 216 kwa kiwango cha changarawe. Katika mwaka wa fedha 2019/ 2020 jumla ya shilingi bilioni mbili na milioni mia nane sabini na nane zimetengwa kwa ajili ya kuendelea kufungua km 90.4 za barabara hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma inaendelea kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka zabuni kwa sehemu ya barabara ya Mtwara - Pachani, Lusewa – Tunduru ambapo kazi hiyo imefikia asilimia 65.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Pamoja na Serikali kuendelea kufungua barabara hizo Serikali inaendelea kuzifanyia matengenezo mbalimbali sehemu ya barabara iliyofunguliwa ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Kituo cha Polisi Lukumbule kiliungua moto miaka iliyopita na mpaka sasa kituo hicho hakina Askari kimefungwa:-
(a) Je, ni lini Serikali itakirejesha kituo hicho hasa ikizingatiwa kuwa kipo mpakani mwa nchi ya Msumbiji?
(b) Je, ni lini Serikali itaweka kituo cha Uhamiaji katika kituo hicho cha Lukumbule?
(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Lukumbule ambacho kimeishia kwenye lenta baada ya Halmashauri kushindwa kumalizia ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Idd Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi Lukumbule kilichomwa moto mwaka 2013 na baadhi ya wananchi wasiotaka kutii sheria katika eneo hilo. Baada ya tukio hilo Jeshi la Polisi kwa kutambua kwamba eneo husika ni la mpakani na nchi ya Msumbiji limekuwa likifanya doria za mara kwa mara na pia kushirikisha taasisi nyingine za Serikali ambazo ni wadau wa ulinzi na usalama katika kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kwa wananchi wa eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa kufungua Kituo cha Uhamiaji Kata ya Lukumbule upo kwenye hatua za mwisho na inatarajiwa kufanguliwa wakati wowote mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuupongeza uongozi wa Halmashauri ya Tunduru kwa ujenzi wa kituo cha Polisi cha Lukumbule ingawa bado ujenzi wake haujakamilika. Hata hivyo, Serikali inatambua umuhimu na uhitaji wa kituo cha Polisi katika eneo hilo. Aidha Serikali kupitia Jeshi la Polisi itafanya tathmini ili kubaini gharama halisi za kukamilisha sehemu ya ujenzi uliobakia na kuona uwezekano wa kukamilisha ujenzi huo.
MHE. DAIMU I. MPAKATE Aliuliza :-
Jimbo la Tunduru Kusini limepakana na Nchi ya Msumbiji kwa upande wa Kusini.
Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Uhamiaji na cha Polisi kuhudumia maeneo hayo ya mpakani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada za ujenzi wa Kituo cha Polisi daraja “C” unaofanywa na Halmashauri ya Tunduru umefikia katika hatua ya lenta. Aidha, ujenzi wa Kituo cha Uhamiaji utategemea makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Msumbiji kama taratibu za ujenzi wa Vituo vya Uhamiaji mipakani unavyotaka. Kwa sasa makubaliano hayo bado hayajafanyika.
MHE. DAIMU I. MPAKATE Aliuliza:-
Jimbo la Tunduru Kusini limepakana na nchi ya Msumbiji kwa upande wa Kusini.
Je, ni lini Serikali itafungua Ofisi za Mamlaka ya Mapato (TRA) Lukumbule?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini kwa kutambua umuhimu wa kulipa kodi na hivyo kuhitaji huduma za kikodi zisogezwe karibu yao. Ni dhamira ya Serikali kutumia fursa kama hii kusogeza karibu huduma za kikodi kwa wananchi ili kurahisisha ulipaji na ukusanyaji wa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inao utaratibu wa kupitia na kufanya tathmini ya sehemu zote ambazo zinaweza kujengwa ofisi kwa ajili ya kurahisisha ukusanyaji wa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huu unazingatia uwiano wa gharama za ukusanyaji wa mapato na kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa pindi ofisi hizo zitakapofunguliwa kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mwenendo wa kukua kwa biashara kati ya Tanzania na Msumbiji, TRA inapenda kuwahakikishia wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini kuwa imelichukua suala hili na italifanyia kazi kwa kutuma timu ya wataalam ili kufanya tathmini ya kina na endapo kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa kitakuwa kikubwa ikilinganishwa na gharama za ukusanyaji wa mapato, ujenzi wa ofisi katika eneo hilo utaanza haraka iwezekanavyo.
MHE. DAIMU I. MPAKATE Aliuliza:-
Je, ni lini barabara ya Mtwara Pachani – Nallasi – Tunduru itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na utayarishaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mtwara Pachani – Lingusenguse – Nallasi Tunduru yenye urefu wa kilometa 300 kwa kiwango cha lami. Kazi hii ilitekelezwa na Mhandisi Mshauri GEG wa Ureno kwa gharama ya shilingi bilioni 2.559 na ilikamilika mwaka jana (2020). Kwa sasa, Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ujenzi wa kiwango cha lami ukisubiri upatikanaji wa fedha, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara nchini, inaendelea kuihudumia barabara hiyo ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka huu wa fedha 2020/2021, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 2.293 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hiyo.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza: -
Jimbo la Tunduru Kusini lina Vijiji sita kati ya 65 vyenye umeme.
(a) Je, ni lini REA Awamu ya Tatu utaanza?
(b) Je, ni lini umeme wa ujazilizi wa maeneo ambayo bado umeme haujafika hasa Vitongoji vya Vijiji vya Azimio, Chiwana, Umoja, Mkandu, Mbesa, Airport, Namasalau, Tuwemacho, Ligoma, Mchuruka na Makoteni vitapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini lenye sehemu (a) na
(b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa Pili ulianza mwezi Machi, 2021. Mradi huu utakamilika ifikapo mwezi Desemba, 2022. Katika jimbo la Tunduru Kusini Vijiji vyote vilivyobaki vitapelekewa umeme kupitia mradi huu wa REA-III unaoendelea kupitia Kampuni Mbili za Wakandarasi M/S JV Guangdong Jianneng Electric Power Engineering CO. LTD na White City International Contractors LTD. Gharama ya Mradi ni shilingi bilioni 27.25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usambazaji wa umeme wa ujazilizi katika vijiji vya Jimbo la Tunduru Kusini vikiwemo vitongoji vya Vijiji vya Azimio, Chimwana, Umoja Mkandu, Mbesa, Airport, Namesalau, Tuwemacho, Ligoma, Mchuruka na Makoteni utaanza mwezi Septemba, 2021 na kukamilika mwezi Desemba, 2022.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza: -
Je, ni lini Mkandarasi wa umeme wa REA ataanza kazi ya kusambaza umeme katika Jimbo la Tunduru Kusini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza kusambaza umeme nchini kuanzia Mwezi Mei, 2021 ambapo Kampuni ya M/S Guangdong Jianneng Electric Power Engineering Co. LTD imepewa kazi hiyo katika Wilaya ya Tunduru ikiwa ni pamoja na Jimbo la Tunduru Kusini.
Mheshimiwa Spika, kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa kilomita 639 za njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33, njia za umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 80, ufungaji wa transfoma 80 na uunganishaji wa wateja wa awali wapatao 1,760. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 36.67.
Mheshimiwa Spika, Mkandarasi kwa sasa anakamilisha usanifu wa kina na uletaji wa vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya umeme. Mradi unatarajiwa kukamilika Mwezi Desemba, 2022 na kufikisha huduma ya umeme katika vijiji vyote 80 vilivyokuwa vimebaki bila umeme katika Wilaya ya Tunduru.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mtwara Pachani, Lusewa, Nalasi hadi Tunduru yenye urefu wa kilomita 320 kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Mtwarapachani – Lusewa – Nalasi – Tunduru yenye urefu wa kilomita 300 ni barabara ya mkoa na inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na utayarishaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami imekamilika mwaka 2020. Baada ya usanifu kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, wakati tukisubiri upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hiyo ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, jumla ya shilingi milioni 1,960.583 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali na ukarabati wa madaraja kwenye barabara hii. Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi barabara ya Tunduru – Namasakata – Misechela kuwa ya Mkoa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007 na Kanuni zake za Mwaka 2009, imeainisha vigezo na utaratibu wa kupandisha au kuteremsha hadhi barabara toka daraja moja kwenda daraja lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaielekeza Halmashauri ya Wilaya Tunduru kupitia TARURA kufuata utaratibu huo ili kuiweka barabara hiyo katika mpango wa kupandishwa hadhi na kuwa ya Mkoa.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kurejesha Kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Tunduru ili kuimarisha ulinzi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama iufatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha ulinzi katika mipaka ikiwa ni pamoja na mpaka wa Kambi ya Wananchi wa Jeshi la Tanzania Tunduru na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ipo katika mchakato wa kurejesha Kambi ya Jeshi la Wananchi Wilayani Tunduru. Tayari Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imekwishaomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kambi hiyo toka Wizara ya Fedha na Mipango.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha Shule za Sekondari za Mchoteka na Nalasi kuwa za kidato cha tano na kidato cha sita Wilayani Tunduru?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge Jimbo la Tunduru, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili shule ya sekondari iwe na hadhi ya kidato cha tano na sita inatakiwa iwe na vyumba vya madarasa viwili kwa mkondo mmoja, matundu ya vyoo manne, bweni, maktaba/chumba cha kusomea, jiko na bwalo la chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa shule za sekondari Mchoteka na Nalasi bado hazijakidhi vigezo vya kuwa na kidato cha tano na sita. Aidha, kwakutambua umuhimu wa shule hizo, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya shule hizo ili ziwe na vigezo vya kupandishwa hadhi na kuwa za Kidato cha Tano na Sita.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga shule ya Kidato cha Tano na Sita katika Jimbo la Tunduru Kusini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Idi Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uhitaji wa shule za kidato cha tano na sita kwa maeneo mengi hapa nchini, Shule ya sekondari ya Mchoteka katika jimbo la Tunduru, wazazi pamoja na halmashauri walijenga hosteli mbili ambazo zimekamilika; hostel moja ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshapeleka kiasi cha shilingi milioni 160 kwa ajili ya kuongeza miundombinu mingine ili kukidhi vigezo vya kupandisha hadhi shule. Hata hivyo, shule hii imeombewa usajili wa mkondo walau mmoja wa kidato cha tano.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Mahakama katika Makao Makuu ya Tarafa za Nalasi, Lukumbule na Namasakata – Tunduru?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama inaendelea na utekelezaji wa Mpango wa ujenzi wa Mahakama hizi ambapo Mahakama ya Mwanzo ya Nalasi inajengwa katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 ikiwa ni sehemu ya Mahakama za Mwanzo 71 zitakazojengwa nchi nzima. Tayari Mshauri Mwelekezi ameanza kufanya kazi, na mradi unatarajiwa kuanza Oktoba, 2023 na kukamilika kabla ya Juni, 2024. Mahakama za Mwanzo za Lukumbule na Namasakata zitaingizwa kwenye mpango ujao wa miaka mitano sambamba na tarafa nyinginezo nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika bajeti ya mwaka huu wa fedha moja ya Mahakama za Wilaya zitakazojengwa ni Wilaya ya Tunduru, ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaboresha Kituo cha Afya Mtina ili kiweze kutoa huduma ya upasuaji pamoja kupeleka vifaatiba katika Kituo cha Afya Mchoteka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga shilingi millioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la upasuaji, jengo la mama na mtoto na maabara katika Kituo cha Afya cha Mtina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga shilingi bilioni 47.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba kwa ajili ya vituo vya afya 159 ambavyo vimekamilika ikiwa ni pamoja na Kituo cha Afya Mchoteka, ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaboresha Kituo cha Afya Mtina ili kiweze kutoa huduma ya upasuaji pamoja kupeleka vifaatiba katika Kituo cha Afya Mchoteka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga shilingi millioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la upasuaji, jengo la mama na mtoto na maabara katika Kituo cha Afya cha Mtina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga shilingi bilioni 47.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba kwa ajili ya vituo vya afya 159 ambavyo vimekamilika ikiwa ni pamoja na Kituo cha Afya Mchoteka, ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza: -
Je, lini wananchi wa Kata za Nalasi Tunduru watapata maji ya uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu,
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kata mbili za Nalasi Mashariki na Nalasi Magharibi zenye jumla ya ya wakazi 21,989; na vijiji saba vya Nalasi, Wenje, Lipepo, Mkapunda, Lukumbo, Nasomba na Chilundundu zinapata huduma ya maji kupitia Skimu ya Maji ya Nalasi na Nasomba zilizojengwa mwaka 2012. Katika kuboresha huduma ya maji kwenye kata hizo, Serikali katika mwaka wa fedha 2023/2024 itafanya ukarabati wa miradi hiyo ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Novemba, 2023 na kukamilika Februari, 2024.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia katika mwaka huu wa sedha 2023/2024, itafanya utafiti wa maji chini ya ardhi pamoja na kuchimba visima virefu vya maji katika Vijiji vya Nalasi, Wenje na Mkapunda ili kupata vyanzo vya uhakika vitakavyosaidia kujenga mradi mkubwa wa usambazaji maji utakaoweza kuhudumia vijiji vyote vya Kata zote mbili za Nalasi Mashariki na Nalasi Magharibi. Kazi ya utafiti wa uchimbaji visima hivyo, inatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Novemba, 2023 na kukamilika Februari, 2024.
MHE. YAHYA A. MHATA K.n.y. MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Je, lini Serikali itaajiri Madereva na Mafundi ambao wamekuwa vibarua wa muda mrefu TANESCO?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limekuwa likiajiri watumishi wa kada mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya kiuendeshaji na uwezo wa kibajeti kwa mwaka husika. Katika ikama na bajeti ya mishahara ya mwaka 2024/2025 pamoja na mambo mengine, shirika limetenga fedha kwa ajili ya nafasi 430 za ajira mpya kwa mchanganuo ufuatao:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wahandisi 67, fundi sanifu 135, fundi mchundo 205 na madereva 23. Aidha, ujazaji wa nafasi hizi utazingatia sheria na taratibu katika utumishi wa umma. Ahsante. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa ghala la mazao Wilayani Tunduru lililoanza kujengwa na Bodi ya Korosho mwaka 2014?
WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa ghala la Tunduru ulisimama baada ya Serikali kusitisha Mfuko wa Kuendeleza zao la Korosho ambao moja ya majukumu yake ilikuwa ni ujenzi wa ghala. Aidha, Serikali imekakilisha majadiliano na mkandarasi aliyekuwa anajenga ghala hilo ili kuruhusu ujenzi kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2024/2025, Serikali imetenga jumla ya shilingi 5,000,000,000 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ghala za korosho katika Halmashauri ya Mkuranga, Mkinga na Tunduru ambazo ujenzi wake ulianza mwaka 2015. Bodi ya Korosho inakamilisha taratibu za manunuzi ili kuanza ujenzi wa ghala hizo.