Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Luhaga Joelson Mpina (17 total)

MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-
Hivi karibuni ulifanyika Mkutano wa Dunia wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Mazingira (COP21) ambapo Katibu Mkuu wa UN alisema Mkataba uliofikiwa ni momental triumph for people and our planet aimed at ending poverty, strengthening peace and ensuring life of dignity and opportunity to all:-
(a) Je, Serikali ya Tanzania ilishiriki vipi katika Mkutano huo?
(b) Je, Serikali itatekelezaje maazimio ya Mkutano huo kisera, kisheria na kiutendaji?
(c)Je, Serikali ina mikakati gani ya kupambana na umaskini, kuimarisha amani, heshima na fursa sawa kwa kila mtu?
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Mkutano wa 21 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi ulifanyika Paris, Ufaransa tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba, 2015. Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Begum Karim Taj, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, wataalam kutoka Ofisi ya Makamu Rais, Kilimo na Zanzibar walishiriki pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushiriki wa Tanzania katika Mkutano huu ulilenga kutekeleza msimamo wa Tanzania katika majadiliano ikiwa ni pamoja na:-
(i) Upatikanaji wa fedha na teknolojia za kushughulikia mabadiliko ya tabianchi;
(ii) Upunguzaji wa gesijoto kwa ajili ya nchi kwa kuzingatia historia ya chanzo cha mabadiliko haya na uwezo wa nchi husika kukabiliana na tatizo hilo;
(iii) Kuweka kipaumbele katika uhimili wa mabadiliko ya tabianchi kwa sekta zote; na
(iv) Kushiriki katika miradi ya kupunguza gesijoto na nchi zilizoendelea kuendelea na jukumu la kutoa feda na tekinolojia kwa nchi zinazoendelea.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itatekeleza maazimio ya Mkutano huo kisera, kisheria na kiutendaji kwa kufanya yafuatayo:-
(i) Tanzania inatarajia kutia saini Mkataba wa Makubaliano ya Paris kati ya tarehe 22 Aprili, 2016 na 21 Aprili, 2017. Hatua hii itaimarisha utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012.
(ii) Serikali pia itahakikisha kuwa Tanzania inanufaika na fursa zilizo chini ya Mfuko wa Dunia wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund), unaofadhili shughuli za Mkataba wa Makubaliano ya Paris.
(iii) Aidha, Serikali itaendelea kuzibana nchi zote zenye kuzalisha hewa ya ukaa ili zipunguze uzalishaji huo kulingana na misingi ya utekelezaji wa Mkataba huo.
(iv)Zaidi ya hayo, Serikali itaendelea kuwasiliana na washirika wa maendeleo ili kuanzisha maeneo ya ushirikano kwa muktadha wa utekelezaji wa Mkataba wa Paris.
(v) Mwisho Serikali itaimarisha juhudi na kujenga uwezo wa elimu kwa umma kuhusu athari za mazingira ya tabianchi na namna ya kukabiliana nazo ili kuimarisha juhudi za kuhimili athari za mabadiliko haya.
(c)Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza mkakati wa kupambana na umaskini, kuimarisha amani, heshima na fursa sawa kwa wote. Mikakati hiyo ni kama MKUKUTA, MKUZA, MKURABITA, na matumizi ya Mifuko mbalimbali katika kukabiliana na tatizo hili kama vile; Mfuko wa Mazingira, Mfuko wa Jamii chini ya Ofisi ya Rais TASAF, Benki ya Wakulima, Benki ya Wanawake na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, juhudi kwa sasa za Serikali ya Awamu ya Tano za kupambana na ufisadi, kuimarisha utawala bora, uadilifu na uwajibikaji, zitatoa mchango mkubwa katika kuleta amani na maendeleo kwa wananchi wote. Kujenga uwezo na kuimarisha ushirikishwaji wa Serikali za mitaa katika utekelezaji wa miradi ya mabadiliko ya tabianchi unazingatiwa ili fursa zinazopatikana ziwafikie Watanzania wengi zaidi kadri iwezekanavyo.
MHE. ALI HAFIDH TAHIR aliuliza:-
Rais wa Tanzania wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete wakati akitembelea Kijiji cha Kichako Punda Uwandani katika Shehia ya Maungani Jimbo la Dimani tarehe 25 Januari, 2008 aliahidi ujenzi wa Kituo cha Afya kwa wananchi wa Kichaka Punda Uwandani pamoja na kuweka umeme na maji kutoka Kijiji cha Jitimai hadi Skuli.
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hizo za muda mrefu?
(b) Je, Serikali itakubaliana nami kuwa utekelezaji wa ahadi hizo utaongeza ari katika umoja uliopo ikiwa ni pamoja na kuimarisha Muungano?
NAIBU WAZIRI (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hafidh Tahir, Mbunge wa Dimani lenye sehemu (a) na (b)kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Mheshimiwa Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa ahadi ya ujenzi wa Kituo cha Afya kwa wananchi wa Kichako Punda Uwandani katika Shehia ya Maungani Jimbo la Dimani pamoja na kuweka umeme kutoka Kijiji cha Jitimai hadi Skuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kuwa Serikali inazitekeleza ahadi hizo, Ofisi ya Wilaya ya Magharibi ilifanya mawasiliano na Wizara ya …

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kuwa Serikali inazitekeleza ahadi hizo, Ofisi ya Wilaya ya Magharibi imefanya mawasiliano na Wizara zinazoshughulikia Sekta za Afya na umeme kwa lengo la kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa haraka katika maeneo husika.
Kwa sasa wananchi wa Kichako Punda wanapata huduma ya afya kutoka Kituo cha Afya Kibondeni na kituo cha Afya cha Meli Tano Fuoni, ambavyo vyote hivyo umbali wake kutoka Kichako Punda siyo zaidi ya Kilomita tatu ambazo kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Zanzibar, masafa hayo yanakidhi haja ya upatikanaji wa huduma hizo. Hata hivyo, mipango ya kujenga Kituo cha Afya katika eneo hilo bado inaendelea kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ahadi ya upatikanaji wa huduma ya umeme kutoka Kijiji cha Jitimai hadi Skuli, imeshatekelezwa; na kwa sasa huduma hiyo imeshafika katika kijiji hicho hadi Skuli.
Aidha, Ofisi yangu itaendelea kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge kufuatia utekelezaji wa ahadi ya Kituo cha Afya katika mamlaka husika ili ahadi hiyo iweze kutekelezwa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na hoja ya Mheshimiwa Mbunge kuwa mashirikiano kwa mambo yasiyo ya Muungano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ni jambo muhimu katika kuimarisha Muungano wetu.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa mara nyingi ikihakikisha Muungano wetu unaimarika kwa kusaidia juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kutoa huduma kwa wananchi wa Zanzibar.
MHE. ALI HASSAN OMARY KING aliuliza:-
Tatizo la Mazingira ni tatizo mtambuka na tumeona jinsi Serikali ilivyojipanga kutatua tatizo hili kwenye maeneo tafauti:-
Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo la mazingira linalojitokeza la kudidimia kwa ardhi kwenye makazi ya watu?
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge wa Jang’ombe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa kumejitokeza tatizo la kudidimia kwa ardhi na nyumba za makazi ya watu kwa vipindi na maeneo tofauti katika maeneo ya Zanzibar hususani 1998 na 2015. Kufuatia matukio haya, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iliunda timu ya wataalam kutoka sekta mbalimbali ili kufanya utafiti wa kina na kubaini chanzo cha tatizo hili chini ya utaratibu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, kupitia Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti huo ulibaini sababu kubwa ya kudidimia kwa ardhi ni udhaifu wa ardhi hususani katika eneo la Jang’ombe ambalo liliwahi kuchimbwa udongo na mchanga kwa ajili ya kujengea nyumba za Mji Mkongwe katika kipindi cha zaidi ya karne tatu zilizopita. Uchimbaji huo uliacha mashimo makubwa yaliyofunikwa na udongo kidogo kidogo kwa miaka mingi na hatimaye maeneo hayo kujengwa nyumba za makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hiyo pia ilichangiwa na kujaa maji katika maeneo hayo kutokana na kiwango kikubwa cha mvua zilizonyesha katika miaka ya matukio yaani 1998 na 2015. Aidha, sababu nyingine zinazoweza kusababisha kudidimia kwa ardhi ni pamoja na udhaifu wa miamba ya chini ya ardhi kuhimili uzito wa majengo, maeneo husika kuwa na asili ya unyevu mkubwa (wetlands) pamoja na sababu zitokanazo na athari za mabadilliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuzuia madhara yanayotokana na kudidimia kwa ardhi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuchukua hatua zifuatazo:-
(i) Kuyafanyia uchunguzi wa kina maeneo yote yenye matatizo ya kudidimia kwa ardhi na kuorodhesha nyumba zilizomo katika maeneo hayo na wahusika watapatiwa maeneo mengine kwa ajili ya kujenga nyumba za makazi ya kudumu. Hivi sasa upimaji wa viwanja 500 katika eneo la Tunguu unafanyika ili wananchi watakaohamishwa katika maeneo yanayodidimia wapatiwe viwanja. (Makofi)
(ii) Kuandaa utaratibu wa kudhibiti ujenzi holela katika maeneo ya miji na vijiji na kuboresha barabara na njia za maji ya mvua ili kuzuia madhara ya mafuriko na kudidimia kwa ardhi; na
(iii) Kuelimisha wananchi kupitia vyombo vya habari na matangazo kuhusu madhara ya mvua kubwa ikiwemo kudidimia kwa ardhi na mafuriko ili kuchukua tahadhari na kuepusha maafa.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
(a) Je, ni viongozi wangapi wa Kitaifa wametembelea Zanzibar kuanzia mwaka 2010 - 2015?
(b) Je, Serikali haioni kwamba viongozi wa Kitaifa kutembelea Zanzibar inaleta chachu ya upendo kwa Wananchi na kuzidi kuimarisha Muungano wetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, viongozi wote wa Kitaifa, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitembelea Zanzibar.
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitembelea Zanzibar mara 20, Mheshimiwa Dkt. Gharib Mohammed Bilal ametembelea Zanzibar zaidi ya mara 30 na Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, ametembelea Zanzibar zaidi ya mara 12.
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na hoja kuwa, Viongozi wa Kitaifa kutembelea Zanzibar inaleta chachu ya upendo kwa wananchi na kuzidi kuimarisha Muungano wetu. Ziara za viongozi wa Kiataifa huambatana na kuangalia utekelezaji wa shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa, kuongea na wananchi na kutoa maagizo na maelekezo kwa viongozi wa Serikali. Aidha, ziara hizo zinatoa fursa ya kufanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa wa Zanzibar hali ambayo pia inastawisha Muungano wetu.
MHE. JORAM I. HONGOLI (K.n.y. MHE. EDWARD F. MWALONGO) aliuliza:-
Uchafuzi wa Mazingira unaosababishwa na mifuko ya plastiki ni mkubwa mno nchini:-
(a) Je, Serikali haioni sasa umefikia wakati wa kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwawezesha wadau wa mazingira kwa kuwanunulia mashine kwa mkopo ili waweze kuchakata plastiki hizo kuzifanya kuwa ngumu na bora zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali inaona umuhimu wa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki nchini. Katika kutekeleza hatua hii Serikali imepitia upya kanuni ya kuzuia uzalishaji, uagizaji, uuzaji, ununuzi na matumizi ya mifuko ya plastiki ya mwaka 2006 ambayo ilikuwa inapiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki iliyo chini ya makroni 30 ambazo zilionekana kuwa na changamoto katika utekelezaji wake. Hivyo Serikali iliandaa Kanuni mpya ya matumizi ya mifuko ya plastiki ya mwaka 2015. Kanuni hizi zinaifuta kanuni ya mwaka 2006 na kuweka viwango vipya vya mifuko na vifungashio vya plastiki kuwa na unene usiopungua makroni 50 ambayo ina uwezo wa kuoza kirahisi kwenye mazingira ukilinganisha na ile ya makroni 30.
Pamoja na kuongeza unene wa mifuko ya plastiki, kanuni hii inapiga marufuku uanzishwaji wa viwanda vipya vya kutengeneza mifuko, vifungashio vya plastiki na pia inapiga marufuku uingizaji nchini wa mifuko ya plastiki ambayo ipo chini ya kiwango vilivyobainishwa na Kanuni. Hatua hii ni mwanzo wa kuelekea katika lengo la kupiga marufuku kabisa (total burn) uzalishaji na matumizi ya mifuko na vifungashio vya plastiki nchini kwa kuzingatia maoni ya wadau.
(b) Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha uwekezaji katika sekta ya mazingira na kuhamasisha uwekezaji katika teknolojia rafiki wa mazingira, Serikali inaandaa kanuni na taratibu za nyenzo za kiuchumi zitakazotoa ruzuku, makato na punguzo la kodi kwa wawekezaji ili kuendeleza na kuimarisha utunzaji wa mazingira. Hatua hii itasaidia wadau wa mazingira kuwekeza katika viwanda vidogo na vikubwa vya uchakataji wa taka ikiwemo taka za plastiki.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana na fasaha ya Naibu Waziri ningependa kuongeza na kulitaarifu rasmi Bunge lako Tukufu kwamba ndani ya Serikali tunafanya mazungumzo pamoja na kuwahusisha wadau mbalimbali na naamini wakati wa bajeti ya Wizara yetu tutakuwa tumefikia muafaka, dhamira ni kwamba tarehe 1 Januari, 2017 iwe mwisho wa matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini, lakini tutafika pahala ambapo uamuzi huo utakapofikia basi tutalitaarifu Bunge lako Tukufu.
MHE. AHMED JUMA NGWALI aliuliza:-
Tanzania iko kwenye mikataba mbalimbali na ushirikiano katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kama Green Climate Fund (GCF), Adaptation Fund (AF), Last Developed Countries Fund (LDCF), UNEP na kadhalika.
Je, Serikali imepokea fedha kiasi gani toka kwa wafadhili kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi tangu mwaka 2010 hadi 2015?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Ahmed Juma Ngwali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea fedha kutoka kwenye Mifuko iliyo chini ya Mikataba ya Mabadiliko ya Tabianchi na ushirikiano wa nchi wafadhili kiasi cha jumla ya Dola za Marekani 89,099,139.87, Euro 10,518,018.50, Shilingi za Tanzania 2,784,382,109/= kwa mchanganuo ufuatao:-
(i) Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund) chini ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, kiasi cha Dola za Marekani 1,324,200.32 zilipokelewa kuanzia mwezi Februari, 2013 hadi Oktoba, 2015. Jumla ya gharama zote za mradi huu ni Dola za Marekani 5,008,564 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Novemba, 2012 hadi Oktoba, 2017.
(ii) Mfuko wa Nchi Maskini Duniani (Least Developed Countries Fund) chini ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi kiasi cha Dola za Marekani 1,056,851.24 zilipokelewa kuanzia Juni, 2012 hadi Machi, 2017. Gharama zote za mradi huu ni Dola za Marekani 3,356,300.00 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Novemba, 2012 hadi Oktoba, 2017.
(iii) Jumuiya ya Ulaya (European Union) Awamu ya Kwanza mwaka 2010 hadi 2013 zilipokelewa Euro 1,975,025.00 Awamu ya pili ziliidhinishwa Euro 8,542,993.50, utekelezaji umeanza kwa mwaka wa 2014 ambao utakamilika mwaka wa 2018.
(iv) Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP), kiasi cha sh. 2,543,882,695/= zilipokelewa kuanzia Aprili, 2012 hadi Juni, 2015 wakati zilizoahidiwa zilikuwa ni Dola za Marekani 2,000,820,000.00.
(v) Serikali ya Norway kiasi cha Dola za Marekani 85,929,553.31 zilipokelewa kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2015.
(vi) Serikali ya Japan kupitia UNDP ilitoa kiasi cha Dola za Marekani 971,533 na Sh. 1,400,070,145 kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2013.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kiwango cha kubadilisha fedha kwa sasa, fedha hizi ni sawa na sh. 224,314,313,555.30 ambapo sh. 7,017,510,977.40 zilipokelewa Ofisi ya Makamu wa Rais na sh. 217,296,802,577.90 zilipokelewa moja kwa moja na wadau wengine wa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi zilipatikana baada ya kuandaa miradi kwa kuzingatia uwezo wa vipaumbele vya vyanzo vya fedha husika. Aidha, pamoja na fedha hizi, baadhi ya wafadhili hutoa fedha zao moja kwa moja kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, taasisi au sekta husika na asasi zisizo za kiserikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali limekuwa refu kulingana na lilivyoulizwa. Ahsante.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-
Mafuriko na uharibifu wa mazingira umewafanya wahanga wa matukio haya kukosa mahitaji muhimu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti mafuriko na uharibifu wa mazingira katika Mkoa wa Mara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua kadhaa za kukabiliana na tatizo la mafuriko na uharibifu wa mazingira Mkoani Mara. Hatua hizo ni kama ifutayo:-
Moja, kuelimisha wananchi kuhusu utunzaji wa hifadhi ya mazingira na madhara yatokanayo na kujenga kwenye mikondo ya maji na mabondeni ili kuepukana na athari za mafuriko na uharibifu wa vyanzo vya maji. Aidha, Kamati ya maafa ya Mkoa wa Mara, huratibu matukio ya maafa yatokanayo na mafuriko pale yanapojitokeza ikiwa ni sehemu mojawapo ya kupambana na athari ya mafuriko katika maeneo husika.
Pili, kubaini na kuwataka wakaazi wote wanaoishi mabondeni waliojenga katika maeneo ya mikondo ya maji, kuhama ili kuepuka athari za mafuriko sambamba na kulinda vyanzo vya maji.
Tatu, kuhimiza kampeni ya upandaji miti nchini, ambapo kila wilaya zikiwemo Wilaya za Mkoa wa Mara zinazopaswa kupanda na kutunza miti isiyopungua 1,500,000 kwa mwaka. Aidha, katika kuimarisha zoezi la upandaji miti nchini, Serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Upandaji Miti wa mwaka 2015 mpaka mwaka 2021, utakaotekelezwa kwa kushirikiana na taasisi za Serikali, mashirika binafsi katika maeneo yote nchini.
Nne, kusimamia na kuendeleza hifadhi ya misitu na kuwaondoa wavamizi wote katika hifadhi za misitu zilizoko Mkoani Mara. Mfano msitu wa Kinyanyali, Kalwilwi, Mrima Mkendo na Kalano, ambapo kaya sita zimeshaondolewa kutoka kwenye msitu wa Kinyang‟ali. Serikali itaendelea kuhimiza wananchi Mkoani Mara na nchini kote kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kwa kutokujenga na kufanya shughuli zisizo rafiki wa mazingira katika maeneo ya mabondeni na kwenye kingo za mito ndani ya mita 60 ili kuepuka uharibifu wa mazingira na athari zitokanazo na mafuriko.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA (K.n.y. MHE. ALBERT O. NTABALIBA) aliuliza:-
Wilaya ya Buhigwe ni Wilaya ambayo upandaji miti haujafanyika vya kutosha.
Je, Serikali haioni kuwa kuna haja ya kuweka bajeti juu ya zoezi hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwepo kwa changamoto kwa baadhi ya wilaya ikiwemo Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma kutokufanya vizuri katika zoezi la kupanda miti. Changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa mbegu, miche na aina ya miti inayofaa kupandwa kwa kila wilaya. Aidha, suala la ukame, upatikanaji wa maeneo na ardhi ya kupanda miti, usimamizi dhaifu wa viongozi na watendaji na mwitikio mdogo wa jamii navyo huchangia kukwamisha zoezi la upandaji miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona umuhimu wa kutenga bajeti kwa ajili ya zoezi la kupanda miti na kwa kutambua hilo, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 imetenga shilingi bilioni mbili katika Mfuko wa Mazingira ambazo zitatumika kwa ajili ya zoezi la upandaji miti nchini. Aidha, tunahimiza Halmashauri zote nchini na taasisi za umma na binafsi kutenga fedha kwa ajili ya kupanda miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nitumie fursa hii kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kushiriki katika upandaji miti na utunzaji wa miti. Aidha, ni matumaini yangu ya kuwa Waheshimiwa Wabunge watakuwa mstari wa mbele katika kushiriki na kuhamasisha wananchi kupanda na kutunza miti ili kuifanya Tanzania iwe ya kijani.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza:-
Kutokana na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea hivi sasa duniani pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira Mkoa wa Simiyu ni moja kati ya maeneo yaliyoathirika kwa kiwango kikubwa na kuna uwezekano mkubwa wa Mkoa huo kugeuka kuwa jangwa:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi wa kuunusuru Mkoa huo na hali hiyo;
(b) Kwa kuwa, hali hiyo inaathiri shughuli za kilimo hasa cha umwagiliaji; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha mazingira ya mito na mabwawa yanatunzwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi katika Mkoa wa Simiyu, Serikali inatekeleza programu ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi ijulikanayo kama Simiyu Resilient Development Programme. Programu hii ina lengo la kuwezesha jamii kuhimili mabadiliko ya tabianchi, hasa ukame kwa kujenga mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Wilaya zote za Bariadi, Meatu, Maswa na Itilima. Programu hii itatekelezwa chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji na utekelezaji wake utagharimu Euro milion 313 kutoka Mfuko wa Dunia wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) na Serikali ya Ujerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kunusuru Mkoa wa Simiyu pamoja na maeneo mengine nchini kutokana na athari ya mabadiliko ya tabianchi na uharibifu mkubwa wa mazingira, Serikali imeweka Sera, Sheria na Mikakati mbalimbali ikiwemo Sera ya Taifa ya Mazingira 1997; Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004; Mkakati wa Hatua za Haraka za Kuhimili Mazingira ya Bahari, Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa ya mwaka 2008, Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012; na kampeni ya Kitaifa ya Upandaji Miti. Sera, sheria na mikakati hii inazitaka Halmashauri zote nchini kuandaa sheria ndogo za mazingira zitakazowezesha hifadhi ya mazingira ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi zikiwemo Halmashauri za Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inahimiza viongozi wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu kuhuisha mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika mipango ya maendeleo ili kunusuru Mkoa huo kugeuka kuwa jangwa.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE aliuliza:-

Kingo za Ziwa Victoria katika mwambao wa Manispaa ya Bukoba katika maeneo ya Kalobela Bandarini, Hoteli ya Spice, Kiroyela, Nyamukazi na Kifungwa zimelika na maji na mawimbi ya maji kusogea kiasi cha kuingia kwenye nyumba zilizoko kandokando mwa ziwa hilo na kuhatarisha maisha ya watu:-
(a)Je, Serikali inachukuliaje hali hii na inawatolea tamko gani wakazi wa maeneo hayo?
(b)Je, Serikali iko tayari kutafuta mfadhili au kuchukua hatua za kujenga ukuta imara wa kuzuia maji kusogea jambo linalooneka kuhatarisha ofisi za Makao Makuu ya Mkoa, nyumba ya Mkuu wa Mkoa na majengo ya Mahakama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwepo kwa mmomonyoko katika fukwe za Ziwa Victoria mwambao wa Manispaa ya Bukoba hali inayohatarisha baadhi ya majengo na miundombinu iliyojengwa karibu na maeneo hayo. Hali hii inawezekana kuwa imesababishwa na kuongezeka kwa kina cha maji na kasi ya mawimbi katika Ziwa Victoria kutokana na matukio ya vimbunga, upepo mkali na mvua nyingi yanayohusishwa na mabadiliko ya tabia nchi. Aidha, hali hii pia yaweza kuwa inasababishwa na uharibifu wa mazingira kando ya ziwa na mito inayoingiza maji ziwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa tamko kwa wakazi wa maeneo ya fukwe za Ziwa Victoria na maeneo mengine nchini kuacha kufanya shughuli za kudumu za kibinadamu zenye athari kwa mazingira ndani ya eneo la mita 60 kutoka kwenye kingo za ziwa kwa mujibu wa kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004. Hatua hii itasaidia kuzuia uharibifu wa mazingira na madhara yanayoweza kutokea kutokana na mmomonyoko wa kingo za Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itafanya tathmini ya kina ili kutambua chanzo na ukubwa wa tatizo na kuchukua hatua stahiki za kuhimili athari hizo mara baada ya tathmini kufanyika. Ufadhili unaweza kutokana na vyanzo vya ndani, mifuko mbalimbali ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi kama vile Adaptation Fund, Least Developed Countries Fund, Green Climate Fund na wadau wengine wa maendeleo.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kunusuru Taifa na janga la mabadiliko ya tabianchi?
(b) Je, ni lini Serikali itahakikisha kwamba Ofisi za Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri zinakuwa na Idara ya Usafi na Mazingira inayojitegemea kuliko kuitegemea Taasisi ya NEMC ambayo inaonekana kuzidiwa na majukumu ya kudhibiti na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi?
(c) Je, Serikali ilipata ushauri gani kuiondoa Idara ya Mazingira kutoka kwenye Kamati ya awali ya Mazingira, Ardhi, Maliasili na Utalii na badala yake kupelekwa kwa Viwanda na Mazingira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali iliandaa Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012. Mkakati huo umeainisha vipaumbele vya kisekta na hatua za kuchukua ili kunusuru Taifa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Baadhi ya hatua hizo ni ambazo Wizara za sekta zimekuwa zikitekeleza ni pamoja na kuhimiza kilimo kinachozingatia mabadiliko ya misimu ya mvua, ufugaji endelevu, kuhifadhi vyanzo vya maji na misitu, ujenzi wa mabwawa ya maji, upandaji miti, matumizi ya nishati mbadala, ujenzi wa miundombinu imara ya barabara, madaraja na mifereji ili kuhimili mafuriko na matumizi ya teknolojia rafiki wa mazingira viwandani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huu unazingatia Wizara zote za kisekta na Serikali za Mitaa kuhuisha suala la mabadiliko ya tabianchi katika mipango yao.
Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama vile ujenzi wa kuta kwenye kingo za bahari, upandaji wa mikoko na kujenga uwezo wa wataalam kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI ilishatoa mwongozo wa uanzishwaji wa Idara ya Usafi na Mazingira katika Halmashauri zote nchini na Halmashauri nyingine zimeshaanzisha idara hiyo. Aidha, kutokana na changamoto za utekelezaji wa majukumu yake, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeandaa mapendekezo ya kuboresha muundo huo.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la muundo wa Kamati za Kudumu za Bunge ni jukumu la Ofisi ya Spika wa Bunge na Wizara haihusiki katika uandaaji wa miundo ya Kamati.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
Baadhi ya maeneo ya Halmashauri ya Mkalama ni kame sana.
Je, Serikali ipo tayari kusaidia mradi wa upandaji miti katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia nafasi hii kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau wengine ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Mkakati wa Taifa wa Miaka Mitano wa Kupanda Miti (2016/2017 hadi 2020/2021). Kiasi cha shilingi bilioni 105 zinahitajika ambapo kila mwaka imependekezwa zitengwe shilingi bilioni 20 kutoka vyanzo mbalimbali vya Serikali na wadau wa maendeleo kwa ajili ya kutekeleza mkakati huu ambao unaelekeza kila mwananchi, taasisi za Serikali, taasisi za madhehebu, asasi zisizokuwa za kiserikali, kambi za majeshi, magereza, shule, makampuni na kadhalika kupanda na kutunza miti katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na miaka mingine iliyopita, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini, itahakikisha kwamba miti inayopandwa inatunzwa na kukua. Aidha, visababishi vinavyochangia miti kutokuwa vimeainishwa na mikakati ya kudhibiti imeandaliwa ikiwa ni pamoja na upandaji wa aina ya miti kulingana na maeneo na utunzaji wa miti hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Allan Joseph Kiula kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza zoezi la upandaji miti kote nchini kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Wakala wa Misitu Tanzania na Halmashauri zote ikiwemo Halmashauri ya Mkalama ambapo kila Halmashauri
inatakiwa kupanda miti 1,500,000 kila mwaka na kuhakikisha inatunzwa. Aidha, pale itakapoonekana inafaa, Halmashauri zihakikishe maeneo ya wazi yanahifadhiwa ili kuruhusu uoto wa asili ulegee au kutumia mbinu zijulikanazo kama kisiki hai ambapo visiki vilivyo hai hutunzwa hadi kuwa miti mikubwa. Iwapo Mheshimiwa Mbunge ana maombi mahususi awasilishe Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ushauri na hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itasimamia utekelezaji wa mkakati wa taifa wa kupanda na kutunza miti na kuendeleza kuhimiza utekelezaji wa kampeni za upandaji miti na mikakati mingine inayolenga kupanda na kutunza miti nchini.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY Aliuliza:-
Maziwa Madogo nchini kama vile Ziwa dogo la asili la Tlawi katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu yanaelekea kukauka kutokana na kuongezeka kwa magugu maji, kadhalika Ziwa Babati na Ziwa Manyara pia yana dalili ya kukauka na Mamlaka za Serikali za Mitaa hazina uwezo wa kuyaokoa:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuyaokoa maziwa hayo muhimu katika ustawi wa nchi yetu na kizazi kijacho?
(b) Je, kwa nini kusiwe na mpango kabambe wa Kitaifa kuyaokoa maziwa hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaona umuhimu mkubwa wa kuokoa Ziwa dogo la Tlawi lililopo Halmashauri ya Mbulu na maziwa mengine kote nchini yanayokabiliwa na tishio la kukauka na magugu maji kutokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu hususan kilimo na ufugaji usio endelevu, uvuvi haramu na athari ya mabadiliko ya tabia nchi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu huo, mwaka 2008 Serikali iliandaa Mkakati wa Taifa wa Hatua za Haraka za Kuhifadhi Mazingira ya Bahari Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa. Mkakati huu unaelekeza Wizara na sekta na halmashauri zote nchini kuchukua hatua za haraka kuzuia shughuli zote za binadamu kufanyika kandokando ya maziwa, mito na mabwawa ili kuzuia uharibifu wa mazingira unaoweza kusababisha kukauka kwa maziwa hayo.
Mheshimiwa Spika, ili kunusuru Ziwa dogo la Tlawi, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imechukua hatua zifuatazo:-
1. Mradi wa DADP’s Wilaya ya Mbulu umetenga Shilingi milioni 100 katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 kwa ajili ya kuondoa magugu maji katika Ziwa Tlawi.
2. Katika Bajeti ya Mwaka 2017/2018, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imepanga kutenga kiasi cha Shilingi 15,742,000 ili kutekeleza shughuli za kunusuru Ziwa Tlawi pamoja na kuainisha mipaka ya ziwa hilo, uvamizi wa watu katika shughuli za kilimo, kuhimiza
kilimo endelevu pamoja na miinuko inayozunguka ziwa hilo, kutoa elimu kwa wananchi ya kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji, kuimarisha Kamati za Mazingira na ulinzi shirikishi kwa ziwa katika ngazi za kata, vijiji na mitaa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada zinazofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Serikali itafanya tathmini ya kina kubaini chanzo cha ukubwa wa tatizo na kuchukua hatua stahiki za ziada kuhimili athari katika Maziwa ya Tlawi, Babati na Manyara ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja kuwa yako kwenye tishio la kukauka.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. MARYAM SALUM MSABAHA) Aliuliza:-
Tangu mwaka 2005 kumekuwa na changamoto nyingi katika kero za Muungano:-
Je, mpaka mwaka 2016 ni kero ngapi zimeshapatiwa ufumbuzi wa kudumu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 hoja 15 ziliwasilishwa kutafutiwa ufumbuzi. Kati ya hoja 15 zilizowasilishwa ni hoja 11 zimeshapatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, Serikali zote mbili yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kushughulikia kero za Muungano kadiri zinavyojitokeza.
MHE. OMARI M. KIGUA Aliuliza:-
Serikali imekuwa ikisisitiza na kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kulinda na kutunza vyanzo vya maji kwa kutokata miti ovyo na kutojenga karibu na vyanzo hivyo, lakini wako baadhi ya wananchi wenye tabia ya kushirikiana na baadhi ya watumishi wachache wa Serikali kukata miti ovyo na kujenga karibu na vyanzo vya maji.
(a) Je, ni lini Serikali itasimamia kikamilifu sheria za kulinda mito na miti nchini?
(b) Je, Serikali haioni umefika wakati sasa kutunga sheria kali zaidi ili kujihami na global warming?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua changamoto za uharibifu wa vyanzo vya maji na misitu nchini, Serikali imechukua hatua za kisera, sheria na kimkakati kukabiliana nazo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004, kifungu cha 57(1) kinazuia shughuli yoyote ya kibinadamu yenye athari kwa mazingira kufanyika ndani ya mita 60 kutoka kwenye kingo za bahari, mito, maziwa na mabwawa ili kulinda vyanzovya maji.
Aidha, kifungu 55 cha sheria hiyo kimetoa mamlaka kwa Halmashauri kuweka miongozo ya kulinda vyanzo vya maji na kuchukua hatua kali kwa yeyote anayekiuka sheria. Vilevile Halmashauri zote nchini zimelekezwa kutunga na kusimamia utekelezaji wa sheria ndogo kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji na misitu katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Sheria ya Misitu ya mwaka 2002 imeweka utaratibu wa kusimamia na kuhifadhi ya misitu ikiwemo kutoa adhabu kwa uharibifu wa misitu na ukiukwaji wa miongozo ya uvunaji endelevu wa rasilimali za misitu. Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji na kuchukua hatua kali kwa wote wanaokiuka Sheria hizi kwa lengo la kulinda vyanzo vya maji na misitu nchini.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 75 (a) mpaka (e) inaelekeza hatua za kuchukua ili kulinda na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na kuongezeka kwa joto la duniani yaani global warming, katika sekta mbalimbali nchini. Aidha, Serikali itaendelea kuhamasisha utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012 kupitia sekta, halmashauri, taasisi za umma na binafsi katika kutekeleza miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika maeneo yaliyoathirika.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Uharibifu wa mazingira nchini umeleta athari kubwa ya mabadiliko ya msimu wa kilimo, uhaba mkubwa wa maji na kukauka kwa vyanzo vya maji nchini.
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani za makusudi za kudhibiti uharibifu huo wa mazingira hasa katika ukataji wa miti?
(b) Je, Serikali inasema nini juu ya kupanda miti katika mashamba ya Serikali na ya watu binafsi ili kusaidia kuondoa hali hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira zinazolikabili taifa hili, Serikali imechukua hatua zifuatazo; kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaokamatwa wakikata miti bila vibali kwa mujibu wa Sheria, kutoa elimu ya mazingira kwa umma ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira hasa misitu na kuhamasisha wananchi kutumia nishati mbadala kama gesi na umeme pamoja na matumizi ya majiko banifu ili kupunguza matumizi ya mkaa na kuni.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeandaa mkakati wa Taifa wa kupanda na kutunza miti unaolenga kuhamasisha upandaji miti katika maeneo ya mashamba na viwanja vilivyo wazi, ikiwemo mashamba ya Serikali na watu binafsi ili kudhibiti hali ya uharibifu wa ardhi nchini. Katika kufanikisha mkakati huu jamii wadau mbalimbali watahusishwa katika utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati umeweka muundo wa kitaasisi wa utekelezaji unahosisha wadau wote ikiwemo Wizara za Kisekta na Idara nyingine za Serikali, asasi zisizokuwa za kiserikali, asasi za kiraia, vijiji, shule, taasisi za dini na sekta binafsi. Kupitia mkakati huu, Serikali imepnga kupanda miti katika hekari laki 185,000 kila mwaka ambazo ni sawa na miti milioni 280. Mkakati huu utatekelezwa ipasavyo na utapunguza uharibifu wa misitu na urejeshaji wa uoto nchini.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI aliuliza:-

Katika Mkoa wa Kagera kuna Ranchi za Taifa zipatazo nne ambazo ni Kagoma, Mabare, Kitengula na Missenyi:-

Je, ni lini Serikali itajenga Kiwanda cha kuchakata ngozi katika Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) K.n.y. WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alfredina Kahigi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba uwepo wa Ranchi za Taifa Kagoma, Mabare, Kitengula na Missenyi pamoja na uwepo wa mifugo mingi katika Mkoa wa Kagera kunatoa fursa kubwa ya uwekezaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo. Aidha, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO)imeandaa mpango mkakati wa kibiashara wa miaka mitano kuanzia mwaka 2017 mpaka mwaka 2022 kwa lengo la kuendeleza na kueneza ufugaji bora hususan ufugaji wa ng’ombe bora wa nyama aina ya boran kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi kwa kutumia mbinu za kisasa. Mpango huu pia unalenga kusaidia NARCO kuingia ubia na kampuni ambazo zinaweza kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo ikiwemo ngozi.

Mheshimiwa Mwenyeki, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Chuo cha DIT, campus ya Mwanza, umeandaliwa mpango kazi kwa kutoa mafunzo kwa vikundi vya vijana na akina mama hususan namna ya kusindika ngozi na uzalishaji wa bidhaa za ngozi, ambayo yakitumika ipasavyo yatasaidia kuongeza wigo wa kimasoko wa zao la ngozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Sekta ya Mifugo, katika Mkoa wa Kagera, Wizara inashirikiana na Wizara ya Viwanda pamoja na Kituo cha Uwekezaji (TIC), kuendelea kutangaza fursa hizo na kutafuta wawekezaji makini wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya kuchakata nyama, ngozi na mazao mengine ya mifugo ili kusaidia kutoa ajira kwa wananchi wa Kagera, kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na kuongeza kipato cha wafugaji.