Answers to supplementary Questions by Hon. Mussa Ramadhani Sima (23 total)
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, moja ya sababu inayosababisha mabadiliko ya tabianchi ni uharibifu wa mazingira kwa ukataji miti. Kwa kuwa hapa nchini ukataji miti uko kwa juu sana kwa sababu watu wengi tunategemea nishati ya kuni au mkaa kwa ajili ya mapishi nyumbani na shughuli nyinginezo. Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba huu uharibifu wa mazingira kwa kutumia nishati hizi ambazo zinapunguza idadi ya miti nchini inakuwa imepunguzwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, majibu ya Serikali inaonesha kwamba wale wachafuzi wa mazingira kupitia viwanda hutozwa faini au baadhi kufungiwa. Serikali haioni kwamba inafaa iwe na mikakati mahsusi ya kudhibiti viwanda hivi kuangalia miundombinu yake kabla haijaanza kazi kwamba haitakuwa inaharibu mazingira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwa nishati mbadala na sisi tumekuwa tukisisitiza na tumeanza mkakati huo na tumeshirikisha na ndugu zetu wa TFS sasa wanatoa miti ambayo inahimili ukame na wanatenga maeneo maalum kwa ajili ya kuvunwa na maeneo maalum kwa ajili ya hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia swali la pili namna ya kudhibiti wamiliki wa viwanda, kama ambavyo nimeeleza kwenye majibu yangu ya swali la msingi kwamba tutaendelea kuzingatia sheria ileile. Niwaombe wamiliki wa viwanda wajue kabisa kwamba wanao wajibu wa kuyatunza mazingira na wanao wajibu wa ku-treat yale maji ambayo yanaleta zile taka hatarishi. Ahsante sana.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uchafuzi wa viwanda, vilevile mifuko ya plastick ni source mbaya sana ambayo inachafua mazingira. Je, kwa nini Ofisi ya Makamu wa Rais haitumii ule Mfuko wa Technological Transfer and Adaptation Fund kuwawezesha hao wenye viwanda wabadilishe teknolojia waweze kuzalisha mifuko ambayo ni rafiki kwa mazingira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa mifuko ya plastick imekuwa ikileta uchafuzi wa mazingira kwa kiasi kikubwa sana. Niseme tu kwamba, Serikali tayari ilishazuia kutoa leseni mpya kwa wazalishaji ama viwanda vipya vinavyokuja kwa ajili ya mifuko ya plastic. Pia, tumeendelea ku-encourage wawekezaji wa viwanda vya mifuko rafiki ili waweze kuwekeza na hatimaye huko mbele tuweze ku-ban kabisa mifuko ya plastic.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yake amesema kwamba wale wanaokiuka taratibu hizi sheria inawapa mamlaka ya kuwafungia ama kuwapiga faini, zote hizo ni force approach. Dunia ya leo ni dunia shirikishi, Wizara ina mpango gani wa kuwashirikisha na kuwaelimisha wenye viwanda na kushirikiana nao kuona tatizo hili linamalizwa kabisa badala ya kutumia nguvu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kwamba kabla ya mwekezaji kuanza kuwekeza hatua ya kwanza sisi huwa tunatoa elimu. Mpaka afikie hatua ya kupata certificate ya EIA, maana yake amekidhi vigezo vyote. Kinachofuata akikiuka utaratibu ambao tumeuweka ni lazima tumpige faini.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuteuliwa lakini vilevile nimpongeze kwa ufafanuzi mzuri. Pamoja na ufafanuzi, ninayo maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Swali la kwanza, maeneo yenye rasilimali muhimu kama hayo ya Ziwa Rukwa pamoja na maelekezo mazuri ya Serikali yanahitaji ufuatiliaji na usimamizi wa karibu. Je, toka Serikali imetoa maelekezo hayo umefanyika ufuatiliaji kujiridhisha kama mazingira hayo hayaharibiwi tena?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, rasilimali muhimu ya gesi ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia inaweza kuinua uchumi wa Tanzania na kukuza uchumi wa Taifa letu kwa ujumla. Je, Serikali ina mkakati gani kuanza kuchimba gesi hiyo ili Taifa linufaike kabla gesi hiyo haijaanza kuchimbwa mahala pengine duniani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Malocha pia kwa ufuatiliaji wake mzuri na nimshukuru kwamba sasa kwenye eneo hili la Ziwa Rukwa tunaweza kuelekeza nguvu kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza linahusu ufuatiliaji. Kwa kweli tuna kila sababu ya kushirikiana naye kwa ajili ya kufuatilia hili kwa kushirikiana na wananchi na viongozi walioko kule. Mheshimiwa Malocha nadhani baada ya Bunge hili tutakuwa pamoja kwa ajili ya kwenda kufuatilia kuona yale maagizo ambayo ameyatoa Mheshimiwa Waziri yametekelezeka kwa kiwango gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye eneo la gesi, ni kweli kabisa imegundulika gesi hii ya helium ambayo ni maalum kabisa katika nchi yetu na sisi kwenye eneo letu la mazingira tayari imeshafanyika Tathimini ya Athari ya Mazingira kwa awamu ya kwanza kwa ajili exploration. Atakapopatikana mwekezaji kwa awamu ya pili tutakuwa tayari kuja kufanya tena Tathmini ya Athari ya Mazingira ili kuhakikisha kwamba gesi hiyo inapatikana na kuweza kutumika. Ahsante sana.
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante lakini nachuka fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ambayo yametoa mchanganuo mzuri na unaleta matumaini na tunatarajia kwamba hizo changamoto zitatatuka karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwongozo huo haufuatwi katika mashirika ya Muungano, je, Serikali lini itatoa utaratibu huo wa mwongozo katika mashirika ya Muungano kuona na yenyewe yanafuata utaratibu huu katika ajira?
Swali langu la pili ni kwamba utaratibu huu umekuwa ukifuatwa kama ambavyo umeelezea, lakini bado umekumbwa na changamoto, kuna mfumo gani ambao unafuatwa ili kufanya assessment kuona kwamba huu utaratibu liowekwa unafuatwa katika taasisi zote za Muungano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Saada Mkuya, lakini pia na mimi nichukue fursa ya kumpongeza kwamba mara nyingi tumekuwa tukishirikiana kwa namna ambavyo tunaweza kutatua changamoto za Muungano, lakini kama nimeeleza kwenye majibu yangu ya swali la msingi kwamba tayari mashirika haya tumeyapa mwongozo na suala kubwa sasa ni ufuatiliaji kwa namna gani wanatekeleza mwongozo ule.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia suala la pili juu ya assessment, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira tunawajibika moja kwa moja kupata taarifa kutoka kwa wenzetu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu wa kufuatilia assessment huu tumeuweka vizuri na tumeweka bayana, tutakavyo kutana nitamuelekeza vizuri namna ambavyo tumetekeleza. Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongezee katika majibu mazuri aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo muhimu sana ambalo linatusaidia kuimarisha Muungano wetu. Lazima nikiri kwamba katika maeneo ambayo hatufanyi vizuri ni hili la uwiano wa watumishi katika Taasis za Muungano na Wizara za Muungano, lazima tukiri ukweli huo. Bahati nzuri maamuzi yalishatoka na sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais na kama Serikali katika kuhakiksha kwamba maamuzi hayo yanatekelezwa kwa haraka tumeshirikiana na wenzetu wa Ofisi ya Rais, Utumishi kuhakikisha kwamba wanafungua Ofisi Zanzibar na kuajiri na kutangaza na kufanya interviews kwa Zanzibar vilevile.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutampa jedwari la kuonesha kila taasisi ya Muungano iwe Benki Kuu iwe TCRA na watu ilionao, Wazanzibari na Wabara ili kuwe na uwazi na tusaidiane katika usukumaji wa jambo hili, hilo la pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa rai vilevile kwa vijana wa Zanzibar ambao wanaomba nafasi katika taasisi za Muungano kuandika address sahihi, kwa sababu msingi wa taarifa tunazopata ni anuani kwenye maombi. Kwa hiyo, wengine ni Wazanzibar lakini wanaandika anuani za Bara; kwa hiyo, hatupati taarifa sahihi kuhusu hasa idadi ya Wazanzibar na watu wa Bara katika nafasi hizi. Kwa hiyo, wito wangu ni kwamba ukiandika anuani sahihi inasaidia kupata takwimu sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingi Wazanzibar wapo wengi zaidi kuliko inavyoonekana kutokana kwamba walioomba kazi hiyo kutokea Bara na waliandika anwani za Bara.
MHE. ABDALLAH HAJI ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Niseme tu kwamba urasimu huu kwa kweli umekuwa ukitupa usumbufu mkubwa sana sana kwa majimbo ya Zanzibar. Nilikuwa naomba ikiwa hili suala halipo kisheria bora lifutwe ili na sisi hizi pesa tuzipate kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nina maswali ya nyongeza mawili madogo kabisa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mfuko huu wa Maendeleo ya Jimbo umeanzishwa mwaka 2009, takribani sasa ni miaka 10. Majimbo yamekua, watu wameongezeka na mahitaji yameongezeka vilevile lakini kiwango kinachotolewa hadi sasa ni kilekile. Je, Serikali ina mpango gani wa kuuongezea Mfuko huu fedha ili upate uweze wa kuendana na mahitaji ya majimbo yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwa na malalamiko kwa utendaji wa baadhi ya Wakurugenzi katika Halmashauri; wanakuwa hawatendi vizuri. Je, Waziri yuko tayari kuzitembelea Halmashauri hususani Halmashauri zetu za Zanzibar kukaa na Wabunge na Wakurugenzi wa Halmashauri ili kulizungumzia au kupeana uzoefu juu ya suala hili ili twende sambamba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hi kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdallah Haji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kabisa kweli kuna ongezeko la watu, mahitaji na vitu vingine lakini nimuahidi tu kwamba kuna haja ya kufanya tathmini ili kubaini hayo ambayo tunayasema sasa. Baada ya tathmini hiyo tutajua nini kifanyike kuhusiana na ongezeko la kiwango kinachotolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa kweli nimshukuru na mimi wakati wowote nitakuwa tayari kwenda Zanzibar na nimuahidi tu kwa sababu nakwenda Zanzibar mara nyingi, nitakuja tukae nanyi pamoja na Wakurugenzi wote kama ambavyo ameshauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina swali moja dogo sana kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi lilikuwa kuhusu ucheleweshaji wa fedha za Mfuko huu upande Zanzibar. Nimefuatilia majibu kwa makini sana, Mheshimiwa Naibu Waziri amejaribu kujibu kwa kiasi alichoweza. Kwa kuwa fedha hizi zinatoka kwenye Serikali ya Muungano na inachukua zaidi ya miezi sita, saba au nane, ametoa mlolongo wa taratibu jinsi fedha hizi zinavyokwenda Zanzibar, naomba atuambie mkakati gani wa ziada walio nao kurekebisha utaratibu huu ili kasoro hii iweze kuondoka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumjibu Mheshimiwa Masoud swali lake la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza utaratibu wa kisheria ambao tuna kila sababu ya kuufuata. Kwenye majibu yangu ya msingi nimesema pia kama ziko changamoto zingine za ucheleweshwaji tutafanya kila jitihada tunavyoweza ili fedha hizi zisichelewe. Niwahakikishie tu ndugu zangu na nichukue fursa hii kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hususani Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa namna inavyoratibu zoezi hili la kuhakikisha fedha hizi za Mfuko wa Jimbo zinafika kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri; hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza. Mji wa Mikindani ni miongoni mwa miji ambayo iko chini ya usawa wa bahari; kwa hiyo hii mifereji ninayoizungumzia ni ile ambayo maji ya bahari yakijaa inapitisha maji kuingia katikati ya mji na iko mingi na tangu zamani hii mifereji ilikuwa imejengewa lakini kutokana na uwezo mdogo wa halmashauri imeshindwa kuifanyia ukarabati mara kwa mara. Swali, je, Serikali iko tayari kuisaidia Manispaa ya Mtwara – Mikindani katika kukarabati mifereji hii ya Mji wa Mikindani kwa sababu kuiachia manispaa peke yake ni kuiongezea mzigo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kwenda Mikindani kuona hicho ninachokizungumzia ili aweze kunielewa zaidi na hatua za haraka ziweze kuchukuliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika,
nichukue fursa hii kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabla sijajibu swali na mimi nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zake na ushirikiano mkubwa ambao anatupa sisi Wizara ya Mazingira katika kukabiliana na hali hii ya mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na swali lake la kwanza; kwanza nipo tayari na tupo tayari pia kusaidia maeneo yote kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu langu la swali la msingi, kuhakikisha kwamba maeneo yote haya tunajitahidi ili tunakabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kupitia mifuko ambayo tunapata fedha kutoka kwa wenzetu, kwa maana ya Global Climatic Change.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu kwenda Mtwara. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ninayo ziara ya kuanzia tarehe 18 Iringa, lakini pia kwenda Mtwara, Njombe, Ruvuma, Lindi na baadaye nitakwenda Mtwara kwa ajili ya kuhakikisha kwamba najionea mazingira halisi ya hiyo mifereji ambayo ameitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu ambayo yalikuwa ni madogo ila hakutoa ufafanuzi, lakini nitakuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa sababu jambo lolote linalokuwa linataka lifanikiwe linakuwa na ratiba au linakuwa na mpangilio maalum. Hata hivi vikao wanavyovifanya kwa vyovyote inabidi viwe na maandalizi na maandalizi yake kuwe na ratiba.
Sasa nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri kabla ya kufanya hivi vikao vyao vya pamoja vya mashirikiano, wanajiandaa kwa ratiba ya pande zote mbili baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu baadhi ya Mawaziri huwa hawashiriki vikao kwa kuwa wanapotaarifiwa hivyo vikao wanakuwa nje ya nchi au wanakuwa na dharura nyingine za vikao vingine ambavyo wameshajipangia. Sasa nataka anijulishe, wanapokuwa wanakaa kufanya vikao hivyo wanakuwa wameandaa ratiba mapema baina ya SMZ na SMT ili wahakikishe kwamba viongozi wote hao wanatakiwa kushiriki? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wamesema kwamba changamoto zilikuwa 15, changamoto 11 zimepatiwa ufumbuzi zimebakia nne, sasa hizo changamoto nne ambazo anasema bado ziko katika maandalizi ya kupata ufumbuzi, ni zipi za SMT na zipi za SMZ katika hizo nne ambazo bado zimo katika changamoto zinazopatiwa ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumjibu Mheshimiwa Fakharia Shomar maswali yake mawili ya nyongeza. Moja kila kikao kinaandaliwa ratiba mapema sana na nimkumbushe tu kwamba tarehe 9 Februari, 2019 kulikuwa na kikao cha Kamati ya Pamoja cha SMT na SMZ kujadili changamoto zote hizi na hasa hizi nne nazo pia zimetolewa maelekezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni kweli hizi changamoto nne kwa mujibu wa swali lake la msingi alivyokuwa ameliuliza, ningependa pia nizitaje, moja ni mgawanyo wa kodi ya misaada; lakini ya pili, ni usajili wa vyombo vya moto; ya tatu, ni hisa za SMZ katika Bodi ya Sarafu ya Afrika ya Mashariki na Benki Kuu; na ya nne ni Tume ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongezee katika majibu mazuri sana yaliyotolewa na Naibu Waziri katika suala hili hasa la ratiba na utaratibu. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mwezi uliopita zimepitisha rasmi utaratibu mpya wa kushughulikia changamoto za Muungano na kuweka ratiba mahsusi ya vikao. Kwa hiyo, kile kikao kikubwa kabisa cha Makamu wa Rais ambacho ni cha Serikali zote Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Mawaziri la SMZ kinakutana mara moja kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna kikao cha Mawaziri na chenyewe kinakutana mara moja kwa mwaka, kikao cha Makatibu Wakuu wote kinakutana mara mbili kwa mwaka na kikao cha Wataalam wa Serikali zote na chenyewe kinakutana mara mbili kwa mwaka. Kwa hiyo ratiba zimetolewa na Waraka wa Serikali (circular) imesambazwa na kueleza Wajumbe wote wa vikao hivi na utaratibu wa kuviitisha, utaratibu wa kuleta ajenda katika vikao ili kuwepo na utaratibu unaotabirika na unaoeleweka na ambao umepitishwa katika mfumo wa Serikali kushughulikia suala hili.
Vilevile, zimeundwa Kamati za hii Kamati ya Pamoja, Kamati ya Fedha, Uchumi na Biashara na Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ili zile changamoto ambazo ni za kutafutiwa majawabu haraka haraka zisingoje kikao kikubwa, Mawaziri waweze kukutana haraka katika hizi Kamati zao na kuzishughulikia. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeweka utaratibu madhubuti kabisa wa kushughulikia changamoto za Muungano katika Serikali hii ya Awamu ya Tano.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwanza kabisa nipende kuzipongeza Serikali zote mbili kwa jitihada ambazo zimekuwa zikichukua katika masuala haya. Kwa kuwa jitihada hizi, wananchi wengi hawana taarifa nazo na hawana uelewa nazo, Serikali sasa haioni umuhimu wa kuanza kuweka utaratibu maalum wa kutoa taarifa hizi ili wananchi waweze kupata uelewa wa pamoja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Khadija Nassir lakini pia nipokee ushauri wake, tufike mahali sasa tuanze kuziweka wazi taarifa hizi japo tumekwishaanza lakini kuweka kwa mapana zaidi. Kwa hiyo, napokea ushauri.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa vijana wengi hasa wa kizazi hiki kipya hawaelewi vizuri umuhimu wa kuuenzi Muungano, Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ya kutosha hasa kwa vijana wa sasa na hata wale wa zamani ili kujua umuhimu wa kuuenzi Muungano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakasaka kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimdhihirishie tu kwamba Serikali inaendelea na mchakato na imeendelea kutoa elimu juu ya faida za Muungano na labda kama bado ziko changamoto ambazo elimu hii haiwafikii vijana walio wengi, nadhani ni wakati muafaka sasa wa kuendelea kuhimiza kuhakikisha kwamba elimu hii inawafikia vijana wote.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mara kadhaa maafisa mbalimbali ambao wanatumia magari ambayo yamekuwa na namba za Zanzibar wamekuwa wakikumbana na vikwazo vya TRA pamoja na Polisi kwamba, namba hizo ni namba za kigeni wakati anapotembea Tanzania Bara. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, yupo tayari sasa kutenga muda mahususi kuwapa taaluma Polisi pamoja na TRA kuona kwamba, Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuambatana na sisi au na mimi kwenda kuangalia namna Maafisa wa TRA wanavyofanya kazi pale bandarini kwamba, unapokuja tu na kilo tano za sukari kutoka Zanzibar au Tv ya nchi 21 unatakiwa ulipe kodi? Je, hili yupo tayari kwenda kulishuhudia Bandari ya Zanzibar ili kutoa mwongozo na taaluma kwa ajili ya shughuli hizo za kibiashara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbarouk, kwa niaba yake Mheshimiwa Juma ameuliza vizuri sana:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza niko tayari kwa yote mawili, lakini kwa ufafanuzi zaidi hili la vyombo vya moto kwa sababu, bado lipo tayari kwenye majadiliano na vikao vinaendelea, nadhani baada ya hivyo vikao sasa nitakuwa tayari kwa ajili ya kutoa hiyo elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, niko tayari kuambatana na wewe na Wabunge wengine ambao wanatoka Zanzibar kwenda kushiriki kwa pamoja kuhakikisha kwamba, eneo hili tunalifanyia ufumbuzi. Ahsante sana.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais watumishi wengi wanakaimu.
Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha watumishi hawa sasa, wale wanaokaimu wanapandishwa madaraja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru. Nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Serikali ina dhamira ya dhati kabisa kuhakikisha maeneo yote ambayo watumishi wanakaimu waweze kufanya kazi yao kwa ukamilifu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tayari ofisi yetu imeshafanya utaratibu wa kuomba kibali kwa ajili ya kuhakikisha watumishi wote wale au maeneo yote, position zote ambazo zinakaimiwa ziweze kupata watalaam ambao wako kamili. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ili nami niweze kufafanua swali la Mheshimiwa Mbunge, Maryam Msabaha. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba nifafanue kidogo juu ya suala zima la kuhusu watumishi kukaimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli watumishi wamekuwa wakikaimu kwa muda mrefu sana na nimekuwa nikilizungumza hili kwamba, hii ni kutokana na watumishi wengi wamekuwa wakikaimishwa na waajiri wao kienyeji na nafasi za kukaimu ni kukaimu tu sio kwamba, ni nafasi ya kuthibitishwa au ni kwamba, umeshapewa ile kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi nafasi za kukaimu ziko katika uwezo wa madaraka kwa maana ya superlative substantive post. Kwa maana hiyo, sisi kama Serikali, tumetoa waraka kwamba, kukaimu mwisho miezi sita. Kwa maana hiyo waajiri wote nchini wanapaswa kuomba kibali na kama unataka mtumishi aendelee kukaimu basi tuandikie tena barua. Kukaimu lazima iwe kulingana na level ya ile nafasi ambayo unastahili kukaimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza. Kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa Muungano umetuletea faida nyingi sana katika nchi yetu na ndiyo maana viongozi wetu, waasisi na sisi wenyewe tumekuwa tukiuenzi na kuulinda kwa nguvu zote na kwa kuwa sasa huko vijijini vijana wetu wengi wamekuwa hawana uwelewa sana wa kutosha kuhusiana na huu Muungano. Je, ni ni kwa nini sasa Serikali isiweke utaratibu wakati wa sherehe hizi elimu itolewe kwa ajili ya vijana wetu na wananchi walioko vijijini kuliko kufanya sherehe kitaifa zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ritta Kabati kwa niaba yake ambapo swali la msingi lilikuwa la Mheshimiwa Martha Moses Mlata. Kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mlata kwa swali hili ambalo litatoa ufahamu mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kutoa rai, siku ya tarehe 26 nafahamu itakuwa siku ya Ijumaa mwezi wa Nne kwamba Taasisi zote za Elimu zitumie fursa hii ya kutoa elimu kuhakikisha kwamba wanakuwa na makongamano na mijadala mbalimbali juu ya historia ya Muungano wetu. Ahsante.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWAKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusikiliza majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza lilikuwa ni mahususi kwa Kasulu Mjini ambapo timu ya watalaam wa NEMC na Wizara ya Maji wakiwa tisa walikuja kufanya survey pale mwaka 2018 na wakaandika ripoti nzuri sana, wakati huo alikuwa Waziri Makamba. Hiyo ripoti iko ofisini kwako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ile ripoti ifanyiwe kazi kwa sababu ilikuwa mahususi kwa ajili ya Mji wa Kasulu na Kasulu Vijijini ambako mito zaidi ya 50 ilibainika pale na moja ya chanjo kipo shambani kwangu, nami ndio nakilinda kwa gharama kubwa ili kisiharibike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni la Kitaifa zaidi. Nimekubaliana naye na sasa napenda nipate time line: Je, huo mradi wa urejeshaji wa ikolojia ya Mto Malagalasi unaanza lini kwa maana ya vijiji vya Buhoro, Busunzu, Msambala na Kabanga?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu amesema ni mradi wa Kitaifa, napenda kujua time line ya huo mradi wa kurejesha ikolojia ya Mto Malagarasi ambayo imeharibika sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko kwa juhudi zake kubwa za kuhifadhi mazingira na ametupa ushirikiano wa kutosha tangu wataalam wamekuja na leo anaikumbuka ile taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kwamba taarifa hiyo sasa nitakwenda kuisoma vizuri na nitakushirikisha kabla Bunge hili halijaisha, ni hatua gani ambazo tutaanza kuzichukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na swali la pili, kwamba hatua gani mbadala na kwa wakati gani? Naomba pia kabla hatujamaliza shughuli zetu za Bunge leo, pia nitakupa taarifa hizi nikiwa nimeshawasiliana na watalaam kwamba wakati gani tunaweza kuanza kazi hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mazingira kwa suala lake zuri ambalo alilolitoa hivi sasa hivi hapa. Lakini pia nimpongeze kwa suala langu la Bunge lililopita wakaja Zanzibar wakaja kutuhimiza ahadi yake ya kuja kuangalia mambo ya hali ya hewa ya mmomonyoko wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza, kwa kuwa mikoko ina mchango mkubwa wa kunusuru mazingira nini mpango wa Serikali katika kuhakikisha inaotesha mikoko ambayo inauwezo wa kunusuru maji chumvi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili bila maji baridi hatima ya kilimo na uhai wa binadamu viko hatarini. Je, kuna tafiti zozote za kuyalinda kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji baridi ahsante? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ridhaa yako nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji Mbunge wa Viti Maalum ni kweli amekuwa mstari wa mbele na sasa hivi amekuwa mwana mazingira tunamtumia sana hasa kwenye eneo hili la Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru kwa maswali yake mawili; moja, tunao mkakati maalum na unaendelea kwa kushirikisha wenzetu wa Serikali za Mitaa hasa kwenye halmashauri zetu kuhakikisha wanaweka miche kwa ajili ya mikoko ambayo itatumiwa kwenye maeneo hayo tuliyoyaeleza ya Pwani pembezoni mwa bahari. Na mkakati huo unaendelea na miche ipo ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili, utafiti zinaendelea na mpaka sasa tupo na utafiti unaendelea na wakati wowote tutaweka suala hili katika utaratibu ambao tutahakikisha maeneo haya kunakuwepo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwenye kila eneo ambalo kuna mwambao wa bahari ahsante sana.
MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu ya kina kuhusu swali langu hili, nampongeza sana, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, yamekuwepo matukio ya ongezeko la kina cha bahari kiasi cha kuwepo kwa tishio la kimazingira katika baadhi ya maeneo. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na suala hilo katika Visiwa vya Unguja na Pemba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tatizo hili ni la muda mrefu kweli, toka lilivyogundulika kuhusu mazingira katika Visiwa vyetu vya Pemba na Unguja. Mheshimiwa Naibu Waziri atakuja lini sasa Zanzibar kuangalia maeneo yaliyoathirika katika Visiwa vya Pemba na Unguja? Nataka unihakikishie utakuja lini Zanzibar mbele ya Bunge letu hili.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mwantum Dau Haji kwani amekuwa mdau mzuri wa eneo hili la mazingira. Nimhakikishie tu kwamba katika miradi ambayo inaendelea na kama nilivyosema kwamba tunashirikiana vizuri na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar sasa tunaifanyia tathmini. Katika tathmini ile ambayo tunaifanya kila baada ya miezi mitatu maana yake sasa nitakuja rasmi baada ya Bunge hili, walau siku mbili hivi kwa ridhaa ya Mwenyekiti, ili tukishirikiana nawe na Wabunge wengine kwenye maeneo ya Pemba kuyaona hayo maeneo vizuri na kuhakikisha tunayapatia ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Suala la mmomonyoko wa udongo ni kubwa na lipo dhahiri kabisa, ukiona mkusanyiko wa udongo na mchanga katika mapito ya njia za maji za mito. Kumekuwa pia na uchimbaji holela wa michanga hii, inazidi kuvunwa au pia vina vya maji vinakuwa vifupi na nyakati za mvua basi husababisha mafuriko. Wizara husika ina mkakati gani kuleta suluhisho katika suala hili ambalo ni muhimu sana na lina effect kubwa sana katika mazingira?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Sware.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikubaliane naye kumekuwa na changamoto kubwa sana ya mmomonyoko wa ardhi hasa kwenye maeneo ambayo kuna mapito ya maji. Eneo hili kwa kweli nikiri kabisa tumeendelea kulifanyia kazi na limekuwa na changamoto kubwa. Mkakati uliopo ni kuhakikisha maeneo yote haya kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri wanatupa taarifa zilizo rasmi ili kutengeneza miradi ya kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuwa tukitoa maelekezo kwenye Halmashauri husika ili kukabiliana na maeneo ambayo yanahitaji kupata ufumbuzi wa muda mfupi lakini yale ya muda mrefu Wizarani tunapata taarifa na tunachukua hatua stahiki.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nizungumze kidogo kidogo ili nifahamike nisiende haraka haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina sehemu mbili ambazo ni Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Nilichouliza ni mipaka ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, kisiwa kile kiko sehemu gani, hicho ndicho nilichouliza. Kisiwa kile kiko Zanzibar au Tanzania Bara. Swali langu la kwanza nafikiri limefahamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, ni sababu gani iliyopelekea Tanzania Bara kudai kisiwa kile ni chao na Zanzibar kudai ni chao? Hata hivyo, kuna ushahidi wa kutosha na naomba nikuletee nakala hii na kuweka record ya Bunge hili ni sababu gani iliyopelekea kuvutana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014 Serikali mbili zilikutana, ya Mapinduzi ya Zanzibar na Tanzania Bara na ikaundwa Kamati ya Wajumbe wawili wazito akiwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Tanzania Bara. Je, ni lini ripoti ile italetwa ili kuondosha fitina hii?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Jaku kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Jaku majibu niliyoyatoa katika swali lako la msingi yamejitosheleza kuelezea kisiwa hiki kiko wapi. Hata hivyo, nyongeza yake, kwa kuwa tayari unayo taarifa, nadhani ni jambo jema sana tukakutana ili uweze kunikabidhi tuone namna gani tunaweza kulifuatilia jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kwamba kila jambo lina utaratibu, hata kama Wanasheria wamekutana lakini ni lazima viko vikao maalum, iko Sekretarieti lakini wako Makatibu Wakuu, iko level ya Mawaziri mpaka zije zikutane Kamati zote mbili za SMZ na Jamhuri ya Muungano ili kuweza kuona ni namna gani mambo haya yanaweza kufikiwa muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Jaku wala asiwe na wasiwasi. Serikali iko kazini tukutane tuone taarifa aliyonayo ili tuone ni namna gani tunaifanyia kazi. Ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kweli kwa maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri wazee wetu watavunjika moyo. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa katika maelezo yake ametuambia hakuna sheria ya kuwatunza wazee hawa kwa kazi zao walizozifanya. Je, ni lini Wizara yake italeta hapa Bungeni sheria hiyo kwa ajili ya kuwaenzi wazee hawa ambao waliiletea nchi yetu heshima kubwa na kuifanya iweze kutambulika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hawa wazee walioitumikia nchi hii kwa juhudi kubwa na kuipa sifa nchi yetu na kuifanya itambulike, je, Wizara haioni umuhimu wa wa kuwapatia bima ya afya ya uzeeni angalau ikawa faraja kwa wazee hao nao wakaona kwamba Serikali na Wizara inawatambua?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Fakharia amekuwa mstari wa mbele kwanza kudumisha Muungano lakini pia na leo amekuja na jambo zuri sana kuhusiana na wazee wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile natambua mchango wa wa wazee hao wanne ambao amewazungumzia kwenye swali lake la msingi. Nichukue fursa hii kwanza kuendelea kuwaombea kheri wazee wetu hawa ambao bado wapo, wapo wawili Moshi; Bi. Khadija Rashid na Mzee Hassan Omar wako Zanzibar lakini pia Bi. Sifaeli Mushi na Mzee Elias Mrema ambao wao wako Moshi. Nichukue fursa hii kuwaomba viongozi wetu walioko kwenye ngazi hizo wawashirikishe kwenye shughuli zozote zile ambazo zinahitaji kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni sahihi kabisa tunawajibika kuhakikisha tunawaenzi wazee hawa na ametoa ushauri kwamba ufike wakati Ofisi yetu iweze kuleta sheria. Nikuahidi Mhehsimiwa Fakharia tutalifanyia kazi wazo lake hili ili kuhakikisha tunawaenzi wazee hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hata suala la bima ya afya na lenyewe nalo naomba tulichukue ili tuweze kushirikiana kwa pamoja kuona namna gani tunawasaidia wazee wetu. Ahsante.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwanza nieleze kuridhishwa na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amejibu kwamba wameanzisha kampeni ili kukabiliana na hali hiyo, lakini ukubwa wa tatizo uliopo katika lango lile la kuingilia bandari ya Tanga siyo jambo linalotaka kampeni bali ni jambo linalotaka hatua za dharura ili kuzuia isije ikatokea barabara ile ikabomoka kama ilivyotokea hapo nyuma. Je, Serikali iko tayari sasa kuliona hili na kulichukulia hatua hizo ninazoziomba?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, athari zilizopo katika eneo la Deep Sea Tanga linafanana kabisa na athari zilizopo katika eneo la Sijuu Kijiji cha Msuka Jimbo la Konde Kaskazini Pemba ambalo ndiyo Jimbo langu. Nina hakika Mheshimiwa Waziri aliwahi kufika huko, kutembelea na kuiona hali ile: Je, Serikali iko tayari kuchukua hatua za dharura ili kuokoa vijiji vya maeneo yale visiendelee kumomonyoka kutokana na athari za kimazingira?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge wa Konde, kaka yangu Mheshimiwa Khatib. Ni kweli kabisa kama anavyosema eneo hili la Deep Sea kuna hatua za dharura ambazo tumeanza kuzichukua mpaka sasa na sasa wataalam wetu wanafanya tathmini na baada ya tathmini hiyo wataleta andiko ofisini ili tuweze kuweka kwenye mifuko yetu ya kimazingira kuhakikisha tunapata fedha kuokoa eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kama alivyosema kule kwenye Kijiji cha Msuka kwenye Jimbo lake Konde nilifika na nimhakikishie Mheshimiwa Khatib hatua zote hizi za kufanya tathmini kwenye maeneo haya ambayo yameathirika kwa nchi nzima tunayafanya kwa pamoja na nitafika tena kwa ajili kuhakikisha kwamba eneo hili tunalitatua kama tulivyokuwa tumepanga.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Suala la Sea Erosion lipo katika nchi yote ya Tanzania ambayo imezungukwa na ukanda wa bahari na linamega kwa kiasi kikubwa ardhi ya Tanzania hali ambayo inahatarisha usalama wa watu wetu, pia kupungua kwa ardhi yetu. Kwa mfano, Msimbati Mkoani Mtwara ardhi ilichukuliwa kwa zaidi ya mita kumi kwa wakati mmoja:-
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhamasisha na wao wenyewe Serikali kushiriki katika kupanda miti ya mikoko maeneo yale ili kuzuia athari hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimeeleza kwenye majibu ya msingi kwamba tayari tunao mpango wa kuhimili mabadiliko ya tabia nchi wa mwaka 2007. Pia tuna mkakati wa mabadiliko ya tabia nchi wa mwaka 2012. Kwa hiyo, mkakati huu ulikwishaanza kwenye maeneo yote yaliyoathirika na nikuhakikishie tu kwamba mkakati unaendelea na pale utakapopata fedha kwa ajili ya kuokoa maeneo haya, maana yake tutafika kwa ajili ya kuhakikisha maeneo haya tunayaweka salama.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya kitaalamu ambayo ameyatoa na mimi kwa uhaba wangu wa elimu naweza nikayagawanya au nikayafanyia summary majibu yake katika mambo matatu kwamba mikoko ina faida ya kiuchumi, kijamii na kimazingira. Ameshaeleza umuhimu wake, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, pamoja na hizo faida za kiuchumi na kijamii zilizopo, je, jamii inayozungukwa na miti hiyo inapewa elimu ya kutosha juu ya umuhimu, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ametaja faida za kimazingira kwamba kuhifadhi udongo, upepo, bionuai na kuhifadhi sumu. Je, ni kipi kipaumbele cha Serikali katika uhifadhi huo wa kimazingira ambacho wamekifanyia kazi hadi sasa? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipokee shukrani zake lakini pia nimpongeze amekuwa mdau mzuri sana wa mazingira tangu tumeanza na tunashirikiana pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kuhusu kutoa elimu, ni kweli na sisi tunaendelea kutoa elimu na hili ni jukumu letu kama Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) na ili tuweze kufanikiwa jambo lolote katika utekelezaji wake elimu tumeipa kipaumbele. Hata hivyo, kipaumbele kikubwa ni mazingira na kwenye majibu yangu ya msingi nimeeleza namna ambavyo mikoko inavyotusaidia katika kuhifadhi kingo za maeneo ya Pwani hasa tunapokuwa na miradi ya mabadiliko ya tabia nchi katika kujenga zile kuta kwenye kingo tunatumia fursa hiyo hiyo katika mradi huo huo kuhakikisha tunapanda miti ya mikoko kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kutunza mazingira. Kwa hiyo, kipaumbele chetu ni kuhifadhi mazingira. Ahsante.