Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Selemani Jumanne Zedi (33 total)

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mwaka jana Bunge lililopita mwezi wa nne niliuliza swali hili hili la kufuatilia ujenzi wa minara hii na jibu nililopewa lilikuwa kwamba, kazi ya ujenzi imeanza na mpaka Waziri wa Mawasiliano wakati ule alinipa barua ya commitment ambayo nilikwenda kuwaonesha wananchi lakini mpaka sasa hivi hakuna chochote ambacho kimefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, nataka kujua inakuaje makampuni ya simu...
MWENYEKITI: Swali la pili eeh?
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Inakuwaje Makampuni ya Simu pamoja na ruzuku wanayopewa kutoka kwenye Mfuko wa Mawasiliano kwa wote yanashindwa kukamilisha ahadi zao?
Swali la pili, Serikali ilituambia kwamba imebaini Makampuni ya Simu yanakuwa reluctant, ni wazito kwenda kujenga minara vijijini kwa sababu ya kifaida kwamba hakuna faida wanapoweka minara vijijini na wakasema kwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote watahakikisha kwamba, minara ya vijijini inajengwa kwa ruzuku ya 100%.
Je, mpango huo upo? Unaendelea na kama unaendelea ni vijiji gani ambavyo wameshabaini na vitanufaika kwa mpango huo?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwenye Bunge hili mwaka 2014/2015, tulisemea maeneo hayo na ni kweli kwamba Makampuni mengi ya Simu, Airtel, Tigo, Vodacom, Zantel wanachelewesha kupeleka mawasiliano vijijini. Kwa mantiki hiyo ndiyo tuliamua kuleta Halotel au Viettel kwa ajili ya kupeleka mawasiliano vijijini haraka. Kwa mtazamo huo huo kuanzia mwezi Mei mwaka huu mpaka mwezi Oktoba mwaka huu, Kampuni ya Halotel au Viettel itajenga takribani mawasiliano kwenye vijiji 1800. Tunaamini na vijiji vya Mheshimiwa Mbunge vilevile vitapata huduma hiyo.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ziara ambayo aliifanya katika Jimbo hili hivi karibuni na vijiji vyote vilivyotajwa kwenye swali hili vya Mwangoye, Mambali na Mbutu, Mheshimiwa Naibu Waziri alivipitia na kutoa maelekezo maalum kwa TANESCO, REA na CHICCO…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Zedi, naomba uulize swali tafadhali.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu ni kwamba kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi katika kijiji cha Mwangoye, Mambali na Mbutu, jambo ambalo limefanya wananchi wengi kufanya wiring na kuwa tayari na fedha ya kulipia, lakini kuna upungufu mkubwa wa nguzo na vifaa vya kuunganishia.
Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutumia forum hii kutoa agizo au kauli maalum kwa watendaji wa REA, TANESCO na CHICCO kuhakikisha kwamba wananchi wote wa Mwangoye, Mambali na Mbutu ambao wameshajiandaa kupata umeme wanapatiwa nguzo na vifaa vya kuunganishiwa ili waweze kupata huduma muhimu ya nishati?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu niongeze maelezo kwenye shukrani alizotoa na mimi namshukuru sana Mheshimiwa Zedi kwa pongezi na shukrani za kuunga mkono. Nampongeza sana pamoja na wananchi wa Bukene. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye swali lake, kimsingi siyo swali lakini anataka wananchi wake wapate uhakika. Ni kweli kabisa nguzo zinaendelea kwenda Bukene katika vijiji vyote vitatu na katika mwezi ujao wananchi wapatao 50 watapatiwa umeme kwa sababu nguzo wameshapelekewa.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pamoja na kuwepo kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa lengo la kuchangia gharama za ujenzi wa minara maeneo ya vijijini, lakini bado speed ya ujenzi wa makampuni haya umekuwa mdogo sana, kulikuwa napendekezo kwamba sasa Mfuko wa UCSAF ugharamie asilimia 100 ya ujenzi wa minara katika maeneo ya vijijini ambayo hayana mvuto kwa biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefikia wapi katika kuona umuhimu huu wa kwamba Mfuko wa UCSAF ugharamie minara ya vijijini kwa asilimia 100 badala ya kuyaachia makampuni ambayo kwa kweli yamekuwa mazito kupeleka minara vijijni kwa sababu hakuna mvuto wa kibiashara?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, mfuko wa mawasiliano kwa wote unagharamia kuanzia asilimia kumi mpaka asilimia 100; inategemea eneo na eneo. Kama eneo hilo halina mvuto wa kibiashara kabisa mfuko wa mawasiliano kwa wote unagharamia asilimia 100. Kuna tatizo ambalo limejitokeza ni kweli makampuni ya simu yamechelewa kujenga minara ya mawasiliano kwenye maeneo mbalimbali na kwa kulijua hilo sasa Serikali itapiga faini makampuni ya simu yote ambayo yamechelewa kupeleka mawasiliano kwenye maeneo hayo. Ahsante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri na hasa wazo la ku-design nyumba moja ambayo itaweza ku-accommodate Walimu sita kwa maana familia sita. Sasa swali langu ni kwamba je, Serikali haioni sasa kwamba kuna umuhimu wa kusambaza hii ramani ya design hii ambayo nyumba moja inaweza ika-accommodate Walimu sita kwa Halmashauri zote na maelekezo maalum ili shule ambazo zipo vijiji sana Halmashauri ziweze kutumia ramani hii na kujenga nyumba? Kwa sababu ukiweza kujenga nyumba mbili tu maana yake tayari ume-accommodate Walimu 12?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikiri katika Jimbo analozungumza Mheshimiwa Mbunge na mimi nilikuwa kule. Aliponiagiza yeye mwenyewe nitembelee Jimbo lake; nikatembelea miradi ya afya na kuona mambo mengine na changamoto za miundombinu. Naomba niseme ushauri huu tumeshaufanyia kazi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhakikisha ramani hizi zinakwenda kila Halmashauri. Tunachokifanya ni kuhakikisha tunaweka mkazo sasa, bajeti yoyote inayopatikana lazima tuelekeze katika mfumo wa ramani mpya ambayo kwa kiwango kikubwa ina tija sana katika Halmashauri zetu kuhusu suala la kupunguza tatizo la upungufu wa nyumba za Walimu katika Halmashauri zetu.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli huyu mshauri yuko site na kazi hii inaendelea, lakini nina swali moja la nyongeza. Kwa sababu barabara hii ilivyo sasa katika Miji ya Bukene na Itobo inapita katikati ya miji na kwa mfano Bukene ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami tutalazimika kuvunja Kituo cha Afya, jengo la Polisi, tanki kubwa la maji, ma-godown makubwa na kuvunja nyumba nyingi tu cha wananchi.
Je, Serikali itakuwa tayari kutoa kauli itakayoondoa hofu na itakayofanya kuepusha fidia kubwa kwamba usanifu huu ujumuishe kuichepusha barabara hii katika miji ya Bukene na Itobo ili isipite katikati ya Miji ya Bukene na Itobo ili kuondoa kwanza fidia kubwa ambayo itatokea baada ya kuvunja taasisi nyingi hizi na nyumba nyingi za wananchi?
Je, Serikali iko tayari kutoa kauli ili wananchi wa Bukene na Itobo wawe hawana hofu kwamba barabara hii itachepushwa pembeni ya miji hii na kuondoa gharama zote hizi ambazo zitajitokeza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia sana hii barabara ambayo inatoka Tabora - Mambali kuja Itobo. Niseme tu kwamba upo utaratibu kwa upande wa Serikali wa kuangalia hizi gharama wakati tukisanifu hizi barabara. Kwa hiyo, niseme kwamba tutazingatia ushauri wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo jambo geni kwa sababu zoezi hili tumelifanya katika Mji wa Nzega, kuna mchepuo; tumefanya katika Mji wa Urambo, kuna mchepuo; lakini pia tumezingatia tulivyosanifu barabara ya kule Kasulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikutoe wasiwasi na niwatoe wasiwasi wananchi wa Bukene kwamba tutazingatia wakati tunakamilisha zoezi la usanifu wa barabara.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza linahusu tafsiri ya kijiji kwenye huu usambazaji wa maji. Ninataka kujua anaposema maji yatafika Kijiji ya Ilagaja, Kijiji cha Ilagaja kina Vitongoji kumi. Je, maji yatafika makao makuu tu ya kijiji au katika vitongoji vyote kumi vinavyounda Kijiji cha Ilagaja?
Swali la pili, sasa maji haya yatakapofika Nzega na kwa sababu maeneo yetu ya Bukene yana shida ya water table kupata maji kutoka chini. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kuanza mipango ya muda wa kati ili maji haya sasa yatakapofika Nzega yatoke Nzega yafikishwe Bukene ambako ni umbali wa kilometa 40?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameomba tafsiri kwamba maji yatafika Kijiji cha Ilagaja, je, vitongoji itakuwaje?
Naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kuwa lengo letu ni kuhakikisha kwamba maji safi na salama yanawafikia wananchi wote. Yatatoka Nzega ambayo ni Makao Makuu ya Wilaya, yataenda Ilagaja yakifika pale basi tutaendelea kuyaendeleza kwenda mpaka kwenye vitongoji mpaka kwenye point ya mwisho ili wananchi wote eneo la Ilagaja na vitongoji vyake wapate maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na labda tu nizungumze kwamba ndio maana katika bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji tunatenga fedha kwa kila Halmashauri. Bomba la KASHWASA maji ya kutoka Ziwa Victoria yakishafika kwenye kitongoji kwa upande wa Halmashauri kile ndio chanzo cha maji, zile fedha tunazotenga basi muendeleze mpeleke kwenye maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, jibu lake ni hivyo hivyo kuwa yakishafika pale basi Halmashauri kile ndio chanzo, watenge fedha waunganishe kutoka pale kwenda kwenye maeneo ambayo hayana maji. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii.
Kwanza kabisa naipongeza Serikali kwa kutupatia shilingi milioni 800 ambazo maboresho makubwa ya Hospitali ya Wilaya ya Nzega yanaendelea. Sasa nataka kuuliza kwamba Serikali mna mpango gani na Vituo vya Afya vya Itobo na Bukene ambavyo vina tatizo kubwa sana la wodi. Je, baada ya kumaliza maboresho ya Hospitali ya Wilaya, mtakuwa tayari sasa kuelekeza nguvu kwenye Vituo vya Afya vya Itobo na Bukene?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kimsingi tutakuwa tayari kama ambavyo tumekuwa tayari siku zote. Hatua kwa hatua tukimaliza vituo hivi ambavyo tumeanza navyo tutakwenda na Vituo vingine vya Afya.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, Mheshimiwa Naibu Waziri ana taarifa kwamba mchakato huu wa kuomba Mji wa Bukene upandishwe hadhi ulianza siku nyingi na mpaka Wizara ikatoa GN Namba 176 ya mwaka 1996 ambayo mpaka sasa haijafanyiwa mchakato wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwenye swali langu la msingi niliuliza, je, muundo wa kuwa na Kata moja inayoundwa na Kijiji kimoja tu ni sahihi? Kwa sabbau muundo huu unapelekea Mtendaji wa Kijiji kutokuwa na tofauti yoyote na Mtendaji wa Kata na Serikali ya Kijiji haina tofauti yoyote na WDC na ni sawa sawa na kuwa na Mkoa mmoja unaoundwa na Wilaya moja tu ambayo kutakuwa hakuna tofauti yoyote ya Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa, kwa sababu mkoa ni mmoja na Wilaya ni mmoja. Je, muundo huu ni sahihi kuwa na Kata moja ambayo inaundwa na Kijiji kimoja tu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza ananiuliza kama najua kwamba kuna GN ambayo ilikuwa imetolewa na kwamba mpaka sasa hivi GN hiyo haijafanyiwa marekebisho yoyote, taarifa hiyo ninayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, anauliza uwezekano wa Kijiji hicho kimoja kikawa Kata, naomba nitoe ufafanuzi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Selemani Zedi anajua kwamba ilikuwa mchakato wa kupandisha Kijiji cha Bukene kuwa Halmashauri ya Mji Mdogo na Bukene kama ilivyo ina vitongoji vyake 11 na lengo lilikuwa hivyo Vitongoji vije vibadilike kuwa Mitaa ambayo ingeweza kutosha katika kubadilisha sasa kuwa na Mamlaka ya Mji Mdogo wa Bukene. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Selemani Zedi, taratibu hizo zingine ziendelee ili ukifika wakati ambapo Serikali itakuwa tayari kuongeza maeneo ya kiutawala na Bukene iwe na sifa ya kuweza kuongezeka.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nichukue fursa hii kuipongeza Wizara ya Madini kwa uamuzi wake wa kuyagawa au kutoa leseni za wachimbaji wadogo kwenye maeneo ambayo awali yalikuwa yana leseni za utafiti za wachimbaji wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu ni kwamba kwa kuwa maeneo haya ambayo yalikuwa na leseni za utafiti za wachimbaji wakubwa yameshafanyiwa utafiti na Serikali ina taarifa za utafiti zinazoonesha wapi kuna madini, yako kiasi gani, yako umbali gani na kadhalika. Je, ili kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo waliopewa maeneo haya wasichimbe kwa kubahatisha na hatimaye kuingia hasara, Serikali iko tayari ku-share, kuwapatia wachimbaji hawa hizo taarifa za utafiti wa haya maeneo ili wachimbaji wadogo wawe wanachimba kwa uhakika wakijua hapa kuna madini na kuondokana na hali iliyopo sasa hivi ambapo wanachimba kwa kubahatisha na hatimaye wanapata hasara?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Zedi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kampuni kubwa na za kati ambazo zinamiliki maeneo ambayo ni ya utafiti sisi sasa hivi kama Serikali tumeamua kuyarudisha, kwa yale maeneo ambayo yalikuwa hayafanyiwi kazi, tumewarudishia wachimbaji wadogo waweze kuchimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amehoji kwa nini tusiwape data zile wachimbaji wadogo kwa ajili ya kuzitumia kwa maana ya kuchimba bila kubahatisha. Ni kwamba Geological Survey of Tanzania (GST) ambayo iko chini ya Wizara yetu ina ripoti nyingi za maeneo mbalimbali ya uchimbaji. Tunawaomba wale ambao walikuwa tayari wameshaanza kufanya utafiti watupe zile data walizozipata katika maeneo waliyofanyia utafiti. Kwa kweli data tunazo, kwa wachimbaji wanaotaka kupata geological data au report kutoka GST waje wafuate taratibu na watapewa data hizo na waweze kuchimba bila kubahatisha waweze kujipatia tija katika uchimbaji.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongezea Serikali kwa kazi ambayo imefanywa kwenye barabara hii. Kimsingi wakati naandika swali hili, kuliwa hakuna kazi yoyote ambayo imefanyika, lakini sasa hivi nakubaliana kabisa na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Mshauri Mhandishi NIMETA Consult ameshaanza kazi, nami mwenyewe ni shuhuda nimemwona akifanya kazi hii ya usanifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba kwa kuwa Serikali imesema kazi ya usanifu wa kina inaisha mwezi Juni, 2019 na hii barabara ni ahadi ya Rais na pia ni jambo ambalo lipo kwenye ilani:-

Je, Serikali inaweza ikatoa kauli hapa kwamba barabara hii kwa kuwa usanifu utakuwa umekamilika mwezi Juni, sasa kwenye bajeti ijayo itatengewa fedha ili Mkandarasi wa kuanza kujenga aanze kazi kabla ya Awamu hii ya Tano haijamaliza muda wake?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunapokea pongezi kwa moya wa dhati kabisa lakini napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Selemani Zedi kwa jinsi ambavyo anafuatilia sana kipande cha barabara hii iliyotajwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mpango wa Serikali na nia ya Serikali kuhakikisha kwamba barabara zote nchini kwanza zimepitika na pili zinaunganishwa kwa kiwango cha lami. Nimhakikishie Mheshimiwa Zedi kwamba barabara yake kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kama ahadi ya Mheshimiwa Rais, tutaijenga kwa kiwango cha lami kabla ya mwaka 2020 kwisha.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, hili eneo la Sojo Kata ya Igusule ambako pameamliwa kujengwa kiwanda hiki liko jimboni kwangu na wananchi wametoa hekari 400 ili kupisha ujenzi wa kiwanda hichi muhimu. Na kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa waziri wamesema mwezi wa tisa ambayo ni miezi minne tu kutoka sasa mkandarasi anakabidhiwa eneo.

Je, nilitaka kujua kwamba Serikali inaweza kutoa commitment kwamba ndani ya kipindi hichi cha miezi minne kabla mkandarasi hajapewa hilo eneo wananchi wote waliotoa hekari 400 watakuwa wamelipwa fidia zao?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na yeye pia nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia mradi huu mkubwa wa ujenzi wa bomba hili la mafuta na tija yake kwa wananchi wa maeneo yake hayo, kwa eneo ambalo limechaguliwa kujenga kiwanda cha kuunganisha mabomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimdhibitishie Mheshimiwa Mbunge moja ya kazi muhimu ambayo imefanyika ni kutambua mkuza ambako bomba litapita na tunatambua bomba hili ambalo litakuwa na urefu wa kilometa 1445 na zaidi ya kilometa hizo 1147 ziko upande wa Tanzania, Serikali yetu kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi na TPDC imetambua ule mkuza na imeshafanya tathimini ya mali mbalimbali ambazo ziko katika huo mkuza ikiwemo eneo hilo la ujenzi wa kiwanda hichi cha courtyard.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimthibitishie tathmini imekamilika na kwa kuwa tupo katika hatua nzuri ya mazungumzo ya Host Government Agreement baada ya hapo tutaenda Share Holders Agreement na kasha kufanya maamuzi ya investment decision na hatua zote hizi zipo katika mchakato wa miezi hii ambayo imesalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge na kwa utashi wa viongozi wetu Marais wan chi mbili hizi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museven wa Uganda kwamba mwezi wa tisa utakapoanza mradi huu wananchi wote watakaopisha mkuza huu wa bomba watakuwa wamefidiwa kwa sababu tathmini ile imekamilika na sasa yapo tu mapitio ya mwisho ambayo yanafanywa baina ya Wizara ya Nishatu wataalamu, TPDC, Wizara ya Ardhi, Maendeleo Nyumba na Makazi na taasisi nyingine za Kiserikali. Nikushukuru sana.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza. Kwa kushirikiana na Mwekezaji anayejenga hii Coating Yard pale Sojo Igusule, Kijiji cha Sojo Igusule tumefaidika kwamba sasa tutapata maji kwa msaada wa huyu mwekezaji na pia tutapata umeme kwa haraka kuliko ulivyokuwa kwenye mpango, lakini pia kituo cha afya cha pale, kitakuwa upgraded kuwa kituo cha afya cha kisasa. Sasa swali langu ni kwamba, je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kufanya mazungumzo na huyu mwekezaji anayejenga hiyo coating yard pale, kwa sababu atawekeza zaidi ya bilioni 600 na hivyo na yeye pia atahitaji masuala ya usalama? Je, Serikali iko tayari kufanya naye mazungumzo ili na yeye achangie ujenzi wa hicho kituo cha polisi kama ambavyo amechangia kuleta maji, umeme na kupandisha hadhi kituo cha afya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kutumia fursa zilizopo ndani ya jimbo lake kwa ajili ya kuweza kueneza huduma mbalimbali za kijami katika jimbo lake. Kuhusiana na wazo ambalo amelitoa, pia ni wazo zuri, lakini nataka nimjulishe kwamba, wazo hilo siyo geni, kwa mfano katika Mradi wa Stiegler’s Gorge ambao unaendelea kule Rufiji, tumefanikiwa kupata kituo, tupo katika mchakato wa ujenzi wa kituo cha polisi, ambapo unatokana na mradi huo. Kwa hiyo, tutatumia mawazo yake pamoja na mbinu ambazo tumetumia kule Stiegler’s Gorge kwa ajili ya kufanya mazungumzo na wawekezaji hao waliopo katika jimbo lake wa mradi huo wa bomba la gesi ili tuone uwezekano wa wao kushiriki kusaidia ujenzi huo wa kituo cha polisi.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, tatizo la miradi hii ya REA ambapo unakuta mradi umefika kwenye eneo kama kijiji lakini unakuta nyumba, taasisi za kidini, taasisi kama shule, zahanati, pampu za maji zimeachwa bila kuunganishiwa umeme, ni tatizo ambalo lipo pia Jimboni kwangu Bukene na Wilaya ya Nzega yote.

Mheshimiwa Spika, sasa ninachotaka kujua ni kwamba pamoja na kwamba Waziri alifanya ziara na akatoa maelekezo maalum kwa Mkandarasi wa Wilaya ya Nzega ambaye ni POMI Engineering kuhakikisha maeneo yaliyoachwa yanaunganishwa, lakini mpaka sasa mkandarasi huyu inaonekana ameshindwa kabisa kupata vifaa vya kuunganishia maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, sasa nilitaka kujua je, Serikali iko tayari kutoa maelekezo maalum au kumsaidia huyu mkandarasi ili aweze kupata hivi vifaa; waya, nguzo ambavyo inaelekea kabisa kumpata…

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. SELEMANI J. ZEDI:...ili aweze kufanya kazi ya kuunganisha maeneo hayo yaliyoachwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zedi, Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze pia Mheshimiwa Zedi kwa kazi nzuri ndani ya Jimbo lake, wiki moja iliyopita tulikuwa katika ziara ya Jimbo lake na nilifanya pia ziara katika Wilaya ya Nzega. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umelisema kwa jumla pia suala hili la vifaa, nataka nimtaarifu Mheshimiwa Zedi na Wabunge wote, kweli zipo changamoto za hapa na pale kuhusu vifaa, lakini tukitathmini mchango wa sekta ya nishati kwenye viwanda vya ndani, kwa sababu changamoto hii imejitokeza baada ya kutoa agizo vifaa vyote vinavyotumika katika mradi huu vizalishwe ndani ya nchi na agizo hili limesababisha kuwezesha viwanda zaidi ya tisa vipya vinavyozalisha nguzo, viwanda zaidi ya vinne vya mita na viwanda zaidi ya vitano vya waya havikuwepo nchini, vyote hivi vimetokana na agizo la kuhakikisha kwamba vifaa vyote vinavyotumika kwenye miradi hii vizalishwe ndani ya nchi ili vilete ajira lakini pia mapato kwa wananchi lakini pia mapato kwa wanaoajiriwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Zedi mimi nikuthibitishie tu sisi kama Wizara tunaendelea kusimamia kuhakikisha changamoto hii inapungua na kama nilivyosema katika majibu mbalimbali ndani ya Bunge lako tukufu, imeendelea kupungua na ndiyo maana leo tunajivunia zaidi ya vijiji 1,400 tumeshaviwasha kwenye REA III mzunguko wa kwanza ukiacha na awamu zingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe wito kwa wakandarasi pamoja na ma-supplier kwa kuwa wanategemeana, wakae pamoja ili kuondoa vikwazo mbalimbali ambavyo vinaonesha kwamba vinachangia kutokuwepo kwa vifaa kwa wakati katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe tu Wabunge muendelee kutuunga mkono katika hili ili mradi huu unaotumia shilingi trilioni moja na bilioni 200 uchangie uchumi wa taifa kwa kutekeleza Sera ya Viwanda, asante sana. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina swali la nyongeza. Wakati mwingine wananchi wetu wanakwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wanakosa dawa siyo kwa sababu dawa hiyo inakuwa haipo kwenye maghala ya MSD, bali ni matatizo ya uagizaji ambayo yanatokana na vituo vyetu vya kutolea huduma za afya kutokuwa na hawa watu muhimu wafamasia na wateknolojia dawa ambao wana utaalam wa kuratibu, ku-forecast na kujua kwamba kipindi hiki tuagize dawa gani, kipindi hiki kuna mlipuko wa magonjwa fulani, kuwe na dawa fulani. Sasa ili kuhakikisha kwamba watu hawa muhimu wanakuwepo muda wote katika vituo vya kutolea huduma za afya:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuruhusu Ma-DMO na Wakurugenzi wa Halmashauri zenye uwezo ku-engage watu hawa ili wawepo muda wote hata kwa mtindo wa internship au mikataba ya muda wakati tukisubiri hizi ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kimsingi tunafahamu kwamba katika vituo vyetu vya huduma za afya kama ambavyo nimetangulia kueleza kwenye jibu la msingi, tuna upungufu wa wataalam hawa wa teknolojia wa dawa na wateknolojia wasaidizi wa dawa. Ni kweli kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge Zedi ameelezea, tunahitaji kuwa na wataalam hawa ili kuhakikisha vituo vyetu vinaweza kuweka maoteo mazuri ya dawa lakini pia uagizaji kulingana na utaalam ili kuhakikisha kwamba dawa zinapatikana katika vituo vyetu.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na jitihada hizi za Serikali, pia Serikali ilishatoa maelekezo kwa Wakurugenzi, kwa Halmashauri zile ambazo zina uwezo wa mapato ya ndani ya kuwaajiri kwa mikataba wataalam hawa, waweze kuwaajiri na kuwasimamia kwa karibu chini ya DMO kuhakikisha huduma hizi za upatikanaji wa dawa katika vituo hivyo zinaboreshwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie kwamba jambo hilo lishafanyiwa kazi na Serikali na nitoe wito kwa Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kutumia fursa hiyo kwa wale ambao wana uwezo wa kuwaajiri ili tuboreshe huduma za afya kwa wananchi.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, yanayoleta matumaini kwa wananchi zaidi ya 80,000 katika vijiji 20 vya Jimbo la Bukene ambao sasa wanakwenda kupata majisafi na salama kutoka Ziwa Viktoria: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari baada ya Bunge hili la bajeti tuongozane kwenda Bukene ili apeleke hizi taarifa njema na kuwaandaa wananchi kupokea mradi huu muhimu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nakushukuru sana kwa kupigilia msumari ruhusa ile ya Spika aliyoiongea jana.

Mheshimiwa Naibu Spika, basi napenda tu kukuhakikishia, kwenda kwenye majimbo yenu Waheshimiwa Wabunge ni moja ya majukumu yangu. Hivyo, baada ya Bunge hili Bukene nitafika, tutafanya kazi vizuri kwa pamoja, lengo ni kuona majisafi na salama yanapatikana bombani kwa wananchi wetu. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja la nyongeza.

Umuhimu wa barabara hii umeongezeka baada ya ule mradi mkubwa wa bomba la mafuta kutoka Uganda mpaka Tanga, umeamua kujenga ile kambi kubwa itakayoandaa mabomba yote yatakayofukiwa njia nzima pembeni ya barabara hii na kwa kuwa wasimamizi wa mradi huu wale ECOP wana package ya miundombinu ya kuboresha barabara; na kwa kuwa kuna kakipande kama kilometa 50 mpaka 60 kutoka Nzega - Itobo mpaka kwenye ile kambi ambako mabomba yatapita.

Je, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi haioni umuhimu wa kukaa na hawa wasimamizi wa mradi huu wa ECOP kwa sababu na wenyewe wana package ya miundombinu wakashirikiana ili kipande hiki cha kilometa 50 mpaka 60 cha Nzega - Itobo mpaka Sojo ambako ni kipande katika barabara hii hii, wakashirikiana na wakapunguza gharama upande wa Serikali na huu mradi ukatoa fedha zake ili kukamilisha barabara hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Zedi, Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Zedi kwa mchango huo na mimi nimhakikishie Wizara pamoja na hawa watu wa ECOP tutakaa nao kuona uwezekano wa kujenga hiki kipande cha kilometa 50 hadi 60 kutoka Itobo hadi Nzega ili kuweza kurahisisha utengenezaji wa hili bomba, kwa hiyo mimi binafsi nimhakikishie Mheshimiwa nitafika Jimboni kwake na tuweze kuangalia uwezekano huo, ahsante.
MHE. SELEMAN J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze Serikali kwa kupeleka milioni 250 katika Kituo cha Afya cha Itobo ili kuboresha miundombinu ya pale, lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vituo vya afya vya zamani kama Kituo cha Afya cha Itobo na Kituo cha Afya cha Bukene vinaitwa vituo vya afya, lakini kimsingi havina ile miundombinu mizuri ambayo inafaa kuitwa kituo cha afya. Unakuta kinaitwa kituo cha afya, lakini hakina maabara, hakina wodi, hakina theater, hakina X-ray. Kwa hiyo, swali langu ni kwamba je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari baada ya Bunge hili na kabla ya Bunge la Februari kwenda Jimboni Bukene atembelee hivi vituo vya afya vya zamani ambavyo ni tofauti kabisa na vituo vya afya vya sasa, japo tunahesabiwa kwamba tuna vituo vya afya, lakini kimsingi haviendani kabisa na hali halisi inayopaswa kuwepo kama kituo cha afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Suleiman Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipokee pongezi zake kwa kazi hii kubwa ambayo imeendelea kufanywa na Serikali Awamu ya Sita, chini ya Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha tunajenga vituo vya afya ikiwemo katika Kata ya Itobo. Hata hivyo, nimhakikishie kwamba Serikali tunatambua vyema kwamba ni kweli vituo vyetu hivi bado vina upungufu wa miundombinu na ujenzi huu kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi ni wa awamu. Kwa hiyo, tuko awamu hii ya kwanza ya ujenzi wa majengo ya kuanzia, lakini awamu ya pili tutakwenda kujenga majengo mengine yakiwemo wodi, lakini na majengo mengine ya vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwahidi Mheshimiwa Zedi kwamba niko tayari, tutakubaliana baada ya Bunge hili, tupange ratiba ya kwenda kule Bukene, tupitie Vituo vya Afya vya Itobo na Bukene, tuweze kufanya tathmini na kuona mpango wa kuendeleza ili viweze kuwa na hadhi ya vituo vya afya. Ahsante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, kata yangu ya Karitu ndiyo kata pekee ambayo bado haijapata mnara wa mawasiliano ya simu Jimboni kwangu. Zaidi ya mara mbili kata hii imekuwa kwenye orodha ya kata ambazo zinapaswa zijengewe minara kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote lakini mwaka unaisha haujajengwa.

Sasa swali langu ni kwamba je, Wizara ina mpango gani au mkakati gani wa kuhakikisha kwamba kata zote zinazokuwa kwenye mpango wa kujengewa minara kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote basi inajengewa kwa mwaka huo husika wa fedha?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kuhusu kata ya Karitu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge alichokisema na hili limekuwa ni tatizo kwa muda mrefu ni kwamba katika zabuni ambazo zimepita tulitangaza ujenzi wa minara katika maeneo 199 lakini watoa huduma walijitokeza katika maeneo 90. Sisi kama Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tunatoa ruzuku, ruzuku ambayo tunayoitoa mtoa huduma anaenda kujiridhisha katika eneo ambalo anatakiwa kujenga mnara na baada ya kuona kwamba business case inaonesha kabisa kwamba baada ya muda mrefu kabisa hawezi kupata faida yoyote hivyo maeneo hayo wanayakwepa.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa Serikali imeanzisha mazungumzo ili tuangalie namna bora ya kuhakikisha kwamba tunapotangaza maeneo haya basi maeneo yote yapate watoa huduma kulingana na market share ya kila mtoa huduma hapa nchini nakushukuru sana.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante; barabara ya kutoka Tabora – Mambari – Bukene – Itobo – Kahama ilishafanyiwa, usanifu wa kina na ilitengewa fedha kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami.

Je, ni sababu zipi zinafanya ujenzi huu usianze licha ya kuwa imeshatengewa fedha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Zedi Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara ya Tabora – Mambari – Ntobwa – Nzega imeshafanyiwa usanifu wa kina na ipo kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mbunge kwamba Serikali inatafuta fedha na itakapopatikana hiyo fedha, tutaanza kwa sababu tayari ipo kwenye mpango na ipo kwenye bajeti. Ahsante. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa kuiweka Kata ya Ikindwa kwenye mpango wa kujenga mnara katika zabuni iliyopitishwa mwezi Oktoba, lakini nina swali la nyongeza kuhusu Kata ya Karitu. Miaka miwili, mitatu iliyopita, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ulifanya tathmini kwenye Kata hii ya Karitu na ukabaini kuna upungufu wa mawasiliano na ukaingizwa kwenye zabuni. Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kinachotakiwa kufanywa ni kutangaza upya, kuingiza upya Kata hii ya Karitu kwenye zabuni, badala ya kwenda kufanya tathmini upya kwa sababu kazi ya tathmini ilishafanyika na ndio maana kata hii iliingizwa kwenye zabuni miaka miwili, mitatu iliyopita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Serikali ilifanya tathmini katika maeneo haya, lakini kulingana na uwekezaji mbalimbali wa makampuni ambayo ni tofauti kabisa na uwekezaji wa Serikali, inawezekana kabisa mahitaji yanayohusika yanaweza kubadilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hivyo, kama nilivyojibu katika swali la msingi ni kwamba maeneo ambayo yalikuwa yameshafanyiwa tathmini katika Jimbo la Bukene yalikuwa ni mengi lakini tunaenda hatua kwa hatua kulingana na upatikanaji wa fedha. Tayari Kata ya Ikindo imeshaingizwa katika mradi ambao umeshatangazwa tarehe 22 Oktoba. Tunaamini kwamba kulingana na fedha zinavyozidi kupatikana basi na hii Kata ya Karitu na yenyewe itaingizwa katika utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ya Naibu Waziri nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kipande cha KM 65 katika barabara hii kutoka Nzega, Itobo mpaka Kagongwa, ndicho kitatumika kubeba mzingo mkubwa wa mabomba ya mradi wa mafuta kutoka Hoima - Uganda mpaka Tanga, kwa hali ilivyo sasa barabara ile ni nyembamba, madaraja madogo haiweze kabisa kubeba mzigo huo mzito wa hayo mabomba ya mradi wa bomba la mafuta.

Mheshimiwa Spika, nilishashauri Wizara ya Ujenzi ikae na Wizara ya Nishati pamoja na wenye mradi EACOP ili waweze kuzungumza namna ambavyo hizi KM 65 kutoka Nzega - Itobo na Kagongwa namna ambavyo wanaweza kuzishughulikia kwa haraka ili mzigo huu mzito uweze kupita.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba Wizara imefikia wapi kukuaa na Wizara ya Nishati na hawa wenye mradi EACOP ili kuzungumzia namna kushughulika na hiki kipande cha KM 65 ili mzigo wa mabomba uweze kupita kwenda kwenye site.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Zedi, Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukuwe nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Zedi kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia barabara hii na hasa hiki kipande alichokitaja. Katika eneo alilolitaja ndio kutakuwa na kituo kimoja kikubwa sana kwa ajili ya ujenzi wa bomba la mafuta. Kwa hiyo, anachosema barabara ile haiwezi kuhimili kubeba uzito wa magari yanayopita na ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo sasa inakuwa ni barabara ya Taifa kwa ajili ya uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea kuratibu pamoja na wadau wengine ikiwemo Wizara ya Nishati, EACOP na wadau wengine kuhakikisha kwamba tunaijenga hii barabara ili tutakapoanza kazi hii barabara isije ikawa ni kikwazo kwa maana ya madaraja na upana wa barabara yenyewe.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge taratibu zipo zinaendelea. Ahsante. (Makofi)
MHE. SELEMAN J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Tangu mashine hii ya Ultrasound ifungwe pale Bukene, hakujawahi kuwa na mtaalam wa hii mashine, na kwa hiyo, wagonjwa wanapofika pale hawapati huduma hii, na badala yake wanapelekwa Kituo cha Afya cha Itobo kilichopo zaidi ya kilometa 20: Je, Serikali inaweza kutoa maelekezo maalum kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri au Wizarani ili mtaalam wa Ultrasound apelekwe, awe station pale kwa sababu hakuna tija yoyote kuwa na mashine ya Ultrasound wakati mtaalam wa kuiendesha hayupo na, kwa hiyo haifanyi kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa jengo mahususi kwa ajili ya kuweka mashine ya X-Ray katika Kituo cha Afya cha Itobo linakamilika; je, ni nini commitment ya Serikali sasa ya kuweka mashine hiyo mara tu jengo hilo litakapokamilika pale Kituo cha Afya cha Itobo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Suleman Jumanne Zedi, Mbunge wa Jimbo la Bukene, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali imepeleka mashine ya Ultrasound katika Kituo cha Afya hiki cha Bukene, lakini safari ni hatua. Tulianza kwanza kuandaa mazingira kwa maana ya kandaa majengo na kupeleka mashine. Sasa hatua inayofuata ni kupeleka mtaalam wa mashine ya Ultrasound ili aanze kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeshatoa maelekezo. Nitumie fursa hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nzenga kuangalia ndani ya wilaya kufanya internal redistribution ya staff kwa ajili ya kwenda kutoa huduma ya Ultrasound, na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutaangalia uwezekano wa kupata mtaalam mwingine kwa ajili ya kwenda kuongeza nguvu kule Bukene.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhusiana na Jengo la X-Ray katika Kituo cha Afya cha Itobo, ni kweli Serikali inaendelea na ujenzi na mara baada ya kukamilika jengo lile, mashine ya X- Ray itapelekwa ili tuendelee kutoa huduma kwa wananchi wa Itobo, ahsante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; Vijiji vya Nsumba na Mboga, Kata ya Semembela na Kijiji cha Idubula na Burunde, Kata ya Karitu vimekuwa vikiwekwa kwenye mpango wa kujengewa minara kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote lakini karibu miaka miwili sasa inapita na minara haijengwi.

Je, sasa Serikali inatoa kauli gani au commitment gani kwamba safari hii vijiji hivi vya Nsumba, Mboga, Idubula na Burunde vitajengewa minara ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zedi, Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya kuhakikisha kwamba utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi inaendelea kutekelezwa kwa kiwango kikubwa. Ni kweli kabisa nchi yetu ina vijiji zaidi ya 12,300; tunakwenda hatua kwa hatua na tayari tunapeleka minara 758, tumefanya tathimini katika vijiji 2,224 lakini vilevile tunakwenda kupeleka minara 600 kwa ajili ya huduma ya mawasiliano katika vijiji vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini kwamba katika awamu ijayo vijiji vya Idubula, Burunde pamoja na vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja tutaviweka katika hatua hizo za utekelezaji ili wananchi wa Bukene wapate huduma ya mawasiliano bila kuwa na changamoto yoyote.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mwaka huu wa fedha unaoisha 2022/2023 Serikali ilitenga milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya kwenye Kata ya Igusule, Jimbo la Bukene Halmashauri ya Wilaya ya Nzega. Sasa, ukizingatia kwamba bado siku chache mwaka huu uishe;

Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kupeleka fedha hizi sasa milioni 500 ambazo ilizitenga kwenye Kata ya Igusule ili ujenzi wa Kituo cha Afya uanze?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakaa na Mheshimiwa Zedi kuona hizi milioni 500 zilizotengwa ni hatua gani imefikiwa kwa ajili ya kuzipeleka kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya kule Igusule, Jimboni Bukene.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru sana kwa jibu zuri sana lililotolewa na Mheshimiwa Waziri na nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya Awamu Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea na kutupatia shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya pale Sojo Igusule.

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu ni kwamba Mheshimiwa Waziri, utakuwa tayari baada ya Bunge hili la bajeti uongozane na mimi kwenda Kijiji cha Sojo ili wananchi wa Sojo Igusule wakakushukuru kwa kutupatia shilingi milioni 500 za kujenga kituo cha afya ambacho tulikuwa tunakihitaji sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Jimbo la Bukene kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Zedi amekuwa akifuatilia sana juu ya ujenzi wa kituo hiki cha afya na Serikali sikivu ya Awamu wa Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, imewasikia wananchi wa Jimbo la Bukene, na kituo hicho kitakuja na niko tayari kuongozana nawe kwenda Sojo ili wananchi waweze kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kutoa fedha kwa ajili ya kituo cha afya hicho. Ahsante. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali la nyongeza. Shamba hili la Kisasiga lenye ukubwa wa ekari 48,000 zoezi la kupima udongo lilishafanyika na lilifanywa na watalamu wa Taasisi ya Kilimo ya TARI Mlingano tangu mwezi Agosti, 2021 na majibu yakaja kwamba shamba lile linafaa kwa Kilimo cha Alizeti. Kwa hiyo upimaji umeishafanyika, majibu yameishakuja.

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu ni Serikali haioni kwamba sasa hivi kinachotakiwa ni kupeleka Watalam wa Miundombinu ya Ujenzi wa Block Farm ili washirikiane na Watalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kufanya tathimini ya Ujenzi wa Miundombinu ya Block Farm ili mwaka huu wa fedha unaokuja ibaki tu kutafuta fedha ili kazi ya ujenzi wa block farm ianze kwa sababu ekari 48,000 zimekaa idle na majibu tangu mwaka 2021 yameishapatika. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kama ambavyo tumejibu katika jibu la msingi kwamba kuna Timu ya Watalam wa Wizara na yenyewe imefika katika eneo la Nzega na baada ya hiyo taarifa hatua zote ambazo Mheshimiwa Mbunge amezisema Wizara itazifanyia kazi. Bahati nzuri sana katika kipindi ambacho Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza msukumo mkubwa katika kilimo ni kipindi cha Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nimthibitishie tu kwamba shamba hilo litajengwa na Watalam watapelekwa kwa ajili ya kufanya hiyo tathimini ya miundombinu na katika mwaka wa fedha tutaliweka katika bajeti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali itakapokuwa tayari kuanzisha maeneo mapya ya kiutawala, je, itakuwa tayari kuzingatia na kutoa kipaumbele kugawanya Kata za Igusule, Mambali na Semembela ambazo maombi yake yalishatolewa na mchakato ulishaanza mpaka umefika hatua ya RCC? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itakapokuwa tayari kuanzisha maeneo mapya ya utawala, itaanza na first in, first out. Kwa hiyo, naipongeza Halmashauri ya Nzega kwa kuwasilisha maombi hayo na pia, halmashauri nyingine ambazo zimeshawasilisha. Tutakapoanza kutoa nafasi hizo, basi tutawapa kipaumbele wale waliowasilisha mapema zaidi. Ahsante sana.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu yanayoleta matumaini kutoka kwa Waziri, nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilitumia fedha nyingi miaka kadhaa iliyopita kujenga skimu hizi za umwagiliaji, hasa hii Skimu ya Kamalanga ambyo iliigharimu zaidi ya shilingi bilioni moja lakini na hii Skimu ya Malolo pamoja na ya Ikindwa. Sasa Mheshimiwa Waziri amesema kwamba Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufufua skimu hizi za umwagiliaji ambalo ni jambo jema na fedha hizo ziko kwenye mwaka huu wa fedha.

Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari wakati wakiendelea na hatua za mwanzo za kufufua skimu hizi, aweze kuongozana na mimi baada tu ya Bunge hili tuende Bukene akayaone hayo Mabwawa ya Malolo, Ikindwa na Nhalanga ili aweze kutia msukumo na kuhakikisha mabwawa hayo yanafufuliwa na yanaleta tija katika kilimo cha mpunga ambacho tunakitegemea sana kwenye Jimbo la Bukene? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge Selemani Zedi, nipo tayari na nitaongozana naye kufika katika maeneo yote niliyotaja, nimhakikishie tu Mheshimiwa Dkt. Samia ametuthibitishia kwamba maeneo hayo yatafikiwa na yatajengwa, ahsante. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameidhinisha ajira mpya 46,000 zikiwemo ajira za kada ya Afya. Je, Serikali itakuwa tayari kutoa commitment hapa kwamba katika hizi ajira mpya 46,000 ambazo ndani yake kuna ajira za kada ya afya, itapeleka angalau mganga mmoja na nesi mmoja kwenye Zahanati za Buhulyu, Luhumbo, Mambali, Ikindwa, Lukuyi, Mbutu na Karitu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwajali wananchi, tayari Mheshimiwa Rais, ametoa kibali cha ajira za watumishi wa sekta ya afya na pia watumishi wa sekta nyingine.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatoa commitment siku ya leo kwamba kwenye zahanati hizi ambazo zina mtumishi mmoja mmoja, tutahakikisha kwenye ajira hizi ambazo zinafuata tunapeleka watumishi ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi, ahsante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba barabara hii inajengwa kwa awamu na awamu, maana yake ni mwaka wa fedha, kwamba ni kidogo kidogo. Swali langu ni kwamba, je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuongeza idadi ya kilometa kwa hii awamu kwa mwaka wa fedha, kwa sababu tukiendelea na kilometa moja moja kwa kila mwaka wa fedha na barabara hii imebakiza kilometa 104, haoni kwamba itatuchukua miaka 104 kumaliza barabara hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali siyo kuijenga hii barabara kwa awamu kwa kipindi chote, lakini mpango wa Serikali ni kuijenga barabara hii yote kwa kiwango cha lami na ndiyo maana imesanifiwa yote. Kwa kadiri tunavyopata fedha Serikali imeona ni bora tuanze kujenga kwa awamu kadiri fedha zinavyopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna uhakika kwamba kadiri tutakavyokuwa tunaendelea, na bajeti itakavyoruhusu, mpango ni kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami kama anavyoomba Mheshimiwa Mbunge, ahsante. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kazi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji imeanza hata Jimboni kwangu Bukene Kampuni ya Sinotech imefika na imeanza kazi hiyo. Hata hivyo wanapeleka umeme kwenye vitongoji ambavyo tu vimepitiwa na line kubwa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha hata vile vitongoji ambavyo havipitiwi na line kubwa (high tension) navyo vinapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba huu mradi wa vitongoji 15 ni mradi jazilizi, kwa hiyo unatekelezwa kwenye maeneo ambayo tayari yana miundombinu. Kwa maeneo ambayo hayana miundombinu tunakuja na mradi kuanzia mwezi wa 12 ambao utahusisha kujenga MV na LV lines, lakini vilevile utahusisha kuweka transfoma kulingana na ukubwa wa maeneo tofauti tofauti. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba yale maeneo ambayo hayana miundombinu na kwa hiyo, yameshindwa kunufaika na huu mradi wa ujazilizi wa vitongoji 15 yataendelea kupata umeme na yataendelea kujengewa miundombinu kwa mradi unaokuja wa kupeleka umeme kwenye vitongoji, ahsante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Bukene ambacho kinahudumia Tarafa nzima ya Bukene yenye kata nane ni kikongwe, kimechakaa na kina upungufu wa majengo. Ni lini Serikali itatoa kipaumbele ili nacho kiweze kukarabatiwa, kiwe sawa na vituo vipya vinavyojengwa sasa hivi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Zedi kwa sababu ameleta orodha ya vituo vyake chakavu, kikiwemo Kituo cha Afya cha Bukene. Pia, nampongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nzega, ameleta orodha hiyo na pia, ameleta tathmini ya gharama inayohitajika kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa kituo hicho. Kwa hiyo, ni suala tu la muda tutatafuta fedha kwa ajili ya kwenda kutekeleza mpango huo, ahsante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Bukene wanapata maji safi na salama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri Jimbo la Bukene linapitiwa na Mradi wa Ziwa Victoria. Tayari tunakwenda kuunganisha Jimbo la Bukene ili waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Takriban wananchi 80,000 wanakwenda kupata huduma ya maji na vijiji 20 vitanufaika na mradi huu kutoka Ziwa Victoria. Vilevile tuna takriban vitongoji 100 vinakwenda kupata huduma ya maji. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, mradi huu uko kwenye utekelezaji, tayari umeshaanza na muda siyo mrefu ukikamilika wananchi wake watapata maji safi na salama. Ahsante sana. (Makofi)