Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ussi Salum Pondeza (32 total)

MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, ni wangapi ambao walipandishwa vyeo ambao waliweza kujiendeleza kielimu toka mwaka 1999 na 2000 mpaka sasa na ni utaratibu upi ambao unatumika kupandisha vyeo kwa vijana wa uhamiaji? Kwa sababu mpaka sasa kuna vijana ambao wana vigezo na viwango vya elimu sawa na waliopandishwa vyeo miaka sita nyuma. Kutoka miaka sita mpaka sasa hivi hakuna hata kijana mmoja kwa upande wa Zanzibar ambaye amepandishwa cheo. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza akatupa sababu ambazo zimepelekea miaka sita mpaka sasa hivi kuwe hakuna mtu ambaye ameweza kupandishwa cheo? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, si kwamba hakuna ambaye amepandishwa cheo. Wamepandishwa vyeo katika nafasi tofauti tofauti, kumbukumbu zinaonesha zaidi ya vijana 137 kwa gap lile alilolisemea la mwaka 1999 – 2000 walipandishwa vyeo katika nafasi tofauti tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wale ambao amesema wa upande wa Zanzibar na lenyewe nitalifuatilia kwa undani wake ili niweze kuwasiliana na Mheshimiwa Mbunge. Kama alichosema ndicho, basi katika hatua zinazofuata tunakokwenda tutazingatia ushauri wa Mheshimiwa Mbunge ili kuhakikisha kwamba jambo linapoletwa na watetezi wa wananchi, Waheshimiwa Wabunge, wawakilishi wa wananchi; sisi Serikali tunalifanyia kazi kuhakikisha kwamba panakuwepo na haki ya watu wetu hao wanaofanya kazi vizuri. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka nyuma kulikuwa kuna utaratibu wa Wizara zetu mbili hizi kukutana na kubadilishana uzoefu na vikao hivyo vilivyokuwa vinafanyika vilikuwa vina tija ndani yake ambavyo vilipelekea Madaktari Bingwa kutoka Muhimbili kuja Zanzibar na kutoa ushirikiano mkubwa. Vikao hivyo sasa hivi havifanyiki kwa muda mrefu kidogo. Je, Serikali ina kauli gani kuhusu vikao hivyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba Serikali ina mpango gani na vikao hivyo? Vikao hivyo havijawahi kufutwa na havitofutwa kwa sababu Wizara hizi mbili (Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Muungano na Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar) zimekuwa na utamaduni huo na zinaona utamaduni huo ni mzuri na zitauendeleza. Hivyo, tutaendelea kuvihuisha ili viwe active zaidi kuliko ilivyokuwa katika mwaka huu mmoja wa uchaguzi uliopita. Lakini kuanzia mwezi Januari tayari tumekwisha kufanya kikao kimoja, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Ussi.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri japo hayakidhi ukweli halisi wa mahabusu.
Je, Waziri yuko tayari apewe ushahidi wa raia ambao wanawapelekea chakula raia ambao wanakuwa mahabusu Zanzibar? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusu haki za binadamu, kila mara kumekuwa na taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu juu ya ukosefu wa hali ya amani katika vyuo vya mafunzo Zanzibar. Je, Serikali imeshatolea ufafanuzi kuhusu chombo hicho? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake lakini niseme tu kitu kimoja amekichanganya kwamba, sijakataa watu kupeleka chakula kwa mahabusu na hiyo ni hospitality ya Kitanzania. Mtu kama ana mtu wake yuko mahabusu akaamua kumpelekea chakula, Magereza ama Polisi hawazuii ndugu kuwapelekea ndugu zao chakula wanapokuwa wako mahabusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ndugu zao kuwapelekea chakula mahabusu haimaanishi kwamba Serikali haikupeleka chakula. Wakati mwingine hata mahabusu wenyewe wanakuwa na chaguo lao la chakula anachokula, wengine wana diet zao wanazotaka kula, kwa maana hiyo haingekuwa vyema sana kwa Serikali kusema lazima mtu akiwa mahabusu ale chakula cha Serikali na nadhani hata ninyi msingekubaliana na utaratibu wa aina hiyo. Sisi tunachosisitiza ni kwamba Serikali inaweka bajeti na huo ndiyo umekuwa utaratibu lakini haizuii watu kupelekewa chakula kufuatana na mahitaji yao ama ndugu wanapokuwa wamepeleka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lile la pili la uvunjifu wa amani, tumelisisitiza na tumeendelea kulisisitiza kwamba vyombo vya dola vinafanya kazi kwa mujibu wa sheria na inapotokea kesi moja moja tunazishughulikia kama kesi moja moja na hatua huchukuliwa inapotokea makosa yamejitokeza.
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJAD: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa majibu mazuri ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri amenipatia, naomba kuulizwa swali, je, haoni sababu ya majibu ya vipimo kutoka Zanzibar ambako amesema huwa yanachukuwa muda mrefu kutokana na umbali yanapotoka. Lakini Zanzibar na Tanzania Bara, Dar es Salaam ambapo anapatikana Mkemia Mkuu kwa sasa hivi hakuna umbali, ni dakika 20 mpaka nusu saa inaweza kufika.Je, haoni kutoa kipaumbele kwa vipimo ambavyo vinatoka Zanzibar kupewa majibu ya haraka, kwa sababu watu wamekuwa wakipata matatizo ya kusubiri muda mrefu huku wengine wanakuwa wapo katika magereza kwa kusubiria criminal cases zao ziweze kupatiwa majibu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, tunaona kuna haja ya kutoa kipaumbele kwa sampuli za makosa ya jinai zinazotokea Zanzibar lakini ni ngumu sana kutoa kipaumbele kwa msingi huo kwa sababu kama ni kesi za jinai zipo nchi nzima na watu wa kila kona ya nchi hii wana haki ya kupata haki ya kusikilizwa kwenye mahakama zetu kwa wakati bila kucheleweshwa. Tunachokifanya kama Serikali kwa sasa, ili kupunguza ucheleweshwaji, ni kuongeza idadi ya mashine za kupima vinasaba ili kwa ujumla wake kupunguza ucheleweshwaji kwa sampuli zote kutoka kila kona ya nchi yetu, Zanzibar ikiwemo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka huu wa fedha, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, tumetenga bajeti ya kununua mashine tatu mpya za vinasaba lakini pia tunaanzisha kituo cha kupima vinasaba pale Mbeya ambacho pia kitatusaidia kupunguza wingi wa case files kutoka kwenye Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na Kanda ya Kati ambazo zinaweza zikatumia huduma za maabara itakayokuwepo pale Mbeya badala ya kutumia maabara moja iliyopo kule Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, ucheleweshwaji si wa makusudi, ucheleweshwaji ni wa kitaalam kwa sababu kuna vigezo vingi ambavyo vingepaswa kuwepo kabla sampuli hazijapatiwa majibu kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa haraka ikiwemo kujenga uwezo wa wachunguzi wetu wa makosa ya jinai kwa maana ya Jeshi la Polisi wa namna ya ku-navigate kwenye crime scene na kuchukua sampuli. Lakini pia namna ya kujua ipi ni sampuli ya maana na ipi sio sampuli ya maana kwenye kesi hii, lakini pia mlolongo wa mpaka sampuli kufika kwenye maabara nao ni mrefu sana.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwa sampuli kutoka Zanzibar ni lazima wachunguzi wakamilishe uchunguzi wao, wakusanye sampuli, wazipeleke kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kule Zanzibar naye aridhike kwamba sampuli zinajitosheleza ziweze kuletwa huku Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
Mheshimiwa Spika, kwa vyovyote vile lazima kuwe kuna ucheleweshwaji, majibu pia yana mlolongo huohuo kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali Maabara, kwenda mpaka kule. Na wataalam tulionao pia ni wachache, kwenda kutoa ushahidi kwenye kesi mbalimbali nchi nzima nayo pia ni sababu nyingine ya ucheleweshwaji.
MHE.USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo ninalo. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni tatizo gani lililopelekea ripoti zenye umuhimu mkubwa kama huu wa haki za binadamu zisichapishwe kwa wakati ili Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla wakaweza kujua hali za haki za binadamu katika nchi yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wabunge kwa upande wa Zanzibar hawapati fursa ya kukagua vituo vya polisi wala vyuo vya mafunzo ili kuwatembelea waliozuiliwa na waliofungwa kujua kama utekekelezaji wa haki za binadamu unafanyika kwa kiwango ambacho kinatakiwa. Je, Serikali iko tayari kuwatengenezea Wabunge wa Zanzibar utaratibu wa kuweza kuvikagua vituo vya polisi na vyuo vya mafunzo ili kuona haki ya binadamu inatendeka kwa kiasi gani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza amezungumzia kuhusu uchapishwaji wa hizi ripoti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ni kwamba, ni kweli taarifa hizi zinapaswa kuwasilishwa Bungeni kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameuliza na ndiyo maana tumetoa maelezo yetu kama Serikali kwamba ziko ambazo zimekamilika lakini ziko ambazo zinasubiri ukaguzi wa mahesabu ndipo ziweze kuchapwa na kuletwa Bungeni kwa sababu ndiyo itakuwa taarifa kamili.
Kwa hiyo, nimuondoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafahamu umuhimu wa taarifa hizi kuwasilishwa mbele ya Bunge na ndiyo maana Tume inaendelea kufanya kazi hiyo kuhakikisha kwamba taarifa hizi zinafika kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la nyongeza la pili ameulizia kuhusu kuwashirikisha Wabunge wa Zanzibar. Kwa mujibu wa Ibara ya 130(1) na kifungu cha 6 cha Sheria Namba 7 ya Tume ya mwaka 2001, Tume imepewa majukumu kufanya kazi hiyo ya kwenda kufanya ukaguzi yenyewe. Kwa hiyo, kazi hii kimsingi ni kazi ya Tume, lakini ambacho tunaweza tukakifanya kwa sababu ya kuombwa ushiriki wa Waheshimiwa Wabunge katika jambo hili na sisi pia tuko tayari kushirikiana nao ili wapate fursa kufahamu hali zilizoko katika maeneo ya magereza na vituo vya polisi.
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJAD: Mheshimiwa Spika, napenda kuuliza swali moja la nyongeza. Je, ni lini watapata fedha na ukarabati wa kituo hicho kwa sababu, eneo hili ni maarufu na lina matatizo sana ya huduma za kipolisi?
Kwa hiyo, kutoa nafasi kwa saa 12 tu haitoshelezi kwa sababu, kuna maeneo mengi ya uhalifu na historia inaonesha na ripoti zipo, lakini muda unakuwa ni mchache ambapo wananchi wakihitaji huduma za kipolisi wanashindwa kuzipata mpaka wazifuate sehemu za mbali na uhalifu unakuwa umeshatendeka. Je, Mheshimiwa Waziri haoni umuhimu kukipa kipaumbele kituo hiki kwa bajeti hii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Pondeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Maruhubi kinafungwa saa 12.00 jioni siyo kwa sababu ya ukosefu wa fedha, lakini kwa mujibu wa taratibu kulingana na Police General Order (PGO) Namba 287(9) inaeleza utaratibu wa vituo vya polisi vilivyo; kuna class A, B na C. Kwa hiyo, Kituo cha Maruhubi ni Class C ambacho kwa kawaida kinapaswa kifunguliwe saa 12.00 na kifungwe saa 12.00 jioni.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Vile vile nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina swali moja la nyongeza. Tatizo la samani katika vituo vya Zanzibar, zaidi katika Majimbo ya Chwaka, lakini yako katika Wilaya nyingi za Zanzibar yote. Jimboni kwangu kuna Kituo cha Chumbuni ambacho kinahudumia wilaya mbili, Wilaya ya Magharibi na Wilaya ya Mjini, lakini kituo hiki hakina samani, hakina gari, kinahudumia watu zaidi ya 70,000 na kinavuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshalisemea sana suala hili na nimeshaliuliza zaidi ya mara tatu, mara nne na nikaahidiwa kitatengenezwa na huduma zitapatikana, lakini mpaka leo hali iko vile vile. Je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini wananchi wa Chumbuni kuhusu suala letu hili?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa mfuatiliaji sana wa masuala ya jimbo lake na masuala yanayohusu Vituo vya Polisi vilivyoko katika Jimbo lake. Amekuja Mara kadhaa akisemea jambo hilo na tulishatuma wataalam wetu wafanye tathmini ili tuweze kujua namna tunavyoweza kulishughulikia. Kwa kuwa tunaelekea kwenye bajeti niendelee tu kumhakikishia kwamba, punde bajeti inavyoruhusu tutaweka kipaumbele kwenye jambo hilo ambalo amekuwa akilisemea mara kwa mara. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza napenda nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake marefu, hata hivyo, nataka nimuulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, nataka nimwambie elimu ya juu ni suala la Muungano na amejibu katika majibu yake ya msingi kwa wanafunzi ambao wameweza kupata kwa mwaka huu ni 33,920. Nataka nimuulize, je, kati ya hao Wazanzibari ni wangapi nataka nijue? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, napenda niipongeze sana Serikali kwa kuweka vigezo vya kuwatambua zaidi yatima na watu wenye hali ngumu katika mikopo hii. Kuna taarifa ambazo zipo na ambazo zina ushahidi, wengi ambao wanaokosa basi ni hawa yatima na hawa wenye hali ngumu. Hii inapelekea kuomba kwetu sisi Wabunge ili tuweze kuwawezesha waweze kupata elimu hii ya juu. Je, Serikali inasemaje kuhusu hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza sifa za upatikanaji wa mikopo hapo awali sifa kuu ni hizo ambazo niliziainisha na kwa kweli tumekuwa hatusemi zaidi kwamba nani Mzanzibari nani Mtanzania bara, na hiyo ni kwa sababu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hata kwa hali iliyopo katika maisha yetu ya kawaida ni vigumu sana hata kuwatenganisha hawa wanafunzi kwa sababu unaweza kukuta kuna mwanafunzi wa Zanzibar yuko Tanzania Bara na anasoma na mwanafunzi wa Tanzania Bara anasoma Zanzibar. Kwa hiyo tunachoangalia zaidi ni vile vigezo na sifa zinazostahiki waweze kupata mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika suala hili la hawa wenye uhitaji maalum kukosa mikopo, niseme tu kwamba Serikali imekuwa ikizingatia sana na kwa wale ambao wana mazingira hayo ninayoyasema ikithibitika watasaidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano katika mwaka huu wa 2017/2018, jumla ya wanafunzi 7,073 waliopata mikopo kati yao 1,224 ni wale ambao wenye mzazi mmoja na 5,849 ni wale ambao pia walikuwa hawana wazazi, lakini wenye ulemavu ni 626 kwa hiyo kimsingi niseme tu kwamba Serikali imekuwa ikizingatia sana uhitaji. (Makofi)
MHE. USSI S. PONDEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza ningependa Hansard isomeke vizuri, mimi sio Mbunge wa Chumbageni, ni Mbunge wa Chumbuni, Zanzibar, Chumbageni ipo Tanga, kwa hiyo ningependa hansard isomeke vizuri.

Mheshimiwa Mwneyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza ambayo ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri. Kwanza angetupatia tafsiri ya viwanda, katika majibu yake mazuri ametuambia kuna viwanda vidogo na viwanda vidogo sana; kwa hiyo tungependa tupate tafsiri nini tofauti ya viwanda vidogo na viwanda vidogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ningependa kumuuliza, kwa kuwa Wizara yake haihusiki na uwekezaji wa viwanda katika Serikali ya Zanzibar; hadi sasa wawekezaji wakitaka kuwekeza Zanzibar wanatakiwa wachukue leseni zitoke BRELA. Je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuiachia Wizara ya Viwanda ya Serikali ya Zanzibar kuweza kusimamia kazi hii ya utoaji wa leseni?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimuombe radhi kwa kukosea Jimbo lake na nashukuru amesahihisha. Pili, napenda kusema kwamba viwanda vidogo sana ni vile ambavyo mtaji wake hauzidi milioni tano na wafanyakazi wake hawazidi wane. Viwanda ni vidogo vile ambavyo mtaji wake ni ule ambao hauzidi milioni 200 na wafanyakazi wake hawazidi 49.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa suala la leseni; suala hilo umelizungumza lakini kimsingi ni kwamba Wizara ya Viwanda na Biashara inashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Viwanda Zanzibar kiasi kwamba shughuli nyingi tunafanya pamoja. Hata hivyo maboresho yoyote yanayolenga kurekebisha na kuleta urahisi wa kuwekeza yatafanyiwa kazi ili kuwawezesha wananchi wetu na wadau mbalimbali wanaopenda kuwekeza wafanye shughuli zao bila shida na kwa uharaka iwezekanavyo.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini nina swali moja dogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, upimaji wa pili wa mipaka uliofanywa mwaka 1985 uliingia mpaka katika maeneo ya wananchi ambapo wamechukua eneo kubwa la wananchi. Wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa ile mipaka mipya imeingia ndani ya maeneo ya wananchi ambao walikuwepo pale tangu miaka 1960 tofuati na ile mipaka ya mwaka 1978. Je, Serikali ipo tayari kuwaachia maeneo yao yale ya mwanzo kwa mipaka ile ya mwaka 1978 kwa sababu mipaka ya mwaka 1985 imeingia katika makazi ya wananchi?. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kutuhakikishia jambo hili ili migogoro hii iweze kuisha?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, bahati nzuri mimi mwenyewe nimetembelea eneo hilo la Kisakasaka na nilipata maelezo ya kina juu ya mgogoro huu. Kilichopo ni kwamba wananchi wanadai eneo ambalo wao wapo ni la kwao wakati Jeshi wanadai walikuwepo muda mrefu katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, kuna wakati CDF Mstaafu, Jenerali Mwamunyange, alikwenda pale; na katika kulimaliza tatizo hili, alitoa agizo la kurekebishwa kwa mipaka ili wananchi waliokuwa ndani ya Kambi ya Jeshi wawe nje. Kazi hiyo ilifanyika lakini bado wananchi wale hawajaridhika na utaratibu huo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama nilivyosema awali, tunaunda Kamati au Tume ndogo itakayopitia matatizo ya migogoro ya ardhi katika Zanzibar nzima, kwa sababu siyo hapa tu, kuna maeneo mengi yana migogoro; ili tuweze kupata ufumbuzi wa kudumu. Kwa wale wanaostahili fidia, watalipwa fidia na wale ambao hawana haki, basi watalazimika kuyaachia maeneo hayo ili Jeshi liweze kufanya shughuli zake.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru sana kwa majibu hayo mazuri ya
Mheshimiwa Waziri lakini je, Serikali ya Muungano au Wizara hii ya Mambo ya Nje inazishauri zile nchi wakati zina mpango wa kuja kutembelea Tanzania kuziarifu kuwa nchi yetu ya Tanzania ina sehemu mbili za Muungano na kila sehemu ina mahitaji yake ya kiuchumi. Hivyo basi, Wizara ingekuwa inazishauri kwa sababu ukiangalia nchi tisa tu ambazo zimekuja Zanzibar naamini zingekuja na hizi nchi nyingine 12 kuna fursa nyingi ambazo ziko Zanzibar ambazo bara hakuna na kuna fursa ambazo ziko bara ambazo Zanzibar hakuna.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Wizara iweze kuzishawishi wakati nchi za nje zinapoweza ku-engage kuja Zanzibar kuja kutembelea Tanzania. Basi iziambie kuwa Tanzania ina nchi mbili na nchi hizo mbili kila upande una vipaumbele vyake vya kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ambalo nataka niliseme, Wizara inafanya jitihada gani kuwashawishi wale viongozi ambao hawakuja Zanzibar kutembelea wakati wa ziara zao lakini kufanya ushawishi wakutane na viongozi wa Zanzibar huku Tanzania Barai ili wale viongozi wa Zanzibar waweze kutoa haja zao na kuweza kutoa ushahwishi wao wa kuiona Zanzibar nayo inanufaika na ugeni ule. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, nchi yetu ni nchi moja kwa mujibu wa Ibara ya 1 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Na masuala ya nje ni sual ala Muungano kwa m ujibu wa Ibara ya 4 nyongeza ya kwanza ya Katiba. Kwa hiyo, uhusiano wetu na mambo ya nchi za nje unachukulia maanani suala la kwamba ni nchi moja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mahusiano yetu mara nyingi tukiwasiliana wanafahamu kwamba kuna nchi moja inaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na hayo, Serikali na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje imekuwa ikifanya jitihada kubwa sana kuhakikisha kwamba kwa sababu ya historia ya Muungano wetu na hali halisi kwamba ni Muungano ambao umetokana na nchi mbili tunahakikisha ya kwamba wakati viongozi hao wanapokuja nchini, tunajenga ushawishi mkubwa ili watembelee Zanzibar na ndiyo maana kuanzia 2015 mpaka sasa viongozi 21 waliotembelea nchini kwetu. Tisa kati yao wametembelea Zanzibar, vile vile ifahamike kwamba kuna wengine vile vile ambao wametembelea Zanzibar tu wala hawajatembelea upande mwingine wa Jamhuri.

Mheshimiwa Spika, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya masuala ambayo yanapewa kipaumbele sana katika uhusiano wa Kimataifa ni Muungano wetu ndiyo maana hata kwenye Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje kuna Idara maalum inahusika na mambo ya Zanzibar. Mualiko wowote au kiongozi yeyote akija ushawishi mkubwa unafanyika ili aweze kutembelea pande zote mbili za Muungano.

Mheshimiwa Spika, sasa mara nyingi kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi mara nyingine linakuwa ni suala la utashi wa kiongozi mwenyewe na hauwezi kumlazimisha. Kwa hiyo, nimueleze tu kwanmba kwa kweli Serikali inajitahidi sana kuhakikisha kwamba viongozi hawa wanapata fursa ya kutembelea maeneo yote na hasa kujaribu vile vile kuelezea kuhusu fursa za kiuchumi na za kitalii zilizopo Zanzibar.
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, amesema kuna upungufu wa maaskari lakini katika Jimbo langu la Chumbuni tuna matatizo sana ya kupatiwa kituo cha polisi. Kuna kituo kidogo cha Polisi ambacho kinahudumia majimbo zaidi ya manne ya Shaurimoyo, Mwera, Mto Pepo na Chumbuni yenyewe ambao watu wanaoishi pale ni zaidi ya 67,000.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikiuliza zaidi ya mara saba au nane humu ndani ya Bunge na nimepata ahadi mara nyingi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri au Wizara kuwa watafanyia matengenezo au watakiboresha kituo kile kidogo. Je, yupo tayari kuniahidi au kuiahidi hadhara hii kuwa watakijenga kituo kile kwa kushirikiana na Mbunge?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhamira yake ya dhati ya kushiriki katika ukarabati wa kituo hicho. Nimhakikishie kwamba tupo tayari kushirikiana naye kuhakikisha kwamba kituo hiki kinafanyiwa matengenezo ili kiweze kutumika vizuri zaidi.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana ningependa nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwanza ningependa kujua katika bajeti yao ya mwaka huu wa 2021 ni wanufaika wangapi ambao wataweza kunufaika na mikopo hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili nilikuwa napenda niulize Serikali ina mpango gani wa kuwezesha wanafunzi ambao wako vyuo vya kati ambao wale ndio wenye mahitaji makubwa zaidi ya hii mikopo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimwa Naibu Spika, ahsante na napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyoeleza katika bajeti yetu wakati tunapitisha katika Bunge la Bajeti kwamba bajeti ya Bodi ya Mikopo imeweza kupanda kutoka shilingi bilioni 464 mwaka 2021 mpaka shilingi bilioni 570 mwaka 2122 na kwa hali hiyo basi wanufaika wa bodi watapanda kutoka 149,000 wale ambao walinufaika katika kipindi kilichopita mpaka kufika 160,000 katika mwaka 2021/2022 katika mchanganuo kwamba wale wanaoendelea 98,000 watakuwa wanaoendelea 62,000 tunakadiria katika watakaodahiliwa katika mwaka wa kwanza. Kwa hiyo kwa ujumla wao watakaonufaika tunakadiria kuwa watakuwa sio chini ya 160,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili amezungumzia kuhusiana na suala la wanafunzi wa vyuo vya kati. Kutokana na ufinyu wa bajeti yetu bado hatujaweza kuwafikia wanafunzi hawa wa vyuo vya kati kwa hiyo naomba tulichukue kama Serikali jambo hili wakati tunaboresha bajeti yetu kama Serikali, lakini ninyi Wabunge ndio ambao tunapitisha bajeti hapa, basi tunaweza kulileta mezani kwa ajili ya mjadala ili tuweze kuona namna gani tunaweza kuwafikia wale wa kada ya kati. Lakini kwa mujibu wa sheria sasa hivi bodi hii inashughulikia wale wa elimu ya juu peke yake, ahsante.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Chumbuni lina matatizo ambayo yanafanana na Jimbo la Mwanakwerekwe ambalo swali la msingi limeulizwa. Nimekuwa nikiuliza kwa miaka mitano kuhusu Kituo chetu cha Chumbuni ambacho kinahudumia karibu wilaya nzima ya pale mjini, shehia zaidi ya sita, tangu kilikuwa kinafunguliwa asubuhi kinafungwa saa kumi na mbili sasa hivi kimefungwa kabisa. Je, ni lini na sisi tutapata kituo cha polisi kwa sababu kinahudumia zaidi ya shehia sita?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Pondeza, Mbunge wa wawanachi wa Jimbo la Chumbuni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna baadhi ya vituo tulivifunga kwa sababu nyingi sana. Kuna vituo vingine vilifungwa kwa sababu kubwa tulikuwa na upungufu hasa wa rasilimali watu, kwa maana ya polisi. Nimwambie tu Mheshimiwa kwa kuwa sasa Jeshi la Polisi tumeshatangaza kuajiri askari wapya tutahakikisha kwamba kituo kile tutakifungua na tutapeleka askari ili wananchi waweze kupata huduma za ulinzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ningependa nimuulize Mheshimiwa Waziri swali moja la nyongeza kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Spika, amenijibu kuwa Serikali ina mpango wa kufanya upimaji na kufanya tathmini. Je, wakati itakapofika kufanya tathmini na upimaji, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari na mimi niambatane naye kwenda kwenye zoezi hilo? (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ahsante, Mheshimiwa Mbunge ni mdau wetu na tutakuwa tayari kuongozana naye wakati zoezi hili likiendelea. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi swali la nyongeza. Ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya lami katika Barabara ya Iboni, Bolisa na Gubali katika Jimbo la Kondoa Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Pondeza Mbunge wa Chumbuni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa barabara zile ambazo ziko Kondoa mjini barabara nyingi zinahudumiwa na halmashauri kwa zile barabara ambazo zinahudumiwa na Wakala wa Barabara TANROADS naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutajenga kama zilivyoainishwa kwenye mpango na kama ilivyo kwenye bajeti yetu ambavyo tumepanga, ahsante. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina swali dogo kabisa la nyongeza la kumuuliza.

Mheshimiwa Spika, tathmini hiyo ambayo imefanywa ya vituo vibovu na nyumba chakavu za askari, lakini katika Jimbo langu la Chumbuni nina vituo viwili ambavyo ni vibovu ambavyo vimefungwa zaidi ya miaka minne. Nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri; yuko tayari kuambatana na mimi kwenda katika jimbo langu kwa ajili ya ukarabati wa vituo vyangu ambavyo nimekuwa navidai sasa ni awamu ya pili? Ni lini na yeye yuko tayari nami niko tayari naomba, anisaidie kwa jambo hili. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, najua katika jimbo lake Kituo cha Kiwanda cha Soda Maruhubi na Kituo cha Chumbuni ndivyo ambavyo vimeathirika sana. Nimwahidi mbele yako kwamba tarehe 22 na 23 mwezi huu wa Februari nitakuwa Zanzibar. Pamoja na mambo mengine nitakayofanya ni kutembelea Vituo vya Chumbuni. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini naomba niulize swali la nyongeza. Serikali imekuwa na majibu mazuri sana kuhusu mfumuko wa bei, lakini uhalisia ulivyo nje katika mitaa na vijiji, hali ilivyo haiko hivyo ambavyo Serikali imekuwa ikijibu. Je, Serikali inaliambia nini Taifa letu la Tanzania juu ya mfumko huu wa bei?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Pondeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali na mipango yake ya Serikali ni kusimamia bei za bidhaa na kuona kwamba wananchi wanapata huduma zao kwa bei nafuu. Ahsante.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niulize swali dogo la nyongeza. Kama ilivyo Jimbo la Chakechake kuhusu kujengewa kituo; nami nimekuwa nikiuliza sana katika Jimbo langu la Chumbuni; na nimekuwa nikipewa ahadi zaidi ya mara sita, saba kwa vituo vyangu viwili vya Marubi na Chumbuni kuwa nitapata msaada kutoka Jeshi la Polisi na kujengewa; na tuliwahi kuuliza ikiwa Serikali iko tayari kuvirasimisha kwetu, kwa wananchi wa Jimbo la Chumbuni? Basi wafanye hivyo, halafu watupe kibali, nasi tunaweza kuendelea wenyewe. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pondeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli amekuwa akiuliza maswali ya Chumbuni na nilimwahidi katika kipindi cha bajeti cha Aprili – Juni. Niliweza kwenda Zanzibar na nilitembelea kituo chake. Kinachogomba ni upatikanaji wa fedha ndiyo maana tunaweka vipaumbele. Mheshimiwa Mbunge avumilie na akubaliane nami kwamba pale tutakapopata fedha, Chumbuni itapewa kipaumbele kama tunavyofanya kwenye maeneo mengine ya Chakechake na kwingineko. Nashukuru. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nilikuwa nataka tu nami nipate majibu ya Mheshimiwa Waziri ya swali langu dogo la nyongeza. Nimekuwa nikiahidiwa mara nyingi sana, zaidi ya mara sita, saba juu ya vituo vyangu katika Jimbo langu la Chumbuni, lakini sijapata mwendelezo wala kujengewa vituo hivi na hali ya kiusalama kila siku zikivyoenda imekuwa siyo nzuri na wananchi wanafuata huduma mbali kiasi ambacho kama kuna mhujumu ametokea, basi watu kupata usaidizi inachukua muda mrefu sana.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba majibu ambayo yataeleza ni lini tutapata huduma hii katika Jimbo letu la Chumbuni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Pondeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ussi anafahamu nilitembelea Zanzibar na kwenye jimbo lake nilifika nikaona hali ya vituo vidogo vya polisi vilivyopo na kwa kweli kwenye eneo lake anastahili kujengewa Kituo cha Polisi.

Mheshimiwa Spika, naomba tu upande wa Kamisheni ya Polisi ya Zanzibar iingize mahitaji ya Kituo cha Polisi eneo la Chumbuni ili iweze kupangiwa bajeti kwa ajili ya kuanza kujengwa kwenye bajeti itakayofuata.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kuuliza swali la nyongeza. Ningependa nimuulize Mheshimiwa Waziri, nimekuwa nikisimama mara nyingi kuhusu matatizo ya vituo vyangu vya Chumbuni. Je, sasa nataka kauli yake, yuko tayari kuongozana na mimi mpaka kwenye jimbo langu kutokana na uhalifu umekuwa ukiongezeka na zaidi ya mara sita nimekuwa nikiuliza bila kupata majibu sahihi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pondeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishasema, tutakapokuwa tunakwenda kwa Mheshimiwa Amour kwa sababu kote ni Zanzibar niko tayari pia kupita kwenye jimbo lake ili kuona kiwango cha uhalifu anachozungumza.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ningependa kujua kwa vile kuna taasisi ya ASA ambayo Serikali iliipa dhamana ya kutoa mbegu katika msimu wa mwaka 2020/2021; zile mbegu hazikufanya vizuri na wakulima wengi ambao wamezitumia zile mbegu wamepata hasara.

Je, nini kauli Serikali katika kuwafidia wale wakulima ambao wamekula hasara kutokana mbegu zile za taasisi ya ASA? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali mmejipangaje sasa kuhakikisha haitokei tena wakulima wadogo wadogo ambao wanapata mbegu kutoka taasisi ile ya ASA wakaingia tena hasara ili wakaendelea kuwa maskini zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika msimu alioutaja Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) alisambaza mbegu za alizeti ambazo katika baadhi ya maeneo zilifanya vizuri na pia katika baadhi ya maeneo hazikufanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, ziko sababu nyingi zilizopelekea kutokufanya vizuri hasa kutokana na misimu ya kupanda na changamoto zingine zilizosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Iko mikoa ambako mbegu hizi zilistawi vizuri na wananchi wamevuna, wamepata mavuno makubwa na tumekuwa tukichukua kama sehemu ya kielelezo.

Mheshimiwa Spika, katika kuitatua changamoto hii katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023 Serikali imetenga fedha kuhakikisha kwamba tunazalisha mbegu, tunazigawa kwa ruzuku kwa wakulima ambazo ni certified seed tofauti na zile ambazo zimewekwa awali na lengo letu ni kuhakikisha kwamba wakulima wazipate mbegu hizi kwa bei rahisi ya ruzuku kwa kilo mbili kwa shilingi 10,000 ili ziweze kuwasaidia kutokana na changamoto ambayo waliipata.

Mheshimiwa Spika, vilevile tumehakikisha kuanzia hivi sasa tumempa maelekezo ASA tutaanza kuzalisha certified seeds ili wakulima wetu waweze kulima na waweze kupata tija kutokana na kilimo cha alizeti.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, kwanza nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza. Kutokana na mpango huu ambao majibu yake ya Serikali ambayo ameelezea nataka nimuulize Zanzibar inanufaikaje na mradi huu wa High Education Economic?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, napenda kumwuliza, Serikali ina mpango gani sasa wa kuzipandisha hadhi campus za UDSM na Mwalimu Nyerere ili ziwe Chuo Kikuu ili kuondosha tatizo hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ussi Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali yetu ilipata mkopo, kutoka Benki ya Dunia wenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 425. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mkopo huu, Serikali imetenga zaidi ya Dola milioni 20 kwa ajili ya Chuo chetu cha Taifa cha Zanzibar, kwa ajili ya uongezaji wa miundombinu pamoja na usomeshaji wa wafanyakazi katika eneo lile. Kwa hiyo, eneo hili tunakwenda kulifanyia maboresho makubwa sana kuhakikisha kwamba tunakuwa na miundombinu ya kutosha; na Zanzibar ni mnufaika mkubwa wa mikopo hii pamoja na vyuo vingine vya elimu ya juu nchini.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, ameulizia kuhusiana na suala la kupandisha hadhi campus zetu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu, hivi sasa Serikali kupitia mkopo huu wa HIT, tunakwenda kuboresha miundombinu katika vyuo vyetu vikuu na taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hatuna dhamira ya kupandisha hadhi campus hizi mbili pamoja na campus nyingine za vyuo zilizokuweko pale mpaka miundombinu pamoja na watumishi waweze kutosheleza mahitaji tunayoyahitaji hivi sasa. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kutokana na kadhia ambayo ipo katika swali la msingi ambalo lililoulizwa, Jimboni kwangu katika Jimbo la Chumbuni nimekuwa nikiahidiwa ahadi kama hizi zaidi ya mwaka wa nne huu sasa hivi na Bunge lililopita Naibu Waziri alisema akija Zanzibar atakuja kwangu, lakini hakuweza kufika. Je, leo hii ananiahidi nini ili tukimaliza Bunge hili aweze kushughulikia vituo vyangu vya Chumbuni? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Nyongeza la Mheshimiwa Pondeza, kama ifuatavyo na kwa kweli kama nimemsikia vizuri: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli niliahidi kwenda Zanzibar na moja ya maeneo ambayo ningetembelea ni eneo alilolibainisha, lakini kutokana na ratiba kuwa finyu, nilishindwa kufika. Ipo ahadi ambayo niliitoa kuhusu kumalizia Kisiwa cha Pemba. Nitakapokwenda kule, eneo lako pia nitalitembelea ili kuona changamoto iliyopo. Nashukuru. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mimi ningependa nimuulize swali dogo la nyongeza Mheshimiwa Waziri. Campus ya Marine Science ambayo iko Zanzibar nayo imekuwa na uhaba wa madarasa;

Je, nayo imo katika mpango wa vile vyuo 21 vitakavyopata matengenezo makubwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chimboni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vyuo 64 tunavyo vizungumza hapa ni kwa upande wa Tanzania bara. Kwa upande wa Tanzania Zanzibar tuna utaratibu maalum ambao tunautumia tukishirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar. Kwa hiyo kwa upande wa ukarabati wakule bajeti itatengwa kwenye Wizara ile ili kuhakikisha maeneo yale ambayo yanahusika na vyuo vya ufundi kwa upande wa Zanzibar yanakwenda kushughurikiwa.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nilikuwa na swali dogo la kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri. Je, sasa Serikali haioni umefika wakati wa kuboresha magereza haya ambayo yapo Tanzania nzima ambayo Serikali imerithi na kujenga ya kisasa ambayo yataendana na mfumo wa sasa hivi wa teknolojia ambayo hata Mahakama sasa hivi wanaendesha kesi kwa mfumo wa mtandao ambao iepushe Serikali kutumia gharama ya kuwatoa mahabusu hapa na kuwapeleka mahakamani. Je, kwa nini Serikali isijenge magereza mapya ambayo yatakuwa yana mfumo wa kiteknolojia? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, yapo mabadiliko makubwa ya teknolojia na uendeshaji wa mashauri, hasa Mahakama imeshapiga hatua kubwa. Kwa msingi huo pia, Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia Jeshi la Magereza pia tumeanza. Magereza yanayojengwa sasa yanazingatia mahitaji hayo ya teknolojia na mengine yaliyo bora zaidi ikiwemo pamoja na ukaguzi, vitawekwa vifaa vya elektroniki, ili kuepusha watu kuguswaguswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa magereza ambayo tunayo haiwezekani yote tuyabadilishe siku moja. Tutaendelea kuyakarabati, yatakayofaa kuingiziwa vitendea kazi vya kisasa, vifaa vya kisasa zaidi, tutafanya hivyo, lakini mengine tutaendelea kuyakarabati ili yatoshe kulingana na uwezekano wa bajeti tutaimarisha kwenda kama anavyoshauri Mheshimiwa Mbunge katika siku zijazo, ahsante.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri baada ya kukubali ombi letu la wananchi wa Jimbo la Chumbuni kutupa ruhusa ya kujenga kituo chetu kikubwa cha Polisi ambacho tunaendelea nacho hivi sasa. Kama swali la msingi lilivyoulizwa kuhusu matatizo ya makazi, nasi tunatarajia kuwa na kituo kikubwa cha Class C; je, anatuahidi nini katika tatizo hili la makazi kwa sababu tunajenga kituo kikubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, tunaweka kipaumbele na kila tunapojenga kituo kikubwa cha polisi, tunazingatia pia makazi ya askari na viongozi wa Jeshi la Polisi. Ushauri wangu kwa Mheshimiwa Mbunge, ni kuhakikisha linapatikana eneo ili mpango wa ujenzi uende sambamba na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za vijana wetu, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami ningependa nimuulize swali moja dogo la nyongeza Mheshimiwa Waziri. Je, Jimbo langu la Chumbuni tumekuwa na matatizo sana ya hivi vituo na tumekuwa hatuna kituo zaidi ya mwaka wa nne, tumekuwa tukisema sana lakini tumekuwa tukiahidiwa na Wizara kuwa itakuja kushughulikia. Mheshimiwa Waziri upo tayari nasi tukijenge kile kituo kwa nguvu zetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Pondeza Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, natambua juhudi za Mheshimiwa Mbunge, wamefanya mambo mengi katika Jimbo lake ikiwemo kuanza ujenzi wa vituo hivi, nilitembelea huko na nikaona. Ninamuahidi katika maeneo tutakayozingatia na kuyapa kipaumbele katika utekelezaji wa mpango wetu wa ukamilishaji na ujenzi wa vituo, Jimbo la Chumbuni litapewa kipaumbele. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami ningependa nimuulize swali moja dogo la nyongeza Mheshimiwa Waziri. Je, Jimbo langu la Chumbuni tumekuwa na matatizo sana ya hivi vituo na tumekuwa hatuna kituo zaidi ya mwaka wa nne, tumekuwa tukisema sana lakini tumekuwa tukiahidiwa na Wizara kuwa itakuja kushughulikia. Mheshimiwa Waziri upo tayari nasi tukijenge kile kituo kwa nguvu zetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Pondeza Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, natambua juhudi za Mheshimiwa Mbunge, wamefanya mambo mengi katika Jimbo lake ikiwemo kuanza ujenzi wa vituo hivi, nilitembelea huko na nikaona. Ninamuahidi katika maeneo tutakayozingatia na kuyapa kipaumbele katika utekelezaji wa mpango wetu wa ukamilishaji na ujenzi wa vituo, Jimbo la Chumbuni litapewa kipaumbele. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza napenda kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa vile majibu mazuri ya Serikali Naibu Waziri amesema kama kuna maduka yalikuwa yamefungwa na Serikali kutokana na utakatishaji wa fedha. Yako maduka ambayo yamefungwa na baadaye ikajulikana kama hayana makosa hayo ya utakatishaji wa fedha. Je, Serikali iko tayari kuwarudishia wale ambao walifungiwa lakini hawana shutuma hizo za utakatishaji wa fedha ambao fedha zao na mali zao zilizochukuliwa na Serikali?

Mheshimiwa Spika, la pili, je, ni lini sasa wale wote ambao wameonekana hawana hatia maduka yao yatafunguliwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haiko tayari kuona kwamba kuna rasilimali fedha ya mtu au rasilimali yoyote imebaki Serikalini kumnyima mtu huyo haki yake. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wale wote ambao wameonekana maduka yao hayana makosa yoyote watarejeshewa fedha zao na rasilimali nyingine zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, maduka yaliyosalia, maduka yote ambayo yamefungwa yalikuwa ni 68 wakati ule. Maduka yaliyobaki sasa ni maduka saba tu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika hayo saba yatafunguliwa muda wowote. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Naungana naye kuongeza taarifa kwamba hiki alichokisema Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Serikali ya Awamu ya Sita haiko radhi kuona fedha za raia mwema zinashikiliwa na Serikali. Kwa kipande kingine kulikuwa na component ya kodi ambayo ilikuwa imezidishwa, niongezee na hiyo kwamba kile kipengele cha kodi ambayo ilikuwa imezidishwa tayari kilisharejeshwa kwa wale waliokuwa wanahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki alichosema Mheshimiwa Naibu Waziri na chenyewe kitaendelea kwa wale ambao walikuwa na baadhi ya vitu ambavyo vilikuwa kwenye mikono ya Serikali. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nilikuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali moja, kwa kuwa somo hili linatakiwa kufundishwa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu tu. Je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kufundisha somo hili la uzalendo katika vyuo vya kati na vikuu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa sera tayari imekubalika ya mtaala huu, je, sasa Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri inaweza ikatuhakikishia kuwa ni lini litaanza kusomeshwa katika shule kwa mustakabali wa vijana wetu na nchi yetu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Pondeza, Mbunge wa Chumbuni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uboreshaji wa mitaala yetu ni suala ambalo ni dynamic siyo static. Ni mitaala ambayo inatakiwa iboreshwe kila wakati kulingana na mahitaji ya wakati huo. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako tukufu kuwa Serikali kupitia vyuo vyetu hivi alivyovitaja vya kati na elimu ya juu tunaendelea kufanya maboresho ya mitaala yetu yote ili kuhakikisha kwamba somo hili la uzalendo linakuwa ni sehemu ya masomo yatakayofundishwa katika vyuo vyetu vya kati na juu.

Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ushauri wake tumeupokea na wakati wa maboresho ya mitaala yetu katika vyuo vyetu vya kati utazingatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili anauliza juu ya lini mtaala huu mpya na sera yetu mpya imeanza kutekelezwa. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako tukufu kuwa mtaala huu tayari tumeanza kuutekeleza kutoka mwezi Januari 2024, lakini tunatekeleza kwa awamu. Kwa hiyo, kwa awamu ya kwanza tunatekeleza kuanzia elimu ya awali, darasa la kwanza na darasa na la tatu. Vilevile kwa upande wa sekondari tumeanza kutekeleza mtaala mpya ambao unabeba masomo haya kwa kidato cha kwanza mwaka huu na kwa ule mkondo wa amali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vyuo vya ualimu vilevile umeanza mwaka huu. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mtaala huu tayari Serikali imeshaanza kuufanyia kazi na utekelezaji wake umeanza toka mwezi Januari, 2024. Ninakushukuru.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha kiuchumi vijana ambao wapo katika Jimbo la Kibiti, ambapo ukipita Jimbo la Kibiti, ukiangalia mazingira watu wengi wanaonekana hali zao ni za chini. Sasa tunataka kujua Serikali yetu hii sikivu inawainuaje kiuchumi na ina mpango gani wa kuwawezesha...

MWENYEKITI: Sawa, umeeleweka. Mheshimiwa Waziri, majibu.

MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, umenifahamu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala lake lina wigo mpana, lakini katika Sekta ya Kilimo, moja ya malengo ya Serikali tuliyonayo kwa Jimbo la Kibiti hususan lile Bonde zima; ni kwamba sasa hivi tumeshatangaza tender kwa ajili ya kwenda kujenga mabwawa mawili makubwa kule na mifumo ya umwagiliaji. Kwa hiyo tukishatengeneza ile miundombinu kwenye maeneo yale maana yake vijana wengi wa Jimbo la Kibiti watanufaika na ile miradi. Kwa hiyo, watakuwa na shughuli za kiuchumi za kufanya. Hiyo ni kwenye Sekta ya Kilimo. Kwa sekta nyingine Waheshimiwa Mawaziri wengine wamesikia na watalifanyia kazi jambo hilo. Ahsante. (Makofi)