Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Doto Mashaka Biteko (31 total)

MHE. SUSANNE P. MASELE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza kauli ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo kipaumbele cha leseni na vibali vya kuchimba madini kwa kuonesha mfano kwa wachimbaji wadogo wa machimbo ya Dhahabu ya Ishokelahela, Misungwi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Susanne Masele naomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama hapa, lakini vile vile nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa Imani kubwa aliyonipatia na akaona naweza kumsaidia kwenye Sekta hii ya Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Susanne Peter Masele Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachimbaji wa Madini wadogo wa Ishokelahela Wilayani Misungwi walivamia na kuanza shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la Leseni kubwa ya utafutaji wa madini inayomilikiwa na Kampuni ya Carlton KitongoTanzania Limited yenye ukubwa wa kilomita za mraba 12.4 tokea mwezi Julai, 2017. Kabla ya hapa wachimbaji hao walikuwepo lakini kwa kiasi kidogo. Mpaka kufikia sasa leseni hiyo imevamiwa na wachimbaji wadogo zaidi ya 1000 ambao wanachimba madini hayo ya dhahabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leseni ya Carlton KitongoTanzania Limited ilitolewa tarehe 5 Agosti, 2014 na itamaliza muda wake wa awali tarehe 4 Agosti 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi kwa kushirikiana na kampuni ya Carlton Kitongo Tanzania Limited ambaye ni mmiliki wa leseni hiyo waliamua kutenga eneo kwa ajili ya kuwaachia wachimbaji wadogo ambalo likuwa linamilikiwa na kampuni hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makubaliano hayo yalihitimishwa rasmi mwezi Desemba mwaka 2017 kati ya mmiliki wa leseni na vikundi ambayo viliungana kuunda kikundi kimoja kwa jina la Basimbi and Buhunda Mining Group. Nakala ya makubaliano hayo ipo Ofisi ya Madini Mwanza na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Misungwi. Vikundi hivyo vilipatikana baada ya Wizara kupitia Ofisi yetu ya Madini Mkoani Mwanza kutoa elimu ya umuhimu ya kujiunga katika vikundi na kuendesha shughuli za uchimbaji madini ili ziweze kuwa na tija zinazozingatia matakwa ya Sheria ya Madini na Kanuni zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza kauli ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuwapatia wachimbaji wadogo kipaumbele cha leseni na vibali vya kuchimba madini, leseni za wachimbaji madini katika eneo hilo zitatolewa kwa vikundi hivyo mara tu baada ya taratibu za kisheria za kushughulikia maombi hayo kukamilika.
MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:-
Mgodi a Tanzanite ulioko Mererani, Wilaya ya Semanjiro ni mgodi wenye idadi kubwa ya vijana wanaofanya kazi katika mgodi huo na kumekuwa na historia ya matukio ya maafa kila mwaka ya vifo vya watu wengi.
(a) Je, Serikali imefanya utafiti gani ili kubaini chanzo cha maafa hayo yanayolikumba Taifa kila mwaka na kusababisha kupoteza nguvu kazi ya Taifa letu?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha utaratibu maalum kwa wamiliki wa vitalu vya Tanzanite kuwalipa kifuta jasho wahanga wote wanaopatwa na maafa wanapokuwa kazini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Joram Gidarya, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mapitio ya taarifa za ajali yanaonesha kuwa ajali nyingi husababishwa na wachimbaji wadogo kutokuzingatia tahadhari ya usalama wanapotekeleza majukumu yao ya uchimbaji madini. Hivyo, Serikali imekuwa ikifanya juhudi za ukaguzi wa maeneo ya uchimbaji na kuwaelimisha wachimbaji kuchukua tahadhari za usalama wakati wa kufanya kazi pamoja na kuwahamasisha kuunda timu za wakaguzi katika maeneo yao kutoka miongoni mwa wachimbaji ambao hupewa elimu ya ukaguzi na wataalam wetu wa Wizara ya Madini. Hivyo, nawasihi wachimbaji wa madini kutambua umuhimu wa kuzingatia taratibu na usalama wa kazi kwa uchimbaji ili kulinda afya na uhai wao.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali imeanzisha Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi kupitia Sheria Namba 20 ya mwaka 2008 ya Fidia ya Wafanyakazi. Wizara itahamasisha wamiliki wa leseni na wachimbaji kujiunga na mfuko huu ili kupata kifuta jasho wanapopatwa na maafa wanapokuwa kazini.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Katika ukanda wa Bonde la Ziwa Rukwa katika Jimbo la Kwela, kwenye ukingo wa Milima ya Lyamba Iyamfipa inayoambaa katika Kata za Mfinga, Mwadui, Kalumbaleza, Nankanga, Kapeta hadi Kaoze, baadhi ya wananchi wamekuwa wakiokota madini mbalimbali bila kutambua ni madini ya aina gani.
(a) Je, Serikali imeshafanya utafiti wowote katika maeneo hayo?
(b) Kama jibu ni hapana, je, ni lini utafiti utafanyika ili kujua eneo hilo lina madini gani?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia miaka ya 1950 Serikali imekuwa ikifanya utafiti mbalimbali wa awali wa madini kwenye maeneo ya Ukanda wa Bonde wa Ziwa Rukwa yakiwemo maeneo ya Jimbo la Kwela kwenye mwambao wa milima ya Lyamba Iyamfipa. Utafiti wa awali ulibaini uwepo wa madini mbalimbali yakiwemo madini ya vito kama vile Garnet, Kyanite, Zircon na Sapphire na mengineyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa za uwepo wa madini katika Ukanda wa Bonde wa Ziwa Rukwa zinapatikana kwenye ofisi zetu za Wakala wa Jiolojia Tanzania. Hata hivyo nachukua nafasi hii kuwashauri sana ndugu zetu wote wakiwemo wa Jimbo la Kwela kutumia Ofisi zetu za Madini za Kanda ya Magharibi iliyoko Mpanda na taarifa zilizopo kwenye ofisi ya Wakala wa Jiolojia iliyoko Dodoma, ambapo wako wataalam watawasaidia kuyachambua madini hayo pamoja na kuwashauri namna ya kufaidika na rasilimali hiyo ya madini.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Mji wa Tunduru yako mabango mengi yanayoelezea ununuzi wa madini jambo linaloashiria upatikanaji mkubwa wa madini kutoka kwa Wachimbaji wadogo wadogo ambao hawatambuliwi kwa mujibu wa sheria:-
Je, ni lini Serikali itawatengea maeneo ya kuchimba madini na kuwatambua Kisheria Wachimbaji hao wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini na kabla sijajibu swali hili naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Profesa Idris Kikula kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume mpya ya Madini.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2017 inawatambua wachimbaji wadogo. Kwa kutumia sheria hiyo Serikali inatoa leseni za uchimbaji za madini (Primary Mining Licenses) kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kuna mabango na maduka mengi yanayotangaza uwepo wa madini ya vito katikati ya Mji wa Tunduru huko Mkoani Ruvuma. Baadhi ya madini ya vito hayo yaliyopo Wilaya ya Tunduru ni pamoja na Sapphire, Ruby, Garnet na kadhalika. Maduka ya madini yenye mabango ni ya wafanyabiashara wakubwa wenye leseni kubwa (Dealers License) ambazo huhuishwa kila mwaka kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2013 Serikali ilitenga eneo la Mbesa, Wilaya ya Tunduru, lenye ukubwa wa hekta 15,605.3 kwa tangazo la Serikali Namba tano la tarehe 22 Februari, 2013, kwa ajili ya uchimbaji mdogo wa madini ya shaba. Hadi Aprili, 2018 jumla ya leseni hai 649 za wachimbaji wadogo wa madini yaani (PML) zimetolewa Wilaya ya Tunduru.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo kadri taarifa za utafiti katika maeneo hayo zitakavyoandaliwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushirikiana na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ili wachimbaji wadogo hao waweze kuchimba madini siyo kwa kubahatisha.
Mheshimiwa Spika, aidha, wachimbaji wadogo wanahimizwa kuomba leseni ili wafanye shughuli za utafutaji wa madini kwa mujibu wa sheria za nchi ili kuinua vipato vyao kutoa ajira kwa Watanzania, kuchangia pato la Taifa kupitia tozo mbalimbali zinazotokana na shughuli za madini.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawapatia wachimbaji wadogo wadogo maeneo yaliyopimwa na kuwa na uwepo wa madini kama dhahabu, ikiwemo Moroko katika Mkoa wa Geita na maeneo mengine yenye madini nchini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 1996, Serikali kupitia Wizara ya Madini imekuwa ikitenga maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini. Tangu kipindi hicho hadi sasa, Wizara ya Madini imetenga jumla ya maeneo 46 katika sehemu mbalimbali nchini yenye ukubwa wa hekta 281,533.69. Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo kadiri yatakavyokuwa yanapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Geita Wizara imetenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini na kutoa leseni kama ifuatavyo: Eneo la Nyarugusu leseni 41; eneo la Rwamgasa leseni 36; eneo la Isamilo/ Lwenge leseni 22 na eneo la Mgusu leseni 22. Kwa sasa eneo la Moroko alilolitaja Mheshimiwa Mbunge lipo ndani ya leseni ya utafiti yenye Na.8278 ya mwaka 2012 inayomilikiwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita. Maeneo mengine ya mkoa huo yataendelea kutengwa kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 16 cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na Marekebisho yake ya mwaka 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara kwa kutumia taasisi zake za GST pamoja na STAMICO itaendelea kufanya utafiti ili kubaini uwezo wa mashapo ya madini katika maeneo mbalimbali nchini na kuyatenga kwa ajili ya uchimbaji mdogo wa madini. Hii itawezesha wachimbaji wadogo wa madini kufanya kazi na kuchimba kwa uchimbaji wa tija. Ahsante.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Je, ni lini mgodi utafunguliwa katika eneo la Nyakafuru Wilayani Mbogwe baada ya utafiti kuchukua muda mrefu kwenye eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Nyakafuru lenye leseni ya ukubwa wa kilomita za mraba 17.53 linamilikiwa na Kampuni ya Mabangu Limited Resources, kampuni ambayo Kampuni tanzu ya Resolute Tanzania Limited kupitia leseni ya kutafuta madini PL Na.5374 ya mwaka 2008. Leseni hiyo ambayo ilihuishwa mara mbili na baadaye kuongezewa muda wa kipindi cha miaka miwili yaani extension kuanzia tarehe 24 Oktoba, 2016 ili kukamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na itamaliza muda wake tarehe 23 Oktoba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 yaliyofanyika mwaka 2017 yaani The Written Laws Miscellaneous Amendment Act 2017 yaliondoa uhitaji wa leseni ya utafutaji wa madini kuongezewa muda wa kufanya utafiti baada ya muda wa leseni kuhuishwa kwa mara ya pili kumalizika. Kwa sasa sehemu ya eneo hilo la leseni hiyo imevamiwa na wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa mashapo yanayofikia takribani tani 3.36 yenye dhahabu ya wakia 203,000 yamegunduliwa na jumla ya Dola za Kimarekani milioni 1.83 zimetumika kufanya utafiti katika eneo la mradi. Aidha, Tathmini ya Athari ya Mazingira ilishafanyika na kupewa cheti cha tarehe 16/10/2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe, Kampuni ya Mabangu Mining Limited kupitia Kampuni mama ya Resolute (Tanzania) Limited inadaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kiasi cha jumla Sh.143,077,421,804 ikiwa ni deni la kodi ambalo wanatakiwa kulilipa. Mgodi wa Nyakafuru unaweza kuendelezwa baada ya deni hilo kuwa limelipwa.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Halmashauri ya Busokelo ina utajiri mkubwa wa madini na gesi asilia aina ya carbon dioxide:-
Je, ni lini Serikali itaenda kufanya utafiti wa kutosha kwenye Kata ya Lufilyo ambapo kuna madini aina ya marble (marumaru)?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Atupele Fredy Mwakibete, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa madini ya marble katika Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ambapo Kampuni ya Marmo Granito inamiliki leseni moja ya uchimbaji wa kati yenye Namba ML 250 ya mwaka 2006 na leseni 10 za uchimbaji mdogo wa madini hayo zenye namba PML 0007657 – 0007666 za mwaka 2008.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utambuzi huo ni kutokana na utafiti wa awali uliofanywa kati ya mwaka 2005 hadi 2007 na Kampuni ya BGR ya Ujerumani kwa ushirikiano wa taasisi za Serikali (STAMICO na GST). Utafiti huo ulipelekea kugunduliwa kwa madini hayo yenye rangi ya kijani na nyeupe katika Kijiji cha Kipangamansi kilichopo katika Kata ya Lufilyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2018/ 2019, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) itaendelea kufanya utafiti wa awali wa kijiolojia ili kubaini maeneo mengine yenye madini hayo katika Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo. Vilevile utafiti wa kina utafanyika ili kubaini ubora na wingi wa upatikanaji wa madini hayo na kuishauri Serikali. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Je, kwa sasa Tanzania ina aina ngapi za madini?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Tanzania ina aina mbalimbali za madini ambayo kijiosayansi yamegawanyika katika makundi matano ambayo ni; madini ya metali kama vile dhahabu, madini ya fedha, chuma, shaba, risasi, aluminum, nickel, niobium, bati na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, yako pia aina nyingine ya madini, ambayo ni madini ya vito (gemstones) ambayo ni pamoja na madini ya Tanzanite, almasi, rubi pamoja na mengineyo

Mheshimiwa Spika, kundi la tatu ni la madini ya viwandani, ambayo yanaintwa industrial minerals kama vile kaolin, mawe ya chokaa, jasi, phosphate pamoja na chumvi na na mchanga wa ufukweni.

Mheshimiwa Spika, madini ya ujenzi ni kundi lingine la madini ambayo ni madini ya nakshi kama vile mawe, kokoto, udongo wa mfinyanzi, mchanga na mawe ya nakshi. Aidha, yapo pia madini ya nishati kama vile makaa ya mawe, gesi na uranium.

Mheshimiwa Spika, madini haya ni muhimu katika kujenga uchumi wa viwanda na kuongeza mchango wa uchumi kwa madini katika Pato la Taifa. Madini haya ni muhimu katika maendeleo ya wananchi kwa kuwa yanatumika katika shughuli mbalimbali za ujenzi, viwanda, mapambo na kuleta fedha za kigeni nchini.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-

Madini ya Tanzanite yanapatikana nchini Tanzania pekee, juhudi za kufanya madini haya kuchimbwa na Watanzania pekee kwa Kanuni za Madini za mwaka 2004 na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 hazijaweza kuzaa matunda:-

(a) Je, kwa nini Tanzania isiyatangaze madini ya Tanzanite kuwa ni Nyara za Taifa itayovunwa na Serikali pekee ili kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa Taifa letu?

(b) Je, kwa nini Serikali isiende kujifunza nchini Zimbabwe kuona jinsi ilivyofanikiwa kuyafanya madini ya Almasi kuwa Nyara ya Serikali na hivyo kuleta manufaa makubwa sana kwa nchi hiyo?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatambua upekee na umuhimu wa madini ya Tanzanite. Kwa muktadha huo, ilipelekea tarehe 20/9/2017 kuliamuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania kujenga ukuta wenye urefu wa kilometa 24.5 kuzunguka eneo hilo. Lengo likiwa ni kudhibiti utoroshwaji wa madini ili kupata manufaa stahiki ya kiuchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, eneo la Mirerani ambako Tanzanite inapatikana lilitangazwa kuwa eneo lililodhibitiwa (Mirerani Controlled Area) kwa GN 450 ya mwaka 2002. Lengo la hatua hiyo ni pamoja na kuthamini upekee na umuhimu wa madini hayo na kudhibiti upotevu wa mapato yanayotokana wa Madini ya Tanzanite ili kuongeza manufaa kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Madini ya Tanzanite yanachimbwa na Watanzania katika Vitalu A, B, C na D-extension. Aidha, kitalu C kimekuwa kikichimbwa kwa ubia kati ya Shirika la STAMICO na Kampuni ya kigeni ya TanzaniteOne Mining Limited (TML). Hata hivyo, tarehe 23 Desemba 2019, STAMICO na TML waliachia eneo hilo na kupewa surrender certificate ya leseni yao na sasa eneo hilo limerudishwa kwenye usimamizi wa Serikali. Baada ya kuachiwa kwa eneo hilo, utaratibu maalum unaandaliwa wa namna bora ya kuligawa kwa kutoa leseni za uchimbaji wa kati kwa Watanzania wenye uwezo wa kulichimba na kuongeza mchango katika uchumi wa madini.

Mheshimiwa Spika, ushauri wa kuyafanya madini ya Tanzanite kuwa Nyara za Taifa na kwenda kujifunza katika nchi kama Zimbabwe, ushauri huo tunaupokea.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-

Katika Kata ya Mbomole maeneo ya Sakale Wilayani Muheza kuna madini ya dhahabu ambayo wananchi wamekuwa wakichimba bila vibali na hivyo kukamatwa kwa kuharibu chanzo cha maji cha Mto Zigi:-

(a) Je, ni lini Serikali itatuma watalaam ili kuweza kujua eneo hilo lina madini gani?

(b) Je, Serikali ipo tayari kuweka utaratibu mzuri ambao utahakikisha kuwa wachimbaji hao wanachimba eneo ambalo hawatasumbuliwa?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tarehe 02/10/2018, Timu ya Wataalamu wa Madini, Mazingira na Maji kutoka Ofisi ya Tume ya Madini Tanga, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC) walitembelea na kukagua eneo la Sakale ili kuangalia athari za uchimbaji uliokuwa unafanywa na wachimbaji wadogo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, baada ukaguzi wa timu hiyo, timu ya wataalam ilibaini uharibifu mkubwa wa mazingira uliofanywa katika vyanzo vya maji na Msitu wa Amani na hivyo shughuli za uchimbaji madini zilisitishwa katika eneo hilo ili kunusuru mazingira, vyanzo vya Maji na Msitu wa Amani katika Kata ya Mbomole.

Mheshimiwa Spika, tafiti mbalimbali za awali zilizofanywa na Taasisi ya Jiolojia Tanzania (GST) ilibaini uwepo wa madini ya dhahabu katika Vijiji vya Mindu, Tengeni, Segoma na Mbambara Muheza na Korogwe.

Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa wachimbaji wadogo wa Kata ya Mbomole eneo la Sakale kuangalia maeneo mengine nje ya Bonde la Mto Zigi ili kufanya shughuli za uchimbaji.
MHE. AGNESS M. MARWA aliuliza:-

Wananchi wengi walibomolewa nyumba zao na Mgodi wa ACACIA uliopo Nyamongo, Wilayani Tarime na wengine hawajalipwa fidia ya maeneo yao mpaka sasa. Aidha, mgodi pia umeanza kuchimba chini ya maeneo ya watu (Underground mining):-

Je, ni lini mgodi wa ACACIA uliopo Nyamongo utalipa fidia kwa wananchi hawa?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agness Mathew Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia sekta ya madini kwa kuhakikisha uwekezaji unafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi ikiwemo kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo miradi ya uendelezaji migodi inataka kufanyika na kulazimika kupisha maeneo yao wanalipwa fidia stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi na wanapewa makazi mbadala ambayo yana hali bora zaidi kuliko makazi waliyokuwa nayo awali.

Mheshimiwa Spika, uthaminishaji katika maeneo yanayozunguka mgodi wa North Mara na ulipaji wa fidia umegawanyika katika awamu nyingi kwa kuzingatia vijiji husika kuridhia. Kijiji cha Nyabirama chenye wakazi 1,974 waliothaminiwa katika awamu ya 20, 35 na 42 wote walilipwa fedha zao isipokuwa wakazi 64 ambao fedha yao iliyoidhinishwa ya shilingi bilioni 1.9 waliikataa hundi zao zikabaki Ofisi ya Mkurugenzi Wilaya ya Tarime. Eneo la Nyabichune lilithaminiwa katika awamu ya 47 kwa kuidhinisha shilingi milioni 224 kwa ajili ya watu 69. Wizara iliagiza uthamini wa maeneo hayo ya Kijiji hicho cha Nyabichune urudiwe kwa sababu wananchi wale walionekana wamepunjwa. Mthamini Mkuu wa Serikali ameshakamilisha uthaminishaji wa maeneo 1,838 ambayo tayari umeshawasilishwa kwenye menejimenti ya mgodi kwa hatua zake za ulipaji.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la mgodi kubadilisha aina ya uchimbaji toka uchimbaji wa wazi (open pit) kwenda underground mining, uamuzi huo ulifikiwa baada ya mgodi huo kufanya utafiti ulioonesha kuwa gharama ya uchimbaji wa chini zilikuwa ndogo ukilinganisha na uchimbaji wa mgodi wa wazi. Naomba niwatoe shaka wana Tarime kuwa Wizara inafuatilia kwa karibu uchimbaji unaofanyika na mpaka sasa uchimbaji wa underground unafanyika katika eneo la Gokona kuelekea Nyabigena ndani ya maeneo waliyokuwa wakichimba toka awali. Hivyo, hakuna eneo ambalo mgodi wa underground unachimba kwenye makazi ya watu.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA aliuliza:-

Katika Kijiji cha Sakale, Kitongoji cha Kwempasi, Tarafa ya Amani katika Wilaya ya Muheza wananchi waligundua uwepo wa madini na shughuli za uchimbaji zilianza, lakini baada ya muda Serikali imefunga machimbo yale:-

Je, ni lini Serikali itaandaa utaratibu wa kufungua machimbo hayo ili wachimbaji wadogo hususan vijana wazawa waweze kunufaika.
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yosepher Ferdinard Komba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) ikishirikiana na wadau wa maendeleo ilifanya utafiti na ulibaini uwepo wa madini ya dhahabu katika Vijiji vya Mindu, Amani, Tengeni, Segoma, Mbambara, Sakale, Muheza na Korogwe. Pia Wilaya ya Muheza ina madini ya ujenzi kama vile mchanga na mawe katika Vijiji vya Magila, Kilapula, Kwakifua, Mhamba, Furaha na Tanganyika na madini ya garnet, ruby na sapphire katika Kijiji cha Misozwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli machimbo yaliyokuwa yakiendelea katika Kijiji cha Sakale yalifungwa tarehe 2 Oktoba, 2018 baada ya timu ya watalaam kubaini uchimbaji huo kutokuzingatia Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya mwaka 2017. Aidha, Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 na kanuni zake haziruhusu kufanya uchimbaji katika vyanzo vya maji ili kuzuia kemikali ya zebaki na uchafu utokanao na uchenjuaji kuingia kwenye mito ambayo inamwaga maji kwenye Bwawa la Bayani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchimbaji huo ulikuwa unafanyika katika vilima vya Kwempasi na Nelusanga ambapo uchimbaji unaweza kutiritirisha majitaka na udongo kutoka juu ya vilima na kuingia katika bonde la Mto Kihara ambao ni moja ya chanzo cha Bwawa la Bayani linalotumiwa na wakazi zaidi ya laki 500 katika Wilaya ya Korongwe, Muheza na Jiji la Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, timu ya watalaam ilishauri mwekezaji mzawa au mgeni anaweza kuruhusiwa kuchimba madini hayo kwa kutumia leseni ya uchimbaji mkubwa na kuweza kufanya tathimini ya kimazingira (EIA) na kuwashirikisha wadau wote muhimu kabla ya kuanza uchimbaji ili kuzuia uharibifu huo wa mazingira.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa utekelezaji mipango yake pamoja na maelekezo ya Mhe. Rais ya kushughulikia kero za wachimbaji wadogo hususani katika maeneo ya uchimbaji ya Ng’apa Mtoni na Muhuwesi?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Napenda kujibu swali la Mheshimwa Engineer Ramo Matala Makani (Mbunge wa Tunduru Kaskazini) kama ifuatavyo;-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 inatambua umuhimu wa wachimbaji wadogo. Wizara kupitia Tume ya Madini inatoa leseni za uchimbaji mdogo ambazo ni maalum kwa watanzania pekee. Aidha, Juhudi hizo ni pamoja na kuwapatia na kuwatengea maeneo mbalimbali ya kuchimba na kuanzisha masoko ya madini katika mji wa Tunduru ambapo Soko la Madini lilifunguliwa tarehe 27 Mei, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuwasaidia wachimbaji wadogo Mkoa wa Ruvuma na Wilaya ya Tunduru mwaka 2012/2013 Serikali ilitenga eneo la Mbesa lenye ukubwa wa hekta 15,605.30 kwa GN Na. 25 la tarehe 22 Februari, 2013 kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya shaba na jumla ya leseni ndogo 441 zilitolewa kwa wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya leseni kubwa za utafiti ambazo zilikuwa hazifanyiwi kazi kufutwa, Wizara ya madini kupitia Tume ya Madini imetenga eneo la Ng’apa Mtoni kwa ajili ya shughuli za wachimbaji wadogo wa madini ya vito lenye ukubwa wa hekta 7,548.59.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika eneo la mto Muhuwesi uchimbaji unafanyika kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Madini za Mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 na Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004. Aidha, kila mmiliki wa leseni ya uchimbaji ndani ya Mto Muhuwesi anatakiwa kupata vibali kutoka mamlaka husika (NEMC na Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini) kabla ya kuanza kufanya shughuli za uchimbaji madini ndani ya Mto.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-

Je, ni kwa nini mgodi wa GGM umegoma kulipa deni la Halmashauri ya Geita la Dola za Kimarekani 800,000?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Geita pamoja na Wilaya ya Geita, kwa pamoja zilikuwa zikidai kiasi cha dola za Kimarekani 800,000, kwa mujibu wa Mkataba wa Maendeleo ya Uwekezaji wa Madini yaani MDA ulioingiwa na Serikali pamoja na Kampuni ya Mgodi ya GGM mwaka 1999. Deni hilo lilitokana na kutokulipwa kwa ushuru wa huduma kiasi cha dola za Kimarekani 200,000 kila mwaka kwa malimbikizo ya miaka minne kuanzia mwaka 2000 - 2003.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Madini, ilielekeza Mgodi wa Dhahabu wa Geita kulipa deni hilo kwa Halmashauri ya Mji wa Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili fedha hizo ziweze kuboresha huduma za jamii na za kiuchumi katika Halmashauri hizo. Aidha, tarehe 26 Oktoba, 2018, Mgodi wa Geita Gold Mining ulilipa deni lote lililokuwa likidaiwa kiasi cha Sh.1,814,249,519.99.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchanganuo wa malipo hayo ya ushuru wa huduma yaani service levy ni kiasi cha Sh.1,296,462,706.99 zililipwa kwa Halmashauri ya Mji wa Geita na kiasi cha Sh.517,786,813 zililipwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA aliuliza:-

Kumekuwa na dalili za upatikanaji wa madini ya dhahabu katika Vijiji vya Kabingo, Ruhuru, Nyakayenzi, Nyamwilonge na Muhange Wilayani Kakonko na katika baadhi ya vijiji uchimbaji umeanza:-

Je, Serikali inatoa ushauri gani kwa vijana ambao wapo tayari kujishughulisha na uchimbaji wa madini?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Christopher Kajoro Chiza, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na dalili za upatikanaji wa madini ya dhahabu katika Vijiji vya Kabingo, Ruhuru, Nyakayenzi, Nyamwilonge na Muhange, Wilayani Kakonko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa katika Kijiji cha Nyamwilonge uchimbaji unaendelea na Serikali imekwishakutoa leseni saba kupitia Tume ya Madini, leseni za uchimbaji mdogo (primary mining licence) kwa madini ya dhahabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo mwezi Mei, 2017, Wizara ya Madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ilifanya utafiti wa awali ambao uliombwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kubaini maeneo yenye madini ya dhahabu. Katika ripoti yake ilibainika uwepo wa dhahabu katika Vijiji vya Nyakayenzi, Nyakahura na Nyamwilongo. Pia ripoti hiyo ilishauri utafiti wa kina ufanyike ili kujua kiwango cha wingi na upatikanaji wa dhahabu katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Madini inashauri vijana wote wanaotaka kujishughulisha na shughuli za uchimbaji madini kwenye maeneo hayo, wafike kwenye Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Kigoma ili waweze kupewa ushauri wa kitaalam pamoja na kuelimishwa kuhusu utaratibu wa kufuatwa kupata leseni ya uchimbaji madini ili waweze kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-

Kwa kuwa Serikali imekuwa ikiwarasimisha wachimbaji wadogo wa madini:-

(a) Je, ni lini Serikali itawarasimisha Wachimbaji wadogo katika vijiji vya Busulwangili, Lwabakanga, Kakola namba Tisa na Wisolele katika Jimbo la Msalala?

(b) Je, ni sawa kwa mwenye leseni au msimamizi wa eneo la wachimbaji wadogo kupatiwa asilimia 30 ya mawe yanayochimbwa katika eneo lake?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 1996, Serikali kupitia Wizara ya Madini imekuwa ikitenga maeneo maalum kwa ajili ya kurasimisha wachimbaji wadogo wa madini nchini. Hadi sasa, Serikali imetenga jumla ya maeneo 46 katika sehemu mbalimbali nchini yenye ukubwa wa hekta 281,533.69. Aidha, Serikali itaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo kadri yatakavyokuwa yanapatikana.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kahama Serikali imeunda Kamati Maalum ya Utengaji wa Maeneo kwa mujibu wa Kifungu cha 15 na 16 cha Sheria ya Madini, Sura 123. Kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuandaa utaratibu wa kugawa maeneo yote tengefu yakiwemo maeneo ya Kinamiyuba-Ilindi-Mwime, Buzwagi-Bumbiti na Nyangalata. Mpaka sasa jumla ya maombi 89 ya uchimbaji mdogo yamepokelewa na mchakato wa kugawa leseni hizo unaendelea. Aidha, Serikali kupitia Tume ya Madini imeifuta leseni ya utafutaji wa madini PL 8125/2012 iliyokuwa inamilikiwa na Kampuni ya Liontown Tanzania Limited iliyoko Kata ya Segese Halmashauri ya Msalala na eneo hilo linatarajiwa kutengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa maeneo ya Lwabakanga na Kakola namba Tisa aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge, yapo ndani ya leseni ya uchimbaji mkubwa SML 44/99 inayomilikiwa na mgodi wa Bulyanhulu Gold Mine Limited. Hivyo, eneo hilo haliwezi kutengwa kwa ajili ya shughuli za uchimbaji mdogo. Aidha, eneo la Busulwangili lipo ndani ya leseni ya utafutaji wa madini PL 10782/2016 inayomilikiwa na Kampuni ya Hai Nan Geology (Tanzania) Company Limited. Hivyo, Serikali ipo katika hatua za awali za kufuta eneo hilo na kulitenga kwa ajili ya wachimbaji wadogo baada ya mmiliki wake kushindwa kufanya kazi ya utafiti.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Madini ilitoa waraka wa ndani Na.3 ulioanza kutumika tarehe 15 Oktoba, 2019, wenye dhumuni la kutoa mwongozo kwa Maafisa Madini Wakazi na watumishi wengine katika kusimamia, kudhibiti shughuli za madini na mapato ya Serikali katika maeneo yenye rush. Waraka huo unawataka wasimamizi kuzingatia ukusanyaji wa kodi za Serikali Kuu na Halmashauri na kuweka mgawanyo wa mapato baina ya mmiliki wa duara (mchimbaji), mmiliki wa shamba na msimamizi. Aidha, kwa Mujibu wa Waraka huo mgawanyo utazingatia kodi za Serikali Kuu na Halmashauri kwanza ambazo ni mrabaha 6%, ada ya ukaguzi 1% na kodi ya huduma 0.3%. Baada ya kutolewa kodi hizo, mmiliki wa ardhi atapata 15%, mmiliki wa shamba 15% na mmiliki wa duara (mchimbaji) 70%.
MHE. SALOME W. MAKAMBA aliuliza:-

Je, ni sifa zipi ambazo mzabuni anatakiwa kuwa nazo ili kupewa nafasi ya usimamizi mapato ya Serikali kwenye migodi midogo midogo (rush) kama Mwabomba, Namba Mbili, Segese na kadhalika?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salome Wycliffe Makamba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Wizara katika kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kufungua masoko ya madini nchi nzima, kumesababisha ongezeko la wachimbaji wadogo ambao wamekuwa wakivamia maeneo mbalimbali (rush) kama vile kwenye maeneo yaliyotengwa, maeneo yenye leseni kubwa za utafiti, maeneo ya uchimbaji mkubwa, maeneo yasiokuwa na leseni na maeneo ambayo leseni zake hazijaendelezwa kwa shughuli za uchimbaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Madini ilitoa Waraka wa Ndani Na. 3 ulioanza kutumika tarehe 15 Oktoba, 2019 wenye dhumuni la kutoa mwongozo kwa Maafisa Madini Wakazi na watumishi wengine katika kusimamia, kudhibiti shughuli za madini na mapato ya Serikali katika maeneo yenye rush. Kwa mujibu wa Waraka huo, utaratibu unaotumika kuwapata wasimamizi wa rush kama alivyouliza Mheshimiwa Mbunge, ni kupitia Kamati ya Uongozi inayofuatilia na kuimarisha usimamizi katika eneo la rush.

Mheshimiwa Spika, Kamati hiyo huteua wasimamizi wa rush ambapo Mwenyekiti wa rush anapaswa kuwa na sifa zifuatazo: Awe mchimbaji mzoefu hasa katika usimamizi wa maeneo ya aina hiyo; asiwe na historia ya wizi wa fedha za Serikali; na awe mwaminifu. Aidha, wajumbe wengine kwenye usimamizi wa rush ni pamoja na Katibu, Mweka Hazina, Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kitongoji, Mjumbe wa REMA, TAWOMA na mwakilishi wa eneo/shamba.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA Aliuliza: -

Je, ni lini mgodi wa makaa ya mawe Kiwira utapata Mwekezaji mpya na kulipa mafao ya waliokuwa wafanyakazi wa mgodi huo?
WAZIRI WA MADINI Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Shirika limeamua kuchukua hatua za ndani za kuendesha mgodi wa Kiwira kwa kuchukua hatua mahsusi za kuendeleza mradi wa Kiwira kwa ajili ya uwekezaji mkubwa wa kuzalisha umeme wa MW 200 badala ya kutafuta mwekezaji mpya. Hatua hizo ni pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu ya mgodi, kuboresha barabara, kurejesha njia za reli katika mgodi wa chini (underground mine), mifumo ya hewa, maji na matengenezo ya mikanda ya kusafirishia makaa kuja nje ya mgodi.

Mheshimiwa Spika, hatua hii ni kuwezesha kuchimba makaa ya mawe kwa wingi kwa ajili ya kuzalisha umeme na matumizi mengine. Ukarabati wa miundombinu ya mgodi huu umefikia asilimia 98. Aidha, hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali ni kuanzisha ushirikiano kati ya STAMICO na TANESCO. Katika ushirikiano huo, STAMICO itahusika na uzalishaji wa makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi kwenye kinu cha umeme (power plant) na TANESCO itahusika na ujenzi wa kinu cha kuzalisha umeme pamoja na miundombinu yake. Kadhalika, TANESCO watahusika na uzalishaji na usambazaji wa umeme kwa wananchi kwa kujenga njia ya umeme yenye urefu wa km 100 kutoka kwenye mgodi huo.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa mgodi unaendelea na uchimbaji wa makaa ya mawe kwa matumizi ya viwanda katika eneo la Kabulo. Makaa hayo yanauzwa kwenye viwanda mbalimbali vya saruji nchini.

Mheshimiwa Spika, kuhusu malipo ya mafao ya waliokuwa wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira, Wizara ya Fedha na Mipango inayafanyia kazi kufuatia kukamilika kwa uhakiki wa madai hayo ambayo yanahusisha stahiki na mapunjo ya watumishi waliokuwa wafanyakazi wa Mgodi wa Kiwira baada ya Mgodi huo kusimamisha uzalishaji wake mwaka 2007. Aidha, katika kipindi hicho mgodi ulikuwa unaendeshwa na kampuni binafsi ya TANPOWER na mwaka 2013 mgodi huo ulikabidhiwa Serikalini kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
MHE. NUSRAT S. HANJE K.n.y. MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuiwezesha GST kufanya utafiti wa madini yanayohitajika kwenye soko la dunia kutengeneza nishati safi?
WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa ni asilimia 16 tu ya nchi yetu ndiyo imefanyiwa utafiti wa kina kubaini aina na kiasi cha madini mbalimbali yanayopatikana kwa kutumia teknolojia ya urushwaji wa ndege (High Resolution Airborne Geophysical Survey). Teknolojia hiyo hutoa picha ya chini ya ardhi inayoonesha mikondo na miamba inayobeba madini ya aina mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wizara ya Madini imekwisha andaa mpango mkakati wa utafiti utakaowezesha kutafiti asilimia 50 ya nchi yetu ili kupata na taarifa za kina ikiwemo za madini ya nishati safi. Mpango huo umekwisha kuainishwa na maeneo ya kipaumbele kulingana na aina ya madini yanayohitajika zaidi nchini kwa sasa. Ili kufanikisha azma hiyo, Wizara inajadiliana na sekta binafsi zinazoonesha nia ya kushirikiana na GST ili kuwezesha utafiti wa kina wa madini mkakati wa teknolojia ya utafutaji, uvunaji na uongezaji thamani madini ya mkakati kwa kuwa ni gharama kubwa sana.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti katika maeneo yanayoonekana kuwa na madini ili wananchi wanufaike?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI K.n.y. WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini nijibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) inaandaa mpango wa kufanya utafiti kwenye maeneo yanayoonekana kuwa na viashiria vya madini ikiwemo madini ya kimkakati. GST imepewa mamlaka ya kisheria kufanya utafiti wa madini nchini kwa lengo la kupata taarifa za kina za uwepo wa madini katika maeneo husika. Wizara ya Madini imeshaielekeza GST kuandaa mpango wa utafiti wa madini wa nchi kwenye maeneo ya kipaumbele ili kuombea bajeti ya kufanya kazi hiyo. Nashukuru.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: -

Je, lini Wananchi wa Komarera, Nyamichele na Murwambe katika maeneo ya Mgodi wa Barrick North Mara watalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI K.n.y. WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara Mbunge wa Tarime Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Barrick North Mara ulionesha nia ya kutaka kuchukua baadhi ya maeneo ya Vijiji vya Komarera, Nyamichele na Murwambe ambavyo ni sehemu ya vijiji vinavyozunguka mgodi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baada ya wananchi wa vijiji hivyo kupata taarifa ya maeneo yao kuhitajiwa na mgodi wa Barrick North Mara, walianza kuongeza majengo haraka haraka maarufu kama Tegesha. Hali hiyo ilipelekea mgodi huo kuachana na maeneo hayo kwani hayaathiri uendeshaji wa shughuli zao za kila siku, ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je ni lini Serikali itafungua Ofisi ya Madini Liwale?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI K.n.y. WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishwaji wa ofisi ya madini unazingatia vigezo mbalimbali ikiwemo uwepo wa shughuli kubwa za madini katika eneo husika. Kigezo hiki kinalenga katika kuhakikisha kunakuwa na usimamizi na udhibiti madhubuti wa rasilimali madini inayoanzishwa katika eneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Lindi, pamoja na kuwa na Ofisi ya Madini ya Mkoa iliyopo Nachingwea pia Wizara imefungua ofisi ndogo iliyopo Lindi Mjini ili kurahisisha uratibu wa shughulil za madini katika maeneo mengine katika mkoa huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za uchimbaji katika Wilaya ya Liwale zipo chini ukilinganisha na Wilaya za Ruangwa, Kilwa na Nachingwea. Kwa sasa wachimbaji wa madini katika Wilaya ya Liwale wanashauriwa kutumia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi ya Nachingwea pamoja na ofisi ndogo ya madini iliyopo Lindi Mjini. Hata hivyo, Wizara itaendelea kuboresha huduma kwa wadau wake kwa kadiri itakavyopata fedha za kutekeleza jukumu hilo.
MHE. KABULA E. SHITOBELA aliuliza:-

Je, Serikali haina njia mbadala ya matumizi ya matimba kama ngazi ambayo yanamaliza miti na hivyo kuharibu mazingira?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabula Enock Shitobela, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa magogo ya miti ni moja ya teknolojia rahisi na muhimu katika ujenzi wa migodi ya chini ya ardhi kwenye shughuli za uchimbaji mdogo wa madini nchini, ambapo miti hiyo hutumika katika ujenzi wa kuta na dari za migodi ili kuweka mazingira salama ya migodi midogo kwa wachimbaji. Wachimbaji wadogo hununua miti hiyo kutoka kwenye hifadhi za misitu na mashamba ya miti kupitia mawakala wa miti kwa kufuata taratibu za uvunaji wa miti. Teknolojia ya matumizi ya magogo ya miti imeenea zaidi kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa inasaidia kuimarisha usalama wa migodi na haihitaji uwekezaji mkubwa wakati wa ujenzi wa migodi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zipo teknolojia nyingine zinazotumika kwenye ujenzi wa migodi ya chini ya ardhi ambazo hutumia zege na vyuma ili kuimarisha kuta na dari za migodi hiyo. Teknolojia ya zege na vyuma hutumiwa zaidi na Wachimbaji wa Kati na Wakubwa kwa sababu ni ghali ukilinganisha na wachimbaji wadogo.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia mikopo katika Wilaya ya Mbogwe?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo mwanzo Serikali ilikuwa na utaratibu wa kuwapatia mikopo wachimbaji wadogo kwa lengo la kuwaongezea mitaji ili kuwafanya wafanye shughuli zao kwa tija. Baadaye tathmini ilifanyika na ilionesha upotevu wa fedha hizo. Kufuatia tathmini hiyo, Serikali inaendelea kuangalia namna bora ya kuwapatia mikopo wachimbaji wadogo nchini wakiwemo wa Wilaya ya Mbogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hatua hiyo, Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeingia makubaliano (MoU) na Benki za CRDB, NMB na KCB kwa ajili ya kuwapatia mikopo wachimbaji wadogo.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: -

Je, lini Kata za Tchenzema, Lingali, Kikeo na Lwale katika Tarafa ya Mgeta - Morogoro zitapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI alijibu:

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza mradi wa kupeleka umeme vijijini katika Mkoa wa Morogoro hususan Tarafa ya Mgeta ambapo mradi unahusisha kusambaza umeme katika Kata za Tahenzewa, Langala, Kikea na Kwale. Mkandarasi anayetekeleza mradi huo katika Tarafa ya Mgeta amekamilisha kazi ya mradi katika Kata ya Tahenzewa katika vijiji vya Tahenzewa na Kibuko na Kata ya Langala, Kijiji cha Pinde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Mkandarasi anaendelea na kazi katika Kata ya Tahenzewa, vijiji vya Bumu, Lusungi, Mwarazi na Kata ya Kikea, vijiji vya Lukunguni, Kododo, Chohelo, Mhale, Kikeo na Ng’owo. Utekelezaji wa mradi katika Tarafa ya Mgeta unatarajia kukamilika mwezi Juni, 2024.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme kwa wananchi wanaoishi kwenye mitaa 17 ya Mamlaka ya Mji Mdogo Rulenge – Ngara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza miradi mbalimbali ya kupeleka umeme kwenye vijiji na vitongoji ambapo kupitia mradi wa REA awamu ya Tatu mzunguko wa pili, vijiji 32 vya Wilaya ya Ngara vitapata umeme. Aidha, Wakala wa Nishati Vijijini yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za ununuzi wa kuwapata wakandarasi wa kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji (Hamlet Electrification Project - HEP), ambapo vitongoji 15 katika Jimbo la Ngara vitapatiwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mitaa 17 katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Rulenge, Serikali kupitia TANESCO na REA itatenga bajeti katika mwaka ujao wa fedha ili kuwapatia umeme wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza: -

Je, lini ujenzi wa Kituo cha Umeme (substation) utaanza Kyela?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikari kupitia TANESCO inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuimarisha na kuboresha upatikanaji wa umeme kwenye gridi ya Taifa (Gridi Imara). Maandalizi yanaendelea ikiwemo upembuzi yakinifu na tathmini ya athari ya mazingira kwa ajili ya kupata gharama halisi ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Wilayani Kyela. Kazi hizi za maandalizi zinatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2024/2025 na utekelezaji wa mradi huo utaanza mara baada ya kupatikana kwa fedha.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI K.n.y. MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

Je, lini Serikali itafunga laini ya pili ya umeme kutoka Geita hadi Sengerema ili kutatua tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao, Mbunge wa Sengerema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo awali Wilaya ya Sengerema ilikuwa ikipata umeme kutokea Mwanza Mjini kupitia njia ya umeme iliyokuwa inapita chini ya Ziwa Victoria. Aidha, wakati wa ujenzi wa Daraja la Kigongo Busisi, kwa bahati mbaya mkandarasi alikata submarine cable na tangu wakati huo Sengerema ikawa inapata umeme kutoka kituo kipya cha kupoza umeme cha Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANESCO imekubaliana na Mkandarasi kuweka sehemu ya kupitisha waya pembeni mwa Daraja la Kigongo – Busisi ambapo waya huo utapitishwa badala ya kupita kwenye maji. Aidha, kazi hiyo itafanyika baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja na kuwezesha Wilaya ya Sengerema kuendelea kupata umeme kutokea Mwanza Mjini kama ilivyokuwa awali.
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza: -

Je, lini Halmashauri ya Morogoro Vijijini na Rufiji zitalipwa fedha za CSR kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Edward Kalogeris, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu kidogo cha 2.1.1 cha Mkataba wa Utekelezaji wa Miradi ya Kijamii uliosainiwa tarehe 12 Desemba, 2018 kati ya TANESCO na Mkandarasi, unaainisha kwamba, hakutakuwepo na malipo ya fedha taslimu yatakayofanyika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kijamii bali Mkandarasi atakabidhi miradi akikamilisha utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Mkandarasi imepanga kujenga Hospitali mbili za hadhi ya Wilaya katika Kata ya Kisaki, Wilaya ya Morogoro Vijijini na Kata ya Nyamwage, Wilaya ya Rufiji zenye gharama ya shilingi bilioni kumi kila moja. Kwa sasa Serikali imekamilisha maandalizi ya nyaraka za msingi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hizo. Aidha, majadiliano kati ya TANESCO na Mkandarasi yanaendelea kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha miradi ya Umeme katika Vitongoji na Vijiji ambavyo havijafikiwa na miradi hiyo Wilayani Karatu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Karatu ina jumla vijiji 57 ambapo vijiji vyote vimeshapatiwa umeme. Aidha, Jimbo hilo lina vitongoji 265 na kati ya hivyo, 125 vina umeme na 140 havina umeme. Kazi ya kusambaza umeme katika vitongoji ambavyo havina umeme inaendelea ambapo Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 10 kupitia mradi wa ujazilizi 2B na vitongoji 15 kupitia Mradi wa Vitongoji 15 kwa kila Jimbo katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, hivyo, vitongoji 115 ndivyo vilivyosalia ambapo kazi ya kuvipelekea umeme itaendelea kuratibiwa na Wakala Nishati Vijijini kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. TUNZA I. MALAPO K.n.y. MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:-

Je, ni lini vijiji vyote vya Mkoa wa Singida vitaunganishiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida una jumla ya vijiji 441 ambapo kati ya hivyo, vijiji 439 vimekwishapatiwa umeme na vijiji viwili bado havijapatiwa umeme. Kazi ya kukipatia umeme Kijiji cha Ndwamuganga inaendelea ambapo ujenzi wa miundombinu umeshakamilika. Hatua inayofuata ni TANESCO kufanya ukaguzi, ili kujiridhisha na kazi kabla ya kuwasha umeme katika kijiji hicho. Aidha, kwa Kijiji cha Mkenene, kulikuwa na changamoto ya kukifikia kutokana na kufurika kwa Mto Iyumbu. Kwa sasa, hali imetulia na mkandarasi ameshaanza hatua za awali za kupeleka nguzo, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kupeleka umeme katika kijiji hicho. (Makofi)