Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Margaret Simwanza Sitta (76 total)

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda kumwuliza maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Tabora kwa muda mrefu umekuwa ukililia barabara hizi za lami; na tunaishukuru Serikali ya Mapinduzi imewezesha kwa kiwango ilichoweza. Sasa alipojibu Mheshimiwa Waziri kwamba tunategemea barabara ikamilike mwezi Juni. Je, haoni kuna umuhimu wa kutaja hapa ni lini fedha zinakwenda? Kwa sababu wakandarasi wapo, hawafanyi kazi kwa sababu hakuna fedha.
Naomba Serikali itamke hapa, ni lini fedha zitapelekwa ili kuiwezesha kampuni ya CHICO ifanye kazi ili kweli barabara ikamilike mwezi Juni? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwamba barabara ya Kilometa 6.3, kutoka nje ya mji kidogo, panaitwa Ndorobo, kufika mjini na kupitiliza hadi Seed Farm haikuwemo kwenye usanifu wa barabara kubwa, ile ya msingi inayokwenda mpaka Kigoma. Lakini alipokuja Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Kikwete, aliahidi mbele ya Mkutano wa hadhara kwamba barabara ile ya katikati ya Urambo itajengwa na Serikali. Pia alipokuja Mheshimiwa Magufuli ambaye sasa hivi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano…
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ndilo hili nauliza. Kwa kuwa ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Nne; na kwa kuwa pia Mheshimiwa Rais ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Ujenzi aliahidi kwamba barabara hiyo itajengwa kwa lami. Je, Serikali haioni kwamba kwa kuwa usanifu tayari na fedha zimeshatengwa, kwa nini wasiwape hao kampuni ya CHICO, inapomalizia kipande kile ambacho hakijamaliziwa, wakati huo huo wamalize na barabara inayopita katikati ya Urambo ili zote kwa pamoja zikutane eneo la Seed Farm? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lini fedha zitakwenda, nadhani atakiri kwamba ndani ya Bunge hili Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano alishatamka kwamba fedha zimeanza kuja, tumeshapokea zaidi ya shilingi bilioni 280. Kwa kweli awamu hii naomba kumwakikishia kwamba hiyo kazi itafanyika na ahadi hiyo itatekelezwa kwa sababu fedha zimeanza kuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili nadhani anaongelea masuala ya procurement. Nina uhakika, kwa sababu CHICO wako pale, vifaa wanavyo, inawezekana kwamba bei watakazozitoa, wao watakuwa na bei rahisi zaidi, kwa hiyo, uwezekano wa wao kushinda ni mkubwa zaidi kwa sababu tayari wana vifaa pale. Naomba tu tufuate taratibu za procurement, muda utakapofika, nina uhakika watu hawa watafikiriwa.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri amekiri kwamba mfumo uliopo una matatizo katika kumhudumia mkulima. Lakini Serikali inashiriki kikamilifu katika kupanga bei katika mfumo mzima. Sasa kwa kuwa Serikali inashiriki kwa kupitia wakala wake bodi au council, je, Serikali haioni kwamba inawajibika kubeba sehemu ya hasara anayopata mkulima?
Kwa kiasi gani mmefaulu kupata wanunuzi zaidi kutoka China ili soko liwe la haraka na wakulima wanufaike?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Tobacco Council au Halmashauri ya Tumbaku inawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya tumbaku. Serikali yenyewe haihusiki moja kwa moja katika kupanga bei lakini imeweka tu utaratibu ambao wadau wenyewe wanaweza kukaa kukutana kwa uhuru wao na kupanga bei. Hata hivyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba bei ya tumbaku inaendelea kuwa nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba tokea mwaka 2013 Bunge hili lilipitisha Sheria mpya ya Vyama vya Ushirika, utaratibu mpya wa Vyama vya Ushirika ni utaratibu ambao pamoja na mambo mengine unawaruhusu wakulima wa mazao mbalimbali kuendesha shughuli zao kwa kuwa na uhuru zaidi. Lakini vilevile mpango ule umeunda Tume ya Ushirika ambayo inakuwa karibu na Vyama vya Ushirika ili kuwezesha kuondoa kero zilizopo. Tunafikiri kwamba utaratibu huu utaleta ufanisi zaidi katika kilimo cha tumbaku pamoja na mazao mengine ikiwa ni pamoja na kusaidia katika suala la bei.
Lakini nitumie tu fursa hii kuwawelezea vilevile Waheshimiwa Wabunge kwamba pamoja na changamoto nyingi zilizopo kwenye sekta ndogo ya tumbaku, tunafikiri sekta ndogo ya tumbaku ni eneo ambalo limeanza kuonesha mifano ya kufanikiwa. Hii ni kwa sababu ndiyo sekta ndogo ya pekee ambayo mkulima anakuwa na uhakika wa kuuza zao lake tokea siku ya kwanza anapoanza kuweka mbegu shambani kwa sababu ni kilimo cha mkataba. Kwa hiyo, tukiondoa changamoto zilizopo tunafikiri ni eneo ambalo bado inawezekana kupata mafanikio makubwa. Lakini vilevile tungependa kutumia fursa hii kuwaeleza wakulima…
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia. Kuwafahamisha kwamba kufanikiwa kutumia mfumo wa mkataba utasaidia tu kama kila mtu akiheshimu mkataba. Kwa mfano, mwaka huu tayari wakulima wanafahamu inatakiwa wazalishe tumbaku kiasi gani, tunaomba wale ambao hawako kwenye mkataba usizalishe tumbaku kwa sababu ukizalisha hautaweza kupata mnunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele cha pili cha swali ni kwamba ni kiasi gani na kwamba tumefikia wapi na kuwapata wanunuzi kutoka China.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajitahidi kuongea na wafanyabiashara kutoka China, tumefika hatua nzuri sana kilichobakia sasa ni wao kumaliza taratibu za nchi mwao ili nao waweze kuingia kwenye mfumo rasmi wa kununua tumbuku ili kuondoa ukiritimba ambao mpaka sasa hivi nchi nzima kampuni zinazonunua tumbaku ni nne tu.
Kwa hiyo, tunafikiri kampuni zikiwa nyingi maana yake tunaondoa monopoly na hivyo bei itakuwa nzuri nashukuru sana.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo;
Kati ya kero zinazowakabili wakulima, mojawapo ni hii ya upatikanaji wa mbolea na bei yake wakiwemo wakulima wa tumbaku. Je, ni lini Serikali itaondoa kodi na tozo mbalimbali zinazoifanya mbolea ipatikane kwa gharama kubwa, tukiamini kwamba zikiondolewa kodi hizo na tozo mbalimbali mkulima atapata nafuu ya mbolea na pembejeo zingine na kwa msingi huo ataweza kulima zaidi.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba tozo na kodi mbalimbali zinachangia gharama ya pembejeo hususan mbolea kuwa kubwa. Nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imefanyia marekebisho baadhi ya tozo hizo na kodi kama mlivyosikia wakati Waziri wa Fedha anawasilisha bajeti, tayari kuna marekebisho kwenye baadhi ya tozo za zao la korosho lakini vilevile pamba na tunaendelea taratibu kuboresha katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niwafahamishe tu Waheshimiwa suala la kodi haliwezi kuwa ni suala la siku moja kwa sababu ni lazima mijadala ifanyike miongoni mwa wadau wa setka mbalimbali vilevile kodi ni suala la uchumi huwezi kuondoa zote kwa siku moja, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kuzifanyia kazi taratibu ili hatimaye kuwe na mazingira ya kikodi ambayo hayamuumizi mzalishaji mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba, tatizo lingine linalosababisha bei ya mbolea kuwa kubwa ni kwa sababu tunaagiza kutoka nje, nimpe habari njema kwamba kwa sasa kuna mikakati ya kujenga viwanda viwili vikubwa vya mbolea nchini; moja kitajengwa Kibaha na kingine kitajengwa Kilwa. Tunaamini kwamba uzalishaji wa mbolea ukifanyika nchini kwetu itakuwa ni rahisi zaidi wakulima kupata mbolea kwa bei ambayo ni nafuu.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala la ubora wa elimu ni muhimu kusimamiwa na Wizara ya Elimu yenyewe; je, Serikali inasemaje kuhusu kuimarisha macho yake ambayo ni ukaguzi ili ijue kinachoendelea katika shule hizo ambazo naona mimi pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kugatua madaraka, lakini kule chini kumezidiwa, mmewapelekea kazi kubwa.
Je, Serikali ipo tayari kuimarisha ukaguzi kwa kuifanya iwe SU yaani chombo kinachojitegemea ili kifanye kazi kikamilifu?
(b) Serikali inasemaje kuhusu hizi shule maalum; inazisimamiaje baada ya kugatua madaraka? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kuhusu Serikali kuboresha ukaguzi, hilo suala la kuboresha ukaguzi ni dhamira ya Serikali kwa sababu tunatambua kwamba wakaguzi ndio jicho letu, ndio wanaotuwezesha kubaini changamoto zilizopo na utaona hata katika bajeti yetu kuna mambo mengi ambayo tumefanya ya kuboresha ukaguzi. Sasa suala la kufanya ukaguzi uwe ni wakala hilo suala tunaliangalia na kuona kwamba je, kuna changamoto gani katika muundo uliopo na kama Serikali itaona kuna umuhimu wa kubadilisha mfumo hakuna tatizo lolote kwa sababu lengo letu sisi ni kuhakikisha kwamba ukaguzi unafanya kazi yake kwa ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la shule za wanafunzi wenye vipaji maalum, kama alivyojibu Mheshimiwa Jafo kama Serikali tunafanya kazi kwa pamoja. Kwa hiyo, usimamizi wa shule upo kwenye Ofisi ya Rais, TAMISEMI lakini bado Wizara yangu inahusika katika kuangalia ubora kinachoendelea shuleni na kuhakikisha kwamba mitaala inafundishwa kama inavyokusudiwa. Kwa hiyo, bado Wizara ya Elimu ina shirikiana na TAMISEMI kuhakikisha kwamba hizi shule zenye vipaji maalum zinaendelea kufanya vizuri.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuulizwa swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo yaliyoko katika swali namba 279 yanafanana sana na hali halisi iliyoko Urambo katika Kata ya Nsenda ambako wakulima wa Lunyeta na Kangeme walichomewa mahindi yao kutokana na mgogoro wa mipaka kama ulivyoelezwa katika suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mgogoro huu umewaacha wakulima bila kujua hatima yao na kusababisha usumbufu sana wa kupata chakula; na Serikali ilikiri kwamba ilifanya makosa kuwachomea wakulima ambao walikuwa wamelima katika eneo hilo, je, Serikali iko tayari sasa kufuatana na mimi kwenda kuangalia hali halisi ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tunazo sheria, lakini ni kweli pia kwamba kuwa na sheria ni sehemu moja au ni jambo moja, lakini utekelezaji wa sheria ni jambo lingine. Inawezekana kabisa kwamba mahali pengine utekelezaji wa sheria unaweza kuwa ni utekelezaji wa sheria unaovunja sheria. Sasa pale ambapo tayari kuna sheria na sheria zinatakiwa kusimamiwa, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria, lakini tunatoa wito kwanza kwa watu wote ambao wanatekeleza sheria, hasa zile sheria ambazo ziko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, waweze kutekeleza sheria hizo bila kukiuka sheria zenyewe, lakini bila kufanya mambo ambayo yanakwenda kinyume cha kanuni na taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala mahsusi ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliuliza, linalohisiana na eneo alilolitaja, napenda kumuahidi kwamba nikitoka hapa nitakwenda kulifuatilia zaidi na mimi nilifahamu kwa sababu ni mahsusi ili niweze kuona kama tunaweza kupata suluhisho katika kipindi hiki ambacho tuko Bungeni; lakini kama itabidi kwenda kuangalia, basi mara tu baada ya kumaliza Bunge la Bajeti, nitaweza kuandamana naye kwenda kuona kuna nini ili tuweze kupata ufumbuzi.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, masoko ya tumbaku yanayumba au kwa lugha nyepesi yanasuasua kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa Bodi ya Tumbaku ambayo ndiyo inapaswa kulipa wale ma-classifiers wanaopanga tumbaku lakini pia na kuajiri ma-classifiers. Je, Serikali katika mwaka huu wa fedha 2016/2017, imeiongezea Bodi ya Tumbaku kiasi gani ili ifanye kazi ipasavyo masoko yaende kama inavyopaswa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali inafahamu kwamba makato mbalimbali yako kwenye pembejeo lakini pia katika bei anayopangiwa mkulima kodi ni nyingi. Lini Serikali itakuja hapa na orodha ya kodi ambazo zimeondolewa ili mkulima apate mapato anayostahili?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba masoko ya tumbaku yanayumba na siyo kwamba yanayumba Tanzania peke yake bali yanayumba dunia nzima mahali tumbaku inakozalishwa kwa sababu ya bei ya tumbaku kidunia imeshuka. Kwa hivyo, hilo jambo linasababisha hata soko letu hapa ndani na lenyewe liyumbe hivyo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kubwa ni hiyo, lakini sababu zingine ni hizi za kwetu za ndani kama hivyo Bodi yenyewe kutokuwa na pesa za kutosha kuendesha shughuli zake kikamilifu. Ndiyo maana mwaka wa fedha uliopita pamoja na kwamba walikuwa wanapata ruzuku ya Serikali kuendesha Bodi yao, ukaanzishwa huo ushuru kwa wanaosafirisha nje tumbaku ili kuisaidia kukidhi mahitaji yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili kwamba kodi ni nyingi ni kweli kodi ni nyingi kama nilivyosema katika jibu langu la msingi. Ndiyo maana Serikali imechukua hatua hii ya kuunda Kamati ya Makatibu Wakuu wapitie hizi kodi za mazao yote siyo zao la tumbaku peke yake ili kuona zile kodi ambazo ni kero na ambazo zinaweza zikafutwa au kuondolewa mara moja ziondolewe na zile ambazo zitakuwa zinaathiri bajeti za Halmashauri zetu au Serikali Kuu basi hizi zitakuja kufutwa katika mwaka wa fedha ujao.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Kwanza naipongeza Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu, lakini kutokana na uhaba mkubwa wa maji unaowakabili wananchi wa Urambo, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza la nyongeza, kwa kuwa mradi huu ndio kwanza mradi wa maji ya kutoka Malagarasi uko katika awamu ya upembuzi yakinifu; na kutokana na umbali wa Mto Malagarasi kutoka Urambo, na shida iliyopo pale Urambo. Nilikuwa nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba hivi Serikali haioni wakati huu wanapoendela na upembuzi yakinifu wakachimba bwawa la maji Mto Ugala ili bwawa hilo lipate maji kutoka Mto Ugala, pia na maji ya mvua ambayo yanapotea bure ili yawasaidie wananchi kupata maji wakati bado huu mradi ambao utachukua muda mrefu unaendelea kushughulikiwa.
Swali la pili la nyongeza, ningependa kujua hizo lot, au awamu ambazo zitatekelezwa katika upatikanaji wa maji kutoka Malagarasi na kuhakikishiwa kwamba Tarafa ya Usoke imo pia?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati tunashughulikia huu mradi mkubwa tumetenga fedha kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kwa ajili ya kuweza kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Urambo kwa ajili ya kuweza kuhakikisha wananchi wa Urambo wana endelea kupata maji wakati tunasubiri huu mradi mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika kufanya usanifu wa Miradi hii tunaangalia kitu kinaitwa cost na benefit. Yaani kuchukua maji Mto Malagarasi itafaidisha vijiji 68 katika Wilaya ya Uvinza, Uyui, Kaliua, kwa hiyo ni mradi ambao una-benefit watu wengi zaidi na ndio maana Serikali ikaona kwamba tuweke, badala ya kuchukua Mto Ugala ambao kiangazi unakauka tuweze kuuchukua huu mradi mkubwa ambao wananchi wengi watapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu suala la bwawa, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwanza tutatembelea eneo lile ili tuone uwezekano kwamba bwawa hili lifanyiwe usanifu kwa ajili ya maji ya umwagiliaji kwa ajili ya wananchi wanaoishi maeneo yale.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililojitokeza katika Wilaya ya Sikonge kama alivyoeleza Mheshimiwa Kakunda ndivyo ilivyo katika Wilaya ya Urambo. Namshukuru Naibu Waziri alifika Urambo ila wananchi wa Urambo wanasikitika alifika lakini vijiji vingi hawajapata umeme. Je, ni kwa sababu ramani ilikosewa na yuko tayari kumtuma mhusika aende kuangalia tena kwa kuwa wananchi wengi hawakunufaika na umeme huo unaokamilika wa awamu ya pili? Hata hivyo, bado wanamkumbuka na wanaomba arudi tena, je, atarudi tena awaone?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile maswali ni mawili, nachagua swali la kwenda pamoja na Mheshimiwa Mbunge. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuhusu suala la kwenda wala sitatuma mtu, nitakwenda mwenyewe na nitakwenda na Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Nami niulize swali la nyongeza kutokana na swali la msingi la Mheshimiwa Zaynab Vullu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imalize tatizo la watoto wanaopata mimba kuendelea na masomo. Tunajisikia vibaya sisi Watanzania wanawake, kwa mfano, chukua Zanzibar, Zanzibar mtoto wa kike akipata ujauzito wanaruhusu anaendelea na masomo. Zambia, Kenya, sisi ndiyo tumebaki peke yetu wa mwisho kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa, kwa kifupi tu, taarifa zinatolewa kila siku watoto 30 wamepata mimba, watoto 20 wamepata mimba, hivi mnaona ninyi raha kutangaza kila siku na wasababishaji mnawajua ninyi wenyewe? Iliyobaki hawa watoto waruhusiwe wakasome, hakuna mjadala hapa.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lolote lile linapotekelezwa ili litekelezwe kikamilifu ni vema wadau wote wakawa pamoja. Sisi wanawake pamoja na hao wanafunzi wa kike hatuishi kwenye jamii peke yetu. Katika utekelezaji wa suala hili si tu kwamba maadam tukisema wanafunzi warudi shuleni basi unakuwa unasema umesema wakati hujui utekelezaji utakuwaje. Ndiyo maana tumewashirikisha…

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Tulieni. Kama majibu ninayo mimi basi sikilizeni. Nasema hivi suala hili linahitaji Wabunge wote kuwa on board kwa misingi kwamba…

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Na msisahau sisi wenyewe tulitunga sheria ya kuhakikisha kwamba yule anayetoa ujauzito kwa mtoto wa shule achukuliwe hatua.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Sasa kama ndivyo tumetunga hiyo sheria bila kuwa na ushirikishwaji na utaratibu maalum wa kuwapata hao wanaoendelea kutoa ujauzito kwa watoto wa shule, utaratibu vipi? Ndiyo maana tunataka sekta zetu zote, wadau wote, tuwe na uratibu wa kuweza kukabiliana na mambo yote mawili.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Kwa hali hiyo, wanafunzi watarudi shuleni lakini wakati huo huo lazima taratibu zetu za msingi za kufanya uratibu katika maeneo yote ikiwemo utoaji wa adhabu hasa wale akinababa ambao wanawanyemelea watoto wa shule uweze kuendelea.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu. Pamoja na majibu yako na jitihada kubwa inayochukuliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kutatua changamoto za zao la tumbaku, naomba niulize maswli ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, msimu wa kuuza tumbaku, yaani msimu wa masoko ya tumbaku ni sasa, ni mwezi huu wa nne, Serikali inatoa kauli gani kuhusu yafuatayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uongozi wa AMCOS ambao umefutwa kutokana na agizo la Serikali na kuwaacha bila uongozi kipindi hiki ambacho masoko yanaanza? Serikali inasema nini kuhusu suala hili? Ikiwemo AMCOS ya Utenge na Nsenga ambazo hazina uongozi hadi
sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali
inasemaje kuhusu kuwasaidia wakulima ambao
wamejitahidi wao wenyewe kutokukopa, lakini hatimaye wamejikuta wanabebeshwa madeni yasiyowahusu na kuwaacha hoi kiuchumi. Serikali inatoa kauli gani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uuzaji wa tumbaku katika mazingira ambayo uongozi wa AMCOS umefutwa au umesimamishwa; taratibu zitaendelea kushughulikiwa kwa kupitia Chama Kikuu katika maana hiyo WETCU na kama nilivyokwishsema tayari WETCU imewekewa utaratibu wa mpito, ili kuweza kufanya kazi zake kama kawaida. Kwa hiyo, kama kuna AMCOS ambazo hazina uongozi uuzaji wa tumbaku utaendelea kushughulikiwa na chama kikuu cha
ushirika, lakini vilevile kwa kushirikiana na vyombo vingine kama Maafisa Ushirika, lakini vilevile kwa kupitia watendaji ambao bado wapo kwenye Bodi ya Tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusu wakulima ambao wanalazimika kubeba mzigo wa madeni ambayo yametokana na wao kuwepo kwenye vyama vya ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya sababu zilizosababisha Mheshimiwa Waziri Mkuu kuchukua maamuzi mazito kuhusiana na WETCU na Bodi ya Tumbaku ni kwa sababu kulikuwa na usimamizi mbovu sana kuhusiana na madeni ya vyama vya ushirika, hali ambayo ilisababisha
wakulima kimsingi kubebeshwa madeni ambayo kwa kiasi kikubwa hata matumizi ya fedha ambazo zimekopwa utaratibu wake haufahamiki sawasawa. Kwa hiyo, hatua ambazo zinachukuliwa ni ili kuondoa hiyo hali, ni ili ifahamike kwamba, mikopo ambayo inachukuliwa inafanya kazi gani, lakini vilevile ni kuwawajibisha wale ambao wamekopa fedha na kuzitumia kwa njia ambazo ni kinyume na taratibu.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu zuri pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kukubali ombi letu la wananchi wa Urambo la kujenga kituo cha kupoza umeme (substation) Wilayani kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza linasema, je, Serikali inaweza kuwahakikishia wananchi wa Urambo kwamba katika Awamu ya Tatu ya REA vijiji vyote vya Wilaya ya Urambo vitapata umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kumpngeza Mheshimiwa Margaret Sitta kwa juhudi kubwa anazofanya kufuatilia maendeleo ya wananchi wa Urambo, hongera sana Mheshimiwa Sitta. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini niseme tu kwamba ni kweli
vijiji vyote 27 vilivyobaki katika Jimbo la Urambo vitapata umeme ikiwemo Yerayera, Igembesabo, Ifuta na vijiji vingine. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyingeza, lakini kabla ya hapo naomba uniruhusu kwa kifupi sana nimshukuru Naibu Waziri Mheshimiwa Kandege alifika Urambo na kujionea mwenyewe, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri, karibu tena, ulifanya kazi nzuri na kusababisha tupate wafanyakazi 17 kama ulivyosema lakini sasa swali la nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa Serikali imeona uhaba wa wafanyakazi uliopo na kutokana na wagonjwa wengi kutoka jirani zangu Kaliua ambako hawa Hospitali ya Wilaya wakiwemo kutoka Ulyankulu, Uyui, Uvinza. Naomba kuwauliza Serikali kama wako tayari kuongeza wafanyakazi ili tuendelee kutoa huduma nzuri?
Swali la pili ni kwamba, kutokana na ongezeko la wagonjwa wengi kutoka Kaliua, Uyui, Uvinza ikiwemo Ulyankulu, je, Serikali iko tayari kutuongezea fedha ikiwemo fedha za Busket Fund ili tuweze kumudu ongezeko la wagonjwa ambao wanatoka jirani? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba wa dhati nipokee pongezi kutoka kwa Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi tulifanya ziara kule na tukajionea kazi nzuri ambayo naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana jinsi ambavyo anahangaika na suala zima la afya za wananchi wa Urambo na tulipata fursa ya kutembelea Hospitali ya Wilaya na katika moja ya ombi ambalo Mheshimiwa Mbunge aliwasilishwa kwetu Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni pamoja na suala zima la kubadilishiwa matumizi kiasi cha shilingi milioni 150 ili ziweze kutumika katika kujenga wodi ambayo ni Grade A wazo ambalo tumelichukua na punde tutalifanyia kazi ataweza kupata majibu ili pesa ile iweze kutumika.
Kuhusiana na suala zima la uhitaji wa watumishi ili kukidhi haja ya wagonjwa ambao wanasafiri kutoka Wilaya nyingine kwenda Wilaya ya Urambo kwanza naendelea kumpongeza, ukiona wagonjwa wanakuja kwako maana yake huduma ambayo inatolewa na hospitali yako ni nzuri ukilinganisha na wengine.
Kwa nia hiyo hiyo njema na katika kuhakikisha kwamba tunakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Urambo, wewe ni shuhuda tulikubaliana, jitihada zinafanywa na Serikali hivi karibuni pesa zitakuja kwa ajili ya kulimalizia ile wodi ambayo ilikuwa imeanzishwa kutoka Wizara ya Afya.
Lakini kama hilo halitoshi, naomba niungane mkono kabisa na Mheshimiwa Magret Simwanza Sitta kwamba iko haja ya kutazama kwa kadri nafasi itakavyoruhusu watumishi wakipatikana ili kuweza kuongeza maana ukienda Kituo cha Afya Usoke pale tumeona kazi nzuri ambayo inafanyika na itakamilika hivi karibuni iko haja ya kuongeza watumishi pale watakapokuwa wamepatikana.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu aliyoyatoa, pamoja na majibu mazuri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Kwanza nakubaliana kabisa na Serikali kwamba jawabu la haraka la matatizo ya Urambo kuhusu maji ni Mto Ugalla, kwa sababu ni kilomita 30 tu kutoka Usoke. Ninaamini kwamba tumefanya hivyo kwa sababu ya suala la quick win ili wananchi wapate maji haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, katika kipindi tulichopita, katika maandalizi ya kupata maji kutoka Ugalla lilikuja tatizo la mazingira kwamba kuna wanyama, sijui kuna msitu; naomba Serikali itoe kauli, tusije tukafika katikati wakaanza tena masuala ya wanyama na misitu wakati sisi tunapata shida ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni vizuri kweli miradi miwili hii ikaenda pamoja kwa sababu kwanza Mto Malagarasi unategemea hayo maji kutoka Ugalla ambayo ndiyo yanatoka Urambo. Kwa hiyo, nashukuru Serikali hivyo, lakini je, Waziri yuko tayari kwenda na mimi uko akajionee mwenyewe uharaka wa kupata maji katika Mji wa Urambo na Usoke? Lini twende naye tufuatane wote wawili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Sera ya Maji ya mwaka 2002 inaendelea kutekeleza Mpango wa Sekta ya Maji nchi nzima ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wanaoishi vijijini wanapata maji safi na salama. Kama alivyoongea Mheshimiwa Waziri, ni kwamba tunatarajia ifikapo mwaka 2025 asilimia 100 ya wananchi wanaoishi vijijini na wale wanaoishi mijini waweze kupata maji.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea na usanifu wa mradi wa kutoka Malagarasi, kupeleka maji hadi Tabora ili kuhakikisha kwamba vijiji vingi vinapata maji hayo. Katika usadifu huo unaoendelea, pia kuna sehemu ambayo itatafiti uwezekano wa kuchota maji, kuweka mradi wa maji kutoka Mto Ugalla na kupeleka Wilaya ya Urambo ambayo itahusisha pia kupeleka maji katika Kata ya Usoke.

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta kwamba nitakuwa tayari kuambatana naye kwenda kuangalia tatizo la maji katika Mji wa Urambo.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri amejibu vizuri. Swali langu lilikuwa ni kuhusu vipingamizi ambavyo vimekuwa vikitumika vya wanyama kwamba ni Mbunga ya Wanyama; na pili suala la misitu. Mimi naomba Serikali itoe kauli yake kwamba hivyo vipingamizi havitakuwepo.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Pia nampongeza Mheshimiwa Sitta kwa namna anavyofuatilia tatizo la maji kwa wananchi wa Urambo. Amekuja Wizarani, tumeongea naye na kimsingi tumekubaliana kwamba maji ya wananchi wa Urambo tutayatoa Mto Ugalla. Suala la kufanya upembuzi yakinifu ni jambo la msingi katika miradi yote. Ni lazima tufanye haya maana kule Ugalla ni Hifadhi. Sasa ni lazima tufanye mawasiliano nao kwamba tutapitisha mabomba sehemu zipi na itaathiri vipi! Masuala haya ni ya msingi lakini haitazuia mradi ule kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nikuhakikishie kwamba tutapeleka maji kupitia kwenye Hifadhi, lakini mawasiliano ya kimsingi kati ya Wizara husika; Maliasili na Utalii pamaja na Ofisi ya Rais, Mazingira, lazima tuyafanye ili tuweze kukubaliana vigezo vipi tuvifanye na mradi uweze kuwa endelevu kwa ajili ya faida ya nchi hii. Ahsante sana.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza linalofanana kabisa na swali la msingi la Mheshimiwa Zedi. Hakuna jambo linalosikitisha kama pale ambapo majengo ya Serikali ambayo yameanza kujengwa halafu yanaachwa nondo zinaoza na kusababisha hasara kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Serikali inasema nini kuhusu jengo la upasuaji lililoanza kujengwa katika Wilaya ya Urambo ambayo mpaka sasa haijakamilika wakati huo jengo la upasuaji katika kituo cha Usoke halijakamilika, jengo la kliniki ya akinamama wajawazito katika Kata ya Usisya na Isongwa yote nondo zinaoza. Serikali inasema nini kuhusu uharibifu huu unaoendelea wakati wananchi wanahitaji huduma katika Wilaya ya Urambo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema hapa mwanzo, nikasema kwanza kuhusu majengo ambayo hayajakamilika wakati mwingine tunakuwa na makosa wakati wa budgeting. Wakati mwingine tunapanga bajeti, jengo halijakamilika na mwaka mwingine tunatenga bajeti bila kuangalia mradi uliopita. Kwa hiyo, kwanza katika vikao vyetu vya awali vya Halmashauri ni jambo la msingi kubainisha miradi ambayo haijakamilika na kuitengea fedha katika bajeti, kwa sababu bajeti hiyo ikishathibitishwa ndipo majengo hayo huweza kumalizika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nampongeza Mheshimiwa Mama Sitta kwa sababu ana-concern kubwa kwa akinamama. Ndiyo maana nimesema kwamba kwa kuona umuhimu wa jambo hilo tumeelekeza Halmashauri zote na barua tumeshaiandika imeenda katika Halmashauri zote; kwamba kila Halmashauri ilete mchanganuo wa majengo ambayo hayajakamilika ili tuweze kupanga kwa pamoja. Jambo hili lilifanywa na Kamati ya Bajeti ya Bunge kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais, TAMISEMI wiki iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu letu kubwa ni kupata mpango mkakati wa namna ya kufanya ili kuondoa haya maboma ambayo tangu mwaka 2007 – 2010 yalianzishwa na hadi sasa hayajakamilika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Sitta nikuhakikishie kwamba mpango wetu uliokuwepo ni mpango wa pamoja baina ya Bunge na Wizara za Serikali kuhakikisha kwamba huduma za afya, ukamilishaji wa majengo unakamilika ili wananchi waweze kupata huduma bora.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba amejibu swali ambalo yeye mwenyewe alifika Urambo na kujionea kwamba mpaka uliowekwa na Serikali upo, beacon zilizowekwa na Serikali zipo, lakini cha kushangaza ni kwamba wananchi waliondolewa kwenye eneo ambalo lina mpaka halali wa Serikali. Kwa hiyo, kuwaondoa wananchi kwangu mimi naona ni kwamba hawakutendewa haki kwa sababu waliidhinishwa na mpaka wa Serikali uliokuwepo. Kwa hiyo, kuwaondoa ni kwamba kumewapunguzia eneo lao la kilimo na la ufugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri ulijionea wewe mwenyewe, je, upo tayari kurudi tena na mimi tukakae na wale wananchi tuondoe huu mgogoro ili wananchi waendelee kutumia maeneo yao waliyoyazoea ambayo sasa hivi tunawapa umaskini kutokana na kuwapunguzia eneo la kulima? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Pori la Hifadhi ya North Ugala lina maeneo mengi ya migogoro ya aina hiyo hiyo kutokana na kubadilishiwa mpaka wa awali na kuwawekea wa pili ambao umesababisha upungufu. Sasa swali langu, je, upo tayari kutenga muda wa kutosha tukakae mimi na wewe muda mrefu hasa Urambo umalize migogoro yote katika mpaka huo wa msitu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana mheshimiwa Mbunge Margaret Simwanza Sitta kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akifanya katika kuwatetea wananchi wake wa Urambo. Kwa kweli anafanya kazi nzuri sana na ni mwanamke wa Jimbo ambaye kwa kweli anaonyesha mfano wa kuigwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nilishawahi kutembelea katika hili eneo na nilijionea hali yenyewe na tulikaa na wananchi tukatoa elimu tukaelimishana vizuri kabisa na niombe kusema kwamba nipo tayari kurudi tena kwenye eneo lile ili twende pamoja, tuambatane na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi na ambao ndio wenye dhamana ya kuthibitisha mipaka. Tukakae na Wizara ya Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii na wananchi ili tupitie hatua kwa hatua kuweza kumaliza migogoro ambayo ipo katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, nipo tayari pia kutenga muda wa kutosha kabisa kuhakikisha tunapitia miogoro yote ambayo ipo katika Jimbo hilo. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Jimbo la Urambo lina uhaba mkubwa sana wa maji, pamoja na kuishukuru Serikali kwa hatua yake ya uamuzi wa kupata maji kutoka Mto Malagalasi. Kwa sasa hivi kutokana na shida kubwa tuliyonayo; je, Serikali inachukua hatua gani za dharura ili wananchi wa Urambo wapate maji wakati wakisubiri mradi ambao utachukua muda mrefu wa maji kutoka Mto Malagalasi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishafika Urambo, tuna huo mradi mkubwa lakini ni kweli mradi mkubwa utachelewa. Hatua za dharura tunaendelea kutenga fedha kila mwaka kupeleka Halmashauri ya Urambo, lakini pia tumeshazungumza Mheshimiwa Mbunge kwamba naomba atukutanishe mimi Naibu Waziri pamoja na Halmashauri yake kwa maana ya Mkurugenzi na Engineer wa Maji ili tuzungumze, tushauriane kuchukua hatua za haraka ili kuweza kupata maji hasa kwa kuzingatia kwamba Tabora haina maji chini ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshazungumza na Mheshimiwa Mbunge, baada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani naomba tukutane na hao watu wake ili tutatue hili suala.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize maswali ya nyongeza, lakini kabla sijafanya hivyo, kwa ruhusa yako, kwanza naomba nichukue nafasi kwa niaba ya wananchi wa Urambo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kupitia Ofisi yake ya Rais, Manejimenti ya Utumishi kwa kauli aliyoitoa hivi karibuni, Mheshimiwa George Mkuchika, Waziri Mhusika, ya kuwarudisha kazini Watendaji wa Vijiji na Madereva waliokuwa wameachishwa kazi kutokana na elimu yao ya darasa la saba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuwarudisha kazini na kuamrisha walipwe mishahara yao yote ambayo wameikosa katika kipindi walichokuwa wamesimamishwa ni ishara na ushahidi tosha kwamba Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi ni sikivu. Tunaiomba Serikali yetu iendelee kuwasikiliza wanyonge na kuwatengenezea yale ambayo wanaona hayakwenda sawa. Ahsante sana Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyotoa lakini pia kuishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Waziri Mkuu mwenyewe kwa kuunda Bodi ya Tumbaku mpya ambayo imeanza kazi vizuri. Ombi langu tu kwa Serikali ni kuiwezesha kwa kuipa vifaa zaidi kama komputa na kadhalika, lakini pia ateuliwe Mwenyekiti ambaye naamini atakuwa ana uzoefu na zao la tumbaku.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikiombwa na wakulima wa tumbaku kutafuta wanunuzi zaidi wa tumbaku ili walime tumbaku zaidi lakini pia ilete ushindani wa bei ili mkulima wa tumbaku anufaike na zao lake, nataka kujua suala hili limefikia wapi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali haiwezi kuagiza mbolea kwa wingi hasa NPK ili mbolea hiyo iwafikie wakulima mapema kuliko kama ilivyokuwa kipindi kilichopita? Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mama yangu Mwalimu Margaret Simwanza Sitta kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia suala hili la zao la tumbaku kule Tabora na Tanzania nzima kwa muda mrefu kuhakikisha kwamba zao hili linakuwa na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija katika maswali yake mawili ya nyongeza ni kweli kabisa Bodi ya Tumbaku haina Bodi ya Wakurugenzi lakini imezinduliwa Disemba, 2017 na sasa hivi tunakaimu Mwenyekiti, ni miezi mitatu tu tangu imezinduliwa. Kwa hiyo, tunaamini kabisa Mheshimiwa Rais akiridhia kuteua Mwenyekiti basi na Bodi hii itaongeza tija katika utendaji wake wa kazi.
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye swali lake hilohilo la nyongeza kuhusu ku-monopolize hii biashara ya tumbaku ni kwamba kama Serikali sasa hivi tuna makampuni manne tu ambayo yananunua tumbaku lakini tuko kwenye majadiliano na Zimbabwe, Misri, China na Vietnam. Vilevile Serikali ya Indonesia kupitia Kampuni ya Star International wao wameshakubali pia kununua tumbaku yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nikija katika swali lake la pili kuhusu ununuzi wa mbolea kwa pamoja, sisi kama Serikali tuna mbolea ya DAP pamoja na UREA ambayo yenyewe ndiyo iko katika mfumo ule wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja, NPK haiko katika mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu na Mheshimiwa Mbunge kwamba mbolea hii ya NPK ambayo inatumika sana katika zao la tumbaku pia tunalichukua suala lake tutalifanyia kazi na hasa ukizingatia kwamba mbolea ya NPK mwaka jana ilitumika tu asilimia 21 ukilinganisha na ile ya UREA ambayo ilitumika asilimia 46. Kwa hiyo, wazo lako Mheshimiwa Mbunge ni zuri tunalipokea ili kuhakikisha kwamba mbolea inafika kwa wakulima kwa msimu. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuimarisha Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC), kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili walimu na matatizo mengi.
Swali la kwanza, ni kwamba, je, Serikali iko tayari kuwatuma wataalam kwa mfano Kenya kwenda kujifunza jinsi ambavyo wenzetu wameweza kuimarisha chombo kama hiki cha TSC ili kifanikishe katika utoaji wa huduma kwa walimu kwa kuwa nao Kenya walikuja kujifunza kutoka kwetu, wao wakaenda wakaimarisha wakafanikisha?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali iko tayari baada ya kuwatuma wataalam Kenya kujifunza jinsi ambavyo wamefanikisha wenzetu, kurudi huku na wahakikishe kwamba, wanachukua hatua za kuimarisha, ili kifanikishe katika kutoa huduma kwa walimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nieleze kidogo kuhusu Mheshimiwa Mama Margaret Sitta. Mheshimiwa Sitta ni hazina kubwa ya kumbukumbu na uzoefu katika sekta ya elimu nchini kama Mwalimu, Afisa Elimu, Kiongozi wa Chama cha Walimu, Waziri na Mbunge. Kwa hiyo, kwa kweli, amekuwa msaada mkubwa sana kwetu Serikali katika kutoa mawazo ya kuiboresha zaidi sekta ya elimu na sisi tutaendelea kufaidika nayo.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijibu maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo, kwa pamoja:-
Mheshimiwa Spika, kwamba ushauri wake wa kwenda kujifunza katika nchi ya Kenya tumeupokea na tutaufanyia kazi. Mapendekezo na ushauri wake katika suala la pili nao tunaupokea na tutaufanyia kazi, ili kuboresha zaidi Tume ya Utumishi wa Walimu. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubali kwamba Serikali inajitahidi sana kusaidia Hospitali ya Wilaya ya Urambo lakini bado tuna changamoto kubwa ambayo ni ukosefu wa theater, ni mradi wa ADB ambao ulijenga theater pale ikafikia lenta. Je, Serikali inawaliwaza vipi wapiga kura wangu wa Urambo kuhusu kumalizika kwa theatre ambayo ipo katika hatua ya lenta?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, nilipata nafasi ya kutembelea Urambo na naomba nimpongeze kwa dhati kabisa Mheshimiwa Sitta amekuwa ni mpiganaji kuhakikisha kwamba afya ya akinamama na watoto kwa ujumla inaboreshwa. Wakafanya kazi nzuri sana, wameanzisha na wodi maalum kwa wale watu ambao wangependa wawe kwenye grade A, ni jambo la kupongezwa na wengine ni vizuri tukaiga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeona ile theater ambayo inajengwa ikafikia usawa wa lenta, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Sitta Serikali itahakikisha kwamba kazi nzuri ambayo imefanyika haiachwi ikapotea, kwa kadri pesa itakavyopatikana tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba tunamalizia ile theater ambayo ilikuwa imekusudiwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa akinamama na watoto. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa tumbaku nyingi inayolimwa Mkoa wa Tabora inatoka Wilaya ya Urambo, Kaliua, Uyui na kwingineko. Je, Serikali iko tayari kuja kuona eneo ambalo lilishatengwa kwa ajili ya kiwanda Wilayani Urambo? Kwa kuwa wakulima wanapoteza kilo nyingi sana kusafirisha tumbaku kutoka Tabora kupeleka Morogoro.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tutakapopata nafasi tutaweza kuja kuona na kushauri kadri itakavyowezekana japo kama ambavyo hapo awali nimeeleza changamoto zinazojitokeza.
MHE. MARGARETH S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Awali ya yote namshukuru Naibu Waziri alifika mwenyewe na kujionea utata uliopo, kati ya mipaka iliyowekwa. Kuna mipaka miwili, wa zamani na wa sasa, ambayo imesababisha wananchi kutolewa kwa nguvu na hata kupoteza mali zao. Swali la kwanza; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri alifika yeye mwenyewe na kujionea utata uliopo anasemaje kuhusu utata ambao aliuona?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana na mimi kwenda kukaa kumaliza kabisa utata uliopo pale ili wananchi waendelee na shughuli zao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue nafasi kumpongeza sana Mheshimiwa Margaret Sitta kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika kuhakikisha kwamba anasimamia uchangishaji wa fedha kwa ajili ya vyoo vya mfano katika shule zetu katika majimbo yote. Nakupongeza sana mama yangu kwa kazi nzuri ambayo umekuwa ukiifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kumpongeza kwa jinsi ambavyo amekuwa akilifuatilia hili suala kwa muda mrefu. Nakumbuka mimi mwenyewe nilifika katika lile eneo kweli, tuliangalia utata wa mipaka iliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia agizo la Bunge la mwezi wa Sita katika kipindi cha bajeti tulikubaliana kwamba mipaka yote lazima iwekwe kwa ushirikishwaji wa wananchi, viongozi, Wizara ya Ardhi pamoja na Maliasili. Kwa hiyo, nasema tu kwamba, tuko tayari tutashirikiana na Wizara zinazohusika na wadau mbalimbali kuhakikisha utata wa migogoro ya mipaka iliyopo unatatuliwa mara moja na wananchi wanaendelea kufanya kazi zao kwa amani na utulivu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, niko tayari kabisa kufuatana naye lakini wakati nitakapofuatana naye nitaomba kwamba twende pamoja na Waziri wa Ardhi ili tuweze kuhakikisha kwamba wote tunajionea uhalisia uliopo katika eneo hilo.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa na mimi niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la mafunzo ya ufundi ni muhimu sana vijijini, sana, kwa hiyo naunga mkono kwa kweli suala la kuhimiza uimarishaji wa utoaji wa elimu ya ufundi vijijini, kwa sababu wengi hawaendelei na kidato cha kwanza na hata wanaomaliza kidato cha nne hawana mahali pa kwenda. Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha hivyo vituo alivyokuwa anazungumzia Mheshimiwa Susan lakini pia FDCs ili viweze kutoa ufundi unaotakiwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYASI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Sitta, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba tunaendeleza elimu ya ufundi nchini. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba tunaboresha mazingira ya elimu ya ufundi. Kwa kuanzia kama alivyouliza, katika bajeti ambayo wametupitishia ya mwaka unaokuja, Wizara ya Elimu itakarabati vyuo 30 vya FDCs, vile vyuo vya wananchi, kati ya 55 vilivyopo. Tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 10 kuhakikisha kwamba vile vyuo vinakarbatiwa lakini tunajaribu kuangalia mahitaji yao ya wafanyakazi ili kuhakikisha kwamba sasa vinafanya kazi katika hali nzuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika azma hiyo hiyo ya kujaribu kuendeleza elimu ya ufundi, Wizara yangu inatekeleza mradi wa unaotiwa ESPJ wa dola zaidi ya milioni 100. Mradi huu kimsingi unajaribu kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika vyuo vyote vinavyotoa elimu ya ufundi katika katika ngazi zote. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba ni kweli tunatambua umuhimu na ndiyo maana tunachukua hatua mbalimbali.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kazi kubwa sana ya kutujengea barabara ya kutoka Ndono - Urambo na sasa hivi inaendelea kutoka Urambo - Kaliua. Je, Serikali haioni kwamba kazi nzuri inaharibiwa na kipande ambacho mpaka sasa hivi hakijajengwa kutoka Posta - Seed Farm? Mheshimiwa Naibu Spika, halafu pili, je, Serikali…
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la mama yangu, Mheshimiwa Margaret Sitta, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, najua Mheshimiwa Mbunge anatambua kwamba hii barabara kutoka Urambo - Kaliua kipande kilichobakia kilometa 48 mkandarasi yuko site. Tutakuwa tumefanikiwa kuunganisha sasa kutoka Tabora Mjini mpaka Urambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua pia kiu ya Mheshimiwa mama hapa hiki kipande cha barabara kutoka Posta – Seed Farm kiunganishwe lakini kwetu tuliona kwamba muunganiko wa barabara kubwa ulikuwa na kipaumbele lakini baada ya hapo tutaendelea mama yangu kukiangalia hiki kipande. Najua pia ana kiu ya kupata round about ambayo tutaiita Mama Round About. Kwa hiyo, tunaendelea kuiangalia uwezekano wa kupata round about ili tuweze kuunganisha vizuri na kuhakikisha kwamba ajali katika makutano ya hii barabara tunaziondoa.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ulimaji wa tumbaku ni uhai kwa wananchi wa Urambo na Mkoa wa Tabora kwa ujumla; na wamekuwa wakiwa na changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na bei isiyoeleweka. Je, Serikali inasemaje kuhusu kufika kwa pembejeo kwa wakati na ununuzi wa tumbaku kwa utaratibu wa bulk procurement ili bei ya tumbaku isibadilike badilike hovyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumbaku ni maisha, kama nilivyokuwa nimesema, hususani katika Mikoa ile inayolima tumbaku ikiwemo na Tabora. Katika swali lake linalohusu pembejeo, ni kweli tumbaku na ile mbolea ya NPK ambayo inatumika sana katika suala zima la zao la tumbaku, sisi tumeviagiza Vyama vyetu vyote vile vya Msingi vya Ushirika kuhakikisha kwamba wanafanya jitihada kwa sababu wao wenyewe ndiyo wakulima ili mbolea na pembejeo hizi zifike kwa wakati kwa msimu unaotakiwa kwa sababu unaeleweka ili wao wenyewe kwa sababu ndio wanaolima, basi ule usumbufu usiweze tena kutokea. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi katika Wilaya ya Urambo wanateseka kutokana na migogoro iliyopo kwenye mapori ya hifadhi. Nichukue nafasi hii kumshukuru Naibu Waziri ambaye anajibu maswali sasa hivi alikuja kumaliza migogoro ile lakini haikuwezekana kutokana na muda mfupi uliokuwepo. Je, anatuambia nini sisi wananchi wa Urambo atakuja kumaliza migogoro iliyopo Runyeta ambako walichomewa nyumba zao na mazao yao, Tevera katika Kata ya Uyumbu na Ukondamoyo ambayo bado kuna mchuano mkubwa sana ambapo wananchi wamekosa mahali pa kulima kutokana na migogoro ya misitu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Sitta, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza kwa jinsi ambavyo amefanya kazi nzuri ya kuhamasisha wadau mbalimbali kuhakikisha fedha zinapatikana kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika shule zetu. Hongera sana mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa nilishafika katika eneo lile, nilikutana na wananchi na tukajadiliana juu ya mgogoro uliopo na Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii atatembelea eneo lile ili aweze kukutana na wananchi na kuhakikisha kwamba sasa ule mgogoro ambao ulikuwepo muda mrefu unaisha mara moja. Kwa hiyo, naomba asubiri kidogo Waziri ataenda katika eneo hilo na sasa watakaa pamoja kulitafutia uvumbuzi wa kudumu tatizo hilo.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Wananchi walioko Urambo katika Kata za Senda, Ukondamoyo na hasa Kijiji cha Yueta wana matatizo makubwa sana ya migogoro ya ardhi kutokana na kupakana na Pori la Akiba la Ugawa na kuwasababishia kukosa nafasi ya kulima na kufanya shughuli zao za mifugo. Je, Serikali itakuja lini Urambo kutatua tatizo hili ili wananchi hawa wanaopakana na Pori la Ugawa wafanye shughuli zao za kilimo na mifugo kwa raha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Sitta, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mashimba Ndaki, tumeelekezwa kupitia upya mipaka na malalamiko ya wananchi kwenye maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge anasema. Kwa hiyo, katika zoezi hili linaloendelea namwomba Mheshimiwa Margareth Sitta kwa sababu, wanaoleta malalamiko haya ni Halmashauri na Mkoa, atuletee malalmiko haya na tutayafanyia kazi.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza, naomba uniruhusu nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jitihada kubwa ambazo amechukua kusaidia zao la tumbaku kwa kuja kila wakati katika Mkoa wa Tabora. Pili, naomba nimshukruu pia Naibu Waziri kwa jibu zuri kwamba wataagiza mbolea kwa pamoja yaani bulk procurement ili kusaidia kupunguza bei lakini kufika kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, upatikanaji au uagizaji wa mbolea kwa wakati unategemea sana makisio. Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuhakikisha kwamba makisio yanatolewa mapema ili mbolea iweze kuagizwa mapema na imfikie mkulima kabla ya mwezi Agosti?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mkulima anapata moyo wa kulima kutokana na bei anayotegemea kupata. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupata wanunuzi wengi zaidi ili soko lipatikane kwa wakati na kwa ushindani ili angalau mkulima apate bei inayoweza kumsaidia kumudu maisha na kazi kubwa anayoifanya ya kulima tumbaku? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niwapongeze wananchi wa Urambo kwa kuchagua Mbunge jembe. Mheshimiwa Mama Sitta anawahangaikia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namwagiza Mrajisi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika afike Urambo haraka iwezekanavyo akae na Mkuu wa Wilaya ili waangalie namna bora ya kuratibu utaratibu wa kukusanya madeni kwa wakulima wa tumbaku hasahasa wale wakulima ambao wanadaiwa lakini wanaendelea na kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kuhusu kufanya makisio mapema. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mama Sitta pamoja na wananchi wake kwamba Serikali tumejipanga kuhakikisha makisio ya wanunuzi yanafanyika mapema ili wakulima waweze kujua ni kiasi gani cha mbolea wanatakiwa kuagiza na mbolea iwafikie kabla ya mwezi Agosti, kama alivyoomba Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusu mkakati wa kuongeza wanunuzi. Naomba niwajulishe Waheshimiwa Wabunge na wakulima wetu kwamba kwa upande wa zao la tumbaku tayari Serikali tumekaa na wanunuzi waliopo na kuangalia changamoto zao ambazo tukizitatua zitawawezesha kununua tumbaku zaidi lakini tunaendelea kuongea na nchi ambazo zina mahitaji ya tumbaku ikiwemo China na Misri. Kwa hiyo, kwa mikakati hiyo Serikali itaweza kuwasaidia wakulima wa tumbaku kupata soko la uhakika na zaidi na kwa kufanya hivyo tutakuwa tumewasiaidia kuhakikisha tumbaku yao inatakiwa na inagombaniwa na wahitaji na kufanya hivyo kutasaidia kuchochea bei kupanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Urambo haikutokea katika orodha ya kwanza iliyotolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa maeneo ambayo hayana usikivu mzuri wa simu, je, kwa kuwa yuko tayari kwenda kwa Mheshimiwa Mwakasaka Tabora Mjini, hawezi pia kupitiliza kuja Urambo ili ajionee mwenyewe maeneo yasiyokuwa na usikivu wa simu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali la mama yangu, Mheshimiwa Margaret Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mwezi Agosti, 2018 tulitangaza orodha ya kata 273 zinazopelekewa minara kwa ajili ya kusambaza mawasiliano na bahati mbaya Jimbo la Urambo halikupata. Hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika vijiji ambavyo aliniletea barua ofisini kwangu, vijiji vya Urambo vitaingizwa kwenye mpango wa mawasiliano kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Namhakikishia nitakapokwenda kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mwakasaka basi nitapitia mpaka Urambo kuangalia changamoto za mawasiliano, kama kuna jipya tutaweza kuongeza zaidi.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza naishukuru sana Serikali yetu kwa kujenga barabara ya Ndono - Urambo ambayo imekuwa msaada kwetu sana. Tatizo tulilonalo katika barabara hiyo ni kona inayoingia Urambo kwa kuanzia Ndorobo. Kona hiyo ni hatari kwa magari na pia kwa watembeaji wa miguu. Je, Serikali ni lini itaturekebishia barabara hiyo inayoingia Urambo Mjini kwa usalama wa watembea kwa miguu na magari kwa kutuwekea round about?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mama yangu Mheshimiwa Sitta, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli eneo analolitaja Mheshimiwa Mbunge hata mimi mwenyewe nimeliona, ni eneo ambalo linaunganisha barabara tatu lakini wataalam wa TANROADS, Mkoa wa Tabora wanapatazama hapa ili tuone kama tutaweza kuwa na design ya kuweka mzunguko hapo tutaweka lakini kama italazimika kuweka eneo lingine ili kuweza kudhibiti usalama wa watumiaji wa barabara maeneo hayo tutafanya hivyo. Tunalitazama kwa upana mkubwa ili tukitengeneza kitu tuweke kitu ambacho kitaweza kusaidia lakini kuleta maana na mahitaji ambayo Mheshimiwa Mbunge anayataja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira wanapatazama kwa sababu kwa namna inavyounganisha barabara tatu pale kidogo kulikuwa kuna changamoto fulani ambazo wataalam wanazifanyia kazi ili tuje tupate mchoro mzuri ambao pia hata gharama zake kuweza kurekebisha zitakuwa nzuri. Tunalifanyia kazi, vuta subira na wananchi wa Urambo wanasikia kwamba tupo pamoja nao.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Wananchi wa Urambo wanaoishi karibu na hifadhi za misitu wamekuwa na migogoro ya muda mrefu sana na hata kusababisha kuchomewa nyumba zao na mali zao hasa katika sehemu ya Kata ya Nsenga, Lunyeta, Ukondamoyo na Uyumbu. Je, Serikali inawaambia nini wananchi kuhusu lini watakwenda kutatua na hasa kwa vile ninavyokuwa na imani na Waziri husika. Lini anamaliza matatizo haya ili wananchi wafanye shughuli zao kwa raha?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margareth Simwanza Sitta, Mbunge wa Jimbo la Urambo, mama yangu, kwa ufupi tu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia maelekezo ya Mheshimiwa Rais aliyoyatoa Januari 15, 2019 kwa Mawaziri wa Wizara nane ambazo ni wadau wa migogoro ya ardhi, tumefanyia kazi jambo hilo kuhusiana na Lunyeta na maeneo mengine ya Mkoa wa Tabora na mikoa mingine hapa nchini na kwa sasa siwezi kusema nini itakuwa hatma yake, lakini kazi ya Mawaziri imekamilika na tumepeleka mbele ya meza ya Mheshimiwa Rais, tunasubiri mwongozo. Baada ya hapo Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa ujumla watapata kujua ni nini itakuwa hatma ya ufumbuzi wa migogoro ambayo imedumu kwa muda mrefu kwenye Sekta ya Ardhi na Maliasili.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto wanayoipata wakulima wakiwemo Wanawake hasa wanaolima tumbaku ni upatikanaji wa pembejeo kwa wakati hususan mbolea aina ya NPK.

Je, Serikali inawahakikishiaje wakulima wa tumbaku kwamba watapata mbolea ya NPK kabla ya mwezi wa Nane mwaka huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Sitta kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli yaani mwaka jana mbolea zilichelewa kufika kwa wakulima na sababu ndiyo mwaka wa kwanza ambao tulikuwa tunatekeleza ule mfumo wa bulk procurement (uagizaji wa mbolea kwa pamoja) na kitu chochote kikiwa cha kwanza lazima kina changamoto zake. Tumeona hizo changamoto, lakini mwaka huu ambao mchakato wa kufahamu kiwango cha uzalishaji na mahitaji ya mbolea tumeshakifanya mapema na tayari sasa hivi watu tuko kwenye mchakato wa kupata Mawakala wa kuagiza hizo mbolea na vyama vyenyewe tumevipa ruhusa ya kuagiza. Kwa hiyo, hilo tatizo mwaka huu halitakuwepo na mbolea zitafika kwa wakati kwa wakulima wa tumbaku na hasa akinamama wa Tabora.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niulize maswali ya nyongeza mawili kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimhakikishie Naibu Waziri aliyejibu maswali pamoja na Bunge kwa ujumla kwamba Mgogoro bado upo kati ya magereza na Kijiji cha Tumaini. Na uthibitisho ninao naomba nikukabidhi vithibitisho nilivyonavyo. Wananchi wanajua haki zao wanajua beacons zilizowekwa na baadaye kuondolewa, kwa hiyo mgogoro bado upo sasa maswali mawili kama ifuatavyo:-

(i) Kwa kuwa Serikali inasema imemamliza mgogoro wananchi wa kijiji cha Tumaini wanasema mgogoro bado upo. Je huoni kwamba kuna umuhimu wa wewe mwenyewe kwenda kuangalia nani anayesema ukweli na kutatua tatizo hili?

(ii) Kwa kuwa urambo kuna migogoro mingi kuhusiana na mipaka na hata ile inayopakana pori la akiba la ugala ikiwemo sehemu Indenda, Lunyeta, Uyumbu, Tevela pamoja na Ukondamoyo.

Je huoni Mheshimiwa Waziri kwamba utakapokwenda kutatua tatizo la Tumaini na magereza pia utatue migogoro mingine iliyopo hapa na ninapendekeza pia kwamba ufuatane na Waziri wa Maliasili kwa sababu pia vinahusiana pamoja?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kulikuwa mgogoro kama ambavyo nimeeleza katika jibu langu la msingi na mgogoro huo ulitatuliwa lakini tukumbuke tu kwamba vijiji hivi vilipimwa mwaka 2013. Lakini wakati huo gereza lile lilipimwa mwaka 1988 maana yake gereza lilitanguliwa likiwa na ekari 10,416 baada ya kuwa na mgogoro walipunguza kiasi cha ekari 7,198 kama nilivyotaja kwa vijiji ambavyo nimevitaja kwenye jibu la msingi la gereza likabaki na ekari 3,218.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akilifuatilia hili suala la mgogoro na ana vielelezo vingi vya wananchi wake wakilalamika nipende kumkubalia alichosema kwamba twende pengine tukaangalie uhakika uliopo nasema nipo tayari kwenda kwa ajili kuangalia mgogoro uliopo ili tuweze kuumaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili alikuwa anaongelea mgogoro wa mipaka katika maeneo mengine ambao yanaingiza kwenye pori la akiba sasa niseme hili pia katika ule msafara wa mawazie nane walikuwa wakipitia migogoro hii yote ilikuwa imehusisha Wizara ya Maliasili, TAMISEMI lakini wakati huo huo aridhi na Mambo ya Ndani pia walikuwapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, cha msingi hapa ni kufanya ufuatiliaji wa kina kwanza tuone hivi vijiji alivyovitaja vya Senda, Tundu na Ukomola kama vipo kwenye vile vijiji 366 ambavyo vilikuwa vimeainishwa katika kile kitabu kibwa cha migogoro. Kama napo kutakuwa kuna shida basi nitakapokuwa nina-solve mgogoro wa hili gereza na vijiji vya tumaini basi tutafika na hili pori la akiba tuweze kuona nini cha kufanya. Ahsante.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Pamoja na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inahimiza sana kilimo.

Je, Serikali inasemaje kutokana na zoezi linalowavunja moyo wakulima wa Urambo la wakulima kunyang‟anywa mali zao, nyumba zao na wengine mpaka wamekimbia miji yao kutokana na madai kwamba waliuza isivyotakiwa kwa mauzo ya tumbaku ya mwaka 2016/2017. Serikali inatoa kauli gani kuhusu hili zoezi linalowavunja moyo wakulima wa Urambo? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto mbalimbali katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo eneo la Urambo kwa baadhi ya viongozi wa Vyama vya Ushirika waliingia kwenye matatizo kwa sababu waliuza tumbaku ya wananchi bila kufata taratibu na wali-collude na wafanyabiashara na hivyo kuathiri bei ile ambayo ingetokana na soko.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, tulikabidhi taarifa kamili ya ukaguzi TAKUKURU ili wawafuatilie viongozi mbalimbali wale ambao walikiuka maadili ya viongozi na ambao hawakusimamia mazao sawasawa wakasababisha hasara kwa wananchi na kwenye Vyama vya Ushirika. Hilo zoezi linaendelea nchi nzima wale viongozi wote wanakamatwa na TAKUKURU.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa kuwa amesema wananchi wanakamatwa, TAKUKURU sidhani kama wanakamata wananchi ambao hawakuvunja hizi taratibu, ila kama kuna tatizo kama hilo, sisi tutafuatilia sasa hivi, tutaongea na viongozi wa TAKUKURU ili watuambie ni kitu gani kinachoendelea kwa wananchi wa Urambo ili tuweze kuhakikisha kwamba tunashirikiana na TAKUKURU na kuchukua hatua kwa wale ambao ni wabadhirifu badala ya wananchi wa kawaida wale ambao ni wakulima, ahsante.
MHE. MARGARETH S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Hussein Bashe kwa kupewa nafasi kubwa kama hivyo hongera sana Mheshimiwa. Pia nampongeza kwa majibu aliyoyatoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yangu ya nyongeza yako kama ifuatavyo: Kwanza hadi leo hii kuna tani 12 za tumbaku ambazo hazijanunuliwa na wakati huo msimu wa kilimo umeshafika, baadhi ya kampuni hazijatoa makisio hadi leo hii. Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha kwamba tumbaku yote inanunuliwa na makisio yanapatikana?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuna taarifa kwamba kampuni ya TLTC ambayo ilikuwa ikinunua tumbaku Kilograms 16 milioni ilikuwa na viwanda vya tumbaku, ilikuwa na maghala na wakati huo ilikuwa na wafanyakazi 300 ambao sasa kampuni hii ikijitoa ni kwamba hawa wafanyakazi wanapoteza kazi. Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuhakikisha kwamba hii kampuni pamoja na kuondoka, Serikali inatoa kauli gani kwamba TLTC ikitoka itakuwaje sasa kwa sababu ndiye ilikuwa mnunuzi mkubwa na kama nilivyosema ilikuwa na maghala, viwanda na wafanyakazi 300.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatoa kauli gani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kwamba kuna tumbaku mikononi mwa wakulima kiasi cha kilo milioni 12, hili jambo la fact na ni ukweli. Serikali imechukua hatua zifuatazo:

Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni ambazo zimekuwa zikinunua tumbaku zimekuwa zikipitia changamoto mbalimbali. Changamoto zingine zinasababishwa na uzembe wa baadhi wa Watendaji katika Serikali, kama Wizara tumechukua hatua, jana tumekutana na kukubaliana na kampuni nne zote za tumbaku ambazo zinanunua tumbaku nchini ambazo zilionesha nia ya kutokununua tumbaku hizo ambazo ziko mkononi mwa wakulima, tarehe 12 Council ya Tobacco takutana na kampuni hizi ili tumbaku hizo kuondoka mikononi mwa wakulima. Jambo la msingi ambalo limekuwa ni kikwazo kikubwa na mimi nitumie nafasi hii kuziagiza taasisi ambazo zipo chini ya Serikali jukumu la taasisi zilizoko chini ya Serikali siyo kuadhibu makampuni yanayochukua bidhaa kutoka kwa wakulima bali ni kuwasaidia ku-facilitate waweze kufanya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, utamaduni wa kuadhibu una-discourage investment na Serikali jana tumefanya maamuzi pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara kesi zote ambazo zinakabili kampuni Nne za tumbaku ambazo zilipigwa faini ya zaidi ya trilioni 11 kesi hizo ziondoke Mahakamani na tumewapa siku Saba na settlement agreement iwe imesainiwa ili wafanyabiashara hawa waweze kurudi kuendelea kufanya biashara. Ni azma ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais John Pombe Magufuli, kuhakikisha kwamba biashara inafanyika na mazingira yanakuwa sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kampuni ya TLTC ambayo ameuliza Mama Sitta tumeanza maongezi na kampuni ya TLTC na tumefikia muafaka na nawashukuru sana TRA kwa hatua waliochukua crisis za VAT wameshakubaliana na settlement agreement imeshafikiwa na kesi imeshatoka Mahakamani. Wameahidi kuongea na Makao Kuu yao Universal ili waweze kuednelea na operation. Lakini watakapokuwa wao hawapo kampuni ya British American Tobacco mwaka huu inanunua tani 2,500 na itashiriki katika soko la kuanzia msimu wa 2019/2020. Kwa hiyo, wakulima hawatokuwa na matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.(Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali kwa kutupa barabara nzuri ya kutoka Ndono mpaka Urambo na inakatisha mpaka katikati ya Mji, naishukuru sana Serikali kwa niaba ya wananchi wa Urambo. Swali ni kwamba ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja kuangalia round about ambayo wameiweka pale inasababisha ajali kwa jinsi ambavyo kona iliyopo ni kali sana, magari yanapata ajali, watu wanapata ajali. Kwa heshima na taadhima naomba kujua ni lini Serikali itakuja kutusaidia round about ya Urambo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisha kwenda Urambo lakini nitakwenda tena kwa sababu nafikiri kuliwa na zoezi hili la kuangalia sehemu bora zaidi ya kufanya marekebisho kuweka round about katika Mji ule. Kwa hiyo, Mama yangu nikuhakikishe kwamba tutakwenda lakini wataalam wanaendelea kukamilisha ili kuona ni wapi patafaa vizuri ili tuweze kuweka huo mzunguko. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kwa niaba ya wananchi wa Urambo, niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika jibu lake imekiri kwamba ilikuwa na kikao na hawa wanunuzi wa tumbaku wanaotaka kuondoka nchini:-

Je, Serikali inaweza kutuambia kwamba baada ya mazungumzo haya ya mwezi wa Tisa imefikia muafaka gani ili kampuni hizi ambazo zilikuwa zinanunua tumbaku nyingi hasa Urambo na Tabora kwa ujumla waendelee kununua tumbaku na pia kulinda ajira ya wale waliokuwa wakifanya kazi katika kampuni hizo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wanaotishia kuondoka, kama kweli hawatakubaliana na Serikali waondoke, Serikali itafanya nini kuhusu viwanda ambavyo walikuwa wamenunua kama kile cha Morogoro na pia magodauni mengi ambayo walikuwa wamenunua sehemu nyingi sana kule ambapo wananunua tumbaku? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza siyo dhamira ya Serikali kuona kwamba kuna mwekezaji yeyote ambaye amewekeza anaondoka nchini. Kwa hiyo, dhamira yetu ni kuendelea kufanya maongezi nao; na kufuatia maongezi tuliyofanya mwezi Septemba, kampuni tatu za tumbaku zilirudi kununua tumbaku ambayo ni maarufu kwa jina la makinikia ambayo ni un-contracted tobacco. Wameenda kununua jumla ya kilo milioni saba kati ya kilo milioni 12 ambazo zilikuwa zimebaki mikononi mwa wakulima. Kwa hiyo, tunaendelea kuongea na makampuni haya ili yaweze kuendelea kununua tumbaku na kuongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kampuni ambayo imeonesha nia ya kuondoka na kufunga shughuli zake, Kampuni ya TLTC; hoja za TLTC zilikuwa ni tatu. Moja, ni suala la kesi iliyokuwepo kati yake na Manispaa ya Morogoro. Tumefanya kikao mwezi wa Kumi katika Mji wa Morogoro na makubaliano yamefikiwa na kesi hiyo kutolewa nje ya Mahakama; na wamefikia settlement agreement ambayo wanaweza kuendelea na shughuli zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, lilihusu VAT returns, nami nitumie nafasi hii kuishukuru Wizara ya Fedha kwa dhati kabisa na kuwashukuru TRA, wameonesha commitment na wame-deploy team kwa kampuni zote za tobacco kuweza kupitia VAT returns zao za muda mrefu na mwezi huu wa Novemba mwishoni ndiyo yalikuwa makubalino juu ya kusaini makubaliano ya transfer pricing na VAT returns. Hatua zinaendelea vizuri na wawekezaji wameonesha positive results kwa kuonesha kwamba hatua za Serikali zinachukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya tatu ilikuwa ni suala la kesi za FCC. Tumefanya vikao na Serikali imewaagiza FCC kukaa na wafanyabiashara hawa ili kuweza kutafuta njia sahihi ya kuwa na suluhu badala ya kuendelea kuwaadhibu kwa sababu inaathiri sekta ya kilimo na inaathiri Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Serikali hatuna nia wala dhamira ya kuhakikisha kwamba kuna mwekezaji yeyote anaondoka, lakini akiondoka, ataondoka kwa mujibu wa sheria; na kwenye ubinafsishaji kulikuwa kuna mkataba na taratibu za kurudisha mali hizo ziendelee kubaki ndani ya nchi. Utaratibu upo katika mkataba waliobinafsishiwa infrastructure zote kuanzia kiwanda na magodauni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba mali zote za Watanzania zitaendelea kubaki kwa ajili ya maslahi ya Watanzania.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya mimi kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sasa hivi tuna Sera ya Elimu Bure ambayo imeleta ongezeko kubwa sana la wanafunzi wanaojiunga na shule na kwa kuwa bado hata private sector inaendelea kujenga vyuo vya ualimu.

Je, Serikali sasa haiwezi kuona kwamba, kuna umuhimu wa kuiweka Urambo kama eneo mojawapo ambalo Serikali itajenga kwa siku zijazo kutokana na mahitaji makubwa naamini ya walimu yanayohitajika sasa hivi kutokana na ongezeko la wanafunzi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema mwenyewe kwa sasa Serikali haina lengo la kuongeza vyuo vingine vya ualimu kwa sababu tuna vyuo 35 na siku hizi fikra ya Serikali ni kujaribu kuboresha zaidi na kupanua zilizopo kuliko kujenga utitiri wa vyuo na ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa kwa watu wa Tabora kuna vyuo viwili vya ualimu tayari, Chuo cha Walimu Ndala na kile cha Tabora, lakini kama mwenyewe anavyosema labda huko mbele kama itatokea haja ya kuhitajika kujengwa chuo kingine sio vibaya kufikiria ombi lake, lakini kwa sasa lengo ni kujaribu kuongeza ubora wa vyuo vilivyopo badala ya kukimbilia kujenga vyuo vingi ambavyo havina ubora.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu maswali vizuri kwa mara ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini napenda Serikali itambue kwamba wananchi wa Urambo wanashukuru kupata hifadhi lakini kwa kuwa kulikuwa na mgogoro wa muda mrefu tangu 2013/2014 kuhusu mipaka, je, Serikali haikuona kwamba kuna haja ya kumaliza ile migogoro kabla ya kuwa na hifadhi ili wananchi waendelee na maisha yao ya kufuga nyuki ambao sasa hivi hawaruhusiwi kufuga mifugo na kulima?

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, lini Mheshimiwa Waziri atakuja ajionee mwenyewe kwa sababu mpaka sasa hivi wameshakuja Naibu Mawaziri wawili, alishakuja Mheshimiwa Ramo wakati ule, Mheshimiwa Naibu Waziri Angelina Mabula alikuja na pia alikuja Mheshimiwa Kiwangalla aliyekuwa Waziri lakini bahati mbaya mvua ilinyesha hakuweza kufika maeneo yale. Je, ni lini Serikali inakuja ione jinsi ambavyo wananchi wanataka maeneo waendelee kuendesha maisha yao kwa kilimo, kufuga nyuki na mifugo pia?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusiana na suala la mgogoro, Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi siku zote imekuwa ikishirikiana na wananchi wake katika kutatua changamoto mbalimbali. Migogoro ya ardhi imeshapatiwa suluhisho kupitia Tume ya Mheshimiwa Rais ya Mawaziri Nane iliyoongozwa na Mheshimiwa Lukuvi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Margaret Sitta kwamba suala hilo nalo limeshapatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili kuhusiana na lini tutakwenda? Nimhakikishie Mheshimiwa Margaret Sitta mara baada ya Bunge hili nitaambatana naye kwenda jimboni Urambo kuhakikisha tunatatua suala hili. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naipongeza Serikali kwa majibu mazuri lakini pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba yake aliyoitoa tarehe 30 Mjini Tabora ambayo ilituhakikishia kwamba tutapata maji na baadaye pia kuongezewa zaidi na Mheshimiwa Waziri wa Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali haioni kwamba changamoto kubwa ya maji sasa inakaribia kupata ufumbuzi baada ya kuhakikishiwa kwamba mradi utafika huko, Mheshimiwa Waziri anaweza kuja Urambo kwa sasa hivi akaangalia hali halisi na huenda akaongezea hata maeneo yatakayonufaika na mradi huo?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tumuandalie mkutano wa hadhara arudishie maneno hayahaya ili wananchi wa Urambo waendelee kuishi kwa matumaini na kushukuru Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa kwa sababu amekuwa ni mfuatiliaji mzuri sana. Kwa kuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais lazima tuitekeleze kwa nguvu zetu zote na Urambo inakwenda kunufaika, niseme niko tayari kuja Urambo na mkutano wa hadhara hapa ndiyo mahala pake. Nitahakikisha naelekeza vema jamii ya Urambo na watamuelewa Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa matatizo ya maji yanakwenda kufikia ukingoni.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niongee kwa uchungu. Wakulima wameuza tumbaku tangu mwezi wa tano mpaka sasa hawajalipwa na wao wanategemea tumbaku ndio waweze kuishi. AMCOS zifuatazo naongea kwa uchungu, AMCA, MISSION, MTAKUJA, IFUTA, TUNAWEZA, KASISI, KATUNGURU, SIPUNGU, MISANGI,
KALEMBERA, BLOKU, JIKOMBOE na UPENDO hawajalipwa hela tangu mwezi wa tano naongea kwa uchungu waishije na sisi tunasema wakulima wanategema kilimo. Lini Serikali itawalipa hawa wakulima ili nao waweze kuendesha maisha yao?

Mheshimiwa Spika, la pili wakati huo bei ya mbolea imefikia hadi laki moja karibu wataanza kutengeneza mabero yao wanafanya nini, hawajalipwa halafu bei ya mbolea imefika mpaka laki moja, naongea kwa uchungu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nimpe pole na nimwambie kwamba kama Serikali tunakiri uwepo wa changamoto hii. La pili ambalo ni vizuri Waheshimiwa Wabunge wakafahamu na yeye ni mmoja kati ya Wabunge ambao mwaka 2019 aliomba Serikali ifanye juhudi za kuhakikisha AMCOS alizozitaja na baadhi ya AMCOS katika Mkoa wa Tabora ambazo hazikuwa na mikataba na ziliachwa na TLTC na ziliachwa na jumla ya tani 12000 ya tumbaku ambazo hazikuwa na wanunuzi.

Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara hawa wa kitanzania ndio walio-rescue sector hii na leo tuko confident bei ya tumbaku imetoka dola 1.4 mpaka dola 1.65, zipo changamoto za kuchelewa kulipwa malipo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na niwahakikishie wakulima wa tumbaku moja tutawahakikishia kwamba waliofanya masoko ya mwezi Mei, Juni na Julai tutahakikisha kwamba malipo yao yanafanyika.

Mheshimiwa Spika, la pili tumebadili mfumo wa uuzaji baada ya matokeo ya mwaka jana kwamba makampuni haya sasa tumbaku yao yote wanayochukua kwa wanunuzi haziondoki ndani ya mipaka ya nchi yetu mpaka fedha zimepatikana. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie kwamba hizi changamoto tutaendelea kuzitatua.

Mheshimiwa Spika, kuhusu bei na kuhusu pembejeo sasa hivi wakulima wa tumbaku tumeshaanza kuwapelekea mbole za mabedi bila wao kulipa hata shilingi. Tumetengeneza utaratibu wa suppliers wanapeleka na watalipwa mwisho wa msimu kwa hiyo nataka nimhakikishie kwamba pembejeo zimekwenda.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kupanda kwa bei ya mbolea ni jambo ambalo limetokea na ni kweli nani suala la kidunia. Hatua tuliyochukua mwezi uliopita tumeenda ku- review bei ya tumbaku na wanunuzi wote na kuifikisha dola 1.65 tuki-accommodate ongezeko la bei ya mbolea ili wakulima hawa wasiweze kupata hasara. Nimhakikishie mama Sitta na niwahakikishie wakulima wa tumbaku tumeanza mazungumzo na taasisi za fedha tutahakikisha msimu ujao changamoto ya delay ya payment inakwisha katika sekta ya tumbaku na tutafata sheria ambapo credit facility ni siku 14 na sekta hii iweze kuwa stable.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, bado hali ya Urambo ni mbaya kuhusu upimaji wa afya ya akinamama na watoto kwa kuwa X- ray ni mbaya. Na wakati huohuo, pamoja na jitihada nzuri ya kupata ultrasound mbili, bado ultrasound hizo hazina watumishi, zimekaa bure. Kwa hiyo, sasa kwa kuwa hakuna X-ray kama alivyojibu Mheshimiwa Waziri, ultrasound tumejitahidi tumepata mbili, hazina watumishi. Je, lini Serikali italeta watumishi wawili angalau zile ultrasound zianze kupima akinamama na watoto? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; pamoja na nia nzuri ya Serikali yetu ya kutujengea kituo cha afya Mlimani katika Kata ya Uyumbu, jengo la akinamama na watoto linakaribia kuisha lakini limepungukiwa milioni 100. Suala hili tulizungumzia Mheshimiwa Waziri mhusika alipokuja kutembelea, Mheshimiwa Dkt. Festo, bado ile hospitali inahitaji kumaliziwa jengo. Je, lini Serikali itatuletea milioni 100 ambazo tumekisiwa zimalize ili wodi ya akinamama ianze kutumika badala ya sasa wanakwenda mbali kwa lengo la kujifungua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza na ameomba hapa kwamba walau wapelekewe watumishi wawili katika maeneo ambayo tumepeleka ultrasound na X-ray katika Wilaya yake ya Urambo. Nimhakikishie kabisa kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto tumekubaliana kwamba Waziri husika anaendelea kufanya utafiti na kuhakikisha ndani ya kipindi hiki kifupi wanapeleka mtaalam katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, commitment ya fedha ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya kumalizia jengo lililoko katika Jimbo la Urambo ambayo inahitajika kuhakikisha hilo jengo linaanza kutumika kwa wakati. Nimhakikishie kabisa kwamba nimewasiliana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ameniagiza kwamba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutapeleka wataalam wetu wakaangalie hiyo tathmini na baada ya hapo tutatoa majibu ya msingi kuhakikisha hilo jengo linakwisha na linaanza kutumika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Wilaya ya Urambo ina hospitali ya wilaya iliyojengwa mwaka 1975 na hali yake siyo nzuri. Je, Serikali yetu inayosikiliza maombi ya wananchi ni lini itakuja kuingalia itengenezwe upya ili iende na wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Urambo ni kweli ni hospitali kongwe sana ambayo imejengwa mwaka 1975 na bahati njema katika ziara yangu pia nilifika katika hospitali ile tukashirikiana vizuri sana na Mheshimiwa Mama Margaret Sitta, tukaikagua hospitali ile na kuona kwa kweli tunahitaji kuweka mpango mkakati wa kuzikarabati hospitali kongwe zote nchini ikiwepo ya Hospitali hii ya Urambo.

Kwa hiyo, naomba nimuhakikishie kwamba mipango ya Serikali tumeshapanga katika mwaka ujao wa fedha kuanza kukamilisha ujenzi wa Hopitali za Halmashauri katika Halmashauri zote ambazo hazina Hospitali za Halmashauri. Lakini baada ya hapo tutakwenda kwenye awamu ya kukarabati au kujenga kulingana na tathmini hospitali nyingine za Halmashauri katika Halmashauri zenye hospitali kongwe sana ikiwepo Urambo.

Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba suala hili tunalifanyia kazi na tutahakikisha kwamba tunalitekeleza. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa heshima naomna niseme maneno machache kabla sijauliza maswali yangu ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, inasikitisha Serikali inapoacha migogoro inakua miaka na miaka na hili suala sio mara yangu ya kwanza kuuliza humu Bungeni, Mheshimiwa Masauni alipokuwa Naibu Waziri alijibu majibu ya hivyo hivyo. Kwa hiyo, naomba Wizara ikasome mafaili yake ya maswali itakuta ni hayo hayo majibu ni hayo na maswali ni hayo. Maswali yangu ya nyongeza ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mgogoro huu umedumu tangu mwaka 1998 baada ya mipaka iliyokuwa halali kuondolewa na kupunguza maeneo ya wananchi ya kulima na kufuga mifugo yao, nini kauli ya Serikali kuhusu kumaliza mgogoro huu? Naomba Serikali itoe kauli yake lini inamaliza mgogoro uliodumu tangu mwaka 1998?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kama kweli Serikali ina nia ya kumaliza mgogoro huu ambao unawasikitisha sana wananchi wa Ukondamoyo na Tumaini, je, Waziri yupo tayari twende naye akaone yeye mwenyewe na ndiyo atakuja kuthibitisha kama kweli majibu yanayotolewa na Serikali ni ya halali? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu na naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge yote mawili kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kama ulivyosema kwamba majibu ya msingi ya Serikali, mgogoro unaonekana haupo, ushahidi wa namna ambavyo Magereza walitoa lile eneo na kuligawanya kwa idadi ya heka ambapo Kijiji cha Tumaini kilipata heka 505, maelezo haya yanaonekana Mbunge hakubaliani nayo, ninaomba nikuhakikishie kwamba nipo tayari baada ya Bunge kwenda nikajionee mwenyewe na kuwasikiliza wananchi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa heshima naomna niseme maneno machache kabla sijauliza maswali yangu ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, inasikitisha Serikali inapoacha migogoro inakua miaka na miaka na hili suala sio mara yangu ya kwanza kuuliza humu Bungeni, Mheshimiwa Masauni alipokuwa Naibu Waziri alijibu majibu ya hivyo hivyo. Kwa hiyo, naomba Wizara ikasome mafaili yake ya maswali itakuta ni hayo hayo majibu ni hayo na maswali ni hayo.

Maswali yangu ya nyongeza ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mgogoro huu umedumu tangu mwaka 1998 baada ya mipaka iliyokuwa halali kuondolewa na kupunguza maeneo ya wananchi ya kulima na kufuga mifugo yao, nini kauli ya Serikali kuhusu kumaliza mgogoro huu? Naomba Serikali itoe kauli yake lini inamaliza mgogoro uliodumu tangu mwaka 1998?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kama kweli Serikali ina nia ya kumaliza mgogoro huu ambao unawasikitisha sana wananchi wa Ukondamoyo na Tumaini, je, Waziri yupo tayari twende naye akaone yeye mwenyewe na ndiyo atakuja kuthibitisha kama kweli majibu yanayotolewa na Serikali ni ya halali? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu na naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge yote mawili kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kama ulivyosema kwamba majibu ya msingi ya Serikali, mgogoro unaonekana haupo, ushahidi wa namna ambavyo Magereza walitoa lile eneo na kuligawanya kwa idadi ya heka ambapo Kijiji cha Tumaini kilipata heka 505, maelezo haya yanaonekana Mbunge hakubaliani nayo, ninaomba nikuhakikishie kwamba nipo tayari baada ya Bunge kwenda nikajionee mwenyewe na kuwasikiliza wananchi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake lakini bado ningeomba kwa kuwa maisha ya sasa yanategemea sana matumizi ya simu na wahusika wanaathirika kwa kiasi kikubwa naomba niyataje maeneo hasa ambayo yanahitaji kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo, Kata ya Itundu, hasa Katuli, Ilani, Kiloleni, Mwinyi, Kalembela, Jumbe na Kikwete Kata ya Muungano ni Muungano yenyewe, Magulungu, Isenda, Utenge na Kangeme, Kata ya Usisya ni Usisya Kati, Mabundulu, Katungulu na Majengo. Kata ya Uyogo ni Uyogo yenyewe, Igembesabo, Kasela, Igunguli na Mirambo, Kata ya Ugala ni Ugala yenyewe Izengamatogile na Isogwa, Songambele, Mlangale na Ukwanga na Kata ya Kapilula ni Kata yote, naomba lini wanapatiwa mawasiliano watu wa Urambo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya wananchi wa Urambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli alichokiongea Mheshimiwa Mbunge ni kweli kabisa, kwasababu tayari tarehe 16 Machi 2021 nilifanya ziara katika Jimbo lake la Urambo, na kweli nikagundua kuna maeneo ambayo bado yana changamoto ya mawasiliano. Lakini katika maeneo ambayo tuligundua yana changamoto ya mawasiliano, tulitoa maelekezo ili tathmini ifanyike na kuhakikisha kwamba wananchi wa Urambo hawapitwi mbali na huduma ya mawasiliano kwa ajili ya kujiletea maendeleo kupitia mtandao wa mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na wananchi wa Urambo wana imani na Wizara hii inafanya kazi kubwa, lakini kwa leo naiomba Serikali itoe kauli hapa. Lini maji haya yanafika Urambo kutokea Tabora ambapo yameshafika kutoka Lake Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la ngongeza la Mheshimiwa Margaret Sitta kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema lini mradi utaanza kutekelezwa, kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha, mradi utaanza kutekelezwa. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imefanya kazi kubwa sana ya kujenga barabara nzuri kutoka Ndondo mpaka Kigoma. Tatizo kubwa linalotukabili sisi Urambo ni kwamba kona ya kuingilia Urambo Mjini inasababisha ajali kubwa sana. Sasa kwa kuwa nilishaomba Serikalini kujengewa round about na Serikali imeshafanya utafiti wake, imeshapata na gharama: Je, Serikali iko tayari sasa kujenga hiyo round about. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama alivyosema kwamba kama tathmini ilishafanyika, maana yake ni kwamba Serikali ina dhamira ya kuijenga. Naomba baada ya hapa, nimwombe Mheshimiwa Margaret Sitta tuweze kuona ni wapi tumekwama ili tuweze kuamua, kwa sababu kama kazi imeshafanyika, maana yake ni kwamba Serikali imeshaona kuna umuhimu wa kujenga.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nimuulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya kuuzia tumbaku ni muhimu sana kwa mkulima; je, wakulima wenyewe wanashirikishwaje katika kufikia uamuzi wa bei gani tumbaku yao iuzwe?

Swali la pili tunaishukuru Serikali kwa kutupa ruzuku, lakini naomba Serikali ituhakikishie sisi watu wa Urambo; je, mbolea ya tumbaku ni miongoni mwa mbolea zilizopata ruzuku? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushiriki wa wakulima, kwa mujibu wa Sheria ya Tasnia ya Tumbaku Namba 24 ya mwaka 2021 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009 na kanuni zake za mwaka 2011 Kifungu cha 43 (1) kimeweka masharti ya ushiriki wa wakulima kupitia vyama vyao vikuu katika majadiliano ya bei na pembejeo. Hivyo, nidhahiri kwamba kupitia sheria hii wakulima wanashiriki kupitia vyama vyao vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu mbolea ya ruzuku; katika mwongozo ambao tumeutoa kwenye mbolea ya zuruku, mbolea ya ruzuku ni kwa mbolea zote ikiwemo mbolea ambazo zinahusiana na zao la tumbaku. Kule kwenye tumbaku wanatumia mbolea hasa za NPK na CAN ambapo hadi hivi sasa kwa mujibu wa maoteo ni jumla ya tani 37,000 zitahitajika na tayari zipo kwenye utaratibu huo kuingia kwenye suala hili la ruzuku.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri kwmaba amekitaja kituo cha kupoozea umeme Urambo: Je, anawahakikishiaje wananchi wa Urambo kwamba lini kituo hicho kinakamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Sitta, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Margaret Sitta na wananchi wa Jimbo lake kwamba katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 kutoka katika Shilingi bilioni 500 ambazo zimewekwa kwa ajili ya uendelezaji wa gridi, vile vituo 15 vitakavyojengwa, na cha kwake cha pale Uhuru kitakamilika bila matatizo yoyote.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningeomba niweke wazi swali langu lililenga kichaa cha mbwa na kwa sababu kwangu Urambo watu 21 waliumwa na mbwa mwaka jana mwaka 2022 na kati ya hao 21 walioumwa na mbwa 12 walifariki ndio maana nikauliza swali hili. Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na kichaa cha mbwa kwa kushirikiana na Wizara nyingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, mtu anaeyeumwa na mbwa mwenye kichaa anatakiwa achomwe sindano tano, na sindano moja ni elfu 30,000. Sindano ya kwanza inabidi alipe 35,000 kwa ajili ya ile ada ya kujiandikisha, sasa wengi wanashindwa kulipa 155,000. Je, Serikali inasemaje kuhusu kupunguza gharama za matibabu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu katika hao wagonjwa wake 21, wengi kabisa amekuwa akija kwangu na akihangaika kuhakikisha wanapata tiba. Nimwambie Mheshimiwa Mbunge sisi na Wizara ya Mifugo tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kwanza, sio tu uwepo wa tiba kwa ajili ya watakao kuwa wameumwa lakini mbwa wetu kuhakikisha wanakuwa wanachanjwa na nitumie fursa hii kuwaomba Wakuu wa Wilaya na Wilaya zetu ma DMO kuhakikisha wanashirikiana na wenzetu kuhakikisha mbwa walioko mtaani wanatafuta solutions lakini pia kuhakikisha wenye mbwa wanakwenda kuchanja mbwa wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini amezungumzia suala la gharama 155,000; Waheshimiwa Wabunge ndiyo maana kila wakati hapa tunakuja na Muswada Bima ya Afya kwa wote, leo hapa nilipokaa kwenye kiti change hapa, nina wabunge zaidi ya watatu mmoja anadaiwa milioni tisa mwingine anadaiwa milioni sita na mwingine milioni 4.8, anatakiwa kulipa na wagonjwa wa jimbo lake wameshindwa kulipa. Maana yake ninashukuru tumefanikiwa kuwasaidia Wabunge lakini tunaweza kuwasaidia wangapi? Ndiyo maana wakati wote tunasema na tusisitiza na nitumie fursa hii kuwaomba Wabunge wenzangu kama tunataka kuondokana na matatizo haya ni lazima wote kwa pamoja tukubaliane kwamba suala la bima ya afya kwa watu wote ni la msingi sana ili tuweze kuondokana na hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nitumie fursa hii kuwaomba Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuwa mtu yeyote akiumwa na mbwa cha kwanza sisi tunachotaka ni kuokolewa kwa maisha, wasifikirie hela wamtibu mtu ndio suala la fedha lifuate. Waache tabia ya kuwanyima watu tiba eti kwa sababu hawana fedha. Pia MSD, niwaagize MSD kwamba kuanzia sasa hatutategemea kusikia hospitali yoyote mgonjwa amekwenda na hakuna dawa za kusaidia watu walioumwa na mbwa. Tunataka dawa zote za magonjwa ambayo sio magonjwa ambayo yanaoneka kila wakati ziwepo, lakini dawa za kichaa cha mbwa ziwepo kwenye kila hospitali na watu wakiumwa wapewa priority ya kutibiwa mapema, ahsante sana.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake lakini naomba atoe kauli hapa kwamba Je, baada ya utafiti kukamilika inawahakikishiaje wananchi wa Urambo kwamba wachimbaji wadogo wadogo nao watapa vitalu ili wanufaike na madini yao. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Sitta kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tumepewa dhamana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba tafiti za madini zinapokuwa zimekamilika na maeneo yenye madini yamepatikana tunahakikisha kwamba yametengwa maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Mama Sitta kwa sababu amekuwa ni mpambaji mkubwa kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo la Urambo hawaachwi nyuma katika kuwekeza kwenye biashara ya madini.

Mheshimiwa Spika, kwa ajili hiyo basi nitumie fursa hii kutoa wito kwa Mikoa yetu yote ya kimadini na wilaya zake, tafiti za madini zinapokamilika na maeneo yenye madini yanapokuwa yamepatikana kuhakikisha kwamba wanayatenga maeneo mahsusi kwa ajili ya wachimbaji wadogo na wawape kipaumbele wale ambao madini haya yamepatikana kwenye maeneo yao.(Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante. Kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Lakini yeye mwenyewe anaelewa kwamba kuna kata tisa. Kwa hiyo ukiangalia idadi ya kata ambazo zinashughulikiwa bado nyingi zitakuwa na matatizo yale yale ambayo yanaendelea na kuwapa shida wananchi.

Je, Serikali, kutokana na umuhimu wa mawasiliano kwa upande wa kiuchumi na kijamii, inatoa tamko gani la kuwapa matumaini kata zile ambazo bado zina matatizo ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya wananchi wa Urambo, na kwa kweli ameonesha ushirikiano mkubwa pale ambapo Serikali inapohitaji msaada wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi, ni kwamba tunatambua kabisa kwamba kuna changamoto ya mawasiliano katika Jimbo hili la Urambo ambapo jimbo hili lenye kata 18; na katika hizo kata 18 kata tisa ndizo ambazo zina changamoto, si kwamba hazina mawasiliano, zina changamoto. Kata hizo ni; Kata ya Uyumbu, Muungano, Vumilia, Busoke pamoja na Songambele. Kata zote hizo tunafahamu kabisa kwamba zina changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Serikali kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidigital tayari tumeanza na kata tatu. kwa hiyo tunaamini kabisa kwamba tunapoenda katika utekelezaji wetu tukishakamilisha kata hizi tatu tunaamini hata zile kata sita ambazo zimebaki tutazifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Swali la kwanza; je, Serikali yetu sikivu ninavyoielewa mimi, haioni umuhimu wa kujenga mahusiano mema kati ya hifadhi na wananchi kwa kuwapa eneo la kuweka mizinga yao na kufuga mifugo yao kama walivyozoea na hasa kutokana na ongezeko la watu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; hivi Serikali haioni kuna haja ya kumaliza suala ambalo linaulizwa kila mwaka kwa kulipatia ufumbuzi wa kudumu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika,
ahsante. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Jimbo la Urambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niahidi tu kwamba tutaangalia maeneo mengine yaliyo jirani na eneo hilo ili warinaji wa asali, hususan wale wafugaji wa nyuki, tuweze kuwahamisha ili tuwapeleke katika misitu ambayo inaendana na uhifadhi wa mazingira yanayohusiana na ufugaji nyuki.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kutokana na tatizo kubwa la kukatikakatika kwa umeme Wilayani Urambo, Serikali inasema nini kuhusu kumaliza ujenzi wa Kituo cha Uhuru ambacho kitakuwa ukombozi kwetu sisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Sitta, Mbunge wa Urambo, kama Ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Kupoza Umeme cha Uhuru kilichopo katika Jimbo la Urambo kinatekelezwa katika mradi tunaouita Mradi wa Gridi Imara ambao unapokea umeme wa kilovoti 33 kutoka Tabora Mjini na mkandarasi tayari ameshapatikana ameshaagiza vifaa, na kabla ya katikati ya mwaka unaokuja tunatarajia Mradi huu wa Gridi Imara utakuwa umekamilika katika maeneo mengi likiwemo eneo la Kituo chetu cha Kupooza Umeme cha Uhuru kwa ajili ya kuhudumia wananchi walioko hapo na kupeleka Gridi ya umeme mpaka katika Wilaya ya Uvinza kupitia pale Uhuru.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Pamoja na kuishukuru Serikali kwa kutuanzishia VETA wilayani Irambo, je, ni lini Serikali itatuongezea majengo ili tupate mafunzo ambayo hatuyapati kutokana na uhaba wa majengo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vyuo hivi vya zamani viko zaidi ya vyuo 44, na ni kweli kabisa vina uhitaji mkubwa wa majengo, vifaa vya kufundishia pamoja na rasilimali watu. Nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kama nilivyokwisha kujibu maswali yaliyotangulia. Kwa upande wa pale Urambo tunajua kwamba chuo kile kina majengo machache ikiwemo na uhaba wa karakana pamoja na mabweni. Katika bajeti yetu ijayo tutahakikisha kwamba tunatenga fedha ili kuongeza miundombinu hiyo ya maabara, karakana pamoja na mabweni kwa ajili ya Chuo chetu cha Urambo. Kwa hiyo tuwasilinae tu Mheshimiwa Sitta ili tuliweke vizuri hili, nakushukuru sana.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kutokana na tatizo kubwa la umeme tulilonalo Wilayani Urambo, ni lini kituo kinachojengwa Kata ya Vumilia eneo la Uhuru litakamilika kama utatuzi wa tatizo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, Kituo cha Uhuru kilichopo Urambo ni mojawapo ya vituo 14 vinavyojengwa katika mradi wetu wa Gridi Imara na kabala ya mwaka huu kuisha kituo hicho kitakuwa kimekamilika kwa sababu tayari mashineumba (transformer) zimeshakaguliwa kiwandani na sasa zimefungwa kwa ajili ya kuja kuwekwa katika kiwanda hicho kwa sababu jengo tayari lilishakamilika na lane inaendelea kujengwa.

Mheshimiwa Spika, hivyo, kabla ya mwaka huu kuisha kitakuwa kimekamilika ili kuweza kuhudumia wananchi. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa mwenyekiti ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa niaba ya Serikali alivyojibu; amejibu vizuri, ahsante.

Swali la kwanza; tuna uhaba wa walimu sita na katibu muhitasi mmoja na uhaba huu unasababisha kwamba mwalimu wa fani moja anapokuwa hayupo hakuna linaloendelea;

Je, Serikali ina mpango gani wa kutuongezea wafanyakazi saba ili shughuli za utoaji wa elimu ya ufundi ziendelee kama zilivyopangwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili jambo muhimu katika mafunzo ya ufundi ni utendaji, yaani practical sasa utendaji au elimu kwa vitendo unahitaji sana vifaa;

Je, Serikali yetu imejipangaje kuhusu upatikanaji wa vifaa ili kweli mafunzo ya ufundi ya vitendo yafanyike?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Margaret Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, Serikali ya Awamu ya Sita imejidhatiti kuhakikisha kwamba vyuo hivi ambavyo vilikuwa havina miundombinu tunaenda kuongezea miundombinu. Na hatukufanya hivi tu kwa chuo hiki cha Urambo peke yake, kuna vyuo kadhaa ambavyo vilikuwa na upungufu wa miundombinu. Tunafahamu upungufu wa miundombinu kwa Mheshimiwa Mwijage kule Muleba, tumeshafanya kazi kule, Mheshimiwa Rais alitoa fedha kwa ajili ya ukarabati pamoja na ujenzi wa miundombinu mingine. Pia kwa Mheshimiwa Dugange kule Wanging’ombe tumefanya hivyo; kwa Mheshimiwa Mtanda Serikali imepeleka fedha vilevile lakini vilevile tumepeleka fedha kule Mikumi kwa Mheshimiwa Londo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hicho tu, katika swali lake la kwanza anataka kufahamu mkakati wa Serikali juu ya walimu. Nimuondoe wasiwasi, Mheshimiwa Rais alitoa kibali cha kuajiri wafanyakazi watumishi wakiwemo na hao walimu 571. Mpaka hivi sasa ninavyozungumza walimu 151 tayari wameshaajiriwa na wameshapelekwa kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo na kwenye baadhi ya hivi vyuo ambavyo vilikuwa tayari vinatoa huduma na vile vyuo vytu 25 vya wilaya na vinne vya mikoa. Kwa hiyo tunaendelea na mchakato huu kwa kukamilisha idadi hii ya waaalimu na watumishi 571 tunaamini na Urambo itafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vifaa naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa na Bunge lako tukufu, tumejidhatiti na kujipanga kwa dhati kabisa kuhakikisha kwamba tunapeleka vifaa kwenye vyuo hhivi vile vya zamani lakini na vile vipya ambavyo tunajenga hivi sasa. Katika bajeti yetu hii inayoendelea tuna package ya vifaa lakini vilevile na katika bajeti ambayo tumeanza kuisoma hapa kutakuwa na eneo la fedha ambayo tumetenga kwa ajili ya ununuzi wa vifaa kwa ajili ya vyuo hivi vya VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itakuja kumaliza migogoro iliyopo kati ya Gereza ya Urambo na wananchi wanaozunguka gereza hilo ambapo migogoro imedumu kwa muda mrefu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili lije kama swali au kama atataka takwimu tutampa.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuishukuru Serikali kwa kutujengea Kituo cha Polisi Kata ya Songambele; je, ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri tutakwenda pamoja Urambo ili ukatatue migogoro kati ya wananchi na Magereza ya Urambo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: MMheshimiwa Spika, nimuombe mama yangu Mheshimiwa Margaret Sitta na nimuahidi kwamba wakati wowote nitakuwa tayari kuambatana naye. Tutaangalia ratiba yetu baada ya Bunge hili ili kwenda kuangalia tatizo lililopo kati ya wanachi na Gereza ili kupata suluhisho la kudumu, nashukuru.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Maswali yangu ni kwamba;

a) Je, ni lini Serikali itafanya tathmini katika kata ambazo hazina mawasiliano ya uhakika ili changamoto ziondolewe nao wapate mawasiliano kama wenzao?

b) Je, ni lini Serikali itaachana na teknolojia ya 2G ili nao waende kisasa 4G na 5G?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote nchini yanapata huduma ya mawasiliano. Kwa upande wa kata ambazo, kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, Serikali inatafuta fedha na fedha zikipatikana tutaenda kufanya tathmini ili kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, kipengele cha pili, kuhusu suala la kuondokana na huduma ya 2G; tunapokuwa na 3G ndani yake 2G imo. Tunapokuwa na 4G ndani yake 2G imo, tunapokuwa na 5G kwa sababu ile ni specific kwa ajili ya voice na hizi zingine ni kwa ajili ya data. Hizi zote zitakuwa zinaenda sambamba na kuhakikisha pamoja na kwamba kuna advancement ya teknolojia lakini hatuwezi kuachana na huduma ya sauti.

Mheshimiwa Spika, huduma ya sauti itaendelea kuwepo hivyo, hatutaweza kuachana kwa sasa kwa sababu ulimwenguni kote huduma ya 2G inaendelea kutumika na sisi kama nchi tutaendelea kuhakikisha kwamba kuna wananchi ambao watakuwa wanaendelea kutumia huduma hiyo basi tutahakikisha kwamba miundombinu ya huduma hiyo itaendelea kuwepo. Ahsante sana.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, sehemu ya pili ya swali la Mheshimiwa Mbunge, nadhani alitaka kujua hiyo huduma ambayo inatolewa sasa, ukiacha hiyo ya voice kama ulivyosema ya 2G, hizo nyingine zitawafikia lini hao wananchi? Ndilo lililokuwa swali la Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, Serikali kuanzia mwaka 2021 tulitoa maelekezo, miundombinu yetu yote ya minara ya mawasiliano inayojengwa, lazima iwe na huduma ya 2G na 3G. Hakuna mnara kuanzia mwaka 2021 ambao umejengwa ukiwa na huduma ya 2G pekeyake.

Mheshimiwa Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, katika jimbo lake la Urambo ambalo hata mimi nimepata kutembelea katika kata zake 12, katika kila mnara unaojengwa sasa hivi Urambo una huduma ya kutoa internet. Nakushukuru sana.

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafai hii.

Je, Serikali itamaliza lini ujenzi wa kituo cha kupozea umeme kinachojengwa katika Kijiji cha Uhuru, wilayani Urambo ili kumaliza tatizo la umeme tulilonalo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, mradi wa kujenga kituo cha kupoza umeme cha Uhuru kilichoko Urambo ni mojawapo ya miradi yetu 14 ya kujenga vituo vya kupoza umeme kwenye Wilaya inayotekelezwa chini ya mradi wetu wa Gridi Imara. Mradi huo tayari umeshaanza na tunatarajia ndani ya miezi kama 12 kuanzia sasa mradi huo pia utakuwa umekamilika katika eneo la Uhuru ili kuhakikisha kwamba umeme unaotoka Tabora kwenda Uhuru kwenda Nguruka basi unawafikia wahitaji kwa wakati.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi ya kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itoe kauli ya changamoto kubwa iliyopo ya mfanyakazi anapandishiwa mshahara vizuri kabisa lakini harekebishiwi mpaka anastaafu, na inampa matatizo ya kupata haki zake. Mheshimiwa hii ni changamoto kubwa naomba Serikali itoe kauli yake. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Sitta Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kwanza kulihakikishia Bunge lako lakini pia kumuhakikishia Mbunge ndani ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunayo idara maalum inayohusika na masuala ya marupurupu, mishahara na nyongeza zote ambazo ni stahiki za mtumishi anatakiwa kupata. Sasa kama wapo watumishi ambao wanachangamoto katika hayo ofisi yetu iko wazi na ningeomba tupate taarifa hizo ili sasa tuweze kushughulikia na wafanyakazi wetu wote waweze kupata haki yao kama ambavyo imeelekezwa katika ratiba yetu. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kutokana na umuhimu wa barabara hiyo katika kuchochea uchumi wa wananchi wa Urambo, ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ikitokea Kahama – Ulyankulu – Urambo – Ussoke – Tutuo – Sikonge ili waendelee wasafiri mpaka Mbeya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kadri tunavyofungua nchi na kuunganisha miji barabara aliyoitaja ni muhimu sana hasa kwa sababu itapunguza sana urefu wanaosafiri watu wa kutoka Kahama na hata watu wanaotoka njia ya Kigoma ambao kama wanaenda Mbeya hawana sababu ya kupita Mjini Tabora. Ndio maana tumesema tunaendelea kuhakikisha kwamba tunafanyia usanifu hiyo barabara ya kutoka Ulyankulu hadi Urambo na kipande cha Ussoke hadi Tutuo ili kuwapunguzia wananchi hawa umbali mrefu wa kusafiri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kinachotakiwa sasahivi tunatafuta fedha sasa ili barabara hii ifanyiwe usanifu na ijengwe kwa kiwango cha lami kwa ajili ya kufungua hilo eneo la Wilaya ya Urambo, lakini pia na kuunganisha na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ahsante.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafsi na mimi niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuishukuru Serikali kwa kutuletea Mradi wa Maji kutoka Lake Victoria ni lini sasa Serikali italeta mabomba ili kazi ianze kwa kasi kutokana na shida ya maji tuliyonayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Sitta kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni lini mabomba yatafika? Mwezi wa saba tunatarajia mabomba yawe yamefika kutoka India na tayari kazi zimeshaanza, wakandarasi wa miji 28 tayari wapo kazini. Nikupongeze kwa ufuatiliaji na nilishakuahidi kwamba tutakwenda pamoja Urambo na kuhakikisha mabomba yanaanza kufanya kazi. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa kuwa wako wananchi ambao huwa wanaumwa na mbwa na kwa kuwa ili kukabiliana na kichaa cha mbwa hutakiwa kuchoma sindano si chini ya tatu, wakati mmoja hadi tano na sindano moja si chini ya shilingi 30,000. Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuondoa gharama hizi ili wananchi wapate sindano hizo bure, kutokana na kwamba wengi hasa vijijini hawana uwezo wa kulipa kiasi hicho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hili swali na hili tatizo la kichaa cha mbwa, Mheshimiwa Mbunge Mama yetu Mama Sitta kwa kweli amekuwa akihangaika nalo hasa kwenye wilaya yake. Mimi niseme, tayari tumeshafanya hesabu kuona kesi za kuumwa na mbwa ziko ngapi nchini na tumeona kwamba inawezekana kugharamia hili kwa Serikali na tumeshatenga bajeti na sasa MSD wameshanunua dawa za vichaa vya mbwa na zimesambazwa sehemu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwaambia Ma-DMO wote na Waganga Wakuu wa Mikoa, wasimamie vizuri kuhakikisha hakuna Mtanzania anayeumwa na mbwa na kucheleweshewa kupata tiba akitafuta fedha kwa ajili ya kupata hiyo sindano. Watibiwe mara moja na wapate sindano hiyo haraka sana. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza: Kwa kuwa ujenzi wa kituo hiki cha umeme umesimama kuanzia mwezi wa Tano mwaka 2022, na kwa taarifa tuliyonayo ni kwamba nguzo zitakazotumika ni za zege: Je, kwanini Serikali isitumie zile nguzo ambazo zimetupwa tangu mwaka 2020 mwezi wa Tano, zitumike kueneza au kusambaza umeme katika maeneo mengine kuliko kuachwa kama zilivyo porini na hata pengine kuzihatarisha na moto na kadhalika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi ambao nguzo hizo za zege zitakazopita wanadai fidia; je, ni lini wananchi hawa watalipwa ili na wenyewe wajiendeleze kiuchumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Margaret Sitta kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba design ya awali ilikuwa inatumia nguzo za miti, lakini baada ya maboresho imeonekana ni vema kubadilisha design hiyo na hivyo tutatumia nguzo nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimwambie Mheshimiwa Margaret, hizi nguzo tutazitumia kwa kadri ya mahitaji. Vile vile nguzo za kupeleka umeme zinatofautiana kulingana na mahitaji. Zile tulizopeleka kule ni za kupeleka msongo mkubwa wa kilovoti 132, ziko zile za msongo wa kilovoti 33 na ziko zile za distribution za kwenye maeneo yetu ya msongo wa kilovoti 400. Kwa hiyo hizi zilizoko kule tukizipeleka kusafirisha na kusambaza umeme kwa wananchi, tutakuwa tunatumia resource kubwa katika maeneo ambayo siyo yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutapata nguzo nyingine kwa ajili ya kuwapelekea wananchi na hizi zitafanya kazi katika maeneo mengine ambapo zinatakiwa kufanya kazi bila kuathiri mahitaji yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili, nadhani wiki hii kabla haijaisha, wale wataalam ambao walikuwa wanafanya survey kwa ajili ya kulipa compansation, wataanza kuonyesha yale majedwali ya wale wanufaika wa compansation kwa wananchi ili waweze ku-verify na kuona kama ndiyo stahiki na baada ya hapo sasa itarudishwa Wizarani kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kusainiwa na kurekebisha upungufu utakaojitokeza. Tunaamini kwamba katika muda mfupi ujao wa mwezi mmoja au miwili basi fidia zitaanza kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Margaret Sitta awaambie wananchi wawe tayari, wiki hii au mwanzoni mwa wiki inayokuja kwenda kukagua zile fidia ambazo wameandaliwa kwa ajili ya kuhakiki ubora wake.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuunga mkono kabisa Dkt. Gwajima mchungaji, ameelezea vizuri. Mimi nina video moja hapa ambayo ukimaliza kujibu maswali tuonane. Hali ni mbaya Tegeta na kuna chanzo chake, ni kwa sababu walipokuwa wanajenga barabara ile ya kwenda Bagamoyo waliziba mifereji. Hali ni mbaya ukirudi hapa Mheshimiwa niruhusu nikuonyeshe video ya hali mbaya iliyoko. Nakupongeza Mheshimiwa kwa kazi uliyofanya hali ni…

MWENYEKITI: Swali?

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali kupitia TANROADS watazibua mifereji waliyoziba walipokuwa wanajenga barabara ya kwenda Bagamoyo? Hali ni mbaya naomba nimuonyeshe na video. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wakati mwingine Serikali inapokuwa inafanya utengenezaji au ukarabati wa miundombinu hasa ya barabara zipo changamoto ndogondogo huwa zinatokea. Siku zote tunapojenga lazima tutabomoa, na tukibomoa lazima kuna kasoro zitajitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuambia Mheshimiwa Mama Sitta kwamba tuko tayari kushirikiana na Wizara inayohusika kwa maana kwamba Wizara nyingine za kisekta. Lengo na madhumuni ni wanapojenga au wanaporekebisha miundombinu ya barabara wahakikishe kwamba wanatengeneza mazingira mazuri ya kupitisha maji ili kipindi cha mvua nyingi maji yaweze kupenya na yaende baharini yasiathiri makazi ya watu, nakushukuru. (Makofi)

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Natumia nafasi hii kuwaelekeza Meneja wa Mikoa TANROADS kote nchini kwenda kwenye maeneo ambayo yana changamoto kama Waheshimiwa Wabunge walivyosema na kuleta haraka iwezekenavyo namna ambavyo tunaweza tukakabiliana na jambo hili kwa dharura, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kuchukua hatua nyingi na kuhakikisha kwamba pembejeo zinazifika kwa wakati; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba cotton twine na jute twine zinafika kwa wakati na pia zinauzwa kwa bei iliyopangwa? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mama Sitta, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kumetokea changamoto msimu huu wa tumbaku cotton twine na jute twine zilichelewa na changamoto ya msingi kwa nini zilichelewa Vyama Vikuu vya Ushirika vilichelewa kupata letter of credit kutoka Taasisi za Fedha, hatukuwa na tatizo hili katika misimu miwili, mitatu iliyopita. Nataka niwaahidi wakulima wa tumbaku na Waheshimiwa Wabunge wote wanaotoka katika maeneo ya tumbaku kama tulivyorekebisha mfumo wa upatikanaji wa mbolea na kufika kwa wakati; tutahakikisha tatizo lililojitokeza mwaka huu la cotton twine na jute twine halitokei kwa sababu tumeshaanza kuongea na viwanda vya ndani vya Watanzania ili viwekeze kwenye eneo la kuzalisha cotton twine kwa sababu pamba inapatikana ndani ya nchi. Majaribio ya awali yameanza Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo waweze kuzalisha cotton twine na tuache kutumia dola milioni nne kuagiza kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie Bunge lako Tukufu kuwataka ginners na wanaoongeza thamani kwenye pamba, Serikali ipo tayari kumpa mwekezaji yeyote concession agreement ya muda mrefu, kwa ajili ya kuzalisha cotton twine na atapata mkataba wa muda mrefu na hatuta-import cotton twine kama atawekeza katika eneo hilo. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itapeleka fedha zaidi katika Chuo cha VETA cha Urambo ili tupate majengo zaidi tuongezee stadi zaidi za ufundi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mama Margaret Sitta, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, chuo chetu kile cha VETA, Urambo katika mwaka wa fedha ule uliopita tulipeleka fedha pale kwa ajili ya kuongeza baadhi ya miundombinu lakini vilevile kufanya ukarabati. Nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Margaret Sitta kwamba katika mwaka huu tena unakuja wa 2024/2025 tutatenga fedha kama tulivyofanya mwaka uliopita kwa ajili ya kuongeza miundombinu lakini vilevile kufanya ukarabati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii tunaifanya kwa Vyuo vyote pale Urambo tumefanya, lakini Wanging’ombe pale tumepeleka fedha, Newala kule napo vilevile tumepeleka kwa hiyo tutafanya kama tulivyofanya mwaka uliopita wa fedha, nakushukuru sana.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wakulima wa tumbaku nao wanapata mbolea ya ruzuku? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; wako wakulima wa tumbaku ambao waliuza tumbaku yao tangu kipindi cha kilimo mwaka 2021. Wameuza tumbaku yao mpaka leo hawajalipwa na wanawadai walionunua zaidi ya shilingi milioni 72. Je, Serikali inawasaidiaje wakulima wa tumbaku wa Urambo ambao jambo hili linawakwaza sana? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mama Samwel Sitta kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madai ya wakulima wa msimu wa 2019/2020 ambapo ni kama jumla ya dola milioni tano kwa Sekta nzima. Nataka tu kumhakikishia cha kwanza Serikali imefutia hizi Kampuni zote ununuzi na ushiriki kwenye Sekta ya Tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; Serikali sasa hivi tuko kwenye hatua za mwisho kuwapeleka Mahakamani kwa ajili ya madai haya ya wakulima. Pia, tunawapeleka Mahakamani pamoja na Wakurugenzi at a personal capacity kwa sababu walikuwa ni guarantor kwenye biashara hii. Kwa hiyo nataka nimhakikishie kwamba Serikali imeendelea kuchukua hatua katika hili na mwaka uliofuata mpaka sasa Kampuni yoyote ambayo imekuwa ikichelewesha malipo ya wakulima tumekuwa hatuiruhusu kuendelea kuwepo katika Sekta ya Tumbaku kwa hiyo tunaendelea kuboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie na ni wahakikishe wakulima wa tumbaku kwamba sasa hivi tumeamua kuwapeleka mahakamani hawa wafanyabiashara na tutachukua hatua ili tuweze ku-recover fedha za wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la ruzuku nataka tu niwahakikishie wakulima wa tumbaku. Katika bajeti yetu mliyotupitishia Waheshimiwa Wabunge mwaka huu, zao la tumbaku tumeliweka kuwa moja ya zao ambalo tunalipatia ruzuku katika uzalishaji kuanzia mwaka ujao wa fedha. Kwa sababu mwaka huu wakulima wa tumbaku wamepata tatizo la mvua nyingi, uzalishaji kwa maana ya quantity haijaathirika lakini ubora wa tumbaku kidogo umeshuka kwa sababu ya mvua nyingi. Serikali imeamua kwamba zao la tumbaku litakuwa sehemu ya subsidy scheme kwenye NPK 10-18-24 yenye thamani ya shilingi bilioni 13 ili kuweza kushusha gharama zao za uzalishaji. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, je, ni lini kituo cha kupozea umeme kinachojengwa eneo la Uhuru, Wilayani Urambo kitakamilika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, Kituo cha Kupoza Umeme cha Uhuru kimeshafikia zaidi ya 97% na kwa sasa hivi tupo katika hatua za kufanya test kwa kutumia jenereta huku tukisubiri line ya kusafirisha umeme inayojengwa na ITDCO ambayo imeshafikia ziadi ya 67% iweze kukamilika. Kwa hiyo, kituo kile kwa kweli kimekamilika kwa zaidi ya 97%. Tunachosubiria ni line ya umeme ambapo pia tunategemea hivi karibuni itakamilika na kituo hiki kuanza kufanya kazi, ahsante.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Jengo la Mahakama ya Mwanzo Wilayani Urambo lina hali mbaya sana. Je, ni lini Serikali itatujengea jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba ni kweli nimeiona Mahakama ya Mwanzo Urambo, hadi picha nililetewa na tumethibitisha kwamba ni mbaya sana. Mahakama imeuweka ukarabati wa Mahakama ya Mwanzo Urambo katika bajeti ya mwaka 2025/2026, nakushukuru.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika barabara inayokwenda Kigoma, Kata ya Vumilia kuna wananchi wa maeneo ya Mbaoni na Motomoto ambao wanaidai fidia Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi ili wabomoe nyumba zao wapishe nguzo za umeme ambazo zinapeleka umeme katika kituo kipya cha kupozea umeme kinachojengwa eneo la Uhuru. Je, ni lini Serikali italipa ili na sisi umeme ufikishwe katika kituo chetu kinachojengwa? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mama Margaret Sitta, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia huwa ni sehemu ya gharama ya mradi. Kwa hiyo, naependa kumhakikishia Mheshimiwa Margaret Sitta pamoja na wananchi wake kwamba waendelee kuwa na subira. Mradi husika utakapokuwa unatekelezwa, basi sehemu ya gharama hiyo ni suala la hizi fidia. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alifika Urambo kuangalia Kituo chetu cha Kupozea Umeme kinachojengwa sehemu ya Uhuru. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri naweza kutwambia lini kituo kile kitaisha ili na sisi tupate umeme kwa sababu tuna tatizo kubwa sana la umeme Urambo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia Kituo hiki cha Uhuru. Kituo cha Uhuru kipo katika hatua za kwenda kumalizika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunakisimamia kwa hali na mali kuhakikisha kinakamilika na kinaanza kuwanufaisha watu wa Urambo. Kwa hiyo, kwa sababu kimeenda vizuri sana na hata fidia watu wa eneo la Urambo wamelipwa, nimweleze Mheshimiwa Mbunge azma ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wa Urambo wanaendelea kupata umeme wa uhakika na tutasimamia Kituo hiki kimalizike ili wananchi wako wa Urambo waweze kupata umeme wa uhakika zaidi.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali; nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza, ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu aliyotoa. Swali la kwanza; kutokana na ile hali ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuwa ndani ya majengo ya Halmashauri ya Wilaya. Je, Serikali haioni kuwa, kuna umuhimu wa kujenga haraka sana ili kutenganisha mamlaka hizi mbili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kutokana na majengo yaliyopo sasa hivi yaliyojengwa mwaka 1974 maana yake ni miaka 50 iliyopita. Je, Serikali haioni kuna umuhimu sasa wa kutujengea majengo ya kisasa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge amefuatilia mara kadhaa kuhusiana na uhitaji wa kujenga majengo haya mawili; Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Urambo, pamoja na jengo la halmashauri.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo, kwa hiyo, lile jengo la ofisi Mheshimiwa Waziri Mkuu amelitumia na sisi tumetoa kipaumbele kuhakikisha kwamba mwaka ujao wa fedha tunaanza ujenzi wa jengo la Ofisi ya Wilaya ya Urambo ili liwe la kisasa na kutoa huduma bora kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nimhakikishie tu kwamba, jengo la halmashauri litakalojengwa pamoja na jengo la Mkuu wa Wilaya ni majengo ya kisasa na ndio maana ombi la fedha shilingi bilioni 5.75 ni majengo yale ya kisasa ya ghorofa ambayo tunaamini yatatoa huduma bora kwa wananchi. (Makofi)