Primary Questions from Hon. Joseph Kasheku Musukuma (25 total)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU (K.n.y. JOSEPH K. MUSUKUMA) aliuliza:-
Hospitali ya Geita imefanywa kuwa Hospitali ya Mkoa tangu tarehe 8 Januari, 2016:-
Je, ni lini DMO aliyekuwa akiongoza Hospitali hiyo atahamia katika hospitali iliyopendekezwa na kikao cha RCC kuwa Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, licha ya kupandisha hadhi ya Hospitali ya Wilaya ya Geita kuwa Hospitali ya Mkoa lakini bado inaendelea kuwa ya Wilaya hadi tarehe 1 Julai, 2017 itakapokabidhiwa rasmi. Hivyo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Geita (DMO) bado anaendelea kuwa msimamizi wa hospitali hii hadi kipindi hicho itakapohamia rasmi ngazi ya Mkoa na kusimamiwa na Mganga Mkuu wa Mkoa.
Mheshimiwa Spika, halmashauri inaendelea na taratibu za kupendekeza kituo cha afya ambacho kitapandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya katika kipindi cha mpito wakati taratibu za kujenga Hospitali ya Wilaya zinafanyika. Natoa wito kwa halmashauri kuwasilisha pendekezo hilo mapema katika vikao vya kisheria ili liweze kujadiliwa na hatimaye kuwasilishwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kupata ridhaa.
MHE. COSTANTINE J. KANYASU (K.n.y MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA) aliuliza:-
Mkandarasi wa REA anayefunga umeme katika Jimbo la Geita Vijijini amemaliza tatizo na yule anayeunganisha kutoka Sengerema yupo pole pole sana.
Je, ni lini sasa Serikali itamsimamia kikamilifu mkandarasi huyo ili aweze kumaliza kazi hiyo na umeme uweze kuwashwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Musukuma Joseph Kasheku, Mbunge wa Geita Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa REA Awamu ya II katika Mkoa wa Geita likiwemo Jimbo la Geita Vijijini unatekelezwa na mkandarasi Nakuroi Investiment Company Limited. Kazi ya kupeleka umeme Geita inajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 161.5; ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 119.2; ufungaji wa transfoma 49 za ukubwa mbalimbali. Pamoja na hayo pia kuunganisha umeme wateja wa awali 2,560 na kazi za mradi zimekamilika kwa asilimia 94 ambapo ujenzi wa laini kubwa umekamilika kwa asilimia 100 na ujenzi wa laini ndogo umekamilika kwa asilimia 84. Kadhalika ufungaji wa transfoma 29 zimefungwa na wateja 846 wameunganishiwa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, umeme umeshafika Nyamadoke kutoka Sengerema Mkandarasi ameelekezwa sasa kuhakikisha kwamba, kazi zote za kuunganisha zinakamilika ifikapo mwezi June mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, REA pamoja na TANESCO wameongeza kasi sasa ya kumsimamia Mkandarasi huyu ili kuhakikisha kwamba kazi za ujenzi zinakamilika ifikapo Juni mwaka huu.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Mgodi wa GGM – Geita unaongoza kwa kuwapiga vijana na kuwachapa viboko na pengine kuwasababishia vifo, lakini wahusika hawachukuliwi hatua stahiki.
Je, Serikali inachukua hatua gani sasa dhidi ya wahusika pale inapotokea wameua watu au kujeruhi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwepo na vitendo vya uonevu na matukio kadhaa baina ya wamiliki wa Mgodi wa GGM na wananchi wanaozunguka mgodi huo. Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikichukua hatua stahiki kwa watuhumiwa mara tu taarifa zinapotolewa polisi. Mathalani, tarehe 14/2/2016 majira ya saa 07.15 ndani ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita, watu wawili walijeruhiwa kwa kupigwa risasi za mpira wakiwa wanaondolewa na mlinzi ambapo mtuhumiwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi Na. CC67/2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kwenye Bunge lako hili Tukufu kutoa rai kwa wananchi wanaozunguka mgodi wa Geita kuheshimu sheria na taratibu ili kuepuka vitendo vya kuvamia mgodi vinavyoweza kusababisha madhara kwao.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA (K.n.y. MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA) aliuliza:-
Sheria ya madini inawataka wachimbaji wakubwa kama vile GGM - Geita, kila miaka mitano wamege sehemu ya maeneo na kuyarudisha kwa wananchi.
(a) Je, ni lini Serikali itawarudishia wananchi maeneo ya Sami na Nyamatagata yaliyoombwa na wananchi kupitia vikao vyote hadi Mkoani?
(b) Je, ni lini eneo la STAMICO - Nyarugusu litafanywa kuwa la wachimbaji wadogo wadogo kama ambavyo Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alivyokwisha tamka mara mbili?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, lililoulizwa na Mheshimiwa Bukwimba Mbunge wa Geita Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya maeneo ya Sami pamoja na Nyamatagata yamo ndani ya leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini ya dhahabu ya kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) kupitia leseni namba SML 45/99. Hata hivyo Serikali inaendelea na mazungumzo na mgodi huo ili kampuni hiyo iweze kuachia baadhi ya maeneo yasiyohitajika kwa ajili ya kuwamilikisha wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la STAMICO na Nyarugusu lipo kitongoji za Buziba lina leseni ya utafutaji Na. PL 6545/2010 inayomilikiwa kwa ubia wa asilimia 45 na 55 kati ya STAMICO na kampuni ya TANZAM 2001, eseni hii itaisha muda wake tarehe 11 Julai 2018. Kwa kuwa eneo la Nyarugusu bado linamilikiwa na STAMICO pamoja na mbia wake ambapo Serikali pia ni mmiliki, Serikali inafanya mazungumzo na wamiliki hawa ili eneo hilo liachiwe sasa kwa ajili ya kumilikishwa wachimbaji wadogo wa eneo hilo.
MHE. MUSUKUMA J. KASHEKU Aliuliza:-
Wakala wa Misitu Tanzania amehamisha vigingi vya mipaka ya misitu vilivyowekwa tangu mwaka 1974 na kuviweka katikati ya vijiji kwa kufuata ramani ya mwaka 1984, vijiji ambavyo vina GN ya Serikali na vinatambuliwa na hata Mheshimiwa Rais amezuia zoezi hilo, lakini hakuna
kilichofanyika hivyo kuwafanya wananchi wa vijiji hivyo kuishi maisha ya mashaka na sintofahamu.
Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Musukuma Joseph Kasheku, Mbunge wa Geita, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Msitu wa Hifadhi wa Geita wenye ukubwa wa hekta 47,700 ulisajiliwa kwa ramani namba Jb 146 ya mwaka 1952 na ulitangazwa rasmi kwa Tangazo la Serikali Namba 110. Sehemu kubwa ya msitu huu ipo kwenye miteremko ya milima ya Geita inayozunguka mji wa Geita sehemu ya Magharibi, Kaskazini na Kaskazini Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1984 Serikali ilifanya mapitio ya soroveya ya mipaka ya msitu kwa lengo la kuweka alama kwa kutumia ramani iliyoanzisha msitu huo. Katika mapitio hayo ilibainika kuwa mpaka halisi wa msitu kwa mujibu wa sheria umepita katikati ya vijiji vilivyoanzishwa na kusajiliwa mwaka 1974 wakati wa operation vijiji. Alama za mipaka zikawekwa kufuata mpaka huu halisi na hivyo kusababisha eneo ambalo wananchi walikuwa wameanza kuishi na kufanya shughuli za kibinadamu na baadaye kusajiliwa kuwa vijiji kuangukia ndani ya eneo la msitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kubaini tatizo hilo Serikali haijafanya operation yoyote ya kuwaondoa wananchi katika maeneo hayo, bali ipo katika mjadala unaotafuta njia za kutatua tatizo hili bila ya kuleta athari hasi na kubwa kwa maisha ya wananchi. Aidha, Mheshimiwa Mbunge anashauriwa kuwa na subira wakati Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea kutafuta suluhisho la mkanganyiko uliojitokeza kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
(a) Je, ni utafiti gani umefanyika katika Ziwa Victoria mpaka kufikia hatua ya kuzuia uvuvi wa aina yoyote kwa kisingizio cha uvuvi haramu?
(b) Je, ni sheria gani inatumika kukamata nyavu na ndani ya dakika kumi zinachanwa bila ya kumpa mvuvi nafasi ya kujitetea?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali haijazuia uvuvi wa aina zote kufanyika katika Ziwa Viktoria. Uvuvi unafanyika nchini kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 pamoja na sheria nyingine za nchi yetu. Aidha, kwa sasa Serikali inapambana na uvuvi haramu katika Ziwa Viktoria kama ilivyo katika maeneo mengine kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, upo utaratibu wa kisheria wa kukamata na kuharibu zana za uvuvi zinazotumika katika uvuvi haramu. Taratibu hizo zimeelezwa vizuri kwenye Kanuni Na. 50(1), (2) na (5) ya Kanuni za Uvuvi za mwaka 2009. Aidha, nyavu haramu huteketezwa kwa idhini ya Mahakama baada ya taratibu zote za kisheria kufuatwa.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA (K.n.y. MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA) aliuliza:-
Katika kutekeleza Mkataba wa Corporate Social Responsibility (CSR), Mgodi wa GGM unatumia bei za manunuzi kutoka nchi ya Afrika Kusini, mfano bei ya bati moja ni shilingi 81,000 na bei ya mfuko wa saruji ni shilingi 48,000.
Je, kwa nini Serikali isiziite pande hizi mbili, Mgodi wa GGM na Halmashauri ili iweze kumaliza mgogoro huo na kuweka utaratibu mzuri?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijijini kama lilivyoulizwa na Mheshimiwa Bukwimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza matakwa ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 kifungu cha 105, Halmashauri ya Mji wa Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita pamoja na Mgodi wa Dhahabu wa GGM zimeandaa Mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii wa mwaka 2018 (Corporate Social Responsibility Plan, 2018).
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuandaa mpango huo uliokuwa shirikishi, GGM iliwasilisha bei ya bati la geji 28 kwa kipimo cha mita za mraba ambapo bei ya mita moja ya mraba ilikuwa ni shilingi 81,000 na bei ya mfuko wa saruji ilikuwa ni shilingi 48,000 kwa mfuko mmoja. Aidha, baada ya bei hizo zilizopendekezwa na mgodi kuonekana kuwa ni kubwa, pande zote mbili ambazo ni Halmashauri ya Mji wa Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita pamoja na Kampuni ya GGM walikaa na kufanya majadiliano ya pamoja na kukubaliana bei zilizopendekezwa na GGM zirekebishwe kwa kuweka bei ya bati moja na siyo bei ya bati kwa mita za mraba ambapo bati moja geji 28 ilikubalika kuwa shilingi 27,000 na mfuko mmoja wa saruji kuwa shilingi 18,000.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Je, ni lini Mgodi wa GGM utawasilisha bajeti yake ya kuhudumia jamii katika Baraza la Madiwani la Geita ili tuweze kuangalia kipaumbele chao na kuwapa vipaumbele vya Halmashauri ya Geita?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, napenda sasa nijibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 105(1)(2) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na mabadiliko yake ya mwaka 2017 kinamtaka mmiliki wa leseni chini ya kifungu cha 7 cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kuandaa Mpango wa Mwaka wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR). Mpango huo lazima ukubalike kwa pamoja na Mamlaka ya Serikali za Mtaa husika kwa kushauriana na Waziri anayehusika na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Waziri anayehusika na Fedha.
Mheshimiwa Spika, mpango huo unapaswa kuzingatia masuala ya mazingira kijamii, kiuchumi na shughuli za tamaduni zilizopewa kipaumbele katika Mamlaka ya Serikali za Mtaa ya jamii inayozunguka mgodi.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 105(3), mmiliki wa leseni anapaswa kuwasilisha kwa Mamlaka ya Serikali za Mtaa husika mpango huo aliouandaa kwa ajili ya kufanyiwa tathmini na kupata idhini kutoka kwa Baraza la Madiwani wa Halmashauri. Aidha, kila halmashauri uliopo mgodi inapaswa kuandaa mwongozo wa utoaji wa huduma kwa jamii kwenye Halmashauri yao, kusimamia utekelezaji wake na kutoa elimu kwa wananchi wa wilaya husika juu ya huduma hizo.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa Mgodi wa GGM, kwa kushirikiana na halmashauri mbili za Geita Mji na Wilaya ya Geita, umeweza kutekeleza mchakato wa kuandaa mpango wake wa kusaidia jamii (CSR) kwa mwaka 2018 kama sheria inavyotaka. Mchakato huo umehusisha wataalam kutoka halmashauri zote mbili na wataalam wa Sekretarieti ya Mkoa.
Mheshimiwa Spika, mpango wa miradi iliyotambuliwa na halmashauri hizo kama vipaumbele umeshawasilishwa kwenye Mgodi wa GGM na umesharidhiwa na mgodi. Mgodi wa GGM unatarajia kutumia takribani shilingi bilioni 9.124 katika kutekeleza miradi iliyo chini ya mpango wa CSR. Kiasi cha shilingi bilioni moja kitatumika kutekeleza miradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, takribani shilingi bilioni 6.824 zitatumika kutekeleza miradi katika Halmashauri ya Mji wa Geita na takribani shilingi bilioni 1.3 zitatumika kutekeleza miradi katika Halmashauri za Bukombe, Chato na Mbogwe.
Baada ya taratibu zote kukamilika, mpango huo utawasilishwa katika Baraza la Madiwani ili uweze kuidhinishwa. Miradi iliyokubaliwa na wadau wote kwa mwaka 2018 itaanza kutekelezwa kabla ya mwezi Juni, 2018.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Halmashauri ya Geita DC ina Majimbo mawili ya Geita Viijini na Busanda ambayo kiutawala husababisha usumbufu na hali tete kwa wananchi kijiografia na mkoa ulishapitisha kuomba Serikali iigawe kuwa na Halmashauri ya Busanda:-
Je, ni lini Serikali itaridhia ombi hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura Na. 287 (Mamlaka za Wilaya) na Sura Na. 288 (Mamlaka za Miji) pamoja na Mwongozo wa Serikali kuhusu Uanzishaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wa Mwaka 2014, mapendekezo ya kuigawa Halmashauri yanapaswa kujadiliwa kwanza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kisha kuwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa uamuzi.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeshajadili suala hili katika Kikao cha Baraza la Madiwani ingawa bado halijapelekwa kwenye Vikao vya Ushauri vya Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC). Mara mchakato utakapokamilika na maombi kuletwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tathmini itafanywa na kuona kama kuna haja ya kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Mheshimiwa Spika, aidha, kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano ni kuimarisha maeneo yaliyokuwa yameanzishwa ili yaweze kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa badala ya kuendelea kuanzisha maeneo mapya ambayo hayaondoi kero ya kusogeza huduma kwa wananchi.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Meli ya MV Chato inafanya safari zake kati ya Chato, Senga, Mshalamba, Izumacheli na Nkome. Inapofika Izumacheli huegesha kwenye jiwe kutokana na kukosekana kwa gati:-
Je, ni lini Serikali itajenga Gati katika Kijiji cha Izumacheli?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHATA J. NDITIYE): alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano ina mkakati wa kuhakikisha kuwa huduma za usafiri zimeboreshwa katika maeneo yote nchini, huku kipaumbele kikiwekwa kwenye maeneo yenye mahitaji maalum na pia maeneo yenye kuchochea kwa haraka shughuli za kiuchumi. Kwa kutambua hilo Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) pamoja na TEMESA imeandaa programu ya namna bora ya uboreshaji wa huduma za usafiri katika Ziwa Viktoria (Lake Victoria Modernisation Programme) kwa lengo la kubaini maeneo yote yanyohitaji ujenzi wa ama bandari au gati.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mpango huu unaendelea ambapo ujenzi wa gati, maghala ya kuhifadhia mizigo na majengo ya abiria katika Bandari za Magarini ambayo iko Muleba na Nyamirembe ambayo iko Chato, Mwigobero ambayo iko Musoma na Lushamba ambayo iko Geita unaendelea. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Izumacheli Mkoani Geita kuwa, Serikali inatekeleza mpango wake kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha hivyo, Serikali itatoa kipaumbele kwa eneo hili awamu zinazofuata, ili kuruhusu kukamilika kwanza kwa miradi iliyokwishaanza katika Ziwa Victoria.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali inahamasisha kilimo cha pamba kwa wananchi huku ikiwa haina uwezo wa kupeleka dawa za kuulia wadudu na zinapopatikana huwa ni chache?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Musukuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza si sahihi kusema kuwa Serikali inahamasisha kilimo cha pamba ikiwa haina uwezo wa kupeleka sumu za kuulia wadudu na hata zinapopatikana huwa ni chache. Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha mazao yote ikiwemo zao la pamba ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kama sehemu ya utekelezaji wa hamasa za kilimo cha pamba, katika msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 eneo la ekari 1,488,406 lililimwa na kuzalisha kiasi cha tani 132,961. Chupa milioni 4.6 za viuadudu zenye thamani ya shilingi bilioni 16.8 na vinyunyizi 15,300 vyenye thamani ya shillingi milioni 462 vilinunuliwa na kusambazwa mwaka huo. Aidha, katika msimu wa 2018/2019 eneo la ekari 1,865,000 lililimwa na kuzalisha kiasi cha tani 222,725 ambapo chupa milioni 6 za viuadudu vyenye thamani ya shilingi bilioni 29 na vinyunyizi 23,000 vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.8 vilinunuliwa. Vilevile, katika msimu wa 2019/2020 eneo la ekari 1,786,890 lililimwa na kuzalisha kiasi cha tani 350,473 ambapo chupa milioni 8.2 zenye thamani ya shilingi bilioni 41 na vinyunyizi 20,000 vyenye thamani ya shillingi bilioni 1.6 vilinunuliwa.
Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2017/2018 jumla ya ekapaki 965,300 na vinyunyizi 3,302 vilisambazwa katika Mkoa wa Geita. Aidha, jumla ya ekapaki 736,345 na vinyunyizi 3,020 vilisambazwa katika mkoa huo katika msimu wa 2018/2019. Kwa msimu wa 2019/2020, Mkoa wa Geita umekwisha kusambaziwa kiasi cha ekapaki 8,748 na usambazaji bado unaendelea.
Mheshimiwa Spika, uchache wa viuadudu vya zao la pamba umechangiwa na baadhi ya wakulima kutumia viuadudu katika kupulizia mazao mengine kama vile mahindi na viazi vitamu ili kudhibiti viwavijeshi. Vilevile, kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya viongozi wa vijiji katika baadhi ya maeneo ukiwemo Mkoa wa Geita ambapo viuadudu havikupelekwa kwa wakulima na badala yake kuuzwa katika maduka ya pembejeo kinyume na taratibu za usambazaji wa viuadudu vya zao la pamba. Watu zaidi ya 12 walikamatwa na kati yao 9 walifunguliwa mashtaka ambapo watu nane (8) walihukumiwa kifungo cha miezi sita jela kila mmoja. Serikali itaendelea kufuatilia upatikanaji wa viuadudu vya zao la pamba na kuhakikisha vinawafikia wakulima kwa wakati.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Je, ni kwa nini mgodi wa GGM umegoma kulipa deni la Halmashauri ya Geita la Dola za Kimarekani 800,000?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Geita pamoja na Wilaya ya Geita, kwa pamoja zilikuwa zikidai kiasi cha dola za Kimarekani 800,000, kwa mujibu wa Mkataba wa Maendeleo ya Uwekezaji wa Madini yaani MDA ulioingiwa na Serikali pamoja na Kampuni ya Mgodi ya GGM mwaka 1999. Deni hilo lilitokana na kutokulipwa kwa ushuru wa huduma kiasi cha dola za Kimarekani 200,000 kila mwaka kwa malimbikizo ya miaka minne kuanzia mwaka 2000 - 2003.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Madini, ilielekeza Mgodi wa Dhahabu wa Geita kulipa deni hilo kwa Halmashauri ya Mji wa Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili fedha hizo ziweze kuboresha huduma za jamii na za kiuchumi katika Halmashauri hizo. Aidha, tarehe 26 Oktoba, 2018, Mgodi wa Geita Gold Mining ulilipa deni lote lililokuwa likidaiwa kiasi cha Sh.1,814,249,519.99.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchanganuo wa malipo hayo ya ushuru wa huduma yaani service levy ni kiasi cha Sh.1,296,462,706.99 zililipwa kwa Halmashauri ya Mji wa Geita na kiasi cha Sh.517,786,813 zililipwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Kituo cha Polisi Nkome kina Askari wa kiume pekee hivyo hata huduma kwa akina Mama ikiwemo upekuzi hufanywa na Askari wa kiume:-
Je, ni lini sasa Serikali itapeleka askari wa kike katika kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vituo vidogo vya Polisi Nkome, Nyamboge, Kakubilo na Nzela ni vituo vilivyo katika maeneo ambayo yanakaribiana na kutokana na changamoto za mazingira magumu na ukosefu wa mazingira rafiki, vituo hivi kwa sasa havina Askari wa Kike ambao wanaishi na kufanya kazi. Hata hivyo, vituo hivi kupata doria maalum kila mara kutoka Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Geita ambapo Askari wa Kike na Kiume hufika na kutoa huduma za kiusalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, endapo kuna mtuhumiwa wa kike amekamatwa katika vituo hivi vidogo hufanyika utaratibu wa kumpata mgambo wa kike wa eneo hilo au mwanamke yeyote mtu mzima mwenye busara anayepatikana kwa urahisi katika maeneo hayo kama ambavyo PGO 288 (8), (a) inavyoelekeza, ambapo hufanya upekuzi kwa mtuhumiwa huyo mwanamke.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kweli kuwa watuhumiwa wa kike hupekuliwa na Askari wa Kiume, Serikali itapeleka Askari wa Kike pindi mazingira ya utendeji kazi hususan makazi yatakapokuwa yameboreshwa.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA Aliuliza:-
Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya michezo ya kubahatisha maarufu kama bonanza kulipiwa kodi ya shilingi laki moja tu kwa mwezi na kutolipa Service Levy kwa Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Musukuma Joseph Kasheku, Mbunge wa Geita, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, michezo ya kubahatisha hapa nchini inasimamiwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania kupitia Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura Namba 41 ya mwaka 2003. Sheria hii inatambua kuainisha michezo mbalimbali ya kubahatisha ikiwemo michezo ya slot machines na imeainisha kodi na tozo iliyopaswa kulipwa kwa kuzingatia aina ya mchezo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya michezo ya slot machine, maarufu kwa jina la bonanza, inalipiwa service levy ya asilimia 0.03 ya mapato ya mwaka yanayotokana na michezo hiyo. Tozo hiyo hukusanywa na mamlaka ya Serikali za mitaa. Hivyo basi michezo ya slot machine inalipiwa service levy kwa mujibu wa sheria iliyopo.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Je, ni lini barabara za kutoka Rubanga – Isulwabutundwe – Mkoba -Kukuruma – Kamhanga - Kishinda na Mkolani zitatengewa fedha na TARURA kwa ajili ya ujenzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Musukuma Joseph Kasheku, Mbunge wa Geita Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vilivyotajwa vinaunganishwa na barabara za Mkoba Bridge – Isulwabutundwe – Lubanga yenye urefu wa kilometa 15 na Geita – Isamilo – Mkolani kwa maana ya Busekeseke yenye urefu wa kilometa 18 ni barabara muhimu sana kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2020/2021 barabara hizi zimetengewa jumla ya fedha shilingi milioni 318.83 kwa ajili ya matengenezo ya kilometa 33 na wakandarasi wanaendelea na utekelezaji wa kazi. Kazi zinatarajiwa kukamilishwa mwezi Julai mwaka, 2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini itaendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuzifanyia matengenezo barabara zote zilizopo Wilaya ya Geita Vijijini kwa kulingana na upatikanji wa fedha.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Mradi wa Maji ambao ulishafanyiwa upembuzi yakinifu kwa Wananchi wa Vijiji vya Nkome, Mchangani, Katome, Nyamboge, Nzera na Rwezera?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijiji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi wa maji ambao utahudumia Vijiji vya Nkome, Mchangani, Katome, Nyamboge, Nzera na Rwezera utaanza katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022. Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 mradi huo umetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kuanza kazi ambazo itahusisha ujenzi wa chanzo cha maji na kituo cha kusukuma maji kwa maana ya booster; ulazaji wa bomba zaidi ya kilometa 70, ujenzi wa matanki ya kuhifadhia maji pamoja na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji. Aidha, mradi huo umepangwa kunufaisha Vijiji vingine vya Mnyala, Ihumilo, Nyambaya, Nyakazeze, Itale, Njingami, Lukaya, Chelameno, Bugando, Igate, Bweya, Idosero na Nyarubanga.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Sekondari Bugando iliyopo Tarafa ya Bugando na Shule ya Sekondari ya Rubanga iliyopo Tarafa ya Isulwabutundwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Jimbo la Geita, kama ifuatavyo: -
Mheshimwa Naibu Spika, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Geita pamoja na wadau wa elimu imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Sekondari Bugando iliyopo katika Kata ya Nzera, Tarafa ya Bugando katika Jimbo la Geita. Shule hii imepata kibali cha kuanzisha Kidato cha Tano na Sita mwaka 2021 kwa michepuo ya PCM na PCB na imepangiwa wanafunzi wa kiume 124 wataoanza kuripoti mnamo tarehe 03 Julai, 2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea na upanuzi wa Shule ya Sekondari Lubanga iliyopo katika Kata ya Isulwabutundwe, Tarafa ya Bugando ili iweze kuwa na Kidato cha Tano na Sita. Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa upo katika hatua ya ukamilishaji na ujenzi wa matundu 12 ya vyoo unaendelea. Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa elimu inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa bweni.
Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imekamilisha ujenzi wa madarasa 4 na ununuzi wa viti 160 na meza 160 katika Shule ya Sekondari Kakubilo na inaendelea na ujenzi wa bweni na bwalo la chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya Shule za Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita na itazipatia kibali cha kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita mara baada ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu muhimu.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara yenye urefu wa kilometa 20 kutoka Nkome hadi Nzera?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Musukuma Joseph Kasheku, Mbunge wa Geita Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Nzera – Nkome ni sehemu ya Barabara ya Geita – Nzera hadi Nkome yenye urefu wa kilometa 54 inayounganisha Mji wa Geita ambayo ni Makao Makuu ya Mkoa na Miji Midogo ya Nzera, Nkome na Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kuandaa makabrasha kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina Barabara yote kutoka Geita – Nzera hadi Nkome (kilometa 54) kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 2,000 kwa ajili ya maandalizi ya kuanza ujenzi. Baada ya usanifu kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea na maandalizi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iweze kuendelea kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka huu wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 1,162 zimetengwa kwa kazi hiyo. Ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU K.n.y. MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi waliohamishiwa Halmashauri mpya Nzera?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Musukuma Joseph Kasheku Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitenga kiasi cha Shilingi Milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ambapo ujenzi wa nyumba hiyo unaendelea na upo katika hatua ya upauaji.
Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Wilaya ya Geita imetengewa kiasi cha Shilingi Milioni 240 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili (2) za Wakuu wa Idara.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Halmashauri nyingine kote nchini zenye upungufu wa nyumba za watumishi kuendelea kutenga bajeti za mapato ya ndani kila mwaka ili kutatua changamoto za upungufu wa nyumba za watumishi. Ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA K.n.y. MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza: -
Je, ni lini ujenzi wa barabara ya kutoka Kata ya Katoma kwenda Nyambaya utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Jimbo la Geita, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Katoma kwenda Nyambaya ina urefu wa kilomita 6.3 ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilianza utekelezaji wa ujenzi wa barabara hii kwa kujenga makalavati manne kwa gharama ya shilingi milioni 22.40 kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itatenga bajeti ya Shilingi Milioni 67.2 kuendelea na ujenzi wa barabara hiyo kupitia fedha za Mfuko wa Barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha katika bajeti zake za kila mwaka kwa ajili ya matengenezo na ujenzi wa barabara za Wilaya ya Geita ikiwemo barabara ya Katoma hadi Nyambaya kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itarudisha hekta elfu nane zilizopo kwenye Pori la Ruande Jimbo la Geita kwani pori hilo limepoteza sifa ya kuwa Hifadhi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Msitu wa Hifadhi Ruande ulianzishwa kwa GN Na.106 ya mwaka 1956 una ukubwa wa Hekta 15,550. Msitu huu unaosimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita umekuwa ukivamiwa kwa shughuli za kilimo na ufugaji unaofanywa na wananchi wa vijiji 13 vinavyouzunguka.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilipokea maombi kutoka katika Vijiji viwili (2) vya Kagu na Kakubilo ya kumegewa sehemu ya hifadhi hiyo kwa shughuli za kilimo. Serikali inayafanyia tathmini maombi hayo kupitia Kamati ya Mawaziri Nane wa Kisekta inayoshughulikia migogoro ya vijiji 975 nchini kote na itatoa maamuzi muafaka kwa kuzingatia maslahi ya pande zote.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za ujenzi wa hosteli katika Shule ya Sekondari ya Rubanga ili iwe ya kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Jimbo la Geita, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuwezesha shule za sekondari kuwa za kidato cha tano na sita ikiwemo upelekaji wa walimu wenye sifa na taaluma stahiki, ujenzi wa miundombinu ya mabweni na madarasa pamoja na upelekaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Kuanzisha shule ya kidato cha tano na sita kunategemea pia eneo, pamoja na uhitaji kulingana na wingi wa wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na itatekeleza kulingana na uhitaji na upatikanaji wa fedha. Aidha, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita tayari ina shule tatu za kidato cha tano na sita za Kamena, Butundwe na Bugando, naomba kuchukua fursa hii kumshauri Mheshimiwa Mbunge tuimarishe shule za kidato cha tano na sita zilizopo ili kuendelea kupokea wanafunzi kulingana na uhitaji kwa sasa.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa barabara ya kilometa tatu kwa kuanzia katika Halmashauri ya Geita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Musukuma Joseph Kasheku, Mbunge wa Jimbo la Geita, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha Lami nyepesi kilomita moja katika eneo la Nzera.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango uliopo ni kuendelea kuweka kwenye mipango na bajeti ya kila mwaka ili kuweza kukamilisha ujenzi wa kilometa tatu ifikapo mwaka 2025.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Je, ni kwa nini miradi ya CSR katika Halmashauri ya Geita haikamiliki licha ya kupokea shilingi bilioni 18 kila mwaka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imekuwa ikipata miradi ya Uwajibikaji wa Makampuni ya Madini kwa Jamii (CSR) yenye thamani ya shilingi bilioni 4.3 kila mwaka kuanzia mwaka 2018. Jumla ya shilingi bilioni 25.8 zimepokelewa hadi kufikia Disemba, 2023. Jumla ya miradi 819 imetekelezwa, kati yake, miradi 661 ni miradi ya elimu, miradi 124 ya afya, miradi tisa ya kilimo, na miradi 25 ya sekta mbalimbali. Aidha, miradi 653 imekamilika sawa na asilimia 80.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya miradi inayotekelezwa kwa mfumo wa Uwajibikaji wa Makampuni ya Madini kwa Jamii (CSR) kutokukamilika kwa wakati kunakosababishwa na kwanza, kupanda kwa gharama za vifaa sokoni, pili, manunuzi ya vifaa kufanywa na makampuni yenyewe na baadhi ya maeneo ya miradi kutopitika hususani nyakati za mvua. Serikali imetunga Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii za mwaka 2023. Kufuatia Kanuni hizi, Kamati ya wataalamu imeundwa ambayo itakuwa inapitia miradi na kushauri namna bora ya utekelezaji, ahsante.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Je, lini Serikali itatoa kipaumbele cha ujenzi wa nyumba za Watumishi wa Halmashauri mpya ikiwemo Geita DC?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2023/2024, Serikali imetoa shilingi bilioni 48.66 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 201 za Wakurugenzi na Wakuu wa Idara. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 13.85 zilitolewa kwa halmashauri mpya 31 zilizohamisha makao makuu kwenda kwenye maeneo yao ya utawala ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Geita iliyopokea shilingi milioni 390 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba tatu za Wakuu wa Idara na moja ya Mkurugenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Mamlaka za Serikali za Mitaa zimetengewa shilingi bilioni 1.30 kwa ajili ya ukamilishaji wa nyumba 24 za Wakurugenzi wa halmashauri na shilingi bilioni 6.72 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 35 za Wakuu wa Idara. Hadi kufikia Machi, 2024 jumla ya nyumba 97 za Wakurugenzi na Wakuu wa Idara zilikuwa zimekamilika. Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi katika Halmashauri ya Geita, ahsante.