Supplementary Questions from Hon. Seif Khamis Said Gulamali (31 total)
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tumekuwa tunapata taarifa za Serikali juu ya kuanza kwa mradi huu kila mwaka na hata mwaka 2014 tulipata taarifa hiyo, je, Serikali inaweza kutuambia katika bajeti hii ya mwaka 2016/2017 imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya kuanza kwa mradi huo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ilikuwa ni ahadi ya Makamu wa Rais kutupatia maji ya Ziwa Victoria katika maeneo ya Choma na Tarafa ya Simbo na iliombwa kwa madhumuni ya kuwa, moja tunakwenda kupata Wilaya mpya, lakini pili katika maeneo hayo tuna hospitali ya rufaa ya Nkinga ambayo inahudumia karibu mikoa mitano, je, Serikali haijaona haja ya kupeleka maji katika maeneo hayo yaliyoombwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa ujenzi wa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda maeneo ya Nzega, Tabora na Igunga ulianza mwaka 2012 na inatarajiwa sasa katika mwaka mpya wa fedha unaokuja 2016/2017 taratibu zile za manunuzi zitakuwa zimekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri mradi huu unafadhiliwa na tayari mfadhili amesha-commit dola milioni 268.35. Kwa hiyo, uhakika wa fedha tunao. Kama nilivyojibu katika hoja ya msingi kwamba sasa hivi tumeshamaliza kutambua Makandarasi na tumepeleka kwa mfadhili Benki ya India kwa jili ya kupata no objection ili tuweze kuendelea na hatua nyingine ili ifikapo mwezi Julai mwaka huu tuwe tumeanza kazi ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kweli taarifa ipo, kwamba Mheshimiwa Makamu wa Rais aliahidi kupeleka maji Manonga, lakini kama nilivyosema kwamba mchakato huu ulianza mwaka 2012 na tukaanza kufanya usanifu na kipindi hicho wakati tunatengeneza memorandum tulikubaliana kwamba kwa maana ya mradi huu utakwenda kilomita 12 kila upande wa bomba litakapopita lile bomba kuu. Kwa hiyo, ahadi imekuja wakati taratibu hii iko nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, huu siyo mwisho, ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais tunayo, kwa hiyo, asubiri tuanze ujenzi. Wakati wa ujenzi tutaangalia tutakachofanya ili kuhakikisha kwamba, tunatimiza ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Naibu Waziri. Kwa kuwa tatizo la umeme lililopo Zanzibar linafanana sana na tatizo la umeme lililopo Igunga, sasa kwa sababu Naibu Waziri anatambua vizuri sana: Je, nini kauli ya Serikali juu malipo ya fidia kwa Kata za Chabutwa, Simbo pamoja na Mwisi ili waweze hasa kujua watapata lini hiyo fidia yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Niabu Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Gulamali, jana na juzi tumehangaikia sana suala la fidia ya wananchi wako. Kama ambavyo tumelifikisha, kwanza nikupongeze. Sasa hivi mthamini wa ardhi wa Mkoa anapitia viwango vya fidia vya wananchi wa Manonga na hasa katika vijiji vya Chabutwa Simbo na maeneo ya jirani ambapo umetaja, ni kweli kabisa kuna wananchi 722 ambao hawajafidiwa na malipo hayo yako katika hatua za mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba jana wakati tunapitia, tulipoongea na Mkuu wa Mkoa wa Tabora nadhani alikwambia kwamba kabla ya mwezi ujao na miezi miwili ijayo wananchi wako watalipwa fidia. Kwa hiyo, nakuomba sana wafikishie taarifa waendelee kuwa na subira jambo la fidia yao linafanyiwa kazi.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali fupi kwa Naibu Waziri.
Ni lini sasa maeneo ya kata za Mwashiku, Ngulu, Uswaya na Igoweko yataweza kupata mawasiliano kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri ameweza kujibu swali la Mheshimiwa Mgimwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Gulamali ni mfuatiliaji sana, siyo wa masuala ya mawasiliano peke yake, bali ni pamoja na barabara zake zile mbili ambazo viongozi wetu wakuu walitoa ahadi, na nyakati zote wakati akifuatilia hiyo miradi nimekuwa nikimhakikishia kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano inatenda inachoahidi. Mheshimiwa Gulamali nikuahidi katika yale uliyoyafuatilia vijiji hivi sikumbuki kama ulinitajia. Kwa hiyo, nitafuatilia ratiba ya utekelezaji wa makapuni yote yanayotuletea mawasiliano nchini kuona kama hivi vimeshaingizwa katika ratiba na kama vitakuwa havijaingizwa namhakikishia tutaviingiza.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza na swali langu napenda kulielekeza kwa Waziri, Wizara ya ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Swali langu linafanana sana na swali lililoulizwa hivi punde; ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Ziba kwenda Ikinga, Simbo mpaka Tabora na Ziba, Choma mpaka Shinyanga hasa ukizingatia hizi ni ahadi za Mheshimiwa Rais na huu ni mwaka wa 2017? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Seif Gulamali na wananchi wote wa Manonga na Wilaya ya Igunga kwa ujumla, kwamba ahadi zote ambazo viongozi wetu wamezitoa katika kipindi hiki cha miaka mitano tutazitekeleza. Lazima twende hatua kwa hatua, hatuwezi kutekeleza ahadi zote kwa mwaka mmoja wa fedha. Na nimhakikishie tu kwamba kabla ya kipindi hiki cha miaka mitano barabara hii tutakuwa tumeitendea haki kama ambavyo viongozi wetu wakubwa wa kitaifa walitolea ahadi.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Napenda sasa katika majibu yake angeweza kufafanua kwa jinsi ambavyo barua ilivyokuwa imeelekeza, kwa sababu tunavyojua katika kikao chetu cha RCC pamoja na uanzishwaji wa Wilaya mpya ya Bukene pia kulikuwa na maombi ya Wilaya mpya ya Manonga.
Kwa hiyo, nilikuwa nafikiria MheshimiwaWaziri atuambie; je, mchakato huo utaenda sambamba pamoja lakini turahisishiwe katika kuanzishiwa Mkoa wetu wa Tabora kwa sababu Mkoa wa Tabora ni mkubwa katika mikoa yote iliyobakia kwa sasa, una kilometa zaidi ya 75,000 na tumeshaona baadhi ya mikoa mingine imegawanywa kama Mkoa wa Mbeya, Arusha na Shinyanga. Naomba sasa Mheshimiwa Waziri atuhakikishie uharakishaji wa kugawa huu mkoa ili kurahisisha kupeleka maendeleo kwa wananchi. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, alichosema Mheshimiwa Mbunge ni kweli, kwa sababu maombi haya yalivyokuja, lengo kubwa lilikuwa ni kuanzisha Mkoa mpya wa Nzega ambao uliainisha mkoa huo utakuwa na Wilaya nne. Ilipendekezwa kwamba kutakuwa na Wilaya hii mpya ya Bukene, Wilaya kongwe ya Nzega, Wilaya ya Igunga, halikadhalika na Wilaya mpya ya Manonga. Kwa hiyo, huo ndiyo mchakato wenyewe ulivyokuwa katika pendekezo lile. Ndiyo maana nimesema kwamba kulikuwa na mapungufu kadhaa, baadaye sasa ofisi yetu ikapeleka mrejesho kwa Katibu Tawala wa Mkoa na wameshafanyia kazi hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nimesema kwamba physical verification imeshaenda kufanyika, sasa kilichobakia ni kwamba iko katika mchakato wa kupelekwa kwa Mheshimiwa Rais naye atafanya maamuzi, lakini tukiwa na angalizo kwamba na Mheshimiwa Rais alifika pale Tabora, kuna mazungumzo aliyazungumza. Kwa hiyo, yeye mwenyewe atapima ataona nini kifanyike kuhakikisha kwamba jambo linafanikiwa kwa kadri yeye mwenyewe atakavyoona inafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya hayo yote ili mradi kufanya jambo hili kwa matakwa yenu na Mheshimiwa Rais aweze kufanya maamuzi.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swlai dogo la nyongeza. Kwa kuwa kukua kwa soko huria katika utoaji wa huduma ya anga nchini, hivyohivyo naweza nikaambatanisha na kukua kwa elimu yetu kuwa huria na nilikuwa nataka tu kupata maelekezo ya Wizara juu ya huria hii ya kutokana na elimu yetu ya Tanzania kuwa huria, hali iliyosababisha baada ya kutoka kwa uhakiki wa vyeti feki imepelekea baadhi ya Madaktari, Walimu, Watumishi, taarifa zao kuonekana ni incomplete. Hii ni kwa sababu ya elimu yetu kuwa huria. Sasa naiomba Serikali itoe maelekezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapozungumza,
kuna watumishi sasa wanaelekea Dar es Salaam kwenda kuhakiki incomplete zao…
Mheshimiwa Mwenyekiti,
swali langu ni kwamba nakata kujua: Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya wafanyakazi ambao taarifa iliyotoka juzi ya uhakiki wa vyeti vyao, hasa wale wote walioandikiwa incomplete? Serikali hasa Wizara hii ya Elimu ituelekeze, maana leo hii watu wanasafiri wengi kwenda kuhakiki vyeti vyao vya Form Four. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni hilo nalielekeza kwa Mheshimiwa Waziri kwa sababu hapa ni mada huria na elimu yetu ni huria, naomba Wizara ya Elimu itoe tamko juu ya kadhia hii ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli kwamba tumekuwa tukitoa elimu huria ili kuwezesha maeneo mbalimbali ya ajira kuweza kupata wataalam wanaohitajika. Katika suala hili la watu kusafiri kuhusiana na kuhakiki vyeti vyao, napenda tu kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna makundi makuu matatu ambayo yameendana na uhakiki uliofanyika. Kuna kundi la kwanza la vyeti feki au vyeti vya kugushi, kundi hili kama kuna yeyote anayeona kwamba hajaridhika, anachotakiwa kufanya siyo kusafiri, bali ni kukusanya vyeti vyake halali na kumwona mwajiri wake ambaye ni DED (Mkurugenzi wa Halmashauri) au Katibu Tawala wa Mkoa ili apeleke huo ushahidi wake na viweze kuwasilishwa. Vitawasilishwa kwa Katibu Mkuu, Utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna kundi lingine,
hili analolizungumza la incomplete (vyeti visivyokamilika). Yawezekana wakati wa kuwasilisha, mtu aliwasilisha labda vyeti vya Chuoni, vyeti vya Kidato cha nne au cha sita hakuwasilisha; au vyeti vingine vinavyohusiana. Kwa hiyo, anachotakiwa kufanya ni vilevile, kupeleka vile vyeti ambavyo vilikuwa havijawasilishwa kwa hao waajiri wake ambao ni Mkurugenzi wa Halmashauri au RAS (Katibu Tawala wa Mkoa).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kundi la tatu la vyeti vyenye utata. Vyeti vyenye utata unakuta kwamba cheti kimoja kimetumika na watu zaidi ya mmoja. Kwa hali hiyo inabidi lazima kumfahamu ni yupi mwenye cheti halisi. Wanachotakiwa kufanya ni kila mtu anayeamini ndiye mwenye cheti hicho, hao ndio wanaotakiwa kusafiri, waende NECTA ili sasa wakahakikiwe na kujulikana mwenye cheti chake ni yupi kwa sababu haiwezekani cheti kimoja kikatumika na mtu zaidi ya mmoja. Huo ndiyo ufafanuzi wangu. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufahamu, je, Serikali ina mpango gani ya kusambaza huduma hii nchi nzima hasa katika Wilaya ya Igunga na Mkoa wa Tabora na ukifuatilia kwamba katika Wilaya ya Igunga na Mkoa wa Tabora hivi karibuni tutaweza kupata maji ya Ziwa Victoria?
Mheshimiwa, la pili, nilikuwa nataka kujua juu ya Wizara hii ya Maji, inatoa tamko gani kwa baadhi ya Mamlaka za Maji nchini ambazo zinatoa bili kubwa kwa watumiaji wa maji kuwabambikiza bili kubwa watumiaji wa maji kuliko matumizi halisi ya wananchi wanaotumia kwenye maji? Nataka kujua tamko la Serikali juu ya ubambikizaji wa gharama za maji, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyopigania wananchi wake. Lakini kikubwa napenda kujibu maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni kuhusu suala zima la usambazaji mkakati wetu kama Serikali. Safari ni hatua na hatua tumeshaianza ya kutekeleza mamlaka saba na kwa kuwa safari moja huanzisha nyingine sisi kama Serikali kwa kupata nafasi ya kuweza kutekeleza mamlaka saba tunaziagiza mamlaka zote zenye uwezo wa kujitosheleza kigharama kutenga bajeti kuhakikisha kwamba wanatengeneza mifumo hii ili kuweza kuyafikia maeneo ya mbali katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, katika baadhi ya mamlaka kuwabambikia wananchi ama wateja gharama ambazo si halisia haipendezi, wala haifurahishi, kuona baadhi ya mamlaka zinawabambikia bei wananchi. Mimi nataka niziagize mamlaka zote nchini kwamba watoe bei halisia ambazo zimeidhinishwa na EWURA. Kama kuna mtu au mamlaka itakayokaidi hata kama ana mapembe marefu kiwango gani tutayakata ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma bila usumbufu wowote.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Nipende tu kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri katika Wilaya ya Igunga Kata ya Mwashiku, Vijiji vya Matinje, Buchenjegele, Ngulu na maeneo ya karibu pale, ni maeneo ambayo wanachimba dhahabu na wafanyabiashara wadogo wadogo wanapata tabu sana katika kufanya transactions za fedha kupitia hii mitandao ya simu, biashara hii za dhahabu wanaifanya kwa muda mrefu sasa. Je, ni lini sasa Serikali itawapelekea mawasiliano ya simu kama mitandao ya Vodacom, Airtel, na mitandao mingineyo ili kuwarahisishia wananchi kutokutoka maeneo yale ya Vijiji vile vya Matinje kwenda mpaka Nzega au Igunga? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo aliyoyataja kwa uelewa wangu ni kwamba yana mawasiliano. Sasa nitapenda tukutane tujadiliane kwa kirefu, labda anaongelea mitandao ya ziada. Kama kuna eneo ambalo halina mtandao tuwasiliane, tukubaliane cha kufanya.
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza; nina maswali (a) na (b).
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imekiri kuwa kati ya kata 19 zilizoko ndani ya jimbo la Manonga kata tisa hazina mawasiliano, kwa maana ya vijiji vyote vilivyoko ndani ya zile kata tisa, je, Serikali haioni kuwa katika maeneo hayo wananchi hawatendewi haki kwa sababu wanakosa mawasiliano? Na je, Serikali kutokana na majibu yake inatuhakikishiaje kuwa mpaka Novemba itakuwa tayari maeneo hayo yamepata minara ya simu katika maeneo yaliyotajwa?
Mheshimiwa Spika, swali b je Waziri atakuwa tayari tuongozane naye ili awezekwenda kujionea hizo kata ambazo hazina mawasiliano ya simu? Kama yuko tayari ni lini ili aweze kuona adha ambazo wananchi wanazipata? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali kwenye jibu la msingi Serikali inakiri kuwa kati ya kata 19, kata 10 zinamawasiliano na kata tisa hazina mawasiliano. Kwetu sisi hayo ni mafanikio makubwa na tutahakikisha kata tisa zilizobaki ambazo ni chini ya asilimia 50 tunazifikishia mawasiliano katika kipindi hiki cha miaka mitano itakapofika mwaka 2020 hilo litakamilika na tutalikamilisha kwa kutumia mkataba tulionao na kampuni ya Viettel kwa kuwa tuna mkataba nao, lakini vilevile Mfuko wetu wa Mawasiliano kwa Wote.
Mheshimiwa Spika, nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge umefika ofisini tumekutana na wataalam, bahati nzuri hivi vyote tuliviorodhesha na sasa unafahamu, labda ni vizuri tu na wananchi wako wakafahamu kwamba kata hizo zote tisa tumeshazichukua na tutazifanyia kazi katika kipindi kifupi kijacho.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kufika katika eneo lake na kuzipitia hizo kata.
Mheshimiwa Spika, kama utakumbuka ndani ya Bunge lako Tukufu alipouliza swali lake la nyongeza nilimjibu kwamba mimi siamini kijiji kama Machinja hakina mawasiliano kwa sababu watu ni wengi sana. na nitumie nafasi hii kuyafahamisha makampuni ya simu tunamaeneo mengi yenye watu wengi sana, mahala ambapo pana biashara kubwa. Maeneo hayo hatuhitaji fedha ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote yaende katika maeneo hayo. Kwa sababu maeneo hayo ni yakibiashara, yana watu wengi na mkipeleka mawasiliano mtapata fedha za kutosha. Its economically viable.
Kwa hiyo karibuni sana Waheshmiwa Wabunge tupeane taarifa maeneo ambayo yana watu wengi sana center kubwa sana makampuni yenyewe yaende tusitumie hela zetu za Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Hela hizi za mfuko wa mawasiliano kwa wote tuzitumie katika maeneo ambayo hayavutii kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, nitakuja katika lengo hilo hilo la kuhamasisha makampuni kwanza yaje, lakini pili tuone UCSAF itafanyaje kazi kama ambavyo tulikuahidi ulipofika ofisini na tukakutana na wataalam. Hongera sana Mheshimiwa kwa kufuatilia suala hili kwa umakini sana.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napenda kujua, pale katika scheme yetu ya umwagiliaji ya Choma Chankola tuna scheme ya umwagiliaji na Mheshimiwa Waziri alishawahi kuja kuona lile eneo na akaahidi tupeleke andiko kwa ajili ya uchimbaji wa bwawa kubwa pale. Tayari andiko limeshapelekwa katika Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. Sasa ni lini fedha zitaweza kutolewa kwa ajili ya uchimbwaji wa bwawa hilo kwa sababu tayari ishapita miaka mitatu?Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza kaka yangu, Mheshimiwa Gulamali kwa namna anavyowatetea wananchi wake, lakini kubwa nataka nimhakikishie kwamba nami naomba nipitie hilo andiko kwa haraka ili mwisho wa siku tupate kushauriana na Mheshimwia Waziri wangu mpya, Mheshimiwa Mbarawa katika kuhakikisha hili jambo tunalikamilisha kama ilivyopangwa. (Makofi)
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nipende sasa kuuliza maswali mawili madogo.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa usanifu ulikwishafanyika, je ni lini sasa huu mpango kabambe utaanza kutekelezwa katika Kijiji cha Chomachankola? (Makofi)
• Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa maeneo ya Ziba, Ndebezi, Nkinga, Mwisi, Simbo, Igoeko na Uswaya wanategemea sana kilimo cha mpunga ambapo sasa wanalima msimu mmoja na hawana scheme wala mabwawa.
Je, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri pamoja na wataalam wako mtaweza kuzuru maeneo hayo mjionee ukubwa wa tatizo ili kuja na majawabu ambayo yataweza kutatua changamoto katika maeneo tajwa? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuliandaa na kulijibu swali vizuri sana. Sasa nijibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni lini tutaanza utekelezaji wa skimu ya Chomachankola. Nimhakikishie tu kwamba mpango kabambe umekamilika na kuanzia mwaka ujao wa fedha tunaanza ku-mobilize fedha na hasa kwa nje na kuanza kutekeleza hiyo progamu kwa sababu hiyo programu itashirikisha taasisi nyingi sana za wadau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mpango kabambe umeanisha maeneo yote, kwa hiyo tutakachofanya ni kuhakikisha kwanza tunajenga chanzo cha maji na baadaye ku-develop hizo skimu ili tuhakikishe kwamba maeneo yote yanayofaa kwa kilimo cha mazao ya aina yote yanalimwa kwa umwagiliaji. (Makofi)
MHE. SEIF K.S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuipongeza Wizara hii ya Nishati ikiongozwa na Mheshimiwa Medard Kalemani pamoja na Mheshimiwa Subira Mgalu kwa kazi kubwa wanasozifanya kuhakikisha kwamba umeme unapatikana katika maeneo yenye shida ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu msingi ambalo nilitaka kujua kwa sababu tumeshaanza utelezaji wa uzambazaji wa umeme katika baadhi ya maeneo yaliyotajwa lakini tumeanza kwa kusuasua. Je, ni lini sasa kama Wizara; Mheshimiwa Waziri pamoja Mheshimiwa Naibu Waziri wataweza kuja kuona maendeleo ya mradi huu katika maeneo hayo yaliyotajwa kwa sababu uzambazaji wa umeme huo mwisho wake ni Juni, 2019? Ujio wao utasababisha msukumo kuwa mkubwa na kazi hii itafanyika kwa haraka zaidi. Je, ni lini wataweza kufika katika maeneo hayo tajwa? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nampongeza sana Mheshimiwa Gulamali kwa jinsi ambavyo anatupa ushirikiano katika kupeleka umeme kwenyeJimbo lake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa katika Jimbo la Gulamali mkandarasi yuko katika Kijiji cha Matinje ambacho pia ni cha wachimbaji wadogo wa madini. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge, wakandarasi watakapotoka Matinje wanakwenda Nsimbo na ili wafike Nsimbo ni lazima wapite Mwamala, Tambarale, Uswaya na Igoweko. Kwa hiyo, vijiji vyake ambavyo amevitaja kimsingi vitapata umeme kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ni lini tutakwenda tena, napenda kutumia nafasi hii kumwambia Mheshimiwa Gulamali kwamba mara baada ya Bunge tutatembelea maeneo yake kwa sababu tunataka tutembelee maeneo yote ya Mkoa wa Tabora. Mkoa wa Tabora unahitaji umeme wa nishati wa kutosha kwa sababu ni mkubwa. Kwa hiyo, tutakwenda Roya kwa Mheshimiwa Ntimizi, tutakwenda Mswaki pamoja na maeneo mengine ya Waheshimiwa Wabunge wa Tabora. Ahsante.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza, napenda kuishukuru Serikali kwa namna ambavyo imeweza kutekeleza upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo tajwa kwa wakati kwa sababu hatua mbalimbali zinaonekana zinaendelea kufanyika. Kwa hiyo, niiombe tu Serikali iongeze speed katika yale maeneo ambayo mradi huu unatekelezwa katika kata hizo.
Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali katika hizo Kata ambazo tumezitaja kwa maana ya Uswaya, Tambarale, Mwamala ni maeneo ambayo yana watu wengi sana, kwa sababu Serikali ilikuwa imeweka mpango huu katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 na bajeti hii sasa inaelekea mwishoni, je, haioni sasa umuhimu wa kuweka katika mpango wa bajeti wa mwaka 2019/2020?
Mheshimiwa Spika, lakini la pili kwa ruhusa yako, kwanza nitoe pole kwako Mheshimiwa Spika lakini pia kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Zungu na wengine wote wadau kwa yale ambayo yametokea kule Misri. Sisi tunawaombea muendelee vizuri yasitokee tena kama yalitokea kule Misri. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanapata mawasiliano ya uhakika kwa asilimia 100. Hadi sasa hivi tunapoongea Watanzania kwa record za Serikali wanawasiliana kwa asilimia 94.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba mwezi Aprili, kuna orodha ya vijiji na kata nyingine itakayotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ambazo zitakuwa zimependekezwa kwa ajili ya miradi ya mawasiliano. Asiwe na wasiwasi, tumejipanga kutekeleza kuhakikisha kwamba Watanzania wanawasiliana.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amasema barabara hizo zitapewa kipaumbele, je, ni vipi atazipa kipaumbele huku tayari bajeti imeshasomwa na pesa hazijatengwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari sasa kwenda kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo ili kuwaambia juu ya barabara hizo kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIAN (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Seif Gulamali kwa kufuatilia mipango ya ujenzi wa barabara lakini pia maendeleo mbalimbali. Mheshimiwa Gulamali nakumbuka wakati wa ziara ya Makamu wa Rais pia amefuatilia na kuzungumza juu ya barabara hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi sasa hivi tunaendelea na kukamilisha kuunganisha mikoa yetu kwa barabara za lami. Pia kama nilivyosema kwamba tutakapokuwa tumefika hatua nzuri tutaingiza kwenye mpango ujenzi wa barabara hizi muhimu ambazo umezungumza kwa sababu zinahudumia watu wanaokwenda kupata huduma ya matibabu pale Nkinga. Kwa umuhimu huo ndiyo maana katika mwaka 2018/2019 kama nilivyojibu tulitenge fedha nyingi karibu bilioni nzima, zaidi ya shilingi milioni mia nane themanini zilitengwa kwa ajili ya kuboresha maeneo korofi ili wananchi waweze kupita katika maeneo hayo bila shaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna ujenzi wa madaraja Mheshimiwa Gulamali anafahamu kule Mto Manonga, daraja kubwa tunaendelea kujenga lakini pia tunaendelea kuwaunganisha wananchi kutoka Ziba - Choma kwenda Kanawa kule upande wa Shinyanga kwa maana ya Wilaya ya Kishapu. Pia iko miradi mingine kutoka upande mwingine wa Shinyanga tunajenga ili kuweza kuwafanya hawa wananchi wawe kwenye mtandao mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, nitakuwa tayari kwenda kuzungumza na wananchi lakini Mheshimiwa Gulamali kumbuka wakati nikiwa na ziara na Makamu wa Rais pia nilipata nafasi ya kutoa ufafanuzi juu ya mpango kabambe wa kuiboresha barabara hii. Hata hivyo, kwa sababu unahitaji twende nitakwenda nizungumze na wananchi ili waone mipango mizuri ya Serikali tuliyojipangia kwa ajili ya kuboresha barabara hizi muhimu.
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kuwepo na milipuko ya magonjwa kwenye mifugo, nini mpango wa Serikali wa kujenga majosho katika Wilaya ambazo zina mifugo mingi hususani Wilaya ya Igunga kutuwekea majosho kwenye minada na vijiji? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Seif Gulamani, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga vyema katika kuhakikisha kwamba tunajenga majosho ya kutosha katika vijiji na Wilaya mbalimbali nchini. Katika mwaka huu tunaokwenda nao wa 2020/2021 Wilaya ya Igunga kwa maana ya Jimbo la Manonga ni miongoni mwa maeneo yatakayopata fursa ya kujengewa majosho, tena utapata pale majosho mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile habari njema kwa Waheshimiwa Wabunge wote; mkakati wa Serikali katika muda wa miaka hii mitano, baada ya kuwa tumefanikiwa sana katika zoezi letu la uogeshaji wa mifugo na kupunguza sana magonjwa yanayoambukizwa kupitia kupe, tutaendelea na zoezi hili la uogeshaji na kwa kujenga majosho ya kutosha. Tunataka kila kijiji ambacho kina wafugaji kipate josho na kwa hiyo tunaomba sana mtuunge mkono katika kuhakikisha kwamba zoezi hili linafanikiwa. (Makofi)
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipatia nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza mawili. Katika Skimu ya Umwagiliaji ya Igunga, kumekuwa na wakulima wakichukua mikopo mikubwa kwa riba ya asilimia 18, kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji pale Mwanzugi.
Je, nini mkakati wa Wizara kuwasaidia wakulima hao waweze kupata nafuu katika kilimo hicho? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wakulima wa Mkoa wa Tabora, wamekuwa wakipata mikopo kwa gharama kubwa (kwa dola) katika zao la tumbaku.
Je, nini mkakati wa Serikali kuwasaidia wakulima wa zao la tumbaku kupata pembejeo kama mlivyowasaidia wakulima wa zao la pamba? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Seif Gulamali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kwamba wakulima katika skimu nyingi za umwagiliaji ikiwemo zilizopo katika Jimbo la Igunga Mjini, lakini maeneo ya Mkoa wa Morogoro, maeneo ya Mbarali, kwa maana ya Mkoa wa Mbeya na maeneo mengine, wamekuwa wakipata financing kutoka katika sekta ya fedha kwa riba zaidi ya asilimia 16 mpaka 20 na zaidi ya hapo na wengine wamekuwa wakipata mikopo kwa gharama ya wastani wa riba ya asilimia 3.5 kwa mwezi, ni gharama kubwa. Tumeshaanza mawasiliano na wenzetu wa Benki Kuu ya Tanzania na hivi karibuni tumekutana MDs wote wa Commercial Banks ili kutengeneza Skimu za financing kwenye sekta ya kilimo ambazo zitakuwa na gharama nafuu na zinaendana na uzalishaji wa sekta ya kilimo. Riba hizi za zaidi ya asilimia 20 kwa mazao ya kilimo, wakulima hawawezi kupata faida kutokana na inputs zao. Kwa hiyo, hili tunalifanyia kazi na hivi karibuni mtasikia taarifa ya Kamati ya Kitaifa iliyoundwa na Waziri wa Kilimo kwa ajili ya kuja na financing models za sekta ya kilimo zinazoendana na sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wakulima wa tumbaku, Wizara ya Kilimo tumechukua hatua na mwaka huu wakulima wa tumbaku hawatoenda kukopa hard cash bank kwa sababu sasa hivi wamekuwa wakikopa fedha kwa dola na wamekuwa wakilipa riba za asilimia 7 mpaka 8 na hizi zimekuwa zikiwasababishia matatizo na wengi kukata tamaa kuendelea na uzalishaji wa tumbaku. Kwa hiyo, tunatengeneza programu na utaratibu ambapo wakulima watapatiwa pembejeo na supplier atapata LC na hao wakulima kupitia AMCOS zao hawatoenda benki kuchukua hard cash kulipia pembejeo, watapata pembejeo na watalipa mwisho wa msimu watakapouza mazao. Hapa transaction itakayokuwepo ni guarantee kati ya Wizara ya Kilimo na taasisi za fedha kuwapa guarantee wakulima wasiweze kwenda kuchukua mikopo ya fedha cash kwa sababu, imekuwa ni mzigo mkubwa. Utaratibu huu tumeufanya kwenye pamba, wakulima wamepata pembejeo bila kwenda kukopa fedha benki na watalipa katika mjengeko wa bei. Hivyo hivyo, tutafanya kwenye korosho na tumbaku.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wilaya yetu ya Igunga hususan Jimbo la Manonga sisi ni wakulima wa pamba, mpunga, madini na mifugo kwa wingi. Katika vijiji kama hicho ambacho nimekitaja cha Ikombandulu, Mwakabuta, Ikungwi Ipina, Utuja na Shalamo ni katika maeneo yenye uzalishaji kwa wingi katika mazao niliyoyataja. Ipi mikakati ya Serikali kuhakikisha maeneo hayo yanapata mitandao ya simu kwa wakati?
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Mwisi, Simbo, Choma, Ibologelo na Indembezi wanapata mawasiliano ya simu lakini mitandao hii ipo chini sana hasa kwenye internet. Je, Serikali kupitia wadau wanaotoa huduma katika maeneo hayo ipi mikakati yao na hasa ukitambua sasa hivi Tanzania tuna- launch 5G, nini mikakati ya Serikali kuhakikisha maeneo hayo niliyoyataja tunapata angalau 4G kwa ajili ya kusaidia wataalam, watafiti na waandishi wa Habari…
SPIKA: Ahsante sana umeeleweka Mheshimiwa.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Hususan kwenye vijiji vilivyopo nchini Tanzania, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilivyojibu katika majibu yangu ya msingi kwamba Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tupo katika mkakati wa kufanyia tathmini Kijiji hicho sambamba na vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameshavitaja ili kuhakikisha kwamba tujiridhishe ukubwa wa tatizo baada ya hapo vitaingizwa katika zabuni ya awamu zinazokuja katika mwaka wa fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, suala la pili kuhusu masuala ya internet. Tunafahamu kwamba kwa sasa hivi tunakoelekea katika uchumi wa kidigitali na tunaelewa kabisa kwamba internet coverage inahitajika ili Watanzania waweze kutumia vizuri katika shughuli zao za hapa na pale. Tumeshaelekeza watoa huduma wote wafanye tathmini katika minara ambayo bado inatumia teknolojia ya 2G ili waweze ku- upgrade na kuweza kutumia teknolojia ya 3G, 4G na hatimaye baada ya kujiridhisha kwamba tutakuwa tunahitaji 5G basi tutakuwa tumefikia huko.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa fedha za ujenzi wa mradi wa maji ya Ziwa Viktoria kutoka Ziba, Nkinga zipo: Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza mradi huu wa kupeleka maji maeneo hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mradi huu alioutaja wa maji kutoka Ziwa Victoria kuelekea maeneo yote ambayo ameyataja, tunatarajia kuutekeleza mwaka ujao wa fedha 2021/2022.
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuweka kumbukumbu vizuri naomba kurekebisha kidogo vijiji vya Ulaya, Nkinga na Barazani, kwamba viko Tarafa ya Manonga na si Tarafa ya Simbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza, kwasababu ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais na sasa ndiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni lini Serikali itapeleka maji ya Ziwa Victoria katika Tarafa ya Simbo hasa Makao Makuu ya Tarafa ya Simbo na Tarafa ya Manonga, hasa Makao Makuu ya Tarafa pale Choma cha Nkola kwa kuwa maeneo hayo yana idadi kubwa ya wananchi wanahitaji huduma hii ya maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Seif Gulamali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti Tarafa hizi mbili, ya Simbo na Manonga zote zipo katika mpango mkakati wa kukamilisha utekelezaji wa kupeleka maji kutoka Ziwa Victoria. Mwaka ujao wa fedha wa 2021/2022 kadiri tutakavyopata fedha tutafikia maeneo hayo yote muhimu. (Makofi)
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Igunga ni wilaya moja wapo inayoongoza kwa mifugo mingi sana hapa Tanzania, je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza idadi ya majosho, hasa Jimbo la Manonga, kutoka majosho matatu hata angalau kufika majosho kumi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika siku 100 za Mheshimiwa Rais, mama Samia Hassan Suluhu, tumemuona akikutana na Mwanamfalme wa Saudi Arabia na wamejadili juu ya masuala ya mifugo, hasa kuuza mifugo lakini pia kuuza nyama nje ya nchi. Je, Wizara imejipangaje kutumia fursa hii; mkakati wake ni upi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni kuongeza idadi ya majosho katika Jimbo la Manonga. Naomba tu nipokee ombi hili la Mheshimiwa Mbunge na nimuahidi kwamba Wizara italifanyia kazi kwa kusudi la kuongeza idadi ya majosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni hili la mkakati wa Serikali juu ya kuongeza biashara ya nyama na mifugo nje ya nchi. Kwanza nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan; katika siku hizi 100 moja ya Wizara ambazo amezifanyia kazi kubwa ni hii Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi. Naomba tu nimhakikishie
Mheshimiwa Mbunge ya kwamba Wizara imejipanga vyema kuhakikisha kwamba fursa hii ya kuuza nyama na mifugo nje inatumika na inatumika ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni kwa kupunguza kodi mbalimbali ambazo zilikuwa ni kikwazo. Lakini pili, ni kuendelea kushirikiana vyema na sekta binafsi ili kuweza kushamirisha biashara ya mifugo. Na mwisho, mkakati wetu wa kopa ng’ombe lipa ng’ombe, kopa mbuzi lipa mbuzi, tutaupa kipaumbele sana ili kuongeza uzalishaji katika nchi. Ahsante sana.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuweza kutekeleza ahadi za Viongozi wa Kitaifa hasa ilikuwa ni ahadi ya kipindi cha kampeni 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu nipende tu kuuliza kulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuwa amekuja pale Chomachankola. Nilikuwa naomba pia kuweza kupata jibu juu ya Kituo cha Afya cha Chomachamkola ambacho Mheshimiwa Waziri Mkuu alituahidi kutupatia fedha kwa ajili ya kujenga majengo ya wazazi pale. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Seif Gulamali, Mbunge wa Jimbo la Manonga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Seif Gulamali kwa kuwasemea kwa dhati kabisa wananchi wa Jimbo la Manonga na ufuatiliaji wake kuhakikisha Serikali inaendelea kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nipokee shukrani zake nyingi kwa Serikali na kwa kweli sisi sote Waheshimiwa Wabunge tumeona kazi kubwa sana inayofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya huduma za afya na ndani ya hii miezi sita Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amepeleka zaidi ya bilioni 58 na milioni 250 kujenga Vituo vya Afya 233 kote Nchini. Kwa hivyo, tunapokea shukrani hizi na tuwahakikishie kwamba tutaendelea kushirikiana naye kuhakikisha tunaendelea kuboresha miundombinu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la Kituo cha Afya ambacho ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba nimuhakikishie kwamba ahadi zote za Viongozi wetu wa Kitaifa zinapewa kipaumbele ikiwemo kituo hiki cha Afya tutaendelea kutafuta fedha na mara zikipatikana tutakwenda kuhakikisha kwamba tunaanza ujenzi wa Kituo cha Afya hicho. Ahsante.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru wa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wakati wa ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu pale Kijiji cha Chomachankola, Tarafa ya Choma, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliahidi kutupatia fedha kuongeza kwenye Kituo cha Afya cha Choma: -
Je, ni lini sasa Wizara italeta fedha kwa sababu ahadi hii imetolewa toka 2018? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Seif Gulamali, Mbunge wa Jimbo la Manonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali iliahidi kupeleka fedha kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Choma, Kijiji cha Chomachankola katika Jimbo la Manonga na ni kweli kwamba Mheshimiwa Mbunge amefuatilia kwa karibu sana, na mwaka wa fedha uliopita tulikosa kifungu cha kupelekea fedha ile, lakini nimeongea naye na tumekubaliana katika mwaka wa fedha huu tutahakikisha fedha inapelekwa ili kitu cha afya kianze kujengwa. Ahsante.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naomba kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na miradi mingi sana ya maji ndani ya jimbo letu na tumekuwa tukikuomba uje uikague miradi hiyo kuona ubora wake na thamani ya fedha inayotumika.
Je, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri na timu yako utapata nafasi ya kuja kukagua miradi hiyo? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimuahidi Mheshimiwa Gulamali baada ya Bunge letu la Bajeti nitafanya ziara katika jimbo lake katika kuhakikisha tunasimamia na kufuatilia miradi katika Jimbo lake la Manonga. Ahsante sana.
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana; je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa lami barabara ya Choma – Ziba – Nkinga – Simbo mpaka Puge?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Choma – Puge ni barabara ambayo Mheshimiwa Mbunge amekuwa anaifuatilia sana. Hata hivyo, kwa kuwa bajeti bado hatujaiwasilisha naomba Mheshimiwa awe na subira tuone nini mwaka huu tutakuwa tumeipangia hiyo barabara.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwanza niishukuru Serikali kutupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari.
Swali langu la nyongeza, Mheshimiwa Waziri majibu yako yamejumlisha fedha zote zilizopo ndani ya Wilaya ya Igunga, hivyo basi nilikuwa nataka kuomba kwa shule zetu shikizi kwa maana ya Shule za Kazima, Mwakipanga, Mwamakingi pamoja na Shule ya Msingi Shikizi Mwasung’o. Je, ni lini Serikali itatuunga mkono kutupatia fedha kwa shule hizi shikizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Shule ya Sekondari ya Mwisi pamoja na Shule ya Sekondari ya Choma tuna uhaba wa mabwalo la chakula. Je, ni lini Serikali itatupatia fedha kwa ajili ya mabwalo kwa watoto wanaotumia kidato cha tano na cha sita? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali, Mbunge wa Jimbo la Manonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Shule Shikizi ambazo amezianisha Mheshimiwa Mbunge lini tutapeleka fedha, nimuhakikishie tu kwamba zipo katika mipango yetu na bahati nzuri siku ya Jumatatu tumezindua mradi wa BOOST na mradi ule unagharimu karibu trilioni 1.1. Kwa hiyo, fedha zile zitakapokuwa zimekuja maana yake tutazipeleka katika shule zote nchini ikiwemo ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziainisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mradi huo katika Shule ya Sekondari Mwisi ambazo hazina mabweni ni sehemu ya mpango ambao sisi kama Serikali tutapeleka maana yake ni component nzima ni pamoja na mabweni. Ahsante sana.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwanza niishukuru Serikali kutupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari.
Swali langu la nyongeza, Mheshimiwa Waziri majibu yako yamejumlisha fedha zote zilizopo ndani ya Wilaya ya Igunga, hivyo basi nilikuwa nataka kuomba kwa shule zetu shikizi kwa maana ya Shule za Kazima, Mwakipanga, Mwamakingi pamoja na Shule ya Msingi Shikizi Mwasung’o. Je, ni lini Serikali itatuunga mkono kutupatia fedha kwa shule hizi shikizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Shule ya Sekondari ya Mwisi pamoja na Shule ya Sekondari ya Choma tuna uhaba wa mabwalo la chakula. Je, ni lini Serikali itatupatia fedha kwa ajili ya mabwalo kwa watoto wanaotumia kidato cha tano na cha sita? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali, Mbunge wa Jimbo la Manonga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Shule Shikizi ambazo amezianisha Mheshimiwa Mbunge lini tutapeleka fedha, nimuhakikishie tu kwamba zipo katika mipango yetu na bahati nzuri siku ya Jumatatu tumezindua mradi wa BOOST na mradi ule unagharimu karibu trilioni 1.1. Kwa hiyo, fedha zile zitakapokuwa zimekuja maana yake tutazipeleka katika shule zote nchini ikiwemo ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziainisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mradi huo katika Shule ya Sekondari Mwisi ambazo hazina mabweni ni sehemu ya mpango ambao sisi kama Serikali tutapeleka maana yake ni component nzima ni pamoja na mabweni. Ahsante sana.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri; je, ni lini Serikali itaongeza fedha za ujenzi wa Zahanati kwenye vijiji hasa Majimbo ya Vijijini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gulamali, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijenga Vituo vya Afya katika maeneo ya vijijini kwa kuchangia nguvu za wananchi kwa kutoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya umaliziaji. Fedha hiyo shilingi milioni 50 ilianza kutolewa mwaka 2016/2017 na ukizingatia kasi ya inflation kwa sasa, tumeshapitia bajeti za ujenzi wa Vituo vya Afya, Zahanati na pia Hospitali za Wilaya. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imeshafanya kazi hiyo ya kubadili au kuongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati. Taarifa rasmi itatolewa na Waheshimiwa Wabunge mtaipata na fedha zinazokuja zitakuwa na mabadiliko ili kuendana na inflation iliyojitokeza, ahsante. (Makofi)
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri; je, ni lini Serikali itaongeza fedha za ujenzi wa Zahanati kwenye vijiji hasa Majimbo ya Vijijini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gulamali, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijenga Vituo vya Afya katika maeneo ya vijijini kwa kuchangia nguvu za wananchi kwa kutoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya umaliziaji. Fedha hiyo shilingi milioni 50 ilianza kutolewa mwaka 2016/2017 na ukizingatia kasi ya inflation kwa sasa, tumeshapitia bajeti za ujenzi wa Vituo vya Afya, Zahanati na pia Hospitali za Wilaya. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imeshafanya kazi hiyo ya kubadili au kuongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati. Taarifa rasmi itatolewa na Waheshimiwa Wabunge mtaipata na fedha zinazokuja zitakuwa na mabadiliko ili kuendana na inflation iliyojitokeza, ahsante. (Makofi)
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa kuwa Serikali ilituahidi kutupatia fedha kwa ajili ya kujenga Kituo chetu cha Afya cha Choma; je, ni lini fedha hizo zitafika kwenye Kituo cha Afya cha Choma? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gulamali, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ilishaahidi kupeleka fedha shilingi milioni 500 kwenye Kituo cha Afya cha Choma na tayari nimeshawasiliana na Mheshimiwa Mbunge mara kadhaa kwamba imeshaingizwa kwenye orodha ya fedha za Benki ya Dunia ambazo tunatarajia wakati wowote mwezi wa Pili au wa Tatu zitatoka kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi hiyo imezingatiwa na Serikali itatekeleza, ahsante.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri mwaka jana katika bajeti ilikuwa ya 2023/2024 tulitengewa kilometa kumi na mwaka huu wa fedha tulikuwa tumetengewa kilometa nyingine. Tulitarajia katika kutangaza zabuni kilometa zaidi ya 22 ziweze kutangazwa. Je, mtazingatia hilo Mheshimiwa Waziri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu kwamba tutaanza hizo kilometa 11, lakini kama hali ya bajeti tutapata fedha tutaendelea kuijenga na lengo si kujenga hii barabara tu kwa awamu, lakini tukiweza kupata hela nyingi zaidi tuna uwezo wa kuijenga hiyo barabara yote, lakini kwa sasa tutaanza na hizo kilometa 11, ahsante.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi kuweza kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza natumia fursa hii kuishukuru Serikali kwa fedha nyingi ambazo wametupatia kwa miradi mikubwa ya maji ya Ziwa Victoria kwa maana tumeona wakandarasi. Tumepokea wakandarasi wawili ambao mmoja anafanya extension ya mradi ule pale Ziba-Nkinga lakini pia tumepata mkandarasi mwingine anautoa Ziba kwenda Simbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na wakandarasi hawa kuwa tayari wapo site wameshaingia kwa ajili ya kuanza kufanya hii kazi, na Mheshimiwa Waziri alikuja na ugeni wa Mheshimiwa Makamu wa Rais, sasa ni lini Mheshimiwa Waziri mwenyewe atapata nafasi ya kuja kuitembelea hii miradi kujionea kazi kubwa na nzuri ya kupeleka maji katika hayo maeneo ambayo inafanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, alipokuja alitupatia fedha kwa ajili ya kupeleka maji pale kwenye Kijiji cha Ntogo. Wakandarasi sasa hivi wameanza kuchimba mtaro kwa ajili ya kupeleka maji. Sasa, kwa sababu tulikuwa tunataka vijiji viwili; kimoja cha Ntogo pale Kaselya tumepata mkandarasi, na kwa kuwa tulikuwa tunataka tupeleke na Kijiji kile kingine cha pili cha Mwamloli, je, Mheshimiwa Waziri hawezi kutupatia shilingi milioni 300 kukamilisha hii kazi nzuri ambayo inafanywa na Chama Cha Mapinduzi ili twende vizuri kwenye mambo yetu yale mengine ya uchaguzi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Mbunge. Utekelezaji wa miradi hii unatokana na kazi kubwa sana ambayo Mheshimiwa Mbunge ameifanya kwa ajili ya kuwasemea wananchi wake wa jimbo lake. Matokeo haya ni kwa sababu ya kazi kubwa sana ya ushirikiano wake mzuri sana na Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali ni wajibu wetu kuhakikisha tunafuatilia utekelezaji wa miradi ili iweze kukamilika kwa wakati. Vilevile, kuhakikisha sehemu ambayo hatujafika, tunaona njia ya kuhakikisha tunafanya utafiti na tathmini ya namna gani tupeleke huduma ya maji kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge alivyoomba. Sasa Mheshimiwa Mbunge kama alivyoomba shilingi milioni 300, naomba nilipokee ili tuweke katika Mpango wa Serikali wa utekelezaji katika bajeti ijayo ya mwaka wa fedha, ahsante sana. (Makofi)