Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (1 total)

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza, nianze kwa kumpa pole Mkuu wangu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Nurdin Babu, pamoja na Mkuu wa Wilaya, Godfrey Mnzava, wananchi wa Mbokomu na familia zilizopata msiba kwa ngema ambayo imeua watu watatu, kwa tukio lililotokea jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niulize swali lifuatalo: Zahanati ya Funduhu katika Kata ya Old Moshi Mashariki ina uhaba mkubwa wa maabara pamoja na vifaa tiba. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wananchi wanaopata huduma katika zahanati hii ili waweze kupata huduma kutoka kwenye Serikali yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Profesa Ndakidemi kwamba, Serikali katika kipindi cha miaka minne imeongeza mara dufu bajeti kwa ajili ya kununua vifaa na vifaa tiba katika vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani ilikuta bajeti kwa ajili ya kununua vifaa na vifaa tiba ni shilingi bilioni 35, lakini wakati huu tunaozungumza, bajeti ile imepanda maradufu hadi kufikia shilingi bilioni 181.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie kwamba, fedha zipo kwa ajili ya kununua vifaa na vifaa tiba. Nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kumwagiza RMO pamoja na DMO wakishirikiana na Mkurugenzi kusimamia na kuhakikisha kwamba, vifaa na vifaa tiba vinapatikana kwa sababu, fedha ipo na inapatikana kwa ajili ya kwenda kutoa huduma bora zaidi katika zahanati hii aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na jengo la maabara, Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba, inaboresha miundombinu katika sekta ya afya kwa kuendelea kujenga majengo ya kutolea huduma za afya msingi, ikiwemo zahanati. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali kupitia fedha za mapato ya ndani na kupitia fedha kutoka Serikali Kuu itaendelea kuhakikisha inaimarisha miundombinu ya kutolea huduma ya afya msingi na itakuja kufika katika jimbo lako, kwa ajili ya ujenzi wa maabara katika zahanati hii aliyoitaja.