Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hussein Nassor Amar (107 total)

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Rais alipokuja mwaka 2015 kwenye mikutano yake ya kampeni katika Jimbo la Nyang‟hwale, aliweza kuwaahidi wachimbaji wadogo wa Jimbo hilo kwamba eneo la Kasubuya litapimwa na kugawiwa wachimbaji wadogo wadogo. Je, Serikali inasemaje kwa hili kwa wachimbaji wadogo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kati ya maeneo 12 tuliyotenga kwenye Mkoa wa Geita pamoja na maeneo mengine ya Kahama ni pamoja na eneo la Kasubuya. Eneo la Kasubuya tumetenga hekta 4,098.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Hussein, wananchi wa Nyang‟hwale tayari wana eneo. Isipokuwa nawaomba sana, hata wakishindwa kupata maeneo pale Kasubuya, tunatenga maeneo mengine. Kule Chato kuna hekta 1,282. Kwa hiyo, wananchi wako bado wanaweza kwenda kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maeneo yale, maeneo ya kwa Mheshimiwa wa Mbunge wa Bukombe tuna hekta 682, wanaweza wakaenda kuchimba Bukombe. Kwa hiyo, tunaendelea kutenga maeneo ili wananchi wa Kasubuya na maeneo mengine wapate maeneo ya kutosha.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kuhusu mpango wa umeme vijijini. Mimi nina kata 15 lakini nina kata tatu ambazo zimepata umeme na ni vijiji vitatu vimepata umeme, je, Kata zifuatazo zitapata umeme katika mpango huu? Kata ya Bukwimba, Nyugwa, Busolwa, Shabaka, Nyijundu, Nyabulanda, Kafita, Kakola, Mwingilo, Kaboha, Nyabulanda na Izunya, je, serikali katika mpango wake wa mwaka huu tutapata umeme katika Jimbo la Nyang’hwale Kata zote hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika Jimbo la Nyang’hwale ni kata tatu tu ambazo zimepata umeme kwa mpango wa REA Awamu ya Pili, lakini REA Awamu ya Tatu pamoja na tathmini inayofanyika sasa katika REA Awamu ya Pili, vijiji vyote na kata zote zilizobaki za Nyang’hwale pamoja na vijiji alivyovitamka vimeingizwa kwenye mpango wa REA unaoendelea utakaonza mwezi Julai mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kadhalika kama nilivyosema bado TANESCO wanaendelea na kazi za kuunganisha umeme katika maeneo yote na maeneo ya Nyang’hwale ambayo hayatapitiwa yataingizwa kwenye mpango wa TANESCO ili vijiji vyote na kata zote za Nyang’hwale zipate umeme mwaka 2017/2018.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa majibu yake mazuri ya kwamba tumetengewa shilingi milioni 850 katika Halmashauri ya Nyang’hwale. Namuomba Mheshimiwa Waziri kwamba kwa kuwa kuna pesa ambayo imetengwa, shilingi milioni 80 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wenye eneo lile. Naomba amuagize Mkurugenzi zoezi hilo la kuwalipa wananchi lifanyike haraka ili ujenzi huo uanze kujengwa mara moja. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, anayezungumza hapa ni Mbunge wa Jimbo hilo, maana yake yeye anayajua ya huko yalivyo na hizo pesa wameshatenga tayari. Hizo pesa kama zipo sasa, nadhani tusifanye ajizi. Namuomba Mkurugenzi haraka sana, kama vigezo vyote vimetimia, hakuna sababu kuwacheleweshea ulipaji wa fidia. Tunachotaka ni kwamba fidia ilipwe, ujenzi uendelee.
Mheshimiwa Naibu spika, kwa hiyo, moja kwa moja Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tunamwelekeza Mkurugenzi wa Nyang’hwale ahakikishe kwamba kama kuna hiyo fedha imetengwa na ipo, watu walipwe fedha zao ili mradi hii kazi hii isiendelee kuchelewa tena kwa sababu ina maslahi mapana kwa wananchi wa Nyang’hwale.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya matumaini kwa wananchi wa jimbo la Nyang‟hwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika kijiji cha Busorwa pameshasimikwa nguzo, nyaya zimetandazwa na transfomer zimeshafungwa takribani zaidi ya miezi minane, kwa nini umeme kijiji cha Busorwa haujawashwa?
Na kwa kuwa kuna baadhi ya vijiji kama vile Izunya, Nyashilanga, Nyamikonze, Nyijundu nguzo na nyaya za umeme zimeshatandazwa lakini transfomer hazijafungwa. Ni lini trasfomer hizo zitafungwa ili umeme huo uweze kuwashwa na kuweza kuchochea maendeleo katika vijiji hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Mheshimiwa Naibu Waziri nakuomba baada ya Bunge hili tuongozane pamoja mimi na wewe ukaone mradi huu unavyosuasua ili uweze kuleta changamoto ili mradi huu uweze kwenda haraka ili wananchi wa jimbo la Nyang‟hwale waweze kupata maendeleo kupitia umeme, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika Jimbo la Nyang‟hwale ni vijiji vitatu tu ambavyo vimeshaunganishiwa umeme, na nitoe masahihisho kidogo, Mheshimiwa na wala siyo vijiji 61, vijiji 62 mbavyo bado kwenye jimbo lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji cha Busorwa ambacho tayari kina transformer na tayari kina nyaya zimeshafungwa kulikuwa na shida ndogo tu ya vikombe ambavyo vilikuwa havijakamilika, na hivi leo vimekamilika kesho saa tisa mchana Mheshimiwa Hussein wanakuwashia umeme pale Busorwa na mtapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ni lini vijiji alivyovitaja vitapata umeme. Ametaja vijiji vitatu lakini kuna vijiji 66 ambavyo vimepatiwa kwa nusu lakini vijiji 40 vikiwemo vijiji vya Busorwa kama ulivyotaja, Kakora, Kanegere, Nyamitongo, Nyabushishi, Nyaruzugwa, Nyaruyeye na Izuguna bado havijapatiwa umeme, kwa hiyo vyote tunavipelekea umeme kama ambavyo nimetaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuongeozana naye, kwa idhini yako kama ningepeta nafasi ningependa kwenda kushuhudia vijiji vitano ambavyo amevitaja vya Nyashilanga, Nyamikonze na Izunya ambavyo vitawashwa umeme Ijumaa ijayo. Lakini kwa ridhaa yako niombe kuongozana nawe Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili ili tukawashe umeme kwenye vijiji vyako kama ambavyo nimekusudia, ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Tatizo la maji katika Jimbo la Nyangh‟wale ni kubwa sana. Kuna mradi ambao unaendelea pale wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyapeleka Wilayani Nyangh‟wale. Mradi huo umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu na nimejaribu kuongea na wakandarasi wanadai kwamba wamesimama kuendeleza mradi ule kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Kuna mabomba mengi ambayo yameshasambazwa na yapo nje yanapigwa jua kwa zaidi ya miaka mitatu. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwapatia fedha hawa wakandarasi ili waweze kukamilisha mradi huo wa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kwamba Bunge lilipitisha Mfuko wa Maji na Mfuko huu tunashukuru kwamba kila mwezi fedha inatoka na ninyi wenyewe ni mashahidi huko mlikotoka kutokana na Mfuko huu tayari yale madeni yanalipwa na tunaendelea kulipa. Kama madeni hayajalipwa basi ujue kuna matatizo madogo madogo ya kiutendaji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Hussein mimi nalibeba niangalie kwa nini huko hakujalipwa ili tuhakikishe kwamba mradi huo wakandarasi wanalipwa ili waweze kuukamilisha.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali. Mheshimiwa Waziri wa Maji nimewahi kuonana naye mara nyingi sana kuhusu mradi wa maji kutoka Nyamtukuza kwenda mpaka Bukwimba. Mradi ule umepangiwa 15,000,000,000 mpaka sasa hivi Serikali imeshatoa bilioni 3.5 lakini cha ajabu hata kijiji kimoja hakijawahi kupata maji. Je Serikali ina mpango gani ili kuweza kukamilisha mradi huo wa maji ili wananchi wa Nyangh’wale waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Hussein tumeweka utaratibu kuhakikisha kwamba miradi yote ambayo ilianza tunaikamilisha kwanza kabla ya kuingia kwenye miradi mipya. Sasa hivi tunaendelea kuzunguka kubaini mahali popote pale ambapo pamehujumiwa Mheshimiwa Mbunge taratibu za kisheria zitafuatwa.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri ya Nyang’wale imeanzishwa zaidi ya miaka minne na pakatokea kosa la kiuandishi katika GN yake, badala ya kuandikwa Nyang’hwale Makao yake Makuu Karumwa, ikaandikwa Makao Makuu Nyang’hwale na taarifa hii tumeshaileta na tayari leo zaidi ya miaka miwili GN ya Nyang’hwale mpaka sasa hivi hatujaipokea. Je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini sisi Wana-Nyang’hwale, kuna tatizo gani ambalo limekwamisha kuitoa GN hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo makosa mengi, siyo kwako tu, lakini utaratibu na masahihisho yote yanafanywa na Katibu wa Bunge. Ikishatolewa ile GN, kama kuna marekebisho, inarudishwa na Katibu wa Bunge anaombwa kurekebisha. Bahati nzuri ya kwako iko tayari imerekebishwa na jana ilikuwa ofisini kwangu. Karibu uje uichukue. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Rais wa Awamu ya Nne alifanya ziara yake katika Wilaya ya Nyang’hwale na kuahidi ujenzi wa barabara kutoka Kahama –Nyang’holongo – Bikwimba – Karumwa – Nyijundu – Busolwa – Ngoma - Busisi (Sengerema) kwa kiwango cha lami. Pia 2010 Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano na yeye alifanya ziara katika Wilaya hiyo ya Nyang’hwale na kuahidi ahadi hiyo hiyo ya ujenzi wa barabara hiyo hiyo. Je, kauli ya Serikali ni lini upembuzi yakinifu utaanza kwa ujenzi wa barabara hiyo ya lami kutoka Kahama - Karumwa - Busisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia sana kuhusu ujenzi wa barabara hii na kwa sababu hiyo anafahamu mimi niliamua kupita barabara hii wakati nikitoka Mwanza na Geita na kweli nimeona umuhimu wa barabara hii walau sasa wataalam watakachokuwa wanaeleza nitakuwa nafahamu wanachosema ni nini. Nikuhakikishie, mara fedha zitakapopatikana kwa shughuli hii kazi hii itafanyika.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa swali langu lilikuwa la Wilaya ya Nyang’hwale na nimejibiwa kimkoa, Nyang’hwale imeshajipanga tayari na imetenga maeneo ya kuweza kujenga Chuo cha Ufundi. Je, Serikali imeshaweka ndani ya mpango 2018/2019 mpango huu wa kujenga VETA katika Wilaya ya Nyang’hwale?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali huwa mipango yake inaenda taratibu na Nyang’hwale ina vijana wengi ambao hawana ujuzi. Je, Serikali iko tayari kuchukua angalau vijana 50 na kuwapeleka katika maeneo mengine mbalimbali nchini kwenda kujifunza ujuzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kuhusu kama katika bajeti ya mwaka 2017/2018 tumetenga fedha kwa ajili ya kujenga Chuo cha VETA Nyang’hwale; nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba tunajitahidi kutenga fedha kadri tunapopata kwa ajili ya kujenga Vyuo mbalimbali vya VETA. Kwa sasa hakuna fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya Nyang’hwale; lakini nimwahidi tu kwamba kwa sababu mpango wetu ni kuhakikisha Wilaya zote zinakuwa na Vyo vya VETA tutaendelea kupangilia na kutafuta fedha na kujenga kadri inavyowezekana.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kama tuko tayari kupeleka vijana 50 kwenye Vyuo vingine nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama wao watajipanga kama Wilaya sisi tuko tayari kushirikiana nao kuhakikisha kwamba vijana hao wanapata nafasi katika Vyuo vingine.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Tatizo la maji la Halmashauri ya Makambako linafanana kabisa na tatizo lililoko Halmashauri ya Nyang‟hwale. Kumekuwa na miradi mingi ya usambazaji wa maji kutoka Ziwa Victoria, leo takribani miaka minne, miradi hiyo haisongi mbele kwa sababu ya ukosekanaji wa pesa. Je, Waziri anatuambia nini wananchi wa Nyang‟hwale, kuhusu miradi hiyo kwamba itaendelea kwa kasi ili tuweze kupunguza tatizo la maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, ndiye ambaye amekuwa ananipa nyaraka nyingi kutoka kwenye Halmashauri yake na ndiye ambaye alinikabidhi hata ile barua ambayo nilikuja kugundua kwamba mwaka 2013, Wizara ilitoa waraka kuhusu utekelezaji wa bajeti katika Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili tatizo la Nyang‟hwale linafanana na maeneo mengine pia, inawezekana kuna matatizo pia katika Halmashauri ya Mheshimiwa Mbunge, lakini kwa utaratibu tuliouweka sasa kama miradi ipo na uzalishaji upo, wakileta certificate tunalipa pesa; lakini tumegundua kuna maeneo ambayo uzalishaji umekwama kwa matatizo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Wizara ya Maji, tukishirikiana na Mheshimiwa Mbunge tutapeana taarifa, ili tuweze kuona ni nini kimekwamisha na kwa bahati nzuri tuko humu humu ndani kwenye Bunge. Nakumbuka Mheshimiwa Mbunge Lusinde kwake kulikuwa na shida, lakini tumeitatua na sasa hivi mradi unaendelea vizuri. Kwa hiyo, tupeane tu taarifa kuna tatizo gani ili tuweze kuiangalia Halmashauri. Pengine ndani ya Halmashauri kuna uzembe, tutauondoa ili kuhakikisha hii miradi inatekelezeka na hasa kwa kuzingatia kwamba sasa fedha inatolewa. Kwa hiyo, hakuna sababu kabisa kwa nini mradi usitekelezwe.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja. Ningependa kujua Wilaya ya Nyangh’wale Makao yake Makuu ni Karumwa, lakini nikiuliza kila mara hapa kuhusu GN ya Makao Makuu ya Wilaya Nyangh’wale ambayo ni Karumwa, leo hili swali ni mara ya tano, kila nikiuliza naambiwa GN iko tayari lakini cha ajabu mpaka leo hatujakabidhiwa katika Halmashauri yetu ya Nyangh’wale. Je, GN hiyo tutakabidhiwa lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba uniruhusu nitoke na Mheshimiwa Amar mara baada ya kipindi hiki twende kwenye Idara yetu ya Sheria ili tuweze kumpatia majibu sahihi.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa uzinduzi wa REA Awamu ya Tatu kimkoa wa Geita ulifanyika kwenye Wilaya ya Nyangh’wale, Kijiji cha Nijundu, mwenzi wa sita mwaka jana, lakini cha ajabu mpaka leo hii hata kijiji kimoja kati ya vijiji 35 vya Wilaya ya Nyangh’wale havijapelekewa nguzo.
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kupeleka nguzo hizo katika hivyo vijiji ambavyo tumepewa vijiji 35?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Amar kwa swali lake zuri, katika Mkoa wa Geita mkandarasi wake ni JV White Service Limited ambaye ameshaanza kazi, na kwa kuwa ameeleza kwamba mpaka sasa katika Wilaya yake, nataka niseme wakandarasi hawa walipoteuliwa unakuta Mkoa mmoja una mkandarasi mmoja, na Mkoa huo unaweza ukawa na Wilaya mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelekezo ya hivi karibuni katika Mkoa wa Geita mkandarasi alikuwa ameshaagiza nguzo takribani 3,000 na tulimpa maelekezo aende kila Wilaya. Kwa hiyo, kama mkandarasi mpaka sasa hivi hajafika katika Wilaya ya Nyang’wale naomba nimuelekeze na nimpe agizo kwamba kama vile tulivyotoa maelekezo tulivyokutana kikao cha tarehe 13 Januari, wakandarasi wote wafanye miradi Wilaya zote, wasijielekeze katika Wilaya moja.
Kwa hiyo, ninamuagiza mkandarasi JV White wa Mkoa wa Geita aelekee kwenye Wilaya zote na afanye kazi ya kuunganisha kupeleka hii miundombinu ya umeme kama ambavyo tulikubaliana katika Kikao cha tarehe 13 Januari, 2018.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mimi Mbunge wa Jimbo la Nyang’wale niliweza kujitolea na kujenga zahanati na kuikamilisha katika Kijiji cha Mwamakiliga na kwa kuwa niliweza kujitolea na kujenga wodi mbili na chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya ambayo ni Hospitali ya Wilaya ya Nyang’wale, nimeweza kuyafikisha majengo hayo kiwango cha asilimia 75 na nimekwama. Je, Serikali inasaidia vipi sasa kuweza kuifungua ile zahanati ya Mwamakiliga ili iweze kufanya kazi na kukamilisha majengo hayo yaliyo katika Kituo cha Afya Kalumwa ili yaweze kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Hussein Nassoro Amar kwa kujitoa kiasi hicho kwa ajili ya wananchi wa Nyangh’wale. Nimwombee dua Mungu apokee swaumu yake katika Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa sadaka hiyo kubwa aliyoitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimhakikishie kwamba sisi tutakuwa pamoja naye, bahati mbaya sikufika pale Kalumwa wala Mwamakiliga nilipokuja kwenye ziara ya Mkoa wa Geita, lakini baada ya Bunge hili nina ziara tena ya kuzunguka mikoani na nitapita Mkoa wa Geita na mahsusi nitafika kwako na kwa Mheshimiwa Musukuma nina ahadi yangu naikumbuka. Nitakapofika pale, nitaongea na wataalam wale tujue ni nini cha kufanya kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI ili kuweza kuunga mkono jitihada nzuri alizozionyesha. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza, lakini naomba nitumie nafasi hii kuwapa pole wananchi wangu wa Jimbo la Nyang’hwale kwa mauaji ya kikatili ambayo yamefanyika wiki iliyopita, akina mama wanne wamenyongwa kwa kutumia kanga zao na wawili wakiwa wajawazito na mauaji hayo yanaendelea kwa Wilaya za jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali dogo la nyongeza ni kama ifuatavyo; je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha kuisaidia Halmashauri ya Nyang’hwale ili kukamilisha ujenzi wa zahanati iliyopo Iyenze na Mwamakiliga? Serikali ina mpango gani kuisaidia Halmashauri?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naishukuru AMREF kwa kukamilisha majengo matatu yaliyopo pale Kituo cha Afya Kharumwa. Serikali ina mpango gani baada ya kukamilishwa majengo hayo kuendeleza kwa kutusaidia kuongeza vifaatiba pamoja na wauguzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kwa dhati kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada zake za kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyo bora ya afya. Yeye hakika ni mfano bora wa kuigwa kwa Waheshimiwa Wabunge wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza, anauliza Serikali kusaidia Halmashauri kumalizia zahanati, ni nia ya dhati kabisa ya Serikali kuhakikisha kwamba tunasaidia, lakini kinachogomba ni uwezo. Kwa hiyo, kadri bajeti itakavyokuwa imeboreka, hakika hatuwezi tukawaacha wananchi ambao Mheshimiwa Mbunge ameonesha jitihada tukaacha kumalizia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili baada ya kazi nzuri iliyofanywa na AMREF, suala la zima la kupeleka vifaa pamoja na wataalam, ili kazi iliyotarajiwa iweze kuwa nzuri, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba vituo vya afya na zahanati zetu zote zinafanya kazi. Muda siyo mrefu, wakati tunahitimisha, Mheshimiwa Waziri wa Utawala atakuja kusema neno kuhusiana na suala zima la kuajiri watumishi wa Serikali. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mwaka wangu wa nane nikiuliza swali la ahadi ya viongozi wetu ambao wamefika katika Jimbo la Nyang’hwale.
Mwaka 2010, Rais wa Awamu ya Nne alikuja akaahidi katika kampeni zake barabara ya lami kutoka Kahama – Nyang’olongo – Busolwa – Karumwa hadi Busisi, Sengerema kujengwa kwa kiwango cha lami. Mwaka 2015 pia Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli alikuja akaahidi vilevile.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hii ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kahama – Nyang’hwale mpaka Busisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuratibu ahadi za viongozi wakuu, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema. Tayari tunaendelea kufanya uchambuzi ili kuendelea sasa kujenga katika kiwango cha lami. Hata hivyo, kwa barabara hii Mheshimiwa Mbunge anayoitaja kuja Kahama ni barabara ambayo kwenye mpango mkakati tumeiweka. Tuwasiliane tu uone namna tulivyojipanga kwa sababu tunaendelea kupata fedha kidogo kidogo ili uweze kuona na wakati mwingine uweze kuwapa taarifa wananchi wa Nyang’hwale kwamba ni lini sasa ujenzi utakuwa umeanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zile hatua za awali tumeshaanza, tunatambua umuhimu wa barabara hii kuiunganisha kutoka Sengerema kuja Kahama. Pia wananchi wajue kwamba eneo la jirani kabisa kutoka Kahama Mjini kwenda Geita, Bunge limepitisha fedha za kutosha, tutaanza ujenzi wa barabara hii ya lami. Kwa maana hiyo tunatambua umuhimu wa kutekeleza ahadi za viongozi pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niwahakikishie tu kwamba tunaendelea kuhakikisha kwamba ujenzi wa barabara unafanyika.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Napenda kuipongeza Serikali kwa kutenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyang’hwale. Napenda niiulize Serikali, huduma ya X-ray kwa Wilaya ya Nyang’hwale ni shida sana. Kuna ajali mbalimbali ambazo zinatokea na kuifuata huduma ya X-ray karibu kilomita 110. Je Serikali ina mpango gani wa kuleta mashine ya X-ray katika Hospitali ya Wilaya ya Nyang’hwale? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge wamefanya vizuri kwenye suala zima la afya kwa maana ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati ni pamoja na kwa Mheshimiwa Amar. Naomba nimpongeze kwa dhati kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba X-ray zinakuwepo ndani ya vituo vyote vya afya na ndiyo maana katika maboresho ambayo yamefanyika hivi karibuni ni pamoja na kuongeza jengo la X-ray. Sasa kama X-ray zinakuwepo kwenye vituo vya afya sembuse hospitali ya wilaya! Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tukitoka hapa tuwasiliane tujue nini hasa ambacho kimetokea mpaka hospitali yake ya Wilaya ikose X-ray. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alikuja jimboni na akaahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kahama – Nyang’olongo – Bukwimba - Kalumwa - Busolwa hadi Busisi Sengerema na Rais wa Awamu ya Tano pia aliahidi hivyo hivyo. Je, Serikali ni lini itatenga fedha ya upembuzi yakinifu ili kuanza kuijenga barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua hii barabara Mheshimiwa Mbunge tumezungumza mara nyingi, ni barabara ambayo inaenda kuunganisha pia katika Jimbo la Msalala kuja Kahama Mjini. Kwa hiyo, kama tulivyozungumza tutaangalia sasa namna nzuri tuweze kuiingiza kwenye usanifu, kwa sababu zile barabara ambazo zinakwenda kuunganishwa na barabara hii Mheshimiwa Mbunge, unajua ile barabara inayokwenda Geita ni muhimu sana kwamba tutaweza kuwa na kipande cha kwenda Sengerema. Ni kipande kifupi Mheshimiwa Mbunge kinahitaji commitment ya fedha siyo nyingi sana. Kwa hiyo, azidi kuvuta subira tutaendelea kutazama kwenye bajeti zinazokuja.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Nataka nipate majibu kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kahama – Nyangolongo - Bukwimba, Kalumwa - Busolwa – Busisi, ni lini ujenzi huo utaanza kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein, Mbunge wa Nyang’wale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ziko barabara nyingi nchini ambazo ziliahidiwa na Mheshimiwa Rais na viongozi wengine wakuu. Ni kweli pia katika eneo hili la Nyang’wale kuna ahadi hii ya barabara kutoka Kahama kwenda hadi Busisi. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge labda baadaye tuonane ili angalau tuzungumze kwa upana ili apate details.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa wachimbaji wa Msalala kero zao zinafanana kabisa na kero ya Wilaya ya Nyang’hwale; nataka kujua ni lini Serikali itatoa leseni kwa wachimbaji wadogo wa maeneo ya Bululu, Ifugandi, Kasubuya, Isonda, Nyamalapa, Lyulu, Lubando na Iyenze ili hao wachimbaji waweze kupata hizo leseni na kuchimba ili waweze kuwa na uhakika wa uchimbaji wao na waweze kupata mikopo kutoka benki waweze kuchimba kisasa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumetenga maeneo mengi na tumetenga maeneo makubwa, zaidi ya maeneo matano katika maeneo hayo.

Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyozungumza katika majibu ya swali la msingi, nimewaomba wananchi wa maeneo hayo wachangamkie hii fursa, waje waombe tuwagawie maeneo haya. Mpaka sasa hivi tuna maombi mengi ambayo tayari yamekwishatolewa na sisi sasa hivi tuko katika mchakato wa kuwagawia wachimbaji wadogo na ni maeneo ambayo ni mazuri, yana reserve ya kutosha na wataweza kuchimba kwa faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo bado tunaendelea kuweka mchakato mzuri wa kuweza kufanya resource estimation katika maeneo mbalimbali ya uchimbaji ili tupate uhakika wa reserve na benki ziweze kuwaamini hawa kutokana na data ambazo tunaweza kuzitoa katika geological reports zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa fursa au kuwaeleza wananchi wa maeneo haya kwamba, wachangamkie fursa tuweze kuwagawia maeneo ya uchimbaji.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda nimuulize Waziri, kwa kuwa kuna mradi mkubwa wa maji kutoka Nyamtukuza katika Wilaya ya Nyang’hwale, kupita Kakora, Kitongo, Ikangala, Kharumwa, Izunya hadi Bukwimba ambao umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu, lakini Serikali ikiwa ikitoa pesa. Je, ni lini sasa mradi huu utakamilika na namwomba Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili aende akauone mradi huo kwa nini unaendelea kusuasua?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge. Kubwa pamoja na mradi huo, lakini tumeshalipa zaidi ya bilioni moja na milioni mia saba certificate yake kwa Mkandarasi anayedai, ili mradi usikwame.

Kuhusu kusuasua kwa mradi, sisi kama Wizara ya Maji, Wahandisi ama Wakandarasi wababaishaji tutawaweka pembeni, nataka nimhakikishie kabla ya Bunge tutakwenda Nyang’hwale katika kuhakikisha tunaenda kuukagua mradi ule na ikibidi kama Mkandarasi hana uwezo wa kutekeleza mradi huo tutamwondoa mara moja. Ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kuna tatizo kubwa upande wa watumishi wa Madini na TMA. Kumekuwa na ucheleweshwaji sana wa ushushaji wa mashine upande wa elution na kusababisha hasara kwa wenye elution na pia kwa wachimbaji:-

Je, Serikali imejipanga vipi kuongeza watumishi upande wa TMA na Madini ili ushushaji wa mashine zile za elution iwe wa kila siku ili kupunguza zile hasara wanazozipata watu wenye elution?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna tatizo kidogo kwa wafanyakazi ambao wapo katika Tume ya Madini. Kwa sababu baada ya mabadiliko ya Sheria TMA ilikufa, imeanzishwa Tume ya Madini. Kwa hiyo, sasa hivi wafanyakazi wote, walioko Mikoani wako chini ya Tume ya Madini. Tuna tatizo kidogo kwa wafanyakazi, lakini sasa hivi tuna kwenda kuongeza wafanyakazi wengi zaidi ili waweze kutoa huduma kwenye zile elution.

Mheshimiwa Spika, bado naendelea kusisitiza, watu wote wenye elution tumeona kuna matatizo makubwa sana yanayofanyika, watu wengine wanaenda kule wanafanya mambo ambayo hayaeleweki. Tunaendelea kudhibiti na tunaendelea kutoa tamko kwamba wanapo-load carbon kushusha dhahabu wasijaribu kushusha bila uwepo wa wafanyakazi wa Tume ya Madini. Tunakwenda kuongeza, lakini sasa hivi tunajitahidi kuhakikisha kwamba kila siku waendelee kutoa huduma hiyo.

Mheshimiwa Spika, namhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, tunaendelea kurekebisha.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba wake wa Wabunge ama waume wa Wabunge wana haki mbalimbali za kupata huduma kama vile kupita njia za VIP lakini cha ajabu ni kwamba wake zetu wanapata shida sana upande wa VIP. Je, wana haki ama hawana haki ya kupata huduma upande wa VIP, kama vile kwenye feri na viwanja vya ndege?

MWENYEKITI: Kwenye viwanja vya ndege?

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano viwanja vya ndege pamoja na feri.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la ndugu yangu wa Nyang’wale, Mbunge mahiri sana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli ulio wazi kwamba wake au waume au wenza wa Wabunge wanayo haki yote ya kutumia VIP na sijawahi kuona hilo tatizo ninapotembelea viwanja mbalimbali vya ndege. Kwa hiyo, Mheshimiwa kama lilikutokea tunaomba radhi lakini siyo kitu cha kawaida, wenza wa Wabunge huwa wanapata huduma zote stahiki za VIP.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kabla ya maswali kuna marekebisho kidogo katika maandishi aliyoandika hapa Mheshimiwa Naibu Waziri, inasomeka barabara ya Busisi - Busolwa, Nyijundu – Kharumwa - Bukwimbwa – Nyang’holongo siyo Nyang’hongo.

Mheshimiwa Spika, baada ya marekebisho hayo, napenda kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Kwa kuwa Serikali inakiri kutekeleza ahadi hizo za viongozi kwa kujengwa barabara ya lami kutoka Kahama hadi Busisi kupitia Kharumwa pindi pesa zitakapopatikana. Swali la kwanza, kwa nini wakati Serikali ikitafuta fedha za kutengeneza hizo kilomita nyingi tusitengewe fedha za kujenga kilomita 3 Makao Makuu ya Wilaya Kharumwa ili kupunguza vumbi kutokana na msongamano mkubwa wa magari uliopo pale?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Naibu Waziri amesema wanaendelea na kupeleka mawasiliano katika kata alizozitaja lakini Kata ya Nyijundu kuna matatizo ya usikivu. Je, Vodacom wako tayari kwenda kufunga mnara huo ili wananchi wa maeneo yale waweze kutuma na kupokea fedha kupitia Mpesa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tumezungumza mambo mengi sana kuhusu uboreshaji wa miundombinu katika Wilaya hii ya Nyang’hwale. Tulifanya discussion na Mheshimiwa Mbunge na anakumbuka nilitoa maelekezo upande wa wenzetu wa TANROADS Mkoa wa Geita kwamba tutazame Makao Makuu ya Mji ya Nyang’hwale. Kama tulivyokubaliana tutaanza na kilometa 2 pamoja na kuboresha mitaro iliyowekwa katika Mji wa Kharumwa, Makao Makuu ya Nyang’hwale. Kwa hiyo, nimtoe hofu tumejipanga kufanya Makao Makuu ya Nyang’hwale kukaa vizuri.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mawasiliano, tunaendelea na hatua ya kuboresha mawasiliano nchi nzima. Nimsihi tu Mheshimiwa Mbunge baadaye tuonane ili tuangalie kwenye orodha maana kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tutapeleka mawasiliano katika vijiji 521 ambavyo viko kwenye kwenye hatua ya manunuzi inawezekana vijiji vyake vikawepo. Kwa hiyo, tuonane tu, ninayo orodha hapa, nawakaribisha na Waheshimiwa Wabunge wengine ili tuone tumejipangaje kupeleka mawasiliano maeneo ambayo tumejipangia katika awamu hii ya nne. Ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Waziri na Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara kwa kutoa leseni 22 kwa wachimbaji wadogo wa Wilaya ya Nyang‟hwale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali kwa kuwa Wachimbaji wengi bado wako maeneo mbalimbali katika Wilaya ya Nyang‟hwale kama vile Isekeli, Isonda, Lyulu, Nyamalapa, Ifungandi, Shibalanga pamoja na Kasubuya, Je, Wizara imejipanga vipi kuwapa tena maeneo hayo wale Wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali imeshatoa leseni kwa Wachimbaji wadogo eneo la Bululu hivi karibuni uzalishaji wa dhahabu nyingi zitaanza kutoka lakini kuna jengo ambalo liko tayari kwa ajili ya ununuzi wa dhahabu. Je Serikali iko tayari sasa kukamilisha vibali vyote ili kufungua Jengo hilo la ununuzi wa dhahabu Wilaya ya Nyang'hwale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa katika majibu ya swali la msingi sisi kama Wizara ya Madini kwa kupitia Tume ya Madini tunaendelea kuhakikisha kwamba yale maeneo yote tunayoyaona kwamba yana madini ambayo wachimbaji wadogo wanaweza wakachimba basi sisi hatuhusiki kabisa kuwapa wachimbaji wadogo na kuchimba na hata katika majibu yangu ya msingi nimetoa wito kwa wale Wamiliki wote wanaomiliki maeneo makubwa ya utafiti na hawayaendelezi yale maeneo na utafiti hauendelei.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tuko tayari kuyafuta maeneo hayo, kufuta leseni hizo za utafiti na kuwapa wachimbaji wadogo ili waweze kuchimba, waweze kulipa Kodi na wao wenyewe waweze kujikimu katika maisha yao. Vilevile niendelee kumshukuru sana Mbunge kwa jinsi anavyofatilia na jinsi anavyokuwa karibu na wachimbaji wadogo katika Jimbo lake kwa sababu tunatambua Jimbo lake lina wachimbaji wadogo wengi sana.

Mheshimiwa Spika, nimuhakikishie katika swali lake la pili ameuliza utayari wa sisi Wizara na Tume ya Madini kuanzisha soko kwa ajili ya kuuza madini katika Jengo ambalo liko tayari nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge sisi tuko tayari na sasa hivi nawaagiza Tume ya Madini waende katika Jengo hilo wakague kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa eneo hilo au wa Wilaya ya Nyang‟hwale walione kama linatimiza vigezo mara moja soko hilo lifunguliwe na madini yaanze kuuzwa katika soko hilo. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imekuwa ikichukua vijana wengi kuwapeleka kwenye mafunzo ya JKT na baada ya mafunzo hayo, vijana wachache sana ambao wanapata ajira na vijana wengi wanakuwa wako mitaani. Kwa nini Serikali isije na mikakati ya hao vijana ambao wanamaliza mafunzo ya JKT kuwatafutia ajira mbalimbali kama vile kwenye migodi na maeneo mengine ili kuweza kupunguza vijana hao kuzurura mitaani na baadaye kuandaa bomu ambalo ni hatari? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza malengo ya kuwapeleka vijana JKT, haina maana kwamba vijana wote watakaopelekwa JKT wataajiriwa na vikosi vyetu vya ulinzi na usalama, ni kwa sababu idadi ya nafasi za ajira zilizopo katika vyombo vyetu hivi ni chache kulinganisha na idadi ya vijana ambao wanaingia JKT. Hata hivyo, kwa kuwa mafunzo haya ya JKT yanaimarisha uzalendo na kujenga ujuzi mbalimbali, kwa hiyo, ni imani ya Serikali kwamba maandalizi ya vijana ambao wanakwenda JKT yatawasaidia kuweza kutumia fursa nyingine zilizopo nchini za kuweza kupata ajira ikiwemo katika taasisi binafsi, taasisi za Serikali, pamoja na kujiajiri wenyewe.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kumuuliza Naibu Waziri, kwa nini Nyanghwale haitengewi pesa za maendeleo ya barabara ilhali kuna barabara ambazo zimeharibika vibaya yakiwemo madaraja kutoka Nyanghwale pale makao makuu kwenda Lushimba. Ni kwa nini Serikali haitutengei fedha za maendeleo ya barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Amar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ya CCM ambayo na yeye Mheshimiwa Mbunge anatokana na CCM anajua kabisa kumekuwa hakuna upendeleo katika kupeleka maendeleo katika nchi yote kwa ujumla. Kwa kuwa yeye ni sehemu ya Madiwani ni vizuri basi wakahakikisha kwanza wanaanza kutenga wao na sisi Serikali Kuu tukapata taarifa. Kimsingi hakuna hata eneo moja ambalo hatutengi fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Naibu Waziri alifanya ziara Vilayani Nyang’hwale mwezi wa Nne na kumpeleka kwenye mradi mkubwa wa maji kutoka Nyamtukuza, Kaluma, Bukwimba na kujionea hali halisi ya Wakandarasi wetu wanavyosuasua kuutekeleza mradi huo; na kwa kuwa aliwaita Wakandarasi Wizarani, tulikuja tukakaa nao pamoja; na Mkandarasi anayeitwa Pety, alielezea tatizo la kwamba amecheleweshewa fedha kwa ajili ya kuagizia pump nje:-

Je, Serikali inatoa tamko gani kukamilisha mradi huu kwa haraka iwezekanavyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Nyang’hwale kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Moja ya changamoto kubwa sana ya Sekta yetu ya Maji ilikuwa eneo la maji vijijini. Nilifika Nyang’hwale tukaona Mkandarasi akifanya kazi kwa kusuasua, baadhi ya kazi tulimnyang’anya tukaomba wataalam wetu wa ndani na anaona kasi inavyofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, tutalifanya hili jambo la haraka. Ile kazi ya kununua pump kama itakuwa imemshinda, tutainunua sisi Serikali ili wananchi wako waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa wakandarasi wa Wilaya ya Nyang’wale wamekuwa wakiuchezea ule mradi na kuchukua muda mrefu na fedha ya Serikali kupotena na juzi Mheshimiwa Naibu Waziri umefanya ziara ukajionea mwenyewe. Je, Serikali inawachukulia hatua gani ya haraka hao wakandarasi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nipende kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ambayo nimejionea mimi kwa macho nilipoenda hapo Nyang’wale, lakini kikubwa tulikuwa tunatabua kabisa na Waheshimiwa Wabunge wamelalamika sana, hususan utekelezaji wa miradi ya maji vijijini, imekuwa na changamoto kubwa sana na ndiyo maana sisi kama Wizara ya Maji tukaleta Muswada wa kuhakikisha kwamba tunakuwa na Wakala wa Maji Viijini.

Mheshimiwa Spika, tunalishukuru Bunge lako Tukufu kwamba limetupitishia haraka na Mheshimiwa Rais ameshatusainia ule Muswada na sasa ni Sheria. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Viongozi wa Wizara ya Maji, hakutokuwa na Mkandarasi ambaye atashindana na sisi, sisi tumejipanga vizuri, mkandarasi yeyote mbabaishaji ama awe mtalaam, kwa maana ya Mhandisi wa Maji, tutamchukulia hatua haraka iwezekanavyo katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma hii muhimu ya maji.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kwenye migodi yetu kuna watu ambao wamejiajiri kwa ajili ya kugonga kokoto zile zinazodhaniwa zina dhahabu, vibarua hawa wamekuwa wakilazimishwa kununua vitambulisho vya ujasiriamali na jana kumetokea sintofahamu, kuhusu hao vibarua na Mtendaji wa Kata ya Nyugwa na kusababisha wale vibarua kuondoka kwenye maeneo yao ya kazi kwa kulazimishwa kununua vile vitambulisho.

Je, Waziri, uko tayari kumwambia Mtendaji huyo aahirishe hilo zoezi? Kwa sababu hawa wanajiajiri wao kwa kugongagonga kokoto kwa mchanga mchana kutwa shilingi 2000, leo unakwenda kumlazimisha mgongaji kokoto huyu kitambulisho cha elfu 20. Je, Waziri uko tayari kusitisha hilo zoezi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mgogoro mkubwa ambao pengine ni kutokutambua au kutokuelewa. Tunasema wajasiriamali, tamko la Mheshimiwa Rais amesema, wajasiriamali wote walipe elfu 20, ambao hawazidi shilingi milioni nne kwa mwaka, yaani mapato yao, hilo ni tamko na tayari kutekelezaji umeanza. Sasa katika masuala ya uchimbaji wa madini, kuna kodi za upande wa uchimbaji wa madini, ambazo kweli tunazitoza, mtu anapopata dhahabu kwa mfano, analipa asilimia sita mrabaha analipa asilimia moja kwa ajili ya clearance, hizo kodi zinaeleweka, lakini hao ni wachimbaji ambao tunawatambua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale wachimbaji wadogo, maeneo mengi, ma-DC wamekuwa wakienda kule na kuhakikisha kwamba, wale kwa sababu wanatambulika na wenyewe kama wajasiriamali, waliojiajiri. Nimshauri tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba, ukichukua elfu 20, ukaigawanya kwa siku 365 ni shilingi 54 tu kwa siku, haiwezekani mtu anafanya biashara, asilipe chochote kabisa. Kwa sababu ile ile biashara ya mawe inaishia huko tu, tunayem-charge kodi kwenye upande wa migodi ni yule ambaye anapata dhahabu, hao wengine tunawapata vipi. Kwa hiyo, wapewe vile vitambulisho, kwanza tuwafahamu, lakini cha pili na wao wachangie kidogo pato la Taifa kwa kulipa shilingi 54 kwa siku, ambayo ni sawasawa na shilingi 20 kwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Nyanghwale ina vijiji 62 na mpaka kufikia leo hii ni vijiji saba tu ambavyo vimeshawashwa umeme na vijiji 13 tayari nguzo zimeshasimama. Nimeongea na mkandarasi kwa nini hajawasha vile vijiji 12 akadai kwamba, kuna upungufu wa nyaya.

Je, Waziri anatuambia nini kuhusu upungufu huo wa nyaya?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza kwa taarifa hiyo nashukuru kuipokea, kwanza umenipa jukumu la kufuatilia, nikuhakikishie nitalifuatilia hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na upungufu wa nyaya naomba nitoe taarifa kupitia Bunge lako Tukufu na kwa Watanzania hivi sasa hapa nchini hatuna shida na nyaya wala nguzo wala mita, changamoto inaweza ikawa ni utaratibu wa wakandarasi wenyewe namna ya kuhifadhi hivyo vifaa.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii Mheshimiwa Mbunge nimfuatilie mkandarasi tumfuatilie tujue changamoto ni nini, lakini tunachomuagiza kupitia Bunge lako Tukufu, napenda nichukue nafasi hii kumuagiza Mkandarasi wa White City anayetekeleza Mradi wa REA katika Mkoa mzima wa Geita, ikiwemo na Nyanghwale, achukue hatua za kuhakikisha vifaa vyote vinapatikana site na kazi ikamilike ndani ya wakati.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika Ilani yake ilieleza kwamba itatoa matibabu bure kwa wazee, kwa Wilaya ya Nyang’hwale kuna wazee takribani 6,000 na wazee hawa ni 100 tu ambao wanapata matibabu bure, Je, Waziri ananiambia nini? Hawa wazee 5,900 waliobaki watapata vitambulisho vya kuweza kupata matibabu bure?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwanza, naomba tukubaliane naye kwamba si wazee wote ambao tumeahidi kuwapa matibabu bure, tumeahidi kutoa matibabu bure kwa wale wazee ambao hawana uwezo, kwa hiyo hilo lazima tuwekane sawa. Na ni ahadi ambayo iko thabiti baada ya kufata procedure zote ambazo zinatakiwa tunaamini kabisa wazee hawa wamefanya kazi kubwa katika kutumikia taifa hili la Tanzania ndiyo wametufikisha hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba wale wote ambao hawana uwezo wanatibiwa bure kama ambavyo sera ya Serikali inavyoelekeza. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Ahadi hii ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami imeahidiwa kwa awamu mbili za Marais wetu, akiwemo Rais Jakaya Mrisho Kikwete, mwaka 2010 alikuja Jimboni kwenye kampeni na akaahidi barabara hiyo kwa ujenzi wa kiwango cha lami. Pia Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli naye alikuja 2015 naye aliahidi hivyo hivyo ujenzi wa barabara hyo kwa kiwango cha lami.

Swali ni lini fedha hizi zitapatikana kwasababu sasa hivi ni miaka 10 tunaahidiwa utafutaji wa hizo fedha, ni lini fedha hizo zitapatikana kwa ajili ya upembuzi yakinifu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili,kwa kuwa barabara hiyo inafungua mikoa mitatu na sasa hivi Wilaya ya Nyang’hwale inakimbia kiuchumi, barabara hayo yanaharibika na vumbi jingi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale, hususan pale Karumwa wananchi wanapata adha kubwa kwa vumbi kwasababu magari ni mengi.Je, ni lini Serikali itakomesha vumbi hilo na kuweza kuwanusuru wananchi wa Jimbo hilo na kuweza kuwanusuru wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale hususan Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale Karumwa kupata maradhi mbalimbali yakiwemo TB?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nassor Mbunge wa Nyang’hwale. Ni kweli barabara hii imeahidiwa na Mheshimiwa kama alivyosema Mheshimiwa wa Awamu ya Nne na Mheshimiwa wa Awamu ya Tano, lakini ni azma ya Serikali na ndiyo mpango wa Serikali kwamba katika Awamu hii ya Tano, kipindi cha pili, barabara zote zinazounganisha mikoa na wilaya lazima zitajengwa kwa kiwango cha lami. Kwahiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaamini katika kipindi hiki Serikali itapata fedha na barabara hii itajengwa. Barabara hii pia hata ukienda kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ipo imeahidiwa,kwahiyo ninahakika Serikali itatekeleza.Kwa maana hiyo tutakapokuwa tumejenga kwa kiwango cha lami maana yake hata lile vumbi linaloonekana Karumwa litakuwa limeondoka ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwanza nimpongeze Naibu Waziri wa Maji pamoja na Waziri wake kwa kuufuatilia Mradi wa Nyanghwale na hivi karibuni unaenda kukamilika, nawapongeza sana. Swali langu ni kwamba, kwa kuwa mradi huu unaenda kukamilika. Je, bajeti ijayo Serikali imejipanga vipi kwenda kuweka mpango wa kusambaza maji kwenye kata zifuatazo: Kata ya Busolwa, Nyanghwale, Ijundu, Kakola, Shabaka na Mwingilo. Je, Wizara imejipanga vipi kwenda kusambaza maji hayo kwenye bajeti ijayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Nyanghwale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuweka mipango mahususi kuhakikisha mradi ule ambao tayari upo kwenye utekelezaji kwenye hatua za mwisho unakwenda kukamilika.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali.

Kwa kuwa, Wilaya ya Nyang’hwale ina upungufu mkubwa sana wa Mahakama za Mwanzo, napenda kuiomba Serikali ianzishe Mobile Court katika Kata za Busolwa, Nyang’hwale, Kaboha na Shabaka; kwa kuwa Wilaya ya Nyang’hwale ina upungufu wa watumishi kama vile Mahakimu na Makarani.

Je, Serikali ipo tayari kuanzisha Mahakama hizo?

Swali la pili; je, Serikali ipo tayari kutuongezea Mahakimu pamoja na Watumishi kama vile Makarani?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nassor Amar Hussein, Mbunge wa Nyang’wale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza hili la mobile court tumelipokea na tutalifanyia kazi ili kuona uwezekano wa kata hizo ambazo hazijapata majengo ziweze kufikiwa na huduma hii.

Mheshimwia Spika, lakini vile vile, kuhusu watumishi tunaendelea kutegemeana na nguvu ya Serikali katika kupata uwezo wa kuajiri. Tunachoweza kuahidi tu ni kwamba tutakapopata nafasi ya kuajiri basi tutaangalia na suala la kupeleka watumishi katika maeneo haya ambayo Mheshimiwa Mbunge anayaeleza. Ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kidogo Wagogo mnapata shida kuita jina Hussein, jina langu ni Hussein Nassor Amar, ni Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kuishukuru Serikali kwa kuendelea kukamilisha mradi ya maji katika Jimbo la Nyang’hwale. Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja na tukafanya nae ziara. Tukawa na upungufu wa shilingi milioni 250 tu ili tuweze kukamilisha mradi huo. Je, Naibu Waziri, ahadi yake ataikamilisha lini ya kupeleka milioni 250 ili kuweza kukamilisha Mradi huo wa Nyang’hwale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Nassor wa Jimbo la Nyng’hwale, kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, hizi fedha tayari tuko kwenye utaratibu wa kuzipeleka, tutazipeleka katika awamu mbili, wiki ijayo tutajitahidi kupunguza awamu ya kwanza na baada ya hapo tutajitahidi kukamilisha kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya kutujengea Hospitali ya Nyang’wale ambayo imekamilika kwa asilimia 90; lakini majengo hayo ambayo yamekamilika, anayatumia Mkurugenzi kama Ofisi zake na jengo la Halmashauri lipo kwenye asilimia 34:

Je, Serikali ipo tayari kuongeza fedha ili kukamilisha jengo la Halmashauri ili Mkurugenzi aweze kuhama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nyang’wale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, majengo haya ya Hospitali za Halmashauri ambayo yamekamilika kwa asilimia 90 na kuendelea, maelekezo ya Serikali ni kuhakikisha majengo yale yanaanza kutoa huduma za awali za afya katika Hospitali hizo za Halmashauri. Ndiyo maana katika hospitali zote 67 za awamu ya kwanza tayari huduma za awali za OPD zinatolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kuelekeza kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Wilaya ya Nyang’wale ifanye utaratibu wa kuhakikisha huduma za afya katika hospitali hii iliyokamilika kwa asilimia 90 kwa wananchi, angalau kwa kuanza na huduma za OPD. Pili, Serikali katika mpango wa bajeti wa mwaka ujao itatenga zaidi ya shilingi bilioni 34 kwa ajili ya kukamilisha Hospitali zote za Halmashauri 67 ambazo zilianza ujenzi mwaka 2018/2019 ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Nyangh’wale.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali inaendelea kukamilisha ahadi za viongozi waliotangulia. Mheshimiwa wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Jakaya Kikwete alitembelea Wilaya ya Nyan’ghwale na kuahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kahama – Nyan’ghwale kwenda Sengerema, lakini mwaka 2015 Hayati Dkt. John Pombe Magufuli naye aliahidi hivyohivyo kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Swali, ni lini Serikali itatenga fedha za upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo la lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye majibu mengine, Barabara ya Kahama
– Nyn’ghwale – Sengerema pale Busisi ni barabara ambazo zimeahidiwa na viongozi wetu na ni barabara muhimu sana kwa kuunganisha maeneo haya. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Nyan’ghwale kwamba, barabara hii itafanyiwa upembuzi yakinifu mara bajeti tunayoiendea itakapokuwa imepitishwa. Kwa hiyo, baada ya kufanya hivyo taratibu nyingine kwa maana ya usanifu wa kina utafanyika, ikiwa ni hatua za awali kuelekea ujenzi wa lami wenyewe. Ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza nianze kuishukuru Serikali kwa kukamilisha kwenda kukamilisha mradi huu ambao ni wa kihostoria.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa sababu unaenda kukamilika mradi huu ambao utahudumia zaidi wananchi 51,500,000 mradi huu unaenda kukamilishwa mwezi Juni. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa yupo tayari kuambatana nami kwa ajili ya kwenda kuukabidhi mradi huo na kufanya sherehe kwa sababu mradi ule ni wa kihistoria kuanzia mwaka 1975? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuendelea kusambaza maji baada ya kukamilisha vijiji hivyo 12 katika kata zifuatazo: Kata ya Nyugwa, Nyijundu, Kaboha, Shabaka, Nyangh’wale na Busolwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kusambaza maji katika kata hizo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Amar Nassor Hussein, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nipende kupokea pongezi za shukrani kutoka kwako na pia suala la kuambatana na Mheshimiwa Mbunge, mimi na yeye tayari tulishafika pale Nyangh’wale, basi nitatoa nafasi hii kwa majimbo mengine ila nikishakamilisha nitaweza kutafuta nafasi ya kuja sasa kusheherekea.

Mheshimiwa Spika, mpango wa kusambaza maji katika kata alizozitaja Mheshimiwa Mbunge upo tayari kwenye mipango mikakati ya mwaka ujao wa fedha. Hivyo naomba tuendelee kuvuta Subira, tutakwenda mwaka ujao wa fedha kuona maji sasa yanaendelea kuwasogelea wananchi katika makazi yao.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa pamekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kwa watumiaji wa maji kubambikizwa bili:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kubadilisha mfumo wa kufunga mita ambao zitakuwa za malipo kwanza kama Luku ya umeme?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, Mzee wangu, Mzee Hussein. Kiukweli kongwe huvusha, tunakushukuru sana. Kubwa ambalo nataka kusema, kizuri huigwa. Tumeona wenzetu wa TANESCO za kuwa na mita hizi za Luku, nasi kama Wizara ya Maji tuna pre-paid meter ambapo tumeshaanza na tumefunga katika baadhi ya taasisi. Mkakati wetu na maelekezo kwa mamlaka zetu zote za maji ni kuhakikisha tunajielekeza huko katika pre-paid meter ili kuhakikisha kwamba wananchi wanalipa bili halisia bila ya usumbufu wowote. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hawa wanyamapori wamekuwa wakivamia vijiji na kushambulia wananchi hususan Wilaya ya Nyang’wale zaidi ya wananchi 10 wameliwa na fisi. Je, Serikali ina mpango gani wa kwenda kuwatembelea na kuwapa pole lakini pia kuwalipa kifuta machozi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Nyang’wale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpa pole sana Mbunge wa Nyang’wale na Wabunge wengine wote ambao wamekumbana na athari hii. Nimhakikishie kwamba hawa fisi ambao wako kwenye maeneo ya Nyang’wale na maeneo mengine yote yanayoathiriwa na wanyama hawa tutaenda kuwahamisha na tutawarudisha hifadhini, kwa sababu Nyang’wale ni eneo ambalo kidogo hifadhi ziko mbali na makazi ya wananchi lakini fisi wanaendelea kwenda kwenye maeneo hayo. Pia tutaongozana naye kwenda kuwaona wananchi hao na tutashirikiana kadri itakavyowezekana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa mimi Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale nilijitokea ujenzi wa kujenga nyumba ya mama na mtoto na jengo hilo tayari limeshakamilika lakini kuna mapungufu ya vifaa vya kutunzia watoto njiti yaani incubator.

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kusaidia Kituo cha Afya vifaa hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa wa Nyang’hwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kujitolea kujenga Jengo la Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto katika Jimbo lake la Nyang’hwale, huu ni mfano mzuri sana wa kuunga mkono nguvu za Serikali katika kuboresha huduma za afya, lakini naomba nimhakikishie kwamba tunatambua kwamba tunahitaji kuwa na vifaa tiba vya kutosha katika vituo vyetu hivi zikiwemo hizi incubator kwa ajili ya kusaidia watoto wachanga na mimi naomba nimhakikishie kwamba Serikali tunalichukua hili na lipo ndani ya uwezo wetu tutalifanyia kazi ili tuweze kupata incubator kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika kituo cha afya hiki kilichojengwa.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuwa barabara ya kutoka Busisi Nyang’wale kwenda Kahama imeahidiwa na viongozi wakuu wa nchi kujengwa kwa kiwango cha lami. Ni lini Serikali itaanza upembuzi yakinifu na ujenzi wa barabara hiyo kuanza mara moja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amar Mbunge wa Nyang’wale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni barabara ambayo katika ilani ya chama itafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika kipindi hiki. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute Subira fedha ikipatikana ya Serikali tutafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kama fedha itaruhusu basi tutaanza kuijenga kwa kiwango cha lami ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Serikali ilishapitisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Geita kwenda Nyang’hwale, tulikuwa tukipewa kilomita nne kila mwaka na sasa hivi tumeshajengewa zaidi ya kilomita nane; miaka miwili iliyopita hatujapewa tena hizo kilomita nne nne: -

Je, Serikali inatoa kauli gani; imeifuta hiyo barabara kwa ujenzi wa lami au la?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, alivyosema Mheshimiwa Hussein Amar Mbunge barabara ya Geita hadi Nyang’hwale ni barabara ambayo tayari imeshaanza kujengwa na Serikali haijaifuta barabara hiyo kuijenga kwa kiwango cha lami. Tumhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii itaendelea kujengwa kadri fedha itakavyoendelea kupatikana. Kwa hiyo, haijaifuta na haina mpango wa kuifuta, lakini itategemea na upatikanaji wa fedha hili kuendeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa huwa Shule ya Sekondari Msalala tumeweza kujenga madarasa na miundombinu yote kwa ajili ya Kidato cha Tano na cha Sita na pia Kata ya Nyangh’wale tumeweza kukamilisha ujenzi huo.

Je, ni lini sasa Serikali itatoa kibali ili tuweze kufungua shule hizo kwa Kata za Nyang’wale na Msalala? Tumeshakamilisha miundombinu, ni lini Serikali itatoa kibali ili tuweze kufungua shule hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Nyang’wale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema katika eneo lao wameshamaliza ujenzi wa shule za sekondari katika Kata za Nyang’wale pamoja na Msalala na anachotaka kujua tu ni lini Serikali itatoa kibali. Kwa sababu ameshalizungumza hapa nitaagiza wataalam wangu waende wakafanye tathmini pale wajihakikishie kama miuondombinu yote imeshakamilika. Wakishajiridhisha na hilo maana yake tutatoa kibali mara moja na shule hiyo itafunguliwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa leo ni mwaka wangu wa 12 nikiwa Bungeni, Rais wa Awamu ya Nne alituahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kahama, Nyang’hwale mpaka Busisi na Rais wa Awamu ya Tano naye pia aliahidi hivyo, na leo tuko Awamu ya Sita.

Je, Serikali inatuahidi nini ama inatoa kauli gani kuweka fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya hiyo barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara zote ambazo zimeahidiwa na viongozi wa Kitaifa zinakuwa zimeratibiwa na zinafanyiwa kazi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara ya Kahama kupita Nyang’hwale hadi Busisi ni kati ya barabara ambazo zipo kwenye Mpango na zitaanza kutekelezwa kadri fedha itakavyopatikana. Labda tuangalie kwa bajeti itakayofuata kama fedha itaruhusu na bajeti itaruhusu, basi tutaiweka kwenye Mpango huo ili iweze kufanyiwa upembuzi na usanifu wa kina. Ahsante. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyonge kwanza niipongeze Serikali kwa kutupatia watumishi 20 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 watumishi watatu kituo cha afya Karumwa na wanne kituo cha afya Nyang’ahwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023 kutokana na upungufu uliopo katika vituo vyetu vya Nyang’gwale ambavyo sasa hivi wilaya hiyo imekuwa na mfumuko mkubwa wa madini na watu wengi wamejazana katika wilaya hiyo huduma bado inaitajika sana kwenye kituo cha afya kama vile wilaya Je, Serikali iko tayari kutuongezea watumishi kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha nyingi katika sekta ya afya na kuweza kukamilisha zahanat zaidi ya 10 ambazo tunatarajia kuzifungua hivi karibuni. Je, Serikali imejipanga vipi kutupatia vifaa tiba na watumishi ili tuweze kuanzisha huduma katika zahanati hizo 10.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nassor Hussein Amar Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipokee pongezi zake nyingi kwa Serikali hii inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo imefanyika katika sekta ya afya. Lakini nimuhakikishie katika mwaka huu wa fedha 2021/2022 kuna vibali vya ajira ambavyo vitatolewa ili kuajiri watumishi kwenda kupunguza upungufu wa watumishi katika vituo vyetu vya afya kote nchini vikiwepo vituo vya afya katika halmashauri na Jimbo hili la Nyang’hwale. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Jimbo la Nyang’hwale katika vituo hivi vitapewa kipaumbele katika ajira inayokuja ili kuhakikisha tunapeleka watumishi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili ni kweli kwamba tumeendelea kujenga vituo vingi katika mamlaka ya Serikali za Mitaa na Serikali imeshafanya tathimini tunajumla ya vitu 1073 ambavyo tunatarajia ifikapo Juni mwaka huu vitakuwa vimekamilika na vitahitaji vifaa tiba, vitahitaji watumishi na tathimini imeshafanyika na maandalizi ya kupata vifaa tiba hivyo na watumishi imeshafanyika kwa hiyo iliyobakia ni suala la utekelezaji. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba vituo vyetu ambavyo vinaendelea kujengwa tayari tathimini inajulikana na kazi yakupeleka watumishi na vifaa tiba itakwenda kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanza nianze kumpongeza Waziri wa Wizara ya Maji pamoja na Naibu kwa kuendelea kutukamilishaia mradi wetu ambao ulikuwa unaitwa ni mradi kichefuchefu wa Wilaya ya Nyang’hwale kutoka Nyamtukuza kwenda Bukwimba kwamba sasa hivi maji hayo tayari tumeanza kuyatumia, lakini kuna tatizo moja maji yale si safi na salama, hawajajenga chujio la maji.

Je, Serikali inatuahidi nini kwenda kujenga hilo chujio la maji ili tuweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amar kutoka Nyang’hwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan huu mradi ulikuwa kichefuchefu lakini kwa sasa hivi kama alivyokiri mwenyewe Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada zake za ufuatiliaji pamoja na mashirikiano mazuri sasa hivi maji yanatoka. Kuhusiana na chujio ni hatua inayofuata na yenyewe pia tutakuja kukamilisha. Ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa sababu alipofanya ziara jimboni kwangu tuliweza kwenda eneo moja ambako mto umekatika, mawasiliano hayakuwepo na akaahidi kutoa fedha, na bahati nzuri fedha imeshatolewa, lakini mkandarasi aliye pale ni jeuri na hafanyi kazi kama inavyotakiwa, na fedha tayari anayo.

Je, Waziri yuko tayari kutusaidia kumsukuma huyo mkandarasi aifanye hiyo kazi mara moja ili kuepusha shida ya upitaji ya pale kwa sababu sasa hivi mvua zinaendelea kunyesha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein, Mbunge wa Nyang’hwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nilifika jimboni kwa Mheshimiwa Hussein na nilishuhudia hayo madaraja mabovu siyo moja tu mengine yameshaanza na kutekelezeka na baadha ya madaraja ambayo nilikuta katika jimbo lake ni madaraja ya miti, ambayo wananchi walikuwa wanalipishwa fedha. Sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tuliagiza fedha hizo ziende, sasa changamoto ambayo imetokea hapa ni mkandarasi kushindwa kufanya kazi kwa wakati. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge moja nimelipokea, lakini pili kutumia Bunge lako Tukufu namuagiza huyu Mkandarasi afanye kazi kwa wakati kinyume na hapo tutavunja mkataba na kupeleka mkandarasi mwingine ili akamalizie hiyo kazi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwanza nianze kuipongeza Wizara ya Maliasili kwa kushirikiana na wananchi wa Jimbo la Nyangh’wale kuweza kutokomeza wanyama wakali kama vile fisi ambao walipoteza maisha ya wananchi wangu wa Jimbo la Nyangh’wale. Sasa swali, je, ni lini Waziri atapanga ziara ya kuja kuwapa pole wananchi wa Jimbo la Nyang’wale lakini pia kifuta machozi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein, Mbunge wa Nyang’wale, kama Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuelezea changamoto hii ya fisi. Ni kweli kumekuwa na changamoto, fisi wanakuwa wamebaki kwenye maeneo ambayo siyo ya hifadhi na wamekuwa wakiwadhuru wananchi. Zoezi hili tulishaelekeza watendaji, pengine na hapa tena nitoe maelekezo kwamba watendaji walioko Kanda ya Mwanza, nikimaanisha magharibi tuandae operation ya kwenda kuwasaka wale fisi wote ambao hawako kwenye maeneo ya hifadhi na kuwarejesha kwenye maeneo ya hifadhi ili kunusuru hali za wananchi wa Jimbo la Nyang’wale. Ahsante. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa Serikali ilitenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa chujio la maji Wilayani Nyang’hwale kwenye bajeti ya 2022/2023 shilingi milioni 220.

Je, Serikali itatoa lini pesa hiyo na ujenzi uanze mara moja?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Hussein kwa sababu tulishafuatilia awali, mradi sasa umefikia hatua nzuri. Suala la chujio, hizi milioni 200 zitaletwa kwa wakati, mgao ujao pia tutapunguza hii fedha, angalau milioni 100 ili kazi ziendelee kufanyika.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi amekuwa akiniahidi sana kila mara kwamba pesa ya upembuzi yakinifu itakapopatikana barabara ya kutoka Kahama - Nyang’hwale itawekwa ndani ya mpango.

Je, ni lini pesa hiyo itapatikana na kuwekwa ndani ya mpango hiyo barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Nassor Mbunge wa Nyang’hwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge baada ya hapa tuweze kuangalia kitabu cha bajeti ili tuone. Naamini kwamba hii barabara itakuwa imetengewa fedha kwa ajili ya mpango kwa mwaka huu. Na kama kutakuwa haijatengwa basi tuangalie Wizara nini cha kufanya ili kuiwekea kwenye mpango wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara hii. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ilikubali kutoa Shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa tenki la kuchujia maji: Je, ni lini pesa hiyo itatolewa ili ujenzi huo uanze?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tulitoa ahadi na ahadi ni deni. Nimwahidi Mheshimiwa Mbunge ndani ya mwezi huu tutaoa pesa kwa sababu tumeshapokea pesa za Mfuko wa Maji na tutawapa kipaumbele katika Jimbo lake.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wilaya ya Nyang’hwale ina vijiji 62 kata 15 na OCD wetu pale Wilayani ana gari moja na si zuri sana; je, Wizara ina mpango gani wa kutuongezea gari nyingine polisi Nyang’hwale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amar, Mbunge wa Nyang’hwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema angalau yeye analo gari haliko vizuri sana lakini at least linatumika. Ushauri wetu gari hilo liendelee kukarabatiwa, lakini kama nilivyokwishasema wakati namjibu Mheshimiwa Asya, tunao utaratibu wa kununua magari na kuyapeleka kule ambako yanahitaji sana.

Kwa hiyo, Nyang’hwale, kama sehemu ya Mkoa wa Geita tutauangalia kulingana na upatikanaji wa hayo magari ili waweze kupata gari linawezesha OCD wetu kufanya kazi yake vizuri. Nashukuru.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Kuna bwawa kubwa pale Kijiji cha Nyamgogwa, Kata ya Shabaka tumeshafanya upembuzi yakinifu na tumeshapeleka andiko mezani kwa Mheshimiwa Waziri, tunahitaji milioni 500 kwa ajili ya kulifufua ama kuliandaa bwawa hilo ambalo linanufaisha zaidi ya vijiji 20. Je, Waziri anatoa majibu gani kuhusu andiko letu hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Amar, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge andiko lake kweli lipo mezani na hivi sasa kwa sababu ya ufinyu wa bajeti tumekuja na mfumo mwingine ambao pia umesaidia ujenzi wa skimu hizi ambao tunakwenda kuutambulisha mfumo huu. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba na yeye pia tutamuingiza kwenye mfumo huo ambao tumeufanya na tumeanza kuufanya kwa Mheshimiwa Mtaturu pale katika miradi ya Magonyi.

Mheshimiwa Spika, mfumo huu tutamchukua benki, tutamchukua na off taker wa mazao ya wakulima na kwa pamoja tunamwomba benki arekebishe miundombinu ya eneo lile, halafu mazao yatakayolimwa katika eneo lile tutamtafuta muuzaji ili basi itumike gharama hiyo ya benki kurekebisha. Wakati huo huo wauzaji wapate uhakika wa mazao yao ya kilimo na mwisho wa siku tutakuwa tumetatua changamoto ya ukosefu wa masoko ya wakulima wetu, lakini pia mradi huu utakuwa umekamilika. Mfumo huu unaitwa Tripartite Agreement ndiyo ambao tunaenda kuutekeleza katika miradi mingi ya skimu za umwagiliaji. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mradi wa Maji wa Nyantukuza, Jimbo la Nyangh’wale umeenda kukamilika na kwa sababu kuna ukame mkubwa wa maji, je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza maji kutoka chanzo hicho kwenye kata zifuatazo: Nyidundu, Nyalubele, Shabaka, Kaboha na Mwingilo, je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza maji hayo kwa haraka ili kupunguza adha hii ya ukame wa maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nyangh’wale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mradi ule ni mradi ambao tunatarajia uondoe matatizo ya maji katika kata hizo hizo ulizozitaja. Naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo sasa Wizara tunapambana kuona tunakabiliana na hili tatizo la ukame, tutafika na kuona uwezekano wa kuweza kusambaza maji katika kata alizozitaja Mbunge. Ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwanza naipongeze Serikali kwa uamuzi wake wa kujenga VETA katika wilaya 63 ikiwemo Nyangh’wale. Naomba niulize maswali mawili: La kwanza, ni kiasi gani cha fedha ambacho kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa VETA katika Wilaya ya Nyangh’wale? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ni lini ujenzi huo utaanza mara moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Amar, Mbunge wa Nyangh’wale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kiasi kilichotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo hiki katika awamu ya kwanza kwa sababu vyuo vitajengwa kwa awamu, tumetenga zaidi ya Shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi huu. Suala la lini; hivi sasa tayari Wizara imeshapeleka maombi kwa wenzetu wa Wizara ya Fedha, tunasubiri upatikanaji wa fedha hizo. Mara tu fedha hizo zitakapopatikana kutoka Wizara ya Fedha, basi huo ujenzi utaanza mara moja.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa hospitali yetu ya Wilaya ya Nyang’hwale inaendelea kukamilishwa na Mkurugenzi anatumia lile jengo la utawala.

Je, Serikali inatuambia nini kuhusu kumuhamisha Mkurugenzi huyo ili hospitali hiyo ianze kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli hospitali imekamilika, lakini kwa sababu ya ukosefu nwa jengo la utawala katika Halmashauri hiyo naomba nilichukue hili tutalifanyia kazi Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuhakikishe Hospitali hii sasa inaanza kutoa huduma na isitumike kama jengo la utawala katika Halmashauri hiyo. Ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, Tarafa ya Nyijundu tuna ujenzi wa Kituo cha Polisi, nami kama Mbunge nimeweza kushirikiana na wananchi hao kwa kuchangia matofali zaidi ya 2,000: Je, Serikali iko tayari kuchangia nguvu za wananchi ili tuweze kukamilisha kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Nyanghwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo spirit ya Wizara kwamba pale ambapo wananchi na wadau wao wamejitokeza kuanza ujenzi wa vituo hivi vya Polisi kwa ajili ya usalama wetu, sisi tutawaunga mkono. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kama ametoa matofali 2,000 na wadau wengine wametoa na ujenzi umeanza, basi katika ukamilishaji tutawanga mkono. Wakati wowote mtakapokuwa mmefikia hatua ya ukamilishaji, tafadhali tuwasiliane ili tuweze kukuunga mkono kituo hicho kikamilike na kuanza kazi, ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imeshatoa takribani shilingi milioni 150 kwa ajili ya upembuzi wa barabara kutoka Kahama - Nyangh’wale – Busisi; je, ni lini upembuzi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, tunategemea barabara hiyo ikamilike mwaka huu wa fedha, kwa maana ya usanifu wa kina.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa hadi leo ni mwaka wa kumi na mbili niko Bungeni na sijawahi kutembelewa na Waziri wa Mifugo katika jimbo langu, je, Waziri atakuwa yuko tayari kutembelea jimbo langu kuja kuongea na wafugaji ikiwemo na changamoto hizo za majosho na mambo mengine?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Nyanghwale, Mbunge ambaye pia ana wafugaji wengi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niko tayari kumtembelea Mheshimiwa Mbunge na jimbo lake. Najua wapo wafugaji wengi na kwa hiyo kumkosa Waziri wa Mifugo au msaidizi wake itakuwa ni tatizo. Sasa niko tayari kufanya hivyo kipindi hiki cha bunge tunaweza kutafuta wikiendi mojawapo twende au baada ya Bunge ili ya kwamba tuweze kukutana na wafugaji wake tutatue matatizo na changamoto zilizoko zinazohusiana na mifugo.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa kukamilisha mradi wa maji kutoka Nyamtukuza Wilayani Nyang’wale na sasa hivi maji tumeyapata lakini maji haya si safi na salama kwa sababu mradi ule haukutengenezewa chujio la kuyatibu yale maji.

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga chujio la kutibu maji ili wananchi wasije wakaugua na kupoteza fedha nyingi kwa ajili ya matibabu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Amor Mbunge wa Nyangwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee shukrani zake kwa sababu mradi huu ni ile moja ya miradi vichefuchefu na hapa tunampongeza Mheshimiwa Waziri ameweza kusimamia mradi sasa unatoa maji, suala la chujio ni suala linalofuata katika mwaka ujao wa fedha tutahakikisha na suala la chujio nalo linapewa nafasi.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Waziri Mkuu alifanya ziara pale Wilayani Nyang’hwale na akatoa ahadi ya ujenzi wa kilometa mbili Makao Makuu ya Wilaya; na Mheshimiwa Waziri Silinde alikuja pale akajionea lile vumbi ambalo linatimka pale katikati ya mji: -

Je, ni lini Serikali itajenga ama kukamilisha ahadi ya Waziri Mkuu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli mimi nimefika pale na ni kweli kabisa kwamba kuna ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi za viongozi wakuu ikiwemo ya Waziri Mkuu ambayo ameitoa, itatekelezeka kwa vitendo. Kwa hiyo, nimwondoe shaka na bahati nzuri nafahamu lile eneo. Kwa hiyo, lipo katika mpango wetu, tumeliweka, na tutalifanyia kazi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa ujenzi wa kilomita moja ya lami Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale pale Kalumwa, mkandarasi aliingia kwa kasi kubwa na akaweka vifusi na akashindilia; na baada ya hapo hajaweka lami; na leo zaidi ya miezi mitatu haonekani site; tatizo ni nini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Nyang’hwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tutalifuatilia jambo hili, na tutawasiliana na Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Geita na vilevile wa Wilaya ya Nyang’hwale kujua ni kwa nini mkandarasi huyu amekwama kuendelea na kazi hii? Vilevile nitakutana na Mheshimiwa Mbunge tuweze kulitafutia majawabu leo hii hii hapa tukiwa katika viwanja vya Bunge. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa VETA Wilaya 63 na Wilaya ya Nyang’hwale tayari upembuzi yakinifu umeshafanyika; je, katika Wilaya 63 na Nyang’hwale ikiwemo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwamba vyuo hivi vinaenda kujengwa kwenye Wilaya na kama tayari tumeshafanya upembuzi yakinifu, tafsiri yake ni kwamba tumeshakuja kufanya Geotechnical Survey, Topographical Survey pamoja na Environmental and Social Impact Assessment. Kama shughuli zozote zimeshafanyika kwenye eneo lako, is likely kwamba chuo hicho kinakuja kujengwa kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kuambatana nami baada ya Bunge hili, kwenda Wilayani Nyang’hwale kuonana na akina mama wakongwe zaidi ya 80 ambao wameorodheshwa na zaidi ya miaka mitatu hawajapata stahiki yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nipo tayari na tutaongozana ili kwenda kuwatambua na tuzungumze kwa pamoja. Siyo tu utambuzi wa hawa, lakini pia suala zima la changamoto zilizopo katika eneo lake la utawala kuhusiana na mradi wetu huu wa TASAF. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.

Kwa kuwa, Serikali imeshatoa Milioni 300 kwa ajili ya upembuzi wa barabara ya kutoka Kahama - Nyang’wale – Busolwa - Busisi - Sengerema kwa kiwango cha lami, na huwa unanijibu majibu ya kisiasa nataka leo unijbu, ni lini upembuzi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tukishatenga fedha kwenye bajeti nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita iko makini, ikishatenga maana yake tunatekeleza, isipokuwa tu ni hatua kuwa hatua ndefu.

Mheshimiwa Spika, barabara inayotwa siyo barabara fupi Kahama Nyang’wale - Ngoma hadi Busisi ni parefu, kwa hiyo iko tayari inafanyiwa kazi nakuhakikishia baada ya kukamilika ndiyo sasa tutajua gharama ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nianze kuipongeza Serikali ya Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusambaza maji vijijini. Je, wizara iko tayari kushusha bei ya maji Wilaya ya Nyang’hwale kutoka 1,700 kwa unit na kufanya iwe 1,500 ili kuhamasisha wananchi wengi kuweza kujiunga na mtandao huo wa maji? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni haki ya mwananchi kupata huduma ya maji lakini mwananchi naye asisahau anao wajibu wa kulipia bill za maji. Kwa hiyo, ameonesha hiyo changamoto na nimuombe basi Saa Saba tuweze kukaa na timu yetu tuone namna nzuri ya kuhakikisha wana Nyang’hwale tunatatua changamoto hiyo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa Wilaya ya Nyang’hwale wachimbaji wadogo wadogo wameendelea kuvumbua maeneo mbalimbali kama vile Isonda, Igalula, Isekeli, Shibalanga, Ifugandi, Rubando, Lihulu, Bululu pamoja na Mahagi.

Je, Wizara ina mpango gani wa kupeleka mitambo ya kufanya utafiti ili uchimbaji ule uwe wa kuendelea?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kupeleka mitambo ya kuwasaidia wachimbaji wadogo, Wizara kupitia taasisi yake ya STAMICO imeagiza mitambo mitano ambayo tayari ilishaagizwa na mingine mitano pia imeshaagizwa kwa ajili ya kuwa na zana mahsusi kwa ajili ya kusaidia uchimbaji wa wachimbaji wadogo waweze kufanyiwa upimaji wa maeneo yao wajue aina ya madini na kiasi kinachopatikana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa upembuzi yakinifu nimekuwa nikijibiwa kila mara kwamba utakamilika. Upembuzi huu ni kwaajili ya barabara kutoka Kahama – Nyangh’wale – Busisi. Je, ni lini upembuzi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, barabara hii ni ndefu na upembuzi unaendelea kadiri muda unavyokwenda, ni kwamba tu hatuwezi tukaruka hatua. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakamilisha upembuzi na baada ya hapo hatua zitakazofuata itakuwa ni kutafuta fedha kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona.

Kwa kuwa, Kituo cha Polisi cha Nyang’hwale hakina hadhi na ni kidogo na kimechakaa. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi cha kisasa cha Wilaya hapo Nyang’hwale?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni kweli maeneo mengi vituo vya Polisi ikiwemo hiki cha Nyang’hwale ni vya muda mrefu, kwa hiyo vimechakaa. Kama nilivosema, moja ya maeneo ambayo Serikali tunaweka mkazo ni kuboresha vituo hivi vya Polisi, hicho ni mojawapo ya Kituo cha Polisi ambacho tutaangalia namna ya kukirekebisha, kukarabati kadri ambavyo fedha zitapatikana. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza naishukuru Serikali kwa kupeleka fedha zaidi ya shilingi milioni 240 kwenye vituo hivyo vya afya, nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa tuna upungufu wa wahudumu wa afya kwenye vituo vya afya ikiwemo Kafita, Nyijundu, Kalumwa na Nyangh’wale na zahanati zote za Jimbo la Nyang’hwale; je, Serikali iko tayari kutupelekea wahudumu wa afya ili kuweza kukidhi mahitaji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa pamoja na kwamba vituo vya afya vimejengwa vingi lakini bado tuna uhitaji wa ujenzi wa kituo cha afya kwenye Kata ya Busolwa; je, Serikali iko tayari kutujengea kituo cha afya kwenye Kata ya Busolwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Amar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napokea shukrani zake kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi za vifaa tiba katika Jimbo la Nyangh’wale na nchi nzima kwa ujumla. Kuhusu upungufu wa watumishi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote tumekuwa mashahidi, katika kipindi cha miaka hii miwili Serikali imeajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya zaidi ya 17,000 na kuwapeleka katika vituo vyetu vipya pamoja na vya zamani ambavyo vinaendelea kutoa huduma. Kwa hiyo zoezi hili ni endelevu, ajira zitaendelea kutolewa kwa awamu ili kuhakikisha kwamba vituo hivi vinaendelea kupata watumishi wa kutosha na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili linalohusiana na Kituo cha Afya cha Busolwa, Serikali imeshaweka mkakati wa kujenga vituo vya afya vya kimkakati katika maeneo ya kimkakati, tukizingatia umbali kutoka kituo cha karibu zaidi, idadi ya wananchi katika maeneo hayo na aina ya jiografia ya eneo husika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya tathmini kuona Kata ya Busolwa kama inakidhi vigezo, na kama inakidhi vigezo tutaanza na mapato ya ndani ya Halmashauri na baadaye Serikali itaona uwezekano wa kuongeza fedha kwa ajili ya kukamilisha, ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Gereza la Wilaya ya Nyang’hwale kwa sababu huduma hiyo tunaipata kwa umbali mrefu sana zaidi ya kilometa 100? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, japo swali ni la polisi, lakini nakubali tu kwamba ni nia ya Serikali kadri huduma za magereza zinapokuwa mbali zinaongeza gharama za kusafirisha washtakiwa au mahabusu kutoa eneo lile kwenda enei lingine ambapo bado inakuwa ni sehemu ya gharama za Serikali. Nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu nina ahadi ya kutembelea Jimbo lake la Nyang’hwale tutajiridhisha kuona eneo kama lipo la kutoa ili Jeshi la Magereza liingize katika mpango wake wa ujenzi, nashukuru. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia vijana wa Wilaya ya Nyang’hwale kupitia mpango wake wa kuwanyanyua vijana kupitia kilimo? Wilaya ya Nyang’hwale hatuna mazao ya kudumu ya kibiashara; je, Serikali ina mpango gani wa kuchukua udongo na kufanya utafiti ili na sisi tuweze kuwa na miche ama mazao ya kibiashara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mkakati wa Serikali wa kuhakikisha ya kwamba tunawahusisha vijana wengi kwenye kilimo na ndio maana tumekuja na programu hii ya BBT. Hatua ya awali ambayo tunaifanya kwanza kabisa tunashirikiana na mamlaka za mikoa husika kwa ajili ya utengwaji wa maeneo; na eneo la pili hivi sasa tumeanza kuichora ramani ya Tanzania kwa afya ya udongo ili tujue sehemu gani wanaweza kulima zao gani na sisi tuwasaidie jambo gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari njema ni kwamba katika mwaka ujao wa fedha tumekwenda kununua mitambo ya kisasa ya upimaji wa afya ya udongo. Badala ile ya mahabara tu tutakuwa pia na mobile laboratory ambazo zitakuwa zinatembea kupima afya za udongo. Tukija kukupimia kwako mkulima tutapima hapo hapo na nitakupa cheti hapo hapo kitakwambia kwamba katika udongo huu unaweza kulima mazao ya aina gani na utumie mbolea aina gani, na hiyo ndio itakuwa mkombozi kwa wakulima wan chi yetu ya Tanzania.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa, kumekuwa na taarifa kwa wachuuzi wadogo wadogo maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Nyang’hwale, kwa kupungukiwa na silver ama sarafu ndogo ndogo kuanzia shilingi 50, 100, 200 na 500 na kusababisha mfumuko wa bei kwenye masoko yetu madogo madogo.

Je, Wizara inalitambua hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ninamuomba tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hili tulichukue tukalifanyie kazi, tukafuatilie tuone kwamba hivyo ndivyo hali halisi ilivyo na tuone ni njia gani ya kulipatia utatuzi suala hilo. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Mji wa Kharumwa unazidi kupanuka na matengenezo yanafanywa ya mara kwa mara kwenye barabara zetu za mitaa pale Kharumwa, lakini zinaponyesha mvua barabara zile huwa zinaharibika kwa ajili ya ukosefu wa mitaro. Je, Wizara iko tayari kutenga fedha kwa ajili ya kujenga hiyo mitaro ili kunusuru uharibifu wa barabara hizo wakati wa mvua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TARURA imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya maboresho ya Mji wa Kharumwa kule Wilayani Nyang’wale anakotoka Mheshimiwa Amar na tutaendelea kuangalia ni namna gani tunapeleka fedha ya kutosha kadri ya upatikanaji wake, kwa ajili ya kuboresha mazingira ya mji huu hasa ujenzi wa mitaro ambayo upo kule Wilayani Nyang’wale. Nimtoe shaka Mheshimiwa Mbunge, yeye ni shahidi vile vile kwamba TARURA imeongezewa fedha zaidi ya mara tatu ya ile iliyokuwepo mwaka wa fedha 2020/2021 na hii ni commitment kubwa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Watanzania kwa kutenga fedha ya kutosha kwa TARURA kuhakikisha barabara nyingi zaidi zinatengenezwa.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Waziri utakuwa tayari baada ya Bunge hili kufanya ziara kuja kuangalia nguvu za wananchi na Mbunge katika ujenzi wa Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Nyijundu, Wilayani Nyang’hwale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuahidi nikitoka Shinyanga kwenda Nyag’hwale ni karibu sana, kwa hiyo, wakati namaliza ziara yangu Shinyanga pale Kishapu, kituo kitakachofuata ni Nyag’hwale ili kuona juhudi za wananchi hatimaye tumuunge mkono Mheshimiwa Mbunge. Nashukuru sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.

Kwa kuwa kituo cha afya cha Kata ya Nyang’hwale kinatoa huduma zaidi ya miaka 30 kuhudumia kata zifuatazo; Kata za Shabaka, Kaboha, Busolwa, Nyabulanda, Nyijundu, Mwingiro hakina huduma ya x-ray je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma hiyo ya x-ray kwenye Kituo cha Afya cha Nyang’hwale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia imeweka kipaumbele katika kuhakikisha wananchi wake wanapata afya iliyobora kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya afya vilevile kwenye vifaa tiba na katika bajeti ya mwaka 2023/2024 Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 112 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba ikiwemo vifaa vya mionzi kama vile x-ray na pale tutapoanza ununuzi wa vifaa hivi tiba tutaweka kipaumbele kwa ajili Kituo cha Afya cha Kata ya Nyang’hwale anapotoka Mheshimiwa Amar kule. (Makofi)

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale wanapenda kujua upembuzi yakinifu kuhusu barabara yao kutoka Kahama – Nyang’hwale mpaka Busisi, Sengerema utakamilika lini? Leo takribani miaka mwili tunaulizia jambo hili hatupati majibu, naomba majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita nilijibu pia hili swali. Hii barabara inahusisha mikoa takribani mitatu; Shinyanga, Geita na Mwanza. Upande wa Mwanza wanafanya Mkoa wa Mwanza, lakini kwa upande wa Shinyanga na Geita wanaosimamia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ni TANROADS Makao Makuu.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba walishakamilisha taratibu zote za kumpata Mhandisi Mshauri. Kwa hiyo, kazi inategemewa kuanza kwa sababu ni utekelezaji wa bajeti hii na wataendelea pia katika mwaka ujao wa fedha kuhakikisha kwamba wanakamilisha kuunganisha hiyo mikoa mitatu kupitia hiyo barabara aliyoitaja, ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kumalizia zahanati na kuna baadhi ya zahanati ambazo tumeshakamilisha katika Wilaya ya Nyangh’wale. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kupeleka vifaa tiba na kuweza kuzifungua zahanati hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Nassoro Amar, Mbunge wa Nyangh’wale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna maeneo mengi ambayo mpaka sasa wameshamaliza vituo vya afya pamoja na zahanati. Sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tumeshafanya uagizaji wa vifaa tiba na baadhi ya tender zipo katika hatua za mwisho kwa ajili ya kuagiza hivyo vifaa. Kwa hiyo mara vifaa hivyo vitakapofika basi tutapeleka katika vile vituo ambavyo vimekamilika ili kuhakikisha kwamba zahanati hizo pamoja na vituo vya afya vinafunguliwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amefungua neema katika Wilaya ya Nyang’ahwale kuwa na machimbo mengi sana ya dhahabu na kuwa kuna mzunguko mkubwa wa kiuchumi ikiwemo ongezeko la vipando vya magari pamoja na pikipiki; pamekuwa panapitika magari zaidi ya elfu moja kwenye makao makuu ya wilaya na kutimua vumbi jingi. Kwa kuwa Serikali imesema itajenga hizo kilometa mbili; je, ni lini kwa kauli ya Serikali ujenzi huo utaanza?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; niishukuru Serikali kwa kuweka mpango wa kujenga kilometa 123 kwa kiwango cha lami kutoka Nyankumbu – Nyalubele – Ijundu – Kharumwa - Bukwimba mpaka Nyang’holongo. Je, ni lini sasa ujenzi huo utaanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang’hwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kilometa hizo mbili ni sehemu ya hiyo barabara ambayo tunategemea kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili baada ya kukamilisha tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, ni lini tutaanza ni pale ambapo tutakamilisha hatua za awali za kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni hatua za awali baada ya hapo tutaanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amesema kuna uchimbaji wa wachimbaji wadogo kwenye maeneo ya leseni, na kuna wachimbaji ambao wanachimba kwenye eneo la rashi; lakini wachimbaji hao wadogo wanatumia fedha na gharama kubwa kutoa ile mifuko ndani ya ardhi. Unakuta anatoa mifuko 100, lakini wasimamizi wa kwenye rashi wanachukua asilimia 40: Kwa kuwa wao husimamia tu: Serikali inatoa kauli gani ili kuwasaidia hawa wachimbaji wadogo, ipunguze hiyo mifuko 40? (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati njema Mheshimiwa Amar ni mchimbaji mzoefu na anajua sekta hii. Tulikotoka ilikuwa mchimbaji mdogo anachimba anatoa mawe, msimamizi au miaka ile walikuwa wanaitwa ma-digger, yeye peke yake anachukua asilimia 70. Serikali tulitoa mwongozo maalum wa usimamizi wa rash na tukasema hivi, katika uchimbaji wowote unaofanyika mahali popote kwenye maeneo yasiyokuwa rasmi, mgawanyo utakuwa kama ifuatavyo: asilimia 15 itakwenda kwa mwenye shamba, asilimia 15 itakwenda kwa msimamizi, na msimamizi fedha hiyo atakayoipata itatumika kwa ajili ya kujenga miundombinu kama vile vyoo na huduma mbalimbali maeneo ya uchimbaji huo. Asilimia 70 yote inayobaki ni kwa ajili ya mchimbaji ambaye yuko kwenye shimo anayetumia nguvu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaratibu ni huo na mwongozo upo. Kama kuna mahali unakiukwa, tuwasiliane Mheshimiwa Mbunge ili tuchukue hatua. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa kusikia kilio change cha ujenzi wa Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Nyang’hwale swali. Ni lini Serikali Itaanza ujenzi wa Gereza la Wilaya ya Nyang’hwale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Amar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa gereza la Nyang’hwale kama lilivyoombwa na Mheshimiwa Amar utaanza baada ya kuwa tumepata fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo, kwa kweli kwa mwaka ujao hatuna bajeti hiyo, lakini tutaingiza kwenye kipaumbele kutokana na mahitaji ya Wilaya ya Nyang’hwale, nashukuru. (Makofi)

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwanza niipongeze Serikali na Wizara yake ya Maji kwa kuzidi kutukamilishia mradi wetu wa maji na maji yameshaingia maeneo mbalimbali katika Wilaya ya Nyang’hwale, lakini wananchi wanalalamika bei ya maji ni kubwa ukilinganisha na mjini. Nyang’hwale tunalipa shilingi 2500 kwa unit moja wakati Mji wa Geita na Mwanza wanalipa 1,350.

Je ni lini Serikali itatoa kauli kwa Wilaya ya Nyang’hwale kupunguza bei ya maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amar, Mbunge wa Nyang’hwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Nyang’hwale pamoja na maeneo mengine kama Karatu tunafahamu bei bado si rafiki sana kwa wananchi na hii ilisababishwa na utekelezaji wa mradi, lakini kama Wizara tunaendelea kufanya mapitio ili kuona kwamba bei zinakwenda kuwa bei rafiki kwa wananchi. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, napenda kujua tunao ujenzi wa kilomita moja ya lami Mji wa Karumwa, takribani miezi 24 na tuta lile limenyanyuliwa zaidi ya mita moja, mvua zinaendelea kunyesha na maji yanaingia kwenye nyumba za watu imekuwa ni kero kubwa. Miezi 24 kilomita moja haijakamilika, nataka kauli ya Serikali ni lini kilomita moja hiyo itakamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninakiri kwamba, Mheshimiwa Mbunge amekuja ofisini kufuatilia hili suala, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mji wa Karumwa, nimeongea na Meneja wa Mkoa wa Geita kwamba hiyo barabara itakamilishwa. Sasa hivi kilichokwamisha tu ni kwamba mvua inanyesha na baada ya hapo kwa sababu ipo chini ya Meneja wa Mkoa wa Geita, wataikamilisha hiyo barabara ikiwa ni pamoja na kutengeneza hiyo mifereji ambayo inaleta adha kwa wananchi wa Karumwa, ahsante. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa wananchi wengi Wilaya ya Nyang’wale wamefungiwa mita za maji na kushindwa kuendelea kutumia maji yale kwa ajili ya mita zao kwenda speed sana na kuwa bili kubwa;

Je, Serikali ipo tayari kutuma tume kwenda kuchunguza mita hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Nyang’wale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tutatuma wataalam waweze kwenda kuchunguza mita hizo ili wananchi waweze kulipia bili kulingana na matumizi yao.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua Serikali ina mpango gani wa haraka kuzuia utekaji unaoendelea katika Jiji la Dar es Salaam na kupoteza maisha ya watu, kwa sababu, utekaji huu unaendelea kila kukicha? Nataka kujua, Serikali ina mpango gani wa haraka kuzuia jambo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussien Amar, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunafuatilia kwa karibu matukio aliyoyaeleza kwamba yanaendelea kutokea katika Jiji la Dar es Salaam kwa madhumuni ya kudhibiti na kuwachukulia hatua za kisheria wale ambao wanahusika katika hicho kilichoitwa utekaji.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa sijaridhika sana na haya majibu, lakini kwa kuwa Mheshimiwa Waziri anasema kwamba mzabuni tayari ameshapatikana…

SPIKA: Mheshimiwa ngoja, hujaridhika kwamba ni majibu hayana..., yaani siyo ya kweli, hayana uhalisia ama? Kwa sababu kanuni zetu zinataka swali lijibiwe kikamilifu. Hujaridhika kwa namna gani?

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, majibu haya hayana uhalisia.

SPIKA: Fafanua.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, naomba nifafanue. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema kwamba mzabuni tayari amepatikana na anaenda kupata Msanifu Mshauri na kuianza kazi hiyo mwaka 2024 na kumaliza 2025. Kwa nini nasema kwamba halipo sawasawa, fedha ambayo ilikuwa imetengwa kwa ajili ya usanifu kwa mwaka wa fedha 2021 na kutolewa mwaka 2022, fedha hiyo ilitengwa shilingi milioni 300 na kutolewa shilingi milioni 150 kwa ajili ya kuanza kazi hiyo mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, leo ananiambia anaenda kupatikana Msanifu mwaka 2024 na kumaliza kazi hiyo mwaka 2025, hapa majibu haya yanakinzana.

Mheshimiwa Spika, niendelee?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hata katika jibu langu la msingi, siyo kwamba Mhandisi Mshauri amepatikana. Ila tayari zabuni ya manunuzi kumpata huyo Mhandisi Mshauri, ndiyo tunakwenda kutangaza.

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti ya 2022/2023 tulitenga bajeti kwa ajili ya kuanza kazi hiyo. Hiyo bajeti ambayo imetupelekea sisi kuanza kutangaza na hata katika mwaka huu wa fedha pia kwenye vitabu vyetu vya bajeti, bado tumetenga katika kuendelea kufanya hiyo kazi ya usanifu wa kina wa barabara hiyo, ahsante.

SPIKA: Sawa, hapo kwenye jibu lako panaposema hivyo, kazi zitakamilika mwezi Februari, 2025. Ni kazi zipi, hizi za usanifu ama za ujenzi?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni kazi za usanifu, kwa barabara ilivyo haiwezi ikafanyika…
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, sawa.

Mheshimiwa Spika, kwenye kikao cha ushauri wa barabara cha mkoa, mwaka 2022 niliambiwa zimeshatoka shilingi milioni 150 na kazi ya upembuzi yakinifu imeanza…

SPIKA: Mheshimiwa Nassor, ngoja. Ili taarifa zetu zikae vizuri kule ulipoambiwa siyo Serikali Kuu inayokuwepo, ni nyinyi watu wa mkoa ule ndiyo mpo kule. Kwa hiyo nilitaka ufafanuzi huu ili taarifa zetu zikae vizuri, kwa hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri amefafanua kwamba kazi zitakazokamilika ni hizi zinazoendelea mpaka sasa.

Sasa kile kikao kule, wewe ulikuwepo ila mimi sikuwepo wala Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa hiyo hawezi kufafanua kuhusu kile ulichoambiwa kule. Kwa hiyo tuanzie hiki cha leo hapa Mheshimiwa, uliza maswali yako mawili ya nyongeza.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, hata kwenye Hansard wakiangalia 2022 ni kwamba imeshatengwa fedha shilingi milioni 150 na kwenye vitabu vya bajeti ilionyesha kabisa kwamba zimeshatengwa na zimetolewa. Sasa hii leo wananiambia ni Msanifu anayeenda kupatikana 2024. Wakati kule tumeambiwa kwamba Msanifu ameshaanza kazi.

SPIKA: Sawa, sasa kwa maelezo yako mwenyewe hapo unasema zimetengwa na zimeshatolewa kwenye bajeti.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Kwenye bajeti, nafikiri huwa tunatenga ama?

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, zilitengwa shilingi milioni 300 kwa 2020/2021 na mwaka 2022 ni kwamba tayari zikawa zimeshatolewa shilingi milioni 150.

SPIKA: Sawa, sasa kwa sababu kwenye jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri, ametaja. Kwa sababu swali lako linasema, je ni lini upembuzi yakinifu utakamilika na kuanza ujenzi wa barabara ya Kahama - Nyang’hwale - Busisi, jibu la msingi linasema utakamilika Februari, 2025. Nilitaka kujiridhisha hapo uliposema, hujaridhika na majibu. Sasa uliza maswali yako ya nyongeza kuhusu hili ambalo umeliuliza kwenye swali lako la msingi.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, basi swali la pili; kwa kuwa ahadi hiyo imechukua muda mrefu, mtoto amezaliwa na amefikisha miaka 14 tangu mwaka 2010 ahadi hii imeahidiwa na Viongozi Wakuu wa Nchi, mpaka leo hii tuna miaka 13 tunakaa tunaambiwa maneno haya. Sisi wana Nyang’hwale tunataka majibu ya Serikali. Hivi ni kweli 2024 unavyosema na 2025 namwomba Mheshimiwa Waziri, baada ya Bunge hili twende akawaambie wananchi dhamira ya Serikali ya kukamilisha ahadi hii. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Mheshimiwa Naibu Waziri anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kaka yangu Mheshimiwa Hussein Amar, naomba hoja yake niichukue. Nimpongeze, juzi tulikuwa tuna kikao, Mheshimiwa Hussein Amar pamoja na Mheshimiwa Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala, tulikaa na Barrick, kuna barabara ya kutoka Kahama kwenda Bulyanhulu kwenda Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Amar, aliomba lami itakapofika kwenye geti la Barrick akaomba kipande cha kwenda Jimboni kwake tukae na Barrick ili kama kutakuwa kuna bakaa tujenge kile kipande. Kwa hiyo kaka yangu Mheshimiwa Amar naomba aendelee kuwa na confidence na Serikali. Hoja yake tumeichukua kwa kadri fedha zitakapopatikana na suala la usanifu tutaweka jitihada, lakini dhamira ya Serikali ni kujenga lami kwenye barabara zote ambazo upembuzi yakinifu umekamilika. Tupo pamoja Mheshimiwa Mbunge na nampongeza kwa namna ambavyo anapambana kwa wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwanza niipongeze Serikali kwa kuendelea kupunguza upungufu wa walimu katika Wilaya ya Nyang’hwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, uko tayari kumuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nyang’hwale azipitie shule zote zikiwemo za sekondari na msingi kuangalia uwiano wa walimu ‘ke’ na ‘me’ kwa sababu, kuna baadhi ya shule za msingi zina wanawake peke yake na baadhi ya shule za msingi zina wanaume peke yake, ikiwemo Shule ya Msingi ya Mama Samia.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amar:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo tayari kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale kuweza kufanya tathmini hiyo na ninaomba kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuchukua nafasi hii kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’hwale kuanza kufanya tathmini hii, kama alivyoshauri Mheshimiwa Amar na kuona ni namna gani anafanya msawazo wa ikama ndani ya halmashauri yake katika walimu. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa kuna Mkandarasi anajenga kilomita moja ya lami pale Mji wa Karumwa anaenda kwa kuasuasua takriban miezi 20 kwa kudai kwamba anaidai Serikali fedha.

Je, Waziri uko tayari kukamilisha malipo ya huyo Mkandarasi ili aweze kumalizia hiyo kilomita moja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza, moja ni kwamba ni kweli wakandarasi wengi ambao wanafanya kazi sasa hivi wamepunguza kasi kutokana na hali halisi kwamba hali ya mvua inayoendelea ni vigumu sana kufanya kazi hasa za barabara ikiwa ni pamoja na kuweka lami kwa sababu kitaalam inakuwa haiwezekani.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la malipo la huyo Mkandarasi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama tulivyosema tayari Serikali kwa maana Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Fedha tumeanza kupokea fedha, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mkandarasi huyo kama bado atakuwa hajalipwa na amesha-raise certificate basi atapewa kipaumbele ili aweze kukamilisha kazi mara mvua itakapokuwa imekata, ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Nyang’hwale, lakini jengo lile ni zuri, kuna thamani nyingi iliyopo pale. Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha kwa ajili ya kuweka uzio kwa ajili ya kulinda mali zote zilizo pale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo tayari kuhakikisha inatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio. Fedha hizo zinaweza zikatoka katika mapato ya ndani ya halmashauri, kwa hiyo, Mkurugenzi aanze kutekeleza hilo, lakini pia linaweza likatoka Serikali Kuu kwa awamu.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inaendelea kufungua barabara za mitaa kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale pale Kharumwa kwa kiwango cha udongo. Je, Serikali ina mpango gani kuziwekea mpango wa kuweka changarawe na baadaye lami hizo barabara za mitaa Kharumwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaweza kuzihudumia barabara za wilaya kwa kiwango cha lami, lakini kama wote tunavyofahamu tunaanza. Kwa hiyo, tayari Serikali imeanza kuhudumia barabara hizi kwa viwango tofauti ikiwemo viwango vya changarawe, lakini mwisho wa siku hatimaye tunataka barabara zetu zote hizi za wilaya ziwe kwa kiwango cha lami ambacho kitafanya barabara ziweze kudumu kwa muda mrefu na ziweze kupitika mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kutenga fedha kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ya barabara zetu hizi za wilaya na hususan pia kwenye Jimbo lako Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna ujenzi wa barabara ya lami kwenye Mji wetu wa Kalumwa, na tayari kuna vigingi upande wa kushoto na kulia mita 30, na lami hii ina upana takribani mita nane, wananchi hawa wanashindwa kubomoa au kuendeleza kujenga zile nyumba zao. Serikali ina mpango gani wa kupunguza vigingi hivyo ili mji ule uendelee kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zote ambazo ni za TANROADS zinalindwa na Sheria ya Mwaka 2007 ambayo upana wake ni mita 30 na hata kama itatumika mita saba lakini maana yake ni kwamba ile hifadhi ya barabara itaendelea kulindwa na itakuja kutumika pale itakapohitajika, ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa kukamilisha usambazaji wa umeme vijiji vyote 62 Wilaya ya Nyang’hwale, lakini kuna changamoto, tranformer hizo zimeanza kuzidiwa kwa sababu wananchi wengi wamefungua viwanda vidogovidogo, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kumwelekeza Meneja wa TANESCO Wilaya ya Nyang’hwale afanye tathmini kwenye transformer ambazo zimezidiwa na kubadilishwa tuwekewe nyingine kubwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, niwape pole wananchi wa Nyang’hwale kwa changamoto hiyo. Ninamwelekeza meneja sasa hivi wafanye tathmini kuweza kuona maeneo ambayo yanahitaji kubadilishiwa transformer ili wananchi wa Nyang’hwale ambao ni wazalishaji wazuri sana waweze kupata huduma na kuwasaidia katika shughuli zao za kiuchumi.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Waziri amekuwa akiniahidi sana kuhusu upembuzi wa Barabara yetu ya kutoka Kahama - Nyang’olongo – Bukwimba - Kahama - Busisi na akaahidi kwamba, mwezi Aprili upembuzi huu utakuwa umekamilika. Je, upembuzi huo umeshakamilika na huu ni mwezi Aprili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, sina uhakika kama 100% tumeshaikamilisha, lakini nimwombe Mheshimiwa Mbunge, baada ya hapa nijiridhishe na wataalamu, kwa sababu ni kati ya barabara moja kubwa na ndefu. Nijiridhishe na wataalamu halafu niweze kumpa jibu la uhakika kama tumeshakamilisha usanifu wa kina, ahsante. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, Bunge lililopita la Bajeti Mheshimiwa Waziri aliahidi kwamba wanakwenda kumtafuta mshauri elekezi kwa ajili ya Barabara yetu ya kutoka Kahama – Nyang’hwale – Busisi kwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Je, huyu mshauri elekezi anaanza lini kazi hiyo? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, taarifa nilizonazo ni kwamba mshauri wa barabara hiyo ambayo inaunganisha Mkoa wa Geita, Mwanza na Shinyanga atasaini mkataba mwezi Septemba mwaka huu, ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kuishukuru Serikali ya Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kiasi cha shilingi 3,000,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa skimu ambayo imeharibika zaidi ya miaka 40, Kijiji cha Nyamgogwa, Kata ya Shabaka, Wilaya ya Nyangh’wale. Je, ni lini Serikali itatangaza zabuni ya ujenzi wa skimu hiyo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ukanda wa Lake Victoria kuanzia Mara, Simiyu, Geita na Mwanza sasa hivi wataalam wetu wanafanya kazi ya usanifu kwa ajili ya kuziangalia skimu na mabwawa ambayo yalishajengwa huko mwanzo na yakaharibika; na kwa kuwa, skimu hii ilipangwa kujengwa mwaka huu wa fedha, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba usanifu ukikamilika tu itatangazwa kwa ajili ya kuanza kujengwa. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; kwa kuwa mtu ni afya lakini pia hata mifugo inahitaji afya bora ikiwa ni pamoja na kuoga, chanjo na matibabu. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga majosho ili ng’ombe wetu nao waweze kuoga na kuwa na afya njema, kwenye Kata ya Shabaka, Mwingiro, Kaboha, Izunya yakafika na Bukwimba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anachosema Mheshimiwa Mbunge na hiyo ndiyo sababu ya mifugo yetu inakosa sifa ya kwenda kuuzwa nje ya nchi kwa sababu haifuati utaratibu unaotakiwa wa Kimataifa. Ndiyo maana Serikali imekuwa ikihamasisha sana mifugo hii iweze kuoshwa katika maeneo mbalimbali na mpango wa Serikali ni kujenga majosho kwa wafugaji wote wanakopatikana ndani ya nchi yetu. Tuko tayari kuja kwenye maeneo hayo aliyoyasema Mheshimiwa Mbunge, kuona kama kuna uwezekano wa kujenga majosho ili mifugo hii iweze kupata hiyo huduma. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga njia za kupitishia wagonjwa na wahudumu kwenye Hospitali ya Wilaya ya Nyang’hwale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ujenzi wa hospitali zetu unafanywa kwa awamu na eneo la kupitishia wagonjwa ni muhimu sana. Kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutafanya tathmini kuona kiasi gani cha fedha kinahitajika katika Hospitali ya Halmashauri ya Nyang’hwale kwa ajili ya ujenzi wa walk ways na ikibidi mapato ya ndani yatatumika au fedha za Serikali Kuu zitapelekwa kwa ajili ya ujenzi wa walkways, ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ziara yake aliyoifanya Wilayani Nyang’hwale na kuacha maagizo pale Kata ya Nyijundu kwamba, kufikia tarahe 19 maji yawe yanatiririka na tayari maji yanatirirka Kata ya Nyijundu. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuzisukuma zile milioni 286 kwa ajili ya kukamilisha usambazaji wa maji kwenye Kijiji cha Iseni, Kabiga, Nyangaramila, Nyamikonze, Kasubuya, Kaboha, Shibuha na Shibumba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge wa Nyang’hwale ameuliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kuna hizo pesa ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziongelea na kwa kweli nampongeza sana kwa sababu tuliweza kuzunguka katika Jimbo lake karibu Kata kwa Kata tulijionea hali halisi. Kweli mradi huu ambao ameutaja unahitaji hizi fedha ili uweze kukamilika kwa haraka. Ninakuahidi kwamba Mheshimiwa Mbunge tutasukuma hizo fedha zitoke haraka ili mradi uweze kukamilika kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, Bunge lililopita la Bajeti Mheshimiwa Waziri aliahidi kwamba wanakwenda kumtafuta mshauri elekezi kwa ajili ya Barabara yetu ya kutoka Kahama – Nyang’hwale – Busisi kwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Je, huyu mshauri elekezi anaanza lini kazi hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, taarifa nilizonazo ni kwamba mshauri wa barabara hiyo ambayo inaunganisha Mkoa wa Geita, Mwanza na Shinyanga atasaini mkataba mwezi Septemba mwaka huu, ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwenye haya magari ambayo unasema umeyaagiza au yameagizwa, kwa Wilaya ya Nyang’hwale tumekuwa na uhitaji mkubwa kwa muda mrefu. Naomba kauli ya Serikali kwenye haya magari na Nyang’hwale itapata? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Nyang’hwale pia, ni Wilaya. Kwa hiyo, watapata gari, kwa ajili ya kulinda mali zao na raia wetu wawe salama. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali iliahidi kutujengea kituo cha afya cha kimkakati kwenye Kata ya Busolwa na Mheshimiwa Naibu Waziri amesema mwaka huu fedha zitapelekwa, je, anatuhakikishia na sisi tupo kwenye hiyo fedha itakayopelekwa kwa mwaka huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, hakika amekuwa akifanya ufuatiliaji mkubwa sana kuhakikisha kwamba kituo cha afya cha mkakati kinajengwa katika jimbo lake. Naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba katika mwaka huu wa fedha kituo cha afya kinajengwa katika kila jimbo. Pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika jimbo lake atapata fedha kwa ajili ya kuanza kujenga kituo cha afya cha mkakati.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inaendelea kufungua barabara za mitaa kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale pale Kharumwa kwa kiwango cha udongo. Je, Serikali ina mpango gani kuziwekea mpango wa kuweka changarawe na baadaye lami hizo barabara za mitaa Kharumwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaweza kuzihudumia barabara za wilaya kwa kiwango cha lami, lakini kama wote tunavyofahamu tunaanza. Kwa hiyo, tayari Serikali imeanza kuhudumia barabara hizi kwa viwango tofauti ikiwemo viwango vya changarawe, lakini mwisho wa siku hatimaye tunataka barabara zetu zote hizi za wilaya ziwe kwa kiwango cha lami ambacho kitafanya barabara ziweze kudumu kwa muda mrefu na ziweze kupitika mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kutenga fedha kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ya barabara zetu hizi za wilaya na hususan pia kwenye Jimbo lako Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante! Kwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanaouza bidhaa kama vile chakula vinywaji na madawa kwa ajili ya matumizi ya binadamu siyo waaminifu kwa kuendelea kuuza bidhaa ambazo zimeisha muda wake. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka ili kuweza kutoa elimu kwa wananchi hasa kule chini kuzuia kuendelea kutumia bidhaa hizo na kusababisha madhara makubwa kwa wananchi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Amar kwamba wapo wafanyabiashara wasiyo waaminifu ambao huweza kuuza bidhaa zilizopitwa na muda wake kwa kulijua hilo na kwa sababu Mamlaka ya Udhibiti wa Viwango ipo makao Makuu Dar es Salaam kwa mujibu wa Sheria ya Viwango, mamlaka za wilaya kwa maana ya halmashauri wataalamu wake wamekasimiwa majukumu ya ukaguzi wa bidhaa katika maduka, pharmacies na kadhalika ili kuwabaini watu hao na kuchukua hatua stahiki. Kweli wanapobainika hatua kali huchukuliwa ikiwa ni pamoja na uharibifu wa bidhaa hizo na kuwafikisha Mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kupitia hadhira hii nihimize Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambao wamekasimiwa jukumu hili…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kwa kifupi sana.

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: …wamekasimiwa jukumu hili kulitekeleza kwa umakini ili kuondoa malalamiko kama haya, ninashukuru.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, nianze kuipongeza Serikali kwa kutambua fidia ile ya wananchi 31 ya Kijiji cha Busengwa. Swali la kwanza; je, Serikali haioni haja ya kuanza kuandaa michoro ya gereza hilo ili fidia hiyo itakapolipwa ujenzi uanze?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Serikali haioni kufanya ujenzi huo kwa haraka, ili kuokoa gharama za wananchi kufuata huduma hiyo ya magereza kutoka Nyang’hwale kwenda Geita zaidi ya kilometa 130?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuandaa michoro. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, michoro itaandaliwa haraka iwezekanavyo lengo letu ni tuhakikishe kwamba, gereza hili linajengwa haraka, ili kuhudumia wananchi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu ujenzi kuanza haraka. Kama nilivyosema, baada ya kukamilisha michoro hatua inayofuata ni tutatenga fedha kwenye Mwaka 2025/2026, baada ya hapo ni kuanza ujenzi mara moja, ili wananchi wasipate tabu ya kutoka Nyang’hwale kwenda Geita ambako ni umbali mrefu. Ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, kabisa naanza kuipongeza Serikali kwa kuanza kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa kilomita mbili kwenye Mji wetu wa Kharumwa ambapo sasa hivi kilomita moja inaenda kukamilika ndani ya wiki hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na ahadi pia, ya kufungiwa taa. Je, ni lini Serikali, baada ya kukamilisha hii kilomita moja, itaanza kufunga taa na kuanza ujenzi wa kilomita ile nyingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema kwenye bajeti, Kharumwa ni Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale na mpango ni kuhakikisha kwamba, miji yote na hasa kwa kuwa, tumejenga lami nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tuna mpango wa kufunga taa karibu katika Wilaya zote, Makao Makuu ya Wilaya, ukiwepo na Mji wa Kharumwa, ahsante. (Makofi)