Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Janeth Maurice Massaburi (9 total)

MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naitwa Nuru Awadh Bafadhili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa kuna baadhi ya walimu mfano katika Halmashauri ya Jiji la Arusha katika Shule ya Msingi Olkerian, Kata ya Olkerian mpaka leo wanasumbuliwa kulipwa fedha zao za likizo na wakati huo huo tayari walishatumia fedha zao. Wanapouliza wanaambiwa andikeni barua ili muweze kulipwa pesa zenu. Je, Waziru anatuambiaje kuhusu suala hilo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimpongeze kwa kurudi tena Bungeni, alikuwa ni Mbunge kipindi cha mwaka 2005-2010, hongera sana na karibu tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua yako madeni mbalimbali ya watumishi wanaodai fedha zao za likizo. Nipende tu kusisitiza kwa waajiri kila mwaka pindi wanapoandaa mapendekezo ya bajeti za mwaka wahakikishe wanatenga fedha kwa ajili ya nauli za likizo katika bajeti ya matumizi ya kawaida au bajeti za OC. Vilevile nipende kusema kwamba kwa yeyote ambaye hakulipwa fedha hizo hilo ni deni na kama Serikali tunalitambua na tunalichukua na tutaendelea kufuatilia kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanapatiwa malipo yao. Niombe tu anisaidie huko baadaye taarifa kamili ili tuweze kushirikiana katika ufuatiliaji, lakini ni haki ya msingi ya mtumishi na ni lazima walipwe.
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kuna baadhi ya makabila wanatumia njia za kienyeji badala ya kwenda kufanyia tohara vijana wao katika hospitali njia ambazo zinasababisha wakati wa kuwafanyia tohara wakati mwingine kutokwa na damu nyingi na kupoteza maisha. Je, Serikali inatuambia nini kuhusu kuwapa elimu ili waweze kupeleka vijana wao katika hospitali zetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni rai yetu kwenye Makabila ambayo yana utamaduni wa kufanya tohara za kiasili maarufu kama kavukavu kama ulivyosema kuwaomba watumie huduma hiyo ya kutoa tohara kwa kwenda kwenye hospitali na kufanyiwa huduma ya tohara ya kitabibu yaani medical circumcision ili kuepukana siyo kutokwa damu nyingi, lakini pia kuepukana na uwezekano wa kuambukizwa magonjwa mbalimbali kwa sababu kule wanakofanya tohara ya kiasili kuna uwezekano mkubwa wakachangia vifaa vya kufanyia tohara yenyewe na hivyo kuhamisha vimelea vya magonjwa, kwa mfano homa ya ini ama virusi vya UKIMWI kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine kwahiyo, nitumie jukwaa lako hili kutoa rai kwa Mangariba wote kwenye makabila ambao wanatoa tohara ya kiasili kuanza kutumia tohara ya kitabibu kwenye hospitali zetu.
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji kwa watumishi wa umma na ambayo yana mwelekeo wa kuifikisha Tanzania kwenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Je, Serikali imejipanga vipi kikanuni kuwa na mfumo endelevu na madhubuti wa uwajibikaji na uwajibishaji kwa awamu zote za utawala zinazofuata?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali haioni umuhimu wa kuajiri vijana waliopo kwenye private sector na wale wanaoshi nchi za nje (Diaspora) kwa kuwashirikisha pamoja ili tuweze kupata chachu ya maendeleo kwa kutumia ujuzi mbalimbali walionao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mbunge wa Kuteuliwa ambaye pia ni wifi yangu Mheshimiwa Janeth Masaburi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ameulizia kuhusu mfumo. Naomba nimueleze Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba sisi kama Serikali sasa hivi tumejipanga kuboresha mfumo mzuri zaidi tofauti na ule tuliokuwa nao ambao tulikuwa tunatumia LAWSON version 9 ambapo sasa hivi tuna mfumo mpya wa utumishi pamoja na mishahara. Mfumo huu unatengenezwa na vijana wetu wa Kitazania na wazalendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu wa utumishi na mishahara wenyewe utakuwa na uwezo mkubwa sana wa capture taasisi zote za umma nchini tofauti na ule ambao tunautumia sasa na ndiyo maana kumekuwa na malalamiko mengi. Mfumo huo tunategemea uanze rasmi Juni, 2019 ambao utahusisha taasisi zote za umma na utaboresha hata mifumo mengine ya utendaji kazi wa mtumishi wa umma mfano OPRAS. Kwa maana hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tumejipanga na mfumo huu ambao utakuwa mpya na uwezo mkubwa utaweza kuhakikisha unapata taarifa za kila mtumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili amezungumzia juu ya kuajiri watumishi ambao watatoka katika taasisi binafsi. Naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali kwa wale wote ambao wanaomba ajira kwa mara ya kwanza hatuna restriction yoyote wala hatubagui na huwa tunatoa matangazo ya kazi na sasa hivi tumejiongeza zaidi tunatumia online kwa maana ya Ajira Portal. Kwa hiyo, mtu yeyote ambaye anataka kuomba kazi Serikalini anakaribishwa mradi sifa, vigezo na mienendo yake na michakato inayotakiwa itafanyika. Ahsante.
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Natambua Serikali imefanya vizuri sana katika sekta hii ya elimu, lakini nina maswali madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa, hivi sasa kwa wastani kwa wahitimu wa vyuo vikuu ni kati ya 10 kwa mmoja kwa wahitimu wanaohitimu vyuo vya ufundi, yaani wasimamizi 10 kwa mtendaji kazi mmoja badala ya msimamizi mmoja kwa watendaji kazi 10. Je, Serikali inasema nini juu ya hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika umuhimu huo wa vyuo vya ufundi ambako ndiko kunakozalisha kundi kubwa la watenda kazi ambalo kundi hili ndilo linajiajiri lenyewe. Je, Serikali inasema nini juu ya kuweka uwekezaji mkubwa katika vyuo vya ufundi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Janeth Masaburi kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukweli kwamba, kwa sasa hakuna uwiano mzuri kati ya watendaji au wafanyakazi katika sekta ya ufundi katika ile maana ya kwamba, wale watendaji wa kada ya kati pamoja na kada ya chini na wale wa ngazi za juu. Serikali ndio maana imechukua maamuzi ya kuongeza udahili katika vyuo vyetu ili tuendelee kuwapata wataalam wengi ambao baadae watatusaidia kujaza ombwe hili na hivyo kurekebisha hali hiyo, ili tuwe na uwiano mzuri katika wafanyakazi wetu katika sekta ya ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili kwamba, Serikali inafanya nini kuwekeza katika vyuo vya ufundi. Kama nilivyosema kwenye jibu langu katika swali la msingi, Serikali inachukua hatua kadhaa za makusudi kuhakikisha kwamba, tunaongeza, sio tunaongeza vyuo vingi, lakini vilevile tunaongeza udahili pamoja na ubora wa vyuo hivyo ambavyo vinatoa fani mbalimbali za ufundi. Ndio maana tunapozungumza sasa tunajenga vyuo 13 vya wilaya, lakini tutajenga vyuo vitano vya mikoa, ambavyo vile vya mikoa vyenyewe vinagharimu shilingi bilioni 118, lakini pia hatujaishia hapo, tunakarabati Vyuo vyote 54 vya Wananchi vile tunaviita FDCs.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kuweza kuwa na vyuo vingi vyenye ubora mzuri, ili tuongeze udahili, ili tuendelee kuwapata mafundi wengi kwa sababu, watatusaidia katika azma yetu ya kujenga uchumi wa viwanda, lakini vilevile kuongeza fursa za ajira. Kwa sababu, kama mnavyofahamu ni rahisi vijana wengi kujiajiri wakisoma ufundi; lakini pia, tunaendelea kujenga vyuo vya ufundi wa kati na ndio maana tumewekeza katika kujenga chuo kikubwa Dodoma, chuo ambacho kina hadhi kama ilivyo DIT na Arusha Technical College.
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuweza kuniruhusu niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kuipongeza TAMISEMI kupitia Mawaziri wake wote kwa kazi nzuri wanayoifanya hapa nchini. Tumekuwa tukiwaona wanatekeleza wajibu wao ipasavyo, lakini katika eneo hili la vijana na wanawake ninaomba niulize maswali kama yafuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa vijana wengi na wanawake hapa nchini wameshindwa kufanya biashara zao kwa tija kutokana na ukosefu wa ujuzi na maarifa wa kufanya biashara hizo. Je, Serikali iko tayari kuiwezesha kutoa mafunzo makundi haya ya ufugaji wa samaki ya uhakika na kwa idadi kubwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa, sekta ya uvuvi imeonesha kuwa na fursa kubwa ya kukuza ajira, kukuza kipato, kuboresha lishe na hata kuiingizia Serikali fedha za kigeni. Je, Serikali iko tayari kuanzisha mpango wa kujenga vizimba pembezoni mwa maziwa na mabwawa na hata kandokando ya mwambao wa bahari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa pongezi ambazo ametutumia kwenye Ofisi ya TAMISEMI kwa kazi ambayo inafanyika tunamshukuru sana.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Masaburi ametoa maswali mawili, swali la kwanza anatuhimiza tuwe na mafunzo kwa vijana na akinamama na kweli hili jambo linafanyika, kwa sababu jambo la msingi ni kwamba tumeshatoa maelekezo kila Halmashauri ina maelekezo na baada ya kugundua kwamba kuna … pia na mafunzo … mtaji ndio maana Bunge hili tukufu likapitisha sheria kwamba kila Halmashauri itatenga mapato yake ya ndani asilimia nne kwa akinamama, nne kwa vijana na mbili kwa watu wenye mahitaji maalum au wenye ulemavu kwa hiyo hii pia ni sehemu ya mtaji.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kila Halmashauri ina Maafisa wa Ustawi wa Jamii na kuna Maafisa wa Vijana katika Halmashauri zote nchini. Naomba nitumie nafasi hii kuwaelekeza washirikiane na Maafisa wa Ugani kwenye Wizara ya Kilimo waende wakatoe mafunzo kwa vijana hawa na kimsingi hata ziara ambazo Mheshimiwa Waziri anafanya, Manaibu, Makatibu Wakuu na Wakurugenzi ndio tunaangalia miradi ambayo imeanzishwa na Halmashauri na kukagua ikiwepo ni pamoja na ufugaji wa samaki katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba tupokee ushauri wake tuwasiliane na viongozi wenzetu wa Wizara ya Uvuvi. Tutalifanyia kazi, ahsante sana.
MHE. JANETH M. MASSABURI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa moja ya sababu inayosababisha ajali nyingi hapa nchini ni wembamba wa barabara zetu, Je, Serikali haioni haja ya kuruhusu magari makubwa ya mizigo kutembea nyakati za usiku? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, ni umri upi unaoruhusiwa kutoa leseni kwa madereva wa magari makubwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Janeth Massaburi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja, kuhusu wembamba wa barabara; ni kweli taarifa za utafiti zinaonesha wembamba wa barabara ni moja ya sababu inayosababisha ajali na hili linafanyiwa kazi na wenzetu wa Uchukuzi na Usafirishaji, ambao ni Wajumbe wa Baraza la Taifa la Usalama barabarani na ndio maana mtaona wakati mwingine tunapanua barabara kule upande wa Mbeya na maeneo mengine inavyoonekana imekuwa changamoto.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, magari ya mizigo yatembee usiku; nadhani sio suluhisho la kudumu kwa sababu tunataka nchi yetu ichangamke kwenye biashara, hatuwezi kuacha kusafirisha wakati wote tukisubiri wakati wa usiku tu.

Mheshimiwa Spika, tunachotakiwa kufanya ni kuimarisha usimamizi wa sheria za usalama barabarani na kuboresha miundombinu ya barabara ili kuwe na usalama wakati wote.

Mheshimiwa Spika, kuhusu umri unaofaa kwa mtu kupewa leseni ya kuendesha magari ya mizigo ni mtu mzima, na kwa Tanzania mtu mzima baada ya miaka 18 amefanya mafunzo na amefuzu kwa vigezo vyote anaweza akapewa leseni ya kuendesha magari.
MHE. JANETH M. MASSABURI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wenzetu wa nchi hizo wamekuwa wakitumia sheria kali ambazo kila dereva anatii sheria na kunusuru maisha ya wananchi wao; je, ni lini Serikali itatunga sheria kali ambazo zitaweza kutusaidia kunusuru maisha ya Watanzania yanayopotea kutokana na ajali za barabarani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali imeshindwa kuwadhibiti madereva wa bodaboda ambao hupita kwenye makutano bila kuzingatia taa za barabarani na hatimaye kusababisha ajali na kusababisha watu kufariki na kuleta walemavu wengi katika nchi yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja, juu ya sheria ya usalama barabarani iliyo kali zaidi; naamini Mheshimiwa Mbunge atakuwa anafahamu kwamba tulishawasilisha hapa sheria ikasomwa kwa mara ya kwanza na kwa busara ya Bunge lako Tukufu ilitakiwa irudishwe kwa ajili ya kuboresha maeneo ambayo yalikuwa na changamoto. Napenda kumhakikishia kwamba uboreshaji uko hatua za mwisho, katika Mabunge yajayo tunatarajia iletwe hapa ili Bunge likiridhia tuwe tumemaliza eneo hilo la sheria kali.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kushindwa kuwadhibiti bodaboda; hatujashindwa. Tulichojifunza ni kwamba hawa vijana namna wanavyoingia kwenye uendeshaji ni kwamba wengine hawajapata kabisa mafunzo. Jeshi la Polisi, hususan Kitengo cha Usalama Barabarani, wameanza na hatua za kuwafundisha.

Mheshimiwa Spika, na bahati nzuri sasa hivi wamewekwa kwenye makundi katika maeneo mbalimbali wanayopangwa katika vikundi. Katika makundi yao yale wanapata mafunzo, traffic police na wenye vyuo vya udereva wanakwenda wanawasomesha ili wajue taratibu za usalama barabarani.

Mheshimiwa Spika, wale wanaokiuka hatua zinachukuliwa. Ndiyo maana tukienda maeneo ya polisi mtakuta pikipiki nyingi ziko kule za wale waliokiuka sheria. Tutaendelea kujenga uwezo wao na kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka. Kupitia Bunge lako, nielekeze traffic police wasiwe na muhali na vijana hawa ambao wanakaidi sheria makusudi, hasa wanaopita kwenye taa za barabarani wakati zimezuia, nashukuru.
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ambayo sijaridhika kidogo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na bajeti kuwa ndogo ambayo haikidhi mahitaji halisi ya barabara za Mkoa wa Dar es Salaam, ukizingatia Dar es Salaam ina wakazi wengi ambao unaweza kulinganisha na Mikoa minne, mitano ama sita katika nchi hii.

Je, Serikali haioni haja ya kuunda mamlaka itakayoshughulika na barabara za Mkoa wa Dar es Salaam? (Makofi)

Swali la pili, kwa kuwa, Mkoa wa Dar es Salaam hatuna ruzuku ya pembejeo, mbolea, shida yetu ni barabara, mifereji, madaraja, labda na panya road.

Je, Serikali haioni huruma kwa adha wanayoipata wananchi kwa kuhangaika na ukizingatia sasa hivi barabara nyingi zimejengwa kutokana na ujenzi wa reli na barabara zile za BRT? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Massaburi:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bajeti ndogo kwa Barabara, nimuarifu Mheshimiwa Masaburi kwamba ni jitihada za Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha barabara za Jiji la Dar es Salaam zinapitika wakati wote na kutengenezwa kwa kiwango cha lami, kwanza kwa kuweka shilingi bilioni 800 na zaidi ya hapo katika Mradi wa DMDP I.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa siku hizi mbili hapa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Angellah Kairuki, amewakaribisha Wabunge wote wa Dar es Salaam kwenda kushuhudia utiaji saini wa mikataba ya consultants katika mradi wa DMDP II ambapo nao ni commitment kubwa ya Serikali katika Jiji la Dar-es-Salaam, kuhakikisha barabara zote zinapitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninakuomba Mheshimiwa Massaburi uwe na subira na wananchi wa Dar es Salaam Serikali inaweka fedha zaidi tena ya bilioni 800 katika kutengeneza miundombinu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili la kwa nini Serikali isiongeze miundombinu kama reli na kadhalika. Hili tunalipokea kama Serikali na tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi kuona ni nanma gani tutaboresha zaidi miundombinu, lakini tayari kama nilivyosema hapo awali katika mradi huu wa DMDP II, Dar es Salaam inakwenda kupendezeshwa chini ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha barabara zinapitika, mito inajengwa vizuri na mifereji ya kupitisha maji ili wananchi wa Dar es Salaam waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi bila kupata bughudha yoyote ya kiusafiri.
MHE. JANETH M. MASSABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu yenye matumaini ya Serikali nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi hii na hasa katika miundombinu ya barabara. Ukiangalia Barabara ya Nyerere mpaka Gongo la Mboto kazi inaenda kwa kasi sana, tunashukuru. Pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya Mwendokasi kutoka Segerea kuelekea Kinyerezi, Malamba Mawili, mpaka Stendi Kuu ya Mabasi kule Mbezi kwa Magufuli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali ina mpango gani pia wa kujenga Barabara ya Mwendokasi kutoka Gongo la Mboto, Pugu, Chanika, Msongola, Chamazi na kuunganisha na Barabara ya Mbagala? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa Barabara ya Matumbi - Segerea ambapo barabara haitaingia kwenye awamu ya tano ya utekelezaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka. Ujenzi wa Barabara hii ya Segerea - Malamba Mawili hadi Stendi ya Magufuli itaingia kwenye awamu ya saba na ya nane ya Mradi wa BRT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kuhusiana na Barabara ya Gongo la Mboto - Chanika – Msongola - Chamazi mpaka Mbagala, tayari Serikali imeshafanya tathmini na itaingiza ujenzi wa barabara hizi kwenye awamu ya saba na ya nane na hivi sasa tayari Mhandisi Mshauri ameshapatikana na kazi iliyobaki sasa ni kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa barabara hizo. Ahsante sana.