Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Shamsia Aziz Mtamba (32 total)

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, pamoja na kupita bomba la gesi katika maeneo mengi ya Mtwara na Lindi, bado vijiji na mitaa mingi haina mtandao wa umeme. Je, ni lini REA III itamaliza tatizo hili kwa mikoa ya kusini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, mkandarasi aliyepewa kusambaza mtandao wa umeme Mtwara yupo slow sana. Je, Serikali inachukua uamuzi gani kwa mkandarasi huyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameuliza; ni lini REA III itamaliza tatizo la kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mtwara. Nataka nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kuwa Mkandarasi wa Mkoa wa Mtwara ni JV Radi Service Limited na ameshalipwa asilimia kumi na yupo Mkoani Mtwara akiendelea na kazi ya upimaji wa njia ya umeme, na kwa kuwa Wizara tumetoa maelekezo kwamba vifaa vyote vya mradi huu REA III vipatikane ndani ya nchi, wakandarasi wanachoendelea nacho sasa ni namna ya kutafuta vifaa vyote na kuagiza ndani ya nchi, na nimhakikishie kazi hii itafanyika kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anaulizia hatua gani zitachukuliwa dhidi ya mkandarasi huyu. Naomba nimwambie ratiba ya REA iko awamu mbili, awamu ya kwanza ni 2017 hii Julai mpaka 2019, kwa hiyo mkandarasi huyu yupo ndani ya muda. Na kwa kuwa amelipwa asilimia 10 na ameanza kazi, nimthibitishie tu zoezi la upelekaji umeme katika Mtwara kwa mkandarasi huyu JV Radi Service itakamilika kwa wakati.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipatia nafasi, ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Tatizo lililopo Lupembe linafanana kabisa na tatizo lililopo Mtwara Mjini, viwanda vingi vimekufa ikiwemo Kiwanda cha Kubangulia Korosho cha Oram ambacho kilikuwa kinatoa ajira kwa wananchi wengi wa Mkoa wa Mtwara. Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua viwanda hivyo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge, kupitia Sera yetu ya Uendelezaji wa Viwanda endelevu, sisi wenyewe kama nchi tuliona kwamba, masuala yote yanayohusiana na uzalishaji yaondoke sasa kwenye mikono ya Serikali iende katika mikono ya sekta binafsi. Jambo ambalo tunafanya sisi ni kuhakikisha kuwa tunaweka mazingira wezeshi kwa kuhakikisha kuwa ile miundombinu inayohitajika pamoja na uunganishaji wa taarifa na vikwazo vyote ambavyo vinawakabili hao wawekezaji viweze kutatuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa korosho, kwanza tunashukuru kwamba kwa sasa hali ya korosho/bei ya korosho imekuwa ni nzuri, lakini sisi kama Taifa tusingependa tu kuuza korosho zikiwa ghafi. Kwa misingi hiyo, tunaendelea kufanya jitihada ya kuhakikisha kuwa viwanda mbalimbali vya korosho vinaimarishwa ili kuhakikisha kuwa tunapata tija katika zao hili.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa nini Serikali haitaki kuwapa gesi wawekezaji wa kiwanda cha mbolea ambao wako tayari kujenga Msangamkuu, Mkoani Mtwara vijijini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, miongoni mwa manufaa ya gesi kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara ni pamoja na kupelekewa umeme lakini mpaka sasa baadhi ya maeneo hakuna umeme Mkoani Mtwara. Naomba kujua kwa nini Serikali haipeleki umeme maeneo mengi ya Mkoa wa Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Shamsia, wifi yangu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuna mwekezaji, ni kweli wapo wawekezaji kampuni ya WD capital ya Egypt pamoja na Oman Petra Chemical ya Oman na LMG ya Ujerumani ambayo iliingia makubalino na Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kuwekeza kiwanda cha mbolea katika Mji wa Msangamkuu ambayo itatumia malighafi ya gesi asilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme sio sahihi sana kwamba walikataliwa kupewa gesi, lakini kikwazo kilikuwa bei ya gesi ambao wawekezaji wetu walikuwa wanaitaka. Kwa mfano, sambamba na huyo pia kuna mradi wa Kampuni ya Ferrestal ambayo waliingia ubia na Kampuni yetu TPDC lakini wote hao walikuwa bei yao ya awali ambayo walikuwa wanaitaka ni iwe USD 2.26 ambako gharama za uzalishaji wa gesi hizi kwa mujibu wa EWURA ni USD 5.6. Kwa hiyo utaona gape yake lakini Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayovutia wawekezaji ili kupitia maagizo ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli iliridhia tuanze mchakato wa mazungumzo. Kupitia mchakato wa mazungumzo ambao ulihusisha TIC ambayo yalifanyika mwezi Machi mwaka huu 2019, tumefikia bei ambayo wenzetu wawekezaji hawa wamerejea ili kuitafakari na baada ya wiki mbili walisema watarejea tena na bei hiyo ni kama USD 3.36 ambayo tunaamini pengine hiyo inaweza sasa ikafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niwathibitishie wakazi wa maeneo ya Kilwa ambako Ferrestal na TPDC watajenga kiwanda hicho na wakazi wa maeneo ya Msangamkuu Mkoani Mtwara kwamba, fursa ya ujenzi wa viwanda vya mbolea ambao faida kubwa itatoa ajira na mapato bado ipo na Serikali hii ya Awamu ya Tano kupitia hata Ofisi ya Waziri Mkuu Uwezeshaji na hata Taasisi ya TIC na taasisi zingine tutahakikisha kwamba fursa hii itafanyika kwa ufasaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ameulizia kwa nini Mkoa wa Mtwara kwa kuwa unatoa gesi haujapelekewa umeme kwa kiwango ambacho Mheshimiwa Mbunge ameulizia. Nataka niseme ni kweli Mkoa wetu wa Mtwara tunautegemea sana kwa gesi megawati 1,600, zinazozalishwa sasa asilimia 52 inatokana na gesi. Pia Mkoa wa Mtwara kwa REA awamu ya tatu inaendelea ina vijiji 167, lakini Manispaa ya Mtwara Mikindani baadhi ya maeneo hata mimi niliyatembelea Mkangaula, Mkanalebi na pale maeneo ya mjini na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo tulikuwa naye pamoja na amekuwa wakiliulizia mara kadhaa hapa ndani ya Bunge kwa kazi nzuri ya kufuatilia miradi hii nimhakikishie tu ujazilizi awamu ya pili unaendelea na utaugusa Manispaa ya Mtwara Mikindani na maeneo mengine na hata Mkoa wa Lindi kwa sababu bado tunatarajia gesi kutoa mchango mkubwa katika kuzalisha umeme ahsante sana.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mara kwa mara Serikali imekuwa ikizungumzia kujenga barabara inayotoka Mtwara Mjini kuelekea Msimbati ambako kuna mitambo na visima vya gesi. Je, ni lini sasa Serikali itajenga barabara hiyo muhimu kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjulisha Mheshimiwa Shamsia kwamba katika kitu ambacho Serikali ya Awamu ya Tano inakifanya, kwanza tumetoa ahadi kujengwa kwa barabara za wilaya, mkoa na za kitaifa na barabara zile ambazo zinaenda maeneo muhimu kwa maana ya uchumi wa Taifa. Kwa hiyo, kama barabara hiyo inaangukia humo, nataka nimhakikishie kwamba kuanzia bajeti tunazoanza na katika Mpango huu ambao tunaendelea nao, nina hakika katika miaka mitano barabara hii itakuwa imejengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilianza mpango wa kulipa fidia kwa wananchi wa Mtwara Vijijini waliopitiwa na bomba la maji mwaka 2015; nataka kujua mradi huu umekwamia wapi wakati uthamini ulishaanza kufanyika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika,ahsante kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia kutoka Mtwara Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi ambao umeshafanyiwa usanifu Serikali tumejipanga tunakuja kuhakikisha kuona kwamba usanifu ule unakamilika na utekelezaji wake utakamilika. Miradi yote namna ambavyo ipo kwenye mikataba namna ambavyo tumekuwa tukiianza tunakwenda kuhakikisha kwamba maji yanatoka na changamoto zote ambazo zilikuwepo huko nyuma kwa kipindi hiki tunakwenda kuzimaliza.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali langu la kwanza: Serikali ilianza mpango wa kulipa fidia kwa wananchi wa Mtwara Vijijini waliopitiwa na bomba la maji kutoka Mto Ruvuma mwaka 2015. Nataka kujua, mradi huu umekwama wapi ikiwa tayari wananchi walishaanza kufanyiwa uthamini ili mradi huo uanze? (Makofi)

Swali la pili: Fedha zilizotengwa ili kutekeleza mradi wa maji wa Mto Ruvuma ambapo wananchi walishaanza kupewa utaratibu wa malipo ya fidia mwaka 2015 zimeenda wapi? Serikali inawaambia nini wananchi wa Mtwara Vijijini kuhusu mradi huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli fidia hii ilianza kutekelezwa mwaka 2015. Mradi huu wa Mto Ruvuma ni ile miradi mikubwa ambayo mkakati wake lazima uwe madhubuti ili mradi usiishie njiani. Hivyo fidia namna ambavyo baadhi wameshalipwa, wale ambao bado hawajalipwa nao wanakuja kukamilishiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi, kufikia mwaka ujao wa fedha 2021/2022 tumeweka mikakati ya kuona kwamba, tunakuja sasa kukamilisha miradi ya maziwa makuu ikiwepo mradi wa Mto Ruvuma pamoja na miradi mingine. (Makofi)
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante; pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kutokana na umuhimu wa barabara ya ulinzi inayozunguka maeneo ya mipaka yet una nchi Jirani ya Msumbiji, je, lini Serikali itaanza kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kurahisisha hata vyombo vyetu vya ulinzi vinapofanya doria vifike kwa wakati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kutokana na uwepo wa miundombinu muhimu ya umeme na visima vya gesi, Vijiji vya Msimbati na Madimba. Je, Serikali haioni sasa ni wakati sahihi wa kuboresha miundombinu ya barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara ya ulinzi aliyoitaja ni barabara muhimu sana na ina urefu zaidi ya kilometa 350 na hadi sasa barabara hii baada ya kwamba ilitumika kipindi kile haitumiki na sasa hivi inafunguliwa upya na tayari na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeshafungua karibu kilometa 250 na inaendelea kuifungua mpaka itakapokamilika. Na baada ya kukamilika kuifungua ndipo tutakapoanza utaratibu wa kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, barabara hii aliyoisema ni lini tutaanza, tayari tumeshaanza ndio maana tumeshafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kilichobaki sasa ni kutafuta tu fedha na tutakapopata basi tutaanza kujenga kwa kiwango cha lami ili kufikia hayo maeneo muhimu ya Mnazi Bay, ahsante.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo Bahi linafanana kabisa na tatizo lililopo Mtwara; viwanda vingi vimekufa kikiwemo Kiwanda cha Kubangulia Korosho cha Olam ambacho kilikuwa kinatoa ajira kwa wnanachi wengi wa Mkoa wa Mtwara.

Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua viwanda hivyo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mkoa wa Mtwara ndiyo ambao unazalisha korosho nyingi hapa nchini kuliko mikoa mingine na pia kumekuwa na viwanda vingi sana vya kubangua korosho ambavyo kama nilivyosema kabla tulikuwa na viwanda 12 vya Serikali ambavyo baadaye vilibinafsishwa. Lakini kuna vingine ambavyo vimekuwa havifanyi vizuri sana na tumeweza kuvirejesha Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda hiki cha Olam anachokisema of course kimefungwa kutokana na changamoto mbalimbali, lakini moja ya changamoto kubwa ambazo zilikuwa zinakabili viwanda vyetu ilikuwa ni upatikanaji wa malighafi, kwa maana ya korosho ghafi kwa ajili ya kubanguliwa katika viwanda hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na moja ya mikakati ambayo Serikali sasa imefanya ni kuona sasa viwanda hivi vinapata malighafi katika mnada wa awali, kwamba viwanda vile vya kubangua korosho vipate malighafi zinazotakiwa, halafu baadaye sasa korosho zinazobakia ziende kwenye mnada wa kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mikakati inayowekwa na Serikali viwanda vingi sasa vitarudi kufanya kazi kwa sababu vitakuwa na uhakika wa malighafi, lakini pia na mazingira wezeshi ambayo Serikali imeanza kuyaweka ili kuvutia wawekezaji zaidi katika viwanda mbalimbali vikiwemo viwanda vya korosho katika Mkoa wa Mtwara.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali inawaambia nini wananchi hasa wazee wenye kadi za Bima ya Afya pindi wanapokwenda kupata huduma na kujibiwa dawa wakanunue madukani; nini majibu ya Serikali juu ya hili?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kutokana na ongezeko kubwa la zahanati vijijini changamoto kubwa ni upatikanaji wa dawa, vifaa tiba kwa maana ya vipimo na waganga. Nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha vifaa hivi vinapatikana bila usumbufu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Spika, ni kweli concern ya Mbunge anayoisema ndiyo concern kubwa ambayo imeonekana kwenye eneo la CHF ambayo wananchi wengi wamekuwa wakienda na wakifika kwenye kituo wanakutana na tatizo hilo la upatikanaji wa dawa pamoja na daktari kumwandikia na CHF ni kwamba haiwezi kumsaidia mtu huyu kupata kwenye maduka mengine dawa zaidi ya kwenye kituo husika.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana sasa hivi Serikali umesikia moja; Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi bilioni 123 kwa ajili ya kuboresha eneo la dawa, maana yake sasa wakienda vituoni watakutana na dawa. Lakini umemsikia Waziri wetu kwa sababu suala la upatikanaji wa dawa vituoni ni zaidi tu ya fedha zenyewe kupatikana ndiyo maana umemsikia Waziri wetu wa Afya pamoja na Waziri wa TAMISEMI wameanza kufanya kazi kubwa sana kwenye eneo la uadilifu kuhakikisha kuna accountability kwenye eneo zima la dawa. Kwa hiyo hilo ndilo jibu la swali lako la kwanza.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili ni upatikanaji vilevile wa dawa na vifaa tiba vituoni; nalo linajibiwa na swali la kwanza kwa sababu tukishakuwa na shilingi bilioni 123 ambayo Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ameshazitoa kimsingi tutakuwa tumetatua hilo tatizo. Lakini vilevile sasa tunapokwenda kwenye Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote maana yake hata tukiingia watu wote wakapata bima ya afya inayofanana na hizi ambazo wafanyakazi wa Serikali wanazo hata kama watakosa dawa kwenye kituo chake, kuna maduka ya dawa ambayo yanatumia Bima ya Afya ambayo ni hii kubwa ya Taifa kwa hiyo tatizo hilo la dawa litaondoka.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kutokana na umuhimu wa barabara inayotoka Mtwara mjini kuelekea Msimbati, ambako kuna visima na mitambo ya gesi. Je, ni lini sasa Serikali itaona umuhimu wa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
MHE. NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyotaja ni barabara muhimu kwa sababu inaenda kwenye maeneo ya kimkakati. Naomba nimuhakikishie kwamba kadri fedha itakavyopatikana katika bajeti zinapokuja, barabara hii tutaijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, tunaifahamu ni barabara muhimu kutegemea na upatikanaji wa fedha na hasa kwa bajeti ambayo tutaanza kuitengeneza mwezi wa tatu mwakani. Ahsante. (Makofi)
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Serikali ilianza mpango wa kulipa fidia wananchi wa maeneo yaliyozunguka Mradi wa Mto Ruvuma, sasa nataka kujua kwa nini Serikali inakwama kuendeleza mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli fidia ilishaanza kulipwa na itaendelea kumaliziwa ndani ya mwaka huu wa fedha, lakini mradi huu wa Mto Ruvuma ni katika ile miradi yetu ya kimkakati ndani ya Wizara kuona kwamba vinakuwa nyanzo vya kudumu kwa kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji uliopo Kata ya Mango Pacha Nne ili kuwatua ndoo kichwani akina mama hawa ambao kwa muda mrefu, tokea tumepata uhuru, hawajawahi kabisa kufurahia huduma hii ya maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mradi utaendelea kuletewa fedha. Ninakupongeza Mheshimiwa Mbunge, ameshafuatilia sana huu mradi, fedha inakuja na mimi na wewe tutakwenda site kuhakikisha kazi inakamilika. Lengo ni kuona mwana mama anatua ndoo kichwani na ni dhamira safi ya Mheshimiwa Rais ambayo anayo kwa muda mrefu.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, bado kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa wataalam wa kusoma vipimo hivi; je, Serikali ina mpango gani wa kutuletea wataalam hao?

Swali langu la pili; je, Serikali haioni umuhimu wa kutusambazia vipimo vikubwa kwenye zahanati zetu pamoja na hospitali yetu ya Wilaya Nanguruwe ili tuweze kupima na magonjwa mengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza nimuondoe hofu, kadri Serikali itakavyoendelea kuajiri na kuongeza wataalam katika kada ya afya maana yake na mgawanyo huo utafika mpaka katika Jimbo lake la Mtwara Vijijini na maeneo mengine ya Taifa. Kwa hiyo, lipo katika mpango wa Serikali na tunaendelea kuajiri kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, umuhimu wa kuongeza vipimo vikubwa hilo lipo na ndiy kazi kubwa anayofanya Rais wa sasa Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Sasa hivi Ofisi ya Rais – TAMISEMI tukishirikiana na Wizara ya Afya, tunatarajia kupokea shilingi bilioni 169.7 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya ununuzi wa vifaa, vifaa tib ana vitendanishi kwa ajili ya maabara. Kwa hiyo tutaendeela kuvileta kwa kadri ambavyo vinapatikana. Ahsante sana.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya uchumi inayoanzia Mtwara Mjini kuelekea Msimbazi kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara iliyoitajwa tayari tumeshaifanyia upembuzi wa kina, Serikali sasa inatafuta fedha kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Katika maeneo yenye changamoto kubwa sana ya maji ikiwemo ni Jimbo la Mtwara Vijijini, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaondoa kero hii ya maji katika Jimbo la Mtwara Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Shamsia, Mbunge wa Mtwara Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge naamini unafahamu jitihada ambazo zinafanywa na Wizara katika eneo lako na tumeshaongea mara nyingi, Mheshimiwa Mbunge naomba tuendelee kuwasiliana kama unavyofanya tutakuja kuhakikisha maji yanafika maeneo yote ambayo tayari miradi inaendelea.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwanza tunaishukuru sana Serikali kwa hatua iliyofikia katika hospitali yetu ya Kanda ya Kusini, lakini tumekuwa na changamoto kubwa sana ya Madaktari Bingwa. Je, ni lini sasa Serikali itatuletea Madaktari Bingwa katika hospitali yetu hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba hospitali ile inahitaji Madaktari Bingwa. Kuna Madaktari Bingwa, lakini Madaktari Bingwa kwa kiwango kinachohitajika kwa Hospitali ya Kanda bado hawajafikia hicho kiwango. Sasa upembuzi yakinifu unafanyika kuweza kuainisha maeneo mengine ili kuamisha na kupeleka kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Spika hivyo hata hivyo cha kwanza tulikuwa tunangojea kukamilisha baadhi ya miundombinu hapa karibuni ndiyo CT-scan imekwenda na MRI mashine, sasa hata ukiwahamisha wataalam wa kibingwa wanaweza wakapata vifaa vya kufanyia kazi ndiyo maana hawajaweza kupelekwa mapema katika eneo hilo.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto kubwa ya maji inayotukumba katika Mkoa wetu wa Mtwara hususan kwenye Jimbo langu la Mtwara Vijijini. Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia chanzo cha maji cha Mto Ruvuma?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, nataka niweke bayana rasilimali za maji tulizonazo juu ya ardhi na chini ya ardhi ni zaidi ya Bilioni 126. Bilioni 105 ni maji yaliyopo juu ya ardhi, kikubwa ni lazima rasilimali hizi toshelevu tulizonazo zitumike. Kwa eneo la Mto Ruvuma kwa maana ya Mtwara
tukitumia chanzo cha Mto Ruvuma tutamaliza kabisa tatizo la maji katika Mkoa wa Mtwara. Kwa hiyo, hiyo ni dhamira yetu na Serikali tuna maongezi na wadau mbalimbali naamini imani hii tunakwenda kuitekeleza na kuhakikisha wananchi wa Mtwara wanaenda kuondokanana tatizo kabisa la maji. (Makofi)
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini sasa Serikali itamaliza kutujengea barabara inayotoka Mayanga kuelekea Mkunwa kwenye Halmashauri yetu ya Wilaya kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja itajengwa kwa kiwango cha lami, na kwa kweli itategemea na upatikanaji wa fedha na kwa kweli sina uhakika kama kwenye bajeti hii imo. Tusubiri hiyo bajeti tuone kama itakuwa ipo kwenye mapendekezo kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii; je, ni lini sasa Serikali itajenga Stendi na Soko katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Mtwara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ujenzi wa stendi na soko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ni moja ya mahitaji ya wananchi na Serikali yetu ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, sasa nitumie fursa hii pia kuendelea kusisitiza kwamba ni wajibu wa Wakurugenzi wa Halmashauri husika kuweka vipaumbele kupitia mapato ya ndani, kuanza ujenzi wa stendi na soko. Halmashauri zetu nyingi zina uwezo wa kufanya hivyo zikiweka kipaumbele, lakini na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa maana ya Serikali Kuu tutaendelea kufanya tathmini na kuona maeneo ambayo yanahitaji kuongezewa nguvu, tutafanya hivyo ili stendi hizo na masoko yaweze kukamilika kwa wakati, ahsante. (Makofi)
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii. Je, ni lini Serikali itatupatia minara ya mawasiliano katika Kata ya Tangazo na Kijiji cha Namgogori hakuna kabisa mnara wa mawasiliano ili wananchi wangu waweze kufurahia huduma hii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Mbunge, maeneo ambayo ameyataja baada ya Bunge lako Tukufu tukutane ili tuweze kuyaweka vizuri na tutume wataalam wetu wakafanye kazi na baada ya hapo tuhakikishe kwamba tunafikisha huduma ya mawailiano, ahsante sana.(Makofi)
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Tatizo lililopo Kyerwa linafanana kabisa na tatizo lililoko Mtwara Vijijini. Kata ya Mpapura Kijiji cha Nanyani tokea Julai, 2017 ujenzi wa zahanati ulishakamilika. Mpaka leo ninapozungumza takribani ni miaka minne. Ni lini sasa Serikali itakwenda kufungua zahanati hiyo ili wananchi waweze kupata huduma kwa sababu wamesubiri kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu kwa kutoa agizo la jumla kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri na Ma-DMO kuhakikisha wanatuletea taarifa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya zahanati zote ambazo zimeshakamilika na zinahitaji usajili ili ziweze kufunguliwa na sisi tuweze kujua namna bora ya kuchukua hatua za kuzifungua mapema.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Katika Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Vijijini hatuna kabisa kituo cha polisi; je, ni lini Serikali itatujengea kituo cha polisi katika halmashauri yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishaeleza katika maswali niliyojibu muda mfupi uliopita, si wilaya zote zina vituo vya polisi vya ngazi ya wilaya kwa kulitambua hilo ndiyo maana tuna mpango mkakati wa kiwizara wa kujenga vituo vya polisi vya OCD katika kila wilaya kulingana na mpango wetu na kwa mujibu wa upatikanaji wa fedha Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mtwara na kwa umuhimu wa ukanda ule kitapewa kipaumbele, nashukuru sana.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Je, ni lini sasa Serikali itajenga barabara inayotoka Mtwara mjini kuelekea Msimbati ambako kuna visima na mitambo ya gesi kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua jambo hili kwenye Ziara ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wewe pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Mtwara mliliulizia na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni barabara hii ni ya muhimu. Kwa hiyo tunaendelea kujipanga kadri fedha zitakapopatikana tutaijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Je, ni lini sasa Serikali itajenga barabara inayotoka Mtwara mjini kuelekea Msimbati ambako kuna visima na mitambo ya gesi kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua jambo hili kwenye Ziara ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wewe pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Mtwara mliliulizia na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni barabara hii ni ya muhimu. Kwa hiyo tunaendelea kujipanga kadri fedha zitakapopatikana tutaijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Tatizo lililopo Bukoba Vijijini linafanana kabisa na tatizo lililopo Mtwara Vijijini. Kata ya Mango Pacha Nne, kuna mradi wa maji hadi leo haujakamilika. Je, ni lini Serikali itamalizia mradi huu ili kumtua ndoo kichwani mama wa Mango Pacha Nne ambaye kwa muda mrefu wamekuwa na changamoto kubwa ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge amefuatilia hili sana na nimhakikishie nitafika Mtwara vijijini lakini tayari naendelea kusisitiza maelekezo tuliyoyatoa kwa watendaji wetu waweze kufanya kazi usiku na mchana ili mradi ule uweze kukamilika na akinamama na familia zote za Mtwara Vijijini ziweze kunufaika na kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan. Tunampongeza Mama Samia tumeshapata fedha asilimia 95 ya bajeti ambayo tunakwenda kuimaliza hivi punde. (Makofi)
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kutokana na Jimbo la Mtwara Vijijini kupakana na Nchi jirani ya Msumbiji; je, Serikali haioni haja sasa ya kujenga Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya ili kuleta tija kwa wananchi wa Jimbo langu la Mtwara Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mchoro wa awali uliotayarishwa upo katika level hiyo niliyoitaja, wazo lake linachukuliwa na tutakwenda kulifanyia kazi.

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Je, ni lini sasa Serikali itatatua changamoto ya maji ambayo ipo kwa muda mrefu katika Kata ya Lipwidi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia lini Kata hii aliyoitaja tunapeleka maji? Mheshimiwa Shamsia kwanza nikupongeze kwa sababu umeishafuatilia sana lakini jitihada zinazoendelea pale Jimboni umeziona viongozi wetu wa Mkoa wa Mtwara wanaendelea kufanyia kazi na Kata hii inakwenda kupatiwa huduma ya maji safi na salama muda siyo mrefu.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kutokana na Jimbo la Mtwara Vijijini kupakana na Nchi jirani ya Msumbiji; je, Serikali haioni haja sasa ya kujenga Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya ili kuleta tija kwa wananchi wa Jimbo langu la Mtwara Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mchoro wa awali uliotayarishwa upo katika level hiyo niliyoitaja, wazo lake linachukuliwa na tutakwenda kulifanyia kazi.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Tangazo na Naumbu, Kijiji cha Namgogori hakuna kabisa minara ya mawasiliano. Je, ni lini Serikali italeta minara ya mawasiliano katika Jimbo la Mtwara Vijijini kiujumla?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo aliyoyataja itabidi tukajiridhishe kama hayapo kwenye mradi wa minara unaoendelea sasa hivi wa rural coverage, tutafanya tathmini na tutaingiza kwenye mradi unaofuata ili wananchi wake wapate huduma za mawasiliano. (Makofi)
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali la nyongeza. Ikiwa Serikali imefanya tathmini na maandalizi ya mchakato wa fidia ulishafanyika, maana yake ni kwamba, fedha ilitengwa kwa ajili ya mradi huo. Sasa nataka kujua, mradi huu umekwama wapi na fedha iliyotengwa tokea mwaka 2015 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu imepelekwa wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Shamsia kwa namna ambavyo anaendelea kupambana na kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika. Mradi huu haujakwama kwa sababu, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, fedha zilitengwa mwaka 2015. Katika upande wa engineering, unapofanya usanifu na baada ya usanifu mradi ukakaa kwa muda mrefu kabla ya kutekelezwa, maana yake ni kwamba inawezekana kuna mabadiliko ya mahitaji ya eneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachofanya sasa kama Serikali ni kufanya mapitio ya usanifu ili tujiridhishe kama mahitaji ambayo yalikuwepo 2015 ni sawa na mahitaji ya sasa au tunapobadilisha ule usanifu maana yake ni kwamba, maeneo ambayo mradi utapita inawezekana kukawa na mabadiliko, ili tujiridhishe kwamba watakaolipwa watalipwa fedha kulingana na njia kuu ya bomba ambapo litapita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu haujakwama na tumeshaanza tayari kuhakikisha kwamba wananchi wa Mtwara wanapata maji, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Tangazo na Naumbu, Kijiji cha Namgogori hakuna kabisa minara ya mawasiliano. Je, ni lini Serikali italeta minara ya mawasiliano katika Jimbo la Mtwara Vijijini kiujumla?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo aliyoyataja itabidi tukajiridhishe kama hayapo kwenye mradi wa minara unaoendelea sasa hivi wa rural coverage, tutafanya tathmini na tutaingiza kwenye mradi unaofuata ili wananchi wake wapate huduma za mawasiliano. (Makofi)
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Serikali itamalizia kilomita 35 Barabara ya Uchumi iliyoanzia Ziwani – Madimba – Msimbati kwa kiwango cha lami ambako kuna mitambo na visima vya gesi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, barabara aliyoitaja ndiyo inaenda kwenye visima vyetu vya gesi kilomita 35 na kama atakuwa ameona, bajeti tumepitisha na ipo kwenye mpango kuanza kuijenga hiyo barabara yote kwa kiwango cha lami katika mwaka unaokuja wa fedha. Ahsante. (Makofi)