Primary Questions from Hon. Rehema Juma Migilla (23 total)
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaondoa vikwazo kandamizi kwa walimu wanaotaka kuhama vituo vyao vya kazi kwa hiari yao kutokana na sababu mbalimbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna vikwazo kandamizi kwa walimu wanaotaka kuhama vituo vyao vya kazi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kufuata wenza wao au ugonjwa. Hata hivyo, katika kuhamisha mwalimu, Serikali inazingatia ikama ili kutoathiri taaluma kwa kuhakikisha wanafunzi wanaendelea kufundishwa masomo yote kwa mujibu wa mitaala ya elimu iliyoidhinishwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hitaji hilo ndiyo husababisha katika baadhi ya maeneo walimu kusubiri apatikane mwalimu mbadala kwanza kabla ya kutolewa kibali cha uhamisho ili wanafunzi wasikose haki yao ya kusoma masomo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba uhamisho wa mtumishi wa umma ni haki yake endapo atazingatia utaratibu uliowekwa. Ndiyo maana kuanzia Julai, 2017 hadi sasa Serikali imetoa vibali vya uhamisho kwa walimu 2,755 nchi nzima. Aidha, taratibu za kutoa vibali vya uhamisho kwa walimu wengine walioomba uhamisho zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuwaelekeza walimu nchi nzima na watumishi wengine wote kuzingatia utaratibu na waache kutumia viongozi mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge kuwaombea uhamisho. (Kicheko)
MHE. NURU A. BAFADHILI (K.n.y. MHE. REHEMA J. MIGILLA) aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali haitaki kujenga Hospitali ya Wilaya ya Tabora Mjini baada ya Hospitali ya Wilaya kupewa hadhi ya Hospitali ya Rufaa?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mhemishimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali Na. 96 la tarehe 18/4/2018 lilioulizwa na Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, Serikali imeanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Tabora Mjini tangu tarehe 19 Oktoba, 2015 kwa kuanza na jengo la OPD kwa gharama ya shilingi milioni 150 chini ya Mkandarasi HERU Construction Company Limited ambapo hadi sasa sehemu ya msingi, nguzo, ngazi na slabu vimekamilika kwa asilimia 100. Mkandarasi ameshalipwa jumla ya shilingi milioni 145.7 kutokana na fedha za ruzuku ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Manispaa ya Tabora imetenga shilingi milioni 70 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa jengo la OPD katika hospitali hiyo. Mkakati wa Serikali ni kuimarisha Vituo vya Afya 513 nchi nzima ili viweze kutoa huduma za dharura pamoja na kujenga Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati kwa kuweka kipaumbele kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa, ndiyo maana Serikali imepeleka jumla ya shilingi bilioni 2.6 Mkoa wa Tabora, kwa ajili ya ukarabati wa vituo sita vya Afya katika Wilaya za Nzega, Tabora-Uyui, Igunga, Kaliua na Urambo kupitia awamu ya kwanza na ya pili ya miradi ya afya iliyoanza kutekelezwa Septemba, 2017. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga shilingi bilioni 101 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya 67 nchi nzima ambapo mbili kati ya hizo zipo katika Wilaya ya Uyui na Sikonge, Mkoani Tabora.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Tumbaku inayolimwa Mkoani Tabora inachangia pato kubwa la Taifa:-
Je, Serikali ipo tayari kuboresha mazingira ya kilimo hicho ili kisiathiri mazingira?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la tumbaku hulimwa katika Mikoa 11 ambayo ni Tabora, Kigoma, Katavi, Singida, Shinyanga, Mbeya, Ruvuma, Iringa, Mara, Songwe na Morogoro. Uzalishaji wa zao hili husimamiwa na Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku Tanzania na kwa kufuata taratibu na kanuni za kilimo kinachojali hifadhi ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora unazalisha tumbaku nyingi zaidi kuliko mikoa mingine inayozalisha tumbaku hapa nchini, na hivyo kuchangia sehemu kubwa ya Pato la Taifa. Aidha, katika msimu wa 2015/2016 Mkoa wa Tabora pekee ulizalisha asilimia 47 ya tumbaku yote iliyozalishwa nchini na asilimia 48 kwa ule msimu wa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku Tanzania inasimamia taratibu na kanuni zote ambazo zinahamasisha kilimo bora cha tumbaku na kinachozingatia hifadhi ya mazingira. Pamoja na mambo mengine, Kanuni zinaelekeza kila mkulima wa tumbaku asajiliwe na awe na eneo la kupanda miti isiyopungua 250 au zaidi kwa kila hekta moja ya tumbaku anayolima.
Miti inayopandwa pamoja na kuwa chanzo cha nishati ya kukausha tumbaku pia husaidia kuhifadhi mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Tumbaku Tanzania imeendelea kuhamasisha na kusimamia ubadilishaji wa mabani ya kukaushia tumbaku kutoka ya awali yanayotumia magogo ya miti na kutumia mabani ya kisasa ambayo yameongezeka kutoka mabani 101,982 mwaka 2014/2015 na kufikia mabani 172,405 mwaka 2016/2017. Aidha, mabani ya zamani yamepungua kutoka mabani 192,975 mwaka 2014/2015 hadi mabani 135,410 mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali ni kuhamasisha wakulima wote wa tumbaku nchini kutumia mabani ya kisasa kuanzia msimu wa mwaka 2018/2019 ikiwa ni pamoja na kuendeleza juhudi za kutafuta nishati mbadala. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Manispaa ya Tabora ipo kwenye mradi mkubwa wa maji toka Ziwa Victoria na Bwawa kubwa la Igombe linalotumika kuhudumia Wakazi wa Tabora Manispaa litakuwa halina matumizi tena.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuliweka Bwawa la Igombe kwenye scheme za umwagiliaji ili wakazi wa Tabora waendeshe Kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kupanga matumizi ya maji kutoka katika chanzo, utunzaji wa mazingira na matumizi ya kijamii hupewa umuhimu zaidi kabla ya matumizi mengine. Ujenzi wa miundombinu ya kutoa maji kutoka Ziwa Victoria umelenga zaidi katika kupunguza upungufu wa maji uliopo kwenye Manispaa ya Tabora ambayo kwa sasa inahudumiwa na Bwawa la Igombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji hayo ni kwa ajili ya matumizi ya kijamii tu kwani hayatatosha kwa Kilimo cha umwagiliaji. Kwa kutambua umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa tija na kukabiliana na mabadiliko tabianchi, Wizara yetu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, ina mpango kabambe wa Taifa wa umwagiliaji unaotekelezwa kuanzia 2018/2019 hadi mwaka 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo katika Manispaa ya Tabora, mpango huu umejumuisha uboreshaji na ujenzi wa skimu za umwagiliaji za Imalamihayo, Inala, Magoweko na Bonde la Kakulungu.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Pamoja na jitihada za vijana wengi kujiajiri wenyewe kwa kuendesha bodaboda wamekuwa wakisumbuliwa na polisi kwa pikipiki zao kukamatwa mara kwa mara:-
Je, kwa nini pikipiki zao zinapokamatwa na wanapoenda kuzichukua hukuta baadhi ya vifaa kama betri hazipo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 168 iliyorejewa mwaka 2002 inampa mamlaka Askari Polisi kusimamisha chombo chochote barabarani na kukikagua kubaini kama kina makosa na hatimaye kukizuia na kukamata. Chombo cha moto kinapokamatwa hutunzwa kituoni kwa mujibu wa mwongozo wa Jeshi la Polisi Namba 229.
Mheshimiwa Spika, inapotokea kielelezo kimeharibiwa uchunguzi hufanyika na hatua kuchukuliwa kwa waliohusika na upotevu huo.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Je, ni lini Shule ya Sekondari Isike iliyopo katika Kata ya Igombe itafunguliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari Isike ilijengwa katika makazi ya wakimbizi kwa lengo la kuhudumia wakimbizi na watoto wa jamii inayowazunguka. Mwaka 2012, Serikali ilitoa maelekezo kwa wakimbizi wote waliokuwa wanaishi katika Kambi ya Ulyankulu warejee kwa hiari nchini kwao. Katika kutekeleza agizo hilo, wakimbizi walirejea makwao na wachache waliomba uraia na kuendelea kuishi katika maeneo hayo, hivyo shule ilibaki na wanafunzi wachache sana.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliamua kuwahamisha wanafunzi waliobaki na kuwapeleka katika Shule ya Sekondari Ulyankulu. Kwa kifupi, kufungwa kwa shule hiyo kulitokana na kuzingatia matumizi sahihi ya rasilimali watu, fedha na vifaa pamoja na mazingira salama na bora kwa wanafunzi kujifunzia.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa wanafunzi wa eneo hilo wamepelekwa na kupangwa katika Shule ya Sekondari Ulyankulu. Serikali itafungua Shule ya Sekondari Isike kama itabainika kuna mahitaji. Ahsante sana.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
(a) Je, kwa nini barabara ya Mpanda – Ulyanhulu – Kahama haikujengwa katika kipindi cha 2015 – 2020 kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2015 - 2025?
(b) Je, ni lini sasa ujenzi wa barabara hiyo utaanza kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu swali la Mheshimwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyanhulu, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mpanda – Ugala – Kaliua – Ulyanhulu yenye urefu wa kilometa 457 inayounganisha Mikoa ya Katavi, Tabora na Shinyanga ni moja ya barabara zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020. Barabara hii ipo kwenye kundi la miradi inayotakiwa kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
Mheshimiwa Spika, mkataba kwa ajili ya Upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa barabara ya Mpanda – Ugala – Kaliua – Ulyankulu – Kahama ulisainiwa tarehe 18 Agosti, 2020 kati ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Kampuni ya Crown Tech Consult Ltd kwa gharama ya shilingi milioni 940.30. Kazi hii itafanyika ndani ya miezi 12 na inatarajiwa kukamilika Septemba, 2021. Mara baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa Kina kukamilika, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, wakati kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiendelea, Wizara yangu kupitia TANROADS, inaendelea kuihudumia barabara hiyo ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Aidha, ninapenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa ili ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ufanyike, hatua mbalimbali hufuatwa ambazo ni pamoja na upembuzi yakinifu, usanifu wa kina, utayarishaji wa nyaraka za zabuni na taratibu za ununuzi wa kumpata mkandarasi wa ujenzi. Hivyo, kuanza kwa hatua tajwa, maana yake ni kuanza kwa mradi husika. Ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Vituo vya Afya vya Mwangozo na Uyowa katika Jimbo la Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2020/2021 imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kiasi cha Shilingi milioni 600 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Uyowa na ujenzi unaendelea. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wananchi inaendelea na ujenzi wa Kituo cha Afya Mwangozo. Hadi Aprili 2021, shilingi milioni 158.69 zinazotokana na michango ya wananchi na mapato ya ndani ya halmashauri zimetumika kujenga jengo la wagonjwa wa nje na wodi ya wazazi ambapo ujenzi unaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, halmashauri imetenga shilingi milioni 25 na katika mwaka wa fedha 2021/2022, Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua imetenga shilingi milioni 140 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya Ulyankulu – Uyui hadi Tabora Manispaa kwa kiwango cha lami ikizingatiwa kuwa barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa Wilaya hizo tatu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya Ulyankulu – Uyui –Tabora yenye urefu wa kilometa 77 kwa wananchi wa Wilaya za Kaliua, Uyui na Manispaa ya Tabora ambapo kwa sasa inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na hatimae kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea na juhudi za kutafuta fedha ili kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami, Wizara yangu kupitia TANROADS inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka ambapo katika Mwaka wa Fedha 2021/22 kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni mia tano kimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatekeleza mchakato wa Wilaya ya Urambo na Kaliua kutumia line yake ya umeme ili kupunguza au kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Wilaya hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya za Urambo na Kaliua zinapata umeme kwa njia moja inayoanzia Kituo cha Kupooza Umeme kilichopo Tabora Mjini. Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inatekeleza mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kupooza Umeme katika Kijiji cha Uhuru, Wilayani Urambo, kitakachopokea umeme mkubwa (Kilovolt 132) kutoka Tabora Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi unaendelea, jengo la kupokelea Umeme (Control Building) limekamilika, upimaji wa njia ya msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Urambo umekamilika, uthamini wa mali za wananchi watakaopitiwa na mradi umekamilika na mikataba ya wazabuni watakaoleta vifaa vitakavyotumika kwenye ujenzi (wa njia na vifaa vya umeme) imekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo hicho kitakuwa na njia za usambazaji umeme (distribution lines) zinazojitegemea kwa kila Wilaya, yaani Urambo moja na Kaliua moja na hivyo kufanya ziwe na Umeme wa Uhakika zaidi. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2022.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuwapatia warithi wa mstaafu asilimia 67 ya michango yake pindi anapofariki?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii hutoa mafao kwa wanachama wake kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi ya Jamii Sura Na. 135 kama ilivyorejewa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Na. 6 ya Mwaka 2019 ambapo fao la warithi ni mojawapo ya mafao yanayotolewa pindi mwanachama anapofariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mfuko wa PSSSF, kupitia Kifungu cha 39(1) cha Sheria ya Mfuko, mstaafu anapofariki Mfuko hulipa mafao ya mkupuo ambayo ni jumla pensheni ya miezi 36 (sawa na miaka mitatu) kwa wategemezi. Kwa upande wa NSSF pia, kwa mujibu wa Kifungu cha 37(1)(2)(3) cha Sheria ya Mfuko, mstaafu anapofariki Mfuko hulipa mafao ya mkupuo sawa na pensheni ya miezi 36 kwa wategemezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulipaji wa mafao huzingatia Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2018 na Marekebisho yake ya Mwaka 2019 na Kanuni za Mafao kama zilivyorejewa mwaka 2022. Mafao yanayolipwa hayazingatii asimilia ya michango isipokuwa wastaafu na wategemezi hulipwa mafao kwa mujibu wa kanuni zinazoongoza ulipaji wa mafao.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -
Je, ni lini Minara yenye Kasi Kubwa itajengwa Kata za Nhwande, Kanoge, Uyowa, Silambo, Makingi, Ichemba, Igombemkulu na Mwongozo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Babari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla Mbunge wa Ulyankulu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetekeleza miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata tano ambazo ni Kata ya Kanoge, ambapo kuna mnara wa Airtel umejengwa katika eneo la Ulanga, Uyowa katika eneo la Uhindi, Ichemba eneo la Ichemba yenyewe, Igombemkulu katika eneo la Imara na Mwongozo katika eneo la Mwanditi ambapo minara hii imekamilika na inatoa huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Minara ya Kata za Kanoge, Ichemba, Igombemkulu na Mwongozo inatumia teknolojia ya 2G/3G hivyo inatoa huduma za mawasiliano yenye kasi kubwa; na mnara huu uliopo Kata ya Uyowa unatumia teknolojia ya 2G pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Uyowa imengizwa kwenye mpango wa kuboreshewa huduma za mawasiliano yenye kasi na zabuni yake itatangazwa katika awamu ijayo kulingana na upatinaji wa fedha. Aidha, Serikali itafanya tathmini ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu yenye kasi kubwa katika Kata za Nhwande, Silambo, na Makingi katika mwaka wa fedha 2023/2024, ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawapatia uraia wananchi 6000 kutoka Burundi waliokamilisha mchakato wa maombi ya uraia katika Jimbo la Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, wananchi wapato 6,000 kutoka Burundi wamekamilisha mchakato wa maombi ya uraia katika Jimbo la Ulyankulu. Wananchi hao walikuwa watoto wa wakimbizi wa Burundi wapatao 162,156 waliopewa uraia mwaka 2009/2010. Wananchi hao pamoja na watoto wapatao 6,620 waliozaliwa baada ya wazazi wao kuwasilisha maombi ya uraia, waliwasilisha maombi ya uraia Serikalini.
Mheshimiwa Spika, kwa ufupi wananchi hao walikamilisha kujaza ipasavyo fomu za maombi ya uraia na kuziwasilisha Serikalini. Maombi yao yalifanyiwa kazi na kwa sasa yapo katika hatua za maamuzi. Mara maamuzi yatakapofanyika, wananchi hao 6,620 watajulishwa hatma ya maombi yao.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -
Je, Serikali imetoa mwongozo gani kuhusiana na kiwango cha ubora wa taa zinazowekwa barabarani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijatoa mwongozo rasmi kuhusiana na ubora wa taa zinazowekwa barabarani. Kwa sasa, Wizara imekasimisha shughuli za usimikaji wa mifumo ya umeme ikiwemo taa za kuongozea vyombo vya moto (traffic lights) na taa za usalama barabarani (street lights) kwa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ambapo hutoa msawazo (specifications) wa taa kwa Taasisi nunuzi unaoendana na mazingira na teknolojia ya wakati husika kwa viwango vya kimataifa.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Je, lini Serikali itawapa ajira za kudumu walimu walioajiriwa tangu mwaka 2002 kwa masharti ya ajira za muda Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2017 – 2021 Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua iliidhinishiwa na kuajiri walimu 13 ambao walitimiza sifa za kuajiriwa kwa masharti ya Ajira ya Kudumu na Malipo ya Uzeeni. Aidha, Walimu 29 wameajiriwa kwa masharti ya Ajira za Mkataba kwa kuwa walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 45. Walimu hawa walikuwa ni wakimbizi waliopatiwa uraia wa Tanzania baada ya kupata sifa kwa mujibu wa sheria.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -
Je ni lini Serikali itaanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa bwawa katika Kijiji cha Ichemba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyankulu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wa ujenzi wa bwawa ambao upo katika Kata ya Ichemba, Wilaya ya Kaliua unategemewa kukusanya maji ya matumizi ya nyumbani, pamoja na umwagiliaji kwenye mashamba na unategemewa kunufaisha wananchi wapatao 18,000 wa Kata ya Ichemba na maeneo mengine ya Ulyankulu. Zabuni ya kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo imeshatangazwa na RUWASA na taratibu zingine zinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2024/2025 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itatenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ambayo zitatoa maji kwenye bwawa na kupeleka mashambani.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:
Je, ni lini Serikali itajenga Shule za Sekondari katika Kata za Sasu, Nhwande, Makingi na Kanonge katika Jimbo la Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migila, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2021/2022, Serikali imetuma fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari 15 kupitia mradi wa EP4R shilingi bilioni 15.0 na shule 232 kupitia mradi wa SEQUIP shilingi bilioni 109.57 katika kata ambazo hazina shule na maeneo ambayo yana wanafunzi wengi ukilinganisha na miundombinu ya shule zilizopo.
Mheshimiwa Spika, kati ya fedha zilizotumwa Jimbo la Ulyankulu limepokea fedha shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule moja ya sekondari ya kata. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kata zote zinakuwa na Shule za Sekondari nchini zikiwemo Kata za Sasu, Nhwande, Makingi na Kanonge ambapo kupitia Mradi wa SEQUIP jumla ya shule za sekondari 1,000 zinatarajia kujengwa nchini ili kuwapunguzia umbali wa kutembea wanafunzi kufuata shule.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -
Je, kuna mpango gani kuruhusu Kata za Kanindo, Igombemkulu na Milambo kufanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Udiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa Kata za Kanindo, Igombemkulu na Milambo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua. Hata hivyo, maeneo hayo bado yana mwingiliano wa makazi ya wakimbizi na raia, hali ambayo huathiri utekelezaji wa shughuli za uchaguzi ndani ya maeneo hayo. Serikali inaendelea kushughulikia suala hili chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kuhakikisha wananchi wa Kata hizo wanapata haki ya kushiriki kwenye shughuli za uchaguzi.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -
Je, bei ya mfuko wa mbolea itakuwa shilingi ngapi baada ya Serikali kuweka ruzuku nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, upangaji wa bei ya mbolea za ruzuku huzingatia bei ya soko kwa kila aina ya mbolea na bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kutoa ruzuku kwa kiasi cha mbolea kinachouzwa kwa wakulima. Katika msimu wa 2022/2023 bei ya mbolea baada ya kuweka ruzuku ilikuwa inafanana kwa maeneo yote nchini ambapo mbolea za UREA, DAP na NPKs ziliuzwa kwa wakulima kwa bei ya shilingi 70,000 na mbolea nyingine ilikuwa kati ya shilingi 50,000 na 60,000 kwa mfuko wa kilo 50.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwahamasisha wafanyabiashara kufikisha mbolea karibu zaidi na wakulima, katika msimu wa 2023/2204 bei ya mbolea kwa wakulima inatofautiana kutokana na umbali. Kwa mfano, bei ya mbolea ya kupandia aina ya DAP kwa mwezi Septemba, 2023 ilikuwa ni shilingi 105,347 bila ruzuku na shilingi 76,018 kwa bei ya ruzuku. Aidha, katika kipindi hicho hicho, bei ya soko ya mbolea ya kukuzia aina ya Urea ni shilingi 73,000 na shilingi 65,000 kwa bei ya ruzuku.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa bwawa katika Kijiji cha Ichemba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imefanya Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bwawa hilo kati ya mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019 ambapo usanifu huo ulijumuisha miundombinu ya bwawa lenye ukubwa wa meta za ujazo milioni 3.6. Ujenzi wa bwawa hilo utakapokamilika utawezesha kumwagiliwa kwa zaidi ya hekta 150 pamoja na kutoa huduma nyingine jumuishi ikiwemo za maji majumbani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kaliua itaanza ujenzi wa bwawa hilo litakalohudumia mashamba pamoja na huduma ya maji majumbani. Aidha, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya umwagiliaji ya mashambani.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE K.n.y MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Je, ni sababu zipi zinasababisha wakulima wa tumbaku kukopeshwa pembejeo na kuuza tumbaku kwa Dola badala ya shilingi ya Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Utaratibu wa wakulima wa tumbaku kukopeshwa pembejeo na kuuza tumbaku kwa Dola za Marekani na kulipwa kwa dola unatokana sababu za msingi zifuatazo:-
(i) Biashara ya tumbaku Kimataifa hufanyika kwa Dola za Kimarekani kuanzia upatikanaji wa pembejeo, ugharamiaji wa uzalishaji hadi uuzaji;
(ii) Uuzaji wa tumbaku kwa Dola za Kimarekani unamlinda mkulima na hasara ambazo zinatokana na mabadiliko ya shilingi na kumhakikishia uimara wa kipato chake;
(iii) Zao la Tumbaku linaendeshwa katika misingi ya kibiashara ya mikataba inayosimamia ubora, madaraja na taratibu zake hadi inapofikishwa katika soko na hupimwa kwa viwango vya Kimataifa; na
(iv) Mfumo huu unaihakikishia nchi upatikanaji wa dola za Kimarekani na usimamizi rahisi wa fedha za mauzo kurudi ndani ya nchi. Mfano, msimu wa Mwaka wa Fedha 2022/2023, wakulima wa tumbaku walilipwa Dola za Kimarekani milioni 286.8 na Taifa letu lilipata Dola za Kimarekani milioni 480 kutokana na kuzalisha na kuuza tani 122.8 za tumbaku nje ya nchi na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa Afrika katika uzalishaji na mauzo ya tumbaku nje ya nchi.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE K.n.y MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Je, ni sababu zipi zinasababisha wakulima wa tumbaku kukopeshwa pembejeo na kuuza tumbaku kwa Dola badala ya shilingi ya Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Utaratibu wa wakulima wa tumbaku kukopeshwa pembejeo na kuuza tumbaku kwa Dola za Marekani na kulipwa kwa dola unatokana sababu za msingi zifuatazo:-
(i) Biashara ya tumbaku Kimataifa hufanyika kwa Dola za Kimarekani kuanzia upatikanaji wa pembejeo, ugharamiaji wa uzalishaji hadi uuzaji;
(ii) Uuzaji wa tumbaku kwa Dola za Kimarekani unamlinda mkulima na hasara ambazo zinatokana na mabadiliko ya shilingi na kumhakikishia uimara wa kipato chake;
(iii) Zao la Tumbaku linaendeshwa katika misingi ya kibiashara ya mikataba inayosimamia ubora, madaraja na taratibu zake hadi inapofikishwa katika soko na hupimwa kwa viwango vya Kimataifa; na
(iv) Mfumo huu unaihakikishia nchi upatikanaji wa dola za Kimarekani na usimamizi rahisi wa fedha za mauzo kurudi ndani ya nchi. Mfano, msimu wa Mwaka wa Fedha 2022/2023, wakulima wa tumbaku walilipwa Dola za Kimarekani milioni 286.8 na Taifa letu lilipata Dola za Kimarekani milioni 480 kutokana na kuzalisha na kuuza tani 122.8 za tumbaku nje ya nchi na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa Afrika katika uzalishaji na mauzo ya tumbaku nje ya nchi.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mabani ya kisasa na ya kudumu ya kukaushia tumbaku, Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO atajibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, suala la ujenzi wa mabani ni jukumu la kila mkulima wa tumbaku kwa mujibu wa kanuni za kilimo bora cha zao la tumbaku. Hata hivyo, kutokana na upungufu wa mabani uliosababishwa na athari za mvua zilizonyesha msimu wa mwaka 2023/2024 na kusababisha mabani mengi kubomoka, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya ujenzi wa mabani ya kisasa 600.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imepanga kujenga mabani ya kisasa kupitia mpango wa pamoja kati ya wanunuzi na vyama vya msingi kwa kuongeza muda wa mikataba ya uzalishaji kutoka mkataba wa mwaka mmoja hadi miaka mitatu ambapo pamoja na mambo mengine, mnunuzi atatakiwa kujenga mabani, kwa ajili ya kukaushia tumbaku. Pia wakulima wanahimizwa kujenga mabani ya kisasa au kuboresha mabani ya zamani ili kufikia malengo ya mabani 250,472 yanayohitajika kuongezwa kwa msimu wa mwaka 2024/2025. (Makofi)