Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rehema Juma Migilla (40 total)

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mzuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna tatizo limejitokeza, kuna Waraka unasema walimu wa arts ambao wamezidi katika shule za sekondari wanahamishiwa shule za msingi. Huu uhamisho unakuwaje ilhali Rais wetu alisema walimu wasihamishwe mpaka pale fungu lao litakapopatikana.
Je, hao walimu wameshaandaliwa mafao yao ya uhamisho ili waende kwenye vituo vyao vipya huku tayari Wizara imeshasema mpaka itakapofikia tarehe 15 Februari walimu hawa wawe wamefika vituoni kwao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, napenda kujua, huu uhamisho wa kuwatoa walimu wa arts kutoka sekondari kuwapeleka primary unaweza kuathiri ufundishaji wa wanafunzi wa huko primary. Je, Serikali imeandaa induction course kwa ajili ya walimu hawa ili waweze ku-coup na ufundishaji wa walimu wa primary? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): MheshimiwaMwenyekiti, swali la kwanza kwa wale wanaohusika ambao wamepata Waraka Rasmi wakiusoma vizuri watagundua kwamba maelekezo yaliyomo katika Waraka ule ni kwamba uhamisho unafanyika kutoka kwenye shule ya sekondari kwenda kwenye shule ya msingi ambayo iko karibu na eneo hilo, siyo kumtoa kwenye Wilaya moja kumpeleka Wilaya nyingine. Uhamisho ule ni wa ndani ya kata kwa hiyo hauna gharama za uhamisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ule uhamisho kutoka shule za sekondari kwenda primary umezingatia kwanza kipaumbele kwa wale walimu ambao walijiendeleza, zamani walikuwa walimu wa shule ya msingi wakajiendeleza wakapata diploma na degree hatimaye wakahamishiwa katika shule za sekondari.
Kwa hiyo, kuwarejesha kwenye shule za msingi ambazo wana uzoefu nazo hakuhitaji induction course ya aina yoyote. Kwa hiyo, hicho ndiyo kipaumbele ambacho kimewekwa na kimezingatia walimu wa diploma na walimu wa degree ya kwanza. Ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa inayoongoza katika uzalishaji wa maembe. Mpaka jina la Unyanyembe likapatikana ni kutokana na uzalishaji wa hizo embe, lakini cha ajabu mkoa huo wa Tabora mpaka leo hauna kiwanda cha usindikaji wa maembe, hali inayopelekea maembe yanazagaa kila mahali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niiulize Serikali ni kwanini haitaki kujenga Kiwanda cha Usindikaji wa Maembe Tabora?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba nirejee tena nazidi kuhamasisha Watanzania pamoja na Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwahamasisha wawekezaji katika maeneo hayo. Kwa mfano hapa Dodoma kuna Kiwanda kizuri cha Matobolo wanasindika maembe wanakausha na maembe hayo yanaweza kutumika kwa muda mrefu. Kwa hiyo, sisi tusisubiri kiwanda kije chenyewe ni lazima tuwahamasishe wadau mbalimbali hata sisi wenyewe tuweze kuwekeza ili kuhakikisha kuwa maembe hayo yanakaa muda mrefu.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali sikivu sana kwa wananchi wake hali iliyopelekea mpaka imewarudisha kazini watumishi wa darasa la saba. Swali langu, je, ni lini sasa Serikali itatoa tamko la kuwarudisha masomoni wasichana wote waliopata ujauzito na kuthibitishwa na Mahakama kuwa walibakwa kwani kwa kutowarudisha ni kuwanyima haki yao ya kupata elimu lakini vilevile ni kuwapotezea ndoto zao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba hata sisi Serikali kwa kweli hatupendi na hatutaki kusikia vitendo vya uonevu dhidi watoto wa kike, kwa sasa mfumo wetu wa elimu umepangwa katika namna ya kuhakikisha kwamba wanafunzi ambao wanapata ujauzito wanapata fursa ya kusoma lakini nje ya mfumo rasmi.
Kwa hiyo, kuna fursa nyingine nyingi za kusoma kama nilivyosema katika swali langu la msingi kwa kupitia Elimu ya Watu Wazima na Vyuo vya Ufundi. Serikali haitarajii na naomba niweke wazi kuwarudisha wanafunzi ambao wamepata ujauzito kwa njia yoyote ile. Ni kwa sababu tukifanya hivyo maana yake tunahalalisha na kuhamasisha ngono shuleni wakati mila na sheria zetu haziruhusu ngono katika ngazi hizo maana yake shule za msingi na shule za sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kubakwa, tunaposema kwamba hawaruhusiwi kuendelea na elimu katika mfumo rasmi siyo kwamba ni adhabu kwa kujifungua, tunachochukulia ni kwamba tayari ana mtoto na hivyo tukifanya hivyo tunakuwa tumefungulia milango ya vitendo kama hivyo kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kuna fursa zingine ambazo watoto wale wanaweza kutumia kupata elimu, zipo.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni ukweli usiopingika kwamba suala la uzazi wa mpango ni makubaliano ya wanandoa kuhusu idadi ya watoto wanaowataka, lini wawazae na kwa wakati gani. Sasa, je, Serikali haioni sasa wakati umefika wa kuibadilisha hii sheria ili kuwawezesha wanandoa kupata watoto wanaowataka kutoka miaka mitatu hadi miwili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwa kuna tabia kwa sekta binafsi kuwa hawawapi nafasi ya likizo wafanyakazi wao kutokana na masharti mbalimbali. Sasa, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba hawa wafanyakazi wa Sekta Binafsi nao wenyewe wanapata likizo badala ya kunyimwa mshahara ili akapumzike au aamue apumzike akose mshahara; Serikali ina mpango gani kwa wafanyakazi hawa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, uzazi wa mpango sisi Watanzania tunaishi katika jamii, sisi ni wamoja. Sasa tumetafuta utaratibu gani unaweza kutuweka sisi pamoja; mwingine anataka azae kila mwaka, mwingine anataka azae kila baada ya mwaka mmoja na nusu, mwingine anataka baada ya miaka minne, baada ya mjadala mrefu Bunge hili likaweka utaratibu kwamba miaka mitatu inatosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusisitiza; sheria hii kwanza inalinda afya ya mtoto mwenyewe kwamba unamwacha akue, lakini mhurumie na huyu unayemzalisha kila mwaka na yeye naye anahitaji kupumzika. Kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba, hii sera Serikali imeweka kwa nia moja; kulinda afya ya mtoto apate kukomaa vizuri kabla hujamtafuta mwingine, lakini pia huyo mama naye anahitaji kupumzika, kumzalisha kila mwaka ukasema ni muafaka kati yetu sisi; hao wanandoa wanaishi katika jamii ambayo ina sheria, taratibu na kanuni na hiyo jamii inaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, sekta binafsi kwamba hawawapi nafasi; hizi labour laws, sheria za masuala ya kazi ni za nchi nzima. Kwa hiyo zinatakiwa ziheshimiwe na watu wote; binafsi na wale waliopo Serikalini na Mashirika ya Umma. Pale inapotokea kwamba mtu kanyimwa likizo ya uzazi ati kwa sababu anafanya kwenye shirika binafsi, Waziri wa Utumishi ajulishwe na ntachukua hatua stahiki.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuongeza swali dogo la nyongeza. Kwanza napenda nimpongeze Naibu Waziri wa majibu yake mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumbaku kwa Mkoa wa Tabora na mikoa mingine inayolima tumbaku, tumbaku ni maisha, tumbaku ni uchumi, lakini tumbaku ni maisha yetu. Napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo. Kwa kuwa kasi ya upandaji wa miti haiendani sambamba na upandaji na tunaona kabisa zoezi hili limefeli, nataka niulize Serikali, ina mpango gani kwa sasa kuzihakikishia hizi AMCOS ambazo zina jukumu la upandaji wa miti ili ziweze kutimiza Sheria ya Namba 24 ya mwaka 2001, ambayo inaitaka kila AMCOS kabla ya kusajiliwa iwe na shamba la miti ambayo itawatosha idadi ya wakulima wake kwa mwaka mzima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, napenda kufahamu; kwa kuwa Bodi ya Tumbaku ndiyo yenye jukumu la kusimamia na kuratibu shughuli zote za tumbaku ikiwa ni sambamba na uhifadhi wa mazingira inashindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na changamoto mbalimbali, je, Serikali ina mpango gani wa kuiwezesha hii Bodi ya Tumbaku kuondokana na changamoto za magari, nyumba na ofisi za wafanyakazi ili iweze kufanya kazi kwa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge ambaye ninaamini kabisa na yeye ni mkulima wa zao la tumbaku kule Tabora na amekuwa akilima hiyo tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika maswali yake mawili ya nyongeza, kuhusu suala AMCOS na wakulima ni kwamba sisi kwenye ile Tobacco Industrial Act. No. 24 ya Mwaka 2001 wakulima wetu wote pamoja na hizo AMCOS na mambo mengine ambayo yanaelezea katika Sheria hiyo Namba 24 ya Mwaka 2001, ni kuhakikisha kwamba, wakulima wote pamoja na hizo AMCOS wanaposajiliwa kuhakikisha kwamba mashamba yao yanaendana na miti isiyopungua 250. Vile vile kuhakikisha kabisa kwamba wanatumia yale mabani ya kisasa na si yale mabani ya zamani ambayo yalikuwa yanatumia magogo kama ilivyokuwa kule mwanzo. Hii yote ni katika kuhakikisha kwamba, tunatunza na kulinda hifadhi ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili la nyongeza, kuhusu Bodi yetu ya Tumbaku; ni kweli sisi kama Serikali tunahakikisha kabisa kwamba tunaimarisha na tunaboresha hizi bodi zetu zote. Naomba niziase bodi zetu zote kwamba zifanye kazi kwa umahiri na kwa ubunifu zaidi, na vile vile waweze kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba wanatumia zile fursa mbalimbali za kilimo zilizopo katika kuboresha mazao yao, ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo kwa majibu yake mazuri, lakini napenda niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa ambayo imepata athari kubwa sana ya uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji wa miti ambayo inatumika zaidi kwa ajili ya mkaa na kuni. Hali hiyo
imepelekea Mkoa wa Tabora na maeneo ya jirani kupata mvua ya kusuasua ambayo ndio inatumika zaidi kwa kilimo. Sasa swali langu, je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuhakikisha kwamba pamoja na athari zote hizo zilizopatikana wananchi wataendelea na shughuli za kilimo kama kawaida?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pamoja na Serikali kuyaingiza maeneo ya Imalamihayo, Inala, Bonde la Kakulungu na Magoweko katika mpango wa umwagiliaji, lakini mpaka leo maeneo haya bado hayajaanza kufanya kazi. Sasa tunataka tupate majibu ya Serikali ni lini maeneo haya na skimu hizi zitaanza kufanya kazi kwani mpango huu unaonesha umeanza kazi tangu mwaka 2018?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekit, nashukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rehema Juma Migilla kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza anataka kujua mikakati ya Serikali kwa ajili ya kuendeleza kilimokwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hapo Tabora. Sisi kama Serikali cha kwanza tulichokifanya, mkakati mkubwa tuliokuwa nao ambao badala ya kutegemea fedha za kibajeti, lakini pia badala ya kusubiri fedha za washirika wa maendeleo kutoka nje ya nchi tumeielekeza Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo kuja kwenye halmashauri mbalimbali nchini kukaa nao na kubainisha yale maeneo yanayofaa kwa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kubainisha kujua mahitaji yenu wataenda kuingia mikopo kwa dhamana ya halmashauri na sisi Serikali tutawadhamini zaidi ya asilimia 80 ili kujenga miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo huu Mkoa wa Tabora ili wakulima waendelee kulima cha kisasa cha uhakika na chenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anasema, ni lini kwamba miradi hi tuliyiotaja kwenye jibu letu la msingi kwamba itaanza kufanya kazi. Hii miradi itaanza kufanya kazi muda mfupi ujao baada ya upatikanaji wa fedha za kibajeti na kama nilivyosema kwenye jibu la awali chanzo kingine cha pesa ni kupitia mikopo kupitia Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini naona majibu haya yamejibiwa kisiasa kuliko uhalisia wenyewe ulioko huko kwa waendesha bodaboda.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli ulio hai kabisa bodaboda hawa wamejiajiri wenyewe na wanafanya kazi katika mazingira magumu na wamekuwa wakisumbuliwa sana na polisi especially hawa PT. Wanawakamata na wakishawakamata hata uchunguzi wa kina haufanyiki na sometimes wanawabambikizia makosa. Wanapowabambikizia makosa wanawaaambia watoe hela, wasipotoa zile hela pikipiki zao zinapelekwa polisi. Zikifika polisi, pindi wanapotaka kuzichukua wanakuta baadhi ya vitu kama betri, mafuta na hata wakati mwingine wanakuta hadi gamba zimebadilishwa na tunaelewa kabisa polisi ni mahali ambapo pana usalama wa kutosha na hakuna mtu ambae anaweza akaenda kubadilisha kitu chochote pasipo kukamatwa.

Mheshimiwa Spika, sasa je, Mheshimiwa Waziri, unataka kutuambia wanaohusika na hili zoezi la kuchomoa vitu au vielelezo ni Polisi au akina nani na tunajua kabisa pale ni mahali salama?

Mheshimiwa Spika, swali la pili nataka kufahamu pia pamekuwa na mrundikano mkubwa sana wa pikipiki katika vituo vya polisi na ukizingatia chanzo cha kukamatwa kwa hizi pikipiki na mrundikano huo ni hawa hawa polisi wanazikamata na kuwataka hao watu walipe…

SPIKA: Sasa swali.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: … swali langu; Je, Serikali ina mpango gani kuwarudishia hawa watu pikipiki zao ambapo kwa kuendelea kukaa pale zinaidi kuharibika?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Rehema, Mheshimiwa Mbunge ambaye kwa muda mfupi tangu alipoingia Bungeni ni Mbunge machachari na nimekuwa nikimpa ushirikiano kwa masuala ya Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Spika, mwanzoni nilikuwa najiuliza kwanini watu wanaoagiza magari bandarini vitu vinachomolewa au watu kwenye viwanda vya ndege kunakuwa na pilferage lakini baadaye nikaja kushangaa hata kwenye vituo vya polisi vitu vichomolewe nikaona ni jambo ambalo linashangaza sana.

Mheshimiwa Spika, nilichofanya, kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kwenye ilani hii ya CCM Ibara ya Nne, CCM imeamua kwamba katika changamoto zile nne za Ibara ya 4 za kupunguza umaskini, za kutatua tatizo la ajira tena tukataja bayana vijana, nataka nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba bodaboda ambazo nimetoa maelekezo ili wapambane na umaskini na tatizo la ajira ni bodaboda za makundi manne tu zitakazochukuliwa kupelekwa kituo cha polisi na hata kwenye bajeti hapa nilisema.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, kundi la kwanza, ni bodaboda ambayo imehusika kwenye uhalifu, kwa sababu bodaboda zinatumika kufanyia uhalifu. Hiyo ikikamatwa itapelekwa kituoni. Kundi la pili ni bodaboda ambayo inahusika na kesi na kesi yenyewe, moja ni kama bodaboda hiyo imehusika kwenye ajali ya barabarani ama bodaboda iliyoibiwa sasa katika recovery ikawa imekamatwa, ni kielelezo. Kundi la tatu na la mwisho ni bodaboda ambayo haina mwenyewe sisi (found and unclaimed property) sasa polisi kwa sababu wanalinda mali za raia wataichukua ikae kituo cha polisi, ikipata mwenyewe ichukuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, boda boda zingine zozote ambazo hazipo kwenye kundi hilo, sijui huyu hana helmet, huyu hana side mirror, huyu amepakia mshkaki, hakuna bodaboda itakayokamatwa kupelekwa kwenye kituo cha polisi. Nimewapata utaratibu wa kuwapa siku saba kama ni faini watalipa na nimeelekeza bodaboda ambazo ziko kwenye makundi matatu ztakazopelekwa kituo cha polisi na zenyewe wataandikiwa hati inayoonesha vitu ambavyo viko kwenye bodaboda ile ili atakapokuja huyu mtu a-cross check na hati aliyopewa ili yule aliyechukua kama kuna upotevu aweze kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi bodaboda nchi nzima wanakula raha mstarehe, wanajinafasi. Kama Tabora suala hilo bado linaendelea, Mheshimiwa Rehema nikuhakikishie itakapofika jioni kama Tabora pale kuna pikipiki ambayo haiko kwenye makundi hayo, ama zao ama zangu. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ambayo hayajaniridhisha, naomba niseme kwamba shule ile ilifungwa kwa sababu alizozitaja lakini mpaka dakika hii Shule ya Sekondari Ulyankulu imefurika wanafunzi mpaka wamehamishiwa Shule ya Sekondari Mkindo ambayo sio ya bweni.

Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuwarudisha wale wanafunzi ambao wanatembea umbali mrefu na kuwaongezea wazazi gharama ambazo hazihitajiki?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, shule ile imefungwa sasa hivi haifanyi kazi ya aina yoyote imekuwa ni makazi ya ngedere na nyani, hali ambayo inasababisha wananchi na Serikali waone kwamba walitupa nguvu zao za bure na za rasilimali fedha pasipokuwa na sababu ya maana.

Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuirudisha tena kwa sababu mahitaji yamekuwa ni makubwa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Naibu Waziri wangu kwa kujibu vizuri maswali yote yaliyokuja hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kumpongeza dada yangu Mheshimiwa Rehema Migilla kuwa Mbunge wa Ulyankulu, dada yangu hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lake tumelichukua kwa sababu tunafahamu eneo lile lilikuwa la wakimbizi, lakini wewe ndiyo uko site kule unaona mahitaji yote ya msingi. Hivi sasa namuagiza Afisa Elimu wetu wa Mkoa wa Tabora aende akafanye tathmini ya haraka atuletee majibu ya haraka ili kuhakikisha kwamba tunawasaidia watoto wa eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo siyo shule hiyo pekee, hata ile shule ambayo juzi katika ziara tulipokuwa na Mheshimiwa Rais tumetoa melekezo, shule hizo zifanyiwe harakati za haraka kama ikiwezekana tuzifungue haraka.

Lengo letu kubwa ni Watanzania waweze kupata huduma vizuri. Ahsante sana.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Majibu ya Serikali kupitia Waziri hayaoneshi matumaini kwa wananchi wetu wa Ulyankulu kwamba wanaenda kupata lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara hii ilikuwemo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2015/2020 lakini pia kwenye Ilani ya Uchaguzi ya 2020/2025 barabara hii imo. Majibu ya Serikali yanaonesha barabara hii kwa kipindi chote hicho itakuwa tu kwenye upembuzi yakinifu.

Je, kwa miaka hii mitano mingine barabara hii ina uhakika wa kutengenezwa ili wananchi wangu waweze kupata barabara ya lami? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ni kwamba Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alipotembea Jimboni kwetu Ulyankulu alitoa ahadi ya kututengenezea kilometa tatu kwenye Jimbo letu la Ulyankulu. Lakini tangu kipindi hicho mpaka leo hakuna hata kilometa moja iliyotengenezwa kwa kiwango cha lami.

Swali langu ni je, kupuuzwa kwa kutekeleza kwa kujengwa kwa hii barabara kwa hizo kilometa tatu ni kupuuza ahadi ya Mheshimiwa Rais au na kuwadharau wananchi wake waliompigia kura? Naomba majibu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Migilla, Mbunge wa Ulyankulu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Migilla kama amenisikiliza kwenye jibu langu la msingi ni kwamba tayari usanifu wa kina unaendelea na utakamilika Septemba mwaka huu. Barabara haiwezi ikaanza kujengwa kabla ya kukamilika kwa usanifu. Atakuwa ni shahidi kwamba wakandarasi wanaofanya usanifu wako field na Wizara inatambua kwamba barabara anayoitaja ni barabara muhimu sana kwani katika Jimbo lake tunatambua lina uzalishaji mkubwa sana wa mazao kama mahindi, mpunga na hata tumbaku.

Mheshimiwa Spika, hii barabara sasa ndiyo inayokwenda kwenye mbuga ambazo zimetambuliwa kama National Park ya Ugalla na nimhakikishie kwmaba katika bajeti ya mwaka ujao pia tumetenga fedha kwa ajili ya kufungua na kuanza ujenzi wa Daraja la Ugalla ili kuunganisha Jimbo lake na Mkoa wa Mpanda. Ni barabara ambayo tayari wakandarasi wapo wakiwa wanaifungua.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimalizie kwa kumhakikishia Mheshimiwa Migilla haitatokea na haiwezekani Serikali hii ikapuuza ahadi za viongozi wetu wa Kitaifa. Ahadi imeahidiwa mwaka uliopita isingekuwa rahisi tuwe tayari tumeshajenga hizo barabara na ndiyo maana tunasema tayari wakandarasi wako site wakifanya usanifu wa kina.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge barabara hiyo itajengwa na wananchi waiamini Serikali yao kwamba yaliyoahidiwa na yaliyoko kwenye Ilani yatatekelezwa. Ahsante sana.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza niipongeze Serikali na kuishukuru pia kwa kuweza kutupatia fedha hizi ambazo nina uhakika zinakwenda kumaliza Kituo cha Afya cha Uyowa, lakini niendelee kuiomba Serikali basi hiki Kituo cha Mwangozo na chenyewe kiweze kufikiriwa ili kiweze kuendelea kutoa huduma. Hata hivyo, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa taaluma mimi ni Mwalimu na tunajua vigezo ambavyo vinatumika kuanzisha hizi shule zetu, lakini ningeomba kujua, je, wataalam wa Afya na TAMISEMI huwa wanatumia vigezo gani wanapoamua kujenga hizi zahanati zetu, kwani tunaona baadhi tu ya majengo ndiyo yanajengwa pasipokuwa na maabara ambapo tunajua maabara ndiyo kigezo kimojawapo ili Daktari aweze kutoa huduma vizuri. Je, kwa nini zahanati nyingi huko vijijini hazina maabara?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kama vigezo hivyo vinazingatiwa, je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kutujengea hizi maabara katika zahanati zetu ili kuweza kuwapunguzia mzigo hawa wananchi wetu ambao wanatembea umbali mrefu kwenda kufuata huduma za maabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyankulu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, napokea pongezi zake kwa Serikali kwa kupeleka fedha shilingi milioni 600 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya cha Uyowa. Pili, vigezo ambavyo vinatumika kujenga zahanati zetu ni michoro ambayo imepitiwa kitaalam na ambayo kimsingi kwa ramani zetu kwa sasa za Ofisi ya Rais, TAMISEMI za zahanati zina provision ya maabara. Kwa hiyo, ramani zote za vituo vya afya, zahanati na Hospitali za Halmashauri zina maabara. Hivyo, tutaendelea kuhakikisha tunatenga fedha kwa awamu kukamilisha yale majengo ya zahanati lakini pia na vyumba vya maabara kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma bora za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tunaona of course umuhimu wa kuhakikisha kwamba tunaendelea kujenga maabara na ndiyo maana kwenye swali la msingi nimeeleza ambavyo Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kujenga vituo hivyo zikiwemo maabara katika maeneo hayo.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Ichemba lililopo katika Kata ya Ichemba lilikuwa kwenye mpango wa upembuzi yakinifu tangu mwaka 2015 lakini mpaka dakika hii halijawekwa kwenye huo mpango na baada ya kuingia RUWASA hilo bwawa limesahaulika kabisa. Tunajua bwawa hilo likikamilika linakwenda kutatua kero katika kata tisa za Jimbo la Ulyankulu.

Je, ni lini bwawa hili sasa litawekwa katika mpango wa upembuzi yakinifu na kukamilika kwa ujenzi? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge na nimpongeze sana; katika kipindi ambacho tunaenda kuandika historia katika Wizara yetu ya Maji ni kipindi hiki kwa sababu Mheshimiwa Rais amedhamiria kwa dhati kabisa. Wanasema, yafaa nini imani bila matendo? Mheshimiwa Rais ametuongezea fedha zaidi ya shilingi bilioni 207 kwa ajili ya kwenda kutatua matatizo ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, maeneo ambayo tutawapa kipaumbele ni maeneo yale yenye changamoto na ninatambua Ulyanhulu ni maeneo ambayo yana changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaunga mkono na tutatoa fedha kuhakikisha ile kazi inaanza na wananchi wako waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu hayo ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, suala la barabara hii limekuwa sasa kama ni hadithi. Hata watangulizi wangu wamekuwa wakipigia kelele sana barabara hii lakini pamoja na umuhimu wake bado Serikali inatuletea hadithi ya kwamba inatafuta bajeti. Wananchi wamechoka na hii hadithi, wanataka wajue je, ni lini barabara hii sasa itawekwa kwa kiwango cha lami?

Swali la pili; kwa kuwa Serikali bado inaendelea kutafuta bajeti kwa hii barabara lakini barabara hii ni muhimu sana, inapitisha mizigo kutoka sehemu mbalimbali na inapitisha abiria na mambo mengine. Lakini barabara hii mpaka leo inatumika kama uchochoro kwa baadhi ya magari ambayo yanakwepa kupima uzito sehemu nyingine. Sasa je, Serikali ipo tayari kutujengea mzani ili barabara hii iweze kuwa katika ubora wake ule ule?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rehema Migilla kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza siyo kweli kwamba hizi ni hadithi nimesema tu kwamba kwa niaba ya Serikali tunaendelea kutafuta fedha tufanye upembuzi yakinifu na usanifu wa kina tuweze kujua tunahitaji upana wa lami kiasi gani na uzito wa mizigo unaoweza kupita katika eneo hilo, madaraja, ili tupate makisio ya bajeti ili tuweze kutafuta fedha. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira katika wakati huo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ameomba mizani. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa wazo hili limepokelewa na litafanyiwa kazi na watapata majibu kwa wakati muafaka. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu haya mazuri ya Serikali tunaomba yasiishie kwenye maandishi, tunataka kwa vitendo na kwa muda husika, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitutangazia bei, hasa sisi watu wa vijijini kwamba, gharama ya kuunganisha umeme ni 27,000/= lakini haikuweka wazi hiyo 27,000/= inajumlisha nini na nini. Sasa tunataka tufahamu;

Je, Serikali inaposema 27,000/= inajumuisha na nguzo bila kuangalia umbali wa mlaji wa mwisho? Kwa sababu, maeneo mengi unalipa 27,000/= lakini hawapelekewi umeme na kila wakiuliza wanaambiwa tatizo ni nguzo, tunataka leo utupe maelezo yanayojitosheleza kuhusu hili tatizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili. Kumetokea mabadiliko ya ghafla sana na ya kimyakimya kuhusu bei ya umeme kulingana na units ambazo mnazitoa. Hapo nyuma wananchi walikuwa wakilipa 10,000 wanapata units 78, lakini sasa hivi mabadiliko haya yameasababisha 10,000 hiyo hiyo wanapata unit 28. Sasa je, tunataka tufahamu nini kimesababisha haya mabadiliko ya kimyakimya kwa hizi units ambayo inawatesa sana hawa wananchi wetu ambao ni masikini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rehema, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la kwanza niombe kutoa maelezo mazuri kabisa fasaha kwa niaba ya Serikali kwamba, ukilipa 27,000/= utaletewa umeme ulipo pale kijijini, hata kama ni kwa nguzo 20, ni nguzo moja, ni bila nguzo, maelekezo ya Serikali, gharama ya kuunganisha umeme kwa kijijini ni 27,000/=. Na mara nyingi unapounganisha umeme utahitaji mita, utahitaji nguzo, utahitaji waya, utahitaji transformer pia, ni 27,000/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna maeneo ambapo tunapata matatizo Waheshimiwa Wabunge, basi tuwasiliane ilki msimamo huu wa Serikali uweze kutekelezwa katika maeneo ambayo yanahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika eneo la pili, kwa taarifa zilizopo, mabadiliko ya bei za umeme ya mwisho yalifanyika mwaka 2016 kwa kanuni zilizotolewa na msimamizi wa bei ambae ni EWURA. Mpaka sasa hatuna taarifa na hatuna maelekezo na hatuna mabadiliko yoyote yale kwenye gharama za umeme. Lakini wale watumiaji wadogo, tunawaita Domestic 1, maarufu D 1, ukiwa na 9,150/= utapata unit 75, lakini kama utatumia zaidi ya unit 75 kwa mwezi unakidhi kutoka kwenye D 1 kwenda T 1 hivyo, 9,150/= haiwezi kununua tena unit 75 unakuwa ume-graduate kwenda kwenye matumizi makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe kama kuna Waheshimiwa Wabunge ambao wananchi wao bado wanatumia unit 75 na pungufu kwa mwezi, lakini gharama za ununuzi wa umeme zimebadilika kwao, basi tuwasiliane ili tuweze kubaini tatizo ni nini, tuondoe hilo tatizo, lakini hakuna mabadiliko ya wazi wala ya kimya ya gharama za umeme. Nashukuru.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu hayo, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Kulingana na majibu ya Serikali, inaonesha kwamba mafao yanayolipwa hayazingatii asilimia ya michango isipokuwa wastaafu na wategemezi hulipwa kulingana na michango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, je, kwa mujibu wa sheria ambayo imepitishwa hivi karibuni mwaka 2022, inasema mstaafu atalipwa asilimia 33 katika mafao yake kama pensheni yake ya mkupuo; kama analipwa asilimia 33 ina maana kwenye asilimia 100 inabaki asilimia 67 kwa ajili ya pensheni limbikizi; sasa kwa mujibu wa majibu haya, kwanini hawa wastaafu pindi anapofariki, ile asilimia 67 iliyobakia kama pensheni limbikizi wasilipwe wategemezi wake au warithi wake pindi ambapo tunajua kabisa kwamba huyu mtumishi kipindi chote cha utumishi wake ame- contribute kwenye mfuko fully? Kwanini wasilipwe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; tunaona kwamba sasa hivi kuna mfumuko wa bei, maisha yamepanda sana, lakini wastaafu waliostaafu kuanzia miaka ya 2000 na kurudi nyuma pensheni yao ni ndogo sana; ile monthly pension, Serikali haioni sababu au umuhimu wa kuongeza pensheni kwa hawa watu ambao pensheni yao haikui? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kumjibu dada yangu, Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, maswali yake mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi, ni kwamba malipo ya mafao yanazingatia kanuni. Mstaafu anapostaafu, kama alivyoeleza, analipwa mafao ya mkupuo na kunakuwa na wastani wa umri wa kuishi. Sasa kwenye majibu ya msingi kama nilivyoeleza, anapofariki haijilishi kama alishavuka ule wastani wa umri wa kuishi au hajavuka, lakini analipwa ile miaka mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kiasi ambacho anakisema cha asilimia 67 kinawekwa kama makisio, lakini mstaafu analipwa kwa kadri anavyoendelea kuishi, anaendelea kupata pensheni ya mwezi. Kwa hiyo, sasa hivi tunalipa kwa miaka mitatu anapofariki bila kujali kama alikuwa ameshazidi ule umri wa wastani wa kuishi baada ya kustaafu.

Mhelshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Migilla kwa kweli ni la msingi la kuhusu Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza mafao kwa wastaafu. Utaratibu wa mifuko ni kwamba inafanya tathmini (actuarial evaluation) na kulingana na ile tathmini ndivyo ambavyo inaweza ikaangalia uhimilivu na uendelevu kuwaongeza wastaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga kufanya tathmini ya mifuko katika mwaka fedha 2022/2023 na baada ya tathmini hiyo ndiyo tutaona uwezekano wa kuongeza kulingana na uwezo wa mifuko yetu.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tarafa ya Ulyankulu yenye kata saba haina kabisa Kituo cha Polisi, hali ambayo inapelekea vitendo vya kihalifu kuwa ni vingi: Je, ni lini Serikali itatujengea Kituo cha Polisi kwenye hii Tarafa ya Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rehema Migilla kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Tarafa ya Ulyankulu haina Kituo cha Polisi chenye hadhi ya tarafa, lakini ni suala la kuweka katika mipango yetu ili kiweze kufikiriwa kujengewa Kituo cha Polisi. Kwa hiyo, bajeti itakaporuhusu tutaliingiza hili na kituo kitajengwa kwenye hiyo Tarafa ya Ulyankulu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri yangu ya Kaliua kuna walengwa wa TASAF wapatao 946 ambao wametolewa kwenye mpango wa TASAF kwa kigezo kwamba wamehitimu ilhali hata uwezo wa kupata milo mitatu hawana. Je, TASAF wanaangalia vigezo gani ambavyo vinawapelekea hao walengwa wa TASAF kutolewa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rehema Migilla, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tathmini ilifanyika nchini kote ambapo kulikuwa kuna kaya 156,000 ambazo zilionekana zimeboreka kiuchumi. Hata hivyo, bado mwongozo ulikuwa haujatolewa kwa wadau na Halmashauri zote nchini ni namna gani bora ya kuweza kuwaondoa. Sasa nitakaa na Mheshimiwa Mbunge kuweza kuona hizi kaya 946 ambazo wametolewa ni walitolewa kwa vigezo gani, halafu nitampatia majibu yake.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali linguine la nyongeza. Pamoja na mjibu mazuri ya serikali lakini nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kabisa minara ya simu au huduma za simu zinafanywa kibiashara, na mwananchi anaponunua vocha yake au internet anadhamiria apate huduma kulingana na pesa aliyoweka. Hata hivyo, cha ajabu kutokana na kasi ndogo ya hii minara au hizi huduma za simu, wananchi wanafikia mwisho wa muda wa kutumia ile fedha yake ilhali hajapata huduma aliyokusudia. Sasa swali langu: -

Je, kwa kuwa hizi fedha za hawa wananchi wangu zinazokuwa zimetumika ilhali hawajapata huduma, je hizi kampuni za simu ziko tayari kuwafidia hao wananchi wetu ambao pesa zao zimetumika bila kupata huduma kwa sababu inaonekana huu ni wizi kama wizi mwingine?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla Mbunge wa Ulyankulu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa labda niseme kuwa minara amabayo imejengwa katika hizi kata 4 ambapo Mheshimiwa Mbunge ameonesha kulalamikia huduma inayotolewa pale, inatoa huduma ya 2G peke yake, haijaanza kutoa huduma ya 3G. Sasa mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaenda ku-upgrade minara hii amabyo ilikuwa inatoa huduma ya 2G kwenda kwenye 3G, ambapo tukishafikia kwenye 3G na 4G maana yake kwamba Mtanzania na mwananchi wa Ulyankulu ataweza kutumia huduma ya internet bila kuwa na changamoto yoyote ile, ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Vijiji vya Ntwigu, kijiji cha Ng’wandwe, kijiji cha Mwanduti na Kipendamoyo ni miongoni mwa vijiji ambavyo vilikuwa kwenye orodha ya kupatiwa usajili kipindi cha usuluhishi wa migogoro ya Mawaziri nane, lakini baada ya lile zoezi vijiji hivi havijapatiwa usajili.

Mheshimiwa Spika, je hivi vijiji baada ya kuwa vimekosa hadhi ya kuwa kwenye Hifadhi kwa sababu hakuna wanyama na wale wananchi wameshakuwa wengi wamevamia hilo eneo. Ni lini sasa hivi vijiji vitapewa usajili wa kudumu ili wananchi wajue mipaka yao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rehema Migilla kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, usajili wa vijiji unafanywa na Serikali za Mitaa. Hivyo nimuombe Mheshimiwa Rehema kwamba atawasiliana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuangalia kama kuna umuhimu wa vijiji hivi kusajiliwa. Na niombe vijiji hivi vinavyosajiliwa viwe na hadhi inayolingana. Kwa sababu kuna vijiji vingine vinapelekwa kwenda kusajiliwa kumbe viko ndani ya hifadhi. Nitoe tahadhari hiyo kwa wananchi kwamba wanapopeleka vijiji hivi kwenda kusajiliwa wajiridhishe kwamba je, wako ndani ya vibali vinavyoruhusiwa kusajiliwa? Ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kuishukuru Serikali kwa kukubali maombi ya hawa raia wangu, lakini swali langu lilitaka ni lini huu mchakato utakamilika na kwenye majibu hawajaonesha. Sambamba na hilo nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza; Jimbo langu la Ulyankulu katika hizo Kata tatu asilimia 99 ya mwananchi hao kwa sasa ni raia wa Tanzania. Ikijumlisha raia tajinisi na raia wazawa kabisa wa Tanzania lakini wananchi hawa wanaishi chini ya Sheria Na.9 ya wakimbizi ambayo sheria hii sasa inazuia kufanya shughuli zozote za maendeleo ikiwa sambamba na uwekezaji na kufanya shughuli nzuri za kuleta maendeleo kwa wananchi wetu. Sasa je, kwa sasa Serikali haioni kuna kila sababu ya kufuta hii Sheria Na.9 ambayo inazuia maendeleo na uwekezaji kwa wananchi wetu wakati huo Serikali inakwenda kujipanga kwenye zoezi zima la sensa ili kupanga shughuli za kimaendeleo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Waziri amesema kwamba hawa raia 6,620 ni watoto wa raia wa Tanzania, yaani wazazi wao kwa sasa ni raia wa Tanzania halafu watoto ni wakimbizi. Sasa je, kwa sababu mchakato haueleweki utakamilika lini, kwa nini sasa hatuoni haja ya UNHCR kuwahudumia hawa wananchi kwa kuwapatia package inayowapatia wakimbizi kwenye makambi mengine ya wakimbizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Migilla, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, la kwanza, kuhusu umuhimu wa kufuta Sheria Na.9 ili waruhusiwe kufanya vitu vya maendeleo kwenye makazi yale nadhani Mheshimiwa asubiri tutakapokamilisha kuwapatia uraia wote then hatua za marekebisho ya sheria husika zitafuata. Lakini kama tunakiri kwamba bado watu wengine hawajapewa uraia itakuwa ngumu sana hilo kulitekeleza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, watoto hawa wapate package kutoka UNHCR, hilo tutalizungumza, lakini nadhani Mheshimiwa Mbunge jambo la msingi ilikuwa kuharakisha wapate uraia wao ili wa-enjoy haki nyingine kama raia kuliko hilo la package lakini maadam Mheshimiwa Mbunge ameliuliza hapa, tutafanya mawasiliano na wenzetu wa UNHCR kuona uwezekano wa kuzingatia hili ombi lake. Nashukuru. (Makofi)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Ulyankulu ambao walipatiwa uraia wana cheti cha NIDA, mara kwa mara wamekuwa wakiambiwa watanyang’anywa vitambulisho vyao vya NIDA.

Je, ni sababu zipi ambazo zinapelekea wananchi hawa kutishiwa kunyang’anywa vitambulisho vyao vya uraia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Migilla kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hatuna utaratibu wa kumnyang’anya kitambulisho mtu aliye na sifa za kupata kitambulisho hicho, sasa kama pana mamlaka au Afisa yeyote wa Serikali anawatishia kwamba atawanyang’anya, tuombe tu Mheshimiwa Mbunge atupatie hizo taarifa ili tuweze kuzifuatilia kwa umakini kuona sababu na nini kilizosababisha watishiwe hivyo, lakini utaratibu huo haupo. Ninashukuru. (Makofi)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kutoa masikitiko yangu kwa Serikali, majibu yaliyotolewa na Serikali kiukweli hayaridhishi. Kama Serikali yenye wajibu wa kutoa mwongozo kuhusu namna gani taa za barabarani ziwekwe haijatoa mwongozo mpaka sasa, hali hii inasababisha mamlaka zilizokasimiwa kufanya shughuli hii kuweka taa za barabarani kwa utaratibu wanaotaka wao. Kwa sasa hivi ukiangalia maeneo mengi taa zilizowekwa barabarani ni hafifu mno, hazina ubora, lakini bado taa hizo hizo zilizowekwa barabarani zimewekwa aidha upande mmoja hali ya kwamba ikitokea labda zimeungua eneo hilo linabaki giza. Hata hivyo, taa hizo hizo hazifanyiwi maintenance kwa muda unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; je, Serikali iko tayari sasa kama yenye mamlaka kutoa waraka au mwongozo ili mamlaka zilizokasimiwa ziweze kuleta maana halisi ya uwekaji wa taa barabarani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Jimbo langu la Ulyankulu tangu kuundwa kwake halijawahi kuwa na barabara ya lami hata kilomita moja. Hata hivyo, kwa sasa kuna ujenzi wa kilomita moja na nusu ambao unatekelezwa kama ahadi ya Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Je, Serikali iko tayari kwanza kumalizia kilomita moja na nusu ya lami iliyobakia na kuweka taa za barabarani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rehema Juma Migila, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba TEMESA ndiyo ambao wamepewa kazi ya kuweka na kusimamia taa za barabarani. Pia TEMESA ndio wataalam wa kufanya kazi hizo kwa upande wa Serikali. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pia kwamba taa kulingana na teknolojia inavyobadilika unaweza ukasema utaweka taa hizi lakini kadri teknolojia inavyobadilika taa zimeendelea kubadilika. Zamani tulikuwa tunatumia umeme sasa hivi tunatumia solar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama unaweza ukaweka Mwongozo unaweza pia ukawa unashindwa kwenda na teknolojia. Ndiyo maana katika jibu langu la Msingi nimesema wanakwenda kulingana na mabadiliko ya teknolojia na nini wenzetu duniani wanachofanya na wataalam ndicho wanachokifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kwamba pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna aina mbili ya barabara na tuna taasisi mbili zinazosimamia barabara. Katika Mkoa wa Tabora ambao Mheshimiwa Mbunge anatoka, katika mtandao wa taa mkoa mzima tuna taa 1,568 mpaka leo ninavyoongea ni taa 50 tu ambazo haziko katika mtaa mmoja ambazo ni mbovu. Kwa hiyo, inawezekana barabara anayoisema inawezekana si barabara ambayo pengine inasimamiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS). Hata hivyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama kuna changamoto ambayo mtaa mzima hauna taa nitaomba baada ya hapa tukutane naye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Ulyankulu tutakamilisha ujenzi na tutamwekea taa za barabarani 47 katika kituo chake hicho cha Ulyankulu, ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa swali la nyongeza. Chuo cha VETA Ulyankulu kimechaka sana na hakina majengo ya kutosha, lakini 2020/2022 kilitengewa bajeti ya shilingi milioni 638; fedha zile zilichukuliwa zikarudishwa Wizarani.

Je, Serikali iko tayari sasa kuzirudisha zile milioni 638 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa chuo changu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, sina taarifa kamili ya fedha hizi labda baada ya kipindi hiki tuweze kuonana na Mheshimiwa Mbunge.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara ya Mpanda – Kaliua – Ulyankulu mpaka Kahama yenye urefu wa kilometa 472 iko kwenye Ilani ya Uchaguzi 2015/2020 lakini iko kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025. Je, barabara hii sasa ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ya kilometa 472 ni kweli iko kwenye Ilani ya 2025 na Serikali ya Chama cha Mapinduzi inatekeleza ilani hii ya 2025. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba kwa kuwa bado tunaendelea na utekelezaji wa ilani hii, uwe na uhakika kwamba pia barabara yako itajengwa.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, NMB kama mdau wa elimu ameandaa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu lakini mikopo hii itatolewa kwa wale wanafunzi ambao wazazi wao ni wafanyakazi. Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha wale wanafunzi wanaohitaji mikopo ambao wazazi wao siyo watumishi wanapata mikopo kwa asilimia zote?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Migilla kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli wenzetu wa NMB walitenga fedha shilingi bilioni 200 katika mwaka wa fedha uliopita na mwaka huu watatenga tena kwa ajili ya kuendelea na zoezi hili. Nimuondoe wasi wasi Mheshimiwa Mbunge pamoja na kigezo kile cha mzazi awe ni mtumishi lakini vilevile tumeweka kigezo cha mzazi kuwa mkulima. Ilimradi amejiunga au yupo ndani ya chama cha ushirika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wazazi wote ambao ni wafanyakazi lakini wazazi wote ambao ni wakulima au wale ambao wako katika vyama mbalimbali wanahusika na mikopo hii na tutakwenda kufanya review kwa kadiri mahitaji yatakavyohitajika, nashukuru.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kuishukuru Serikali kwa hatua iliyofikia kuhusu hawa walimu wangu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na Serikali kutuambia kwamba hawa walimu 13 ambao walikuwa ni raia wa Burundi, wakimbizi, wamepatiwa ajira, lakini mpaka tunavyoongea hivi, hakuna barua waliyopewa inayoonesha kwamba wamepewa ajira za kudumu: Je, Serikali iko tayari kuiambia Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua na mamlaka zinazoshughulikia masuala ya walimu kuhakikisha hawa walimu wanapata barua zao za ajira na stahiki nyingine? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Kuna walimu hawa 29 ambao umri wao umevuka miaka 45 walikuwa wanajazishwa mikataba ya muda, lakini pamoja na kujazishwa mikataba ya muda walikuwa hawapewi gratuity yao.

Je, pamoja na kwamba wamejazishwa hii mikataba, lini watapewa stahiki zao kulingana na mikataba waliyokuwa wamejaza? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la kwanza la Mheshimiwa Migilla la hawa 13 kwamba bado hawajapata barua za ajira zao, tutakaa na Mheshimiwa Mbunge na kuwasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kaliua na kuona changamoto iko wapi kwa ajili ya hao walimu kupata barua zao kama ambavyo kibali kilitolewa na Ofisi ya Rais, Utumishi kwa ajili ya kuweza kuwaingiza katika ajira ya kudumu.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, hili ni suala la kisheria. Ni sheria iliyopitishwa na Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba, mtumishi yeyote wa umma ni lazima anapoingia katika utumishi wa umma asiwe amevuka umri wa miaka 45 ili aweze kuwa amechangia katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa miaka isiyopungua 15. Ndiyo maana hawa baada ya kupata uraia wao na vibali kutoka Ofisi ya Rais, Utumishi walikuwa wameshavuka ule umri wa miaka 45.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi, Katibu Mkuu Utumishi alitoa kibali kwa hawa 29 kuendelea kuwa na ajira ya mkataba, ambapo ni mikataba ya miaka mitano mitano, tofauti na mikataba mingine ya mwaka mmoja mmoja. Watapata kiinua mgongo chao pale watakapofikia umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria ilivyo ya kustaafu.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kumekuwa na tabia wagonjwa wa magonjwa ya kuambukiza wakienda kwenye dispensary na vituo vya afya hawapewi dawa za magonjwa ya kuambukiza kama presha. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha inatoa dawa kwa wagonjwa wetu hata huku kwenye ngazi ya dispensary na vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anachokisema Mheshimiwa Mbunge tulikuwa na tatizo hili, lakini kama Wabunge wanakumbuka juzi nilijibu swali kwamba kwenye eneo la dispensary zimeongezeka dawa zinazotolewa kutoka 243 mpaka 459, maana yake madawa hayo ya presha, sukari yameongezwa kwenye level ya dispensary, kwa hiyo tatizo hilo halitakuwepo tena. (Makofi)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru majibu ya Serikali. Bwawa hili la Chemba ni bwawa kubwa sana na likikamilika lina uwezo wa kwenda kuhudumia kata zangu tisa za Jimbo la Ulyankulu na bwawa hili lina maji mengi sana baada ya upembuzi yakinifu na tayari Serikali imeshatutengea milioni 750 kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hili kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Sasa Je, upi ni mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba maji haya yataendelea kutumika pia kwenye shughuli za umwagiliaji?

Lakini swali lingine la pili, Je, Mheshimiwa Naibu Waziri upo tayari kuongozana na mimi ili Bunge linapokwisha hapa uende uone hali halisi ya bwawa hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ya kwamba kwa kutambua kwamba tunalo bwawa kubwa ambalo ni chanzo kizuri cha maji kwenye kilimo cha umwagiliaji, Serikali itahakikisha kwamba katika mwaka wa fedha ujao tunafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili maji yale pia yatumike kama sehemu ya kilimo na yaguse eneo kubwa zaidi ya kata tisa za Ulyankulu ili wananchi waweze kunufaika na bwawa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda jimboni kuangalia jambo hili pamoja na watalaam wetu ili kuweza kuharakisha zaidi ili wakulima wa Ulyankulu waanze kulima kupitia chanzo hiki cha maji kupitia mfumo wa umwagiliaji.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kutoa elimu bure kwa wanafunzi wetu lakini bado kuna michango mingi sana ambayo inakera kwa wazazi. Mfano katika shule za kwetu huko vijijini, shule inaambiwa iwe ya bweni, mzazi anahitajika atoe mpaka kitanda, na kuna baadhi mpaka hela ya chakula. Sasa inapotokea mzazi ameshindwa kutoa hizo huduma ambazo anatakiwa achangie mtoto anaadhibiwa.

Je, Serikali ina kauli gani kuhusu hizi shule ambazo zinatoa adhabu kwa wanafunzi, badala ya kwa mzazi ambaye ameshindwa kuhudumia hiyo michango?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake fasaha.

Mheshimiwa Spika, pia niipongeze sana Young Africans kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, pamoja na sera ya elimu bila malipo, ambayo Serikali tunaendelea kuitekeleza, katika hili nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sera ya elimu bila malipo na kama Mheshimiwa Waziri wa Fedha alivyosoma hoja yake ya Bajeti Kuu, na sasa hivi tunaenda mpaka Form Five na Form Six tunamshukuru na kumpongeza sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa michango ya wazazi, kwenye masuala ya uendeshaji wa shule za sekondari, upo mwongozo ambapo Bodi au Kamati za Shule zinashirikisha wazazi au walezi. Kwa hiyo, ningependa kutoa maelekezo kwa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu kushirikisha wazazi au walezi kupitia mwongozo ambao Serikali imeutoa namna tunavyoshikirikisha wazazi au walezi kwenye ile michango tunahitaji kushirikisha wazazi au walezi kuendesha shule zetu.

Mheshimiwa Spika, mwongozo upo bayana kwa hivyo maelekezo yangu kwa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu, ni kuwashirikisha wazazi kupitia vikao ambavyo vimepangwa kwa taratibu zilizopo, bodi za Shule na Kamati za Shule, hayo ndiyo maelekezo yangu. Ninashukuru. (Makofi)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kata hizi ambazo nimezitaja kwenye swali langu la msingi ziko mbali sana na mojawapo ina mto katikati, kwa hiyo wanafunzi wanapata shida sana kwenda shuleni. Shule inayo-accommodate wanafunzi wa kata hizi ambazo hazina kabisa sekondari ni Shule ya Sekondari Mkindo. Sasa je kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuifanya hii sekondari ya Mkindo kuwa ni sekondari ya bweni ili iweze kuwasaidia wanafunzi ambao wanatoka maeneo ya mbali waweze kufikia ndoto zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali iliona umuhimu wa kujenga vituo vya afya kwa kupitia pesa za tozo lakini pia pesa za COVID-19. Je, kwa kata hizi zenye maeneo ambayo hayana sekondari, kwa nini isilete mpango mahsusi kama ilivyofanya kwenye Wizara ya Afya ili kuhakikisha na hizi kata ambazo hazina sekondari na zenyewe zinapata sekondari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amehitaji kwamba katika Kata ya Mikindo tuifanye kuwa shule ya bweni, tulipokee wazo hili na tutakwenda kufanya tathmini tutafute fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hii.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali ina mpango mahususi na mpango wetu ni kujenga sekondari 1,000. Mwaka wa fedha huu ambao unaisha 2021/2022 tumeshapeleka fedha katika kata 232, karibu bilioni 109.57 na katika mwaka wa fedha ambao Wabunge wameshatupitishia bajeti kwa maana ya 2022/2023 tutajenga shule za sekondari 234, manake tutapeleka katika kata zote katika majimbo ambayo bado hawajapata. Mwakani vilevile na mwaka kesho kutwa tutafanya hivyo hivyo. Kwa hiyo ndani ya miaka ya Mama Samia tutamaliza shule zote 1,000 ambazo Mheshimiwa Rais ameahidi kupitia mradi wa SEQUIP. Kwa hiyo nimwondoe shaka kwenye hilo. (Makofi)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nataka nijue nini kauli ya Serikali kuhusu wananchi kuuziwa nguzo za umeme, kwani mpaka hivi leo kuna wananchi wanataka kuingiza umeme kwenye majumba yao, wanauziwa nguzo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema, Mbunge wa Ulyankulu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) hatukubali na haturuhusu watu kuuziwa nguzo katika umeme mkubwa. Pale ambapo ni sehemu ya gharama ya kuunganishiwa umeme inawekwa katika gharama hizo. Lakini pale ambapo Mheshimiwa Mbunge au mwananchi ana taarifa yoyote ya mwananchi kuuziwa nguzo ambapo ni wajibu wa TANESCO kuzipeleka, basi atuletee taarifa hiyo na tutashughulika na hilo tatizo haraka iwezekanavyo.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na napenda kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, maeneo mengi kwenye Halmashauri wametenga maeneo kwa ajili ya wamachinga, namaanisha wamewajengea vibanda na vibanda hivi wanakwenda kuwapangisha. Hawa wamachinga mtaji wao ni kuanzia shilingi 20,000 mpaka shilingi 4,000,000; je, Halmashauri ziko tayari kuwapatia bure hivi vibanda kwa ajili ya kufanya biashara zao?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika mikakati ya kuhakikisha tunawezesha wajasiriamali na hasa wamachinga ni kuwatengea maeneo, lakini pia kuwawekea miundombinu wezeshi ikiwemo vibanda hivyo ambavyo vinasaidia kufanya biashara zao katika mazingira mazuri, lakini kama ulivyosema katika Halmashauri huenda wanakusanya fedha kidogo kwa ajili ya kuvikarabati au kuhakikisha vile vibanda vinakaa muda mrefu viweze kuwasaidia wajasiriamali au wamachinga hao. Kwa sababu ametoa wazo hilo nadhani tutaongea na wenzetu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kuona namna gani ya kuwasaidia vizuri zaidi wajasiriamali au wamachinga ambao hawana uwezo wa kulipia vibanda hivyo kutokana na hali halisi na maeneo husika. Nakushukuru sana.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kutoa elimu bure kwa wanafunzi wetu lakini bado kuna michango mingi sana ambayo inakera kwa wazazi. Mfano katika shule za kwetu huko vijijini, shule inaambiwa iwe ya bweni, mzazi anahitajika atoe mpaka kitanda, na kuna baadhi mpaka hela ya chakula. Sasa inapotokea mzazi ameshindwa kutoa hizo huduma ambazo anatakiwa achangie mtoto anaadhibiwa.

Je, Serikali ina kauli gani kuhusu hizi shule ambazo zinatoa adhabu kwa wanafunzi, badala ya kwa mzazi ambaye ameshindwa kuhudumia hiyo michango?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake fasaha.

Mheshimiwa Spika, pia niipongeze sana Young Africans kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, pamoja na sera ya elimu bila malipo, ambayo Serikali tunaendelea kuitekeleza, katika hili nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sera ya elimu bila malipo na kama Mheshimiwa Waziri wa Fedha alivyosoma hoja yake ya Bajeti Kuu, na sasa hivi tunaenda mpaka Form Five na Form Six tunamshukuru na kumpongeza sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa michango ya wazazi, kwenye masuala ya uendeshaji wa shule za sekondari, upo mwongozo ambapo Bodi au Kamati za Shule zinashirikisha wazazi au walezi. Kwa hiyo, ningependa kutoa maelekezo kwa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu kushirikisha wazazi au walezi kupitia mwongozo ambao Serikali imeutoa namna tunavyoshikirikisha wazazi au walezi kwenye ile michango tunahitaji kushirikisha wazazi au walezi kuendesha shule zetu.

Mheshimiwa Spika, mwongozo upo bayana kwa hivyo maelekezo yangu kwa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu, ni kuwashirikisha wazazi kupitia vikao ambavyo vimepangwa kwa taratibu zilizopo, bodi za Shule na Kamati za Shule, hayo ndiyo maelekezo yangu. Ninashukuru. (Makofi)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kusema majibu ya Serikali kiukweli sijaridhika nayo kutokana na sababu zifuatazo. Serikali inatambua kwamba hizi kata zipo na ni maeneo yao kiutawala na huko nyuma hizi kata zilikuwa zinafanya uchaguzi wa kumchagua diwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na kwa kuwa kwenye majibu ya Serikali imesema kwamba kuna mwingiliano wa makazi ya wakimbizi na raia lakini wakati huo huo kuna uchaguzi unafanyika kumchagua Rais lakini pia kuna uchaguzi wa kumchagua Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu ni; je, ni sifa zipi ambazo hawa raia au hawa wakazi wa eneo hili wanazo ambazo zinawafanya waweze kumchagua Rais na kuweza kumchagua Mbunge? Lakini ni sifa zipi ambazo hawa raia wanazikosa kuweza kumchagua Diwani na Wenyeviti wao wa Serikali za Mitaa na Vitongoji na Vijiji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; tunajua kabisa katika maeneo ya kata kiongozi wa kushughulikia shughuli za maendeleo katika Kata husika huwa ni Diwani; sasa kata hizi hazina madiwani. Je, ni nani msimamizi wa shughuli za maendeleo katika hizi kata au ni kuniongezea mimi Mbunge majukumu ambayo yangefanywa na madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba nianze kwa kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu wa wananchi hawa na vijiji hivi na kata hizi kuwa na viongozi wanaochaguliwa. Kwa sababu za kiusalama; maeneo yale yana mchanganyiko wa raia na mchanganyiko wa wakimbizi lakini na wale wakimbizi ambao wamepewa uraia hivi karibuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu za kiusalama kuna kazi ya ziada inatakiwa kufanyika ili kujiridhisha na usalama wa wale ambao watakuja kushiriki katika shughuli za uchaguzi ili chaguzi hizo ziweze kwenda kwa mujibu wa taratibu lakini kwa kuzingatia usalama wa nchi yetu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hilo linahitaji umakini mkubwa ili twende katika njia ambayo ni salama zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la kwamba wanachagua viongozi wa Kitaifa kwa maana ya Mheshimiwa Rais lakini pia Mheshimiwa Mbunge; ni sawa lakini ikumbukwe kwamba Mwenyekiti wa Kijiji atatoka ndani ya Kijiji kile, utajiridhishaje beyond reasonable doubt kwamba yule Mwenyekiti siyo mkimbizi au ni raia ambaye bado hajapata uraia rasmi? Kwa hiyo, ndiyo maana taratibu zinaendelea na nikuhakikishie tu kwamba Serikali inaendelea na mchakato huo kuhakikisha kwamba tunakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji na kata hizi zina maafisa wanaoitwa Wakuu wa Makazi ya Wakimbizi ambao wale wanawajibika kutoa taarifa mbalimbali za Kiserikali kwenda ngazi ya halmashauri, wilaya na ngazi nyingine. Kwa hiyo, pamoja na kwamba hakuna madiwani na wenyeviti lakini kuna uwakilishi wa Wakuu wa Makazi ya Wakimbizi katika maeneo yale, ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyojibu Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kwa msimu wa 2022/2023 kwamba mbolea zote ziliwekewa ruzuku, lakini napenda nimwambie kwamba mbolea ya tumbaku NPK haikuwekewa ruzuku na bei yake ilikuwa ina-range kwa dola shilingi 75. Hizi mbolea nyingine zilikuwa zinauzwa kwa nusu ya bei kutoka laki na ishirini mpaka elfu sabini mpaka elfu sitini; na hii mbolea ya ruzuku ya tumbaku kwa mwaka huo NPK imewekewa ruzuku kidogo na mbaya zaidi mbolea hii...

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa Rehema.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo naenda huko. Mbolea hii haiuzwi madukani bali inakopeshwa kwa wananchi wetu. Sasa swali langu, ni kwa nini mbolea hii ya tumbaku NPK haiuzwi bali inakopeshwa kwa wananchi wetu na haipo wazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kumekuwa kuna malalamiko mengi sana kutoka kwa wakulima wetu kwamba mbolea wanayotumia kuweka kwenye mazao yao inakuwa haina nguvu hali inayosababisha mazao yao kuwa yana udumavu na yasiyokuwa bora, katika kuthibitisha hili Mkuu wetu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Batilda Burian juzi amekamata Kampuni ya YARA ambayo ni wasambazaji na wauzaji wa hii mbolea wakiwa wanauza mbolea iliyokwisha muda wake yaani mbolea fake na wanabadilisha vifungashio.

Je, Serikali mna mpango gani wa kuhakikisha mnawasaidia hawa wananchi wote ambao wameuziwa mbolea ya tumbaku na mazao mengine, mbolea fake hali inayosababisha hao wananchi wapate mazao yasio bora? Mna mpango gani wa kuwasaidia hao wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, natambua concern ya Mheshimiwa Mbunge hususan katika mbolea ya NPK katika zao la tumbaku na kwenye tumbaku utaratibu wake ni tofauti na ruzuku inapita katika vyama vya ushirika ambavyo vyama vile ndiyo huwa vinakopesha wakulima wake na wakulima hulipa baada ya muda wa msimu. Mwaka huu baada ya malalamiko makubwa ambayo yalitokea mwaka wa fedha uliopita kwamba walikosa ruzuku, mwaka huu Serikali iliongeza ruzuku kwa kiwango kidogo na jambo hili tutalipitia upya ili kuona namna gani tutaongeza ruzuku zaidi kuwanufaisha wakulima wa tumbaku nchini. Kwa hiyo, hicho ni kitu ambacho mimi mweyewe nakifahamu na nilifika katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge anaelezea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kampuni ya YARA kuuza mbolea iliyopita muda wake, mamlaka ya mbolea Tanzania (TFRA) ndiyo wenye jukumu la uthibiti na usimamizi wa mbolea nchini na kuna hatua wameshaanza kuzichukua ikiwemo kuitaka Kampuni YARA kutoa maelezo na baada ya hapo tutatoa taarifa kamili ya hatua ambazo sisi tutakuwa tumezichukuwa. Kwa hiyo, jambo hili na lenyewe lipo ofisini kwetu na tunalifanyia kazi.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Bwawa la Maji la Ichemba, tunashukuru Mungu limepewa bajeti ya kujengwa lakini tatizo mkataba ulioingiwa wa kujenga lile bwawa ulikuwa na kodi ya ongezeko la thamani.

Je, ni lini sasa hili ongezeko la thamani or VAT inclusive litaondolewa, ili huyu mkandarasi aweze kuanza kazi kwa wakati? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa ambayo ameifanya, nimuombe sasa labda tukutane ofisini, ili tuweze kulishughulikia hili jambo kwa haraka ili ujenzi wa bwawa hili uanze mara moja na wananchi wake waende kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na kwanza tuipongeze Serikali kwa kuanzisha hii teknolojia ya kutumia gesi kwenye magari yetu, lakini magari mengi yanayotumia hii gesi ni magari ya petroli tu.

Je, Serikali ina mpango upi wa kuhakikisha kwamba magari yanayotumia dizeli nayo yaanze kutumia gesi kwani tunaona Kampuni ya Dangote magari yake yanatumia dizeli, lakini wamefanya installation ya mitungi ya gesi, mpango ni upi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tumeanza programu hizi na kwa sasa hivi tulikuwa tuna vituo vitano tu, lakini ili kuelekea kuwa na vituo vingi zaidi tumeanza mazungumzo na hao wawekezaji wa kwenye sekta binafsi ili kuhakikisha wanaona namna ya kuwa na mifumo yote miwili, yaani petroli pamoja na dizeli. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tunaendelea kulifanyia kazi ili kupata namna ya kuyafanya magari yanayotumia dizeli nayo kuweza kubadilishwa mfumo.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu haya yanakatisha tamaa kabisa hasa kwa wananchi wangu ambao wana ndoto kabisa za kutumia hili bwawa, lakini sambamba na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa bwawa hili umekuwa kwenye Ilani ya Uchaguzi kwa awamu mbili mfululizo mwaka 2015 mpaka 2020 limo ikapita bila, lakini mwaka 2020 mpaka mwaka 2025 bwawa hili na lenyewe limo. Ujenzi wa bwawa hili ukikamilika utakwenda kuzisaidia kata zangu tisa na vijiji 27 lakini cha ajabu mpaka leo hivi tunavyoongea hakuna shughuli yoyote iliyoanza kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo.

Je, hatuoni kwamba kucheleweshwa kwa ujenzi wa bwawa hili siyo tu kwamba unamchonganisha Mheshimiwa Rais na wananchi, lakini pia unaniletea mimi ajali kwa wananchi wangu kwamba siwajibiki kwao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, tumeona miradi mingi ya ujenzi wa maendeleo inapofanyika, wale wananchi wanaozunguka maeneo hayo hulipwa fidia, lakini cha ajabu wananchi wanaozunguka mradi wa hili bwawa hawajafanyiwa hata tathimini juu ya kulipwa fidia au kifuta jasho.

Je, ni upi mpango wa Serikali ili kuwapa kifuta jasho au fidia wananchi hao ambao kwa ridhaa yao wameacha maeneo yao ambayo walikuwa wanafanyia shughuli zao za kimaendeleo ili kuacha mradi ufanyike, upi ni mpango?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, jambo la kwanza nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali haiko hapa kukatisha tamaa wananchi na wala wewe Mbunge kukutengenezea ajali kwa wananchi wako, hiyo siyo wajibu wa Serikali. Jukumu letu sisi kama Serikali ni kuhakikisha tunatatua changamoto kwa wananchi hususani kwenye hili eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelitaja la ujenzi wa bwawa, bwawa hili tunajenga kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tulishakubaliana kwamba katika eneo lolote ambalo tunajenga bwawa ni lazima Wizara tatu tuhusike ikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa maana ya kusaidia wananchi wale hususani wafugaji pamoja na kufuga samaki katika maeneo yale. Kwa hiyo, hizi kazi tunafanya kwa pamoja na ndiyo maana unaweza kuona limechukua muda mrefu kidogo kwa sababu ni lazima lizingatie Wizara zote tatu katika ujenzi wa aina moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana katika hatua za sasa Wizara ya Maji wako katika hatua za mwisho ili waweze kuja kumtangaza mkandarasi ambaye ataanza ujenzi na sisi Wizara ya Kilimo tutachukua jukumu la kutoa maji katika bwawa na kutengeneza zile irrigation schemes kwenda kwenye mashamba ya wananchi, huo ndiyo wajibu wetu ambao sasa hivi tuko katika hiyo hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la fidia hakuna jambo lolote ambalo Serikali tutafanya bila kuzingatia maslahi ya wananchi wa eneo husika.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, Ahsante. Kumekuwa kuna unyanyapaa mkubwa sana kwa hawa wasichana ambao walipata mimba pindi wanapoamua kurejea kwenye shule zao walizokuwa wanasoma awali. Unyanyapaa huu unasababishwa kwanza na walimu wenyewe na pia, wanafunzi ambao wanasoma darasa moja.

Mheshimiwa Spika, je, sasa Serikali haioni sababu ya kutenga madarasa maalum kwa hawa ambao wanarudi mashuleni kwa sababu, ni watu maalum na wana mahitaji maalum? Kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuanzisha hayo ma…?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Najibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Rehema Migilla, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Migilla anasema kuwarudisha kwenye shule hizo kunaleta unyanyapaa; kwanza tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Migilla. Tutakwenda kufanya tathmini ya kina, lakini tunadhani kuwatenga na kuanzisha madarasa yao ndiyo unyanyapaa zaidi kuliko tutakapoanzisha ile elimu changamano.

Mheshimiwa Spika, lakini tumesema kwenye majibu ya swali la msingi, mwanafunzi huyu anapotaka kurudi shuleni ni ushauri wa mzazi au mlezi pamoja na mwanafunzi yeye mwenyewe kwamba, ni eneo gani anahisi kwa upande wake yeye litakuwa ni rahisi na jepesi kurudi bila kupata changamoto yoyote. Kwa hiyo, ngoja tukafanye tathmini ya kina kwenye maeneo hayo kwa sababu, waraka huu ni wa mwaka 2021 ndiyo tunaendelea kuutekeleza tuweze kuona performance yake halafu tukiona kwamba matokeo yake siyo chanya, tutafanya marekebisho na kufuata ushauri wa Mheshimiwa Migilla. Nakushukuru sana.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Mheshimiwa Waziri Serikali huwa inatenga shilingi 1,000 kwa ajili ya masuala ya lishe kwa watoto wetu chini ya miaka mitano, lakini mimi kama mwakilishi wa wananchi sijawahi kuona matumizi ya zile fedha hata siku moja kwenye halmashauri zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kauli ya Serikali kuhusu matumizi ya fedha hizo kwa walengwa wetu ambao ni watoto wa chini ya miaka mitano?
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rehema Migilla amesema jambo zuri na nimelisema, kwanza tunaona ongezeko la shilingi 1,000 zinazotengwa kwa ajili ya lishe katika halmashauri mbalimbali, kwa hiyo na mimi naomba nirudishe jukumu kwenu Waheshimiwa Wabunge kuangalia pia au kufuatilia matumizi ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya kutekeleza hafua za lishe katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie pia fursa hii kuwataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, lakini na Wakurugenzi wetu wa Halmashauri kuhakikisha fedha zile shilingi 1,000 zinazotengwa kwa ajili ya kutatua changamoto za lishe zitumike kwenye masuala yenye tija yanayogusa moja kwa moja wananchi na siyo mambo ambayo hayana tija.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kutokana na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kuweza kututengea shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kujenga mabani mapya 600 ya kisasa. Ni ukweli kwamba Serikali mmekiri kuna upungufu mkubwa wa haya mabani na kutokana na ukubwa wa tatizo la athari ya mvua ya msimu uliopita mabani haya 600 ni machache sana. Je, sasa Serikali haioni kuna umuhimu wa kutoa ruzuku ili kuweza kuwajengea wakulima wetu wa tumbaku ambao kwa kiasi kikubwa walipata athari kubwa, hali ambayo imesababisha uzalishaji wao kuwa wa kusuasua?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kulingana na ukubwa wa athari ya mvua iliyonyesha msimu uliopita, wakulima wengi wa tumbaku wamelowesha mashamba yao, mabani yao yameanguka, na hata mitaji yao kuweza kupotea. Hali hii imesababisha hao wakulima waweze kushindwa kufidia au kulipa madeni kwenye vyama vya msingi. Kutokana na hali hiyo kampuni za ununuzi ziliweka madalali wa kufilisi dhamana na mali za wale wakulima wetu, hali ambayo kampuni hizi za udalali zimesababisha taharuki kubwa sana kwa hao wakulima wetu, wakulima wamenyang’anywa mashamba, nyumba na mali zao nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni sababu na haja kubwa ya kusitisha hawa madalali wa kufilisi wakulima wetu, ilhali hali halisi ya athari ya mvua wameiona? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Rehema kwa kazi nzuri anayoifanya katika jimbo lake, hususani kufuatilia wakulima wa tumbaku. Nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya jitihada ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha athari zote zilizosababishwa na mvua kwa wakulima sisi tunakuwa sehemu na ndiyo maana sehemu ya kwanza tumetenga fedha shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kusaidia kujenga mabani ya kisasa, lakini tutaendelea kutenga fedha hata katika mwaka unaokuja, ili kuhakikisha lengo la mabani yote yaliyopo tunaweza kulifikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu tutaendelea kutoa ruzuku katika maeneo mengine ikiwemo mbolea na dawa kwa wakulima wa tumbaku. Vilevile kwenye hili jambo tutaendelea kutenga fedha ili kuhakikisha kwamba tunawasaidia wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wale madalali ambao wametumika kunyang’anya mali za wakulima wa tumbaku, niseme sisi kama Wizara, jambo hili tunalifahamu. Tumekuwa tukilifuatilia na tumesema baada ya hapa tutaendelea kufanya vikao zaidi ili kupunguza athari ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa wakulima kuuziwa mali zao. Kwa hiyo, tunalifahamu na tunalifanyia kazi, nimuondoe shaka Mheshimiwa Mbunge, ahsante. (Makofi)