Supplementary Questions from Hon. Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro (10 total)
MHE. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote niwashukuru wananchi wa Songea Mjini kwa kunichagua kuwa Mbunge na kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu. Pili nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi, Chama Tawala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo lililopo katika Jimbo la Mbogwe ni sawa na tatizo ambalo lipo katika Jimbo la Songea Mjini katika ujenzi wa Vituo vya Afya hususan katika Kata tatu za Ndilimalitembo, Ruvuma na Likuyufusi ambazo wananchi wamejitolea kwa mguvu na wanahitaji msaada wa Serikali. Je, ni lini Serikali itatoa fedha kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya katika Kata ya Ndilimalitembo, Kata ya Ruvuma na Kata ya Likuyufusi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kumpongeza kwa ushindi wake na karibu sana Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake anataka kujua lini Serikali itapeleka pesa kwa ajili ya kukamilisha vituo vya afya katika Kata zake hizo mbili. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba vituo vya afya vinajengwa tena vinajengwa vingi ili kuondoa adha ya matibabu kwa wananchi kwa kutokwenda umbali mrefu kupata huduma ya matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanza na vituo 205 baada ya hivi 205 kukamilika ni azma ya Serikali kuhakikisha na maeneo mengine na hasa ambayo kuna upungufu mkubwa na hasa kwa mijini kumekuwa na msongamano mkubwa sana wa wananchi kufuata huduma ya afya katika hospitali za Mikoa na Wilaya. Ni azma yetu kuhakikisha kwamba vituo vya afya vinajengwa ili kupunguza mrundikano ikiwa ni pamoja na maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa tatizo la wingi wa wagonjwa katika Hospitali ya Morogoro inafanana na wingi wa wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Songea ambao unasababishwa na kukosekana kwa Hospitali ya Wilaya ya Songea. Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya Songea?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali imetukabidhi hospitali za rufaa za mikoa na tunaendelea na maboresho; lakini kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuna fedha ambazo wamezitenga kwa lengo la kuhakikisha kwamba baadhi ya Wilaya ambazo hazina Hospitali za Wilaya ziweze kujenga. Lengo ni kuhakikisha kwamba ule mtiririko wa huduma kutoka katika zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za mkoa, hospitali za kanda mpaka hospitali maalum za kitaifa unazingatiwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, naomba kuongezea kidogo katika majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kutambua umuhimu wa kuwepo na hospitali za wilaya za kutosha, katika bajeti ya mwaka 2018/2019 tunaenda kujenga Hospitali za Wilaya 67. Sina uhakika na naomba Mungu iwe katika hizo Wilaya 67 na Songea ikawepo, ni vizuri tukatizama katika orodha ili tukaona nao kama wapo, nashukuru. (Makofi)
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Napenda kumuuliza swali la nyongeza kwamba wakati utaratibu wa kumpata Mkandarasi wa kutengeneza uwanja huo unaendelea, kwa nini huduma ya ndege isiendelee? Maana yake hivi sasa huduma ya ndege imesitishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa nini huduma za ndege katika Uwanja wa Songea ambazo zinawasaidia wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Njombe zisiendelee wakati Mkandarasi anaendelea kutafutwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tumesimamisha kwa muda huduma za usafiri wa ndege katika kiwanja hicho ili kupisha marekebisho yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea kuongeza tabaka la lami, kwa sababu sasa hivi ndege ikitua na kuondoka inapeperusha changarawe ambapo tuna wasiwasi zinaweza zikaingia kwenye propeller zikahatarisha usalama wa abiria, lakini na ndege vilevile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunafanya ukarabati wa uwanja kwa kuondoa mashimo ambayo yako kwenye uwanja ule ili tuepushe ajali. Hata hivyo, tunahakikisha kwamba huduma zitarudi hivi karibuni baada ya kuwasiliana na TAA kwamba wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba hizo changamoto zilizoko katika uwanja huo zinarekebishwa.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Tatizo la barabara katika Jimbo la Songea Mjini hususan barabara itokayo Songea Mjini kupita Kata ya Ruvuma na Kata ya Subira ni kubwa sana kiasi kwamba haipitiki na hata mimi Februari hii nilikwama wakati natumia barabara hiyo. Je, Mheshimiwa Waziri ni lini barabara hiyo itaweza kutengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuwahudumia wananchi wa Jimbo la Songea Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, ni lini barabara hiyo itaweza kutengenezwa kwa kiwango cha lami, najua kiu yake kubwa angetamani hata kesho barabara ikakamilika, lakini ni ukweli usiopingika kwamba kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami inahitaji pesa za kutosha.
Mheshimiwa Spika, hivyo, ni vizuri katika vipaumbele vya halmashauri yake na katika vyanzo vya mapato walivyonavyo wakaweka kama ni kipaumbele. Pia ni vizuri nikipata fursa wakati nikiwa katika ziara kwenda Ruvuma nitapita ili tushauriane na Mheshimiwa Mbunge tukiwa site ili tuone umuhimu wa barabara hii.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa Mkoa wa Ruvuma unapakana na nchi za Msumbiji na Malawi. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza idadi ya magari pamoja na boti kwa polisi ili kudhibiti uhalifu katika sehemu za mipakani?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, hata nilipotembelea Songea Mheshimiwa Mbunge pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma walileta hoja hiyo ya magari. Niseme tu kwamba Serikali tutazingatia maombi hayo punde tutakapopata magari. (Makofi)
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kutokana na umuhimu wa barabara hii ambao unatupeleka kwenye Stiegler’s Gorge na kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Pwani katika maeneo ya Kibiti, je, ni lini barabara hiyo itakamilika kwa kiwango cha lami ili masuala ya kiuchumi ya Stiegler’s Gorge, kilimo na utalii yaweze kunufaika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tatizo hilo linafanana na tatizo lililopo la kuunganisha kati ya Wilaya ya Malinyi Mkoa wa Morogoro na Namtumbo Mkoa wa Ruvuma. Je, ni lini barabara hiyo inayounganisha Malinyi, Kilosa Mpepo, Londo mpaka Lumecha itaweza kujengwa angalau ipitike kwa kiwango cha changarawe kwa sababu sasa hivi haipitiki kabisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaona umuhimu wa kutengeneza barabara hizi ambazo zinaelekea eneo hili la Stiegler’s Gorge kwa kutokea Kibiti hali kadhalika ile barabara inayotokea upande wa Morogoro kama nilivyojibu katika swali la msingi. Mheshimiwa Mbunge atakumbuka pia katika mwaka wa fedha kuna kiasi cha shilingi bilioni 5 zilitengwa na kupitishwa na Bunge kwa ajili ya kuboresha barabara hii kutoka Kibiti kuelekea sehemu ya Stiegler’s Gorge.
Mheshimiwa Spika, jambo kubwa niseme kama Serikali tumejipanga kwanza kuhakikisha barabara hii inapitika ili iweze kutoa huduma kwa shughuli ambazo zitakuwa zinaendelea kufanyika katika eneo hili. Ule utaratibu wa kujenga katika kiwango cha lami utafanyika katika siku za usoni.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, barabara inayotoka upande wa Malinyi, Kilosa kwa Mpepo kwenda Lumecha kule Namtumbo ukitokea Ifakara (km 499) usanifu ulishakamilika, Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kujenga barabara hii. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira pindi fedha zitakapopatikana barabara hii muhimu itaanza kujengwa. Hata hivyo, kuhusu kuboresha barabara hii ipitike Mheshimiwa Mbunge anafahamu yako maeneo ambayo ni hatari, yana milima mikali, tunajipanga ili kuhakikisha kwamba tunafungua barabara hii ili iweze kupitika muda wote kabla hatujaijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Kumekuwa na ahadi ya Serikali ya kujenga reli ya standard gauge kutoka Mbambabay - Mchuchuma - Songea mpaka Mtwara. Je, ni lini Serikali itajenga reli hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iko kwenye mchakato wa kuhakikisha reli ya Kaskazini ya kutoka Tanga mpaka Musoma na reli ya Kusini kuanzia Masasi mpaka Mbambabay inajengwa kwa kiwango cha kisasa na mpaka sasa hivi ninavyoongea tayari Serikali ilikwishamaliza usanifu wa kina pamoja na upembuzi yakinifu na sasa hivi tuko kwenye hatua za kutafuta mshauri muelekezi wa masuala ya kifedha kwa ajili ya kumpata mwekezaji under PPP tukayeshirikiana na Serikali kujenga reli hizo.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tatizo la uwanja ambalo limeongelewa na Mheshimiwa Matiko ni sawa sawa kabisa na tatizo la Uwanja wa Ndege wa Songea, uwanja ambao unahudumia Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Njombe. Tangu mwezi wa tatu mwaka huu uwanja huo umefungwa na hautumiki tena. Jitihada za Serikali kuleta ndege hazisaidii kwa sababu ndege haziwezi kutua katika uwanja huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni, je, ni lini uwanja huo utafanyiwa ukarabati na kuanza kutumika ili kuwanufaisha wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Njombe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua umuhimu wa huduma hii ya usafiri wa ndege katika Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliarifu tu Bunge kwamba tulishapata mkandarasi wa kufanya ukarabati wa uwanja huu; taratibu za manunuzi zilikuwa zinakamilishwa ili ujenzi kwa haraka ufanyike. Sambamba na ukarabati wa uwanja huu wa Songea tutafanya pia uwanja wa ndege wa Iringa ili lengo sasa la kuweza kufanya haya mashirika ya ndege yaweze kujiendesha kwa faida kwa maana ya viwanja vyote vitatu cha Mtwara, Ruvuma pamoja na Iringa kwa pamoja tukikarabati tutafanya na wao waweze kufanya kazi kwa tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa vuta subira, tuko tayari kufanya matengezo kwenye uwanja huo. (Makofi)
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nimshukuru Waziri kwa majibu yake mazuri na kueleza mkakati, lakini naomba niulize swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hizi hospitali 67 ambazo zitajengwa, je, Wilaya ya Songea Mjini ipo? Kwa sababu kuna wakazi 300,000, Kata 21 na hakuna Hospitali ya Wilaya na kuna kituo hata kimoja tu cha afya. Je, Wilaya ya Songea Mjini ambapo Jimbo la Songea Mjini lipo itapata hizo hospitali 67?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, Mbunge wa Songea Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke nilipo-table budget speech yangu mwaka huu tarehe 14, niliainisha hospitali hizo ambapo kwa mara ya kwanza tunakwenda kuweka historia katika nchi yetu. Katika Mkoa wa Ruvuma tunakwenda kujenga hospitali Namtumbo, Songea DC pamoja na Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme wazi kwamba kwa Songea Mjini bado hatujatenga bajeti yake kwa sababu pale tuna Hospitali ya Mkoa. Hata hivyo, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge tumewasiliana mara kadhaa. Tulichokifanya ni nini? Hapa katikati tutafanya resource mobilization kusaidia watu wa Songea Mjini waweze kupata japo kituo kingine acha afya as a backup strategy kupunguza idadi ya wagonjwa ambao wengi wanakwenda katika hospitali ya mkoa. Kwa hiyo, tutakwenda kulifanyia kazi suala hili katika kuimairisha vituo vya afya.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara ya Likuyufusi – Mkenda mpaka Msumbiji ambayo inaunganisha Jimbo la Mheshimiwa Jenista Mhagama na nchi ya Msumbiji ambayo katikati hapa kuna wawekezaji wengi sana wamefungua na viwanda lakini barabara hiyo bado ni ya vumbi.
Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kunufaisha Jimbo la Songea Mjini, Jimbo la Peramiho pamoja na wawekezaji waliopo ikiwa kuleta masoko nchini Msumbiji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Ndumbaro kwa sababu ukikutana naye yaani ni barabara ya mchepuo, barabara ya Likuyufusi – Mkenda, kwa hiyo, nimpongeze pia Mheshimiwa Jenista kwa sababu mara nyingi sana amefuatilia barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme tu tumetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii ya Likuyufusi – Mkenda lakini pia tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja kule Mkenda, najua hii ndio changamoto ilikuwa kubwa sana ya eneo hili kwa maana hiyo kwamba tumetenga fedha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nitaendelea tu kukupa mrejesho na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo Mheshimiwa Jenista usiwe na wasiwasi eneo hili tumelitengea fedha.
Mheshimiwa Spika, pia daraja hili la Mkenda ni muhimu sana pia kwa wananchi ambao wanakwenda Mbamba Bay kwa sababu ukitoka Mkenda kwenda kule Tingi hii ni muhimu sana wanaitegemea barabara hii ili waweze pia kutembea na kuvuka kuja upande huu wa Peramiho. Kwa hiyo, tumejipanga vizuri. (Makofi)