Primary Questions from Hon. Dr. John Danielson Pallangyo (23 total)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami Barabara ya King’ori kutoka Malula Kibaoni hadi King’ori Madukani, Maruvango, Leguruki, Ngaranyuki hadi Uwiro?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Meru imekamilisha usanifu wa barabara ya Malula-King’ori-Leguki-Ngarenanyuki yenye urefu wa Kilomita 33 ili kuijenga kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.259 ili ipitike majira yote ya mwaka. Serikali inaendelea kutafuta fedha za kukamilisha ujenzi huo. Aidha, ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ni mpango wa muda mrefu ambao utekelezaji wake utategemea upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya barabara hiyo katika mwaka wa fedha 2017/2018 kiasi cha shilingi milioni 221 kilitumika kufanya matengenezo ya kawaida katika barabara hiyo. Vilevile mwaka wa fedha 2019/2020 kiasi cha Shilingi milioni 35.7 kimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya kawaida.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO Aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatoa amana na hisa za wateja waliokuwa wamewekeza katika Benki ya Wananchi Meru ambayo ilifungiwa kutoa huduma za kibenki Mwaka 2018?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo tarehe 4 Januari, 2018 Benki Kuu ya Tanzania iliifutia leseni Benki ya Wananchi wa Meru kutofanya biashara za kibenki kwa mujibu wa vifungu Na. 11(3)(1), 41(a), 58(2) na 61(1) ya Sheria ya mabenki na taasisi ya fedha ya mwaka 2006.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kufuatia leseni benki hizo Benki Kuu ya Tanzania iliiteua Bodi ya Bima ya Amana kwa ufilisi. Katika kutimiza wajibu wake wa msingi kisheria, Bodi ya Bima ya Amana ilianza zoezi la kulipia fidia ya kulipia fidia ya bima ya amana hadi shilingi 1,500,000 kwa wateja waliostahili kulipwa bima ya amana, na zoezi hilo bado linaendelea kwa wateja ambao hawajajitokeza kuchukua fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwisho wa mwezi wa Februari, 2021 jumla ya shilingi bilioni 1.47 zimeshilipwa kwa wateja waliokuwa na amana katika benki hiyo. Malipo hayo ambayo ni sawa na asilimia 78.70 ya kiasi cha shilingi bilioni 1.86 zilizotengwa kwa ajili kulipia fidia. Aidha, jumla ya wateja waliolipwa 4,679 kati ya wateja 13,138, ikiwa ni asilimia 35.61 ya wateja waliokuwa na amana zinazostahili fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, wateja waliokuwa na amana inayozidi shilingi 1,500,000 watalipwa kiasi kilichobaki chini zoezi la ufilisi, ambapo kwa mujibu sheria na taratibu za ufilisi kiasi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatika kutokana na kuuza mali za benki husika. Zoezi hili la kukusanya madeni na mali za Benki ya Wananchi Meru ili kupata fedha ya kuwapatia wateja wenye amana zenye thamani ya shilingi 1,500,000 pamoja na wanahisa wa benki hii bado linaendelea. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi katika ujenzi wa Zahanati na Vituo vya Afya Kata za Arumeru Mashariki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuunga mkono jitihada za wananchi katika Halmashauri zote nchini kwa kutoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya miundombinu ya afya kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Meru shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma ya Zahanati za Ngabobo, Shishtoni na Mikungani.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma ya Zahanati za Ngejisosia, Imbaseni na Msitu wa Mbogo. Vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Maroroni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi kuboresha miundombinu ya afya ikiwemo maboma ya zahanati na vituo vya afya kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Majengo ya Mahakama za Mwanzo katika Kata za Nkoanrua na Nkoaranga ambazo majengo yake yamebomoka?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jengo la Mahakama ya Mwanzo Nkoanrua lilichomwa moto na wananchi na hivyo kushindwa kuendelea kutoa huduma katika eneo hilo. Aidha, jengo la Mahakama ya Mwanzo Nkoaranga katika Tarafa ya King’ori ni chakavu na hivyo kuhitaji kujengwa upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) yanaendelea ambapo utajumuisha mahitaji yote ya ujenzi na ukarabati wa Mahakama katika ngazi zote. Mpango huu utaweka kipaumbele zaidi kwenye ujenzi na ukarabati wa Mahakama za Mwanzo nchini. Lengo la Mahakama ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa Tarafa zote 570 zilizopo nchini zinakuwa na Mahakama ya Mwanzo ifikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Mahakama za Mwanzo za Nkoanrua na Nkoaranga zitapewa kipaumbele katika ujenzi na ukarabati kwenye mpango huo.
Napenda kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa Mahakama katika maeneo yetu, kwani kitendo cha kuchoma moto majengo ya Serikali hasa Mahakama, ni kitendo cha kulaaniwa na hakipaswi kurudiwa tena. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawasha umeme kwenye Vijiji na Vitongoji vyote katika Jimbo la Arumeru Mashariki ambavyo umeme bado haujawashwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vyote ambavyo havijapata umeme katika katika Jimbo la Arumeru Mashariki vinapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA awamu ya tatu, mzunguko wa pili ulioanza Mwezi Machi, 2021. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kukamilika Mwezi Disemba, 2022. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 2.07.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitongoji vya Jimbo la Arumeru Mashariki ambavyo havijafikiwa na umeme vitaendelea kupatiwa umeme kupitia mradi wa ujazilizi yaani densification unaotarajiwa kuanza mwezi Julai, 2021. Aidha, kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji ni endelevu, Serikali kupitia TANESCO na REA itaendelea kupeleka umeme katika vitongoji kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara zinazopanda milimani Arumeru Mashariki ili kuwafikishia Wananchi huduma pamoja na kupunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara kwa barabara hizo ambapo gharama zake ni kubwa kutokana na ugumu wa kijiografia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali imeidhinisha jumla ya shilingi bilioni 1.93 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za milimani zenye jumla ya urefu wa kilomita 82.1 pamoja na barabara za ukanda wa chini zenye jumla ya urefu wa kilomita 22.3 kwa kiwango cha changarawe, kujenga daraja moja, makalavati 63 pamoja na kuchimba mifereji ya kuondoa maji barabarani yenye urefu wa kilomita nane.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, barabara zenye urefu wa kilomita sita za ukanda wa milimani zitafanyiwa usanifu kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami. Barabara hizo ni Leganga – Mulala kilomita mbili; Police – Magarisho kilomita mbili; Sangisi – Ndoombo kilomita mbili kwa gharama ya shilingi milioni tano kwa ajili ya usanifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021, Serikali ilifanya matengenezo ya barabara za Maji ya Chai – Sakila kilomita tatu; Police – Ngurdoto kilomita 3.5; Mji Mwema – Dispensary kilomita 0.5; Leganga – Ngarasero kilomita 0.8; Kisimiri Sekondari kilomita nne; Ngarenanyuki –Ngabobo kilomita 2.5; Ubungo – Irrikolanumbe kilomita 2.6; Sangisi – Ndoombo kilomita tano; Tengeru – Nambala kilomita mbili; Poli – Seela kilomita mbili pamoja na ujenzi wa barabara ya Sangis – Nambala kilomita 1.9 kwa kiwango cha lami kwa jumla ya gharama ya shilingi bilioni 1.38.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa barabara zinazopanda milimani Arumeru Mashariki kadri ya fedha zinavyopatikana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO Aliuliza: -
Je, lini Serikali itawaunganishia umeme wa REA wananchi wa Vijiji vilivyopo katika Kata za Jimbo la Arumeru Mashariki ambazo hazina umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Arumeru Mashariki lina jumla ya Kata 26 na vijiji 90. Ni vijiji 12 tu ambavyo havina umeme na sasa vinapatiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaotekelezwa katika Jimbo la Arumeru Mashariki. Kazi zinazofanyika sasa ni usanifu wa kina, upimaji, uandaaji wa michoro na manunuzi ya vifaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi huu unahusisha ujenzi wa njia za umeme ya msongo kilovoti 33 zenye urefu wa kilomita 40.30; kilomita 12 ya njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4; ufungwaji transfoma 12 za KVA 50; pamoja na kuunganisha wateja wa awali 264. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 2.071 na utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika Mwezi Desemba, 2022.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua nyingine Serikali imefanya uhakiki na kuainisha uwepo wa vitongoji takriban 37,610 visivyokuwa na umeme Tanzania Bara na inakadiriwa kuwa shilingi trillion 7 zitahitajika ili kukamilisha mahitaji ya umeme katika vitongoji hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekwishaanza utekelezaji wa miradi ya ujazilizi unaolenga kufikisha umeme katika vitongoji vyote Tanzania Bara awamu kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha ikiwa ni pamoja na Vitongoji vya Jimbo la Arumeru Mashariki.
MHE. SUMA I. FYANDOMO K.n.y. MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza: -
Je, ni lini Shirika la Nyumba la Taifa litaanza ujenzi wa Safari City nje kidogo ya Jiji la Arusha?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Safari City una jumla ya viwanja 1,713 kwa ajili ya uendelezaji wa nyumba na makazi, majengo ya biashara, maeneo ya viwanda vidogo vidogo, huduma za jamii kama shule, hospitali, maeneo ya kuabudia, sehemu za michezo, sehemu za mapumziko na maeneo ya usalama wa mji kama kituo cha polisi na zimamoto pamoja na maeneo ya wazi. Kwa kipindi cha kuanzia Juni, 2022 hadi sasa jumla ya viwanja 970 vyenye thamani ya shilingi bilioni 19.64 vimeuzwa ambapo Shirika la Nyumba la Taifa limekusanya shilingi bilioni 12.33 sawa na asilimia 62.78 ya mauzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi wa Safari City tayari umeanza ambapo mamlaka zinazohusika zinaendelea na uwekaji wa miundombinu muhimu ya barabara, maji na umeme. Pia Shirika la Nyumba la Taifa tayari limejenga nyumba 10 za gharama nafuu za mfano kuwawezesha wanunuzi wa viwanja takribani 23 kuanza ujenzi ambapo baadhi yao tayari wamehamia katika makazi yao.
Aidha, baadhi ya taasisi za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi (NACTVE) zinaendelea na ujenzi katika eneo la mradi. Vilevile Taasisi nyingine ni pamoja na LATRA, OSHA na EWURA zimekamilisha ununuzi wa viwanja na zinatarajia kuanza uendelezaji katika viwanja vyao.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga soko la Tengeru kwa kiwango cha Kimataifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na soko la kisasa kutokana na ongezeko kubwa la shughuli za kiuchumi katika eneo la Tengeru. Kwa sasa eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 2.3 linatumika kama gulio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uhitaji uliopo eneo hilo ni dogo na halikidhi mahitaji ya soko hilo. Hivyo, Halmashauri ya Meru imetenga eneo la Madiira lenye ukubwa wa ekari 15.5 lenye uwezo wa kubeba miundombinu yote ikiwemo miundombinu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri inatarajia kukamilisha na kuwasilisha andiko la mradi huo wa kimkakati Ofisi ya Rais, TAMISEMI Februari, 2023 kwa ajili ya maombi ya fedha, ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA K.n.y. MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati miundombinu ya maji katika Kata za Jimbo la Arumeru Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Arumeru hali ya huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama ni asilimia 71.5 huduma hii inapatikana kutoka kwenye skimu 39 zilizojengwa kabla ya mwaka 2000. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imeendelea na ukarabati wa miundombinu ya miradi ya maji kwenye skimu za Kikwe-Msitu wa Mbogo, Kata ya Kikwe na Mbuguni Olkungabo - Ngabobo (Kata ya Ngarenanyuki na Ngabobo na Ngurdoto-Sakila - Ngyeku Kata za Imbaseni, Maji ya Chai na Kikatiti. Kazi hii itakamilika Mwezi Juni, 2022. Aidha, katika kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji, miradi mipya itajengwa kwa ajili ya kutoa huduma kwenye Kata za Nkoarisambu na Akheri ambapo kazi hii itakamilika Septemba, 2022.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/ 2023, ukarabati wa miundombinu ya maji utaendelea ili kuhakikisha huduma ya upatikanaji wa maji katika Kata zote inakuwa endelevu.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kukarabati miundombinu ya Hospitali ya Wilaya ya Arumeru?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali Kongwe Nchini. Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 17.1 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali 19. Aidha, hadi kufikia mwezi Februari, 2023, kiasi cha shilingi bilioni 12.95 zimekwishatolewa kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya hospitali kongwe kumi na nne 14.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali itatenga shilingi bilioni 27.9 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe 31 ikiwepo Hospitali ya Halmashauri ya Meru ambayo imetengewa shilingi milioni 900. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza: -
Je, ni lini mradi wa ujenzi wa soko la kisasa Tengeru utatekelezwa ili kuongezea mapato na kuboresha huduma kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Meru imetenga eneo la Madiira lenye ukubwa wa ekari
15.5 kwa ajili ya ujenzi wa soko litakalokuwa na miundombinu muhimu ya soko ikiwemo huduma za wafanyabiashara wadogo wadogo.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri inaandaa michoro ya soko la Madiira na itakapokamilika itawasilisha Ofisi ya Rais – TAMISEMI kama mradi wa kimkakati kwa hatua zaidi.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakuja na mpango wa ujenzi wa vizimba vya ufugaji wa samaki katika Ziwa Duluti?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvivu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Duluti ni sehemu ya Hifadhi ya Msitu wa Asili wa Ziwa Duluti ambao unasimamiwa na Wakala ya Huduma za Misitu (TFS). Hifadhi hiyo ni kivutio cha utalii wa ikolojia, picha, kutembea msituni, kuangalia ndege na viumbe wengine, boti za kupiga kasia na uvuvi wa burudani. Kutokana na hadhi ya eneo tajwa, shughuli za kiuchumi zinadhibitiwa ili kutokuharibu ikolojia na bioanuwai iliyopo katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumuahidi Mheshimiwa John Danielson Pallangyo Mbunge, kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara yangu itafanya utafiti kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi TAFIRI kwa kushirikiana na TFS ili kuona kama ufugaji wa Samaki wa vizimba unaweza kufanyika bila kuathiri ikolojia na bioanuai katika Ziwa Duluti.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, lini ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Tengeru utaendelea ikiwa ni mwendelezo wa barabara ya Sakina – Holili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga kuendeleza ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Tengeru kwa kutumia fedha za mkopo nafuu kutoka Shirika la Maendeleao la Japan (JICA). Ujenzi utahusisha sehemu ya barabara ya Tengeru – Usa River yenye urefu wa kilometa 9.3, sehemu ya Moshi Mjini yenye urefu wa kilometa 8.4 na ujenzi wa daraja jipya la Kikafu lenye urefu wa mita 360. Kwa sasa mchakato wa manunuzi ya kumpata Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kufanya kazi ya usanifu wa kina wa barabara na daraja upo katika hatua za mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika kwa usanifu, kazi ya ujenzi itaanza. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, ni lini ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Mbuguni kuanzia Tengeru Sokoni, Arumeru hadi Mererani utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza maandalizi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa Barabara ya Tengeru Sokoni – Arumeru hadi Mererani yenye urefu wa kilometa 28 ambapo TANROADS wanaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina itakamilika Agosti, 2023. Baada ya usanifu kukamilika Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE K.n.y MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa kiasi cha fedha ilizoahidi kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Malula Kibaoni hadi Ngerenanyuki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Malula - King’ori – Leguluki - Ngarenanyuki yenye urefu wa kilomita 33.7 kwa kiwango cha changarawe. Ujenzi wa Barabara hiyo umefikia asilimia 70 ambapo kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni uchongaji wa barabara kilomita 33.7, karavati 16 na uwekaji wa tabaka la changarawe kilomita Tisa umekamilika na ujenzi unaendelea. Ujenzi huu unatarajiwa kukamilika Tarehe 28 Juni, 2022.
MHE. DOROTHY G. KILAVE K.n.y MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatoa kiasi cha fedha ilizoahidi kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Malula Kibaoni hadi Ngerenanyuki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Malula - King’ori – Leguluki - Ngarenanyuki yenye urefu wa kilomita 33.7 kwa kiwango cha changarawe. Ujenzi wa Barabara hiyo umefikia asilimia 70 ambapo kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni uchongaji wa barabara kilomita 33.7, karavati 16 na uwekaji wa tabaka la changarawe kilomita Tisa umekamilika na ujenzi unaendelea. Ujenzi huu unatarajiwa kukamilika Tarehe 28 Juni, 2022.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza: -
Je, upi mkakati wa kuwapa Wananchi ardhi mbadala wanapoondolewa kwenye maeneo yao kupisha uhifadhi na miradi ya mkakati?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri, kunakuwepo na ulazima wa wananchi kuachia ardhi pale ardhi inapohitajika kwa matumizi ya umma. Mahitaji hayo ni pamoja na ardhi ya uhifadhi na ardhi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati.
Mheshimiwa Spika, mfumo wa sheria nchini, umeweka wazi juu ya takwa na haki ya wamiliki wa ardhi kulipwa fidia ya ardhi na maendelezo pale ardhi inapotwaliwa kwa matumizi ya umma. Aidha, sheria inaruhusu fidia hiyo kulipwa kwa fedha taslimu au kupatiwa ardhi mbadala. Pamoja na sheria kuruhusu wananchi kupewa ardhi mbadala pindi ardhi yao inapotwaliwa, wananchi wamekuwa wakipendelea fidia ya fedha badala ya ardhi mbadala ili kuwawezesha kutafuta maeneo mengine wanayoyahitaji. Ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU K.n.y. MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Skimu za Umwagiliaji katika Tarafa za King’ori na Mbuguni pamoja na eneo la Kusini mwa Tarafa ya Poli – Arumeru Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Tarafa za King’ori, Mbuguni na Poli zina skimu 13 za umwagiliaji zenye ukubwa wa hekta 18,032 na zinanufaisha wakulima 13,546. Skimu hizo ni Kisimiri Juu, Kisimiri Chini, Ukombozi, Olkung’wado, Ngabobo, Mwakeny, Kyamakata, Momela, Nasula, Mapama, Domikwa, Kammama na Valeska. Aidha, mazao makuu yanayolimwa katika skimu hii ni nyanya, mahindi, maharage na mbogamboga.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika Skimu za Kisimiri Juu na Kisimiri Chini zenye ukubwa wa hekta 802. Vilevile, skimu za Kyamakata, Ukombozi, Ngabobo, Mapama, Momela, Mwakeny, Olkung’wado, Kimosonu, Eyani, Maktemu na Oldonyo Wass zipo kwenye mpango wa kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kujua gharama halisi za ujenzi. Baada ya usanifu kukamilika, skimu hizi zitaingizwa kwenye mpango wa ujenzi.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, lini Serikali itatenga fedha kumalizia usambazaji wa maji safi na salama Kata ya King’ori, Wilayani Meru hususani katika Vijiji vya Meru kwa Philipo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Maleu, eneo la kwa Philipo, Kata ya King’ori, Wilayani Meru kinapata huduma ya maji safi na salama kupitia Skimu ya Maji ya Makilenga ambayo kwa sasa haitoshelezi mahitaji kutokana na kuhudumia vijiji 22 vyenye mahitaji ya jumla ya lita 4,931,000 za maji kwa siku wakati uzalishaji ukiwa lita 2,465,500 kwa siku. Katika kuboresha huduma ya maji katika kijiji hicho, Serikali katika mwaka wa fedha 2024/2025 itashirikiana na Shirika la Korea International Cooperation Agency (KOICA) kutekeleza mradi wa usambazaji maji safi na salama katika vijiji sita kikiwemo Kijiji cha Maleu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zitakazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa vyanzo vya maji na uboreshaji wa mitambo ya maji. Muda wa utekelezaji wa mradi huo ni miezi 18 ambapo kukamilika kwake kutanufaisha wananchi wapatao 16,584 waishio katika vijiji sita vya Maleu, Oldonyongiro, Shambarai Burka, Msitu wa Mbogo, Sakina Chini na Sakina Juu.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuelekeza Benki za CRDB, NBC na NMB kufungua Matawi eneo la Kikatiti linalokua kwa kasi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, katika mchakato wa kufungua tawi jipya la benki, benki husika hufanya upembuzi yakinifu kwa lengo la kujiridhisha kama kuna fursa za kibiashara kukidhi gharama za uendeshaji na kutengeneza faida. Upembuzi huo, pamoja na mambo mengine, huiwezesha benki husika kufanya maamuzi ya kufungua tawi katika eneo husika. Aidha, jukumu la Serikali ni kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwemo huduma ya ulinzi na usalama, miundombinu ya barabara, nishati, maji na TEHAMA.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ukweli kwamba CRDB, NBC na NMB hazina matawi Kikatiti, wananchi wa eneo hilo wanaendelea kupata huduma za kibenki kupitia kwa mawakala. Ahsante.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA K.n.y. MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, nini kauli ya Serikali kuhusu kutokuwepo uwiano katika bei ya kuunganisha umeme nchini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kutokuwepo kwa uwiano katika bei ya kuunganisha umeme nchini hasa katika maeneo ya mijini kunatokana na umbali alipo mteja kutoka sehemu unapochukuliwa umeme na aina ya njia ya umeme iliyoombwa na mteja (Single Phase/Three Phase), gharama hizi anazotozwa mteja ni zile zilizoidhinishwa na EWURA kupitia Tangazo la Serikali Na. 1020 la Mwaka 2020. Aidha, kwa upande wa vijijini, wateja wanaunganishiwa umeme kwa gharama ya shillingi 27,000 tu, ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuelekeza Benki za CRDB, NBC na NMB kufungua Matawi eneo la Kikatiti linalokua kwa kasi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, katika mchakato wa kufungua tawi jipya la benki, benki husika hufanya upembuzi yakinifu kwa lengo la kujiridhisha kama kuna fursa za kibiashara kukidhi gharama za uendeshaji na kutengeneza faida. Upembuzi huo, pamoja na mambo mengine, huiwezesha benki husika kufanya maamuzi ya kufungua tawi katika eneo husika. Aidha, jukumu la Serikali ni kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwemo huduma ya ulinzi na usalama, miundombinu ya barabara, nishati, maji na TEHAMA.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ukweli kwamba CRDB, NBC na NMB hazina matawi Kikatiti, wananchi wa eneo hilo wanaendelea kupata huduma za kibenki kupitia kwa mawakala. Ahsante.