Supplementary Questions from Hon. Benaya Liuka Kapinga (46 total)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kufanya marekebisho, Naibu Waziri amesema Mbunge wa Mbinga Mjini mimi ni Mbunge wa Mbinga Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri yanayotia moyo. Pia nashukuru katika bajeti inayokuja ametutengea kilometa 5. Hofu yangu ni kwamba ikiwa mpango utakuwa ni wa kilometa tano tano barabara hii tunaweza kuikamilisha kwa muda wa miaka kumi na sita na kidogo. Je, Serikali ipo tayari kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara hii ambayo imesubiriwa kwa muda mrefu na wananchi wa Jimbo la Mbinga Vijijini, Jimbo la Nyasa na wananchi wa Mkoa wa jirani wa Njombe?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa hali ya barabara zinazohudumiwa na TANROADS kwa jimbo la Mbinga Vijijini sasa hivi hazipitiki ama zinapitika kwa shida sana. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzifanya barabara hizi zipitike msimu mzima?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimuombe radhi sana Mheshimiwa Mbunge kwamba huyu ni Mbunge wa Mbinga Vijijini na si Mbinga Mjini. Kwa hiyo, hata wananchi huko wanajua kwamba Mheshimiwa wao wa Mbinga Vijijini yupo anatetea barabara zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, sasa nijibu maswali yake mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Mbunge anafahamu mara baada ya kuteuliwa hii barabara ni kati ya barabara ambazo mimi nimebahatika kwenda kuzitembelea, kwa hiyo, ninaifahamu vizuri sana. Hata hivyo, tukubali tu kwamba ni jitihada za Serikali kwamba fedha inapopatikana hata kama ni kiasi kidogo zile barabara ziendelee kutengenezwa. Hata hizi kilometa 5 zilizotengenezwa zimesaidia sana kurahisisha usafirishaji wa makaa ya mawe, kwa hiyo, magari makubwa yanayopita pale hayawezi kukwama.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini tutatenga fedha zote, Serikali inafanya jitihada fedha zitakazopatikana naamini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha barabara hii. Kwa sasa kadri tunavyopata fedha tutaendelea kutengeneza barabara kwa awamu na ndiyo maana hata hizi kilometa tano zilizotengenezwa zimetoa msaada mkubwa sana. Ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali japo siridhiki nayo kwa sababu maeneo ya kujenga Hospitali ya Wilaya katika Jimbo la Mbinga Vijijini yapo mengi katika maeneo tofauti tofauti, ni uamuzi tu wapi tujenge hospitali hiyo. Je, Serikali inawahakikishia nini wananchi wa Mbinga Vijijini katika bajeti ijayo ikiwa bajeti mbili tofauti zimepangwa na hizi fedha hazikupelekwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wananchi wa Mbinga Vijijini kwa kuunga mkono juhudi za Serikali wamejenga na kukamilisha zahanati sita; zingine zina miaka miwili toka zikamilike. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka wahudumu katika zahanati hizi ili zifunguliwe zianze kuwahudumia wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kujibu kwenye swali la msingi, kigezo muhimu cha kupeleka fedha katika Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri ambacho Serikali iliweka ilikuwa ni Halmashauri husika kuainisha eneo na kuwasilisha taarifa ya uwepo wa eneo husika ndipo fedha ziweze kupelekwa kwenye Halmashauri hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mbinga Vijijini imekuwa na mivutano ya muda mrefu kuhusiana na wapi Makao Makuu ya Halmashauri iwepo. Januari hii wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu alipopita ndipo ilipata majibu ya kuwa na Makao Makuu ya Halmashauri yawepo. Kwa sababu hizo, hawakuwa na eneo rasmi ambalo liliwasilishwa Serikalini na ndiyo maana fedha haikupelekwa. Hata hivyo, kwa sasa, kama nilivyosema kwa sababu wamekwishawasilisha eneo ambalo limetengwa, katika shilingi bilioni 27 ambazo zimetengwa na Serikali, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba watapata fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mbinga Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na zahanati sita ambazo zimekamilika na hazijaanza kutoa huduma kwa sababu ya upungufu wa watumishi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Kapinga kwamba Serikali inathamini sana kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa Mbinga Vijijini. Kwa sababu zahanati hizi zimekamilika tutakwenda kuona utaratibu mzuri kwanza kwa kutumia watumishi waliopo ndani ya halmashauri kufanya internal redistribution ya watumishi hao angalau kuanza huduma za afya. Katika kibali cha ajira kinachokuja Halmashauri ya Mbinga Vijijini tutawapa kipaumbele ili watumishi hao waweze kwenda kutoa huduma katika zahanati hizo.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nishukuru kwa Serikali kuzitamka barabara hizi lakini kwa namna majibu yalivyosemwa yanatofautiana kabisa na uhalisia ahadi hizi zilitolewa na Mheshimiwa Rais Samia Hassan Suluhu mwaka jana. Ujenzi wa kilomita nne unazosema ulijengwa miaka ya nyuma sana, nikiri mwaka jana kulikuwa na ukarabati wa eneo korofi kama mita chache sana siyo ujenzi. Sasa swali langu la msingi lilikuwa lini tutaanza kutekeleza lini Serikali itaanza kutekeleza ahadi hizi zilizotolewa na Mheshimiwa Rais wetu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili Serikali ilitoa ahadi hapa kwamba tutaanza kujenga barabara ya Kitai hadi Kigonsera kilomita tano juzi nimepita pale hakuna kilichofanyika wananchi wananiuliza. Je, Serikali mnawaambia nini wananchi wa Jimbo hili la Mbinga Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wakati huo akiwa Makamu haingekuwa imeanza kutekelezwa lazima itaanza kutekelezwa katika awamu hii ya bajeti tunayoiendea.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge uvute subira lakini kama tulivyosema ahadi hizi zote ambazo zimeahidiwa ni ahadi ambazo zinatakiwa zitekelezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu barabara ya Kitai, Litui barabara hii ni kati ya barabara za kimkakati ambayo inaenda inapita kwenye makaa ya mawe ya Ngaka na atakubaliana nami Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kilometa tano zimeshajengwa na naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba muda si mrefu kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha barabara hiyo tena inaendelea kujengwa itatangazwa mapema sana kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha na kwa kuhakikishia Mheshimiwa Mbunge unaweza ukawasiliana na TANROAD watakuambia taratibu wako kwenye hatua za mwisho kabisa ili mkandarasi aanze kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lako kwamba barabara zilijengwa muda wa nyuma ndiyo mpango wenyewe kwamba tayari tulishaanza kujenga na kwa hivyo tayari hizo kilomita tano tunazitambua tulizijenga na bado tutaendelea na hasa baada tena ya Mheshimiwa Rais kuongezea ahadi yake.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Mbinga wafahamu kwamba barabara zao zitajengwa kwa kiwango cha lami kama Serikali ilivyoahidi na kama ilivyo kwenye mpango ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina swali moja dogo la nyongeza. Mradi wa Maji wa Litembo una uchakavu mkubwa wa miundombinu hali iliyopelekea Kijiji cha Langandondo kukosa maji kwa miaka minne mvululizo, lini mradi huu unaenda kukarabitiwa na wananchi wale wa Langandondo waweze kupata maji Kata ya Litembo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Liuka Benaya, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uchakavu wa Mradi wa Litembo kama Wizara tunautambua na tayari tumetoa maagizo kwa Meneja wa RUWASA tayari na yeye anaendelea kujipanga ili kuhakikisha kwamba mwaka ujao wa fedha nao tuweze kutupia jicho la utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumpongeza Mheshimiwa Liuka amekuwa ni mfuatiliaji mzuri, tumeondoka hapa wakati wa weekend tumekwenda Mbinga Vijijini tumefanya kazi nzuri na miradi hii yote ya uchakavu pale anafahamu tulishakubaliana utekelezaji wake utafanyika kwa haraka.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nishukuru kwa majibu yanayoridhisha ya Serikali. Ni kweli kituo hiki cha Mapera kuanzia mwezi Julai kimeanza kutoa huduma. Kituo cha Muungano, wananchi hawa kituo hiki wamekijenga wenyewe kwa asilimia 100 kwa kusaidiwa na mapato ya ndani kidogo sana, hiyo shilingi milioni 60, lakini sasa wanahangaika kujenga jengo la wazazi. Je, Serikali ina mpango gani kuunga jitihada hizi mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kata ya Kipololo imejenga Zahanati ya Kipololo, Kata ya Mbuji imejenga Zahanati ya Mnyao, Kata ya Litembo imejenga Zahanati Lituru lakini pia Kata ya Mkako Kiukuru wamejenga zahanati. Zahanati hizi zimekamilika, zingine sasa zina miaka mitatu, miwili mpaka leo hazijaanza kazi. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka watumishi katika zahanati hizi ili ziweze kuanza kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Benaya Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameomba tu Kituo cha Afya Muungano ambacho kimejengwa na wananchi kwa asilimia 100 na sasa hivi kuna jitihada za kujenga jengo la wazazi, anataka commitment ya Serikali. Niseme tumelipokea na tutaliweka katika mipango inayofuata ili kuhakikisha tunaingiza katika bajeti zetu hiki Kituo cha Afya cha Muungano ili kiweze kukamilika.
Mheshimiwa Spika, la pili kuhusu kata alizozitaja katika vijiji alivyoviainisha kama Kata ya Kipololo, Mbuji, Litembo na Likako ambazo zimejenga zahanati na mpaka sasa hivi bado hazijafunguliwa. Niseme tunalipokea na naamini watendaji wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambao wanasimamia Idara ya Afya wamelisikia hili, hivyo sasa tutajua namna ya kupanga watumishi waliopo na vile vile kama Serikali itaajiri hapo mbele kidogo tutapeleka watumishi ili vituo hivi vianze kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Utekelezaji wa REA III, round ya pili Jimbo la Mbinga unakwenda kwa kusuasua sana. Mpaka nakuja hapa Mkandarasi alikuwa bado hajafanya chochote.
Nini kauli ya Serikali juu ya Mkandarasi huyu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kapinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wakandarasi wa REA wanazo hatua kadhaa za utekelezaji wa miradi. Wanafanya survey, wanafanya uhakiki, wananunua vifaa na baadaye wanaanza kujenga. Hizi hatua tatu za mwanzo mara nyingi hawaonekani site, wanapoanza kujenga ndiyo wanaonekana. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mkandarasi atakuwa kwenye mojawapo ya hatua hizo na kabla ya mwezi Machi ataonekana site kwa ajili ya kuendelea na kazi ambayo tayari amepewa kwa sababu deadline yake ni mwezi wa Desemba, 2022 na tunaamini ataikamilisha.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali yenye nia ya dhati kabisa kuondoa adha kubwa ambayo wananchi wa wilaya hizi mbili, mikoa hii miwili ya Ruvuma na Njombe, kwa sababu mto huu una mamba wengi lakini ni mto mkubwa sana. Kwa hiyo, ni hatari kubwa sana kwa wananchi pale, kwa hiyo kwa majibu nashukuru sana. Ombi tu kwamba waharakishe ili daraja hili liweze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ombi hili, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Barabara ya Unyoni kuelekea Maguhu inapitika kwa shida sana lakini ipo barabara kutoka hapo Maguhu Mapera kuelekea Kambarage, barabara hii iko hatarini kutoweka. Kuna korongo kubwa sana kutokana na mvua hizi zinazoendelea kunyesha.
Sasa je, Serikali ipo tayari kutoa fedha za dharura ili kuokoa ile barabara iweze kutumika kama inavyotumika siku zote? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu dogo la pili, jiografia ya Wilaya ya Mbinga hususan Jimbo la Mbinga Vijijini ni milima na mabonde hali ya kwamba inahitaji madaraja mengi lakini na barabara zinapitika kwa shida sana. Nahitaji commitment ya Serikali, je, iko tayari kuongeza fedha tofauti na ile hali ya kawaida katika Jimbo la Mbinga Vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Liuka Kapinga Benaya, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, bahati nzuri nilifika jimboni kwake, niliona kazi nzuri anayoifanya na jinsi wananchi wanavyomkubali kwa kuwa anafuatilia kwa ukaribu zaidi matatizo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba swali la kwanza alilouliza ni kwamba je, tupo tayari kutoa fedha za dharula ili kusaidi hili korongo kubwa linapita katika hizi barabara ambazo ameziainisha. Niseme tu katika Bunge lako Tukufu baada ya agizo la Mheshimiwa Spika tumeshafanya tathmini ya awali ya kugundua maeneo yote ambayo ni korofi nchi nzima. Kwa hiyo, ambacho tutakwenda kuangalia tu katika eneo lako la Mbinga kama maeneo hayo yametengwa. Kama halipo maana yake tutamuagiza meneja wa TARURA katika halmashauri yako afanye tathmini ili tuone namna ambavyo tunaweza tukasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuhusu kuongeza fedha, tumewaagiza Mameneja wote wa TARURA Mikoa pamoja na katika Halmashauri. Katika mwaka huu wa fedha, watakavyoleta zile bajeti zao walete bajeti kulingana na uhalisia wa maeneo husika kwa hiyo, hilo ndiyo agizo. Kwa hiyo, naamini kwamba maeneo haya ambayo
Mheshimiwa Mbunge ameyaainisha yatakuwepo katika bajeti hizo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Mradi wa maji wa Litembo, Mahenge kutokea Mwogelo, mwaka jana niliuliza swali hapa na nikapewa majibu mazuri na Mheshimiwa kwamba tayari fedha imetengwa na mradi unaanza kujengwa. Kwa bahati mbaya mradi huu unatoa maji Litembo tu.
Je, ni lini maji yatatoka Mahenge na Langandondo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ni kweli anachokiongea Mheshimiwa Mbunge lakini Mheshimiwa Mbunge unafahamu kwa namna ambavyo tumekuwa tukiwasiliana tumeweza kufanya kazi sasa Litembo inapata maji. Kwa hiyo, maeneo haya ya Mahenge tayari tunapeleka Mkandarasi ambaye ataanza kazi hivi karibuni na kuona kwamba maeneo yote haya mawili yaliyobaki nayo yanakwenda kunufaika na maji bombani.
Mheshimiwa Spika, ninaomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kwa pamoja kama ambavyo umekuwa ukifanya. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Ni lini Serikali itaimarisha, kuboresha na kudhibiti korongo kwenye Mlima wa Mawono, barabara ya Unyoni kuelekea Maguu wakati tunasubiri utekelezaji wa ujenzi wa lami kama Serikali ilivyoahidi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Benaya Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, korongo alilolisema naomba nitumie nafasi hii kumuagiza Meneja wa Mkoa wa Ruvuma aende akalitathmini na aone kazi ilivyo ili tuweze kupata gharama na tuweze kulikarabati ili isije ikaleta madhara ya kukata mawasiliano ili tuweze kulikarabati kabla ya kuanza kujenga hiyo barabara ama kuifanyia usanifu kwa maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. BENEYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Wilaya ya Mbinga hatuna Chuo cha VETA na tulipata ahadi ya Serikali kwamba awamu hii tutaingia kwenye mpango wa kujengewa Chuo cha VETA, tayari tuna eneo. Ni lini sasa chou hiki kinaenda kuanza kujengwa?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kapinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema Wilaya zote ambazo hazina Vyuo vya VETA tunaanza kujenga VETA mwaka huu tumekubaliana kwenye hizo bilioni 100 ambazo tumezipata kutoka Hazina tutaanza ujenzi mwaka huu na mwakani tutapata bilioni 100 nyingine na kumalizia ujenzi. Kwa hiyo, tutafanya hivyo pamoja na Wilaya ya Mbinga na ujenzi utaanza siku za karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu kwa Wabunge wote ni kwamba kuhakikisha tunapata maeneo mapema, tunapata hati miliki ili tuweze kujenga kwa sababu hatuwezi kwenda kujenga chou mahali ambapo hatumiliki ardhi chini ya utaratibu wa VETA. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa majibu hayo lakini nimkumbushe tu Mheshimiwa Waziri kwamba vituo hivi vya kimkakati tulikubaliana, pamoja na kujengwa Makao Makuu ya Kata, lakini pia vijengwe kwenye kata zile za mbali. Kwa hiyo, Kata ya Ukata iko mbali sana na hiki kituo cha Mkumbi. Kwa hiyo, nini maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali ilipeleka fedha milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mapela na mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya vifaa tiba Shilingi milioni 320, lakini mpaka leo hii vifaa tiba katika kituo hiki cha afya havijafika. Sasa nataka kujua fedha hizi ziko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kituo hiki cha Mkundi, Matiri, pamoja na Muungano, sasa hivi vimeshakamilika. Ni lini sasa tutapeleka watumishi pale ili vianze kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ilitoa mwongozo wa kujenga vituo vya afya kwenye maeneo ya kimkakati, vigezo vikiwa kwanza idadi ya wananchi katika eneo husika, lakini pili, umbali wa kituo kile kutoka kituo cha karibu zaidi au hospitali ya karibu zaidi. Kwa hiyo, ukitoa kata yoyote ambayo inakidhi vigezo hivyo ina sifa ya kuwa kata ya kimkakati kwa ajili ya kituo cha afya. Kwa taarifa tulizonazo bado idadi ya watu sio kubwa sana, kwa hivyo inakosa ile sifa kuwa kituo cha afya cha kimkakati kwa maana ya idadi ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi milioni 400 zilipelekwa katika kituo cha afya alichokitaja Mheshimiwa Mbunge na milioni 320 za vifaa tiba tayari zimepelekwa Bohari Kuu ya Madawa (MSD) kwa ajili ya kuleta vifaa hivyo. Tunaendelea kushikirikiana na Wizara ya Afya, kuhakikisha vifaa hivyo vinaletwa mapema iwezekanavyo ili huduma za afya zianze kutolewa katika kituo kile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na hivi vituo vitatu vilivyokamilika, kwanza tumshukuru Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi kukamilisha vituo vya afya vitatu na nimhakikishie Mbunge kwamba mpango wa ajira kwa watumishi kwa awamu ni kuhakikisha kwamba tunaleta watumishi kwenye vituo hivyo pia ili huduma zianze kutolewa.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri, nina swali moja la nyongeza lenye sehemeu (A) na (B).
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa lane iliyopo sasa ni hiyo ambayo inayotumika Songea, inatumika Mbinga pia inatumika Nyasa. Kwa kuwa kuna ongezeko kubwa sana la utumiaji wa umeme kutokana na uchimbaji mkubwa wa makaa ya mawe pale Mbinga, viwanda vikubwa vya kubangua kahawa, viwanda vya kusaga sembe na viwanda vya maji ni vingi hali inayopelekea umeme kuwa wa low voltage au kukatikakatika.
Je, Serikali iko tayari kurudisha mpango wake nyuma badala ya mwaka 2024/2025 uwe 2023/2024 ili kuwafanya wananchi nao wapate nafasi ya kutumia umeme ambao sasa haukatikikatiki.
Mheshimiwa Spika, ikiwa hili haliwezekani, je, Serikali itaisaidiaje Mbinga kuondokana na hali hii ya kukatika katika kwa umeme?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Benaya Kapinga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nikweli kwamba Mkoa wa Ruvuma umekuwa na changamoto ya maeneo kuwa na matatizo ya low voltage, na kwa sasa kwenye bajeti ya mwaka huu, kama tulivyosema tumeiweka Mbinga, kuna line ya kujengwa inayotoka Songea kwenda Tunduru ambayo ina kilometa kama 211. Serikali ilifanya uhakiki wa matatizo na ikagundua kwamba hapo kuna changamoto kubwa zaidi, na wako wale wenye changamoto kidogo na ambao hawana changamoto zaidi. Kwa hiyo eneo la Mbinga limewekwa kwenye wale wasiokuwa na changamoto sana kama hao wengine.
Mheshimiwa Spika, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuifanyia marekebisho na matengenezo ya mara kwa mara hii line ya kutoka Songea kwenda Mbinga na tuone uwezekano wa kuivuta mapema kabla ya ule muda uliopangwa kulingana na bajeti itakavyokuwa imewekwa.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Njiapanda - Rugali – Ndembe – Longa Km. 10, kwa mbele kuna lami lakini kipande hiki hakina lami. Je, ni lini Serikali itaunganisha kipande hiki kutoka Mbinga Mjini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Benaya Kapinga, Mbunge wa Mbinga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoisema ni kweli ilijengwa mbele kwa sababu ya changamoto ya huko ilikojengwa ili kuhakikisha kwamba inapitika. Sasa hivi nimuhahakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatafuta fedha ili kukamilisha hiko kipande kilichobaki kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongezaa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe masikitiko yangu, Kata ya Ukata haina mnara wa Vodacom. Watu wa Vodacom walikuja wakajenga mnara kata ya Ukata ukakamilika lakini baadae wakauporomosha waliko upeleka hatujui. Pia hiyo minara ya Halotel ya Kata ya Kipololo Kijiji cha Lunoro na kijiji cha Litoho kweli imejengwa lakini haijawashwa tangu mwaka 2017 hadi leo sasa niombe Serikali itueleze itatupa lini mawasiliano katika hivi vijiji nilivyo vitaja?
Mheshimiwa Spika, la pili, Kata hii ya Kihangimahuka iko kilometa 25 kutoka Mbinga Mjini lakini hadi leo haina mawasiliano. Niombe ule mchakato uharakishwe ili wananchi hawa nao wapate mawasiliano, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, minara hii ilijengwa na inapojengwa baada ya hapo tunafanya technical auditing na baada ya kukamilisha technical auditing maana yake kwamba wanawasha; lakini kuna scenario mbili ambazo huwa zinatokea, ya kwanza wanaweza wakawasha baadaye kukawa na changamoto ya vifaa ambavyo wametumia. Shoti hizo huwa zinatokea lakini baada ya hapo huwa tunatoa maelekezo ya namna ambavyo wanatakiwa kwenda kurekebisha.
Mheshimiwa Spika, changamoto ilikuwepo hapa katikati ni changamoto ya uzalishaji wa vifaa, ambayo tumekuwa nayo kutokana na janga ambalo lilikuwa limetoka katikati. Nchi zote Afrika inawezekana kabisa supplier anakuwa ni yule yule kiasi kwamba tunajikuta tunakuwa kwenye queue ya kusubiri vifaa hivyo viweze kuzalishwa na ili waweze kununua na kulete kwa ajili ya kurekebisha katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, lakini vile vile suala la Kata ya Hukata, ni kweli kabisa nakiri, Kata ya Hukata ambayo nafahamu kabisa ndipo ambapo Mheshimiwa Mbunge anatoka. Nalijua tatizo hili kwa upana huo lakini kilichofanyika ni kwamba baada ya kujenga mnara katika kata ile na scope ya eneo ambalo ilitakiwa kupata mawasiliano haikuwezekana ikabidi tuhamishe mnara uende sehemu nyingine ili kuweza kufikisha mawasiliano katika eneo la Hukata.
Mheshimiwa Spika, changamoto iliyokuwepo; changamoto iliyopo ni kwamba mawasiliano yaliyopo pale kwa sasa bado ni hafifu, kwa hiyo sasa tunaandaa timu yetu iende ikajiridhishe na kuona namna gani sasa tutaenda kulitatua kwa ukubwa wake, ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi.
Ni lini Serikali itatekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu ya kupeleka maji Kijiji cha Mtunduwalo iliyothibitishwa kwamba maji yale sasa hayawezi kutumika kwa matumizi ya binadamu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, maelekezo ya viongozi wakuu yote tunayatekeleza na suala hili la kupeleka maji Ruanda nalo pia lipo kwenye utaratibu wa kuona kwamba hivi punde tunakuja kuhakikisha maji Ruanda yanaletwa.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Arumeru kwanza kabisa tutoe shukrani kwa majibu mazuri ya Serikali, vilevile kwa niaba ya Mheshimiwa Pallangyo anatoa shukrani nyingi sana kwamba aliomba Shilingi Bilioni 2.7 fedha hizo zimefika na tayari zimeanza kufanya kazi, lakini nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, mradi wa maji Kijiji cha Litoho, Kata ya Ukata, unaotokea Liwanga unatoa maji muda wote sijui nisema machafu lakini yasiyokuwa pure yana udongo kwa hiyo yanahitaji ujenzi wa chujio. Je, ni lini Serikali itajenga chujio katika mradi huo.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali kwanza nipende kupokea shukrani kutoka kwa Mbunge wa Arumeru, kwa kweli kupeleka fedha ni wajibu wetu na kipekee tumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu anaendelea kutoa fedha kwenye miradi hii mikubwa ili wananchi waweze kuondokana na matatizo ya maji na kubeba ndoo kichwani.
Mheshimiwa Spika, kwenye ujenzi wa chujio naomba nitoe ahadi kwamba ni moja ya majukumu yetu kama Wizara nimelipokea tutalifanyia kazi. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Je, ni lini Serikali itatoa fedha za dharura tayari tulishaandika andiko kwa ajili ya barabara ya Kambarage – Mapera – Litoho - Mgumbo pamoja na Mkongotingisa kwenda Muungano, kwa sababu mvua bado zinanyesha na barabara hizi zinataka kutoweka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ambayo ameainisha Mheshimiwa Mbunge ambayo ipo katika mpango wa Serikali ninaamini kabisa kwamba tuko katika hatua za mwisho za kutafuta fedha ili kuhakikisha hiyo barabara inafanyiwa kazi. Kwa hiyo, nimwondoe hofu mara tutakapopata hiyo fedha maana yake tutaanza ujenzi. Ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mbinga Vijijini, Jimbo la Mbinga Vijijini kutokana na ukubwa wake tulipata ahadi ya Serikali ya kuligawa. Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Benaya Kapinga Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ninawaomba Jimbo la Mbinga kwa maana ya Halmashauri ya Mbinga wapitie hatua zile kwa mujibu wa sheria, wawasilishe hayo maombi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutafanya tathmini lakini tutawapa mrejesho baada ya kufanya tathmini na hatimaye tutawasilisha kwa mamlaka husika, ahsante. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana na nishukuru kwa majibu ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kituo hiki cha Mapela, ndio kituo pekee cha Serikali katika Halmashauri ya Mbinga Vijiji ambayo ina kata 29. Hicho kituo cha Maguo alichokitaja Mheshimiwa Naibu Waziri ni kituo cha Mission, tu nashukuru wanatusaidia, sina hakika kama gharama zake zinalingana, sina hakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti nina maswali maswali mawili ya nyongeza.
Je, ni lini Serikali itapeleka wahuduma wa afya, katika zahanati saba Kipolopolo, Lukiti, Kihuruku, matuta, Mwihayo, Ikwela na Lituru; zahanati hizi nimeuliza mwaka jana swali hapa. Lini zitafunguliwa maana wananchi wamejenga na wamekamilisha, lini sasa zitafunguliwa ili ziweze kutoa huduma kwa wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Halmasauri ya Mbinga, ina upungufu mkubwa wa watumishi, zaidi ya asilimia 80 hatuna watumishi. Je, katika mgao huu unaokuja, Serikali ipo tayari kuwaonea huruma na kutoa kipaombele katika halmashauri ya Wilaya ya Mbinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Halmashauri ya Mbinga Vijijini ina kata 29 na ina kituo kimoja cha afya; lakini nimuhakikishie Mheshimiwa Rais wetu mama Samia Hassan ameweka mkakati wa uhakika wa kujenga vituo vya afya vya kimkakati katika kata za mkakati na tarafa za kimkakati. Tulishakuomba na ulishaleta hapa orodha ya kata ambazo zitajengewa vituo vya afya. Nikuhakikishie Serikali hii sikivu tutahakikisha tunajenga vituo vya afya katika Jimbo la Mbinga Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, kuhusiana na watumishi kuhitajika katika zahanai saba; kwanza niwapongeze sana wananchi wa Mbinga Vijijini kwa kutoa nguvu kujenga zahati saba ambazo zimekamilika, lakini na Serikali ilichangia. Nimhakikishie kwamba tunakwenda kuzisajili zahanati hizi. Kwa upande wa ajira hizi ambazo zimetangazwa tutakwenda kutoa kipaumbele kikubwa kwenye halmashauri zote zenye upungufu mkubwa wa watumishi ikiwepo Halmashauri ya Mbinga Vijijini. Ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona, Barabara ya Nyoni – Mlima mkali wa Mawono – Mapela – Maguu kilomita 25 ipo kwenye Ilani ni lini sasa barabara hii itaanza ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kapinga Mbunge wa Mbinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ipo kwenye miinuko na tunachofanya kwa sasa nikuhakikisha kwamba inapitika kwa muda wote wakati tukifanya hivyo Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuweza kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. BENAYA L KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri ambayo yanatia moyo wananchi hawa wa Wilaya ya Mbinga kwa maana ya barabara hii ya Litembo ambayo imesubiriwa kwa muda mrefu na inaahadi za Marais Watatu kujengwa kwa kiwango cha lami, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Matiri kwa maana ya Kigonsera hadi Matiri ambako kuna kilimo kikubwa cha maharage na mahindi inapitika kwa shida sana, sasa wakati tunasubiri mchakato huo kuendelea, Serikali inampango gani wa kuifanya hii barabara iweze kupitika kwa msimu mzima?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya kutoka Liyombo kuja hadi Rwanda kupitia Mdunduwalo ambayo Makaa ya Mawe yanapita hivi sasa ama haipitiki baadhi ya siku, ama inapitika kwa shida sana, tumeleta maombi maalum ni lini sasa Serikali itaitengeneza barabara hii kupitisha makaa ya mawe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Matiri - Kigonsera kama alivyoisema kweli ni barabara ya changarawe ambapo sasa hivi ni kipindi kikubwa ambacho mvua kubwa sana inanyeesha naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeshatoa taarifa kwa mameneja wote wa TANROADS Tanzania kuhakikisha kwamba barabara zote ambazo zinachangamoto waweze kuzisimamia kwa ukaribu na narudia tena kumsisitiza Meneja wa Mkoa wa Ruvuma ahakikishe kwamba barabara ya Matiri – Kigonsera inapitika.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala lake la pili la kutoka Liyombo hadi Rwanda hii ndiyo barabara ambayo inasafirisha sana Makaa ya Mawe na kuna migodi kama minne, ambayo pia Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo tuweze kuitengeneza.
Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii tutahakikisha kwamba inapitika na kama nilivyosema kwamba kwenye barabara zingine Mkandarasi yuko site kwenye hayo maeneo lakini inategemia na hali ya hewa. Kwa hiyo, Mkandarasi yuko site kuhakikisha kwamba patakapotokea nafuu ya hali ya hewa wataendelea kuitengeneza hiyo barabara ili iweze kupitika. Ahsante. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ni lini Serikali itatoa fedha kujenga Daraja la Mto Ruvuma kati ya Lusomba -Magabula kwa Mheshimiwa Jenista Mhagama hadi Iyale ambapo Mheshimiwa Jenista tumehangaikia sana hili daraja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itajenga daraja hili la Lusonga hadi Liyanja kadri ya upatikanaji wa fedha; na tutaangalia kama imetengewa fedha katika mwaka huu wa fedha ambao tumepitishiwa ili tuweze kwenda kuweka kipaumbele katika daraja hili ili wananchi waweze kupata huduma hiyo.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Kata ya Litumbandyosi tulipata skimu katika bajeti hii. Ni lini sasa skimu hii inaenda kuanza ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bonde la Litumbandyosi ni kati ya mabonde 22 ambayo tarehe 20 mwezi wa tatu mwaka huu tulisaini mkataba na wakandarasi kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kazi hii inaendelea. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii inakamilika mwaka wa fedha huu ambao unaishia. Kuanzia Julai kazi itaanza ili kuwafanya wananchi wako waweze kufanya Kilimo cha Umwagiliaji.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini niiombe uhakiki huu unaoshirikisha wananchi uhusishe pia Kijiji cha Chunya - Kata ya Mpapa; Kijiji cha Barabara - Kata ya Matili; lakini pia Kijiji cha Kimbindachini - Kata ya Muungano. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mbinga ni milimani, na kwa hiyo, sasa kutokana na uhifadhi maeneo mengi ya milimani tunapewa…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kapinga naomba uulize swali moja kwa moja. Swali la kwanza na la pili, tafadhali; uliza swali lako la msingi.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio nilikuwa nauliza swali hapo, kwamba basi acha ulivyonielekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kuwafanya wananchi hawa waweze kuishi na misitu katika milima iliyopo Wilaya ya Mbinga? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali inatoa kauli gani katika maeneo yaliyoanzishwa Miradi ya Panda Miti Kibiashara bila kushirikisha wananchi, ili kuwarejeshea maeneo haya wananchi husika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mpango wa kutoa elimu, nitoe tu maelekezo kwa watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii hususan Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, tunapoenda kuainisha hii mipaka wahakikishe kwamba tunashirikisha wananchi walioko katika maeneo hayo ili kuwepo na urahisi wa kutambua mipaka iliyopo na kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutalizingatia, lakini pia tutaendelea kutoa elimu ya namna ya uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la pili ambalo amelisema kwenye Mradi wa Panda Miti Kibiashara; kikawaida mradi huu unawawezesha wananchi kujiinua kiuchumi kupitia mazao ya miti, na mara nyingi tunashirikisha wananchi kabla ya mradi huu kufika katika eneo husika. Kwa hiyo, kama kuna maeneo ambayo tumepeleka mradi huu halafu hatukushirikisha wananchi, basi tumefanya makosa na tutaenda kupitia upya utaratibu uliopo ili wananchi waweze kufaidika na miradi hii ya Panda Miti Kibiashara.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha afya katika Tarafa ya kimkakati ya Mbuji yenye kata tano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, ni kipaumbele cha Serikali kuhakikisha inajenga vituo hivi vya afya katika kata za kimkakati. Na tutaangalia katika mwaka wa fedha unaofuata tuweze kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya hiki.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Tarafa ya Hagati ina shule ya Sekondari ya Hagati ni shule kongwe.
Je ni lini Serikali itatenga fedha na kuikarabati shule hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokuwa nimeshasema kwenye maelezo yangu ya awali. Serikali hii ya Awamu ya Sita ilikuwa imeshatenga fedha ya kukarabati shule kongwe 89 kote nchini na hiyo ilikuwa ni katika awamu ya kwanza na bado Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule zingine kongwe ikiwemo hii Shule ya Hagati iliyopo kule Jimboni kwa Mheshimiwa Kapinga.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Barabara ya Nyoni - Maguu inayopitia Mawono kwenye mlima mkali, ni lini tutaanza ujenzi kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara anayoitaja Mheshimiwa Kapinga ni kweli, na ipo kwenye ilani kwamba ijengwe kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kuijenga, lakini kitu ambacho tunategemea tukifanye kwanza ni kuhakikisha kwamba yale maeneo yote yenye miinuko tunajenga aidha kwa zege ama kwa lami nyepesi ili kupunguza changamoto kwa wasafiri ambao wanasafiri katika hiyo barabara ya Nyoni – Maguu, ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na mgao huu wa Walimu 13,100 Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ziko shule zilionekana zina upungufu sana wa Walimu, lakini katika mgao huo hazikupata Mwalimu hata mmoja, ikiwemo Shule ya Msingi Litoho. Je, ni lini, sasa Serikali itapeleka Walimu kwenye Shule hii ya Msingi Litoho na shule nyingine za Halmashauri ya Mbinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upungufu ambao ameuzungumzia Mheshimiwa Kapinga uliokuwepo kule Wilayani Mbinga, Serikali ndio maana imekasimu mamlaka kwa Makatibu Tawala wa Mikoa kufanya msawazo wa Walimu kuhakikisha shule mbalimbali zinapata Walimu kwa kutoa maeneo yenye Walimu wengi zaidi na kuwapeleka kwenye maeneo yenye uhitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi nichukue nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu, kumwelekeza Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kwamba anapeleka Walimu kwa kufanya msawazo ndani ya Mkoa wake katika shule alizozitaja Mheshimiwa Kapinga.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwanza niishukuru Serikali kwa kutoa watumishi hao 68. Lakini sasa kutokana na ongezeko hili kubwa la ujenzi wa vituo vya afya, ambapo tuna vituo viwili tayari vimekamilika, Kituo Cha Afya cha Mkumbi na Kituo cha Afya Matili, pamoja na ongezeko hili havijapata watumishi;
Je, ni nini kauli ya Serikali?
Mheshimiwa Spika, kutokana na upungufu uliopo Serikali iko tayari kuipa kipaumbele halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kutokana na upungufu Mkubwa uliopo wa watumishi?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nijibu maswali mawili ya myongeza ya Mheshimiwa Benaya Kapinga. Kwanza hili la vituo viwili vya afya ambavyo vimejengwa na havijapata watumishi, naomba nitumie Bunge lako Tukufu kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuweza kufika katika vituo hivi viwili vya afya ambavyo amevitaja Mheshimiwa Kapinga na kufanya tathimini yake na kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukafanya msawazo wa watumishi ndani ya Mkoa wa Ruvuma walau kuanza kupeleka watumishi wachache ili waanze kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili, Serikali itaweka kipaumbele cha kupeleka watumishi kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa ikiwemo kule Mbinga Vijijini kwa Mheshimiwa Kapinga. Na Kadri tutakavyoendelea kluajiri basi tutaweka kipanumbele kwenye maeneo hayo.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga pamoja na kwamba kata nyingi kutokuwa na mawasiliano ziko kata nne minara imekamilika sasa hivi zaidi ya miaka minne; Kata ya Muhongozi, Kipololo, Kijiji cha Lunolo, Kata ya Ukata Kijiji cha Litoho, kata hizi zimekamilisha minara. Ni lini itawashwa hii minara?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mbinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, changamoto ya minara iliyopo katika Jimbo la Mbinga tayari Mheshimiwa Mbunge tumeshawasiliana na tayari hatua tumeshaanza kuchukua. Changamoto iliyokuwepo kwa kipindi kile ni kwamba mnara ukishasimama hiyo ni hatua ya kwanza ambayo ndio passive equipment. Lakini kuna hatua ya pili ambayo ni kuweka vile vifaa vya kurusha mawimbi ambayo ndio active equipment. Hapa katikati tumekuwa na changamoto kubwa sana ya covid-19, sasa hii changamoto imesababisha production ya vifaa kutoka katika nchi ambazo tunaagiza ndio imekuwa changamoto katika ukamilishaji wa vifaa hivi.
Mheshimiwa Spika, lakini mpaka sasa tayari TTCL wameshaagiza vifaa na vingine vimeshaingia nchini. Hivyo Mheshimiwa Mbunge atarajie kwamba minara hiyo ambayo tayari imeshasimama itawashwa hivi karibuni na mawasiliano yataanza kupatikana katika Jimbo la Mbinga. Ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, shida iliyopo Mbinga Mjini inalingana sawasawa na Mbinga Vijijini kwa wahudumu wa afya tulitakiwa kuwa nawatumishi 751 waliopo ni 210 tu tuna upungufu zaidi ya asilimia 80. Je, Serikali ipo tayari angalau kupunguza upungufu wa watumishi huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Kapinga nimhakikishie kwamba tunafahamu kuna upungufu wa watumishi wa afya lakini pia wa elimu katika Halmashauri ya Mbinga Vijijini na mkakati ni kwamba kufuatia tathimini yetu halmashauri zile zenye upungufu mkubwa zaidi kama Mbinga Vijijini tutaleta watumishi wa kutosha zaidi, ahsante. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini naomba niweke kumbukumbu sawa, barabara hii ina urefu wa zaidi ya kilometa 25, lakini hizo kilometa 25 ndizo ahadi ziko kwenye Ilani ya CCM kwamba zitajengwa kwa kiwango cha lami na barabara hii ndiyo barabara pekee inayotoa wananchi wa Hagati kuja mjini ni barabara pekee hiyo hiyo tu.
Mheshimiwa Spika, swali langu nimeuliza ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara hii?
Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili; barabara hii inaenda mpaka Nyasa, kwa hiyo, kule chini bado haijafunguliwa, je, Serikali iko tayari kuifungua barabara hii hadi kufika Wilaya ya Nyasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante na napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, barabara hii tunatafuta fedha ili iweze kujengwa yote kwa kiwango cha lami, lakini Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba barabara hii inapita kwenye maeneo mengi yenye miinuko na makorofi na ndiyo maana Serikali iliona bora ianze kwanza kwa kujenga kwa kiwango cha lami yale maeneo yote ambayo ni korofi ili iendelee kupitika lakini maeneo mengine yakiwa ya changarawe.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuifikisha hii barabara hadi Nyasa naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwakuwa tunaona ni barabara muhimu kuunganisha Mbinga na Nyasa, Wizara yangu kusaidiana na wenzetu wa TAMISEMI - TARURA tutakubaliana namna ya kuhakikisha kwamba tunafungua hii barabara hadi Nyasa ili kurahisisha mawasiliano kwa wananchi hawa. Ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi. Wilaya ya Mbinga pamoja na ukongwe wake haina Chuo cha VETA. Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Wilaya ya Mbinga?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kapinga, kaka yangu, Mbunge wa Mbinga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tukiri kweli Wilaya ya Mbinga ni Wilaya kongwe, lakini nikuondoe wasiwasi kaka yangu nazani ulishawahi kufika mpaka ofisini kwa ajili ya kufuatilia suala hili na Mheshimiwa Mbunge nadhani nilikueleza mpango wetu kama Serikali ni kuhakikisha kwamba Wilaya zile ambazo hazijafikiwa na ujenzi huu wa Vyuo vya VETA katika mwaka ujao tunahakikisha kwamba tunazipa kipaumbele hasa hasa zile Wilaya kongwe ambazo zina miundombinu hafifu lakini vilevile ni ngumu sana kufikika. Kwa hiyo, nikuondoe wasiwasi eneo hili la Mbinga tunakwenda kulifanyia kazi na tunahakikisha tunajenga chuo katika eneo hilo.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi; Kijiji cha Kizota Kata ya Muungano, Kindimbachini wanajenga zahanati tangu mwaka 2013, je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Benaya Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka uliopita peke yake ambao tunaumaliza Juni 30 Serikali imejenga jumla maboma 574 ya zahanati, lakini mwaka ujao wa fedha Serikali imetanga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa maboma 300 ya zahanati kuchangia nguvu za wananchi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutakwenda kuona pia uwezekano wa kupeleka fedha kwenye boma hilo la zahanati, ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nia hii ya kugawa kata tuna nia pia ya kugawa vijiji na mwaka unaokuja ni mwaka wa uchaguzi. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa Halmasahuri ya Wilaya ya Mbinga ambayo vijiji vingi vimeleta maombi ya kugawanywa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kauli ya Serikali ni kwamba taratibu za kisheria za maombi ziendelee, na Serikali itapokea maombi hayo kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, itafanya tathimini ya vigezo lakini kipaumbele cha kwanza kwa sasa ni kuboresha kwanza maeneo ya kiutawala yaliyopo. Lakini hili halizuii kuendelea na taratibu katika ngazi ya halmasahuri, ahsante. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mapera kuelekea Kambarage tumeleta maombi ya dharura kutokana na mvua zilizokwisha ilitengeneza korongo kubwa sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Benaya Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi ya Halmashauri ya Mbinga yamefika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nay apo katika hatua za mwisho za utekelezaji wa hili jambo. Ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naishukuru sana Serikali kwa majibu haya mazuri ambayo yanaleta shangwe kubwa katika Tarafa hii ya Hagati. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shule hii ya Hagati Secondary, Halmashauri ya Mbinga ina shule ya wasichana inaitwa Mbinga Girls na yenyewe iko katika hali nzuri. Kupitia barua yenye Kumb. Na. MDC/E.80/136/135, tumeomba kibali cha shule hii nayo ichukue kidato cha tano na cha sita. Je, Serikali iko tayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, halmashauri hii kwa kushirikiana na wananchi tumejenga shule za Benaya Secondary na Nguzo Secondary. Shule hizi zina upungufu wa miondombinu na sasa hivi zipo kidato cha pili. Je, Serikali iko tayari kutoa fedha kwa ajili ya miundombinu ikiwemo maabara? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Benaya Kapinga; hili la kwanza kuhusu Mbinga Girls nayo kuweza upandishwa hadhi na kuwa A – Level, Serikali ipo tayari kuweza kupandisha hadhi shule hii lakini kuna taratibu zile zilizowekwa kwa ajili ya upandishaji hadhi wa shule kuweza kuwa ya A – Level. Hivyo basi, nimtake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbinga Vijijini kuweza kuanza taratibu za kupandisha hadhi shule hii, kwa mujibu wa sheria inavyotaka. Kwa maana lazima kwanza ifanyike assessment, pili waweze kumpeleka yule Mkaguzi wa Elimu pale na kisha waandike Wizara ya Elimu kwa ajili ya kuweza kuomba kupandisha hadhi shule hii.
Mheshmiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili la fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika shule alizozitaja ikiwemo Shule hii ya Benaya: Tutaendelea kutafuata fedha kama Serikali kwa ajili ya kuweza kuboresha miundombinu ya shule mbalimbali hapa nchini ikiwemo Mbinga DC. Hivyo basi, nimtake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbinga DC kuweza kuorodhesha mahitaji yale ambayo yanahitajika katika shule hizi ili aweze kumwandikia Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, TAMISEMI na kuweza kuona namna gani Serikali itapeleka fedha kadri ya upatikanaji wake. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kipaumbele hiki cha Serikali, sisi wawakilishi wa wananchi kwenye maeneo haya tunaona kuna uhitaji wa kugawanya haya maeneo. Mazingira ya Kata hizi za Nkasi yanafanana kabisa na Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Kata ya Mkumbi, Kata ya Nyoni, Kata ya Langilo na Kata ya Maguu. Je, Serikali inatoa kauli gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Kapinga kwa kufuatilia uanzishaji wa maeneo mapya ya utawala katika Halmashauri ya Mbinga Vijijini. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwamba, Serikali inatambua umuhimu wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala kwa sababu, yanasogeza huduma za jamii karibu na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku ni lazima tuwe na vipaumbele. Tuna majengo mengi ya wakuu wa wilaya hayajakamilika, majengo ya utawala ya halmashauri, ofisi za kata na maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, Serikali kwa sasa kwanza itakamilisha miundombinu hiyo ili ofisi hizo ziweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi kwa wananchi na baadaye tutakwenda kuanzisha maeneo mapya ya utawala. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, suala hilo litafanyiwa kazi wakati utakapofika. Ahsante sana.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nishukuru kwa majibu ya Serikali lakini swali langu mimi nimeuliza ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami? Na hii ni ahadi ya Rais, ni lini siyo hayo maelezo ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyatoa.
Kwa hiyo, bado naendelea kuuliza ni lini Serikali itaanza kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Barabara za Jimbo la Mbinga Vijijini kutokana na mvua zilizonyesha zimeharibika sana na zimeleta usumbufu mwingi sana kipindi hiki cha mvua. Barabara ya kutoka Kingori hadi Paradiso, Barabara ya kutoka Njia Panda Rugali - Mkumbi pia Barabara ya Nyoni - Tingi barabara hizi ni mbovu sana. Je, Serikali ina mkakati gani kupitia hizi fedha za dharura kuzijenga barabara hizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge swali la pili kama Mheshimiwa Naibu Spika ulivyoelekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara za Jimbo la Mbinga kwa maana ya Wilaya ya Mbinga zimeharibika na hii ni pamoja na barabara zote nchi nzima kutokana na mvua ambazo zimenyesha sana. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote, Serikali imeshafanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu na hasa barabara nchi nzima na tayari sasa hivi tupo tunatafuta fedha na nina uhakika Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kipaumbele kikubwa kuhakikisha kwamba baada ya kurejesha mawasiliano tutahakikisha kwamba tunarudisha barabara zote kwenye hali yake ya kawaida.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kwamba mpango upo mkubwa ambao Serikali inafanya kuhakikisha kwamba inarejesha mawasiliano, ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, hata hivyo, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; hii Kata ya Ngima wananchi kwa kushirikiana na mimi Mbunge tumejenga tayari madarasa manne. Je, Serikali iko tayari kutenga fedha japo kidogo kukamilisha madarasa haya ili yaweze kutumika mwakani Januari?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; wananchi wa Kata ya Matiri pamoja na Kata ya Nguzo nao wamejenga Shule ya Sekondari Nguzo pamoja na Benaya Sekondari hazina miundombinu ya kutosha. Je, Serikali iko tayari kupeleka fedha kukamilisha miundombinu ya shule hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali ina nia ya kuendelea kuboresha miundombinu ya shule na hivyo kwa kadri ya upatikanaji wa fedha Serikali itaweza kujenga madarasa hayo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, Serikali inatambua jitihada ambazo zimefanywa na wananchi wa Mbinga DC za kujenga Shule ya Sekondari ya Benaya na Nguzo na shule hizo tayari zimeshasajiliwa na zina wanafunzi mpaka kidato cha pili. Kwa kuzingatia miundombinu ambayo bado haijakamilika katika shule hizo, Serikali kupitia bajeti ya halmashauri ya 2024/2025 imepanga kutumia shilingi milioni 62.5 kwa ajili ya shule hizo. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kufanya tathmini ya ukamilishwaji wa miundombinu ya shule hizo ili kuongeza fedha kulingana na upatikanaji wake kwa ajili ya kuhakikisha kuwa ujenzi wa shule hizo unakamilishwa na kuunga mkono jitihada za wananchi. Ahsante. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Kiwombi - Kata ya Amanimakoro, Kijiji cha Sala - Kata ya Muhongozi, Kijiji cha Kihangimauka - Kata ya Kihangimauka, vijiji hivi vilikuwa na makubaliano na UCSAF lakini hadi leo hakuna kinachoendelea. Ni lini minara hii inaenda kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante, nikupongeze Mheshimiwa Mbunge hili suala tumeliongea jana tu na tumeshakubaliana mimi na wewe tutakwenda, lakini nimeshatoa maagizo kwa Meneja wa Kanda Nyanda za Juu Kusini anashughulikia hii minara. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itakamilisha kipande cha Amanimakoro – Ruanda ambacho muda wake umekwisha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba mkandarasi yuko site na Waziri ametembelea. Tumeongea na mkandarasi huyo kuondoa changamoto ambazo zilikuwa zinamfanya achelewe. Kwa hiyo, tuna uhakika baada ya majadiliano tutamwongeza muda ili aweze kuijenga hiyo barabara yote kwa kiwango cha lami kwa sababu tayari yuko site, ahsante. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Mbinga – Litembo kupitia Ndengu ambayo mwaka jana ilitangazwa upembuzi yakinifu, itaanza lini kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja tupo tunakamilisha taratibu za usanifu na kwa kuwa tumeshaanza, tutakapokuwa sasa tumeshakamilisha kwa 100% usanifu wa kina, barabara hiyo itatafutiwa fedha kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, mwaka jana niliuliza swali hapa kuhusiana na ujenzi wa sub-station Wilaya ya Mbinga na Serikali iliahidi kujenga sub-station mwaka huu. Je, ni lini sasa sub-station ya Wilaya ya Mbinga itajengwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na namshukuru Mheshimiwa Benaya kwa swali lake zuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, mradi wa kujenga kituo cha kupoza umeme pale Mbinga, upo katika hatua za kuweza kutekelezwa. Kama mnafahamu, mradi huu unatakiwa uanze kwa awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza ya sasa hivi kukamilika. Kwa kweli kwa awamu ya kwanza tumefanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyokuwa kwa Mheshimiwa Profesa Kabudi kwamba unatekelezeka ndani ya awamu ya pili na ndivyo hivyo kwa kituo cha kupooza umeme Mbinga. Kwa kweli tutasimamia kwa weledi mkubwa sana na nguvu kubwa sana ili sub-station ya Mbinga iweze kujengwa. Kwa kweli kwa pale Mbinga, kwa sasa hivi tumefanya miradi mikubwa sana, kwanza tumeanza ku-stabilize line ambayo inapeleka umeme kutoka Songea hadi Mbinga. Vilevile, line za Mbinga Vijijini kwa sababu umeme ulikuwa unakatika katika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama ambavyo tumeanza kupeleka miradi ikiwemo miradi ya ujalizi ambayo kwa kweli Mbinga Vijijini ina miradi mingi sana, ina vitongoji vingi sana vya ujazilizi na inategemea kuanza hivi karibuni. Tutaendelea kuboresha ili kuhakikisha wananchi hawa wa Mbinga Vijijini wanendelea kupata umeme mzuri ili waweze kuboresha shughuli zao za maendeleo kwa sababu wananchi wa Mbinga Vijijini ni wachapakazi na wanajiendeleza sana katika maeneo ya viwanda vidogo katika maeneo ya kahawa na mahindi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. BENAYA l. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali kuweka haya maeneo ya kiutawala ni pamoja na kusogeza huduma kwa wananchi. Kwa kuweka hiki kipaumbele cha kuboresha miundombinu wakati wananchi wanaifuata hiyo huduma mbali, haioni kwamba inapingana na kipaumbele cha kusogeza huduma kwa wananchi?
Je, Serikali inaahidi nini Wananchi wa Tarafa ya Hagati na Mbuji wanaopata huduma hii mbali sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba, Serikali imeanzisha maeneo mengi sana ya kiutawala, maeneo mengi bado hatuna Ofisi za Halmashauri. Waheshimiwa Wabunge wameendelea kuomba hapa na Serikali imeendelea kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya utawala ya Wakurugenzi, Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Ofisi za Kata, Ofisi za Vijiji, bado tuna gap kubwa sana kwenye ujenzi wa miundombinu ya ofisi za utawala ambazo zipo kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, tuliona ni busara tukamilishe kwanza miundombinu katika mamlaka zilizopo ili ziweze kutoa huduma na baadaye tuendelee na hatua ya kuanzisha mamlaka nyingine, kwa sababu haina faida kuanzisha mamlaka ambazo hazina miundombinu na haziwezi kuhudumia wananchi kwa ufanisi unaotakiwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, suala hilo Serikali inalitambua na dhamira yake ni kusogeza huduma pamoja na kuwa na miundombinu bora zaidi na tutaendelea kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili niwahakikishie wananchi wa Tarafa ambazo Mheshimiwa Mbunge umezitaja katika Jimbo la Mbinga Vijijini kwamba Serikali inatambua changamoto zao na Mheshimiwa Mbunge amezisemea na Serikali inaendelea kuzifanyia kazi, kuhakikisha wanapata huduma karibu zaidi, ahsante. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nishukuru kwa majibu ya Serikali lakini swali langu mimi nimeuliza ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami? Na hii ni ahadi ya Rais, ni lini siyo hayo maelezo ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyatoa.
Kwa hiyo, bado naendelea kuuliza ni lini Serikali itaanza kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Barabara za Jimbo la Mbinga Vijijini kutokana na mvua zilizonyesha zimeharibika sana na zimeleta usumbufu mwingi sana kipindi hiki cha mvua. Barabara ya kutoka Kingori hadi Paradiso, Barabara ya kutoka Njia Panda Rugali - Mkumbi pia Barabara ya Nyoni - Tingi barabara hizi ni mbovu sana. Je, Serikali ina mkakati gani kupitia hizi fedha za dharura kuzijenga barabara hizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge swali la pili kama Mheshimiwa Naibu Spika ulivyoelekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara za Jimbo la Mbinga kwa maana ya Wilaya ya Mbinga zimeharibika na hii ni pamoja na barabara zote nchi nzima kutokana na mvua ambazo zimenyesha sana. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote, Serikali imeshafanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu na hasa barabara nchi nzima na tayari sasa hivi tupo tunatafuta fedha na nina uhakika Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kipaumbele kikubwa kuhakikisha kwamba baada ya kurejesha mawasiliano tutahakikisha kwamba tunarudisha barabara zote kwenye hali yake ya kawaida.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kwamba mpango upo mkubwa ambao Serikali inafanya kuhakikisha kwamba inarejesha mawasiliano, ahsante.