Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dennis Lazaro Londo (19 total)

MHE. DENNIS L. LONDO Aliuliza: -

(a) Je, ni Watumishi wangapi wamerejeshwa kazini baada ya kuondolewa kimakosa wakati wa zoezi la uhakiki wa vyeti feki na Wafanyakazi hewa?

(b) Je, ni Watumishi wangapi waliorejeshwa kazini wamelipwa stahiki zao kama mishahara ambayo hawakupata kutokana na kuondolewa kazini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia ofisi yangu imewarejesha kazini na kuendelea kuwalipa mishahara jumla ya watumishi 4,380 walioondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kimakosa wakati wa zoezi la uhakiki wa vyeti vya elimu na watumishi hewa. Idadi hii inajumuisha Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Mitaa wapatao 3,114.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwarejesha watumishi tajwa, Serikali pia ilitoa msamaha wa kuwarejesha kazini watumishi walioondolewa kazini kwa kukosa sifa ya elimu ya Kidato cha Nne na baadaye wakajiendeleza na kupata sifa tajwa hadi kufikia mwezi Disemba, 2020 ambao hawakudanganya katika taarifa zao kuwa wana elimu ya Kidato cha Nne au kubainika kughushi vyeti. Pia, mnamo tarehe 07 Mei, 2021 Serikali kupitia ofisi yangu ilitoa maelekezo na utaratibu kwa waajiri kuhusu namna ya kushughulikia hatima za ajira za watumishi walioondolewa kazini kwa kukosa sifa ya elimu ya Kidato cha Nne pamoja na malipo ya stahiki zao. Napenda kuwakumbusha waajiri wote kukamilisha utekelezaji wa maelekezo hayo kwa haraka na kwa usahihi ili watumishi husika waweze kupata haki zao mapema.

Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kusisitiza kwamba msamaha uliotolewa unawahusu watumishi wale tu walioajiriwa baada ya tarehe 20 Mei, 2004 bila sifa ya elimu ya Kidato cha Nne lakini baadaye wakajipatia sifa za kuajiriwa na haiwahusu watumishi waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi au waliotoa taarifa za uwongo katika kumbukumbu zao rasmi za kiutumishi. Utaratibu wa kushughulikia watumishi waliobainika kughushi vyeti ulishatolewa awali na Serikali na watumishi wote waliobainika kughushi vyeti hawastahili kurudishwa kazini.

Mheshimiwa Spika, Serikali imelipa madai ya mishahara ya jumla ya shilingi 2,613,978,000 kwa watumishi 1,643 waliorejeshwa kazini baada ya kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kimakosa. Uhakiki wa madai yaliyobaki unaendelea na yataendelea kulipwa kwa kadri yanavyohakikiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wanaoishi kwenye vijiji vinavyopakana na hifadhi pamoja na mali zao wanakuwa salama kwani wanyamapori wamekuwa wakiingia na kufanya uharibifu kwenye vijiji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba kutoa pole kwa Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mikumi kwa kadhia hiyo ya kupambana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vinavyozunguka hifadhi za wanyamapori nchini vinakabiliwa na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kama vile tembo, simba, fisi, nyati, viboko na mamba. Pamoja na mambo mengine, hali hii hii inasababishwa na kuvamiwa kwa maeneo ya kinga (buffer zone) na mapito ya wanyamapori.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu, Serikali imeunda kikosi maalum ambacho kimekuwa kikishirikiana na wadau mbalimbali kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yanayozunguka hifadhi kwa kadri taarifa za matukio zinavyopatikana. Aidha, Serikali imeandaa mpango mkakati wa kitaifa wa kushughulikia wanyamapori wakali na waharibifu unaotoa mwongozo wa namna nzuri ya kuwawezesha wananchi kutumia maeneo yao bila kuathiriwa na uwepo wa wanyamapori.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati hiyo ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa hifadhi kuhusu mbinu bora za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu. Mafunzo haya ni endelevu na yatafanyika katika maeneo yote yenye changamoto hapa nchini. Pili, kuimarisha vikosi vya doria za kudhibiti wanyamapori vikiwemo vitendea kazi ili viweze kufanya doria ipasavyo. Tatu, kushirikiana na Halmashauri za wilaya na vijiji, ili kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe rai kwa wananchi wa Mikumi na maeneo mengine yanayozunguka hifadhi waendelee kutoa ushirikiano na kuendelea kufuata maelekezo ya wataalam wa wanyamapori kwa kutekeleza mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori hao ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:-

Je, ni lini upanuzi wa Kiwanda cha Sukari cha Ilovo utakamilika, na kwa kiasi gani upanuzi huo utaenda sambamba na kuondoa kero ya Mizani na Vipimo vya Sucrose kwa wakulima wa Miwa?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kinaendeshwa na Kilombero Sugar Company Limited, Kampuni hii inamilikiwa kwa ubia kati ya Kampuni ya Ilovo Sugar Africa yenye asilimia 75 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye asilimia 25 katika hisa hizo. Katika kutekeleza sera ya Serikali ya kujitosheleza kwa mahitaji ya sukari nchini ifikapo mwaka 2025, Kampuni ya Kilombero Sugar itatekeleza mradi wa upanuzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kwa gharama ya shilingi bilioni 571.6.

Mheshimiwa Spika, matokeo tunatarajia mradi huu ni kuwa na Kiwanda cha kisasa, ambacho kitakuwa kikubwa mara nne kuliko cha sasa, kuongeza uzalishaji wa sukari mara mbili kutoka tani 127,000 za sasa hadi tani 271,000 kwa mwaka. Kuongeza mara tatu matumizi ya miwa kutoka kwa wakulima wadogo kutoka tani 600,000 hadi tani milioni 1.7 na kuongeza zaidi ya mara tatu idadi ya wakulima wanaouza miwa kutoka wakulima 7,500 hadi 15,000 mpaka 16,000. Mazungumzo kati ya wabia kuhusu mradi huu yamekamilika na utekelezaji wake utaanza mwezi Juni, ambao ni mwezi huu na unatarajiwa ukamilike mwezi Julai mwaka 2023.

Mheshimiwa Spika, kuhusu sehemu yake ya pili ya swali, Serikali inatambua changamoto ya kero ya mizani na upimaji wa ubora wa miwa kwa wakulima wa miwa huko Kilombero. Katika kutatua changamoto hii, Serikali inalenga kuwa na mizani huru tofauti na ya sasa, ili tuwe na wapimaji huru na nimeshawaelekeza Work and Measures Agency wafanye utafiti kuona uwezekano wa wao wenyewe kupima, badala ya kupima na Kiwanda cha Kilombero. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Bwawa la Zombo linatumika kikamilifu kwa ufugaji wa samaki na kuondoa tatizo la ajira kwa vijana?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa ina mpango endelevu wa kufanya tathmini ya mabwawa yaliyopo katika halmashauri mbalimbali nchini ili kufahamu uwekezaji unaofaa kwenye bwawa husika kulingana na jiografia ya eneo hilo. Kwa kuwa shughuli hii ni endelevu na hufanyika kwa awamu, Bwawa la Zombo litaingia kwenye mpango wa tathmini katika mwaka wa fedha 2022/2023 ili kujua aina ya uwekezaji unaofaa katika Bwawa hilo.

Mheshimiwa Spika, vile vile, wataalam wa Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Kingolwira – Morogoro watatoa mafunzo maalum ya ufugaji samaki kwa vijana wa Jimbo la Mikumi ili kuwapa stadi za ufugaji samaki wenye tija kwenye mabwawa kwa lengo la kutengeneza ajira. ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, ni kesi ngapi za wakulima kulishiwa mazao yao zimeripotiwa na ngapi zimepelekwa mahakamani katika Wilaya ya Kilosa?
NAIBU WAZIRI OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kesi zilizoripotiwa polisi za wakulima kulishiwa mazao yao Wilayani Kilosa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2018 hadi 2022 ni kesi 1,403. Katika kesi hizo zilizofikishwa mahakamani ni 1,037 na zilizotolewa hukumu na mahakama ni kesi 540.

Mheshimiwa Spika, vilevile kesi 356 ziliondolewa ama kufutwa mahakamani kutokana na sababu mbalimbali. Nakushukuru.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, kuna Wataalam wangapi wa huduma za utengamano na mazoezi ya viungo physiotherapist katika Mkoa wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Morogoro una jumla ya wataalam 15 kati ya 30 wanaohitajika wa huduma za utengamao na mazoezi ya viungo ambapo Kilosa kuna mtaalam mmoja, Hospitali ya Rufaa Morogoro kuna wataalam wanne, Mvomero mtalaam mmoja, Ifakara Hospitali wanne na Mzinga Hospitali wataalam watano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha watalaam tisa wa huduma za utengamao wameombewa kibali cha ajira katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023. Ahsante. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya kuunganisha Ruaha Mbuyuni, Malolo hadi Uleling’ombe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali barabara hii ya Ruaha Mbuyuni - Malolo hadi Uleling’ombe ilikuwa haijaingizwa katika mtandao wa barabara zinazohudumiwa na TARURA. Serikali kupitia TARURA itatenga fedha kiasi cha shilingi milioni 100 katika mpango na bajeti wa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya usanifu wa awali wa barabara ya Ruaha Mbuyuni, Malolo mpaka Uleling’ombe yenye urefu wa kilometa 27.9. Lengo la usanifu huo ni kupata gharama halisi za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya kupata gharama halisi za usanifu, Serikali kupitia TARURA itaweka katika mipango yake ya bajeti kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Ruaha Mbuyuni, Malolo hadi Uleling’ombe kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je! Tanzania ina Diaspora wangapi na ni upi mchango wao katika uchumi wa nchi?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi zetu za uwakilishi wa Kibalozi, idadi ya diaspora wa Tanzania ni milioni 1.5. Aidha, Wizara inakamilisha mfumo wa kidigitali wa uandikishaji wa diaspora (Diaspora Digital hub), ambao unaotarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2023. Mfumo huu utawezesha ukusanyaji endelevu wa takwimu za diaspora.

Mheshimiwa Spika, diaspora huchangia katika maendeleo ya nchi kwa kutuma fedha za kigeni nchini (remittances), kuwekeza, kuleta mitaji, utaalam na teknolojia inayoweza kuchangia kukuza uzalishaji wa mazao, bidhaa na huduma mbalimbali zenye tija kiuchumi. Aidha, diaspora hutangaza fursa za kiuchumi, biashara, utalii na uwekezaji zinazopatikana nchini.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Desemba, 2022, diaspora wa Tanzania walituma nchini kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.1 sawa na shilingi trilioni 2.6. Vilevile, katika kipindi hicho diaspora walifanya uwekezaji kupitia ununuzi wa nyumba na viwanja wenye thamani ya shilingi bilioni 4.4 na ununuzi wa hisa zenye thamani ya shilingi bilioni 2.5. Ahsante sana.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, ni watumishi wangapi wa umma wamefikishwa Mahakamani kwa rushwa, wangapi wameshinda kesi na kurejeshwa kazini kwa kipindi cha 2010 – 2020?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2010 mpaka 2020, jumla ya Watumishi 2,060 walifikishwa Mahakamani na kushtakiwa kwa makosa mbalimbali ya rushwa. Kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 ya Sheria za Tanzania. Kati ya watumishi hao 2,060 walioshtakiwa, watumishi 1,157 walitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu mbalimbali kwa mujibu wa sheria, huku watumishi 863 wakishinda kesi na kuachiwa huru waendelee na kazi.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:-

Je, mchakato wa ujenzi wa geti jipya la kuingilia Hifadhi ya Mikumi kutokea Kilangali na Tindiga umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Londo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha tathmini ya awali kwa ajili ya kujenga lango la kuingilia watalii kupitia maeneo ya Kilangali na Tindiga Wilaya ya Kilosa. Kufuatia tathmini hiyo, gharama za ujenzi wa lango hilo na miundombinu ambata ya lango husika ni jumla ya shilingi bilioni 2.8. Aidha, michoro pamoja na BOQ imekamilika. Hatua inayoendelea kwa sasa ni kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa lango hilo. Kwa ujumla, lango husika litafungua fursa za watalii watakaosafiri na treni ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam na Dodoma kuingia Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali kwa kuona umuhimu wa hifadhi hiyo imejipanga kuongeza malango ya kuingilia watalii katika maeneo yote muhimu ambapo kwa sasa kupitia Mradi wa Kukuza Utalii Kusini (REGROW), malango mawili ya kisasa yanajengwa kwa ajili ya kuingilia watalii katika maeneo ya Doma na Kikwaraza (Mji mdogo wa Mikumi). Ujenzi huo umeanza mwezi Agosti, 2023 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2024.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, ajali ngapi za barabarani zimetokea kati ya Mikumi na Ruaha Mbuyuni kwa Mwaka 2010 hadi 2022?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi 2022 ajali za barabarani zilizosababishwa na vyombo vya moto katika eneo la Mikumi hadi Ruaha Mbuyuni, barabara ya Morogoro kwenda Iringa ni 128. Mchanganuo wa ajali hizo ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ajali zilizohusisha mabasi ya abiria ni 30, malori 42 na magari madogo 56, nashukuru.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, nini hatma ya madai ya maslahi ya waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari Kilombero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, taarifa zilizopo katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii zinaonesha kuwa hakuna madai ya mafao ya malimbikizo ambayo yapo kwa waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari Kilombero. Wafanyakazi wote waliofungua madai wamelipwa. Iwapo kuna mfanyakazi yeyote ambaye hajafungua madai, ninashauri afungue madai yake ili aweze kulipwa mafao yake kwa mujibu wa sheria na kanuni za mifuko zilizopo, ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO K.n.y. MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je Serikali ina mpango gani wa kuunganisha barabara Kata za Ulaya, Kisanga, Malolo na Uleling’ombe katika Jimbo la Mikumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deniss Lazaro Londo Mbunge wa Jimbo la Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali inaifanyia matengenezo barabara ya Kidodi – Vidunda yenye urefu wa kilomita 4.14 ambayo itawezesha uunganishaji wa Kata za Vidunda na Kidodi. Pia, ujenzi wa daraja la Ruhembe kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.00 utawezesha kuunganisha Kata za Ruhembe na Kidodi.

Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2022/2023, TARURA imetenga Shilingi Bilioni 1.00 kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Ulaya – Kisanga kilomita 42.1 ambayo itaunganisha Kata za Ulaya na Kisanga. Aidha, kiasi cha Shilingi Milioni 500.00 zimetengwa kwa ajili ya ukamilishaji wa daraja la Ruhembe linalounganisha Kata za Ruhembe na Kidodi.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kuunganisha Kata ya Malolo na Uleling’ombe katika Jimbo la Mikumi kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. FLORENT L. KYOMBO K.n.y. MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je Serikali ina mpango gani wa kuunganisha barabara Kata za Ulaya, Kisanga, Malolo na Uleling’ombe katika Jimbo la Mikumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deniss Lazaro Londo Mbunge wa Jimbo la Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali inaifanyia matengenezo barabara ya Kidodi – Vidunda yenye urefu wa kilomita 4.14 ambayo itawezesha uunganishaji wa Kata za Vidunda na Kidodi. Pia, ujenzi wa daraja la Ruhembe kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.00 utawezesha kuunganisha Kata za Ruhembe na Kidodi.

Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2022/2023, TARURA imetenga Shilingi Bilioni 1.00 kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Ulaya – Kisanga kilomita 42.1 ambayo itaunganisha Kata za Ulaya na Kisanga. Aidha, kiasi cha Shilingi Milioni 500.00 zimetengwa kwa ajili ya ukamilishaji wa daraja la Ruhembe linalounganisha Kata za Ruhembe na Kidodi.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kuunganisha Kata ya Malolo na Uleling’ombe katika Jimbo la Mikumi kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:-

Je, Serikali inamiliki hisa kiasi gani, kwenye makampuni mangapi na hisa hizo zina thamani kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imewekeza katika Taasisi, Mashirika ya Umma na Kampuni zipatazo 304 na uwekezaji wa Serikali una thamani ya shilingi trilioni 76. Kati ya uwekezaji huo, Serikali ina hisa zipatazo milioni 420 katika kampuni 54 ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache, nakushukuru.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:-

Je, Serikali imetoa na kukusanya kiasi gani kutokana na mkopo wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi na kiasi gani kimerudi kuendeleza mpango huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali ilitoa bilioni 50 kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK). Fedha hizo zilikopeshwa bila riba kwenda kwenye halmashauri 57 ambacho kilikuwa ni kiasi cha shilingi bilioni 43.6. Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Iringa kiasi cha shilingi milioni 450, Vyuo vya Ardhi vya Tabora vilipata milioni 644, Morogoro vilipata bilioni 1.2 na Chuo Kikuu Ardhi kilipata milioni 892.8 ambazo zimewezesha jumla ya kupanga na kupima viwanja 218,337.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufika Machi, 2024, jumla ya shilingi bilioni 23.5 sawa na asilimia 47 zimekwisharejeshwa. Halmashauri 12 zimekamilisha marejesho yenye kiasi cha shilingi bilioni 11.3, halmashauri 43 zimerejesha sehemu ya fedha yenye jumla ya shilingi bilioni 10.9, Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Iringa imerejesha shilingi milioni 581.3, Chuo cha Ardhi Morogoro milioni 250, Chuo cha Ardhi Tabora milioni 100, Chuo Kikuu Ardhi milioni 100 na halmashauri mbili ambazo ni Shinyanga Manispaa shilingi bilioni 1.055 na Musoma DC shilingi milioni 200 hazijarejesha kabisa. Wizara yetu itaendelea kufuatilia halmashauri ambazo hazijakamilisha kurejesha fedha hizo ili zitekeleze wajibu huo kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Wizara na halmashauri hizo.
MHE. HAMISI S. TALETALE K.n.y. MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, ni nini msingi kwa wafanyabiashara kutoza bei tofauti au fedha za kigeni kwa wateja ambao ni raia wa kigeni na nini athari zake?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Serikali imeandaa sheria na kanuni ili kumlinda mlaji na kuhakikisha kuwa bei za bidhaa na huduma zinapangwa kwa msingi wa nguvu ya soko. Kwa mantiki hii, biashara zimekuwa zikiendeshwa chini ya utaratibu wa soko huria ambapo bei za bidhaa na huduma hupangwa kuendana na uwiano wa uhitaji na upatikanaji wa bidhaa husika. Hata hivyo, wafanyabiashara wanaweza kutoza bei tofauti kwa bidhaa na huduma baina ya wazawa na raia wa kigeni au kwa fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine Serikali inatambua na imeendelea kukumbusha kuwa shilingi ndio fedha halali kwa ajili ya malipo mbalimbali hapa nchini. Kutokana na hilo, raia wa kigeni hawatakiwi kulazimishwa kulipa kwa fedha za kigeni hususan pale wanapokuwa na shilingi za Kitanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, wageni wanaruhusiwa kutumia fedha za kigeni ili kurahisisha ufanyaji wa biashara pale wanapokosa shilingi za Kitanzania na viwango vya ubadilishaji fedha havikitakiwi kutofautiana na vile vinavyotozwa katika masoko ya fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna athari za kimsingi za uchumi kwa wafanyabiashara kutoza bei tofauti baina ya wateja raia wa kigeni na wazawa kwani bei hizo huamuliwa katika soko huru na hivyo inatarajiwa kupanda na kushuka kulingana na nguvu za mahitaji na ugavi sokoni, ahsante. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutunza mazingira ya Bwawa la Zombo Kilosa ili litumike kwa shughuli za ufugaji wa samaki na kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kutunza mazingira ya Bwawa la Zombo. Hatua hizo ni pamoja na upandaji wa miti kuzunguka bwawa katika eneo la hifadhi ya bwawa ndani ya eneo la meta 60.

Mheshimiwa Spika, aidha katika kipindi cha msimu wa mvua 2024/2025 Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwa kushirikiana na Bonde la Wami - Ruvu, imepanga kupanda miti 5,000 ili kuongeza uoto wa asili na kuzuia mmomonyoko wa udongo katika maeneo yanayozunguka bwawa, aidha kulinda eneo la hifadhi ya bwawa ndani ya meta 60, kuzunguka bwawa dhidi ya shughuli zisizoendelevu na kuendesha doria za mara kwa mara na utoaji wa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi katika vijiji vinavyonufaika na bwawa husika hususan kilimo na ufugaji, nakushukuru.
MHE. HAMISI S. TALETALE K.n.y. MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, ni nini msingi kwa wafanyabiashara kutoza bei tofauti au fedha za kigeni kwa wateja ambao ni raia wa kigeni na nini athari zake?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Serikali imeandaa sheria na kanuni ili kumlinda mlaji na kuhakikisha kuwa bei za bidhaa na huduma zinapangwa kwa msingi wa nguvu ya soko. Kwa mantiki hii, biashara zimekuwa zikiendeshwa chini ya utaratibu wa soko huria ambapo bei za bidhaa na huduma hupangwa kuendana na uwiano wa uhitaji na upatikanaji wa bidhaa husika. Hata hivyo, wafanyabiashara wanaweza kutoza bei tofauti kwa bidhaa na huduma baina ya wazawa na raia wa kigeni au kwa fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine Serikali inatambua na imeendelea kukumbusha kuwa shilingi ndio fedha halali kwa ajili ya malipo mbalimbali hapa nchini. Kutokana na hilo, raia wa kigeni hawatakiwi kulazimishwa kulipa kwa fedha za kigeni hususan pale wanapokuwa na shilingi za Kitanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, wageni wanaruhusiwa kutumia fedha za kigeni ili kurahisisha ufanyaji wa biashara pale wanapokosa shilingi za Kitanzania na viwango vya ubadilishaji fedha havikitakiwi kutofautiana na vile vinavyotozwa katika masoko ya fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna athari za kimsingi za uchumi kwa wafanyabiashara kutoza bei tofauti baina ya wateja raia wa kigeni na wazawa kwani bei hizo huamuliwa katika soko huru na hivyo inatarajiwa kupanda na kushuka kulingana na nguvu za mahitaji na ugavi sokoni, ahsante. (Makofi)