Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Deus Clement Sangu (6 total)

Hitaji la Posho za Kujikimu kwa Wafanyakazi Wanaojitolea

MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-

Je, kwa nini Serikali isiwalipe posho sawa ya kujikimu wafanyakazi wanaojitolea ili kuondoa matabaka ya malipo kulingana na sehemu wanazofanya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaruhusu waajiri mbalimbali katika utumishi wa umma kuwatumia wahitimu wa vyuo katika ngazi mbalimbali za elimu kufanya kazi kwa kujitolea katika maeneo yao ya kazi ili kupata uzoefu wa kazi kwa fani zao. Kwa kuwa wahitimu hao siyo watumishi wa umma, miongozo ya kiutumishi haijaelekeza utaratibu wa kuwalipa mishahara au posho ya kujikimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maelezo ya hapo juu, Serikali inatambua umuhimu wa wafanyakazi wanaojitolea katika utumishi wa umma. Katika kuhakikisha matumizi sahihi ya mfanyakazi wa kujitolea, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Mwongozo wa Kujitolea katika Utumishi wa Umma ambao utaweka utaratibu kwa waajiri na kada mbalimbali wa namna ya kuwapata, kuwasimamia na kuwalipa masilahi wafanyakazi watakaojitolea katika taasisi zao, nashukuru.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuanzisha Mfumo utakaowezesha kupata idadi sawa ya nafasi za ajira katika kila Jimbo badala ya mfumo wa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kwa ruhusa yako, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu katika nafasi hii kama Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, nachukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehma kwa namna ambavyo amenijalia na leo nimesimama mbele katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuniteua kushika nafasi hii. Naomba nitoe ahadi kwake na kwa Watanzania kwamba nitaitumikia nafasi hii nikitanguliza uadilifu, uchapakazi na maslahi ya Taifa mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatu, nakushukuru wewe kwa miongozo yako na namna ambavyo umeendelea kutulea na Waheshimiwa Wabunge wote kwa namna ambavyo tumekuwa tukishirikiana kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, wananchi wangu wa Jimbo la Kwela ambao wamenifanya niwepo ndani ya Bunge hili niwaahidi nitaendelea kuwatumikia na kutanguliza yale waliyokuwa wamenituma ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo ya utangulizi naomba kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, nijibu swali la Mheshimiwa Amandus Julius Chinguile, Mbunge wa Jimbo la Nachingwea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2008 Toleo la pili aya ya 4.2, nafasi za ajira hutolewa kwa ushindani na kwa kuzingatia sifa stahiki kwa mujibu wa miundo ya maendeleo ya utumishi wa kada husika. Vilevile nafasi za wazi za ajira hutolewa kwa kuzingatia ikama ya watumishi katika taasisi husika ambayo imejumuishwa katika mahitaji halisi yaliyopo katika taasisi husika.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hati idhini iliyoidhinishwa kila taasisi mahitaji ya watumishi katika taasisi moja hutofautiana na taasisi nyingine kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukubwa wa taasisi na uwingi wa majukumu. Aidha, idadi ya Taasisi za Umma zinatofautiana kwa kila jimbo; kwa misingi hiyo, idadi ya nafasi za ajira hutofautiana jimbo moja na jimbo lingine.

Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo hayo katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imetoa kibali cha ajira na nafasi 47,404 za ajira mpya kwa waajiri wote ambapo kila mwajiri katika kila jimbo amepata nafasi kwa kuzingatia ikama ya watumishi katika maeneo hayo. Aidha, katika kutekeleza kibali hicho Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira kwa watumishi wa umma imetangaza nafasi kada ya Elimu na afya kimkoa na usaili utafanyika katika ngazi ya mkoa, nashukuru.
MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuendeleza ustawi wa familia kwa kuweka wanandoa waajiriwa katika vituo vya kazi vya jirani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini ustawi wa familia ambao ni muhimu kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla. Ni kwa msingi huo, Serikali imeweka kipindi cha chini cha watumishi kukaa katika kituo kimoja cha kazi kabla ya kuhamishwa kuwa ni miaka mitatu na baada ya kipindi hicho kupita watumishi wanaweza kuwasilisha maombi ya uhamisho kwenda maeneo mengine kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuungana na wenza wao. Hata hivyo, maombi hayo yanapaswa kuzingatia uwepo wa mahitaji ya rasilimali watu kwa kada husika katika maeneo hayo. Katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2023/2024, jumla ya vibali vya uhamisho 8,846 vimetolewa vikiwemo vya watumishi wa kufuata wenza wao.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inafanya zoezi la tathmini ya mahitaji wa watumishi (HR Assesment), baada ya tathmini hii kukamilika Serikali itajua mahitaji halisi ya watumishi katika maeneo tofauti na kusaidia kufanya msawazo katika maeneo ambayo yatakuwa na upungufu, zoezi hili litasaidia kujaza nafasi katika maeneo yenye upungufu kwa kuzingatia hali ya ndoa. Nashukuru.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR aliuliza: -

Je, kwa kiasi gani mifumo ya TEHAMA inasaidia kuongeza uwajibikaji wa Watumishi wa Umma nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujenga na kuimarisha mifumo na miundombinu ya TEHAMA, ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019 na Kanuni zake za mwaka 2020, kwa ajili ya kusimamia matumizi ya Mifumo ya TEHAMA Serikalini.

Mheshimiwa Spika, Serikali imejenga mifumo mbalimbali ya TEHAMA ikiwemo, e-Watumishi, e-Utendaji, e-Mrejesho na e-Office ili kuimarisha uwajibikaji katika Utumishi wa Umma. Matumizi ya Mifumo hii yameboresha uendeshaji wa shughuli za Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi. Aidha, kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024, uwajibikaji katika utendaji kazi kwa Watumishi na Taasisi za Umma ulipimwa kupitia mfumo wa e-Utendaji ambapo jumla ya Watumishi wa Umma 507,136 sawa na 87% na Taasisi za Umma 531 sawa na 93% zilipimwa utendaji wake ambapo zoezi hilo limesaidia kuongezeka kwa uwajibikaji, nashukuru.
MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuendeleza ustawi wa familia kwa kuweka wanandoa waajiriwa katika vituo vya kazi vya jirani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini ustawi wa familia ambao ni muhimu kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla. Ni kwa msingi huo, Serikali imeweka kipindi cha chini cha watumishi kukaa katika kituo kimoja cha kazi kabla ya kuhamishwa kuwa ni miaka mitatu na baada ya kipindi hicho kupita watumishi wanaweza kuwasilisha maombi ya uhamisho kwenda maeneo mengine kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuungana na wenza wao. Hata hivyo, maombi hayo yanapaswa kuzingatia uwepo wa mahitaji ya rasilimali watu kwa kada husika katika maeneo hayo. Katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2023/2024, jumla ya vibali vya uhamisho 8,846 vimetolewa vikiwemo vya watumishi wa kufuata wenza wao.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inafanya zoezi la tathmini ya mahitaji wa watumishi (HR Assesment), baada ya tathmini hii kukamilika Serikali itajua mahitaji halisi ya watumishi katika maeneo tofauti na kusaidia kufanya msawazo katika maeneo ambayo yatakuwa na upungufu, zoezi hili litasaidia kujaza nafasi katika maeneo yenye upungufu kwa kuzingatia hali ya ndoa. Nashukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya mapitio katika kubaini kaya maskini ili kuondoa malalamiko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, TASAF imekuwa ikitumia utaratibu wa kutambua na kuandikisha kaya maskini kupitia Mkutano Mkuu wa Kijiji, Mtaa au Shehia kwa usimamizi wa watendaji kutoka maeneo ya utekelezaji kwa kuzingatia vigezo vilivyoainishwa na jamii husika.

Mheshimiwa Spika, katika kushughulikia malalamiko ya walengwa, wananchi na viongozi kuhusu utekelezaji wa Mpango wa TASAF imekuwa ikitumia njia mbalimbali ikiwemo kufanya uhakiki ili kuziondoa katika Mpango kaya zilizoimarika kiuchumi. Katika mapitio yaliyofanyika kwenye kaya 750,000 kutoka vijiji, mitaa na shehia 12,000 ilibainika kuwa kaya 394,505 zimeimarika kiuchumi na hivyo kukidhi vigezo vya kuhitimu na kutoka katika Mpango. Aidha, kwa sasa Serikali ipo kwenye maandalizi ya usanifu wa Mpango utakaofuata baada ya Mpango wa sasa kufika katika ukomo hapo Septemba, 2025. Ninashukuru.