Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava (15 total)

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA Aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa wodi ya wazazi utaanza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa Hospitali za Rufaa za Mikoa zinazoboreshwa. Napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba Mshauri Elekezi wa Ujenzi wa Wodi ya Wazazi ameshapatikana, ambaye ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, hatua inayoendelea hivi sasa, ni mchakato wa zabuni ya kupata mkandarasi atakayefanya kazi ya ujenzi, ambapo ujenzi huo unategemewa kuanza mwezi Machi, 2021. Mradi huu utatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza:-

(a) Je, Serikali inawatumia vipi wanafunzi wanaohitimu Shahada ya Science in Industrial Engineering Management katika Uchumi huu wa kati wa Viwanda?

(b) Je, ni wanafunzi wangapi waliohitimu katika fani hiyo wameajiriwa Serikalini tangu mwaka 2019 hadi 2020?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Shahada ya Sayansi katika Menejimenti ya Uhandisi wa Viwanda (Bachelor of Science in Industrial Engineering Management), ilianzishwa mwaka 2015/2016 katika Chuo Kikuu cha Mzumbe. Shahada hiyo ilianzishwa ikilenga kuzalisha wataalam wa kusimamia shughuli za uzalishaji katika viwanda ambavyo vinamilikiwa na Serikali na vile vya mashirika na makampuni binafsi.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2019/2020, wahitimu wengi katika fani hiyo wameajiriwa katika sekta binafsi hususan katika viwanda vya kuzalisha bidhaa kama vile viwanda vya saruji, vinywaji, nguo, sukari, vyakula, mbao, vifungashio, mafuta na kadhalika na katika uchimbaji wa madini. Pia, wahitimu hao wameajiriwa katika taasisi za Serikali zinazoshughulikia masuala ya ubora kwa mfano Shirika la Viwango Tanzania - TBS, Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda-TIRDO, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Taasisi ya Uhandisi na Usanifu wa Mitambo -TEMDO, huduma za viwanda vidogo Vidogo-SIDO na mengineyo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali yetu inatekeleza azma ya ujenzi wa viwanda, yaani uchumi unaoongozwa na viwanda, wahitimu katika fani hiyo walioajiriwa wanatumika katika usimamizi wa shughuli mbalimbali za viwanda vilivyopo katika sekta ya umma na sekta binafsi na hivyo kuleta tija katika uzalishaji na uendeshaji wa taasisi za umma na za binafsi.

(b) Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2019/2020 jumla ya wahitimu wa shahada hiyo walikuwa 228. Kati ya hao, wahitimu 55 walipata ajira. Aidha, kati ya hao 55 waliopata ajira, katika mashirika na taasisi za Serikali ni wahitimu saba.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itazirejesha fedha za ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Msalala zilizorudishwa na mfumo baada ya mwaka wa fedha 2019/2020 kuisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ilipatiwa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Hadi Juni 30 mwaka 2020, Halmashauri hiyo ilikuwa imetumia shilingi milioni 22.4 pekee na hivyo shilingi milioni 477.59 zilirejeshwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti Namba 11 ya Mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2015. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Msalala shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa awamu hadi ujenzi wa hospitali hiyo utakapokamilika.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Kata za Mwamala, Samuye, Busanda, Usule, Bukene na Imesela?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji katika Kata ya Mwamala, Samuye, Busanda, Usule, Bukene na Imesela kupitia mpango wa muda wa kati na muda mrefu. Kwa mwaka wa 2020/2021, kazi zilizofanyika ni pamoja na kufanya usanifu wa matanki mawili yenye lita 100,000 na lita 200,000, mtandao wa kusambaza maji wa urefu wa kilometa 44.8 na vituo vya kuchotea maji 39.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022, ujenzi wa miundombinu ambayo itatumia maji kutoka mradi wa maji wa Masangwa, Ilobashi, Bubale utafanyika ili kuongeza upatikanaji wa maji katika Kata za Mwamala na Samuye.

Aidha, kwa mpango wa muda mrefu ni kutumia maji ya bomba kuu la kutoka Ziwa Victoria kupeleka maji Tinde, Shelui, ambapo kata zote sita zitapata huduma ya maji kwa zaidi ya asilimia 85 ifikapo mwezi Desemba, 2022.
MHE. JERRY W. SILAA K.n.y. MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawapatia maji wananchi wa Vijiji vya Kata za Imasela, Ilola, Lyamidati, Lyabukande na Nyida ambao wapo ndani ya Kilometa 12 kutoka katika mtandao wa maji ya Ziwa Victoria?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa huduma ya maji katika Kata za Imasela, Ilola, Lyamidati, Lyabukande na Nyida zenye jumla ya vijiji 21 ni wastani wa asilimia 49.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa Vijiji vya Kata za Imasela, Ilola, Lyamidati, Lyabukande na Nyida vilivyopo ndani ya Kilometa 12 vinapata huduma ya maji kutoka katika mtandao wa maji ya Ziwa Victoria, Serikali imepanga kupeleka maji Kata ya Imasela kupitia awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa Tinde - Shelui. Utekelezaji wa mradi huo, ulianza mwezi Agosti, 2021 na kwa sasa, umefikia asilimia 15. Natarajia kuwa ifikapo mwezi Agosti, 2022 mradi utakuwa umekamilika.

Aidha, Serikali imepanga kufanya usanifu wa mradi wa maji wa Kata za Ilola, Nyida na Lyamidati ambao utaanza mwishoni mwa mwezi Februari, 2022 na kukamilika mwezi Juni, 2022. Ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Kata ya Lyabukande, usanifu umekamilika kwa ajili ya upanuzi wa mradi wa maji wa Ziwa Victoria katika vijiji vya Mwashagi na Buzinza. Ujenzi wa mradi katika Kijiji cha Mwashagi Kata ya Lyabukande utatekelezwa ndani ya mwaka huu wa fedha kwa kutumia fedha za UVIKO – 19, ambapo Mkataba wa ujenzi ulisainiwa tarehe 07 Januari, 2022 na unatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwezi Juni,2022. Kwa upande wa Kijiji cha Buzinza, utekelezaji wa mradi utaingizwa katika bajeti ya 2022/2023.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, nini chanzo cha vifo kwa akinamama wanaojifungua kwa njia ya upasuaji siku chache baada ya upasuaji?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ufuatiliaji wa vifo vitokanavyo na uzazi uliofanywa na Wizara ya Afya kuanzia mwaka 2018 hadi 2021 umeonesha kuwa vifo ambavyo vilisababishwa na matatizo ya dawa za ganzi (nusu kaputi) na upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni ni 58 yaani 3.3% mwaka 2018; vifo 80 yaani 4.8% mwaka 2019; vifo 65 yaani 4.0% mwaka 2020; na vifo 65 yaani 4.1% mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, sababu kuu za vifo hivi ni nne ambazo ni ajali ya dawa za ganzi/nusu kaputi, kupoteza damu wakati au baada ya upasuaji, tatizo la damu kuganda na maambukizi ya bakteria baada ya upasuaji.

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na vyama vya kitaaluma inatekeleza mkakati wa kuwajengea uwezo watumishi wa vituo vya huduma za afya kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za Taifa katika eneo la utoaji ganzi (nusu kaputi) na upasuaji kwa usalama kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Afya. Ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, kuna utafiti wowote ambao umefanyika ili kubaini dawa za ganzi/nusu kaputi zinazosababisha vifo kwa wanaojifungua kwa upasuaji?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tafiti mbalimbali zilizofanyika zinaonesha kuwa sababu zimegawanyika katika makundi matatu:-

(a) Sababu za vinasaba (DNA);
(b) Sababu zinazohusiana na ganzi ila siyo za moja kwa moja; na
(c) Sababu zenye mahusiano ya moja kwa moja na ganzi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, vifo vya namna hii hutokea mara chache sana na ndiyo maana wakati wote tunawashauri akinamama wajawazito kuhudhuria kliniki ili kutoa muda wa kutosha kufuatiliwa na pale inapohitajika kufanyiwa upasuaji usiwe wa dharura. Aidha, jamii inahamasishwa kutoa lishe bora kwa wajawazito.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga kama ilivyoanishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mhe. Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga ni miongoni mwa miradi ya ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege vinne ambavyo ni Kigoma, Tabora, Sumbawanga na Shinyanga inayotarajiwa kutekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank - EIB).

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa matakwa ya kimkataba kati ya Serikali na EIB yamekamilishwa na mfadhili tayari ameshatoa fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi hii. Aidha, Mhandisi Mshauri pamoja na mkandarasi wameonesha utayari wa kuanza kazi na mikataba kati yao na Serikali ilishasainiwa tangu mwaka 2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi huu umechelewa kuanza kwa wakati, Mhandisi Mshauri pamoja na mkandarasi wameomba ongezeko la fedha katika kipengele cha price adjustment ili kuweza kuendana na mabadiliko ya bei ya bidhaa kwa soko la sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imejipanga kuanza utekelezaji wa mradi huu kabla ya mwaka wa fedha 2021/2022 haujaisha, nah ii itatokana na endapo mkandarasi atawasilisha hati ya dhamana ya malipo ya awali kwa wakati. Ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Kahama – Solwa hadi Mwanza kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Kahama – Solwa hadi Mwanza kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha ambapo kipande cha kilometa 5.65 kuanzia Kahama kuelekea Solwa pamoja na kipande cha mita 540 katika Mji Mdogo wa Bulige tayari imejengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 750.62 kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 1.2 kati ya Solwa na Bulige ambapo mkandarasi tayari amepatikana na amekabidhiwa mradi ili kuanza kazi. Kazi imepangwa kukamilika mwezi Septemba, 2023.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara hii kwa awamu hadi kukamilika yote kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaipandisha hadhi Zahanati ya Solwa kuwa Kituo cha Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii mbele ya Bunge lako Tukufu kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa kufanya ukaguzi na kutoa ushauri wa kitaalamu katika Zahanati ya Solwa ili kuona kama inakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pindi Mkoa utakapojiridhisha na miundombinu iliyopo, watawasilisha ombi hilo Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Wizara ya Afya kwa ajili ya hatua za kuipandisha hadhi Zahanati ya Solwa na kuwa Kituo cha Afya.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kutoka Old Shinyanga kupitia Iselamagazi, Solwa hadi Salawe kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sehemu ya Solwa - Salawe yenye urefu wa kilometa 15.35. Kwa sehemu iliyobaki kutoka Solwa kwenda Iselamagazi hadi Old Shinyanga yenye urefu wa kilometa 64.66 kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inaendelea. Baada ya kazi ya usanifu kukamilika na gharama ya ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha ili kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, ni kuna mpango gani wa kukarabati skimu ya umwagiliaji ya Masengwa-Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu ya Masengwa iliyopo Kata ya Masengwa Wilaya ya Shinyanga, Mkoani Shinyanga inachangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa zao la mpunga na mbogamboga kupitia kilimo cha umwagiliaji. Skimu hii ina uwezo wa kumwagilia hekta 540. Kutokana na uchakavu wa mfereji mkuu wa skimu hiyo eneo linalomwagiliwa kwa sasa ni hekta 133. Aidha, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kupitia wataalamu wake wa ndani waliopo katika ngazi ya Wilaya na Mkoa wanaendelea na kazi ya kubaini mahitaji halisi ya ukarabati wa skimu hii ili iweze kuwekwa katika mpango wa bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha ahadi yake ya kuifanya Zahanati ya Solwa iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kuwa kituo cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Zahanati ya Solwa ilianza kutoa huduma mwaka 1964. Aidha, eneo ilipojengwa zahanati lina ukubwa wa ekari 1.5 ambalo halitoshelezi kwa ujenzi wa miundombinu ya kituo cha afya.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeelekeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kutafuta eneo lenye ukubwa wa kuanzia ekari 15 ambalo litawezesha ujenzi wa kituo cha afya, ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga uzio katika Shule ya Wasichana ya Abdulrahim Busoka ya kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2021/2022 mpaka 2023/2024, Serikali Kuu imepeleka shilingi milioni 166.4 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa saba na matundu ya vyoo nane katika Shule ya Wasichana ya Abdulrahim Busoka kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2024/2025 Serikali kwa kushirikana na Barrick Tanzania itatoa kiasi cha shilingi milioni 227.2 kwa ajili ya kujenga bweni moja, madarasa matatu na matundu sita ya vyoo. Serikali inatambua umuhimu wa uzio kwa ajili ya ulinzi wa mali na wanafunzi wa bweni.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa sasa kipaumbele cha Serikali kuu ni ujenzi wa miundombinu ya msingi inayowezesha kuongeza nafasi za udahili wa wanafunzi.
MHE. DKT.CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango mkakati gani juu ya Kiwanda cha Nyama kilichopo Shinyanga ambacho hakifanyi kazi iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Nyama cha Shinyanga ni miongoni mwa viwanda vitatu vya nyama vilivyokuwa vinamilikiwa na Kampuni ya Tanzania Packers Limited (TPL). Kiwanda kilianza kujengwa mwaka 1975 na kukamilika mwaka 1978 kwa 84% ila kiwanda hakijawahi kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Nyama cha Shinyanga kilibinafsishwa kwa Kampuni ya Triple S Beef Limited, mwaka, 2007. Hata hivyo, mwekezaji hakuweza kuendeleza kiwanda hicho kulingana na makubaliano ya mkataba wa ubinafsishaji, jambo lililosababisha Serikali kuamua kukirejesha mwaka 2017 na kwa sasa kiwanda kipo chini ya usimamzi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta mwekezaji mahiri mwenye nia thabiti ambaye atawekeza katika kiwanda hicho ili kiweze kufanya kazi iliyokusudiwa kwa maslahi ya Taifa.