Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Godwin Emmanuel Kunambi (15 total)

MHE. NAPE M. NNAUYE (K.n.y. MHE. GODWIN E. KUNAMBI) aliuliza: -

Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba ni Halmashauri mpya iliyotoka Wilaya ya Kilombero: -

(a) Je, ni lini Serikali itaipa Mlimba hadhi ya kuwa Wilaya hasa ikizingatiwa umbali mrefu wa takriban Km 200 ambao Wananchi wanatembea kufuata huduma Makao Makuu ya Wilaya?

(b) Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa majengo ya Halmashauri na kuboresha miundombinu ya barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa miongozo na taratibu, uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala unahusisha uhitaji wa wananchi, Viongozi wa Wilaya na Mkoa ambao huwasilisha maombi ya mapendekezo yao kwenye vikao vya Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na kisha kuwasilishwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa hatua zaidi. Ofisi ya Rais-TAMISEMI, haijapokea maombi rasmi ya Mkoa wa Morogoro kuomba Mlimba kuwa Wilaya. Serikali inashauri utaratibu huu uliowekwa ufuatwe.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba. Mwezi Januari mwaka huu, Serikali imekwisha peleka kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuanza shughuli za ujenzi wa jengo hilo la utawala.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa miundombinu ya barabara, katika mwaka wa fedha 2019/ 2020, Serikali imefanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 54, imejenga kalvati 22 na madaraja manne (4) kwa gharama ya shilingi milioni 545.87. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali kupitia TARURA imetenga kiasi cha shilingi milioni 517.56 kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba.
MHE. NAPE M. NNAUYE K.n.y. MHE. GODWIN E. KUNAMBI Aliuliza: Serikali ina mpango wa kuunganisha mikoa yote kwa mtandao wa barabara za lami, ikiwemo barabara yenye urefu wa kilometa 223 inayounganisha Mikoa ya Njombe na Morogoro kupitia Mlimba ambayo pia iko katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM):-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara anayozungumzia Mheshimiwa Mbunge ni Barabara ya Ifakara – Mlimba – Taweta – Madeke yenye urefu wa kilometa 220.22 ambayo ni barabara ya mkoa inayosimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu ya kutoka Ifakara hadi Kihansi (kilometa 126) ili kuunganisha na kipande cha barabara ya lami (kilometa 24) kilichojengwa hapo awali kati ya Kihansi na Mlimba.

Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sehemu iliyosalia kati ya Kihansi na Madeke (kilometa 94.2) umepangwa kufanyika katika mwaka huu wa fedha wa 2020/2021 kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Kazi hii ipo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kumpata Mhandisi Mshauri.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ina kamilisha usanifu wa kina, imeendelea kutenga fedha na kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika kipindi chote cha mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2020/2021, jumla ya shilingi bilioni 2.29 zimetengwa. Ahsante.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya mashamba pori yasiyoendelezwa Mkoani Morogoro?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwezi Julai 2020 hadi Julai 2021, jumla ya mashamba 160 yamekaguliwa katika Mkoa wa Morogoro. Kati ya mashamba hayo, mashamba 123 yapo Kilosa, Kilombero (3), Mvomero (13) na Morogoro (21). Aidha, mwezi Aprili, 2021 Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan, amebatilisha umiliki wa mashamba 11 yenye ekari 24,159 kutokana na wamiliki wake kukiuka masharti ya umiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafanya utaratibu wa kuyapanga na kuyapima kwa ajili ya matumizi ya wananchi, uwekezaji na ardhi ya akiba na hivi sasa wataalam wanaofanya kazi hiyo wako kwenye maeneo hayo. Kwa sasa Serikali inaendelea na ukaguzi wa mashamba mengine katika Wilaya za Morogoro, mashamba 44 na Mvomero, mashamba 86. Baada ya ukaguzi huo hatua za kisheria zitafuata kwa wamiliki watakaokiuka masharti ya umiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa ukaguzi na uhakiki wa mashamba katika Mkoa wa Morogoro ni zoezi endelevu likiwa na maslahi mapana ya Taifa ya kuhakikisha kuwa tunaondoa migogoro inayojitokeza kwa kuwepo mashamba yasiyoendelezwa ipasavyo.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, ni lini Ujenzi wa Barabara ya Ifakara – Kihansi – Madeke utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Ifakara – Kihansi hadi Madeke yenye kilometa 220.22 ni sehemu ya barabara ya Ifakara – Mlimba – Taweta – Madeke – Lupembe hadi Kibena Mkoa wa Njombe ambayo ni barabara ya mkoa inayounganisha mikoa ya Morogoro na Njombe katika Kijiji cha Madeke.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kuandaa nyaraka za zabuni kwa sehemu ya Ifakara hadi Kihansi yenye urefu wa kilometa 126. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza maandalizi ya kutangaza zabuni kwa ajili ya kupata Mkandarasi wa ujenzi wa kilometa 50 kati ya Ifakara hadi Mlimba kwa kiwango cha lami ndani ya mwaka wa fedha wa 2021/2022. Aidha, kipande cha barabara kati ya Kihansi na Mlimba chenye urefu wa kilometa 24.26 kimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, sehemu iliyobaki itaendelea kujengwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha hadi barabara yote ikamilike kwa kiwango cha lami. Pamoja na juhudi hizi, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali ili kuhakikisha inapitika majira yote ya mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya shilingi bilioni 2.729 zimetengwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua migogoro ya wakulima na wafugaji katika Jimbo la Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa changamoto mbalimbali zinazosabisha migogoro ya matumizi ya ardhi ikiwemo hiyo ya wakulima na wafugaji. Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha migogoro ya matumizi ya ardhi katika Mkoa wa Morogoro hususan Wilaya ya Kilombero inatatuliwa.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kumilikisha ardhi kupitia Mradi wa Kuwezesha Umilikishaji wa Ardhi (LTSP) ambapo jumla ya vijiji 58 viliandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi na Hakimiliki za Kimila 150,006 zilisajiliwa. Kati ya vijiji hivyo 58, vijiji 32 vipo katika Halmashauri ya Mlimba ambapo jumla ya Hakimiliki za Kimila 41,797 zimesajiliwa na 30,699 zimechukuliwa na wananchi.

Mheshimiwa Spika, nasisitiza Serikali za Halmashauri kuhakikisha zinasimamia mipango ya matumizi ya ardhi iliyoandaliwa ili kupunguza uwezekano wa kuibuka au kuendelea kwa migogoro baina ya watumiaji wa ardhi.

Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni kudhibiti na kuimarisha mbinu za utatuzi wa migogoro kwa kutoa elimu kupitia mikutano ya wananchi kuhusu mipango ya matumizi ya ardhi iliyowekwa kwa pamoja, kutungwa kwa Kanuni za Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi na kuhimiza matumizi ya ardhi yenye tija.

Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara kwa kushirikiana na Wizara nyingine za kisekta zitaendelea kudhibiti na kushughulikia migogoro na kuitafutia ufumbuzi iliyopo ili kuimarisha ustawi wa jamii baina ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA K.n.y. MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, ni watumishi wangapi wamesimamishwa kazi tangu mwaka 2015 hadi 2022 ambao mashauri yao hayajaisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, usimamizi wa nidhamu katika Utumishi wa Umma ni suala muhimu ambalo limeainishwa katika Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298; Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003; Taratibu za Uendeshaji katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2003; Taratibu Bora za Nidhamu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2007 na Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2015 hadi mwaka 2022, idadi ya watumishi waliosimamishwa kazi katika Taasisi mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa, pamoja na Serikali Kuu ambao mashauri yao hayajahitimishwa ni watumishi 836. Watumishi hawa ni miongoni mwa watumishi 1,477 waliokuwa wamesimamishwa kazi kwa kukiuka sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia nidhamu katika Utumishi wa Umma. Mashauri haya yapo katika hatua mbalimbali za mamlaka za nidhamu ambazo ni waajiri mbalimbali na mamlaka za rufaa ambazo ni Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Walimu na Ofisi ya Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuwakumbusha Waajiri/Mamlaka za Nidhamu kuongeza kasi ya kuhitimisha mashauri ya nidhamu yaliyopo kwa kuzingatia taratibu za uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE K.n.y. MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, ni lini mgogoro wa mipaka kati ya Vijiji vya Utengule, Ovindembo, Ipinde, Tanganyika na Kampuni ya Kilombero North's utatatuliwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi Mbunge wa Jimbo la Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Uwindaji ya Kilombero North’s Limited imekodishwa Kitalu cha Uwindaji cha Mlimba North’s ambacho ni sehemu ya Bonde la Mto Kilombero. Maeneo ya kitalu hicho ni chanzo muhimu cha maji yanayoingia katika Mto Kilombero ambayo pia yanachangia katika Mradi wa Kitaifa wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Eneo la Kitalu cha Uwindaji cha Mlimba ni moja kati ya maeneo yanayoshughulikiwa na Kamati ya Mawaziri nane inayofanyia kazi migogoro hiyo iliyopo katika vijiji 975. Kufuatia Kamati hiyo, timu ya wataalamu ya Kitaifa inayohusika na utatuzi wa migogoro kwa kushirikiana na Mkoa wa Morogoro na Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga imeshakwenda kwenye eneo lenye mgogoro huo kwa lengo la kufanya tathmini na kubaini maeneo halisi yanayostahili kuhifadhiwa kwa maslahi mapana ya Taifa na maeneo mengine wataachiwa wananchi ili waendelee kufanya shughuli zao ikiwemo kilimo, makazi na ufugaji.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, lini vituo vidogo vya treni vya Njage na Itongowa katika reli ya TAZARA vitarejeshwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAZARA ilipokea barua za maombi ya kufunguliwa kwa vituo vidogo vya Njage na Itongowa katika vipindi tofauti tangu mwaka 2022. Tathmini iliyofanywa ilibainisha yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kidogo cha Itongowa. Kituo hiki kinachoombwa kuanzishwa kipo kati ya Stesheni kubwa za Chita na Mngeta. Katikati ya Stesheni mbili hizo za Chita na Mngeta kipo kituo kidogo cha siku nyingi cha Ikule. Kituo hiki cha Ikule kipo kilometa sita kutoka aidha Chita ama Mngeta. Kituo cha Itongowa kinachoombwa kuanzishwa kitakuwa kilometa sita kutoka Mngeta stesheni au kilometa saba kutoka Ikule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kidogo cha Njage. Kituo hiki kinachoombwa cha Njage kipo kati ya Stesheni kubwa za Mngeta na Mbingu ambazo treni za abiria zinasimama. Umbali kati ya stesheni hizo ni kilometa 18 yaani Mngeta na Mbingu. Kitongoji cha Njage kipo katikati Mngeta na Mbingu yaani kilometa tisa kutoka kila upande, Mngeta au Mbingu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Wizara imeelekeza sasa TAZARA ifanye tathmini ya haraka kwa kina kuona uwezekano wa kuanzisha vituo hivi vilivyoombwa na Mheshimiwa Mbunge ili wananchi wasitembee umbali mrefu.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa majengo yaliyobaki ya Kituo cha Afya Mlimba utakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Jimbo la Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali ilitenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi mbili; jengo la upasuaji na nyumba ya mtumishi katika Kituo cha Afya Mlimba. Ujenzi wa majengo hayo umekamilika na kwa sasa kituo kinatoa huduma katika ngazi ya kituo cha afya ikiwemo huduma za upasuaji wa dharura wa akina mama wajawazito.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itakamilisha ujenzi wa majengo yaliyobaki ya Kituo cha Afya Mlimba, kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kuhusu ujenzi wa barabara ya Mafinga hadi Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nami kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako kama Naibu Waziri wa Ujenzi, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, maana ametoa kibali hiki. Nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini ili niweze kumsaidia katika nafasi ya Unaibu Waziri wa Ujenzi, pia nikuahidi kwamba nitatoa ushirikiano wa hali ya juu kwa Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nijibu swali. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara inayoanzia Mafinga, eneo la Kinyanambo ‘C’ hadi Kihansi (Mlimba) yenye urefu wa kilometa 126.39, ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya milioni 250 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Baada ya kukamilika usanifu na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi. Ahsante.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, lini mgogoro wa ardhi wa Shamba la Kambenga utatatuliwa?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Kijiji cha Namwawala ilimpatia Ndugu Kassim Seif Kambenga ardhi yenye ukubwa wa ekari 1,000 mwaka 1989. Mgogoro uliibuka miaka ya 2000 baada ya Serikali ya Kijiji cha Namwawala kugawa ekari 900 kati ya 1,000 kwa wananchi wengine kutokana na ndugu Kambenga kufanya upimaji wa awali na kukamilisha umilikishwaji wa ekari 100 tu. Mgogoro huu ulifikishwa kwenye vyombo vya sheria hususan Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya kupitia Shauri Na. 2/2007 na Mahakama Kuu (Kitengo cha Ardhi) kupitia Shauri Na. 2/2012 ambapo Kassim Seif Kambenga alipewa ushindi kuwa ni mmiliki halali wa shamba lenye ekari 1,000.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mahitaji ya ardhi ya wananchi wanaozunguka shamba hilo, Serikali kupitia uongozi wa Wilaya na Mkoa inaendelea na mazungumzo na familia ya ndugu Kassim Seif Kambenga ili akubali kumega kiasi cha shamba lake kwa ajili ya kuwapatia wananchi. Hivyo, wananchi wanaombwa kuwa na subira wakati Serikali inapoendelea kushughulikia suala hili.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro kati ya wananchi na TAWA katika Bonde la Mto Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Jimbo la Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza kutekeleza maamuzi yaliyotolewa na Baraza la Mawaziri tangu Oktoba, 2021. Utekelezaji wa maamuzi hayo ulianza katika mikoa yenye migogoro ikiwemo Mkoa wa Morogoro hususan Pori Tengefu la Kilombero. Timu ya Wataalam ya Kitaifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi iko uwandani, inaendelea na zoezi la tathmini kwa kushirikisha mkoa, wilaya na wananchi wa maeneo hayo. Aidha, timu hiyo inafanya tathmini ya makazi na shughuli zenye athari kwenye uhifadhi wa vyanzo vya maji na rasilimali za wanyamapori ndani ya eneo la Pori Tengefu na Bonde la Mto Kilombero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utatuzi wa migogoro hiyo utaanza baada ya tathmini kukamilika.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza:-

Je, lini Mradi wa Umwagiliaji wa Udagaji katika Kata ya Ching’anda Mlimba utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Jimbo la Mlimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Skimu ya Umwagiliaji ya Udagaji/Mgugwe yenye ukubwa wa hekta 1,280 ni miongoni mwa skimu tatu za Bonde la Mto Kilombero ambazo zilifanyiwa upembuzi yakinifu na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) mwaka 2016. Skimu zingine zilizofanyiwa upembuzi yakinifu kupitia ufadhili huu ni Mpanga, Ngalamila yenye ukubwa wa hekta 28,141 na Kisegese yenye ukubwa wa hekta 16,130 zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba katika Bonde la Mto Kilombero.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga bajeti kwa ajili ya kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu na kufanya usanifu wa kina wa skimu hizo. Aidha, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ipo katika hatua za manunuzi na kumpata Mshauri Elekezi wa kutekeleza kazi husika. Hivyo, ujenzi wa Skimu ya Udagaji Mlimba unatarajiwa kuanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 baada ya kukamilika kwa kazi ya usanifu wa kina ili kubaini gharama halisi za ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, lini Serikali itarejesha eneo lililokuwa linamilikiwa na RUBADA kwa wananchi wa Utengule – Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shamba Namba 949 linalojulikana kwa jina la Ngalimila lina ukubwa wa hekta 5,128.483 (sawa na ekari 12,820). Shamba hili lipo Mkoa wa Morogoro katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba katika Kata ya Utengule. Shamba hili limezungukwa na Vijiji vya Ngalimila, Ipugasa, Ngombo, Mpanga, Miembeni na Viwanja Sitini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya mwaka 2009 ardhi hii ilikuwa inamilikiwa na Kijiji cha Ngalimila ambapo tarehe 18 Mei, 2009 kilifanyika kikao maalum kwa ajili ya kujadili maombi ya ardhi kwa ajili ya RUBADA kutoka kijiji cha Ngalimila kwa ajili ya uwekezaji. Wanakijiji walikubali kutoa ardhi hiyo kutokana na manufaa ambayo walielezwa yangepatika na kutokana na uwekezaji mkubwa katika kilimo cha mpunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 16 Aprili, 2014 iliandaliwa taarifa ya kusudio la kuhaulisha ardhi ya kijiji kuwa ya kawaida. Baada ya RUBADA kufutwa, mali mbalimbali ikiwemo shamba la Ngalimila zilirejeshwa Wizara ya Fedha na Mipango na kuwa chini usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia ardhi ya shamba hili kutoendelezwa kwa muda mrefu, Serikali ilipokea maombi ya wananchi kurejeshewa shamba hili. Hata hivyo, uchambuzi wa maombi hayo ulibaini kuwa eneo lenye ukubwa wa hekta 1,820.494 sawa na asilimia 35 ya shamba hilo lipo katika eneo la Pori Tengefu la Kilombero. Aidha, ili kufika katika shamba hili, sharti kuvuka Mto Mpanga na Mto Mnyera ambayo ndiyo chanzo cha kupeleka maji katika mradi wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme wa maji wa Julius Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa wananchi wanaotumia shamba hili kwa sasa ambao ni wavamizi kutokuweka miundombinu ya kudumu ili kuepusha hasara inayoweza kujitokeza endapo Serikali itatoa maamuzi tofauti na maombi yao. Aidha, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa suala hili litashughulikiwa na kutolewa maamuzi kwa uharaka unaohitajika kwa maslahi mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla, ahsante. (Makofi)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Mradi wa Umwagiliaji katika Bonde la Mto Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2016 Serikali ilifanya upembuzi yakinifu wa awali (prefeasibility) wa miradi ya umwagiliaji katika bonde la Kilombero lenye ukubwa wa hekta 53,344 ambapo skimu za Kisegese, Udagaji, Mgungwe na Mpanga - Ngalamila zilihusishwa katika kazi hiyo. Upembuzi yakinifu wa awali ulibaini kuwa kuendelezwa kwa skimu hizo kutanufaisha kaya 15,102 na kutoa ajira 69,476.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina (feasibility study and detailed design) wa miradi ya umwagiliaji katika Bonde la Mto Kilombero kupitia Mshauri Elekezi ambaye yupo eneo la kazi. Baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, bonde hilo litaingizwa katika mpango wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.