Supplementary Questions from Hon. Godwin Emmanuel Kunambi (26 total)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali moja la nyongeza. Kama alivyojibu Mheshimiwa Waziri, barabara hii ni barabara ya kitaifa yaani National Road na ni barabara inayounganisha Mkoa wa Njombe na Morogoro. Kutoka hapo Ifakara sehemu moja mpakani mwa Njombe na Morogoro, Mto Mfuji kuna kilomita takribani 225 na kwa kuwa barabara hii ni muhimu na ni barabara ya kitaifa, je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara kutoka Ifakara ng’ambo ya mto Lumemo kwenda kupita Mlimba, kwenda Mfuji, Madeke Njombe?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna haja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu…
NAIBU SPIKA: Hilo ni swali la pili? Au hilo hilo la kwanza?
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu aliwahi kufanya ziara Jimbo la Mlimba na katika ziara yake aliahidi ujenzi wa kilomita 60. Je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii walau kwa kilomita hizo 60?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Asenga kwa juhudi ambazo anazifanya katika kufuatilia barabara hii ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Kilombero wanafaidika na barabara hii ya lami ambayo wanaifuatilia. Baada ya maneno hayo, nitoe tu jibu la jumla, kwamba katika hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati wa kuzindua Bunge hili la Kumi na Mbili, ukurasa wa 26 na 27, Mheshimiwa Rais ameahidi kwamba barabara zenye urefu kilomita 2500 ambazo zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami zitakamilishwa katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ameenda mbali zaidi kwenye hotuba kwamba pia barabara zingine ambazo zitaanza kujengwa zenye urefu wa kilomita 6006 ikiwepo barabara hii pia zitakamilishwa ambazo ni zile ambazo ziko kwenye ilani lakini na ahadi zake mwenyewe. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba hizi barabara Serikali itazikamilisha kama ilivyoahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, wananchi wa Jimbo la Mlimba ukiwauliza tatizo lao kubwa ni barabara unaweza kuacha yote lakini barabara ni kipaumbele cha kwanza.
Naomba niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo kwa niaba ya wananchi wa Mlimba; ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi rasmi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Ifakara - Ng’ambo - Mto Lumemo mpaka Lupembe Madeke yenye urefu wa kilometa 223? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Kunambi, Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ambayo ambayo ameitaja inayoanzia Mikumi, Ifakara, Mlimba, Madeke hadi Lupembe na hadi Kibena Junction ni barabara inayounganisha mikoa miwili na imetengewa fedha kwenye bajeti ambayo itaanza kutekelezwa kuanzia upande wa Njombe na kuanzia upande wa Jimbo lake kwenye sehemu mbili.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mara bajeti itakapoanza kutumika kama tulivyoahidi kwenye bajeti barabara hiyo itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Kwa kuwa Mkoa wa Morogoro ni Mkoa pekee nchini ambao haujaunganishwa kwa kiwango cha lami na mikoa mitatu; Mkoa wa Lindi, Mkoa wa Ruvuma, na Mkoa wa Njombe.
Sasa swali langu dogo la nyongeza ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye kilometa 223 kutoka Ifakara – Mlimba mpaka Madeke -Lupembe – Njombe? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Godwin Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kunambi kwa kufuatilia hiyo barabara. Mikoa aliyoitaja ni kweli barabara hazijaunganishwa kwa kiwango cha lami, lakini barabara zipo japo zinapitika kwa shida sana.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kunambi kwamba katika bajeti tunayoanza kuitekeleza atakubaliana nami kwamba Serikali imetenga fedha kuanza ujenzi wa barabara hiyo ya kuanzia Ifakara – Mlimba – Madeke mpaka Kibena Junction kwa kiwango cha lami.
Kwa hiyo, kwenye bajeti tunayoanza kuitekeleza naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kunambi na wapiga kura wa Jimbo la Mlimba kwamba Serikali imejipanga utekelezaji kwa kiwango cha lami wa barabara hiyo utaanza. Ahsante. (Makofi)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa kuwa changamoto ya wananchi wa Chwaka inafanana kabisa na ya wananchi wa Jimbo la Mlimba, kwenye Kituo cha Polisi cha Mlimba: Je, Mheshimiwa Waziri haoni hayo magari yatakapofika katika mpango wake, basi aweze kukumbuka pia na Kituo hiki cha Polisi Mlimba? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Godwin Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli tunafahamu kwamba changamoto hii, kama nilivyosema, iko katika vituo vingi. Naamini hata Kituo cha Polisi cha Mlimba ambacho kina hadhi ya Kituo cha Wilaya kina changamoto kubwa sana ya gari. Kwa kawaida hata angalau magari yakipungua sanakwenye Kituo cha Wilaya, yanapaswa kuwa angalau matatu au manne, lakini pale kuna gari moja na lingine bovu.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo yenye changamoto za miundombinu, changamoto za shughuli za uzalishaji ndiyo zitapewa kipaumbele magari haya yatakapofika.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; ni lini Serikali itatatua mgogoro wa Shamba la Balali lenye ekari 2,000? Kwa sasa shamba lile yapata takribani miaka 20 Balali hajaliendeleza na wananchi wamekuwa wakilima humo. Ni lini sasa Serikali itafuta hati ya Balali na umiliki ule kupewa wananchi wa Jimbo la Mlimba, Kata ya Chita, pale Melela?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni lini Serikali itatatua mgogoro wa Shamba la Kambenga? Ahsante.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba marehemu Balali alikuwa anamiliki, sasa hivi msimamizi wa mirathi ambaye ni mke wake anamiliki shamba hilo alilolisema na nafahamu kwamba halijaendelezwa. Hata hivyo, Serikali ilifanya jitihada za kumtafuta yule mwekezaji na kumpa notisi, akajieleza, lakini bado tulichukua hatua ya kutaka kuchukua sehemu ya shamba hilo ili wananchi waweze kunufaika na yeye kumpa mpango wa muda mfupi aweze kuliendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya wakati wa kupima hilo shamba wananchi hawakuelezwa vizuri, walifikiri wale wapimaji wanakwenda kumsaidia yule mwenye shamba wakachoma vifaa na magari yaliyokuwa yanatumika kwa kazi ile ya Wilaya ya Kilombero, ni bahati mbaya sana. Kwa hiyo tunachukua hatua nyingine, nimeelekeza kule kwamba sasa tutapeleka notisi ya kumwomba huyu mwenye shamba ajieleze, lakini pia tunafikiria namna ya mwenye shamba kuweza kulipa fidia ya vifaa na mali zilizopotea katika kutekeleza jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili jambo nalifahamu vizuri na nikiwa nje nitamweleza mengine ambayo yalisababisha hili, lakini kwa hapa itoshe tu kwamba Serikali inalitambua na tunachukua hatua juu ya shamba hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; Shamba la Kambenga lilikuwa na mgogoro na vijiji na bahati mbaya sana mkuu wa mkoa aliyepita aliunda timu. Wizara yangu ilitaka kuingilia lakini Mkuu aa Mkoa mpya aliyekuja ameniomba muda kidogo atafsiri ile taarifa ya Kamati aliyoiunda mwenzake. Baada ya taarifa hiyo tutaamua, nilishaamua kumpeleka Kamishna kule, lakini nilisitisha kidogo baada ya maombi ya Mkuu wa Mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo yote haya mawili nayajua, yako ndani ya uwezo wa Wizara. Naomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kukumbushana tutayashughulikia haya yote mawili.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa changamoto ya wananchi wa Nanyumbu inafanana kabisa na changamoto ya wananchi wa Jimbo la Mlimba pale Kata ya Mchombe.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Mchombe tayari tuna majengo pale. Huko awali kulikuwa na kituo kidogo cha VETA na vijana walikuwa wakijifunza pale, sasa kituo kile kilifungwa na majengo yale hayatumiki.
Je, Wizara haioni umuhimu inavyoenda kufanya tathmnini Nanyumbu hiyo timu ya wataalamu ikafanya pia tathmini pale Mlimba Mchombe, kwa sababu majengo ya Serikali yanaendelea kuharibika tu?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kunambi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama ulivyoeleza kwenye utangulizi wako Mheshimiwa Kunambi nadhani wakati tunaunda hii timu kwa vile barabara ni hiyo hiyo moja ya kwenda Nanyumbu nadhani ni lazima tupite Morogoro, tutaona busara itakavyotutuma nadhani timu hii itapita katika eneo hilo. Ahsante sana.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kupitia bajeti ya mwaka huu wa fedha (2021/2022), Serikali imepamga kujenga barabara kwa kiwango cha lami Morogoro - Njombe Boda walau kwa kuanza na kilomita 50. Swali langu: Je, ni lini Serikali itatangaza zabuni walau ujenzi huu uanze kwa kilomita 50 hizi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Godwin Kunambi, Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge nataka nikuhakikishie kwamba barabara zote ambazo zimetengewa fedha tayari ziko kwenye michakato ya manunuzi. Kwa hiyo, mara tu hizo hatua zitakapokamilika, nikuhakikishie kwamba zitatangazwa kwa ajili ya kuanza ujenzi. Ahsante.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara ya Morogoro – Njombe – Boda, umuhimu wake inaunganisha Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na ni barabara inayotoa alternative, yaani ni barabara mbadala kwa Mikoa ya Mbeya - Iringa - Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu dogo la nyongeza ni kwamba, barabara hii ina urefu wa kilomita takribani 222 na kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha zimetengwa fedha ili ujenzi uanze walau kilomita 50; na taarifa nilizonazo, imeshapata kibali: Ni lini sasa Wizara itaanza utekelezaji wa barabara hii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GEOFREY G. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunambi, Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema, taratibu za manunuzi zinaendelea na mara zitakapopatikana, basi kilomita hizo zitaanza kujengwa. Siwezi nikasema ni lini na tarehe gani, kwa sababu taratibu za manunuzi zina utaratibu wake, zinaweza zikachukua wiki au mwezi. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii itaanza kujengwa katika kipindi hiki cha bajeti. Ahsante. (Makofi)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Naomba niulize kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara hii inaunganisha mikoa ya nyanda za juu kusini; Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Njombe, Mkoa wa Ruvuma, Mkoa wa Mbeya mpaka Rukwa na inatoa alternative route ya barabara ya Iringa - Morogoro yaani kupitia Kitonga. Sasa katika majibu ya Serikali, ameeleza kwa habari ya kipande cha kutoka Ifakara mpaka Kihansi, kuna kipande cha kutoka Kihansi kwenda Masagati - Madeke mpaka Kibena Junction; kipande hiki, zabuni ya kumtafuta Mkandarasi wa kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ilitangazwa mwaka wa fedha uliopita, hadi sasa hajapatikana.
Mheshimiwa Spika, swali langu sasa: -
(a) Ni lini sasa Serikali inakwenda kukamilisha kazi hii ya kumpata Mkandarasi huyo?
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa za nchi yetu, Mikoa mingi haijaunganishwa kwa lami; swali langu lingine ni kwamba:-
(b) Ni lini Serikali inakwenda kuunganisha mikoa hii michache ambayo haijaunganishwa kwa lami, ukiwemo Mkoa wa Morogoro?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunambi Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama alivyosema, ni lini tunakwenda kuunganisha mikoa yote? Ndiyo kazi inayoendelea. Hata katika jibu la msingi, ndiyo maana hata hii barabara tunaiunganisha kati ya Morogoro na Njombe.
Kwa hiyo, tunaendelea na ni kipaumbele kikubwa sana kwa Serikali kuhakikisha kwamba mikoa hii inaunganishwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, Mbunge jitihada unaziona, tayari tunatangaza tender katika kuhakikisha kwamba hizi barabara zinaunganishwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Mkandarasi upande pili wa kutoka Lupembe - Madeke kuja Taveta, tender inatangazwa tena baada ya kukosa Mhandisi Mshauri. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba taratibu zinaendelea na Mkandarasi na Mshauri atakapopatikana, ataanza kufanya kazi ya kufanya ufanifu wa barabara hiyo. Ahsante.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba imeanza ujenzi wa Kituo cha Afya kwa mapato ya ndani, na jengo la la wagonjwa wa nje (OPD) limekamilika. Sasa ni nini mpango wa Serikali kuisaidia halmashauri hiyo kukamilisha majengo yaliyobaki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Godwin Kunambi, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa ujenzi wa vituo vya afya unahusisha nguvu za wananchi katika michango yao na kujenga vituo hivyo. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kwanza kuwapongeza sana wananchi wa Jimbo hili la Mlimba, ambako Mheshimiwa Kunambi ndiye Mbunge, kwa kazi nzuri na kubwa ambayo wameifanya ya kujenga kituo cha afya. Nimhakikishie, kwa awamu tutatafuta fedha ili kuhakikisha kwamba tunakamilisha miundombinu ambayo inabaki.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwakuwa Serikali imetangaza zabuni ya ujenzi wa barabara ya Morogoro, Njombe boda walau kwa kilometa 100 route one na route two. Je ni lini kazi hii itaanza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ipo kwenye hatua za manunuzi. Najua Mheshimiwa Mbunge anaifuatilia; ipo kwenye hatua za manunuzi kwa ajili ya kuanza kuijenga hiyo barabara kwa hivyo ipo kwenye hatua mbalimbali za manunuzi ili iweze kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. EMMANUEL KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali langu la kwanza, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba ina vijiji 62; na katika mpango wa Land Tenure Support Programme, vijiji 30 tu vilifanyiwa kazi: Je, ni lini Serikali inakwenda kukamilisha kazi hii ya vijiji 32 vilivyobaki?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari mara baada ya Bunge hili kuambatana nami kwenda kufanya ziara ndani ya Jimbo langu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Kunambi maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, la kwanza naomba kukiri mbele ya Bunge lako kwamba kweli ule mkakati ulipofanyika mara ya kwanza, yaani ile programme ya LSTP ulipita katika vijiji 32 ndani ya Halmashauri ya Mlimba ambayo ina vijiji 62. Nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tumeshatenga fedha, basi tutakwenda kwa ajili ya kumalizia vijiji hivyo vilivyobakia kwa sababu programme hii ili kuwa ni kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, la pili nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya Bunge kwisha tutakwenda pamoja katika Halmashauri yake ili Kwenda kujadili siyo tu matatizo haya ya mipango ya matumizi bora ya ardhi, lakini pia na kutatua kero nyingine zinazoendelea katika maeneo ya matumizi ya ardhi. (Makofi)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kuhusu ujenzi wa barabara ya Morogoro - Njombe boarder Serikali imedhamiria kujenga kilometa 100 kwa maana ya lot one na lot two.
Swali naomba Serikali ithibitishie Wananchi wa Mrimba je, ni lini hizi kilometa 100 kwa lot zote hizi mbili zitaanza kujengwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tunavyosema sasa hivi zabuni zimeishaandaliwa na tuko kwenye hatua za mwisho kutangaza hizo lot mbili ambayo ndiyo barabara inayokwenda kuunganisha na barabara ya Kibena - Madeke, ahsante. (Makofi)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali moja dogo la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na changamoto kubwa kwa watumishi wa umma hasa hawa ambao mashauri yao yanaendelea kusikilizwa kwamba yanachukua muda mrefu sana na hii inawanyima haki kama watumishi wa umma. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha haya mashauri yanakamilika kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Godwin Kunambi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotoa maelezo kwenye majibu yangu ya msingi, mashauri ambayo yapo, ya watumishi wanaotakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ni watumishi 1,477; mashauri yaliyokuwa kwenye Tume ya Utumishi wa Umma ni mashauri 598; na kati ya rufaa hizi ambazo zimetajwa kule Tume ya Utumishi wa Umma, rufaa 411 zina vielelezo vilivyokamilika; na rufaa 187 hazina vielelezo, kwa hiyo, zimerudishwa kwa waajiri na mamlaka za nidhamu ili ziweze kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kama nilivyoitoa awali, ni kwamba hawa ambao wanapeleka mashauri Tume ya Utumishi wa Umma hayana vielelezo, yaweze kuwa yamewasilishwa na vielelezo kamili ili haki ya watumishi ambao Mheshimiwa Kunambi ameizungumzia hapa, iweze kupatikana kwa haraka zaidi. (Makofi)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante, Kituo cha Polisi cha Mlimba ni kituo ambacho kinatumia majengo ya Shirika la Reli (TAZARA) na majengo yenyewe ni chakavu. Nini sasa mpango wa Wizara kujenga kituo cha polisi pale Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunambi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri swali hili tumelijibu jana lilikuwa limeulizwa na Mbunge mwingine anayetoka Ifakara. Tunatambua uchakavu wa kituo hicho, ahadi ya Serikali ni kwamba kadiri tutakavyopata fedha katika bajeti ya mwaka 2024/2025, vituo hivi tena viwili, Ifakara na Mlimba vitawekwa kwenye mpango wa ujenzi.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tarehe 22 Mwezi wa Nane 2022 Serikali ya kuanza kujenga Barabara ya Morogoro – Njombe boarder kwa kiwango cha kilometa 100 kutoka Ifakara kwenda Chita.
Je, Wananchi wa Mlimba wangependa kujua taa inaweza kuwa component kwenye tenda hasa kwenye maeneo ya miji kama Mchombe na Mgeta na Mlimba Mjini? Ahsa nte.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwa sasa barabara zote ambazo tunazi – design na kuzijenga, miji yote ambayo inapitiwa na hiyo barabara inawekewa taa. Kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Mlimba, kwamba miji yote ambayo itapitiwa na hiyo barabara kilometa 100 taa itakuwa ni sehemu ya hiyo kandarasi, ahsante.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo (a) na (b): -
(a) Ningependa kujua kwa kupata commitment ya Serikali, ni lini sasa vituo hivi vitarejeshwa?
(b) Wananchi wa maeneo haya Njage na Itongowa wamekuwa wakipata adha kubwa sana ya usafiri hasa ukizingatia wakati huu wa masika sisi Wananchi wa Mlimba usafiri wetu mkubwa ni treni ya TAZARA. Sasa namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri lini atakuwa tayari kuambatana nami tupande treni hiyo ya TAZARA anaposema hapo Ifakara mpaka Mbingu tushuke kwenda Njabi umbali wa kilometa tisa halafu apate hiyo adha na yeye ataona najua atachukua hatua. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wote wanaotumia vituo hivi vya Stesheni ya Reli ya TAZARA kwamba tarehe 28 Ijumaa ya wiki hii tunatuma timu ya wataalam kwenda kufanya tathmini ya kina. Itafanya kazi hii kwa wiki moja, mpaka tarehe 06 ya mwezi wa tano, na watatoa taarifa ama ripoti ambayo hiyo itakuwa msingi wake katika kufanya maamuzi. Hata hivyo swali lake la pili ni lini kwenda huko, Mheshimiwa Mbunge mimi na wewe nitakwenda pamoja na wewe siku ya weekend wakati vikao vya Bunge vinaendelea, tutaomba ruhusa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na Spika ili twende kuona adha hii kwa wananchi na hatimaye kufanya maamuzi sahihi.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa haya majengo yanayoelezwa yamejengwa kwa nguvu za wananchi na fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri: Ni lini Serikali kwa maana ya Wizara ya TAMISEMI itapeleka fedha kukamilisha majengo haya yaliyobaki; jengo la maabara, jengo la mochwari na jengo la mganga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, kwanza nipongeze jitihada za wananchi wa Mlimba kwa kuweza kujenga kituo hiki cha afya kwa shilingi milioni 500. Serikali kwa sasa itatafuta fedha kadiri ya bajeti itakavyoruhusu ili tuweze kwenda kujenga maabara, mochwari na nyumba ya mganga. Tayari Mheshimiwa Mbunge hili alikuwa amekuja kulifuatilia na tunaona uwezekano wa upatikanaji wa hizi fedha katika bajeti ya mwaka huu tunaoenda kuanza 2023/2024. Kama ikikosekana hapo, basi tutenge katika mwaka 2024/2025.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara ya Mafinga - Kihansi inaungana na barabara ya Ifakara – Mlimba - Madeke mpaka Njombe Kibena junction, ninaishukuru Serikali kwa kuwa mwaka huu wa fedha bajeti ilitengwa ujenzi wa kiliometa 100 ianze kujengwa barabara hii ya Ifakara – Mlimba – Njombe, mpaka sasa taarifa nilizonazo mkataba umeshasainiwa ujenzi wa kilometa 62.5 uanze kujengwa. Swali langu dogo hapo ni kwamba; je, ni lini sasa mandarasi atakabidhiwa site na ujenzi uanze mara moja? (Makofi)
Kwa kuwa, barabara hii kwa mujibu wa bajeti ilitengwa kilometa 100 na kilometa 62.5 mkataba ulishasainiwa na kulikuwa na Lot I na Lot II. Lot zote mbili zilitangazwa mara moja. Swali langu la pili; je, hii Lot II kilometa 37.5 lini mkataba huu utasainiwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Lot I kilometa 62.5 imeshasainiwa na Mkandarasi tayari alishapatikana na kazi hii imeshainiwa. Kinachosubiriwa sasa hivi, Mkandarasi baada ya kusaini anatakiwa atoe performance guarantee (dhamana ya utendaji) na lazima iwe imetolewa ndani ya siku 28. Kwa hiyo, tunaamini atakapokuwa amekamilisha takwa hilo la kisheria atakabidhiwa hiyo barabara ili aanze kufanya mobilization na inatakiwa ifanyike ndani ya siku 28.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara hii ni kweli kama alivyosema ni kilometa 100 lot mbili, hizi kilometa 37.5 ambazo zimebaki, tayari kila kitu kimekamilika tunachosubiri ni kusaini tu, hii ni pamoja na barabara nyingine ambazo zilikuwa zinasubiria utaratibu wakuzisaini. Kwa hiyo, tunaandaa utaratibu ili barabara hizo ziweze kusainiwa halafu wakandarasi waanze kuzijenga. Ahsante. (Makofi)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa msingi wa maamuzi wa Mahakama unatokana na offer iliyotolewa tarehe 2 Julai, 1990 na offer hiyo ilikuwa ni ya miaka 33 mpaka leo tukihesabu ndugu Kambenga hana umiliki tena wa shamba hilo;
(a) Je, Serikali pamoja na nia njema ya mazungumzo yanayoendelea haioni sasa imefika wakati wa kurejesha shamba hilo kwa wananchi?
(b) Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuambatana na mimi kwenda kusikiliza wananchi hawa ili asikilize kilio chao? Ahsante.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunambi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, suala la kuwa na offer ya miaka 33 na offer ikaisha haimnyimi uhalali kama ameomba tena kuendelea kulimiliki, na wakati huo huo kama hakuna mwombaji mwingine ambaye ameomba maana yake lile eneo linaweza likawa liko wazi kwa ajili ya wengine. Mpaka sasa tunavyoongea mwenye shamba hilo bado analitumia kwa hiyo tunaweza kusema kwamba bado anayo haki yake kwa ajili ya kumiliki eneo lile kwa sababu mpaka sasa hakuna mwombaji mwingine yeyote aliyeomba eneo lile.
Mheshimiwa Spika, suala la pili la lini niko tayari kuambatana naye, tutaangalia ratiba kwa sababu tayari tukimaliza Bunge hili tumeshajipangia ratiba ya kuzunguka katika Mikoa, tutaangalia Morogoro iko lini na tutafika kama iko kwenye awamu hii.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jamhuri kwa niaba ya Mamlaka ya Uhifadhi kwa maana ya TAWA iliwashitaki Wenyeviti wawili wa vitongoji ndani ya Kijiji cha Mkangawalo, kesi ya jinai namba 281 kwa kosa la kufanya shughuli za kilimo kwenye hifadhi, na tarehe 27 Septemba, 2021 Mahakama iliwaacha huru watu hawa na kuagiza warudishiwe ardhi yao na mali zao kwa maana ya trekta walizonyang’anywa.
Je, ni lini Serikali sasa itarejesha mali zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wa Jimbo la Mlimba ni wakulima, wafugaji na wavuvi. Mamlaka hii ya Uhifadhi kwa maana ya TAWA imekuwa ikiwasumbua mara kwa mara. Je, Waziri ni lini sasa atakuwa tayari kuambatana nami kwenda Jimboni pale Mlimba kwenda kushuhudia kero hizi na kuzitatua? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Godwin Kunambi, Mbunge wa Jimbo la Mlimba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala hili ambalo lilikuwa mahakamani na Mheshimiwa Mbunge ametuthibitishia hapa kwamba watuhumiwa hawa wameshaachiwa huru na mali zao zilishikiriwa na TAWA, nitoe tu ufafanuzi katika eneo hili, kwamba mtuhumiwa anapokamatwa ushahidi na vitu vyote vinapelekwa mahakamani. Na pale ambapo inathibitika kwamba mtuhumiwa ameshinda kesi, basi mtuhumiwa anarejeshewa mali zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama mali hizi ziko upande wa TAWA, nimuhakikishie tu Mbunge kwamba tutaenda kulishughulikia suala hili ili mali hizi zirejeshwe kwa watuhumiwa. Lakini ninavyofahamu tunapopeleka kesi hizi mahakamani, tunapeleka na vithibitisho vyote na vinakuwa chini ya Mahakama. Kwa hiyo, kama iko kwetu basi nimuhakikishie kwamba vitarejeshwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na suala hili la pili kwamba niko tayari kwenda kutoa ufafanuzi. Nimhakikishe tu Mheshimiwa Kunambi kwamba wananchi wa Mlimba watambue kwamba Serikali iko kazini na kama nilivyosema, Timu ya Kitaifa ambayo imeteuliwa na Baraza la Mawaziri iko uwandani, inafanya tathmini bila kufanya taharuki yoyote na inashikirisha mkoa, inashirikisha wilaya na wale wananchi tukimaanisha viongozi walioko kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishatambua Serikali inapaswa kurejesha kama wale ambao tunatakiwa kuwaondoa hifadhini kwamba watalipwa ama hawastahili kulipwa, wananchi watapewa taarifa na baada ya hapo tutaanza kutatua hii migogoro kwa kushirikishana, hatutaenda kwa nguvu kwa kuwa Mheshimiwa Rais alishasema, hataki kuona taharuki.
Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mbunge kwamba pamoja na kuwa ametaka niende kule, lakini kwa kuwa timu ya tathmini iko uwandani, tuiache ifanye kazi. Tunapoenda sasa kuongea na wananchi tuwe na kitu cha kuwaambia wananchi bila kuweka taharuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kwamba tutatatua tatizo hili na tutaambatana naye baada ya tathmini kukamilika.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Skimu ya Umwagiliaji ya Njage ilisanifiwa kutoa huduma kwenye hekta 1,750, mpaka sasa ni hekta 750 tu ambazo miundombinu ya umwagiliaji imefika.
Je, ni lini Serikali itakamilisha hizi hekta 1,000 zilizobaki?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Skimu ya Idete ni skimu inayonufaisha Jeshi la Magereza tu na Idete, wananchi wa Kata ya Idete hawanufaiki; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi pia wa Idete wawe sehemu ya kunufaika kwenye mradi huu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kumjibu Mheshimiwa Kunambi Mbunge wa Jimbo la Mlimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja, tunatambua kwamba Skimu ya Njage ambayo hekta ambazo zinatumika mpaka sasa hivi ni 750 na 1,000 bado hazijafanyika. Nimwondoe hofu kwamba nimezungumza na DG wa Tume ya Umwagiliaji kuhusu expansion ya mradi huu kumalizia hizi 1,000. Kwa hiyo, amesema tutaliweka katika mipango yetu ya kibajeti ili kuhakikisha tunalikamilisha kwa wakati ili wananchi wake waweze kupata faida ya kulima katika eneo kubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Skimu ya Idete ambayo inatumika na Magereza na yenyewe tumekubaliana kwamba tutakwenda kufanya usanifu wa kina kuongeza expansion ili wananchi wa Kata ya Idete waweze kufaidika. Magereza watumie na wananchi wa kawaida wa Kata ya Idete na wenyewe waweze kunufaika na skimu hiyo. Ahsante sana.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba hapo awali shamba hili lilikuwa linamilikiwa na Kijiji cha Utengule, na kwa kuwa wananchi hawa kwa nia njema kabisa waliridhia shamba hili litwaliwe na Serikali kwa ajili ya uwekezaji, lakini sasa yapata miaka 13 hamna uwekezaji wowote: Swali langu, ni lini Serikali itakabidhi shamba hili kwa wananchi wa Kata ya Utengule? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Kunambi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla ya kutoa maelezo ya majibu, nampongeza sana Mheshimiwa Kunambi na wananchi wa Mlimba kwa kumpata kiongozi ambaye ni mfuatiliaji, ana hamasa ya kweli kwa maendeleo ya wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi ni kwamba Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, wanaendelea na mchakato wa jinsi ya kuharakisha maamuzi ya shamba hili aidha kurudishwa sehemu ya shamba hilo kwa wananchi na ile sehemu ambayo imewekwa kwa ajili ya uwekezaji mkubwa wa bwawa letu la Mwalimu Nyerere, nalo kuangaliwa katika umbo zima la namna ya kulilinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe tu comfort Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itatoa maamuzi kwa haraka ili kuharakisha manufaa yatakayotokana na matumizi ya ardhi hii ambayo kimsingi haijatumika ipasavyo kwa muda mrefu, ahsante.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
(a) Mheshimiwa Spika, Skimu ya Umwagiliaji ya Njagi ni skimu ambayo haijakamilika na wananchi wameanza kunufaika nayo. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kuhifadhia maji?
(b) Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Mlimba tumelazimika kuishi kwa matumaini, je, sisi wananchi wa Kata ya Utengule, Chisano, Ching’anda, Mgeta, Mchombe na Idete, tungependa kujua ni lini mradi huu utaanza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mradi wa Skimu ya Njagi umeshaanza na kinachosubiriwa ni bwawa na liko katika awamu inayofuatia, kwa hiyo, nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge, mradi huo upo katika mpango wa ujenzi wa bwawa katika mwaka wa fedha unaokuja. Kwa hiyo, ninaamini utatekelezeka katika kipindi kinachokuja.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mradi wa eneo la Kata za Utengule, Chisano, Ching’anda, Mgeta, Mchombe na Idete na zenyewe kwa sababu Mshauri Elekezi yuko site na tumekubaliana kwamba katika next financial year tunaliingiza katika mpango wa bajeti, maana yake tutaanza utekelezaji katika mwaka wa fedha unaokuja, ahsante.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Uchukuzi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Mlimba usafiri wa reli ya TAZARA ndiyo usafiri unaotegemewa, sasa lini mpango wa Serikali katika kuboresha reli hii ikiendana sambamba na kuongeza mabehewa na route za safari ya reli hii kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya TAZARA kama inavyofahamika ilijengwa miaka 1975 baina ya Serikali tatu, China, Tanzania na Zambia na kipindi chote hicho designed capacity ilikuwa ni metric tons milioni tano, lakini kutokana na ubovu wa miundombinu hatukufikia lengo. Habari njema kutoka kwa daktari wa maendeleo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania amefanya kikao na Waziri wa Zambia pamoja na Rais wa China, hivi ninavyozungumza tupo kwenye hatua za mwisho za majadiliano, reli nzima inakwenda kufumuliwa upya. Moja, kuongeza uwezo wa reli wa kubeba mzigo, lakini pili tutaongeza mabehewa pamoja na vichwa vya kutosha ya mizigo na abiria. Kwa hiyo, Wana-Mlimba na watumiaji wote wa reli hii inayotoka Dar es Salaam mpaka Kapiri Mposhi kilometa 1,860 waendelee kusubiri habari hii njema ambayo inakuja kwa Watanzania wote. (Makofi)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Uchukuzi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Mlimba usafiri wa reli ya TAZARA ndiyo usafiri unaotegemewa, sasa lini mpango wa Serikali katika kuboresha reli hii ikiendana sambamba na kuongeza mabehewa na route za safari ya reli hii kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya TAZARA kama inavyofahamika ilijengwa miaka 1975 baina ya Serikali tatu, China, Tanzania na Zambia na kipindi chote hicho designed capacity ilikuwa ni metric tons milioni tano, lakini kutokana na ubovu wa miundombinu hatukufikia lengo. Habari njema kutoka kwa daktari wa maendeleo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania amefanya kikao na Waziri wa Zambia pamoja na Rais wa China, hivi ninavyozungumza tupo kwenye hatua za mwisho za majadiliano, reli nzima inakwenda kufumuliwa upya. Moja, kuongeza uwezo wa reli wa kubeba mzigo, lakini pili tutaongeza mabehewa pamoja na vichwa vya kutosha ya mizigo na abiria. Kwa hiyo, Wana-Mlimba na watumiaji wote wa reli hii inayotoka Dar es Salaam mpaka Kapiri Mposhi kilometa 1,860 waendelee kusubiri habari hii njema ambayo inakuja kwa Watanzania wote. (Makofi)