Answers to Primary Questions by Hon. Hamad Hassan Chande (115 total)
MHE. BONIPHACE M. GETERE Aliuza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kufukia mashimo makubwa yaliyosababishwa na ulimaji wa barabara na uchimbaji wa madini hasa katika Mikoa ya Mara, Geita na Shinyanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004 inaelekeza maeneo yaliyoharibiwa kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini kurejeshwa katika hali yake awali ikiwemo kufukia mashimo, kupanda miti na kudhibiti taka. Aidha, wamiliki wa migodi yote wanatakiwa kuweka Hati Fungani (Environmental Performance Bonds) kama dhamana ya Usimamizi wa Mazingira katika migodi husika.
Aidha, Sheria ya Madini, Sura ya 123 inawataka wamiliki wote wa leseni za uchimbaji madini kuhakikisha uzingatiaji wa utunzaji wa mazingira katika maeneo ya uchimbaji wa madini ikiwemo ufukiaji wa mashimo yatokanayo na shughuli hizo.
Mheshimiwa Spika, Mikakati mbalimbali imewekwa ili kuzingatia utekelezwaji wa Sheria hizi ikiwemo:-
(i) Serikali kupitia Kamati ya Kitaifa ya Kufuatilia Utekelezaji wa Mipango ya Ufungaji Migodi inahakikisha hatua zote za urejeshwaji wa maeneo ya uchimbaji ikiwemo kufukia mashimo yaliyotokana na shughuli za uchimbaji zinazingatiwa ipasavyo; na
(ii) Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika migodi husika mara kwa mara imekuwa ikifanya ufuatiliaji na ukaguzi wa uzingatiaji wa matakwa haya ya kisheria.
Mheshimiwa Spika, mashimo makubwa yote yaliyotokana na uchimbaji wa madini katika Mikoa ya Mara, Geita na Shinyanga yanapaswa kufukiwa. Serikali inaendelea kufuatilia na kuhakikisha kuwa matakwa haya ya kisheria yanazingatiwa. Aidha, kwa upande wa mashimo makubwa yanayotokana na ulimaji wa barabara, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeendelea kuhimiza uzingatiaji wa masuala ya hifadhi ya mazingira wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI Aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kufanya mapitio kuimarisha miundombinu ya miradi ya maji ya African Adaptation Program (AAP) iliyojengwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi ili kuondokana na mahitaji makubwa ya maji kutokana na ongezeko la watu katika Jimbo la Nungwi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA Alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya ufadhili wa Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la UNDP ilitekeleza mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kupitia African Adaptation Program (AAP) mwaka 2011 katika eneo la Nungwi, Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja na kufaidisha jumla ya watu 11,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa ipo haja ya kufanya mapitio ya kuimarisha miundombinu ya miradi ya maji kupitia mpango wa African Adaptation Program (AAP) ili kukabiliana na mahitaji makubwa ya maji kutokana na ongezeko la watu katika Jimbo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaandaa mpango wa kuimarisha miondombinu ya maji katika maeneo mbalimbali Unguja ikiwemo eneo la Nungwi kupitia Mradi wa Uimarishaji wa Usambazaji Maji Safi na Salama na Misingi ya Maji Machafu Zanzibar chini ya mkopo wa Benki ya Exim ya India. Katika mpango huo, matenki mawili ya zege yatajengwa, moja la lita 500,000 na lingine la lita 300,000 ambapo mtandao wa maji utakuwa na urefu wa kilometa
14. Ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaweka matumbawe bandia na kupanda mikoko katika bahari ili kurejesha mazalia na makulia ya samaki yaliyoharibika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kuweka matumbawe bandia katika maeneo kadhaa ya mwambao wa Dar es Salaam, Unguja na Pemba. Katika eneo la Sinda Pwani ya Dar es Salaam eneo la mita za mraba 2000 limepandikizwa matumbawe bandia. Vilevile, kwa upande wa Unguja na Pemba jumla ya matumbawe bandia 90 aina ya reef ball yalipandikizwa katika Kijiji cha Jambiani; na matumbawe bandia 46 na mapande maalum 6 katika Kijiji cha Kukuu. Matumbawe hayo yalifuatiliwa ukuaji wake kitaalam na matokeo yameonyesha mafanikio makubwa kwa kuimarika kwa mazalia ya samaki na hivyo kuongezeka kwa kiwango cha samaki katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na upandaji wa mikoko, Serikali imekuwa ikiongeza jitihada zaidi katika upandaji wa mikoko katika fukwe mbalimbali nchi nzima kwa kushirikiana na asasi binafsi na washirika wa maendeleo. Takribani hekta 7 za mikoko zilipandwa Unguja na hekta 10 zilipandwa Pemba kwa mwaka 2020/2021. Upandaji wa hekta 13.5 unaendelea mpaka sasa na matarajio ni kupanda hekta 15 kwa mwaka huu. Aidha, kwa upande wa Tanzania Bara, hekta 105 zimepandwa katika Delta ya Rufiji na matarajio ni kupanda hekta 2000 kwa pwani yote ya Tanzania Bara ifikapo mwishoni mwa mwaka 2022.
Mheshimiwa Spika, ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunatunza, tunahifadhi na kusimamia matumbawe na mikoko pamoja na mifumo ya ikolojia inayopatikana ndani ya bahari zetu. Ahsante.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga tuta kuzuia maji ya Bahari ya Hindi yasiathiri mashamba na mazao ya Wakulima wa Vijiji vya Nanguji, Jundamiti, Mwambe na Kiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Abdalla Rashid, Mbunge wa Jimbo la Kiwani, kutoa maelezo mafupi yafuatayo kuhusu ongezeko la kina cha maji bahari (Sea Level Rise):-
Mheshimiwa Spika, mojawapo ya athari ya mabadiliko ya tabianchi katika dunia yetu ni kuongezeka kwa ujazo wa maji ya bahari (Sea Level Rise). Kwa mujibu wa takwimu za kisayansi zilizopo, kina cha maji ya bahari kimeongezeka kwa wastani wa sentimeta 21. Ili kutimiza lengo la kupambana na mabadiliko ya tabianchi, nchi wanachama wa mkataba zilianzisha mifuko ya fedha kama vile Least Developed Coutries Fund, Adaptation Fund, Green Climate Funds na Global Environment Facility. Nchi zilizoendelea ziliahidi kuchanga fedha na kuziweka kwenye mifuko hiyo. Hata hivyo, kuna changamoto ya urasimu ndani ya sekretarieti ya mifuko ambayo husababisha uidhinishaji wa miradi kuchukua muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdalla Rashid, Mbunge wa Jimbo la Kiwani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ujenzi wa kuta za bahari hugharimu fedha nyingi, ambazo ni vigumu kuzipata kutokana na ufinyu wa bajeti, Serikali itaendelea kuandaa miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na kuendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kupata fedha kupitia mifuko hiyo na kuwezesha Serikali kujenga kuta hizo mara fedha zitakapopatikana. Aidha, wakazi wa maeneo ya Nanguji, Jundamiti, Mwambe na Kiwani kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge wanahimizwa kuibua miradi ya ujenzi wa matuta wakati wa TASAF ya III Awamu ya Pili ambayo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwezi Septemba, 2021.
MHE. MWANAHAMIS KASSIM SAID aliuliza:-
Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa waliokuwa Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano waliostaafishwa kwa maslahi ya Umma tarehe 30 Juni, 1996?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. HAMAD HASSAN CHANDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu ya Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said wa Jimbo la Magomeni, Zanzibar kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais ilipokea malalamiko ya wastaafu saba waliopunguzwa kazini kwa manufaa ya Umma mwaka 1996. Baada ya uchambuzi wa suala hili na kuwasiliana na Wizara ya Fedha na Mipango, ilibainika kwamba stahili zao zote zilishalipwa kipindi walipostaafishwa. Hivyo, hawastahili kulipwa pensheni kutokana na masharti yao ya ajira, bali walilipwa kiinua mgongo cha mkupuo ambacho ni stahili ya watumishi walioajiriwa chini ya masharti ya “Operational Services.” Hii ni kwa mujibu wa Kanuni Na. 6 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi Serikalini za Mwaka 1994 na Sheria Na. 36 ya Mwaka 1964 (The National Provident Fund Act).
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mto Msimbazi ambao umeainishwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira; kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas Mbunge Jimbo la Kinondoni naomba kutoa maelezo yafuatayo kuhusu Mto Msimbazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inatekeleza mradi wa kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project) kwa mkopo nafuu wa Dola za Marekani milioni 300 kutoka Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza DFID, inatekeleza programu ya Tanzania Urban Resilience Programme ambayo imelenga kuzisaidia halmashauri na Serikali Kuu katika kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi. Kwa kuanzia, programu itaanza kutatua changamoto zinazolikabili Bonde la Mto Msimbazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari DFID imeshatenga kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 20 kwa ajili ya Bonde la Mto Msimbazi. Pia Benki ya Dunia, kupitia mradi wa DMDP, imekubali mkopo wa nyongeza wa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 100 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za Bonde la Mto Msimbazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Abbas Tarimba Gulam Mbunge wa Kinondoni:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kubadili eneo la bonde la Mto Msimbazi kuwa eneo la uwekezaji na fursa mbalimbali. Ili kufikia azma hiyo, usanifu wa mradi huo umekamilika. Utekelezaji wa mradi utaanza baada ya kupata idhini ya Serikali kuhusu matumizi ya fedha hizo za mkopo kupitia Wizara ya Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ili kupunguza athari za mafuriko kwa sasa, kipande cha Mto Msimbazi cha daraja la Jangwani kinafanyiwa usafi wa mara kwa mara na wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
MHE. GEORGE N. MALIMA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza kingo za korongo linalopita katikati ya Mji wa Mpwapwa lisiendelee kutanuka ili kunusuru maisha na makazi ya wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa naomba kutoa maelezo yafuatayo kuhusu Korongo lililoko katikati ya Mji wa Mpwapwa:-
Mheshimiwa Spika, Mji wa Mpwapwa umejengwa pembezoni mwa mto ambao ni maarufu kwa jina la Mto Shaaban Robert, ambao sasa unaonekana kama Korongo linalopita katikati ya Mji. Kutokana na wananchi kufanya shughuli zao mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwenye kingo za mto huo, kumekuwa na kubomoka kwa kingo hizo. Hali ambayo imeleta athari kubwa kwenye miundombinu na makazi ya watu walioko karibu na kingo za mto huo.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na uharibifu huo wa mazingira, Serikali imefanya upembuzi wa awali kwenye mto kiasi cha urefu upatao kilometa mbili ambazo ziko jirani na makazi ya watu ili kufahamu gharama za kudhibiti kingo zake. Katika upembuzi huo, inakadiriwa kwamba zinahitajika kiasi cha shilingi bilioni 2,170 kwa ajili ya ukarabati huo. Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kufanya yafuatayo:-
(i) Kuweka gabioni kiasi cha mita za ujazo 8,870;
(ii) Kujenga vizuri mmomonyoko kwa zege kiasi cha mita za ujazo 52;
(iii) Kujaza udongo maeneo yote yaliyoporomoka kiasi cha mita za ujazo 9,000; na
(iv) Kurudisha mto kwenye mkondo wake wa asili ambapo kinahitajika kifusi kiasi cha meta za ujazo 6,000. Serikali imetenga fedha ili kuweza kutekeleza mradi huo.
Mheshimiwa Spika, pia, napenda kuchukua fursa hii kuwasihi wananchi kuacha shughuli zinazosababisha uharibifu wa mazingira katika kingo za mito na badala yake wajitahidi kupanda miti, kupanda majani ambayo yatazuia mmomonyoko wa kingo hizo. Ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
(a) Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na wizi wa vyuma unaosababishwa na kushamiri kwa biashara ya chuma chakavu nchini?
(b) Je, Serikali haioni kwamba biashara ya vyuma chakavu ni hatarishi hata kwa usalama wa raia na mali zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kupitia vifungu vya 133 hadi139, Serikali imeweka kanuni za udhibiti wa taka hatarishi ikihusisha ukusanyaji, usafirishaji na uhifadhi wa taka hizo. Sambamba na uwepo wa kanuni, Serikali imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali pamoja na elimu kwa jamii katika ulinzi wa miundombinu. Aidha, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na jeshi la polisi imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika viwanda ili kudhibiti suala la uhujumu wa miundombinu ya Serikali na watu binafsi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya vyuma chakavu imesaidia kuziondoa taka hizi katika mazingira na hivyo kutengeneza mazingira safi na salama kwa afya ya binadamu. Aidha, vyuma chakavu ni malighafi ya viwanda hasa viwanda vya nondo na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali imekuwa ikifanya ufuatiliaji ili kudhibiti hujuma ya miundombinu ya Serikali na watu binafsi. Aidha, wananchi na vyombo mbalimbali vinaombwa kushiriki kwa pamoja katika kulinda miundombinu dhidi ya watu waovu na wale watu wasio na uzalendo, ahsante.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -
Je, Taasisis ngapi zimeweza kujisajili hadi sasa na Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) nchini, na miradi mingapi imeshaombewa kupitiwa mfuko huo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira). Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge Jimbo la Donge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) ulianzishwa mwaka 2010 na kuanza kufanya kazi mwaka 2015. Taasisi inayotaka kuomba fedha kutoka katika Mfuko huu, ni lazima iwe imesajiliwa au kupata ithibati chini ya Mfuko huu. Ithibati au usajili hutolewa baada ya taasisi husika kutimiza vigezo stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko wa mabadiliko ya Tabianchi unaruhusu taasisi za kitaifa, kikanda na kimataifa, kusajiliwa ili kuweza kuomba fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya mabadiliko ya tabianchi. Hadi kufikia mwezi Machi 2021, mfuko huu ulikuwa umesajili jumla ya taaisis 74 ulimwenguni kote. Hapa nchini, taasisi iliyopata usajili ni moja tu, ambayo ni Benki ya CRDB. Tunaipongeza Benki ya CRDB kwa kuweza kupata ithibati ya mfuko huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa usajili wa taasisi katika mfuko huu wa mabadiliko ya Tabianchi hauna ukomo. Serikali inaendelea kuhamasisha taasisi nyingine za hapa nchini kujisajili na mfuko huu, ili kuwa na uwezo wa kupata fedha na kutekeleza miradi mbalimbali ya mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi, hadi sasa jumla ya miradi sita imeombewa fedha kutoka Mfuko huu kupitia taasisi mbalimbali. Hata hivyo, ni miradi miwili tu ambayo fedha yake imeidhinishwa. Miradi hiyo ni Pamoja na mradi wa Maji kwa Kuwezesha uhimili katika Mkoa wa Simiyu (Dola za Marekani millioni 120), na mradi wa pili, ni mradi wa kuandaa Uwezo wa CRDB (Dola za Marekani 560,000) ahsante.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mashindano ya michezo mbalimbali kwa kila mwaka wakati wa sherehe za Muungano ili kudumisha hamasa za Muungano kwa vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ninakubaliana na Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, kuwa mashindano ya michezo kuelekea maadhimisho ya Muungano yalikuwa yanaleta hamasa kubwa kwa wananchi kila ifikapo Aprili kila mwaka. Kwa kutambua hilo, Serikali italifanyia kazi suala hili na Ofisi ya Makamu wa Rais itaratibu utekelezaji wake kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwani ni ukweli usiopingika kuwa michezo ina umuhimu mkubwa sana katika kudumisha Muungano wetu huu adimu na adhimu. Baada ya utekelezaji huo, Serikali itatoa taarifa, ahsante.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha vikundi vya wananchi ili kuhamasisha uhifadhi wa mazingira hasa katika fukwe za Bahari ya Hindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali tayari ina mpango wa kushirikisha wananchi kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais. Pia Serikali imeandaa mkakati wa kuhifadhi mazingira ya Bahari, Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa. Aidha, kufuatia utekelezaji wa mkakati huu na kwa kutambua umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika kuhifadhi mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanzisha vikundi vya usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi vinavyofahamika kwa jina la “Beach Management Units” – BMUs. Vikundi hivi vimeanzishwa katika ngazi ya Kijiji/Mtaa kwa mujibu wa Kifungu cha 18 cha Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003. Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi una jumla ya vikundi 157 ambapo Tanga ina vikundi (31), Pwani (46), Dar es Salaam (23), Lindi (46) na Mtwara (11). Ahsante. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuvisaidia vikundi vya BMU ili kuendeleza kasi ya upandaji mikoko na kusafisha fukwe kuanzia Pwani ya Bagamoyo, Pangani hadi Tanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari ina mipango ya kuvijengea uwezo wa uelewa ili kujisimamia vikundi vyote vya BMUs katika kuendeleza kasi ya upandaji mikoko na kusafisha fukwe za bahari yetu. Jumla ya vikundi 18 vya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti vimepatiwa mafunzo ya kupanda, kuhifadhi na kusimamia mikoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, vikundi vya BMUs vya Mlingotini Bagamoyo vimewezeshwa kupanda miche 7,000 ya mikoko. Vilevile, vikundi vya BMUs vya vijiji vya Moa, Ndumbani na Mahandakini Wilayani Mkinga vimepatiwa mafunzo ya usimamizi wa mazingira ikiwemo upandaji wa mikoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kupitia mradi wa South West Indian Ocean Fisheries (SWIOfish) unaoratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Vikundi vya BMUs vya Bagamoyo na Pangani wamepata uelewa wa kukusanya maduhuli ambapo kiasi cha fedha kinachokusanywa kitatumika katika kuendeleza shughuli za upandaji wa mikoko na usafi wa mazingira. Ahsante.
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: -
Je, Serikali haioni umuhimu wa kukutana na Wafanyabiashara na kutafuta namna bora ya kuwa na utaratibu wa ukadiriaji kodi wenye usawa na unaozingatia mabadiliko ya biashara ili kulinda mitaji ya wafanyabiashara wa ndani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa idhini yako naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Rahim, ambaye ametujalia afya na uzima. Jambo la pili, nimshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Tatu ninaomba niwashukuru sana Wabunge wenzangu kwa ushirikiano wao mkubwa kwangu, dua na sala zao kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukadiriaji wa kodi hufanyika kwa mlipakodi kuandaa taarifa za biashara yake na mwisho wa mwaka kufanya makadirio ya kodi kulingana na taarifa hizo. Kwa msingi huo, mlipakodi hufanya makadirio mwenyewe (Self-Assessment). Kazi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni kuhakiki usahihi wa makadirio aliyofanya mlipakodi endapo yamefuata matakwa ya sheria. Kwa hiyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania hukutana na walipakodi mara kwa mara kwenye michakato ya ukadiriaji wa kodi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa wafanyabiashara kujikadiria kodi wenyewe ni utaratibu unaotumika na kukubalika duniani kote. Utaratibu huu umewekwa kwa madhumuni ya kukuza mwamko wa ulipaji kodi kwa hiari (Voluntary Tax Compliance), kurahisisha ukusanyaji kodi na kupunguza gharama za ukadiriaji. Hata hivyo, biashara ambazo hazifuati misingi ya utunzaji kumbukumbu hulazimika kuingizwa kwenye utaratibu wa ukadiriaji kulingana na mauzo (Presumptive Tax System) ambapo TRA hutoa makadirio ya kodi kulingana na mauzo ya biashara husika katika kipindi cha mwaka. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: -
Je, Serikali haioni umuhimu wa kukutana na Wafanyabiashara na kutafuta namna bora ya kuwa na utaratibu wa ukadiriaji kodi wenye usawa na unaozingatia mabadiliko ya biashara ili kulinda mitaji ya wafanyabiashara wa ndani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa idhini yako naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Rahim, ambaye ametujalia afya na uzima. Jambo la pili, nimshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Tatu ninaomba niwashukuru sana Wabunge wenzangu kwa ushirikiano wao mkubwa kwangu, dua na sala zao kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukadiriaji wa kodi hufanyika kwa mlipakodi kuandaa taarifa za biashara yake na mwisho wa mwaka kufanya makadirio ya kodi kulingana na taarifa hizo. Kwa msingi huo, mlipakodi hufanya makadirio mwenyewe (Self-Assessment). Kazi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni kuhakiki usahihi wa makadirio aliyofanya mlipakodi endapo yamefuata matakwa ya sheria. Kwa hiyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania hukutana na walipakodi mara kwa mara kwenye michakato ya ukadiriaji wa kodi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa wafanyabiashara kujikadiria kodi wenyewe ni utaratibu unaotumika na kukubalika duniani kote. Utaratibu huu umewekwa kwa madhumuni ya kukuza mwamko wa ulipaji kodi kwa hiari (Voluntary Tax Compliance), kurahisisha ukusanyaji kodi na kupunguza gharama za ukadiriaji. Hata hivyo, biashara ambazo hazifuati misingi ya utunzaji kumbukumbu hulazimika kuingizwa kwenye utaratibu wa ukadiriaji kulingana na mauzo (Presumptive Tax System) ambapo TRA hutoa makadirio ya kodi kulingana na mauzo ya biashara husika katika kipindi cha mwaka. Ahsante. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -
Utoaji wa leseni za biashara kwa biashara ndogo za maduka katika Manispaa ya Kinondoni umekuwa na changamoto kutokana na wafanyabiashara hao kutokuwa na Tax Clearence kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Je, ni kwa nini Serikali isiiagize TRA kwenda mitaani na kubaini biashara hizo na kuzisajili kwa lengo la kurahisisha utoaji wa Tax Clearance ili leseni ziweze kutolewa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa changamoto zinazopelekea wafanyabiashara kutopatiwa Tax Clearance ambalo ni takwa la kupatiwa leseni ya biashara, ni pamoja na wafanyabiashara hao kutosajiliwa na kupatiwa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN Number).
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutatua changamoto hii kwa wafanyabiashara, Serikali imeongeza kasi ya zoezi la usajili wa walipakodi katika jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea na kampeni ya mlango kwa mlango ili kutatua changamoto zinazowakabili walipakodi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya kodi, kuwatambua walipakodi wapya na kuwasajili. Lengo la kampeni hii ni kurahisisha zoezi la usajili wa walipakodi kwa kuwasogezea karibu huduma hii wafanyabiashara wote nchini, kwa kuwafuata katika maeneo yao ya biashara badala ya kuwasubiria waje katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hili maalum limeanza mwezi Agosti, 2021 katika mikoa yote ya kikodi katika Jiji la Dar es Salaam ikiwemo Manispaa ya Kinondoni na litaendelea nchi nzima. Ni matumaini ya Serikali kuwa zoezi hili litaongeza idadi ya walipakodi waliosajiliwa na hivyo kurahisisha upatikanaji wa tax clearance ili leseni za biashara ziweze kutolewa kwa uharaka zaidi. Ahsante.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: -
Je, ni lini wananchi waliokuwa wameweka fedha zao katika Benki ya Wakulima wa Kagera ya KFCB iliyofungwa na Benki Kuu Mwaka 2018 watarejeshewa fedha zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benardeta Kasabago Mushashu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 4 Januari, 2018, Benki Kuu ya Tanzania iliifutia leseni ya kufanya biashara, Benki ya Wakulima wa Mkoa wa Kagera (Kagera Farmers’ Cooperative Bank Limited) kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka, 2006.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuifutia leseni benki hiyo, Benki Kuu ya Tanzania iliiteua Bodi ya Bima ya Amana (Deposit Insurance Board – DIB) kuwa mfilisi wa Benki hiyo kwa mujibu wa sheria. Ambapo kuanzia mwezi Machi, 2018 ilianza zoezi la kulipa fidia ya Bima ya Amana ya kiasi cha hadi shilingi 1,500,000 (Pay-out of insured deposits), kwa wateja waliostahili kulipwa Bima ya Amana. Zoezi hilo bado linaendelea kwa wateja ambao hawajajitokeza kuchukua fidia hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sanjari na zoezi hilo la kulipa fidia kwa wateja ambao hawajajitokeza, Bodi ya Bima ya Amana inaendelea na zoezi la ufilisi wa Benki hiyo kwa kukusanya mali na madeni ya Benki hiyo ili kupata fedha za kuwalipa wateja waliokuwa na amana zao katika benki hiyo, isiyozidi shilingi 1,500,000/=, ambapo kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufilisi kiasi kitakacholipwa kitategemea, fedha zilizopatikana kutokana na kuuza mali za benki hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Disemba, 2021 jumla ya Sh.737,137,082.44 zimeshalipwa kwa wateja 1,389 waliokuwa na amana kwenye Benki ya Wakulima wa Mkoa wa Kagera - KFCB kati ya wateja 7,096 wanaostahiki kulipwa fidia hiyo. Malipo hayo ni sawa na asilimia 90.25 ya kiasi cha Sh.816,801,700.15 zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE K.n.y. MHE. KATANI A. KATANI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawalipa wakulima wa Korosho fedha zao walizofanya biashara msimu wa 2017/2018 na iliyokuwa Benki ya Covenant iliyofungwa kabla ya wakulima hawajatoa fedha zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmed Katani, Mbunge wa Tandahimba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Benki Kuu ya Tanzania iliifutia leseni iliyokuwa Benki ya Covenant mnamo tarehe 4 Januari, 2018 kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Kifedha ya mwaka 2006.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuifutia leseni, Benki Kuu iliiteua Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kuwa mfilisi wa Benki hiyo kwa mujibu wa sheria. Kuanzia mwezi Machi, 2018, Bodi ya Bima ya Amana ilianza zoezi la kulipa fidia ya Bima ya Amana ya kiasi kisichozidi shilingi 1,500,000 kwa wateja waliostahili kulipwa Bima ya Amana wakiwemo wakulima wa korosho wa Wilaya ya Tandahimba na zoezi hilo bado linaendelea kwa wateja ambao hawajajitokeza kuchukua fidia hiyo.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Desemba, 2021, jumla ya shilingi 332,715,894.00 zililipwa kwa wakulima wa korosho 1,078 kati ya wakulima 1,346 wa Wilaya ya Tandahimba waliokuwa na amana katika Benki ya Covenant. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 98 ya kiasi cha shilingi 337,992,095.00 zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia katika Kituo cha Tandahimba.
Mheshimiwa Spika, aidha, Bodi ya Bima ya Amana inaendelea na zoezi la ufilisi wa Benki hiyo kwa kukusanya mali na madeni ya Benki hiyo ili kupata fedha za kuwalipa wateja waliokuwa na amana zinazozidi shilingi 1,500,000 ambapo kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufilisi kiasi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na kuuza mali za Benki hiyo. Ahsante.
MHE. LUCY J. SABU aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka Dirisha Maalum la Vijana kwenye kila Benki za Serikali nchini ili kuwawezesha vijana kupata mitaji na mikopo yenye riba nafuu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania inatekeleza sera na mikakati mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa riba za mikopo zinashuka ili kuwezesha makundi yote likiwemo kundi la vijana yanapata mikopo yenye riba nafuu na kuweza kushiriki vyema katika shughuli za kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Benki za Serikali zinatoa huduma za mikopo kwa makundi yote likiwemo kundi la vijana kwa kuzingatia taratibu za utoaji mikopo za mabenki ambapo kwa wale wenye vigezo hupatiwa mikopo bila usumbufu wowote.
Mheshimiwa Spika, aidha, kwa kutambua umuhimu wa kundi la vijana katika suala zima la upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuwawezesha kufanya shughuli za kiuchumi, Serikali ilianzisha programu maalum ya utoaji mikopo ya uwezeshaji yenye riba nafuu kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2019 ambapo halmashauri zote zinatakiwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi hayo. Vijana wengi nchini wameendelea kunufaika na mikopo hiyo hadi sasa.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha vijana wote wanaokidhi vigezo na masharti ya kupata mikopo wanapatiwa mikopo ili kuendesha shughuli zao na hatimaye waweze kuwa na mchango kwenye ukuaji wa uchumi na pato la Taifa letu. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -
Je, ni lini kiasi cha shilingi milioni 204 zilizorejeshwa Hazina mwaka wa fedha 2019/2020 zitatolewa kwa ajili ya ujenzi wa majengo mawili ya Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante; kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, kiasi cha shilingi milioni 500 kilitengwa na kutolewa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo. Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2020 kiasi cha shilingi milioni 204 kilikuwa hakijatumika, hivyo kilirejeshwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti kifungu namba 29(1).
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za afya karibu na maeneo yao. Hivyo kutokana na umuhimu wa mradi huu, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali ilitenga na kutoa shilingi bilioni moja kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa hospitali hii. Vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 676.6; shilingi milioni 300 kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi na shilingi milioni 376.6 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.
Mheshimiwa Spika, hivyo Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo inahimizwa kuomba fedha hizo mapema ili kuendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali hiyo ya Wilaya ikiwemo majengo mawili aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge. Ahsante. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE K.n.y. MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -
Je, ni fedha kiasi gani zimerudishwa kwa wadai wa VAT wanaoidai Serikali kuishia mwaka wa fedha 2021/2022?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2021/2022, jumla ya Shilingi bilioni 916.68 zililipwa kwa wadai wa VAT, sawa na ufanisi wa asilimia 431.7 ikilinganishwa na bajeti iliyotengwa. Ufanisi huu umetokana na hatua iliyochukuliwa na Serikali ya kuhakiki maombi ya wadai kwa kuzingatia viashiria hatarishi badala ya utaratibu wa awali wa kuhakiki maombi yote kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Spika, utaratibu huo umeongeza kasi ya uhakiki na ulipaji wa madai ya marejesho ya VAT na kupunguza ucheleweshwaji kwa kuwa uhakiki unafanyika kwa wakati. Hatua na mafanikio hayo yanalenga kuchochea ukuaji wa uchumi, uwekezaji na kulinda mitaji ya wawekezaji na wafanyabiashara hapa nchini. Ahsante.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani juu ya mfumuko wa bei unaoendelea nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq Salim Turky, Mbunge wa Mpendae, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2021/2022, mfumuko wa bei uliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 4.0 ikilinganishwa na asilimia 3.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2020/2021. Pamoja na ongezeko hili, mfumuko wa bei umeendelea kubaki kwenye wigo wa tarakimu moja na upo ndani ya lengo la Jumuiya ya Afrika Mashariki la asilimia 8.0 na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika la kati ya asilimia 3.0 hadi 7.0.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali ikiwemo: kuimarisha sekta za uzalisha ili kuongeza upatikanaji wa bidhaa unaoendana na mahitaji; kutoa ruzuku kwa ajili ya kupunguza bei ya nishati ya mafuta kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa mwezi ambapo shilingi bilioni 500 zimetengwa; kutoa ruzuku ya pembejeo za mbegu na mbolea na kutoa unafuu wa kodi katika uagizaji wa baadhi ya bidhaa muhimu.
Mheshimiwa Spika, Serikali inachukua hatua nyingine katika suala hili ikiwemo: kuruhusu watu wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei nafuu; kuanzisha mfuko wa kuhimili ukali wa bei za mafuta baada ya bei za mafuta kutulia katika soko la dunia; kuanzisha hifadhi ya mafuta ya kimkakati na kuanzisha upokeaji wa mafuta katika ghala moja. Ahsante.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -
Je, ni nini kinachosababisha kesi 1,097 za kodi za muda mrefu zenye thamani ya shilingi trilioni 360 na dola za Marekani milioni 181.4 kutoamuliwa hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hadi Agosti, 2022 kulikuwa na idadi ya mashauri 854 kwenye hatua mbalimbali za usikilizaji yenye kodi inayobishaniwa ya jumla ya Shilingi trilioni 4.21 na dola za Marekani milioni 3.48 katika Taasisi za Rufani za Kodi ambazo ni TRAB na TRAT. Hivyo, kwa sasa TRAB na TRAT zinaendelea kusikiliza mashauri hayo pamoja na mashauri mapya yanayoendelea kusajiliwa. Aidha, kwa nyakati tofauti idadi ya mashauri ya kodi hupungua au kuongezeka kulingana na kasi ya usikilizaji na usajili. Ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: -
Je, ni lini Sheria ya Manunuzi na Ukandarasi kupitia Public Private Partnership itaanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 ipo na inatumika, sambamba na Sheria ya PPP, Sura 210, ambapo mchakato wa zabuni za miradi ya PPP unazingatia sheria zote mbili. Pamoja na sheria hizo kutumika kama rejea wakati wa ununuzi wa miradi ya ubia, Serikali inaendelea na utaratibu wa kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau ili kurekebisha vifungu vyenye changamoto katika utekelezaji wake. Ni matarajio yetu kwamba, marekebisho ya sheria zote mbili yatakamilika katika mwaka 2022/2023. Ahsante.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali italipa madai ya shilingi trilioni 7.91 ya watoa huduma kama yalivyoripotiwa kwenye ripoti ya CAG 2021?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, deni la shilingi trilioni 7.91 linajumuisha madeni ya wafanyakazi na watoa huduma kwa mashirika ya umma 71. Ili kuhakikisha madeni hayo yanalipwa na kudhibiti uzalishaji wa madeni mapya, mashirika yote ya umma yameelekezwa kuendelea kulipa kwa haraka iwezekanavyo na kuandaa mkakati wa kukabiliana na madeni na kuwasilisha Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mkakati huo, kila taasisi inatakiwa kuonesha namna itakavyodhibiti uzalishaji wa madeni mapya na kulipa madeni yaliyopo. Lengo ni kuhakikisha kuwa kiwango cha madeni kinafikia asilimia mbili ya jumla ya bajeti ya mashirika ya umma ifikapo mwaka 2025. Aidha, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Idara ya Usimamizi wa Bajeti ya Serikali itatumia mkakati huo katika uchambuzi na uidhinishaji wa mapato na matumizi ya kila mwaka. Ahsante.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuza: -
Je, Serikali inaweza kutoa idadi na aina ya mikopo ya Zanzibar baada ya makubaliano na kuiwezesha Zanzibar kukopa yenyewe?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Mwera, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepewa mamlaka ya kupokea misaada yenyewe kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Kwa mujibu wa kifungu cha 3 na 13, mamlaka ya kukopa na kutoa dhamana yamewekwa chini ya Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anaweza kuyakasimu kwa Waziri wa Fedha wa SMZ baada ya kushauriwa na Kamati ya Kitaifa ya Madeni yenye Wajumbe toka pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, yaani 2019/2020 - 2021/2022, thamani ya mikataba ya mikopo kutoka vyanzo vya nje iliyosainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya SMZ ikiwemo barabara, afya, elimu na mapambano dhidi ya janga la UVIKO-19 ni takribani shilingi trilioni 1.1. Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia mfuko uliopo BoT wa trilioni moja kutoa dhamana kwa waagizaji mbolea kwa njia ya hedging/options?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia Agosti, 2021 BoT ilianzisha mkopo maalum wa shilingi trilioni 1.0 kwa benki na taasisi za kifedha ili kuziwezesha kutoa mikopo kwenye sekta ya kilimo ikiwemo mifugo, uvuvi na misitu. Kupitia mkopo huu, mkopaji anaruhusiwa kutumia kwa kununua au kuagiza mbolea na pembejeo za kilimo kwa utaratibu atakaoona unafaa ikiwemo hedging or options. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA K.n.y. MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafungua Matawi ya Benki ya Kilimo katika Wilaya za Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Kilimo (TADB) imefanikiwa kufungua matawi katika kanda tano ambazo ni Kanda ya Kati, Dodoma; Kanda ya Mashariki, Dar es Salaam; Kanda ya Magharibi, Tabora; Nyanda za Juu Kusini, Mbeya na Kanda ya Ziwa, Mwanza ambayo inahudumia Mkoa wa Kagera na wilaya zake. Aidha, Benki ipo katika hatua za mwisho za kufungua Ofisi ya Kanda ya Kusini, Mtwara na hatua za awali za kufungua Ofisi ya Kanda ya Kaskazini, Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilisha ufunguzi wa Ofisi za Kanda, TADB itaangalia uwezekano wa kufungua ofisi katika mikoa na ikiwezekana wilaya, lakini hili litazingatia uwezo wa benki wa kifedha ikiwa ni pamoja na faida na ukuaji wa mtaji. Ahsante.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaondoa utaratibu wa biashara mpya kutakiwa kulipa kodi ya mapato kabla ya biashara kuanza?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali ilifuta utaratibu kwa walipakodi kulipa kodi kabla ya kuanza biashara. Kufuatia mabadiliko hayo, walipakodi wote wanatakiwa kulipa kodi miezi Sita (6) baada ya kufungua biashara, ili kutoa nafasi ya kujiimarisha kibiashara. Aidha, utozaji wa kodi ya mapato hufanyika kulingana na mapato yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka husika. Ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -
Je, ni hatua gani zitachukuliwa kwa walipa kodi walioshindwa kulipa na kuwa na malimbikizo makubwa lakini wapo tayari kulipa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Usimamizi wa Mapato, Sura 438 Kifungu cha 70 na Kanuni zake kinampa mamlaka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kusamehe adhabu na riba kama kuna suala na sababu maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais, Serikali kupitia TRA inaendelea kujadiliana na wafanyabiashara wenye malimbikizo ya kodi ili kuwapa unafuu wa kulipa malimbikizo ya kodi kwa awamu bila kuathiri ukwasi, mwenendo na uendeshaji wa biashara. Ahsante.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: -
Je, ni lini Ofisi ya TRA itajengwa katika Halmashauri ya Kibondo ili kuzuia biashara holela katika masoko ya ujirani mwema kati ya Tanzania na Burundi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, TRA ilifanya utafiti katika maeneo yote nchini yenye uhitaji wa ofisi za kudumu za usimamizi wa kodi ikiwemo Halmashauri ya Kibondo na kubaini kuwa gharama za usimamizi wa kodi katika Wilaya ya Kibondo zitakuwa kubwa ikilinganishwa na kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa. Kwa muktadha huo, TRA itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa ukuaji wa shughuli za kiuchumi na ukusanyaji wa kodi katika wilaya hiyo ili mara tu itakapokidhi vigezo, TRA itafungua ofisi za kudumu. Aidha, TRA itaendelea kuimarisha mfumo wa sasa wa kuhudumia walipakodi wa Wilaya ya Kibondo ili kuwawezesha kulipa kodi bila usumbufu wowote. Ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO K.n.y. MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -
Je, ni lini Benki Kuu itaweka utaratibu mzuri kwa Serikali na taasisi zake kuweka fedha katika Benki za biashara ili kuwa na mzunguko mzuri wa fedha?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa sasa wa Serikali na taasisi zake kutunza fedha za Benki Kuu ni mzuri na wa uwazi zaidi kwa kuwa unachochea ukuaji wa huduma jumuishi za kifedha. Aidha, mfumo wa sasa unaiwezesha Serikali kusimamia kwa ufanisi utulivu wa uchumi jumla, hususan sarafu yetu na mfumuko wa bei nchini ambao ni msingi wa ukuaji endelevu wa uchumi jumuishi. Vilevile, utaratibu wa sasa unatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sura ya 197. Ahsante sana.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Forodha katika mpaka wa Olaika Wilayani Ngorongoro?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Lekishon Shangai, Mbunge wa Ngorongoro, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, TRA ilifanya utafiti katika maeneo yote nchini yenye uhitaji wa Ofisi za kudumu za usimamizi wa kodi ikiwemo mpaka wa Olaika Wilayani Ngorongoro na kubaini kuwa gharama za usimamizi wa shughuli za forodha katika mpaka wa Olaika zitakuwa kubwa ikilinganishwa na kiwango cha ushuru wa forodha unaotarajiwa kukusanywa. Kwa muktadha huo, TRA itaendelea kufuatilia mwenendo wa ukuaji wa shughuli za forodha katika mpaka huo ili kufungua kituo cha forodha cha kudumu. Aidha, TRA itaendelea kuimarisha mfumo wa sasa wa kuhudumia mpaka huo ili kuwawezesha wananchi kuendesha shughuli zao za kibiashara kwa ufanisi zaidi.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapitia gharama za leseni kwa Wabunifu wa Apps za huduma za kifedha na kuwawezesha kutumia mifumo iliyopo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mifumo ya Malipo ya mwaka 2015 inazitaka kampuni zinazotaka kuendesha huduma za malipo kuwa na leseni ya kutoa huduma inayosimamiwa na sheria hiyo. Leseni hii hutolewa na Benki Kuu ya Tanzania mara baada ya kampuni kukamilisha taratibu zote za kupata leseni. Kampuni ikikamilisha taratibu zote, hutakiwa kufanya malipo ya leseni ambayo ni shilingi milioni 12 na hufanyika mara moja kila baada ya miaka mitano. Aidha, Sheria ya Mifumo ya Malipo inakataa kutoa huduma za malipo bila leseni na adhabu zake zimeainishwa kwenye vifungu vya sheria husika.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mwenendo wa maombi ya leseni kutoka kampuni mbalimbali za huduma za malipo na kiwango cha uwekezaji wa kampuni hizo, ni maoni ya Serikali kuwa gharama za leseni kwa wabunifu wa App za huduma za kifedha zinaendana na mahitaji ya soko. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. KHADIJA S. TAYA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Sensa ya Watu na Makazi inajumuisha takwimu za watu wenye ulemavu na aina ya ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, dodoso la sensa ya watu na makazi itakayofanyika nchini mwezi Agosti, 2022 limejumuisha maswali 10 yanayohusu hali ya ulemavu. Maswali hayo yataulizwa kwa watu wote ikijumuisha umri, jinsi na ulemavu na hivyo kutoa takwimu za hali ya ulemavu nchini. Kupitia sensa hiyo, ni matarajio yetu kuwa Serikali itapata takwimu rasmi za hali ya ulemavu nchini kwa maeneo ya kiutawala, jinsi, hali ya ndoa, kiwango cha elimu, ajira na viashiria vingine muhimu vilivyoainishwa katika dodoso la sensa.
Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuungana na Serikali kuwahimiza wananchi kushiriki kikamlifu katika Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti, 2022 - Sensa kwa Maendeleo, jiandae kuhesabiwa.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kugawa mashine za kutolea risiti EFD kwa Wafanyabiashara ili kuongeza wigo wa walipa kodi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kuwa kila mfanyabiashara anapata mashine za EFD kwa njia rahisi na isiyo na gharama, Serikali kupitia TRA ilianzisha mfumo rahisi wa utoaji wa risiti ujulikanao kama Visual Fiscal Devices (VFD). Mfumo huu wa kisasa wa utoaji wa risiti pasipo kuhitaji kutumia mashine kama ilivyo sasa badala yake mtumiaji anaweza kutumia vifaa vingine vya kieletroniki kama vile simu janja, kompyuta na vishikwambi kutoa risiti zilizounganishwa na mfumo wa TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo unaendelea kutumika na kusambaa nchi nzima na hauna gharama badala yake mtumiaji ataingia gharama ndogo ya bando ili kupata mtandao wakati wa matumizi. Aidha, wafanyabiashara wanaruhusiwa kisheria kujirejeshea gharama ya ununuzi wa mashine za EFD wakati wa uandaaji wa hesabu zao za kodi wanazopaswa kulipa. Ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaunda tena Bodi ya Wataalam wa Ugavi na Ununuzi (PSPTB) baada ya kuvunjwa kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kufuatia uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi uliofanywa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara iliteua Wajumbe wa Bodi ambapo uteuzi wao ulianza Desemba 19, 2021. Ahsante.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: -
Je, mgawanyo wa mapato ya tozo za miamala upoje kwa pande za Muungano na vipi yataboresha huduma kwa upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Seleiman Ramadhan, Mbunge wa Chake Chake, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ilianzisha tozo ya miamala ya kutuma na kutoa fedha kwa njia ya simu kwa lengo la kugharamia miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na madarasa. Utaratibu wa mgawanyo wa fedha za tozo ya miamala kwa pande zote mbili za Muungano unasimamiwa na Kanuni ya saba ya Kanuni ya Tozo za Miamala ambapo fedha zinatoka na miamala inayofanyika Zanzibar huwasilishwa Bodi ya Mapato ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Februari, 2022 jumla ya shilingi bilioni 231.54 zilikusanywa kwa Tanzania Bara na shilingi bilioni 2.96 kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa upande wa fedha zilizokusanywa Zanzibar, mchanganuo wa matumizi yake utatolewa ufafanuzi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, kwa Tanzania Bara, fedha hizo zimeelekezwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na madarasa katika tarafa ambazo hazikuwa na miundombinu hiyo. Ahsante sana.
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -
Je, ni kwa nini Serikali isiweke ulazima wa hitaji la kisheria kuwa Taxpayer Tax Audit ifanyike kila mwaka badala ya kusubiri miaka mitatu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura 438 kifungu cha 45 imeainisha mamlaka ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kufanya ukaguzi au uchunguzi wa masuala ya kodi kwa walipakodi wote, wakati wowote na sio kwa kuzingatia muda wa miaka mitatu isipokuwa ni pale tu inapoonekana kuna viashiria vya upotevu wa mapato ya Serikali ili kukomboa kodi ambayo haijakusanywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa viashiria hivyo ni Pamoja na: -Mwenendo usioridhisha wa ulipaji kodi; Mlipakodi kutokufuata Sheria za kodi; aina ya biashara au shughuli ya kiuchumi anayofanya mlipakodi husika; na suala lingine lolote ambalo Kamishna Mkuu ataona ni muhimu ili kuhakikisha kuwa kodi stahiki inakusanywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa ili kupunguza ulazima wa Kamishna Mkuu kufanya uchunguzi na ukaguzi wa mara kwa mara kwa walipa kodi ni muhimu walipakodi wote kuzingatia matakwa ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya kodi iliyopo. (Makofi)
MHE. NG'WASI D. KAMANI aliuliza: -
Je, Serikali inatoa kauli gani kwa Makampuni Binafsi yanayouza Hisa na hayajatoa gawio miaka mingi pamoja na kujiendesha vizuri?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ulipaji wa gawio kwa wanahisa wa kampuni unafanyika kwa kuzingatia Kifungu cha 180 cha Sheria ya Kampuni, Sura 212.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria hii, Serikali haiwezi kuingilia maamuzi na taratibu za kampuni kulipa gawio. Aidha, napenda kutoa rai kwa wanahisa wa kampuni mbalimbali kushiriki vikao vya mwaka vya wanahisa katika kampuni zao ili kuwa sehemu ya maamuzi yanayotolewa kwenye Mikutano Mikuu wa Mwaka.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -
Je, ni lini BOT itashusha riba inapokopa kupitia Hati Fungani kufikia asilimia 10 ili wananchi waweke fedha kwenye Benki za Biashara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, viwango vya riba za hati fungani vilifanyiwa marekebisho mwezi Aprili 2022 ambapo hati fungani ya miaka 25 ilishuka kutoka asilimia 15.95 hadi 12.56; Miaka 20 kutoka asilimia 15.49 hadi 12.10; Miaka 15 kutoka asimilia 13.5 hadi 11.15; Miaka 10 kutoka asilimia 11.44 hadi 10.25; Miaka saba kutoka asilimia 10.08 hadi 9.48; Miaka mitano kutoka asilimia 9.18 hadi 8.6; na miaka miwili kutoka asilimia 7.82 hadi 7.6. Riba za hati fungani zilishushwa ili kuendana na riba za soko na pia wananchi waweze kuweka fedha zao kwenye benki za biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, wastani wa riba za hati fungani za Tanzania zipo chini ikilinganishwa na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afika Mashariki. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa riba za hati fungani za Serikali na kuchukua hatua stahiki ili kutoathiri akiba za fedha katika benki za biashara, ahsante.
MHE.OMAR ALI OMAR K.n.y. MHE. MOHAMMED SAID ISSA aliuliza: -
Je, ni vigezo gani Serikali inavitumia kusamehe kodi ya VAT kwa viwanda mbalimbali nchini ili kuleta usawa kwa wote?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohammed Said Issa, Mbunge wa Konde kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa Msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani umewekwa kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148. Sheria imeelezea kwa kina vigezo vinavyotumika kutoa misamaha ya Kodi ya VAT. Vigezo vinavyotumika kusamehe VAT kwa sekta ya viwanda ni kama ifuatavyo: -
i. Uagizaji wa malighafi zinazotumika kutengenezea vyandarua;
ii. Uagizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa Serikali zitakazotumika kwenye miradi inayotekelezwa kwa fedha za Serikali, mikopo na misaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo;
iii. Uagizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa ajili ya unafuu wa majanga ya asili; na
iv. Uagizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa kampuni yenye makubaliano na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ahsante.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kusaidia makampuni ya wazawa yenye mikopo katika taasisi za fedha kutokana na athari za UVIKO-19?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taofiq Salim Turky, Mbunge wa Mpendae kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza hatua za kiutawala na kibajeti kwa kuwa athari zilizojitokeza za UVIKO-19 zilitokana na kuvurugika kwa mnyororo wa uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma katika nchi washirika wa kibiashara ikilinganishwa na soko la ndani. Aidha, uamuzi huo ulichukuliwa kwa kuwa shughuli zote za kibiashara hapa nchini ziliendelea kama kawaida.
Mheshimiwa Spika, hatua za kiutawala na kibajeti zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na: -
i. Kuiagiza benki na taasisi za fedha kutoa unafuu katika urejeshwaji wa mikopo kwa kuongeza muda wa urejeshwaji wa mikopo.
ii. Kushirikisha sekta binafsi kupitia zabuni za watoa huduma na wakandarasi katika utekelezaji wa Mpango wa Kukabiliana na Athari za UVIKO-19 kwa lengo la kuiwezesha kutengeneza faida na kurejesha mikopo katika benki na taasisi za fedha.
iii. Kutoa kipaumbele kwa malipo ya malimbikizo ya madeni, madai na marejesho ya kodi yaliyohakikiwa ili kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi; na
iv. Kutoa unafuu wa kikodi, ikiwemo kodi ya kuendeleza ufundi stadi kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia nne na kupandisha kiwango cha chini cha idadi ya waajiriwa wanaostahili kulipiwa kodi kutoka asilimia nne hadi 10 ili kupunguza gharama za uendeshaji kwa waajiri na hivyo kuwezesha marejesho ya mikopo kwenye benki na taasisi za fedha.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani kuirejeshea Halmashauri ya Liwale fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati iliyorudishwa Hazina ili iweze kujenga Stendi ya Kisasa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa stendi ya kisasa ya Liwale ni moja kati ya miradi ya kimkakati ya kuongeza mapato kwa Halmashauri, ambapo mwaka 2018 Serikali iliingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi kutekeleza mradi huo kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.2.
Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa. Hivyo, kutokana na umuhimu wa mradi huu, katika mwaka 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya ya Liwale imetengewa Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa ya Liwale. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI inahimizwa kukamilisha taratibu za maombi ya fedha na kuwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango. Ahsante.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN K.n.y. MHE. ALI HASSAN OMAR KING aliuliza: -
Je, TRA itasitisha lini kukusanya na kuzirudisha fedha za VAT ilizokusanya kutoka kwenye miamala ya mtandaoni iliyofanywa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan Omar King, Mbunge wa Jimbo la Jang’ombe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa pande zote mbili za Muungano zimeweka msingi wa kutoza na kukusanya VAT pale ambapo huduma inapotolewa. Kwa muktadha huo, huduma ikitolewa Tanzania Bara, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatoza VAT ya asilimia 18 kwa mujibu wa Sheria ya VAT inayotumika Tanzania Bara na huduma ikitolewa Zanzibar, Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) inatoza VAT ya asilimia 15 kwa mujibu wa Sheria ya VAT inayotumika Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutambua sehemu ambapo huduma imetumika, Serikali za pande zote mbili za Muungano ziliunda mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama Electronic Revenue Collection System (e-RCS) wenye uwezo wa kutambua miamala yote inavyofanyika na hivyo kusaidia kutunza takwimu sahihi za mauzo yanayotokana na miamala ya mitandao inayofanywa na watumiaji wa kila upande. Mfumo huu unasimamiwa na kamati ya wataalam wa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifumo ya kampuni zote za simu hapa nchini imeunganishwa na mfumo wa Serikali wa e-RCS na taarifa za miamala ya mitandao hutolewa kila mwezi ikiainisha bayana huduma zilizotumika Tanzania Bara na zile zilizotumika Zanzibar. Ahsante.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kupata mkopo wa fedha wa muda mrefu kwa masharti nafuu ili kulipa madeni sumbufu ya awamu zote sita?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kusimamia deni la Serikali kupitia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134 iliyobainisha vigezo vya kuzingatia wakati wa kutafuta fedha za mikopo kutoka ndani na nje ya nchi ili kugharamia shughuli za Serikali, hususan miradi ya maendeleo. Sheria hiyo pia inatumika kama nyenzo ya kudhibiti ongezeko la deni la Serikali kwa kulipa mikopo iliyoiva na kutoa kipaumbele kwa mikopo yenye masharti nafuu.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha awamu zote sita Serikali imeendelea kukopa na kulipa mikopo kulingana na mtiririko wa malipo kwa kila mkopo na hakuna mikopo ambayo Serikali imeshindwa kulipa. Aidha, malipo ya madeni yote ikiwemo madeni sumbufu yanaendelea kulipwa kupitia mpango na bajeti za Serikali za kila mwaka, ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuondoa kodi kwenye vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, vifaa tiba, kinga, dawa na vitendanishi ni miongoni mwa bidhaa zenye sifa za kupata msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kupitia Jedwali la II la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura 148. Jedwali hilo hufanyiwa maboresho mara kwa mara ili kuhakikisha huduma zitokanazo na bidhaa hizi zinapatikana kwa gharama nafuu, ahsante.
MHE. NG'WASI D. KAMANI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaona haja ya kuondoa malipo ya Kodi kwa Wajasiriamali kabla ya kuanza rasmi kufanya biashara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng'wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019, kifungu cha 43 imetoa unafuu wa kutolipa kodi kwa kipindi cha miezi sita kwa biashara mpya tangu mhusika anapopewa namba ya Utambulisho wa Mlipakodi. Lengo la hatua ni kumpa mjasiriamali nafasi ya kustawi kibiashara.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha Misamaha ya VAT inayotolewa inaleta tija kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha misamaha ya kodi inakuwa na tija katika uchumi na jamii kwa ujumla, orodha ya bidhaa na vifaa vinavyostahili msamaha wa kodi inaandaliwa, kuhakiki orodha ya bidhaa na vifaa, kuhakikisha mwombaji anajaza fomu maalum inayothibitisha ununuzi wa bidhaa au vifaa husika pamoja na kufanya kaguzi za mara kwa mara dhidi ya misamaha iliyotolewa ili kuthibitisha iwapo matumizi ya bidhaa au vifaa vilivyosamehewa kodi vimetumika kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kutekeleza matakwa ya kisheria husika katika ufuatiliaji na tathmini ya misamaha ya kodi ikiwemo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ili kuhakikisha kuwa misamaha ya kodi inatolewa kwa kuzingatia sheria na inatumika kama ilivyokusudiwa.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza: -
Je, Serikali ipo tayari kuondoa kodi kwenye vifaa vinavyotumiwa na Watu wenye Ulemavu wakati wa kuingia nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), SURA 148 na ushuru wa forodha kwenye vifaa vilivyotengenezwa mahsusi kwa ajili ya Watu Wenye Ulemavu. Msamaha wa VAT umeainishwa katika kipengele cha 8 na 12(d) cha Jedwali lililopo kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa vilivyopewa msamaha wa kodi ni pamoja na baiskeli na magari yaliyotengenezwa mahususi kwa matumizi ya watu wenye ulemavu. Vile vile, Serikali imetoa msamaha wa VAT kwenye huduma za elimu zinazotolewa katika vituo vya mafunzo ya mwili na akili kwa watu wenye ulemavu, ahsante.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza kutengeneza Bajeti kwa jicho la jinsia?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2023/2024 umetoa maelekezo kwa Maafisa Masuuli kuzingatia masuala ya jinsia, wakati wa uandaaji, uwasilishaji, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini pamoja na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa Mpango na Bajeti zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maelekezo hayo, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake - UN Women inaendelea kushirikiana na Serikali kujenga uwezo katika maandalizi ya nyaraka za sera kwa kuzingatia masuala ya kijinsia. Aidha, katika mwaka 2022/2023, Wizara ya Fedha na Mipango imeunda kikosi kazi kwa ajili ya kuboresha Mwongozo wa maandalizi ya mipango na bajeti ya Serikali kwa jicho la kijinsia, ahsante.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawalipa fedha zao waathirika wa Benki ya FBME iliyofilisiwa tangu Mei, 2017?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, na kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haji Makame Mlenge, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi mwezi Machi, 2023, Serikali kupitia Bodi ya Bima ya Amana - DIB imelipa jumla ya shilingi bilioni 2.43 kama malipo ya awali ya fidia ya Bima ya Amana kwa wateja 3,446 waliojitokeza wa Benki ya FBME iliyofilisiwa mnamo mwezi Mei, 2017. Malipo ya fedha za ufilisi (liquidation proceeds) kwa wateja wenye amana zaidi ya shilingi 1,500,000 yanayotokana na uuzaji wa mali, makusanyo ya madeni na fedha nyingine za Benki ya FBME yatafanyika baada ya Mahakama ya Cyprus kutoa uamuzi kuhusu pingamizi lililowekwa na Benki Kuu ya Cyprus la kuitambua DIB kama Mfilisi wa benki yote ikijumuisha Makao Makuu pamoja na tawi la Cyprus.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, uamuzi wa Mahakama unatarajiwa kutolewa ndani ya mwaka huu wa fedha 2022/2023, ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha ukusanyaji mapato kwa biashara zinazofanyika mtandaoni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato, Serikali kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022 ilifanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura Na.
332 na Sheria ya Ongezeko la Thamani, Sura Na. 148 ili kuwezesha kutoza kodi kwenye biashara zinazofanyika kwa njia ya mtandao. Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania imeanzisha kitengo maalum kinachosimamia biashara za mtandao, ikiwa ni pamoja na kubuni na kuboresha mifumo ya usimamizi wa biashara za mtandao ili kuwezesha utambuzi, usajili na ukusanyaji wa kodi stahiki.
Mheshimiwa Spika, mikakati mingine ni pamoja na kuwajengea uwezo Maafisa wa Kodi juu ya namna ya kutathmini na kukusanya mapato ya kodi yanayotokana na biashara za mtandao, ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -
Je, Serikali ipo tayari kuandaa mazingira kuwezesha biashara kati ya China na Tanzania kufanyika kwa shilingi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chusmi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika biashara za Kimataifa, wafanyabiashara wanao uhuru wa kutumia sarafu yoyote inayorahisisha biashara na inayokubalika na nchi nyingine kwa lengo la kupunguza gharama za miamala na muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itafanyia kazi jambo hili ili kuona ni nini kinapaswa kufanyika kuwezesha wafanyabiashara wa nchi ya China kukubali matumizi ya sarafu ya Tanzania, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA aliuliza:-
Je, hatua zipi zimechukuliwa kuhusu Itifaki ya Forodha kati ya Tanzania na DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, DRC imeshawasilisha hati ya kukubali kutekeleza Itifaki ya Umoja wa Forodha (Instrument of Ratification) kwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, DRC inaendelea na mchakato wa kufanya marekebisho ya sheria zake za ndani ili ianze kutumia Sheria ya Pamoja ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilisha mchakato huo, DRC itafanya vikao na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kukubaliana kuhusu utaratibu wa utekelezaji wa mpango wa utekelezaji (road map) ili kujua lini itaanza utekelezaji wa Itifaki ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO K.n.y. MHE. AMEIR A. AMEIR aliuliza: -
Je, ni asilimia ngapi ya Wafanyabiashara hawajaingizwa katika Mfumo rasmi wa kodi na Serikali inachukua hatua gani kuwafikia?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdalla Ameir, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kupanua wigo wa kodi. Hadi Juni 30, 2023 Mamlaka ya Mapato Tanzania ilikuwa imesajili jumla ya walipa kodi 4,696,999, sawa na asilimia 16 ya idadi ya nguvu kazi iliyopo nchini ambayo ni takribani milioni 33. Idadi ndogo ya usajili wa walipakodi, ikilinganishwa na fursa ya nguvu kazi iliyopo inatokana na sehemu kubwa ya shughuli za kiuchumi hapa nchini kuendeshwa na sekta isiyo rasmi inayokadiriwa kuajiri takribrani watu milioni 27.7.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kurasimisha sekta isiyo rasmi ni pamoja na kampeni ya mlango kwa mlango inayolenga kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara wasiotambulika, kutenga na kujenga maeneo maalumu ya masoko kwa wafanyabiashara wadogo na kuendelea kutoa elimu na ufafanuzi wa kina kwa wananchi kuhusu masuala ya kodi ili kuhamasisha wananchi kurasimisha biashara na shughuli za kiuchumi kwa hiari, nakushukuru.
MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza kodi kwa kampuni changa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salim Mussa Omar, Mbunge wa Jimbo la Gando kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na utaratibu wa kuzingatia misingi ya utozaji kodi, Serikali imetoa unafuu kwa biashara na kampuni changa kwa kuzitoza kodi miezi sita baada ya kuanzishwa kwake na kodi ya mapato kwa kampuni hizo huanza kutozwa baada ya kuanza kutengeneza faida ambayo hukokotolewa kulingana na faida iliyopatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na zoezi la mapitio ya mfumo wa kodi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya bajeti ya mwaka 2023/2024. Mwelekeo wa Serikali ni kuboresha zaidi mazingira ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji hasa kwa kampuni changa ikiwemo uboreshaji wa mifumo ya usimamizi wa kodi, kufanya tathmini ya tozo mbalimbali zilizopo kwa lengo la ama kupunguza viwango au kuzifuta kabisa pale ambapo zinaonekana ni kero kwa biashara au kampuni changa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza:-
Je, lini Serikali itashawishi mabenki kufungua benki nchini Congo DRC katika Miji ya Kalemie na Uvira ili kurahisisha biashara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo Mei, 2021 Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania iliipa Benki ya CRDB kibali cha kufungua kampuni tanzu Lubumbashi, nchini Congo ambapo inatarajia kuanza kutoa huduma za kibenki mara tu itakapopewa leseni na Benki Kuu ya nchi hiyo ya Congo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkakati wa Miaka Mitano wa Biashara wa Benki ya CRDB wa mwaka 2023 - 2028 unaonesha kuwa benki hiyo inatarajia kufungua kampuni tanzu zitakazotoa huduma za kibenki kwenye Miji ya Bukavu, Uvira na Kalemie nchini Congo. Hivyo, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano kwa benki za biashara za hapa nchini kuanzisha kampuni tanzu nje ya nchi ili kusambaza huduma za kibenki katika nchi mbalimbali kwa lengo la kurahisisha ufanyaji wa biashara baina ya nchi na nchi, ahsante.
MHE. LUCY J. SABU aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanzisha Benki ya Vijana Wajasiriamali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa uwezeshaji vijana kiuchumi, Serikali ipo katika hatua ya kuandaa mkakati wa upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, ambao utawezesha vijana kupata mitaji kupitia benki, taasisi za huduma ndogo za fedha, masoko ya mitaji, mifuko na programu za Serikali za uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, katika hatua ya utekelezaji wa mkakati huu, Serikali inatarajia kuanzisha taasisi mahsusi ya fedha itakayosimamia upatikanaji na utoaji wa mikopo kwa makundi maalum wakiwemo vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na wafanyabiashara wadogo wadogo wakiwemo wamachinga. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE K.n.y. MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-
Je, lini Benki ya CRDB itafungua tawi katika Mji wa Mangaka?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya CRDB imeanza ujenzi wa tawi katika Mji wa Mangaka. Tawi hilo linatarajiwa kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa mji huo kabla ya mwezi Septemba 2023, ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza:-
Je, nini kauli ya Serikali kuhusu ucheleweshaji fedha zinazotumwa Nje ya Nchi kutokana na Mabenki kuwa na uhaba wa fedha za Kigeni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua kadhaa katika kupunguza athari kwenye soko la ndani la fedha za kigeni ili kusaidia shughuli za biashara na miamala kuendelea kufanyika. Hatua hizo ni pamoja na:-
a) Kuanzia Machi 2023 Benki Kuu imeongeza kiasi cha fedha za kigeni kinachouzwa katika soko la jumla la fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani milioni moja hadi Dola za Marekani milioni mbili kila siku.
b) Kuongeza kiwango kinachoruhusiwa kuuzwa kwa muamala mmoja kwa njia ya rejareja kwenye soko la fedha za kigeni baina ya Mabenki kutoka Dola za Marekani 250,000 hadi Dola za Marekani 500,000.
c) Kuhakikisha ukwasi wa Shilingi ya Tanzania unabakia katika viwango vinavyoendana na mahitaji halisi ya kiuchumi kwa kutumia nyenzo mbalimbali za sera ya fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, benki za biashara nchini zimeendelea kutunza amana ya kutosha katika akaunti kwenye benki nje ya nchi ili kufanikisha miamala ya ulipaji wa bidhaa na huduma mbalimbali zinazoagizwa na kuuzwa nje ya nchi. Aidha, nazielekeza benki zote nchini, kuhakikisha kuwa zina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni kabla ya kupokea fedha kutoka kwa mteja anayetarajia kuzituma nje ya nchi ili kuepuka ucheleweshaji.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itawasaidia Wananchi wa Mtwara Mjini waliojiunga na PRIDE kurejeshewa fedha zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya tathmini ya hali ya Kampuni ya PRIDE na kufuatiwa na ukaguzi maalum uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu kutambua mali na madeni ya kampuni hiyo. Kufuatia tathmini hiyo, Serikali inaendelea na taratibu za kisheria za kuifilisi PRIDE.
Mheshimiwa Spika, Madeni yatalipwa kwa kuzingatia sheria na taratibu za ufilisi na yanatarajiwa kukamilishwa ifikapo Julai 2023. Ahsante.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI K.n.y. MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza:-
Je, lini Mifumo ya Malipo ya Kimataifa itaruhusiwa ili wabunifu/watu wanaofanya kazi za ushauri kwa taasisi za nje wapate malipo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya mwaka 2015 inawataka watoa huduma za mifumo ya malipo kupata leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania ili kutoa huduma hizo nchini. Utaratibu huu unaiwezesha Benki Kuu kuwa na usimamizi wa moja kwa moja kwa watoa huduma za mifumo ya malipo nchini na kuhakikisha panakuwa na mifumo ya malipo inayoaminika na salama kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sheria hiyo, Benki Kuu imeweza kutoa leseni kwa watoa huduma za mifumo ya malipo wa kimataifa ambapo wamefungua ofisi zao nchini, ambapo hadi Aprili mwaka 2023 jumla ya taasisi 10 za kimataifa ambazo si benki za biashara zimepewa leseni ya kutoa huduma za mifumo ya malipo nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa leseni za kutoa huduma za mifumo ya malipo zinatolewa kwa watoa huduma wote, wa ndani na nje ya nchi, waliotayari na wanaokidhi matakwa ya sheria ili kutoa fursa kwa wananchi kupata huduma stahiki za mifumo ya malipo zinazozingatia usalama wa fedha zao na maslahi mapana ya nchi. Ahsante.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza:-
Je, Serikali imejiimarisha vipi kukagua miamala ya uhamishaji bei ya mauziano ya bidhaa/huduma za makampuni ya Kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia vihatarishi vilivyopo kwenye miamala husika, Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali zinazolenga kuimarisha udhibiti na kuzuia upotevu wa mapato. Hatua hizo ni pamoja na:-
a) Kuanzisha Kitengo Maalum cha Usimamizi wa Kodi za Kimataifa ndani ya Mamlaka ya Mapato ya Tanzania kuanzia 2011.
b) Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa kanuni na miongozo kuhusu ukaguzi wa kodi kwenye kampuni zenye mahusiano.
c) TRA imenunua Kanzidata ya Orbis kwa ajili ya kupata taarifa za kusaidia kufananisha bei za Miamala ya Kimataifa ili zisaidie kujenga hoja wakati wa ukaguzi unaofanywa kwenye Kampuni za hapa nchini.
d) Tanzania imejiunga na Jukwaa la Kimataifa la Ubadilishaji wa Taarifa za kikodi kwa lengo la kuhakikisha nchi yetu inajenga uwezo wa kubadilishana taarifa za kikodi na nchi nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatarajia kusaini Mkataba ujulikanao kama “Multilateral Convention on Mutual Administrative Assistance in Tax Matters” ambao utaiwezesha TRA kupata taarifa mbalimbali kutoka katika nchi 146 duniani ambazo zitasaidia katika kuongeza ufanisi wa ukaguzi wa Miamala ya Kimataifa. Ahsante.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:-
Je, Mkoa wa Kagera unachangia kiasi gani kwenye Pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya National Accounts for Tanzania Mainland inayoandaliwa na kusambazwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, hadi kufikia mwaka 2021 Mkoa wa Kagera ulichangia 2.6% ya pato la Taifa ikilinganishwa na 2.5% ya pato la Taifa kwa mwaka 2020, ahsante.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Manyovu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha usanifu wa kituo cha huduma za pamoja mpakani (One Stop Boarder Post) cha Manyovu kilichopo Mkoani Kigoma na ujenzi upo kwenye taratibu za awali za kumpata mkandarasi, ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI K.n.y MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali isisamehe kodi na kuondoa baadhi ya tozo katika Sekta ya Elimu na Afya ili kuvutia taasisi binafsi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa misamaha ya kodi katika Sekta ya Elimu na Afya kwa kuzingatia sheria na miongozo mbalimbali kama ifuatavyo: -
(a) Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332:-
(i) Wafanyabiashara wanaojihusisha na utoaji wa huduma za afya na elimu wanasamehewa kulipa kodi ya makampuni yanayotangaza kupata hasara kwa mfululizo wa miaka zaidi ya mitatu;
(ii) Mchango wowote anaofanya mfanyabiashara kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa Elimu anajirejeshea kama gharama wakati wa kutengeneza faida;
(iii) Taasisi yoyote iliyoanzishwa kwa ajili ya kujishughulisha na uendelezaji wa elimu na afya au kutoa huduma za umma kwenye Sekta za Afya na Elimu imepewa hadhi ya charitable organization na kupata unafuu wa kodi.
(b)Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148:-
(i) Msamaha wa kodi umetolewa katika ujenzi wa majengo kwa ajili ya kutoa huduma za afya na elimu kwa jamii;
(ii) Bidhaa na huduma zinazoingizwa nchini na Serikali au kununuliwa katika soko la ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi katika Sekta ya Afya na Elimu zimesamehewa Kodi ya VAT; na
(iii) Madawa na vifaa vya utabibu na huduma za afya zilizoorodheshwa katika para 7 la jedwali la kwanza la misamaha zimesamehewa Kodi ya VAT.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha miongozo na taratibu za usimamizi wa kodi ili kuimarisha biashara na kuvutia wawekezaji, ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Je, Serikali ipo tayari kuiwekea SUMA JKT mazingira rafiki ili iweze kukopa na kutekeleza miradi yake kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, SUMA JKT wanaruhusiwa kukopa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134 kama ilivyo kwa mashirika mengine ya Serikali. Hivyo shirika litatakiwa kuwa na hali nzuri ya kifedha inayothibitisha uwezo wa taasisi kukopa na kulipa.
Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Uandaaji, Utekelezaji na Usimamizi wa Miradi na Majadiliano ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 2020 umeelekeza hatua muhimu za kuzingatia kwa Wizara au Taasisi ya Serikali ikiwa inaomba mkopo, dhamana na msaada, kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ahsante.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuinusuru Benki ya Wakulima Mkoa wa Kagera ambayo ipo chini ya uangalizi wa BOT?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 4 Januari, 2018 Benki Kuu ya Tanzania iliifutia leseni ya kufanya biashara Benki ya Wakulima Mkoa wa Kagera baada ya kushindwa kutimiza masharti ya leseni. Sambamba na uamuzi wa kuifutia leseni, Benki Kuu iliamua kuiweka benki hii chini ya ufilisi na iliiteua Bodi ya Bima ya Amana (Deposit Insurance Board - DIB) kuwa mfilisi wa benki hiyo. Kwa muktadha huo, iliyokuwa Benki ya Kagera Farmers’ Cooperative Bank Limited haipo chini ya uangalizi wa Benki Kuu ila ipo chini ya ufilisi wa DIB baada ya kufutiwa leseni ya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha, 2006, benki ikishafutiwa leseni na kuwekwa chini ya ufilisi hakuna tena uwezekano wa benki kuendelea kuwepo na hivyo Serikali haina mpango wa kuifufua benki hiyo ila inafanya ufuatiliaji ili kuhakikisha kuwa zoezi la ufilisi linakamilika. Hadi Machi 2023, Bodi ya Bima ya Amana ilikuwa imelipa fidia ya bima ya amana jumla ya shilingi milioni 846.11 kwa wateja 1,389 waliokuwa na amana kwenye Benki ya Wakulima ya Kagera kati ya jumla ya shilingi milioni 899.56 zilizopaswa kulipwa kwa wateja 2,797 kulingana na matakwa ya sheria, ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaweka Kituo kidogo cha Forodha katika Kata ya Itiryo – Bikonge Tarime Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Tarime Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania imeanza utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano (2022/2023 – 2026/2027) wa ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na ofisi katika maeneo yote yaliyobainishwa kupitia utafiti wa mwaka 2021/2022 kuhusu mahitaji ya ofisi za TRA nchini. Mpango huo umejumuisha Mkoa wa Mara na utekelezaji umeanza katika ujenzi wa nyumba mbili za wafanyakazi na usanifu wa ujenzi wa Ofisi ya Forodha mpakani Kilongwe – Rorya. Aidha, usanifu wa ujenzi wa majengo ya nyumba za watumishi mpakani Sirari umekamilika na ujenzi utaanza mapema baada ya kumpata mzabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji katika vituo vingine vya Mkoa wa Mara utaanza kadri ya upatikanaji wa fedha, ikiwa ni pamoja na Kogaja, Borega, Kirumi na Itiryo – Bikonge.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kufanya mapitio sheria ya Manunuzi ya umma kwa kuwa ni kikwazo kwa utekelezaji wa miradi katika Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imefanya mapitio ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 na kuandaa mapendekezo ya kutunga upya sheria hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo hayo yamekamilika na muswada wa kutunga upya sheria ya ununuzi wa umma unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge la Kumi na Mbili.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa changamoto za biashara za mpakani hasa utitiri wa tozo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Felix, Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, utozwaji wa kodi ya forodha kwa bidhaa zinazoingia nchini kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki unasimamiwa na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya mwaka 2004.
Mheshimiwa Spika, Kodi zinazotozwa kwa bidhaa zinazoingia nchini ni pamoja na Ushuru wa forodha ambayo ni ya Afrika Mashariki; kodi ya VAT ambayo hutozwa na kila nchi mwanachama; kodi ya ushuru wa bidhaa ambayo hutozwa kwa baadhi ya bidhaa na tozo ya maendeleo ya reli.
Mheshimiwa Spika, tozo nyingine hutozwa kwa huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali za Serikali zinazohusika na uondoshwaji wa mizigo mipakani ambazo husimamiwa kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha taasisi hizo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo Serikali imefanya jitihada kubwa ya kupunguza changamoto za biashara nchini hususani kupunguza utitiri wa tozo kutoka tozo 380 hadi tozo 148 katika kipindi cha mwaka 2017/2018 hadi 2020/2021. Hivyo Serikali itaendelea kuondoa changamoto za kufanya biashara nchini ikiwemo sehemu za mipakani.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kubadilisha Mfumo wa Uandaaji Mpango wa Bajeti ili uwe wa zaidi ya miaka mitano?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali unaongozwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambapo katika kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Serikali iliandaa Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa miaka 15 kuanzia 2011/2012 hadi 2025/2026 uliogawanywa katika vipindi vitatu vya muda wa kati wa miaka mitano ya utekelezaji (Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa 2011/2012 hadi 2015/2016, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa 2016/2017 hadi 2020/2021 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa 2021/2022 hadi 2025/2026.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mfumo wa uuandaji wa mpango na bajeti wenye kutoa mwelekeo wa zaidi ya miaka mitano ambapo mpango na bajeti unaoandaliwa kila mwaka ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -
Je, Serikali inatumia utaratibu gani kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Mipango na Bajeti zinazopitishwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali husimamia na kufuatilia utekelezaji wa mipango na bajeti zinazopitishwa na Bunge kwa utaratibu ufuatao: -
(a) Wizara ya Fedha na Mipango kila mwaka huandaa na kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Maandalizi na Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali;
(b) Kutoa Waraka Na.1 wa Mwaka wa Fedha wa utekelezaji wa bajeti unaoelekeza na kusisitiza utekelezaji wa vipaumbele;
(c) Kuandaa mwongozo wa maombi na utoaji fedha kwa lengo la kuhakikisha fedha inatolewa wakati wa uhitaji na inatumika kwa wakati;
(d) Kusimamia uwasilishwaji wa taarifa za utekelezaji wa mipango na bajeti na ambazo huchambuliwa ili kutathmini utekelezaji wa mipango kwa kuoanisha na malengo tarajiwa na bajeti zilizotengwa; na
(e) Kubainisha viashiria hatarishi vya utekelezaji wa bajeti na kufanya ufuatiliaji na tathmini ili kujiridhisha na uhalisia na kuchukua hatua stahiki, ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -
Je, ni lini mianya ya majadiliano yanayopelekea rushwa kwenye mfumo wa ukadiriaji wa kodi kwa Wafanyabiashara itaondolewa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ukaguzi na makadirio ya kodi huongozwa na Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura 438 na Kanuni zake, pamoja na miongozo inayotolewa na Serikali kupitia TRA. Hivyo, mawasiliano yote yanayofanyika baina ya TRA na Mlipakodi kabla ya makadirio ya kodi kutolewa yanaongozwa na misingi iliyotajwa hapo juu. Aidha, TRA inachukua hatua mbalimbali ili kuondoa mianya ya rushwa kama ifuatavyo: -
(i) Kutoa elimu kwa walipa kodi kujua haki na wajibu wao;
(ii) Kuimarisha usimamizi wa sera ya maadili kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania;
(iii) Kurahisisha utoaji wa taarifa za watumishi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa kupitia tovuti na kupiga simu kupitia namba za simu zisizo na gharama; na
(iv) Kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali katika kuelimisha, kuzuia na kushughulikia vitendo vya ukiukwaji wa maadili ndani ya mamlaka.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kuunda, kutumia na kuimarisha utendaji kazi wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA ili kupunguza vitendo vya ubadhilifu na rushwa vinavyosababishwa na utaratibu wa kuonana ana kwa ana kwa Afisa wa Kodi na Mlipa Kodi wakati wa ukadiriaji wa mapato. Ahsante.
MHE. JOSEPH A. TADAYO K.n.y. MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itarekebisha Sheria ya Utakatishaji Fedha inayozuia dhamana kwa Watuhumiwa hata kwa makosa ya kawaida?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 12 cha Sheria ya Kudhibiti Utakasishaji wa Fedha Haramu, Ufadhili wa Ugaidi na Ufadhili wa Silaha za Maangamizi, Sura 423, kinabainisha makosa ya utakasishaji wa fedha haramu pekee. Sheria hiyo haihusishi makosa mengine yoyote, hususan kuzuia au kutozuia dhamana kwa watuhumiwa wa makosa ya kawaida. Aidha, utaratibu wa dhamana kwa makosa mbalimbali, ikiwemo utakasishaji wa fedha haramu unasimamiwa na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura 20.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, hakuna sababu ya kurekebisha Sheria ya Kudhibiti Utakasishaji wa Fedha Haramu, Ufadhili wa Ugaidi na Ufadhili wa Silaha za Maangamizi, Sura 423 kwa kuwa haizuii dhamana kwa watuhumiwa wa makosa ya kawaida. Ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHWALE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaongeza geti lingine ndani ya Jimbo la Momba kutokana na geti la Tunduma kuzidiwa katika kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichwale, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kurahishisha biashara kati ya nchi ya Tanzania na Zambia na kuondoa changamoto ya msongamano wa magari katika Kituo cha Tunduma, Serikali inaendelea kuchambua na kutathmini taratibu zilizopo ili kuona kama kuna uwezekano wa kuongeza Kituo cha Forodha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuondokana na changamoto ya msongamano wa magari ambapo Januari, 2021 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliingia makubaliano na Mamlaka ya Mapato ya Zambia yanayoelekeza hatua mbalimbali za kuchukua kwa kila nchi. Hatua hizo ni pamoja na: -
i. Kuunganisha mfumo wa TANCIS wa TRA na mfumo wa ASCUDA World wa Zambia ili kuiwezesha Idara ya Forodha Zambia kupata taarifa za shehena ya mzigo husika kabla kuwasili mpakani; na
ii. Serikali ya Zambia kufanya maboresho ya miundombinu ya barabara na eneo la kuegesha magari kupitia ufadhili wa Trademark East Africa (TMEA).
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na makubaliano hayo, Serikali kwa upande wa Tanzania imefanya yafuatayo: -
i. Uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja cha Forodha ambacho kimesaidia taasisi zote za Serikali kuwa sehemu moja na kuwasiliana kwa haraka; na
ii. Serikali kupitia ufadhili wa TMEA imenunua scanners tatu ambazo ni baggage scanner, body scanner na cargo scanner. Aidha, baggage scanner na body scanner zinafanya kazi na cargo scanner inatarajiwa kuanza kufanya kazi mwezi Julai, 2022, ahsante.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -
Je, Serikali inadaiwa fedha kiasi gani ilizokopa Mifuko ya Hifadhi za Jamii na kiasi gani cha madeni kimelipwa na kwa utaratibu gani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ilikopa fedha kutoka katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na deni la michango ya wastaafu waliokuwa katika utumishi kabla ya mwaka 1999. Mchanganuo wa madeni na kiasi kilicholipwa ni kama ifuatavyo: -
(i) Mfuko wa PSSSF shilingi bilioni 506.88 na imeshalipwa shilingi bilioni 500 kwa utaratibu wa kibajeti; na deni la michango ya wastaafu waliokuwa katika utumishi kabla ya mwaka 1999 shilingi trilioni 4.46 na shilingi trilioni 2.17 zimeshalipwa kwa utaratibu wa hatifungani maalum. Aidha kiasi kilichobaki cha deni la Mfuko wa PSSSF shilingi bilioni 6.88 na shilingi trilioni 2.29 zitalipwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023.
(ii) Mfuko wa NSSF shilingi bilioni 292.59 zilizokidhi vigezo baada ya uhakiki wa deni la shilingi bilioni 490.16 zitalipwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023; na
(iii) Mfuko wa NHIF shilingi bilioni 80.68 zilizokidhi vigezo baada ya uhakiki wa deni la shilingi bilioni 209.72, zitalipwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali itaendelea kuhakiki sehemu iliyobaki ya deni la Mfuko wa NSSF na NHIF ili yaweze kujumuishwa katika mpango wa malipo.
MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza:-
Je, Serikali inachukua hatua gani za kukabiliana na athari mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na hali ya kisiasa duniani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, na kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inafuatilia kwa karibu athari na fursa za kiuchumi na kijamii zinazosababishwa na hali ya kisiasa duniani ikiwemo vita kati ya Urusi na Ukraine. Aidha, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na: -
(i) Kufanya tathmini ya athari za kiuchumi na jamii zinazotokana na vita ya Urusi na Ukraine kwa Tanzania;
(ii) Serikali kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta kwa kipindi cha kuanzia Juni 1, 2022;
(iii) Kuruhusu wafanyabiashara wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei nafuu ili kuhakikisha uwepo wa mafuta nchini. Mpango huu unatarajiwa kupunguza bei ya mafuta kuanzia mwezi Agosti 2022;
(iv) Kuhamasisha wafanyabiashara kuagiza ngano kutoka nchi nyingine zinazozalisha ngano ikiwemo Afrika Kusini, Canada, Australia, Uswiss na Ujerumani;
(v) Kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya kuzalisha mbolea nchini ambapo kutokana na uhamasishaji huo, kampuni ya Itracom Fertilizers Limited kutoka Burundi inaendelea na ujenzi wa kiwanda mkoani Dodoma. Kiwanda hicho kitakapokamilika kinatarajiwa kuzalisha tani 500,000 kwa mwaka.
(vi) Serikali kuendelea kutekeleza mikakati mahususi ya kukuza utalii wa ndani na kikanda kupitia fursa za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Kamisheni ya Utalii ya Shirika la Utalii Duniani kwa Kanda ya Afrika.
(vii) Kuimarisha sekta ya uzalishaji ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na tathmini ya hatua mbalimbali zinazopaswa kuchukuliwa kwa kila sekta ili kukabiliana na athari za kiuchumi na kijamii zinazotokana na hali ya kisiasa duniani ikiwemo vita ya Urusi na Ukraine, ahsante.
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA aliuliza: -
Je, ni lini majimbo ya Zanzibar yatapata fedha za Mfuko wa Jimbo kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Hafar Idrissa Juma, Mbunge wa Mtoni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, fedha za Mfuko wa Jimbo kwenda Majimbo ya Zanzibar hupelekwa kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za fedha, ambapo fedha hizo huamishwa moja kwa moja kutoka Wizara ya Fedha na Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, katika mwaka 2021/2022 fedha za mfuko kiasi cha Shilingi Bilioni 1.4 zimeshatolewa kwa ajili ya Majimbo ya Zanzibar. Ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE K.n.y MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha stakabadhi za mashine za EFD ili zisifutike baada ya muda mfupi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kufutika kwa stakabadhi za mashine za EFD baada ya muda mfupi kumesababishwa na matumizi ya karatasi zenye ubora hafifu. Aidha, karatasi zinazopaswa kutumika ni zile zenye ubora wa "thermal paper".
Mheshimiwa Spika, baada ya kubaini changamoto hiyo, TBS kwa kushirikiana TRA imeshatengeneza viwango vya ubora wa karatasi hizo vinavyotakiwa na sasa wanaendelea na usimamizi kuhakikisha karatasi zote zinakidhi ubora unaotakiwa.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo TRA imeboresha mfumo wa usimamizi wa mashine za EFD kwa kuwezeshe kupokea taarifa zote za kila risiti inayotolewa na kuitunza katika saver zake na hivyo kuwezesha nakala ya risiti hizo kuweza kupatikana wakati wowote inapohitajika. Ahsante.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza: -
Je, lini Serikali itabadili muonekano wa Noti na Sarafu ili kutoa fursa ya kuweka picha ya Rais Mwanamke wa kwanza Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, uamuzi wa kuondoa picha ya Rais kwenye noti ulifanyika katika kipindi cha Awamu ya Tatu chini ya Rais mstaafu Hayati Benjamin Mkapa. Miongoni mwa sababu ya kuondoa picha za viongozi kwenye sarafu yetu ilikuwa ni gharama za mara kwa mara za uchapishaji wa noti kwa ajili ya kubadilisha picha za viongozi mara muda wao wa kuwa madarakani unapokoma. Hivyo, kuanzia toleo la noti la mwaka 1997, picha ya Kiongozi Mkuu wa Nchi iliondolewa na badala yake picha za wanyama kama vile tembo (shilingi 10,000), kifaru (shilingi 5,000) na simba (shilingi 2,000) zimeendelea kuonekana kwenye sarafu ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuenzi michango ya waasisi wa Taifa letu, noti ya shilingi 1,000 imeendelea kuchapishwa ikiwa na picha ya baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na noti ya shilingi 500 ilichapichwa ikiwa na picha ya Rais wa awamu ya kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume. Hata hivyo, noti ya shilingi 500 ilibadilishwa kuwa coin mwaka 2014 ambapo picha ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume imeendelea kuwepo. Ahsante. (Makofi)
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-
Je, ni kwa kiasi gani lengo la Benki Kuu la kutoa mikopo kwa sekta binafsi limefikiwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Fedha ya Mwaka 2021/2022, imeainisha shabaha ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi wa asilimia 10.6 ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa gharama nafuu na kuongeza ukwasi katika uchumi. Kutokana na utekelezaji wa sera hiyo, kiwango cha ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kimeendelea kuongezeka kufikia wastani wa asilimia 8.4 katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Aprili, 2022, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 4.3 katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Aprili, 2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kuanzia mwezi Desemba, 2021, ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulikuwa zaidi ya asilimia 10 ambapo mwezi Aprili, 2022, ukuaji huu ulifikia asilimia 13.4. Kutokana na mwenendo huu ni matarajio yetu kuwa, lengo la ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi la asilimia 10.6 kwa mwaka 2021/2022 litafikiwa na hivyo kuchangia uwekezaji, uzalishaji na kuongeza ajira nchini, ahsante.
MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza:-
Je, kuna mpango gani wa kupunguza kodi, tozo na ushuru wa bidhaa za chakula/mboga kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, Mbunge wa Chaani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, bidhaa za chakula na mbogamboga halisi zinazotoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar hazitozwi kodi, tozo na ushuru wa aina yoyote kwa mujibu wa sheria, lakini bidhaa za chakula kutoka viwandani hutozwa tozo ya uchakataji nyaraka za forodha ya asilimia 0.6 tu kwenye thamani ya mzigo huo. Lengo la tozo hii ni kugharamia huduma ya uchakataji wa nyaraka za forodha na hutozwa kwa wateja wote wanaotumia mfumo wa forodha.
Mheshimiwa Spika, bidhaa za chakula na mbogamboga halisi hazitozwi tozo ya uchakataji wa nyaraka kwa sababu, hazihitaji kufanyiwa mchakato wa nyaraka katika mfumo wa forodha, ahsante.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza:-
Je, ni kwa kiwango gani Serikali imejiimarisha kukagua miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma baina ya makampuni ya Kimataifa.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TRA imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kiukaguzi wa miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma baina ya makampuni ya Kimataifa kwa lengo la kuzuia upotevu wa mapato. Hatua hizo ni pamoja na:-
(i) Kuendelea kuboresha mifumo ya ndani ya ukusanyaji kodi kama vile Mfumo wa Usimamizi wa Mashine za Utoaji wa Risiti za Kielektroniki na Mfumo wa Kuwasilisha return Kielektroniki;
(ii) Kutoa mafunzo ya vitendo kwa watumishi katika nchi mbalimbali zenye uzoefu wa kushughulikia miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma baina ya makampuni ya Kimataifa;
(iii) Kuimarisha utekelezaji wa mkataba wa kubadilishana taarifa kati ya Serikali ya Tanzania na nchi nyingine;
(iv) Kuendelea kufanya majadiliano na wadau mbalimbali ili kuona uwezekano wa kujiunga na Global Forum on Tax Transparency na ubadilishanaji wa taarifa kwa lengo la kupanua wigo wa upatikanaji wa taarifa. Ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuweka Kituo cha Forodha Kakozi Momba ili kuunga mkono jitihada za kujenga Soko la Mazao la Kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania ina utaratibu wa kupitia na kufanya tathmini ya sehemu zote ambazo zinaweza kujengwa ofisi kwa ajili ya ukusanyaji kodi. Utaratibu huu unazingatia uwiano wa gharama za ukusanyaji wa mapato na kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa pindi ofisi hizo zitakapofunguliwa kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mwenendo wa kukua kwa biashara kati ya Tanzania na nchi jirani, Serikali inaendelea kufanya tathmini ya kina katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kakozi Momba na mipaka mbalimbali hapa nchini. Aidha, maeneo yatakayokidhi vigezo vya kujengwa ofisi za forodha kulingana na tathmini hiyo, taratibu za uanzishwaji wa ofisi hizo zitaanza kwa kuzingatia upatikanaji wa rasilimali watu na fedha. Ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzisaidia Community Banks kama MUCOBA Bank Iringa ili kukuza uchumi wa Wananchi wa hali ya chini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kuweka mazingira bora ya kisera na kimfumo ili kuziwezesha benki za biashara na za kijamii (Community Banks) kukua na kushamiri, ikiwemo benki ya MUCOBA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu ni pamoja na kutafuta mwekezaji mpya wa MUCOBA ambaye ni Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ); kurekebisha kanuni za usajili wa wakala wa benki kwa kuondoa kigezo cha uzoefu wa miezi 18; kuanzisha mfuko maalum wa shilingi trilioni 1 kwa ajili ya mikopo kwa benki na taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwa wakulima kwa riba ya asilimia 3 kwa mwaka; kutoa unafuu wa kiasi cha amana ambacho benki na taasisi za fedha zinatakiwa kuweka Benki Kuu kwa benki zinazota mikopo kwa sekta ya kilimo; kupunguza kiwango cha riba kinachotolewa katika akaunti za wateja wa watoa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi kuwa sawa na riba za amana za sekta ya benki; na kudhibiti uwiano wa gharama za uendeshaji wa benki na pato la benki usizidi asilimia 55 na mikopo chechefu isizidi asilimia 5 ya mikopo yote, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA K.n.y. MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Je, lini Serikali italipa fidia eneo la Makaburi Idefu – Makambako ili kupisha ujenzi wa One Stop Centre?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshalipa fidia ya shilingi bilioni 4.6 kwa wananchi waliopisha eneo kwa ajili ya Mradi wa Ujenzi wa One Stop Centre. Aidha, Serikali imeanza taratibu za tathmini ya eneo la makaburi ya Idefu, Makambako na taratibu za malipo zitaanza baada ya kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali.
MHE. HAMISI S. TALETALE K.n.y. MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -
Je, ni nini msingi kwa wafanyabiashara kutoza bei tofauti au fedha za kigeni kwa wateja ambao ni raia wa kigeni na nini athari zake?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Serikali imeandaa sheria na kanuni ili kumlinda mlaji na kuhakikisha kuwa bei za bidhaa na huduma zinapangwa kwa msingi wa nguvu ya soko. Kwa mantiki hii, biashara zimekuwa zikiendeshwa chini ya utaratibu wa soko huria ambapo bei za bidhaa na huduma hupangwa kuendana na uwiano wa uhitaji na upatikanaji wa bidhaa husika. Hata hivyo, wafanyabiashara wanaweza kutoza bei tofauti kwa bidhaa na huduma baina ya wazawa na raia wa kigeni au kwa fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine Serikali inatambua na imeendelea kukumbusha kuwa shilingi ndio fedha halali kwa ajili ya malipo mbalimbali hapa nchini. Kutokana na hilo, raia wa kigeni hawatakiwi kulazimishwa kulipa kwa fedha za kigeni hususan pale wanapokuwa na shilingi za Kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, wageni wanaruhusiwa kutumia fedha za kigeni ili kurahisisha ufanyaji wa biashara pale wanapokosa shilingi za Kitanzania na viwango vya ubadilishaji fedha havikitakiwi kutofautiana na vile vinavyotozwa katika masoko ya fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna athari za kimsingi za uchumi kwa wafanyabiashara kutoza bei tofauti baina ya wateja raia wa kigeni na wazawa kwani bei hizo huamuliwa katika soko huru na hivyo inatarajiwa kupanda na kushuka kulingana na nguvu za mahitaji na ugavi sokoni, ahsante. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kurahisisha mfumo mzuri wa kutoa msamaha wa kodi kwa wakandarasi wanaojenga barabara Halmashauri ya Msalala?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, msamaha wa kodi kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kimkakati ya Serikali unatolewa kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani yaani VAT kama ilivyofanyiwa maboresho na Sheria ya Fedha ya mwaka 2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, maboresho ya sheria hiyo yalilenga kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji wa msamaha wa kodi ambapo awali mamlaka ya kutoa msamaha yalikuwa chini ya Waziri wa Fedha. Aidha, kwa marekebisho hayo, mamlaka ya kutoa msamaha yakakasimishwa kwa Kamishna Mkuu wa TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maboresho ya sheria, Serikali kupitia TRA, ilianzisha kitengo maalumu kwa ajili ya kushughulikia misamaha ya Kodi ya Ongezeko la Thamani. Kuanzishwa kwa kitengo hicho kumesababisha kuwa na muda mfupi zaidi wa kushughulikia maombi ya msamaha wa kodi hiyo ukilinganisha na wakati wa awali kabla ya maboresho hayo. Vilevile katika jitihada za kuongeza ufanisi na kutoa msamaha wa kodi ndani ya muda mfupi, Serikali ilianzisha mfumo wa kieletroniki wa kuwasilisha maombi hayo TRA (Tax Exemption Management System), ahsante. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-
Je, hasara na faida gani Taifa linapata kuwa uchumi wa kati na asilimia ngapi ya wananchi wanafahamu na kuishi uchumi wa kati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Tanzania kuingia kwenye kundi la nchi za uchumi wa pato la kati la chini kunaambatana na fursa pamoja na changamoto mbalimbali. Fursa hizo ni pamoja na kuongezeka kwa wigo wa upatikanaji wa fedha za mikopo ya kibiashara kwa ajili ya miradi ya maendeleo, uhuru wa kupanga matumizi ya fedha za mikopo ya kibiashara, kuchochea uwekezaji kutokana na ukuaji wa wastani wa pato la mtu na mtu, na kuzidi kuaminika katika taasisi za kifedha za Kimataifa kutokana na kutengamaa kwa viashiria vya uchumi.
Mheshimiwa Spika, changamoto ni pamoja na kupungua kwa upatikanaji wa misaada na mikopo yenye masharti nafuu, kuongezeka kwa kiwango cha michango kwa taasisi na mashirika mbalimbali ya Kimataifa. Ni matumaini ya Serikali kupitia juhudi ya vyombo vya habari kuwa wananchi walio wengi wanafahamu kuhusu nchi kuingia katika uchumi wa kati wa chini. Hali hiyo imejidhihirisha kwa kuona mabadiliko chanya kwa mwananchi mmoja mmoja na ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI K.n.y. MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Je, kwa nini Kodi ya Jengo na Kodi ya Ardhi zisiunganishwe na kuwa moja ili kumwondolea usumbufu mwananchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Kamati ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi inaendelea kufanya uchambuzi na tathmini ya mifumo ya kodi, ada na tozo za huduma kwa lengo la kuondoa urasimu na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Tathmini hiyo inajumuisha mapendekezo ya maboresho ya mfumo wa usimamizi wa kodi ya jengo na kodi ya ardhi kama inavyopendekezwa na Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hiyo, Serikali inaandaa mfumo wa kielektroniki wa kutoa ankara ya pamoja kwa huduma zinazolandana ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wanaostahili kulipa kodi ya jengo na kodi ya ardhi. Ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI K.n.y. MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafanya tathmini kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Manunuzi wa Umma ya Mwaka 2013 katika Sehemu ya 64(2)(C) ya Kanuni ya 30(c) kama ilivyofanyiwa Marekebisho?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 pamoja na kanuni zake, Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) hufanya tathmini ya ununuzi na kuchapisha taarifa ya tathmini hiyo kila mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo ya tathmini ya mwaka 2020/2021 kuhusu kutenga fedha za ununuzi asilimia 30 kwa makundi maalumu imeonesha kuwa, kati ya taasisi 86 zilizofanyiwa ukaguzi taasisi mbili zilitenga fedha hizo, taasisi tatu zilitenga kiwango pungufu na taasisi 81 hazikutenga kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na matokeo hayo, Serikali imezielekeza taasisi nunuzi zote kuzingatia matakwa ya sheria na umuhimu wake katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii; na kuviagiza vitengo vyote vya ukaguzi wa ndani kuhakikisha kuwa ripoti za kila robo mwaka ambazo huwasilishwa PPRA kuwa na taarifa kuhusu utekelezaji wa sheria katika eneo hilo, ahsante.
MHE. MUSSA R. SIMA K.n.y. MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga ofisi za Mamlaka ya Mapato – TRA katika Wilaya ya Mkalama?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inao utaratibu wa kupitia na kufanya tathmini kwa nchi nzima yenye lengo la kubaini maeneo yote yenye uhitaji wa kujengwa ofisi za TRA kwa ajili ya ufuatiliaji, usimamizi na ukusanyaji kodi ili kusogeza huduma za kikodi karibu na wananchi. Utaratibu huu unazingatia pamoja na mambo mengine uwiano wa gharama za ukusanyaji wa mapato na kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa pindi ofisi hizo zitakapofunguliwa kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2021/2022 Mamlaka inakamilisha tathmini ya nchi nzima ambayo, itabainisha maeneo yenye uhitaji wa kujengwa ofisi kulingana na vigezo. Aidha, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa maeneo yote ikiwemo Wilaya ya Mkalama yatakayokidhi vigezo stahiki yanajengwa ofisi za TRA, ahsante.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
Je, sababu gani zilisababisha maduka ya kubadilisha fedha kuondolewa katika biashara na wananchi wengi kupoteza ajira zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwaka 2016, Benki Kuu ya Tanzania ilifanya ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na kugundua miamala mbalimbali kwa baadhi ya maduka kinyume na matakwa ya sheria na kanuni za usimamizi wa maduka ya fedha za kigeni na udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu. Kufuatia hali hiyo, mwaka 2018 na 2019, Benki Kuu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali ilifanya operation ya ukaguzi maalum kwenye maduka yote ya kubadilisha fedha za kigeni nchini na kubaini makosa mbalimbali ikiwemo:-
(i) Kutofanya utambuzi wa wateja kabla ya kutoa huduma kinyume na kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Udhibiti wa Utakatishaji Fedha Haramu, Sura 423 na kanuni ya 17 ya Kanuni za Udhibiti wa Utakatishaji Fedha Haramu;
(ii) Kugawa miamala ya wateja kwa lengo la kukwepa kutunza kumbukumbu muhimu zinazoonyesha uhalali wa miamala kinyume na Kanuni ya 23(4) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni, 2015;
(iii) Kutokutoa stakabadhi za miamala kinyume na Kanuni ya 23(1) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni, 2015;
(iv) Kutokuwasilisha taarifa sahihi za miamala Benki Kuu na hivyo kuathiri upatikanaji wa takwimu muhimu kwa ajili ya shughuli za kiuchumi; na
(v) Baadhi ya maduka yalikuwa yanajihusisha na uhamishaji wa fedha nje ya nchi bila kuwa na kibali au leseni kutoka Benki Kuu.
Mheshimiwa Spika, baada ya operesheni hiyo, Benki Kuu ya Tanzania ilibatilisha leseni za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni yaliyokutwa na makosa. Maamuzi hayo yalifanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 36(1)(b) na 2(d) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni, 2015 iliyorejewa mwaka 2019, ahsante.
MHE. SUBIRA K. MGALU K.n.y. MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza:-
Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuweka huduma za Wakala wa Forodha katika Bandari ya Nyamisati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembene, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maandalizi ya kutoa Huduma za Wakala wa Forodha katika Bandari ya Nyamisati yanaendelea ambapo Novemba, 2023, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilifanya tathmini kujiridhisha na mawanda ya shughuli zinazofanyika katika eneo hilo. Matokeo ya tathmini hiyo yanaonesha kuwa, eneo hilo lina uhitaji wa huduma za forodha. Hivyo, Serikali inatarajia kufungua ofisi za forodha katika Bandari ya Nyamisati mwaka 2024/2025. Ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:
Je, Serikali ina mpango gani wa kuyauza magari mabovu yaliyopo kwenye halmashauri zetu nchini na kwenye Ofisi za Serikali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa miongozo iliyopo ya ufutaji na uondoshaji wa mali chakavu ikijumuisha vyombo vya moto katika halmashauri na taasisi za Serikali, Wizara ya Fedha ina jukumu la kuhakiki na kutoa vibali vya ufutaji na uondoshaji wa mali chakavu. Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Fedha ilitoa jumla ya vibali vya kuondosha mali chakavu 160 katika Halmashauri na Ofisi za Serikali. Kati ya vibali hivyo, kulikuwa na vibali vya magari chakavu 976 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.4. Aidha, magari chakavu 223 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 yaliondoshwa kwa njia ya mnada kwa taasisi 54. Vilevile ufualitiaji na tathmini ya magari ya miradi ulifanyika na kubaini magari 339 yenye thamani ya shilingi 479,565,000 kuwa ni chakavu na taratibu za uondoshaji wake zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya Julai na Agosti, 2024 vibali 70 vya uondoshaji wa magari chakavu vimetolewa kwa halmashauri na Ofisi za Serikali. Aidha, Septemba, 2024 Wizara ya Fedha itaratibu na kusimamia minada kwenye taasisi 54 ya uondoshaji wa vyombo vya moto 150 katika mikoa tisa ambayo ni Dar es salaam, Mbeya, Arusha, Morogoro, Mtwara, Njombe, Lindi, Pwani na Dodoma, ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Je, Serikali inatambua athari hasi kwa jamii ya Watanzania zinazotokana na ongezeko kubwa la michezo ya kubahatisha?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na faida za kiuchumi na kijamii zinazotokana na michezo ya kubahatisha, Serikali inatambua athari zake katika jamii endapo hazitaendeshwa kwa weledi. Miongoni mwa athari hasi zinazoweza kujitokeza katika jamii ni uraibu na kugeuza michezo ya kubahatisha kuwa mbadala wa ajira, ushiriki wa watoto katika michezo ya kubahatisha na uwepo wa michezo haramu isiyo na usajili wa mamlaka ya udhibiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kifungu cha 7(2)(i) cha Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura 41, mamlaka ya udhibiti ina jukumu la kuhakikisha kuwa, jamii inalindwa ipasavyo dhidi ya athari hasi za michezo ya kubahatisha. Katika kutekeleza jukumu hilo, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kuzuia na kudhibiti athari hasi zitokanazo na uwepo wa michezo ya kubahatisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati hiyo ni pamoja na kuimarisha udhibiti na uratibu wa sekta kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na matumizi ya Mifumo ya TEHAMA, kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za michezo ya kubahatisha, kufanya mapitio ya mara kwa mara ya mifumo ya usimamizi wa michezo ya kubahatisha na kufanya kazi ya udhibiti kwa kushirikisha wadau na mamlaka nyingine kama vile Jeshi la Polisi, TCRA na TRA. Ahsante.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuza:-
Je, lini Serikali itaondoa mzigo wa kodi kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa suala la ulinzi na usalama wa nchi, Serikali imekuwa ikitoa msamaha wa kodi kwa vyombo vya usalama na ulinzi ikiwemo misamaha inayotolewa kupitia Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, kwa mwaka 2024/2025, Serikali imefanya marekebisho kwenye Kipengele cha 18 cha Sehemu ya Kwanza ya Jedwali la Msamaha wa Kodi ili kujumuisha magari pamoja na vifaa vinavyotumiwa na vyombo vya ulinzi. Lengo la hatua hii ni kuwezesha vyombo vya ulinzi na usalama kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-
Je, ni muda gani Hazina hulipa malipo ya katikati ya mwezi kwa Wastaafu kwa Mfuko ulioanza mwaka 1992 kwa kuwa hawalipwi kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha inahusika kulipa michango ya mwajiri kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (PSSSF, ZSSF, WCF na NHIF) kila mwezi pamoja na malipo ya nyongeza ya pensheni. Aidha, Wizara ya Fedha hulipa pensheni za kila mwezi pamoja na mafao ya hitimisho kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina. Ahsante sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuelekeza Benki za CRDB, NBC na NMB kufungua Matawi eneo la Kikatiti linalokua kwa kasi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, katika mchakato wa kufungua tawi jipya la benki, benki husika hufanya upembuzi yakinifu kwa lengo la kujiridhisha kama kuna fursa za kibiashara kukidhi gharama za uendeshaji na kutengeneza faida. Upembuzi huo, pamoja na mambo mengine, huiwezesha benki husika kufanya maamuzi ya kufungua tawi katika eneo husika. Aidha, jukumu la Serikali ni kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwemo huduma ya ulinzi na usalama, miundombinu ya barabara, nishati, maji na TEHAMA.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ukweli kwamba CRDB, NBC na NMB hazina matawi Kikatiti, wananchi wa eneo hilo wanaendelea kupata huduma za kibenki kupitia kwa mawakala. Ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:-
Je, lini Serikali itaboresha Mpaka kati ya Zambia na Tanzania, ili kudhibiti njia za panya ambazo mazao na bidhaa nyingine hutoroshwa bila kulipiwa kodi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, katika kudhibiti utoroshwaji wa mazao na bidhaa katika mipaka ya Tanzania na Zambia, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA) ziliingia makubaliano yanayoelekeza hatua mbalimbali za kuchukua kwa kila nchi. Utekelezaji wa hatua hizo ni pamoja na:-
(i) Mfumo wa Uondoshaji Mizigo wa TANCIS umeunganishwa na Mfumo wa ASYCUDA World wa Zambia, ili kubadilishana taarifa na kurahisisha taratibu za uondoshaji mizigo;
(ii) Serikali imesimika midaki za kukagua mizigo inayobebwa na abiria pamoja na magari;
(iii) Serikali ya Zambia kupanua barabara na eneo la maegesho ya upande wa Nakonde, ili kupunguza msongamano upande wa Tunduma; na
(iv) Kuendelea kubainisha vihatarishi vilivyopo katika magari ya mizigo yanayopita Mpaka wa Tanzania na Zambia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja hatua hizo, Serikali kupitia TRA inaendelea kuimarisha doria, kwa ajili ya kudhibiti maeneo yote ya mpaka wa Tanzania na Zambia kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, ili kulinda mapato ya Serikali. Ahsante sana.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kuondoa miradi chini ya shilingi milioni 100 katika Mfumo wa NeST ili kupunguza ucheleweshaji?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, Mfumo wa NeST unawezesha matumizi ya njia ya ununuzi wa thamani ndogo usiotumia fedha taslimu (Minor Value Procurement Method) kwa kazi za ujenzi hadi zenye thamani ya shilingi milioni 100. Kwa njia hii, taasisi nunuzi inaweza kununua moja kwa moja kutoka kwa muuzaji wa bidhaa, mkandarasi au mtoa huduma bila kuhitaji kuwashindanisha wazabuni zaidi ya mmoja. Kwa kupitia mfumo wa NeST, taasisi nunuzi itatumia siku zisizozidi tatu kukamilisha mchakato wote hasa kwa ununuzi wa miradi yenye thamani chini ya shilingi milioni 100.
Mheshimiwa Spika, hivyo taasisi nunuzi zinashauriwa kutumia mfumo wa NeST na kuchagua njia ya ununuzi inayoendana na thamani ya mradi ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hasa hasa yenye thamani chini ya shilingi milioni 100, ahsante sana.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza: -
Je, nini mkakati wa Serikali kumaliza tatizo la wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, TRA imekuwa ikijikita kwenye matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuboresha ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha ulipaji kodi unafanyika kwa uwazi na usahihi. Matumizi ya TEHAMA yameleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa kodi nchini hasa kupitia zana kama vile Electronic Fiscal Devices na mifumo mingine ya kidijiti kama vile E-filing, EFDMS, ITAX na TANCIS. Matumizi ya TEHAMA katika mifumo ya kodi yameimarisha uwajibikaji, uwazi na kuongeza ufanisi wa TRA katika ukusanyaji wa mapato. Hii imepunguza ukwepaji kodi, kuimarisha nidhamu ya walipa kodi na kurahisisha shughuli za biashara nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendesha kampeni za uelimishaji ili kuwawezesha wafanyabiashara kuelewa umuhimu wa kulipa kodi na mchango wake katika maendeleo ya Taifa letu. Elimu hii hutolewa kupitia njia mbalimbali zikiwemo semina, redio, televisheni, elimu ya mlango kwa mlango, mikutano ya wadau, pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii kama vile facebook, instagram, twitter (X) na whatsapp. Lengo ni kuhakikisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wanapata uelewa wa kutosha kuhusu haki na wajibu wao wa kulipa kodi.
Mheshimiwa Spika, vilevile sheria za kodi zimeimarishwa ili kuhakikisha kuwa hatua kali zinachukuliwa dhidi ya wale wanaokwepa kodi. Adhabu hizi ni pamoja na faini kubwa, kufungwa kwa biashara au kufunguliwa mashtaka ya jinai kwa wafanyabiashara watakaobainika kukwepa kodi. Ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa sheria za kodi, TRA pia inafuatilia kwa karibu utendaji wa Maafisa wake ili kuondoa uwezekano wa rushwa au upendeleo unaoweza kusababisha ukwepaji wa kodi.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo, Serikali pia imeboresha mfumo wa kodi ili kuhakikisha viwango vya kodi vinawiana na hali halisi ya biashara, hivyo kuwaondolea wafanyabiashara mzigo wa kodi usio wa lazima na kuwatia moyo kulipa kodi kwa hiari bila kujihisi wanaonewa. Uboreshaji huu unalenga kuunda mazingira rafiki ya kufanya biashara bila kuathiri juhudi za Serikali kuongeza mapato, ahsante.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuza: -
Je, lini Serikali itaondoa mzigo wa kodi kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa suala la ulinzi na usalama wa nchi, Serikali imekuwa ikitoa msamaha wa kodi kwa vyombo vya usalama na ulinzi ikiwemo misamaha inayotolewa kupitia Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, kwa mwaka 2024/2025, Serikali imefanya marekebisho kwenye Kipengele cha 18 cha Sehemu ya Kwanza ya Jedwali la Msamaha wa Kodi ili kujumuisha magari pamoja na vifaa vinavyotumiwa na vyombo vya ulinzi. Lengo la hatua hii ni kuwezesha vyombo vya ulinzi na usalama kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-
Je, ni muda gani Hazina hulipa malipo ya katikati ya mwezi kwa Wastaafu kwa Mfuko ulioanza mwaka 1992 kwa kuwa hawalipwi kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha inahusika kulipa michango ya mwajiri kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (PSSSF, ZSSF, WCF na NHIF) kila mwezi pamoja na malipo ya nyongeza ya pensheni. Aidha, Wizara ya Fedha hulipa pensheni za kila mwezi pamoja na mafao ya hitimisho kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina. Ahsante sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuelekeza Benki za CRDB, NBC na NMB kufungua Matawi eneo la Kikatiti linalokua kwa kasi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, katika mchakato wa kufungua tawi jipya la benki, benki husika hufanya upembuzi yakinifu kwa lengo la kujiridhisha kama kuna fursa za kibiashara kukidhi gharama za uendeshaji na kutengeneza faida. Upembuzi huo, pamoja na mambo mengine, huiwezesha benki husika kufanya maamuzi ya kufungua tawi katika eneo husika. Aidha, jukumu la Serikali ni kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwemo huduma ya ulinzi na usalama, miundombinu ya barabara, nishati, maji na TEHAMA.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ukweli kwamba CRDB, NBC na NMB hazina matawi Kikatiti, wananchi wa eneo hilo wanaendelea kupata huduma za kibenki kupitia kwa mawakala. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA K.n.y. MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-
Je, nini mpango wa kuwalipa Wazabuni wanaotoa huduma mbalimbali hususani chakula kwenye Shule za Serikali wanaodai kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utaratibu wa ulipaji wa madeni mbalimbali ikiwemo madeni ya wazabuni wa chakula waliotoa huduma katika shule mbalimbali. Ulipaji huzingatia upatikanaji wa mapato na uhakiki wa madeni unaofanywa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali kufanya uhakiki ni kutekeleza azma ya usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma kulingana na sheria ya Bajeti Sura Namba 439 na Sheria ya Fedha za Umma Sura Namba 348.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha inazielekeza halmashauri zote nchini kulipia huduma mbalimbali wanazopokea kutoka kwa watoa huduma kwa wakati ili kuepuka ulimbikizaji wa madeni na kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa watoa huduma, ahsante.
MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI aliuliza: -
Je, akaunti ya fedha ya pamoja ya Muungano imeshafunguliwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali mbili zinaendelea na mashauriano juu ya mapendekezo yaliyowasilishwa na Tume ya pamoja ya fedha kuhusu utaratibu wa kudumu wa kuchangia matumizi na kugawana mapato ya Muungano. Uamuzi wa pamoja utakapofikiwa na pande zote mbili za Muungano ndiyo utakaowezesha kufunguliwa kwa akaunti ya fedha ya pamoja, ahsante.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kwa matumizi ya Sarafu za Kidijitali (Central Bank Digital Currency) hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Benki Kuu ya Tanzania kwa sasa inaendelea na hatua ya utafiti wa uanzishwaji wa matumizi ya Sarafu za Kidijitali za Benki Kuu (Central Bank Digital Currency).
Mheshimiwa Spika, Benki Kuu imebaini kwamba, kama ilivyo kwa mataifa mengi, uanzishwaji wa Sarafu za Kidijitali za Benki Kuu, unahitaji kuanzishwa kwa uangalifu na umakini bila kuleta athari hasi katika mifumo ya malipo iliyopo nchini. Pia, kuweza kutatua tatizo halisi la malipo ambapo kwa sasa bado mifumo iliyopo nchini inakidhi hali halisi ya uwezeshaji mwananchi kutuma fedha na kufanya malipo.
Mheshimiwa Spika, aidha, soko letu bado linahitaji kuendelea kuboreshwa katika kuimarisha mifumo iliyopo kwa kutumia vyanzo vinavyopatikana kwa urahisi na wananchi wengi (simu za kawaida) tofauti na matumizi ya Sarafu za Kidijitali zinazoitaji matumizi ya simu janja (smartphones). Nchi nyingi ikiwa ni pamoja na majirani zetu na ukanda wetu bado wapo katika hatua hizi za awali za utafiti na kuboresha mifumo ya malipo iliyopo. Ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-
Je, lini Serikali itairejeshea Halmashauri ya Liwale fedha za miradi ya kimkakati iliyorudishwa Hazina ili iweze kujenga stendi ya Kisasa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa stendi ya kisasa ya Liwale ni moja kati ya miradi ya kimkakati ya kuongeza mapato kwa Halmashauri ambapo Serikali iliingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi kwa gharama ya shilingi bilioni 1.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Februari, 2024 kiasi cha shilingi milioni 452.8 kimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ambapo fedha hizi zimetolewa kulingana na madai yaliyowasilishwa kulingana na mpango kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka ujao wa fedha 2024/2025, kiasi cha shilingi milioni 412.8 kimetengwa kwa ajili ya mradi huo. Aidha, kwa shughuli ambazo hazikutekelezwa kulingana na mkataba kutokana na sababu mbalimbali, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale inaelekezwa kutenga bajeti ya kugharamia shughuli hizo. Azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa mradi wa stendi ya kisasa ya Liwale unatekelezwa kulingana na mkataba ulivyopangwa. Ahsante sana.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani kufuatilia na kuchukua hatua kwa Taasisi za Fedha zinatoa mikopo yenye riba kubwa kinyume na mwongozo wa BOT?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera, kiutawala na kisheria ili kudhibiti tabia ya baadhi ya taasisi za fedha kutoa mikopo kinyume na miongozo iliyopo. Hatua hizo ni pamoja na:
(i) Kusimamia utekelezaji wa Sera ya Fedha inayolenga kusimamia ukwasi katika mfumo wa kibenki ili kuendana na mahitaji halisi ya kiuchumi na kuweka mazingira rafiki ya utoaji mikopo.
(ii) Kuendelea kuhimiza benki kuwasilisha taarifa za wakopaji pamoja na kutumia kanzidata ya taarifa za wakopaji wakati wa uchambuzi wa maombi ya mikopo ili kupunguza vihatarishi vya ongezeko la mikopo chechefu.
(iii) Kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya fedha ili kumsaidia mwananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu fursa za mikopo zilizopo, viwango vya riba na athari zake, vigezo vya kuzingatia na umuhimu wa kurejesha mikopo.
(iv) Kuitisha vikao mbalimbali vya majadiliano na wadau katika sekta ya fedha ili kutambua changamoto zilizopo na kushirikishana mikakati ya kukabiliana nayo; na
(v) Kufanya kaguzi, ufuatiliaji na tathmini ya uzingatiaji wa sera, sheria na miongozo iliyopo ili kuboresha na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wale wanaobainika kukiuka taratibu hizo, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -
Je, lini Serikali itapeleka huduma ya benki ya NMB na CRDB kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha uchumi wa maeneo yote ya nchi ili kuweka mazingira yatakayovutia benki na taasisi za fedha kuanzisha huduma za kibenki katika maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki za NMB na CRDB hazina matawi kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Micheweni. Hata hivyo, wananchi wa Wilaya ya Micheweni wanapata huduma za kibenki kutoka Benki za CRDB na NMB kupitia mawakala wa benki, ambapo hadi kufikia Oktoba, 2024 kulikuwa na jumla ya mawakala wanne wa Benki ya CRDB na mawakala 14 wa Benki ya NMB wanaotoa huduma za kibenki katika Wilaya ya Micheweni.
Mheshimiwa Naibu Spika, uamuzi wa kufungua matawi ya benki hufanywa na benki yenyewe. Kabla ya benki kufanya uamuzi wa kufungua tawi jipya, benki husika hufanya upembuzi yakinifu ukiwa na lengo la kuangalia kama kuna uwepo wa biashara ya kutosha ambayo italeta faida kwa benki husika. Benki zikishafanya upembuzi yakinifu katika sehemu husika huwasilisha mapendekezo yao kwa Benki Kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Benki Kuu haina kizuizi chochote katika suala la benki kufungua matawi, kama benki husika itatimiza masharti yote ya kufungua matawi kama yalivyoanishwa katika kanuni namba 31 ya Kanuni za Utoaji Leseni za Benki na Taasisi za Fedha za mwaka 2014.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE aliuliza: -
Je, kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa wastaafu kuhakikiwa kwenye halmashauri au kata badala ya utaratibu wa sasa wa kuhakikiwa mkoani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, uhakiki wa wastaafu wanaolipwa na Hazina umekuwa ukifanyika katika ngazi ya halmashauri. Hata hivyo, ili kupunguza gharama za wastaafu kwenda kujihakiki na kuwaondolea usumbufu wa kusafiri umbali mrefu ili kupata huduma ya kuhakikiwa, Serikali inatengeneza mfumo wa kidigitali utakaowawezesha wastaafu kujihakiki wenyewe kupitia simu zao za mkononi au kwa kutumia huduma za kibenki.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilika kwa taratibu zote wastaafu watapewa elimu ya jinsi ya kujihakiki wenyewe na watatangaziwa siku ya kuanza kujihakiki, ahsante. (Makofi)
MHE. HAMISI S. TALETALE K.n.y. MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -
Je, ni nini msingi kwa wafanyabiashara kutoza bei tofauti au fedha za kigeni kwa wateja ambao ni raia wa kigeni na nini athari zake?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Serikali imeandaa sheria na kanuni ili kumlinda mlaji na kuhakikisha kuwa bei za bidhaa na huduma zinapangwa kwa msingi wa nguvu ya soko. Kwa mantiki hii, biashara zimekuwa zikiendeshwa chini ya utaratibu wa soko huria ambapo bei za bidhaa na huduma hupangwa kuendana na uwiano wa uhitaji na upatikanaji wa bidhaa husika. Hata hivyo, wafanyabiashara wanaweza kutoza bei tofauti kwa bidhaa na huduma baina ya wazawa na raia wa kigeni au kwa fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine Serikali inatambua na imeendelea kukumbusha kuwa shilingi ndio fedha halali kwa ajili ya malipo mbalimbali hapa nchini. Kutokana na hilo, raia wa kigeni hawatakiwi kulazimishwa kulipa kwa fedha za kigeni hususan pale wanapokuwa na shilingi za Kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, wageni wanaruhusiwa kutumia fedha za kigeni ili kurahisisha ufanyaji wa biashara pale wanapokosa shilingi za Kitanzania na viwango vya ubadilishaji fedha havikitakiwi kutofautiana na vile vinavyotozwa katika masoko ya fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna athari za kimsingi za uchumi kwa wafanyabiashara kutoza bei tofauti baina ya wateja raia wa kigeni na wazawa kwani bei hizo huamuliwa katika soko huru na hivyo inatarajiwa kupanda na kushuka kulingana na nguvu za mahitaji na ugavi sokoni, ahsante. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kurahisisha mfumo mzuri wa kutoa msamaha wa kodi kwa wakandarasi wanaojenga barabara Halmashauri ya Msalala?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, msamaha wa kodi kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kimkakati ya Serikali unatolewa kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani yaani VAT kama ilivyofanyiwa maboresho na Sheria ya Fedha ya mwaka 2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, maboresho ya sheria hiyo yalilenga kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji wa msamaha wa kodi ambapo awali mamlaka ya kutoa msamaha yalikuwa chini ya Waziri wa Fedha. Aidha, kwa marekebisho hayo, mamlaka ya kutoa msamaha yakakasimishwa kwa Kamishna Mkuu wa TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maboresho ya sheria, Serikali kupitia TRA, ilianzisha kitengo maalumu kwa ajili ya kushughulikia misamaha ya Kodi ya Ongezeko la Thamani. Kuanzishwa kwa kitengo hicho kumesababisha kuwa na muda mfupi zaidi wa kushughulikia maombi ya msamaha wa kodi hiyo ukilinganisha na wakati wa awali kabla ya maboresho hayo. Vilevile katika jitihada za kuongeza ufanisi na kutoa msamaha wa kodi ndani ya muda mfupi, Serikali ilianzisha mfumo wa kieletroniki wa kuwasilisha maombi hayo TRA (Tax Exemption Management System), ahsante. (Makofi)