MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na nitauliza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 52A, Waziri Mkuu ametajwa kuwa ndio mdhibiti, msimamiaji wa shughuli za Serikali za kila siku. Idara za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa zimekuwa zikitekeleza mpango, wakati huo huo zinajifanyia tathmini zenyewe. Mfano, hai ni Wizara ya Fedha na Mipango imekuwa na kitengo cha tathmini ndani ya Idara ya Mipango.
Mheshimiwa Spika, sasa ili tuweze kuisimamia na kuidhibiti Serikali ipasavyo: Je, hatuoni haja ya kuwa na taasisi inayojitegemea ya kuisimamia Serikali na kufanya tathmini, kutunga mifumo ya ufuatiliaji na tathmini nchini?
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mbunge wa Mkoa wa Tanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo umepata shida kulielewa vizuri lakini niseme suala la tathmini na kuona mwelekeo wa kazi hiyo baada ya tathmini, mbali ya kwamba tumeipa Wizara ya Fedha na tukaiita Wizara ya Fedha na Mipango, lakini bado kila Wizara na kila sekta yenyewe tunaitengea bajeti hapa Bungeni kwa ajili ya kujiwekea mpango wake na kwenda kufanya tathmini yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanapokuja awamu ya pili, wanaweza kuweka mipango yao kutokana na tathmini waliyoifanya msimu uliopita. Kwa hiyo, hatujaishia Wizara ya Fedha na Mipango pekee, kila Wizara na kila sekta tumeipa mamlaka hiyo na utakuta pia hata kwenye maombi ya fedha ya bajeti ya miradi kuna element ya usimamizi.
Mheshimiwa Spika, tunaposema usimamizi, maana yake wanakwenda kuikagua mipango waliyoiweka katika kipindi cha mwaka na kuitekeleza ili kupata mwelekeo wa kama: Je, wamefanikiwa au hawajafanikiwa? Kama hawajafanikiwa inawawezesha kuweka mpango ule kuwa endelevu kwa msimu ujao. Kwa hiyo, hiyo tumeishusha mpaka Wizarani na kwenye sekta zetu, hatujaishia kwenye Wizara ya Fedha pekee.
Mheshimiwa Spika, nalichukua hilo, tutafanya mapitio huku kuona swali lako limetokana na nini? Je, kazi hiyo inafanywa na Wizara ya Fedha pekee? Hapo baadaye naweza kukupa majibu kwa namna nyingine ili uweze kupata uelewa mpana juu ya wajibu huo na kama huko kuna udhaifu, basi tutaangalia na kuweza kuboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla wake, suala la mipango na tathmini lipo katika kila sekta.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, awali ya yote niipongeze Serikali kwa kuanzisha East Africa Commercial and Logistics Centre pale Ubungo ili kuwawezesha Watanzania waliokuwa wakihangaika kwenda China na mitaji yao midogo kuweza kujipatia bidhaa zao hapa nchini.
Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kuwalinda, kukuza na kujenga ushindani wa wawekezaji wazawa ikiwemo kutoa preferences kwa wawekezaji wa ndani na kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji wao na kuondoa vikwazo vinavyoweza kukwamisha uwekezaji na uzalishaji nchini ili zile bidhaa wanazoweza kuzalisha wao wazalishe badala ya kutegemea zile zinazoletwa na Wachina nchini?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri Mkuu.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, sikuyapata vizuri maelezo ya awali ya swali lake yaliyojenga msingi wa swali zima, kwa hiyo, naomba arudie tena.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ulenge uliza swali vizuri, fupi lieleweke.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kulinda na kukuza uwekezaji wa wawekezaji wazawa ikiwemo kutoa preferences kwa wawekezaji wa ndani na kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji wao ili zile bidhaa ambazo zinaweza kuzalisha nchini zizalishwe kuliko kutegemea kuletewa na Wachina?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ulenge, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa hamasa kwa wawekezaji wa ndani ili waweze kuwekeza na waweze kuzalisha bidhaa badala ya kutegemea bidhaa kutoka nje kama ambavyo Mheshimiwa engineer ameeleza kutoka China.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja tumetengeneza mazingira nafuu ya uwekezaji wa Mtanzania kwa kupunguza kiwango cha kuwa mwekezaji, tumepunguza kutoka dola 100,000 kuja mpaka dola 50,000. Hii inamfanya sasa mwekezaji wa ndani kuweza pia kutafuta mtaji. Akishapata dola 50,000 anaingia kwenye orodha ya wawekezaji na akishaingia kwenye orodha ya wawekezaji mazingira yanamwezesha Mtanzania kuweza kuwekeza moja anapata mazingira rahisi ya kupata ardhi, mwenyeji anamiliki ardhi, lakini wageni wanapata hati tu ya kuwa wawekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbili; tumeona namna ambavyo bidhaa hizi zinavyoweza kuwekezwa na kufanyiwa biashara, hivyo tumetengeneza mazingira ya kumwezesha mfanyabiashara huyu au mwekezaji huyu kuendesha biashara yake katika mazingira rahisi. Tumeweka fursa na tumetengeneza mazingira ambayo yatamfanya afanye biashara vizuri, tumepunguza kodi, tumehakikisha kuwa hatua zile za kupata ardhi zinarahisishwa zaidi, lakini pia uendeshaji wa biashara anayoizalisha kama kuna biashara inazalishwa ndani ya nchi na kuna biashara aina hiyo hiyo inatoka nje ya nchi, ile inayotoka nje ya nchi tumeiongezea kodi ili kuipa nafasi hii kuingia kwenye masoko na kuweza kupata masoko yake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira haya tumeendelea kuwahamasisha kwa Watanzania, lakini pia tumeweka masharti ya wawekezaji wa nje wanapokuja kuwekeza Tanzania lazima waambatane na Mtanzania kuwa mwekezaji mwenza ili Watanzania wapate nafasi ya kuwa wawekezaji wakubwa hapa ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mazingira haya yote tumeendelea kufanya maboresho ya uwekezaji ndani ya nchi na kuhakikisha kuwa kila mwekezaji ambaye ni Mtanzania anafuata mazingira hayo ili kumwezesha kuwekeza kwa urahisi na kwa gharama nafuu na masoko yake tunayo ndani ya nchi, lakini na nchi jirani na tumeendelea kujenga mahusiano na nchi jirani kwa kuja kufanya biashara ili wawekezaji wetu waweze kuwekeza vizuri na kupata faida kwenye uwekezaji wao. (Makofi)