MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Upungufu wa watumishi katika Halmashauri zetu limekuwa ni tatizo kubwa sana; na kwa mfano tu, Halmashauri yangu ya Mkalama ina upungufu wa zaidi ya walimu 800; na kwa kuwa nchi yetu sasa haina tatizo la wataalam na vijana wengi wanasubiri ajira: -
Mheshimiwa Spika, kwa nini sasa Serikali isianze kujaza nafasi wazi mara moja pale mtumishi anapostaafu au anapotangulia mbele ya haki kwa sababu mtumishi huyo tayari yuko kwenye bajeti inayoendelea, badala ya utaratibu wa sasa wa kusubiri Halmashauri ziombe vibali jambo ambalo huchukua muda mrefu na linaongeza ukubwa wa tatizo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mkalama kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ndani ya Serikali kupitia Wizara ya Ofisi ya Rais, Utumishi imeweka utaratibu mzuri tu wa kupata watumishi katika kuziba mapengo au watumishi wapya. Pale ambapo inatokea bahati mbaya mtumishi ametangulia mbele za haki, tunao utaratibu wa kujaza pia kwa kutangaza nafasi mpya, lakini hili linafanywa baada ya kufanya uhakiki wa kina kwa vipindi vya miezi mitatu, miezi sita au mwaka ili kuona tuna upungufu wa watumishi kwa kiasi gani; na wangapi wa kada ipi wanahitajika kujazwa?
Mheshimiwa Spika, kupitia Wizara ya Utumishi, Tume ya Utumishi wanacho kitengo maalum ambayo pia wanafanya uratibu kupitia Wizara zote na mahitaji yake. Kwa hiyo, unaweza kuona tunachelewa kutangaza nafasi hizo kwa sababu kwanza lazima tupate data base ya mapengo ya watumishi wa Serikali kwa kada na Idara, ili tuone Idara hii tutakapotangaza, mahitaji ni mangapi kwa ajili ya Wizara zote; ili tutakapotangaza, tunatangaza mara moja kwamba tunahitaji watumishi 1,000 halafu wanagawiwa kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kazi hii inapofanywa katika kipindi cha miezi sita au mwaka tunaona kama inachelewa lakini inasaidia Serikali pia kutambua idadi ya wafanyakazi waliopo na mahitaji, lakini pia na kuziba, halafu tuendelee kusimamia maslahi yao wakati wote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi hilo la kuziba mapengo linaendelea, kuanzisha sekta mpya na kujaza sekta hizo. Kwa ujumla vibali hivi vinapokamilika utafiti huu, tunaomba kibali kwa Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Rais Mama Samia tunamwona anatoa vibali wakati wote kwa ajili ya kuajiri kada mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwahakikishie tu kwamba kazi hiyo inaendelea kufanyika na mamlaka husika hupeleka takwimu na taarifa Wizara ya Utumishi kupitia Tume ya Utumishi na zinatangazwa wakati wote. Ahsante sana. (Makofi)