Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jacquline Andrew Kainja (21 total)

MHE. JACKLINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii niweze kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na kwamba tunajua Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inajitahidi kupunguza ajali za bodaboda, tukiangalia kwa mwaka 2019 tulikuwa na ajali 567 lakini mwaka 2020 tuna 240. Je, Jeshi la Polisi lina mpango gani wa kuhakikisha ajali hizi zinapungua zaidi? Tukiangalia wahanga wakubwa ni vijana na wanawake ndiyo wanaopata shida ya kupoteza vijana ambao ni nguvukazi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; utafiti unaonyesha askari wastaafu wanachelewa kupata mafao yao, je, Wizara husika ina mpango gani wa kuhakikisha askari hawa baada ya kustaafu wanapatiwa mafao yao kwa haraka ili kuepusha wanapokuwa kazini kuchukua rushwa ili kujilimbikizia akiba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika jibu la msingi inaonekana Mheshimiwa tumempa sababu moja au njia moja ambayo tunaweza tukaitumia katika kuepuka hizi ajali. Zipo njia ambazo tumeshazichukua kama Serikali na nyingine tuko mbioni kuzichukua kwa kushirikiana na Wizara nyingine au kushirikiana na taasisi nyingine kuhakikisha kwamba hizi ajali za barabarani zinapungua. Cha kwanza tumefikiria kuendelea kuwafundisha zaidi hasa vijana wa bodaboda namna ya kutumia alama za barabarani ambazo zina uwezo mzuri wa kuwaeleza kwamba wanakoelekea wanaweza wakapata ajali.

Mheshimiwa Spika, lingine tuna mpango sasa wa kutengeneza mfumo wa kufunga au ku-control ajali kwa kutumia vidhibiti mwendo, ambapo tunahisi hivi vinaweza kupunguza ajali. Pia tuna mpango wa kufanya marekebisho ya sheria ambayo yanakwenda moja kwa moja kwenye masuala ya faini na adhabu katika mambo haya ya usalama barabarani.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge atusaidie pia kuwaelimisha vijana kwa sababu naamini katika mkoa wake vijana wa bodaboda wapo, basi azidi kuwaelimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kujibu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kuhusu mafao ya Askari. Kwa kweli Wizara inajitahidi sana kuhakikisha kwamba tunawalipa wastaafu posho zao mara tu baada ya wao kustaafu. Katika kipindi cha 2018/2019 tumejitahidi kati ya wastaafu 591; jumla ya wastaafu 479 tayari tulishawapatia mafao yao na sasa hivi wengi wanaishi maisha mazuri.

Mheshimiwa Spika, kikubwa kinachokuwa kinatukabili kama sehemu ya changamoto, inafika wakati inakuwa OC nazo na bajeti nayo inakuwa mtihani, kwa hiyo, ndiyo maana kuna wakati wanachelewa kidogo kulipwa. Hata hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kama itakuwa kuna mtu ambaye hajapata mafao yake na amestaafu, basi tukitoka hapa tuonane, tuone tunamsaidia vipi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na jitihada nzuri za Wizara inavyofanya kuzitangaza zao la asali nchini, lakini bado hatujafanya vizuri kwa masoko ya nje ambayo inapelekea wafanyabiashara wengi wa nchini wanashindwa kufanya vizuri kwa masoko ya nje hususan ni Mkoa wa Tabora na tukiangalia kinamama wengi wa Mkoa wa Tabora wamejikita kwenye uvunaji wa asali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Wizara inakuja na mkakati upi kuhakikisha soko la nje la zao la asali linafanya vizuri kama ambavyo zao la asali linafanya vizuri ndani ya nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, pamoja na jitihada nzuri zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuhakikisha zao la asali linaendelea kuwa na thamani, mpaka kupata wafadhili kutoka Umoja wa Ulaya.

Je, Wizara imeweka mikakati ipi na mipango madhubuti ya kutenga pesa kwa ajili ya kuhakikisha mradi huu walioweka kusaidiwa na Umoja wa Ulaya unaweza kuendelea hata kama mradi ule, hata kama wafadhali watachelewesha pesa au hawatoleta pesa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jacqueline, Mbunge wa Viti Maalum Tabora kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tabora Mheshimiwa Jacqueline kwa kuona umuhimu wa zao hili la asali. Ni kweli Tanzania tunafaidika kwa asilimia kubwa kwa soko hili la asali kuuza ndani na nje ya nchi. Mkakakati wa Wizara na Serikali kwa ujumla ni kuhakikisha kwamba asali yetu inakuwa na ubora zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba kwa sasa hivi wizara inashikirikiana na Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani kupeleka sampuli za kemikali za asali ambazo huwa zinachakatwa na kuangalia ubora wa asali ya Tanzania. Na kwa asilimia 90 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 tulipeleka asali yetu ya Tanzania na ikaonekana kwa asilimia 90 ni nzuri na inafaa kuuzwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Tanzania sasa itaanza kupeleka asali kwenye nchi za Ulaya na Marekani kwa kuwa tumekidhi vigezo vya viwango vya ubora wa asali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwenye mikakati ya kutenga fedha nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa sasa tuna mkakati wa kuanzisha viwanda vitano. Viwanda vitatu tayari vimeshajengwa na viwili tunakarabati. Lakini pia hii ni mwanzo wa kuhakikisha kwamba tayari tuna vyanzo vyetu sisi wenyewe bila kutegemea misaada mingine ambavyo vitaweza kukusanya asali yote nchini na itachakatwa kwenye viwanda hivi na kuhakikisha soko la ubora wa asali linapatikana na tunaweza kuuza nje na ndani ya nchi. Ahsante. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Kutokana na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri yanayowapa matumaini wafanyabiashara wa usindikaji wa mbogamboga hasa kwa Mkoa wa Tabora hususan kinamama.

Je, ni lini Serikali kushirikiana na FAO inaweza kuanza mradi huu wa kuwawezesha kina mama kuweza kufanya biashara ya Kitaifa na Kimataifa?

Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi kuwezesha mazao haya ya usindikaji wa mbogamboga ambayo wakinamama wengi wa Mkoa wa Tabora wamejikita katika biashara hiyo kuhakikisha kwamba yanakuwa yana masoko ndani ya nchi na ukizingatia unaweza ukaenda kwenye hoteli nyingi hatuna mboga za asili, tunatumia mboga ambazo ni roast na zilizoungwa ungwa zaidi. Naomba kupata jibu, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naoba kumjibu Mheshimiwa Jacqueline maswali yake ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, lini tunaanza mradi wa FAO, tunaaza mwaka wa fedha unaokuja; ni mradi wa miaka mitano, tunaanzia majaribio katika Wilaya ya Kaliua ndipo tutakapoanzia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kuwasaidia wakinamama wa Mkoa wa Tabora na Watanzania wote kuweza kuingia katika masoko. Sasa hivi tunapata project pamoja na wenzetu wa SIDO ili waweze kukidhi vigezo vya viwango vinavyoweza kuwasaidia kuingia katika masoko ndio maana mmesikia katika Mkoa wa Tabora tumesema kwamba Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Umoja wa Wanyabiashara sasa hivi pamoja na SIDO inatafutwa eneo moja ambalo litakuwa ni center ya kina mama kwa ajili ya kukaushia na hapo kuweza kufanya packaging waweze ku- meet standard za masoko. Kwa hiyo, ni hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo la msingi sio tu kuzalisha, je tunachokizalisha kinaweza kukidhi vigezo vinavyotakiwa vya sokoni, hiyo ndio kazi tunayoifanya katika sekta ya mbogamboga na matunda.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwamba na wewe umeweza kuona hili swali halijajibiwa na mimi nimegundua hivyo, lakini nimpongeze Waziri kwa majibu mazuri yanayoonyesha namna gani Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan imeendelea kupanga bajeti kuendelea kuhakikisha maboma ambayo yanatakiwa kukamilishwa yakamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tu nipatiwe majibu mazuri, ambayo yanaendana na swali langu ili niweze kuridhika sasa kwamba ni lini Serikali inaweza ikaona kuna mpango mzuri kwenye hizi Kata ambazo ni kubwa hazina zahanati ili wananchi hawa waweze kupata zahanati na siyo kwamba kuna maboma hakuna hata hayo maboma ambayo yanatakiwa kukamilishwa yaani ni ujenzi mpya, Serikali ina mpango gani na njia ipi madhubuti kuhakikisha kwamba Kata ambazo ni kubwa mfano, Kata hii ya Ng’ambo ambayo iko Tabora Mjini na zingine nyingi ambazo sijaziainisha zinaweza kupata ufumbuzi huo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa sasa Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwanza tunamaliza ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Tarafa zote nchini. Tangu uhuru tulikuwa tuna Tarafa 570 na tulikuwa na Tarafa 363 tu pekee ambazo zilikuwa na Vituo vya Afya na katika Awamu ya sasa hivi tulikuwa na Vituo vya Afya kama 207 ambavyo Serikali tayari imeshapeleka fedha kwa awamu mbili ambazo nafikiri kila Mbunge anazo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tukija kwenye level ya zahanati kwa kila Kijiji lengo la Serikali ambalo tumeliweka na ndiyo maana nimejaribu kuelezea hapa fedha ambazo tumezitenga ni kwa ajili ya kwenda kumalizia zahanati ambazo zimeanzishwa na nguvu za wananchi na nyingine zimeanzishwa na mapato ya ndani ya Halmashauri na ndiyo maana kwenye swali hili la msingi lilipokuwa linaulizwa, tumemshauri Mbunge wa Jimbo na Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Tabora kwamba, hamasisheni wananchi mkishirikiana na vyanzo vya ndani muanze ujenzi ili sisi kutoka Serikali Kuu tulete fedha kwa ajili ya kumalizia hiyo zahanati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukisema kwamba tutajenga zahanati vijiji 12,000 kwa wakati mmoja kwa sasa hivi hatuwezi kudanganya kwenye hilo, ukweli wetu ni kwamba tunamaliza Vituo vya Afya Tarafa zote, tunamaliza Hospitali katika Halmashauri zote halafu kwenye ngazi ya vijiji tutapeleka fedha, kwenye vijiji vyote ambavyo zahanati wananchi wamepeleka nguvu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hilo ndiyo jibu letu, ahsante. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa jibu zuri la Serikali, lakini kutokana na umuhimu wa hospitali hii ya Kanda ambayo inajumuisha mikoa mitatu; Kigoma, Katavi na Tabora; nataka majibu ambayo yataweza kutuonesha Wana-Kanda ya Magharibi ni lini hasa hospitali hii itaanza kujengwa kutokana na kwamba eneo lilishatengwa kama ambavyo amesema na katika Kata ya Magili kwa hekari 200? Hii itasaidia wananchi wasianze kufanya shughuli za maendeleo kwa kuzingatia ni muda mrefu mchakato huu walishasema utafanyika lakini bado haujafanyika.

Je, Serikali inaweza kutueleza ni lini hasa kazi hii inaweza ikafanyika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ambavyo nimeshaeleza kwenye swali la msingi kuhusu tathmini; kwanza fedha za kwanza ambazo makadirio ya kuanza, kwa sababu ni fedha ambazo hazitamaliza, lakini zimeshatengwa shilingi bilioni 10 za kuanza, lakini kazi inayofanyika ni kuangalia kwenye mikoa hiyo kuhusu umbali, kwa sababu hatuangalii tu Hospitali ya Kanda kwamba tunaweka Magharibi au wapi, tunaangalia ni mikoa ipi na ni mkoa upi upo mbali na facilities kama hizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukiangalia kutoka Tabora kuja Benjamin Mkapa ni Kilomita ngapi? Tabora kuja hospitali nyingine ya Kanda ni Kilomita ngapi? Hii itasaidia tuweze kuamua eneo sahihi ambalo huduma itawasogelea wananchi walio wengi na tuangalie eneo ambalo vile vile huduma nyingine ziko mbali na wananchi ambazo wengine wako karibu nazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, upembuzi bado unafanyika ili kutambua eneo ambalo hospitali itaenda kuwekwa kwa kutumia busara kusogezea huduma wananchi walio wengi zaidi. Ahsante.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha usanifu wa matenki na michoro ya miundombinu katika Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria inayoenda katika Miji ya Urambo, Sikonge na Kaliua inaisha? Kwani usanifu huu ulitakiwa uishe Desemba, 2022 na ukizingatia Miji hii tayari ipo kwenye exemption ya kodi ili Mkandarasi aweze kwenda site na wananchi wa maeneo haya waweze kupata maji kwa urahisi. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jacqueline, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, usanifu ulipaswa kukamilika Desemba na sasa ni Januari, tuko mwishoni kabisa kukamilisha na lengo letu ni kuhakikisha dhumuni la kupeleka maji maeneo haya aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge tunakwenda kukamilisha kwa wakati.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nishukuru majibu mazuri ya Serikali. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali bado tuna changamoto nyingi hasa kwenye upande wa magari katika taasisi hii ili waweze kufanya kazi zao vizuri na kurahishisha kazi zao;

Je, Serikali ina mpango gani kuhusiana na masuala mazima ya magari ya usafiri kwa Taasisi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili;

Je, Seriikali ina mpango gani wa kuongeza watumishi katika Taasisi hii, ambao bado maeneo mengi tuna changamoto kubwa ya watumishi kwenye taasisi hii, ili waweze kufanya kazi vizuri na tukiangalia Taasisi hii ina - deal na masuala ya rushwa na bado tuna changamoto nyingi sana katika nchi hii kuhusu suala la rushwa?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto ya usafiri, hili linachukuliwa umuhimu wa pekee, na hata kwenye bajeti ijayo tunaomba nafasi ya kuongeza vyombo vya usafiri, ili kuwasaidia maafisa wetu wa TAKUKURU kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile suala la kuongeza watumishi tunaendelea nalo ni zoezi endelevu. Kwa ushahidi Waheshimiwa Wabunge wote mnajua hata mwaka huu TAKUKURU ilipata nafasi na mpaka sasa kwenye kipindi hiki, bado wanaendelea na mchakato. Tangazo lao la mwisho lina kama wiki mbili hivi bado wanaendelea kufanya mchakato wa kupata watumishi zaidi. Kwa hiyo hili zoezi la kuongeza watumishi ni zoezi endelevu kulinganna na upatikanaji wa fedha na namna Serikali itakavyopata nafasi ya kuongeza nafasi zaidi.
MHE. JACQUELINE K. ANDREW: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili. Swali langu la kwanza; katika mikoa yetu ambayo ina hifadhi changa, Wakuu wetu wa Mikoa wamejitahidi kujitokeza

kuhakikisha wanatangaza utalii katika hifadhi hizi changa. Je, Serikali ina mpango gani katika kuhakikisha inasaidia viongozi hawa wa mikoa ili kuweza kukuza utalii katika hizi hifadhi changa na tukizingatia bado miundombinu ni mibovu, magari pia hayatoshi, wanapata wakati mgumu hasa wanapokuwa wanafanya kazi za kutangaza hifadhi hizi kujikuta sasa inabidi waazime magari kutoka sehemu zingine, tunaonaje kama Serikali tuweze kusaidia kutangaza sekta hii ya Maliasili na Utalii?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; bado tunachangamoto nyingi kwenye upande wa ajira. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha ajira zinapatikana na kukuza sekta hii ya utalii hasa katika hifadhi hizi changa, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jacquiline Kainja, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali kwa sasa imejikita katika maeneo mapya ya utalii zikiwemo hifadhi hizi ambazo imezitaja na malengo makuu ni kuhakikisha kwamba tunapanua wigo wa namna ambavyo watalii wataweza kufika katika maeneo hayo. Mikoa yote ya Tanzania tumeendelea kuwahimiza waendelee kuhamasisha utalii ikiwemo utalii wa ndani lakini pia tumejikita kuboresha miundombinu zikiwemo barabara, maeneo ya malazi na chakula ili sasa iwe rahisi kwa watalii kuweza kufika katika maeneo hayo. Kwa hiyo tunaendelea kuwahimiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya waendelee kuhamasisha masuala mazima ya utalii.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ameongelea kuhusu ajira. Tumeendelea kuwasiliana na Ofisi ya Rais, Menejimenti Utumishi na Utawala Bora kuangalia namna ya kuongeza watumishi ambao tutawasambaza katika maeneo mapya yaliyoko katika hifadhi hizo.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuulizwa maswali mawili ya nyongeza.

Swali langu la kwanza, je, ni kiasi gani GST imewezeshwa kufanya kazi?

Swali langu la pili, je, Serikali ina mpango gani mahsusi kuhakikisha Watanzania wananufaika na madini haya yanayopatikana nchini Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jacqueline Kainja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la kwanza GST katika bajeti hii ambayo ilipitishwa na Wizara ya Madini imetengewa kiasi cha fedha shilingi bilioni mbili na milioni mia nne kwa ajili ya shughuli zake mbalimbali ikiwemo kipande kidogo kwa ajili ya utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli hizi za utafiti zinahitaji fedha nyingi sana kwa hiyo shilingi bilioni 2.4 peke yake haitoshi, wenzetu wa GST tayari wameshaanza kufanya proposal za kupata fedha kutoka maeneo mengine ili kuweza ku-complement kwenye zile fedha ndogo ambazo wanazo kwa ajili ya kukamilisha hii kazi ambayo wamepatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili ni mkakati wa Serikali ambao unafahamika wazi kwamba madini yanayochimbwa Tanzania yanawanufaisha Watanzania wote, uniruhusu nitoe mfano mmoja kwa juzi Barrick imetoa CSR kiasi cha shilingi bilioni 30 ambayo kwa kuanzia imetoa Shilingi Bilioni 10, hata sisi ambao hatuko katika yale maeneo ya mgodi tumepata fedha hiyo. Kwa hiyo, Watanzania wote Serikali imeweka mpango wa kuhakikisha kwamba kila mmoja anayetakiwa kunufaika nayo ananufaika kwenye eneo lake.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, ni pikipiki 85 zilizotoka kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii zimetoka kwa Mikoa 21 na Mkoa wangu wa Tabora zimetoka pikipiki nne. Pikipiki mbili zimeenda Wilaya ya Urambo kwa Kata ya Kazaroho na Uyumbu na zingine zimeenda Kaliua. Sasa Serikali ina mpango gani kuhakikisha inatenga pikipiki nyingi za kutosha kwa ajili ya kuwezesha Afisa Maendeleo, kwa ajili ya kazi hizi za kufatilia mikopo?

Swali la pili, Kanuni ya utoaji mikopo Februari 2021 iliwaagiza Wakurugenzi kutenga pesa 500,000 hadi milioni 5,000, 000 kwa ajili ya ufuatiliaji wa mikopo lakini siyo kila Halmashauri ina uwezo wa kuwa na pesa za kutosha. Swali langu kwa Serikali, haioni kama na Serikali yenyewe ni chanzo cha mikopo hii chefuchefu ambayo tunashindwa kukusanya na kufuatilia vikundi hai na ambavyo siyo hai.

Je, ina mpango gani kuhakikisha sekta hii ya Maafisa Maendeleo ya Jamii wanapata vitendea kazi vya kutosha? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Jacqueline Kainja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la kwanza la utengaji wa pikipiki hizi nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utengaji au upatikanaji wa pikipiki hizi kigezo cha kwanza ni upatikanaji wa bajeti. Kwa hiyo, kama Serikali tutaendelea kutenga bajeti ili tuweze kuwafikia wananchi wote ikiwezekana Kata zote au Wilaya zote za Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili kwamba Halmashauri nyingine hazina uwezo wa kutenga pesa kwa ajili ya kupeleka Maafisa wetu kwenda kuangalia au kufuatilia vikundi hivyo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa haya pia ni maelekezo ya Serikali kwamba Wakurugenzi wote katika Halmashauri zote wahakikishe kwamba wanaendelea kutenga fedha kama ambavyo imeelekezwa na wale ambao watashindwa maelekezo yetu ni kwamba wawasiliane na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kuona ni jinsi gani tunatatua tatizo hilo. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa majibu mazuri ya Wizara, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuweka motisha kwa Walimu walioko vijijini, ili tuweze kupata Walimu wengi waweze kwenda kuajiriwa vijijini ili tuweze kuondokana na upungufu maeneo ya vijijini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Serikali haioni kuna haja ya ajira hizi zinazotoka nyingi zielekezwe vijijini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza aliyouliza Mheshimiwa Kainja. La kwanza hili la motisha kwa Walimu vijijini, tayari Serikali inalifanya hili kwa kupitia Wakurugenzi wa Halmashauri husika, kuna Halmashauri ambazo Walimu wanaporipoti kazini wamekuwa wakipatiwa magodoro na vifaa vingine vya kuweza kuwapa motisha kubaki katika maeneo yao ya kazi. Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kule imekuwa ikifanya hivyo na maeneo mengine nchini na tutaendelea kuona ni namna gani tunatoa motisha kwa Walimu hawa wanaoenda vijijini kadri ya upatikanaji wa fedha na uwezo wa Serikali na bajeti kuruhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, la haja ya ajira hizi hawa Walimu kwenda vijijini. Walimu hawa wanaajiriwa kutokana na upungufu uliopo kwenye maeneo husika hasa maeneo haya ya vijijini. Sasa naomba nitoe rai hapa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ambao ndio waajiri wa Walimu hawa na wale wa Mkoani Tabora kule anakotoka Mheshimiwa Kainja vile vile, kuhakikisha kwamba hawa wanaopangiwa maeneo haya kwenda kufundisha wanabaki kule kwenye maeneo yale kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma. Kwa sababu Serikali ilifanya review ya maeneo yote yenye upungufu wa Walimu na ndiyo maana hawa wanaajiriwa kwenda kuziba mapengo yale yaliyokuwepo kwenye maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kila mmoja akiomba kuhama, ina maana mapengo yale yanazidi kuwepo. Vile vile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote Serikali itaendelea kuajiri Walimu hawa kwa ajili ya kuziba mapengo haya na upungufu uliopo kadri ya bajeti itakavyoruhusu.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza; kwa nini Serikali inapotenga pesa za majengo ya zahanati na vituo vya afya isitenge sambamba na pesa za vifaa? Kwa sababu mara nyingi majengo yanafunguliwa wakati vifaa hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; nini tamko la Serikali kwa majibu mazuri yaliyojibiwa hapa kwamba kuna pesa zimetengwa kwa ajili ya vifaa, tamko la Serikali katika Mkoa wetu wa Tabora kwa zahanati ambazo hazina vifaa na tayari wananchi wanachangishwa pesa za mabenchi kama Zahanati ya Goweko, Kalangale, Wilaya ya Uyui lakini vilevile Wilaya ya Igunga, Kagongo, Kata ya Itunduru na Ibuta - Kata ya Mbutu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, la kwanza, kwa nini Serikali isitenge fedha ya vifaa tiba kwanza; kimekuwa ni kipaumbele cha Serikali kujenga miundombinu kwanza ili huduma zile za msingi ziweze kuanza kutolewa na baada ya kuwa majengo yale yamekamilika na huduma za msingi kuanza kutolewa, ndipo Serikali inatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na kuvipeleka kwenye zahanati hizo.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilisema kwenye majibu yangu ya msingi, katika mwaka huu wa fedha ambao tunaumaliza, Serikali ilitenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba ambapo tayari bilioni 12.90 imeshanunua vifaa tiba hivyo na vimeanza kusambazwa katika zahanati zote nchini.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili; tamko la Serikali kwa zahanati kupata vifaa tiba katika Mkoa wa Tabora anaotoka Mheshimiwa Mbunge, Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika kuhakikisha vifaa tiba vinakuwa katika zahanati zote, vituo vyote vya afya vilevile katika hospitali za wilaya kote nchini katika kuhakikisha afya za Watanzania zinaboreka.

Mheshimiwa Spika, na kwa ajili ya kutekeleza hilo, Serikali imetenga shilingi bilioni 112 kwenye mwaka wa fedha 2023/2024 na vifaa tiba hivyo vitaanza kununulia mara moja mwaka wa fedha unapoanza, na tutaanza kuvisambaza katika maeneo yote nchini ya zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya, yakiwemo maeneo yale ambayo ameyataja Mheshimiwa Jaqueline Kainja.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi. Kwa kuwa Mkoa wetu wa Tabora una maeneo mengi ya kutosha na wafugaji ni wengi; nini mpango wa Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye viwanda vya maziwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kweli kama nilivyosema Tabora pia ni eneo ambalo kuna wafugaji wengi na ng’ombe wengi, kama nilivyosema hamasa kubwa ni kuona tunaendelea kuhamasisha uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani pia hata wa nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwaomba watanzania wenzangu hata Wabunge wenzangu kuendelea na kushiriki, kutumia fursa hizi zilizopo katika maeneo yetu. Bahati nzuri, Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kodi nyingi kwenye maeneo haya kwenye viwanda vya maziwa, kwenye storage facilities. Kwa hiyo, tutumie fursa hii kuwekeza huko ili tuweze kukwamua au kuwasaidia wafugaji ambao wanakosa soko la kuuza maziwa yao ambayo naamini tukizalisha bidhaa zinazotokana na maziwa tutapata fursa kubwa ya kuuza ndani ya nchi pia nje ya nchi kwa sababu tayari bidhaa hii inahitajika sana, nakushukuru sana.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi. Kwa kuwa Mkoa wetu wa Tabora una maeneo mengi ya kutosha na wafugaji ni wengi; nini mpango wa Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye viwanda vya maziwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kweli kama nilivyosema Tabora pia ni eneo ambalo kuna wafugaji wengi na ng’ombe wengi, kama nilivyosema hamasa kubwa ni kuona tunaendelea kuhamasisha uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani pia hata wa nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwaomba watanzania wenzangu hata Wabunge wenzangu kuendelea na kushiriki, kutumia fursa hizi zilizopo katika maeneo yetu. Bahati nzuri, Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kodi nyingi kwenye maeneo haya kwenye viwanda vya maziwa, kwenye storage facilities. Kwa hiyo, tutumie fursa hii kuwekeza huko ili tuweze kukwamua au kuwasaidia wafugaji ambao wanakosa soko la kuuza maziwa yao ambayo naamini tukizalisha bidhaa zinazotokana na maziwa tutapata fursa kubwa ya kuuza ndani ya nchi pia nje ya nchi kwa sababu tayari bidhaa hii inahitajika sana, nakushukuru sana.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Mkoa wetu wa Tabora ni wa tatu kwa ukubwa kwa population na vilevile, ni wa kwanza, kijiografia, Serikali haioni kuna haja ya kutuwekea walimu wengi wa kutosha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, idadi ya walimu wa shule za msingi tunayohitaji kwa mkoa wetu ni 19,666 na waliopo ni 8,950; upungufu ni 10,716. Je, Serikali ajira zinazofuata imepanga Mkoa wetu wa Tabora kutuletea walimu wangapi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, la kwanza hili haioni haja ya kuweka walimu wengi zaidi Tabora? Naomba kwa ridhaa yako nijibu yote mawili kwa pamoja kwa sababu yanakaribiana.

MWENYEKITI: Ndiyo.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la kwanza la kwamba haioni haja ya kuweka walimu wengi Mkoa wa Tabora; na la pili, je, ajira za walimu zinazofuata kama Mkoa wa Tabora nao utapata mgao wa walimu hao; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali hii inatambua upungufu wa walimu uliopo na ndiyo maana inaendelea kuajiri walimu kadri ya upatikanaji wa fedha. Pale ambapo ajira hizi zitatangazwa hivi karibuni kama alivyotoa tangazo Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, basi ajira zile zikishakamilika na hao walimu kupatikana, Mkoa wa Tabora ni kati ya mikoa ambayo itapewa kipaumbele kwa ajili ya kuweza kupata walimu hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ajira zilizopita katika mwaka wa fedha uliopita, Mkoa wa Tabora ulipata walimu jumla 262 wa sekondari na walimu 476 wa shule za msingi. Kwa hiyo, Serikali imekuwa ikipeleka walimu katika Mkoa wa Tabora kwa kutambua ni Mkoa mkubwa na una watu wengi.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nimeuliza maswali kuhusu uzio wa shule za mabweni za wasichana. Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa pamoja kwa ajili ya ujenzi wa majengo, madarasa pamoja na mabweni ili ziende sambamba na uzio wa shule hizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; mwaka 2023 Shule ya Sekondari ya Uyungu, Kidato cha Sita walivamiwa na vibaka. Je, hawaoni sababu ya kuweka uzio katika shule hizo ambazo ni Shule ya Margaret Simwanza Sitta pamoja na Shule ya Sekondari ya Urambo Day?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, amekuwa ni mtetezi mkubwa sana wa mazingira ya wanafunzi kwa kuhakikisha wanasoma katika mazingira yaliyo mazuri, bora na yenye usalama zaidi. Naomba nijibu maswali yake yote mawili kwa pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa miundombinu ikiwemo hiyo ya uzio. Kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu yangu ya msingi, kwamba Serikali imeweka kipaumbele zaidi katika ujenzi wa miundombinu ya msingi ambayo inawawezesha wanafunzi wote kupata fursa ya elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa uzio katika shule zetu hizi, naomba nimkumbushe Mkurugenzi wa Halmashauri afanye tathmini na kuweka katika mipango ya kibajeti katika halmashauri inayotokana na mapato ya ndani ili kuona kwa kadiri fedha zitakapokuwa zinapatikana waweze kujenga uzio huo.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali vitabu ambavyo vimesambazwa na ambavyo havijasambazwa ni sawa sawa na asilimia tisa; je, Serikali imejipanga vipi kukamilisha asilimia tisa zilizobaki?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kutokana na Jiografia ya Mkoa wetu wa Tabora na ukubwa na ni ya kwanza kwa ukubwa kwa nchi nzima. Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuhakikisha mkoa huu unapata kipaumbele katika usambazaji wa vitabu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jacqueline, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna baadhi ya mikoa ambayo vitabu hivi havijafika kwa 100% na naomba niitaje mikoa hiyo kama ifuatavyo: ni Mkoa wa Iringa, Katavi, Mara, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga, Simiyu, Songwe pamoja na Tabora aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kazi ya upelekaji wa vitabu hivi vilivyosalia asilimia tisa inaendelea na tunakadiria mpaka kufika mwisho wa mwezi huu tutakuwa tumekamilisha usambazaji wa vitabu hivi kwa 100%.

Mheshimiwa Spika, katika eneo lake la pili kuhusiana na suala la Tabora kuipa kipaumbele, nimwondoe wasiwasi kwa vile tunatarajia ndani ya mwezi huu vitabu hivi viwe vimefika katika mikoa yote ukiwemo na Mkoa wa Tabora basi na Mkoa wa Tabora nao tutaupa kipaumbele kuhakikisha kwamba ndani ya Mwezi huu wa Tano vitabu hivi vyote vinafika kwa 100%, nakushukuru.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; tuna taasisi kubwa ambayo imewekeza katika wilaya zote za nchi hii viwanja vizuri vya mpira lakini ni chakavu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inashirikiana na taasisi hii ili kuboresha viwanja hivi hasa katika halmashauri ambazo hazina mapato ya kutosha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; tuna wilaya 139 katika nchi hii na ambazo Waziri mejibu katika swali langu ambazo zimeanza kufanya marekebisho ni wilaya sita. Je, wameshafanya tathmini ya kuangalia bajeti ya Wilaya zote, ukarabati wa viwanja ni kiasi gani ili wanapoelekeza halmashauri ziweze kukusanya fedha kwa ajili ya ukarabati huu? Je, kila halmashauri inahitaji fedha kiasi gani hasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Urambo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kama ambavyo nilishajibu kipindi cha nyuma, bado Serikali inafanya majadiliano na taasisi husika ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja kuhusu namna ambavyo tunaweza kufanya ukarabati na namna fedha ambazo tutazitumia zitaweza kurudishwa kwenye mfuko wa umma ambao tutazitoa. Hata hivyo, lengo hasa ni kwa Serikali kuutumia Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ambao kwa sasa unapata asilimia tano ya mapato kutoka kwenye sports betting. Lengo letu ni kuutunisha Mfuko ule kwa kuuongezea vyanzo vipya vya mapato ili kuhakikisha unakwenda kuleta athari chanya hasa kwenye maendeleo ya michezo nchini ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya michezo. Kwa hiyo, tutakapokuwa tayari, hata majadiliano na taasisi ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja tutawapa taarifa na namna ambavyo tunakwenda kulitekeleza jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa sasa kwa mpango huu tulionao ambapo mamlaka husika tulizozitaja, mikoa, halmashauri na manispaa zinajenga viwanja vyake vya michezo, wajibu wa kupata gharama halisi ya kukarabati miundombinu hii bado unabaki kwa mamlaka husika. Kwa ufahamu wangu, gharama zinatofautiana kutoka mamlaka moja mpaka nyingine, lakini tutakapokuwa tayari na hasa tutakapotaka kuzisaidia halmashauri ambazo hazina uwezo mkubwa wa kifedha kutengeneza viwanja hivi, tutaingia moja kwa moja pamoja na mambo mengine, kufanya tathmini ya kiasi gani kinahitajika kwa kila miundombinu ya michezo. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali.

Swali langu la kwanza, ni nini mpango wa Serikali kudhibiti matumizi holela ya dawa za binadamu ambayo imeonekana ni moja ya sababu inayochangia ugonjwa huu wa figo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ni nini mpango wa Serikali kuwezesha hospitali zake kutoa huduma ya kusafisha figo ili kuondoa adha wanayopata wagonjwa wa figo katika huduma na gharama za matibabu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge Kainja kwa namna ambavyo anafuatilia masuala ya afya, hasa kwenye Mkoa wa Tabora ambao wakati wote amekuwa akifuatilia hata masuala ya watu binafsi kuhakikisha mambo yanakaa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, ni nini Serikali inafanya kuondoa matumizi holela ya dawa? Moja ni kuendelea kuelimishana na kutumia fursa hii kwamba matumizi ya dawa yazingatie maelezo ya daktari na unapokwenda kwenye duka la dawa, basi uwe umepata prescription ya daktari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Waheshimiwa Wabunge mliona kampeni yetu na tumeleta katuni hapa inayozungumzia holela holela itakuletea matatizo. Maana yake tunaendelea na hilo suala la kuelimisha kuhusu alichosema dada yangu Mheshimiwa Kainja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, tunafanyaje kuhusu kuhakikisha tunawapunguzia wananchi mzigo wa matibabu hasa wanapopata matatizo wanapokwenda hospitali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, suala la Bima ya Afya kwa Wote na mmeona wiki hii Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa Arusha akiwa kwenye tamasha kubwa sana la kujipanga kuhakikisha tunafikia suala la Bima ya Afya kwa Watu Wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunapambana kuhakikisha sasa vifaatiba, dawa na kila kitu tunakwenda kununua kiwandani moja kwa moja, badala ya kununua kwa wauzaji wa kawaida ili kushusha gharama ya matibabu kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali ina utaratibu na ndiyo maana kila hospitali ina Maafisa Ustawi wa Jamii ambapo wale watu wanaoshindwa kulipa, basi kuna utaratibu wa kufuata ili waweze kutibiwa bila malipo, ahsante. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kutokana na majibu mazuri ya Serikali, kwa kuwa Shule ya Sekondari ya Igunga, ipo mjini na bajeti ya uzio huo ni shilingi milioni 276. Halmashauri imetenga shilingi milioni 55.

Je, Serikali sasa haioni kuna haja kutoa fedha Serikali Kuu na ku-support uzio huu ili uweze kukamilika kwa ajili ya usalama wa watoto hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, ni lini Serikali sasa itaweza kutenga fedha kwa pamoja za majengo ya madarasa pamoja na uzio ili viende sambamba? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kweli amekuwa akifuatilia kwa ukaribu sana masuala ya elimu na hasa kwa watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza, sisi sote ni mashahidi kwamba kutokana na utekelezaji wa Sera ya Elimu Bila malipo kumekuwa na ongezeko kubwa la udahili wa wanafunzi wa shule za msingi, lakini sekondari. Kwa hiyo, kwa kipindi hiki katika kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanapata udahili kuingia katika shule za msingi na sekondari, Serikali imeweka kipaumbele cha kuhakikisha inajenga miundombinu ya msingi kwa maana ya madarasa, lakini pia maabara za sayansi na mabweni. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa ujenzi wa uzio katika shule zetu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele kwa sasa ni kuhakikisha kuna kuwa na miundombinu ya kutosha ya madarasa ili wanafunzi wote waweze kupata udahili kuingia katika shule zetu hizi za msingi, lakini shule za sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, la Mheshimiwa Mbunge ambalo anataka Serikali Kuu iweze kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio, lakini kwa misingi ile ile ya ugatuzi wa madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mamlaka za Serikali za Mitaa zina jukumu la msingi la kutafuta bajeti, kupata mapato, lakini kuhakikisha inajenga miundombinu ya msingi ikiwepo miundombinu katika sekta ya elimu kwa maana ya madarasa mabweni na uzio.

Kwa hiyo, nichukue nafasi hii, kwanza kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga kwa kutenga fedha hii shilingi milioni 55 kwa ajili ya kuanza kujenga uzio huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kutoa wito kwa Mamlaka zote za Serikali za Mitaa, kuendelea kutenga fedha katika mipango na bajeti zao kwa ajili ya kujenga miundombinu muhimu kama hii ya uzio kutegemeana na hali ya eneo husika.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, Serikali tayari imeanza kujenga uzio kupitia fedha zilizotengwa katika mapato ya ndani na Mkurugenzi huyu na Serikali itahakikisha inaendelea kutenga fedha kwa utaratibu huo ili uzio uweze kujengwa kwa maslahi mapana ya wanafunzi wetu. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nami kupata nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ukubwa wa Wilaya ya Sikonge na Tarafa ya Kiwele kutoka Kata ya Kitunda kwenda Kipili ni umbali wa kilometa za hewani 140. Je, Serikali kutokana na Mpango wa 2025 imepanga kuweka minara mingapi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante! Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Jacqueline kwa ufuatiliaji wa mawasiliano ya uhakika kwa wananchi wa eneo hili lakini pili kama mwenyewe ulivyokiri ni umbali wa kilometa 140 wataalamu wetu wataendelea kufanya study ya kuona ni kiasi gani tuweze kuweka minara lengo ni kuhakikisha taarifa, mawasiliano, redio ziweze kusikika katika maeneo haya ambayo umeuliza.