Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jafari Chege Wambura (20 total)

MHE. JAFARI W. CHEGE Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Daraja la Mto Mori kwani mto huo umekuwa ukisomba watu na kusababisha vifo kwa wananchi wanaofuata huduma upande wa pili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Mori unakatisha katika barabara ya Kirogo-Nyamaguku yenye urefu wa kilomita 15, ikiunganisha Tarafa za Luo-imbo, Suba na Nyancha katika Wilaya ya Rorya. Barabara hii ilifunguliwa mwaka 2008 kwa nguvu za wananchi kupitia Mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto huu umegawanyika katika matawi mawili ambayo ni Mto Mori Mkuu wenye upana wa mita 43 na Wamala wenye upana wa mita 16 ambapo madaraja mawili (2) yanahitajika kujengwa. Hivyo, kwa sasa, barabara hii haipitiki kutokana na kutokuwepo kwa madaraja hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa barabara hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya imewasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI, maombi maalum ya Shilingi bilioni 1.54 ambayo ni makisio kwa ajili ya ujenzi wa daraja katika Mto Mori na matengenezo ya kawaida katika Barabara ya Nyamaguku- Kirogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali itatenga fedha kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ajili ya usanifu wa madaraja mawili ya Mto Mori ili kufahamu mahitaji na gharama halisi za ujenzi wa madaraja hayo na kisha kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi. Aidha, ujenzi wa madaraja na miundombinu ya barabara hizi utatekelezwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:-

Je, ni lini Kituo cha Afya Kinesi kitapandishwa hadhi na kuwa Hospitali kamili kutokana na kituo hicho kuhudumia wananchi zaidi ya vijiji 27 katika Jimbo la Rorya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, na kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya katika Wilaya ya Rorya katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilipatia Halmashauri ya Wilaya ya Rorya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ambapo tayari ujenzi wa majengo saba ya awali umekamilika na huduma za wagonjwa wa nje zinatolewa.

Mheshimiwa Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tatu ambapo tayari Halmashauri imeshazipokea fedha hizo na fedha shilingi milioni 500 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba. Vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya Rorya. Hivyo, Serikali haikusudii kupandisha hadhi Kituo cha Afya Kinesi kuwa Hospitali ya Halmashauri kwa kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Rorya shilingi milioni 900 kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Afya Utegi kilichopewa shilingi milioni 500 na Kituo cha Afya Kinesi kilichopewa shilingi milioni 400 ambapo ujenzi na ukarabati wa vituo hivyo umekamilika na huduma za upasuaji zimeanza kutolewa. Aidha, Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.

Mheshimiwa Spika, vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo kimoja cha afya wilayani Rorya na shilingi milioni 150 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma matatu ya zahanati.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, ni lini Hospitali ya Wilaya ya Rorya itaanza kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Jimbo la Rorya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ambapo kati ya mwaka wa fedha 2018/2019 hadi 2020/2021 Serikali imeipatia shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tisa na shughuli za ujenzi zinaendelea ambapo ujenzi wa majengo saba ya awali umekamilika na tangu Juni 2020 inatoa huduma ya wagonjwa wa nje (OPD). Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Rorya.

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya inatarajiwa kuanza kutoa huduma za upasuaji wa dharula na kulaza wagonjwa ifikapo Disemba, 2021.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:-

Je, ni lini Bandari ya Sota eneo la Shirati itaanza kurekebishwa ili kuinua uchumi, lakini pia kuboresha shughuli za kibiashara eneo la mpakani mwa Tanzania na Kenya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari ya Sota ni miongoni mwa Bandari za kati na ndogo 693 zilizoainishwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari (TPA) ili kutangazwa katika Gazeti la Serikali kwa lengo la kuzirasimisha. Aidha, mpango huo wa urasimishaji unakwenda sambamba na zoezi la kuhuisha Mpango Mkuu wa TPA wa kuendeleza Bandari zote nchini unaojumuisha Bandari ya Sota.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mpango huo unafanyiwa mapitio na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, mwaka huu 2021. Baada ya mpango huo kukamilika, orodha ya bandari kwa ajili ya uendelezaji ikiwemo Bandari ya Sota eneo la Shirati itatolewa kwenye tangazo la Serikali ili zihuishwe, ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaboresha mpaka wa Kirongwe kwa kujenga One Border Post ili kuimarisha na kuongeza mapato ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kuboresha mpaka wa Kirongwe kwa kuweka miundombinu wezeshi itakayotoa kutoa huduma kwa pamoja. Aidha, katika mwaka 2021/2022, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi million 407 kwa ajili ya usanifu na ujenzi wa nyumba za makazi za watumishi Kirongwe. Vilevile, katika mwaka 2022/2023 Serikali imepanga kuboresha mipaka mbalimbali nchini ikiwemo mpaka wa Kirongwe ili taasisi za Serikali ziweze kutoa huduma kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha mipaka yetu kwa kujenga nyumba za makazi kwa watumishi wa taasisi zinazofanya kazi mipakani na ofisi za kutolea huduma kwa pamoja mipakani ili kuboresha ulinzi na usalama wa nchi na pia kuongeza mapato ya Serikali.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani juu ya uchimbaji wa madini ya Helium katika Kijiji cha Nyamusi hasa ikizingatiwa kuwa Wananchi wamezuiwa kufanya shughuli yoyote katika eneo lenye Madini hayo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza tangu niteuliwa kuwa naibu Waziri wa Madini kuzimama katika Bunge lako tukufu, naomba nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama kibali cha kusimama mbele ya bunge lako alaasiri hii ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee kabisa nimshukuru Mheshimiwa Raisi wetu mpendwa mama Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kunipa dhamana hii kubwa ya kulitumikia Taifa letu kupitia sekta hii ya Madini na nimuahidi kwamba nitaifanya kazi hii kwa weledi mkubwa na uaminifu wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya salamu hizo naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Madini nipende kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege (Mbunge wa Jimbo la Rorya) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa taarifa kwa Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa kwa sasa hakuna maombi ya leseni za utafutaji au uchimbaji wa madini ya Helium yaliyopokelewa kutoka katika Kijiji cha Nyamusi. Hata hivyo, katika eneo hilo kuna chanzo cha maji moto ambacho kitalaam ni kiashiria cha uwepo wa madini ya Helium kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa awali na watafiti mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania Geological Survey of Tanzania au kwa kifupi (GST) inaendelea kuhakiki vyanzo vyote vyenye viashiria vya uwepo wa madini ya Helium katika maeneo mbalimbali nchini ambapo katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 GST kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilifanya uhakiki kwenye mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Dodoma na Shinyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nipende kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa katika mwaka wa 2022/2023 GST itafanya tena utafiti zaidi katika eneo hilo. Vilevile nipende kutoa taarifa kwamba Wizara yangu haijazuia wananchi kuendelea na shughuli katika eneo hilo. Hata hivyo, nitoe wito kwa wananchi kuendelea kuliacha wazi eneo hilo ili kuepusha migogoro na usumbufu iwapo madini hayo yatagundulika kuwa yapo ya kutosha kuchimbwa na wawekezaji kupatikana, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano katika Kata za Ikoma, Roche, Gobire na Bukura zilizopo mpakani mwa Tanzania na Kenya?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Bukura Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeingia makubaliano na Kampuni ya Simu ya Halotel tarehe 30 Agosti, 2022 kwa ajili ya ujenzi wa mnara katika Kijiji cha Kirongwe kilichopo katika Kata ya Bukura. Mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2023.

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa Kata za Ikoma na Roche zilizopo katika Jimbo la Rorya zimejumlishwa katika kata 763 ambazo zabuni ya kata hizo kwa ajili ya kupeleka huduma za mawasiliano inatarajiwa kutangazwa mapema mwezi Oktoba, 2022.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kata ya Gobiro, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umepokea changamoto hiyo na kwamba eneo husika litafanyiwa tathimini na litaingizwa kwenye zabuni za miradi ya mawasiliano itakayotangazwa kwa mwaka wa fedha 2023/ 2024.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, ni lini Mamlaka ya Mji Mdogo Shirati katika Wilaya ya Rorya itaanza kufanya kazi kama Mamlaka kamili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mji Mdogo wa Shirati itaanza mara baada ya Halmashauri mama ya Rorya kukamilisha mchakato wake wa kukusanya na kuimarisha mapato ya ndani ili iweze kuzihudumia Halmashauri mama na Mamlaka ya Mji mdogo wa Shirati.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, ni lini uchimbaji wa madini ya dhahabu utaanza katika eneo la Utegi, Tarafa ya Girango?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini imeendelea kutoa leseni za utafutaji wa Madini nchini. Katika Eneo la Utegi kuna leseni za utafutaji wa madini za Kampuni ya North Mara Gold Mine Limited na ABG Exploration Limited. Kwa sasa kampuni hizi zinaendelea na utafutaji wa madini katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, uchimbaji wa madini hutegemea kukamilika kwa mafanikio kwa zoezi la utafutaji wa madini ambalo huhusisha shughuli za kijiolojia. Aidha, shughuli hizi huchukua gharama kubwa na muda mrefu. Kwa msingi huo, eneo la Utegi linatarajiwa kuanza uchimbaji baada ya utafiti kukamilika na kuonekana kwa mashapo yenye kutosheleza kuanzisha uchimbaji kwa faida. Aidha, Serikali kupitia Tume ya Madini inafuatilia kwa karibu shughuli za utafutaji wa madini zinazofanyika nchi nzima.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mradi wa maji safi na salama katika Kata ya Rabour?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimwa Spika, Kata ya Rabour ina jumla ya Vijiji vitatu vya Oliyo, Rabour na Makongoro. Vijiji vya Oliyo na Rabour vinapata huduma ya maji kupitia visima virefu. Katika kuboresha huduma ya maji katika Kata ya Rabour (Kijiji cha Rabour), Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 inatekeleza mradi wa maji katika kijiji hicho. Kazi zilizopangwa kutekelezwa ni ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 225,000 na ujenzi wa mtandao wa usambazaji maji wenye urefu wa kilometa 12.8. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2022 na utanufaisha wananchi wapatao 4,792.

Mheshimwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali itaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika Vijiji viwili vya Oliyo na Makongoro. Kukamilika kwa miradi hiyo kutaboresha huduma ya maji safi na salama katika Kata yote ya Rabour.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, nini mpango wa Serikali kumaliza ujenzi wa zahanati kwa vijiji vilivyokamilisha ujenzi wa maboma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018 hadi 2021/2022 kiasi cha shilingi bilioni 71.95 zimetolewa kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 1,214 ya zahanati nchini kote. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 15 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati 300, hadi kufikia Februari, 2023 kiasi cha shilingi bilioni 14.6 zimekwishatolewa.

Mheshimiwa Spika, Jumla ya zahanati 762 kati ya 1,514 ujenzi umekamilika na zimeanza kutoa huduma. Aidha, Ujenzi wa maboma 752 ya zahanati upo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaimarisha ulinzi na usalama wa maeneo ya maziwa na bahari ili kulinda rasilimali pamoja na wavuvi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi ina wajibu wa kulinda maisha na mali za wananchi wake. Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/2024, tumepanga kutenga shilingi billioni 4.5 kwa ajili ya kununulia Boti 10 za doria zitakazotumika kwenye maeneo ya bahari na maziwa. Pindi boti hizo zitakapofika zitagawiwa maeneo yenye changamoto kubwa za uhalifu wa majini likiwemo eneo ya Rorya.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:-

Je, lini TANESCO watalipa fidia kwa wananchi wa Rorya waliopisha eneo la kupitisha umeme mkubwa toka mwaka 2011?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge ahsanteni sana na kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa mbele, naomba nitumie dakika moja kwa ajili ya shukrani. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya rehema na baraka. Kipekee na kwa unyenyekevu mkubwa naomba kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa aliyoiweka juu yangu na kuniteua niweze kumsaidia kama Naibu Waziri wa Nishati nikimsaidia Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Dotto Mashaka Biteko ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu. Napenda nimwahidi Mheshimiwa Rais imani hiyo aliyonijalia nitaitumikia kwa weledi na ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, TANESCO tayari imekamilisha uthamini na uhakiki wa marudio ya mali zilizoathiriwa na mradi na kwa sasa ipo katika hatua za maandalizi ya malipo. Malipo hayo yanatarajiwa kuanza mwezi Novemba, 2023 na kukamilika mwezi Desemba, 2023.

Mheshimiwa Spika, tunawaomba wananchi wanaosubiri kulipwa fidia wawe na subira wakati maandalizi ya malipo yakiwa yanaendelea kufanyika.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha umeme unafika kwenye vitongoji vyote nchini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imekamilisha uhakiki wa vitongoji 36,101 visivyokuwa na huduma ya umeme na kuandaa mradi kabambe wa kusambaza umeme katika vitongoji vyote uliopewa jina Hamlet Electrification Project (HEP) vikiwemo vijiji 262 vya Wilaya ya Rorya. Mradi huu utagharimu takribani shilingi 6,700,000,000,000.

Mheshimiwa Spika, Serikali inakamilisha mipango ya upatikanaji wa fedha hiyo na mradi huu unatarajiwa kutekelezwa ndani ya miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2024. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Jimbo la Rorya litapatiwa fedha kutoka REA ya kufikisha umeme katika vitongoji 15 vya kuanzia, nashukuru.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Mradi wa Maji wa Tarafa ya Suba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Jimbo la Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Tarafa ya Suba ina vijiji 17 ambapo kati yake vijiji 16 vinapata huduma ya maji kupitia Vyanzo vya Ziwa Victoria, visima virefu na visima vifupi. Hata hivyo, kulingana na jiografia sio vitongoji vyote kwenye vijiji hivyo vinafikiwa na huduma ya maji.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wananchi wa vijiji hivyo 16 wanapata huduma ya maji salama na ya kutosheleza ikiwemo Wananchi wa Kijiji cha Kibui ambacho wananchi wake hawana maji, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 itafanya usanifu wa mradi wa kutoa maji kwenye bomba kuu litakalopeleka maji Miji ya Tarime na Rorya ili kupeleka maji Vijiji vya Tarafa ya Suba. Baada ya kujengwa kwa mradi huo wananchi wote katika Tarafa ya Suba watapata huduma ya majisafi, salama na ya kutosheleza.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itafanya maboresho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, rasimu ya Sera ya Taifa ya mwaka 1995, Toleo la 2023 liliwasilishwa na kujadiliwa katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri, tarehe 18 Agosti, 2023. Aidha, Wizara imekamirisha maboresho ya rasimu ya sera kwa kuzingatia maoni ya Baraza la Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, hatua inayofuata ni rasimu hiyo ya sera kujadiliwa katika Mkutano wa Kazi wa Baraza la Mawaziri kwa tarehe itakayopangwa, ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa Mradi wa Maji wa Miji 28 utaanza kutekelezwa katika Wilaya ya Rorya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Rorya - Tarime kwa kutumia chanzo cha maji ya Ziwa Victoria. Kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa dakio (intake) yenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 29 kwa siku, ujenzi wa miundombinu ya kutibu maji (water treatment plant) yenye uwezo wa kutibu maji lita milioni 28 kwa siku, ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 110, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji (booster station) pamoja na ujenzi wa matanki matatu yenye jumla ya ujazo wa lita milioni 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa 12.5% na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2025 na utanufaisha wakazi wapatao 460,885 waishio kwenye Wilaya za Rorya, Tarime pamoja na Mji wa Sirari.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, lini Serikali itahamisha Mabaraza ya Ardhi kwenda kwenye Mfumo wa Mahakama?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kuboresha mfumo uliopo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini, Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeandaa mapendekezo ya kuhamisha shughuli zinazofanywa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenda katika mhimili wa Mahakama. Pindi taratibu zitakapokamilika, Serikali italifahamisha Bunge lako Tukufu, nakushukuru. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa soko la bidhaa za samaki na dagaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya inahitaji Soko la Kisasa la Samaki na Dagaa kutokana na shughuli za uvuvi kuwa miongoni mwa shughuli Kuu za kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutekeleza mpango huu, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Serikali kupitia Halmashauri imetenga shilingi milioni 76, mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Soko la Dagaa, Mkengwa ambalo ujenzi wake hadi kukamilika utagharimu shilingi milioni 300.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha bidhaa zitokanazo na samaki na dagaa zinapata soko la uhakika, Serikali kupitia Halmashauri inatarajia kujenga soko kubwa na la kisasa eneo la Mpakani Kirongwe, ambapo hadi sasa tayari mkopo wa shilingi bilioni nne umeombwa kutoka Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo muhimu kwa Halmashari ya Wilaya ya Rorya na maeneo ya jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Halmashauri ya Rorya itaendelea kutenga fedha za Mapato ya ndani kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Soko la Kisasa la Samaki na Dagaa kwa maendeleo ya wananchi wa Rorya. Ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti wahalifu wanaovamia wavuvi wakiwa ziwani na kuwanyang’anya mali zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa spika, wajibu wa Serikali ni kulinda maisha ya watu na mali zao. Katika kudhibiti uhalifu wanaofanyiwa wavuvi wakiwa ziwani, Serikali kupitia Jeshi la Polisi kikosi cha wanamaji hufanya doria kwa kutumia boti na kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limewashirikisha wavuvi na vikundi vya Ulinzi na utunzaji wa mazingira ya fukwe kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi ili kudhibiti na kupata…

SPIKA: Mheshimiwa sogea huku ili mnapozungumza mtumie sauti kidogo. Simama, sogea pale alipo ama Mheshimiwa Waziri aje aketi nawe hapo, itarahisisha kidogo.

Mheshimiwa Naibu Waziri.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba nianze upya.

Mheshimiwa spika, wajibu wa Serikali ni kulinda maisha ya watu na mali zao. Katika kudhibiti uhalifu wanaofanyiwa wavuvi wakiwa ziwani, Serikali kupitia Jeshi la Polisi kikosi cha wanamaji hufanya doria kwa kutumia boti na kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limewashirikisha wavuvi na vikundi vya Ulinzi na utunzaji wa mazingira ya fukwe kuanzisha vikundi vya Ulinzi shirikishi ili kudhibiti na kupata taarifa za wahalifu wa ziwani. Serikali katika kuhakikisha matukio ya uhalifu unaovuka mipaka ziwani haufanyiki, imeweka utaratibu wa kufanya mikutano ya ujirani mwema kwa mikoa jirani ya nchi zinazotumia ziwa ili kudhibiti uhalifu huo na kupambana na vikundi vya uhalifu, ahsante.