Contributions by Hon. Francis Kumba Ndulane (35 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuzungumza ndani ya Bunge lako Tukufu. Kwanza, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa mmoja wa wajumbe wa Bunge hili tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, napenda niwashukuru wapiga kura wa Jimbo langu la Kilwa Kaskazini kwa kuniwezesha kuwepo ndani ya Bunge hili kwa kunipa kura nyingi wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujikita kwenye maeneo matatu katika Hotuba ya Mheshimiwa Rais iliyosomwa wakati wa ufunguzi wa Bunge letu hili la Kumi na Mbili. Maeneo hayo ni sekta ya utalii, sekta ya afya na michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili la michezo, kwa kuwa halijazungumzwa na Mbunge yeyote ndani ya Bunge lako hili, napenda unipe upendeleo angalau wa dakika mbili za nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 23 - 25 sekta ya utalii imefanunuliwa vizuri na kwa hakika kuna malengo mengi mazuri yametolewa.
Napenda niseme tu kwamba katika Wilaya yangu ya Kilwa kuna vivutio vingi vya utalii kama magofu Kilwa Kisiwani; kumbukumbu nyingi za kale kule Songo Mnara; mapango makubwa na madogo katika Wilaya yetu ya Kilwa; mabwawa yenye viboko wengi wenye tabia tofauti na maeneo mengine katika Bwawa la Maliwe katika Kijiji cha Ngeya kule Mitole na pia Mto Nyange kule Makangaga; Kumbukumbu za Vita vya Majimaji katika Kata ya Kipatimu, Tarafa ya Kipatimu, Kijiji cha Nandete; na pango kubwa ambalo linasadikiwa kuwa ni la pili kwa ukubwa Barani Afrika linalojulikana kwa jina la Nang’oma lililopo katika Kijiji cha Nandembo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naiomba Wizara yetu tushirikiane kuhakikisha kwamba tunavitangaza vizuri vile vivutio ili kuongeza vivutio vya utalii katika nchi yetu ambavyo vitatuhakikishia mapato mengi kwa ajili ya Serikali yetu. Yale mapango ya Nang’oma ni mapango yana historia kubwa na watafiti wengi kutoka nchi mbalimbali kama Italia, Ujerumani na Uingereza wamekuwa wakija mara kwa mara, lakini kuna changamoto kubwa katika hivyo vivutio nilivyovitaja kwenye suala la miundombinu ya usafiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara haziko katika hali nzuri, kwa mfano ukitaka kufika kule ambako vita vya majimaji vilianzia Nandete au kule kwenye pango la Nang’oma ambako inasadikiwa kwamba wakati wa vita vya majimaji akinamama na watoto walikwenda kujificha kule wakati akinababa walipokuwa wanaendelea na vita vya majimaji. Ningeomba miundombinu iboreshwe kwa barabara ya kutoka Tingi pale Kijiji cha Njia Nne kwenda Kipatimu lakini vile vile barabara ya Nangurukuru – Liwale ambayo ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM basi ifanyiwe taratibu za haraka ili kuweza kuhakikisha kwamba inaboreshwa na vile vile barabara inayokwenda Makangaga – Nanjilinji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyotolewa siku ya Ijumaa tarehe 2 Juni, 2023 kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuitangaza nchi yetu ya Tanzania kupitia filamu ya Royal Tour hali iliyopelekea watalii wengi kuja Tanzania kutembelea vivutio via utalii.
Pia napenda kumpongeza Mheshimiwa Mohamed Omari Mchengerwa, Waziri wa Wizara hii ya Maliasili na Utalii pamoja na timu nzima ya Wizara yake kwa usimamizi wa Wizara hii. Pamoja na mambo mengi mazuri yanayotekelezwa na Wizara hii naomba kuishauri Serikali katika maeneo yafuatayo; kwanza malikale na maadhimisho; napenda kuishauri Serikali iweze kuyapa GN Maadhimisho ya Majimaji ya Nandete Kilwa mkoani Lindi ili yaweze kuingia katika urithi wa Taifa. Pia itenge bajeti kila mwaka kuanzia mwaka 2023/2024 na kupangiwa taasisi simamizi smbamba na kujenga miundombinu muhimu ya kutunzia kumbukizi muhimu zilizotumika wakati wa vita hivi vilivyopiganwa chini ya wakoloni wa Kijerumani kuanzia mwaka 1905 hadi 1907.
Mheshimiwa Spika, maboresho katika kumbukizi hii yataboresha na kuongeza mapato ya Serikali na kuinua uchumi hapa nchini kwa kuwa kumbukizi hizi zipo karibu na vivutio vingi vya utalii kama vile pango kubwa kuliko yote Afrika Mashariki la Nang’oma lililopo Kijiji cha Nandembo. Boma la wakoloni wa Kijerumani la Kibata, ziwa lenye viboko wengi la Maliwe lililopo katika Kijiji cha Ngea, magofu ya kale ya Kilwa Kisiwani, Songomnara na Kivinje, viboko albino waliopo katika Mto Nyange, Jiwe la Jahazi Kilwa Kisiwani na Pori la Akiba la Selous.
Mheshimiwa Spika, pili ni kuhusu urejeshaji wa malikale zilizochukuliwa na wakoloni, naishauri Serikali ifanye jitihada za dhati ili kuhakikisha malikale mbalimbali zilizochukuliwa na wakoloni ziweze kurejeshwa kama vile kurejeshwa kwa mjusi mkubwa (dinosaur) ambaye alichukuliwa katika Kijiji cha Tendeguru Wilayani Lindi mkoani Lindi na urejeshaji wa mafuvu ya machifu na kadhalika.
Kuhusu malipo ya fidia zinazotokana na athari za vita vya Majimaji, naishauri Serikali isimamie na kuweka mkakati wa kulipwa fidia za vita ya Majimaji kwa kuwashirikisha wananchi wa jamii zilizohusika na vita hivyo. Naishauri Serikali ianzishe mchakato wa kudai fedha hizo ili zikipatikana ziweze kutumika kwa kujenga miundombinu ya kijamii kama hospitali, shule na barabara.
Mheshimiwa Spika, uwepo mpango (succession plan) kwa watumishi wa Idara ya Makumbusho kwa kuanzia na makumbusho mbili za Dkt. Livingstone za Tabora Kwihala, Tabora na Kigoma Ujiji; Tabora Kwihala kuna Mzee wa miaka 73 anaendelea kuhudumu na Kigoma Ujiji kuna Mzee wa miaka 69 anahudumu pale.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE.FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika taarifa ambazo zimetolewa leo katika Kamati zetu tatu za PAC, LAAC na PIC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu, tangu nimeingia hapa Bungeni nimeweza kutumika katika kamati hizi zote tatu. Kwa hiyo, ninao uelewa wa kutosha na nimezielewa vizuri taarifa ambazo zimetolewa leo, lakini kwenye taarifa zao zilizotolewa, nitachangia kidogo kwenye Kamati ya LAAC na nitachangia kwa upana zaidi kwenye Kamati ya PIC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kujikita kwenye eneo lile la matumizi yasiyo sahihi ya Force Account. Ni ukweli kwamba taratibu, kanuni na sheria zimekuwa hazizingatiwi katika matumizi ya Force Account.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna zile kamati ambazo huwa zinahusika na fedha, manunuzi na mapokezi ya vifaa. Zile Kamati zimekuwa dormant, hazifanyi kazi yake sawa sawa kama ambavyo Mheshimiwa Mpakate amezungumza muda mfupi uliopita. Kwa hiyo, zinatumika tu kuhalalisha mambo, lakini kazi yenyewe inafanywa kule Makao Makuu ya Halmashauri zetu. Kwa hiyo, kuna jambo hapa ambalo tunatakiwa tulifanye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ushauri uliotolewa na Kamati ya LAAC, nilikuwa nashauri kuwa Serikali yetu iangalie uwezekano wa kupanga viwango vya fedha zinazowekezwa kwenye mradi ambazo zitatumia aidha Force Account au wazabuni. Leo tumeona hata majengo ya Ofisi za Halmashauri zetu zenye thamani ya shilingi bilioni mbili, shilingi bilioni tatu na miradi mingine inaongezewa fedha, inakwenda mpaka shilingi bilioni nne hadi tano bado zinatumia Force Account. Hii ni hatari kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa napendekeza, mradi ambao unazidi shilingi milioni 200, usitumie utaratibu wa Force Account, kwa sababu zile fedha ni nyingi. Hizi fedha zikifika kule, fuatilieni tu, nakuomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Fedha mweke utaratibu mzuri wa kuwa na zile technical audit kutoka Wizarani, mtashuhudia haya mambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zile shilingi milioni 470 ambazo tuliletewa kwenye miradi hii ya SEQUIP hazikumaliza ile miradi, na hata hizi zilizoletwa juzi za miradi ya BOOST shilingi milioni 331 kila jimbo hazijamaliza ile miradi. Unakuta mradi unatekelezwa asilimia 80 au 85 na ukizidi sana 95. Mwisho hii imekuwa ikitusumbua. Kipindi unapoenda kupanga matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo, unakuta Mkurugenzi naye anakusogelea, analeta request ili akamalizie vyoo na huduma nyingine katika ile miradi. Kwa hiyo, imekuwa shida kweli kweli. Kwa hiyo, hapa tunapaswa kupaangalia vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika yale marekebisho au maboresho ya utekelezaji wa miradi kupitia Force Account, nashauri kwamba tuzingatie viwango vya pesa vinavyowekezwa kwenye mradi, ikizidi shilingi milioni 200 tupeleke kwenye zabuni, na ikiwa chini ya hapo, kama ni kujenga madarasa, sijui kujenga ofisi za shule na vitu kama hivyo, hizo tunaweza kupeleka. Kujenga zahanati, tunaweza kutumia Force Account, lakini siyo miradi ambayo inagharimu fedha nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nije kwenye taarifa iliyotolewa na Kamati ya PAC. Nakwenda moja kwa moja kwenye ukurasa wa 31 na 46 kwenye kipengele Na. 2.4.7 na 3.2.10. Pale Kamati yetu ilizungumzia kutokamilika kwa miradi katika taasisi ambazo zinatumia mtaji wa umma kwa wakati. Jambo hili limejitokeza katika maeneo mengi na pale wame-cite mifano ya NSSF, katika ule mradi wa pale Mkulazi wamelazimika kuongeza fedha kiasi cha dola milioni 32, lakini kuna miradi ya RUWASA hasa ile inayotumia fedha za National Water Fund, imekuwa ni shida kweli kweli kumaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na shida kubwa na wakati mwingine fedha zinachelewa kuja na wakati mwingine mlolongo wa malipo unakuwa ni mrefu sana, hasa hizi fedha za wafadhili wa nje. Matokeo yake sasa mradi ukichelewa, unakuta bei ya vifaa inaongezeka, inflation inatokea, na riba inazaliwa kutoka kwa wakandarasi hasa wanapokuwa ni wa kutoka nje. Kwa hiyo, imekuwa ikileta shida kweli kweli na kufanya lile kusudio la Serikali la kuwekeza mitaji katika hizo taasisi kuwa halitekelezwi na mwisho wa siku ziada haizalishwi mapema kama ilivyokusudiwa, na mwisho wa siku kunakuwa na ufanisi mdogo katika utekelezaji wa ile miradi na vile vile tija inakuwa haipatikani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali iliangalie hili eneo ili tuweze kunasuka na hii hali ambayo imejitokeza. Pia naomba Serikali iongeze usimamizi wa hiyo miradi, lakini pale inapohitajika kupeleka fedha, basi zifike kwa wakati kwenye zile taasisi ili waweze kutekeleza hiyo miradi iliyokusudiwa ili ufanisi na tija viweze kupatikana katika uwekezaji wa hayo maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo napenda kulizungumza ni suala la ongezeko la riba itokanayo na ucheleweshaji wa kulipa wakandarasi au wazabuni. Hili limekuwa jambo ambalo kama limezoeleka. Nataka nikwambie, jumla ya shilingi bilioni 63.77 ambazo zimeainishwa kwenye ukurasa wa 28 na 29 kwenye taarifa ya Kamati ya PIC, kama tungezinusuru kulipwa riba au tusingezigharamia kulipia riba, tungeweza kujenga vituo vya afya visivyopungua 127 kwa fedha zile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tungeweza kujenga zahanati zisizopungua 318 kwa thamani ya ile pesa ambayo inakwenda kutumika kwa ajili ya kulipa riba; tungeweza kujenga madarasa ya kisasa yenye thamani ya shilingi milioni 24 kila moja yasiyopungua 2,600; na pia tungeweza kujenga mabweni au maabara katika shule zetu za sekondari zisizopungua 1,822.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni fedha nyingi, lakini mwisho wa siku tumejikuta tunarudi nyuma kwa sababu tunatumia fedha nyingi kuwekeza katika maeneo ambayo tayari uwekezaji ulishafanyika kwa kuokoa hizo riba zinazotakiwa zilipwe na hazilipwi sasa. Kama tulikopa, unakuta hazilipwi na donors, inabidi tutafute chanzo kingine cha pesa kwa ajili ya kugharamia hayo malipo ya hao wakandarasi kutokana na kuchelewesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na sababu nyingi za ucheleweshaji, lakini leo hapa napenda nitanabahishe, niliwahi kufuatilia baada ya kuona ile hoja ya CAG na nikakuta kuna utaratibu ambao huwa unatumika katika malipo hasa kule kwenye upande wa barabara. TANROADS, wanatumia mfumo unaoitwa FIDIC, ule mfumo unataka malipo yakamilike ndani ya siku 56. Consultant na Mkandarasi wanatakiwa wafanye mambo yao ndani ya siku 28 na siku 28 inatakiwa taasisi zetu za Serikali kuanzia TANROADS pamoja na Wizara ya Kisekta, Wizara ya Ujenzi pamoja na Wizara ya Fedha waweze kufanya kazi zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANROADS ina mfumo wake mzuri wa malipo na udhibiti wa fedha na umekamilika kabisa, lakini utakuta TANROADS wanafanya procedure zao, lakini lazima iende Wizara ya Kisekta, Wizara ya Ujenzi. Pale kuna maafisa wasiopungua wawili, lazima wacheze na ule mfumo wa malipo. Ukienda Wizara ya Fedha utakuta zile transactions zinatakiwa zipite kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani, naye ana wasaidizi wasiopungua wawili; pia inatakiwa ipite kwa Kamishna wa Fedha za nje, naye ana wasaidizi wasiopungua watatu lazima wapitie hiyo transaction ya fedha; vile vile Kamishna wa bajeti naye lazima apitie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nasema hii milolongo imekuwa mirefu, naishauri Serikali ipunguze milolongo ya malipo ili tulipe kwa wakati, tupunguze hizi riba. Kama haitoshi, pia tuwe na mfumo wa kufuatilia kuona ni wapi kuna laxity katika kulipa haya malipo ambayo yanazalisha riba ili hizo fedha tuweze kuzi-save ziende zikafanye kazi nyingine kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na ni fedha ambazo zinatokana na jasho la walipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja zote na taarifa zote zilizotolewa na Kamati zetu zote tatu za PIC, PAC pamoja na LAAC, ahsante sana.
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, kwanza, napenda kumpongeza Rais wetu, mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amejikita katika kusimamia vizuri Serikali tangu alipoapishwa kuwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuweza kutuletea hapa Mpango wetu uliowalishwa tarehe 8 na Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha.
Mheshimiwa Spika, mimi napenda kujikita kwenye eneo la kilimo hasa kilimo cha ufuta. Kilimo cha ufuta kimekuwa kikifanyika kwa wingi sana maeneo mengi ya nchi yetu kadri siku zilivyokuwa zinakwenda hadi kufikia sasa. Ukiangalia kwa mfano katika Mkoa wa Lindi peke yake, katika mwaka 2020 zao la ufuta liliweza kuchangia au kuuzwa kwa thamani ya shilingi bilioni 110.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kumekuwa na changamoto nyingi kwa wakulima wetu kuhusiana na hili zao ambazo napenda sasa Wizara ya Kilimo inayohusika na zao hili basi iweze kushughulikia hizo changamoto ili hatimaye tupunguze umaskini kwa wakulima wetu wa ufuta lakini tuongeze tija katika uzalishaji na pia tuweze kukuza uchumi wa Taifa letu kutoka wa kiwango cha kati chini kuwa cha kati juu.
Mheshimiwa Spika, kuna tatizo la upungufu wa watumishi katika sekta hii ya kilimo. Naomba hilo lizingatiwe na Wizara husika ili tuweze kuona namna ambavyo tunaweza tukakuza zao hili.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna suala la mbegu bora, Serikali imeahidi kwamba itaendelea kuongeza uzalishaji wa mbegu bora. Naomba suala hili lizingatiwe kwa sababu imeonekana kwamba katika zao la ufuta kumekuwa na ongezeko pale mbegu bora zinapokuwa zinatumika. Mbegu bora ukilinganisha na zile za asili zimekuwa zikiongeza tija kwenye uzalishaji karibu mara mbili ya zile mbegu za asili. Kwa hiyo, naomba hilo eneo hili lizingatiwe.
Mheshimiwa Spika, vilevile kwenye eneo la vyama vyetu vya ushirika, kumekuwa na baadhi ya makarani ambao si waaminifu. Kwa mfano, katika Wilaya yangu ya Kilwa katika Kata ya Miguruwe, wakulima 110 hadi hivi sasa tunapozungumza waliuza mazao yao mwaka 2019/2020 lakini mpaka leo hawajalipwa fedha zao. Fedha hizo zilipotelea kwa hawa makarani wa AMCOS na TAKUKURU waliingilia kati suala hilo lakini mwisho wa siku mpaka leo matunda hayajaonekana. Kwa hiyo, naomba Wizara husika ilisimamie.
Mheshimiwa Spika, lakini kuna changamoto ya wanyamapori …
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, leo Mheshimiwa Francis anasoma kabisa yaani hana wasiwasi, hongera sana Mheshimiwa Francis. (Makofi/Kicheko)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kumekuwa na changamoto ya wanyamapori. Kuna Kijiji kule katika Kata ya Kandawale kinaitwa Ngarambeliyenga, kwa wale wasiofahamu ndiyo kule ambako yule shujaa wa Vita vya Majimaji Kinjekitile Ngwale alikuwa anaishi. Kwa hiyo, katika hiki kijiji kumekuwa na uvamizi mkubwa wa wanyama aina ya pofu na ndovu pamoja na Kata ya jirani ya Miguruwe. Kwa hiyo, naomba sana wenzetu wa Idara ya Maliasili watusaidie katika kudhibiti changamoto hizi sababu mpaka leo napozungumza wananchi wengi wamekimbia makazi yao lakini mazao yao yamekuwa yakiliwa na wanyama aina ya ndovu na pofu. Kwa hiyo, naomba sana Wizara inayohusika itusaidie.
Mheshimiwa Spika, katika upande wa mifugo Wilaya ya Kilwa pamoja na Mkoa wa Lindi kwa ujumla kumekuwa na shida kubwa ya wafugaji wahamiaji, kwa sababu kwa asili Wilaya za Mkoa wa Lindi ni Wilaya za Wakulima. Kwa hivi karibuni tumewakaribisha wenzetu wafugaji katika Wilaya ya Kilwa peke yake. Katika siku za hivi karibuni imeingia mifugo zaidi ya 350,000, lakini huduma za ile mifugo zimekuwa zikikosekana. Kwa mfano kumekua na huhaba wa ujenzi wa malambo, majosho na hata watumishi wamekuwa wachache sana katika kushughulikia hii Sekta. Naomba hilo jambo lishughulikiwe.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kwa sababu ya muda. Nakushukuru sana Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye bajeti ya Wizara ya Utumishi na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningependa kujikita kwa kuanzia kwenye maeneo mawili; eneo la upungufu wa watumishi pamoja na eneo la madeni, lakini kama muda utaniruhusu nitaongeza mambo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya upungufu wa watumishi imekuwa ni changamoto kubwa na ambayo imekuwepo Serikalini kwa muda mrefu sana. Mimi nimefanya kazi kama mtumishi wa umma kwa zaidi ya miaka 20 kabla sijawa Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini. Miaka yote ambayo nimehudumu kama Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri, kama Mhasibu TANROADS, kama Mkurugenzi katika Halmashauri, changamoto ya upungufu wa watumishi na madeni kwa watumishi imekuwa ni changamoto kubwa ambayo imesababisha kuwepo kwa hoja za CAG ambazo zimeshindikana kufungwa kwa sababu changamoto zimekuwa zikiendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya Halmashauri katika nchi yetu na idara mbalimbali za Serikali zimekuwa na upungufu mkubwa wa watumishi kiasi kwamba baadhi ya majukumu yamekuwa yakishindwa kufanyika. Na niseme tu kwamba unapokuwa na upungufu mkubwa wa watumishi ni sawasawa na timu ya mpira ambayo inatakiwa kucheza wachezaji kumi na moja halafu unakuwa na wachezaji pungufu, hatutarajii timu ya namna hiyo iweze kushinda, ili timu iweze kushinda inatakiwa iwe na wachezaji kumi na moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba kumekuwa na hii changamoto hata katika Wilaya yangu ya Kilwa kumekuwa na changamoto hii kubwa, kuna baadhi ya zahanati zina watumishi mmoja-mmoja. Unaweza ukaona wale watumishi mmoja-mmoja wanaofanya kazi katika zahanati wanawezaje kufanya kazi wakati wanahitaji kuwa likizo, wakati fulani wanaumwa na kadhalika, lakini kuna zahanati moja kule katika Kata ya Kinjumbi, Kijiji cha Miyumbu ilikaa miaka tisa ikiwa inasubiri watumishi kwa sababu watumishi wachache. Mwaka jana ndio angalau tulipata mtumishi mmoja, lakini kuna zahanati katika Kijiji cha Bugo, Kata ya Chumo ina miaka zaidi ya mitano sasa hivi haijafunguliwa kwa sababu watumishi ni wachache, lakini leo tunacho Kituo cha Afya tunatarajia kukifungua hivi karibuni pale Somanga, tunafikiria, tunaumiza vichwa kwamba hali itakuwaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeomba Serikali katika hili jambo, Wizara yetu ya Utumishi ilitilie maanani sambamba na suala la madeni ambalo nalo limekuwa ni shida. Madeni yamekuwa yakihakikiwa; katika utumishi wangu wa umma wa zaidi ya miaka 20 kila mwaka tumekuwa tukihakiki madeni; tunahakiki, tunahakiki, taarifa zinakuja watumishi kutoka Wizarani, Wizara za Kisekta zimekuwa zikija kuhakiki madeni, lakini mwisho wa siku madeni yanakuwa hayalipwi inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika,kwa hiyo, kuna utitiri mkubwa, kuna kiasi kikubwa cha madeni kwa watumishi wetu kiasi kwamba inapunguza morali ya kufanya kazi kwa watumishi wetu, kwa hiyo, ningeomba hilo nalo lishughulikiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile nikirudi kwenye suala la watumishi katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini kuna shule shikizi saba. Katika zile shule shikizi zote zinahudumiwa na walimu wa kujitolea ambao wanalipwa viposho vidogo sana na wananchi baada ya kuwa wanachangia. Kwa hiyo, niseme kwamba, kwa kweli haya matatizo mawili ni matatizo makubwa hili la upungufu wa watumishi na madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali kupitia Wizara ya Utumishi na Utawala Bora, niiombe iandae mpango kazi maalum ili ndani ya miaka minne ijayo wakati tunakwenda kwenye uchaguzi wa mwaka 2025 basi tuhakikishe hii changamoto imekwisha ili tuzipunguzie Halmashauri zetu na idara zetu hii hoja ambayo inaweza ikafungwa, lakini vilevile tuweze kuwasaidia wananchi wetu wapate huduma inayotakiwa katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa kulichangia ni suala la michezo ya watumishi. Miaka mitano iliyopita kulikuwa na Sera ya Michezo, kulikuwa na Mashindano ya SHIMIWI kwa watumishi wa sekta ya umma, lakini kule kwenye Serikali za Mitaa pia kulikuwa na michezo inafanyika kwa watumishi ili kujenga afya bora, lakini vilevile kupambana na maradhi kama ya UKIMWI na changamoto nyingine za kiafya, lakini hata kwenye mashirika ya umma pia walikuwa na michezo yao wanafanya, lakini ndani ya miaka mitano iliyopita michezo hiyo tumekuwa hatuioni na niseme tu kwamba, nafahamu Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa, ni mwanamichezo nimuombe kwa interest aliyonayo kwenye michezo, lakini vilevile katika kuboresha afya za watumishi wetu basi tuweze kurejesha ile michezo katika taasisi za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kuna Mbunge mwenzangu amezungumza muda mfupi uliopita, kulikuwa na Wakurugenzi saba, RAS mmoja, pamoja na ma-DAS watatu walishiriki kwenye uchaguzi wa kura ya maoni mwaka 2010, lakini kwa masikitiko makubwa wale Wakurugenzi waliondolewa kwenye payroll ya Serikali na hatimaye mpaka leo hii hawajarudishwa, lakini nafahamu kwamba, wapo watumishi wengine wengi maelfu kwa maelfu walishiriki kwenye ule uchaguzi wa kura za maoni, walipotoka kwenye ule uchaguzi baada ya kuwa hawakupata nafasi ya kuendelea na uchaguzi uliofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020 walirudishwa kazini baada ya kutoa taarifa kwamba, wametoka na hawakuvuka kwenye kura za maoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara iwasaidie wale watumishi kumi na moja, RAS mmoja, ma-DED saba, pamoja na ma-DAS watatu ili waweze kuridishwa kazini na wapate haki zao za msingi. Ahsante. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kwa mara ya pili leo kuinuka kwenye kiti changu na kuweza kuzungumza na kuweza kuchangia bajeti ya Wizara ya Michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwanza ninapenda kujikita kwenye michezo na baadaye kama nafasi itaruhusu basi nitaongelea pia upande wa habari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwanza nashukuru na kuwapongeza uongozi mzima wa Wizara ya Michezo kwa namna ambavyo imekuwa ikishirikiana vizuri na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na ningependa nijitambulishe uhusika wangu kwenye michezo, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho wa Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), lakini pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania. Na nimekuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa miaka 14 hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo napenda kwanza kupongeza ushirikiano uliopo kati ya Serikali na TFF, Serikali imetusaidia mambo mengi katika kuboresha mpira wetu wa nchi hii ya Tanzania. Tumeshuhudia mwaka juzi wakati tunajiandaa na mashindano ya Under Seventeen Barani Afrika iliweza kujitolea jumla ya shilingi bilioni moja, kwa kweli zilitusaidia sana na zimeboresha mambo mengi katika yale mashindano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kutokana na ushirikiano uliopo ndani ya miaka minne iliyopita tumeweza kushiriki mashindano ya CHAN pamoja na mashindano ya AFCON kwenye senior teams. Lakini vilevile tumetoa mataji tisa kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo mataji kwa timu za wanawake na vijnaa, lakini vilevile tumekuwa na mafanikio makubwa kwenye ligi yetu ya Tanzania Bara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ligi yetu miaka minne iliyopita ilikuwa kwenye nafasi za ishirini huko, lakini kutokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali, wawekezaji kwenye football, lakini na TFF basi sasa ligi yetu inashika nafasi ya nane kwa ubora Barani Afrika. Tunazizidi nchi za Nigeria na Algeria ambazo kwa miaka mingi zilikuwa kwenye nafasi tano za juu, sasa zinashika nafasi ya tisa; ya kumi na kuendelea, sisi nafasi ya nane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na kutokana na maboresho ya ligi ambayo tunayo ndiyo maana vilabu vyetu ambavyo vinatuwakilisha katika mashindano ya kimataifa vya Simba na Namungo vimetuwezesha kufika katika hatua nzuri ya mafanikio kuliko kipindi chochote tangu Uhuru wa nchi hii. Hii inatokana na ubora wa ligi ambayo inaendeshwa katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo napenda kuwapongeza Klabu ya Simba ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Mbunge wa Jimbo langu mstaafu, Ally Murtaza Mangungu pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, pamoja na Mtendaji Mkuu wa Club ya Simba, Dada yangu Barbara Gonzalez. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nitakuwa mchache wa fadhila kama nisipoipongeza timu ya Namungo kwa kazi nzuri ambayo wamefanya hasa msimu huu uliopita, katika msimu wake wa kwanza klabu ya Namungo imeweza kufanya vizuri katika ligi kuu pamoja na mashindano ya FA na hatimaye ikaweza kutuwakilisha katika mashindano ya kimataifa kwenye kombe la shirikisho kwa mafanikio makubwa na mafanikio haya yaliongozwa na kaka yangu, rafiki yangu Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, Mheshimiwa Hassan Zidadu, hongera sana Mheshimiwa Hassan Zidadu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile ningependa sasa kushukuru kwa namna ambavyo hotuba ya Wizara, lakini pia hotuba ya Mheshimiwa Rais wetu alipofika hapa Bungeni kwa kuonesha nia ya dhati ya ku-support timu zetu za Taifa. Katika nchi za jirani ambazo zimepiga hatua kuliko sisi kwenye rank za sifa na mambo mengine tumeshuhudia zikiwa zina- support timu zao kwenye mambo mengi kwenye training session zao, lakini vilevile zinapokwenda kushiriki mashindano mbalimbali katika maeneo ya kuwapa usafiri wa kwenda kwenye mashindano hapo Kenya tu na Uganda wamekuwa wakifanya hivyo kwa miaka mingi hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye masuala ya accommodation wanapokwenda kucheza mashindano nje ya nchi, lakini pia kwenye posho za kujikimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ningeomba tu kwa kuanzia Serikali yetu niishauri iwekeze kwenye hayo maeneo katika kuzi-support timu zetu za Taifa. Lakini vilevile pamoja na mafanikio ya timu ya Simba kulikuwa na wimbi la watu wengi kujaribu kuipiga vita timu ile, wamekuwa wakipokea wageni jambo ambalo mimi sijawahi kuliona katika nchi yoyote wakati nilipokuwa naongozana na timu ya Simba kwenda katika mashindano mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka juzi nilipata nafasi ya kuwa head of delegation wakati timu ya Simba ilipokwenda kucheza na timu ya Nkana FC, lakini pia ilipokwenda kucheza na timu ya Saura kule Algeria, tulipofika Algeria tulioneshwa vidole saba, kwa sababu mwaka uliotangulia timu yetu ya Taifa ilifungwa goli saba kule Algeria, Algiers. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tulipofika Zambia kule Kitwe tulivyotua na ndege tu pale Ndola tulikuwa tunaonyeshwa vidole vinne kwa sababu kwa mara ya mwisho Simba ilipokwenda Zambia ikacheza katika uwanja wa Ndola ilifungwa goli nne, lakini cha ajabu na cha kusikitisha katika nchi hii wametokea watu hivi sasa timu ngeni zikija zinapata kupokelewa na ukiangalia yale mapokezi huwa yanaratibiwa na watu ambao wana akili zao, siyo wale washabiki wa kule Uzuri kwa Mfugambwa au kule Somanga, Kilwa. (Makofi)
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe Taarifa.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi ningeomba Serikali ijikite katika kuwafundisha uzalendo wananchi wetu ili mwakani tunapokwenda kucheza timu nne basi hizi vurugu vurugu zisiwepo timu zetu ziweze kufanikiwa vizuri.
T A A R I F A
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ndulane kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Gulamali.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa Taarifa mzungumzaji anayezungumza sasa hivi kwanza moja atumie lugha ya Kibunge anapochangia na kuzungumzia juu ya kutoa lugha ambazo zinaonesha kama vile hao wanaounga timu zingine, lugha hizo ambazo anatumia si nzuri. Lakini kingine…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali ngoja lugha gani iliyotumiwa, kwa sababu mimi hapa nasikiliza Wabunge wote wanaochangia, lugha gani ya Kibunge aliyoisema?
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, lugha ambayo imetumika ni kuonesha kama vile timu ambayo wanayoizungumzia kwa mapenzi yake yeye ni kama timu ya Taifa ya Tanzania. Kwa hiyo, timu ni moja tu ya Tanzania ambayo ni uzalendo kwa watu wote …
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali nisikilize kwanza, nisikilize kwanza, ulipewa nafasi ya kuchangia wewe kuhusu timu yako na yeye anachangia kuhusu timu yake kwa hiyo wewe ulisema unataka kumpa taarifa sasa sioni kama unataka kutoa taarifa naona unataka kukosoa uchangiaji wake. (Makofi)
Alikuwa amekaa hapa Mheshimiwa Spika wewe ulipata fursa ya kuchangia ukamaliza mchango wako, kuhusu timu yako kwa hiyo muache na yeye amalizie kuhusu timu yake hakuna lugha ambayo si ya kibunge aliyoizungumza.
Mheshimiwa Ndulane malizia mchango wako. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, mimi siipokei taarifa yake kwanza, nazungumza kama Mbunge, lakini pili nazungumza kama mmoja kati ya wanafamilia ya mpira katika nchi hii, kwa hiyo na-balance story yangu, nai-balance. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ningependa…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ndulane kuna taarifa nyingine simuoni Mbunge akisimama, ni wapi.
T A A R I F A
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu spika, nipo hapa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Massare.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumza kwamba siku zote unaposema ukweli unauma sana hasa kwa mtu ambaye anaguswa na jambo lake. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ndulane unapokea taarifa hiyo?
MHE. FRANCIS N. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeipokea kwa mikono miwili. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio yote ambayo tumeyapata vilevile kunachangamoto kwenye utambuzi wa mchezo wa mpira wa miguu kama profession na nina fikiri hapa ndipo tunapokwama. Mpira ni profession kama zilivyo profession nyingine kwa hiyo zinatakiwa zitengenezewe msingi imara wa kufundishwa, lakini vifaa vya ufundishaji vipatikane na vilevile mafunzo yawezwe kuendeshwa kama mafunzo ya profession zingine, hapa ndipo tunapo-fail. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ningeiomba Serikali yangu pamoja na kuwekeza kwenye national team pia iweze kuwekeza kwenye mafunzo kuanzia watoto wadogo kule wanakosoma kwenye shule za msingi na shule za sekondari, twende tukafundishe walimu wengi wa mpira na michezo mingine, lakini vilevile twende tukahakikishe kwamba watoto wanafundishwa angalau kila Halmashauri kuwe na kituo kimoja cha uendelezaji wa soka la vijana ili vipaji vyote viweze kukusanywa na viweze kuendelezwa na hatimaye tuweze kupata wachezaji ambao wanafaa kutusaidia kutuvusha katika mashindano mbalimbali. (Makafi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wachezaji ambao tunao hivi sasa wanatokea from nowhere, wanaokotwa okotwa tu halafu mwisho wa siku unasikia tayari wanacheza national timu kwa hiyo hawana zile ethics za uchezaji mpira. Kwa hiyo, naomba Serikali iwekeze kupeleka fedha kwenye halmashauri kwa kusudio maalum kama tulivyofanya kwenye miradi mingine na kwenye mradi huu maalum uwepo wa kuendeleza vipaji vya watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ningependa vilevile kuchangia kwenye changamoto. Shirikisho letu la mpira Tanzania limekuwa likiendeshwa kwa shida sana, wakati fulani Shirikisho letu lilikuwa na deni la jumla ya shilingi milioni 10.18 wakati wa utawala wa Tenga, Malinzi na hata sasa wakati wa utawala wa Wallace Karia. Deni limelipwa kwa kiasi cha kutosha kama nusu ya deni sasa hivi TFF inadaiwa kodi jumla ya shilingi bilioni 5.009, ndani ya deni hilo lipo deni la shilingi bilioni 4.55 linalotokana na kodi zilizotokana na michezo mbalimbali ambayo ilifanyika hapa Tanzania ya kimataifa na kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mwaka 2010 timu yetu ya Taifa ya Tanzania ilipocheza na timu ya Taifa ya Brazil ile mechi aliyeialika timu ya Taifa ya Brazil haikuwa TFF na hata mapato yaliyopatikana pale uwanjani ambayo yalivunja rekodi ya mapato hayakwenda TFF, lakini mwisho wa siku lile deni la VAT lilipelekwa TFF.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna fedha za kuwalipwa makocha zimekuwa zikilipwa na Hazina tangu enzi za akina Marcio Maximo, kuna mkusanyiko wa pay as you earn kulikuwa na jumla ya shilingi bilioni 1.3, lakini TFF imehangaika kulilipa limebaki jumla ya shilingi bilioni 1.049.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kawaida ya malipo ya mishahara kwa watumishi wa Serikali ambao vilevile wale makocha walikuwa wanapitia kama Marcio Maximo alikuwa analipwa na Hazina, lakini wakawa wanalipa ile net figure halafu deni bado linabaki la kodi na yale makato mengine ya kisheria yalikuwa yanabaki kwa TFF, kwa hiyo total sasa hivi ya deni lililobaki ni jumla ya shilingi bilioni 5.809. Kwa hiyo, ningeiomba Serikali ijitahidi kuifutia TFF deni hili ili waweze kuongeza ubora wa kusimamia mpira wa nchi hii, ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa habari ningeomba kwanza niishukuru Wizara yetu kwa kufanya kazi nzuri, nikianza na Mkurugenzi wetu wa Habari, kwanza Waziri, Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, Mheshimiwa Bashungwa pamoja na Mheshimiwa Gekul. Lakini vilevile kuna Mkurugenzi Mkuu wa Habari Ndugu Gerson Msigwa kwa kweli amekuwa akifanya kazi kubwa ya kutujuza taarifa mbalimbali zinazohusu Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile nivipongeze vyombo vya habari vya TBC, ITV, Azam Tv, Redio Abood, Redio Mashujaa kule Lindi na Mtwara, Millard Ayo, pamoja na Clouds FM. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami leo niweze kuchangia bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kuipongeza Serikali chini ya uongozi wake Mheshimiwa Rais wetu, Mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuisimamia vizuri Serikali yetu kiasi kwamba imekuwa ikiendelea kutekeleza miradi ya kimkakati na miradi mikubwa kwa ufanisi mkubwa pia napenda kuwapongeza wasaidizi wake Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Baraza zima la Mawaziri, kwa namna ambavyo wanachapa kazi usiku na mchana kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wananachi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu imeonesha ukomavu, usikivu, unyenyekevu na hekima kubwa na busara kubwa kwa wananchi wake katika kuiendesha nchi yetu, naipongeza sana Serikali yetu. Suala la kutengwa kwa Milioni 500 kila Jimbo suala la kuwekwa tozo ya shilingi 100 kwenye mafuta ni mambo ambayo wananchi wengi yamewafariji sana na ni imani yangu kwamba sasa barabara nyingi zitaweza kupitika muda wote wa mwaka bila kuwa na kikwazo chochote, lakini vilevile kutenga Milioni 600 kwa ajili ya shule za Sekondari ni imani yangu kwamba sasa tunakwenda kutatua changamoto kubwa iliyokuwa inalikabili Taifa letu, changamoto ya mimba za utotoni, pamoja na utoro kwenye shule zetu kwa sababu hapo kabla watoto walikuwa wanasoma shule za mbali sana kwa sababu kwenye Kata zao kulikuwa hakuna shule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale kwangu Somanga kulikuwa hakuna shule kwa hiyo nina imani kwa kupitia hizi Milioni 600 basi tutapata suluhisho la matatizo na changamoto ambazo zilikuwepo, walikuwa wanasoma umbali wa Kilometa 15 kwenda kwenye Kata za Jirani. Nieleze tu taarifa ya masikitiko kwenye Jimbo langu la Kilwa Kaskazini siku ya tarehe moja ya mwezi huu wa Juni, kulitokea msiba wa mwananchi wangu anaitwa Walivyo Uwiro, katika Kijiji cha Kipindimbi, mkazi wa Kijiji ya Kipindimbi kata ya Njinjo, alifariki dunia kutokana na migogoro ya wakulima na wafugaji, ninamuombea kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na tukio hilo na matukio yanayoendelea ambayo kwa kweli hali ya usalama sio nzuri sana kule, kule katika kata za Miguruwe, za Kandawale, pamoja na kata hiyo ya Njinjo niliyoisema na Mitowe ningeomba tu Serikali sasa wakati tunaelekea kutekeleza bajeti ya mwaka 2021/2022 iweze kurekebisha mambo fulani na kutuboreshea mambo fulani ili kuhakikisha kwamba matukio ya namna hii hayajitokezi tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivi kwa sababu tumekuwa na tunu zetu za Taifa ambazo ni amani, utulivu, na mshikamano katika Taifa letu ambazo ni msingi imara kwa maendeleo ya Taifa letu ambazo kwa sasa zinaonekana kule Jimboni kwangu katika baadhi ya kata zimeanza kupungua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali kwa kushirikisha zile sekta ambazo zinahusika kwenye kilimo, ufugaji, pamoja na ardhi watusaidie kuharakisha kuwepo kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi, ili kuhakikisha kwamba hii migogoro haiendelei tena. Lakini vile vile ningeomba Wizara ya Mifugo ijikite kwenye kuboresha mazingira bora ikiwemo ujenzi wa malambo, ili kuwafanya wale wafugaji ambao wamehamia katika maeneo yetu wasiwe wanahangaika hangaika sana na kuingia kwenye mashamba ya wananchi na hatimaye kuzua migogoro ya namna hii. Lakini vile vile Serikali kwa kushirikiana na vyombo vyake vya dola basi ijitahidi kufanya operations za mara kwa mara ili kuzuia wahamiaji ambao siyo rasmi ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo wanaosumbua na kuleta hii migogoro ambayo ipo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ninaomba nijikite kwenye sekta ya uvuvi kuna mambo matatu hapa nitayazungumza, kwanza ninaomba Serikali kupitia Wizara ya uvuvi itusaidie kujenga masoko ya kisasa katika maeneo yetu, Pwani yetu ya Bahari ya Hindi ikiwemo Jimboni kwangu Kilwa Kaskazini ni maarufu sana kwenye uvuvi ukifika pale Somanga Samaki wanavuliwa sana, wengine wanasafirishwa hadi nje ya nchi wanapelekwa hadi Spain, Portugal pamoja na Italy na China Samaki aina ya robusta pamoja na prawns pweza wamekuwa maarufu sana kule Kilwa hasa pale Somanga na Kivinje, lakini hali ya masoko kwa kweli ni mbaya lakini wataalam pia wamekuwa wachache kwenye sekta hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mtaalam ambaye anatoa leseni ambaye yupo chini ya Wizara ya Uvuvi ni mmoja tu kwa Pwani yote ya Mkoa wa Lindi na Mtwara, kwa hiyo mtu akitaka kusafirisha bidhaa zake kama hao Samaki ambao wanauzwa hadi nje nchi wanahangaika sana wale wafanyabiashara. Vilevile ningeomba wavuvi waboreshewe miundombinu ya kuvulia Samaki, vifaa vya kisasa vipatikane lakini vilevile maelekezo kutoka kwa wataalam, wataalam wetu wawe karibu na wavuvi wetu ili kuboresha kipato chao na kipato cha Taifa kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la utalii wa uvuvi pia kama alivyotangulia kuzungumza Mbunge mwenzangu aliyetangulia bahari ya Hindi ina visiwa vingi, Kilwa peke yake kuna Songosongo, kuna Simaya kuna Ukuza lakini vile vile kuna kisiwa cha Simaya, kwa hiyo niombe iweke mkazo Wizara yetu ya Utalii ikishirikiana na Wizara ya Uvuvi kwenye eneo hilo, hii tunaiita sports fishing iweze kufanyika nchi kama Seychelles , Maldives na Mauritius na nchi ya Mexico na Latin America zimekuwa zimepiga hatua kubwa sana zimekuwa zikiingiza fedha nyingi kila mwaka kupitia hii sport fishing au uvuvi wa utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niombe kuzungumzia mchezo wa mpira wa miguu, nimefarijika sana kusikia kwenye bajeti yetu kwamba kutakuwa na msamaha wa kodi ya VAT kwenye kuingiza nyasi za bandia ambazo zitatumika kwenye viwanja vyetu, nimefarijika sana kusikia kwamba TFF itapewa jukumu la kusimamia, kwa sababu TFF ndiyo yenye jukumu la kusimamia mchezo wa mpira wa miguu katika nchi yetu na wanajua standards za vile viwanja zinavyotakiwa kuwa, aina ya nyasi bandia zinazotakiwa wanazijua kwa hiyo nafikiri ni jambo ambalo limekaa vizuri, isipokuwa ningeomba kushauri katika eneo moja kwa Serikali yetu niiombe isitoe ile privilege au ile exemption kwa Majiji peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu dhamira ni njema ya kukuza vipaji na kuendeleza vipaji vya vijana wetu, vipaji vimetapakaa nchi nzima kwa hiyo niombe kwenye Majiji, kwenye Manispaa kwenye Halmashauri za Wilaya kote misamaha itolewe ili wenye uwezo wa kununua hizo nyasi waweze kupata huo msamaha wa kodi ya VAT.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ningependa kuizungumzia TFF, TFF ni taasisi ambayo siyo ya kibiashara lakini katika manunuzi yake yote hata mapato ya mlangoni yalikuwa yakitozwa VAT asilimia 18, lakini kwenye mapato ya mlangoni unakuta wanakata kwenye ile gross figure, gross revenue yale mapato ghafi kabla ule mgao wa vilabu na maeneo mengine haujatolewa unakuta wanakata ile asilimia 18, hii imeleta uchungu na inasumbua sana kwa vilabu vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilabu vyetu vingi ni vichanga vinacheza mpira wa ridhaa sio profession football kwa hiyo mwisho wa siku ukikata asilimia 18 ya VAT maana yake unakuwa unavididimiza na kuvifanya vilabu visiwe na mapato ya kutosha, kwa hiyo ningeomba hii ikiwezekana ifutwe na kwa kuzingatia kwamba kama nilivyosema mpira wetu hauendeshwi kibiashara, TFF siyo taasisi ya kibiashara ningeomba ifutiwe hii kodi ya VAT. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile sasa hivi kuna mradi unaogharimu kama Bilioni 10 wa uendelezaji wa vituo vya michezo kule Kigamboni - Dar es Salaam na Tanga tayari pale inaonekana 1.8 Bilioni ambazo zile fedha zimeletwa na FIFA tayari 1.8 Bilioni zitakwenda kwenye VAT kwa hiyo zitapinguza ufanisi kwenye ile miradi ambayo inakwenda kujenga vipaji na kukuza mpira wa nchi hii, ndiyo maana ninasisitiza Mheshimiwa Waziri wa Fedha tusaidie kwanza kuiondoa kwenye legislation ya VAT TFF ili hatimaye iweze kufanya mambo yenye tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuzungumza jioni hii ya leo kuchangia taarifa za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG. Nitachangia kwenye Kamati mbili, Kamati ya LAAC pamoja na Kamati ya PAC. Kabla ya kuchangia ninaishukuru sana Serikali inayoongozwa na Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya maendeleo ambayo kupitia hiyo miradi ndiyo taarifa nyingi tumezipata hapa ambazo zinaonesha kwamba kuna hoja nyingi katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane kwanza na Mbunge wa Kasulu, Mheshimiwa Vuma, ambaye asubuhi aliongea kwa kirefu kuhusiana na mapengo katika Bodi za Wakurugenzi kwa Taasisi zetu nyingi za Umma. Kwa kweli kutokuwa na Bodi za Wakurugenzi au kuwa na Bodi za Wakurugenzi zenye mapungufu kumepelekea kuwa na mapungufu makubwa katika uendeshaji wa taasisi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachelea kusema kwamba ilitolewa taarifa hapa kutoka kwa Mheshimiwa Mtaturu, akitolea mfano wa Klabu ya Simba na ubora wa Bodi yake ya Wakurugenzi, akazungumzia namna ambavyo timu fulani maarufu ambayo jana ilicheza katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, namna ambavyo imeshindwa ku-cope na mazingira ya utawala bora ambayo yanafanikishwa katika Klabu ya Simba, ambayo tangu wameunda Bodi ya Wakurugenzi imara, miaka mitano iliyopita wamekuwa wakifanya vizuri kwa kucheza hatua za makundi katika mashindano ya vilabu Barani Afrika na kuweza kuiwakilisha nchi yetu katika hatua mbalimbali ikiwemo kufika hatua ya robo fainali. (Makofi)
T A A R I F A
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Ngoja kwanza kuna taarifa, nafikiri Mheshimiwa alikuwa anataka kuelezea pia kwamba Bodi hiyo inasaidiaje kwenye timu za ndani au ni nje tu. Karibu Mheshimiwa Getere. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji anayechangia, mchango huo haupo kwenye taarifa za Kamati. Mimi naomba aifute.(Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndulane unapokea taarifa?
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hii taarifa kwa sababu hii mifano tunayoitoa ni mifano muhimu. Wenyewe mmeona jana hali ilivyokuwa.
T A A R I F A
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma, taarifa.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji anachozungumza ni vitu ambavyo vinagusa watu rohoni na yaliyotokea jana ni mambo ya kawaida, sasa huwa yanatokea bahati mbaya hata yeye mwenyewe yalishamtokea, sasa ningeomba hiyo hoja aiache. (Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndulane zingatia yaliyokutokea huko nyuma, unapoke taarifa ya Mheshimiwa Musukuma?
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninaipokea kwa lengo la kuweka msisitizo kwenye jambo hili. Tunawaombea ndugu zetu katika mechi ya marudiano kwa sababu hakuna nafasi nyingine ya kuwasaidia ni kupitia mazungumzo kama haya ndiyo maana tumeamua kusema, kwa hiyo, wana nafasi ya kujirekebisha kwenye mechi ya marudiano. Tulisema tangu kwenye Kikao cha Bajeti wakati tunachangia Wizara ya Michezo kwamba jamani hakuna dhambi kwenda kusikiliza ushauri kutoka kwa watani! Hapa kwenye Bunge hili tunae mmoja wa wanabodi ya Wakurugenzi ya Simba.
T A A R I F A
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa kuna taarifa, Mheshimiwa Rama eeh!
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, tungemuomba mchangiaji ajielekeze kwenye hoja zilizoko mezani. Simba na Yanga hapa siyo hoja ya leo ya kujadili. Kwa hiyo, ajielekeze kwenye hoja za Kamati zilizosomwa za PAC LAAC na PIC. Tuendelee mbele nchi hii inataka kusikiliza mawazo yake siyo habari za Simba na Yanga.
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Ndulane unapokea taarifa?
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Siipokei taarifa lakini niishie hapo na ninawatakia kila la kheri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijikite kwenye taarifa rasmi za Kamati zetu tatu, especially zile mbili za LAAC na PAC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianzia na Kamati ya LAAC, taarifa ambayo waliitoa ilikuwa ni nzuri, imebainisha madhaifu mengi ambayo yalitokana na taarifa ya ukaguzi ya CAG. Nikienda moja kwa moja kwenye usimamizi wa miradi, dosari zilijitokeza nyingi lakini nijikite pale ambapo ilionekana kwamba kuna upotevu kwenye interest ambazo zilikatwa kutokana na malipo ya jumla ya Shilingi Bilioni 664,0 ambayo ilizalisha interest jumla Shilingi Bilioni 68.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukailaumu taasisi ya TANROADS wakati kumbe mfumo wetu wa malipo una changamoto nyingi. Huko tulikotoka tulikuwa tunatumia mfumo katika kulipa na kuandaa malipo ya Wakandarasi. Katika mfumo huu unatoa siku 56 ambapo inatakiwa Serikali imlipe Mkandarasi anapokuwa amefanya kazi, kinachoonekana kule nyuma tulikuwa tunakwenda vizuri kwa sababu hizi siku 56 zilikuwa zinagawanywa, siku 28 Consultant anatakiwa aandae certificate, iwe approved, ipitiwe lakini mwisho wa siku wanaisukuma TANROADS. Ikifika TANROADS kuna kitengo kinaitwa IDA kinasimamia malipo yote ya kazi za wale development partners, yale malipo ambayo yanafadhiliwa na wafadhili mbalimbali wa nje ya nchi. Tukifika pale nao wanapitia zile certificates, pamoja na wale Engineers wanapitia, wakishapitia inaenda kwa Desk Officer wa Wizara ya Fedha na Mipango ambapo kazi yake ni kuangalia usahihi wa yale malipo ambayo yameandaliwa au yale madai ambayo yameandaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatimaye akishapitisha, na ni kazi inachukua kama masaa mawili tu, baadae zile claims zinarudi TANROADS, baadae zinakwenda kwa development partner naye anajiridhisha, malipo yako sawa. Baadaye yanalipwa ndani ya siku 56 Mkandarasi anakuwa tayari ameshalipwa. Hii ilikuwa inazuia kupatikana kwa hizi interest ambazo tunaziona leo kwenye hoja za ukaguzi za CAG.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichopo sasa hivi certificate ikishaandaliwa ikitoka kwa Mkandarasi inakwenda kwa consultant, ikitoka kwa consultant inakwenda TANROADS wanaipeleka Wizara ya Ujenzi. Pale kuna maafisa wasiopungua wawili wanashughulikia lakini ikitoka hapo inakwenda kwa Permanent Secretary wa Wizara ya Fedha na Mipango. Ikitoka pale kuna Maafisa zaidi ya Kumi wanasimamia, unapita katika mlolongo wa Maafisa zaidi ya Kumi. Ikitoka hapo inarudi TANROADS. TANROADS baadae inarudi kwa development partner, nae anajiridhisha hatimaye ndiyo inalipwa. Kwa hiyo kuna maafisa zaidi ya 15 wanahusika na malipo na matokeo yake ndiyo haya sasa tunayoyaona leo kwamba kuna fedha nyingi Serikali inalazimika kuongeza kulipia ile miradi kwa sababu ya uwepo wa riba kutokana na ucheleweshaji wa malipo. Kwa maana zile siku 56 zinakuwa hazitoshi kulipa Mkandarasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwa upande wa Serikali zetu za Mitaa, nilikuwa naperuzi vizuri sana kuhusiana na wingi wa hoja za ukaguzi katika Halmashauri zetu. Katika Halmashauri zetu nilitazama Halmashauri ya Korogwe nilikuta ina hoja ambazo hazijafungwa 91. Halmashauri ya Bumbuli ilikuwa na hoja za ukaguzi 89 ambazo hazikufungwa mpaka wanakuja kwenye Kikao cha LAAC. Kuna Halmashauri ya Msalala ilikuwa na hoja 61. Halmashauri ya Bunda ilikuwa na hoja 56 ambazo hazijafungwa mpaka wanafika kwenye Kamati ya LAAC. Nini nataka kusema?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi kikubwa, Halmashauri hizi zimekuwa na hoja nyingi za ukaguzi ambazo wameshindwa kuzijibu kwa sababu wameshindwa kuvitumia vizuri vyomba vya ndani ya Halmashauri katika kukabiliana na hizi hoja. Kwa mfano, tunavyo vitengo vyetu vya ukaguzi wa ndani, vile vitengo vimekuwa havitumiki sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwanza, haviwezeshwi kufanya kazi zake sawasawa. Vifaa vya usafiri hawana, vifaa vya ofisi hawana lakini mwisho wa siku hata ile audit independence imekosekana kwa hiyo wanajikuta mwisho wa siku, wale Wakaguzi wa Ndani wamekuwa kama ni watoto yatima ndani ya Halmashauri wakati ilitakiwa wawe msaada mkubwa kwa Maafisa Masuuli katika kuisimamia halmashauri. Kwa hiyo, ombi langu katika jambo hili ni kwamba Halmashauri ziwatumie vizuri Wakaguzi wa Ndani katika kipindi hiki cha mpito, na kwakuwa Wizara ya Fedha iliahidi kwamba itarekebisha mfumo wa usimamizi wa hawa wakaguzi wa ndani. Ninawaomba waharakishe ule mchakato ili mwisho wa siku ikiwezekana hawa Wakaguzi wa Ndani wapelekwe katika Ofisi ya Chief Internal Auditor wa Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna hii inaitwa Audit Committee, hii ndiyo msaada kwa Maafisa Masuuli wa Halmashauri ambao ni Wakurugenzi. Kuwepo kwa Kamati hii inawezesha kwanza kufanya mapitio ya fedha zinazoidhinishwa za bajeti kabla hazijaenda kwenye Baraza la Madiwani na kabla hazijaja huku kwenye Bunge. Pia mwisho wa siku inawezesha kupitia hoja zote za ukaguzi wa ndani na nje ili kuwezesha kuboresha kile ambacho kinaonekana kina dosari. Kwa hiyo, ninaomba pia Maafisa Masuuli wazitumie vizuri hizi Kamati za Ukaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuzungumza. Kwanza, napenda kuishukuru na kuipongeza Wizara ya Kilimo kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kwa wakulima wetu na kuongeza kasi ya maendeleo katika sekta hii ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, mimi napenda kujikita katika zao la ufuta. Wilaya ya Kilwa ninayotoka ni wilaya ambayo inaongoza kwa kilimo cha zao la ufuta katika Mkoa wa Lindi. Katika zao hili kumekuwa na changamoto kubwa hasa wakati wa minada. Katika mwaka uliopita Wilaya nzima ya Kilwa yenye vijiji 90, kata 23, tulishuhudia tukiwa na kituo kimoja tu cha mnada wa zao hili la ufuta hali ambayo ilipelekea kuwepo kwa biashara ya holela ya zao hili la ufuta almaarufu kule tunaita chomachoma, wenzetu wale wa Kagera nilisikia pale asubuhi kuna kitu wanaita butura. Kule kwetu tunaita chomachoma yaani biashara ya magendo ambayo ina dhulumati nyingi kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Spika, vilevile wapo wakulima walikata tamaa kuuza zao hili wakabaki na ufuta wao mpaka mwaka huu. Hivi napozungumza sasa hivi hawajauza ufuta wa mwaka jana kutokana na hii hali ya kuwa mnada ni mmoja tu na uko eneo la mbali, ambalo ni zaidi ya kilometa 200 toka kule ambako mashamba yaliko. Pia mzunguko wa fedha ukawa umepungua lakini hata bei kwa wale ambao walimudu kupeleka sokoni au mnadani mazao yao walijikuta wanauza kwa bei ya chini sana. Hii ni kutokana na kwamba wale wanunuzi walikuwa wanafidia gharama zao za usafirishaji wa yale mazao toka kwenye vyama vya msingi. Kwa hiyo, kwa ujumla kumekuwa na shida katika huu mfumo wa minada.
Mheshimiwa Spika, jana kulikuwa na taharuki kubwa katika Wilaya ya Kilwa kwa sababu ratiba ambayo ilitumika mwaka jana ndio ambayo jana imetangazwa tena, tuna kituo kimoja tu cha mnada kupitia Chama cha Ushirika cha Msingi cha Muungano kule Kilanjelanje. Naomba Wizara itusaidie kuhakikisha kwamba inaongeza vituo vya minada ili wakulima wetu waweze kuuza mazao yao maeneo ya karibu.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuwa na vituo vingi itasaidia wakulima kushiriki kikamilifu na kuwa na ownership wakati mnada unafanyika tofauti na hali ilivyo sasa. Mnada ukiwa mbali wakulima wanashindwa kuhudhuria mnada badala yake wanakuwa na wawakilishi tu ambao pengine ni viongozi wa vyama vya msingi na hatimaye unakuta hata bei wanayoipata inakuwa ni shida. Kwa hiyo, naomba Wizara ilisimamie suala hili, ile ratiba iliyotolewa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Mwambao iweze kurekebishwa tupate hata maeneo matatu au manne katika Wilaya ya Kilwa ya kufanya minada na kuuza mazao yetu bila shida ili wakulima wetu waweze kunufaika na bei ambazo zinaridhisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo napenda kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Kilimo ni suala la Kampuni ya Mbolea Tanzania. Katika taarifa ya CAG kampuni hii imekuwa ni miongoni mwa taasisi za umma 11 ambazo zilishindwa kuwasilisha hesabu zake za mwaka kwa CAG katika mwaka wa fedha uliopita. Siyo mwaka huo tu, hata miaka mitano, sita iliyopita kulikuwa na hali kama hiyo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Ndulane Francis, dakika zako zimekwisha.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyeiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia bajeti ya Wizara ya Utalii. Kwa kuwa muda ni mfupi, nitaongelea jambo moja tu, suala la kumbukumbu za Vita vya Majimaji. Naona nilipoongea Vita vya Majimaji, au kule kwetu Kilwa Kaskazini wanavitambua kama Ngondo ya Machemache, naona Mheshimiwa Jenista Mhagama ameshituka kidogo pamoja na Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vita hivi vilianza tarehe 15 Julai, 1905 katika Kijiji cha Nandete Jimboni kwangu Kilwa Kaskazini, Tarafa ya Kipatimu. Ilihusisha; kama ilivyokuwa kule Songea, kulikuwa na Machifu 12, huku kwetu kulikuwa na viongozi wa koo tisa, ndio ambao waliongoza hivi vita. Naomba niwataje, alikuwepo kiongozi wa Kiroho aliyejulikana kwa jina la Kinjeketile Ngwale, alikuwepo ambaye alikuwa anaishi Kijiji kinaitwa Ngalambilienga, alikuwepo Jemadari wa vita hivyo, alikuwa anaitwa Sikwako Mbonde, alikuwa anaishi Kijiji cha Nandete.
Pia alikuwepo Ngulumbali wa Mandai, alikuwa anaishi Nandete; Lindimio Machela, Mabiga Nandete, Bibi Ntabilwa Naupunda ndiye ambaye alibeba ile dawa ya maji, Nandete na vile vile alikuwepo Mpeliadunduli Kipengele; alikuwepo Libobo Mpanyu Kipengele; alikuwepo Mataka Nkwela Mwiru; alikuwepo Kilambo Mpetamuba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwa miaka mingi wenzetu wa kule Songea Jimboni kwa Mheshimiwa Waziri, wamekuwa wakiadhimisha miaka karibu takriban 114 kuhusu Uwepo wa vita hivi au kumbukumbu za vita hivi, lakini kwa upande wa Kilwa Kasakazini hili jambo limekuwa halifanyiki. Hata miundombinu ya utalii imejengwa kule Songea. Kuna kumbukumbu; National Museum ipo, lakini kwa upande wa Kilwa Kaskazini haipo. Kwa hiyo, hata kumbukumbu za hawa wazee maarufu ambao walikuwa na uthubutu wa kupambana na Wakoloni wa Kijerumani mpaka sasa haipo. Kwa maana hiyo, hii historia imekuwa ikififia na hatimaye kutoleta tija katika sekta ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, siyo tu vita vya majimaji peke yake, bali kulikuwa na mazingira ambayo yaliambatana na hivyo vita. Kulikuwa na mapango; Pango kubwa la Nang’oma ambalo ni kubwa Kusini mwa Jangwa la Sahara, Barani Afrika, lipo pia lile la Namaengo; lipo kaburi la mzungu ambaye alizikwa kutokana na vile vita vya majimaji. Kule tunaita lisikolian nungu, lipo katika Kijiji cha Kinywanyu, Kitongoji cha Mbongwe, Kata ya Chumo. Pia lipo boma la Mjerumani mahali ambako Wajerumani waliweka makazi yao kwa ajili ya kudumisha utawala katika eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, hivi vivutio ni vivutio vizuri vya utalii, naomba tuvisimamie…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri, hivi vivutio vya utalii ni vizuri. Naomba tuvisimamie, tuvitangaze, lakini tuviwekee miundombinu bora na kuhakikisha kwamba kunakuwa na makumbusho kwa ajili ya kudumisha kumbukumbu za vita vya majimaji na kuvutia watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2022/2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia napenda tu kutoa taarifa kwamba, leo alfajiri nilipokea taarifa ya kusikitisha ya kuondokewa na mzee wetu, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM kati ya mwaka 2012 hadi 2017 katika Wilaya ya Kilwa. Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu Mwenyekiti wetu, Yusuf Bakari Kopakopa mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa taarifa hiyo, naomba niendelee kuchangia sasa. Kwanza naishukuru Serikali yetu ya Awamu ya Sita ikiongozwa na mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanya kwa Watanzania katika kuwaletea maendeleo na kuondoa kero mbalimbali ambazo zimekuwa zikitokea kupitia miradi ya maendeleo ambayo imekuwa ikifanikishwa na Serikali yetu.
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, siyo kwamba namkatiza Mheshimiwa Ndulane, lakini yuko vizuri kabisa, mnamuona yuko na karatasi zake vizuri kabisa bila wasiwasi wowote ule. (Kicheko)
Mheshimiwa Ndulane, endelea bwana na tunakupa pole kwa msiba wa Mheshimiwa Mwenyekiti wetu, poleni sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kwa kweli Serikali yetu imefanya kazi kwa ufanisi mkubwa ndani ya kipindi kifupi na kwa kweli mambo mengi yameonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu unafahamu vizuri sana ramani ya jimbo langu, kuna mambo yamefanyika, haya kwa mfano ya madarasa, kwenda shule za sekondari na shule shikizi mpaka katika maeneo ambayo yalikuwa hayatarajiwi. Hii imeleta hamasa kubwa kwa wananchi wangu kuweza kui-support Serikali yetu. Vilevile maji, madawati na huduma nyingine. Kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kutuongoza vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, isipokuwa nina angalizo tu; taratibu nyingi zimetolewa za ufuatiliaji na usimamizi wa miradi hii. Naomba katika kipindi hiki cha utekelezaji wa miradi sisi Wabunge wote tutakapotoka hapa Bungeni twende tukafuatilie na kuisimamia vizuri hiyo miradi ili tija iweze kupatikana. Vilevile kitengo cha ukaguzi wa ndani katika kila halmashauri kiweze kuimarishwa vizuri na kitumike kufuatilia vizuri miradi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nyongeza napenda katika Mpango sasa ambao tunauendea wa 2022/2023 tuweze kuona changamoto nyingine za miundombinu, hasa hii ya elimu na afya ziweze kutekelezwa vizuri. Kwa mfano, kuna eneo la mabweni; mpaka sasa hivi kuna baadhi ya shule zetu za kata ziko mbali sana na kule wanapotoka wanafunzi. Nafikiri kwamba kunahitajika ujenzi wa mabweni ya wavulana na wasichana katika kuboresha huduma ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo katika jimbo langu ninakotoka, shule za kata ziko umbali wa kilometa mpaka 43, kilometa15, sehemu nyingine 17 toka shule iliko. Kwa hiyo naiomba Serikali yetu katika Mpango wa 2022/2023, basi tuone namna ambavyo huduma ya mabweni, lakini pia huduma ya matundu ya vyoo, vifaa vya maabara na maabara zenyewe, iweze kuimarishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujikita katika eneo la kilimo. Tumekuwa na Benki hii ya Maendeleo ya Kilimo, kwa kweli imefanya kazi nzuri, lakini kuna changamoto katika utekelezaji wa majukumu yake. Benki hii imetoa pesa nyingi, zaidi ya bilioni 100, tangu ilipoanzishwa mwaka 2014, lakini kumekuwa na shida katika kuwafikia wakulima wadogo wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yangu ya Kilwa nina kaya zisizopungua 42,000 ambazo napenda kukuthibitishia mpaka kufikia wakati huu hakuna kaya hata moja ambayo imefikiwa na benki hii. Kwa hiyo naomba hii benki iongezewe mtaji ili iweze kuhudumia wananchi mpaka wale wa vijijini kabisa badala ya kuhudumia wananchi ambao wako katika zile skimu maalum za kilimo kama umwagiliaji na nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alternative ya pili kwenye hili inawezekana mtaji ukawa mdogo katika ku-support hii TADB, basi naomba vilevile ikiwezekana tuanzishe Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo ambao uta-operate kutokea kwenye halmashauri zetu na utashirikiana na AMCOS zetu, utashirikiana na SACCOS zetu zilizopo katika maeneo ambayo wakulima wanatoka hasa hawa wadogowadoo wa vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kwamba upatikanaji wa pesa za mikopo za TADB unahusisha kujaza fomu nyingi ambazo wanavijiji wetu hawawezi kupata huo mkopo kiharaka, hasa ukizingatia kwamba Ofisi za TADB ziko mbali sana na maeneo ya vijijini. Hapa karibuni nilikuwa nauliza kwa mfano watu wa Singida wanapata wapi huduma za TADB, nikaambiwa wanapata Dodoma. Sasa yule mwananchi wa kule ndanindani kabisa Singida atafikaje Dodoma kirahisi, inakuwa ni ngumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Kilwa tunapata huduma kutokea Mtwara. Kwa hiyo nafikiri wakiongozewa mtaji, basi wanaweza wakatusaidia, lakini vilevile tukiunda Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo ambapo mikopo itatolewa bila riba, hii itasaidia sana wakulima wetu wa vijijini kuweza kuinuka kiuchumi na kuweza kuendelea mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa ni suala la michezo. Msimu uliopita tulikuwa na performance nzuri sana hasa kwenye mashindano ya vilabu ya kimataifa, lakini mwaka huu mambo yamekwenda ndivyo sivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata michezo mingine pia, tuliona Simba na Namungo ambavyo zilifanya vizuri msimu uliopita na kutuweka katika ramani ya juu kabisa Barani Afrika na duniani kwa ujumla, lakini mwaka huu haikuwa hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia Timu yetu ya Biashara United ikishindwa kusafiri kwenda kucheza mechi ya marudiano Nchini Libya. Pia hata katika mchezo wa volleyball tumeshuhudia timu yetu ya Taifa ambayo ilitakiwa kwenda kushiriki mashindano kule Nchini Burundi ikishindwa kufika kwenye mashindano na hatimaye kufungiwa kama ambavyo Biashara United pia ilifungiwa.
Kwa hiyo niiombe Wizara ya Fedha ikishirikiana na Wizara ya Michezo kwa pamoja zishirikiane katika kuona namna ambavyo tutaweza kuzilea timu zetu za Taifa pamoja na timu hizi za vilabu ambazo zinapata nafasi ya kucheza katika mashindano haya ya kimataifa ili ziweze kutuwakilisha vizuri, zisipate huo upungufu ambao ulijitokeza, hasa wa kifedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, kwanza kama walivyotangulia kuongea wenzangu napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu, Bunge lako Tukufu pamoja na Wabunge wote kwa namna ambavyo kwa pamoja tunashirikiana katika kuhakikisha kwamba miradi ya maendeleo inatekelezwa vizuri inasimamiwa vizuri na tunaishauri vizuri Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru zaidi Mheshimiwa Rais kwa sababu ameweza kutenga fedha nyingi katika mwaka wa fedha huu tunaoumaliza ili kuhakikisha kwamba miradi mingi inakwenda na kwa kweli inakwenda, kwa kweli nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ningependa kujikita katika maeneo machache sana leo katika kuchangia kwenye bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza ningependa kuzungumzia miundombinu ya barabara pamoja na madaraja, ninaanza kwanza na barabara kuu.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na barabara nyingi ambazo zimefanikishwa na Serikali kujengwa na madaraja mengi kama hayo ya Tanzanite, barabara ya njia nane kutoka Ubungo kwenda Kimara mpaka Kibaha, lakini kule kwenye barabara ya Kilwa Serikali imefanya kazi kubwa sana kuanzia pale gerezani kwenda mpaka bandarini, kwenda mpaka rangi tatu kuna kilometa 20 pale kazi inakwenda moto moto katika kuhakikisha kwamba barabara ya mwendo kasi inajengwa kwa speed kubwa ili kuwaondolea adha wananchi ambao wanakwenda Mikoa ya Kusini ya Lindi, Mtwara Ruvuma mpaka Njombe siku hizi wanatumia barabara ile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kuna shida katika eneo la kutoka pale Rangi Tatu eneo wanaita Tanita kwenda kutokea pale Kongowe kuna shida kubwa, kuna kipande pale cha kilometa kama 12 hivi kimesahaulika, kile kipande tangu enzi za hayati Rais wetu wa Serikali ya Awamu ya Tano alipokuwa Waziri wa Ujenzi kile tayari kililengwa kujengwa kwa kiwango cha lami barabara nne mbili zinakwenda mbili zinarudi matokeo yake leo ni zaidi ya miaka 10 sasa hivi, diversion zimewekwa kwenye barabara ile sasa zinaota nyasi na kuota miti bado barabara ile haijaanza kujengwa toka pale Tanita kwenda Kongowe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninaiomba Serikali katika bajeti ya Mwaka 2022/2023 tuweze kuijenga ile barabara kwa kiwango cha lami njia nne ili kupunguza adha ambayo inawakuta wananchi ambao wanakwenda kwenye Mikoa hiyo niliyoitaja.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli barabara ile ikifika asubuhi wakati watu wengi wanakwenda katikati ya Jiji au wakati wa jioni wakati watu wanarudi majumbani kwao, kwa kweli imekuwa na adha, kipande kile cha kilometa 12 watu wanatumia masaa matatu hadi manne pale foleni ilivyokuwa imekaa vibaya, kwa hiyo naomba sana Serikali iangalie ile barabara ikiwezekana kwenye bajeti ya 2022/2023 basi iweze kufanyiwa kazi.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nikienda kwenye upande wa TARURA naishukuru Serikali pia kwa kazi kubwa ambayo imefanya ya kuongeza fedha hasa zile za maendeleo kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara, lakini nilikuwa na rai kwenye upande mmoja. Barabara zile pamoja na kwamba zimekuwa zikiletewa fedha nyingi na Serikali tena kwa wakati lakini taratibu za manunuzi zimekuwa zikichelewa sana kiasi kwamba hadi mvua kubwa za mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka zinapoanza unakuta bado miradi haija-take place kwa sababu zabuni inatangazwa katikati ya mwaka wa fedha, kwa hiyo, unakuta kipindi kama hiki sasa ndiyo wanahangaika sasa kuchakarika kuweza kutengeneza barabara wakati fedha zilishakuja muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninaomba Serikali isimamie TARURA ili iweze kutengeneza utaratibu ili angalau 60 percent ya zabuni ziweze kutangazwa kipindi kama hiki ili mwaka unapoanza wa utekelezaji wa miradi mwezi Julai basi tuweze kuendelea vizuri bila shida ili hiyo asilimia 40 inaweza ikatangaza zabuni zake baadaye kama ambavyo wanafanya wenzetu wa TANROADS. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia ningeomba Serikali itenge fedha za dharura kwaajili ya TARURA. Nchi yetu miaka ya karibuni imekuwa na bahati nzuri ya kuwa na neema ya kuwa na mvua nyingi, na matokeo yake kwa kuwa miradi inachelewa lakini vile vile kwa kuwa fedha za emergency hazipo basi inapofika mahali imetokea mvua kubwa, madaraja, makalavati yamebomoka inakuwa shida kupata fedha za kurekebisha hali inayojitokeza kwa haraka ya uvunjifu makalavati na madaraja hayo.
Mheshimiwa Spika, kwahiyo ningeomba Serikali itenge pia fedha za dharura ili ikitokea emergency basi mara moja fedha ziweze kwenda na TARURA iweze kuchukua nafasi na kufanya kazi yake sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine, ningeomba Serikali itenge fedha kwa ajili ya miradi maalum. Kama walivyotangulia kuongea baadhi ya Wabunge wenzangu siku ya leo, kwamba kuna baadhi ya maeneo kwenye baadhi ya majimbo kuna mabonde makubwa. Mimi pia pale kwangu, katika Jimbo langu, kuna bonde la Mto Hanga kutoka Kinjumvi kwenda Mtialambuko, lina urefu wa zaidi ya kilometa tano, ambapo wakati wa mvua maji yanajaa sana. Kwahiyo katika miradi kama ile unaweza ukakuta ukitegemea ile bilioni 1.5 ya maendeleo unaweza ukajikuta hela yote inazama kwa ajili ya kujenga tuta na kujenga daraja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwahiyo nilifikiri kwamba Serikali itafute vyanzo vya ziada ili tupate hela za ziada kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa kama ile ambayo inahitaji fedha nyingi.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni la pembejeo. Kumekuwa na shida katika mwaka uliopita, lakini nimefurahi Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Naibu wake hivi karibuni walikuja na ajenda ya 10/30 ambayo inaonekana itakuwa muarubaini sasa kwenye mambo ya pembejeo na miundombinu mingine ya uendeshaji wa shughuli za kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kwa kwakweli hali ilikuwa mbaya kutokana na changamoto ambayo imeelezwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya uwepo wa COVID 19. Hata hivyo bado Serikali inatakiwa iweke mkakati wa kudumu wa kuhakikisha kwamba changamoto ya upatikanaji wa mbolea pamoja na pembejeo isiwe endelevu ili tutatue hii changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano mwaka jana msimu uliopita tulikuwa na ununuzi wa mbolea aina ya urea ambayo ilifikia wastani wa shilingi 104,000 kwa pakti moja, mbolea ya aina ya sulpher iliuzwa mpaka shilingi 86,000. Wakati huo huo kwa wakulima wa mahindi walio wengi, Serikali ilinunua gunia moja kwa shilingi 55,000. Kwahiyo unaweza ukaona namna ambavyo wakulima wetu wanavyoumia, hasa wale ambao hawapewi ruzuku za bure. Tunaishukuru Serikali msimu uliopita kwa zao la korosho walitoa ruzuku ya bure, lakini kwa mazao mengine ilikuwa shida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini tumepata promise ya Mheshimiwa Waziri kwamba mazao mengine ya kimkakati nayo yatasaidiwa. Basi pale ambapo itashindikana tujitahidi kudhibiti hizi bei za pembejeo, hususani mbolea, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanalima kilimo chenye tija ili kuusukuma mbele uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, lakini nikienda kwenye uvuvi na mifugo; tumeanza kupata ahueni kupitia ajenda 10/30 kule kwenye kilimo. Wataalam wetu wa mifugo na uvuvi wamekuwa na shida ya vyombo vya usafiri. Wale wa kilimo tayari wameshapewa pikipiki 6,704. Naomba Serikali ielekeze jicho lake sasa kwa wataalam wetu wa mifugo na uvuvi ili nao waweze kupatiwa vitendea kazi hususani hivi vitendea kazi vya usafiri na hizo kits za kufanyia kazi katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile ningependa niiombe Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo na benki nyingine ambazo zinatoa mikopo ziwafikie wakulima, wavuvi na wafugaji wadogo kwa sababu wakulima, wavuvi na wafugaji wakubwa ndio wamekuwa wakipata mikopo hii kwa wingi. Na kwa sababu wao wana mitaji, wana uwezo wa kuajiri mtu wa kuandika maandiko; na kwa sababu masharti ni magumu na very complicated kiasi kwamba hayawezi kuwa attained na wale wafugaji, wakulima wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba tuwe na special funds. Kwamba, tunaweza tukaanzisha mfuko maalum wa maendeleo kwa ajili ya wakulima, wavuvi pamoja na wafugaji wadogo ili hata yule mkulima mwenye heka tatu aweze kunufaika na mikopo hii. Kwa sababu kwa hali iliyopo sasa hivi ni ngumu, kuna taratibu nyingi ambazo zinawafanya wale wakuliwa wasiweze kupata mikopo hiyo. Kwa hiyo ningeomba kwamba turekebishe, tushirikiane na watu wa vyama vya ushirika, tushirikiane na watu wa halmashauri; na ikiwezekana taratibu zake zifanane fanane na zile asilimia 10 zinatolewa na halmashauri ili kuwarahisishia…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: …wakulima, wavuvi na wafugaji kupata hiyo mikopo ili waweze kuboreshewa zana zao za kufanyia kazi, waweze kuchakata mazao vizuri, lakini vile vile waweze kuongeza thamani ya mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitangulie kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, jioni ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa namna ambavyo kwa haraka sana ameleta mabadiliko katika kuisimamia Wizara hii ambayo leo tunaijadili bajeti yake. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri Dada yangu, Mheshimiwa Angeline Mabula kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kushirikiana na Naibu Waziri wake pamoja na watendaji katika Wizara yake pamoja na watendaji katika taasisi mbalimbali zilizo chini yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza na takwimu. Katika sensa ya nchi yetu mwaka 2012 tulikuwa na watu milioni 44.9. Miaka kumi baadaye, yaani mwaka 2022 wananchi wetu waliongezeka hadi kufikia milioni 61.9 na kwa mujibu wa projection iliyopo, tunatarajia ifikapo 2025 wananchi wetu watakuwa milioni 67.9 na mwaka 2050 tunatarajia idadi ya watu katika nchi yetu ya Tanzania itakuwa milioni 151.2. Katika watu hao milioni 151.2 inatarajiwa asilimia 48 watakuwa wanaishi katika miji mbalimbali hapa nchini, kutokana na watu wengi wanaohamia katika miji lakini wanaozaliwa pia katika miji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Jiji letu la Dar es Salaam ndilo jiji ambalo linaongoza kwa sasa kwa kuwa na idadi kubwa ya watu, ikiwa na watu milioni 5.4 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 na inachukua asilimia 8.7 ya wananchi wote wa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kwa kusema, kwa mujibu wa taarifa za kiuchunguzi za UN zinaonesha kwamba Jiji letu la Dar es Salaam ni la tatu kwa kuwa na ongezeko kubwa la wananchi kwa mujibu wa Sensa ya Mwaka 2022. Pia kwa mujibu wa taarifa hizo hizo za UN, inaonesha kwamba nchi yetu ya Tanzania inakadiriwa ifikapo mwaka 2100 itakuwa ni nchi ya tisa yenye watu wengi hapa duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimetoa takwimu hizi makusudi ili mwone kwa namna gani tunatakiwa kujipanga katika kuhakikisha wananchi wetu tunawapatia makazi muhimu na Madhubuti. Ni lazima tuwe na mpango madhubuti wa makazi kwa wananchi wetu hasa wananchi wa hali ya chini wakiwemo watumishi pamoja na wale ambao wanafanya shughuli nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi uliopita Kamati yetu ya PIC (Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma) ilitembelea miradi inayosimamiwa na Taasisi yetu ya NHC. Kwa kweli tuliona mambo mazuri. Mheshimiwa Rais wetu amefanya mambo mazuri, amepeleka fedha nyingi kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa mradi wa nyumba pale Morocco Square na pia pale Kawe Seven Eleven, miradi ambayo ilisimama kwa muda mrefu. Nampongeza Mheshimiwa Rais, naipongeza Wizara kwa kazi nzuri inayoendelea katika ile miradi miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mradi mpya wa Samia Housing Scheme ambao unasimamiwa pia na watu wa National Housing, lakini ukiiangalia ile miradi na matarajio ya pesa zitakapouzwa zile apartments, kwa kweli ni fedha nyingi sana watahitaji kulipa wale watu ambao watanunua zile nyumba. Kwa hiyo, sioni nafasi ambayo Serikali imetoa kwa ajili ya uwekezaji kwenye nyumba za watu wa kawaida au watu wa hali ya chini kama watumishi wenye vipato vidogo vidogo, wakulima wadogo wadogo, wafanyabiashara wadogo wadogo na watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya mwanzoni kabisa mwa Uhuru tulishuhudia viongozi wetu, waasisi wa Taifa letu akiwemo Mzee wetu Abeid Amani Karume pamoja na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakiwekeza kwa kiasi kikubwa kwa wananchi wa vipato vya chini. Kwa hiyo, naiomba Serikali, turudi katika ule mwanzo mzuri ambao walituanzishia waasisi wetu. Pale Magomeni kulikuwa na sehemu ile ambayo sasa inaitwa Magomeni Mapipa, nyumba zilikuwa zikiezekwa kwa mapipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale Magomeni Quarters kulikuwa na nyumba zilikuwa zimeezekwa kwa makuti, lakini Hayati Baba wa Taifa akasema Hapana, ni lazima twende na mkakati wa kuanzisha nyumba ambazo wananchi watakodishwa au kukopeshwa kwa masharti nafuu. Watakuwa katika utumishi wao na mwisho wa utumishi wao watakuwa tayari wanajimilikia zile nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna hali inayojitokeza ambayo wananchi wetu hasa watumishi wa hali ya chini wamejikuta wakijenga nyumba baada ya kupata kipato chao cha kustaafu, wengine wanajikuta sasa wanatumia ile hela yote na kikokotoo kimebadilika sasa hivi, kwa hiyo, unajikuta wanatumia hela yote kujenga nyumba na hawamalizi, kwa hiyo mwisho wa siku wanabaki na stress, wanakufa mapema na mwisho siku ni lazima sasa tuone namna ambavyo tutatengeneza hii skimu mpya ambayo itawasaidia watu wa kipato cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kule Zanzibar kulikuwa na magorofa ya Michenzani yalijengwa na Hayati Abeid Karume kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini. Kwa hiyo, rai yangu kwa Wizara yetu, twende tukabuni revolving fund ambayo itapelekwa kwenye taasisi zetu ambazo zimehusika na ujenzi kama NHC, TBA pamoja na Mwananchi Housing ili waweze kujenga nyumba za aina hiyo, wananchi waweze kukopeshwa kwa bei nafuu wakiwa ndani ya utumishi wao, wakiwa na nguvu zao ili wanapofika umri fulani, basi wanamilikishwa zile nyumba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukatumia kwa mfano vifaa vya ujenzi tukaweka mle charge kidogo. Kwa mfano, kwenye cement kila mfuko wa cement tukiweka kwa mfano Shilingi mia moja, mia moja, mifuko mingapi ya cement inazalishwa hapa nchini kwenye viwanda vyetu? Tutajikuta tuna hela nyingi ya kuweza kuhudumia hao wananchi, na hiyo population ambayo tunatarajia ikue mpaka kufikia 2100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilifikiri kwamba kuna sheria nyingine za umilikaji wa ardhi zimepitwa na wakati pamoja na mali. Kwa mfano, sasa hivi mwananchi ambaye sio raia wa Tanzania haruhusiwi kumiliki ardhi katika nchi ya Tanzania. Sikusudii hapa kuzungumzia suala ya uraia pacha (duo citizenship), ninachoweza kuzungumza hapa ni kwamba, kama mtu anauwezo wa kuja kujenga apartments katika nchi yetu ambazo zitawasaidia wananchi wetu, zile nyumba hawezi kuondoka nazo, hata kama yeye sio raia wa nchi hii. Tuliona kule Dubai, ona leo Zanzibar, mambo haya yanaendelea, yanafanyika vizuri kabisa. Watu wanaruhusiwa kuwekeza, wanajenga majumba, na watu wanakodi, wengine wananunua, maisha yanaendelea, yanazidi kuboreka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuihudumia ile population ya mwaka 2001 ni lazima twende na hii mikakati…
MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndulane, kuna taarifa.
TAARIFA
MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mchangiaji. Kwa Hayati Mzee Karume, alizijenga nyumba hizi ambazo amezizungumza mchangiaji, mijini na vijijini zote zikiwa na hadhi moja. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndulane, taarifa unaipokea?
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru ndugu yangu hapa, Mheshimiwa Ali, kwa kweli naipokea taarifa yake kwa asilimia 100. Kwa hiyo, naomba tuliangalie hili jambo katika Wizara yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo napenda kulizungumzia ni kuhusu matumizi bora ya ardhi katika Wilaya yangu ya Kilwa, maana yake usije ukasemea Taifa halafu mwisho wa siku ukajikuta wewe kwako hujisemei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa matumizi bora ardhi, mwaka uliopita tulipitisha bajeti ya Shilingi bilioni 205, ilisomwa hapa, lakini baadaye ilirekebishwa, ikaongezwa hadi kufikia Shilingi bilioni 300. Kwa kweli Serikali ilifanya jambo zuri, lakini nasikitika kusema, katika vijiji kumi na moja ambavyo Wilaya yetu ya Kilwa ilitakiwa kuvipima katika mpango huu wa matumizi bora ya ardhi kupitia fedha zile ambazo niliomba hapa kwa kilio, bahati mbaya sisi wengine hatuna uwezo wa kuruka sarakasi, wala kupiga magoti, wala kulia ndani ya Bunge, ni wavumilivu sana, lakini zile pesa hazijafika hadi kufikia wakati huu. Naiomba Wizara, katika huu mwezi mmoja uliobaki ituletee fedha, tuendelee na upimaji na kuboresha mpango wa matumizi bora ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kulikuwa na mgogoro katika Kijiji cha Mtepela na katika utatuzi wa huo mgogoro tulijitahidi mimi pamoja na Mheshimiwa Diwani wangu wa Kata ya Miguruwe kusuluhisha. Pia Kamati ya Mawaziri nane ilifika, lakini kikubwa walichosisitiza pale wale Mawaziri, ni suala la ulinzi wa maji katika chanzo cha Mto Matandu. Mambo mengine hayakuzungumzwa, lakini juzi tumeona, wafugaji wanaambiwa ifikapo mwakani wawe wameondoka, wakulima ifikapo mwezi ujao, Julai tarehe 30 wawe wameondoka. Naomba, kabla ya utekelezaji wa kuwaondoa wale wananchi wa Kijiji cha Mtepela pale, basi uwepo mpango madhubuti wa kulipa fidia pamoja na kuzingatia mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika hotuba ya bajeti iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitangulie kutoa taarifa za masikitiko makubwa. Katika Jimbo letu la Kilwa Kaskazini, siku nne zilizopita tulipatwa na maafa makubwa ya mafuriko kutokana na mvua kubwa za El-Nino zinazoendelea kunyesha katika Milima ya Matumbi zilizosababisha kupoteza maisha ya watoto wetu wawili waliokuwa wakisoma darasa la sita katika Kijiji cha Chumo. Tulimpoteza kijana wetu mdogo anaitwa Hawa Haji Kekarange, lakini pia tulimpoteza Abdul Aziz Kapanda. Mwenyezi Mungu aziweke roho zao marehemu hawa mahali pema peponi. Amina. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kuchangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu moja kwa moja leo nitajikita katika upande wa sekta ya barabara ambayo imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa mvua za El-Nino hapa nchini. Changamoto ni kubwa na tusipozifanyia kazi katika kipindi hiki, basi hata ile asilimia 5.4 ya ukuaji wa uchumi inaweza isifikiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa barabara hii ya Tingi - Kipatimu. barabara ile ambayo ipo katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini imeathirika sana. Barabara ile tangu tarehe 9 Desemba, 2023 ilipata changamoto kubwa za kutopitika. Vilevile, sababu siyo tu mvua za El-Nino bali pia kumekuwepo na malori yenye uzito mkubwa usiolingana na uwezo wa barabara, madaraja na makalavati yaliyopo kule ambao umesababisha madaraja yabomoke kabla hata ya mvua na mafuriko ya juzi na matokeo yake upitikaji wa barabara umekuwa mgumu. Tuzingatie kwamba yale malori yamekuwa yakifanya kazi kubwa ya kupeleka malighafi za ujenzi wa bandari ya uvuvi kule Kilwa Masoko (Mradi mkubwa wa kimkakati ambao Serikali yetu imewekeza kwa kiasi kikubwa). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuzorota kwa barabara ile kumesababisha hata ule Mradi wa Kilwa Masoko wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi nao umezorota kwa sababu hayapeleki ile malighafi ya mawe ya ujenzi kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kutokana na El-Nino mambo ndiyo yamekuwa magumu zaidi, juzi tu yalipotokea yale mafuriko maeneo manne ya tuta la barabara yaliyo jirani kabisa na madaraja pamoja na makalavati yamekatika na sasa barabara ile haipitiki kabisa kwa asilimia mia moja pamoja na umuhimu wake huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba barabara ile inakwenda kwenye kumbukumbu za Maji Maji ambazo zitatuongezea ufanisi katika utalii ambazo umepata GN hivi majuzi. Kwa hiyo, naiomba Serikali iiangalie ile barabara kwa jicho la pekee na kwa kuwa barabara ile ina milima mirefu ambayo inatiririsha maji kila siku. Kwanza Serikali ichukue hatua ya kurekebisha miundombinu ya barabara ile ili sehemu kubwa ya barabara ipite juu ya milima badala ya kupita bondeni. Kwa mfano, mafuriko yaliyotokea juzi yametokea katika Bonde la Chumo ambalo lina urefu wa zaidi ya kilometa tano na barabara imepita humo humo kwenye bonde. Kwa hiyo, nafikiri kwamba sasa wataalam wetu wabuni utaratibu ambao barabara hii isipite sehemu ya mabonde pale ambapo hakuna ulazima wa kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ambayo napenda kuishauri Serikali ni kwamba, barabara ile katika maeneo yenye miinuko mikali, tutengeneze barabara za zege ili ziwe na uhakika wa kupitika muda wote wa mwaka. Pia wawepo wenzetu wa TARURA na TANROADS waweze kuhudumia ipasavyo kupitia bajeti ambayo tutaipitisha hapa keshokutwa na pia hata zile fedha za dharura zinazopelekwa kwa ajili ya barabara zetu za TANROADS na TARURA, nyingi zimekwenda katika maeneo ambayo siyo ya kipaumbele. Kwa mfano, kuna barabara ya kijijini kutoka Kipatimu kwenda Kibata makalavati na madaraja yalivunjika tangu tarehe 9 Desemba, mvua kubwa za El-Nino zilipokuwa zimepamba moto, mpaka wakati huu ile barabara ambayo ilipewa first priority na wenzetu wa TARURA haijashughulikiwa. Badala yake milioni 200 zilizoletwa kwa ajili ya dharura zimepelekwa kwenye barabara ambayo ni priority namba sita kwa mujibu wa ushauri wa wataalam wetu. Naomba priorities za wataalam zizingatiwe ili kule ambako kuna changamoto kubwa, basi solution iweze kupatikana mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nina ushauri wa kitaifa, janga la El-Nino limetokea nchi nzima na maafa yamekuwa makubwa. Kwa hiyo, tunahitaji uwekezaji mkubwa kwenye barabara zetu zote hapa nchini, kwamba bajeti ya Wizara yetu ya Ujenzi iweze kuongezwa hadi kufikia asilimia 30 ya bajeti nzima ya Serikali Kuu ili asilimia 60 za zabuni ziweze kutangazwa mapema mara tunapokuwa tumepitisha bajeti zinazohusika na barabara. Keshokutwa tukipitisha kuanzia TARURA basi wapewe ruhusa ya kuweza kutangaza zabuni. Pia TANROADS wapewe ruhusa angalau asilimia 60 itangazwe mara moja tutakapopitisha bajeti ili mwaka wa fedha unapoanza na kazi ya marekebisho makubwa ya barabara ambazo zimeathirika kwa kiasi kikubwa na mvua za El-Nino ianze. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la nne ambalo ningependa kushauri ni kwamba, fedha za dharura pia zitengwe, tusisubiri mpaka dharura itokee. Hata kama zitakaa Makao Makuu ya TANROADS au Wizarani siyo mbaya ili dharura itakapotokea mara moja kazi ya kurekebisha miundombinu iliyoathirika iweze kwenda kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitengo vinavyohusika na technical audit kule TANROADS na kule TARURA pia viimarishwe kwa kupewa fedha za kutosha kwa ajili ya kumudu kufanya kazi zao. Kuongezewa vile vile watumishi au wataalam wa kutosha ili waweze kushughulika na changamoto zote zinazoendelea na waweze kupewa vitendea kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina hakika changamoto ambayo ilionekana Mkoani Lindi na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ya kukuta mtaalam wa falsafa anasimamia barabara na maeneo mengine inasemekana wapo wataalam wa minyororo baridi na wataalam wa saikolojia ambao wanasimamia barabara. Hili tatizo lingeweza kuonwa na technical auditors kama kitengo hiki kingefanya kazi zake sawasawa na marekebisho yangefanyika mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitengo hiki pia kipewe jukumu la kufanya utafiti wa barabara zetu zote, madaraja yetu yote, makalavati yetu yote ili kuhakikisha kwamba kabla athari kubwa hazijajitokeza, ziweze kushughulikiwa mapema. Kwa sababu miundombinu mingi ya barabara imeanza kujengwa tangu mwanzoni mwa mwaka 2000, kwa hiyo, lifespan ya hizi barabara, madaraja na makalavati sehemu kubwa zimekwishapitwa na wakati. Hata hivyo, kwa kuwatumia wataalam wetu hawa wa technical audit wanaweza wakatuwekea mambo sawasawa na tukaweza kufanya preventive maintenance na hatimaye hizi barabara zikapitika kwa kiwango kinachostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa licha ya Waziri na Naibu Waziri kuwa wanatutembelea katika maeneo mengi hata kama Barabara yangu ya Tingi – Kipatimu Mheshimiwa Waziri hajaweza kufika, basi ajitahidi afike kila maeneo. kwa sababu Mawaziri hawana uwezo wa kufika kila eneo wawatume Maafisa Waandamizi waje wakague hizo barabara ili waone uhalisia. Unaweza ukakuta unapokea taarifa mezani, mwisho wa siku hali sivyo ilivyo huko ambako barabara zinajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja namba saba ambayo ningependa kuishauri Serikali ni ujenzi wa mifereji pembezoni mwa barabara. Barabara zetu nyingi hasa zile za vumbi na hata zile za lami baadhi hazina mifereji. Unakuta barabara imejengwa tu mifereji ya kupitisha maji hakuna, mvua zikinyesha zinapita katikati ya barabara na kuharibu barabara vibaya sana. Kama mvua za El-Nino zilivyo mwaka huu, barabara zimegeuka kuwa mito na hatimaye zimekuwa na madhara kama haya ambayo nimeyasema. Kwa hiyo, naomba tuone namna ya kufanya ili ujenzi uweze kuimarishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia utafiti wa barabara zetu na namna ya ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ndulane, muda wako umekwisha.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kutoa mchango wangu kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2023/2024. Mimi ningependa kujikita kwa kuanzia na sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali kwa kuongeza fedha katika bajeti yake toka shilingi bilioni 294 hadi shilingi bilioni 954 kati ya mwaka jana na mwaka huu wa fedha. Na ningependa kuchangia eneo hili kwanza kwa sababu, wananchi wetu asilimia 65 ajira zao ziko kwenye kilimo, lakini pia hata Pato la Taifa ni asilimia 26 ya Pato la Taifa linatokana na mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ningependa kusema kwamba, bado sekta hii haijatumika vizuri katika kuifanya nchi yetu iweze kupata mapato mengi zaidi. Ni imani yangu kwamba, kama rasilimali tulizonazo za ardhi, lakini pia kuwa na utaratibu bora wa kusimamia hiki kilimo ungefanyika basi mambo yangekwenda vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiifuatilia taarifa iliyotolwa na Mheshimiwa Waziri na ile iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, nimeona pale tuna jumla ya hekta milioni 29 za ardhi ambazo zinafaa kwa ajili ya kilimo; lakini ni asilimia 2.75 tu ya eneo hilo ndilo linalotumika kwa kilimo hivi sasa. Kwa hiyo kuna hekta zaidi ya milioni 28 hazitumiki kwa kilimo hivi sasa. Kwa hiyo nilikuwa nafikiri kuna jambo la kufanya katika eneo hili; kwanza ni kuhakikisha kwamba, hizi pesa ambazo zimeongezwa ziendelee kuongezwa ili tuweze kuhudumia miundombinu mbalimbali pamoja na mikakati mbalimbali ya kuboresha kilimo chetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano nimeona hapa idadi ya mabwawa ambayo yatajengwa hapa nchini kulingana na ule mpango wa maendeleo ni machache sana. Nilifikiri Serikali yetu niishauri ijikite katika kuongeza idadi ya mabwawa katika mikoa yote ya nchi nzima na si baadhi tu ya mikoa, kwa sababu nafahamu katika mikoa yote karibu ina idadi kubwa ya mito ambayo inatiririsha maji katika kipindi cha mwaka mzima. Kwa hiyo, ukiondoa Dar-es-Salaam mikoa mingine yote tuna uwezo wa kujenga mabwawa na kuwafanya wakulima wetu wakaweza kuzalisha kwenye hili eneo kubwa ambalo limebaki idle halitumiki kwa ajili ya shughuli za kilimo na kufanya uzalishaji wa mazao ya kilimo, yale ya chakula na ya biashara, yaweze kuzalishwa kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itaongeza uchumi kwa sababu, sasa hivi bei ya chakula imepanda sana. Na imepanda si kwa sababu, sisi Tanzania hatulimi, tunalima, lakini tunalima kwa kiasi kidogo na tunahuidumia hadi nchi zinazotuzunguka ambazo kwa sasa zina hali mbaya ya chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ningeomba Serikali ijikite katika vile vituo ambavyo ni vya kutolea huduma kwa wakulima. Kwanza iviongezee majukumu nje ya yale ambayo yameainishwa kwenye mpango wa maendeleo. Moja kati ya majukumu ambayo ningependekeza yaongezwe ni kufuatilia wakulima wetu, mpaka wale wadogo kabisa, ili kujua changamoto zao zikoje, lakini pia kuona namna ya kutatua hizo changamoto ambazo zinawakabili. Wapo wakulima ambao wanakosa mitaji kwa ajili ya kulima, lakini wapo wakulima wengine wana changamoto mbalimbali. Kwa hiyo zitajulikana kupitia hivi vituo. Na hivi vituo visambae si tu kwa mikoa mitano bali viwepo katika mikoa yote ambayo inalima, ukiondoa Dar-es-Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ningependa kuzungumzia masuala ya utalii. Tumepata mafanikio makubwa kupitia mpango ambao uliasisiwa na Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, wa Royal Tour kuhusu ongezeko la mapato kutokana na watalii ambao waliongezeka. Taarifa inaonesha kwamba, asilimia 114.7 iliongezeka katika mwaka wa fedha huu uliopita ukilinganisha na ule uliotangulia. Kiasi kama cha dola zaidi ya 1,000 milioni ziliongezeka kwenye pato la Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba sekta hii ya utalii imechangia kwa asilimia 17 katika mwaka wa fedha uliopita kwenye Pato la Taifa. Kwa hiyo nilikuwa naomba hii Royal Tour iwe extended.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitarajia nione kwenye mpango wa Serikali wa maendeleo uainishe basi ni wapi sasa tunakwenda baada ya mafanikio yale ambayo tumeyapata katika mwaka uliopita. Kwa hiyo nilitarajia zile hifadhi zetu mbalimbali ambazo hazijapitiwa na mpango ule wa kwanza, mbuga, mapori ya akiba, kumbukumbu za majimaji kule Lindi kwa maana ya Kilwa na Songea, lakini pia hata yale magofu ya kule Kilwa Kisiwani na Songo Mnara. Kuna wale viboko maalbino tuone waingie hata kama kwa phases.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, tuone namna ambavyo tutaboresha miundombinu, kwa sababu hizi sekta za usalishaji zinategemeana sana na miundombinu ya barabara. Tuone barabara mbalimbali ambazo sasa zina changamoto kubwa zinakwendaje kusapoti katika uendelezaji wa hizi sekta ambazo ni za uzalishaji mali; kuna barabara ya Nangurukuru – Liwale pale kilometa 258 ipo miaka inaenda miaka inarudi, ule upembuzi yakinifu umefanyika, lakini bado haijajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimalizie na sekta ya elimu. Niiombe Serikali sasa iangalie pia kwa walimu. Walimu wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu, hawana nyumba, walimu wanakaa watatu-watatu kwenye nyumba za vyumba vitatu-vitatu na familia zao kubwa. Wangalie na upande huo pia ili kuboresha elimu yetu kwa kusudio ambalo limekusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nasema naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii ya kuweza kuchangia kwenye taarifa zilizotolewa kwa umakini mkubwa na Wenyeviti wetu wa Kamati ya Bajeti pamoja na Kamati ya PIC. Leo nitapiga sana kwenye Kamati ya PIC ambapo mimi ni Mjumbe wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitangulie kumpongeza Mwenyekiti wangu au Mwenyekiti wetu wa Kamati ya PIC, Mheshimiwa Deus Sangu kwa kuisoma taarifa yetu kwa umakini mkubwa kama ambavyo tulikuwa tumeijadili kabla ya kuileta hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nita-concentrate na TTB peke yake leo. Nataka niidadavue kwa mapana na marefu. Kwa mujibu wa Sheria Na. 364, majukumu makubwa ya TTB ni kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi ya Tanzania, kuhamasisha uendelezaji wa miundombinu ya utalii, kufanya tafiti za utalii na kutoa elimu kwa Umma kuhusu umuhimu wa Sekta ya Utalii. Mimi nita-concentrate na mambo matatu ya kwanza katika haya mambo niliyoyataja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitaanza na suala la kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya Tanzania. Bado hatujafanya kazi kubwa ya kuiwezesha TTB au Tanzania Board for Tourism iweze kufanya kazi yake sawa sawa. Sababu kubwa inayosababisha kazi hii isifanyike kwa utimilifu mkubwa ni kutokana na taasisi hii kuwa na upungufu wa fedha za uendeshaji wa shughuli zake. Tunafahamu Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan alifanya Filamu ya Royal Tour na ambayo imeongeza kwa kiasi kikubwa sana kutangaza vivutio vyetu vya utalii na pia kwa haraka sana kuwafanya watalii waweze kuongezeka kutoka nje ya nchi na hivyo, kuongeza hata pato la Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna kazi kubwa ya kufanya katika eneo hili kwa sababu bado kuna maeneo mengi ya vivutio vya utalii hayajatangazwa. Kwa mfano, kuna wakati nilikuwa nasafiri na ndege ya shirika moja kubwa la ndege la nchi ya jirani, tukielekea katika hiyo nchi ya jirani. Wakati tunakaribia kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, yule Air Hostess alisikika akisema, “Sasa tunakaribia kutoka katika anga ya Tanzania na kuingia anga ya Kenya.” Aka-pause kidogo, halafu baadaye akasema, wakati ile ndege ilipofika kwenye kile kilele ikawa ina-corner hivi, bawa moja limeshuka chini na lingine limekwenda juu, wakati tunakiona vizuri sana kile kilele kwa chini upande wa kulia kwetu, akasema, “on your right-hand side you can see the peak of Mount Kilimanjaro.” Aka-pause. Baada ya muda wakati tunakiacha kile kilele pale, akasikika akisema, “Sasa tunajiandaa kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta.” Tulichukua zaidi ya dakika 40 mpaka tulipotua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaona wenzetu walivyokuwa makini katika kuhakikisha kwamba wanatumia matangazo hadi kwenye mashirika ya ndege, kuhakikisha kwamba wanatangaza rasilimali ambazo hata nyingine siyo za kwao, lakini katika mazingira ya kuleta karibu na nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku nyingine niliwahi kupanda ndege ya zile Wings of Kilimanjaro, (Shirika letu la ATCL). Wakati tunapita katika eneo lile la Mlima Kilimanjaro, kulikuwa kimya tu. Yule Air Hostess hakuzungumza chochote mpaka tulivyofika safari yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini ninachotaka kusema hapa? Wenzetu wanatumia rasilimali zote walizonazo katika kuhakikisha kwamba wanatangaza hivi vivutio vizuri. Kwa hiyo, hata taasisi yetu ya TTB tunatakiwa tuendelee kuiimarisha, kuiwezesha kifedha ili kuhakikisha kwamba inakwenda kuwezeshwa kutangaza vilivyo, ikiwemo kupitia Shirika letu la Ndege la ATCL, mashirika ya kigeni ambayo tuna uhusiano nayo mzuri katika kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya kwamba tayari kuna mipango mizuri ya kutumia watu maarufu kama wacheza mpira maarufu kama wakina Christiano Ronaldo, Lionel Messi, kutumia hayo mashirika ya ndege lakini bado hatujapiga hatua nzuri. Shida ni uwezeshaji wa kifedha kutokana na kuwa na bajeti ndogo ya TTB. Naiomba Serikali iongeze fedha kwa TTB ili tuweze kuiwezesha hii TTB iweze kufanya kazi yake ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye suala la utafiti ambalo ni jukumu la pili kwa taasisi ya TTB; niliwahi kusoma na baadaye nikathibitishiwa na wataalamu wetu ambao wanafanya kazi kubwa ya utafiti tangu mwaka 2016 katika Visiwa vya Mafia. Imegundulika tangu mwaka 2016 kuna Mji wa Rhapta ambao ulizama baharini. Utafiti wa mji ule ambao ulikuwa umefikia kiwango cha metropolis lakini pia ulikuwa na eneo kubwa la kibiashara, ulikuwa na urefu wa Kaskazini Kusini Kilometa tatu, mapana kilometa tano. Ulikuwa mji maarufu ambao tangu karne ya kwanza mpaka ya tano Warumi waliweza kufanya safari nyingi na kushirikiana nao enzi zaa dola ya Warumi kabla haijaanguka kuweza kufanya biashara. Waliandika kumbukumbu nyingi ambazo baada ya ule mji kuzama, waliweza kuzitumia kuutafuta ule mji na ndiyo imekuja kugundulika mwaka 2016, hapo kwenye Visiwa vya Mafia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijaona input ya TTB katika kufanya research ile. Kuna taasisi binafsi ambayo ina hoteli jirani na pale, ndiyo ambayo imekuwa ikishirikiana na wataalamu wetu kutoka University of Dar es Salaam katika kuhakikisha kwamba wanafanya huo utafiti kwa mafanikio. Mpaka leo tayari wamefanya kazi kubwa ambayo imetangazwa mpaka Marekani. Kuna Taasisi ya Discovery Channel kutoka Marekani iliyokuja kuchukua film na hivi karibuni wataanza kuicheza nchini Marekani. Sisi wenyewe tupo, kwa sababu hatujaiwezesha TTB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mapango ambayo yalifanyiwa utafiti na Serikali ya Wakoloni ya Ujerumani mwaka 1901 lakini alitokea mtu mmoja anaitwa Truman kutoka Ujerumani mwaka 1911 na baadaye alikuja mtu mmoja anaitwa Herbat Daniel Galabawa Garabao kutoka Ujerumani na timu yake mwaka 1994 – 2000. Katika Milima ya Matumbi waligundua kuna mapango zaidi ya 20. Kule Tanga kuna sehemu inaitwa Mwinyigongo, kuna pango la pili kwa urefu hapa Tanzania pale Mwinyigongo. Bado kuna mapango mengine ya Amboni, acha lile tunaloliona, tisa ukichanganya na lile la 10. Bado walikwenda kule Zanzibar kuna pango linaitwa Mangapwani. Kwa hiyo, jumla ni kama 33 likiongezwa na Pango la Nang’oma lililoko katika ardhi ya Matumbi au Milima ya Matumbi ambalo ndilo pango refu kuliko yote, lina Kilometa 7.51. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijaona TTB wakifanya kazi ya utafiti kule, japokuwa moja kati ya core function zake ni kufanya utafiti. Hata kutangaza basi, baada ya kuwa hawa Wajerumani na wataalam wengine wametaja hiyo Rhapta na kwingineko, hakuna hatua zilizochukuliwa katika kuwezesha kuendeleza hivyo vituo vya utalii ili viweze kuleta utalii mwingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati niliwahi kutembelea Marrakesh wakati ina-deal na mambo ya michezo. Kule kuna kitanda ambacho aliwahi kulala Mtume (S.A.W.) enzi zake katika safari zake kule Afria Kaskazini. Mpaka leo kimehifadhiwa, kinaingiza fedha nyingi kule Marrakesh na kinaleta pesa nyingi. Kwa hiyo, nina imani hata sisi hizi kazi zilizofanyiwa utafiti, tukizifanyia kazi inayotosha kupitia TTB, basi tutaweza kupiga hatua kubwa katika kuingiza mapato katika nchi yetu kupitia Sekta ya Utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, jukumu lingine katika Bodi hii ni suala la uendelezaji wa miundombinu ya utalii. Pale Kilwa kuna mradi unaitwa Regrow, unaojenga Kiwanja cha Ndege cha Kilwa ambapo kutoka kwenye kile kiwanja cha ndege kwenda kwenye lango la Selous ni Kilometa 70, kwenda kwenye Viboko Albino kule Pindilo ni kilometa 120, kwenda Kumbukumbu za Majimaji na haya mapango niliyoyazungumza ni kilometa 120, lakini mpaka leo ule mradi unasuasua. Serikali iwezesheni TTB ili iweze kukamilisha ule mradi. Tutapata faida kubwa kwa sababu watalii wakija wataweza kupelekwa katika hivyo vivutio na hatimaye tutapata pesa nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, mwezi Novemba mwaka 2023 Muswada ulikuja hapa kuhusu kuboresha Ofisi ya TR kwa kuundwa Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania. Ule Muswada tunaona kama umeyeyuka vile. Hatujui umepotelea wapi? Naomba ule Muswada uje haraka Bunge lijalo ili tuweze kuupitisha, uwe sheria kamili ili hatimaye kuiwezesha hii mamlaka isimamie Uwekezaji wa Mitaji ya Umma katika mashirika mbalimbali ili mashirika hayo yaweze kuleta faida na tija kubwa kwa wananchi wa Tanzania ili hizi faida ziweze kuzalishwa, ajira ziweze kuzalishwa, tija na ufanisi uweze kupatikana katika taasisi hizo na hatimaye nchi yetu iweze kupiga hatua kubwa za kiuchumi na kulijenga Taifa letu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono taarifa zote zilizotolewa hapa na mapendekezo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika hotuba ya bajeti iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitangulie kutoa taarifa za masikitiko makubwa. Katika Jimbo letu la Kilwa Kaskazini, siku nne zilizopita tulipatwa na maafa makubwa ya mafuriko kutokana na mvua kubwa za El-Nino zinazoendelea kunyesha katika Milima ya Matumbi zilizosababisha kupoteza maisha ya watoto wetu wawili waliokuwa wakisoma darasa la sita katika Kijiji cha Chumo. Tulimpoteza kijana wetu mdogo anaitwa Hawa Haji Kekarange, lakini pia tulimpoteza Abdul Aziz Kapanda. Mwenyezi Mungu aziweke roho zao marehemu hawa mahali pema peponi. Amina. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kuchangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu moja kwa moja leo nitajikita katika upande wa sekta ya barabara ambayo imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa mvua za El-Nino hapa nchini. Changamoto ni kubwa na tusipozifanyia kazi katika kipindi hiki, basi hata ile asilimia 5.4 ya ukuaji wa uchumi inaweza isifikiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa barabara hii ya Tingi - Kipatimu. barabara ile ambayo ipo katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini imeathirika sana. Barabara ile tangu tarehe 9 Desemba, 2023 ilipata changamoto kubwa za kutopitika. Vilevile, sababu siyo tu mvua za El-Nino bali pia kumekuwepo na malori yenye uzito mkubwa usiolingana na uwezo wa barabara, madaraja na makalavati yaliyopo kule ambao umesababisha madaraja yabomoke kabla hata ya mvua na mafuriko ya juzi na matokeo yake upitikaji wa barabara umekuwa mgumu. Tuzingatie kwamba yale malori yamekuwa yakifanya kazi kubwa ya kupeleka malighafi za ujenzi wa bandari ya uvuvi kule Kilwa Masoko (Mradi mkubwa wa kimkakati ambao Serikali yetu imewekeza kwa kiasi kikubwa). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuzorota kwa barabara ile kumesababisha hata ule Mradi wa Kilwa Masoko wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi nao umezorota kwa sababu hayapeleki ile malighafi ya mawe ya ujenzi kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kutokana na El-Nino mambo ndiyo yamekuwa magumu zaidi, juzi tu yalipotokea yale mafuriko maeneo manne ya tuta la barabara yaliyo jirani kabisa na madaraja pamoja na makalavati yamekatika na sasa barabara ile haipitiki kabisa kwa asilimia mia moja pamoja na umuhimu wake huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba barabara ile inakwenda kwenye kumbukumbu za Maji Maji ambazo zitatuongezea ufanisi katika utalii ambazo umepata GN hivi majuzi. Kwa hiyo, naiomba Serikali iiangalie ile barabara kwa jicho la pekee na kwa kuwa barabara ile ina milima mirefu ambayo inatiririsha maji kila siku. Kwanza Serikali ichukue hatua ya kurekebisha miundombinu ya barabara ile ili sehemu kubwa ya barabara ipite juu ya milima badala ya kupita bondeni. Kwa mfano, mafuriko yaliyotokea juzi yametokea katika Bonde la Chumo ambalo lina urefu wa zaidi ya kilometa tano na barabara imepita humo humo kwenye bonde. Kwa hiyo, nafikiri kwamba sasa wataalam wetu wabuni utaratibu ambao barabara hii isipite sehemu ya mabonde pale ambapo hakuna ulazima wa kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ambayo napenda kuishauri Serikali ni kwamba, barabara ile katika maeneo yenye miinuko mikali, tutengeneze barabara za zege ili ziwe na uhakika wa kupitika muda wote wa mwaka. Pia wawepo wenzetu wa TARURA na TANROADS waweze kuhudumia ipasavyo kupitia bajeti ambayo tutaipitisha hapa keshokutwa na pia hata zile fedha za dharura zinazopelekwa kwa ajili ya barabara zetu za TANROADS na TARURA, nyingi zimekwenda katika maeneo ambayo siyo ya kipaumbele. Kwa mfano, kuna barabara ya kijijini kutoka Kipatimu kwenda Kibata makalavati na madaraja yalivunjika tangu tarehe 9 Desemba, mvua kubwa za El-Nino zilipokuwa zimepamba moto, mpaka wakati huu ile barabara ambayo ilipewa first priority na wenzetu wa TARURA haijashughulikiwa. Badala yake milioni 200 zilizoletwa kwa ajili ya dharura zimepelekwa kwenye barabara ambayo ni priority namba sita kwa mujibu wa ushauri wa wataalam wetu. Naomba priorities za wataalam zizingatiwe ili kule ambako kuna changamoto kubwa, basi solution iweze kupatikana mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nina ushauri wa kitaifa, janga la El-Nino limetokea nchi nzima na maafa yamekuwa makubwa. Kwa hiyo, tunahitaji uwekezaji mkubwa kwenye barabara zetu zote hapa nchini, kwamba bajeti ya Wizara yetu ya Ujenzi iweze kuongezwa hadi kufikia asilimia 30 ya bajeti nzima ya Serikali Kuu ili asilimia 60 za zabuni ziweze kutangazwa mapema mara tunapokuwa tumepitisha bajeti zinazohusika na barabara. Keshokutwa tukipitisha kuanzia TARURA basi wapewe ruhusa ya kuweza kutangaza zabuni. Pia TANROADS wapewe ruhusa angalau asilimia 60 itangazwe mara moja tutakapopitisha bajeti ili mwaka wa fedha unapoanza na kazi ya marekebisho makubwa ya barabara ambazo zimeathirika kwa kiasi kikubwa na mvua za El-Nino ianze. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la nne ambalo ningependa kushauri ni kwamba, fedha za dharura pia zitengwe, tusisubiri mpaka dharura itokee. Hata kama zitakaa Makao Makuu ya TANROADS au Wizarani siyo mbaya ili dharura itakapotokea mara moja kazi ya kurekebisha miundombinu iliyoathirika iweze kwenda kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitengo vinavyohusika na technical audit kule TANROADS na kule TARURA pia viimarishwe kwa kupewa fedha za kutosha kwa ajili ya kumudu kufanya kazi zao. Kuongezewa vile vile watumishi au wataalam wa kutosha ili waweze kushughulika na changamoto zote zinazoendelea na waweze kupewa vitendea kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina hakika changamoto ambayo ilionekana Mkoani Lindi na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ya kukuta mtaalam wa falsafa anasimamia barabara na maeneo mengine inasemekana wapo wataalam wa minyororo baridi na wataalam wa saikolojia ambao wanasimamia barabara. Hili tatizo lingeweza kuonwa na technical auditors kama kitengo hiki kingefanya kazi zake sawasawa na marekebisho yangefanyika mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitengo hiki pia kipewe jukumu la kufanya utafiti wa barabara zetu zote, madaraja yetu yote, makalavati yetu yote ili kuhakikisha kwamba kabla athari kubwa hazijajitokeza, ziweze kushughulikiwa mapema. Kwa sababu miundombinu mingi ya barabara imeanza kujengwa tangu mwanzoni mwa mwaka 2000, kwa hiyo, lifespan ya hizi barabara, madaraja na makalavati sehemu kubwa zimekwishapitwa na wakati. Hata hivyo, kwa kuwatumia wataalam wetu hawa wa technical audit wanaweza wakatuwekea mambo sawasawa na tukaweza kufanya preventive maintenance na hatimaye hizi barabara zikapitika kwa kiwango kinachostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa licha ya Waziri na Naibu Waziri kuwa wanatutembelea katika maeneo mengi hata kama Barabara yangu ya Tingi – Kipatimu Mheshimiwa Waziri hajaweza kufika, basi ajitahidi afike kila maeneo. kwa sababu Mawaziri hawana uwezo wa kufika kila eneo wawatume Maafisa Waandamizi waje wakague hizo barabara ili waone uhalisia. Unaweza ukakuta unapokea taarifa mezani, mwisho wa siku hali sivyo ilivyo huko ambako barabara zinajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja namba saba ambayo ningependa kuishauri Serikali ni ujenzi wa mifereji pembezoni mwa barabara. Barabara zetu nyingi hasa zile za vumbi na hata zile za lami baadhi hazina mifereji. Unakuta barabara imejengwa tu mifereji ya kupitisha maji hakuna, mvua zikinyesha zinapita katikati ya barabara na kuharibu barabara vibaya sana. Kama mvua za El-Nino zilivyo mwaka huu, barabara zimegeuka kuwa mito na hatimaye zimekuwa na madhara kama haya ambayo nimeyasema. Kwa hiyo, naomba tuone namna ya kufanya ili ujenzi uweze kuimarishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia utafiti wa barabara zetu na namna ya ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ndulane, muda wako umekwisha.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo kwenye taarifa zetu za Kamati ya PIC, PAC na LAAC. Kwa ujumla niwashukuru Wenyeviti wetu wa Kamati zote tatu kwa kuweza kusoma taarifa zetu kwa umahiri mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikiwa mjumbe wa Kamati ya PIC, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, najikita moja kwa moja kwenye taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Augustine Vuma wa Kamati ya PIC kwenye maeneo mawili. Eneo la kwanza ni kwenye ukurasa wa 29 hadi 31 wa taarifa yetu ambayo imezungumzia kuhusu gharama za kuunganisha umeme katika maeneo ya vijiji-miji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajenga hoja kwenye hilo eneo, nitangulie kusema ninaishukuru Serikali yetu ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza kwa ufanisi kwenye Miradi yetu ya REA. Hivi juzi tu tuliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa REA kwenda katika Kijiji cha Zinga-Kibaoni ambapo tuliweza kuzindua umeme. Sasa utekelezaji wa miradi ya umeme awamu ya tatu, mzunguko wa pili imefikia 99% ya utekelezaji katika jimbo la Kilwa Kaskazini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishukuru Serikali, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri inayoendelea. Wananchi wangu walipata bonus kubwa sana ya kugawiwa majiko ya gesi 231 katika mpango wa Serikali unaoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Samia Hassan, Rais wetu wa kupambana na nishati isiyokuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninapozungumza, hata jana tayari Kijiji cha Ngarambilihenga umeme umewaka na kesho tunatarajia vijiji viwili vya mwisho umeme utawashwa; Kijiji cha Liyomanga na Nambondo katika Kata ya Mingumbi na Kata ya Namayuni. Naipongeza Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia kwa nguvu zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii changamoto imekuwa kubwa na mara kadhaa tuliifahamisha Serikali. Nakumbuka katika Bunge la mwaka juzi la Bajeti, Mheshimiwa Waziri wa Nishati wa wakati ule, Mheshimiwa Januari Makamba wakati anahitimisha hotuba yake ya bajeti aliipokea hoja hii ya gharama kubwa za uunganishaji wa umeme katika vijiji-miji. Mwaka huu Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko naye alipokea na akaahidi kwamba itafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani katika Bunge lililopita la mwezi Agosti na Septemba, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara hii Dada yangu Mheshimiwa Judith Kapinga naye aliipokea akaahidi kwamba itatekelezwa. Mheshimiwa Mwenyekiti ameeleza vizuri katika taarifa ya Kamati yetu. Hili jambo bado linaendelea kusumbua wananchi wetu, na kwa kuwa wananchi wetu wanaishi katika vijiji-miji ambavyo either viko katika majiji yetu, either katika manispaa zetu, either katika halmashauri zetu za miji, au halmashauri zetu za wilaya ambavyo bado ni vijiji vimekuwa registered kama vijiji vina hali ya ukijiji. Kwa hiyo, vipato vya wananchi wetu vimekuwa vidogo, lakini bado wanalazimika kulipishwa shilingi 320,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo, ufanisi wa miradi hii ya REA, tija imekuwa ndogo sana kwa sababu wananchi hawana kipato cha kuweza kutosheleza kulipa gharama hizo. Kwa hiyo, naungana na Kamati yangu ya PIC kuiomba Serikali iweze kuboresha eneo hili. Kwa mfano Kilwa tu, pale Somanga Kaskazini na Somanga Kusini katika Kata ya Somanga ni vijiji ambavyo vipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, haviko hata ndani ya Mamlaka ya Miji Midogo, ni vijiji kabisa. Ukienda Hoteli Tatu the same wanalazimishwa walipe shilingi 320,000. Kwa hiyo ni watu wachache ambao wamechangamkia hii fursa ambayo kama wangeweza kuunganishiwa mapema wangeweza kupata manufaa makubwa kimaendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kwa hiyo, niombe Serikali yetu ya Awamu ya Sita iliangalie kwa haraka hilo jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kamati tumesema tumeipa Serikali time frame ya miezi sita, lakini kwa sababu tayari Serikali iliahidi kulishughulikia jambo hili tangu mwaka juzi mwaka jana na mwaka huu ninaona pengine inaweza ikalishughulikia jambo hili mapema zaidi. Kwa hiyo, kama itaweza hata ndani ya miezi mitatu hili jambo walishughulikie likamilike ili tunapokwenda kwenye mambo ya uchaguzi na mambo mengine mambo yawe yamekaa sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuzungumzia suala la Bodi ya Mkonge na ufanisi wake, Bodi yetu ya TSB Tanzania Sisal Board. Kwanza niishukuru Serikali na kuipongeza kwa juhudi kubwa ambazo imefanya ya kufufua zao hili. Nakumbuka Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya kazi kubwa sana kuanzia Mwaka wa Fedha 2019/2020 ya kufufua zao hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ya zao hili inaonesha mwaka 1964 Tanzania iliongoza duniani kwa kuzalisha zao la mkonge. Tulizalisha tani 230,000. Kwa hiyo, ndiyo tulikuwa wa kwanza duniani katika ranking za uzalishaji na zao la mkonge lilichangia 65% kutuingizia fedha za kigeni. Kwa hiyo, ndiyo zao pekee ambalo lilikuwa limeingiza fedha nyingi kuliko mazao mengine yoyote. Kwa hiyo, kwa umuhimu huu, naiomba Serikali iongeze juhudi za kuwekeza mtaji mkubwa, kuwekeza fedha nyingi katika zao hili ili taasisi hii au Bodi hii ya zao la mkonge Tanzania iweze kujiimarisha na kuweza kuzalisha ili turudi kule tulikotoka kwa sababu viwango vya uzalishaji hapa katikati vilishuka sana vikawa chini ya tani 50,000. Sasa hivi imepanda baada ya juhudi ambazo Serikali imefanywa, sasa hivi tunazalisha wastani wa tani 80,000 ingawa malengo kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ni tani 120,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili tufikie huko na turudi enzi zile za miaka ya 1960, tunahitaji kuiwezesha kifedha hii Bodi ya Mkonge Tanzania. Ninao ushauri au mapendekezo katika eneo hilo kwa sababu hili zao linahitajika sana na lina soko sana katika Nchi za China, Morocco, Saudi Arabia, Misri na nchi zaidi ya 26 hapa duniani. Kwa hiyo, naomba Serikali iongeze mtaji, iongeze fedha kwa Bodi ya Mkonge Tanzania ili hii Bodi iweze kutafuta mitambo, iweze kulima, iweze kununua mitambo ya corona na hatimaye kuzalisha zaidi na zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi pia, waweze kufikia hata yale maeneo ambayo yalikuwa na uzalishaji mkubwa. Kwa mfano, vijiji vinavyozunguka Mkoa wa Lindi wote, kuanzia Kilwa mpaka Lindi Vijijini, kule Kitumbikwela, mpaka kule Kikwetu, Somanga na vijiji vyote vya Mkoa wa Lindi vinalima sana mkonge lakini kutokana na mtaji kuwa mdogo, Bodi imeshindwa kuvifikia vijiji hivyo na hatimaye imeshindwa kuhamasisha na tumejikuta bado tuna mark time lile ongezeko la uzalishaji limekuwa dogo. Kwa hiyo naomba Serikali iangalie. Vilevile, iwaongezee fedha kwa ajili ya kuanzisha ile block farming ambao ndiyo utaratibu wa kisasa ambao unatumika maeneo mengi duniani na ambao sisi Tanzania tumeanza kuutumia katika mazao mbalimbali ili kuboresha uchumi wetu kupitia mazao hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika kwa kuboresha zao la mkonge, kwa kuipatia mahitaji hii bodi, kwa kuipatia mtaji basi tutasonga mbele na tutarudi katika enzi mpya za mafanikio na kuweza kukuza uchumi wetu kwa kasi kubwa na hatimaye kufikia malengo ambayo tumejiwekea katika Serikali yetu na hatimaye kupata maendeleo katika nyanja zote kiuchumi pamoja na kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika mjadala huu wa leo. Kwanza napenda nimpongeze CAG kwa kufanya kazi nzuri ya kukagua Halmashauri zetu katika ukaguzi maalum ambao ulifanyika mwezi Mei hadi Julai, mwaka 2021. Kwa hakika CAG ametufungua macho. Kama tafsiri halisi ilivyo, lile ni jicho letu sisi Wabunge na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla. Kwa hiyo, ameifanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyotangulia kuzungumza wazungumzaji wenzangu waliochangia hii taarifa ya LAAC. Kwa ujumla kuna madudu mengi sana yameonekana katika ule ukaguzi maalum uliofanyika mwaka 2021, lakini hatua hazijachukuliwa. Ukienda pale katika Halmashauri hizo nne ambazo zilifanyiwa ukaguzi maalum; Halmashauri ya Ubungo, Kigamboni, Ilemela pamoja na Iringa DC, kuna karibu Shilingi bilioni tisa ambazo zimevuja kutokana na miamala kufutwa kinyume cha utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, ukienda kwenye suala la ubadhirifu wa fedha za umma kutokana na matumizi ya fedha kabla ya kuzipeleka benki, yaani fedha mbichi, kuna shilingi milioni 858, Halmashauri nne tu.Kwa hiyo, kuna shida katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilicho kibaya zaidi, pale katika Halmashauri ya Ilemela ule mfumo sijui ukoje! Kwa sababu imefikia hatua watumishi waliohama wamekuwa na wale ambao wamestaafu wamekuwa na access ya kuingia kwenye mifumo. Pia hii inaonesha namna gani mifumo yetu haiko vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ombi langu nilikuwa naiomba Wizara yetu ya TAMISEMI inapokuja na mfumo mpya wa TAUSI, baada ya kuachana na ule wa LGRCIS, izingatie suala la security ya hii mifumo. Inaonesha mifumo yetu haiko madhubuti kwenye security. Tusije tukarudia makosa. Haya makosa yaliyojitokeza yawe fundisho kwetu ili tunapotengeneza ile database ya Mfumo wa TAUSI, basi iwe madhubuti makini katika ku-trace makosa mbalimbali ambayo yatafanyika ikiwemo haya ya watu ambao wamehama au kustaafu kuweza kuingia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ningeomba wizara ya TAMISEMI ifanye kazi kwa karibu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ningeiomba TAMISEMI ifanye kazi kwa karibu sana na hizo Halmashauri zetu, kuna wakati niliwahi kusema kwamba CAG anapofanya ukaguzi ni kama vile mvuvi ambaye anakuwa anavua kwa njia yile ya kokoro. Kwa hiyo, ndani ya zile hoja zinapotengenezwa unakuta kuna mapendekezo yanahitaji utekelezaji wa Wizara ya TAMISEMI nyingine Sekretariati za Mikoa, nyingine Halmashauri zenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hakuna muunganiko mzuri wa kujibu hizi hoja tutaendelea kupigwa kila siku na mwisho wa siku hizi hoja zitabaki zinaelea hazijibiki. Kwa hiyo, ninaiomba TAMISEMI kwanza ichukue hatua dhidi ya wale wote waliohusika na hizi changamoto, kwa sababu imeonekana tangu mwaka juzi ukaguzi ulivyofanyika na hizi taarifa zikawasilishwa Wizara ya TAMISEMI na kule kwenye Halmashauri zetu mwezi Septemba hatua madhubuti hazijachukuliwa kuwadhibiti hawa Watumishi ambao wamefanya huu ubadhirifu. Hii inaonesha kwamba ni kwa namna gani TAMISEMI imetengeneza gap kati yake na Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba TAMISEMI tumieni nafasi yenu kwa sababu hizi hoja ni mtambuka, zingine zinahitaji utekelezaji wa moja kwa moja na TAMISEMI, kama haya masuala ya kinidhamu chukueni hatua na mchukue hatua haraka. Mna-premises nyingi hapa Dodoma, mnaweza mkaziita zile Halmashauri husika, mkakaa nazo mkajadili kwa pamoja ili hoja ambayo inahusika na TAMISEMI utekelezaji wake unatakiwa utekelezwe na TAMISEMI kama uchukuaji wa hatua zile za kinidhamu, basi chukueni hatua haraka ili kudhibiti vitendo hivi vya ubadhirifu wa fedha za Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalia kila siku mapato ya Halmashauri ni madogo lakini udhibiti ukifanyika basi mapato yataongezeka. Security zikiongezeka kwenye mifumo yetu tutajikuta tayari mapato yetu yanaweza kulindwa na kuweza kutumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika. vilevile kumekuwa na changamoto kubwa kwenye manunuzi, imefika mahali kule kwa mfano kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, hospitali inajengwa vifaa vinapokelewa, vinaonekena vimezidi hata idadi ya vile vifaa vilivyokuwa vinatakiwa. Sasa hii inatokeaje? Ni ukosefu wa kuzingatia Kanuni na Sheria ya Manunuzi. Kwa hiyo, ninaiomba TAMISEMI pamoja na Sekretariati zichukue majukumu yake ya kuzilea hizi Halmashauri pia kuchukua hatua pale inapoonekana kwamba kuna shida.
Mheshimiwa Naibu Spika, pesa nyingi inakwenda kwenye manunuzi, matumizi ya fedha za Serikali sehemu kubwa inakwenda kwenye eneo la manunuzi, ndiyo maana nafikiri huyu CAG amezingatia sana hayo maeneo hayo muhimu, kwa hiyo niombe Serikali isimamie vizuri hizi Halmashauri ili hatua zichukuliwe kwenye maeneo yote ambayo yanaonekana taratibu hazifuatwi lakini kuna ukiukwaji mkubwa wa taratibu za mapato na mambo mengine ambayo yanafanyika kule kwenye Halmashauri ili kuondoa haya madudu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya nasema naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii muhimu ya kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo ya Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2025/2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nitangulie kuishukuru Serikali na kuipongeza kwa kutuletea mpango mzuri na mapendekezo mazuri kupitia kwa Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Mipango na Uwekezaji. Huyu ni rafiki yangu na schoolmate wangu wa high school (Pugu High School). Pia, taarifa nzuri imesomwa na mapendekezo kutoka kwa rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu, Waziri wa Fedha. Kwa hiyo, tunapongeza kwa hatua hii ambayo Serikali imetuongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ningependa nichangie katika maeneo matatu. Eneo la kwanza ni katika sekta ya utalii; eneo la pili ni miundombinu ya barabara za vijijini; na eneo la tatu nitakwenda kwenye michezo kwa sababu mimi ni mwanamichezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepiga hatua kubwa sana katika sekta ya utalii kutokana na filamu ambayo iliongozwa na Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan; na katika miaka ya karibuni tumeshuhudia watalii wakiongezeka na hivyo fedha za kigeni nyingi zikapatikana hadi kufikia 25% ya fedha zote ambazo zimekusanywa katika mwaka 2022/2023 kutokana na sekta hii ya utalii. Watalii wameongezeka hadi kufikia 3,784,254 kwa mwaka 2023/2024. Sasa, kwa mujibu wa mapendekezo yaliyotolewa tuna lengo la kufikisha watalii 5,000,000 ifikapo Mwaka wa Fedha 2025/2026. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kwamba tumekuwa na changamoto nyingi katika sekta hii. Ndiyo maana inatufanya sasa pamoja na kwamba sisi Taifa letu kuwa ni la pili kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii bado hatupo hata kwenye 10 bora katika kuingiza fedha nyingi za utalii hapa duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nipende kwanza niainishe changamoto ambazo zinakabili sekta hii, ambazo ni ubovu na ukosefu wa miundombinu ya kuweza kuvifikia vivutio hivi, hasa kwenye hifadhi zetu pamoja na mapori yetu ya akiba. Pia, kuna bajeti ndogo ya kutangaza vivutio hivi ndani na nje ya nchi yetu; vilevile kuna changamoto katika ubunifu wa vyanzo vipya hata vile ambavyo vinaonekana kabisa bado hatujaweza kuviingiza katika mtiririko wetu kuvifanya viweze kujulikana, lakini pia viweze kutumika katika kutuingizia fedha za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ya huduma ya utafiti. Mara nyingi tumekuwa tukitegemea watafiti kutoka nje ya nchi pale wanapoguswa na mambo mbalimbali na wakati mwingine taasisi ambazo zinahusika na shughuli za utafiti kama Tanzania Board of Tourism ambayo hata hivyo imekuwa ikipewa mtaji mdogo sana kwa ajili ya kufanya kazi hii na wakati mwingine hata wataalam wamekuwa wakikosekana. Mfano, halisi ni kule katika ule mji uliozama wa Rhapta ambao ulishamiri kuanzia Karne ya Saba kabla Kristo mpaka Karne ya Nane baada ya Kristo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kufuatilia nimegundua kwamba kuna Profesa mmoja anafanya kazi kule ya kuendesha utafiti, lakini anadhaminiwa na taasisi mbalimbali za nje. Sisi kama Watanzania hatuwekezi vya kutosha; lakini hata wataalam anaowatumia walio wengi wanatoka nje ya nchi. Ile kazi, kwa sababu ule mji ulizama na ulitafutwa kwa miaka mingi watu wa Ulaya waliandika maandiko mengi kuutafuta ule mji. Unakuta wale diving archeologists wengi wanatoka nje ya nchi, lakini sisi hatuna hata mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaiomba Serikali iliangalie katika mpango huu itenge bajeti kwa ajili ya utafiti, lakini pia kwa ajili ya kuwaendeleza wataalam hasa katika zile fani ambazo hatuna watalaam, lakini ambazo ni za muhimu ambazo zitatuletea hawa watalii. Kama watu wameandika maandiko mengi kuanzia karne iliyopita hadi karne hii kule Ulaya ni wazi kabisa kugundulika kwa Rhapta kuanzia miaka hii ya 2000 ni kwamba kutaleta watalii wengi, kama ambavyo watu walikuwa na hamu ya kujua hii Rhapta ilipotelea wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusema kwamba kuna kumbukizi za kihistoria na kiutamaduni zilizopo Kilwa Kisiwani. Kwa hakika Tanzania tumejaliwa kwa kiasi kikubwa sana kuwa na kumbukizi za utamaduni na kihistoria (historical and cultural tourism), lakini nazo bado hazijaendelezwa kwa kiasi cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali yetu kwa kuziona kumbukizi zilizopo Kilwa Kisiwani, vilevile imeziona kumbukizi kama zile zilizopo katika Milima ya Umatumbi, Kumbukizi za Majimaji ambazo zimepata GN mwezi Machi mwaka huu, pia mapango kupitia GN namba 163 na 166, likiwemo pango refu kuliko yote. Serikali imewekeza kiasi cha kutosha na inajenga jumba la makumbusho kule na pia inakwenda kutengeneza ngazi za kushukia kwenye lile pango kubwa kuliko yote katika ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwenye Dola ya Kilwa katika Karne ya 11 hadi 15 ambayo ilishuhudia maendeleo makubwa na hata kuwavutia watalii tangu Karne ya 13. Mtalii wa kwanza maarufu kuja Kilwa Kisiwani alikuwa ni Ibn Battuta katika mwaka 1331 na alishuhudia mambo mengi ya kistaarabu yakiwa yamefanyika katika Dola ya Kilwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na fedha zinatengenezwa Kilwa, ambayo ndiyo sehemu ya kwanza kutengenezwa fedha za sarafu ambazo tunaziona leo. Pia, kulikuwa na msikiti mkubwa, wanaita Msikiti Mkuu wa Karne ya 11. Ule msikiti ilikuwa watu kutoka Rwanda, Burundi na Kongo wasiokuwa na uwezo wa kwenda Macca na Madina walikuwa wanakuja kuhiji pale. Tunazishukuru Serikali ya ufaransa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania waliweza kuufukua kwa sababu ulikuwa unaelekea kuzama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kule Kilwa pembezoni ya ule Msikiti wa Ijumaa au Msikiti Mkuu kuna sehemu ambayo Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikwenda kupata baraka kule wakati anapigania uhuru mwaka 1958; na alifikia kwenye nyumba inayojulikana kama nyumba ya buluu (blue house). Ile nyumba ipo hadi leo. Alikuwepo mzee mmoja ambaye alishikilia karabai usiku ule wakati wale wazee wakiwa wanampa baraka yule mzee akiwa ameongozana na mzee wetu mwingine shujaa Mzee Kawawa, mama Bibi Titi Mohamed pamoja na Mzee Oscar Kambona na wengine kama akina Lau Nagwanda Sijaona. Ile nyumba imetelekezwa mpaka leo, haijapewa uzito unaostahili Kilwa Kisiwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna nyumba pia ambayo katika kumbukizi nilimsikia Shekhe Mkuu wa BAKWATA na Mufti wa Tanzania Shekhe Abubakar Zubeir Ally Mbwana katika mazungumzo yake wakati fulani akielezea historia ya Uislamu katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aliitaja Kilwa kama ndiyo sehemu ya kwanza ambayo watu wake ama Waislam wake wa kwanza kwenda kuhiji Madina. Walikwenda kundi la kwanza katika Karne ya Sita na walimkuta Mtume Muhammad (Swallallahu Alayh Wasallam) akiwa hai. Wale Waislamu wa Kilwa walipoona kwamba Waislamu wenzao hawakurudi, kundi la pili ilikwenda tena katika Karne ya Sita na lilikuta Mtume Muhammad akiwa amekwishafariki wiki mbili zilizotanguliwa. Hii ni simulizi ya kweli ambayo Shekhe Mkuu wa BAKWATA aliye hai leo alisimulia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo tunaona kwamba wale Waislamu walipotoka kule walirudi na Quran ya kwanza Afrika Mashariki; kuna nyumba pale ipo ambayo Quran ya kwanza ilifikia, ni pale, siyo sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna sehemu inaitwa Nguruni, sehemu ambayo tunashukia ukitoka huku upande wa Bara ya Kilwa Masoko kuna sehemu ambayo kuna gati ya kushukia. Pale ndiyo fedha ya Kilwa ilikuwa inatengenezwa, lakini hakuna kumbukumbu zozote katika maeneo hayo muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali iangalie na ikiwezekana iwekeze katika museum inayohusika na utamaduni wa watu wa Kilwa ambao unaenda sambamba na utamaduni wa dini ya kiislam. Haya mambo ya kuwa na museum hizi ambazo zinaendana na utamaduni wa kidini zipo. Ukienda Ethiopia unazikuta, ukienda Ephesus unazikuta, ukienda Makka na Madina unazikuta, ukienda Jerusalemu unazikuta, ukienda Thessaloniki unazikuta na ukienda Galathia unazikuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo zinaingiza fedha nyingi kwa wale wenzetu. Kwa hiyo hata sisi tukiwekeza katika eneo hili, basi fedha nyingi itaingia kupitia utalii wa kihistoria na kiutamaduni. Suala la pili ni kuhusiana na suala la michezo. Mheshimiwa Waziri…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa muda wako umekwisha tafadhali.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika mbili.
MWENYEKITI: Naomba hitimisha tuna changamoto ya muda.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake ya bajeti alihitimisha kwa kusema kwamba atafanya jitihada za kuweka VAR katika mashindano ya ligi yetu kuu hapa nchini Tanzania. Tumeshuhudia mambo mengi ya hovyo yakifanywa na waamuzi wetu katika ligi kuu ya Tanzania bara. Mfano mzuri ni mechi ya tarehe 19 mwezi uliopita ulishuhudia mwenyewe Mheshimiwa Waziri, lakini tunamshukuru Waziri…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda umekwisha tafadhali.
MHE. FRANSIC K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hoja mbalimbali katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa siku ya leo ningependa kwa kuanzia nijikite kwenye ukurasa wa 32 na 33 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Kipengele cha 34 kinachohusu uthibiti ubora. Kwa ujumla wathibiti ubora ni wataalamu wetu muhimu sana katika kutuboreshea elimu yetu, kwa sababu wamekuwa wakisimamia Sera ya Elimu kwa shule zetu za msingi, sekondari, vyuo pamoja na shule za awali; pia wamekuwa wakitoa ushauri mzuri kwa wataalamu wetu kama walimu, wakufunzi pamoja na wadau wengine; vile vile wamesimamia vizuri ufundishaji na ufundishwaji unaozingatia mtaala wa elimu uliopo; vilevile wamefuatilia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya elimu unaozingatia viwango vilivyowekwa. Hata hivyo nasema, kwa kiasi kikubwa hawa wathibiti ubora wamesahaulikana sijui ni kwa nini? Labda kwa sababu ya nature ya kazi yao au sababu ni ipi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri miaka saba iliyopita; vitu vingi wanakuja kuomba; vifaa vingi vya kutendea kazi wanakuja kuviomba, kama vile vyombo vya usafiri, ofisi; wanaomba kwa Wakurugenzi kama siyo kwa ma-DC. Kwa hiyo, naomba Serikali ijaribu kuona kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia namna ambavyo wataboresha kwa kuwapatia vitendea kazi sawia vinavyoweza kuboresha shughuli zao kutokana umuhimu wa shughuli zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mwaka 2014 Serikali ilitoa waraka ulioitwa Waraka Na. 3 wa mwaka 2014. Waraka huu ulihusiana na maslahi ya mishahara, posho za madaraka kwa watumishi wa sekta ya elimu, ulitolewa na Wizara ya Utumishi kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Utumishi. Ulieleza kinagaubaga namna wale viongozi wetu wa ngazi ya wilaya wanaohusika na masuala ya uthibiti ubora watakavyolipwa mishahara yao. Ulieleza kwa uwazi kwamba wale Wasimamizi wa Ofisi za Wilaya kwenye masuala ya uthibiti ubora watalipwa mshahara wa kiwango cha LSS E1 sawasawa na Maafisa Elimu wa Wilaya, Maafisa Elimu wa Shule za Msingi wa Wilaya na wa Sekondari. Ila wale wa kanda mishahara yao kwa mujibu wa ule waraka ilionesha kwamba, wangelipwa mishahara sawasawa na wale Maafisa Elimu wa Mikoa ambayo ni LSS E3.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha ajabu ni kwamba, hawa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya, mishahara yao ilipanda mara moja kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016, lakini wale Maafisa Uthibiti Ubora wa Wilaya na Kanda mishahara yao haijapanda mpaka leo.
Kwa hiyo, naomba Serikali iweze kuwapandishia mishahara hawa Maafisa wa Wilaya na ikiwezekana wawalipe na arrears zao ili waweze kulitumikia Taifa letu ipasavyo. Bila assurance kwenye masuala ya elimu tutakuwa tunafanya kazi bure kwa sababu uthibiti utakuwa haufanyiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, masuala mengine ninayopenda kuchangia leo ni changamoto ambazo zimebaki baada ya kuwa tumepata miundombinu ya madarasa, kumekuwa na upungufu bado wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi kwenye shule zetu za sekondari. Naomba hili Serilikali ilifanyie kazi ili tupunguze idadi ya upungufu huu uliopo na hatimaye tuweze kuboresha elimu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa shule shikizi, kama nilivyosema hapo mwanzo, kwenye jimbo langu peke yake, madarasa 23 yamejengwa, lakini watoto bado wanasoma shule za mbali licha ya madarasa kuwepo, kwa sababu hakuna walimu wa kufundisha kwenye zile shule. Kuna baadhi ya shule katika jimbo langu, kwa mfano kule Tipo Mkongo, Kata ya Kandawale, pale Kipatimu, kuna sehemu wanaita Ngingama, kuna sehemu kule Mbelenje, Kibata, lakini kuna sehemu wanaita Namadhugutungu; ukitoka shule mama kwenda shule ile ambayo imejengwa yenye madarasa ya kutosha, lakini walimu hawapo, wanalazimika kutembea umbali mrefu, tena ni watoto wadogo wenye umri mdogo sana. Kwa hiyo, naomba Serikali iliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali iangalie katika eneo la tundu za vyoo katika shule, ziko chache; meza na viti katika shule zetu za sekondari ni pungufu, lakini pia watoto wetu wa shule za sekondari wanatembea umbali mrefu sana. Wanatembea kati ya kilometa 12 kwenda na kurudi hadi kilometa 18 kwenda katika shule ambazo wanasoma. Kwa hiyo, katika eneo hili naomba kuishauri Serikali iwekeze pia katika eneo la mabweni, tuwe na mabweni ya kutosha ili watoto ambao wanatoka mbali, basi waweze kukaa shuleni wasome pale, walale pale, ili waweze kukaa katika mazingira mazuri ambayo yanaendana na taaluma zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye maslahi ya walimu; miaka ya 1990 Serikali ilifuta kitu kinaitwa Teaching Allowance. Hili ni jambo ambalo siyo zuri sana kwa upande wangu ninavyoliona, kwa sababu walimu wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kutia nuru kwenye vichwa vya watoto wetu kwa maana ya kuwafundisha na wana kazi nyingi nje ya muda wa kawaida wa masomo.
Mheshimiwa Naibu Spika, walimu wanatakiwa kuandaa lesson notice, walimu wanatakiwa kuandaa lesson plan, walimu wanatakiwa kuandaa scheme of work, walimu wanatakiwa kuandaa teaching aids na mambo mengine mengi ambayo wanayaandaa nje ya muda wa kawaida mpaka nyumbani wanapofika, wanakuwa wanaandaa vitu kama hivyo kwa ajili ya kuwezesha watoto wetu waweze kusoma vizuri, lakini hii allowance iliondolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inafanana na ile ya On- Call Allowances ambayo inatolewa kwa watumishi wa afya ambayo mpaka leo haijafutwa, lakini pia wapo watumishi wa kawaida wanalipwa Extra Duty Allowances. Kwa nini walimu tu peke yao ndio wakose malipo ya ziada, tena kwa kazi halali ambayo wanaitumikia nchi hii? Kwa hiyo, nilikuwa naomba Wizara ilitafakari hili jambo kwa kina ili kuongeza morali ya walimu katika kufundisha, walipwe Teaching Allowance. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna Maafisa Elimu wa Kata. Kwa bahati nzuri Serikali yetu ya Awamu ya Tano mwaka 2016 iliwakabidhi pikipiki watumishi, hawa Maafisa Elimu Kata. Zile pikipiki kwa sasa zimechoka sana. Naomba Serikali ione uwezekano wa kuwapa pikipiki upya kwa sababu ni miaka zaidi ya mitano imepita wakiwa na hizo pikipiki. Ninaamini kwamba nafasi hizi za Maafisa Elimu Kata ni za muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Bajeti ya Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anachapa kazi katika kuiendeleza nchi yetu ikiwemo katika Sekta hii ya Maji. lakini pili nawapongeza pia Mheshimiwa Waziri rafiki yangu Mheshimiwa Aweso pamoja na dada yangu Maryprisca kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Wizara hii na kuhakikisha kwamba wanaisimamia vizuri miradi ambayo inatekelezwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi binafsi katika Jimbo langu nimenufaika sana. Tangu nimeingia madarakani miezi 18 iliyopita tayari miradi zaidi ya 11 imekuwa ikitekelezwa yenye thamani ya jumla ya Shilingi Bilioni 2.18. Kwa hiyo naipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ndani ya jimbo langu na nchi nzima kwa ujumla. Kwa mfano kuna vijiji vya njia nne tayari kuna mradi umeshakamilika pale. Somanga kuna mradi umekamilika, Mtumbei Mpopera kuna mradi umekamilika, Kipatimu kuna mradi unaendelea kutekelezwa. Vilevile kuna ukarabati wa visima vifupi unaendelea kufanyika katika vijiji mbalimbali. Kipindimbi kuna mradi wenye thamani ya Shilingi Milioni 497 wa UVIKO-19. Lakini pia kuna Vijiji vya Malendego, Chumo, Chapita, Kinjumbi kuna miradi inaendelea kutekelezwa iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna uchimbaji wa visima unaendelea kufanyika katika Vijiji vya Mitole, Zinga Kibaoni Namayuni pamoja na Kisima Mkika. Pia nina furaha kubwa kusikia katika mpango wa bajeti wa mwaka ujao katika Kitongoji cha Nasaya, Kijiji cha Mtekimwaga pamoja na Kijiji cha Miteja, Kitongoji cha Masaninga Serikali imepanga kuchimba visima virefu ili kuweza kuwahudumia wananchi waweze kupata huduma ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na ufanisi huu uliopatikana bado kuna baadhi ya maeneo takribani vijiji visivyopungua 15 vina changamoto kubwa sana ya maji. Wamekuwa wakitumia majitope wakati wa masika, wakati wa kiangazi wanapata tabu sana kusafiri mbali kutumia visima vya asili kupata maji; navyo ni Vijiji vya Nandete, Nandembo, Namatewa, Ngarambi kwa Kinjeketile Ngwale huko, Nambondo, Bugo, Kinywanyu, Namakoro, Ngorongoro, Lyombanga, Somanga Simu, Handa, Mtende pamoja na Mwegei. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ulizungumza hapa, kuna kauli zilitolewa na baadhi ya Wabunge jana na leo zinagongana kidogo. Lakini mimi niseme katika baadhi ya maeneo yetu ni kweli kuna hali fulani yakutoeleweka. Kwa sababu mgao wa fedha katika baadhi ya Majimbo au Wilaya umekuwa ni mdogo sana. Kwa mfano, tarehe 14 mwezi Machi mwaka 2022 mimi pamoja na Kamati yetu ya PAC tulitembelea katika mradi mmoja wa maji kule Manyara katika Kijiji cha Hydom kuna mradi pale wa bilioni 12 umewekezwa lakini unahudumia kata tatu tu.
Mheshimiwa Spika, lakini katika jimbo langu miradi yote iliyowekezwa pamoja na UVIKO-19 ina gharimu shilingi bilioni 2.18 tu, haifiki hata robo ya mradi mmoja tu ule ambao umewekezwa kule Manyara. Kwa hiyo kwa kweli jambo hili ni lazima Wizara ilifanyie kazi ili kuhakikisha hii keki inayopatikana iweze kugawanywa vizuri.
Mheshimiwa Spika, nimesema hapa kuna vijiji 15 bado vina shida ya maji. Kwa hiyo tukiigawa vizuri ile keki ni wazi kabisa kwamba mambo yatakwenda vizuri. Na mimi katika kuzingatia hilo ningependa kusema kwamba nimefuatilia kuhusu utekelezaji wa maji kutoka Mto Rufiji kwa karibu sana kupitia DAWASA na RUWASA Wilaya ya Kilwa. Kule DAWASA tayari wameshapata designer wa mradi wa maji kutoka Mto Rufiji. Tayari walitanga zabuni wameshapata, na tayari wako katika hatua mbalimbali za kuelekea kutekeleza ule mradi ambapo wataweka chujio pale katika Kijiji cha Mloka kule Rufiji.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa upande wa Kilwa wao walikuwa nyuma kidogo tarehe 19 mwezi huu wanatarajia kufungua zabuni ya kumpata designer, yule Mhandisi mshauri kwa ajili ya ku-design mradi wa maji kutoka Mto Rufiji.
Kwa hiyo ombi langu na ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba hii miradi miwili iunganishwe. Inawezekana kwenye ku-design mradi ikawa wametofautina, lakini kwenye utekelezaji wa mradi ningeomba basi iuanganishwe ili apatikane mkandarasi mmoja ambaye atajenga huu mradi wa maji kutokea kule Mloka Rufiji, bomba basi kama litapita Ikwiriri au litakwenda kule Kibiti, likifika pale linagawanyika lile lingine linakwenda Kusini kuanzia wilaya ya Mheshimiwa Mchengerwa pale Rufiji inaendelea mpaka wilaya yangu linakwenda mpaka kwa mama Kikwete kule Mchinga Liwale, Nachingwea, Newala na maeneo mengine yote ya kusini. Lakini pia na hawa wa Kaskazini kwa maana ya Mkoa wa Pwani, Bungu Mkuranga mpaka Dar es salaam nao waweze kupata maji mengi yanayotokana na maji ya Mto Rufiji.
Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna hii miradi ambayo inatekelezwa na Mfuko wa Maji, imekuwa na tatizo sana kwenye ulipaji. Pale mimi ninao ule mradi wa Kinjumbi pale ambao una gharimu shilingi milioni 326 za Serikali Mkandarasi hivi sasa ana miezi miwili ali-rise claim lakini mpaka leo haulipwi. Sababu ukifuatilia unaambiwa shida ni kwamba mlolongo mrefu kwenye hii miradi ambayo inatekelezwa na mfuko wa maji.
Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali ijaribu kuona namna ya kupunguza mlolongo ili tusije tukaangukia kwenye changamoto ya kulipa riba ikaigharimu zaidi Serikali.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nasema nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuzungumza jioni ya leo. Naunga mkono hoja kwa asilimia 100.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Afya. Kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kuliletea maendeleo Taifa letu la Tanzania ikiwemo kwenye sekta hii ya afya.
Mheshimiwa Spika, pili, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya, dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kazi nzuri. Niseme tu kwamba, Mheshimiwa Waziri alipokuwa ametoka kwenye Wizara hii kwa kweli tulimkumbuka sana, amerudi mambo mengi yanakwenda vizuri kama yalivyokuwa wakati ule alipokuwepo, wakati ule wa mwanzo. Pia nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, rafiki yangu Mheshimiwa Mollel kwa kazi nzuri na namna ambavyo anachapa kazi katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo katika kupongeza katika kuthibitisha mambo yanavyokwenda vizuri, napenda niseme katika Wilaya yetu ya Kilwa yenye Kata 23 tumepata fedha nyingi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita. Jumla ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.5 zimewekezwa kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa wodi maalum Sh.300,000,000 katika Hospitali ya Kilwa Kivinje ya Kinyonga. Pia tumepewa fedha Sh.500,000,000 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya pale Mandawa na vile vile tumepewa fedha Sh.250,000,000 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya pale Kipindimbi, Kata ya Njinjo na pia tumepewa zaidi ya Sh.400,000,000 kwa ajili ya umaliziaji wa Zahanati katika Vijiji nane vya Miumbu, Mtepela, Nakindu, Pungutini, Kisongo Namakongoro, Kiswele pamoja na Songomnara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali pia ilifanya kazi nzuri na wadau wa maendeleo wa PAN AFRICA na wametuwezesha kushirikiana nao na kujenga Vituo vitatu vya Afya, Chumo, Somanga pamoja na Songosongo na pia Zahanati moja imejengwa kwa kushirikiana na hao wadau wa PAN AFRICA pale katika Kijiji cha Nahama na Mayunu. Pamoja na mafanikio hayo, bado kumekuwa na changamoto zinaendelea. Changamoto ya kwanza ni kutokuwepo kwa ambulance, ambulances zetu nyingi zililetwa zaidi ya miaka 10 iliyopita katika Wilaya ya Kilwa na hivyo sasa hivi haziwezi kufanya kazi ya kuweza kubeba wagonjwa na kuwaharakisha kwenda hospitali.
Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali imekuja na mpango wa kuleta katika kila Halmashauri angalau ambulance moja, lakini sisi Kilwa tuna majimbo mawili kwa hiyo itapendeza kama Mheshimiwa Waziri atatuletea ambulance mbili, moja ikaenda Kilwa Kaskazini na nyingine ikaenda Kilwa Kusini. Vile vile tuna changamoto ya vifaa tiba, kutokana na ujenzi wa vituo vingi vya Afya na Zahanati vifaa tiba vimekuwa adimu au vichache. kwa hiyo, tungeomba Serikali itusaidie vifaatiba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna changamoto kubwa ya watalaam au watumishi katika Wilaya yetu ya Kilwa tunauhitaji wa watumishi 1,315 waliopo ni 357 tu. Kwa hiyo, tuna uhaba wa watumishi 958 sawa na asilimia 76 ya uhitaji. Kwa hiyo, ningeshauri Serikali kupitia zile ajira ambazo zimetangazwa hivi karibuni basi watupunguzie huu uhaba ili shughuli ziweze kwenda tiba iweze kutolewa kama ambavyo inatakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hospitali yetu ya Wilaya ya Kinyonga pale Kilwa Kivinje ni ya zamani sana imejengwa tangu wakati wa ukoloni wa Waingereza imechakaa sana inahitaji ukarabati mkubwa ningeomba Serikali itenge fedha kwa ajili ya ukarabati wa ile hospitali ya Wilaya ya Kilwa ya Kinyonga pale Kivinje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna shida katika baadhi ya vijiji vyetu kuna vijiji kama Tisa Jimbo langu peke yake bado havina zahanati. Kwa hiyo, wanalazimika wananchi kutembea umbali mrefu kwenda kusaka tiba katika zahanati za vijiji vya jirani au Vituo vya Afya ambavyo vipo mbali. Kuna kijiji cha Kinywanyu, Ingerito, Namayuni, Namakoro, Ngorongoro, Bugo, Nambondo na Naipuli havina zahanati, pia kati ya Kata 23 za Wilaya ya Kilwa tuna vituo vya afya Saba tu, Kata 16 hazina Vituo vya Afya. Kwa hiyo, ningeshauri Serikali itenge fedha za kutosha ili kupunguza uhaba wa Vituo vya Afya na Zahanati katika Wilaya yetu ya Kilwa ili wananchi waweze kupata huduma katika maeneo ya jirani huduma ambayo ipo bora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nasema naishukuru Wizara, narudia kusema naishukuru Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuzungumza.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika bajeti hii ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kwanza, napende kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara yetu hii kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika kipindi cha siku hizi za karibuni, kwa kuzingatia utawala bora katika nchi yetu, hasa kwenye ile misingi ya utawala bora ambayo ni haki na usawa, ukweli na uwazi, ushirikishwaji, uhuru na misingi ya kidemokrasia, kufuata sheria pamoja na kusimamia maslahi ya wengi hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuanza kuchangia kwenye suala la mafunzo kwa Maafisa Utumishi. Maafisa Utumishi wetu wengi wamekariri Standing Orders au zile Kanuni za Utumishi wa Umma. Wengi ni mambumbumbu katika Sheria Mama katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta Maafisa Utumishi wengi wanashindwa ku-cope na mazingira na wakati mwingine wanajikuta wanakosea na kuwanyima baadhi ya watumishi wetu haki zao kwa sababu wamekariri tu mambo fulani ambayo yapo kwenye Kanuni za Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimpelekea Afisa Utumishi kwenye sheria mama, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, unakuta hajui. Kwa hiyo, napenda kusisitiza, naiomba Serikali iwekeze kwenye kutoa mafunzo kwa hawa Maafisa Utumishi ili waweze kutenda haki kwa watumishi wetu ambao wanatumikia Taifa letu katika ngazi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika hili, unakuta kuna baadhi ya Halmashauri, Mkurugenzi anajiamulia tu. Unaweza ukakuta Mkurugenzi kila baada ya miezi sita anahamisha watendaji kata bila ya kuzingatia taratibu na haki zao ambazo wanazostahili. Unakuta Mtendaji Kata leo amehamishiwa kata hii, baada ya miezi sita anahamishiwa kata nyingine, halipwi disturbance allowance, halipwi haki yake yoyote. Shida ni kwamba kanuni na sheria na taratibu, hawa Maafisa Utumishi wanashindwa kuwaelekeza hawa Maafisa Masuuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la upungufu wa watumishi. Bado kumekuwa na upungufu mkubwa wa watumishi, japokuwa Serikali imejitahidi kwa miaka ya hivi karibuni, na hivi karibuni wametangaza hizo ajira 21,200, lakini bado tatizo ni kubwa. Tatizo limekuwa kubwa zaidi hasa kwa Halmashauri zetu za Wilaya. Watumishi wengi wakiajiriwa, unakuta wakishapata tu uthibitisho kazini, wanahama kutoka kwenye Halmashauri zetu za Wilaya zenye vijiji vingi, kwenda Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali katika eneo hili ijitahidi kudhibiti taratibu za uhamisho ili wakishaajiriwa waendelee kubaki kule kwenye vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda kwenye zahanati na shule, utakuta walimu ni wachache; manesi, utakuta ni mmoja tu, na ndio huyo huyo, hakuna Clinical Officer, hakuna daktari. Kwa hiyo, ni shida juu ya shida. Pamoja na kwamba tumeongeza miundombinu ya madarasa, maabara na zahanati, lakini unakuta zahanati hizo zimebaki zikiwa hazina watumishi wa kutosha, na mwisho wa siku wananchi wanakosa huduma muhimu katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme, Mbunge mwenzangu, Mheshimiwa Ally Kassinge, Mbunge wa Kilwa amezungumza hapa kwa uchungu kabisa na kwa hisia kubwa. Naye alikuwa Mwalimu siku zilizopita. Anajua vizuri katika masuala ya ualimu. Upungufu wa Walimu umesababisha hasa kwenye masomo ya sayansi, walimu wamefikia hatua wanapangiwa vipindi kati ya 35 mpaka 64 kule kwenye Halmashauri yetu ya Wilaya ya Kilwa, lakini standard ni vipindi 24 mpaka 30. Kwa hiyo, unaweza ukaona hali halisi ilivyo. Kwa hiyo, Walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu na mwisho wa siku maisha yao yamekuwa magumu vile vile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna madai mbalimbali ya walimu. Yamekuwa aidha yakichelewa kulipwa na wakati mwingine hayalipwi kabisa na wanapigwa danadana tu. Unakuta madai ya tangu mwaka 2015 mpaka leo bado hayajalipwa. Hata yakilipwa, mtu anadai Shilingi 500,000/= analipwa Sh. 180,000/=, anaambiwa hii utalipwa baadaye na ndiyo imetoka hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba kwa watumishi nayo ni changamoto kubwa. Hii imelazimu sasa watumishi wengi wanaolazimika kukaa maeneo ya mbali yenye nyumba zinazostahili ambazo ziko mbali na vituo vyao vya ajira. Kwa hiyo, naomba Serikali iliangalie jambo hilo ili kuboresha hasa kwenye sSekta hii ya elimu na sekta ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuzungumzia suala la wathibiti ubora. Mwaka 2022 nilizungumza juu ya changamoto iliyopo kwa watumishi hawa muhimu wathibiti ubora, wamekuwa wakifanya kazi kubwa katika mazingira magumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwaka 2014 nilishawahi kusema, ulitoka waraka ambao unahusu viwango vya mishahara pamoja na viwango vya posho za madaraka kwa viongozi wa elimu, lakini yale mabadiliko ambayo yalitolewa kulingana na waraka ule wa mwaka 2014, yameweza kutumika tu kwa wale ambao wako kwenye kada ya elimu yenyewe; walimu wakuu, waratibu wa elimu, Maafisa Elimu wa Wilaya na Mikoa, lakini hawa Wathibiti Ubora wa Wilaya na wa Kanda hawajaweza kubadilishiwa. Pamoja na kuzungumza mwaka 2022 mpaka leo hii, hawajabadilishiwa miundo yao, hawajabadilishiwa posho zao, hawalipwi stahiki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali kwamba iwalipe stahiki zao pamoja na arrears zake ili waweze kufanya kazi kwa bidii na kwa umahiri ili tuweze
kupata elimu iliyo bora. Kwa sababu unaweza ukafundisha darasani, lakini kama hakuna assurance kwenye elimu, ni kazi bure. Utakuta hiyo elimu haifuatiliwi, kama kuna uzembe haufatiliwi, au kuna kulegalega katika kufuatilia mambo kama hayo. Kwa hiyo, kwa ujumla napenda hilo nalo lizangatiwe ili basi hawa wathibiti ubora nao waweze kusaidiwa na kuweza kupata haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la wastaafu. Wenzangu wamezungumza sana kwa kirefu, nami labda nizungumze kwa kifupi tu. Wastaafu wamekuwa wakichelewa sana kupewa haki zao. Naomba hao wazee wetu wapewe kipaumbele. Katika mwaka wa fedha unaokuja watengewe bajeti inayotosha kulipa haki zao za mizigo na haki nyingine ili hatimaye pale wanapostaafu, walipwe mara moja na waweze kwenda kurudi katika maeneo yao ambayo wanatokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuipongeza Serikali yetu ya awamu ya sita kwa kazi kubwa ambayo imekuwa ikiifanya katika kuhakikisha kwamba inamtua mama ndoo kichwani. Pili napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri rafiki yangu bwana Aweso pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya. Nakumbuka wamepita hadi kwenye jimbo langu mara kadhaa kwa ajili ya kuhimiza na kuisimamia miradi ya maendeleo ya sekta hii ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningependa kuanza kuchangia kwa kupongeza zaidi Serikali kwa sababu ndani ya miaka mitatu iliyopita imewekeza zaidi ya shilingi bilioni tano katika Wilaya yetu ya Kilwa yenye vijiji tisini, na tayari miradi katika vijiji vinne tayari imekamilika; maji yanamwagika katika Kijiji cha Chapita, Chumo, Likawage pamoja na Somanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ipo miradi ambayo ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji ikiwemo uchimbaji wa visima pamoja na kuweka mtandao wa mabomba katika Vijiji vya Marendego, Nasaya, Masaninga, Kisima Mkika Zinga Kibaoni, Matandu, Hoteli Tatu, Mbwemkulu, Nainokwe, Kipimbimbi, Kilwa Masoko, Kikole, Nakiu, Kilwa Kisiwani, Hoteli Tatu pamoja Nakinjumbi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado kuna maeneo ya vijiji 32 kati ya vijiji 90 bado vina changamoto kubwa ya maji na bado havijafikiwa na mtandao wa maji wa RUWASA. Nitavitaja baadhi ya vijiji; kipo kijji cha sehemu fulani za baadhi ya vitongoji vya Zinga Kibaoni. Pia vipo vijiji Vya Ngalambi; Lienga Kijiji cha Namatewa; Mwengei; Pungutini pamoja na Nandete, Nandembo pamoja na vijiji vingine, kama nilivyosema vijiji 32 kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa hapa napitia ukurasa wa 55, 56 kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, pamoja na majedwali ya miradi ya maendeleo ambayo inakwenda kutekelezwa katika mwaka huu ujao. Nimeona pale katika ukursa huu wa 55, 56 amehimiza kuhusu uwepo wa miradi ambayo itatokana navyanzo vikubwa vya maji ile miradi ya kimkakati ikiwemo mradi wa maji kutoka mto Rufiji. Lakini pia nimeenda mbele zaidi ukurusa wa 111 katika yale majedwali yanayofafanua kuhusu miradi ya maendeleo, nimekuta Kilwa pamoja na Wilaya ya Lindi mkoani Lindi imeeleza kwamba tutapata maji kutoka kwenye Mto Rufiji vijiji viwili tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitanabaishe hapa; kutoka main stream ya Mto Rufiji ni kilometa 52 mnalikuta jimbo langu, yaani ni mpaka wa Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Lindi. Lakini pia uipita njia ya mkato kama unataka kwenda Kipatimu unatembea kilometa 47 tu unakuta tayari umeingia katika jimbo langu Mkoani Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inanishangaza kidogo, au sijui kuna typing error kuona mradi huu utatambaa kutoka Mto Rufiji utakwenda mpaka Kilwa mpaka Wilaya ya Lindi lakini utagusa vijiji viwili tu. Nafikiri hii haiko sawasawa. Na kwa mujibu wa maelezo yao kwenye yale majedwali wanasema wananchi wa vijiji viwili wapatao elfu hamsini laki tisa arobaini na nne watanufaika na mradi huu wa maji ya Mto Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napata mashaka kidogo vijiji viwili kuwa na wananchi 50,000 kwa. Kwa hiyo naomba, kwanza hizi takwimu zikapitiwe upya ili kuona accuracy ya hivyo vijiji ambavyo vimezungumzwa hapa. Lakini, vijiji viwili ni vichache kwa umbali ambao bomba litatambaa. Na kwa kutokana na ukubwa wa tatizo nimeshasema hapa ni vijiji 32 bado vya Wilaya ya Kilwa havina maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo ningeomba Mheshimiwa Waziri wakafanye review katika utekelezaji wa mradi kutoka mto Rufiji ili ikiwezekana angalau mkazo hivu vijiji vyetu 32 ambavyo havina uhakika wa maji. Kwa sababu nina hakika chanzo cha uhakika cha kuweza kututoa kwenye tatizo hili la maji ni hiki cha Mto Rufiji. Na kama nilivyosema mwanzo, ni kiasi cha bilioni tano tu zimetengwa, na miradi ya kiasi cha bilioni 1.4 ndiyo ambayo imekamilika kwa miaka hii mitatu. Kwa hiyo tunahitaji sana maji kutoka Mto Rufiji ili yaweze kumaliza changamoto ya maji katika Wilaya ya Kilwa. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji na kumuongezea, kwamba maji ya Mto Rufiji yanahitajika sana kwenye Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Mtwara kwa ujumla, tunahitaji maji kutoka Mto Rufiji.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Francis unapokea hiyo taarifa?
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea kwa asilimia 100. Wiki moja iliyopita tulipewa taarifa hapa na Wizara, kwamba Wizara pamoja na kutekeleza huu mradi kwa vijiji viwili vya Wilaya za Kilwa na Lindi pia watatengeneza mabomba mawili kupitia njia ya Mkuranga na Kisarawe ili yapeleke maji Dar es salaam. Lakini tunaona uwekezaji wa kuelekea Dar es salaam ni mkubwa sana. Ni kwa nini uwekezaji kama huo usifanyike kwa mikoa ya Kusini kama alivyozungumza mwenzangu Mheshimiwa Kuchauka? Kwa hiyo niseme tu kwamba tunahitaji nguvu kubwa ielekezwe katika wilaya za Mkoa wa Lindi za Kilwa, Lindi vijijini, Lindi Mjini pamoja na Liwale kwa kuanzia ili wananchi wetu waweze kupata hii huduma ya maji safi na salama…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Francis Ndulane.
MHE FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona na kuwa mchangiaji wa kwanza katika Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi jioni ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Wizara yetu ya Ujenzi na Uchukuzi kwa namna ambavyo inachapa kazi katika kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu hapa nchini. Hongera sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Prof. Mbarawa, pamoja na Wasaidizi wako katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuanza kuchangia kwa kuizungumzia barabara inayoanzia katika Kijiji cha Nandete, inayopita katika Vijiji vya Gezaulole Mkoa wa Pwani, pamoja na Kijiji cha Tawi kwenda kutokea Nyamwage.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 16 Agosti, 2010 wakati wa maadhimisho ya kumbukizi za sherehe ya miaka 100 ya Majimaji, aliyekuwa Rais wetu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, alielekeza Mamlaka ya TANROADS iweze kuifungua hii barabara kutoka Nandete kupitia Gezaulole – Tawi kwenda kutokea Nyamwage yenye urefu wa kilometa 46 ili iweze kupandishwa daraja na kuwa barabara ya Mkoa. Lakini kwa masikitiko makubwa, napenda nieleze kwamba mpaka kuifikia leo hatujawahi kuona dozer wala grader likifika pale kuweza kuitengeneza hii barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa watu wa TANRODAS wa Mkoa wa Lindi – kwa sababu mimi nilikuwa jikoni pale TANROADS Lindi – nilishuhudia ofisi yetu ya TANROADS wakati ule ikitengeneza write-up ya ujenzi wa ile barabara ambao ulitarajiwa kugharimu shilingi bilioni 1.2 kwa gharama za wakati ule ili iweze kufunguliwa, kukatwa milima, ku-fill kwenye mabonde lakini mwisho wa siku kuijenga kwa kiwango cha changarawe. Kwa hiyo kwa masikitiko makubwa nasema kwa miaka 13 sasa hii barabara ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wetu wa Serikali ya Awamu ya Nne, haijaweza kushughulikiwa hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha kidogo kwa sababu kuna barabara juzijuzi hapa, mwaka 2021, kwa mfano kuna barabara ile inayoanzia Bigwa kwenda kutokea Kisaki pale Morogoro ambayo inapita kwenye Majimbo matatu, Jimbo la Mheshimiwa Abood, Jimbo la Mheshimiwa Innocent Kalogeris pamoja na jimbo la Mheshimiwa Taletale, yenyewe yalitolewa maagizo kama haya na Mheshimiwa Rais wetu, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli wa Serikali ya Awamu ya Tano, na leo hii tumepewa taarifa hapa kwamba mwezi Juni utasainiwa mkataba kwa sababu taratibu za manunuzi zimefanyika, ile barabara inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunahitaji angalau changarawe tu kwa kuanzia zile kilometa 46 ili kuweza kuwainua kiuchumi wananchi wa Wilaya za Kilwa, Liwale pamoja na wananchi wa Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani. Kwa hiyo ninaomba Serikali itilie uzito. Tusisubiri mpaka baadaye Kiongozi anafariki ndiyo unaanza kusema tunamuenzi kiongozi. Tumuenzi Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa hai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku niseme tu kwamba wananchi wa Kilwa Kaskazini kupitia mikutano yao ya Mabaraza mbalimbali tayari walishaibatiza jina hiyo barabara, walishasema ikitimia ikawa kwa kiwango cha lami wataiita barabara ya Jakaya Mrisho Kikwete. Kwa hiyo, ninaomba Serikali iishughulikie. Nina hakika ikitengwa bilioni 2.5 ile barabara inaweza kufunguliwa, kuwekwa makalavati na changarawe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda niizungumzie barabara ya pili inayotoka Njia Nne kwenda Kipatimu yenye urefu wa kilometa 50. Barabara hii kwa miaka miwili na nusu iliyopita imeweza kujengwa kwa kiwango cha lami kilometa 1.9 na hivyo kuacha kilometa 48.1 zikiwa hazijajengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa scenario iliyopo inaonesha kumekuwa kukijengwa wastani wa mita 700 mpaka mita 600 kwa mwaka, kiwango ambacho ni kidogo sana. Ninaomba katika eneo hili Serikali ije na mradi wa kimkakati wa angalau kilometa 20 katika ile barabara mwaka ujao wa fedha ili mwaka huo unaofwata tuweze kuimaliza ile barabara kwa sababu itabaki eneo dogo tu. Kwa hiyo, niiombe Serikali iongeze fedha katika ile barabara kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024 ili barabara ile iweze kuendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na iweze kuwa na urefu wa kutosha wa kiwango hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya tatu ninayopenda kuizungumzia ni barabara ya Nangurukuru – Liwale. Nimesoma kwenye randama ya bajeti yetu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, nimeona Serikali imekusudia kujenga umbali wa kilometa 50 kutoka Nangurukuru kwa kiwango cha lami. Lakini ile barabara ina urefu wa kilometa zaidi ya 230 toka Nangurukuru kwenda Liwale. Kwa hiyo ukiangalia kilometa 50 haifiki hata robo ya umbali ambao unatakiwa kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaiomba Serikali iongeze angalau kilometa 50 nyingine tuanze na kilometa 100 baadaye tujenge tena 100 ili katika mwaka wa tatu basi tuweze kumaliza. Ikiwezekana mwaka 2025/2026 tuweze kumaliza ile barabara kwa kiwango cha lami kwa sababu wananchi wameteseka kwa miaka mingi katika ujenzi wa ile barabara.
MHE. ZEBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndulane, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kuchauka.
TAARIFA
MHE. ZEBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa mzungumzaji kuhusiana na hiyo barabara ya Nangurukuru – Liwale kwamba siyo tu kwamba imetengwa fedha kilometa 50, mimi ombi langu ni kwamba hizo kilometa 50 fedha hizo zitoke kwenye bajeti hii.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Francis Ndulane, unaipokea hiyo taarifa?
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yake nimeipokea kwa mikono miwili kwa kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ambalo ninapenda kulizungumza siku ya leo ni kuhusiana na upanuzi wa barabara kulingana na Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 (The Roads Act, 2007). Katika mwaka 2007 upana wa barabara ulipanuliwa kwa barabara kuu kutoka mita 45 hadi mita 60 na zile barabara za mkoa zilipanuliwa upana kutoka mita 30 hadi mita 45.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwaambia kuwa hadi kufikia leo katika lile eneo ambalo barabara ilipanuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Barabara ya mwaka 2007, wananchi wote wa Mkoa wa Lindi hawajalipwa fidia zao. Kwa hiyo ninaomba Serikali ije na maelezo ni lini itaanza kutekeleza mkakati wa kulipa fidia katika lile eneo ambalo waliliongeza kwa mujibu wa sheria.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
TAARIFA
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mchangiaji kwamba, siyo kwake tu ambako bado hawa wananchi hawajalipwa, hata kwangu Mwibara wananchi wengi wanateseka kwa sababu hawajalipwa fidia zao. Tunaomba Serikali iwalipe fidia zao.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Francis.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naipokea taarifa yake rafiki yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili inaonekana ni janga la Kitaifa, kwa hiyo naomba Wizara ikadirie fedha, ikiwezekana ianze kulipa kwa awamu katika hizi barabara wakianzia na barabara kuu baadaye waende kwenye barabara za Mikoa na nyinginezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa, kuna barabara inayotoka Rangitatu kwenda mpaka Kongowe, yenye urefu kama kilometa 12 hivi. Ile barabara ilipangwa kujengwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, lakini sijasikia leo hapa kama kuna kasma yoyote imetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ile kwa kiwango cha barabara nne. Kwa hiyo, ninaomba wakati Mheshimiwa Waziri anakuja ku-wind up atuambie ni lini ile barabara itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami njia nne kutoka Kongowe mpaka Rangitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. FRACIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Kwa ujumla ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dokta Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anashughulikia ipasavyo utatuzi wa kero mbalimbali na changamoto mbalimbali za wananchi wetu wa Tanzania katika tasnia hii ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda nimpongeze sana sana sana Ndugu yangu Nape Moses Nnauye ambaye leo ningependa kumtunukia mimi binafsi cheo cha ujemadari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini miaka 118 iliyopita ililshuhudia majemadari 30 wakiongoza Vita vya Majimaji kwa ajili ya kutokomeza ukoloni wa Wajerumani. Leo nimeamua kumtunukia ujemadari Nape Moses Nnauye siyo kwa ajili ya kutupa mikuki dhidi ya wakoloni, bali ni kwa ajili ya kupambana na adui ujinga, umaskini na maradhi kupitia tasnia ambayo anaiongoza ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Bila tasnia hii kusimamiwa vizuri, adui ujinga, maradhi na umasikini hawezi kuondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia wiki moja iliyopita Serikali yetu imesaini mikataba kwa ajili ya ujenzi wa minara 758 katika Kata 713 hapa nchini. Hili ni tukio kubwa la kimapinduzi ambalo linakwenda kuipeleka nchi yetu katika mstari wa mbele kabisa wa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipoingia madarakani kwa nafasi ya Ubunge, Jimbo langu la Kilwa Kaskazini lilikuwa na vijiji 22 ambavyo vilikuwa havina mawasiliano ya simu lakini ndani ya mwaka mmoja ilipofika mwaka 2021 Serikali iliweza kutujengea minara minne katika Vijiji vya Pungutini, Nandete, Chapita na Mwengei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia juzi Serikali imeingia mkataba na kampuni mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa minara ya simu. Napenda nikutaarifu, sisi Wilaya ya Kilwa tumepata minara 15 ambayo itajengwa katika vijiji 21 vya Wilaya ya Kilwa, na jimbo langu litapata minara minane ambayo itaweza kutoa mawasiliano katika vijiji vipatavyo 10. Kwa hiyo, ukichukua ile takwimu ya vijiji 22, ukitoa vile vinne vya mwaka 2021, ukitoa hivi 10 ambavyo vinaenda kupata huduma ndani ya miezi tisa ijayo, tayari tutakuwa na vijiji vipatavyo vinane, ndiyo vitabaki kuwa havina mawasiliano ya simu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naipongeza Serikali kwa kuweza kufanya kazi kubwa ndani ya kipindi kifupi. Ndiyo maana nimempa huu wadhifa wa ujemedari ndugu yangu Mheshimiwa Nape Moses Nnauye. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba maeneo yafuatayo yazingatiwe katika utekelezaji wa hii miradi ya ujenzi wa minara 15. Katika jimbo langu kuna Kijiji kinaitwa Zinga Kibaoni kimeainishwa kwamba nacho kitapelekewa mnara. Hiki kijiji ni kipana sana. Uki-calculate ile dimension ya kijiji toka kona moja mpaka nyingine, ni zaidi ya kilometa 40. Sasa tayari pale katikati ya kijiji kuna mawasiliano ya Halotel. Kuna kitongoji ambacho kina watu wengi zaidi kinaitwa Nambunju, naomba mnara huu upelekwe Nambunju. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna Kijiji inaitwa Namatewa, kinajengewa minara miwili, lakini wakati huo Makao Makuu ya Kata hakuna mnara hata mmoja uliojengwa pale Kandawale. Kwa hiyo, naomba mnara mmoja ambao ulikuwa ujengwe Kandawale na Airtel upelekwe Kandawale ili pale Namatewa ubaki mnara mmoja. Naomba hilo lizingatiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna changamoto katika ile minara minne ambayo ilijengwa mwaka 2021 katika Vijiji vya Pungutini, Nandete, Mwengehi, pamoja, Chapita, pamoja na Kijiji cha Mtopera. Ile minara inatumia teknolojia ya solar kwa ajili ya kuipa nguvu iweze kufanya mawasiliano. Hili limesababisha changamoto kwa ile minara kuweza kufanya kazi kwa masaa yasiyozidi 10 kwa siku, na matokeo yake kumekuwa na malalamiko mengi. Kwa sababu mwingine anaweka bundle litatumika masaa 24, lakini mwisho wa siku ndani ya masaa 14 ya saa hizo 24 mawasiliano yanakuwa hayapo na wakati bado bundle lake lilikuwepo kwenye simu. Matokeo yake anashindwa kupata haki yake ya kutumia lile bundle mpaka liweze kwisha. Kwa hiyo, naomba Serikali iunganishe hii minara yote na mtandao wa umeme wa REA ambao upo katika hatua za mwisho za kukamilisha katika hivyo vijiji vyote nilivyovitaja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nivitaje vijiji vinane ambavyo vimebaki ambavyo havitakuwa na mawasiliano ya simu baada ya mradi huu wa maeneo 15 kukamilika. Vijiji hivyo ni vya Hanga, Kinywanyu, Ingirito, Kongwe, Marendego pamoja na Namanungutungu na pia kipo Kijiji cha Nandombo pamoja na Kijiji Nambondo. Naiomba sana Serikali katika awamu ijayo ya ujenzi wa minara hivyo vijiji vinane vifikiriwe ili tuweze kupata mawasiliano mwanana jimbo zima na wilaya nzima ya Kilwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa naipongeza TBC kwa kazi kubwa wanayoifanya, na nimeona jana pale nilipokuwa napita kwenye banda lao, wamelenga kujenga kituo kikuu cha mawasiliano ya TBC katika Wilaya ya Kilwa pale Nangurukuru. Naomba kazi hiyo iendelee ifanyike kwa haraka kwa sababu kuna changamoto kubwa ya Mawasiliano ya TBC.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni ya leo na mimi niweze kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningependa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo iliyopo katika sekta hii ya nishati ambayo kwa sasa inakwenda kwa speed kubwa lakini inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa sana, nampongeza sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ningependa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo kwa kushirikiana na Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu, pamoja na Viongozi wa Taasisi mbalimbali zilizo chini yake wanavyoisimamia vizuri miradi hii, kwa kweli miradi inakwenda vizuri nawapongeza sana, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mradi LNG umeanza kutekelezwa, unapozungumzia Mradi wa LNG kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara ni mradi ambao ni very sensitive kwa kweli, pale katikati ulipokuwa umekwama kwa miaka saba watu wengi katika Mikoa ya Lindi na Mtwara walisononeka sana. Pia, napongeza namna ambavyo Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere unavyotekelezwa, nimefarijika sana kusikia kwamba pale Mkoani Lindi kunaenda kujengwa Chuo cha Masuala ya Umeme, Masuala ya Mafuta pamoja na Gesi tena chuo chenyewe ni chuo chenye hadhi ya Kimataifa hongera sana Mheshimiwa Waziri na timu yako kwa kazi nzuri mnayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maeneo kadhaa ya kushauri, katika Mkoa wetu wa Lindi tuna changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa umeme, umeme umekuwa ukikatikakatika mara kwa mara inafika wakati, kwa mfano kama katika Wilaya yangu ya Kilwa ndani ya massa 24 umeme unaweza ukakatika hata masaa nane, mara nane kwa hiyo hii ni changamoto kubwa lakini hata taarifa nilizonazo kule kwa Mheshimiwa Kuchauka - Liwale, kule kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu - Ruangwa, Nachingwea na hata Manispaa ya Lindi kwa kweli kadhia hii imekuwa kubwa sana, ninamuomba Mheshimiwa Waziri ule mwarobaini anaopeleka Mkoani Mtwara basi pia aweze kuuleta katika Mkoa wetu wa Lindi ili wananchi wetu wapate umeme wa uhakika.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ambayo ningependa kuizungumza ambayo niliizungumza pia mwaka jana na Wabunge wengi walichangia mwaka jana, kumekuwa katika maeneo fulani ya vijiji watu wetu wananchi wetu wamekuwa wakitozwa gharama ya shilingi 320,000 kwa ajili ya kuunganishiwa umeme, hiyo kadhia bado ipo inaendelea, ningeomba wizara ichukue hatua katika kuhakikisha kwamba wananchi wetu wa vijijini wanaendelea kulipa kiasi cha shilingi 27,000 badala ya 320,000 kuna vijiji vya Somanga Kaskazini, Somanga Kusini, Masoko, Kivinje, Nangurukuru wanatozwa 320,000 kuunganishiwa umeme, kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri tusaidie katika hili jambo ili wananchi wetu waweze kuunganishiwa umeme kwa ile ada ambayo wanatakiwa kutozwa katika level ya vijiji.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yetu ya Kilwa ilikuwa ikipata CSR kubwa tu inayozidi bilioni moja kwa mwaka kutoka taasisi ambayo inachakata gesi pale Wilayani Kilwa katika eneo letu la Somanga, Taasisi inaitwa Pan African lakini kadri miaka inavyoendelea mbele kile kiasi ambacho tulikuwa tunapatewa kama CSR kimekuwa kikipungua sana, sasa hivi tunapata chini ya nusu ya kiwango ambacho tulikuwa tunapata mwaka 2005 wakati mradi huo ulipoanza kutekelezwa. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri tunajua pale Kilwa tumepata miradi mingi tu tumetekelezewa kupitia hiyo CSR, kwa mfano pale Somanga Kituo cha Afya kimejengwa, Chumo Kituo cha Afya kimejengwa, Songosongo hivi sasa Kituo cha Afya kinajengwa, zile fedha zinatusaidia sana, kwa hiyo niombe lile fungu lile la CSR lirudi kama lilivyokuwa zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la ulipaji wa fidia katika Kitongoji cha Cheketu, Kijiji cha Somanga Kusini. Tangu mwaka 2017 ilifanyika tathmini ili lile eneo ijengwe miundombinu ya umeme ya TANESCO, lakini mpaka leo zaidi ya milioni 300 wale wananchi wanadai hazijaweza kulipwa, mwaka jana tuliahidiwa mwaka huu wa fedha zile fedha zingelipwa, ninaomba Mheshimiwa Waziri alichukue hili na wale wananchi walipwe haki yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la umeme wa REA. Katika Wilaya yangu ya Kilwa utekelezaji wa umeme wa REA unakwenda vizuri katika vile vijiji vilivyolengwa. Tunayo shida tu kidogo katika visiwa vilivyopo kwenye Bahari ya Hindi. Kilwa Kisiwani, Songomnara, havijaainishwa katika utekelezaji wa umeme wa REA katika kipindi hiki, kwa hiyo ningeomba hilo liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna maeneo ambayo ni umbali mrefu sana kutoka Kijiji kimoja kwenda kingine wakati kuna vijiji vya Mkoa wa Pwani kule kwa mpwa wangu Mheshimiwa Mchengerwa vyenyewe vinakaribiana na tayari vilishaletewa huduma ya umeme. Kwa mfano kuna Kijiji cha Ngalambilienga, chenyewe ni kilomita saba unakwenda kwenye Kijiji cha Wilaya ya Rufiji, kile Kijiji cha Wilaya ya Rufiji tayari kilishafikishiwa umeme katika zile awamu za awali za utekelezaji wa umeme wa REA, ningeomba badala ya kwenda kuchukua umeme Makao Makuu ya Kata ya Kandawale ambako ni kilomita 38, tutengeneze utaratibu wa kuvuta huu umeme kilomita hizi saba toka Mkoa wa Pwani ili tuweze kufanya serving ya zile kilomita 31 ambazo ningependekeza zipelekwa sasa maeneo mengine kwa mfano, kuna kitongoji ambacho kinakua kwa kasi sana katika Kijiji cha Zinga Kibaoni kilomita 22, ningependa ile ziada ya kilomita 31 ipelekwe kule ili wananchi wa kule nao waweze kupata matumaini kwani tayari walishakuwa wamekata tamaa. Kwa hiyo ningeomba hilo lifanyike lakini zile kilomita zitakazobaki basi zinaweza zikapelekwa katika Makao Makuu ya Tarafa za Kipatimu, Njinjo pamoja na Miteja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo sina la ziada, zaidi ya kuendelea kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri wanayofanya, naomba nihitimishe kwa kusema naunga mkono hoja kwa asilimia 100. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa mwisho katika wachangiaji wa Bajeti yetu ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Moja kwa moja nitangulie kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kuhamasisha na kuwekeza fedha nyingi kwa ajili ya kusaidia mchezo wa soka hasa kwa Vilabu vyetu vya Simba na Yanga ambavyo mwisho wa siku vimepata mafanikio makubwa. Hongera sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan na nimwombe tu Mheshimiwa Rais huko anakonisikia aendelee kutuunga mkono katika mchezo huu ambao unapendwa zaidi kuliko michezo yote duniani ili tuweze kusonga mbele zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia hapa hamasa ambayo imetolewa na Mheshimiwa Rais wetu imepelekea kushuhudia Vilabu vyetu vikifanya vizuri ndani na nje ya nchi kwenye mechi zake. Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia Timu za Simba na Yanga zote kwa pamoja zikifanya vizuri katika medani ya soka. Pia tumeona Yanga imekwenda fainali, hongera sana, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona Club ya Simba ikiwa na consistency kwa zaidi ya miaka mitano ikifanya vizuri na hivyo kupandisha kiwango cha soka kwa vilabu vyetu kwenye ranking za CAF. Kwa Club ya Yanga kutoka nafasi ya 63 hadi kwenda nafasi ya 18, kwa Club ya Simba kutoka nafasi ya 12 kwenda nafasi ya tisa na hivyo kupelekea Club ya Simba kutunukiwa nafasi ya kucheza Super League ya Afrika. Kwa taarifa nilizonazo nyepesi nyepesi hivi karibuni mashindano hayo yatafanyika na huenda yakafanyika nchini Tanzania. Hii itatuongezea fursa nyingine ya kuweza kuongeza zile fursa zilizotokana na royal tour. Kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uwezeshaji wake kwa hamasa yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nihamie kwenye eneo la Sanaa. Sanaa yetu bado kuna maeneo haijafanya vizuri japokuwa juhudi kubwa zimewekezwa na Serikali yetu ya Awamu ya Sita. Katika Nchi za Uturuki, Marekani na hata Afrika Kusini, hapa Afrika kumekuwa na zile sinema au filamu zinazoendana na historia. Ukienda Uturuki kuna filamu ambazo zinatamba sana sasa hivi za akina Osman, Ertugrul Bey lakini hata Marekani kuna zile filamu za kivita za akina Rambo, Michael Dudikoff na zingine. Niliwahi kushuhudia sinema au filamu inayohusiana na utawala wa King Shaka kule South Africa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nafikiri wakati umefika hivi sasa kwa Serikali yetu kuwekeza kwa wasanii wetu kwa ajili ya kucheza picha ambazo zinaendana na historia. Kwa mfumo huu tutaweza kuongeza ajira katika filamu, lakini pia tutaongeza hisia za kizalendo, tutadumisha utamaduni zikiwemo lugha za asili ambazo Tanzania hapa zinatumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hainingii akilini kuona wale wasanii wetu hawawezi kucheza filamu ile ya Mtwa Mkwawa wakati alipowaongoza Wahehe kupambana na Wajerumani na akawashinda katika awamu ya kwanza na yule Jemedari Zelewski akauawa. Vijana wetu hawawezi hizo lakini hawawezi kucheza sinema ya Vita vya Maji maji ambavyo wananchi wa Kabila la Wamatumbi waliwaongoza wananchi wa kabila zingine kupambana na Wajerumani na katika battle la kwanza waliweza kuwashinda Wajerumani siku 31 mwezi Julai mwaka 1905, pale katika Kijiji cha Kibata. Je, hawawezi vijana wetu kucheza picha zenye mvuto ambazo za wale Walugaluga kule wakiongozwa na Chief Milambo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kwa wakati huu sinema za namna hii zimekuwa maarufu sana duniani na zimekuwa zikiingiza kipato sio tu kwa nchi hadi kwa msanii mmoja mmoja. Kwa hiyo niwaombe Serikali tuweke mkakati mzuri, tuwezeshe hizi taasisi zetu za BASATA, COSOTA, TaSuBa pamona na Mfuko huu wa Wasanii Tanzania au Mfuko wa Sanaa tuwezeshe fedha kwa sababu tunajua sinema za namna hii au filamu za namna hii zinagharimu fedha nyingi. Tuwekeza, fedha itolewe ruzuku kwa sababu hili jambo lina manufaa ya kitaifa sio tu kwa msanii mmoja mmoja ili tuweze kuendeleza hizi filamu za namna hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hapa majuzi nilikuwa namsikia Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo akizungumza na Deutsche Welle kuhusiana na fidia kwa waathirika wa vita mbalimbali ambazo Wakoloni wa Kijerumani walipambana na wananchi au mababu zetu. Alizungumzia Vita vya Maji Maji, akazungumzia vita vya Mtwa Mkwawa na Wajerumani, lakini ilitolewa mifano kule Namibia kulikuwa na Waherero na Wamakwa walipambana na Wajerumani, walilipwa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe Wizara itakapokuja ku-wind up kuhusiana na hii hotuba ambayo imetolewa, waje watuambie mkakati walionao katika kudai fidia, lakini sio fidia tu kudai pia zile malikale ambazo zilitaifishwa na Wakoloni wa Kijerumani kama dinosaur ambaye alitolewa kule Tendeguru, Lindi lakini pia hadi mafuvu na sijui wanayatumia kwa shughuli gani mpaka leo, yarudishwe nchini Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ije itupe taarifa wamefikia wapi katika mkakati huo. Vile vile ningeomba jamii zilizo husika na vile vita katika kudai fidia washirikishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia bajeti ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi. Kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa tuzo muhimu ambayo ameweza kuipata ambayo inaendelea kuitangaza nchi yetu na kuendelea kuboresha mambo mbalimbali katika nchi yetu, pili napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Ardhi pamoja Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja nijikite kwenye Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi. Mwaka 2006 katika Mkoa wetu wa Lindi Serikali iliridhia kuingiza mifugo kutoka katika Bonde la Ihefu, hii ilisababisha mifugo mingi kuhamishiwa katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Lindi. Katika Wilaya ya Kilwa peke yake kati ya mwaka 2006 hadi 2007 mifugo isiyopungua Laki Moja iliingia katika Wilaya ya Kilwa. Pia hii ilisababisha sasa Serikali Kuu kupitia Wizara ya Ardhi pamoja na Halmashauri yetu ya Wilaya ya Kilwa pamoja na Taasisi ya BTC (Belgium Technical Cooperation) kuweza kushirikiana kwa pamoja kuweza kupima na kuweza kuboresha matumizi ya ardhi iliyopo katika Wilaya yetu ya Kilwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi iliweza kupimwa jumla ya hekta 337,500 kwa ajili ya kulisha ng’ombe wapatao 168,750, lakini kwa vipindi tofauti kati ya mwaka 2007 hadi sasa takribani miaka 15 iliyopita, mifugo mingi imeendelea kuingia katika Wilaya ya Kilwa pamoja na Mkoa wa Lindi kwa ujumla. Wilaya ya Kilwa peke yake mifugo inayokadiriwa kufikia 350,000 imeingia, vilevile wale waliokuwepo tangu mwaka 2006 wameendelea kuzaana na mifugo mingi imeingia kwa kupitia njia za holela, mingine imepita kupitia Pori la Akiba la Selous, mingine imeingia kutokea Mkoa wa Pwani, kwa hiyo, sasa hivi kuna takribani ng’ombe, ng’ombe peke yake wanakaribia 500,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, imesababisha hali kuwa ngumu sana ya maisha ya wakulima wetu, pia wafugaji wenyewe kwa sababu, mpango wa matumizi bora ya ardhi umeshapitwa na wakati kwa sababu una zaidi ya miaka 15 tangu ulipofanyika. Na kwa mujibu wa utaratibu mpango wa matumizi bora ya ardhi unatakiwa uwe reviewed angalao kila baada ya miaka 10, kazi ambayo haijafanyika na hiyo imesababisha kuwepo na changamoto kubwa, mapigano ya mara kwa mara, lakini mifugo kuweza kutangatanga hovyo katika Wilaya nzima ya Kilwa na Wilaya zote za Mkoa wa Lindi. Kwa hiyo, sasa hivi tuna hali ngumu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda utambue ndani ya miezi 12 iliyopita wananchi wanne walipoteza maisha, wawili katika Kijiji cha Nanjilinji, mmoja katika Kijiji cha Nakiu, pia katika Kijiji cha Kipindimbi kuna mwananchi mmoja alipoteza maisha kwa hiyo, jumla ni wananchi wanne walipoteza maisha ndani ya miezi 12 iliyopita, lakini pia kumekuwa na vurugu za hapa na pale nyingi. Kwa mfano, Tarehe 07 mwezi Aprili mwaka huu katika Kijiji cha Ngarambi, WEO wa Kijiji kile, Afisa Mtendaji Kata, alivamiwa na kundi la wafugaji lakini bahati nzuri alikimbia na badaye alijisalimisha katika Kituo cha Polisi kule Somanga, lakini na wale wafugaji walichachamaa baada ya kuwa mifugo yao ambayo iliingia kiholela katika Wilaya ya Kilwa ilipokuwa imekamatwa, baAdae walimvamia Askari wa mgambo ambaye alikuwa analinda ile mifugo na kumjeruhi, matukio ya namna hii yamekuwa mengi mno kiasi kwamba, yanawakatisha tamaa wakulima wetu, lakini yanawafanya hata wale wafugaji wasiweze kufuga ng’ombe wao na mifugo yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali katika hili ijitahidi kuweza kuona sasa katika zile fedha kidogo zilizotengwa kwa ajili ya maboresho au Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi waweze kutumia hizo fedha, vilevile zije Kilwa tuweze kuona namna ambavyo tunatatua ile migogoro. Nina imani kama mpango wa matumizi bora utafanyika katika Wilaya ya Kilwa ambao katika kipindi kilichopita ule mwaka 2006/2007 ulifanyika katika vijiji 35 tu wakati Kilwa tuna vijiji 90, ni imani yangu kwamba, tutapunguza kwa kiasi fulani hii migogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uzoefu na kazi ambazo zimefanywa za maboresho ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kule Kilombero. Kulikuwa na mradi mmoja unaitwa Land Tenure Support Program, umesaidia sana katika Bonde la Kilombero hasa Wilaya za Malinyi, Ulanga pamoja na Mlimba. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba, tukitekeleza vizuri ule mradi basi haya mambo ya mauaji, haya mambo ya watu kujeruhiwa basi yatapungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli niseme ningependa kwa kuanzia Kata ambazo zinaongoza ziko 12 ambazo ni Kata ya Somanga, Kata ya Mingumbi, Kinjumbi, Kipatimu, Kandawale, Mitole, Njinjo, Miguruwe, Nanjilinji, Kikole, Likawage pamoja na Kiranjeranje, ikikupendeza kupitia Wizara ya Ardhi basi tuanze na maeneo hayo ambayo yamekithiri kwa migogoro kila kukicha. Nashukuru Mheshimiwa Waziri wakati tunatekeleza ule mradi wa Land Tenure Support Program kule Bonde la Kilombero wakati ule ulikuwa Naibu Waziri na mara kadhaa ulikuja katika Bonde la Kilombero kuhakikisha ule mradi unatekelezwa kwa ufanisi. Na kwa kuwa, ulitekelezwa kwa ufanisi, ulitatua changamoto nyingi sana ambazo zilikuwa zinawakabili wananchi wa maeneo yale ya Malinyi, Ulanga, Mlimba pamoja na Kilombero yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme nikuombe Mheshimiwa Waziri basi na sisi utufanyie kama vile ambavyo experience inaonesha kule tuliweza kutatua ile migogoro ya wakulima na wafugaji, kwa sababu ule mradi kupitia wataalam wetu wabobezi, kulikuwa na Dada mmoja anaitwa Siyabumi Mwaipopo, sasa hivi sijui yuko Mbeya, sijui yuko wapi, walifanya kazi nzuri sana. Kwa kweli, nawapa hongera kwa kazi ambayo ilifanyika kule, Kilwa basi tunaomba Mheshimiwa Waziri utuletee ule mradi, hata kama siyo ule, lakini angalao ulete fedha basi ili baadae ule mradi utafanyika kwa mfumo ule wa revolving, kwa maana tutapata hela kupitia zile hati za kimila pamoja na kazi ambayo itafanyika watu watalipia kidogokidogo na mwisho wa siku tutajikuta vijiji vyote 90 tuweze kuvikamilisha kuvipima, lakini vilevile kuweza kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na pia kupima mipaka kati ya vijiji hadi vijiji ambayo iko mingi tu sasa hivi katika Wilaya ya Kilwa. Siyo katika Wilaya ya Kilwa tu hadi Kilwa na Wilaya za majirani kama Liwale na Rufiji kwa kweli hali siyo nzuri kuna migogoro ya hapa na pale kati ya vijiji vya Wilaya moja kwenda Wilaya nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni imani yangu kwamba, kwa kupitia utaratibu huu wananchi watapata hati za kimila, lakini vilevile watadumisha usalama na amani katika maeneo yao. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri utusaidie katika hilo ili tuondoe hii hali ambayo inaendelea kukua ya mapigano ya mara kwa mara, watu wanajeruhiwa, wanakufa na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri kuna suala la migogoro kati ya vijiji vyetu vya Wilaya ya Kilwa pamoja na Hifadhi ya Pori la Akiba la Selous. Kuna vijiji vinne katika Jimbo langu peke yake, kuna Kijiji cha Nakingombe, kuna Kijiji cha Ntepela, kuna Kijiji cha Zinga, kuna Kijiji cha Nakingombe, hivi vijiji vinne vinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Pori la Akiba la Selous kwa hiyo, niombe Mheshimiwa, tuliliongea hili wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja mwezi Oktoba mwaka jana kwa uchungu na masikitiko makubwa sana. Kulikuwa na mgogoro mkubwa sana kati ya TAWA na wananchi wa hivyo vijiji, bahati nzuri ilikuja Tume ya uchunguzi, ingawa majibu hatujayapata mpaka leo na sasa ni ktakribani miezi Sita inakaribia tangu ile Tume ilipokuja kuchunguza ule mogogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba majibu tupate mapema ili wananchi watulie waendelee kufanya shughuli zao za kiuchumi katika hayo maeneo…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndulane, muda wetu umemalizika wa siku ya leo.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi siku ya leo kuwa mchangiaji wa pili jioni ya leo katika Bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumpongeza nakumtakia kila la heri Mheshimiwa wetu Waziri, jirani yangu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa pamoja na Naibu Waziri wetu Mheshimiwa Pauline Gekul, Katibu Mkuu Hassan Abbas pamoja na Naibu Katibu Mkuu Ndugu Saidi Yakubu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema haya kwa sababu kuna mambo mengi tangu wameingia katika Wizara hii kwa pamoja wameweza kuyafanikisha wakishirikiana na watumishi waliopo katika Wizara hii. Tumeshuhudia sinema ya Royal Tour waliisimamia vizuri na leo inaitangaza nchi yetu ya Tanzania katika medani ya utalii pia wamesimamia timu yetu ya michezo ya Tembo Warriors, Timu ya Taifa ya walemavu ambayo iliweza kufuzu katika mashindano ya Kombe la Dunia ya Timu za Walemavu.
Mheshimiwa Spika, juzi tu hapa tumeshuhudia Timu yetu ya Taifa ya Wasichana chini ya miaka 17 ikifuzu kwa kucheza Kombe la Dunia kule nchini India jambo ambalo halijawahi tokea. Timu zetu za mpira wa miguu hazijawahi tokea wakati wowote ule ukiondoa ile ya walemavu kufuzu kwa ajili ya mashindano haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nitakuwa mtovu wa fadhila kama sitaipongeza Klabu ya Young Africans kwa kuwa na mafanikio makubwa sana katika msimu huu. Mafanikio ambayo yalikuwa adimu katika klabu yao kwa miaka mfululizo minne iliyopita. Nawapongeza lakini nawapongeza pia katika hata zile point ambazo tulipata za kutuwezesha kuendelea kuwa na washiriki wanne katika mashindano ya vilabu barani Afrika wao wamechangia alama 0.5 kati ya alama 30.5. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nawapongeza klabu ya Namungo kwa kuendelea kuchangia katika timu ambazo zinakwenda kucheza msimu ujao wa mashindano ya vilabu Barani Afrika kwa kuwekeza point mbili pale. Hongera sana naona Mwenyekiti yupo hapa wa Namungo, hongera sana Mheshimiwa Hassan. Sana sana niipongeze Klabu ya Simba, Klabu ya Simba imetutangaza vilivyo katika medani ya Kimataifa hasa katika mashindano ya vilabu Barani Afrika, kuweza kushiriki mashindano ya Kimataifa ya vilabu Barani Afrika mara nne, ukaweza kupata nafasi ya kucheza robo fainali mara tatu, si jambo la mchezo ni jambo ambalo linatakiwa kuigwa, ni jambo la mfano ambalo limeiweka nchi yetu katika level ya juu kabisa ya mashindano ya vilabu Barani Afrika. Simba kutokana na mafanikio ya miaka minne wamechangia alama 28 kati ya 30.5 ambazo zimetufanya tuendelee kuwa na vilabu vinne. Alama za klabu ya Simba peke yake zimezizidi alama za nchi maarufu hapa Barani Afrika kama Libya na Nigeria overall kwa timu zao zote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ningeomba tujifunze kutokana na Simba, haikuwa rahisi sana kwa klabu ya Simba kuweza kupata mafanikio katika medani za Kimataifa haya ambayo wameyapata. Mimi ni mdau wa mpira wa miguu katika mpira wa miguu kuna mambo matatu huwa tunayazungumza ambayo ndiyo msingi wa kuboresha mpira mahala popote unapochezwa. Jambo la kwanza ni utawala bora katika klabu, jambo la pili ni kuwekeza katika wachezaji bora, jambo la tatu ni kuwekeza katika benchi la ufundi. Kwa hiyo, hayo ni mambo matatu ambayo ni ya msingi sana ambayo Simba yote walifanikiwa kuwa nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia Simba walijiongeza kwa kuongeza factors zingine, factor iliyoongezeka ya nne ilikuwa ni kuwekeza rasilimali fedha ya kutosha kwenye klabu. Kama huna fedha huwezi kucheza mpira lakini pia walikuwa na washabiki bora wa mfano Barani Afrika, pia walitumia vyombo vya habari vizuri … (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Ndulane kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mwita Boniphace Getere.
T A A R I F A
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba pamoja na umaarufu wa Simba lakini anadaiwa na TRA bilioni sita, Yanga anadaiwa bilioni tatu. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, futa usemi.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante.
SPIKA: Unajua mimi humu ndani napima tu mashabiki gani ni wavumilivu, wapi uvumilivu hamna. Mheshimiwa Ndulane unaipokea taarifa hiyo.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante nimeipokea taarifa yake lakini ni imani yangu kwamba klabu ya Simba haina shida ya kulipa deni kama hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la sita; ni kwamba Simba waliboresha miundombinu ya uendeshaji wa klabu yao ikiwemo kiwanja cha mazoezi pamoja na program nzima za mazoezi na ushiriki wa timu kwenye mashindano mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nini nichotaka kusema, sifikiri kwamba Simba wamefika mahali ambapo wanatakiwa kufika, lakini wamejitengenezea brand ambayo inapaswa kuigwa na vilabu vingine. Vilabu vingine vinapaswa kujifunza kutokana na Simba ili tuweze kwenda mbele. Nina imani kama vilabu vingine vitajifunza kutokana na Simba sitashangaa kwa speed hii ambayo wanakuja nayo Yanga na vilabu vingine, mwakani sitashangaa kuona vilabu vyetu vinne vyote vikishiriki angalau hatua ya robo fainali Barani Afrika pia sitashangaa pia kuona vilabu vyetu nchini Tanzania vikifikia angalau viwili vikifikia hatua ya nusu fainali kwenye mashindano ya vilabu Barani Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niviombe vilabu vingine viendeshe mpira kisayansi kama ambavyo wanafanya Simba, ingawa niseme tu hapa katikati Mheshimiwa Rais wetu Mstaafu aliwahi kusema wakati fulani tatizo la nchi yetu kuna baadhi ya vilabu vinaendesha mpira, wanawekeza kwenye Kamati za ufundi badala ya benchi ya ufundi, hilo ningeomba lizingatiwe lakini pia tuweze kuona namna ambavyo timu zitasonga mbele.
Mheshimiwa Spika, Simba nao nafikiri hawajafika pale ambapo tunatarajia, haiwezekani miaka minne tunaishia robo fainali, nilifikiri wanapaswa sasa kupiga hatua kwenda mbele zaidi. Ninafikiri hilo linawezekana kwa sababu wametoka mbali, wamefika mbali. Kwa hiyo, niwaombe Viongozi wa Klabu ya Simba wakishirikiana na Serikali yetu kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo waweze kuboresha mazingira ya klabu zetu ili hatimae ziweze kufanya vizuri zaidi. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Ndulane kengele ya pili imeshagonga.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2024/2025. Awali ya yote napenda kumpongeza schoolmate wangu wa Pugu High School, Profesa Kitila Alexander Mkumbo, pamoja na rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu, Waziri wetu wa Fedha pamoja na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ambaye pia ni schoolmate wangu katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawapongeza kwa sababu wametuletea taarifa nzuri zenye mwelekeo mzuri, lakini sana nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuonesha dira kupitia hotuba yake aliyoitoa tarehe 19 mwezi Machi mwaka 2021 wakati alipoapishwa kushika hatamu za uongozi wa nchi yetu. Pia, kwenye hotuba yake aliyoitoa hapa Bungeni siku ya tarehe 22 mwezi Aprili, mwaka 2021, kwa kweli imezingatiwa kwa kiwango cha kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ningependa kuchangia katika sekta mbili tu; Sekta ya kwanza ni ya utalii na sekta ya pili ni ya mifugo. Tumeona kwenye taarifa ongezeko la mapato na idadi ya watalii katika nchi yetu imeongezeka sana na mapato ya Serikali yetu yameongezeka sana kupitia sekta hiyo. Takwimu zinaonesha kwamba mwaka 2021 watalii waliongia hapa nchini walikuwa 922,692, lakini mwaka uliofuata mwaka 2022, waliongezeka hadi kufikia 1,454,920 sawa na ongezeko la watalii takribani 500,000 hivi sawa na asilimia 57.7.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko hili limewezesha ongezeko la fedha zilizopatikana kutokana na sekta hii toka dola milioni 1.31 mwaka 2021 hadi kufikia dola milioni 2.53 mwaka 2022. Ni ongezeko kubwa na hili linaonesha namna ambavyo tumekuja kunufaika kutokana na maono ya Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia ile Filamu ya Royal Tour. Narudia kumpongeza Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia vizuri hizi taarifa zote tatu, sijaona mwendelezo wa Royal Tour. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri tuone namna ambavyo tutaendeleza mwenendo mzuri uliotokana na Filamu ya Royal Tour. Kwa sababu hata taasisi za Kimataifa ambazo zilifanya assessment ya shughuli za utalii zinavyoendeshwa hapa Tanzania na nchi nyingine za kiafrika imei-rank nchi yetu kuwa namba moja kwa vivutio vingi vya utalii. Duniani imekuwa ranked kama namba 12. Kwa hiyo, haya ni mafanikio makubwa. Haya hayatufanyi tubweteke, tunatakiwa tubuni vyanzo vipya kama ambavyo malengo yetu ambayo yameandikwa kupitia huu mpango yalivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napendekeza au naishauri Serikali, tuwe na mkakati wa kuwa na Royal Tour Na. 2 au Phase II. Naomba tuweze kuzingatia maeneo yafuatayo: moja, katika hii Royal Tour Na. 2 tuyatazame maeneo ya hifadhi zetu za Taifa, tukianzia na ile ya Ruaha, tuangalie kule misitu ya Udzungwa, pori la Akiba la Selous, twende tukaioneshe dunia maajabu ambayo Mwenyezi Mungu alituumbia sisi Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niliona tunahitaji kuwekeza katika malikale kupitia hiyo Royal Tour Na. 2. Pale Kilwa kuna Magofu ya Kilwa Kisiwani yaingie, Songo Mnara yaingie, viboko albino pale Pindiro, Makangaga yaingie, viboko katika Bwawa wa Maliwe au Ziwa la Maliwe pale Mitole liingie, vilevile kumbukizi za mambo mbalimbali ya kale kama vile Vita vya Majimaji kule Kilwa pale Nandete, Kibata na maeneo mengine na kule Songea pia, yaingie katika Royal Tour. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi hapa alikuja hata Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani, alifika mpaka Songea. Hiyo inaonesha kwa jinsi gani hata watu walio nje ya nchi ambao tulikuwa tunashirikiana kwa majukumu mbalimbali siku zilizopita, bado wanaikumbuka Tanzania na wanaona kuna fursa nyingi za kuweza kushirikiana nasi. Kwa hiyo, naomba hilo nalo liingie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna utalii wa mapango. Kati ya mwaka 1994 na mwaka 2000 kulikuwa na Wataalam wa Kijerumani walikuja hapa nchini wakafanya utafiti kwenye mapango 25, wakiongozwa na Albert Daniel Galabawa. Walianzia Tanga, wakafanya exploration ya mapango tisa yakiwemo nane ya Amboni, lakini kulikuwa na mapango mengine Zanzibar moja, kule wanaita Mangapwani, pia walikwenda katika Milima ya Matumbi ndani ya Jimbo langu Kilwa Kaskazini, walifanya exploration na utafiti kwenye mapango 15, likiwemo Pango la Nang’oma ambalo ni kubwa, namba moja katika Afrika Mashariki kulikuwa na Pango la Naliotoke, kulikuwa na pango la Kiongolo, Mpachawa, Kilindima, Namaingo, Lupondo, Kibwe, Shingya, Kimambo, Nampombo, Likolongomba pamoja na pango la Mtumbukile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu ule utafiti umefanyika, hakuna uendelezaji wowote uliofanyika. Hata Waheshimiwa Mawaziri tu, nakumbuka Waziri mmoja tu alifika mwaka 2021 katika Pango la Nang’oma lile ambalo nimesema ni kubwa kuliko yote Afrika Mashariki. Kwa hiyo, nilifikiri hapa tunapaswa kujenga Information Center, lakini vilevile tuone namna ambavyo tutaendeleza hivi vyanzo vya utalii. Nina hakika nchi yetu itapiga hatua katika sekta ya utalii na vilevile tutaweza kupata pesa mara tatu hadi mara nne inayotokana na hivi vyanzo ambavyo inaonekana vimesahaulika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikenda kwenye sekta ya mifugo, naomba niwaeleze Waheshimiwa Wabunge wenzangu. Sisi Tanzania hapa hatufugi, tunachunga. Hii imepelekea changamoto kubwa. Kuna uharibifu wa mazingira ambao unapelekea kuwepo kwa athari za tabianchi lakini pia kumekuwa na mapigano ya mara kwa mara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha tuna mifugo isiyopungua milioni 28.3, lakini mifugo hii inachungwa, imezagaa tu nchi nzima. Ni lazima tuwe na mipango mizuri ya kuendeleza sekta hii ya mifugo, vinginevyo tutaendelea kushuhudia majanga, tutaendelea kushuhudia matatizo; achilia mbali migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imejaa kule hasa Mkoa wetu wa Lindi katika Wilaya za Kilwa, Nachingwea pamoja na Wilaya ya Liwale. Pia hata miundombinu ya hii mifugo haipo. Tumesomewa hapa kwenye taarifa, kuna ujenzi wa majosho 246. Sasa majosho 246 kwa mifugo milioni 28.3, wapi na wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna utoaji wa chanjo, mifugo 696 imetolewa kwa mwaka uliopita. Hii mifugo 696 kwa mifugo milioni 28.3 wapi na wapi? Bado hatujafanya juhudi za kuhakikisha kwamba tunaidhibiti hii mifugo, lakini tunaifuga katika namna ya kisasa ili iweze kuzalisha kwa kiwango cha kutosha. Kwa hiyo, nimeangalia hata ulaji wa nyama, inaonekana sisi katika top ten hatumo…
MWENYEKITI: Ahsante, kengele ya pili hiyo Mheshimiwa.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali ichukue hatua za kutosha ili kuzuia haya mapigano ya wafugaji na wakulima, na pia kuruhusu sekta nyingine nazo ziweze kushamiri na kutuleta fedha nyingi, kuzalisaha ajira na kutuletea maendeleo katika nchi yetu, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Hotuba ya Bajeti iliyotolewa na Waziri wa Fedha siku ya tarehe 14 Juni, 2022. Kwanza napenda nitanabaishe kwamba Bajeti iliyoletwa mbele yetu sisi Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekwenda sambamba na falsafa ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutaka kuleta maendeleo kwa wananchi wa nchi yetu ya Tanzania na kuwakwamua kutokana na changamoto mbalimbali za kiuchumi ambazo zinawakabili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu pia bajeti hii imeakisi hotuba iliyotolewa na Mheshimiwa Rais siku aliyokuwa anaapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku ya tarehe 19 Machi, 2021. Pia imeakisi hotuba ambayo Mheshimiwa Rais aliitoa hapa Bungeni siku ya tarehe 22 Aprili, 2021 ambayo ililenga katika mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza lilikuwa ni kuongeza ajira; jambo la pili, ni kuongeza tija katika uwekezaji; jambo la tatu, kuongeza mishahara; jambo la nne, kuongeza tija katika biashara ndogo ndogo na kubwa; lakini pia kuongeza tija katika ukuaji wa uchumi wenye manufaa kwa wananchi wetu wa Tanzania na kubana matumizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kwanza nizungumzie changamoto iliyopo duniani. Dunia imepitia katika changamoto ya COVID-19, lakini pia sasa inapita katika changamoto ngumu zaidi ya vita kati ya Urusi na Ukraine. Vita hivi pamoja na janga hilo la COVID-19 vimefanya gharama za maisha kuwa juu, gharama za bei ya petroli kuwa juu, lakini vilevile bei ya chakula, ikiwemo mafuta ya kula, ngano na bidhaa zingine kuwa juu. Kwa sababu zile nchi ambazo zinapambana ni nchi ambazo ni mabingwa katika uzalishaji wa hizi bidhaa ambazo nimezungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme tu kwamba, kwa takwimu ambazo zimetolewa hivi karibuni, siku ya tarehe 8 Juni, 2022, zinaonesha kwamba takriban watu milioni 179 hadi 181 watakumbwa na uhaba wa chakula katika nchi zipatazo 41 kati ya Nchi 53 Barani Afrika. Sasa na miongoni mwa nchi ambazo zitapata changamoto hii ya uhaba wa chakula ni pamoja na jirani zetu wa Kenya, Uganda, DRC, Mozambique pamoja na Malawi. Kwa hiyo tuna kila sababu kuwekeza katika kilimo hasa cha mazao ya chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tuendelee na juhudi za kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya kilimo. Tumeanza kuona bajeti imetoka kwenye bilioni 200 ya kilimo kwenda bilioni 900 na ushee. Kwa hiyo, niiombe Serikali iendelee kuwekeza katika eneo hilo na isimamie Taasisi ambazo zinahusika na uzalishaji wa mazao kwenye mashamba makubwa. Tunazo Taasisi za Kijeshi kama Magereza, JKT na maeneo mengine zihimizwe na ziwezeshwe kuweza kuzalisha mazao mengi ya chakula ili janga ambalo linazinyemelea nchi za jirani lisiweze kutufikia na tuweze kunusurika na hii hali ya uhaba wa chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mafuta, nchi yetu kama zilivyo nchi zingine duniani imeathiriwa na tatizo hili kutokana na vita vile vya Russia na Ukraine. Niishukuru Serikali yetu kwa kuchukua hatua ya kuwekeza bilioni 100 kwa kuanzia kwa ajili ya ku-stabilize bei za mafuta, lakini wasiwasi wangu ni kwamba hii vita inaweza ikachukua miaka mingi, je, tutaendelea kuwekeza hizi bilioni 100, 100 tutakuwa na uwezo huo? Panaingia mashaka kidogo hapa. Kwa hiyo naona kwamba ni vizuri tuwe na mpango mbadala wa muda mrefu wa kuona namna ya kukabiliana na changamoto hii kubwa. Nasema hivyo kwa sababu zile bilioni 100 tumetumia running bajeti, tumechomoa chomoa kwenye vifungu vya bajeti huku na huku ndiyo tumeweza kuzipata. Kwa hiyo tuna kila sababu ya kuona uwezekano wa kuanzia Fuel Price Stabilization Fund ili iweze kutuokoa na janga hili. Niishauri Serikali ifanye huo utaratibu ili kutuokoa na janga hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye upande wa Mfuko wa asilimia 10. Kwa miaka kadhaa sasa ule Mfuko umekuwa ukigaiwa kwa formula ya 4:4:2 ili kuwasaida Akinamama, Vijana na Walemavu, lakini nataka niwatanabaishe leo hapa kuna kundi limesahaulika. Wakati nafanya kampeni na wakati nilipokwenda kuwashukuru wananchi kule Jimbo la Kilwa Kaskazini nilikutana na wajomba zangu na baba zangu walisema kwamba Mheshimiwa tunatarajia kukupa dhamana. Baada ya kushinda wakaniambia tumekupa dhamana, lakini sisi akinababa, wajomba zako na baba zako mbona hatukumbukwi katika ile asilimia 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitanabaishe kwamba katika nchi yetu tumekuwa tukiishi kwa usawa, dhana ya usawa wa jinsia, rangi, makabila, imekuwa ikituongoza tangu uhuru. Kwa hiyo, nina pendekezo, kwanza asilimia 10 ibaki isiende kwa wale wamachinga, wamachinga tuwaanzishie Mfuko wao tofauti na tutafute vyanzo ili kuweza kuwasaidia. Pia hii formula tuibadilishe, wale akinababa wanahitaji pia kusaidiwa. Tuende na formula ya 3:3:3:1 wanaume, wanawake, vijana na wenye ulemavu, sikusudii kuwapunja walemavu.
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.
T A A R I F A
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa Ndugu yangu Francis Ndulane, kwamba tumeweka fedha za kusaidia wazee kwenye TASAF, maana amesema tusaidie, kwa hiyo nataka tu nimpe taarifa hiyo, anaweza kuwasaidia wajiandikishe kwenye TASAF basi watapata msaada.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndulane unaipokea hiyo taarifa?
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei kwa sababu hata wakina mama wanapata hizo fedha za TASAF, vijana wanapata hizo fedha za TASAF ili mradi tu wamekidhi vigezo. Kwa hiyo, niseme tu kwamba ninaiomba kwa mapenzi makubwa ya Baba zetu na Wajomba zetu nao wapewe fedha hizo za asilimia 10. Wapo Wajomba zangu kule, Baba zangu wakubwa, wadogo akina Mzee Ngombano na wengine wakina Mzee Kimbwembwe Baba wa hiyari wa Marehemu Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli walinipa hii hoja na kwa kuwa walinipa leo hii naona ni bora niiwasilishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda katika suala la watumishi waliotumbuliwa niseme tu kwamba kuwaondolea mishahara ambayo walikuwa wanayo ni kuwaonea, kwa sababu wale watumishi wengine waliondolewa siyo kwa sababu za upotevu wa fedha au ubadhilifu wengine tu ni mamlaka ilibadilika wakajikuta tayari wako nje ya ulingo. Kwa hiyo, kule kutumbuliwa tu tayari ni adhabu lakini ikumbukwe kwamba walipokuwa wanapokea ile mishahara wengine walikopa, sasa unapomtoa eneo moja ukamtumbua ukampeleka kutumikia nafasi nyingine ya chini itamuathiri, zile fedha alizokopa atarudisha kutoka wapi? Kwa hiyo, tuna kila sababu ya msingi ya kuhakikisha ile mishahara inabaki tutafute cha kuweza kubana matumizi ili mambo ya Serikali yaweze kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuzungumza katika Bunge lako Tukufu. Kwanza, nipende kutoa shukurani na pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya kazi nzuri ndani ya miaka mitatu ya utawala wake, kuongeza watalii wengi katika nchi yetu na hivyo kuliongezea Taifa letu mapato mengi kama ambavyo amesoma Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nimpongeze Mheshimiwa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Menejimenti nzima ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kazi nzuri ambayo wameifanya kwa Kilwa. Katika Wilaya yetu ya Kilwa kama mnavyofahamu katika karne ya 13 mnamo mwaka 1,331 Mwanazuoni maarufu aliwahi kuzuru katika Wilaya ya Kilwa kwa shughuli za utalii. Aliandika kitabu mnamo waka 1,332 akiusifu sana Mji wa Kilwa Kisiwani, ukiwa ni mji maarufu kabisa kuliko miji yote kwa wakati ule katika Pwani ya Afrika Mashariki na Kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tukirudi nyuma tunakumbuka kati ya karne ya 12 mpaka karne ya 15, Dola ya Kilwa Kisiwani ilikamata kasi kwa maendeleo, lakini hapa katikati tulipoteana. Kilwa ikashuka, Kilwa ambayo ilikuwa na Dola yake, ilikuwa na fedha zake na ilikuwa na utawala wake, ilipotea katika uso wa dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Mheshimiwa wa Rais, ameweza kufanya mambo makubwa katika Wilaya ya Kilwa na sasa Kilwa inakwenda juu kwa kasi kubwa. Ukiachia kwenye sekta nyingine, lakini kwenye sekta ya utalii peke yake wamewekeza. Wizara ya Utalii imewekeza fedha nyinyi kwa ajili ya uendelezaji wa Makumbusho ya Magofu Kilwa Kisiwani ya pamoja na Makumbusho ya kule Songomnara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru mwezi Machi, mwaka huu tulipata GN ya Kumbukizi za Majimaji. Kumbukizi ambazo tulizihangaikia kwa miaka mingi tangu baba zetu hadi leo. Tunashukuru kwamba sasa zimeweza kupatikana. Hii ni kazi kubwa ambayo imefanywa na Mheshimiwa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri, ambaye anahusika na Wizara hii, tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumelipwa fidia kwa watu wetu wengi, fidia zinazotokana na madhila yaliyotokana na wanyama waharibifu na wanyama wakali. Tunashukuru watu wengi wamelipwa, ni jambo jema sana ambalo tulikuwa tunalipigania kwa miaka zaidi ya mitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi nyuma kusisitiza kwenye utalii wa utamaduni na historia (cultural and historical tourism) kama nilivyosema mwanzo Kilwa ilikuwa imeshamiri sana kwa utalii wa aina hii tangu karne ya 13. Kumbukumbu za kihistoria zinasema wakati Ibn Battuta, alipofika Kilwa aliikuta Kilwa Kisiwani yenye ukubwa usiozidi square kilometer mbili ilikuwa na misikiti 99, ukiwemo msikiti wa karne ya 11. Msikiti ambao ulijengwa kwa umahiri mkubwa haijawahi kutokea katika zama zile katika Ukanda wote wa Pwani ya Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, alikuta watu wa Kilwa, wamestaarabika sana kiasi kwamba, walikuwa wanajua hadi kusoma na kuandika. Walikuwa ni hodari wa kuandika mashari kwa Lugha ya Kiswahili. Nisema nasisitiza kwenye utalii huu, kwa sababu hata walipotokea wavamizi katika Kilwa Kisiwani ile misikiti 99, ilihusika katika kuomba dua kiasi kwamba, ile merikebu ambayo ilikuja kuvamia Kilwa Kiswani iligeuka kuwa jiwe la jahazi lipo mpaka leo. Utalii wa kihistoria na utamaduni umenufaisha nchi nyingi ikiwemo: Nchi ya Misri, Algeria, Morocco, Israeli, Saudi Arabia, Jordan, Palestina, Uturuki, Iraq, Syria na Tunisia. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuwekeza kwenye utalii wa utamaduni na kihistoria. (Makofi)
Mheshimimiwa Mwenyekiti, ukienda Misri unakuta kuna yale ma-pyramid ya Mafarao likiwemo lile pyramid kubwa kabisa lililopo kule Giza, la Farao Khufu au Cheops, ambaye aliishi katika karne ya 26 kabla ya Kristo. Ukienda Uturuki unakuta kuna mjini unaitwa Antioch una kumbukumbu muhimu sana za kidini, hasa dini ya kikristo. Wakati Mtume Paulo alipokuwa anafanya kazi zake kule Antioch. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sisi tumejitahidi kuwekeza kwa kushirikiana na taasisi za dini na kadhalika. Israeli mambo yapo hivyo hivyo, Palestina yapo hivyo hivyo. Sasa ningeomba Serikali iendelee kuwekeza kwa kutangaza hivi vivutio vya utalii, kuendeleza utafiti lakini pia kuendeleza kuboresha miundombinu kuelea kwenye vivutio vyetu vya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nje ya Kilwa, kulikuwa na Rhapta Makao Makuu ya Mji wa Dola ya Azania, nyuma kidogo kabla ya Dola ya Kilwa. Pia, kuna Visiwa vya Fanjove pale Songosongo, kuna Kilwa Kiswani, Songomnara Kumbukizi za Majimaji, Mapango ya Namaingo na Nan'goma ambayo yapo pale Kilwa Kaskazini. Pia kuna viboko albino kule Mpindilo, kuna Kumbukizi Dainosari (mjuzi mkubwa). Kwa hiyo, nina imani hivi vyote vikiunganishwa vikitangazwa vizuri vikiendelea kutafitiwa vikawekewa miundombinu mizuri ya kufikika, ni wazi kwamba tutaongeza tija na ufanisi katika sekta ya utalii na tutapata fedha nyingi pengine kuliko nchi yoyote Barani Afrika. Kwa hiyo, niiombe Serikali iongeze nguvu katika hayo maeneo. Pia, kule kwenye Kumbukizi za Majimaji ninaomba Mheshimiwa Waziri, tuteue taasisi ambayo itasimamia kumbukizi zile baada ya kuwa zimepata GN. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tuweke bajeti kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025, bajeti hii tunayokwenda kuipitisha tarehe 3, kwa hiyo, ningeomba iwekwe bajeti pia. Kwa hiyo, niseme tu kwa ujumla tutatoboa sana. Kwa ujumla, nirudie kupongeza Wizara na Mheshimiwa Rais kwa ujumla, kwa kufanya kazi nzuri. Kwa ujumla, nasema Mungu ibariki Kilwa, Mungu ibariki Tanzania, Mungu akubariki sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri unayofanya na Mungu ambariki Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya. Ni wazi kwamba, tutatoboa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante mtani wangu kwa kunipa nafasi ya kujadili bajeti ya Wizara yetu ya Nishati jioni ya leo. Kwanza nitangulie kwa kutoa taarifa za kusikitisha, ambazo zilitokea juzi katika Jimbo letu la Kilwa Kaskazini, katika Mji Mdogo wa Somanga ambapo tulipoteza wananchi wetu (wapigakura wetu) 13 katika ajali mbaya iliyotokea katika Mji Mdogo wa Somanga. Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia taarifa ya pili ningependa kuikumbusha Serikali. Wilaya yetu ya Kilwa imekuwa ikikumbwa na mafuriko kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa na hivyo kupelekea athari mbaya za vifo, nyumba zaidi ya 200 kuanguka, mashamba kusombwa na maji, lakini pia hifadhi za chakula kusombwa na maji. Tunaiomba Serikali iiangalie Wilaya yetu ya Kilwa kwa jicho la huruma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia kwa kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya ya kuwekeza fedha nyingi akiwa na dhamira njema ya kuhakikisha kwamba anatatua tatizo la nishati katika nchi yetu ya Tanzania. Pia nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Mashaka Biteko kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya. Kwa muda mfupi tangu ameingia madarakani kwa nafasi hii kwa kweli amefanya kazi kubwa inayostahili pongezi kwa kushirikiana na msaidizi wake, Naibu Waziri dada yangu Judith Kapinga. Nawapongeza sana, pamoja na watumishi wote wa Wizara ya Nishati na taasisi zote zilizo chini ya Wizara yao. Hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pia kuzungumzia Bwawa la Mwalimu Nyerere. Kazi imefanyika kwa ufanisi mkubwa. Sasa hivi tuko katika hatua za mwisho za utekelezaji wa mradi ule ambao utatugharimu jumla ya shilingi trilioni 6.5 ambapo sasa umefikia asilimia 97.43. Ni hatua kubwa imepigwa. Kwa hiyo niiombe Serikali iendelee kuusimamia vizuri mradi ule. Pia ili kuepuka ulipaji wa riba naomba mkandarasi aendelee kulipwa kwa wakati ili tupate matokeo mazuri na tija ambayo itakuza uchumi na kuleta maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, napenda kuzungumzia mradi wa megawati 20 ambao umetekelezwa hivi karibuni na Kampuni ya kizalendo ya Power Associate Limited kule Mtwara. Kwa kweli mradi umekwenda kwa ufanisi mkubwa, umegharimu fedha kidogo jumla ya shilingi bilioni 3.6 na umekamilika kwa wakati. Hii inaonesha namna gani Wizara yake Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu haikufanya makosa kumpa mkandarasi mzalendo kazi hii. Niiombe Serikali iendelee kuwaamini wakandarasi wetu wazalendo, siyo tu kwa Wizara ya Nishati bali wizara zote pamoja na halmashauri zetu zote na taasisi zote za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kuwa sasa umeme unapatikana kwa uhakika, baada ya kuwa tumekarabati ule mtambo wa uzalishaji wa umeme pale Somanga wa Megawati 2.5. Kazi iliyobaki ni kukarabati pia miundombinu na usambazaji wa umeme. Tunahitaji sana nguzo za zege, kwa sababu tumetoka kwenye kukatika umeme kwa zaidi ya mara 15 kwa siku. Jana naangalia ripoti ambazo huwa wanatutumia wataalam wetu wa TANESCO. Jana umeme umekatika mara nne Wilaya ya Kilwa. Mara moja walikuwa wanakata miti kwa hiyo wakalazimika kukata umeme, lakini shida mara tatu ulikatika kwa sababu ya miundombinu ambayo ni dhaifu. Kwa hiyo, naomba ile miundombinu iondolewe iwekwe ya zege ili umeme ufike kwa uhakika iwe mvua iwe jua, kukitokea hata ule moto kichaa, basi mambo yote yaweze kwenda vizuri. Nina hakika sasa kusini inakwenda kufunguka na uwekezaji utaongezeka, uchumi utakua pia hata wale wafanyabiashara wadogo wadogo ambao walikuwa wanategemea umeme, wataweza kutumia umeme na kuleta ufanisi katika shughuli zao za kibiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia ule mradi unaotekelezwa kupeleka gridi ya Taifa kutokea Songea na Tunduru kupitia Masasi uweze kutekelezwa kwa haraka ili hii tija sasa iweze kuongezeka na tuwe na alternatives nyingi za kupata umeme wa uhakika katika Mikoa yetu ya Lindi na Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa REA, napenda kuzungumzia kijiji changu kimoja, kinaitwa Kijiji cha Hanga. Tangu mwaka 2020, wakati vijiji vingine vilipokamilisha utekelezaji wa umeme wa REA II kile kijiji kimetelekezwa. Ningeiomba Wizara na Taasisi yake ya REA, iweze kukiangalia Kijiji cha Hanga. Wale wananchi wamekuwa wakilalamika tangu wakati wa kampeni, hadi uchaguzi unafanyika mpaka leo lakini kile kijiji hakijaweza kuunganishiwa umeme. Naomba REA na Wizara wakisimamie ili kipate umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu CSR naomba Bomba la Gesi limepita kutokea Mtwara katika kata zangu tatu. Kata mbili hizi zimekuwa angalau zinaonja manufaa ya kupita kwa gesi katika yale maeneo, Kata ya Tingi na Somanga, lakini Kata ya Miteja kwa kweli haijawahi kunufaika na chochote. Pamoja na juhudi zinazoendelea za kupeleka umeme wa mitaani katika Mji Mdogo wa Somanga, niiombe Serikali basi iangalie Kata ya Miteja ili angalau tujengewe hata kituo cha afya, kwa sababu wananchi wa kata ile wamekuwa wakihangaika kwenda katika maeneo ya mbali kufuata huduma ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, linguine, naomba kuzungumzia LNG. Mpaka sasa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ufahamu haujatolewa wa kutosha kuhusiana na utekelezaji wa miradi ya LNG katika Mikoa ya Lindi na Mtwara. Ningeomba ufahamu wa kutosha utolewe ili watu wa Mikoa yetu hii ya Lindi na Mtwara wajue kinagaubaga, kwamba watanufaika na nini na ule mradi. Pia hata sisi Wabunge katika maeneo mengi tumekuwa hatujui sana haya mambo. Kwa hiyo hata viongozi tunastahili pia kupewa elimu ya kutosha kuhusu utekelezaji wa miradi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)