Primary Questions from Hon. Stephen Lujwahuka Byabato (3 total)
MHE. STEPHEN L. BYABATO aliuliza: -
Je, lini Barabara ya Lake Oil - Ijuganyodo hadi Kyamunene itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2024/2025 Barabara ya Lake Oil – Ijuganyodo hadi Kyamunene imetengewa shilingi milioni 40 kwa ajili matengenezo ya changarawe urefu wa kilometa 2.078 na ujenzi wa mifereji mita 800. Aidha, mkandarasi wa kazi hiyo ameshapatikana na anatarajiwa kuanza hivi karibuni. Katika mwaka 2025/2026 barabara hiyo pia imewekwa kwenye mpango wa bajeti kwa kutengewa shilingi milioni 33 kwa ajili ya matengenezo ya kiwango cha changarawe urefu wa kilometa mbili ili kukamilisha urefu wa kilometa 4.078.
MHE. STEPHEN L. BYABATO aliuliza: -
Je, Serikali imeweka utaratibu gani wa kuwatambua wakandarasi wazawa wanaofanya kazi nzuri ili kuwapa motisha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI Alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) huwatambua makandarasi wanaofanya kazi nzuri kwa kuwapatia tuzo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na tuzo za ukuaji haraka kwa wale wanaoonesha ukuaji mzuri tangu usajili, tuzo kwa wakandarasi wanaozingatia usalama kazini na tuzo kwa ajili ya kumpuni zinazomilikiwa na wanawake zenye mafanikio katika miradi. Aidha, mkandarasi anapokamilisha kazi aliyopewa vizuri kulingana na mkataba mwajiri hutoa hati maalum ya kukamilisha kazi (Final Completion Certificate) ambayo hutambua kuwa kakamilisha kazi yake vizuri.
MHE. STEPHEN L. BYABATO aliuliza:-
Je, kwa nini watumishi wanaojitolea wanapoajiriwa wasipangiwe katika Vituo walivyokuwa wakijitolea kama kipaumbele cha kwanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu ya Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo Na.2 la Mwaka 2008, ikisomwa pamoja na Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298, Ajira katika Utumishi wa Umma hupatikana kwa ushindani na uwazi. Kujitolea katika Utumishi wa Umma huwezesha vijana kujipatia ujuzi wa ziada pamoja na kuwapa uzoefu na uwezo wa kushindana pindi ajira zinapotangazwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale ambapo wanaojitolea wanafaulu usaili, majina yao hupelekwa kwa waajiri ambao huwapangia vituo vya kazi kulingana na mahitaji ya ikama iliyoidhinishwa katika vituo husika. Ninakushukuru.