MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pia ningeomba niende mbele zaidi kwa sababu uhalisia unaonesha wanafunzi wanaosoma shule za binafsi hawapati mkopo either wote au kiasi, lakini pia kwa sababu ya umuhimu wa baadhi ya fani kama udaktari na gharama kubwa ya kusomesha watoto kwenye fani hizo, Serikali inaonaje kuwa na mpango wa muda mrefu ili wanafunzi wote wameweze kupata mikopo kwa asilimia mia moja?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kama ilivyotokana na jibu langu la msingi, Serikali inaendelea kupanua wigo wa bajeti katika Bodi yetu ya Mikopo. Kwa hiyo naomba nilichukue suala la Mheshimiwa Mbunge kwa vile kutoka mwaka 2017, Serikali imeweza kuongeza bajeti katika bodi ya mikopo kutoka bilioni 427 mpaka hivi sasa tuna bilioni 460. Kutokana na hivyo basi, wanufaika ni wengi na wanaendelea kuongezeka kutoka wale laki moja katika kipindi cha mwaka 2015 mpaka kufikia laki moja na arobaini mwaka 2021.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunapoongeza bajeti hii tuna hakika tunaweza kufanya coverage kubwa ya wanafunzi. Naomba kutoa taarifa katika waombaji wa mwaka huu wale wa mwaka wa kwanza maombi yote yalikuwa 66,000, lakini waliopata jumla karibu walikuwa 55,000. Kwa hiyo tunaendelea kuongeza ule wigo kwa lengo kuhakikisha kwamba wanufaika wanakuwa wengi zaidi.
MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nishukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali na yenye kutia moyo.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kama tuna majengo ambayo yana hadhi yuko tayari kununua vifaa, je, atakuwa tayari hata ndani ya Bunge hili wakati linaendelea, kutembelea Kiteto ukiongozana na mimi kukagua baadhi ya majengo tuliyonayo ili tuweze kuangalia kama hilo linawezekana?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Vyuo vya VETA ni muhimu sana kwa taifa letu na hususan kwa vijana; na kwa kuwa Wilaya ya Kiteto ni wilaya kongwe sana nchini, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuwahakikishia wananchi wa Kiteto kwamba Wilaya ya Kiteto VETA iko kwenye priority list na Chuo cha VETA kitajengwa kwa manufaa ya Taifa letu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Olelekaita, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la kutembelea Kiteto liko wazi, nitamuomba Mheshimiwa Mbunge baada tu ya kikao hiki tuweze kuonana ili kuiweka ratiba yetu vizuri ya kwenda kuona huko Kiteto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la pili alilolizungumza ni dhahiri, nilibainishie tu Bunge lako Tukufu kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi kwamba Serikali ina azma thabiti ya kuhakikisha kwamba tunakwenda kujenga vyuo vya VETA katika kila wilaya na mkoa nchini.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, vijana wetu hawa pamoja na kupata taaluma katika vyuo hivi vya VETA, tuna vyuo vyetu vilevile vya FDC. Mfano, hukohuko Kiteto Chuo cha Wananchi cha Tango kinafanyiwa ukarabati mkubwa na kitaanza kutoa fani za mifugo, kilimo, umeme, ushonaji na uwashi. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Mbunge vijana wetu sasa wanaweza kwenda kujipatia taaluma zao pale, lakini tuna vyuo vingine vya VETA vilivyoko katika Mkoa wa Manyara ambapo napo vilevile wanaweza kwenda kupata mafunzo hayo. Hata hivyo, suala la mpango wa Serikali wa kujenga vyuo vya VETA katika kipindi kijacho tutakapopata fedha tutahakikisha tunapeleka chuo katika Wilaya ya Kiteto. Ahsante.