Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Geoffrey Idelphonce Mwambe (11 total)

MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza: -

Je ni lini serikali itajenga Chuo cha Ualimu Masasi baada ya Chuo cha Ualimu Ndwika kuwa shule ya Sekondari ya Wasichana?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Idelphonce Mwambe, Mbunge Jimbo la Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilibadili Chuo cha Ualimu Ndwika kuwa Shule ya Sekondari ya Wasichana kutokana na mahitaji ya wakati huo. Kwa sasa Serikali ina vyuo 35 vya Ualimu vyenye uwezo wa kudahili wanachuo 25,054 ambapo hadi sasa jumla ya wanachuo 22,085 wamesajiliwa. Idadi hii ni chini ya uwezo wa vyuo hivyo katika udahili kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeelekeza nguvu katika ukarabati wa vyuo hivyo ili kuweka mazingira wezeshi ya ufundishaji na ujifunzaji. Aidha, Serikali itaendelea kujenga Vyuo vya Ualimu katika maeneo mbalimbali kulingana na mahitaji na rasilimali.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itauboresha uwanja wa mpira wa Boma uliopo Masasi Mjini kwa kiwango kinachofaa kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana wa Masasi?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Mwambe, Mbunge wa Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Taifa ya mwaka 1995 kifungu cha 7(i) hadi (vii), jukumu la ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya michezo ni jukumu la Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa pamoja na wadau wa sekta ya michezo zikiwemo taasisi, mashirika na watu binafsi.

Mheshimiwa Spika, hivyo, napenda nitoe rai kwa Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Mji Masasi kuzingatia matakwa ya sera ya michezo kwa kutenga fedha kutoka katika mapato ya ndani kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo kwenye maeneo yao kama zilivyofanya Halmashauri za Ruangwa, Geita, Nyamagana, Bukoba na Babati Mjini, ahsante.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa stendi mpya ya Mji wa Masasi ikiwa ni mradi funganishi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Masasi hadi Mnivata?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Idelphonce Mwambe, Mbunge wa Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa ushirikiano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ipo katika hatua za mwisho za kumpata Mkandarasi wa ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara ya Mnivata – Newala – Masasi yenye urefu wa kilomita 160. Taarifa ya uchambuzi wa zabuni za kumpata mkandarasi zimekamilika na kuwasilishwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya kupata idhini ya kuendelea na hatua ya kusaini mkataba (no objection). Kwa vile mradi wa ujenzi wa Stendi mpya ya Mji wa Masasi ni moja ya miradi itakayotekelezwa kama mchango kwa jamii chini ya mradi wa ujenzi wa barabara hii, kazi za ujenzi wa stendi mpya ya Mji wa Masasi itaanza baada ya mkataba wa ujenzi wa barabara kusainiwa na kazi za ujenzi kuanza. Ahsante.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itasimika taa kwenye barabara za mitaa Mji wa Masasi ili kuongeza usalama, kupunguza uhalifu na kuhamasisha shughuli za biashara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Idelphonce Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwepo kwa uhitaji wa taa za barabarani katika Halmashauri ya Mji wa Masasi kutokana na kukua kwa shughuli za kimaendeleo, kiuchumi na kijamii.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa wedha wa 2022/2023, Serikali kupitia TARURA - Wilaya ya Masasi imetenga shilingi milioni 192 kwa ajili ya kusimika taa 48 kwenye barabara za Mji wa Masasi ambazo zitawekwa kwenye barabara za TANESCO - Yatima na Barabara ya Mkapa.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza:-

Je, lini Vijiji vya Namikunda, Chipole, Machombe, Mtakateni, Machenje, Matawale, Mpekeso, Chakama na Kata ya Temeke vitapewa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Mwambe, Mbunge wa Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini inatekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambapo vijiji vyote ambavyo havina umeme Tanzania Bara vitafikiwa na huduma ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Masasi, Mkandarasi NAMIS Corporate Limited alipewa jumla ya vijiji 17 ambavyo havikuwa na umeme. Hadi kufikia tarehe 15 Agosti, 2023, vijiji 11 vimeshawashwa umeme na vijiji sita vitakamilika kabla ya mkataba wa Mkandarasi kwisha tarehe 31 Desemba, 2023. Aidha, vijiji vya Namikunda, Mtakateni, Matawale, Mpekeso na Chakama vimeshawashwa umeme. Vilevile, hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2023, Vijiji vya Chipole na Machombe vitakuwa vimepatiwa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa zoezi la kusimamisha nguzo katika Kata ya Temeke bado linaendelea na nguzo tayari zimesimamishwa katika Kijiji cha Machenje na zoezi la kuvuta waya linatarajiwa kufanyika mwezi Septemba, 2023. (Makofi)
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kilometa 1,000 za reli ya Standard Gauge kati ya Mtwara - Mbamba Bay na Songea – Ludewa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Idelphonce Mwambe, Mbunge wa Masasi Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili wa ujenzi wa kilometa 1,000 za reli ya Standard Gauge ya Mtwara hadi Mbamba Bay na matawi yake ya kuelekea Liganga na Mchuchuma. Aidha, taarifa hiyo ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali, ilionesha kuwa mradi huu unaweza pia kutekelezwa kwa utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership - PPP).

Mheshimiwa Spika, hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kumuajiri Mshauri wa Kifedha (Transaction Adviser) ili aweze kufanya mapitio ya upembuzi uliokamilika mwaka 2016 kwa lengo la kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa mwekezaji kwa utaratibu wa ubia (PPP), ahsante.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha usanifu wa mradi wa maji ya Mto Rufiji yatokayo Bwawa la Julius Nyerere kupeleka Mikoa ya Lindi na Mtwara?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Idelphonce Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Masasi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na taratibu za tathmini ya awali ya usanifu wa Mradi wa Maji wa Mto Rufiji kutoka katika Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, kupeleka kwenye Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo la kuhakikisha inaongeza hali ya upatikanaji wa maji katika mikoa hiyo. Aidha, Serikali inaendelea na mapitio ya usanifu wa Mradi wa Kutoa Maji katika Mto Ruvuma kwenda kwenye Mikoa ya Mtwara na Lindi na maeneo ya pembezoni yatakayopitiwa na bomba kuu.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha usanifu wa mradi wa maji ya Mto Rufiji yatokayo Bwawa la Julius Nyerere kupeleka Mikoa ya Lindi na Mtwara?
WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Idelphonce Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Masasi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na taratibu za tathmini ya awali ya usanifu wa Mradi wa Maji wa Mto Rufiji kutoka katika Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, kupeleka kwenye Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo la kuhakikisha inaongeza hali ya upatikanaji wa maji katika mikoa hiyo. Aidha, Serikali inaendelea na mapitio ya usanifu wa Mradi wa Kutoa Maji katika Mto Ruvuma kwenda kwenye Mikoa ya Mtwara na Lindi na maeneo ya pembezoni yatakayopitiwa na bomba kuu.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Kituo kipya na cha kisasa cha Polisi na kuboresha Makazi ya Askari Polisi Wilayani Masasi?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Idelphonce Mwambe, Mbunge wa Masasi Mjini, kama ifutatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetenga fedha kiasi cha Shilingi 798,000,000 kutoka kwenye bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Masasi. Aidha, tathmini kwa ajili ya ukarabati wa nyumba 13 za makazi ya Askari Polisi imefanyika na kiasi cha Shilingi 123,172,200 zinahitajika. Fedha hizo zinatarajiwa kutengwa kutoka Mfuko wa Tuzo na Tozo katika Mwaka wa Fedha 2025/2026. Nashukuru.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Mabweni na Mabwalo katika Shule za Sekondari za Marika, Temeke, Chanikanguo, Anna Abdallah na Mtandi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka kipaumbele katika ujenzi wa mabweni kwenye shule za sekondari za kidato cha tano na sita nchini ambapo katika mwaka 2022/2023, Serikali ilijenga jumla ya mabweni 683 kupitia fedha za mradi wa SEQUIP, Barrick Tanzania na Serikali Kuu. Aidha, katika mwaka 2023/2024, Serikali imetenga shilingi bilioni 7.41 kwa ajili ya ukamilishaji wa mabweni 57.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele cha ujenzi wa mabweni na mabwalo ya kidato cha tano na sita kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wote wanaofaulu kidato cha nne wanapata fursa ya kusoma kidato cha tano na sita. Aidha, Serikali itaendelea na jitihada zake za kuhamasisha wananchi kupitia mamlaka za Serikali za Mitaa kujenga na kuziendesha hosteli katika shule za sekondari za kidato cha kwanza hadi cha nne.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza utekelezaji wa Miradi ya TACTIC kwenye Halmashauri ya Mji wa Masasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa TACTIC umegawanyika katika makundi matatu na Halmashauri ya Mji wa Masasi ipo katika kundi la tatu ambalo utekelezaji wake utaanza kwa usanifu kufanyika mwezi Novemba, 2024 kwa kipindi cha miezi nane. Baada ya usanifu, zabuni ya kumpata mkandarasi itatangazwa mwezi Julai, 2025 na baada ya kumpata mkandarasi, ujenzi utaanza mwezi Oktoba, 2025.