Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Priscus Jacob Tarimo (4 total)

MHE. PRISCUS J. TARIMO Aliuliza:-

Kumekuwa na wimbi la kukosa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wenye ufaulu mzuri waliomaliza kidato cha sita kwenye shule binafsi kwa madai kuwa wanafunzi wanaosoma shule binafsi wazazi au walezi wao wana uwezo wa kuwalipia ada ya chuo.

Je, Serikali katika kuleta usawa kwenye fursa hii ya mikopo ya elimu ya juu haioni haja ya kutoa mikopo hiyo kwa kuzingatia ufaulu wa wanafunzi wote?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa vile na mimi ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele kwenye Bunge lako tukufu, nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniona na kuniamini kwamba na mimi naweza nikawa miongoni wa watu wa kuweza kumsaidia.

Mheshimiwa Spika,baada ya hayo sasa, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge Moshi Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inawalenga vijana wenye sifa za kitaaluma za kujiunga na taasisi za elimu ya juu lakini hawana uwezo wa kumudu gharama za elimu. Upangaji na utoaji mikopo unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (Sura 178) ambayo inabainisha sifa za msingi za mnufaika ambazo zinajumuisha.Awe Mtanzania; awe amedahiliwa kwenye chuo kinachotambulika; awe ameomba mkopo, asiwe na vyanzo vingine vinavyogharamia masomo yake. Aidha, kusoma shule binafsi za sekondari siyo kigezo cha mwanafunzi mwombaji kunyimwa mkopo wa kugharamia elimu ya juu. Wapo wanafunzi waliosoma shule binafsi na wanapata mkopo baada ya kuthibitisha uhitaji wao kwa mujibu wa vigezo vya utoaji mikopo.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa mujibu wa sheria tajwa, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, ina mamlaka ya kuweka utaratibu wa kubaini wahitaji. Kwa sababu hiyo, Bodi huandaa mwongozo unaopaswa kuzingatiwa na waombaji na kuweka masharti ya utoaji mikopo kwa mwaka husika. Sifa za ziada zinazoainishwa kwa waombaji ni pamoja na; uyatima, ulemavu au wazazi wenye ulemavu na wale ambao masomo yao ya sekondari au stashahada yalifadhiliwa ambapo katika kundi hili wapo waombaji wengi waliosoma katika shule za sekondari za kulipia.

Mheshimiwa Spika, nashauri Waheshimiwa watusaidie kutoa elimu ili kuwezesha jamii kubadili mtazamo huu. Aidha, wawashauri waombaji wajaze kikamilifu fomu za maombi na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Bodi wakati wa uombaji wa mikopo ikiwa ni pamoja na kuambatanisha nyaraka zote muhimu ili kuepuka uwezekano wa mwanafunzi mwenye sifa stahiki kukosa mkopo kutokana na kutojaza kwa usahihi fomu ya maombi ya mkopo.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa hii nafasi.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, Sera ya kuwainua wananchi kiuchumi imekuwa na mafanikio sana kwenye ile mikopo inayotolewa na halmashauri kwa ajili ya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu. Hata hivyo, kumekuwa na tatizo haswa kwa vijana, vijana wanavyopewa mikopo wakifikisha umri wa miaka 35 vijana wa kike wanaenda kwenye kundi la akinamama, vijana wa kiume wanabaki hawana cha kufanya. Sasa swali langu, ni nini mpango wa Serikali wa kuwainua wanaume kiuchumi kwa sababu sera inasema ni wananchi kwa kufanya moja kati ya haya? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimo, Mbunge wa Manispaa ya Moshi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha Mifuko kadhaa ambayo inawanufaisha Watanzania kulingana na eneo lile ambalo Mfuko huo umeanzishwa. Tunatambua kwamba kundi la vijana limechanganya maeneo yote, lengo pale ilikuwa ni vijana. Hata hivyo, iko Mifuko ya wananchi wote ambao pia wananufaika na Mifuko hii, lakini pia tumejiunganisha na taasisi za kifedha ambazo yeyote yule anakuwa na fursa ya kwenda kukopa.

Mheshimiwa Spika, tuliposema vijana, wanawake, wenye mahitaji maalum, Mheshimiwa Tarimo anajua kwamba sera ya nchi yetu sasa tumeelekeza katika kumwezesha mtoto wa kike, lakini na wanawake wote kwa ujumla ili na wao waweze kuchangia pato la nchi hii kwa kufanya shughuli mbalimbali. Kwa hiyo akishapata mkopo anaweza kuanzisha biashara na Mheshimiwa Tarimo anajua, ukimwezesha mwanamke unakuwa umeliinua Taifa hili. Ukimwelimisha mwanamke unakuwa umelielimisha Taifa hili. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuliona eneo hili, kwa kuwa tunatambua kwamba ukimwezesha mwanamke unaliwezesha Taifa hili, ukimwelimisha mwanamke unaelimisha Taifa, kwa hiyo tuliona tuwawekee eneo lao ambalo wanakuwa na uhuru mkubwa wa kukopa. Anaweza kwenda kwenye Mfuko wa Halmashauri ambao una kipengele cha wanawake, anaweza kwenda Benki akakopa, anaweza kwenda kwenye Mfuko mwingine, Mifuko iko mingi, tuna Mifuko 42 ingawa sasa tutaipunguza ibaki michache, ifahamike kila mmoja aweze kwenda kukopa.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme tu bado hatujafikiria kuanzisha Mfuko wa Wanaume, lakini tayari wigo wa wanaume hao kupata mikopo upo kupitia Mifuko hiyo na taasisi za fedha. Hapo baadaye tukiona kuna umuhimu mkubwa, ama kuna udhaifu mkubwa pia tunaweza tukaanzisha kadiri itakavyowezekana. Sheria hizi na Mifuko hii tunapoianzisha tunaileta kwenye Kamati zetu za Bunge na kuona umuhimu wa kuanzisha hicho kitu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, urasimishaji wa makazi yaliyojengwa holela kwenye miji mingi katika nchi yetu ni zoezi ambalo lina gharama kubwa lakini mwisho wake yale makazi hayawi na ubora unaotakiwa hata kufikika na hata kwenye anuani za makazi yana shida kwa sababu barabara na huduma nyingine haziko vizuri:-

Mheshimiwa Spika, ni nini mpango wa Serikali wa kupima maeneo katika maeneo ya Miji, Manispaa pamoja na Majiji na yale maeneo ya pembezoni ili kuhakikisha sasa tunaipanga miji yetu vizuri na huduma zinawafikia wananchi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amezungumzia suala la upimaji wa ardhi kwenye maeneo yetu ikiwemo na maeneo ya miji ambayo yeye ameeleza. Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango huu ni endelevu ndani ya Wizara yetu ya Ardhi, kuhakikisha kwamba tunapima maeneo yote ya ardhi nchini na kwenye vipimo hivi tunabainisha huduma zote zinazotakiwa kutumika kwenye ardhi hiyo; kwanza makazi, maeneo ya taasisi, maeneo ya huduma za jamii kama vituo vya mabasi na masoko na kila kitu. Huo ndiyo mkakati ambao sasa unaendelea chini ya Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Spika, sasa nini kinafanyika baada ya kuwa tumekamilisha kupima, tunakabidhi kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa ambapo wao ndiyo wanaitunza ile ardhi na kuitumia na kuitoa kwa Watanzania ambao wako kwenye maeneo hayo. Pia hata kwenye mamlaka yenyewe inaweza kuwa inapanga sasa mipango yake. Kwa mfano, pale Moshi Mjini, baada ya kuwa tumeupima ule mji na kupanga matumizi yake, tunawakabishi Manispaa ya Moshi ili waanze kupanga sasa, hapa panatakiwa masoko, hapa vituo vya mabasi, maeneo mengine makazi na kila kitu. Kwa hiyo, mkakati huu ni endelevu na siyo tu kwa maeneo ya miji, tunakwenda sasa mpaka vijijini.

Mheshimiwa Spika, tunataka Watanzania sasa wapate maeneo yaliyopimwa, yanayotambulika rasmi ili pia tuweze kuwapa hati. Ile hati inawasaidia pia kama mtaji wa kukopea kwenye mabenki na taasisi nyingine za fedha. Kwa hiyo, malengo yetu ni endelevu na ni mapana kidogo kwa sababu tunataka kila Mtanzania anufaike na ardhi iliyoko nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naitaka sasa Wizara ya Ardhi kuendelea kukamilisha zoezi hili ili Watanzania wanufaike na ardhi waliyonayo kwenye maeneo yao. Kwa kufanya hivyo, itawezesha pia hata wawekezaji kujua wanapofika wanaambiwa eneo la uwekezaji lile pale, litakuwa limeshapangwa tayari. Kwa hiyo, mnakamilisha kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo pia kuna Afisa wetu wa Ardhi. Hhii sera ni endelevu na itakuwa na msaada mkubwa kwa Watanzania, ahsante. (Makofi)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.

Mheshimiwa Waziri Mkuu sera ya Serikali ya kuwa na shule ya sekondari kila kata imefanyika vizuri na imekuwa na mafanikio, na nia yake ni kuhakikisha watoto wote ambao wanastahili kwenda sekondari wanakwenda, lakini kupunguza umbali ambao Watoto/wanafunzi walikuwa wanatembea na wakawa wanapata tabu kidogo, lakini zaidi kupunguza pia gharama ya nauli kwa wazazi ambao walikuwa na watoto wale wa sekondari. Sasa mafanikio hayo yamepelekea kwamba watoto wale wanaofaulu form four sasa wanapangiwa shule mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, sasa kumekuwa na wimbi kubwa la kupangiwa shule za mbali mtoto anatoka Mtwara kwa mfano anapangiwa Kagera, anatoka Kilimanjaro anapangiwa Kigoma, sasa ile gharama ya nauli ile imekuwa kidogo inakuwa nzito kwa wazazi, lakini pia usalama wa wale watoto. Najua zamani kulikuwa kuna utaratibu wa kuwasafirisha kwa treni kabla ya kipindi ambacho nimesoma mimi.

Sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu, swali langu ni nini mkakati wa Serikali, aidha kwa kuwapangia shule za karibu au kutafuta namna nzuri zaidi ya kuwasafirisha wanafunzi hawa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimo, Mbunge wa Manispaa ya Moshi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza mkakati wa ujenzi wa shule za sekondari kila kata nchini kuanzia mwaka 2006 kwa lengo la kuwezesha watoto wanaotoka kwenye kata hiyo wasome eneo lililo karibu ili kupunguza gharama pia usumbufu. Zoezi hili limeendelea vizuri na leo hii angalau kila Wilaya au Halmashauri tumefikia ujenzi wa zaidi ya asilimia 95 wa shule za kata kwenye maeneo yake na kazi hiyo inaendelea kwa malengo yale yale ya kupunguza gharama za wazazi kuwasomesha Watoto, lakini hao watoto wenyewe kuwapunguzia usumbufu wa kutembea umbali mrefu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua Serikali ina mkakati gani wa mpango wetu wa kuwasomesha watoto shule za mbali.

Sasa kwenye sekondari huku tuna kidato cha kwanza mpaka cha nne, lakini kuna kidato cha tano mpaka cha sita. Wanaosoma mbali ambao tunaweza kuwatoa Dodoma kuwapeleka Kagera, Lindi na maeneo mengine ni wa kidato cha tano na sita. Sisi tuliona Serikali kwamba ni muhimu pia Watanzania hawa wakatambua pia jiografia ya nchi yao, lakini pia tukaimarisha uzalendo, pia waweze kujua jiografia ya maeneo mengine na waweze kuingiliana na makabila mengine. Kwa sababu Tanzania ya leo hatuna suala la udini, ukabila wala rangi kwa sababu Watanzania tunaingiliana tulitaka tulidumishe hilo, na kwenye elimu ya sekondari tunalifanya sana kwenye kidato cha tano na sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa suala la usumbufu kwa kuwa Serikali imesema kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne wanasoma bure, tunaamini mzazi tunampa nafasi ya kujiandaa kwa mtoto wake kwenda kidato cha tano popote atakapopangiwa nchini ili kumuimarisha vizuri kitaaluma na aweze kuendelea vizuri kwa kufahamu jiografia ya nchi yake na namna nyingine yoyote ambayo tunaweza kujifunza kwa utaratibu huo. Na huko atakakokwenda tunajitahidi pia kupunguza gharama zake, shule yoyote ya kidato cha tano na cha sita ni zile shule ambazo zinagharamiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali halafu kiasi kidogo wananchi wanachangia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tumeendelea kumpungia mzigo wa kuchangia elimu kwa mtoto wa kidato cha tano na cha sita. Kwenye sekondari kidato cha tano wanalipa shilingi 70,000 lakini gharama zake ni kubwa na Serikali inapeleka chakula na huduma nyingine. Kwa hiyo, haya yote yanalenga kukuza ule utamaduni ambao tuliujenga kutoka Serikali ya Awamu ya Kwanza ambayo ilikuwa imeimarisha sana watanzania kuondoa watu kukaa eneo moja na kujigawa kuwa ndio wako sehemu moja ili kila mmoja aweze kufahamu maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapokea ushauri, lakini tunaendelea kuangalia namna bora ya kuwapunguzia mzigo wazazi kwenye upatikanaji wa elimu na tutakuwa tunafanya maboresho kadri tunavyoendelea, kama ambavyo Wizara ya Elimu sasa inaendesha mjadala wa mtaala haya yote yatakuwa yanaingia kwenye mtaala na kuona namna bora ya kuendesha elimu na namna nzuri ya kuwapunguzia gharama wazazi, ahsante sana. (Makofi)